17 Jan 2014

KATIKA hitimisho la makala yangu iliyochapishwa wiki mbili zilizopita, iliyobeba kichwa cha habari ‘Ni mwaka wa siasa za hovyo CCM, CHADEMA, niliahidi kuendeleza utabiri wa mwaka huu 2014, kwa kuangalia anga za kimataifa.
Kwa bahati nzuri, siku nne tu baada ya kuchapishwa makala hiyo, moja ya mambo niliyotabiri - kuendelea kwa mgogoro wa CHADEMA na uwezekano wa migogoro ndani ya vyama vya upinzani kuwa ya hadharani - limetokea.
Ninaomba niweke bayana kuwa masikitiko yangu kuhusu maendeleo mapya katika mgogoro wa CHADEMA ni makubwa zaidi ya furaha yangu kuona nilichotabiri wiki iliyopita kweli kimetokea. Nitakuwa mbinafsi na mnafiki ‘kusherehekea usahihi wa utabiri wangu’ katika jambo lisilopendeza. Laiti ingekuwa ni chaguo langu basi ningetamani mabaya yote niliyotabiri yasitokee, lakini kwa bahati mbaya hali halisi haikwepeki.
Takriban wiki mbili zilizopita, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) Zitto Kabwe alirusha ‘bomu zito’ ambapo alitoa tuhuma kubwa na hatari dhidi ya Mwenyekiti wake taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, na chama hicho kwa ujumla. Pengine ili kuleta ladha halisi ya alichosema Zitto ni vema nikanuu ‘waraka’ mzima kama ifuatavyo:
"Lissu anasema nimepewa magari 2 na Mzee Mkono. Anasema kaambiwa na Mkono. Naamini Mkono alimwambia pia mwaka 2005 alimpa Freeman Aikaeli Mbowe tshs 40m ili Mbowe asifanye kampeni Musoma Vijijini.
“Nadhani alimwambia pia mwaka 2008 (baada ya orodha ya mafisadi kutangazwa 2007) Mkono alimpa Freeman tshs 20m za uchaguzi wa Tarime na Freeman akasema kwenye chama ametoa mkopo na akalipwa. Nadhani alimwambia pia kuwa mwaka 2010 Mkono alimpa Mbowe tshs 200m za kampeni ya Slaa.
“Pia hakusahau kumwambia kuwa Rostam Aziz alimpa Mbowe tshs 100m za kampeni. Lissu anajua kuwa gazeti la Tanzania Daima limeanzishwa na fedha za chama kutoka Conservative Party?
“Nimefanya internship yangu kwa Mkono and Company Advocates kuhusu masuala ya mikataba. Mzee Mkono ni Mzee wangu na alisaini petition ya kumtoa Waziri Mkuu Pinda. Lissu awaambie waliyemtuma wamwambie ukweli wote. Lissu ajue yeye ni kifaranga tu, Mimi namtaka mama wa kifaranga ajitokeze. Aeleze aliingia deal gani na Kinana na Sumaye mwaka 2005 kufuatia deni lake NSSF. Aweke wazi mkataba kati yake na NHC kuhusu nyumba ya umma ilipo Club Bilicanas.
“They must know I am not a push over. Chacha died, I won't. Mtu ambaye hawezi kuheshimu mke wake aliyemzalia watoto hawezi kunyooshea mtu kidole kuhusu maadili."
Zitto alibandika waraka huo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, lakini kwa sababu anazojua yeye pekee, baadaye aliuhariri na kutojumuisha tuhuma hizo. Aidha kwa kutofahamu au makusudi, uhariri uliofanywa na mwanasiasa huyo katika waraka huo haukuzuia kusambaa kwa kasi mtandaoni.
Niliposoma waraka huo nilipatwa na mshtuko mkubwa, nikabaki ninajiuliza iwapo Zitto alikuwa ‘mzima’ wakati anaandika alichoandika.  Japo inawezekana alifanya hivyo kwa kuzingatia kile kinachofahamika mtaani kama ‘umemwaga ugali na mie namwaga mboga...bora tukose wote,” ukweli ni kwamba bandiko hilo lina madhara makubwa, kwa Zitto binafsi na kwa pengine ustawi wa CHADEMA kwa ujumla.
Madhara kwa Zitto ni ya kisheria zaidi. Tayari Mbowe ameonyesha nia ya kumburuza Zitto mahakamani kuthibitisha tuhuma hizo nzito. Bila kujali kuwa tuhuma hizo zina ukweli au la, mtu yeyote mwenye uelewa wa ‘dili za siri’ atafahamu kuwa ni vigumu kuzithibitisha kisheria, yayumkinika kuhisi kuwa Zitto atakuwa na kazi ya ziada katika ‘kesi’ hiyo (iwapo itafunguliwa).
Iwe ni tuhuma za Nimrod Mkono kumpa Mbowe shilingi milioni 260 katika mazingira ambayo si tatanishi tu bali pia kwa namna fulani ni hujuma dhidi ya CHADEMA, au Rostam Aziz kumpatia Mbowe shilingi milioni 100, au ‘dili’ kati ya Mbowe na Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, sidhani kama Zitto anaweza kuthibitisha tuhuma hizo iwapo Mbowe atatimiza azma yake ya kufungua kesi. 
Je, inawezekana kuwa kwa kutambua ‘kosa hilo la kisheria’ ndio maana muda mfupi baadaye Zitto alihariri ‘post’ hiyo? Wakati jibu analo Zitto mwenyewe, ukweli unabaki kuwa tuhuma hizo ni nzito mno, na iwapo ni za kweli basi zinapoteza kabisa hadhi ya CHADEMA.
Ikumbukwe kuwa katika waraka uliopelekea Zitto kuvuliwa nyadhifa zake mbalimbali ndani ya CHADEMA, walioandika waraka huo waligusia walichokiita ‘udhaifu wa wanayemtaka’ (wakimaanisha Zitto), na kudai, “Maneno yake mara nyingine hayazingatii anayazungumza katika mazingira gani na hivyo kuwasha masikio ya wanataasisi jambo linalompunguzia kukubalika kwake taratibu.” 
Kadhalika, walieleza kuwa; “Kuna wakati tunayemtaka (Zitto) hujibu kwa taharuki kubwa dhidi ya mashambulizi yanayoelekezwa kwake jambo linalomfanya achukue maamuzi yasiyo sahihi kwa wakati huo. Kwa kifupi kuna wakati tunayemtaka (Zitto) huonekana kufanya maamuzi kwa hisia zaidi badala ya kutulia kwanza na kutafakari kwa kina ikiwa ni pamoja na kutafuta ushauri kwa wenzake kabla ya kujibu.”
Ndugu msomaji, huhitaji kuwa mwanasaikolojia kuhisi kuwa huenda kilichomsukuma Zitto kuandika ‘waraka’ huo kwenye ukurasa wake wa Facebook ni kile Waingereza wanakiita “putting emotions in front of common sense”, yaani kwa tafsiri isiyo rasmi, kuweka mbele jazba badala ya busara.
Kwa kujaribu kuonyesha kuwa Mbowe si mwadilifu (kwa maana ya kupokea misaada kutoka kwa ‘wanasiasa kama Mkono na Rostam waliowahi kutajwa na CHADEMA kuwa ni mafisadi’), linakuja swali la msingi, kwanini Zitto alikalia kimya tuhuma hizo nzito kwa takriban miaka minane hadi sasa baada ya kuvuliwa madaraka? Hivi kuna neno stahili kuelezea hali hiyo zaidi ya unafiki?
Tukiamini tuhuma hizo za Zitto, je naye si sehemu ya ‘uhuni wa CHADEMA’ wa kukemea mafisadi hadharani ilhali pembeni wanapokea misaada ya watu hao hao wanaowatuhumu? Ninasema hivyo kwa sababu Zitto hakuwa katibu wa shina bali Naibu Katibu Mkuu (taifa)  wa chama hicho, na mbunge, na kwa vyovyote vile naye ni mnufaika wa fedha hizo ‘za mafisadi.’
Laiti angekuwa haridhii vitendo hivyo basi aidha angejitoa mhanga na kuweka ukweli hadharani wakati huo (na hiyo ingeweza kuzuia kurejea kwa vitendo kama hivyo) au angeweza kujiuzulu kwa kuona ‘chama chake kinashirikiana na watuhumiwa wa ufisadi. Kwa nini hakufanya hivyo? Jibu jepesi ni hilo nililoandika hapo juu: alikuwa mnufaika wa vitendo hivyo (iwapo kweli vilitokea, maana tayari baadhi ya aliowataja wamekanusha ‘kumpa msaada’ Mbowe).
Binafsi, ninadhani moja ya matatizo yanayomkabili Zitto ni wanaojiita au kujitambulisha kama wafuasi wake. Wengi kati yao ni wenye mapenzi na CCM, na ushabiki wao kwa Zitto ni wa kirafiki (kimaslahi?) zaidi. Ndio, tofauti za kiitikadi hazimaanishi uadui, lakini wengi wetu tunaufahamu msemo ‘nionyeshe marafiki zako na nitakwambia wewe ni nani,’ yaani mara nyingi watu wanaotuzunguka hutoa picha fulani kuhusu sisi wenyewe.
Lakini tatizo jingine kuhusu ‘wafuasi na marafiki hao wa Zitto’ ni kutokuwa washauri wazuri kwake. Ukisoma mengi ya wanayoandika, hususan huko kwenye mitandao ya twitter, utabaini kuwa kimsingi wanachofanya ni ‘kumvimbisha kichwa Zitto’ bila kutoa ushauri unaoweza kusaidia ustawi wa kisiasa wa mwanasiasa huyo kijana.
Na mfano wa hivi karibuni ni baada ya Zitto kubandika waraka huo wenye tuhuma nzito huko Facebook. Wengi wa wafuasi wake walionekana kuchekelea ‘Mbowe alivyoumbuka’ bila kujali athari za kisheria kwa Zitto na ustawi wa CHADEMA kwa ujumla (kwanini wajali ilhali wengi wao ni wanaCCM)?
Kwa wafuasi wa Zitto, mwanasiasa huyo ni majeruhi wa siasa za chuki na mizengwe ndani ya CHADEMA. Lakini kwa wengine, Zitto anaonekana kama mtu anayeendeshwa na ‘ego’ kubwa inayomfanya kujiona yeye ndiye-au zaidi ya- CHADEMA.
Ni vigumu kubashiri hatma ya maisha ya kisiasa ya Zitto lakini kwa hali ilivyo ni vigumu mno kuona mustakabali wake ndani ya chama hicho. Ninakumbuka mwanasafu mmoja wa gazeti hili alimshauri mwanasiasa huyo hivi karibuni kuwa suluhisho la busara kwake kwa sasa ni kutosubiri kuvuliwa uanachama, ajiondoe mwenyewe huko CHADEMA, na kuitaka Mahakama isiingilie kazi ya chama.
Mwisho, bado ninaamini kuwa Zitto ni mwanasiasa mzuri lakini pengine kwa upungufu wa kibinadamu au makusudi, washauri wabovu au sababu nyinginezo, hazingatii umuhimu wa busara hizi tatu katika medani ya siasa: moja, waweke marafiki zako karibu lakini waweke maadui zako karibu zaidi, na pili, hakuna marafiki au maadui wa kudumu katika siasa, na tatu, hakuna mwanasiasa anayeweza kuwa mbadala wa chama (hasa katika mazingira ya siasa zetu ambapo kwa kiasi kikubwa chombo pekee cha uongozi wa kisiasa ni chama cha siasa. Bila chama, mwanasiasa hata awe maarufu kiasi gani anabaki kuwa raia wa kawaida tu).
Katika waraka wake, Zitto aliandika, “They must know I am not a push over. Chacha died, I won't” (lazima wafahamu mie sio mtu wa ‘kupelekeshwa.’ Chacha (Wangwe?) alikufa, mimi sitokufa). Hiki ni kiburi, utoto au? Ni mwanadamu mwenye uhakika wa kutokufa? Nihitimishe kwa kumshauri kwamba labda kweli ana uhakika wa kuishi milele lakini kwa kutanguliza hisia badala ya busara, yayumkinika kubashiri kuwa anaweza kuwa anajiua mwenyewe kisiasa (committing political suicide).



0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.