13 Dec 2007

Makala ya wiki hii ndani ya gazeti la Mtanzania inaangalia namna mafisadi wa kigeni wanavyonufaika kutokana na uzembe wa baadhi ya Watanzania wenzetu tuliowakabidhi dhamana za uongozi.Lakini hata kama wawekezaji hao wangekuwa waadilifu hivi kweli ndoto ya "maisha bora kwa kila Mtanzania" itatimia wakati Waziri mwenye dhamana ya maendeleo ya sekta ya Maji (Waziri wa Maji) nae ni miongoni mwa wadaiwa sugu wa maji waliokatiwa huduma hiyo na DAWASCO?Makala nzima hii hapa chini

Waziri wa Maji anasubiri nini ofisini?

na evarist chahali, uskoch


Hadi muda huu haijaniingia akilini niliposoma habari kwamba aliyekuwa mwekezaji kwenye hoteli ya Millenium Tower “ameingia mitini” na kuacha deni kubwa la kodi ya jengo na bili nyingine.Kwa mujibu wa uongozi wa LAPF ambao ndio wamiliki wa jengo hilo,mwekezaji huyu alianza kuonyesha dalili za ubabaishaji muda mrefu kidogo kabla hajaamua kutoroka,lakini nachoshindwa kuelewa ni kwanini uongozi huo haukuchua hatua za tahadhari kuhakikisha kwamba wanalipwa kilicho chao kabla huyu jamaa hajaondoka kimyakimya.

Pengine ni vema nikitoa mfano halisi wa taratibu za upangaji zilivyo hapa Uingereza.Ukitembelea miji mikubwa kama London,Manchester,Birmingham na mingineyo,au hata kwenye mji mdogo kama Aberdeen (hapa ninapoishi) utakuta kuna jamaa wanaopata hifadhi ya makazi kwenye viambaza vya maduka na majengo mengine huko mjini kati.Hawa ni watu wasio na makazi,na japo wengine wameishia katika hali hiyo kutokana na uzembe wao,wapo wale ambao si rahisi kwao kupata makazi kutokana na ugumu katika utaratibu mzima wa kuingia mikataba ya makazi.Wamiliki wa majengo ya kupangisha wako makini mno kuhakikisha kwamba hawapangishi wababaishaji.

Na kwa wageni inakuwa suala zito zaidi kwani nyaraka kadhaa zinahitajika kabla mwenye jengo hajakukabidhi funguo la pango la kuishi.Mara nyingi taratibu za kupanga jengo huhusisha wanasheria ili pindi upande mmoja utakapokwenda kinyume na mkataba wa pango basi iwe rahisi kuhakikisha haki inapatikana.Hapa nawazungumzia wamiliki binafsi na sio makampuni yenye majengo ya kupangisha.

Pengine wamiliki wa nyumba za kupanga wanakuwa makini kwa vile wana uchungu na mali zao,lakini pengine ni kutokana na utaratibu mzuri wenye kumnufaisha mwenye nyumba na mpangaji.Lakini hata huko nyumbani kuna taratibu kama hizo japo zinatofautiana kwa kiwango flani.Inawezekana mwenye nyumba unayotaka kuhamia asijali sana kudadisi ulikotokea,lakini mara nyingi utaratibu unaofahamika ni kutanguliza malipo ya awali ambayo huweza kuwa sawa na kodi ya nusu mwaka au mwaka mzima.Na wengine hufikia hatua ya kuomba “kilemba” kana kwamba anayetaka kupanga anachumbia kwa mwenye nyumba,yote hiyo ni kwa mwenye mali yake kuhakikisha kuwa hatoishia kujilaumu baada ya kumruhusu mpangaji kuingia kwenye jengo lake.

Naamini kabisa kwamba laiti jengo la hoteli ya Millenium Tower lingekuwa mali ya mtu binafsi basi huyo mwekezaji tapeli asingeweza kutoroka kirahisi namna hiyo.Na kwanini watueleze sasa kuwa mpangaji wao kaingia mitini ilhali walishakuwa na matatizo naye kwa muda mrefu?Jibu jepesi kwangu ni kwamba hawana uchungu na fedha za waliowezesha jengo hilo kufikia hapo lilipo.Na hili ni tatizo kubwa sana katika hii inayoitwa mifuko ya jamii.Maamuzi ya mali zinazomilikiwa na mifuko hiyo yamebaki mikononi mwa watu wachache ambao pindi hasara ikitokea wanaishia kutoa sababu moja au nyingine na wala sio kuelezea namna gani hasara hiyo itakavyofidiwa

Natambua kwamba ni vigumu kuiwezesha demokrasia ichukue mkondo wake katika mfuko wa jamii wenye wanachama elfu kadhaa kama sio laki na kitu.Demokrasia nayozungumzia hapa ni ile ya maamuzi yanayofikiwa kwa makubalino ya wanachama wote.Hata hivyo,hiyo haitoi nafasi kwa wachache waliokabidhiwa dhamana ya kufanya maamuzi kwa niaba ya wanaowawakilisha wakafanya mambo kiholela kwa vile tu fedha zinazoteketea hazitoki mifukoni mwao.

Tumeshuhudia sehemu kadhaa zikibadilishwa majina kila mwaka baada ya wawekezaji wa awali kuondoka na kurusha mpira kwa wawekezaji wapya.Kubadili jina la biashara sio kosa kisheria kwani hata jina la mtu binafsi linawezwa kubadilishwa mahakamani.Tatizo hapa ni kwamba wawekezaji matapeli hutumia misamaha ya kodi na masharti mepesi wanayopatiwa wakati wanaingia mikataba na wakishachuma faida ya kutosha wanaondoka kistaarabu (kwa kutangaza kwamba wamekuwa wanapata hasara) au kibaradhuli (kwa kuingia mitini kama huyo mwekezaji wa zamani wa hoteli ya Millenium Tower).

Mwaka juzi nilialikwa kumtembelea rafiki yangu mmoja aliyeko Marekani.Nilipofika ubalozi wa nchi hiyo jijini London kuomba viza,nilijionea mwenyewe namna gani wenzetu wanavyojithamini wao kwanza kabla ya wageni.Utaratibu wa kuingia hapo hauna tofauti na ule wa zamani katika ubalozi wa Uingereza hapo Dar ambapo waomba viza walikuwa wanalazimika kukesha usiku kucha kuwahi foleni ya kuonana na maofisa wa ubalozi huo.Japo sina hakika lakini nadhani utaratibu wa sasa wa kufanya maombi mtandaoni unaweza kuwa umepunguza tatizo hilo.Katika ubalozi huo wa Marekani hapo London,raia wa Marekani hawapatwi na usumbufu wa kukaa kwenye foleni ndefu au kupigwa na mvua au kibaridi (kulingana na majira ya mwaka) bali hupewa upendeleo maalumu.

Na hata kwenye maeneo ya kuangalia nyaraka za uraia na makazi kwenye viwanja vya ndege,wenzetu hujitahidi kuhakikisha kuwa raia wao hawapati usumbufu mkubwa kama ule tunaoupata wageni na wapita njia kama akina sie.Angalau pale uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere kuna kutenganishwa kati ya Watanzania,raia wa Afrika Mashariki na wengineo,lakini wengi mtakubaliana nami kuwa tuna kasumba ya kuwanyenyekea wageni kulko tunavyowanyenyekea Watanzania wenzetu.Wawekezaji feki wamekuwa wakiitumia vizuri fursa hiyo sambamba na ubabaishaji wa taratibu za mikataba kuhakikisha kwamba wanachuma vya kutosha na pale wanapovimbiwa wanaamua kuondoka bila matatizo.

Wageni hapa Uingereza wana uwezo wa kuomba viza ya makazi kwa kigezo cha biashara ndogondogo kwa wale wenye uwezo mdogo au biashara kubwa kwa wale wenye uwezo wa kutosha.Nizungumzie hilo kundi la kwanza ambalo kimsingi linatoa mwanya kwa wageni wengi zaidi kutokana na ukweli kwamba mtaji unaohitajika sio mkubwa sana.Kinachowakwamishwa wengi ni umakini katika utaratibu mzima ambao hautoi fursa hata chembe kwa wababaishaji.Mwingereza hawezi kukubali uje uwekeze nchini mwake kwenye sekta ya usafiri wa reli ilhali unategemea mabehewa na injini chakavu kutoka huko ulikotoka.

Tatizo la kunyenyekea haliishii kwenye uwekezaji pekee bali hata kwa taasisi nyingine zinazopaswa kujiendesha kibiashara badala ya kutegemea ruzuku ya serikali.Niliposikia Dawasco ikitangaza kwamba itakata huduma ya maji “kwa vigogo” nilibaki najiuliza kama mamlaka hiyo ingeweza kutoa tishio la namna hiyo iwapo wadeni wake wangekuwa ni wale wa “uswahilini” (kama maji yangekuwa yanapatikana huko).Kama ilivyo kwa Tanesco (na pengine hata TTCL),malalamiko makubwa ya makampuni hayo ni kwamba huwa wanaingiliwa na vigogo kila wanapowabana wadaiwa sugu.Nisichoelewa ni hofu ya vigogo wa makampuni hayo kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vigogo wanaowatisha hasa ikizingatiwa kuwa Mkurgenzi wa Dawasco au Tanesco anateuliwa na Rais,kwahiyo wakitishiwa na vigogo wengine wanaweza kabisa kukimbilia kwa Rais kumjulisha wanavyosumbuliwa na vigogo wadaiwa sugu.Japo najua itakuwa ni usumbufu usio na lazima kwa Mkuu wa nchi,lakini naamini kwamba iwapo makampuni yanayokwamishwa na vigogo ambao ni wadeni sugu yakiwajulisha vigogo hao kwamba yanawakatia huduma na “wakileta zao za kuleta” watawaripoti kwa Rais ni lazima watalipa madeni hayo.

Lakini pengine taarifa za hivi karibuni kuwa miongoni mwa wadaiwa wa DAWASCO ni pamoja na Waziri wa Maji zinaweza kutufanya tuionee huruma Mamlaka hiyo.Katika utetezi wake,Waziri huyo anadai kuwa hajawahi kupata huduma ya maji kwa miaka kadhaa,na amekuwa akinunua maji kutoka kwa wafanyabiashara.Swali linakuja,je iwapo yeye kama waziri wa maji anatumiwa bili ilhali hapatiwi huduma ya maji alifanya jitihada gani kuhakikisha sio yeye tu bali Watanzania wengine hawakumbani na adha hiyo?Mbona alikuwa kimya siku zote hizi?Hivi karibuni,Mkuu wa polisi wa usalama barabarani huko Wales alilazimika kujiuzulu baada ya kunaswa na kamera zinazodhibiti mwendo kasi barabarani akiwa anaendesha gari yake zaidi ya kiwango kinachoruhisiwa kisheria.Kwa kuvunja sheria aliyopaswa kuisimamia,kamanda huyo alilazimika kujiuzulu.

Sitarajii waziri wa maji kujiuzulu kutokana na deni hilo,na wala sitarajii hilo kwa mawaziri na vigogo wengine wanaodaiwa kwa vile msamiati “KUJIUZULU” ulishafutika kwenye kamusi ya medani ya uongozi huko nyumbani.Ni udhaifu wa namna hii unaowapa jeuri wawekezaji feki kwani kabla ya kuingia mikataba huwa wanasema udhaifu wa hao waliopewa mamlaka ya kusaini mikataba ya uwekezaji.Kwa mtaji huu,ndoto ya maisha bora kwa kila Mtanzania ina safari ndefu sana kutimia.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.