Showing posts with label WATANZANIA. Show all posts
Showing posts with label WATANZANIA. Show all posts

20 Feb 2008

Ukumbi maarufu wa mtandao (web forum) kwa Watanzania,JAMBOFORUMS,hauko hewani.Kwa mujibu wa taarifa kutoka KLH NEWS,wanachama wawili wa Jamboforums walikuwa wakishikiliwa na polisi kwa tuhuma zinazoashiria kuhusishwa na ushiriki wao kwenye Ukumbi huo.Kwa habari zaidi,soma HAPA na HAPA

22 Aug 2006

KULIKONI UGHAIBUNI-21

Asalam aleykum,

Leo nina jambo muhimu sana kuhusiana na maslahi ya Taifa letu.Nawaomba wasomaji wapendwa tuwe pamoja kwa makini ili tusipoteane njiani na hatimaye kuleta tafsiri potofu ya ninachotaka kuzunguzia.Natanguliza rai-au niite tahadhari-kwa vile mada yangu ya leo ni nyeti,na ni kuhusu suala ambalo mara nyingi limekuwa likikwepwa na watu wengi.Lakini kabla sijaingia kwa undani,nielezee uzoefu wangu mimi mwenyewe katika suala hilo.

Kwa wafuatiliaji wa makala hii watatambua kwamba mara zote huwa naanza na asalam aleykum.Nimezowea sana kuwasalimia ndugu zangu kwa namna hiyo.Pengine ni kwa vile nimewahi kukaa miji ambayo salamu hiyo inatumika sana,au pengine wengi wa marafiki zangu ni Waislam.Robo ya elimu yangu ya msingi niliipata mkoani Kigoma katika kitongoji cha Ujiji.Nakumbuka kuna wakati flani katika darasa nililokuwa nasoma tulikuwa Wakristo watatu tu na waliosalia (nadhani zaidi ya silimia 90) walikuwa Waislam.Niliwahi kufundisha sekondari flani mjini Tanga na takribani robo tatu ya wanafunzi wangu walikuwa Waislam pia.Na nikipiga hesabu ya harakaharaka,katika marafiki zangu kumi bora saba ni Waislam.Hata siku moja,tangu nikiwa Kigoma,Tanga,Dar na kwengineko sikuwahi kujiona nimezungukwa na watu tofauti nami ambaye ni Mkristo Mkatoliki.Wanafunzi wenzangu,wanafunzi niliowafundisha na marafiki zangu walinichukulia kama Mtanzania mwenzao japo tulikuwa tunatoka madhehebu tofauti.Na hivi karibuni nilipokuja huko nyumbani kwa utafiti wa PhD nayosoma,wengi wa niliohojiana nao walikuwa Waislam.Sikuwahi kupata matatizo yoyote hata pale nilipokutana na wanaoitwa mujahidina.Katika levo ya familia,kaka-binamu yangu mmoja ambaye ni Mkatoliki wa kwenda kanisani kila Jumapili ana mke ambaye ni Mwislam wa swala tano.Uzoefu wangu huo mdogo unatoa picha moja muhimu:Watanzania tumekuwa tukijichanganya sana bila kujali tofauti zetu za kidini.Nikisema kujichanganya namaanisha kujumuika pamoja na sio vinginevyo.

Kuanzia kwenye miaka ya 80 kulianza kujitokeza dalili zilizoashiria kwamba mambo si shwari sana katika eneo la dini nchini.Tunakumbuka uvunjaji wa mabucha ya nguruwe,matukio kwenye msikiti wa Mwembechai,mihadhara ya kidini,suala la Ustaadh Dibagula na mengineyo.Wapo waliosema kwamba kulikuwa na kikundi cha watu wachache kilichokuwa kinachochea vurugu za kidini kuganga njaa zao.Wapo pia waliokuwa wanadai kuwa vurugu za kidini zilikuwa na sura ya kisiasa huku mara kadhaa chama cha CUF kikibebeshwa lawama.Yayumkinika kusema kuwa japo viongozi wetu walikuwa wakikemea vurugu hizo hakukuwa na jitihada za makusudi za kubaini chanzo hasa ni nini.Wanataaluma wetu nao kwa namna flani wamekuwa wakilikwepa suala hili pengine kwa vile linagusa hisia za wengi au pengine kutokana na hisia kwamba matokeo ya tafiti zinahusu migogoro ya kidini huweza kuchangia kuleta utata zaidi badala ya ufumbuzi wa matatizo.Mwalimu wangu wa zamani katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Dr John Sivalon alichapisha kitabu ambacho kilitokana na thesis yake kuhusu mahusiano kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Tanzania.Bila kuingia kwa undani kujadili kitabu hicho cha mhadhiri huyo wa Kimarekani ambaye pia ni Padre,ukweli ni kwamba kimekuwa ni nyenzo muhimu katika mihadhara na mijadala ya kidini nchini,japo sina hakika kama kimesaidia katika kuwa sehemu ya utatuzi wa matatizo yaliyopo.

Hebu sasa niingie kwenye ishu yenyewe.Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mijadala inayoendelea kwenye forums mbalimbali za Watanzania kwenye internet.Suala hilo ambalo limegusa hisia zangu ni madai kwamba Rais Jakaya Kikwete amekuwa akiwapendelea Waislam katika teuzi mbalimbali anazoendelea kuzifanya tangu aingie madarakani.Na pengine kinachotajwa zaidi ni ule uteuzi wake wa kwanza wa mabalozi wa mwanzo (akina Adadi na wengineo) ambao kwa mujibu wa majina yao wote ni Waislam.Pengine bila kudadisi sifa za walioteuliwa,wanaolalamika wakaangalia dini zao.Teuzi nyingine nazo zimeendelea kuzua mijadala isiyo rasmi japo sina uhakika kama na huko nyumbani nako hali ni kama hii niliyoiona kwenye mtandao.Ila niliona kwenye mtandao makala mbili tofauti ambazo nadhani zilitolewa kwenye magazeti ya huko nyumbani ambapo mwandishi mmoja mkongwe alikuwa akijibu hoja za mwanasiasa flani ambaye nadhani pia ni kiongozi wa kidini,na mada yenyewe ilikuwa ni hiyohiyo eti Kikwete anawapendelea Waislam.

Mimi siamini kabisa kwamba yeyote kati ya aliyeteuliwa-iwe kwenye uwaziri,unaibu waziri,wakuu wa mikoa,wakurugenzi na kadhalika-wamepewa dhamana zao kutokana na Uislam au Ukristo wao.Unajua kwa miaka mingi sisi tumekuwa Watanzania kwanza halafu ndio vinafuatia vitu kama Ukristo au Undamba wangu.Na ndio maana kule Ujiji,Tanga,Dar na kwingineko nilikokuwa sikuwahi kupata matatizo na waliokuwa karibu nami kwa vile cha muhimu kwetu haikuwa dini au kabila bali urafiki au mahusiano yetu kikazi.Na naamini kabisa kuwa Kikwete ni Mtanzania kwanza,na anaongoza Watanzania kwa misingi ya umoja wao na sio tofauti za kidini,na kwa mantiki hyo hata anapochagua viongozi haangalia dini bali sifa za wateuliwa.

Hata hivyo,kuna matatizo kadhaa yanayohusiana na suala la dini nchini.Tusijidanganye kwamba hatufahamu kuwa kumekuwa na manung’uniko miongoni mwa Waislam kuhusu usawa katika sekta ya elimu na ajira.Iwapo chanzo cha tatizo hilo ni sera za kibaguzi za wakoloni au kuna mbinu za makusudi za kuchochea matatizo hayo,hiyo sio muhimu sana kama ilivyo kwa umuhimu wa serikali,taasisi mbalimbali,wanataaluma na wananchi kwa ujumla kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.Matokeo ya awali ya utafiti wangu unaohusu harakati za Waislam nchini yanathibitisha kwamba matatizo yapo na yanajulikana ila kinachokosekana ni jitihada za makusudi za kupata ufumbuzi wa kudumu.Habari nzuri ni kwamba,hilo (la kupata ufumbuzi) linawezekana iwapo busara zitatumika na wadau kujumuishwa kwa karibu.Namalizia kwa kusisitiza kwamba wanaoleta madai ya udini wanatumia haki yao ya kikatiba kutoa mawazo yao,japo siafikiani nao.Hivi mtu anapooa au kuolewa na mtu anayetoka naye dini moja anaitwa mdini?Hapana.Kitakachojadiliwa hapo ni sifa za huyo mume au mke.Hivyohivyo,Jakaya hawezi kuitwa mdini pindi akichagua Muislam kama yeye alimradi ana sifa zinazostahili.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Naanza makala yangu kwa kuelezea majonzi makubwa niliyonayo kufuatia kifo cha mwanataaluma maarufu huko nyumbani,Profesa Seith Chachage.Majonzi yangu yanachangiwa na ukweli kwamba mimi ni miongoni mwa wanafunzi wake wa zamani hapo Mlimani.Mungu ndiye mtoaji na yeye ndiye mchukuaji kama Maandiko Matakatifu yanavyosema,lakini pengo aliloliacha msomi huyu aliyebobea ni vigumu kuzibika.Nimepitia tovuti mbalimbali na nimegundua kuwa marehemu alikuwa kipenzi cha wengi hasa wale wenye uchungu na Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.Kwa tuliomjua Profesa Chachage tutakumbuka jinsi alivyokuwa akichanganya usomi wake na kauli za utani.Yaani ilikuwa vigumu kuchoka kusikia mhadhara wake.Kwa tunavyowajua wasomi wetu ni nadra kumkuta mmoja wao akipenda vitu kama bongofleva,lakini nimesoma kwenye tovuti moja kwamba marehemu alikuwa anapenda muziki wa kizazi kipya na inasemekana aliweza hata kuimba verses za wimbo maarufu wa TID uitwao Zeze.Mungu ailaze ahali pema roho ya marehemu Profesa Chachage,Amen.

Alhamisi ya tarehe 13/06 mwaka nilisoma kwenye tovuti ya gazeti la Uhuru habari iliyonukuu Rais mstaafu Benjamin Mkapa akisema kwamba “katika baadhi ya mashirkika kama ATC serikali iliingia mikataba bila kuwa na tathmini halisi ya faida ambayo ingepata kwenye mashirika hayo.”Hizi si habari njema hasa ikizingatiwa kwamba serikali haitegemei wataalamu wa njozi kujua kama mkataba flani una manufaa au la bali inapaswa kuwatumia wataalam wake kuhakikisha kuwa kinachofanyika sio bahati nasibu ila ni kitu cha maslahi kwa Taifa.Tunaweza kutomlaumu Chifu MangungO alisaini mikataba feki na akina Karl Peters nyakati za ukoloni kwa sababu enzi hizo hakukuwa na wataalamu wa kupitia mikataba na kujua kama ina manufaa au la.Lakini zama hizi hali ni tofauti.Pale serikali inapoona kwamba jambo flani liko nje ya uwezo wake ina uwezo wa kutafuta na kupata uhakiki flani kutoka nje ya nchi.Yaani hapo namaanisha kwamba yapo makampuni kadhaa ya kimataifa ambayo yanaweza kutoa huduma ya ushauri kwa serikali iwapo itaonekana kwamba wataalam wetu wa ndani wameshindwa kazi hiyo.Hivi inawezekanaje mtu akaingia mkataba bila kujua faida yhalisi ya mkataba huo?Utapangishaje nyumba yako kama huna hakika kuwa kwa kufanya hivyo wewe mwenyewe au familia yako mnaweza kuishia kulala gesti hausi?Na je inapobainika kwamba kuna tu flani,kwa sababu anazozijua yeye,alisaini mkataba usio na faida kwa Taifa,tunafanyaje?Suala hapa sio kunyooshena vidole bali ni kuhakikisha kuwa makosa ya aina hiyo hayajirudii.Na njia nyepesi ya kufanya hivyo ni kuwachukulia hatua wale waliofanya makosa hayo-iwe walifanya kwa makusudi,uzembe au kutojali maslahi ya nchi yetu.

Nilishawahi kuandika huko nyuma kwamba kuna watu hawana uchungu na Taifa letu,na hawa ni pamoja na hao wanaosaini mikataba kama ile ya Chifu Mangungu utadhani wakati wanasaini mikataba hiyo walikuwa bwii(wamelewa) au wamesainishwa wakiwa usingizini.Marehemu Chachage na baadhi ya wasomi wengine wa nchi hii walijikuta wakitengeneza maadui kila walipojitahidi kukemea mambo yanayoendana kinyume na maslahi ya Taifa.Kuna watu hawapendi kuambiwa ukweli hata pale wanapoharibu na si ajabu makala hii ikapata upinzani wao.Lakini hiyo haitatuzuwia sie wenye uchungu na nchi yetu kusema yale yanayotupeleka pabaya.

Nimesikia kuna kampuni ya Kisauzi Afrika imepewa haki za utafutaji mafuta huko nyumbani.Pia kuna tetesi kwamba nchi yetu ina utajiri wa Uranium.Mungu akitujalia,siku moja na sisi tutakuwa na sauti kwenye siasa za kimataifa kwa vile mafuta ni silaha,ukiwa nayo lazima utaheshimika.Lakini bila mipango madhubuti utajiri hio unaweza kuwa kama laana kwa Taifa kama letu lililozowea amani.Huko Nigeria kumekuwa na matukio kadhaa ya vurugu ambazo kimsingi zinatokana na ukweli kwamba wenye ardhi (wananchi) wanaishia kuona tu mabomba ya mafuta na magari ya thamani kwa wale wanaowatumikia wenye makampuni ya mafuta ya kutoka nje,huku walalahoi wakizidi kuwa masikini.Mwanafalsafa Karl Marx aliwahi kusema kuwa masikini hana cha kupoteza anapoamua kupigania haki yake.Watu hawawezi kuendelea kuwa kimya wakati utajiri wao wa asili kwenye nchi yao unawanufaisha wachache kutoka nje na wapambe wao wanaosaini mikataba hewa.

Naomba ieleweke kwamba sizilaumu serikali za awamu zilizotangulia kuwa mikataba yote zilizoingia ilikuwa bomu.Kilio changu hapa ni kwenye hiyo mikataba ya iliyosainiwa ndotoni.Nafahamu kwamba wataalamu wazalendo wanatoa ushauri mzuri tu kabla ya mikataba kusainiwa lakini tatizo linakuja pale maslahi binafsi yanapowekwa mbele ya maslahi ya Taifa.Kwa kuwa mtu ana mamlaka ya kupuuza ushauri wa kitaalamu basi anatumia fursa hiyo kujifanya madudu kana kwamba madhara ya anachokifanya hayatamgusa kwa namna flani.

Naamini serikali ya Awamu ya Nne haitawalea wazembe wanaotaka kutulostisha.Narudia kusema kwamba sisi sio masikini wa namna tulivyo kwa sababu tuna raslimali za kutosha ambazo zinaweza kabisa kutuweka pazuri.Tunachopaswa kuelewa ni kwamba miaka 25 au 50 ijayo vizazi vya wakati huo vinaweza kutushangaa sana pale vitakapokuta kila kitu kimeuzwa na faida ya mauzo hayo haionekani.Inaweza kuwa vigumu sana kwa walimu wa somo la Historia wa wakati huo kuwaelewesha wanafunzi wao kuwa tofauti na mikataba feki ya kina Karl Peters na baadhi ya machifu wetu,mikataba iliyobomoa nchi yao ilifanywa na Watanzania haikuwa ya kilaghai bali ni sababu ya kitu kidogo (sijui wakati huo watakuwa wanatumia msamiati gani kumaanisha rushwa),

Alamsiki

18 Jun 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Hivi umeshawahi kuulizwa swali moja zaidi ya mara mia na kila unapoulizwa hujiskii kulizowea swali hilo?Pengine imeshakutokea.Mimi imekuwa ikinitokea mara nyingi zaidi ya ninavyoweza kukumbuka.Ilianza nikiwa huko nyumbani.Kabila langu ni Mndamba,natokea Ifakara mkoani Morogoro.Sio siri kuwa Wandamba sio kabila maarufu ukilinganisha na makabila mengine ya mkoa naotoka,kwa mfano Waluguru au Wapogoro.Kwa hiyo kila nilipokuwa naulizwa “hivi wewe ni kabila gani” na mimi kujibu “mie Mndamba” mara nyingi swali lililofuata ni “hivi Wandamba wanatoka mkoa gani?”Au wakati mwingine nilipoulizwa mkoa naotoka na kujibu Morogoro,wengi walipenda kudhani mimi ni Mluguru.Niliposema hapana,wangeniuliza iwapo ni Mpogoro.Sikuwalaumu kwa vile mara nyingi jina la mkoa unaotoka huwa linahusishwa na kabila kubwa au maarufu katika mkoa huo.Ukisema unatoka Mwanza,watu watahisi wewe ni Msukuma,ukitoka Songea watu watahisi wewe Mngoni,au Tabora watahisi wewe Mnyamwezi,na kadhalika.

Nilipokuja huku Ughaibuni swali likageuka kuwa “wewe unatoka nchi gani?”Mara nyingi napojibu “natoka Tanzania” swali linalofuata ni “hivi Tanzania iko wapi?”Wengine wanajua iko Afrika lakini hawana uhakika ni sehemu gani katika bara hiko lenye nchi zaidi ya hamsini.Kuna wakati huwa nawalaumu wanaoniuliza swali hilo kwamba hawakuwa makini kwenye somo la Jiografia,lakini yayumkinika kusema kuwa hata kama ulipata A kwenye somo hilo sio rahisi kujua kila nchi ilipo kwenye ramani ya dunia,kama isivyo rahisi kwa kila Mtanzania kujua Wandamba wanatoka mkoa gani.Hata hivyo,kila napoulizwa ilipo Tanzania,huwa natumia fursa hiyo kufanya kazi ya wenzetu tuliowapa majukumu ya kuitangaza nchi yetu kwa kueleza kuwa nchi hiyo “iko kusini mwa Kenya na Uganda,mashariki ya DRC,Rwanda na Burundi…”,na kadhalika.Wakti mwingine natumia vivutio vyetu kujibu swali hilo,yaani nasema kuwa “Tanzania ndipo ulipo Mlima Kilimanjaro,au Ziwa Victoria,au Mbuga ya Selous…”

Wakati sote tunajua kuwa ni vigumu kwa kabila Fulani kufanya kampeni ya kujitangaza (na jitihada kama hizo zikifanyika utaambiwa unaleta ukabila) kila nchi ina jukumu la kujitangaza yenyewe.Inauma ninapoangalia kwenye runinga na kuona matangazo kama hili hapa: “mtoto huyu anahitaji sana msaada wako…anapenda kujiendeleza na elimu lakini anatoka Tanzania,moja ya nchi masikini sana duniani…kwa kutoa paundi tatu kwa mwezi unaweza kuwasaidia watoto kama huyu…”Yaani nchi yetu inapata nafasi ya kusikika lakini sio kwa sifa nzuri bali umasikini wake.Na huwezi kuwalaumu wanaotoa matangazo ya aina hiyo kwa kuwa wanafanya hivyo kwa nia nzuri,na sio jukumu lao kuitangaza nchi yetu kwa mtizamo wa kuvutia watalii au vivutio vilivyopo huko.Hiyo ni kazi ya Watanzania wenyewe.

Naamini kuna watu wana majukumu ya kuitangaza nchi yetu.Hebu nikupe mfano.Uganda inadhamini kipindi Fulani kwenye kituo cha televisheni cha CNN International cha Marekani.Zambia nao wanatoa matangazo ya kuitangaza nchi yao kwenye kituo hicho na kuwakaribisha wageni waende kushuhudia Maporomoko ya Victoria.Hata Malawi,Rwanda na Burundi nao hawako nyuma,kwani nimeshaona matangazo yao kwenye gazeti maarufu duniani la TIME.Lakini sie tuko nyuma katika eneo hili.Pengine kuna watu wanaona sio muhimu kujitangaza kwa vigezo kwamba “chema chajiuza kibaya chajitembeza.”Tunachopaswa kufahamu ni kwamba katika zama hizi za ushindani wa kuvutia watalii (na hata wawekezaji wa kweli) ni muhimu sana kuitangaza nchi yako.Ukitaka kuhakikisha nayosema sio utani ingia kwenye internet na tafuta habari kuhusu vivutio vilivyopo nchini kwetu.Ni dhahiri utagundua kuwa taarifa zilizopo ni chache,na hata hizo chache hazijitoshelezi,na mara nyingi huwa zimewekwa na wasio Watanzania.Kuna watu wengi wanaoamini kuwa Mlima Kilimanjaro uko Kenya kwa vile nchi hiyo imekuwa ikiutangaza Mlima huo kama uko kwake,na sie tumekaa kimya.Ukienda kwenye tovuti ya Bodi ya Biashara za Nje (BET) wao wanaonekana wako bize zaidi na Maonyesho ya Sabasaba.Nilipotembelea tovuti yao leo ilikuwa inasema iko kwenye matengenezo lakini inakupeleka kwenye kiungo (link) ya Maonyesho ya 30 ya Kimataifa ya Dar Es Salaam (DITF),pengine kuonyesha kuwa Maonyesho hayo (ambayo ni ya mara moja tu kwa mwaka) ni muhimu zaidi kwao kuliko kuitangaza nchi yetukila siku.Angalau Bodi ya Utalii wamejitahidi kiasi japokuwa tovuti yao haina habari za kutosha kuhusu vivutio tulivyonavyo.Tuna Kituo cha Biashara (Tanzania Trade Centre) hapa Uingereza,lakini tovuti yake ni kama imeandaliwa haraka haraka kwa vile taarifa zilizopo humo sio za kutosha sana.Wahusika wasikasirike kusoma haya nayoandika kwa sababu tumewakabidhi dhamana ya kuitangaza nchi yetu.Badala ya kuchukia kukosolewa wanapaswa waone hii kuwa ni changamoto kwao.

Kilio changu kingine ni kukosekana kwa AIR TANZANIA ya Watanzania.Kama wenzetu Kenya wameweza kwanini sisi tushindwe?Angalia Wahabeshi wa Ethiopia wanavyoweza kuchuana na mashirika makubwa ya ndege duniani na kujiingizia mapato makubwa kupitia sekta ya usafiri wa anga na Ethiopian Airlines yao.Kwa kurusha Air Tanzania “the Wings of Kilimanjaro” tulikuwa tunaitangaza nchi yetu na wakati huohuo kuujulisha ulimwengu kuwa Mlima Kilimajaro uko kwetu.Tuna vivutio vingine vingi vya kuvitangaza huku nje ikiwa ni pamoja na moja ya hifadhi kubwa kabisa duniani,Selous,na ziwa la pili kwa ukubwa duniani,Victoria.

Tukubali kwamba hatujajitahidi vya kutosha na tusisubiri kuulizwa.Hatuna sababu ya msingi ya kuwa hapa tulipo,na kwa kuwa tunatambua kuwa hatujitendei haki sie wenyewe kwa kung’ang’ania kuwa katika nafasi isiyo yetu ni lazima tuchakarike sasa.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI

Asalam aleykum.

Hapa Uingereza kuna chama cha siasa kinachoitwa British National Party au kwa kifupi BNP.Hiki ni chama kinachofuata siasa za mrengo wa kulia kabisa,far right kwa “lugha ya mama.”Siasa za namna hiyo ndio zilizokuwa zinahusudiwa na Manazi chini ya Hitler na Mafashisti chini ya Mussolini.Hawa jamaa wa BNP ni wabaguzi waliokithiri.Majuzi wakati wa uchaguzi mdogo huko England mmoja wa watu muhimu katika BNP,Dokta Phill Edwards (jina lake halisi ni Stuart Russell) alizua mjadala mkubwa kuhusu siasa za chama hicho pale alipotoa matamshi ya kuchefua dhidi ya watu weusi.Alirekodiwa kwa siri na kituo cha televisheni cha Sky akisema kuwa watu weusi wana IQ (uwezo wa akili) ndogo,na watoto weusi wakikua sanasana wataishia kukaba watu (vibaka au majambazi).Aliendelea kusema,hapa namnukuu “suala hapa sio kama tunawachukia watu weusi bali ni kama wao ni tishio kwa amani,utulivu na utamaduni wa jamii ya Kiingereza…watoto weusi wakikua watanyonya uchumi wetu na kujaza magereza yetu na pengine kukukaba…huko Afrika kusini mwa jangwa la Sahara hakuna ustaarabu wowote,na hakuna maendeleo ya sayansi…”Kwa kweli ilikuwa inauma kuangalia upuuzi huo kwenye runinga,lakini ni hali tunayoishi nayo hapa kila siku.

Miongoni mwa mambo “halali” yanayowapa nguvu wabaguzi hawa ni vitendo vya baadhi ya wageni na hasa weusi kujihusisha na uhalifu au mambo mengine yasiyofaa katika jamii.Kwa wao,samaki mmoja akioza basi wote wameoza,yaani mtu mmoja mweusi akihusika kwenye uhalifu basi watu wote weusi ni wahalifu.Na kwa BNP sio weusi tu wanaolengwa.Chama hicho kilipata “pumzi” ya kutosha kupinga sera za uhamiaji na ujio wa wageni hapa Uingereza baada ya matukio ya kujilipua mabomu kwa kujitoa mhanga mjini London mwezi Julai mwaka jana. “Vita” ya BNP dhidi ya wageni ikapamba moto na sasa walengwa wakuu wakawa watu wenye asili Asia (hasa Wapakistani).Watatu kati ya waliojilipua mabomu ya muhanga walikuwa Waingereza wenye asili ya Pakistani,na kwa chama hicho cha kibaguzi hiyo ilikuwa sababu tosha ya kuwajumuisha watu wenye asili ya Pakistani na Asia kwa ujumla,na wageni wengine kuwa ni tishio kwa maisha ya Taifa hili.

Huko nyubani moja ya mambo ambayo Watanzania tunajivunia sana ni jinsi “tunavyojichanganya” bila kujali kabila,dini au jinsia.Nikisema “kujichanganya” namaanisha ushirikiano,upendo na maelewano,na sio kukosa msimamo kama maana halisi ya neno ilivyo.Niliwahi kusikia stori flani siku za nyuma inayohusu timu moja ya soka kutoka nchi flani ya jirani.Wachezaji wa timu hiyo walipokuwa wanafanya mazoezi walikuwa wanavuta umati mkubwa wa wakazi wa mji wa Arusha,ambako kulikuwa na michuano ya kimataifa.Kilichokuwa kinawashangaza wachezaji hao ni jinsi watazamaji walivyokuwa “wanajichanganya” kana kwamba ni watu wa kabila moja.Nchi wanayotoka wachezaji,kama zilivyo nchi kadhaa za Afrika,inasifika sana kwa ukabila.Inasemekana katika nchi hiyo ni nadra watu wanaotoka makabila tofauti kuwa marafiki wa dhati.Sasa walipoona baadhi ya watazamaji “wanagongeana sigara” na kutia stori kana kwamba wanaishi nyumba moja,ilikuwa ni jambo la kushangaza sana kwao.Huenda waliondoka Arusha wakiwa na fundisho flani.
Rafiki yangu mmoja,Profesa Tunde Zack-Williams,aliwahi kuniambia kwamba napaswa kujivuna kuwa Mwafrika kutoka Tanzania.Alinieleza kwamba kwa uzoefu wake mwenyewe kama mwanataaluma na Mwafrika,Watanzania ni watu waliojaliwa na “karama” ya mshikamano,upendo na umoja,na wanawaheshimu sana wageni bila kujali wanatoka wapi.Profesa huyo ni mzaliwa wa Sierra Leone,nchi ambayo imeathiriwa sana vita vya wenyewe,na amekuwa akiwasaidia sana kitaaluma vijana wa Kiafrika.Rafiki yangu mwingine anayetoka Sudan aliniambia kwamba alishangaa sana alipofika Tanzania kwa mara ya kwanza,kwa sababu licha ya nchi yetu kuwa na makabila zaidi ya 120 hakuona dalili zozote za watu kubaguana kwa misingi ya kikabila.

Hata hivyo,katika siku za hivi karibuni kumeanza kujitokeza dalili za baadhi ya watu kuchoshwa na “ujiko” huo tulionao ndani na nje ya Afrika.Binafsi,nafanya utafiti unaohusu masuala ya dini na siasa.Sintoongelea sana utafiti huo kwa vile bado “uko jikoni” lakini miongoni mwa matokeo yake ya awali ni dalili kuwa kuna watu au vikundi flani vya jamii vinavyotumia dini kujenga mpasuko katika jamii kwa manufaa yao binafsi.

Kibaya zaidi ni dalili kwamba baadhi ya Watanzania ambao tuna haki ya kuwaita “wageni” wanapoanza kujiingiza kwenye kuleta chokochoko kwenye jamii yetu iliyozowea amani.Siku zote tumekuwa tukiheshimiana na kupendana bila kujali kuwa flani alizaliwa Ifakara au New Delhi.Lakini kama BNP inavyopata “nguvu halali ya kusema ovyo” pindi wageni “wanapoharibu” inaweza kufika mahali Watanzania wazawa wakaanza kujenga chuki dhidi ya wale ambao licha ya “ugeni” wao wanachochea mpasuko katika nchi yetu.Na si “wageni” tu bali hata wale wanaotumia nafasi zao za juu katika jamii kutukoroga.Waasisi wa Taifa letu walifanya kazi kubwa sana kutufikisha hapa tulipo,na nawausia Watanzania wenzangu tusifumbe macho pale wale tulikowakaribisha kwa upendo (na maswahiba zao) wanapoanza kutuletea dharau na chokochoko kwenye nchi yetu.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Mambo?

Siku chache zilizopita nilibahatika kuwa na maongezi na babu mmoja wa Kiskotishi ambaye kwa maelezo yake mwenyewe yeye ni “mkazi wa dunia nzima” (global citizen).Babu huyo anadai kuwa dunia ingekuwa mahala bora sana kama kusingekuwa na mipaka na sheria kali za uhamiaji.Na katika kutimiza azma yake ya kuwa mkazi wa dunia nzima anadai ametembelea takribani nchi 10 katika kila bara.Sijui kama alikuwa anasema ukweli au “ananifunga kamba” tu.Katika maongezi yetu hayo aligusia jambo flani ambalo liliniingia sana na ambalo ndio mada yangu ya wiki hii:UZALENDO.

Kwa mujibu wa babu huyo,enzi zao wakiwa vijana suala la uzalendo lilikuwa likitiliwa mkazo sana.Alidai kuwa japo kwa sasa hali ni tofauti kidogo lakini bado nchi nyingi za magharibi zinatilia mkazo sana suala hilo.Alieleza kwamba akiwa kijana babu yake alikuwa akimwambia kuwa mazingira mazuri watakayoyaweka wakati huo yatakuja kuvinufaisha zaidi vizazi vijavyo.Baba yake pia alikuwa akimweleza hivyo hivyo.Na yeye alipokuwa mtu mzima alikuwa akiwaeleza wanae hivyohivyo.Na sasa anasema amekuwa akitoa changamoto ya aina hiyohiyo kwa wajukuu wake.Furaha aliyonayo ni kwamba utabiri wa babu na baba yake umetimia.Maendeleo yaliyopo hivi sasa yamechangiwa na msingi mzuri uliojengwa karne kadhaa zilizopita.Na kilichowasukuma hao waliotengeneza misingi hiyo si kingine zaidi ya uchungu wao kwa taifa lao na vizazi vijavyo.

Huko nyumbani kuna tatizo kuhusiana na suala la uzalendo.Wapo wapuuzi fulani ambao wanaendesha mambo utadhani hakuna kesho au labda Tanzania haitakuwepo miaka 50 ijayo.Na hawa ndio baadhi yao waliripotiwa kutishia maisha ya waandishi wa KULIKONI na THIS DAY kwa sababu magazeti hayo yameapa “kula nao sahani moja” (kuwaweka hadharani).Hawa ni watu ambao hawana uchungu si kwa nchi yao tu bali hata kwa wajukuu zao.Ukweli ni kwamba mtu anayekula fedha iliyotolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule hana upeo wa kufikiria kwamba kwa kufanya hivyo huenda wajukuu wa mtoto wake wa mwisho watakaopaswa kwenda shule miaka 20 ijayo wanaweza kukosa nafasi hiyo kwa upuuzi uliofanyika mwaka 2006.Kuna watu wanafanya mchezo na maisha ya Watanzania wenzao kwa kutumia fedha za wenzao bila hata kuwashirikisha hao waliowekeza.Jamani,hata sheria za kawaida mtaani si kwamba bwana au bibi harusi mtarajiwa hawezi kutumia michango ya harusi yake mwenyewe pasipo kuwajulisha wanakamati?Sembuse hao ambao wamekabidhiwa fedha ambazo baadae wanapaswa kuzirejesha kwa wahusika!Nadhani mnaniapata hapo.

Wabadhirifu wa mali za umma na wala rushwa ni sawa na majambazi tu.Ni majambazi ambao silaha yao kubwa ni dhamana walizokabidhiwa kuwatumikia wananchi.Majambazi hawa wanachoiba sio fedha tu bali hata haki za Watanzania wenzao.Na kama walivyo majambazi wengine,hawa wakishahisi kuwa wanafahamika hukimbilia kutumia silaha kuu mbili:rushwa na vitisho.Kama gazeti linachimba maovu yanayofanywa na watu flani wasio na uchungu na nchi yao,basi waandishi wa gazeti hilo watafuatwa ili “wadakishwe kitu kidogo kuua soo.”Na itapoonekana kuwa gazeti hilo na waandishi wake wako ngangari katika kutetea maslahi ya Taifa na hivyo kukataa kuuza taaluma yao kwa kupokea rushwa basi hapo ndipo vitakapoanza vitisho.Sio huko nyumbani pekee ambako waandishi wa habari wanaovalia njuga kufichua maovu katika jamii wanakumbana na vitisho kutoka kwa wahusika.Mwaka 1996,Veronica Guerin, mwandishi wa habari wa kike huko Northern Ireland alipigwa risasi na kuuawa kutokana na makala za uchunguzi kuhusu biashara ya madawa ya kulevya nchini humo.Mwaka juzi,waandishi kadhaa wa magazeti ya Daily Record na Sunday Mail ya hapa Uingereza waliripoti kupokea vitisho kutokana na habari za uchunguzi walizokuwa wakiandika kuhusiana na magenge ya uhalifu.Kadhalika,mwaka jana waandishi wa habari wa magazeti kadhaa nchini Italia waliripoti kupokea vitisho baada ya kuripoti tuhuma za rushwa kuhusiana na klabu ya soka ya Genoa ya nchini humo.

Mifano hiyo michache inaonyesha ni jinsi gani watu waovu wanavyopenda kuendelea na maovu yao bila kubughudhiwa.Lakini haiwezekani watu wenye uchungu na nchi yetu wawaachie kufanya ufisadi wao wapendavyo.Naamini kila mzalendo anaelitakia mema Taifa letu atahakikisha kuwa wanahabari wanaosimama kidete kuwafichua wala rushwa na wabadhirifu hawabughudhiwi hata kidogo.Mjenga nchi ni mwananchi na mvunja nchi ni mwanachi pia.Tukiendelea kuwalea hawa majambazi wa mali na haki zetu basi tujue kuwa sio tu tunajitengezea “future” mbaya bali pia vizazi vijavyo vitatuhukumu kwa kuwaachia watu wachache wasio na uchungu na nchi yetu kutuharibia mambo.Tukiamua kwa nia moja tunaweza kuwadhibiti majambazi hao.

Alamsiki.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.