3 Jan 2017



Kuna msemo wa kisiasa unaosema "in politics, perception is reality." Maana yake katika tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili ni kwamba 'katika siasa, kitu kinavyoonekana ni sawa na uhalisi wake. 

Kwa mantiki hiyo, kura ya maoni iliyobandikwa na gazeti la Raia Mwema katika akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter ikiwa na swali kama linavyoonekana katika 'tweet' husika hapa chini, inaweza kuwa na uzito.

Ndio, siyo kura ya kisayansi lakini idadi ya watu 448 'waliopiga kura' (hadi wakati ninaandaa makala hii) ni sampuli ya kutosha kwa kura ya maoni. 
Natambua makada wa CCM hawatopendezwa na makala hii, na huenda kuna watakaohoji kwanini niipe uzito kura ya maoni ya Twitter. Jibu langu ni hilo kwenye sentensi ya kwanza, "in politics, perception is reality." Lowassa kuongoza katika kura hiyo ya maoni kunajenga perception flani ambayo kwenye siasa ni reality. 

Neno la tahadhari kuhusu kura hiyo ya maoni ni kwamba bado inaendelea na haijafikia tamati. Kwahiyo, matokeo ya mwisho yanaweza kuwa tofauti, hasa ikzingatiwa kuwa tofauti ya asilimia ni kiduchu.

Pengine moja ya vitu vinavyompunguzia umaarufu Rais Magufuli ni baadhi ya kauli zake...kama hii hapa pichani chini. Ikumbukwe kuwa moja ya sifa ya uongozi bora ni pamoja na kutumia lugha isiyojenga picha ya dharau au kukosa huruma kwa wananchi. Na tukiamini kuwa 'in politics, perception is reality,' basi picha hasi inayoweza kutokana na baadhi ya kauli za Rais Magufuli zaweza kujenga taswira hasi kumhusu yeye na uongozi wake, hata kama hatamki kwa nia mbaya.




29 Dec 2016


ATIMAYE mwaka 2016 unafikia ukingoni ambapo siku nne zijazo tutaingia mwaka mpya 2017. Makala hii inafanya tathmini ya jumla ya matukio makubwa zaidi, hususan ya kisiasa, kitaifa na kimataifa.
Tukio kubwa zaidi kimataifa ni kuyumba kwa itikadi ya siasa za kiliberali katika nchi za Magharibi, suala lililokwenda sambamba na kukua kwa siasa za mrengo mkali wa kulia. Kadhalika, nchi kadhaa za Magharibi zinaendelea kushuhudia ujio wa zama mpya za siasa, zinazojulikana kama ‘post-truth,’ ambazo kwa tafsiri fupi ni ‘kupigia chapuo uongo, na upinzani dhidi ya ukweli.’
Ni katika mazingira hayo, kulijitokeza mshtuko mkubwa katika nchi hizi za Magharibi, na pengine duniani kwa ujumla, pale Uingereza ilipoamua kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (EU) katika kura ya maoni iliyofanyika mwezi Juni. Kampeni za kura hiyo zilijenga msingi imara wa siasa za ‘post-truth.’
Miezi mitano baadaye, Marekani nayo ilikumbwa na wimbi hilo la siasa za ‘post-truth,’ pale mfanyabiashara bilionea, Donald Trump, aliyekuwa na kila sifa mbaya ya kumnyima japo ‘ujumbe wa nyumba kumi,’ alifanikiwa kumbwaga mwanasiasa mkongwe, Hillary Clinton. Trump na wafuasi wake walitumia kila aina ya hadaa huku wakisaidiwa na mlipuko wa habari zisizo za kweli hususan katika mitandao ya kijamii.
Kinachotisha kuhusu zama hizi za siasa za ‘post-truth’ ni ukweli kwamba zimekumbatiwa na vyama vya siasa na vikundi vyenye mrengo mkali kabisa wa kulia, pamoja na vyama/vikundi vya kibaguzi.
Kinachoendelea kusaidia ‘uongo kuwa muhimu kuliko ukweli’ ni ukweli kwamba tabaka la siasa, tabaka la uongozi, tabaka la wanataaluma na wataalamu, tabaka la wafanyabiashara, na makundi kama hayo, yanaangaliwa kama yaliyoweka pamba masikioni. Hayasikii vilio vya tabaka la watu wa chini, na hata wakisikia hawafanyii kazi vilio hivyo.
Ndio maana, watu ‘hatari’ kama vile Nigel Farage wa hapa Uingereza, Donald Trump huko Marekani, Marine Le Pen wa Ufaransa, Norbert Hofer wa Austria (ambaye almanusura ashinde urais wa nchi hiyo), Geert Wilders wa Uholanzi, Frauke Petry wa Ujerumani na kadhalika, wamemudu kutumia uongo na hadaa kwa ufanisi kutokana na ‘ukweli’ kupoteza maana yake.
Mashambulizi ya kigaidi huko Ufaransa, Ubelgiji na Ujerumani na kuendelea kuwepo kwa tishio la vitendo hivyo kumeongeza umaarufu wa siasa za mrengo mkali wa kulia ambazo zinahusisha ugaidi na sera za ukarimu kwa wahamiaji.
Mwaka 2017 unatarajiwa kushuhudia michuano mikali ya kisiasa barani Ulaya ambapo nchi zinazotupiwa jicho zaidi ni Ufaransa na Ujerumani zinazokabiliwa na hatari ya kuwa chini ya utawala wa wanasiasa wenye mrengo mkali kabisa wa kulia.
Kwa huko nyumbani, tishio kubwa halikuwa kwenye siasa bali ajali zinazoendelea kugharimu maisha ya Watanzania kwa idadi kubwa, japo janga hilo halionekani kuwasumbua wananchi na viongozi.
Kwenye ulingo wa siasa, Rais ‘mpya’ Dk. John Magufuli ndiye aliyetawala zaidi katika anga za siasa. Kwa upande mmoja, hali hiyo ilitokana na matumaini makubwa waliyonayo wananchi kwake, na kwa upande mwingine, udhaifu unaozidi kukua miongoni mwa vyama vya upinzani.
Hata hivyo, kwa kulinganisha kasi aliyoanza nayo na hali ilivyo sasa, yayumkinika kusema kuwa ‘kasi ya Magufuli imepungua.’ Huku ‘tumbua majipu’ ikizidi kuwa ya msimu (na baadhi ya utumbuaji ukituhumiwa kufanywa kutokana na majungu), sera iliyowapa matumaini makubwa, ya kuanzishwa kwa mahakama maalumu ya ufisadi iliyogeuka kuwa kichekesho ambapo tangu mahakama hiyo ianzishwe imeendesha kesi moja tu.
Na kituko kikubwa zaidi ni pale waziri mwenye dhamana ya mahakama hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe, alipotuhadaa kuwa uchache wa kesi katika mahakama hiyo ni dalili ya mafanikio, yaani ufisadi umepungua.
Lakini kama kuna suala ambalo baadhi yetu tunapata shida mno kumwelewa Rais Magufuli ni ‘kutengeneza maadui wasio wa lazima.’ Hatua za kuzuia mikutano na maandamano ya vyama vya upinzani na kukatisha matangazo mubashara ya vikao vya Bunge ni hatua ambazo sio tu hazikuwa na tija bali hazikuwa na umuhimu wowote.
Matumizi ya sheria ya makosa ya mtandao pale tu rais anapotukanwa, huku maelfu kwa maelfu ya Watanzania wakiendelea kuwa waathirika wa matusi imetufanya baadhi ya ‘tulioupigia debe’ muswada wa kuanzisha sheria hiyo tujilaumu.
Jinsi serikali ilivyowatimua wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kana kwamba walijichagua wenyewe kujiunga na masomo, na kuwakashifu kuwa ni ‘vilaza,’ uamuzi wa kutishia ajira za mahakimu wasio na shahada za chuo kikuu, kupuuza jitihada za Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete za kuwashawishi Watanzania wa Diaspora kushiriki katika harakati za maendeleo huko nyumbani na badala yake ‘kuwaharamisha’ kwa kuwazuia kumiliki ardhi, na hatua kama hizo, ni baadhi ya mambo yaliyotawala zaidi mwaka huu katika siasa za Tanzania.
Hata hivyo, Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kurejesha nidhamu ya kazi, angalau kwa kujenga mwamko wa wananchi kutegemea kipato halali badala ya shughuli zilizo kinyume cha sheria. Na japo matukio ya ujambazi yameendelea kutawala, kumekuwa na dalili nzuri ya kupungua biashara ya dawa za kulevya na ujangili. Na kama tetesi kuhusu uwezekano wa mabadiliko ya baraza la mawaziri hivi karibuni ni za kweli, basi huenda ‘timu mpya’ ikaufanya mwaka ujao kuwa ‘mwema’ zaidi kwa Watanzania.
Nimalizie makala hii kwa kuahidi kuwaletea ubashiri wa mwenendo wa mambo mbalimbali kwa mwaka kesho katika makala ijayo.
Nawatakia heri ya mwaka mpya 2017

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali 

23 Dec 2016

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Maradhi ya Binadamu (NIMR), Dk. Mwele Malecela.


  • Virusi vya Zika viligundulika kuwepo Tanzania mwaka 1952
  • Dkt Mwele na wanasayansi wenzie 'wanakuna vichwa' wakisumbuliwa na swali la kitafiti je, virusi vya Zika vilivyoko kwenye nchi za Afrika mashariki vina madhara sawa na vile vya Brazil?
  • Alichowasilisha ni ripoti ya utafiti kuhusu virusi vya Zika, na sio kutangaza mlipuko wa ugonjwa huo.
  • Sheria iliyoanzisha NIMR ilimpa ruhusa/ mdaraka ya kutoa taarifa husika.
  • Waziri husika alikabidhiwa ripoti  (kumbukumbu namba NIMR/HQ/D13) MIEZI MINNE kabla Dokta Mwele hajatoa ripoti hiyo hadharani.


ANGALIZO: Japo ninafahamiana na Dokta Mwele Malecela (kama dada-rafiki), makala hii ya kiuchunguzi ni jitihada zangu binafsi kupata undani na usahihi kuhusu hatua iliyochukuliwa na Rais Magufuli wiki iliyopita kutengua wadhifa wa Dkt Mwele wa Ukurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR). Ikumbukwe sasa tunaishi katika zama za 'post truth politics' (siasa za hadaa/uongo) ambapo moja ya tabia muhimu ni kupingana na ukweli na kuugeuza uwe uongo, na uongo uwe ukweli. Ni jukumu la kila mmoja wetu kupambana na janga hili ambalo limetawala mno mwaka huu 2016 na kupelekea 'balaa' la Brexit (Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya) na Donald Trump kushinda Urais huko Marekani. 

Dokta Mwele Malecela ni nani?

Kwa faida ya wasiomjua vizuri Dkt Mwele, historia yake kwa kifupi ni kama ifuatavyo: Amekuwa mtumishi wa NIMR kwa miaka 30 mfululizo, ambapo alianza ngazi ya awali kabisa kama mwanasayansi 'wa ngazi ya mwanzo' (junior scientist). Yaani kama jeshini basi tungesema alianza kama 'private' na kupanda ngazi hadi kuwa Jenerali. Hili linaweza kuonekana ni jambo dogo lakini ukweli ni kwamba dunia ina mahitaji makubwa ya wansayansi, hususan katika nchi zilizoendelea. Mahitaji hayo ni makubwa zaidi kwa wanasayansi wa kike ambao kwa hakika ni wachache mno. Kuitumikia NIMR kwa miaka 30 mfululizo licha ya vishawishi mbalimbali vya ajira bora zaidi kama mwanasayansi wa kimataifa, Dokta Mwele aliweka mbele maslahi ya nchi yake Tanzania.

Lakini pengine kubwa zaidi kuhusu mwanasayansi huyo ni ndoto yake ya tangu utotoni ya kuwa mwanasayansi mtafiti. Kwa kuzingatia kwamba wakati anakua, baba yake, Mzee John Malecela alikuwa katika nyadhifa mbalimbali kitaifa na kimataifa, kubwa zaidi ikiwa Uwaziri Mkuu. Kwa wadhifa huo wa baba yake, Dkt Mwele angeweza 'kupata chochote,' pengine hata kujikalia tu nyumbani na 'kula maisha.' Hata hivyo, aliwekeza nguvu zake katika kufikia malengo yake ya kuwa mtafiti. 

Kielimu, alifanikiwa kuhitimu shahada ya kwanza chuo kikuu cha Dar es Salaam (BSc in Zoology) na baadaye kupata shahada ya uzamili (MSc) na ya Uzamifu (PhD) katika stadi kuhusu parasitolojia (Medical parasitology) katika taasisi maarufu ya London School of Hygiene and Tropical Medicine ya chuo kikuu cha London, hapa Uingereza.



Watanzania wengi wamemfahamu Dokta Mwele katitka kazi yake kubwa ya kutokomeza magonjwa yasiopewa kipuambele hususan matende na mabusha. Katika sehemu nyingi za Tanzania kama Pangani na Mtwara alijulikana kama mama matende. Kazi hii ilimpatia nishani ya kutambulika kwa kazi hii muhimu kutoka seriakli ya marekani (Neglected Tropical Disease Champion Award). Hivi sasa takwimu za Mtwara zinaonyesha kushuka kwa ugonjwa wa matende na mabusha kutoka asilimia 60-80 mwaka 2002 hadi asilimia 0 mwaka 2014. Juhudi hizi zimeendeshwa na Watanzania wakiongozwa na Mtanzania.

Wasifu mfupi wa Dokta Mwele upo HAPA na maelezo yake mwenyewe kuhusu safari yake hadi kuwa mwanasayansi wa kimataifa yapo HAPA 

Ni kutokana na ueledi wake mkubwa kitaaluma na kitaalamu, kitaifa na kimataifa, watu wengi wamepatwa na mshtuko mkubwa kufuatia uamuzi wa Rais Magufuli kumwondoa Dokta Mwele madarakani.



Japo taarifa ya Ikulu kuhusu uamuzi huo wa Rais haikutoa sababu yoyote, ni siri ya wazi kuwa ulitokana na taarifa aliyoitoa Dkt Mwele kwa waandishi wa habari kuhusu utafiti wa virusi vya ugonjwa wa Zika. Kwamba taarifa yake ilitafsiriwa vibaya au kulikuwa na mpango wa makusudi kumwondoa katika nafasi hiyo, ni jambo ambalo kwa sasa tunaishia kuhisi tu. Kilicho bayana ni kwamba hakutangaza MLIPUKO wa ugonjwa wa Zika bali aliripoti tu kuhusu MATOKEO ya utafiti uliofanywa na taasisi ambao ulibani kuwa sampuli 88 za damu kati ya 533 zilikuwa na virusi vya ungonjwa huo.

Historia ya Zika na uwepo wake Tanzania


Kabla ya kuingia kwa undani zaidi, ni muhimu kujielimisha vya kutosha kuhusu ugonjwa wa Zika na 'mahusiano yake na Tanzania yetu.' Kwa kifupi ugonjwa huu sio mgeni na uko katika kanda za tropiki zenye mbu na uligunduliwa kwa mara ya kwanza katika msitu zika (zika forest) Uganda mwaka 1947. Swali ambalo liko kwenye vichwa vya watafiti wa virolojia wa Afrika mashariki ni kuwa je, virusi vya zika vilivyoko kwenye nchi za Afrika mashariki vina madhara sawa na vile vya Brazil? 

Ifuatayo ni historia fupi ya Zika na uwepo wake Tanzania [Tafsiri ya Kiswahili katika maandishi mekundu]

Historia ya ZIKA

Kuanza kusambaa kwa virusi vya Zika kuliambatana na hali ya watoto kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo isivyo kawaida kunakohusiana na kutokamilika maendeleo ya ubongo (kwa kitabibu, 'microcephaly') na ugonjwa unaofahamika kama 'Guillain-Barre syndrome.' Baada ya kugundulika katika nyani nchini Uganda mwaka 1947, virusi hivyo viligundulika katika binadamu mwaka 1952. Mlipuko wa kwanza wa maradhi yanayotokana na maambukizo ya Zika uliripotiwa katika kisiwa cha Yap mwaka 2007. Hivi sasa kuna nchi kadhaa ambazo zimekumbwa na mlipuko wa  virusi vya Zika.

Zika: Asili na kusambaa kwa virusi hivyo vinavyosambazwa na mbu

Maelezo yafuatayo yanatoa muhtasari wa kusambaa kwa maambukizi ya Zika tangu yalipogunduliwa mwaka 1947 hadi mwezi Februari mwaka huu 2016 



1947: Wanasayansi waliokuwa katika uchungui wa kawaida wa homa ya manjano katika msitu wa Zika nchini Uganda wanabaini virusi vya Zika katika nyani.

1948: Virusi (vya Zika) vyatambuika katika mbu aina ya Aedes Africanus, kwenye msitu wa Zika


1969 - 1983 Uwepo wa Zika unasambaa hadi Asia ya Ikweta, ikiwa ni pamoja na India, Indonesia, Malaysia na Pakistani, ambapo virusi vya Zika vyagundulika katika mbu. Kama ilivyokuwa Afrika, maambukizi ya virusi hivyo yabainika lakini pasipo milipuko, na maradhi kwa binadamu yaendelea kuonekana adimu na ya wastani.

2007: Zika yasambaa kutoka Afrika na Asia na kusababisha mlipuko mkubwa wa kwanza katika binadamu katika kisiwa cha Yap kilichopo kwenye Bahari ya Pasifiki, Shirikisho la Mikronesia. Kabla ya tukio hili, hakukuwahi kuwepo mlipuko wa Zika na kesi 14 tu za uwepo wa Zika zilikuwa zimeripotiwa dunia nzima.

2013 - 2014: Milipuko ya Zika katika visiwa vingine vinne katika Bahari ya Pasifiki; French Polynesia, Kisiwa cha Easter, Visiwa vya Cook, na New Caledonia. Mlipuko katika Kisiwa cha French Polynesia wapelekea hofu ya maelfu ya maambukizi ya Zika, na uchunguzi wa kina waanza.Matokeo ya uchunguzi yaripotiwa kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) Novemba 24, 2015 na Januari 27, 2016.

Machi 2, 2015 Brazili yaifahamisha WHO kuhusu ripoti ya maradhi yanayoambatana na vipele kwenye ngozi katika majimbo ya Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo. Kuanzia mwezi Februari 2015 hadi tarehe 29 Aprili 2015, takriban kesi 7000 za maradhi yanayoambatana na vipele kwenye ngozi yaripotiwa. Kesi zote hizo ni za wastani na hakuna taarifa za vifo. Hakukuwa na hisia kuhusu Zika wakati huu na wala hakukufanyika vipimo vya kugundua maambukizi ya virusi hivyo. 

Februari Mosi 2016: WHO yatangaza rasmi kuwa mahusiano ya hivi karibuni kati ya maambukizi ya Zika na dalili za 'microcephaly' na matatizo  megine ya ki-nyurolojia ni janga la afya kimataifa.

Historia hiyo inatufundisha nini?

Kwahiyo, kwa kuangalia tu historia ya virusi vya ugonjwa wa Zika, ni dhahiri kuwa taarifa ya Dokta Mwele, ambayo wala haikuwa yake binafsi bali ya taasisi za NIMR na Chuo Kikuu cha Bugando, haikukiuka kanuni au utaratibu wowote, kitu ambacho kinazua maswali kuhusu uamuzi wa Rais Magufuli kutengua wadhifa wa mwanasayansi huyo wa kimataifa.

Uamuzi wa Rais Magufuli kutengua ukurugenzi Mkuu wa Dkt Mwele NIMR:

Lakini kinachoashiria kuwa 'kuna namna' katika hatua hiyo ya Rais ni masuala yafuatayo:

Kwanza, taarifa iliyotolewa na Dokta Mwele ilishawasilishwa kwa Waziri husika kwa kufuata taratibu zilizopo, tarehe 12 mwezi Agosti 2016 na kupokelewa wizarani tarehe 16 mwezi huohuo. (kumbukumbu namba NIMR/HQ/D13) Kwa maana hiyo, sio kwamba Waziri husika alikuwa hana taarifa kuhusu matokeo ya utafiti huo. 

Na kwa vile alishawasilisha taarifa ya utafiti huo kwa Waziri, Dokta Mwele alikuwa na wajibu wa kutoa matokeo ya utafiti kwa watafiti na umma wa Watanzania wote. Sheria ya bunge namba 23 ya mwaka 1979 ya kuundwa kwa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (www.nimr.or.tz) kipengele cha "vi" kinaitaka taasisi kutoa matokeo ya utafiti wote unaofanyika ndani ya Tanzania. 

Dokta Mwele amekuwa akitoa taarifa hii kwa miaka saba ambayo amekuwa mkurugenzi mkuu. Ni lazima ieleweke kuwa hakuwa anatangaza MLIPUKO wa Zika - kazi ambayo ni ya Waziri/wizara - bali ripoti ya utafiti kuhusu Zika, na hivyo ni vitu viwili tofauti. Yayumkinika kuhisi kwamba tatizo hapa ni siasa kuwekwa mbele ya utaalamu na taaluma.

Kadhalika, wakati macho yameelekezwa kuhusu Zika pekee, Dokta Mwele siku hiyo aliongelea pia kuhusu utafiti wa magonjwa ya chikungunya, dengue na virusi vya West Nile.

Kumekuwa na nguvu kubwa inayotumika kujenga picha kuwa Dokta Mwele amekuwa insubordinate kwa Waziri husika. Lakini ukweli ni kwamba ramani hizo hapo juu zimethibitisha uwepo wa virusi vya Zika nchini Tanzania kwa muda mrefu. Kadhalika, utafiti uliofanywa na NIMR umesaidia kuongeza kile kiutafiti kinachofahamika kama 'body of evidence' ya kuelewa zaidi kuhusu kuenea kwa virusi vya ugonjwa huo na ugonjwa wenyewe.

Pili, Dokta Mwele aliongea na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) Alhamisi Desemba 15, 2016 kueleza alichosema kuhusu utafiti huo wa Zika. Kipindi hicho kilirushwa na BBC saa 12 asubuhi ya siku iliyofuata, Ijumaa Desemba 16, 2016. Sio kweli kwamba Dokta Mwele 'alifanya utovu wa nidhamu kwa kuongea na waandishi wa habari baada ya Press conference ya Waziri.' Ukweli ni kwamba aliongea kabla ya Waziri. Jitihada zinazofanyika kujenga picha ya 'utovu wa nidhamu' zaweza kutafsiriwa tu kama mbinu ya kuhalalisha hatua 'ya kionevu' iliyochukuliwa dhidi ya mwanasayansi huyo.

Pili, Dokta Mwele aliongea na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) Alhamisi Desemba 15, 2016 kueleza alichosema kuhusu utafiti huo wa Zika. Kipindi hicho kilirushwa na BBC saa 12 asubuhi ya siku iliyofuata, Ijumaa Desemba 16, 2016. Sio kweli kwamba Dokta Mwele 'alifanya utovu wa nidhamu kwa kuongea na waandishi wa habari baada ya Press conference ya Waziri.' Ukweli ni kwamba aliongea kabla ya Waziri. Jitihada zinazofanyika kujenga picha ya 'utovu wa nidhamu' zaweza kutafsiriwa tu kama mbinu ya kuhalalisha hatua 'ya kionevu' iliyochukuliwa dhidi ya mwanasayansi huyo.

Wakati uchunguzi huu unafanyika, ilibainika kuwa kuna jitihada za makusudi zinazoendelea mitandaoni 'kumchafua' Dokta Mwele. Kwa 'macho ya juu juu,' ni kama wananchi tu wanatoa maoni yao kuhusu suala hilo, lakini kwa yeyote atakayeangalia kwa 'jicho la tatu,' hatoshindwa kubaini kuwa kuna co-ordinated efforts' za kumchafua mwanasayansi huyo. Kwa bahati nzuri, juhudi hizo zinagonga mwamba kutokana na wananchi wengi kuonekana kumuunga mkono Dokta Mwele huku baadhi wakiamini kuwa ameonewa tu.

Kwa muda mrefu kulikuwa na kile kilichohisiwa kuwa jitihada za makusudi kuhakikisha Dokta Mwele anang'oka katika wadhifa huo. Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kuvujishwa hadharani mawasiliano ya kiofisi (yaliyopaswa kubaki ndani ya NIMR pekee) na tuhuma za ufisadi ambazo uchunguzi uliofanyika ulibaini kuwa hazikuwa na ukweli.

Mwaka jana, wakati Dokta Mwele alipochukua fomu za kuwania kuteuliwa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, zilifanyika jitihada za kudukua mawasiliano yake, na uchunguzi ulibaini uhusika wa mwanasiasa mmoja maarufu wa chama hicho ambaye pia anahusishwa na jitihada za muda mrefu 'kuhakikisha Dokta Mwele anang'oka NIMR.' 

Hitimisho: 

Ripoti hii ya kiuchunguzi inaonyesha bayana ukweli kuhusu Dokta Mwele ameondolewa madarakani bila ya hatia yoyote. HAKUFANYA KOSA LOLOTE. Sheria ya NIMR inamruhusu kuripoti kuhusu tafiti mbalimbali kama hiyo ya kuhusu virusi vya Zika. Pia Waziri husika alipewa ripoti ya utafiti huo miezi minne kabla ya Dokta Mwele kuitangaza hadharani. 


Katiba inampa nguvu Rais kuteua na kutengua viongozi wa taasisi mbalimbali za umma. Rais Magufuli alitumia nguvu hiyo ya Kikatiba kuchukua uamuzi huo dhidi ya Dokta Mwele. Hata hivyo, pengine Rais atapata wasaa wa kujiuliza kwanini waziri husika alikuwa na taarifa za utafiti huo tangu mwezi wa Agosti mwaka huu lakini hakuziwasilisha kwake?  Kadhalika, kama Waziri husika hataki kuona ripoti za tafiti mbalimbali zikitangazwa na 'watu walio chini yake' basi na awasilishe muswada bungeni ili sheria iwezeshe hilo.

Mara kadhaa Rais Magufuli amekuwa akiwakumbusha Watanzania kuwa msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Basi itakuwa vema asiishie kwenye kuhubiri tu kuhusu usemwa kweli bali sasa atekeleze kwa vitendo na kutafakari upya ukweli kuwa Dokta Mwele hajatendewa haki. Licha ya Dokta Mwele kuwa mchapakazi, kitu ambacho NIMR inajua, Watanzania wanajua na ulimwengu unajua, pia hana kosa katika suala hili. Hii haimaanishi kumfundisha kazi Rais au kumwekea shinikizo bali kushauri haki itendeke.

Kwa upande mwingine, japo ni dhahiri kuwa kutakuwa na nafasi luki za kimtaifa zinazomsubiri Dokta Mwele, hatua iliyochukuliwa dhidi yake inaweza kuwa na athari kubwa katika namna watafiti wanafanya kazi nchini Tanzania. Ikifika mahala watafiti kuhofi kutangaza matokeo ya tafiti zao hata kama wamefuata taratibu zote, watakaoathirika zaidi ni Watanzania.

Na mwisho, kwa vile tumebahatika kuwa na Rais msomi na mwanasayansi basi ni matarajio yetu kuwa ataweka kipaumbele kwenye ukweli kuliko majungu, maana sayansi is all about ukweli na sio hisia. Kadhalika, ni matarajio ya Watanzania kuwa Rais hatoruhusu siasa kuingilia utaalam na/au taaluma. Ikumbukwe kuwa moja ya vikwazo vikubwa vya maendeleo yetu ni siasa kuingilia kila eneo. Ili azma za Tanzania, kwa mfano sera ya 'Tanzania ya viwanda' zitimie, ni lazima tuwasikilize watafiti. Na linapokuja suala la afya ambalo ndio uhai wetu, hatuna hiari wala uchaguzi kuwapuuza wataalamu katika sekta hiyo kama Dokta Mwele.

MUNGU IBARIKI TANZANIA



22 Dec 2016

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Maradhi ya Binadamu (NIMR), Dk. Mwele Malecela.
IJUMAA iliyopita, kulijitokeza tukio ambalo hadi wakati ninaandika makala hii limezua utata. Usiku wa siku hiyo, Rais Dk. John Magufuli alitengua wadhifa wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Maradhi ya Binadamu (NIMR), Dk. Mwele Malecela.
Siku moja kabla, Dk. Mwele alizungumza na waandishi wa habari kuwaeleza kuhusu matokeo ya utafiti wa takriban mwaka mzima kati ya NIMR na Chuo Kikuu cha Bugando kuhusu ugonjwa huo na ilibainika kuwa kati ya sampuli za damu 533, 88 zilikutwa na virusi vya ugonjwa wa zika.
Hata hivyo, siku iliyofuata, serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto ilitoa taarifa kuwa ugonjwa huo haujaingia nchini, kana kwamba taarifa ya Dk. Mwele ilizungumzia kuingia kwa ugonjwa huo.
Pengine kabla ya kuingia kwa undani katika kujadili suala hili, ni vema niweke bayana ukweli kuwa Dk. Mwele ni dada-rafiki yangu, na nimesikitishwa sana na tukio hilo, hususan jinsi wadhifa wake ulivyotenguliwa.
Ni kwamba, wakati taarifa ya wadhifa wake kutenguliwa ilitolewa usiku wa Ijumaa iliyopita, saa chache baadaye, Jumamosi asubuhi, kukatangazwa uteuzi wa Profesa Yunus Mgaya kuchukua wadhifa ulioachwa wazi na Dk. Mwele.
Kama nilivyoeleza awali, hadi wakati ninaandika makala hii kuna utata unaoendelea kuhusu suala hilo. Hiyo imetokana na vitu kadhaa. Kwanza, taarifa ya Ikulu kuhusu uamuzi wa Rais Magufuli kutengua ukurugenzi wa Dk. Mwele haikueleza kwa nini rais alichukua uamuzi huo, tena usiku.
Kadhalika, utata huo unachangiwa na hisia kuwa huenda ‘siku za Dk. Mwele zilikuwa zinahesabika,’ kwani katika mazingira ya kawaida, sio rahisi mkurugenzi wa taasisi nyeti kama NIMR kuondolewa madarakani usiku kisha mbadala wake akapatikana asubuhi.
Hisia hizo zinachangiwa pia na ukweli kuwa Dk. Mwele ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, mzee John Malecela. Miezi minane iliyopita, familia ya mwanasiasa huyo mkongwe ilikumbwa na ‘balaa’ kama hili, ambapo Rais Magufuli alimwondoa madarakani mke wa mzee Malecela, mama Anne Kilango, aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Tofauti na wadhifa wa Dk. Mwele ulivyotenguliwa bila maelezo, tukio la mama Kilango liliambatana na maelezo kwamba alitangaza kwenye vyombo vya habari kuwa mkoa wake hauna watumishi hewa jambo ambalo lilisababisha Ikulu kufanya uchunguzi wake na kubaini wafanyakazi hewa 45 katika awamu ya kwanza huku awamu ya pili ya uchunguzi bado ukiendelea.
Katika mazingira ya kawaida, huwezi kumlaumu mtu anayeweza kuhoji “tatizo lilikuwa utendaji kazi wa mama Kilango na Dk. Mwele au ‘mlengwa’ ni mzee Malecela?”
Wasomi kadhaa waliozungumzia hatua ya rais dhidi ya Dk. Mwele wameonyesha kushangazwa kwao, hasa ikizingatiwa kuwa rais naye ni miongoni mwa wasomi. Kwamba, alichofanya Dk. Mwele ni kuripoti tu matokeo ya utafiti husika, lakini kukajitokeza mkanganyiko katika tafsiri ya ripoti ya matokeo hayo.
Laiti busara ingetumika, basi Dk. Mwele angefahamishwa tu kuwa taarifa yake imezua mkanganyiko, na angeitisha mkutano na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi. Ikumbukwe kuwa dada huyo ni mmoja wa wanasayansi wachache kabisa kutoka Afrika na hususan Tanzania wanaoheshimika mno kimataifa.
Japo sijapata idhini yake ‘kutoa siri hii,’ mwishoni mwa mwaka jana alinieleza kuwa anahitajiwa na taasisi moja ya kimataifa inayohusiana na masuala ya afya duniani, lakini akasema hayupo tayari kuacha kuwatumikia Watanzania wenzake. Binafsi nilimshauri akubali tu nafasi hiyo kwa vile atakapoitumikia dunia, atakuwa akiitumikia Tanzania pia. Hata hivyo, Dk. Mwele alikataa nafasi hiyo.
Vile vile, baada ya jina lake kutopitishwa kuwania kuteuliwa katika nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM mwaka jana, Dk. Mwele alielekeza nguvu zake kumuunga mkono mgombea aliyepitishwa, Dk. Magufuli na kila jioni alitumia muda wake baada ya kazi kufanya ‘majukumu ya kisomi’ katika kampeni za chama chake. Na licha ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, baadhi ya vijana aliowakabidhi majukumu ya kampeni za Dk. Magufuli hawajalipwa stahili zao hadi leo (licha ya Dk. Mwele kufuatilia suala hilo kwa zaidi ya mwaka sasa). Linganisha hilo na makada ‘waliozawadiwa’ nafasi mbalimbali licha ya kampeni zao ndani au nje ya chama dhidi ya Dk. Magufuli alipokuwa mgombea.
Mwaka jana nilipata fursa ya kuandika wasifu wake kwenye blogu yangu. Pamoja na mengineyo mengi, alieleza kuwa tangu alipokuwa binti mdogo alikuwa na ndoto ya kuwa mtafiti wa maradhi. Na licha ya kuwa mtoto wa waziri mkuu, ambapo alikuwa na fursa ya ‘kufanya chochote atakacho,’ alifuata ndoto yake ya kitaaluma na kitaalamu, akatumia muda mwingi ‘vichakani na misituni’ kujifunza kuhusu maradhi mbalimbali ya binadamu. Kwa hakika, safari yake tangu utotoni hadi kupata shahada ya uzamivu na hatimaye kuwa mkurugenzi mkuu wa kwanza wa kike wa NIMR, inatoa hamasa kubwa.
Kuna wanaoona kuvuliwa madaraka kwa Dk. Mwele ni kama mwendelezo wa kile kilichomkumba aliyekuwa Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru, ambaye kutenguliwa kwa wadhifa wake hivi karibuni kunatafsiriwa kama matokeo ya yeye kutoa maoni yake ya kitaalamu kuhusu suala fedha za taasisi za serikali kuwekwa kwenye akaunti za muda maalumu (fixed deposits).
Nihitimishe makala hii kwa kumpa pole Dk. Mwele huku nikiamini kuwa muda si mrefu ataipatia fahari Tanzania kama mwanasayansi wa kimataifa. Kadhalika, inasikitisha kuona tukio hili ilhali majuzi tumeshuhudia teuzi za baadhi ya mabalozi zikifanywa kwa kigezo cha ukada

15 Dec 2016


KATIKA toleo la Oktoba 20, 2016 la gazeti hili niliandika makala iliyokemea madai ya uongo yaliyokuwa yakisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu elimu ya Rais Dk. John Magufuli. Kwa mujibu wa madai hayo, shahada ya uzamifu ya kiongozi huyo ilikuwa feki, na kama sio feki basi athibitishe hadharani.
Binafsi nilikerwa sana na madai hayo. Nilijaribu kuyakemea huko kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, kwa kuwashauri wenye kuhitaji uthibitisho wa elimu ya Dk. Magufuli waende Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, taasisi ambayo ndiyo ilimtunuku shahada hiyo kiongozi huyo.
Hata hivyo, ushauri huo haukupokelewa vema na kada wa Chadema, Ben Saanane, aliyekuwa mstari wa mbele kumtaka Dk. Magufuli ahakiki PhD yake. Badala ya kuzingatia ushauri kuwa kuna njia rahisi ya kusaka ukweli kuhusu suala hilo, kijana huyo alitumia lugha isiyopendeza dhidi yangu.
Baada ya kuona suala hilo linazidi kupamba moto hasa huko Facebook, nikaamua kuandika makala katika gazeti hili toleo la Oktoba 20 mwaka huu. Katika makala hiyo, niliepuka kutaja jina la mhusika mkuu katika madai hayo ya uongo dhidi ya elimu ya rais wetu.
Katika toleo la wiki iliyofuata (Oktoba 27, 2016), kada maarufu wa Chadema Ben Saanane alijitokeza kujibu makala hiyo, huku akidai kuwa ni haki kuhoji elimu ya Dk. Magufuli. Licha ya kutumia mifano mingi ya watu mbalimbali maarufu ‘waliofeki’ taaluma zao, Saanane hakuweza kuthibitisha madai yake kuwa PhD ya Magufuli ni feki pia.
Japo mara zote nimekuwa nikikwepa kujibishana na wasomaji wa makala zangu, ilinilazimu kujibu makala ya Saanane kwa vile ilinitaja moja kwa moja. Nilifanya hivyo katika toleo la gazeti hili la Novemba 3, 2016. Katika makala hiyo nilieleza bayana kuwa tatizo la madai ya kada huyo wa Chadema na wenzake sio kuhoji kuhusu elimu ya Rais bali kumtuhumu Rais kuwa PhD yake ni feki. Basi angalau yeye na wenzake wangejihangaisha kuonyesha ‘ukweli’ wa tuhuma zao badala ya kumtaka Rais athibitishe kuwa ‘tuhuma hizo dhidi yake ni za uongo.’
Wiki iliyopita, zilipatikana taarifa kuwa kada huyo ‘hajulikani alipo kwa zaidi ya wiki tatu sasa.’ Hadi wakati ninaandika makala hii, jitihada zilikuwa zinaendelea kumtafuta kada huyo. Hata hivyo, pengine kwa vile Saanane ‘alishikia bango’ tuhuma kuwa PhD ya Dk. Magufuli ni feki, tayari ‘kupotea’ kwake kunahusishwa na tuhuma zake hizo.
Wakati ninaungana na familia ya Saanane na makada wenzake wa Chadema kumwombea awe salama, kuna vitu viwili muhimu vya kuzingatia. Kwanza, wakati Saanane ‘alipojipa uhuru wa kudhalilisha elimu ya Rais,’ makada wenzake hawakuona haja ya japo kumsihi apunguze ukali wa lugha yake dhidi ya kiongozi mkuu wa nchi. Badala yake walimmwagia sifa, huku wakimshambulia kila aliyejaribu kumsihi kada huyo asitumie lugha isiyofaa.
Hili ni tatizo sugu katika mitandao ya kijamii. Kuna wenzetu wakiwa mtandaoni wanajiona kama majabali fulani, wenye uhuru wa kudhalilisha watu, kutukana watu, kunyanyasa watu na tabia mbaya kama hizo. Watu hawa hutumia kisingizio cha ‘uhuru wa kujieleza’ huku wakipuuza haki ya kila mtu kuheshimiwa. Uhuru wa kufanya jambo bila kujali kuwa linakiuka haki za wengine ni uhuni.
Pili, kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu ‘kupotea’ kwa kada huyo. Inaelezwa kuwa ‘alipotea’ katikati ya mwezi uliopita, lakini taarifa kuhusu ‘kupotea’ kwake zimeibuka zaidi ya wiki tatu baadaye. Licha ya wadhifa wa Mkuu wa Sera na Utafiti wa Chadema, Saanane alikuwa pia ‘msaidizi binafsi’ (Personal Assistant) wa mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe. Hadi wakati ninaandika makala hii, si Mbowe au kiongozi yeyote wa ngazi za juu wa chama hicho aliyetoa tamko kuongelea suala hilo.
Kuna wanaohoji, hivi inawezekana kweli msaidizi binafsi wa mwenyekiti wa taifa wa chama kikuu cha upinzani ‘apotee kwa zaidi ya wiki tatu’ lakini kiongozi husika asionekane kuguswa na tukio hilo? Kwa nini ‘wanaomtafuta’ Saanane wasiubane uongozi wa juu wa Chadema, ambao ‘ukimya’ wake katika suala hilo ni kama unaashiria kufahamu alipo kada huyo?
Nihitimishe makala hii, kwanza, kwa kuutaka uongozi wa Chadema kitaifa kujitokeza kuongelea suala hili (kama lina uzito stahili kwao), sambamba na Jeshi la Polisi kusaidiana na wahusika kumsaka kada huyo

9 Dec 2016

Leo ni siku ya Uhuru wa nchi yetu, tunatimiza miaka 55 kama taifa huru. Siku kama ya leo, miaka 55 iliyopita, Tanganyika ilikabidhiwa uhuru wake kutoka kwa Mwingereza. Japo kuna wanaohoji iwapo tupo huru kweli, kwa leo tusherehekee tukio hilo la mkoloni kutukabidhi nchi yetu.

Pia siku ya leo ni siku yangu ya kuzaliwa. Ninamshukuru Mungu kwa kila kitu. 


Ninawashukuru pia wazazi wangu ambao japo ni marehemu kwa sasa, kiroho nipo nao siku zote: marehemu baba Mzee Philemon Chahali na marehemu mama Adelina Mapango. Bwana Mungu awajalie pumziko la milele na mwanga wa milele awaangazie mpumzike kwa amni. Amen. Naishukuru familia yangu hasa dadangu Sr Maria-Solana Chahali na wadogo zangu mapacha Peter (Kulwa) na Paul (Doto). Naomba Bwana Mungu atujalie maisha marefu zaidi, afya njema na mafanikio katika shughuli zetu za kila siku.

Katika maadhimisho haya ya siku yangu ya kuzaliwa, ninatoa zawadi ya kopi za bure za kitabu changu hicho pichani chini.



BONYEZA HAPA kuki-download BURE

8 Dec 2016


KESHOKUTWA, Desemba 9, Tanzania itatimiza miaka 55 tangu ipate uhuru. Siku hiyo hiyo, nami nitatimiza miaka kadhaa tangu nizaliwe. Naam, mimi na nchi yangu ‘tulizaliwa tarehe inayofanana’ japo katika miaka tofauti.
Nijiongelee mwenyewe kwanza. Wakati kwa watu wengi, siku zao za kuzaliwa huandamana na sherehe na chereko mbalimbali, maadhimisho ya siku yangu ya kuzaliwa huwa ni ibada – kumshukuru Mungu kwa kuniweka hai na baraka nyingine anazonijalia – na kufanya tafakuri ya wapi nimetoka, nilipo na ninapoelekea.
Moja ya mafanikio makubwa kwangu kwa mwaka huu ni uamuzi niliouchukua Aprili Mosi kuachana na moja ya tabia hatari kabisa maishani ya uvutaji wa sigara. Hadi nilipochukua uamuzi huo, tabia hiyo hatari kiafya na kiuchumi ilikuwa na ‘umri’ wa miaka ishirini na ushee.
Katika kusherehekea siku yangu ya kuzaliwa, nimeamua kugawa bure kitabu changu cha kielektroniki, kinachoitwa “Mwongozo wa Kitabibu wa Jinsi ya Kuacha Sigara na Ushauri wa Mvutaji Mstaafu.” Ni mwendelezo wa utamaduni mpya, ambapo zamani tulizoea kuona wanaosherehekea siku za kuzaliwa wakizawadiwa, lakini sasa namna maarufu ya kuadhimisha sherehe hiyo ni kutoa zawadi.

Hiyo ni kwa upande wangu. Sijui ‘mwenzangu’ Tanzania atakuwa na ‘zawadi’ gani ya kutupatia katika maadhimisho yake ya siku ya kuzaliwa. Hata hivyo, siku chache kabla ya siku hizo, kuna jambo moja ambalo linaonekana kugusa hisia za wengi. Nalo ni uteuzi wa mabalozi wapya ulifanywa na Rais Dk. John Magufuli wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa baadhi ya vyombo vya habari, uteuzi wa makada waandamizi wa chama tawala CCM umetafsiriwa kuwa ni ‘hesabu za kisiasa.’ Sina hakika hesabu hizo zina malengo gani, lakini nahisi labda ni Magufuli analenga kujiimarisha katika uongozi wake kama Mwenyekiti wa Taifa wa CCM.
Kama hilo ni kweli, basi uteuzi huo wa makada sio habari njema kwetu sisi wenye matarajio ya kuona teuzi mbalimbali zikifanywa kulingana na uwezo wa kutekeleza majukumu au uchapakazi na sio ukada.
Pengine nitumie fursa hii kukumbusha kuwa kuna wimbi kubwa la mabadiliko linaloendelea duniani, hususan huku nchi za Magharibi. Muda mfupi kabla sijaanza kuandika makala hii, Austria imenusurika kuwa taifa la kwanza kurejea kuwa chini ya utawala wa mrengo mkali kabisa wa kulia. Hofu kuwa mgombea urais Norbert Hofer wa chama chenye mrengo mkali wa kulia cha Freedom Party angeshinda ilipotea baada ya mchakato wa kupiga kura kumalizika, na mgombea binafsi Alexander Van der Bellen kushinda kwa asilimia 53. Lakini muda mfupi baada ya habari hiyo njema kutoka Austria, mambo hayakwenda vizuri nchini Italia, ambapo Waziri Mkuu Matteo Renzi alishindwa kwenye kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba ya nchi hiyo, na kulazimika kujiuzulu. Wapinzani wake katika kura hiyo walikuwa ni pamoja na chama chenye mrengo mkali wa kulia cha Northern League na kile cha upinzani wa tabaka tawala (anti-establishment) cha Five Star Movement (F5S).
Sasa macho yanaelekezwa huko Ufaransa na baadaye Ujerumani na Uholanzi ambako kwa nyakati tofauti watakabiliwa na kazi ya upigaji kura. Mtihani mkubwa katika nchi hizo ni jinsi ya kukabiliana na wimbi linalozidi kukua la upinzani dhidi ya tabaka tawala na mfumo wa utawala unaoonekana kutosikiliza sauti za wananchi wa kawaida. Kwa bahati mbaya, wimbi hilo lipo mikononi mwa vyama vya siasa za mrengo mkali wa kulia na vya kibaguzi.
Katika mazingira kama hayo tunahitaji mabalozi wanaoelewa kwa nini wametumwa kutuwakilisha huko nje, na sio wanaojua wameteuliwa kutokana na nafasi zao za kisiasa nchini.
Na wiki chache kabla ya maadhimisho ya miaka 55 ya uhuru wetu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi Dk Mohammed Ali Shein alisaini sheria inayofanya masuala ya mafuta na gesi ya Zanzibar kuwa sio suala la Muungano, hatua ambayo ni uvunjifu wa Katiba mchana kweupe. Hilo limefanyika kwa vile Shein na SMZ wanajua hakuna mwanasiasa kutoka Bara mwenye jeuri ya kugusia suala hilo, ikiwa ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Magufuli.
Lakini pamoja na hayo, Tanzania yetu itasherehekea miaka 55 ya kuzaliwa kwake ikiwa nchi yenye amani, angalau amani kwa maana ya kutokuwa vitani au kwenye machafuko. Kazi kubwa kwa watawala wetu ni kutumia nguvu zao zote kuhakikisha kuwa amani hiyo inadumishwa kwa nguvu zote.
Happy birthday Tanzania.

7 Dec 2016

ANGALIZO: Makala hii ilipaswa kuchapishwa katika toleo la wiki iliyopita la gazeti la Raia Mwema lakini haikuchapishwa kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Rais Dokta John Magufuli alitimiza mwaka kamili tangu aapishwe kuwa Rais wa tano wa nchi yetu. Nyingi ya tathmini mbalimbali zilizofanyika kuhusu mwaka wake mmoja wa urais zilionyesha anafanya kazi nzuri.

Hata hivyo, tukifuatilia kwa karibu utendaji kazi wa Rais, twaweza kubaini kuwa baadhi ya mawaziri wake hawaendani na kasi yake. Katika mazingira ya kawaida, Rais angelazimika kuchukua hatua pale tu hatua stahili zisingewezekana kufanywa na mawaziri wake.

Japo wanachohitaji wananchi ni kuona serikali inachukua hatua stahili, lakini suala la mtendaji gani wa serikali anayechukua hatua husika linaweza kueleza kiwango cha ushirikiano na uchapakazi kwa pamoja.

Na kwa ‘kusubiri hadi Rais achukue hatua’ kuna uwezekano wa kujengeka taswira kuwa ‘Rais anaingilia kazi za watendaji wake,’ au mbaya zaidi ni pale maagizo yake yatapokutana na upinzani wa namna flani.

Mfano mzuri ni hatua ya majuzi ambapo Rais aliitumbua Bodi ya Mamlaka ya Mapato (TRA).  Baadaye alieleza kuwa Bodi hiyo iliyokuwa na watendaji hao wakuu wa idara na taasisi za Serikali ilifanya dhambi ya kuidhinisha uamuzi wa menejimenti kuweka mabilioni ya shilingi katika benki za binafsi.

Juzi hapa tumekuta Sh26 bilioni zilizokuwa zimetolewa TRA kwa ajili ya matumizi ya TRA zikapelekwa kwenye mabenki matatu kama ‘fixed deposit account’ na bodi ikapitisha. Ndiyo maana nilipozipata hizo hela; hela nikazichukua na bodi kwaheri,” Rais alikaririwa

Swali hadi hapo ni je Waziri husika na wasaidizi wake walikuwa wapi wakati hayo yanatokea? Je inawezekana maamuzi hayo ya menejimenti na Bodi ya TRA yalikuwa na baraka za Waziri husika, na ndio maana hakuna hatua zilizochukuliwa hadi Rais alipoingilia kati?

Miongoni mwa wajumbe wa Bodi iliyotumbuliwa ni Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu, ambaye wiki iliyopita alinukuliwa akitoa kauli inayokinzana na msimamo wa Rais. Gavana Ndulu alidai kuwa TRA kuweka fedha kwenye fixed accounts sio kosa kisheria, na hakuna hasara kiuchumi kuweka fedha kwenye akaunti ya aina hiyo.

Kwa tunaojua ‘kusoma katikati ya mistari’ Tunaelewa bayana kuwa Gavana Ndulu alikuwa anamjibu Rais Magufuli. Na pengine sio kumjibu tu bali kumkosoa. Na hii si mara ya kwanza kwa ‘kiongozi huyo wa benki kuu kupishana lugha na Rais.’ Mwezi Machi mwaka huu Dkt Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza huko Benki Kuu, ambapo pamoja na mambo mengine, alitoa agizo kwa Gavana Ndulu kupitia upya orodha ya wafanyakazi wa Benki hiyo, na kuwaondoa mara moja wale wote ambao hawana ulazima wa kuwa wafanyakazi katika benki hiyo.

Siku chache baadaye, Gavana huyo alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa orodha yenye majina 14 ya ‘watoto wa vigogo’ iliyokuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ‘haina jipya.’ Hata hivyo alieleza kuwa agizo la Rais kuhusu kupunguza wafanyakazi lingejadiliwa kwenye vikao vya taasisi hiyo na taarifa rasmi ingetolewa. Kwa kumbukumbu zangu, hadi leo hakujatolewa taarifa yoyote.

Wakati akieleza kuhusu sababu zilizopelekea kuvunja Bodi ya TRA, Rais pia aliionya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwamba imepewa zaidi ya shilingi bilioni 30 na “badala ya kuzipeleka kwenye miradi ya elimu kama kujengea madarasa na kusaidia masuala mengine ya elimu nchini lakini wameamua kuweka kwenye fixed account wakati kuna miradi ya elimu imesimama kwa kukosa pesa.

Na hapa tena tunapaswa kujiuliza, Waziri husika (na wasaidizi wake) yupo wapi? Au hapa pia, uamuzi huo wa Mamlaka hiyo una baraka za Waziri husika ndio maana haikuchukua hatua hadi Rais alipoingilia kati?

Tukiweka kando hilo la ‘kila jambo kusubiri hadi Rais achukue hatua,’ maamuzi ya baadhi ya mawaziri yanaweza ‘kumgombanisha’ kiongozi huyo mkuu wa nchi na sie wananchi anaotuongoza. 

Wiki mbili  zilizopita, Waziri wa Sheria na Katiba, Dokta Harrison Mwakyembe, ‘alilipuka’ kwa kutangaza kuwa serikali ina mpango wa kuwatimua kazi mahakimu wote wa mahakama ya mwanzo wenye elimu ya cheti na diploma. Waziri huyo ambaye ni mwanasheria kitaaluma, alisema, “Tunahitaji mahakimu wenye uwezo wa sheria ambao wamehitimu shahada ya kwanza, hivyo serikali itawafuta kazi mahakimu wote wenye elimu ya cheti na diploma.”

Tungetegemea kuwa kiongozi msomi kama Dkt Mwakyembe angetambua bayana athari za tamko hilo kwa ari na tija wa mahakimu wa mahakama za mwanzo, wengi wao wakiwa wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi. Tamko hilo la Mwakyembe linaweza kupelekea mahakimu kuamua “serikali inataka kumwaga ugali, basi nasi tutamwaga mboga.”

Lakini hata tukiweka kando athari za tamko hilo kwa ari na tija ya mahakimu wa mahakama za mwanzo, kwanini Mwakyembe na wenzake hawakuzingatia busara kwamba elimu pekee sio kigezo cha ufanisi wa mwajiriwa bali pia uzoefu ni muhimu kwenye utaalamu.

Kwahiyo, serikali yenye busara ingeandaa mazingira ya kuwahamasisha mahakimu hao kujiongezea viwango vya elimu wakiwa kazini, hususan kwa kusaka shahada ya sheria kupitia Chuo Kikuu Huria.

Tukio jingine linaloashiria kuwa baadhi ya watendaji wa Dkt Magufuli 'wanamwangusha' ni sakata kati ya serikali ya jiji la Mwanza na wamachinga. Kwa mara nyingine tena, tumeshuhudia ikilazimu Rais kuingilia kati na kumuru kuwa wamachinga waliokuwa wakibughudhiwa huko Mwanza wasisumbuliwe tena.

Hapa pia waweza kujiuliza kuhusu Waziri husika. Alikuwa usingizini kiasi cha kutofahamu kilichokuwa kinaendelea Mwanza hadi imlazimu Rais kuingilia kati? Au Waziri huyo aliridhia kuhusu unyanyaswaji wa wamachinga na ndio maana hakuchukua hatua stahili?

Kuna suala la kiwanda cha Dangote. Kauli za mawaziri husika na watendaji wengine wa serikali zimekuwa sawa na 'kujiumauma.' Sio ngumu kuhisi kuwa 'kuna namna' katika sakata hilo ambalo miongoni mwa atahri zake ni pamoja na kupotea kwa ajira za Watazania wenzetu zaidi ya 1,000.

Kwa jinsi mazingira yalivyo ambapo 'kila kitu lazima kimsubiri Rais,' yayumkinika kuhisi kuwa ufumbuzi pekee wa sakata hilo a Dangote utapatikana kwa Rais kuingilia kati. 

Wakati watendaji 'wanaomwangusha' hawawezi kuwa na kisingizio zaidi ya aidha uzembe wao au hujuma dhidi ya Rais, kwa uapnde mwingine Rais naye anaweza kubeba lawama kwa kuyavumilia majipu yanayomzunguka.


Nihitimishe makala hii kwa kutarajiwa kuwa Rais Magufuli atawakumbusha watendaji wake majukumu yao ili kuondoa taswira ya ‘kila kitu mpaka aje Rais,’ sambamba na kuwakumbusha kutumia busara hasa pale wanapotoa kauli zinazoweza kujenga chuki kati ya ‘waathirika’ wa kauli hizo na serikali


Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  




Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.