Rais Kikwete amefungua milango
KWA mara ya pili ndani ya takriban kipindi cha wiki moja, Tanzania imepoteza wabunge wawili. Kabla majonzi hayajatuisha kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CHADEMA, Regia Mtema, taifa likapatwa na msiba mwingine wa Mbunge wa Arumeru Mashariki kwa tiketi ya CCM, Jeremiah Sumari.
Kila kifo kinaacha pengo lakini kifo cha kiongozi (awe wa familia kama mzazi au wa jamii) kinaacha pengo linalowagusa na kuwaathiri wengi. Japokuwa yayumkinika kuhisi kuwa katika zama hizi za siasa za kuendekeza maslahi kuna wanaofurahi vifo vya viongozi kwa vile vitatoa nafasi ya wao kugombea, ukweli unabaki kuwa ni vigumu kupata mrithi atakayelingana kwa kila kitu na marehemu (hasa katika utekelezaji wa majukumu).
Kama nilivyoandika katika makala ya wiki iliyopita kuhusu kifo cha Regia, njia bora ya kumuenzi marehemu Sumari ni kudumisha mema yote aliyofanya wakati wa uhai wake. Kwa wanaofikiria kumrithi nafasi yake (na kwa atakayeteuliwa kumrithi nafasi ya Marehemu Regia) changamoto kubwa itakuwa kwenye kuwaenzi viongozi hao kwa kuwajibika ipasavyo. Japo utendaji kazi bora wa kiongozi anayerithi madaraka kutoka kwa kiongozi marehemu hauwezi kurejesha uhai, kwa kiasi fulani unasaidia kupunguza machungu ya wananchi walioathiriwa na pengo lililotokana na kifo husika.
Katika mila na desturi za kiafrika, shughuli ya msiba inatawaliwa na majonzi na kwa kiasi kikubwa ni kumbukumbu kwa kila aliyehai kuwa sote “tulitoka kwenye udongo na tutarejea kwenye udongo.” Misiba inapaswa kutukumbusha kuwa sote ni wasafiri na kila nafsi ya mmoja wetu itaonja mauti.
Moja ya matukio yaliyotawala msiba wa Regia ni habari kwamba Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbroad Slaa, alikwepa kusalimiana na Rais Jakaya Kikwete. Habari hiyo ilichukua uzito mkubwa kiasi cha kukaribia kufunika tukio la huzuni lililowakutanisha viongozi hao huko Ifakara.
Kwa sababu anazozijua mwenyewe, jamaa mmoja aliamua kusambaza waraka katika blogu kadhaa ndani na nje ya nchi kukemea kitendo hicho cha Dk. Slaa. Mtu huyo ambaye hakufanya jitihada za kuficha itikadi yake ya siasa, akaenda mbali zaidi na kudai kuwa kilichosababisha Katibu Mkuu huyo wa CHADEMA kutosalimiana na Rais ni amri iliyotolewa na mwenza wa Dk. Slaa (Josephine).
Pengine kwa kuelewa kuwa kukalia kimya jambo hilo kungeibua maneno zaidi, hatimaye Dk. Slaa alieleza kilichomfanya ashindwe kusalimiana na Rais Kikwete. Kwa wanaojua protokali, mtu hakurupuki tu na kwenda kusalimiana na kiongozi mkuu wa nchi hasa ikizingatiwa kuwa kumkaribia kiongozi huyo (hata kama ni kwa nia nzuri) kunawafanya walinzi wake watafsiri kama tishio la usalama kwake.
Kadhalika, Dk. Slaa alieleza bayana kuwa kilichompeleka Ifakara ni kumzika Regia na si vinginevyo. Kwa lugha nyingine, alimaanisha kuwa isingehitaji kutokea kifo cha mbunge au kiongozi wa chama ndipo “mahasimu wawili” (kama ‘wazushi’ wa habari hiyo walivyojaribu kutuaminisha) wakutane na kupeana mikono.
Lakini kama kuwasuta wanaokuza matukio madogo, siku chache baadaye vyombo vya habari vilitawaliwa na picha inayomwonyesha Rais Kikwete na Dk. Slaa wakipeana mikono baada ya mazungumzo kati ya Rais na viongozi wa CHADEMA yaliyofanyika Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam.
Sijui waliozusha kuwa Josephine alimkataza Dk. Slaa wanasemaje kuhusu hilo. Labda watazusha kuwa alimtoroka mwenza wake kama sio kuzusha kuwa kiongozi huyo wa CHADEMA aliamua kuambatana na viongozi wenzie Ikulu ili kujisafisha kutokana na tukio la Ifakara.
Inasikitisha kuona mambo ya msingi yakigubikwa na porojo zisizo na mashiko. Binafsi, moja ya mambo ya msingi yaliyonigusa na kunipa matumaini mapya ni jinsi Rais Kikwete na takriban uongozi wake mzima (serikalini na huko CCM) walivyoweza kuweka kando tofauti za kiitikadi na kumzika Regia kama kiongozi wa Watanzania na si mbunge wa CHADEMA pekee.
Mara kadhaa nimekuwa nikishutumiwa kwa kumkosoa au kumlaumu Rais Kikwete. Lakini siku zote nimejitahidi kusisitiza kuwa lawama hizo na kukosoa hakumaanishi chuki au husuda bali ni kwa minajili ya ustawi wa taifa letu.
Natambua kuna uwezekano wa baadhi ya wasomaji kuhisi nimefikia hatua ya kumpongeza Rais Kikwete kwa vile tukio husika linaihusu CHADEMA (ambayo nimekuwa nikituhumiwa kuipendelea na baadhi ya watu, huku wengine wakidai mimi ni mwanachama wa chama hicho.)
Yeyote aliyesoma salamu za rambirambi zilizotolewa na Rais Kikwete kwenda kwa familia ya marehemu Regia na CHADEMA hatoshindwa kubaini kuwa zilikuwa zimetoka moyoni kwa dhati. Hakukuwa na hata chembe ya tofauti za kiitikadi bali hisia za kibinadamu pindi zinapopatikana habari za kifo.
Naomba nisisitize kuwa tukio hilo sio pekee au la kwanza kwa Rais Kikwete kuonyesha kile wanachokiita Waingereza ‘human side’ (ubinadamu wake, kwa tafsiri isiyo rasmi). Mara nyingi mkuu huyo wa nchi ameonyesha kuguswa kwa dhati kila anapokuwa kwenye matukio ya huzuni.
Japo wakati mwingine huishia kulaumiwa kuwa ‘haisaidii kuonyesha uchungu ilhali janga husika lingeweza kuzuilika’ (kwa mfano kwenye matukio ya milipuko ya mabomu huko Mbagala na Gongo la Mboto), hiyo haindoi ukweli kuwa ameguswa na matukio hayo.
Lakini pamoja na pongezi hizi kwa Kikwete na CCM kwa ujumla pengine ni muhimu kukumbushana kuwa kama tunaweza kushikamana wakati wa misiba kwa nini basi iwe vigumu kufanya hivyo nyakati nyingine?
Kwa lugha nyingine, kwa nini tusubiri hadi kiongozi wa chama cha upinzani afariki ndipo tuonyeshe kuwa tofauti za kiitikadi haziondoi ukweli kuwa sote ni Watanzania tunaoweza kutofautiana kimtizamo au kiitikadi pasipo umuhimu wa ‘kuong’oana’ macho.
Japo Kikwete si mahiri katika kuendekeza siasa za uhasama (aidha kwa vile si muumini wa dhana hiyo au anatumia wasaidizi wake kukwepa lawama zinazoweza kuelekezwa kwake), kiujumla chama anachoongoza, yaani CCM, kimekuwa kikifanya jitihada kubwa kuuaminisha umma kuwa vyama vya upinzani ni mithili ya mikusanyiko ya maharamia wasioitakia mema nchi yetu.
Ukisikiliza hotuba za baadhi ya viongozi wa CCM wanapovizungumzia vyama vya upinzani unaweza kabisa kutamani kwenda Idara ya Uhamiaji kuhoji iwapo viongozi hao wa upinzani ni raia halisi wa nchi hii. Hivi haiwezekani kukosoana pasipo kupandikiza chuki ya uadui miongoni mwetu?
Katika tafiti za kitaaluma, kuna hatua ambapo mtafiti huwezi kubashiri matokeo ya utafiti husika kwa kuzingatia dhana alizotengeneza (hypothesis). Japo makala hii si sehemu ya utafiti lakini ningependa kutengeneza dhana kuu mbili zinazoweza kubashiri matokeo fulani.
Ya kwanza, kwa vile Rais Kikwete na CCM wameweza kututhibitishia kuwa tofauti zao za kiitikadi na CHADEMA si za kiadui, na ndio maana wameshiriki kikamilifu katika msiba wa marehemu Regia, Tanzania inaingia kwenye zama mpya za siasa za upendo na kukosoana kistaarabu.
Ya pili, kwa vile siku chache baada ya msiba wa mbunge wa CHADEMA, Rais Kikwete aliwaalika viongozi wa CHADEMA kufanya majadiliano nao, tunaanza kushuhudia ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Rais (na pengine CCM kwa ujumla) katika uongozi wa nchi.
Matokeo yanayotarajiwa ni kwamba badala ya muda mwingi wa ujenzi wa taifa letu kutumika kunyoosheana vidole, kuitana majina ya ajabu ajabu na upuuzi mwingine, sasa tunaweza kuona uongozi wa nchi ukifanya kazi bega kwa bega kwa lengo la kuikomboa Tanzania yetu kutoka katika lindi la umasikini (licha ya rasilimali lukuki tulizojaliwa) na kuunganisha nguvu kukabiliana na kundi la maharamia walioigeuza nchi yetu kuwa ‘shamba la bibi’ kwa ufisadi.
Unaweza kudhani labda aya tatu za hapo juu nimeziandika nikiwa ndotoni. La hasha. Kila nililoandika linawezekana kwani sababu (ya kushirikiana) ipo, na uwezo wa kufanya hivyo upo (kama ilivyothibitika katika tukio hilo la msiba wa marehemu Regia), ila kinachokosekana ni nia tu.
Ni matarajio ya safu hii kuwa Rais Kikwete (ambaye naamini anasoma makala hizi au anasimuliwa na wasaidizi wake) hatorudi nyuma katika kufungua sura mpya ya siasa za maelewano na ushirikiano kwa manufaa na ustawi wa Tanzania yetu. Penye nia pana njia.