Showing posts with label TAIFA. Show all posts
Showing posts with label TAIFA. Show all posts

27 Jul 2007

Asalam aleykum,

Katika makala iliyopita niliwapa kituko kimoja kuhusu memba 7 wa kabineti ya Bwana Gordon Brown ambao walikiri hadharani kuwa walishawahi kuvuta bangi wakati wa ujana wao.Maendeleo zaidi (“update”) kuhusu stori hiyo ni kwamba hadi sasa idadi hiyo imefikia mawaziri 10.Lakini wananchi wanaonekana hawajashtushwa sana na “confessions” (vitubio…naamini niko sahihi hapa,au kuna neno jingine linalowakilisha wingi wa kutubu?BAKITA msaada tafadhali) pengine kwa sababu wananchi mawaziri hao watahukumiwa na utendaji wao wa kazi na sio historia zao za kale.Joji Bushi,huyu raisi wa sasa wa Marekani alikuwa “mtu wa matingas” (mlevi) kabla hajamrejea Bwana,lakini ulevi wake wa zamani haukuwa kikwazo kwa yeye kugombea nafasi hiyo ya juu kabisa ulimwenguni.Hata mie nadhani sio vema kumhukumu mtu kwa mambo alofanya zamani,alimradi anayofanya sasa yawe yanaridhisha.Wengi tunafahamu kwamba kuna wale waliosoma seminari na baadae kuingia kuutumikia umma,lakini si ajabu kukuta baadhi yao ni wala rushwa.Kwa maana hiyo,yayumkinika kusema kuwa bora kuwa mtu ambaye kwenye ujana wake alifanya mambo yasiyopendeza lakini sasa anafanya yale yanayotakiw,a kuliko yule ambaye CV yake ya ujana wake ni “supa” lakini kwa sasa anashiriki kuhujumu uchumi wa Taifa letu “changa” (nadhani neno “changa” sasa limeshapitwa na wakati maana taifa letu lina umri wa miaka 45,na naamini huko mtaani ukimwita mtu mwenye umri huo “mchanga” basi patakuwa hapakaliki hapo).

Kwa wale waliokuwa wanafuatilia stori ya Shambo,yule ng’ombe “mtakatifu” kwa Wahindu wa huko Skanda Valle,magharibi ya Wales,habari “latest” ni kwamba “ng’ombe-mungu” huyo amepelekwa mbele ya haki baada ya polisi 30 kuvamia hekalu lake na kumchukua kwa ajili ya kwenda kumchinja.Kwa wale ambao stori hii iliwapitia kando,ni kwamba Shambo alitakiwa kuuwawa baada ya kugundulika kuwa ana kifua kikuu (TB),na hivyo kuhatarisha afya za mifugo mingine katika eneo hilo.Lakini,Shambo si ng’ombe wa kawaida,bali ni “mungu” wa Wahindu,na waumini waliapa kuwa hawako tayari kuona “mungu” wao huyo akiuawa na binadamu.Baada ya mamlaka husika (DEFRA) kuwafahamisha waumini kuwa Shambo anapaswa kuuawa ili kuzuwia kuenea ugonjwa aliokuwa nao.Waumini walipinga uamuzi huo na hatimaye wakakata rufaa Mahakama Kuu ambapo amri ya kumuua “mungu” huyo ilitengeliwa.Lakini mamlaka husika zikaamua kukata rufaa Mahakama ya Rufaa ambapo iliamualiwa kuwa Shambo anastahili kuuawa.Zoezi la kumchukua “ng’ombe-mungu” huyo halikuwa jepesi kwani waumini walijitutumua kadri ya uwezo wao kuhakikisha kuwa Shambo hachukuliwi,na hapo ndipo ikabidi waletwe polisi kumaliza songombingo hiyo iliyochukua zaidi ya masaa 12,huku sakata zima kati ya waumini na DEFRA likiwa limedumu kwa wiki 12.Pengine kufanana kwa namba 12 katika matukio hayo kunaweza kuwa uhusiano na “umungu” wa ng’ombe huyo.

Tukiachana na “safari ya mwisho” ya ngombe-mungu Shambo,tuelekeze macho yetu huko nyumbani.Hebu ngoja kidogo.Kuna nchi inaitwa Guam.Je unaweza ku-guess iko wapi?Enewei,nilikuwa nachemsha kidogo ubongo wako.Nchi hiyo ni “koloni” la Marekani (well,iko chini ya mamlaka ya Marekani) na kwa mujibu wa sensa ya karibuni Guam ina wakazi 173,456.Bila kuingia kwa undani kuhusu jiographia,siasa na porojo nyingie kuhusu ka-nchi hako ambako ni kisiwa,ngoja nikudokezee kuhusu timu yake ya taifa.Hebu angalia matokeo ya mechi zake za hivi karibuni.Ilifungwa 10-0 na China,ikafungwa 15-1 na Hong Kong,na ikalambwa 9-0 na Korea ya Kusini.Kwa sasa inashilia nafasi ya 199 kwenye listi ya FIFA ya ubora wa soka duniani.Nafasi hiyo ndio ya mwisho kabisa,lakini habari njema kwa nchi hiyo ni kwamba haiko pekee kwenye nafasi hiyo kwani Djibouti, East Timor, Belize, the US Virgin Islands, Montserrat, American Samoa, Sao Tome e PrĂ­ncipe na Aruba pia zinashikilia kwa pamoja nafasi hiyo ya 199.Wahenga walisema kilio cha wengi ni harusi.Kocha wa timu hiyo anawalaumu zaidi wachezaji wake kwa tabia yao ya kuendekeza pati,kujichanganya na magelifrendi wao (au wake zao) na kuthamini zaidi mambo ya binafsi kuliko majukumu yao ya soka.Pia wachezaji wa timu hiyo wanashutumiwa kwa kuzembea mazoezi,na hata wanapofika mazoezini wengi wao huwa wamechoka kutokana na “kujirusha” (sio kujirusha kimazoezi bali “kiaina”).Kiungo wa timu hiyo,Alan Jamison,ameeleza kuwa mara kwa mara akiwa usingizini amekuwa akisumbiliwa na ndoto moja:anaota kuwa amefunga goli (la mpirani…) na uwanja unalipuka kwa mayowe.Kwa bahati mbaya kila asubuhi anapoamka anagundua kuwa timu yake haijapata na haitarajii kupata ushindi hivi karibuni.

Nimeizungumzia timu ya taifa ya Guam ili kutengeneza mazingira mazuri ya kuitupia madongo timu yetu ya iliyokwenda kutuaibisha huko Aljeria.Kulikuwa na umuhimu gani wa kuingia gharama ya kuwapeleka watalii hao kama walikuwa hawajajiaanda kwa mashindano?Enewei,mie najua kwanini walipelekwa hivyohivyo:POSHO.Posho ya safari.Linapokuja suala la posho ya safari usishangae chama cha mchezo wa bao au drafti (kwa mfano) kumpeleka mchezaji kipofu.Wanajua kabisa kuwa kipofu hawezi kucheza drafti au bao lakini hilo haliwasumbui viongozi hao kwani tayari watakuwa wamejipatia visenti vya kupeleka kwenye nyumba ndogo zao (utafiti usio rasmi umeonyesha kuwa asilimia kubwa ya fedha inayopatikana kwa rushwa au ubadhirifu inaishia kwenye nyumba ndogo).Viongozi walichagua wanamichezo wazembe wanastahili lawama nyingi zaidi kuliko wazembe hao waliokwenda kututia aibu huko Aljeria (ukiachia huyo mmoja aliyeambulia medali ya fedha).Nawalaumu zaidi viongozi hao kwa vile hawana cha kujitetea kwa kuchagua wanamichezo wasio na uwezo wa kutuletea ushindi.Angalau timu ya taifa ya Guam inaweza kujitetea kwani kijinchi chenyewe kina watu wachache zaidi ya wilaya ya Kinondoni.Tanzania ina watu zaidi ya milioni 30,na miongoni mwao ni wanamichezo wenye vipaji ambavyo aidha vinapuuzwa,haviendelezwi au vinaminywa na viongozi walafi wa madaraka na fedha lakini hawana hata chembe ya mawazo endelevu ya ushindi kwenye michezo.Kwenye nchi za kidikteta viongozi kama hawa wanaporejea kutoka mashindanoni wanapokelewa na karandinga kuelekea Segerea.

Majuzi tumesikia EWURA ikidai kwamba waziri Meghji kadanganya kuhusu uwezo wa mamlaka hiyo kuwabana wafanyabiashara wa mafuta.Sijui nani anasema ukweli kwani sijaona sheria iliyoanzisha mamlaka hiyo ila ni dhahiri kuwa kuna kitu hakiko sawia.Kuna umuhimu gani wa kuwa na mamlaka isiyo na uwezo wa kisheria katika kutekeleza majukumu yake?Au kwa mfano sahihi,kuna umuhimu gani wa kufuga mbwa mwenye mapengo na ambaye akisikia kelele za “mwizi,mwizi” anakwenda kujificha?Inanikumbusha mchapo mmoja nilowahi kusimuliwa huko Tanga kuwa baba mwenye nyumba mmoja alipoamshwa na mkewe na wanawe kuwa wamesikia watu wanavunja dirisha akaanza kulia na kuwaacha watoto hawajui la kufanya.Tukiachana na mifano hiyo,swali la muhimu ni kuwa hivi huku kurushiana mpira kunamsaidia vipi mwananchi wa kawaida?Nilishapendekeza huko nyuma kwamba njia nyepesi ya kudhibiti bei ya mafuta ni “kuchimba mkwara wa nguvu” kwamba atakayezidisha bei stahili ya mafuta atafutiwa leseni.La muhimu hapa sio kwamba amri hiyo itolewe na Meghji au EWURA,bali itekelezwe.Hakuna mfanyabiashara aliye tayari kufutiwa leseni na kwa hakika watatekeleza amri hiyo.

Mwisho,tumeambiwa na Profesa Maghembe kuwa wizara yake ina baadhi ya watendaji ambao kwa jina jepesi tunaweza kuwaita mafisadi.Hao ni pamoja na wale wanaoshiriki kwenye biashara ilopigwa marufuku ya kusafirisha magogo nje.Waziri anastahili pongezi kwa kuweka bayana uozo huo.Lakini unategemea nini kwenye wizara ambayo Severe alipewa uhamisho na akagoma kuhama na hadi leo bado anapeta?Prof Maghembe anasema amepeleka majina ya wahusika kwenye “ngazi za juu” kwa vile yeye hana uwezo kisheria kuwawajibisha.Pengine tunachopaswa kufahamu ni kuwa lini majina hayo yamewasilishwa huko ngazi za juu,na kwanini mafisadi hao bado wanaendelea kuuza maliasili zetu.Sintoshangaa kusikia mmoja wao akiitisha press conference kama ile ya gavana wetu na “kutupa somo la uzalendo.”Kwa vile mafisadi hawa wanajulikana,kuendelea kuwaacha madarakani ni sawa na kuwapa nafasi ya kufuja kwa kasi zaidi (kwa vile wanaelewa kuwa maamuzi kutoka “ngazi za juu” yanaweza kuwahamisha kutoka kwenye ulaji) na kuharibu ushahidi dhidi ya tuhuma zinazowakabili.Sheria ichukue mkondo wake ili kuzuia virusi vya ufisadi kusambaa zaidi (wanaoona mafisadi hao wanazidi kupeta wanashawishika kuiga ufisadi wao).

Nimalizie kwa kumpongeza Waziri Mwapachu kwa kuhitimisha bethidei yake kwa kuwatembelea watumishi wa Wizara yake huko Dodoma.Ni mfano wa kuigwa.Pia hoja yake ya kuwa na “data bank” ya simu ni nzuri (japo ufanisi wake ni mgumu) na inaweza kuigwa kwenye maeneo mengine kwa mfano kuanzisha daftari la kudumu la wala rushwa.

Alamsiki


22 Aug 2006

KULIKONI UGHAIBUNI-21

Asalam aleykum,

Leo nina jambo muhimu sana kuhusiana na maslahi ya Taifa letu.Nawaomba wasomaji wapendwa tuwe pamoja kwa makini ili tusipoteane njiani na hatimaye kuleta tafsiri potofu ya ninachotaka kuzunguzia.Natanguliza rai-au niite tahadhari-kwa vile mada yangu ya leo ni nyeti,na ni kuhusu suala ambalo mara nyingi limekuwa likikwepwa na watu wengi.Lakini kabla sijaingia kwa undani,nielezee uzoefu wangu mimi mwenyewe katika suala hilo.

Kwa wafuatiliaji wa makala hii watatambua kwamba mara zote huwa naanza na asalam aleykum.Nimezowea sana kuwasalimia ndugu zangu kwa namna hiyo.Pengine ni kwa vile nimewahi kukaa miji ambayo salamu hiyo inatumika sana,au pengine wengi wa marafiki zangu ni Waislam.Robo ya elimu yangu ya msingi niliipata mkoani Kigoma katika kitongoji cha Ujiji.Nakumbuka kuna wakati flani katika darasa nililokuwa nasoma tulikuwa Wakristo watatu tu na waliosalia (nadhani zaidi ya silimia 90) walikuwa Waislam.Niliwahi kufundisha sekondari flani mjini Tanga na takribani robo tatu ya wanafunzi wangu walikuwa Waislam pia.Na nikipiga hesabu ya harakaharaka,katika marafiki zangu kumi bora saba ni Waislam.Hata siku moja,tangu nikiwa Kigoma,Tanga,Dar na kwengineko sikuwahi kujiona nimezungukwa na watu tofauti nami ambaye ni Mkristo Mkatoliki.Wanafunzi wenzangu,wanafunzi niliowafundisha na marafiki zangu walinichukulia kama Mtanzania mwenzao japo tulikuwa tunatoka madhehebu tofauti.Na hivi karibuni nilipokuja huko nyumbani kwa utafiti wa PhD nayosoma,wengi wa niliohojiana nao walikuwa Waislam.Sikuwahi kupata matatizo yoyote hata pale nilipokutana na wanaoitwa mujahidina.Katika levo ya familia,kaka-binamu yangu mmoja ambaye ni Mkatoliki wa kwenda kanisani kila Jumapili ana mke ambaye ni Mwislam wa swala tano.Uzoefu wangu huo mdogo unatoa picha moja muhimu:Watanzania tumekuwa tukijichanganya sana bila kujali tofauti zetu za kidini.Nikisema kujichanganya namaanisha kujumuika pamoja na sio vinginevyo.

Kuanzia kwenye miaka ya 80 kulianza kujitokeza dalili zilizoashiria kwamba mambo si shwari sana katika eneo la dini nchini.Tunakumbuka uvunjaji wa mabucha ya nguruwe,matukio kwenye msikiti wa Mwembechai,mihadhara ya kidini,suala la Ustaadh Dibagula na mengineyo.Wapo waliosema kwamba kulikuwa na kikundi cha watu wachache kilichokuwa kinachochea vurugu za kidini kuganga njaa zao.Wapo pia waliokuwa wanadai kuwa vurugu za kidini zilikuwa na sura ya kisiasa huku mara kadhaa chama cha CUF kikibebeshwa lawama.Yayumkinika kusema kuwa japo viongozi wetu walikuwa wakikemea vurugu hizo hakukuwa na jitihada za makusudi za kubaini chanzo hasa ni nini.Wanataaluma wetu nao kwa namna flani wamekuwa wakilikwepa suala hili pengine kwa vile linagusa hisia za wengi au pengine kutokana na hisia kwamba matokeo ya tafiti zinahusu migogoro ya kidini huweza kuchangia kuleta utata zaidi badala ya ufumbuzi wa matatizo.Mwalimu wangu wa zamani katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Dr John Sivalon alichapisha kitabu ambacho kilitokana na thesis yake kuhusu mahusiano kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Tanzania.Bila kuingia kwa undani kujadili kitabu hicho cha mhadhiri huyo wa Kimarekani ambaye pia ni Padre,ukweli ni kwamba kimekuwa ni nyenzo muhimu katika mihadhara na mijadala ya kidini nchini,japo sina hakika kama kimesaidia katika kuwa sehemu ya utatuzi wa matatizo yaliyopo.

Hebu sasa niingie kwenye ishu yenyewe.Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mijadala inayoendelea kwenye forums mbalimbali za Watanzania kwenye internet.Suala hilo ambalo limegusa hisia zangu ni madai kwamba Rais Jakaya Kikwete amekuwa akiwapendelea Waislam katika teuzi mbalimbali anazoendelea kuzifanya tangu aingie madarakani.Na pengine kinachotajwa zaidi ni ule uteuzi wake wa kwanza wa mabalozi wa mwanzo (akina Adadi na wengineo) ambao kwa mujibu wa majina yao wote ni Waislam.Pengine bila kudadisi sifa za walioteuliwa,wanaolalamika wakaangalia dini zao.Teuzi nyingine nazo zimeendelea kuzua mijadala isiyo rasmi japo sina uhakika kama na huko nyumbani nako hali ni kama hii niliyoiona kwenye mtandao.Ila niliona kwenye mtandao makala mbili tofauti ambazo nadhani zilitolewa kwenye magazeti ya huko nyumbani ambapo mwandishi mmoja mkongwe alikuwa akijibu hoja za mwanasiasa flani ambaye nadhani pia ni kiongozi wa kidini,na mada yenyewe ilikuwa ni hiyohiyo eti Kikwete anawapendelea Waislam.

Mimi siamini kabisa kwamba yeyote kati ya aliyeteuliwa-iwe kwenye uwaziri,unaibu waziri,wakuu wa mikoa,wakurugenzi na kadhalika-wamepewa dhamana zao kutokana na Uislam au Ukristo wao.Unajua kwa miaka mingi sisi tumekuwa Watanzania kwanza halafu ndio vinafuatia vitu kama Ukristo au Undamba wangu.Na ndio maana kule Ujiji,Tanga,Dar na kwingineko nilikokuwa sikuwahi kupata matatizo na waliokuwa karibu nami kwa vile cha muhimu kwetu haikuwa dini au kabila bali urafiki au mahusiano yetu kikazi.Na naamini kabisa kuwa Kikwete ni Mtanzania kwanza,na anaongoza Watanzania kwa misingi ya umoja wao na sio tofauti za kidini,na kwa mantiki hyo hata anapochagua viongozi haangalia dini bali sifa za wateuliwa.

Hata hivyo,kuna matatizo kadhaa yanayohusiana na suala la dini nchini.Tusijidanganye kwamba hatufahamu kuwa kumekuwa na manung’uniko miongoni mwa Waislam kuhusu usawa katika sekta ya elimu na ajira.Iwapo chanzo cha tatizo hilo ni sera za kibaguzi za wakoloni au kuna mbinu za makusudi za kuchochea matatizo hayo,hiyo sio muhimu sana kama ilivyo kwa umuhimu wa serikali,taasisi mbalimbali,wanataaluma na wananchi kwa ujumla kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.Matokeo ya awali ya utafiti wangu unaohusu harakati za Waislam nchini yanathibitisha kwamba matatizo yapo na yanajulikana ila kinachokosekana ni jitihada za makusudi za kupata ufumbuzi wa kudumu.Habari nzuri ni kwamba,hilo (la kupata ufumbuzi) linawezekana iwapo busara zitatumika na wadau kujumuishwa kwa karibu.Namalizia kwa kusisitiza kwamba wanaoleta madai ya udini wanatumia haki yao ya kikatiba kutoa mawazo yao,japo siafikiani nao.Hivi mtu anapooa au kuolewa na mtu anayetoka naye dini moja anaitwa mdini?Hapana.Kitakachojadiliwa hapo ni sifa za huyo mume au mke.Hivyohivyo,Jakaya hawezi kuitwa mdini pindi akichagua Muislam kama yeye alimradi ana sifa zinazostahili.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Naanza makala yangu kwa kuelezea majonzi makubwa niliyonayo kufuatia kifo cha mwanataaluma maarufu huko nyumbani,Profesa Seith Chachage.Majonzi yangu yanachangiwa na ukweli kwamba mimi ni miongoni mwa wanafunzi wake wa zamani hapo Mlimani.Mungu ndiye mtoaji na yeye ndiye mchukuaji kama Maandiko Matakatifu yanavyosema,lakini pengo aliloliacha msomi huyu aliyebobea ni vigumu kuzibika.Nimepitia tovuti mbalimbali na nimegundua kuwa marehemu alikuwa kipenzi cha wengi hasa wale wenye uchungu na Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.Kwa tuliomjua Profesa Chachage tutakumbuka jinsi alivyokuwa akichanganya usomi wake na kauli za utani.Yaani ilikuwa vigumu kuchoka kusikia mhadhara wake.Kwa tunavyowajua wasomi wetu ni nadra kumkuta mmoja wao akipenda vitu kama bongofleva,lakini nimesoma kwenye tovuti moja kwamba marehemu alikuwa anapenda muziki wa kizazi kipya na inasemekana aliweza hata kuimba verses za wimbo maarufu wa TID uitwao Zeze.Mungu ailaze ahali pema roho ya marehemu Profesa Chachage,Amen.

Alhamisi ya tarehe 13/06 mwaka nilisoma kwenye tovuti ya gazeti la Uhuru habari iliyonukuu Rais mstaafu Benjamin Mkapa akisema kwamba “katika baadhi ya mashirkika kama ATC serikali iliingia mikataba bila kuwa na tathmini halisi ya faida ambayo ingepata kwenye mashirika hayo.”Hizi si habari njema hasa ikizingatiwa kwamba serikali haitegemei wataalamu wa njozi kujua kama mkataba flani una manufaa au la bali inapaswa kuwatumia wataalam wake kuhakikisha kuwa kinachofanyika sio bahati nasibu ila ni kitu cha maslahi kwa Taifa.Tunaweza kutomlaumu Chifu MangungO alisaini mikataba feki na akina Karl Peters nyakati za ukoloni kwa sababu enzi hizo hakukuwa na wataalamu wa kupitia mikataba na kujua kama ina manufaa au la.Lakini zama hizi hali ni tofauti.Pale serikali inapoona kwamba jambo flani liko nje ya uwezo wake ina uwezo wa kutafuta na kupata uhakiki flani kutoka nje ya nchi.Yaani hapo namaanisha kwamba yapo makampuni kadhaa ya kimataifa ambayo yanaweza kutoa huduma ya ushauri kwa serikali iwapo itaonekana kwamba wataalam wetu wa ndani wameshindwa kazi hiyo.Hivi inawezekanaje mtu akaingia mkataba bila kujua faida yhalisi ya mkataba huo?Utapangishaje nyumba yako kama huna hakika kuwa kwa kufanya hivyo wewe mwenyewe au familia yako mnaweza kuishia kulala gesti hausi?Na je inapobainika kwamba kuna tu flani,kwa sababu anazozijua yeye,alisaini mkataba usio na faida kwa Taifa,tunafanyaje?Suala hapa sio kunyooshena vidole bali ni kuhakikisha kuwa makosa ya aina hiyo hayajirudii.Na njia nyepesi ya kufanya hivyo ni kuwachukulia hatua wale waliofanya makosa hayo-iwe walifanya kwa makusudi,uzembe au kutojali maslahi ya nchi yetu.

Nilishawahi kuandika huko nyuma kwamba kuna watu hawana uchungu na Taifa letu,na hawa ni pamoja na hao wanaosaini mikataba kama ile ya Chifu Mangungu utadhani wakati wanasaini mikataba hiyo walikuwa bwii(wamelewa) au wamesainishwa wakiwa usingizini.Marehemu Chachage na baadhi ya wasomi wengine wa nchi hii walijikuta wakitengeneza maadui kila walipojitahidi kukemea mambo yanayoendana kinyume na maslahi ya Taifa.Kuna watu hawapendi kuambiwa ukweli hata pale wanapoharibu na si ajabu makala hii ikapata upinzani wao.Lakini hiyo haitatuzuwia sie wenye uchungu na nchi yetu kusema yale yanayotupeleka pabaya.

Nimesikia kuna kampuni ya Kisauzi Afrika imepewa haki za utafutaji mafuta huko nyumbani.Pia kuna tetesi kwamba nchi yetu ina utajiri wa Uranium.Mungu akitujalia,siku moja na sisi tutakuwa na sauti kwenye siasa za kimataifa kwa vile mafuta ni silaha,ukiwa nayo lazima utaheshimika.Lakini bila mipango madhubuti utajiri hio unaweza kuwa kama laana kwa Taifa kama letu lililozowea amani.Huko Nigeria kumekuwa na matukio kadhaa ya vurugu ambazo kimsingi zinatokana na ukweli kwamba wenye ardhi (wananchi) wanaishia kuona tu mabomba ya mafuta na magari ya thamani kwa wale wanaowatumikia wenye makampuni ya mafuta ya kutoka nje,huku walalahoi wakizidi kuwa masikini.Mwanafalsafa Karl Marx aliwahi kusema kuwa masikini hana cha kupoteza anapoamua kupigania haki yake.Watu hawawezi kuendelea kuwa kimya wakati utajiri wao wa asili kwenye nchi yao unawanufaisha wachache kutoka nje na wapambe wao wanaosaini mikataba hewa.

Naomba ieleweke kwamba sizilaumu serikali za awamu zilizotangulia kuwa mikataba yote zilizoingia ilikuwa bomu.Kilio changu hapa ni kwenye hiyo mikataba ya iliyosainiwa ndotoni.Nafahamu kwamba wataalamu wazalendo wanatoa ushauri mzuri tu kabla ya mikataba kusainiwa lakini tatizo linakuja pale maslahi binafsi yanapowekwa mbele ya maslahi ya Taifa.Kwa kuwa mtu ana mamlaka ya kupuuza ushauri wa kitaalamu basi anatumia fursa hiyo kujifanya madudu kana kwamba madhara ya anachokifanya hayatamgusa kwa namna flani.

Naamini serikali ya Awamu ya Nne haitawalea wazembe wanaotaka kutulostisha.Narudia kusema kwamba sisi sio masikini wa namna tulivyo kwa sababu tuna raslimali za kutosha ambazo zinaweza kabisa kutuweka pazuri.Tunachopaswa kuelewa ni kwamba miaka 25 au 50 ijayo vizazi vya wakati huo vinaweza kutushangaa sana pale vitakapokuta kila kitu kimeuzwa na faida ya mauzo hayo haionekani.Inaweza kuwa vigumu sana kwa walimu wa somo la Historia wa wakati huo kuwaelewesha wanafunzi wao kuwa tofauti na mikataba feki ya kina Karl Peters na baadhi ya machifu wetu,mikataba iliyobomoa nchi yao ilifanywa na Watanzania haikuwa ya kilaghai bali ni sababu ya kitu kidogo (sijui wakati huo watakuwa wanatumia msamiati gani kumaanisha rushwa),

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa gazeti hili maridhawa.

Leo nina mada nzito na nakuomba msomaji uifatilie kwa makini kwa manufaa ya Taifa letu.Labda kabla “sijaivaa” mada hiyo nitoe mfano mmoja wa hapa Uingereza.Miongoni mwa matatizo makubwa ya kijamii yanayoikabili nchi hii ni suala la matumizi ya madawa ya kulevya hususan miongoni mwa vijana.Watu wanabwia unga kama hawana akili nzuri.Kipindi hiki cha summer nacho kinasaidia kupata “jeshi jipya la wabwia unga" hasa kwa vile baadhi ya vijana huenda mapumzikoni (summer holiday) nje ya nchi wakiwa mbali na wazazi wao.Ukisimuliwa vituko vinavyotokea pwani za sehemu kama Hispania (kwa mfano Ibiza,Majorca na kwingineko) utabaki mdomo wazi.Hata hivyo,serikali na taasisi nyingine zimekuwa zikifanya jitihada kubwa kupambana na tatizo hilo japokuwa mafanikio si makubwa sana.

Kwa huko nyumbani tatizo naliona kubwa sana zaidi ya kubwia unga ni matumizi ya bangi.Sijui ni kwa vile madhara ya bangi ni ya polepole zaidi ya kubwia unga,au sijui kwa vile bangi imezoeleka sana,ukweli unabaki kuwa hatua madhubuti dhidi ya uvutaji bangi hazijatiliwa mkazo sana na vyombo husika.Kwa bahati mbaya sijaona utafiti wowote rasmi uliofanywa kuonyesha ukubwa wa tatizo hili,lakini naamini pindi utapofanyika matokeo yake yatakuwa ya kutisha.

Kuna kundi maalumu nitalolizungumiza hapa:wasanii hususan wale wa Bongofleva.Nilipokuwa huko nyumbani nilijaribu kufanya utafiti usio rasmi kujua msanii gani anatumia bangi na nani hatumii.Kwa kuwa utafiti huo haukuwa rasmi naomba nisitoe “takwimu” zangu lakini ukweli ni kwamba bangi imekuwa ina wafuasi wengi sana miongoni mwa wasanii wetu.Unajua tatizo mojawapo la uvutaji bangi ni kwamba huwezi kujificha iwapo ni mtumiaji.Kuna vitu flani-flani huwa havifichiki pindi mtu akishapuliza majani hayo haramu.Ilinishtua nilipogundua kuwa karibuni robo tatu ya wasanii wa kundi flani maarufu huwa hawawezi kutumbuiza jukwaani bila kupata misokoto kadhaa ya bangi.Jamani,hii sio hadithi ya kutunga au Isidingo bali ni hali halisi.Kwa bahati mbaya,watu hawajali sana.Na ndio maana hata kwenye tungo za baadhi ya wasanii maarufu wa Bongoflava unasikia bangi ikitajwa kwa namna ya kusifiwa utadhani imekuwa chai.Sintotaja majina ya watu hapa lakini kwa harakaharaka nimesikia nyimbo tatu,mbili kati ya hizo zikiwa zimeimbwa na msanii mmoja ambapo baadhi ya maneno ni kama “mimi nina kijiti cha…na wewe leta kijiti cha …” (kijiti ni bangi,na ukisikia kijiti cha mwanza basi inamaanisha bangi inayotoka mwanza),nyingine kuna maneno “…nitembezee chata…” (kutembeza chata ni kupasiana bangi) na msanii mwingine hakuona aibu kusema waziwazi “…pobe nakunywa,bangi navuta…”Wahusika wanaweza kujitetea kwamba hizo ni nyimbo tu na wao hawatumii kilevi hicho lakini haihitaji PhD kujua kwamba mtu hawezi kusifia kitu kibaya kama hakitumii au kukipenda.

Miongoni mwa hofu zangu kuhusu matumizi ya bangi kwa baadhi ya wasanii ni kwamba mara nyingi (kwa mujibu wa utafiti wangu usio rasmi) baada ya kuvuta bangi na kutumbuiza,msanii husika hujikuta “akizidishiwa ulevi” kwa ofa za pombe kutoka kwa mashabiki au wapambe.Lakini pia kuna watu wanaoitwa “groupies” ambao mara nyingi ni akinadada ambao wanamwandama msanii na wako tayari kufanya lolote kumridhisha msanii huyo.Sasa mtu akishakuwa na “cocktail” ya bangi na pombe,je akipewa ofa ya tendo la ndoa na “groupie” kondom inakumbukwa kweli?Lakini hilo ni tatizo dogo ukilinganisha na lile la “utaahira”.Najua ni vigumu kumshawishi mvuta bangi aamini kuwa bangi inachangia katika kuleta madhara kwenye ubongo,lakini ukweli ndio huo.

Naomba ieleweke kwamba simaanishi kuwa wasanii wote ni wavuta bangi bali pointi yangu ni kwamba ulevi huo haramu umepata wafuasi wengi kwenye fani kama wanavyosema wenyewe.Nawajua wasanii kadhaa ambao wanajiheshimu ambao wanaelewa kuwa licha ya bangi kuwa ni kitu haramu pia ina madhara kwa afya ya mvutaji.Kwenye utafiti wangu “bubu” niligundua kwamba miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya vijana kujiingiza kwenye utumiaji wa bangi ni hoja ya kipuuzi kwamba “inaleta kujiamini na hisia za ubabe!!!”Nilidokezwa na rafiki yangu mmoja aliewahi kufanya “shooting” ya video ya tangazo flani lililokuwa limemhusisha msanii mmoja wa “mkoani” kwamba nusura amwombe bosi wake atafute mtu mwingine wa kutokea kwenye tangazo hilo kwa vile msanii huyo alibugia misokoto kama minane hivi siku waliyokuwa wanajiaandaa na shooting hiyo.

Sasa nyie vijana,na hasa baadhi ya wasanii,mnaoendekeza uvutaji bangi mkae mkielewa kwamba mnajitafutia matatizo kwenye maisha yenu.Lakini pia wakati umefika sasa kwa uvutaji bangi kuonekana kama tatizo sugu linalohitaji kutupiwa jicho kali.Wale wanaovuta bangi kwa kisingizio cha “imani zao za kidini” (ndio,wapo wanaodai kuwa wao ni marastafari na bangi ni majani matakatifu) watambue kwamba wanavunja sheria na wakati huohuo wanatuletea uwezekano wa kuwa na mataahira siku za mbeleni.Watambue kuwa nchi yetu ni masikini na wakati huu ambao jitihada zinaelekezwa katika kupambana na majanga kama ya ukimwi wao wanatuongezea mzigo mwingine wa kukabiliana na tatizo la uchizi unaosababishwa na weed (bangi).

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Kombe la Dunia mwaka 2006.Wenyewe wanaiita shughuli hii “the biggest show on earth.” (yaani mashindano makubwa kabisa duniani).Inaweza kuwa kweli.Kombe la dunia linawaunganisha mamilioni kwa mamilioni ya watu katika takriban kila pembe ya sayari hii.Wapo wale wanaofuatilia timu zao za taifa zikitafuta nafasi katika vitabu vya historia ya soka,wengine tukiwamo Watanzania tunafuatilia michuano hiyo kwa vile wengi wetu tunapenda soka japokuwa kwa sababu zinazoweza kuchukua mwaka mzima kuzitaja hatujui lini nasi tutakuwa washiriki.

Kuna mjadala mdogo japo muhimu unaoendelea huku Ughaibuni na pengine hata kwingineko kuhusu kama ni kweli michuano hii na michezo kwa ujumla inaleta umoja na sio mpasuko miongoni mwa timu au nchi shiriki na mashabiki ulimwenguni kote.Pengine hakuna sehemu nzuri zaidi ya kuanzia mjadala huu kama hapa Uingereza.Pengine ni vema kuielezea Uingereza kwa kutumia majina wanayotumia wenyewe.United Kingdom ni muungano wa “nchi” nne:England,Scotland,Wales na Northern Ireland. Great Britain ni hizo tatu za mwanzo ukitoa Northern Ireland (ambayo kijiografia haiko katika ardhi moja na hizo tatu).Kwa hiyo kuna wakati utasikia nchi hii ikiitwa The United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland.Kwa kawaida,katika mashindano mbalimbali Uingereza huwakilishwa na timu za taifa au klabu kutoka “nchi” hizo nne kama vile ilivyo kwa timu za Taifa za Bara na Zanzibar zinavyoiwakilisha Tanzania.

Katika mchakato wa kutafuta nafasi ya kushiriki katika Kombe la Dunia ni England pekee iliyofanikiwa na kuziacha Wales, Scotland na Northern Ireland kubaki watazamaji tu.Hapo ndipo shughuli inapoanza.Kwanza Waziri Mkuu (First Minister) wa Scotland Jack McConnell aliweka msimamo wake wazi kwamba hatashabikia England,ambayo kwa hapa Scotland inajulikana kwa jina la kiutani kama Auld Enemy (Adui wa zamani) na badala yake angeshabikia Trinidad and Tobago-au kwa kifupi T&T.Na si yeye pekee mwenye mtizamo huo.Asilimia kubwa ya Waskotishi walishabikia T&T ilipopambana na England.Wapo waliotoa kisingizio kwamba ushabiki wao ulitokana na ukweli kwamba kuna mchezaji wa T&T mwenye ubini Scotland (anaitwa Jason Scotland,anayechezea timu ya daraja la kwanza ya St Johnstone) lakini wengine hawakuwa hata na haja ya kutoa visngizio bali kusema ukweli kwamba ushindi kwa England ni karaha kwao.Kama kuna sehemu zaidi ya nchini T&T ambako jezi za timu yake ya taifa ziliuzika sana basi si kwingine bali Scotland.
Kuna hii kitu inayoitwa “bendera ya Mtakatifu Joji” (St George flag).Nadhani kwa wale wanaofuatilia mechi za England watakuwa wameona bendera hiyo nyeupe yenye msalaba mwekundu.Bendera hiyo ina historia ndefu ambayo pengine hapa si mahala pake,lakini lililo wazi ni kwamba inahusishwa kwa kiwango flani na hisia za ubaguzi wa rangi (racism).Hata baadhi ya taasisi zimekuwa na wasiwasi pale watumishi wake wanapopeperusha bendera hizo.Kwa mfano,hivi karibuni supamaketi kubwa iitwayo Tesco ilipiga marufuku madereva waliokuwa wanaleta mizigo kwenye supamaketi hiyo huku wakipeperusha bendera ya Mtakatifu Joji,japo baadaye uamuzi huo ulibatilishwa.Pia mamlaka ya viwanja vya ndege (BAA) ilipiga marufuku kupeperusha bendera hiyo kwenye majengo yanayofanyiwa ukarabati Terminal 5 Heathrow Airport.Mkanganyo zaidi kuhusu bendera hii umeongezwa na ukweli kwamba BNP,chama cha siasa chenye mtizamo wa kibaguzi,kimekuwa kikiitumia bendera hiyo katika harakati zake dhidi ya wahamiaji na wageni.Watetezi wa bendera hiyo wanasema inawaonyesha uzalendo na sio alama ya ubaguzi.

Tofauti na huko nyumbani ambako hadi hivi karibuni kitendo kutundika bendera ya Taifa dirishani kingeweza kukupeleka Segerea (jela) huku kwa wenzetu bendera ni miongoni mwa alama za kujivunia utaifa/uzalendo wao.Hata hivyo,wapo wanaotumia utaifa kama kifuniko (cover) cha dhamira zao za kibaguzi.Mara nyingi vikundi vinavyoendekeza siasa za kibaguzi vimekuwa vikitumia sana bendera za mataifa yao kujitambulisha (kama ilivyo kwa BNP).Utaifa uliopindukia ni mithili ya ulafi:kula sio kitendo kinachoudhi lakini kula kupita kiasi (ulafi) unaudhi kwa vile unaweza kuwaathiri watu wengine,kwa mfano kuwalaza na njaa.Wachambuzi wa soka la Hispania walikuwa na wasiwasi iwapo timu yao ingefanya vizuri kwenye Kombe la Dunia kutokana na ukweli kwamba Waspanishi wengi wanajali zaidi timu zinazotoka katika miji yao (kwa mfano Real Madrid,Barcelona au Valencia) kuliko timu ya taifa.Hapo tatizo ni zaidi ya utaifa bali asili ya mtu anakotoka katika taifa.

Na pengine ni kwa vile waandaaji wa Kombe la Dunia wanafanya kila jitihada kupambana na wakora wa soka ndio maana inapunguza na vitendo visivyopendeza machoni wa watu kwa mfano kutoa sauti kama za nyani kuwakashifu watu weusi.Matukio ya ubaguzi katika soka yamekuwa ni tatizo linalowagusa watu wengi.Hali ni mbaya sana huko Ulaya Mashariki ambapo kwa mfano baadhi ya timu za hapa zenye wachezaji weusi huwa zinatahadharishwa mapema kabla ya kwenda huko kuwa zitegemee wachezaji hao weusi kunyanyaswa na mashabiki wabaguzi.Soka la Hispania katika siku za karibuni limegubikwa mno na kelele za kibaguzi dhidi ya wachezaji weusi.Italia pia inasifika kwa hilo kama ilivyo kwa Ujerumani yenyewe.Hata hapa Uingereza kuna hisia kwamba miongoni mwa sababu zinazoifanya timu kama Chelsea “kuchukiwa” ni kwa vile mmiliki Roman Abramovich si Mwingereza, kocha Jose Maurinho ni Mreno na wachezaji wengi ni kutoka nje ya Uingereza.

Kwa kumalizia,ngoja niwachekeshe kidogo.Hapa kuna kundi la akina mama wanaojiita “Wajane wa Kombe la Dunia.”Hawa ni wale wanaoyaona mashindano haya kama adhabu kwa vile waume zao wakereketwa wa soka huwasahau kwa muda wake zao na akili yote kuelekezwa kwenye michuano hiyo.Huenda hata huko nyumbani kuna “wajane” pia.Si unajua tena wapo wanaotumia kisingizio cha kwenda “kucheki boli” kupata wasaa wa kuzungukia nyumba ndogo…huo ni utani tu.

Alamsiki

18 Jun 2006

KULIKONI UGHAIBUNI

Asalam aleykum.

Hapa Uingereza kuna chama cha siasa kinachoitwa British National Party au kwa kifupi BNP.Hiki ni chama kinachofuata siasa za mrengo wa kulia kabisa,far right kwa “lugha ya mama.”Siasa za namna hiyo ndio zilizokuwa zinahusudiwa na Manazi chini ya Hitler na Mafashisti chini ya Mussolini.Hawa jamaa wa BNP ni wabaguzi waliokithiri.Majuzi wakati wa uchaguzi mdogo huko England mmoja wa watu muhimu katika BNP,Dokta Phill Edwards (jina lake halisi ni Stuart Russell) alizua mjadala mkubwa kuhusu siasa za chama hicho pale alipotoa matamshi ya kuchefua dhidi ya watu weusi.Alirekodiwa kwa siri na kituo cha televisheni cha Sky akisema kuwa watu weusi wana IQ (uwezo wa akili) ndogo,na watoto weusi wakikua sanasana wataishia kukaba watu (vibaka au majambazi).Aliendelea kusema,hapa namnukuu “suala hapa sio kama tunawachukia watu weusi bali ni kama wao ni tishio kwa amani,utulivu na utamaduni wa jamii ya Kiingereza…watoto weusi wakikua watanyonya uchumi wetu na kujaza magereza yetu na pengine kukukaba…huko Afrika kusini mwa jangwa la Sahara hakuna ustaarabu wowote,na hakuna maendeleo ya sayansi…”Kwa kweli ilikuwa inauma kuangalia upuuzi huo kwenye runinga,lakini ni hali tunayoishi nayo hapa kila siku.

Miongoni mwa mambo “halali” yanayowapa nguvu wabaguzi hawa ni vitendo vya baadhi ya wageni na hasa weusi kujihusisha na uhalifu au mambo mengine yasiyofaa katika jamii.Kwa wao,samaki mmoja akioza basi wote wameoza,yaani mtu mmoja mweusi akihusika kwenye uhalifu basi watu wote weusi ni wahalifu.Na kwa BNP sio weusi tu wanaolengwa.Chama hicho kilipata “pumzi” ya kutosha kupinga sera za uhamiaji na ujio wa wageni hapa Uingereza baada ya matukio ya kujilipua mabomu kwa kujitoa mhanga mjini London mwezi Julai mwaka jana. “Vita” ya BNP dhidi ya wageni ikapamba moto na sasa walengwa wakuu wakawa watu wenye asili Asia (hasa Wapakistani).Watatu kati ya waliojilipua mabomu ya muhanga walikuwa Waingereza wenye asili ya Pakistani,na kwa chama hicho cha kibaguzi hiyo ilikuwa sababu tosha ya kuwajumuisha watu wenye asili ya Pakistani na Asia kwa ujumla,na wageni wengine kuwa ni tishio kwa maisha ya Taifa hili.

Huko nyubani moja ya mambo ambayo Watanzania tunajivunia sana ni jinsi “tunavyojichanganya” bila kujali kabila,dini au jinsia.Nikisema “kujichanganya” namaanisha ushirikiano,upendo na maelewano,na sio kukosa msimamo kama maana halisi ya neno ilivyo.Niliwahi kusikia stori flani siku za nyuma inayohusu timu moja ya soka kutoka nchi flani ya jirani.Wachezaji wa timu hiyo walipokuwa wanafanya mazoezi walikuwa wanavuta umati mkubwa wa wakazi wa mji wa Arusha,ambako kulikuwa na michuano ya kimataifa.Kilichokuwa kinawashangaza wachezaji hao ni jinsi watazamaji walivyokuwa “wanajichanganya” kana kwamba ni watu wa kabila moja.Nchi wanayotoka wachezaji,kama zilivyo nchi kadhaa za Afrika,inasifika sana kwa ukabila.Inasemekana katika nchi hiyo ni nadra watu wanaotoka makabila tofauti kuwa marafiki wa dhati.Sasa walipoona baadhi ya watazamaji “wanagongeana sigara” na kutia stori kana kwamba wanaishi nyumba moja,ilikuwa ni jambo la kushangaza sana kwao.Huenda waliondoka Arusha wakiwa na fundisho flani.
Rafiki yangu mmoja,Profesa Tunde Zack-Williams,aliwahi kuniambia kwamba napaswa kujivuna kuwa Mwafrika kutoka Tanzania.Alinieleza kwamba kwa uzoefu wake mwenyewe kama mwanataaluma na Mwafrika,Watanzania ni watu waliojaliwa na “karama” ya mshikamano,upendo na umoja,na wanawaheshimu sana wageni bila kujali wanatoka wapi.Profesa huyo ni mzaliwa wa Sierra Leone,nchi ambayo imeathiriwa sana vita vya wenyewe,na amekuwa akiwasaidia sana kitaaluma vijana wa Kiafrika.Rafiki yangu mwingine anayetoka Sudan aliniambia kwamba alishangaa sana alipofika Tanzania kwa mara ya kwanza,kwa sababu licha ya nchi yetu kuwa na makabila zaidi ya 120 hakuona dalili zozote za watu kubaguana kwa misingi ya kikabila.

Hata hivyo,katika siku za hivi karibuni kumeanza kujitokeza dalili za baadhi ya watu kuchoshwa na “ujiko” huo tulionao ndani na nje ya Afrika.Binafsi,nafanya utafiti unaohusu masuala ya dini na siasa.Sintoongelea sana utafiti huo kwa vile bado “uko jikoni” lakini miongoni mwa matokeo yake ya awali ni dalili kuwa kuna watu au vikundi flani vya jamii vinavyotumia dini kujenga mpasuko katika jamii kwa manufaa yao binafsi.

Kibaya zaidi ni dalili kwamba baadhi ya Watanzania ambao tuna haki ya kuwaita “wageni” wanapoanza kujiingiza kwenye kuleta chokochoko kwenye jamii yetu iliyozowea amani.Siku zote tumekuwa tukiheshimiana na kupendana bila kujali kuwa flani alizaliwa Ifakara au New Delhi.Lakini kama BNP inavyopata “nguvu halali ya kusema ovyo” pindi wageni “wanapoharibu” inaweza kufika mahali Watanzania wazawa wakaanza kujenga chuki dhidi ya wale ambao licha ya “ugeni” wao wanachochea mpasuko katika nchi yetu.Na si “wageni” tu bali hata wale wanaotumia nafasi zao za juu katika jamii kutukoroga.Waasisi wa Taifa letu walifanya kazi kubwa sana kutufikisha hapa tulipo,na nawausia Watanzania wenzangu tusifumbe macho pale wale tulikowakaribisha kwa upendo (na maswahiba zao) wanapoanza kutuletea dharau na chokochoko kwenye nchi yetu.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa gazeti hili.

Leo tuzungumzie muziki.Muda mfupi uliopita nilikuwa nasoma makala flani kumhusu msanii wa kizazi kipya Albert Mangwea.Yalikuwa ni mahojiano kati ya msaanii huyo na tovuti ya Darhotwire.com.Niliguswa sana na kilio cha msanii huyo ambacho kimekuwa pia kikisikika kutoka kwa takribani kila msanii wa Bongofleva.Kuna wajanja flani,(hapana,hawa si wajanja,bali ni WEZI) ambao wamekuwa wakiwanyonya vijana wetu bila hata chembe ya huruma.Wezi hawa wanafahamika zaidi kwa jina la “wadosi”.Binafsi sijui kwanini wanaitwa wadosi lakini la muhimu hawa sio jina wanaloitwa bali unyonyaji wanaowafanyia wasanii wetu.

Pengine kabla ya kujadili wizi wa mchana mweupe unaofanywa na wadosi hao,tuangalie maendeleo ya Bongofleva huko nyumbani na huku Ughaibuni.Mimi ni mfuatiliaji sana wa mambo yanayotokea huko Bongo. “Ibada” yangu ya kila asubuhi inaanza kwa kutembelea tovuti za ki-Tanzania ili kujua yanayojiri huko.Sasa,kabla ya kuja huko mwaka jana mwishoni mwa mwaka jana nilikuwa nahisi kuwa habari kwamba Bongofleva imeikamata Tanzania kwa “kasi ya tsunami” ni porojo tu.Lakini nilipokuja nilishihudia mwenyewe jinsi gani hatimaye nyimbo zinazotengenezwa na kuimbwa na Watanzania zilivyokamata soko na mioyo ya wapenzi wa muziki.Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu nilibahatika kushuhudia tamasha la “Piga Kura au Upigike” kwenye viwanja vya Biafra Kinondoni.Licha ya picha kadhaa nilizochukua kwa ajili ya kuwajulisha marafiki zangu hapa,nilijionea jinsi gani watu wa rika mbalimbali wanavyovutiwa na kazi za wasanii wa muziki wa kizazi kipya.Nadiriki kuamini kuwa mashabiki waliofika viwanja hivyo walikuwa wanawakilisha karibu kila kona ya jiji la Dar es Salaam.Kitu kingine nilichobaini ni kwamba jinsi gani wasanii wanavyotumika katika masuala ya muhiu kwa Taifa.

Nakumbuka niliwahi kusoma katika gazeti moja la huko nyumbani kwamba msanii Juma Nature “alimfunika” mwenyeji wake-mgombea aliyemwalika msanii huyo katika kampeni zake.Yaani watu walikuwa na kiu zaidi ya kusikia muziki wa Nature kuliko hotuba ya mheshimiwa huyo.Na pengine umati kubwa uliojitokeza kwenye mkutano huo ulifuata buridani hiyo ya bure.Yayumkinika kusema kuwa mchango wa wasanii katika kufanikisha uchaguzi,na hata kuwapatia ushindi baadhi ya wagombea,ulikuwa mkubwa.Kwa bahati mbaya,au pengine kwa makusudi,baada ya kukamilisha kazi ya kuhamasisha jamii kuhusu uchaguzi na wagombea,wasanii wetu wamerudi kulekule walikokuwa:wamesahauliwa na wanaendelea kunyonywa.

Napenda kuwafumbua macho wasanii wetu kwa kuwaambia kuwa muziki wao huku guhaibuni unauzika sana miongoni mwa watu waliotoka Afrika Mashariki.Wamuulize Banana Zorro aliyealikwa hapo London kwenye pati ya Muungano,wamuulize Mr Nice,Ray C na TID,na Profesa J ambaye nasikia amewachengua vilivyo huko Sweden na Holland.Wasanii wa nyumbani wakija huku wanababaikiwa kama vile akina Shaggy au Sean Paul wanavyobabaikiwa wakija huko nyumbani.Lakini,safari za nje sio jambo la kukurupuka tu,ni kitu kinachotaka maandalizi.Kwa mantiki hiyo si lazima kusafiri ili kunufaika na kazi za sanaa bali hata kutafuta namna ya kupenyeza muziki katika soko la kimataifa kunaweza sana kuwainua wasanii wetu.Hivi wasanii wetu wanajua kuwa CD zao huku zinauzwa hadi paundi 10 (zaidi ya shs 24,000/=)?Nimesoma kwenye internet kwamba tarehe 12/06/2006 kampuni moja iitwayo Townsend Records itatoa CD iitwayo Bongoflava (Swahili Rap from Tanzania) ambayo itauzwa paundi 10.99 (takriban shs 27,000/= kwa exchange rate za leo).Sijui kama na hawa ni wadosi au la,lakini huo ni uthibitisho kuwa Bongoflava ina soko zuri tu kuhu Ughaibuni.Na watu wanapenda kweli kazi za wasanii wa nyumbani.Niliporudi kutoka Tanzania jamaa zangu kibao walikuwa wananiulizia kama nimekuja na CD za Bongofleva.Kila mmoja anasema wanaposikia wasanii wetu wanakumbuka sana nyumbani.

Mheshimiwa Kikwete alinukuliwa akiwataka Watanzania walioko nje kuwasaidia wenzao walio nyumbani hasa katika nafasi za masomo.Ujumbe huo unaweza pia kupanuliwa na kuwahusisha wasanii wa nyumbani,kwa maana kuwa Watanzania walio nje hasa wale wenye upeo na mambo ya muziki wawasaidie wasanii wetu wa nyumbani kwa namna yoyote ile inayowezekana.Lakini ili hilo liwezekane wasanii wetu hawana budi “kuchangamka.”Wanaoitwa “wadosi” wanawanyonya na kuwaibia kwa vile wanajua dhahiri kuwa wasanii hao hawana njia mbadala.Jamani,dunia siku hizi imekuwa kama kijiji (japo ni kinadharia) na unachohitaji ni kwenda tu kwenye internet cafĂ© na kuperuza kurasa za mtandao kujua wapi unaweza kupata huduma au kuuza ulichonacho kwa mtu aliye bara jingine.Hapa ndipo umuhimu wa shule (elimu) unapojidhihirisha.Lakini hata kama shule haipandi,si unaweza kumwomba rafiki yako akusaidie kutafuta soko la kazi zako za sanaa nje ya nchi?

Serikali inapaswa kuwasaidia wasanii wetu kwa kuipa meno sheria ya hatimiliki.Sambamba na hilo ni wasanii wenyewe kusimama kidete kutetea maslahi yao badala ya kuendelea kulalamika au kufikiria kuingia kwenye fani nyingine kukwepa wizi wa kazi zao.Pia wasione aibu kuomba msaada kwa wenzao walio nje.Mwisho naiomba serikali ipanue vita dhidi ya wala rushwa na majambazi na kujumuisha “wadosi” pia.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI

Mambo yakoje huko nyumbani?Natumaini kila mmoja anawajibika kwa namna yake katika ujenzi wa Taifa.

Kuna jamaa mmoja hapa anaitwa David Cameron.Huyu ni kiongozi wa chama cha wahafidhina (Conservative Party).Nia yangu si kuzungumzia wasifu wake,bali nataka nimlinganishe na mwanasiasa nyota wa huko nyumbani kwa muda huu,au kwa lugha ya “kwa mama” tunaweza kumuita “a man of the moment.” (kwa tafsiri ya haraka, “staa wa muda huu”).Nadhani msomaji mpendwa umeshajua ni nani ninayemzungumzia.Lakini hapa namuweka kando kidogo ili nikupashe kuhusu huyo Bwana Cameron na chama chake cha Conservatives (au Torry,kama kinavyojulikana hapa).Kwa tafsiri nyepesi hawa Conservatives ni watu wenye mrengo wa kulia na ndio wapiga kelele wakubwa kuhusu sera za uhamiaji na nyinginezo ambazo zinawagusa makabwela hususan wale ambao si wazawa wa hapa.Pengine jeuri kubwa ya wahafidhina hawa inatokana na uwezo wao wa kifedha.Fedha wakati mwingine huwa na tabia ya kumfanya binadamu asiwafikirie wenzie aliowazidi kiuwezo,na aghalabu anapowafikiria basi huwa ni kwa manufaa yake binafsi.

Kuibuka kwa Cameron kulichochewa zaidi na mwelekeo usioridhisha wa chama chake katika chaguzi mbalimbali.Wachambuzi wengi wa mambo ya siasa walikuwa wanahusisha mwenendo mbaya wa chama hicho na kile kinachoitwa kuwa “out of touch.”Nitafafanua.Chama kilicho “out of touch” ni kile ambacho machoni mwa watu wa kawaida kinaonekana kama hakijihusishi na maslahi ya walio wengi.Kwa mfano,hawa wahafidhina kwa miaka kadhaa wamekuwa wakikumbatia zaidi Waingereza weupe hasa wale wa tabaka la juu na la kati huku wakiwasahau wale wa tabaka la chini pamoja na Waingereza wengine ambao ni “wakuja” (kwa mfano wale wenye asili ya Asia,Caribbean,Afrika,n.k).Pia wamekuwa wakiwaona wageni (ikiwa ni pamoja na wanafunzi wanaochangia mamilioni ya paundi kwenye uchumi wa nchi hii) kama watu wanaokuja kuharibu uchumi,utamaduni na mazingira ya hapa.

Baada ya Waziri Mkuu wa mwisho kutoka Conservative kushika wadhifa huo,John Major,alipoangushwa na Tony Blair mwaka 1997,chama hicho kimebadilisha viongozi kadhaa lakini bila mabadiliko hayo kuwanufaisha kwenye chaguzi mbalimbali.Ndipo katika mchakato huo alipoibuka Bwana Cameron,kijana (ana miaka 40 tu),ana mvuto na haiba ya kutosha.Huyo bwana aliamua kuwapa wenzake kitu “laivu” kwamba chama chao hakina mvuto kwa wapiga kura,kinaonekana kuwa kiko zaidi kwa maslahi ya mabwanyenye kuliko makabwela,na hakizungumzi “lugha ya mtu wa kawaida mtaani.”Kuna mengi ya kumzungumzia huyo bwana lakini kilichonisukuma kuandika makala hii ni jinsi navyomuona anafanana na Jakaya Kikwete.Ukiachilia ukweli kwamba wote ni handsome lugha wanayoongea inafanana:lugha inayomgusha mtu wa kawaida na sio makundi flani tu katika jamii hususan wale wenye nguvu za kiuchumi.

Jakaya amenukuliwa mara kadhaa akiwausia viongozi wenzie kwamba wako madarakani kuwahudumia hao waliowaweka madarakani.Sio dhambi kuwa karibu na matajiri lakini ukaribu huo usiwe kwa ajili ya kuwaumiza wasio nacho.Utajiri sio dhambi,na kuna matajiri kadhaa (mfano Mzee Mengi huko nyumbani au Bill Gates huko Marekani) ambao utajiri wao umekuwa faraja kwa mamilioni ya wale wasio nacho.Matajiri wa aina hii ni muhimu kwao kuwa karibu na viongozi wa serikali,vyama vya siasa na taasisi nyingine kwa vile ni kwa ukaribu huo ndio miradi mbalimbali wanayoifadhilia inaweza kuwa na manufaa kwa wananchi.

Juzijuzi nilimwona Bwana Cameron kwenye luninga akiwa kwenye mtaani wakati wa kampeni za chama chake kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kwa upande wa England.Jinsi alivyokuwa akijichanganya na watu ilitosha kabisa kumfanya hata mtu aliyekuwa akikichukia chama cha wahafidhina afikirie upya.Siku chache baadae nikasoma kwenye mtandao kuwa Jakaya ameweka historia kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kutembelea wafungwa magerezani.Yalipotokea mauaji ya kutatanisha ya wale wachimba madini wa Mahenge hakukawia kuunda tume,na kinyume ya ilivyozoeleka mara baada ya kupewa ripoti na tume akaweka matokeo hadharani.Aliporejea tu kutoka Kusini mwa Afrika hakukawia kwenda kuwaona majeruhi wa tukio la uporaji wa fedha za NMB pale Ubungo,na kutoa maagizo papo hapo.Lakini si Jakaya pekee bali hata “luteni” wake Lowassa.Ghorofa lilipoanguka Keko hakusubiri kuletewa taarifa bali alikwenda kujionea mwenyewe na kuchukua hatua hapohapo, “mafuriko” yalipoielemea Sinza hakukawia kwenda kushuhudia hali ilivyo na kuwaamuru wahusika wachukue hatua za haraka.

Laiti kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya aliyokuja nayo Kikwete itaweza kufikia hatua ya kuigwa na viongozi kuanzia ngazi ya serikali ya mtaa,kata,tarafa,wilaya na mkoa,basi muda si mrefu Bongo itakuwa sehemu ya neema.Na mwenyewe Jakaya amekuwa akisema kuwa Tanzania yenye neema inawezekana.Enyi viongozi mliolala hebu amkeni,msisubiri kuamshwa.Jisikieni aibu pale mnapokwenda kinyume na spidi ya kiongozi wenu mkuu.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Mambo?

Siku chache zilizopita nilibahatika kuwa na maongezi na babu mmoja wa Kiskotishi ambaye kwa maelezo yake mwenyewe yeye ni “mkazi wa dunia nzima” (global citizen).Babu huyo anadai kuwa dunia ingekuwa mahala bora sana kama kusingekuwa na mipaka na sheria kali za uhamiaji.Na katika kutimiza azma yake ya kuwa mkazi wa dunia nzima anadai ametembelea takribani nchi 10 katika kila bara.Sijui kama alikuwa anasema ukweli au “ananifunga kamba” tu.Katika maongezi yetu hayo aligusia jambo flani ambalo liliniingia sana na ambalo ndio mada yangu ya wiki hii:UZALENDO.

Kwa mujibu wa babu huyo,enzi zao wakiwa vijana suala la uzalendo lilikuwa likitiliwa mkazo sana.Alidai kuwa japo kwa sasa hali ni tofauti kidogo lakini bado nchi nyingi za magharibi zinatilia mkazo sana suala hilo.Alieleza kwamba akiwa kijana babu yake alikuwa akimwambia kuwa mazingira mazuri watakayoyaweka wakati huo yatakuja kuvinufaisha zaidi vizazi vijavyo.Baba yake pia alikuwa akimweleza hivyo hivyo.Na yeye alipokuwa mtu mzima alikuwa akiwaeleza wanae hivyohivyo.Na sasa anasema amekuwa akitoa changamoto ya aina hiyohiyo kwa wajukuu wake.Furaha aliyonayo ni kwamba utabiri wa babu na baba yake umetimia.Maendeleo yaliyopo hivi sasa yamechangiwa na msingi mzuri uliojengwa karne kadhaa zilizopita.Na kilichowasukuma hao waliotengeneza misingi hiyo si kingine zaidi ya uchungu wao kwa taifa lao na vizazi vijavyo.

Huko nyumbani kuna tatizo kuhusiana na suala la uzalendo.Wapo wapuuzi fulani ambao wanaendesha mambo utadhani hakuna kesho au labda Tanzania haitakuwepo miaka 50 ijayo.Na hawa ndio baadhi yao waliripotiwa kutishia maisha ya waandishi wa KULIKONI na THIS DAY kwa sababu magazeti hayo yameapa “kula nao sahani moja” (kuwaweka hadharani).Hawa ni watu ambao hawana uchungu si kwa nchi yao tu bali hata kwa wajukuu zao.Ukweli ni kwamba mtu anayekula fedha iliyotolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule hana upeo wa kufikiria kwamba kwa kufanya hivyo huenda wajukuu wa mtoto wake wa mwisho watakaopaswa kwenda shule miaka 20 ijayo wanaweza kukosa nafasi hiyo kwa upuuzi uliofanyika mwaka 2006.Kuna watu wanafanya mchezo na maisha ya Watanzania wenzao kwa kutumia fedha za wenzao bila hata kuwashirikisha hao waliowekeza.Jamani,hata sheria za kawaida mtaani si kwamba bwana au bibi harusi mtarajiwa hawezi kutumia michango ya harusi yake mwenyewe pasipo kuwajulisha wanakamati?Sembuse hao ambao wamekabidhiwa fedha ambazo baadae wanapaswa kuzirejesha kwa wahusika!Nadhani mnaniapata hapo.

Wabadhirifu wa mali za umma na wala rushwa ni sawa na majambazi tu.Ni majambazi ambao silaha yao kubwa ni dhamana walizokabidhiwa kuwatumikia wananchi.Majambazi hawa wanachoiba sio fedha tu bali hata haki za Watanzania wenzao.Na kama walivyo majambazi wengine,hawa wakishahisi kuwa wanafahamika hukimbilia kutumia silaha kuu mbili:rushwa na vitisho.Kama gazeti linachimba maovu yanayofanywa na watu flani wasio na uchungu na nchi yao,basi waandishi wa gazeti hilo watafuatwa ili “wadakishwe kitu kidogo kuua soo.”Na itapoonekana kuwa gazeti hilo na waandishi wake wako ngangari katika kutetea maslahi ya Taifa na hivyo kukataa kuuza taaluma yao kwa kupokea rushwa basi hapo ndipo vitakapoanza vitisho.Sio huko nyumbani pekee ambako waandishi wa habari wanaovalia njuga kufichua maovu katika jamii wanakumbana na vitisho kutoka kwa wahusika.Mwaka 1996,Veronica Guerin, mwandishi wa habari wa kike huko Northern Ireland alipigwa risasi na kuuawa kutokana na makala za uchunguzi kuhusu biashara ya madawa ya kulevya nchini humo.Mwaka juzi,waandishi kadhaa wa magazeti ya Daily Record na Sunday Mail ya hapa Uingereza waliripoti kupokea vitisho kutokana na habari za uchunguzi walizokuwa wakiandika kuhusiana na magenge ya uhalifu.Kadhalika,mwaka jana waandishi wa habari wa magazeti kadhaa nchini Italia waliripoti kupokea vitisho baada ya kuripoti tuhuma za rushwa kuhusiana na klabu ya soka ya Genoa ya nchini humo.

Mifano hiyo michache inaonyesha ni jinsi gani watu waovu wanavyopenda kuendelea na maovu yao bila kubughudhiwa.Lakini haiwezekani watu wenye uchungu na nchi yetu wawaachie kufanya ufisadi wao wapendavyo.Naamini kila mzalendo anaelitakia mema Taifa letu atahakikisha kuwa wanahabari wanaosimama kidete kuwafichua wala rushwa na wabadhirifu hawabughudhiwi hata kidogo.Mjenga nchi ni mwananchi na mvunja nchi ni mwanachi pia.Tukiendelea kuwalea hawa majambazi wa mali na haki zetu basi tujue kuwa sio tu tunajitengezea “future” mbaya bali pia vizazi vijavyo vitatuhukumu kwa kuwaachia watu wachache wasio na uchungu na nchi yetu kutuharibia mambo.Tukiamua kwa nia moja tunaweza kuwadhibiti majambazi hao.

Alamsiki.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.