Showing posts with label BLAIR. Show all posts
Showing posts with label BLAIR. Show all posts

20 Jul 2007

Asalam aleykum,

Juzi nilipata barua-pepe kutoka kwa rafiki yangu mmoja aliyeko huko nyumbani.Huyu jamaa alikuwa akinilaumu “kirafiki” kwamba inaelekea nimeanza kuishiwa pointi za kuandika ndio maana takriban nusu ya makala yangu iliyopita ilikuwa ina habari “nyepesi nyepesi.”Sikukasirika kwani siku zote nathamini sana ushauri wenye lengo la kujenga au kuleta maendeleo.Nilimjibu kwamba nina pointi lukuki za kuandika,lakini kuna wakati inabidi “tupunguze kasi ya maisha” kwa kuangalia habari za vituko mbalimbali hususan vinavyojiri huku Ughaibuni.Pia nilimhakikishia kuwa “nyepesi nyepesi” hizo sio “fiksi” bali ni habari zinazohusu matukio ya kweli,ila tu yanachekesha kwa namna moja au nyingine.Kicheko ni afya.

“Nyepesi” za wiki hii ni pamoja na taarifa kwamba “wanene” 7 ndani ya baraza jipya la mawaziri la Gordon Brown (mrithi wa Tony Blair) wamekiri katika nyakati tofauti kuwa walishawahi kutumia “widi” (kwa wale ambao lugha ya mtaani ni mgogoro, “widi” ni bangi au marijuana).Siku kadhaa zilizopita,kiongozi wa chama cha wahafidhina (Conservative Party) David Cameron naye alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kupatikana nyeti kuwa alikuwa akivuta bangi katika siku za ujana wake.Cameron amekataa kuendelea na mjadala wa suala hilo akisema kuwa kila binadamu anaweza kufanya makosa hususan akiwa kijana.Alitaka wanaomshupalia wamhukumu kwa utendaji wake wa kazi wa sasa na sio mambo aliyofanya nyma.Kali zaidi ya zote ni pale Katibu wa Ofisi ya Mambo ya Ndani (Home Office-yaani ni sawa na Wizara ya Mambo ya Ndani huko nyumbani),Jacqui Smith,na waziri mmoja katika ofisi hiyo (hapa katibu wa wizara ni mkubwa kicheo kuliko waziri),Tony McNulty,walipotangaza hadharani kuwa nao walishawahi kuvuta bangi huko nyuma.Na “ushuhuda” huo umekuja wakati mwanamama huyo (Smith) akitangaza mpango wa serikali kuangalia upya uamuzi wa awali wa serikali ya Blair wa kushusha daraja (declassifying) la bangi.Habari kwamba viongozi hao wawili (ambao pamoja na majukumu mengine wana dhamana ya kudhibiti mihadarati) waliowahi kuwa wavuta bangi zimezua mjadala kama kweli wanapaswa kuendelea na nyadhifa zao.Pengine kinachowasaidia ni ukweli kwamba kuna wanasiasa wengine (wakiwamo mawaziri vivuli wa upinzani) ambao nao wameweka bayana kuwa walishawahi kuvuta bangi walipokuwa vijana.Uwazi na ukweli au vituko vya siasa?


Kuna habari nyingine ya majonzi lakini kwa namna flani inaweza inachekesha.Mwanamke aliyekuwa na uzito mkubwa kuliko wote hapa Uingereza,Nazima Hussein,amefariki na kuwaacha wanandugu wakiwa na wakati mgumu baada ya kubambikwa ushuru wa pauni 4,000 (zaidi ya shilingi milioni 8) kutoka kwa manispaa huko Southall,London.Ushuru huo ulitokana na gharama za kuuhudumia mwili wa marehemu ambao ulihitaji watumishi wa kikosi cha zima moto (firemen) 13 kuutoa mwili huo (uliokuwa na unene wa futi 3) kutoka katika flati aliyokuwa akaishi.Na walipoufikisha mochwari huko Uxbridge ilizuka kasheshe nyingine kwani hakuna toroli la kubebea maiti lililomtosha marehemu na pia mafriji yote ya kuhifadhia maiti hayakuweza kumudu ukubwa wa mwili wa marehemu huyo.Marehemu Nazima alifariki akiwa na uzito wa kilo 349 .Habari njema ni kwamba baada ya watu wa Manispaa “kusomeshwa” walikubali kupunguza gharama hadi pauni 3,000 (zaidi ya shilingi milioni 6).Ukiskia msiba mzito ndio huo.

Turejee nyumbani.Siku chache taifa limepewa changamoto ya kutosha kutoka kwa JK kuhusu suala la “kupima ngoma” (ukimwi).Na kwa mujibu wa taarifa za magazeti mbalimbali ya huko nyumbani watu kadhaa wameitikia wito wa Rais kwa kwenda kwenye vituo vya afya kupima ukimwi.Kwa mtizamo wangu,hamasa aliyotoa JK inaweza kuwa na matokeo makubwa sana kwani kwa upande mmoja inaweza kuwasaidia wale waliokuwa hawajui kama wameathirika kuanza kuchukua tahadhari ambazo zitawasaidia kuishi maisha marefu zaidi.Pia kwa wale ambao vipimo vitaonyesha hawajaathirika wanaweza kuachana kabisa na matendo ya ngono zisizo salama,na hata kumrejea Mola wao.Kadhalika,kwa wale watakaokutwa wana virusi vya ukimwi na wakati huohuo wana familia zinazowategemea wanaweza kupata nafasi mwafaka ya kuandaa “future” za familia zao.Jingine ni kwamba kampeni hiyo inaweza kuwafumbua macho wale vichwa sugu na viwembe wanaopenda kujidanganya kuwa ukimwi ni ajali kazini,na eti ajali haina kinga.

Waziri wa Afya amelielezea Bunge kuwa kuna mpango wa kuwapima ukimwi wale wote wanaofika hospitali kwa matibabu.Wazo hilo ni zuri sana lakini linahitaji tahadhari ya namna flani.Wapo wanaosema kuwa ukimwi ni sawa na maradhi mengine yasiyo na tiba kama kansa au kisukari.Hapana,ukimwi ni tofauti sana hasa kwenye namna jamii yetu inavyowaangalia walioathirika na ukimwi (unyanyapaa).Nadhani wapo watakaokubaliana nami kwamba baadhi ya watumishi wa taasisi za afya wana tabia ya kukiuka maadili ya taaluma yao kwa kutoa siri kuhusu afya za wagonjwa.Naamini baadhi ya wasomaji wameshawahi kunong’onezwa na dokta au nesi flani kuwa “yule nanihii anao (ukimwi).” Sasa kama Wizara ya Afya itatekeleza dhamira yake ya kutaka watu wote wanaofika hospitali wapime ukimwi inapaswa pia kuboresha mambo kadhaa ikiwa pamoja na kuhakikisha kuna washauri nasaha wa kutosha watakaoweza kuwasaidia hao watakaobainika kuwa “wanao.” Naamini pia kuwa kuna sheria inayowabana watumishi wa afya kutoa “siri” ya ugonjwa wa mtu,na katika mpango huu wa Wizara ni muhimu sheria hiyo ikaimarishwa zaidi kwani bila kufanya hivyo si ajabu watu wanaweza kukwepa kwenda hospitali sio kwa kuhofia kupimwa na kukutwa wanao bali kwa kuwaogopa hao wauguzi wasioweza kuhifadhi siri za wagonjwa.Pia Wizara inapaswa kuweka bayana iwapo mpango huo wa kumpima kila mgonjwa utakuwa ni suala la hiari au la lazima.Kwa hapa,wagonjwa wanahamasishwa kupima ukimwi lakini hawalazimishwi.Pasipo kuweka misingi mizuri,nia nzuri ya Wizara ya Afya inaweza kuleta mkorogano usio wa lazima,maana si ajabu tukasikia flani kanyimwa nafasi ya kuonana na daktari kwa vile tu kukataa kupima ukimwi.Ifahamike kuwa suala la kupima au kutopima ni haki ya mtu binafsi.

Pia nimesoma habari iliyonisikitisha husu kilio cha Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwamba imekuwa ikipata ushirikiano hafifu kutoka kwa waajiri katika suala la kuhakiki vyeti vya taaluma za waajiriwa.Unajua utandawazi umeleta mambo mengi sana ikiwa ni pamoja na fursa ya mtu kujipatia taaluma bila kutia mguu chuoni.Vipo vyuo kadhaa duniani vinavyotoa kozi kwa njia ya mtandao,lakini tatizo ambalo limekuwa likizisumbua hata nchi za Magharibi ni lile la baadhi ya vyuo vya kitapeli ambavyo vinaweza kukupatia cheti cha Udaktari wa Falsafa kwa wiki moja.Ukiona mfumuko wa madokta (sio wale wa hospitali) usikimbilie kufikira kuwa pengine siku hizi PhD zimekuwa rahisi.Ukweli ni kwamba PhD feki zimetapakaa sana kutokana na vyuo feki (japo vingine vimeandikishwa kisheria) ambavyo wanachojali wao ni fedha tu ya huyo anayehitaji PhD ya chapchap.Inatuuma sana sie wengine ambao tunazeekea maktaba kutafuta huo udokta “wa kwelikweli” huku wenzetu “wanasomea baa au kwenye nyumba ndogo zao” na wanaamka asubuhi na “hangover” wakiwa madaktari wa falsafa.Nadhani falsafa pekee waliyonayo “vilaza” hawa ni kuhusu waganga gani wa kienyeji wanasaidia mtu kula rushwa na aendelee kuonekana mwadilifu au namna ya kutogonganisha magari kati ya mama watoto na nyumba ndogo.

Ukweli mchungu ni kwamba TCU ina wakati mgumu kufanikiwa katika azma yake hiyo njema,kwani wengi wetu tunajua kuwa baadhi ya waajiri nao wana elimu za kutilia mashaka.Pia nadhani kuna mapungufu ya kisheria kuhusu matumizi ya vyeti feki,kwani nakumbuka jeshi la polisi halikuchukua hatua yoyote lilipobaini kuwa mbunge mmoja hakuwa mkweli kuhusu elimu yake ya sekondari.Sasa kama ufeki wa vyeti vya sekondari “sio big deal” kwa polisi je hao wenye PhD feki wataweza kuguswa?Enewei,tuna vita kadhaa tunazopenda zianze dakika hii:dhidi ya wala rushwa,majambazi,wabadhirifu,wauza unga,nk.Pengine siku moja itatangazwa vita ya kitaifa dhidi ya vyeti na taaluma feki.Yote yanawezekana.

Alamsiki


18 Jun 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Mwaka juzi gazeti maarufu duniani la TIME lilimtangaza George W.Bush kuwa “mtu wa mwaka (2004)” –au “Person of the Year” kwa lugha ya kwa mama.Katika uchambuzi wake kuhusu Bush,gazeti hilo lilimnukuu Rais huyo wa Marekani akisema kwamba “inapotokea kuwa hoja au mawazo yako yanazua mjadala au upinzani basi ni dalili kwamba yana uzito…kwa maana yangekuwa ya kipuuzi wala watu wasingejishughulisha nayo.”Alikuwa anazungumzia upinzani anaokumbana nao katika utendaji wa kazi zake za kila siku.Sio siri kuwa Bush anachukiwa na watu wengi hata ndani ya nchi yake.Lakini japo mie sio shabiki wake,namhusudu kwa jinsi anavyoweza kufanya mawazo yake yakubalike hata kwa wale ambao aidha hawayapendi au hawaafikiani nae.

Mwaka jana wakati nakuja huko nyumba,nilibahatika kukaa kiti kimoja na mama mmoja wa Kimarekani.Ni mtu mwongeaji sana,nami niliitumia nafasi hiyo kumdadisi siasa za Marekani hasa kuhusu mgawanyiko mkubwa wa kiitikadi nchini humo baina ya wale wa mrengo wa kulia(conservatives) na wale wa mrengo wa kushoto (liberals).Mwanamama huyo ambaye alinifahaisha baadaye kuwa ni mwanaharakati wa mazingira,alieleza kuwa kwa kiasi kikubwa mgawanyiko huo unachangiwa na siasa za Bush na maswahiba zake kama Dick Cheney,Donald Rumsfield,Paul Wolfowitz,na wengineo ambao wanajulikana kiitikadi kama “neo-conservatives” (sijui wanaitwaje kwa lugha yetu ya Taifa!).Miongoni mwa imani za hawa jamaa ni kuhakikisha kuwa Marekani inatumia ipasavyo nafasi yake kama Taifa lenye nguvu kabisa duniani.Kwa maana hiyo,ni “haki” yake kutumia “ubabe” wake kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuvamia zile nchi zinazoonekana kuwa “korofi”.Ipo siku nitawazungumzia kwa kirefu jamaa hawa ambao takriban wote ni wadau wa taasisi moja isiyo ya kiserikali iitwayo “The Project for The New American Century” (Mradi wa Karne Mpya ya Marekani,kwa tafsiri isiyo rasmi).Turudi kwa yule mama.Basi akanambia kuwa japo yeye binafsi ni mpinzani wa Bush na hao neo-conservatives wenzake kuna wakati huwa “anamzimia sana” kutokana na jinsi anavyoweza kufanya maamuzi yake yatekelezwe hata pale kwenye upinzani mkubwa.Waingereza wana msemo “kama humuwezi unayeshindana nae basi bora uungane nae tu,”na ndio maana hata wale wasioafikiana na Bush mwishowe hujikuta hawana jinsi bali kuendana na mawazo au maamuzi yake.

Muda mfupi uliopita nilipata ujumbe kutoka kwa rafiki yangu flani aliyeko huko nyumbani akinijulisha kuwa kuna mwandishi mmoja ameandika makala katika gazeti flani la kila siku (la hapo Bongo) kupingana nami katika hoja ya makala yangu moja ya hivi ambayo nilimfananisha Rais Jakaya Kikwete na kiongozi wa chama cha Conservatives cha hapa Uingereza,David Cameron.Kwa mujibu wa ujumbe niliopata,mwandishi huyo aliyepingana nami anadai sikuwa sahihi kuwalinganisha wanasiasa hao .Kwa bahati mbaya hadi natayarisha makala hii nilikuwa sijapata hoja zote zilizotolewa kukosoa makala yangu.Kwa mantiki hiyo itakuwa vigumu kujibu hoja baada ya hoja bali nachoweza kusema kwanza ni kwamba makala ya mwandishi huyo ni uthibitisho tosha kuwa gazeti hili la KULIKONI ni kipenzi cha wengi,na ndio maana linazaa hoja na makala katika magazeti mengine.Pili,kama gazeti la TIME lilivyomnukuu Bush naamini makala yangu hiyo ilikuwa na uzito ndio maana ikamsukuma mwandishi huyo kuijadili japo hakuafikiana na nilichokiandika,kwa kuwa laiti ingekuwa ya kipuuzi asingepoteza muda wake kupingana nayo.”

Kwa faida ya mwandishi huyo,Kikwete anashabihiana sana na David Cameron katika maeneo flani.Kwa mfano,wote wawili wako katika vyama ambavyo kabla ya wao kushika hatamu za uongozi kwa kiasi flani vilikuwa vinaonekana kama ni vya “wateule wachache” tu.Ushindi wa tsunami kwa Kikwete ni dalili tosha kuwa hata baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani walimpigia kura kuonyesha kuwa kuteuliwa kwake kuwa mgombea urais kuliiongezea nguvu CCM.Hoja nyingine japo inaweza kuwa si nzito sana ni kwamba wanasiasa hao wana sifa inayofanana ya kuwa handsome,na kwa taarifa yako u-handsome unalipa sana kwenye siasa.Lakini kingine ni lugha zao wanazotumia.Wanaongea lugha za watu wa kawaida wa mtaani,yaani wanajua wananchi wanatarajia nini kwao.Ndio,Cameron anafuata siasa za mrengo wa kulia kuelekea kati (right-centre) na Kikwete kama mwana CCM nadhani atakuwa ni wa siasa za mrengo wa kushoto kuelekea kati (left-centre),na japo Cameron ni Mwingereza na Kikwete ni Mtanzania,la muhimu hapa ni jinsi wananchi wanavyowahusudu kutokana na utendaji wao.Kura za maoni hapa Uingereza zinaonyesha kuwa Cameron amempiku Tony Blair kwa kupendwa na wananchi na naamini kuwa hata kama Watanzania wataamshwa usingizini kupiga kura za maoni,Kikwete ataibuka kidedea kwa sana.Kwenye siasa umaarufu wa mwanasiasa haugemei sana kwenye itikadi zake au chama chake,sehemu aliyozaliwa au umri wake bali kukubalika kwake miongoni mwa wananchi,na hicho ndicho kilichonipelekea kuwafananisha wanasiasa hao.

Mwisho,siamini kuwa mwandishi wa makala hiyo alikuwa anatafuta umaarufu kupitia makala yangu au gazeti hili la KULIKONI,bali alikuwa anatumia haki yake ya kikatiba kutoa mawazo yake.Nampa changamoto aendelee kusoma gazeti hili ilimradi isiwe kwa nia ya kupinga kila kitu hata kama ameishiwa na hoja.Kama alivyoimba Mista Two (Joseph Mbilinyi) kwenye wimbo wake “Sugu” kwamba huwezi kuizuia mvua kunyesha,KULIKONI ni kama jua na mvua,halizuiliki.

Alamsiki.

KULIKONI UGHAIBUNI

Mambo yakoje huko nyumbani?Natumaini kila mmoja anawajibika kwa namna yake katika ujenzi wa Taifa.

Kuna jamaa mmoja hapa anaitwa David Cameron.Huyu ni kiongozi wa chama cha wahafidhina (Conservative Party).Nia yangu si kuzungumzia wasifu wake,bali nataka nimlinganishe na mwanasiasa nyota wa huko nyumbani kwa muda huu,au kwa lugha ya “kwa mama” tunaweza kumuita “a man of the moment.” (kwa tafsiri ya haraka, “staa wa muda huu”).Nadhani msomaji mpendwa umeshajua ni nani ninayemzungumzia.Lakini hapa namuweka kando kidogo ili nikupashe kuhusu huyo Bwana Cameron na chama chake cha Conservatives (au Torry,kama kinavyojulikana hapa).Kwa tafsiri nyepesi hawa Conservatives ni watu wenye mrengo wa kulia na ndio wapiga kelele wakubwa kuhusu sera za uhamiaji na nyinginezo ambazo zinawagusa makabwela hususan wale ambao si wazawa wa hapa.Pengine jeuri kubwa ya wahafidhina hawa inatokana na uwezo wao wa kifedha.Fedha wakati mwingine huwa na tabia ya kumfanya binadamu asiwafikirie wenzie aliowazidi kiuwezo,na aghalabu anapowafikiria basi huwa ni kwa manufaa yake binafsi.

Kuibuka kwa Cameron kulichochewa zaidi na mwelekeo usioridhisha wa chama chake katika chaguzi mbalimbali.Wachambuzi wengi wa mambo ya siasa walikuwa wanahusisha mwenendo mbaya wa chama hicho na kile kinachoitwa kuwa “out of touch.”Nitafafanua.Chama kilicho “out of touch” ni kile ambacho machoni mwa watu wa kawaida kinaonekana kama hakijihusishi na maslahi ya walio wengi.Kwa mfano,hawa wahafidhina kwa miaka kadhaa wamekuwa wakikumbatia zaidi Waingereza weupe hasa wale wa tabaka la juu na la kati huku wakiwasahau wale wa tabaka la chini pamoja na Waingereza wengine ambao ni “wakuja” (kwa mfano wale wenye asili ya Asia,Caribbean,Afrika,n.k).Pia wamekuwa wakiwaona wageni (ikiwa ni pamoja na wanafunzi wanaochangia mamilioni ya paundi kwenye uchumi wa nchi hii) kama watu wanaokuja kuharibu uchumi,utamaduni na mazingira ya hapa.

Baada ya Waziri Mkuu wa mwisho kutoka Conservative kushika wadhifa huo,John Major,alipoangushwa na Tony Blair mwaka 1997,chama hicho kimebadilisha viongozi kadhaa lakini bila mabadiliko hayo kuwanufaisha kwenye chaguzi mbalimbali.Ndipo katika mchakato huo alipoibuka Bwana Cameron,kijana (ana miaka 40 tu),ana mvuto na haiba ya kutosha.Huyo bwana aliamua kuwapa wenzake kitu “laivu” kwamba chama chao hakina mvuto kwa wapiga kura,kinaonekana kuwa kiko zaidi kwa maslahi ya mabwanyenye kuliko makabwela,na hakizungumzi “lugha ya mtu wa kawaida mtaani.”Kuna mengi ya kumzungumzia huyo bwana lakini kilichonisukuma kuandika makala hii ni jinsi navyomuona anafanana na Jakaya Kikwete.Ukiachilia ukweli kwamba wote ni handsome lugha wanayoongea inafanana:lugha inayomgusha mtu wa kawaida na sio makundi flani tu katika jamii hususan wale wenye nguvu za kiuchumi.

Jakaya amenukuliwa mara kadhaa akiwausia viongozi wenzie kwamba wako madarakani kuwahudumia hao waliowaweka madarakani.Sio dhambi kuwa karibu na matajiri lakini ukaribu huo usiwe kwa ajili ya kuwaumiza wasio nacho.Utajiri sio dhambi,na kuna matajiri kadhaa (mfano Mzee Mengi huko nyumbani au Bill Gates huko Marekani) ambao utajiri wao umekuwa faraja kwa mamilioni ya wale wasio nacho.Matajiri wa aina hii ni muhimu kwao kuwa karibu na viongozi wa serikali,vyama vya siasa na taasisi nyingine kwa vile ni kwa ukaribu huo ndio miradi mbalimbali wanayoifadhilia inaweza kuwa na manufaa kwa wananchi.

Juzijuzi nilimwona Bwana Cameron kwenye luninga akiwa kwenye mtaani wakati wa kampeni za chama chake kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kwa upande wa England.Jinsi alivyokuwa akijichanganya na watu ilitosha kabisa kumfanya hata mtu aliyekuwa akikichukia chama cha wahafidhina afikirie upya.Siku chache baadae nikasoma kwenye mtandao kuwa Jakaya ameweka historia kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kutembelea wafungwa magerezani.Yalipotokea mauaji ya kutatanisha ya wale wachimba madini wa Mahenge hakukawia kuunda tume,na kinyume ya ilivyozoeleka mara baada ya kupewa ripoti na tume akaweka matokeo hadharani.Aliporejea tu kutoka Kusini mwa Afrika hakukawia kwenda kuwaona majeruhi wa tukio la uporaji wa fedha za NMB pale Ubungo,na kutoa maagizo papo hapo.Lakini si Jakaya pekee bali hata “luteni” wake Lowassa.Ghorofa lilipoanguka Keko hakusubiri kuletewa taarifa bali alikwenda kujionea mwenyewe na kuchukua hatua hapohapo, “mafuriko” yalipoielemea Sinza hakukawia kwenda kushuhudia hali ilivyo na kuwaamuru wahusika wachukue hatua za haraka.

Laiti kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya aliyokuja nayo Kikwete itaweza kufikia hatua ya kuigwa na viongozi kuanzia ngazi ya serikali ya mtaa,kata,tarafa,wilaya na mkoa,basi muda si mrefu Bongo itakuwa sehemu ya neema.Na mwenyewe Jakaya amekuwa akisema kuwa Tanzania yenye neema inawezekana.Enyi viongozi mliolala hebu amkeni,msisubiri kuamshwa.Jisikieni aibu pale mnapokwenda kinyume na spidi ya kiongozi wenu mkuu.

Alamsiki

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.