23 Mar 2009


KADA maarufu wa Chama cha Mapinduzi, Nape Nnauye, amesema malumbano yanayoendelea sasa nchini ni ishara kwamba mafisadi wamejipanga kuifanya nchi isitawalike.

Nape alitoa kauli hiyo jana alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu hali ya kisiasa nchini, hususani malumbano yanayoendelea sasa kati ya Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.

Bila kutaja majina ya watu, Nape alisema chimbuko la malumbano hayo aliyoyaita ya kipuuzi ni kashfa nzima ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, iliyosababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, kujiuzulu.

Huku akiwa makini kuchangua maneno ya kuzungumza, Nape alisema malumbano hayo yanaonyesha kuna baadhi ya watu hawakuridhika na taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Mwakyembe, hivyo kuna ulazima wa hoja hiyo kurudishwa tena bungeni ili kukata mzizi wa fitna.

“Kuna kila dalili kuwa mafisadi wamejipanga kuhakikisha nchi haitawaliki, ndiyo maana mijadala isiyo na kichwa wala miguu inaibuka kila kukicha hata kwa mambo ambayo yamekwishaamuliwa na chombo kikubwa kama Bunge,” alisema.

Katika kuthibitisha kauli yake, Nape alisema ana taarifa za siri kuwa kuna baadhi ya mafisadi wamekuwa wakifanya mikutano ya faragha ambapo pamoja na mambo mengine, wamepanga kuhakikisha nchi haitawaliki kwa kuibua hoja na mijadala kupitia baadhi ya vyombo vyao vya habari.

“Tunakoenda ni kubaya, ila naamini serikali iko imara na CCM kama chama tawala, tutaomba tulizungumze kwenye vikao vyetu kwa nia njema ya kuliokoa taifa linalovurugwa na watu wachache wenye fedha,” alisema Nape.

Nape alisema ili kuhakikisha Tanzania haiyumbishwi, aliwataka wananchi kupuuzia mjadala wa sasa kwa madai kuwa hauna tija na una lengo la kuhatarisha amani na utulivu uliopo nchini.

Kuhusu mjadala wa ununuzi wa mitambo ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans iliyorithi kutoka Kampuni ya Richmond, kada huyo wa CCM alisema anashangazwa na uamuzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuomba kibali cha Bunge au kamati zake.

“Kwani TANESCO wanapoenda kununua transfoma na vifaa vingine, wanaomba kibali cha Bunge? Kama si hivyo, kwa nini wanataka kuhalalisha ununuzi wa mitambo ya Dowans kupitia kamati za Bunge? Hata hivyo, Bunge lilishatoa msimamo wake juu ya hilo, kama kuna mtu hakuridhika, alirudishe bungeni na si kuwagawa Watanzania kwa mijadala isiyoisha na vitisho,” alisema Nape.

Mwanasiasa huyo machachari aliwataka mafisadi kutambua kuwa hata wakiibua mijadala ya kuwagawa Watanzania kama ilivyo sasa, hakutabadili ukweli kwamba Richmond na hata mrithi wake Dowans, ndio waliolifikisha taifa hapa lilipo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Maswa, John Shibuda, alisema malumbano yanayoendelea sasa kati ya Dk. Mwakyembe na Rostam kumetokana na upepo wa kisiasa ambao wakati mwingine huleta tija katika kukuza demokrasia.

Hata hivyo, Shibuda ambaye hupenda kuzungumza kwa mafumbo, alisema mjadala huo umejikita kwenye hila na visa vya kufunika mema na mazuri ya mtu.

“Mimi naona hayo ni mapepo ya kisiasa na mtenguko wa fikra ambao umeleta mng’atuko dhidi ya dhulma, lakini ni mjadala wa heri kwa maana kuwa unawafanya watu kutoa manung’uniko yao, bila hivyo hali ingekuwa mbaya siku moja, kwa hiyo naona mjadala uendelee,” alisema Shibuda.

Mbunge wa zamani wa Morogoro Vijijini, Semindu Pawa (CCM), aliiambia Tanzania Daima jana kuwa, mjadala huo sasa umechacha na kuwataka waandishi wa habari kuachana nao.

“Mimi sitaki kusema nani yuko sahihi, lakini nasema mjadala huo umechacha, umepitwa na wakati, wanahabari mkiacha tu, hautausikia tena, lakini naweza kusema wanahabari ndio mnaoukuza, waacheni,” alisema Semindu Pawa.

Mwishoni mwa wiki, Dk. Mwakyembe alijibu tuhuma zinazomhusisha na kumiliki kampuni binafsi ya kuzalisha umeme kuwa ni kazi mahususi inayofanywa na majeruhi wa vita ya ufisadi, ambao waliumizwa na matokeo ya kazi ya Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza mkataba wa Kampuni ya Richmond, ambayo yeye alikuwa mwenyekiti wake.


Hatua ya Mwakyembe kujibu tuhuma hizo, ilikuja baada ya magazeti mawili ya kila siku, (si Tanzania Daima) kuchapisha habari zinazomhusisha yeye na umiliki wa hisa 1,000,000 zenye thamani ya jumla ya sh bilioni 1.5 katika Kampuni ya Power Pool East Africa Ltd.

Mbali ya habari hizo kuandikwa katika magazeti hayo mawili; moja la binafsi na jingine la serikali, nyaraka kadhaa zinazomhusisha Mwakyembe na kampuni hiyo, zimesambazwa katika mtandao wa intaneti.

Taarifa hizo pia zinamtaja Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya TANESCO, kuwa miongoni mwa wanahisa wa kampuni hiyo binafsi ambayo wakati fulani Mwakyembe alipata kuwa mtendaji mkuu wake.

Taarifa hizo zinajaribu kujenga hoja zinazojaribu kumuondolea Mwakyembe uhalali wa kuendelea kudai kupambana na ufisadi ndani na nje ya Bunge ilhali yeye mwenyewe akionekana kuwa na ukwasi mkubwa unaotiliwa shaka.

Pia zinaonyesha kuwa, Mwakyembe licha ya kuwa na hisa nyingi katika kampuni hiyo, ameisaidia katika mambo mbalimbali ambayo hata hivyo hayakufafanuliwa, wakati akiwa katika wadhifa wa mtendaji mkuu.

Kwa mujibu wa uchunguzi wetu, lengo kuu la kusambaza nyaraka hizo ni kujaribu kumnyoshea kidole Mwakyembe na kujaribu kumuondolea uhalali wa kuendelea kupigania sekta ya nishati ilhali yeye mwenyewe akijua kuwa na maslahi.

Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema kuwa katika Kampuni ya Power Pool East Africa Ltd, hakuwezi kukamsababishia akaingia katika mgogoro wowote wa kimaslahi kutokana na ukweli kwamba, kampuni hiyo iliyosajiliwa kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA), bado ipo katika hatua ya awali ya mradi ambao bado haujaanza kuzalisha.

Alipotakiwa kueleza ni kwa nini wakati alipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyoichunguza Richmond kuanzia Oktoba mwaka juzi na kuwasilisha ripoti yake mwaka jana, hakueleza lolote kuhusu kuwa na kampuni ya kuzalisha umeme, Mwakyembe alisema asingeweza kufanya hivyo wakati mkakati wao wa kikampuni ukiwa katika hatua ya mradi tu.

‘‘Kwa mujibu wa sheria ya makampuni, majina yanakuwapo mpaka hapo kampuni itakapoanza ‘ku-take off’ (kuanza kazi). Sikuweza kuitaja kuwa ni sehemu ya makampuni yangu, kwa kuwa bado ilikuwa katika hatua ya mradi,” alisema Mwakyembe.

Mwanasiasa huyo alikwenda mbele zaidi na kuwaeleza wanahabari hao ambao miongoni mwao walionekana dhahiri kukabiliana naye kwa njia ya malumbano kuwa, hata wakati akiandikisha mali anazomiliki chini ya sheria ya viongozi kutangaza mali wanazomiliki, hakuitaja kampuni hiyo ya Power Pool kwa sababu hizo hizo za kutoanza kwake kazi.

Akifafanua tuhuma hizo dhidi yake, alimgeukia mbunge mwenzake wa CCM, Rostam Aziz na kumtuhumu kuwa nyuma ya habari zote mbaya zinazoandikwa dhidi yake.

Huku akilitaja jina la Rostam mara kadhaa, Mwakyembe alisema ni jambo ambalo haliingii akilini kwa mtu ambaye amechafuka kuamua kutumia maji taka kujisafisha.


WALA TUSINGEFIKA HAPA TULIPO IWAPO SHERIA INGEFUATA MKONDO WAKE.VINARA WALIOTUINGIZA MKENGE KWENYE UTAPELI WA RICHMOND HAWAJACHUKULIWA HATUA BAADA YA KUJIUZULU,NA SASA WAMEPATA JEURI YA KUTAKA KUTULIZA MARA YA PILI KWA KUTUUZIA MITAMBO MITUMBA ILEILE ILE YA RICHMOND a.k.a DOWANS.HUU MTINDO WA KULINDANA UTALIPELEKA TAIFA MAHALA PABAYA.

HOWEVER,LET IT BE KNOW TO MAFISADI AND THOSE WHO SHIELD THEM THAT IF THEY TURN OUR BELOVED COUNTRY INTO ANOTHER MADAGASCAR THEY TOO WOULDNT BE SAFE!

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.