Showing posts with label KERO ZA MUUNGANO. Show all posts
Showing posts with label KERO ZA MUUNGANO. Show all posts

1 Jun 2012


Ya Zanzibar si mageni, hata Uskochi yapo
Evarist Chahali
Toleo la 241
30 May 2012


WIKI iliyopita, Waziri wa Kwanza (First Minister, cheo ambacho ni kama Waziri Mkuu) wa Uskochi, Alex Salmond, alizindua kampeni za chama chake cha Scottish Nationalist Party (SNP) kuhamasisha kura ya ‘Hapana’ katika referendum (kura ya maoni ) ya uhuru wa nchi hii inayotarajiwa kufanyika huko mbeleni.
Hoja ya Uskochi kujitenga na Uingereza (kwa maana ya kile kinachoitwa The United Kingdom of Great Britain-England, Uskochi na Wales- and Northern Ireland) imekuwa ikivuma kwa muda mrefu na imepata nguvu zaidi baada ya Salmond na SNP yake kuingia madarakani mwaka 2007.
Kimsingi, sera kuu ya mwanasiasa huyo na chama chake ilikuwa kuhakikisha kuwa hatimaye Uskochi inajitenga kutoka Uingereza.
Walipoingia madarakani tu, SNP walieleza bayana kuwa wana mpango wa kufanyareferendum kusikia maoni ya Waskochi kuhusu wazo hilo la kujitenga.
Hata hivyo, kikwazo ambacho wamekuwa wakikumbana nacho tangu mwanzo ni ukweli kwamba pamoja na tofauti za hapa na pale, ni vigumu kuchora mstari unaoweza kuwatenganisha Waskochi na Waingereza wengine.
Mwingiliano katika takriban kila nyanja ya maisha unawafanya watu hawa kuwa wamoja zaidi kuliko tofauti.
Na wakati naandaa makala hii, Salmond amepata ‘habari mbaya’ kutoka kwa mwendesha kura za maoni (pollster) maarufu hapa Uingereza, Peter Kellner, Rais wa taasisi ya kura za maoni ya YouGov.
Kwa mujibu wa Kellner, kura ya maoni iliyoendeshwa na YouGov Ijumaa iliyopita inaonyesha kuwa wakati ni asilimia 33 tu ya Waskochi wanataka ‘uhuru’ (kujitenga), asilimia 57 wanataka Uskochi iendelee kubaki sehemu ya Uingereza.
Mwendesha kura za maoni huyo amemtahadharisha Salmond kuwa ‘ana mlima mrefu wa kupanda’ kubadili upeo wa wengi wa Waskochi kuhusu nchi yao kujitenga na Uingereza.
Kadhalika, alieleza kuwa kuna ‘vitisho’ kadhaa vinavyoweza kuchangia Waskochi wengi kupinga wazo la kujitenga, na akatoa mfano wa hoja kama wawekezaji kujiondoa Uskochi (kwa kutokuwa na uhakika kama Uskochi itamudu ‘kusimama yenyewe’),  kupoteza ruzuku inayotolewa na Serikali Kuu ya Uingereza (ambayo ni kubwa zaidi ya kodi inayolipwa na Uskochi), matumizi ya sarafu ya pauni ya Kiingereza (British Pound) ambapo kama Uskochi itaamua kutumia sarafu hiyo baada ya kujitenga, Uingereza inaweza kuanzisha hatua za ukalifu (austerity measures) zitakazoathiri uchumi wa Uskochi.
Kadhalika, Salmond ametahadharishwa kwamba hofu nyingine zinazoweza kuwatisha Waskochi kuunga mkono wazo la kujitenga ni pamoja na gharama kubwa za kuendesha nchi kamili (hasa katika kipindi hiki ambapo uchumi wa dunia unayumba) kama vile kumudu kuwa na jeshi kamili, ofisi za ubalozi nchi za nje na gharama za uendeshaji wa taasisi za utumishi wa umma (civil service).
Kimsingi,  katika zoezi lolote lile la kupiga kura, hali ya kutokuwa na uhakika au hofu ya “huko mbele hali itakuwaje” inatosha kuwafanya wapiga kura wengi kuamua kubaki na chama kilichopo au muundo uliopo (iwapo ni referendum ya jambo fulani).
Mbinu hii inatumiwa sana na vyama tawala (ikiwa ni pamoja na CCM) kwenye chaguzi ambapo ujumbe huwa mithili ya ‘zimwi likujualo halikuli likakwisha’ (kwa maana ya chama unachokifahamu ni bora zaidi ya kile kinachoahidi tu pasipo kuwa na mifano hai ya uongozi wa nchi).
Hata hivyo, Salmond na SNP yake wanaendelea na jitihada zao huku wakijipa imani kuwa utajiri mkubwa uliopo Uskochi (kuna mafuta huko Bahari ya Kaskazini) utawezesha kumudu gharama za kuendesha nchi endapo Waskochi wataafiki wazo la kujitenga na Uingereza.
Wakati hayo yakijiri hapa Uskochi, mwishoni mwa wiki huko nyumbani kumekumbwa na habari za kusikitisha ambapo maandamano ya kupinga Muungano huko Zanzibar yaligeuka kuwa machafuko makubwa.
Kama nilivyoeleza katika ujumbe wangu wa Makala za Sauti (Audio Messages, unaoweza kusikia hapa http://goo.gl/r6ngT ), machafuko hayo huko Zanzibar na suala zima la Muungano vinapaswa kuangaliwa kwa mtizamo mpana zaidi.
Binafsi, ninaona kuwa asili ya tatizo la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni waasisi wake, yaani Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume. Hapa naomba nieleweke vizuri.
Wazo la Muungano lilikuwa zuri kwa kuzingatia sababu mbalimbali, kubwa zaidi ikiwa ni ukaribu wa asili za watu wa Bara na wa Visiwani.
Lakini tatizo ambalo pengine lilichangiwa zaidi na mazingira ya kisiasa wakati huo, Nyerere na Karume walidhani kuwa ridhaa yao ilikuwa inawakilisha ridhaa ya Watanganyika na Wazanzibari wote.
Kuna ‘busara’ moja ya Kiingereza inayosema kuwa “jambo zuri si lazima liwe na manufaa. Kwa mfano, wakati kumpa chakula kingi mtu mwenye njaa ni jambo zuri lakini matokeo yake yanaweza kupelekea hata kifo kwenye mtu huyo mwenye njaa kali aliyeishia kupewa chakula kingi.”
Ndiyo, kula chakula kingi ukiwa na njaa kali ni hatari, na ndiyo maana watu wanapofunga au wakiwa hawajala muda mrefu huanza mlo kwa kinywaji cha moto (uji au chai).
Sasa, wazo la Muungano lilikuwa zuri lakini kutosaka ridhaa ya wengi ndiko kumetufikisha hapa tulipo sasa. Kwa muda mrefu kumekuwa na manung’uniko kuhusu Muungano, hususan miongoni mwa Wazanzibari.
Hoja kuu imekuwa ni kwamba wanapunjwa, wanaonewa na wengine wanakwenda mbali zaidi na kudai lengo la Muungano lilikuwa ‘kuimeza Zanzibar.’
Kwa bahati mbaya, siasa za Zanzibar zina tofauti kwa kiasi fulani na za Bara. Kwa Visiwani, dini ina nafasi ya kipekee katika siasa. Kwa hiyo, mara nyingi masuala ya kisiasa yanaweza pia kubeba hisia za kidini, jambo ambalo pasipo uangalifu linaweza kuzua balaa kubwa.
Ninapenda kusisitiza kuwa pamoja na hatari zinazoweza kujitokeza kwa kuchanganya dini na siasa, uzoefu na historia vimeonyesha kuwa laiti busara na maslahi ya jamii yakiwekwa mbele ya hisia binafsi, dini inaweza isiwe na madhara katika siasa.
Huko Marekani, kwa mfano, dini bado ina nafasi ya kipekee. Pengine mfano mzuri zaidi ya namna dini inavyoweza kutoharibu siasa ni Ujerumani ambapo chama cha Kansela Angela Merkel (Christian Democratic Union-CDU) ni cha Kikristo. CDU ndio chama kikubwa zaidi cha siasa katika taifa hilo tajiri.
Kadhalika, chama kinachotawala nchini Uturuki, Justice and Development Party-AKP, ni chama cha Kiislamu. Hata hivyo, chama hicho kimefanikiwa kuifanya Uturuki iendelee kuwa taifa lisiloelemea kwenye siasa zinazoongozwa na dini.
Hata hapa Uingereza, Malkia ambaye ndiye mkuu wa nchi (kiheshima zaidi kuliko kiutendaji) pia ni Mkuu (kiheshima) wa Kanisa la Anglikana, na japo Ukristo ni kama ‘dini ya taifa’ lakini nchi hii inaendeshwa kwa sheria za ‘kidunia’ na si za kidini.
Hata hivyo, tatizo la dini ni ukweli kwamba licha ya kugusa hisia binafsi za muumini, mambo ya kidini hayahitaji uthibitisho wa kisayansi (au kidunia).
Tofauti na dini, siasa ni suala la itikadi zaidi kuliko imani (japo imani kwenye itikadi inaweza kuwafanya wafuasi wa chama kukiona kina umuhimu kama dini). Kadhalika, masuala ya dini yanahusisha ‘maisha ya baadaye baada ya haya ya duniani’ ilhali siasa imejikita zaidi kwenye masuala ya sasa au ya hapahapa duniani.
Balaa linakuja pale muumini wa dini anapoanza kuamini kuwa anapopinga Muungano,  kwa mfano, anafanya kazi ya kiroho na inampendeza Muumba. Ni vigumu sana kumdhibiti mtu wa aina hii kwani hata harakati zake zikihatarisha maisha yake, au akaishia kufa, anaamini kuwa atalipwa na Muumba wake.
Kimsingi machafuko yaliyotokea Zanzibar yamechangiwa zaidi na wanasiasa wetu ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wanachelea kile kinachofahamika kama ‘kuogopa laana ya waasisi wa Muungano pindi Muungano huo ukiwavunjikia mikononi mwao.’
Badala ya kuzishughulikia kero za Muungano na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu, watawala wetu wamekuwa wakijikita zaidi kwenye kujaribu kutuaminisha kuwa wanalishughulikia suala hilo kwa dhati ilhali wanaligusa juu juu tu.
Tumekuwa na Tume ya Kero za Muungano miaka nenda miaka rudi lakini ufanisi wake umekuwa wa kufikirika zaidi kuliko uhalisia.
Tuache unafiki, ‘kelele’ za kudai mabadiliko ya muundo wa Muungano (na hata hizo za kutaka uvunjiliwe mbali) haziwezi kwisha kwa kuzipuuza au kuwa na ‘tume ya milele’ ya kushughulikia kero hizo pasipo kuja na ufumbuzi.
Lakini kingine ni kuwanyamazia mafashisti wanaohubiri chuki dhidi ya wenzao kwa kisingizio cha kero za Muungano. Huko Zanzibar, baadhi ya wanasiasa wamediriki kudai ni Wabara wanaosababisha Wazanzibari kukosa ajira. Lakini huo ni mlolongo tu wa shutuma za aina hiyo, kwani huko nyuma Wabara walishawahi kutuhumiwa kuwa ndio waliopelekea ukimwi Visiwani humo.
Kwa vile hadi wakati huu ninaandaa makala hii bado hali huko Visiwani haijatulia, naomba nihitimishe kwa kutoa pendekezo la umuhimu wa kuwa na kura ya maoni itakayofidia kosa lililofanywa huko nyuma la kusaka ridhaa ya wananchi kuhusu Muungano.
Kama kura hiyo ya maoni itaamua tuwe na serikali tatu, basi hilo liheshimiwe. Kama itaamuliwa Muungano uvunjwe, basi na iwe hivyo (by the way, kuvunjika kwa Muungano hakutomaanisha kufa kwa Tanzania Bara au Zanzibar, kama ambavyo kuvunjika kwa ndoa hakumaanishi kifo kwa mume au mke aliyetalikiana na mwenzie).
Mwisho kabisa, wakati nikiwasihi viongozi wetu kuharakisha kura ya maoni ninayoamini itasaidia kuleta ufumbuzi wa kudumu wa matatizo ya Muungano wetu, ni muhimu kabisa kwa Serikali zote mbili (ya Muungano na ya Zanzibar) kuchukua hatua kali dhidi ya magaidi waliogeuza ‘madai halali kuhusu Muungano’ kuwa sababu ya kuwashambulia Wabara na kuchoma moto makanisa na mali zake.
Wanachofanya wahalifu hawa hakilengi kusaka suluhu ya Muungano bali wanapenda mbegu za uhasama wa kidini kati ya Wakristo na Waislamu.
Mungu Ibariki Tanzania


27 May 2012

Naomba kuwaletea toleo la tatu la mfululizo wa Makala za Sauti.Kamanilivyobainisha katika matoleo mawili yaliyopita,hadi sasa bado nipo katika hatua ya majaribio.Ninafanya kila linalowezekana kupata vitendea kazi bora kabisa(ikiwa ni pamoja na softwares mwafaka) ili kukupatia wewe msikilizaji ubora unaostahili.

Katika toleo hili ninazungumzia Vurugu zinazoendelea huko Visiwani Zanzibar na sualazimala Muungano kwa ujumla.Kwa hakika,kiwango cha ubora wa makala hiyo bado sio cha kuridhisha,na pia sijapata kujiamini vya kutosha katika uwasilishaji wa mada husika (kwa mfano kutumia muda kidogo kuamua nitumie neno gani) lakini huu ni mwanzo,na ninadhamiria kwa zaidi ya asilimia 100 kuwa muda si mrefu nitawaletea kitu bora kabisa na mnachostahili kwa dhati.

Labda la mwisho ni kwamba ninafanya kila linalowezekana ili toleo zima la makala husika liwe kwa lugha ya taifa,yaani Kiswahili.Hiyo ni moja ya sababu ya wakati flani kuwa ninahangaika nitumie nheno gani mwafaka la kiswahili.Si kwamba nimesahau lugha yangu ila moja ya madhara ya kuwa huko nje kwa muda mrefu ni hilo.

Karibuni sana,na msisite kunitumia maoni (chagua player yoyote kati ya hizi mbili hapa chini)
 


12 Apr 2012

Kisiwani Zanzibar walikusanyika kundi la watu katika baraza la wawakilishi wakitaka kuitishwe kura ya maoni.
Wananchi wa Zanzibar wataka kuitishwe kura ya maoni
Wananchi wa Zanzibar wataka kuitishwe kura ya maoni
Huko Zanzibar Tanzania, kundi la watu walikusanyika leo (11.04.2012) katika viwanja vya baraza la wawakilishi wakidai kuitishwa kura ya maoni kuhusu suala la Muungano kati ya iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar 1964 na kuundwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliopo hii leo.
Mohamed Abdul-rahman alizungumza na Rashid Hadi anayedaiwa kuwa kiongozi wa kikundi hicho na kwanza anaelezea sababu za kukusanyika kwao.
(Sikiliza maogezi hayo hapa chini)


Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri: Daniel Gakuba

22 Aug 2011


Imetumwa na mdau Kato Lukaija

Wapo watu wanoamini kwamba pakipatikana suluhisho la matatizo ya biashara na uchumi kati ya bara na Zanzibar, basi kero za muungano zitakua zimekwisha. Hawa wanafanana na viongozi wetu wanaoamini kwamba muungano wa kiuchumi wa Afrika mashariki ni atua itakayotosheleza kuleta muungano wa kisiasa na kiutamaduni .Kwa mtazamo huu, uchumi ndio msingi wa kila jambo, liwe la kitamaduni,kisiasa au kitaifa. Na ndio maana nguvu zinaelekezwa zaidi kwenye diplomasia ya uchumi.

Lakini Muungano wetu,pamoja na kuunganisha uchumi wetu kwa matumizi ya sarafu moja,bado umegubikwa na hali ya kutosikilizana.Hali imekua hivyo kwa muda mrefu. Kwa hiyo kero zake,kama mijadala mingi inavyoonesha,haisababishwi na matatizo ya uchumi peke yake. Kuna tatizo la utata wa historia yenyewe ya muungano.

Kuna historia mbili za Muungano. Watu wa bara wanaona Muungano ni matokeo ya Mapinduzi ya Zanzibar yalioundoa utawala wa kitumwa wa Waarabu. Lakini nje ya madarasa rasmi ya historia hiyo,wapo vijana wanaharakati wa Zanzibar, kama Harith Ghasany,mwandishi wa KWAHERI UKOLONI,KWA HERI UHURU. Wanaharakati hawa wanadai kwamba Mapinduzi ya Zanzibar ni tunda la usuda ya Nyerere na kanisa dhidi ya waislamu na waarabu wa Zanzibar.Hivyo Muungano unaonekana kama ukoloni.

Hali hii inahitaji Wazee wakae na kukubaliana kuandika historia moja.  Wafanye kama Rais Kagame. Pamoja na kuangaikia uchumi,Kagame amehakikisha kwamba historia ya kweli ya mauaji ya 1994 ndio inayofundishwa na watu wote.Kagame anajua kwamba mtu haishi kwa mkate tu,ila kwa kila neno litokalo kwa bwana. Kwa hiyo vijana tunaomba wazee waandike historia moja tu. Wazee  wakisimamia historia moja tu, Muungano wetu utapona.

                             ------Kato Lukaija,  P.O.BOX 10351, DAR ES SALAAM.
                                         

22 Oct 2008


Na Hilary Komba 

WATANZANIA Bara hawawezi kulazimika kuingia Zanzibar kwa pasipoti kutokana na sheria ya uraia kukataza utaratibu huo ndani ya Jamhuri moja. 

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Naibu Kamishina wa Uhamiaji, Wizara ya Mambo ya Ndani Bw. Abdi Ijimbo, wakati akizungumza na Majira kuhusu hoja zilizoripotiwa na vyombo vya habari hivi karibuni, vikiwanukuu baadhi ya watu wakisema ni vyema Watanzania Bara waingie Zanzibar kwa pasipoti. 

Bw. Ijimbo alisema sheria za Uhamiaji zinaruhusu Mtanzania anayetaka kutoka nje ya nchi kuwa na pasipoti, ili ajulikane kuwa ni Mtanzania aliyefuata taratibu ambazo zipo duniani kote. 

"Hadi sasa Serikali haina sababu ya kuanzisha pasipoti kuingia Zanzibar, kwa vile hakuna sheria inayosema hivyo na Zanzibar ipo katika Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, ndiyo maana hata huko nyuma hati ya kuingilia Zanzibar ilifutwa," alisema. 

Bw. Ijimbo aliongeza kuwa katika Serikali ya Awamu ya Pili, Watanzania Bara walikuwa wanaingia Zanzibar kwa hati ambayo ilikuwa pia haina hadhi ya pasipoti, bali ulikuwa ni utaratibu fulani tu uliowekwa na baadaye kuonekana hauna sababu ya kuendelea kuwapo. 

Alisema anashangaa kuona baadhi ya Watanzania wanazungumzia jambo hilo ndani ya nchi zilizoungana na kuwa kwenye Jamhuri ya Muungano. 

Nayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesisitiza kwamba vitambulisho vinavyotolewa vya Mzanzibari mkazi ni kwa wale tu wanaoishi visiwani humo, anaripoti Ali Suleiman. 

SMZ imesema Watanzania kutoka Bara wataweza kutambuliwa kwa vitambulisho hivyo, baada ya kutimiza masharti yaliyopo. 

Imesema vitambulisho hivyo havina malengo ya kisiasa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu kwamba ni mikakati ya CCM kushinda katika uchaguzi mkuu ujao. 

Akitoa juzi majumuisho ya mjadala wa sera ya vitambulisho vya Mzanzibari, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya Serikali Zanzibar, Bw. Suleiman Othman Nyanga, alisema Zanzibar haiwezi kutoa vitambulisho vya uraia kwani yenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Serikali ya Muungano. 

Alisema sera iliyoandaliwa ni ya vitambulisho vya Mzanzibari mkazi na si ya vitambulisho vya Mzanzibari. 

“Mheshimiwa Spika ni vyema kutambua kuwa hii sera ni ya vitambulisho vya Mzanzibari kwa sababu michango mingi iliyotolewa, imezungumzia suala la Mzanzibari, lakini hapa tunasema ni sera ya vitambulisho vya Mzanzibari mkazi kwa sababu Mzanzibari tunayetaka kumpa kitambulisho ni yule ambaye anakaa Zanzibar,” alisema Waziri huyo. 

Waziri Nyanga alisisitiza, kwamba vitambulisho hivyo hatapewa Mzanzibari anayekaa nje ya visiwa hata kama anakaa Dar es Salaam, lakini ikiwa si mkazi, hatakuwa na halali ya kupata kitambulisho hicho, ambacho ni kwa ajili ya Wazanzibari wanaoishi Unguja na Pemba. 

“Tunayemsema sisi hapa ni Mzanzibari mkazi ndiye tutakayempa kitambulisho, kama anakaa Dar es Salaam maadam si mkazi yeye hahusiki na kitambulisho hiki cha sera hii, ambayo tunataka kuipitisha,” alisema. 

Waziri huyo alisema SMZ haitatoa vitambulisho vya uraia kwa sababu suala hilo ni la Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hata Rais wa kwanza wa Zanzibar, marehemu Abeid Amaan Karume alitoa vitambulisho vya uraia kwa Zanzibar. 

“Wakati huo vitambulisho kweli vilitolewa na viliitwa pasi ya uraia iliyotolewa wakati huo na kwa kuwa kuna neno uraia, na uraia kwa Tanzania ni mmoja, kwa hivyo vitambulisho hivyo kama utavitazama vitakuwa vimeandikwa pasi ya uraia na vimeandikwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Zanzibar ... haikuwa pasi ya uraia ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,” alisema. 

Alisema watakaopaswa kupewa vitambulisho ni wale walioamua kuwa wakazi wa Zanzibar, ambao watakuwa na makazi yao ya kudumu na watakuwa wanahitaji huduma za kila siku za Serikali ambao takwimu zao zitasaidia kupanga mipango ya maendeleo ya visiwa vya Unguja na Pemba. 

Hata hivyo, Waziri Nyanga alisema Mzanzibari yeyote anayeishi nje ya Zanzibar anapoamua kurudi Zanzibar, basi ana haki ya kuomba kitambulisho na atapewa baada ya kuthibitisha kuwa na sifa zinazohitajika. 

“Kwa hiyo akiweza kuthibitisha sifa zilizotajwa, atapewa vitambulisho ingawa wengine walitoa maoni kwamba vielezwe kuwa ni vitambulisho vya uraia kwa kuwa suala la uraia ni la Jamhuri ya Muungano na hakuna raia wa Zanzibar, kwa hiyo vitambulisho hivi vitakuwa bado ni vya Mzanzibari mkazi na si vitambulisho vya uraia wa Zanzibar," alisema. 

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipitisha sera ya vitambulisho vya ukazi vya Zanzibar, hatua ambayo itasaidia kuweka kumbukumbu na kusaidia takwimu za nchi katika maendeleo.

CHANZO: Majira

21 Oct 2008


BAADHI ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamepinga sera ya vitambulisho vya Mzanzibari mkazi na kusema suala hilo linafanywa zaidi kisiasa na kutaka kurudishwa kwa hati ya kusafiri kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ambayo iliondoshwa mwaka 1995. 

Hayo yalisemwa jana na Waziri Kivuli Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bw. Abdalla Juma, wakati akisoma maoni ya kambi ya upinzani katika suala la sera ya vitambulisho vya Mzanzibari mkazi. 

Alisema haiwezekani Wazanzibari kuitwa wakazi katika nchi yao na kuongeza kwamba vitambulisho hivyo havifai. 

"Vitambulisho hivi kwa kweli havifai, sera hii haifai isipitishwe, kwa sababu inaonekana wazi kuwadhalilisha Wazanzibari katika nchi yao," alisema Bw. Abdalla. 

Wajumbe wengine wa Baraza walitaka kurudishwa kwa utaratibu wa zamani wa kuwapo hati za usafiri wakati wa kuingia katika visiwa vya Unguja na Pemba. 

Mwakilishi wa Magomeni, Bw. Salmin Awadh, alitaka kurudishwa kwa hati za usafiri na kusema kuondoshwa kwake kwa kiasi kikubwa kumesababisha kasi ya ujambazi na uhalifu. 

"Tunataka kurudishwa kwa hati za usafiri kati ya Zanzibar na Tanzania Bara...tunataka kuwepo kwa udhibiti katika eneo la bandari pamoja na uwanja wa ndege'alisema Awadh. 

awadh alisema sera ya vitambulisho vya uzanzibari ukazi lengo lake ni ulinzi kwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba na kuweza kuwatambuwa hasa Wazanzibari na wageni. 

mwakilishi wa viti maalumu kutoka katika chama cha wananchi CUF Zakia Omar naye alitaka kurudishwa kwa utaratibu huo ambao alisema ulisaidia sana kudhibiti vitendo vya uhalifu. 

alisema kuondoshwa kwa hati za kusafiria kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kiasi kikubwa kumerudisha wimbi la vitendo vya uhalifu. 

hati ya kusafiri kati ya Tazania Bara na Zanzibar pasipoti iliondolewa katika miaka ya 1995,baada ya kubainika kuwepo kwa vikwazo vya usafiri katika nchi moja ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na kuonekana kwenda kinyume na katiba
.

CHANZO: Majira

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.