24 Sept 2014
1 Jun 2012
2 Nov 2007
- 2.11.07
- Evarist Chahali
- CONSERVATIVES, IRAK, LABOUR, MUUNGANO, SNP, UINGEREZA
- No comments
Kwa hapa UK,moja ya masuala ambayo kwa siku kadhaa sasa yametawala duru za habari ni kuhusu “Muungano” wa Uingereza (the United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland). Kumekuwa na mjadala wa muda mrefu kuhusu mambo makuu mawili: kwa upande mmoja ni umuhimu wa Muungano huo (miongoni mwa wale wanaopendelea kuona unadumu milele) na upande mwingine ni hoja kwamba muungano huo unazipunja baadhi ya sehemu zinazounda nchi hii.Katika uchaguzi mkuu uliopita,chama tawala cha Labour kilibwagwa na chama cha SNP (Scottish National Party) kwa upande wa Scotland.Hofu ya awali kwa Labour na “wapenda Muungano” baada ya ushindi wa SNP ilikuwa kwenye ukweli kwamba miongoni mwa malengo ya muda mrefu ya SNP ni kuiona Scotland ikiwa nchi huru inayojiendesha pasipo kuelekezwa na “serikali” ya London.Na katika manifesto yao ya uchaguzi,SNP hawakuogopa kutamka bayana matamanio yao uhuru wa Scotland.Chama hicho kilikuwa kinaelewa bayana kwamba sera hiyo ingeweza kuwapatia ushindi au kushindwa kwenye uchaguzi huo,kwani suala la uhuru wa Scotland ni miongoni mwa mambo yanayowagawa sana watu hawa.Kura mbalimbali za maoni kuhusu suala hilo zimekuwa na matokeo yanayothibitisha mgawanyiko huo,ambapo takriban nusu ya Waskotishi wanadhani uhuru ni wazo zuri huku takriban nusu nyingine wakipinga wazo hilo.Jeuri ya madai ya uhuru inachangiwa na kile Waskotishi wengi wanachokiona kama utajiri katika eneo hili (mafuta) ambao wanadhani unapaswa kuwanufaisha zaidi wao sambamba na kuwa na maamuzi ya namna ya kutumia utajiri huo badala ya kusubiri maelekezo kutoka England.Lakini wapo wanaoonya kwamba Scotland haiwezi kujimudu yenyewe kwa kutegemea tu utajiri wa mafuta,na baadhi ya wachumi wamekwenda mbali zaidi kwa kuonyesha pengo la bajeti litakaloikumba Scotland pindi ikijitoa kwenye Muungano huu.
Mjadala bado unaendelea na ni vigumu kusema bayana iwapo uhuru utapatikana au Muungano utaendelea.Majuzi,kiongozi wa chama pinzani cha Conservatives,David Cameron amewasha tena moto kuhusu suala hilo baada ya kutamka kwamba ana nia ya kusukuma sheria itakayowabana wabunge wa Scotland waliopo kwenye bunge la jumla la Uingereza (yaani linalojumuisha wabunge wa England,Wales,Scotland na Northern Ireland) wasipige kura kwenye masuala yanayoihusu England pekee.Hili ni suala linalujulikana kama “the West Lothian Question” (jina linalotokana na swali lililoulizwa mwaka 1977 na mbunge wa jimbo la Scotland la West Lothian,Tam Dalyell,wakati wa mjadala wa bunge kuhusu kuanzisha serikali-devolved governments-za Scotland na Wales).Swali hilo lilihusu uhalali wa wabunge wa “nchi” hizo mbili kushiriki katika mijadala na maamuzi yanayowahusu watu wa England pekee,ilhali wabunge wa England hawana nafasi kama hiyo kwa vile hawaingii kwenye mabunge ya sehemu hizo.Chama cha Labour kimemshutumu Cameron kwa kile walichokiita sera za kuvunja Muungano lakini kwa vyovyote vile hoja hiyo ni habari njema kwa Alec Salmond (First Minister wa Scotland) na chama chake cha SNP pamoja na wale wote wanaotaka uhuru.
Na kuna mambo yanayoshangaza kuhusu Muungano huu.Kwa mfano,wakati noti zinazotolewa na benki ya England (English Pounds) zinatumika nchi nzima,na zinakubalika mahala popote duniani kama sarafu halali ya nchi hii,noti zinazotolewa na mabenki ya Scotland (ambazo zina thamani sawa na English pounds) zinakataliwa katika baadhi ya maeneo ya England.Nilipokuja huko nyumbani mwaka jana,nilishindwa kabisa kubadilisha Scottish pounds na ilinilazimu nizitume huku ili zibadilishwe kuwa English pounds.Sheria za elimu ya juu na huduma za afya pia zinatofautiana kwa namna flani,ambapo kwa Scotland huduma nyingi zinatolewa bure ilhali kwa England zinaendelea kulipiwa.Scotland pia imekuwa ikilalamikia suala la uhamiaji ambapo sheria zinazotawala ni zile za nchi nzima ilhali mahitaji ya “nguvu-kazi” kutoka nje (kupitia uhamiaji wa wageni) unaathiriwa na sheria “kali” zinazotawala nchi zote zilizopo kwenye Muungano huu. Wakati Scotland imekuwa ikiendesha program kadhaa za kuvutia wageni,ikiwa ni pamoja na kuwashawishi wale walio hapa waifanye “nchi” hii kuwa makazi ya pili (second home) au makazi ya kudumu,kelele za wanasiasa huko England ni kwamba wageni wamezidi na lazima serikali idhibiti zaidi wahamiaji.
Masuala ya muungano ni nyeti na yamekuwa chanzo cha matatizo katika sehemu mbalimbali duniani.Lakini tofauti na wenzetu hawa ambao wanadiriki kutoa mawazo yao hadharani na kukaribisha mijadala kuhusu suala hilo,huko nyumbani kuzungumzia kuhusu Muungano inaelekea kuwa sio wazo la busara sana kwa mwanasiasa anayotaka mafanikio.Kuna kile kinachoitwa “jinamizi la Mwalimu kwa atakayetaka kuvunja Muungano” ambacho kimsingi nakiona ni kama kikwazo kwa wale wote wanaodhani kwamba ni muhimu kuwa na mjadala kuhusu hatima ya Muungano wetu.Tukiendelea kuogopa kuujadili,yayumkinika kusema kwamba tunautengenezea mazingira mazuri ya kuuharibu.Sio siri kwamba wenzetu wa Visiwani wamekuwa wakipiga kelele sana kwamba Muungano unawaumiza,lakini hofu yangu kubwa ni pale wenzao wa Bara nao “watakaposhikilia bango” hoja hiyo ya kuumizwa na mzigo wa Muungano.Na “the West Lothian Question” ya Uingereza “ina-fit” kabisa mazingira yalivyo huko nyumbani ambapo wabunge kutoka Zanzibar wamekuwa wakishiriki (katika bunge la Muungano) katika kujadili na kutoa maamuzi katika baadhi ya mambo ambayo yanayowahusu Wabara pekee ilhali wabunge wa Bara hawana nafasi hiyo kwani hawaingii kwenye Baraza la Wawakilishi huko Zanzibar.
Nafahamu kuwa kuna kitu kama “tume” au “kamati” iliyoundwa kujadili kero za Muungano,lakini japo sijui imefikia hatua gani katika majadiliano yao,yayumkinika kusema kwamba kasi nzima ya kulitafutia ufumbuzi wa kudumu suala hilo sio ya kuridhisha.Pengine katika kuepuka maamuzi yanayotoka juu kwenda chini (yaani kutoka kwa viongozi kwenda kwa wananchi) japo waathirika au wafaidika wakubwa ni hao wa chini,sio wazo baya kufikiria kuitisha kura ya maoni ili kupata mawazo ya wadau wakubwa wa Muungano huo (wananchi).Ashakum si matusi,lakini ni vema Muungano ukavunjika kwa ridhaa kuliko ukadumu kwa manung’uniko,kwani manung’uniko hayo yasipopatiwa tiba yanaweza kabisa kuuvunja Muungano huo pasipo kusubiri ridhaa ya wadau.Kikubwa nilichojifunza katika mjadala wa Muungano wa Uingereza ni namna ambavyo unavyoendeshwa kwa uwazi na upana zaidi kiasi kwamba sauti zote,zinazopinga na kukubali suala hilo,zinasikika waziwazi.Ukiniuliza iwapo Muungano wetu ni muhimu,jibu nitakalokupa hata niwapo usingizini ni “ndio”.Hata hivyo,umuhimu wa Muungano huo hauondoi haja ya kuufanya uwe bora zaidi,wa manufaa kwa pande zote mbili na wenye mazingira yatakayoufanya udumu daima dumu.Tusipoziba ufa leo,kesho tutajenga ukuta.
Mwisho, napenda kutoa pongezi kwa kizazi kipya cha vijana wabunifu. Hivi karibuni, mchora katuni na mtangazaji maarufu Masudi “Kipanya” alizindua duka la nguo za lebo yake ya “KP Wear”. Na msanii wa bongoflava AY nae anaelekea kufuata mkondo huo. Hawa na wengineo wenye mawazo kama hayo wanatumia vizuri umaarufu walionao kwenye jamii na wanastahili sapoti yetu. Wito wangu kwao ni kwamba wanapomiminiwa sifa kwa jitihada zao, wazitumie sifa hizo kuwa chemchem ya kusaka mafanikio zaidi. Pia wanaweza kwenda mbali zaidi kwa kutumia mianya ya biashara ya kimataifa kama vile katika e-Bay ili kuwawezesha Watanzania popote walipo duniani kunufaika na ubunifu wao. Kwa lugha ya mtaani, mie “nawapa tano”.Tanzania ya “masupastaa” wanaovuma kwa ubunifu wao,na sio kwa skendo,inawezekana.
Alamsiki