1 Dec 2014

Kwanza niombe samahani kwa ku-update blogu hii kitambo. Nilitingwa na majukumu. Pili, makala hii chini ilichapishwa katika gazeti la RAIA MWEMA toleo la Jumatano Novemba 26, 2014, lakini kwa sbabau nisizofahamu tovuti ya gazeti hilo haikuwa up-dated hadi asubuhi hii. Licha ya kuwa na nakala halisi ya makala hii, nilionelea ni vema kusubiri 'edited version' ya makala hii pindi ikichapishwa kwenye tovuti ya RAIA MWEMA. Endelea kuisoma
KWANZA, nianze makala hii kwa kuomba samahani kwa ‘kutoonekana’ kwa takriban mwezi mzima sasa. Hali hiyo ilitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu. Ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wasomaji mbalimbali walionitumia barua-pepe kuulizia kuhusu ‘ukimya’ huo.
Wiki iliyopita, Rais wa Marekani, Barack Obama, aliandika historia kwa kuweka hadharani mpango kabambe kuhusu hatma ya takribani wakazi milioni 12 wanaoishi isivyo halali nchini humo.
Ujasiri wa Obama katika suala hilo unatokana na ukweli kwamba licha ya jitihada za muda mrefu, uhasama wa kisiasa kati ya vyama vikuu vya siasa nchini humo, Democrats na Republicans, ulikuwa kikwazo kikubwa katika kufikia mwafaka na ufumbuzi.
Wakati vyama vyote viwili vinaafikiana kuhusu uwepo wa wakazi hao wasio halali milioni 12, wahafidhina wa Republicans wamekuwa wapinzani wakubwa kuhusu ‘ufumbuzi rahisi’ wa kutoa msamaha (amnesty) kwa wahamiaji hao na kisha kuimarisha udhibiti katika mianya inayotumiwa na ‘wahamiaji haramu.’
Lakini suala hilo limekuwa mzigo mkubwa kwa Obama ambaye hata kabla hajaingia madarakani aliahidi kutafuta ufumbuzi hasa ikizingatiwa kwamba licha ya utajiri wa Marekani, hakuna uwezekano wa kuwatumia wahamiaji hao wote.
Kadhalika, mara kadhaa Obama alikuwa akieleza kwamba kulipuuza tatizo hilo hakutolifanya lipotee lenyewe, bali litazidi kuwa kubwa na gumu kulitatua.
Hatimaye Obama aliwatahadharisha Republicans kuwa atalazimika kutumia ‘Nguvu ya Kirais’ (Executive Order) ambayo haihitaji kuridhiwa na Bunge la nchi hiyo, iwapo wanasiasa wataendeleza malumbano pasipo kuja na ufumbuzi.
Hata hivyo, Republicans walitoa vitisho mbalimbali kwa Obama dhidi ya kutumia ‘executive order,’ huku baadhi wakitishia kumburuza mahakamani ili kumng’oa madarakani kwa madai ya ‘kukiuka katiba.’
Licha ya vitisho hivyo, na upinzani wa wengi wa wananchi wa kawaida (ambao kura za maoni zilionyesha wananchi wengi kutoafiki Rais kutumia ‘executive order’ katika suala hilo), hatimaye Obama aliweka hadharani mpango huo kabambe utakaowapatia ahueni ya kimakazi takriban wahamiaji milioni tano.
Matokeo ya uamuzi huo ni bayana: Republicans wamekasirishwa mno na hatua hiyo, huku chama cha Democrats ambacho kwa kiwango kikubwa kimekuwa mstari wa mbele kuwanusuru wahamiaji hao, kikinufaika kwa sapoti kutoka kundi muhimu katika siasa za chaguzi za Marekani, Walatino.
Kundi hili linatajwa kuwa muhimu mno kwa vyama vyote viwili, kwa Democrats kubaki madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2016, na Republicans kukamata Ikulu baada ya miaka 10 ya Obama. Kidemografia, idadi ya Walatino inaongezeka kwa kasi kuliko kundi lolote lile la ‘asili ya watu’ kwa maana ya Wamarekani Weupe na Wamarekani Weusi, na makundi mengine madogo.
Sasa ni wazi kuwa ili mgombea wa chama chochote kile afanikiwe kuingia Ikulu, ni lazima apate sapoti na kura za kutosha kutoka kwa Walatino.
Uamuzi huo wa Obama umekuwa kama mtego kwa Republicans. Laiti chama hicho kikiendeleza upinzani dhidi ya suala hilo, si tu kitajipunguzia umaarufu wake kwa Walatino na hivyo kuathiri nafasi yao katika uchaguzi mkuu ujao, lakini pia kitawatenga Wamarekani wasio Walatino lakini wanaotaka ‘wahamiaji haramu’ kupatiwa makazi ya kudumu nchi humo.
Lakini kwa upande mwingine, chama hicho kinatambua kuwa kwa kiasi kikubwa ‘Wamarekani hao wapya’ (kwa maana ya ‘wahamiaji haramu’ watakaopewa makazi ya kudumu) wataisapoti Democrats kama kulipa fadhila kwa kushughulikia tatizo lao.
Nitaendelea kuwaletea maendeleo ya suala hili katika makala zijazo hasa kwa vile uamuzi huo wa Obama ni kama umeanzisha ‘vita’ ya kisiasa kati yake binafsi (na chama chake) dhidi ya Republicans ambao mapema mwezi huu walifanikiwa kukamata uongozi wa mabunge yote mawili ya nchi hiyo, yaani Seneti na Congress.
Lengo hasa la kuzungumzia tukio hilo la nchini Marekani ni hali ilivyo huko nyumbani hivi sasa. Hadi wakati ninaandaa makala hii, ‘mshikemshike’ unaotokana na skandali ya ufisadi wa ESCROW sio tu unazidi kukua lakini pia unaleta dalili za uwezekano wa Rais Kikwete kulazimika kufanya mabadiliko kwenye Baraza lake la mawaziri kwa mara nyingine.
Kwa vile takribani kila Mtanzania anafahamu kinachoendelea kuhusu skandali hiyo ya ESCROW, sioni haja ya kuizungumzia kiundani. Hata hivyo, pasi haya, na huku nikitambua kuwa Rais wetu Jakaya Kikwete yupo katika matibabu nchini Marekani, ukweli unabaki kuwa yeye ndiye chanzo cha yote haya.
Nikirejea uamuzi wa Obama kutumia ‘nguvu ya kirais’ kupata ufumbuzi katika tatizo la ‘wahamiaji haramu,’ Kikwete alipaswa kuchukua hatua kama hiyo muda mrefu uliopita. Hapa ninamaanisha Rais kutumia nguvu alizopewa na Katiba kupambana na uhalifu.
Ninaandika hivyo kwa sababu Kikwete ana uelewa wa kutosha kuhusu ‘mgogoro wa IPTL’ ikizingatiwa kuwa huko nyuma alishawahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini. Lakini wakati miaka yake 10 ikielekea ukingoni, hakuna jitihada yoyote ya maana iliyofanywa nae kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
Lakini hata tukiweka kando uzoefu wake katika suala hilo, utawala wake utakumbukwa zaidi kwa kuandamwa na mlolongo wa matukio ya ufisadi ambayo hatma yake imekuwa kuwashawishi mafisadi wengine ‘kujaribu bahati zao’.
Naam, kama Kikwete alidiriki ‘kukumbushia haki za binadamu’ za mafisadi wa EPA, na kuwapa deadline ya kurejesha mabilioni waliyoiba, kwanini mafisadi watarajiwa waogope kufanya uhalifu?
Yayumkinika kuhitimisha kwamba laiti idadi ya safari alizokwishafanya nchi za nje ingelingana na hatua dhidi ya ufisadi/ mafisadi, huenda leo hii tungekuwa tunazungumzia ‘mafanikio ya kihistoria ya uchumi wa Tanzania’.
Badala yake, tumekuwa tukiandamwa na vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu taifa letu lilivyoukumbatia ufisadi kiasi cha kuruhusu ndege ya msafara wa Rais wa China kuondoka na vipusa, sambamba na taarifa mpya kuwa kuna mpango wa serikali kuwatimua wafugaji wa Kimasai katika makazi yao ili kukabidhi eneo hilo kwa familia ya kifalme ya mojawapo ya nchi za Kiarabu.
Sasa badala ya viongozi wetu kushughulikia changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa letu, wamekuwa ‘bize’ kupambana na vyombo vya habari vya kimataifa kukanusha tuhuma hizo. Hivi wazembe hawa hawaoni haya na kujiuliza “kwa kipi hasa cha kuvifanya vyombo vya habari vya kimataifa vituandame bila sababu?”
Kwa upande mwingine, skandali hii ya ESCROW ni uthibitisho mwingine kuwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa (TISS) imepoteza mwelekeo, haitimizi wajibu wake, na ni kama ipo likizo ya muda mrefu.
Hivi inawezekana vipi huyo ‘Singasinga’ anayetajwa kuwa mhusika mkuu katika skandali hiyo aliruhusiwa kuishi Tanzania huko rekodi yake ikionyesha bayana kuwa ni mtu hatari kwa usalama wa taifa letu?
Hii haikuhitaji hata operesheni maalum kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa kwani habari za mtu huyo zipo wazi kwenye mtandao. Hivi Idara hiyo imejaa uzembe kiasi cha kushindwa japo ku-Google taarifa za mtu huyo?
Lakini kama ambavyo lawama nyingi katika skandali hii zinaelekezwa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Katibu na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi, sambamba na Mwanasheria Mkuu, Frederick Werema, huku Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akishutumiwa kwa kushindwa kusimamia vema watendaji walio chini yake, wenye kustahili kubeba lawama kubwa zaidi ni Rais Kikwete na idara yetu ya Usalama wa Taifa.
Ninaandika makala hii kabla ya taarifa za uchunguzi za CAG na TAKUKURU kusomwa hadharani na ‘Kamati ya Zitto’ (PAC), kwahiyo ni vigumu kubashiri hatma ya suala hili. Hata hivyo, uzoefu wa skandali zilizopita, kuanzia Richmond, EPA, Mabilioni  yaliyofichwa Uswisi, Meremeta, Tangold, nk, si ajabu iwapo wahusika wakuu watalindwa na Watanzania kuachwa ‘wanang’aa macho tu.’
Muda mfupi uliopita, zimepatikana taarifa kwamba ripoti hiyo ya PAC imeonekana mitaani huku kurasa zenye majina ya wahusika zikiwa zimenyofolewa. Binafsi ninaamini huo ni ‘uhuni’ tu unaofanywa kuwachanganya Watanzania.
Lakini ukijumlisha na tukio linalodaiwa la kunyweshwa sumu Mbunge Nimrod Mkono, ni muhimu kutodharau nia, sababu na uwezo wa mafisadi kupambana na ukweli kuhusu skandali hii.
Nihitimishe makala hii kwa kumkumbusha Rais Kikwete- kwa mara nyingine - kuwa chini ya mwaka mmoja kutoka sasa atarejea ‘uraiani.’ Ni muhimu kwake kutumia miezi hii michache iliyobaki kurejea ahadi aliyotoa mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wetu mwaka 2005 kuwa hatowaonea aibu mafisadi. Tungependa tumkumbuke kwa mema lakini sio rekodi ya kuliingiza taifa kwenye korongo refu la ufisadi.
Kwa ndugu zangu wa Idara ya Usalama wa Taifa, ninawasihi mtambue mzigo mkubwa mnaowabebesha Watanzania masikini kumudu gharama za operesheni zenu. Kwanini msijiskie aibu  kuwasaliti wanyonge hawa –wengi wakiwa ni ndugu, jamaa na marafiki zenu – kwa kutotimiza majukumu yenu ipasavyo?
TUSIPOZIBA UFA TUTAJENGA UKUTA

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.