Showing posts with label MAREKANI. Show all posts
Showing posts with label MAREKANI. Show all posts

18 Jun 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Hivi umeshawahi kuulizwa swali moja zaidi ya mara mia na kila unapoulizwa hujiskii kulizowea swali hilo?Pengine imeshakutokea.Mimi imekuwa ikinitokea mara nyingi zaidi ya ninavyoweza kukumbuka.Ilianza nikiwa huko nyumbani.Kabila langu ni Mndamba,natokea Ifakara mkoani Morogoro.Sio siri kuwa Wandamba sio kabila maarufu ukilinganisha na makabila mengine ya mkoa naotoka,kwa mfano Waluguru au Wapogoro.Kwa hiyo kila nilipokuwa naulizwa “hivi wewe ni kabila gani” na mimi kujibu “mie Mndamba” mara nyingi swali lililofuata ni “hivi Wandamba wanatoka mkoa gani?”Au wakati mwingine nilipoulizwa mkoa naotoka na kujibu Morogoro,wengi walipenda kudhani mimi ni Mluguru.Niliposema hapana,wangeniuliza iwapo ni Mpogoro.Sikuwalaumu kwa vile mara nyingi jina la mkoa unaotoka huwa linahusishwa na kabila kubwa au maarufu katika mkoa huo.Ukisema unatoka Mwanza,watu watahisi wewe ni Msukuma,ukitoka Songea watu watahisi wewe Mngoni,au Tabora watahisi wewe Mnyamwezi,na kadhalika.

Nilipokuja huku Ughaibuni swali likageuka kuwa “wewe unatoka nchi gani?”Mara nyingi napojibu “natoka Tanzania” swali linalofuata ni “hivi Tanzania iko wapi?”Wengine wanajua iko Afrika lakini hawana uhakika ni sehemu gani katika bara hiko lenye nchi zaidi ya hamsini.Kuna wakati huwa nawalaumu wanaoniuliza swali hilo kwamba hawakuwa makini kwenye somo la Jiografia,lakini yayumkinika kusema kuwa hata kama ulipata A kwenye somo hilo sio rahisi kujua kila nchi ilipo kwenye ramani ya dunia,kama isivyo rahisi kwa kila Mtanzania kujua Wandamba wanatoka mkoa gani.Hata hivyo,kila napoulizwa ilipo Tanzania,huwa natumia fursa hiyo kufanya kazi ya wenzetu tuliowapa majukumu ya kuitangaza nchi yetu kwa kueleza kuwa nchi hiyo “iko kusini mwa Kenya na Uganda,mashariki ya DRC,Rwanda na Burundi…”,na kadhalika.Wakti mwingine natumia vivutio vyetu kujibu swali hilo,yaani nasema kuwa “Tanzania ndipo ulipo Mlima Kilimanjaro,au Ziwa Victoria,au Mbuga ya Selous…”

Wakati sote tunajua kuwa ni vigumu kwa kabila Fulani kufanya kampeni ya kujitangaza (na jitihada kama hizo zikifanyika utaambiwa unaleta ukabila) kila nchi ina jukumu la kujitangaza yenyewe.Inauma ninapoangalia kwenye runinga na kuona matangazo kama hili hapa: “mtoto huyu anahitaji sana msaada wako…anapenda kujiendeleza na elimu lakini anatoka Tanzania,moja ya nchi masikini sana duniani…kwa kutoa paundi tatu kwa mwezi unaweza kuwasaidia watoto kama huyu…”Yaani nchi yetu inapata nafasi ya kusikika lakini sio kwa sifa nzuri bali umasikini wake.Na huwezi kuwalaumu wanaotoa matangazo ya aina hiyo kwa kuwa wanafanya hivyo kwa nia nzuri,na sio jukumu lao kuitangaza nchi yetu kwa mtizamo wa kuvutia watalii au vivutio vilivyopo huko.Hiyo ni kazi ya Watanzania wenyewe.

Naamini kuna watu wana majukumu ya kuitangaza nchi yetu.Hebu nikupe mfano.Uganda inadhamini kipindi Fulani kwenye kituo cha televisheni cha CNN International cha Marekani.Zambia nao wanatoa matangazo ya kuitangaza nchi yao kwenye kituo hicho na kuwakaribisha wageni waende kushuhudia Maporomoko ya Victoria.Hata Malawi,Rwanda na Burundi nao hawako nyuma,kwani nimeshaona matangazo yao kwenye gazeti maarufu duniani la TIME.Lakini sie tuko nyuma katika eneo hili.Pengine kuna watu wanaona sio muhimu kujitangaza kwa vigezo kwamba “chema chajiuza kibaya chajitembeza.”Tunachopaswa kufahamu ni kwamba katika zama hizi za ushindani wa kuvutia watalii (na hata wawekezaji wa kweli) ni muhimu sana kuitangaza nchi yako.Ukitaka kuhakikisha nayosema sio utani ingia kwenye internet na tafuta habari kuhusu vivutio vilivyopo nchini kwetu.Ni dhahiri utagundua kuwa taarifa zilizopo ni chache,na hata hizo chache hazijitoshelezi,na mara nyingi huwa zimewekwa na wasio Watanzania.Kuna watu wengi wanaoamini kuwa Mlima Kilimanjaro uko Kenya kwa vile nchi hiyo imekuwa ikiutangaza Mlima huo kama uko kwake,na sie tumekaa kimya.Ukienda kwenye tovuti ya Bodi ya Biashara za Nje (BET) wao wanaonekana wako bize zaidi na Maonyesho ya Sabasaba.Nilipotembelea tovuti yao leo ilikuwa inasema iko kwenye matengenezo lakini inakupeleka kwenye kiungo (link) ya Maonyesho ya 30 ya Kimataifa ya Dar Es Salaam (DITF),pengine kuonyesha kuwa Maonyesho hayo (ambayo ni ya mara moja tu kwa mwaka) ni muhimu zaidi kwao kuliko kuitangaza nchi yetukila siku.Angalau Bodi ya Utalii wamejitahidi kiasi japokuwa tovuti yao haina habari za kutosha kuhusu vivutio tulivyonavyo.Tuna Kituo cha Biashara (Tanzania Trade Centre) hapa Uingereza,lakini tovuti yake ni kama imeandaliwa haraka haraka kwa vile taarifa zilizopo humo sio za kutosha sana.Wahusika wasikasirike kusoma haya nayoandika kwa sababu tumewakabidhi dhamana ya kuitangaza nchi yetu.Badala ya kuchukia kukosolewa wanapaswa waone hii kuwa ni changamoto kwao.

Kilio changu kingine ni kukosekana kwa AIR TANZANIA ya Watanzania.Kama wenzetu Kenya wameweza kwanini sisi tushindwe?Angalia Wahabeshi wa Ethiopia wanavyoweza kuchuana na mashirika makubwa ya ndege duniani na kujiingizia mapato makubwa kupitia sekta ya usafiri wa anga na Ethiopian Airlines yao.Kwa kurusha Air Tanzania “the Wings of Kilimanjaro” tulikuwa tunaitangaza nchi yetu na wakati huohuo kuujulisha ulimwengu kuwa Mlima Kilimajaro uko kwetu.Tuna vivutio vingine vingi vya kuvitangaza huku nje ikiwa ni pamoja na moja ya hifadhi kubwa kabisa duniani,Selous,na ziwa la pili kwa ukubwa duniani,Victoria.

Tukubali kwamba hatujajitahidi vya kutosha na tusisubiri kuulizwa.Hatuna sababu ya msingi ya kuwa hapa tulipo,na kwa kuwa tunatambua kuwa hatujitendei haki sie wenyewe kwa kung’ang’ania kuwa katika nafasi isiyo yetu ni lazima tuchakarike sasa.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI

Mambo yakoje huko nyumbani?Natumaini kila mmoja anawajibika kwa namna yake katika ujenzi wa Taifa.

Kuna jamaa mmoja hapa anaitwa David Cameron.Huyu ni kiongozi wa chama cha wahafidhina (Conservative Party).Nia yangu si kuzungumzia wasifu wake,bali nataka nimlinganishe na mwanasiasa nyota wa huko nyumbani kwa muda huu,au kwa lugha ya “kwa mama” tunaweza kumuita “a man of the moment.” (kwa tafsiri ya haraka, “staa wa muda huu”).Nadhani msomaji mpendwa umeshajua ni nani ninayemzungumzia.Lakini hapa namuweka kando kidogo ili nikupashe kuhusu huyo Bwana Cameron na chama chake cha Conservatives (au Torry,kama kinavyojulikana hapa).Kwa tafsiri nyepesi hawa Conservatives ni watu wenye mrengo wa kulia na ndio wapiga kelele wakubwa kuhusu sera za uhamiaji na nyinginezo ambazo zinawagusa makabwela hususan wale ambao si wazawa wa hapa.Pengine jeuri kubwa ya wahafidhina hawa inatokana na uwezo wao wa kifedha.Fedha wakati mwingine huwa na tabia ya kumfanya binadamu asiwafikirie wenzie aliowazidi kiuwezo,na aghalabu anapowafikiria basi huwa ni kwa manufaa yake binafsi.

Kuibuka kwa Cameron kulichochewa zaidi na mwelekeo usioridhisha wa chama chake katika chaguzi mbalimbali.Wachambuzi wengi wa mambo ya siasa walikuwa wanahusisha mwenendo mbaya wa chama hicho na kile kinachoitwa kuwa “out of touch.”Nitafafanua.Chama kilicho “out of touch” ni kile ambacho machoni mwa watu wa kawaida kinaonekana kama hakijihusishi na maslahi ya walio wengi.Kwa mfano,hawa wahafidhina kwa miaka kadhaa wamekuwa wakikumbatia zaidi Waingereza weupe hasa wale wa tabaka la juu na la kati huku wakiwasahau wale wa tabaka la chini pamoja na Waingereza wengine ambao ni “wakuja” (kwa mfano wale wenye asili ya Asia,Caribbean,Afrika,n.k).Pia wamekuwa wakiwaona wageni (ikiwa ni pamoja na wanafunzi wanaochangia mamilioni ya paundi kwenye uchumi wa nchi hii) kama watu wanaokuja kuharibu uchumi,utamaduni na mazingira ya hapa.

Baada ya Waziri Mkuu wa mwisho kutoka Conservative kushika wadhifa huo,John Major,alipoangushwa na Tony Blair mwaka 1997,chama hicho kimebadilisha viongozi kadhaa lakini bila mabadiliko hayo kuwanufaisha kwenye chaguzi mbalimbali.Ndipo katika mchakato huo alipoibuka Bwana Cameron,kijana (ana miaka 40 tu),ana mvuto na haiba ya kutosha.Huyo bwana aliamua kuwapa wenzake kitu “laivu” kwamba chama chao hakina mvuto kwa wapiga kura,kinaonekana kuwa kiko zaidi kwa maslahi ya mabwanyenye kuliko makabwela,na hakizungumzi “lugha ya mtu wa kawaida mtaani.”Kuna mengi ya kumzungumzia huyo bwana lakini kilichonisukuma kuandika makala hii ni jinsi navyomuona anafanana na Jakaya Kikwete.Ukiachilia ukweli kwamba wote ni handsome lugha wanayoongea inafanana:lugha inayomgusha mtu wa kawaida na sio makundi flani tu katika jamii hususan wale wenye nguvu za kiuchumi.

Jakaya amenukuliwa mara kadhaa akiwausia viongozi wenzie kwamba wako madarakani kuwahudumia hao waliowaweka madarakani.Sio dhambi kuwa karibu na matajiri lakini ukaribu huo usiwe kwa ajili ya kuwaumiza wasio nacho.Utajiri sio dhambi,na kuna matajiri kadhaa (mfano Mzee Mengi huko nyumbani au Bill Gates huko Marekani) ambao utajiri wao umekuwa faraja kwa mamilioni ya wale wasio nacho.Matajiri wa aina hii ni muhimu kwao kuwa karibu na viongozi wa serikali,vyama vya siasa na taasisi nyingine kwa vile ni kwa ukaribu huo ndio miradi mbalimbali wanayoifadhilia inaweza kuwa na manufaa kwa wananchi.

Juzijuzi nilimwona Bwana Cameron kwenye luninga akiwa kwenye mtaani wakati wa kampeni za chama chake kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kwa upande wa England.Jinsi alivyokuwa akijichanganya na watu ilitosha kabisa kumfanya hata mtu aliyekuwa akikichukia chama cha wahafidhina afikirie upya.Siku chache baadae nikasoma kwenye mtandao kuwa Jakaya ameweka historia kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kutembelea wafungwa magerezani.Yalipotokea mauaji ya kutatanisha ya wale wachimba madini wa Mahenge hakukawia kuunda tume,na kinyume ya ilivyozoeleka mara baada ya kupewa ripoti na tume akaweka matokeo hadharani.Aliporejea tu kutoka Kusini mwa Afrika hakukawia kwenda kuwaona majeruhi wa tukio la uporaji wa fedha za NMB pale Ubungo,na kutoa maagizo papo hapo.Lakini si Jakaya pekee bali hata “luteni” wake Lowassa.Ghorofa lilipoanguka Keko hakusubiri kuletewa taarifa bali alikwenda kujionea mwenyewe na kuchukua hatua hapohapo, “mafuriko” yalipoielemea Sinza hakukawia kwenda kushuhudia hali ilivyo na kuwaamuru wahusika wachukue hatua za haraka.

Laiti kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya aliyokuja nayo Kikwete itaweza kufikia hatua ya kuigwa na viongozi kuanzia ngazi ya serikali ya mtaa,kata,tarafa,wilaya na mkoa,basi muda si mrefu Bongo itakuwa sehemu ya neema.Na mwenyewe Jakaya amekuwa akisema kuwa Tanzania yenye neema inawezekana.Enyi viongozi mliolala hebu amkeni,msisubiri kuamshwa.Jisikieni aibu pale mnapokwenda kinyume na spidi ya kiongozi wenu mkuu.

Alamsiki

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.