Ya Zanzibar si mageni, hata Uskochi yapo
WIKI iliyopita, Waziri wa Kwanza (
First Minister, cheo ambacho ni kama Waziri Mkuu) wa Uskochi, Alex Salmond, alizindua kampeni za chama chake cha
Scottish Nationalist Party (SNP) kuhamasisha kura ya ‘Hapana’ katika
referendum (kura ya maoni ) ya uhuru wa nchi hii inayotarajiwa kufanyika huko mbeleni.
Hoja ya Uskochi kujitenga na Uingereza (kwa maana ya kile kinachoitwa The United Kingdom of Great Britain-England, Uskochi na Wales- and Northern Ireland) imekuwa ikivuma kwa muda mrefu na imepata nguvu zaidi baada ya Salmond na SNP yake kuingia madarakani mwaka 2007.
Kimsingi, sera kuu ya mwanasiasa huyo na chama chake ilikuwa kuhakikisha kuwa hatimaye Uskochi inajitenga kutoka Uingereza.
Walipoingia madarakani tu, SNP walieleza bayana kuwa wana mpango wa kufanyareferendum kusikia maoni ya Waskochi kuhusu wazo hilo la kujitenga.
Hata hivyo, kikwazo ambacho wamekuwa wakikumbana nacho tangu mwanzo ni ukweli kwamba pamoja na tofauti za hapa na pale, ni vigumu kuchora mstari unaoweza kuwatenganisha Waskochi na Waingereza wengine.
Mwingiliano katika takriban kila nyanja ya maisha unawafanya watu hawa kuwa wamoja zaidi kuliko tofauti.
Na wakati naandaa makala hii, Salmond amepata ‘habari mbaya’ kutoka kwa mwendesha kura za maoni (pollster) maarufu hapa Uingereza, Peter Kellner, Rais wa taasisi ya kura za maoni ya YouGov.
Kwa mujibu wa Kellner, kura ya maoni iliyoendeshwa na YouGov Ijumaa iliyopita inaonyesha kuwa wakati ni asilimia 33 tu ya Waskochi wanataka ‘uhuru’ (kujitenga), asilimia 57 wanataka Uskochi iendelee kubaki sehemu ya Uingereza.
Mwendesha kura za maoni huyo amemtahadharisha Salmond kuwa ‘ana mlima mrefu wa kupanda’ kubadili upeo wa wengi wa Waskochi kuhusu nchi yao kujitenga na Uingereza.
Kadhalika, alieleza kuwa kuna ‘vitisho’ kadhaa vinavyoweza kuchangia Waskochi wengi kupinga wazo la kujitenga, na akatoa mfano wa hoja kama wawekezaji kujiondoa Uskochi (kwa kutokuwa na uhakika kama Uskochi itamudu ‘kusimama yenyewe’), kupoteza ruzuku inayotolewa na Serikali Kuu ya Uingereza (ambayo ni kubwa zaidi ya kodi inayolipwa na Uskochi), matumizi ya sarafu ya pauni ya Kiingereza (British Pound) ambapo kama Uskochi itaamua kutumia sarafu hiyo baada ya kujitenga, Uingereza inaweza kuanzisha hatua za ukalifu (austerity measures) zitakazoathiri uchumi wa Uskochi.
Kadhalika, Salmond ametahadharishwa kwamba hofu nyingine zinazoweza kuwatisha Waskochi kuunga mkono wazo la kujitenga ni pamoja na gharama kubwa za kuendesha nchi kamili (hasa katika kipindi hiki ambapo uchumi wa dunia unayumba) kama vile kumudu kuwa na jeshi kamili, ofisi za ubalozi nchi za nje na gharama za uendeshaji wa taasisi za utumishi wa umma (civil service).
Kimsingi, katika zoezi lolote lile la kupiga kura, hali ya kutokuwa na uhakika au hofu ya “huko mbele hali itakuwaje” inatosha kuwafanya wapiga kura wengi kuamua kubaki na chama kilichopo au muundo uliopo (iwapo ni referendum ya jambo fulani).
Mbinu hii inatumiwa sana na vyama tawala (ikiwa ni pamoja na CCM) kwenye chaguzi ambapo ujumbe huwa mithili ya ‘zimwi likujualo halikuli likakwisha’ (kwa maana ya chama unachokifahamu ni bora zaidi ya kile kinachoahidi tu pasipo kuwa na mifano hai ya uongozi wa nchi).
Hata hivyo, Salmond na SNP yake wanaendelea na jitihada zao huku wakijipa imani kuwa utajiri mkubwa uliopo Uskochi (kuna mafuta huko Bahari ya Kaskazini) utawezesha kumudu gharama za kuendesha nchi endapo Waskochi wataafiki wazo la kujitenga na Uingereza.
Wakati hayo yakijiri hapa Uskochi, mwishoni mwa wiki huko nyumbani kumekumbwa na habari za kusikitisha ambapo maandamano ya kupinga Muungano huko Zanzibar yaligeuka kuwa machafuko makubwa.
Kama nilivyoeleza katika ujumbe wangu wa Makala za Sauti (
Audio Messages, unaoweza kusikia hapa
http://goo.gl/r6ngT ), machafuko hayo huko Zanzibar na suala zima la Muungano vinapaswa kuangaliwa kwa mtizamo mpana zaidi.
Binafsi, ninaona kuwa asili ya tatizo la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni waasisi wake, yaani Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume. Hapa naomba nieleweke vizuri.
Wazo la Muungano lilikuwa zuri kwa kuzingatia sababu mbalimbali, kubwa zaidi ikiwa ni ukaribu wa asili za watu wa Bara na wa Visiwani.
Lakini tatizo ambalo pengine lilichangiwa zaidi na mazingira ya kisiasa wakati huo, Nyerere na Karume walidhani kuwa ridhaa yao ilikuwa inawakilisha ridhaa ya Watanganyika na Wazanzibari wote.
Kuna ‘busara’ moja ya Kiingereza inayosema kuwa “jambo zuri si lazima liwe na manufaa. Kwa mfano, wakati kumpa chakula kingi mtu mwenye njaa ni jambo zuri lakini matokeo yake yanaweza kupelekea hata kifo kwenye mtu huyo mwenye njaa kali aliyeishia kupewa chakula kingi.”
Ndiyo, kula chakula kingi ukiwa na njaa kali ni hatari, na ndiyo maana watu wanapofunga au wakiwa hawajala muda mrefu huanza mlo kwa kinywaji cha moto (uji au chai).
Sasa, wazo la Muungano lilikuwa zuri lakini kutosaka ridhaa ya wengi ndiko kumetufikisha hapa tulipo sasa. Kwa muda mrefu kumekuwa na manung’uniko kuhusu Muungano, hususan miongoni mwa Wazanzibari.
Hoja kuu imekuwa ni kwamba wanapunjwa, wanaonewa na wengine wanakwenda mbali zaidi na kudai lengo la Muungano lilikuwa ‘kuimeza Zanzibar.’
Kwa bahati mbaya, siasa za Zanzibar zina tofauti kwa kiasi fulani na za Bara. Kwa Visiwani, dini ina nafasi ya kipekee katika siasa. Kwa hiyo, mara nyingi masuala ya kisiasa yanaweza pia kubeba hisia za kidini, jambo ambalo pasipo uangalifu linaweza kuzua balaa kubwa.
Ninapenda kusisitiza kuwa pamoja na hatari zinazoweza kujitokeza kwa kuchanganya dini na siasa, uzoefu na historia vimeonyesha kuwa laiti busara na maslahi ya jamii yakiwekwa mbele ya hisia binafsi, dini inaweza isiwe na madhara katika siasa.
Huko Marekani, kwa mfano, dini bado ina nafasi ya kipekee. Pengine mfano mzuri zaidi ya namna dini inavyoweza kutoharibu siasa ni Ujerumani ambapo chama cha Kansela Angela Merkel (Christian Democratic Union-CDU) ni cha Kikristo. CDU ndio chama kikubwa zaidi cha siasa katika taifa hilo tajiri.
Kadhalika, chama kinachotawala nchini Uturuki, Justice and Development Party-AKP, ni chama cha Kiislamu. Hata hivyo, chama hicho kimefanikiwa kuifanya Uturuki iendelee kuwa taifa lisiloelemea kwenye siasa zinazoongozwa na dini.
Hata hapa Uingereza, Malkia ambaye ndiye mkuu wa nchi (kiheshima zaidi kuliko kiutendaji) pia ni Mkuu (kiheshima) wa Kanisa la Anglikana, na japo Ukristo ni kama ‘dini ya taifa’ lakini nchi hii inaendeshwa kwa sheria za ‘kidunia’ na si za kidini.
Hata hivyo, tatizo la dini ni ukweli kwamba licha ya kugusa hisia binafsi za muumini, mambo ya kidini hayahitaji uthibitisho wa kisayansi (au kidunia).
Tofauti na dini, siasa ni suala la itikadi zaidi kuliko imani (japo imani kwenye itikadi inaweza kuwafanya wafuasi wa chama kukiona kina umuhimu kama dini). Kadhalika, masuala ya dini yanahusisha ‘maisha ya baadaye baada ya haya ya duniani’ ilhali siasa imejikita zaidi kwenye masuala ya sasa au ya hapahapa duniani.
Balaa linakuja pale muumini wa dini anapoanza kuamini kuwa anapopinga Muungano, kwa mfano, anafanya kazi ya kiroho na inampendeza Muumba. Ni vigumu sana kumdhibiti mtu wa aina hii kwani hata harakati zake zikihatarisha maisha yake, au akaishia kufa, anaamini kuwa atalipwa na Muumba wake.
Kimsingi machafuko yaliyotokea Zanzibar yamechangiwa zaidi na wanasiasa wetu ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wanachelea kile kinachofahamika kama ‘kuogopa laana ya waasisi wa Muungano pindi Muungano huo ukiwavunjikia mikononi mwao.’
Badala ya kuzishughulikia kero za Muungano na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu, watawala wetu wamekuwa wakijikita zaidi kwenye kujaribu kutuaminisha kuwa wanalishughulikia suala hilo kwa dhati ilhali wanaligusa juu juu tu.
Tumekuwa na Tume ya Kero za Muungano miaka nenda miaka rudi lakini ufanisi wake umekuwa wa kufikirika zaidi kuliko uhalisia.
Tuache unafiki, ‘kelele’ za kudai mabadiliko ya muundo wa Muungano (na hata hizo za kutaka uvunjiliwe mbali) haziwezi kwisha kwa kuzipuuza au kuwa na ‘tume ya milele’ ya kushughulikia kero hizo pasipo kuja na ufumbuzi.
Lakini kingine ni kuwanyamazia mafashisti wanaohubiri chuki dhidi ya wenzao kwa kisingizio cha kero za Muungano. Huko Zanzibar, baadhi ya wanasiasa wamediriki kudai ni Wabara wanaosababisha Wazanzibari kukosa ajira. Lakini huo ni mlolongo tu wa shutuma za aina hiyo, kwani huko nyuma Wabara walishawahi kutuhumiwa kuwa ndio waliopelekea ukimwi Visiwani humo.
Kwa vile hadi wakati huu ninaandaa makala hii bado hali huko Visiwani haijatulia, naomba nihitimishe kwa kutoa pendekezo la umuhimu wa kuwa na kura ya maoni itakayofidia kosa lililofanywa huko nyuma la kusaka ridhaa ya wananchi kuhusu Muungano.
Kama kura hiyo ya maoni itaamua tuwe na serikali tatu, basi hilo liheshimiwe. Kama itaamuliwa Muungano uvunjwe, basi na iwe hivyo (by the way, kuvunjika kwa Muungano hakutomaanisha kufa kwa Tanzania Bara au Zanzibar, kama ambavyo kuvunjika kwa ndoa hakumaanishi kifo kwa mume au mke aliyetalikiana na mwenzie).
Mwisho kabisa, wakati nikiwasihi viongozi wetu kuharakisha kura ya maoni ninayoamini itasaidia kuleta ufumbuzi wa kudumu wa matatizo ya Muungano wetu, ni muhimu kabisa kwa Serikali zote mbili (ya Muungano na ya Zanzibar) kuchukua hatua kali dhidi ya magaidi waliogeuza ‘madai halali kuhusu Muungano’ kuwa sababu ya kuwashambulia Wabara na kuchoma moto makanisa na mali zake.
Wanachofanya wahalifu hawa hakilengi kusaka suluhu ya Muungano bali wanapenda mbegu za uhasama wa kidini kati ya Wakristo na Waislamu.
Mungu Ibariki Tanzania