24 Nov 2016


KAMA nilivyoahidi katika toleo lililopita la gazeti hili, wiki hii ninaendelea na uchambuzi kuhusu uchaguzi wa Rais wa Marekani uliofanyika wiki mbili zilizopita na kushuhudia mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump, akiibuka mshindi dhidi ya mpinzani wake mkuu, Hillary Clinton wa Democrat.

Makala yangu katika toleo la wiki iliyopita ilibeba swali ‘je Trump atabadilika?” Swali hilo lilitokana na ukweli kwamba kauli za Trump na tabia yake kwa ujumla, kabla ya kuwa mgombea, akiwa katika mchakato wa chama chake kupata mgombea, na wakati wa kampeni kama mgombea wa chama chake, zilisheheni kasoro lukuki; ubaguzi dhahiri wa kidini, unyanyasaji wa wanawake na dhihaka kwa walemavu, kupandikiza chuki dhidi ya Wamarekani wasio weupe, chuki dhidi ya wageni, na mengineyo mengi yaliyoibua wachambuzi wa siasa kutodhani kuwa Trump angeweza kushinda katika uchaguzi huo.
Lakini tatizo halikuwa kwa Trump pekee bali pia watu waliomzunguka na baadhi ya makundi ya wafuasi wake. Moja ya kundi muhimu kwa ushindi wa bilionea huyo ni lile linalofahamika kama ‘alt-right’ (kifupi cha ‘alternative right’ yaani mbadala wa wahafidhina/wenye mrengo wa kulia). Kundi hili limekuwa ‘mwiba’ sio kwa waliberali pekee bali pia hata wahafidhina wenye msimamo wa wastani.
Na kundi hilo hatari ndilo analotoka mmoja wa wateule wa awali kabisa wa Trump, Steve Bannon, aliyeteuliwa kuwa mkuu wa mikakati wa Trump. Bannon alikuwa mmoja wa viongozi wa kampeni ya bilionea huyo na kabla ya hapo alikuwa mwenyekiti wa gazeti ‘hatari’ la mtandaoni, Breitbart. Gazeti hatari kwa sababu lengo lake kuu ni kuamsha hisia za makundi fulani kwa kubeza, kulaani na hata kutukana makundi kama vile Wamarekani weusi (gazeti hilo lilidai kuwa kiasili ni wahalifu), Walatino, wahamiaji, Waislam (gazeti hilo limewaita kila jina baya), watetezi wa haki za wanawake ikiwa pamoja na waathirika wa vitendo vya kubakwa, na takriban kila baya usilotarajia kuliona kwenye gazeti maarufu ambalo mwezi uliopita pekee, tovuti yake ilitembelewa na wasomaji zaidi ya milioni 19.
Kwa kumteua Bannon, ni wazi kuwa Trump ameamua kukumbatia makundi yaliyomuunga mkono hata kama yanajenga taswira isiyopendeza kwa urais wake. Tayari makundi mbalimbali ya utetezi wa haki za kiraia Marekani yanamtaka Trump kutengua uteuzi wa Bannon, mtu mwenye ajenda za kibaguzi na muumini wa ‘ukuu wa watu weupe’ (white supremacist).
Lakini taswira ya kuogofya kuhusu aina ya watu ambao Trump atawakumbatia katika urais wake haijaishia kwa Bannon pekee bali pia hata chaguo lake la mshauri wake wa masuala ya usalama wa taifa, Luteni Jenerali (mstaafu) Michael Flynn na Mwanasheria Mkuu, Seneta Jeff Sessions. Wakati Jenerali Flynn alitimuliwa na utawala wa Rais Barack Obama kutokana na kile kinachoelezwa kuwa kasoro za kiuongozi, Sessions ana tuhuma za ubaguzi wa rangi. Kadhalika, msimamo wa Jenerali huyo kuhusu masuala ya ugaidi wa kimataifa unaotajwa kuwa unaweza kuikosanisha Marekani na mataifa ya kiislamu kwa vile anaamini kuwa tatizo la ugaidi linachangiwa na Uislamu na sio magaidi kutumia kisingizio cha Uislamu kuhalalisha unyama wao.
Mteule mwingine wa Trump kushika nafasi ya ukuu wa shirika la ujasusi la nchi hiyo, CIA, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Mike Pompeo, naye anatazamwa kama mtu anayeweza kulirejesha shirika hilo katika zama zake za hatari kabisa, hasa kutokana na msimamo wake mkali kupindukia kwenye masuala ya intelijensia na usalama. Ikumbukwe kuwa katika zama zake hatari, CIA ilishiriki katika operesheni chafu kama vile mauaji ya Rais wa zamani iliyokuwa Zaire, Patrice Lumumba.
Tukiweka kando dalili za awali za mwelekeo wa serikali ya Trump, tugeukie kwanza swali muhimu: “..kwa nini Hillary Clinton alishindwa na Trump.” Sababu zinaweza kuwa nyingi, lakini za muhimu zaidi ni pamoja na ukweli kwamba Hillary alikuwa mmoja wa wanasiasa wanaochukiwa mno Marekani, japo chuki dhidi yake ilikuwa pungufu kidogo kulinganisha na Trump.
Kadhalika, kasoro kubwa iliyomwandama Hillary ni kuonekana kama sio mwaminifu hususan kutokana na skandali iliyomwandama muda wote wa kampeni yake kuhusu matumizi ya ‘server’ binafsi kwa mawasiliano ya barua-pepe alipokuwa ‘Waziri wa Mambo ya Nje.’
Vile vile, Hillary alishindwa kuwa na kauli mbiu yenye kueleweka kirahisi, kulinganisha na mpinzani wake, Trump, ya ‘Ifanye Marekani jabali tena’ (Make America Great Again). Sambamba na hilo ni ukweli kwamba ilikuwa vigumu mno kwa Democrat kuendelea kuwa Ikulu baada ya miaka minane ya urais wa Barack Obama. Kwa Marekani, ni ngumu sana kwa chama kilichokuwa madarakani kwa mihula miwili mfululizo kushinda muhula wa tatu.
Kingine kilichomwangusha Hillary ni kuzidiwa kwa kura na Trump miongoni mwa Wamarekani weupe, hususan wale ambao hawana elimu ya chuo. Kuongeza majeraha zaidi, ngome zake kuu, yaani wanawake, Wamarekani weusi na Walatino hawakumpigia kura nyingi kama ilivyotarajiwa huku Trump naye akifanikiwa kupata kura za kutosha katika makundi hayo yaliyotarajiwa kumwangusha.
Pengine kubwa zaidi ni kilichotukumba sote tuliokuwa tunafuatilia kwa karibu uchaguzi huo. Ilionekana kama jambo lisilowezekana kwa Trump kushinda urais. Kauli zake zilikuwa chafu kupita maelezo, hasa ile aliyorekodiwa akiwatusi wanawake na kujigamba kuwa ‘ukiwa mtu maarufu wanawake wanakupapatikia,’ kashfa dhidi ya walemavu, wanawake, Waislamu na Walatino (aliowaita wabakaji), na kila neno chafu ambalo mgombea japo wa ukiranja shule ya msingi, achilia mbali urais wa Marekani, hakupaswa kuropoka.
Ni kwamba, katika mazingira ya kawaida, na kwa kuamini kuwa Wamarekani wana akili timamu, isingewezekana Trump kushinda uchaguzi huo. Na katika kutupatia matumaini zaidi, takriban kura zote za maoni (opinion polls) zilionyesha Hillary akiongoza kati ya asilimia mbili na 14. Japokuwa kulikuwa na tahadhari kuwa kura hizo za maoni zilikuwa na walakini, wengi wetu tuliamini kuwa suala sio iwapo Hillary angeshinda bali angeshinda kwa kiasi gani.
Na hii inaleta swali, kwa nini takriban kura zote za maoni ziliashiria kuwa Hillary angeshinda lakini ikawa kinyume chake? Hali kama hiyo ilitokea kwenye uchaguzi mkuu wa Uingereza, Mei mwaka jana na ikajirudia kwenye kura kuhusu Uingereza kubaki au kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya. Katika kura zote hizo, matokeo yalikuwa tofauti kabisa na ubashiri wa kura za maoni.
Moja ya maelezo kuhusu ‘ubashiri fyongo’ wa kura za maoni, sio kwenye uchaguzi huo wa Marekani tu bali pia kwenye uchaguzi mkuu wa UK mwaka jana na kwenye kura ya ‘Brexit’ Juni mwaka huu, ni kile ambacho Profesa Timur Kuran wa Chuo Kikuu cha Harvard huko Marekani amekieleza katika kitabu chake ‘ukweli faraghani, uongo hadharani’ (Private Truths, Public Lies), katika kanuni (theory) yake inayojulikana kama ‘preference falsification.’ Kwa kifupi, kanuni hiyo inaeleza kuwa baadhi ya watu wanaohojiwa kwenye kura za maoni kuhusu masuala yanayogusa hisia za jamii hutoa majibu wanayoona yanaendana na ‘mtazamo wa jamii’ japo misimamo yao ni kinyume.
Kwa mfano, katika suala la Brexit, kwa kuzingatia kanuni ya Profesa, kulikuwa na hisia kuwa wanaotaka Uingereza ijitoe Umoja wa Ulaya ni wabaguzi wa rangi (racists). Kadhalika, kwa vile Trump alishatoa kauli kadhaa za kibaguzi na makundi mbalimbali ya kibaguzi kama vile KKK yalitangaza kumuunga mkono, ilijengeka picha kuwa ‘wafuasi wa Trump ni wabaguzi.’ Kwa hiyo, baadhi ya waliohojiwa kwa minajili ya opinion pools za Brexit na Trump ‘walibaki na ukweli wao faraghani na kuongea uongo hadharani,’ na katika mazingira hayo, uungwaji mkubwa kutaka UK ijitoe EU na hiyo ya Trmp miongoni mwa wapigakura haikuweza kuonekana kwa waendesha kura za maoni (pollsters).
Kwa upande mwingine, Hillary alikuwa mwathirika wa zama mpya za ‘siasa za uongo,’ wenyewe wanaita ‘post-truth politics,’ ambapo vitu muhimu kwenye mijadala na kampeni za kisiasa, kama vile ukweli na hoja za kitaalamu, vinazidiwa nguvu na kauli za uongo lakini za kugusa hisia na imani za watu. Kampeni ya Brexit hapa Uingereza ilitawaliwa na ‘post-truth politics’ na ikawezesha kambi iliyotaka Uingereza ijitoe ishinde kwenye kura ya maoni, na kwa mara nyingine tena imemwezesha Trump kushinda huko Marekani.
Kama nilivyoandika katika makala yangu kwenye toleo lililopita, tatizo la ‘post-truth politicis’ ni ‘waumini’ wa aina hiyo ya siasa. Takriban wote, angalau kwa kuangalia aina ya watu na vikundi vyao, ni waumini pia wa siasa za kibaguzi za mrengo mkali wa kulia.
Ndio, ‘post-truth politics, ni matokeo ya tabaka tawala, tabaka la wanasiasa, tabaka la wasomi na mfumo wa siasa, uchumi na jamii kushindwa kusikiliza vilio vya wananchi wa kawaida, lakini kwa bahati mbaya au makusudi, viongozi wa siasa hizo ni watu hatari zaidi ya viongozi waliopo kwenye mfumo tulionao sasa, angalau kwa nchi za Magharibi.
Je ‘post-truth politics,’ na ufanisi wake kwa Brexit na ushindi wa Trump ni vitu vinavyoweza kuenea kwa upana zaidi? Hilo ni suala la muda. Kipimo cha kwanza ni uchaguzi mkuu nchini Ufaransa Aprili hadi Juni mwakani, na kura ya maoni/chaguzi nchini Italia, Austria na Ujerumani.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wanadai kuwa ‘siasa za umaarufu’ (populist politics) kama hizo za ‘post-truth’ zina ‘uhai’ (life-span) wa kati ya miaka mitano hadi saba tu. Kwa hiyo wanabashiri kuwa hazitodumu kwa muda mrefu, na pengine hiyo itazifanya zisisambae sehemu kubwa ya dunia.
Kwa huko nyumbani, na pengine Afrika kwa ujumla, ‘siasa za hadaa/uongo’ zimekuwa sehemu muhimu ya siasa zetu za kila siku. Tofauti na kinachojiri huku nchi za Magharibi ni kwamba siasa za uongo zinatumiwa na watu wanaotaka kuondoa mfumo uliopo madarakani ilhali kwa akina ‘siye’ siasa za aina hiyo ndio zimeweka mfumo uliopo madarakani.
Je ‘siasa za hadaa/uongo’ zinaweza kuung’oa mfumo uliowekwa madarakani kwa hadaa/uongo? Mwamuzi ni muda. Hata hivyo, ukweli kuwa kuna vuguvugu la kushinikiza mapinduzi dhidi ya mfumo ulioshindwa kuutumiakia umma unaweza kuwa chachu kwa nchi kama zetu kuwahamasisha kuwa ‘imetosha.’ Na kama Trump licha ya kasoro zake zote ameweza kushinda urais kwa kisingizio cha ‘kupigania haki za wanyonge dhidi ya mfumo uliowatelekeza,’ basi yayumkinika kuhisi kuwa hata akina sie tunaweza kukumbwa na hali hiyo, japo binafsi naona uwezekano huo ni mdogo kwa sasa.
Na pengine ‘post-truth politics’ na wimbi la kudai mapinduzi dhidi ya mfumo ulioshindwa kuhudumia umma vinaweza visiwe na matokeo bora kwa nchi zetu za Afrika kutokana na kushamiri rushwa, siasa za kujuana na uwezo wa mfumo uliopo madarakani kutumia kila aina ya nguvu kusambaratisha jitihada zozote za kuupinga.
Mwisho, moja ya athari tarajiwa za Trump – kama akiendelea na msimamo wake wa kibaguzi – ni pamoja na bara la Afrika kutokuwa kipaumbele cha sera za nje za Marekani, kama ambavyo yawezekana uadui kati ya Marekani na nchi za kiislamu kuzorota maradufu, hususan kutokana na imani fyongo ya Trump na baadhi ya wasaidizi wake kuuhusisha Uislam na ugaidi.
Nihitimishe makala hii kwa upande mmoja kuikumbusha CCM kuwa wimbo wa upinzani dhidi ya mfumo unaoonekana kuwapuuza wananchi wa kawaida unapamba moto, na kwa vile CCM ni sehemu ya mfumo ambao baadhi ya Watanzania wanaona umewatelekeza, basi ni muhimu kujirekebisha. Kwa upande mwingine, Brexit na urais wa Trump ni funzo kwa vyama vya upinzani kuwa kusimama upande wa waliochoshwa na mfumo unaowapuuza kunaweza kusaidia kuleta ushindi kwa chama/mfumo mbadala.
Nimalizie makala hii kwa kuahidi kuendelea na uchambuzi huu katika toleo lijalo, kwa kuangalia athari za urais wa Trump duniani kwa ujumla hususan barani Afrika, kwa nini Hillary ameshindwa na kwa nini kura za maoni zilibashiri matokeo ya uchaguzi huo “ndivyo sivyo” na nini tunaweza kujifunza kutokana na uchaguzi huo

17 Nov 2016

JUMANNE iliyopita inaweza kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu mbaya kutokana na uchaguzi mkuu nchini Marekani ambao mshindi alikuwa mgombea wa chama cha kihafidhina cha Republican, Donald Trump.
Trump – mwongo wa waziwazi, mnyanyasaji wa wanawake, mzinzi, mbaguzi wa rangi, mbaguzi wa kidini na mwasisi wa harakati za kibaguzi dhidi ya uraia wa Rais wa sasa wa nchini hiyo, Barack Obama, alifanikiwa kumshinda mpinzani wake mkuu, mgombea wa chama cha Democrat, Hillary Clinton.
Kibaya zaidi ni kwamba mfumo fyongo wa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo ulimwezesha Trump kuwa mshindi licha ya kupata kura pungufu (60,350,241) dhidi ya mpinzani wake Hillary (aliyepata kura 60, 981, 118). Kura hizo zilizopigwa siku ya uchaguzi hujulikana kama popular vote, lakini kura muhimu zaidi na zinazoamua mshindi wa uchaguzi ni zinazofahamika kama electoral votes. Mshindi hutakiwa kupata kura hizi 270 au zaidi.
Inabidi kuelezea kwa kifupi kuhusu mfumo huo unaokanganya. Kimsingi, Wamarekani hawamchagui Rais wao moja kwa moja, badala yake kila jimbo lina watu wanaofahamika kama electors (wachaguzi) ambao hukutana mwezi Desemba mara baada ya kura zilizopigwa na kila aliyejiandikisha kupiga kura Novemba 8 ya mwaka wa uchaguzi.
Kama tulivyoona kwenye matangazo ya runinga, kila jimbo lina idadi yake ya "wachaguzi." Na jumla ya wachaguzi hao kutoka majimbo yote 51 ya Marekani ni 538.
"Wachaguzi" hao nao huchaguliwa na vyama vyao. Kila chama kina kanuni zake za uchaguzi wa "wachaguzi" hao. Uchaguzi wao hufanyika kwa hatua mbili. Kwanza, chama huchagua orodha ya "wachaguzi watarajiwa" na pili, "wachaguzi halisi" huchaguliwa na wapigakura siku ya uchaguzi. Majina ya wanaogombea kuwa “wachaguzi" yanaweza kuonekana katika karatasi ya kura au yasionekane, kutegemea kanuni husika.
Hakuna sheria inayowabana "wachaguzi" kumpigia kura mgombea aliyeshinda popular vote. Na ni katika mazingira haya ndio maana kumekuwa na jitihada za kuwashawishi "wachaguzi" hao kutompigia kura Trump, ili kumkwamisha na hatimaye kumwezesha Hillary achaguliwe. Hata hivyo, uwezekano wa hilo kutokea ni mdogo. Kihistoria, asilimia 99 ya "wachaguzi" hupiga kura kwa mshindi wa "popular vote."
Kila jimbo lina "ikulu" yake (state capitol), na hapo ndipo "wachaguzi" kutoka kila jimbo hukutana Desemba kupiga kura zao. Masanduku ya kura walizopiga hufunguliwa mwezi Januari katika kikao cha "Baraza la Wawakilishi".
Iwapo katika matokeo kutakuwa hakuna mgombea mwenye kura nyingi, au wagombea wawili watakuwa na kura sawa, Baraza la Wawakilishi litamchagua Rais miongoni mwa wagombea watano wenye kura nyingi zaidi.
Kila jimbo hupewa "kura za wachaguzi" (electoral votes) kulingana na jumla ya maseneta na wawakilishi. Kiwango cha chini kwa kila jimbo ni kura tatu. Majimbo makubwa huwa na kura nyingi kwa vile uwakikishi katika Baraza la Wawakilishi hutegemea idadi ya wakazi katika jimbo husika.
Tukirejea kwenye matokeo ya uchaguzi, Trump alipata kura za “wachaguzi” 290 huku Hillary akiambulia 228. “Wachaguzi” katika kila jimbo watakutana Desemba 17 kupiga kura zao, huku matarajio makubwa yakiwa wataheshimu jinsi wingi wa kura za “wachaguzi” alizoshinda Trump.
Kwa hiyo japo kinadharia kuna uwezekano wa “wachaguzi” hao kuamua kumnyima kura Trump na badala yake kumpa kura hizo Hillary, hali itakayosababisha matokeo ya uchaguzi huo kubadilika, uwezekano huo kiuhalisi ni mdogo mno.
Tathmini ya uchaguzi huo inahitaji zaidi ya makala moja, na katika makala hii nitagusia mambo muhimu kwa kifupi tu kwa matarajio ya kuendeleza mada hii katika makala zijazo.
Ushindi wa Trump umetokana na nini? Nchi za Magharibi zinapitia zama mpya ya siasa inayofahamika kama “post-truth politics.” Hii ni aina ya siasa inayotawaliwa na hisia na ushawishi kuliko ukweli au hoja za kitaalamu. Aina hii mpya ya siasa ilikuwa na ufanisi sana hapa Uingereza, katika kampeni za kura ya kuamua iwapo nchi hii iendelee kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) au ijitoe. Wanasiasa wa kambi iliyotaka Uingereza ijitoe walishutumiwa mara kadhaa kwa kutumia takwimu za uongo na kujenga hoja za chuki dhidi ya wageni na EU kwa ujumla, huku wakipinga kwa nguvu zote takwimu za kitaalam zilizoonyesha bayana madhara ya nchi hii kujitoa EU.
Tulipopiga kura Juni 23 mwaka huu, kambi hiyo iliyotumia hadaa na hoja za chuki ndiyo iliyoibuka mshindi, japo tayari nchi hii inashuhudia kipindi kigumu kiuchumi kama ambavyo wataalamu mbalimbali walivyoonya wakati wa kampeni.
Ukweli (facts) una sehemu tukufu katika siasa za kidemokrasia za Magharibi. Kila wakati demokrasia ilipokwenda mrama, kila ilipotokea wapigakura kufanyiwa ulaghai au wanasiasa kukwepa maswali, tulikimbilia kwenye ukweli kama mkombozi.
Lakini kwa sasa, ukweli unaonekana kupoteza nafasi yake katika kujenga mwafaka. Tovuti ya kutofautisha ukweli na uongo ya PolitiFact ilibaini kuwa takriban asilimia 70 ya hoja za Donald Trump ziliangukia makundi ya “karibu na uongo” “uongo” and “uongo kabisa." Lakini hiyo haikumzuia kushinda urais wa Marekani
Kadiri siasa zinavyozidi kuwa za uhasama na kutawaliwa na ufanisi wa wahusika kwenye nyenzo za teknolojia kama vile runinga na mitandao ya kijamii, "afya" ya ukweli (facts) kwenye mijadala na midahalo inakuwa tete. Matarajio ya wasikilizaji, watazamaji na wasomaji yanaelemea zaidi kwenye ushawishi wa mtoa hoja hata kama hoja hizo ni za uongo wa waziwazi.
Taratibu, nafasi ya wajuzi, wasomi, wazoefu na makundi mengine tuliyozoea kuyaamini kutupatia mwongozo sahihi inazidi kudidimia na mbadala wake ni hoja za kugusa hisia za watu hata kama zinapanda mbegu za mfarakano, kutumia uongo hata pale unapoonekana waziwazi ilimradi tu unaweza kuvutia kuungwa mkono na sehemu ya hadhira, kupandikiza hasira ili kuipa nguvu hadhira kuchukua hatua hata kama zinapanda athari na kwa ujumla, kutotoa fursa kwa ukweli (facts).
Aina hii mpya ya siasa ni hatari, sio tu kwa sababu unafanya ukweli kuwa uongo na uongo kuwa ukweli, bali pia kwa vile imetokea kuwa chaguo mwafaka la wanasiasa waumini wa siasa za mrengo mkali wa kulia; wabaguzi wa rangi, wabaguzi wa kidini; na viumbe hatari kama hao.
Nitazungumzia zaidi mada hii siku nyingine.
Kwa upande mwingine, ushindi wa kambi iliyotaka Uingereza ijitoe EU (licha ya hoja zao za uongo na kupandikiza chuki) na ushindi wa Trump huko Marekani ni ujio wa mapinduzi ya kimfumo; upinzani wa umma dhidi ya tabaka la wanasiasa, wasomi na taasisi za kisiasa na uchumi. Hii ingepaswa kuwa habari njema lakini tatizo ni kwamba wanaoendesha kampeni ya mapinduzi haya ni wanasiasa hatari kabisa katika nchi zao na kimataifa.
Ushindi wa Trump umepokelewa kwa shangwe kubwa na viongozi wa vyama vya kisiasa vya kibaguzi na vyenye mrengo mkali wa kulia, kama Marine LePen wa Ufaransa, Victor Orban wa Hungary, Frauke Petry wa Ujerumani, Heinz-Christian Strache wa Austria na Geert Wilders wa Uholanzi. Na kwa hapa Uingereza, mwasisi wa harakati za nchi hii kujitoa EU, Nigel Farage, amekuwa mwanasiasa wa kwanza wa nchi hii kukutana na Rais-Mteule, Donald Trump.
Kwa hali ilivyo Marekani hivi sasa ambapo kuna maandamano mbalimbali ya kupinga ushindi wa Trump, mustakabali utategemea zaidi jinsi kiongozi huyo atakavyomudu kubadilika na kuwa kiongozi wa Wamarekani wote na sio kundi la Wamarekani weupe wasio na elimu ya chuo, Wakristo wenye msimamo mkali, na magenge ya wabaguzi wa rangi kama vile kundi la Klu Klux Klan (KKK) pekee.
Je, Trump atabadilika? Kwa jinsi ambavyo kila kitu kuhusu Trump ni vigumu kukibashiri kwa ufasaha (mwenyewe anasema kutotabirika ni siri ya mafanikio), jibu fupi ni kwamba; “…hakuna ajuaye isipokuwa Trump mwenyewe.” Jibu refu ni kwamba awali kauli zake kuwa atachukua mazuri na kuacha mabaya ya mpango wa bima ya afya ya jamii ujulikanao kama Obamacare (ambao Trump aliahidi kuufuta mara moja wakati wa kampeni) ziliashiria dalili za mabadiliko.
Pia taarifa kuwa amezitoa hofu nchi za Japan na Korea Kusini kuhusu msaada wa kijeshi wa Marekani kwa nchi hizo, zilileta dalili ya matumaini kwamba huenda ameanza kubadilika. Japan inakabiliwa na tishio kutoka China, na Korea Kusini inakabiliwa na tishio kutoka Korea Kaskazini, na Jeshi la Marekani ni ngao muhimu kwa mataifa hayo.
Vile vile, tovuti ya kampeni za uchaguzi ya Trump iliondoa tamko lake la kuwazuia Waislamu kuingia nchini humo pindi akishinda urais. Hatua hiyo Ilitafsiriwa kuwa ni dalili za ‘msema ovyo’ huyo kulegeza msimamo.
Hata hivyo, tayari Trump ameeleza kuwa ataanza utekelezaji wa dhamira yake ya kuwatimua wahamiaji haramu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 11 nchini humo, ambapo ametangaza kuwa ataanza kuwatimua ‘wageni haramu’ milioni tatu mara tu baada ya kuapishwa.
Nihitimishe makala hii kwa kugusia vitu viwili. Kwanza, kushamiri kwa wimbi la “post-truth politics” na “mapinduzi dhidi ya tabaka la wanasiasa, wataalam au taasisi za siasa na uchumi” hasa kwa vile mwezi ujao, Italia itakuwa na kura ya maoni kuhusu katiba za nchi hiyo na Austria itakuwa na uchaguzi mkuu, Uholanzi itakuwa na uchaguzi wa bunge mwezi Machi mwakani, Ufaransa itakuwa na uchaguzi mkuu Aprili hadi Juni mwakani, na Ujerumani itakuwa na uchaguzi wa wabunge mwezi Septemba mwakani. Mataifa yote hayo yanakabiliwa na vuguvugu kubwa la upinzani dhidi ya Umoja wa Ulaya na chuki dhidi ya wageni, pamoja na “post-truth politics.”
Pili, moja ya makundi yaliyomsaidia sana Trump kushinda urais ni linalofahamika kama ‘alt-right.’ Kwa lugha rahisi, hawa ni zaidi ya wahafidhina. Ni wabaguzi wa rangi na dini, wapinzani wa harakati za wanawake na wanaosherehesha unyanyasaji wa wanawake, na kwa kifupi, “watu waliofanikiwa kuhamasisha kuwahadaa watafiti wa kura za maoni kuhusu nafasi ya Trump katika uchaguzi wa rais Marekani.”
Nimalizie makala hii kwa kuahidi kuendelea na uchambuzi huu katika toleo lijalo, kwa kuangalia athari za urais wa Trump duniani kwa ujumla hususan barani Afrika, kwa nini Hillary ameshindwa na kwa nini kura za maoni zilibashiri matokeo ya uchaguzi huo “ndivyo sivyo” na nini tunaweza kujifunza kutokana na uchaguzi huo.
ITAENDELEA TOLEO LIJALO


16 Nov 2016

Moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dkt John Magufuli ni ukusanyaji mapato, ikiwa ni pamoja na yale yatokanayo na madeni. Ni katika utekelezaji wa kipaumbele hicho, Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa taasisi za Elimu ya Juu (HESLB) imeanza 'msako mkali' dhidi ya 'wadaiwa sugu.' watu walionufaika na mikopo hiyo lakini hawajaanze kuirejesha.

Kwanza, nianze makala hii kwa kuipongeza serikali kwa hatua hii muhimu ambayo ikifanyika kw aufanisi, itasaidia ukusanyaji wa mapato makubwa yatakayowezesha udhamini wa serikali kwa wanafunzi wengi zaidi. Sote twatambua umasikini wa Tanzania yetu, na ni jukumu letu kuisaidia nchi yetu.

Binafsi, nilisoma kwa mkopo wa serikali kuanzia mwaka 1996 hadi nilipohitimu mwaka 1999. Wakati huo, na hadi ninaondokaTanzania mwaka 2002, hakukuwa na utaratibu wowote wa urejeshaji wa mkopo huo.

Hali hiyo imeendelea hadi mwaka huu 2016, ambapo ghafla serikali kupitia HESLB imeamka usingizini na kuanza kufuatilia fedha inayotudai, lakini sio kistaarabu (kwani sio kosa letu wadaiwa kutotengenezewa mfumo stahili wa kufanya marejesho ya mikopo tuliyopewa, bali kosa la serikali) na tunaitwa WADAIWA SUGU. Mdaiwa sugu ni mtu ambaye amedaiwa zaidi ya mara moja na hajalipa. Si sahihi kumwita mtu 'mdaiwa sugu' wakati hujamwelekeza jinsi ya kulipa deni unalomdai wala hujahangaika kumdai.



Sina hakika kama kuna watu walishawahi kupewa utaratibu wa kurejesha mikopo ya elimu waliyopewa, lakini kwa uelewa wangu na ufuatiliaji wa yanayojiri huko nyumbani, sijawahi kuona hilo.

Hata hivyo, kwa vile lawama hazijengi, na lengo la serikali 'kukurupuka' ni jema (kukusanya mapato), basi ni vema kuweka kando lawama na sote tunaodaiwa kuanza utaratibu wa malipo ya fedha tunazodaiwa.

Kwa upande wangu, nimetuma barua pepe kwa HESLB kuulizia kiwango ninachodaiwa na taratibu za malipo. 


Nimefainya hivyo ili, kwanza, kuunga mkono jitihada za serikali kukusanya mapato ikiwa ni pamoja na malipo ya mikopo tuliyokopeshwa. Pili, dawa ya deni ni kulipa. Ninawahamasisha wadaiwa wenzangu kuhusu umuhimu wa kulipa fedha tunazodaiwa. Na, tatu, ku- preempty jitihada zozote za watakaotaka kutumia suala hili la 'udaiwa sugu' kuchafua jina langu. Ni matarajio yangu kuwa kwa hatua hizi za dhati nilizochukua hakutajitokeza 'mchawi' wa kusema "ah wewe Chahali unajifanya mzalendo kumbe fisadi unadaiwa..." haha. 

Anyway, nitatumia ukumbi wangu huu kuwafahamisha majipu nitakayoletewa na HESLB na mustakabali wa 'udaiwa sugu.' 

10 Nov 2016


JUMAMOSI iliyopita ilikuwa siku ya maadhimisho ya mwaka mmoja kamili tangu Dk. John Magufuli aapishwe kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Siku moja kabla ya maadhimisho hayo, Magufuli alifanya mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari.
Mkutano huo umeibua lawama za aina mbili. Kwanza, lawama nyingi dhidi ya wanahabari kwa kutouliza maswali ya msingi na pili, dhidi ya Rais kwa kutotoa majibu ya kuridhisha.
Kuhusu hizo lawama dhidi ya wanahabari, binafsi sikushangazwa maana tunawaelewa vema wanahabari wetu. Wengi wao wamezoea kupewa habari na kuziandika (mara nyingi kwa mujibu wa matakwa ya mtoa habari). Wanahabari wetu wengi ni waoga katika kuuliza maswali magumu.
Kwa mtazamo wangu, chanzo cha tatizo hilo ni kasumba iliyojengeka zama za chama kimoja, ambapo kimsingi viongozi walikuwa waongeaji na wananchi (ikiwa ni pamoja na wanahabari) ni wasikilizaji tu. Huu utaratibu wa kuuliza maswali viongozi (ambao walikuwa kama miungu-watu katika zama za chama kimoja) bado unaonekana kama mgeni na hakuna jitihada za kutosha miongoni wa wanahabari kuondokana na kasumba hiyo.
Malalamiko kwamba Magufuli hakutoa majibu ya kuridhisha kwa maswali aliyoulizwa, yanategemea mtoa malalamiko hayo. Binafsi, ninampongeza Rais sio tu kwa kujibu maswali kwa umahiri na maelezo ya kina bali pia kwa kuwapa wanahabari wetu muda wa kutosha kuuliza maswali yao.
Siku moja kabla ya mkutano huo, baadhi ya wafuasi wa Chadema walisambaza taarifa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ikidai kuwa wanahabari watakaohudhuria mkutano wao na Rais wamekwishaandaliwa maswali ya kuuliza. Kwa lugha nyingine walikuwa wanajaribu kupoteza ‘credibility’ ya mkutano huo. Kwa vile njia ya mwongo ni fupi, jinsi wanahabari walivyopewa uhuru mkubwa wa kuuliza maswali ilionyesha bayana kuwa hakuna mwanahabari aliyepewa maswali ya kuuliza kabla ya mkutano huo.
Wengi wa wanaolalamikia majibu ya Rais ni hao hao wenye tofauti za kiitikadi na CCM, chama ambacho Magufuli ni mwenyekiti wake wa taifa. Kwa hiyo, hata kama Rais angejibu vizuri kiasi gani maswali aliyoulizwa, bado wapinzani wake wa kisiasa wangemlaumu. Ndio siasa zetu zilipofikia.
Pamoja na uchaguzi mkuu uliopita kutimiza mwaka mzima sasa tangu umalizike na kutupatia Magufuli kama Rais wetu, bado kuna kundi kubwa tu ambalo, kwa upande mmoja, ni kama haliamini kuwa mpinzani mkuu wa Magufuli kwenye uchaguzi huo, mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa, kweli alishindwa katika uchaguzi huo.
Hali hiyo inaendana na upinzani mkali dhidi ya kila linalofanywa na Rais Magufuli na serikali yake. Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu mwenendo wa chama kikuu cha upinzani cha Chadema baada ya uchaguzi mkuu na yayumkinika kuhitimisha kuwa ajenda kuu ya chama hicho kwa sasa ni kumpinga Dk. Magufuli kwa nguvu zote, hata katika masuala yenye maslahi kwa taifa.
Kwa namna fulani, upinzani huo, ambao sio kosa kisheria, umezaa genge dogo lakini lenye ushawishi mkubwa miongoni mwa wafuasi wa Chadema ambalo kwa ‘anything goes’ (lolote sawa tu) ilimradi urais wa Dk. Magufuli na uongozi wa serikali yake uonekane bomu.
Utekelezaji wa ahadi zake mbalimbali umepokelewa na watu hao kwa mtazamo hasi. Si suala la elimu ya bure au kutumbua majipu, sio kufufua Reli ya Kati au ununuzi wa ndege mbili ili kufufua Air Tanzania kunakowafanya watu hao wathamini jitihada za kiongozi huyo.
Na alipoanzisha operesheni ya kuhakiki vyeti vya elimu kwa watumishi wa umma, ikaibuliwa hoja ya kizandiki kuwa kabla hajaanza kuhakiki vyeti vya watumishi wa umma, aanze na shahada yake ya uzamivu (PhD) ambayo waliituhumu kuwa ni feki.
Na mmoja wa wahubiri wa tuhuma hiyo kuhusu elimu ya Magufuli aliandika makala katika toleo lililopita la gazeti hili akitetea ‘haki ya kuhoji PhD’ ya kiongozi huyo. Tatizo sio kuhoji bali kumtuhumu Rais kuwa shahada yake hiyo ni feki. Na licha ya kutoa mifano mingi ya hadaa mbalimbali za kitaaluma, mtoa lawama alishindwa kuthibitisha tuhuma zake. Unapomtuhumu mtu kuhusu kosa fulani ni jukumu lako mtoa tuhuma kuzithibitisha tuhuma hizo na sio mtuhumiwa. 
Dk. Magufuli hakujipa shahada ya uzamivu, alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Yeyote mwenye shaka kuhusu shahada hiyo au mbili zilizotangulia (BSc na MSc) anaweza kuwasiliana na chuo hicho au Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kupata uhakika. Kuhoji sio tatizo. Kutuhumu ni zaidi ya tatizo. Ni uzandiki. Na uzandiki (kumfarakanisha Rais na wananchi anaowaongoza kwa kumtuhumu kuwa ana PhD feki) ni tishio kwa usalama wa taifa.
Lakini tatizo hasa sio ndege mbili za Magufuli au PhD yake au majibu yasiyoridhisha kwenye mkutano kati ya Rais na wanahabari. Tatizo ni hao wenzetu ambao ni kama bado wapo kwenye ‘mode’ ya uchaguzi (election mode), hawataki kukubali kuwa mgombea wa chama chao alishindwa kihalali, na sasa tuna Rais mpya ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya mwaka sasa. Na wenye nia njema na Tanzania yetu wanaridhishwa mno na utendaji kazi wa Rais huyo, hususan katika mapambano yake dhidi ya rushwa na ufisadi, ajenda iliyokuwa nguzo ya Chadema kabla ya kumpokea Lowassa (mwanasiasa ambaye chama hicho kilimtuhumu kwa miaka tisa mfululizo kuwa ni fisadi, kabla ya kugeuza ‘gia’ angani na kumteua kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho).
Japo kila mgombea anapaswa kuwaaminisha wafuasi wake kuhusu fursa za kushinda katika uchaguzi, binafsi ninaona kama matumaini ambayo Lowassa aliwapatia wafuasi wake yalikuwa ya kina mno kiasi kwamba mwaka mmoja baada ya mwanasiasa huyo kubwagwa kwenye uchaguzi mkuu, bado wafuasi wake wengi hawaamini kilichotokea.
Lakini pia kuna kundi ambalo sio tu liliamini kuwa ushindi wa Lowassa ulikuwa sio wa mwanasiasa huyo pekee bali nao walikuwa na matarajio ya nyadhifa fulani, hususan wale ambao jitihada zao za kuwania nafasi kama ubunge ziliishia kwenye ngazi ya kura za maoni tu. Kwa Lowassa kushindwa kwenye uchaguzi huo ilimaanisha kuwa nao ndoto zao za madaraka ziliota mbawa.
Nimalizie makala hii kwa kumpongeza Dk. Magufuli kwa kutimiza mwaka mmoja wa urais uliosheheni mafanikio lukuki. Amefanikiwa sio tu kuitoa Tanzania yetu kutoka chumba cha wagonjwa mahututi bali pia ameweza kurejesha nidhamu ya kazi na kuondoa dhana kwamba uhalifu (ufisadi, ujangili, kuuza unga, nk) ndio njia halali ya kipato. Wengi wa wanaomlaumu Dk. Magufuli kuwa amefanya maisha kuwa magumu ni watu waliokuwa wakiishi kwa kutegemea ‘dili.’
Na kwa wanaolalamika kuwa Dk. Magufuli ni dikteta, anaminya uhuru wa vyama vya upinzani labda kwanza waanze kudai demokrasia ndani ya vyama vyao ambavyo baadhi vimekuwa kama vya kisultani kwa kuwa na sura zile zile za viongozi wakuu miaka nenda miaka rudi pasi chaguzi kuu.

3 Nov 2016


JUMAMOSI wiki hii, Rais Dk. John Magufuli atatimiza mwaka mmoja kamili tangu aingie madarakani kama Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kufanya tathmini ya tangu Magufuli atangaze nia ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM, na hatimaye kuchaguliwa kuwa mgombea wake, kabla ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana na kuapishwa, kabla ya kuanza jukumu zito la kuiongoza nchi yetu, ni kitu kinachohitaji kitabu kizima.
Bahati nzuri, huko nyuma niliandika kitabu kuhusu ‘safari’ hiyo ya Dk Magufuli, japo tathmini iliisha kwenye takriban miezi mitatu tangu aingie rasmi madarakani. Wakati huu, ninaandaa kitabu kitakachochambua mwaka mzima wa kiongozi huyo tangu aingie madarakani.
Hata hivyo, hata bila kutumia kitabu, yawezekana kufanya muhtasari wa tathmini ya kipindi cha mwaka mmoja wa Magufuli na serikali yake ya Awamu ya Tano kwa ujumla. Na njia nyepesi ya kufanya tathmini hiyo ni kuangalia maeneo tunayoweza kuyaita mafanikio na yale yasiyo mafanikio.
Katika mafanikio, Rais Magufuli amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutimiza ahadi alizotoa binafsi kama mgombea wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na zilizotolewa na chama chake katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Moja ya ahadi hizo ilikuwa mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Katika eneo hili, Rais Magufuli amefanikiwa mno.
Kwa vile tayari Magufuli na serikali yake wameonyesha kuwa mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ni kitu kinachowezekana, ni rahisi kwa baadhi ya watu kuona kuwezekana huko ni suala la kawaida tu. Ni rahisi pia kusahau ugumu uliotawala suala hilo kwa miaka kadhaa, kiasi kwamba baadhi ya tafiti kuhusu maoni ya wananchi kuhusu rushwa na ufisadi zilionyesha kuwa idadi kubwa tu ya wananchi “walishasalimu amri” kwa rushwa na ufisadi kuwa ndio hatima yao. Kwamba hata zifanyike jitihada za aina gani, rushwa na ufisadi vitaendelea kushamiri.
Kwa hiyo, licha ya kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi, Dk. Magufuli amekuwa akipambana na mfumo pia ulitoa mizizi kwenye saikolojia ya taifa letu. Kwa mafanikio yaliyokwishapatikana hadi muda huu, huku tukisubiri kuanza rasmi kwa mahakama ya ufisadi, kwa hakika Magufuli anastahili pongezi.
Ndio, kuna changamoto kadhaa kwenye sekta mbalimbali kama vile afya na elimu, lakini ni muhimu kufahamu kuwa ili tuwe na ufanisi kwenye sekta mbalimbali ni lazima kwanza tujenge nidhamu ya mapato na matumizi, sambamba na kubana mianya ya rushwa na ufisadi, ambayo kimsingi ndio iliyodidimiza sekta hizo. Sasa, kama ambavyo maradhi huingia mwilini na pengine kusambaa kwa kasi lakini huchukua kitambo kuyatibu, ndivyo ambavyo tunahitaji ustahimilivu kabla ya jitihada za Magufuli hazijaanza kuonekana kwa wingi na kwa wazi zaidi zikileta mabadiliko katika maeneo mbalimbali.
Eneo jingine ambalo Magufuli amefanikiwa ni kurejesha heshima ya kazi. Kwa muda mrefu, kulikuwa na imani fyongo kwamba ‘uhalifu unalipa’ (crime pays) na wenzetu waliofanya bidii kwenye kazi halali au kujiajiri kwa biashara au kilimo walionekana kama vituko. Lakini sasa tunashuhudia wimbi kubwa la wenzetu wakiwekeza kwenye kilimo na shughuli nyingine za kujiingizia kipato halali. Kadhalika, imani kwamba mtu anaweza kuishi kwa kutegemea kipato halali imeanza kurejea kwa kasi. Hili nalo si jambo dogo kwa sababu sio tu linahusu mfumo bali pia saikolojia ya taifa.
Awali nilikuwa miongoni mwa wasiopendezwa na jinsi Serikali ya Magufuli ilivyoonekana kuvibana vyama vya upinzani. Na katika kuthibitisha hilo, niliandika makala moja kuishauri serikali kuhusu suala hilo. Hata hivyo, nilichokishuhudia tangu wakati huo hadi sasa, kinaweza kuhalalisha umuhimu wa serikali kuchukua msimamo mkali dhidi ya baadhi ya vyama vya siasa au wafuasi wa vyama hivyo.
Sawa, kila mwananchi ana haki ya kumkosoa rais au serikali yake. Hata hivyo, kuna kukosoa kwa ajili ya kujenga na kukosoa kwa ajili ya kubomoa. Kwa makusudi, baadhi ya Watanzania wenzetu huko kwenye upinzani, pengine kutokana na kukosa ajenda yoyote kwa maendeleo ya vyama vyao, wamewekeza nguvu kubwa mno kuchochea chuki kwa wananchi dhidi ya serikali yao.
Kwa vile hatupaswi kutoa fursa yoyote ile ya kuruhusu uvunjifu wa amani, hasa katika kipindi hiki ambapo serikali ya Magufuli inafanya jitihada kubwa za kuiweka Tanzania yetu katika mahali inapostahili kuwepo, ninaunga mkono hatua za serikali dhidi ya yeyote anayejaribu kuchochea uvunjifu wa amani. Demokrasia ya kuchochea wananchi dhidi ya serikali yao ni uhuni. Watanzania wanahitaji maendeleo na sio kuwachonganisha na serikali yao.
Kama kuna eneo ambalo ninaweza kumkosoa Rais Magufuli ni kuhusu baadhi ya watu aliowakabidhi dhamana ya kumsaidia. Awali alieleza kuwa angeunda baraza la mawaziri dogo tu lenye ufanisi na atakayevurunda atawajibishwa. Nina hakika rais anawafahamu vema baadhi ya mawaziri ‘mizigo’ ambao wana kila dalili ya kumchafua kwa wananchi. Naam, wakiboronga wao, atakayelaumiwa ni aliyewateua. Ingekuwa vema rais akitumia maadhimisho haya ya mwaka mmoja madarakani kutathmini utendaji wa baadhi ya mawaziri wake na wale walioshindwa kuendana na kasi yake, wapumzishwe.
Sambamba na hilo ni doa la kisiasa huko Zanzibar linaloendelea kuchafua sura ya Tanzania. Wakati ni Wazanzibari wenyewe wanaoweza kufikia mwafaka wa kudumu wa mgogoro wa muda mrefu wa kisiasa visiwani humo, kuna haja kubwa tu kwa Serikali ya Muungano ‘kutomwagia petroli kwenye moto,’ kwa maana ya kujiepusha na kauli ambazo zinaweza kuchochea mfarakano zaidi visiwani humo.
Nimalizie makala hii kwa kukupongeza Rais Magufuli kwa kutimiza mwaka mmoja tangu uapishwe kuwa rais wetu. Wengi wanaokupinga au kukulaumu ni watu waliozoea kula vya bure, waliovuna wasichopanda, waliofakamia keki ya taifa kifisadi, watu ambao zama za Ujamaa tuliwaita kupe. Endelea kukaza uzi ili mabadiliko unayokusudia na yanayohitajiwa mno na Watanzania yatimie. Asante kwa kuanzisha safari ya Tanzania yetu kuelekea mahali inapostahili kuwa na kamwe usiyumbishwe na wanaotaka kutukwaza.

14 Oct 2016


HISTORIA FUPI YA MWALIMU NYERERE
MPAKA MAUTI YALIPOMFIKA

Tarehe ya kuzaliwa 13 Aprili 1922
Mahali pa kuzaliwa Butiama
Tarehe ya kifo 14 Oktoba 1999
Rais wa Tanzania
Alingia ofisini 1964
Aliondoka ofisini 1985
Alitanguliwa na (alikuwa rais wa kwanza)
Alifuatwa na Ali Hassan Mwinyi
Dini Mkristo Mkatoliki
Elimu yake Chuo Kikuu cha Edinburgh - Uskoti Digrii
anazoshika M.A. ya historia na uchumi
Kazi mwalimu, mwanasiasa Mengine Nyerere alikuwa
mwenyekiti wa chama cha TANU na baadaye wa CCM.
Mara nyingi aliitwa "Mwalimu Nyerere".
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa rais wa
kwanza wa Tanzania. Alizaliwa Butiama, mkoani Mara
pembezoni mwa Ziwa Nyanza tarehe 13 Aprili, 1922.
Alifariki dunia 14 Oktoba, 1999. Aliiongoza Tanzania toka
mwaka 1961 hadi mwaka 1985.
Yeye ni mwasisi wa itikadi ya ujamaa na kujitegemea.
Kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa ni mwalimu. Kazi
hii ndiyo ilimpatia jina ambalo lilimkaa maisha yake yote la
"Mwalimu." Mwalimu Nyerere ni kati ya viongozi wachache
wa Afrika ambao wameacha madaraka kwa hiyari baada
ya kutawala kwa muda mrefu. Alipostaafu urais mwaka
1985 alirudi kijijini kwake Butiama ambako aliendesha
shughuli za kilimo. Aliendelea kuwa na athari kubwa
katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.
Maisha Ya Mwalimu
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922
( katika kijiji cha Butiama, wilaya ya Musoma, mkoa wa
Mara, Tanzania (wakati ule: Tanganyika). Alikuwa
mojawapo kati watoto 26 wa Nyerere Burito, chifu wa
kabila la Wazanaki. Alipokuwa mtoto Nyerere alichunga
mifugo ya babake; katika umri wa miaka 12 aliingia shule
akitembea kilomita 30 hadi Musoma. Baada ya kumaliza
shule ya msingi aliendelea kusoma shule ya wamisionari
Wakatoliki huko Tabora. Katika umri wa miaka 20
alibatizwa akawa mkristo Mkatoliki hadi mwisho wa
maisha yake.
Mapadre wakaona akili yake wakamsaidia kusoma ualimu
huko Makerere, Kampala, Uganda kuanzia 1943 - 1945.
Makerere akaanzisha tawi la Umoja wa wanafunzi
Watanganyika pia amejihusisha na tawi la Tanganyika
African Association (TAA). Baada ya kumaliza masomo ya
ualimu alirudi Tabora akifundisha shule ya St.Mary´s.
Mwaka 1949 alipata skolashipu ya kwenda kusoma
kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh huko Uskoti /Uingereza
akasoma M.A. ya historia na uchumi(alikuwa mtanzania
wa kwanza kusoma katika chuo kikuu cha Uingereza na
mtanzania wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya
Tanzania).
Aliporejea Tanganyika kutoka masomoni, Nyerere
alifundisha Historia, Kingereza na Kiswahili katika shule ya
St. Francis iliyo karibu na Dar es Salaam. Mwaka 1953
alichaguliwa kuwa raisi wa chama cha Tanganyika African
Association (TAA), chama ambacho alikisaidia kukijenga
alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere.
Mwaka 1954 alikibadilisha chama cha TAA kwenda katika
chama cha Tanganyika African National Union (TANU)
ambacho kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko TAA. Ndani ya
mwaka mmoja chama cha TANU kilikuwa tayari chama cha
siasa kinachoongoza Tanganyika.
Uwezo wa mwl. Nyerere uliwashitua uongozi wa kikoloni
na kumlazimisha Nyerere kuchagua kati ya siasa na kazi
ya ualimu. Nyerere alisikika akisema kuwa alikuwa
mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati
mbaya. Alijiuzuru ualimu na kuzunguka nchini Tanganyika
kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta
muungano katika mapigano ya uhuru. Pia alizungumza
kwa niaba ya TANU katika Trusteeship council na Fourth
committee ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York.
Uwezo wake wa kimaongezi na kuunganisha watu
ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata uhuru bila
umwagaji wa damu. Ushirikiano mzuri aliouonyesha
aliyekuwa gavana wa wakati huo bwana Richard Turnbull
ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa uhuru. Nyerere
aliingia katika bunge la kikoloni mwaka 1958 na
kuchaguliwa kuwa waziri mkuu mwaka 1960. Mwaka 1961
Tanganyika ilipata uhuru wake na tarehe 9/12/1961
Nyerere alichaguliwa kuwa waziri mkuu wa Tanganyika
huru na mwaka mmoja baadae Nyerere alikuwa raisi wa
kwanza wa jamhuri ya Tanganyika. Nyerere alikuwa kiungo
muhimu katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar
kutengeneza Tanzania baada ya mapinduzi ya Zanzibar
mwaka 1964 yaliyomtoa madarakani sultani wa Zanzibar
Jamshid bin Abdullah.
Sifa zake
Bado anakumbukwa na watanzania hasa wa hali ya chini
kutokana na sera zake za kujali utu na ubinadamu.Pia
ataendelea kukumbukwa na waafrika kote barani hasa kwa
mchango wake mkubwa wakati wa harakati za kupigania
uhuru katika nchi mbali mbali barani Afrika.
Ni mmoja wa viongozi wachache wanaokumbukwa kwa
kutojilimbikizia mali pamoja na kutawala kwa miaka zaidi
ya 24.
Mwishoni mwa maisha yake Nyerere aliishi kama mkulima
wa kawaida kijijini kwake Butiama. Alipatwa na kansa ya
damu (leukemia) na kufariki Uingereza wakati wa kutibiwa
katika mji wa London tarehe 14 Oktoba, 1999. Alizikwa
mahali pa kuzaliwa kwake, kijiji cha Butiama.
Machapisho ya mwl.Julius K. Nyerere.
• Freedom and Socialism.Mkusanyiko wa maandiko na
hotuba, 1965-1967 (1968)
• Freedom & Development, Uhuru Na Maendeleo (1974)
• Ujamaa - Essays on Socialism' (1977)
• Crusade for Liberation (1979)

CHANZO: Jamii Forums


13 Oct 2016

NIANZE makala hii kwa kueleza masikitiko yangu kutokana na tukio lililoripotiwa wiki iliyopita ambapo walimu wanafunzi kadhaa walionekana katika video wakimwadhibu mwanafunzi katika namna isiyofaa na isiyokubalika kabisa. Laiti mtu akiiona video husika bila ya maelezo anaweza kudhani mwanafunzi aliyekuwa akipigwa na walimu hao wanafunzi alikuwa mwizi.
Pamoja na kukerwa mno na kitendo hicho, sikushangazwa na suala zima la vurugu (violence) dhidi ya mwanafunzi husika. Sikushangazwa kwa sababu jamii yetu imekuwa ikisherehesha vurugu. Ni mara ngapi tumeshuhudia polisi wetu wakitumia nguvu nyingi zaidi hata pale ambapo busara tu ingetosha? Ni watumishi wa nyumbani wangapi ambapo tulichokishuhudia kwenye video husika ndio maisha yao ya kila siku, kwa maana ya unyanyasaji wanaofanyiwa na waajiri wao na hawana sehemu ya kukimbilia?
Na je, ni watoto wangapi – hususan watoto wa kambo – ambao kila siku ya maisha yao ni zaidi ya unyanyasaji aliofanyiwa mwanafunzi wa kwenye video husika? Je, ni Watanzania wenzetu wangapi ambao ulemavu wao wa ngozi yaani ualbino umekuwa chanzo cha wao kuwindwa, kukatwa viungo na kuuawa? Na wazee wetu wangapi wameuawa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa vile tu wana macho mekundu (imani fyongo kuwa ni dalili ya ushirikina)?
Na kuhusu vurugu shuleni, kama hilo tukio la walimu hao wanafunzi, sheria za nchi zimehalalisha vurugu kwa kuendelea kuruhusu adhabu za kikoloni kama hiyo ya viboko. Tatizo letu ni kuamini zaidi katika adhabu badala ya kukarabati tabia. Angalia magereza zetu zilivyojaa vibaka na wezi wa kuku badala ya kuwapa kifungo cha nje na kuweka mkazo katika kuwageuza kuwa raia wema.
Tukio hilo sio tu liifumbue macho serikali kuhusu umuhimu wa mitandao ya kijamii katika kutuhabarisha yale ambayo pengine vyombo vyetu vya habari vya asili visingeweza kuripoti (na hili ni angalizo kwa Rais Dk John Magufuli kuhusu matamanio yake kuona malaika wakishuka na kuifunga mitandao ya kijamii) bali pia liiamshe kuhusu suala la viboko shuleni. Adhabu ya viboko imepitwa na wakati, ni kandamizi, ni mwendelezo wa vurugu dhidi ya watoto na si ya kistaarabu.
Baada ya kuzungumzia suala hilo la kipigo cha walimu hao kwa mwanafunzi, nigusie mada ya wiki hii ambayo pia inahusu elimu. Mwishoni mwa mwezi uliopita, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipiga marufuku wanafunzi kwenda shuleni pekupeku au na nguo zilizochanika.
Alitoa maagizo hayo katika ziara yake mjini Kibiti, Pwani wakati akizungumza na wananchi wa eneo hilo kwenye mkutano wa hadhara. Waziri Mkuu alisema;  “Zile fedha mlizokuwa mnatumia kulipa ada na michango sasa zitumieni kununua sare na chakula cha watoto wenu, ni marufuku mtoto kwenda shule huku akipekua au akiwa amevaa sare zilizochanika,”
Hivi kweli Majaliwa anadhani wazazi wa watoto wanaokwenda shuleni wakiwa pekupeku au na nguo zilizochanika wanafanya hivyo kama ‘fasheni’ ya suti za waheshimiwa wetu? Hivi kweli Majaliwa hajui kuwa ni umasikini wa kupindukia unaosababisha baadhi ya Watanzania wenzetu kutomudu uwezo wa kuwanunulia watoto wao viatu na sare nzuri?
Moja ya masuala yaliyonikera sana katika miaka 10 ya Awamu ya Nne ni pale viongozi wakuu wa serikali, Rais na Waziri Mkuu wake, wakieleza bayana kuwa hawajui kwa nini Tanzania ni masikini. Lakini angalau wao, licha ya kutoelewa chanzo cha umasikini wetu, hawakuja na amri ya kushangaza kama hiyo ya Majaliwa.
Pamoja na heshima kubwa niliyonayo kwa Waziri Mkuu wetu, ninaomba kutofautiana naye kuhusu amri hiyo. Anachopaswa kufanya ni kutilia mkazo sera zitakazoziwezesha familia masikini sio tu kumudu fedha za kuwanunulia watoto wao sare na viatu, bali angalau kuwa na uhakika wa mlo ujao.
Ni hivi, Waziri Mkuu, kimsingi amri yako ina- criminalise umasikini, kwamba ni kosa kisheria kwa mzazi kuwa masikini kiasi cha kushindwa kumnunulia mwanaye sare bora za shule.
Amri hiyo ya Waziri Mkuu inaonesha jinsi baadhi ya viongozi wetu walivyo mbali na wananchi wanaowaongoza kiasi cha kutoelewa shida wanazokabiliana nazo katika maisha yao.
Nihitimishe makala hii kwa kumsihi Majaliwa atafakari upya kuhusu amri yake hiyo na kwa vile ninaamini anawajali Watanzania wote, wenye kujimudu kimaisha na masikini wasiomudu kununua sare bora za shule kwa watoto wao, atatengua amri hiyo.

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.