Showing posts with label RAIA MWEMA. Show all posts
Showing posts with label RAIA MWEMA. Show all posts

9 Mar 2017


KATIKA hitimisho la makala yangu katika safu hii wiki iliyopita niliahidi kuwaletea uchambuzi kuhusu mivutano ya kugombea madaraka (power struggles) ndani ya chama tawala CCM.Kwa bahati nzuri, kati ya makala hiyo na hii, kumejitokeza tukio ambalo linaweza kuhusishwa na mada hiyo ninayoiongelea katika makala hii.
Wiki iliyopita, Rais Dk. John Magufuli alimteua Salma Kikwete, mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri.Uteuzi huo umepokelewa kwa hisia tofauti, na kuzua mjadala unaoendelea hadi wakati ninaandika makala hii.
Kwa upande mmoja, inaonekana kama kuna mwafaka wa kutosha kwamba Rais ametumia madaraka yake kikatiba kufanya uteuzi huo.
Kwa upande mwingine, pengine kutokana na ukweli kuwa hii ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa Rais kumteua mke wa mtangulizi wake kuwa mbunge, kuna hisia za hapa na pale kwamba uteuzi huo hauleti picha nzuri.
Kwamba, labda kwa vile Salma alikwishakaa Ikulu kwa miaka 10 kama mke wa Rais basi pengine nafasi hiyo ya ubunge wa kuteuliwa ingeenda kwa mtu mwingine.
Hata hivyo, licha ya kuwa Rais ameshaeleza kwa nini alifanya uteuzi huo, ukweli unabaki kuwa Katiba inamruhusu kufanya hivyo, na Salma Kikwete kama Mtanzania mwingine ana haki ya kuteuliwa kushika wadhifa wowote ule bila kujali historia yake kama mke wa rais mstaafu.
Lakini licha ya kuruhusiwa na Katiba kufanya uteuzi, kwa sisi tunaofuatilia kwa karibu siasa za Tanzania, tunauona uteuzi huo kama wa kimkakati, kwa maana ya Dk. Magufuli kujipanga vyema kwa ajili ya mitihani miwili ya kisiasa inayomkabili:  uchaguzi mkuu wa CCM baadaye mwaka huu, na kubwa zaidi, kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Ni hivi, katika nchi zetu zinazoendeshwa kwa mazoea, ni dhahiri kuwa kiongozi wa aina ya Magufuli hawezi kuwa maarufu miongoni mwa waliozoea kuona mambo yakiendeshwa sio yanavyopaswa kuwa, au kwa njia sahihi, bali kwa mazoea, hata kama mazoea hayo yana matokeo hasi.
Viongozi wa aina ya Magufuli wanaominya mianya ya ulaji, wanaozuia safari za ‘matanuzi’ ughaibuni, na wanaojaribu kuwa upande wa wananchi wanyonge badala ya kuendelea kutetea masilahi ya tabaka tawala, hawawezi kuwa na marafiki wengi.
Na ukweli kuhusu Dk. Magufuli ni kwamba kwa muda mfupi aliokaa madarakani ametengeneza maadui wengi tu serikalini na ndani ya chama chake. Kwa serikalini, maadui hao sio tishio kwake kwa sababu mfumo wa utawala sio tu unamwezesha kuwadhibiti kirahisi maadui hao bali pia hata kufahamu dhamira zao ovu mapema.
Changamoto kubwa zaidi kwake ipo ndani ya chama chake. Sio siri kwamba CCM aliyoirithi Magufuli imekuwa, kwa muda mrefu, kichaka cha mafisadi, sehemu ambayo watu waliohitaji kinga dhidi ya mkono mrefu wa sheria walikimbilia huko. Hii haimaanishi kuwa CCM nzima imesheheni watu wa aina hiyo.
Kwa vile licha ya kuwa Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho tawala, Magufuli ni kama mgeni kwenye medani za uongozi wa juu wa chama hicho, maadui zake ndani ya chama wanaweza kutumia fursa walizonazo – kama vile ushawishi wao au kukubalika kwao – kumhujumu kiongozi huyo.
Lakini kama ilivyo serikalini, Magufuli ametengeneza maadui ndani ya chama chake kwa sababu ile ile ya kuanzisha zama mpya za kuachana na siasa za/uongozi wa mazoea.
Katika ngazi mbalimbali za uongozi wa chama hicho, kuna viongozi waliozoea kujiona kama wanaendesha kampuni binafsi, huku wakitumia fursa zao kufanya ufisadi. Hali hiyo ilisababisha baadhi ya watu kuiona alama ya jembe na nyundo kwenye bendera ya CCM ikigeuka kuwa umma na bunduki kuashiria ulaji.
Uadui mkubwa ni kinyang’anyiro cha urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020. Kwa mujibu wa wajuzi wa mambo, kuna jitihada za chinichini ndani ya chama hicho tawala kuangalia uwezekano wa kumfanya Magufuli awe rais wa awamu moja.
Angalau hadi muda huu hakuna dalili kuwa uchaguzi mkuu wa CCM unaweza kuwa na athari zozote katika uenyekiti wa Magufuli japo ni wazi maadui zake watatumia kujipanga kwa ajili ya kinyang’anyiro cha mwaka 2020.
Kwa kumteua Salma Kikwete, Magufuli amemleta karibu mtu muhimu katika siasa za CCM, na pengine kujenga ngome imara ya kumwezesha sio tu kushinda uchaguzi mkuu ujao kwa tiketi ya CCM bali pia kumrahisishia kazi ngumu ya kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho tawala.
Nimalizie kwa kuahidi kuendelea na uchambuzi huu katika makala zijazo
Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

2 Mar 2017


MWAKA 1990 nikiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, kuliibuka mgomo mkubwa uliodumu kwa siku kadhaa. Kwangu, mgomo huo ulikuwa ni mtihani mkubwa, kwani sikuwa ‘mwanafunzi’ wa kawaida, bali nilikuwa kamanda wa wanafunzi au chifu.
Shule hiyo, pamoja na Sekondari ya Wasichana Tabora, zilikuwa shule pekee nchini zilizokuwa na mchepuo wa kijeshi. Hata sare zetu zilikuwa ‘magwanda,’ na baadhi ya walimu wetu wakiwa askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).
Huo wadhifa wa kuwa chifu ulikuwa ni ukiranja mkuu. Kwa hiyo mgomo huo ulitokea wakati nikiwa kiranja mkuu katika shule hiyo yenye historia ya kipekee. Chanzo kikuu cha mgomo huo kilikuwa madai ya wanafunzi kuwa chakula kilikuwa duni.
Nimesema kuwa mgomo huo ulikuwa mtihani kwangu kwa sababu kwa upande mmoja nilikuwa mwanafunzi kama wenzangu waliogoma, na upande mwingine, nilikuwa sehemu ya uongozi wa shule hiyo. Na kwa hakika, nilikuwa kiungo kati ya utawala na wanafunzi.
Hatimaye mgomo huo ulimalizika na kwa vile sikuwa nimeelemea upande wowote wakati wa mgomo huo, kumalizika kwake kuliniacha nikiwa ‘sijauudhi’ upande wowote – wa utawala wa shule na wa wanafunzi wenzangu. Na nyenzo yangu muhimu ilikuwa kusimamia kwenye kanuni na sheria, sambamba na kushawishi matumizi ya busara ili kufikia mwafaka. Mara nyingi huwa vigumu kuziridhisha pande zote za mgogoro husika.
Nimelikumbuka tukio hilo muhimu baada ya kutupia jicho baadhi ya mambo yanayoendelea kwenye Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli. Ni kwamba, kwa kiasi kikubwa, baadhi ya mawaziri wameonyesha bayana kuwa aidha hawaendani na kasi ya Dk. Magufuli au wanamhujumu kwa makusudi.
Baadhi yetu tunaofuatilia siasa za Tanzania tulikwishahisi mapema kuwa uamuzi wa Dk. Magufuli kuzileta baadhi ya sura zile zile ambazo zilikuwa mzigo kwa taifa huko nyuma, ungeweza kusababisha matatizo mbele ya safari.
Kwa kurejea tukio la mgomo nililolielezea hapo juu, Rais anajikuta kwenye ‘mtihani’ kwa sababu kwa upande mmoja anapaswa kuwa upande wa watendaji wake aliowateua kwa umakini mkubwa (ndio maana ilichukua wiki kadhaa kabla Rais hajatangaza Baraza lake la Mawaziri) na kwa upande mwingine yeye sio rais wa mawaziri wake pekee bali Watanzania wote.
Sakata la vita dhidi ya dawa za kulevya lililoibuliwa upya na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, limechangia kwa kiasi kikubwa kuonyesha kukosekana ‘visheni’ ya pamoja miongoni mwa mawaziri katika Baraza la Mawaziri la Rais Magufuli.
Kwa mtazamo wangu, pengine ingekuwa vema kama Rais alipounda Baraza lake la Mawaziri angeepuka kuwaingiza makada wengi wa chama chake kwenye baraza hilo. Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba chama hicho tawala kimeshika hatamu za uongozi wa taifa na ukada unawapa jeuri baadhi ya watendaji wa serikali. Na si kosa lao kwa sababu ukada umekuwa nyenzo muhimu katika uongozi wa Tanzania huku baadhi ya wakosaji wakiepuka adhabu kwa vile tu ni makada muhimu.
Wakati wa sakata la dawa za kulevya lililoibuliwa na RC Makonda, angalau waziri mmoja alijitokeza waziwazi kupingana na uamuzi wa kutangaza majina ya watuhumiwa, akidai hatua hiyo ingeathiri chapa (brands) za wasanii waliotajwa katika orodha ya watumiaji au wauzaji wa dawa za kulevya.
Kanuni muhimu ya uongozi ni uwajibikaji wa pamoja, na pindi mtendaji mmoja akikosea, basi kuna fursa ya kuongea tofauti za kimtazamo faragha badala ya kuitisha mikutano na waandishi wa habari kuonyesha mpasuko.
Naomba ieleweke kuwa sio ninakemea uhuru wa kujieleza miongoni mwa watendaji wa serikali, ikiwa pamoja na mawaziri, lakini uhuru huo sharti uzingatie kanuni.
Hata tukiweka kando hali tata iliyotokana na sakata hilo la dawa za kulevya, haihitaji uelewa mkubwa wa siasa za nchi yetu kutambua kuwa baadhi ya watendaji wa Rais Magufuli ni mzigo kwake. Ni mzigo kwa vile aidha hawaendani na kasi yake au wanafanya makusudi kwa minajili ya kumkwamisha.
Ndio maana, picha inayopatikana mtaani ni kwamba mara kadhaa ni mpaka rais aingilie kati ndio hiki au kile kifanyike. Swali linalojitokeza ni je, rais haoni hali hiyo? Je, washauri wake (kwa mfano ndugu zetu wa Idara ya Usalama wa Taifa) nao hawaoni hali hiyo?
Nimalizie makala hii kwa kumshauri Rais Dk. Magufuli kuwa pengine imefika wakati mwafaka kufanya utumbuaji kwa watu baadhi ya aliowakabidhi dhamana ya uwaziri kwenye kabineti yake. Asipochukua hatua mapema, inaweza kugharimu urais wake.
Nitaendelea na makala hii wakati mwingine kujadili kile Waingereza wanaita ‘power struggles’ zinazoendelea ndani ya CCM na ambazo kwa kiasi fulani zinachangia utendaji duni wa baadhi ya watendaji wa Rais Magufuli (kwa maana ya utendaji duni kama mkakati wa makusudi).

Baruapepe: [email protected] Tovuti: www.chahali.com Twitter: @chahali

23 Feb 2017


MOJA ya sababu zilizosababisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kifikie hatua ya kuwa chama kikuu cha upinzani ni msimamo mkali ambao chama hicho ulikuwa nao dhidi ya ufisadi.
Kadhalika, Chadema sio tu kilionyesha dalili za kuweza kuwa mbadala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bali pia kiliweza kujijengea hadhi kubwa ya ‘sauti ya wasio na sauti’ (voice of the voiceless) na chenye kupigania haki za wanyonge.
Chadema hawakuuchukia ufisadi kwa maneno matupu bali kwa vitendo, ambavyo mara nyingi vilisababisha viongozi wakuu wa chama hicho kuchukuliwa hatua na Bunge au serikali/vyombo vya dola. Katika harakati za kuwapigania wanyonge, baadhi ya wafuasi wa chama hicho walipoteza maisha na wengine kuachwa na ulemavu wa kudumu.
Japo kwa kiasi kikubwa, mafanikio ya Chadema kisiasa yalichangiwa na ‘madudu’ ya chama tawala CCM takriban katika kila eneo, hiyo sio kusema kuwa chama hicho cha upinzani ‘kilidondoshewa’ mafanikio hayo.
Kupitia viongozi wake makini, chama hicho kiliwekeza vya kutosha katika upatikanaji wa taarifa sahihi, ambazo japo kila zilipotolewa zilikutana na vitisho vya “nitawaburuza mahakamani,” hakuna mmoja wa waliotoa vitisho hivyo aliyethubutu kwenda mahakamani.
Orodha ya ufisadi ulioibuliwa na Chadema ni ndefu, lakini matukio muhimu kabisa, na yatakayobaki katika historia ya taifa letu ni pamoja na skandali nzito kama ile ya Richmond, EPA, Buzwagi, Meremeta, Tangold, ‘Minara Pacha’ ya Benki Kuu na Deep Green Finance.
‘Dream team’ ya Dk. Willbrord Slaa, Zitto Kabwe na Freeman Mbowe ilikuwa ‘moto wa kuotea mbali’ kiasi kwamba ingekuwa ni ushirikiano wa ushambuliaji katika soka basi ni sawa na ‘MSN’ ya Messi, Suarez na Neymar huko Barcelona.
Ilifika mahala ambapo mstari ulichorwa bayana kwamba Chadema kilikuwa chama cha kutetea maslahi ya wanyonge wa Tanzania, hususan kwa kupambana na kila aina ya ufisadi, ilhali chama tawala CCM kikionekana kama kichaka cha kuhifadhi mafisadi, huku kikiandamwa na skandali moja baada ya nyingine.
Kwa hakika, tukiangalia jinsi Tanzania yetu ilivyotafunwa katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, ni maajabu makubwa kushuhudia Mahakama Maalumu ya Ufisadi ikiwa haina kesi huku waziri husika, Dk. Harrison Mwakyembe akituhadaa kuwa kukosekana kwa kesi ni ishara ya mafanikio ya mahakama hiyo. Nchi yetu haiishiwi vituko.
Laiti dhamira nzuri ya Rais Dk. John Magufuli kuanzisha mahakama hiyo ya ufisadi ingeambatana na utashi wa kisiasa ili kuifanya iwe na ufanisi, basi kazi kubwa iliyofanywa na Chadema huko nyuma ingekuwa imeirahisishia kazi mahakama hiyo.
Sogeza mbele (fast-forward) hadi mwaka 2015 na kuendelea (hadi muda huu ninapoandika makala hii), Chadema ile iliyowanyima usingizi mafisadi na kuwapa matumaini walalahoi imegeuka kuwa kama taasisi inayoendeshwa na matukio. Kimsingi, sidhani kama hata uongozi wa juu – achilia mbali wananchama na wafuasi wa kawaida wa chama hicho – wanaofahamu chama hicho kinasimamia nini kwa sasa.
Kwa tunaofahamu ‘yanayoendelea nyuma ya pazia’ ya siasa za Tanzania, Chadema ilihujumiwa vya kutosha, huku miongoni mwa waliokihujumu chama hicho wakiwa watu muhimu walioshiri kukifikisha chama hicho katika umaarufu wa kisiasa. Tamaa ya madaraka kwa baadhi ya viongozi muhimu wa chama hicho ilitoa fursa mwafaka kwa hujuma hizo kufanikiwa.
Lakini kosa kubwa kabisa walilofanya Chadema, na ambalo linaweza kuwa na madhara makubwa zaidi yenye utata unaoendelea hivi sasa ni kumpokea aliyekuwa kada maarufu wa CCM, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, sio tu kujiunga na chama hicho bali pia kuwa mgombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Uamuzi wa Chadema kumpokea Lowassa na kumfanya mgombea wa urais ulikuwa ni kioja cha kihistoria, hasa ikizingatiwa kwamba Chadema hiyo hiyo ilitumia takriban miaka tisa mfululizo kumtambulisha Lowassa kama kinara wa ufisadi nchini Tanzania. Sasa kwa busara japo ‘kiduchu’ tu, huwezi kumchafua mtu kwa miaka tisa mfululizo kisha ukajaribu kumsafisha kwa miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu.
Ninakumbuka wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka juzi, kada mmoja wa ngazi za juu wa CCM alinieleza kuwa “kwa kumpokea Lowassa, Chadema wameturahisishia safari yetu ya Ikulu,” akibainisha kuwa ajenda ya ufisadi ingeweza kuiangusha CCM katika uchaguzi huo. Hata hivyo, kwa Chadema kumkumbatia ‘mwanasiasa waliyemwita fisadi miaka nenda miaka rudi,’ chama hicho kilijinyima uhalali wa kushikilia hoja ya ufisadi dhidi ya CCM.
Kibaya zaidi, Chadema haijaona umuhimu wa kufanya sio tu tathmini ya kina ya ‘athari za ujio wa Lowassa,’ bali pia jitihada za kuwarejesha wafuasi wa chama hicho ‘walioondoka na Dk. Slaa (yaani waliokerwa na ujio wa Lowassa na kuamua kujiweka kando)
Nimalizie makala hii kwa kuikumbusha Chadema kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa chama hicho kujitathmini upya, na kifanye jitihada za kurudi zama zile za ‘List of Shame,’ EPA, Richmond, nk – yaani kuwa sauti ya wasio na sauti na wapigania haki za wanyonge. Ukimya wa Lowassa katika kipindi muhimu kama hiki cha vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya huku Mwenyekiti Freeman Mbowe akitajwa kuwa mtuhumiwa wa biashara hiyo ni ishara mbaya kwa chama hicho kilichowahi kuwa mbadala wa CCM.

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

16 Feb 2017


KATIKA nchi nyingi za huku Magharibi, kila mwanzoni mwa mwaka Idara zao za Usalama wa Taifa huchapisha ripoti inayoelezea kwa kina maeneo yanayoonekana kuwa yanaweza kuwa tishio kwa usalama wa mataifa husika.
Kwa ‘akina siye’ kwa maana ya nchi nyingi za Afrika na Dunia ya Tatu kwa ujumla, kila chapisho la Idara ya Usalama wa Taifa ni siri kuu isiyopaswa kuonekana kwa mwananchi wa kawaida.
Na ni katika mazingira haya ya kufanya ‘kila taarifa ni siri’ hata zile ambazo zingepaswa zifahamike kwa wananchi, ndio tunashuhudia uhusiano kati ya Idara zetu za Usalama wa Taifa na wananchi wa kawaida sio mzuri, uliojaa shaka na kutoaminiana, kwa kiasi kikubwa wananchi kuziona taasisi hizo kama zipo dhidi yao.
Na hiyo ndio moja ya sababu kuu zilizonifanya, mwaka jana, kuchukua uamuzi wa kuandika kitabu kuhusu taaluma ya uafisa usalama wa taifa, si kwa Tanzania pekee, bali duniani kwa ujumla. Na kama nilivyotarajia, wasomaji wengi wamenipa mrejesho kuwa kitabu hicho kimewasaidia mno kutambua kuwa Idara za Usalama wa Taifa ni ‘rafiki mwema’ kwao na ni taasisi muhimu mno kama moyo au ubongo kwa nchi husika.
Kadhalika, wasomaji wengi wamekiri kuwa kabla ya kusoma kitabu hicho walidhani kuwa kazi kuu za watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa ni kutesa watu, u-mumiani (kunyonya damu) na vitu vingine vya kuogofya, na kwamba hakuna lolote jema kwa masilahi ya wananchi.
Sitaki kujipongeza lakini ninaamini kuwa kitabu hicho kimesaidia sana, pamoja na mambo mengine, kujenga taswira nzuri kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa, hasa ikizingatiwa kuwa kutokana na wananchi wengi kutofahamu umuhimu wa taasisi za aina hiyo, imekuwa ikibebeshwa lawama nyingi isizostahili.
Lakini lengo la makala hii sio kuongelea kitabu hicho au shughuli za Idara za Usalama wa Taifa, bali kuzungumzia maeneo ambayo kwa utafiti, uchambuzi na mtazamo wangu yanaweza kuwa tishio kwa usalama wa taifa letu.
Eneo la hatari zaidi ni kuminywa kwa kile kinachoitwa kwa kimombo ‘political space,’ yaani mazingira ambayo shughuli za kisiasa hufanyika pasi kuingiliwa na dola. Bila hata haja ya kuingia kiundani kwenye hili, ukweli ni kwamba kuminya ‘political space’ sio tu kunajenga chuki ya wananchi kwa dola bali pia kunazuia fursa ya wananchi kujadiliana kuhusu manung’uniko yao, ambayo sote tunafahamu kuwa ‘yakijaa sana bila kuwepo upenyo wa kuyapunguza, yatapasuka pasipotarajiwa.’
Suala jingine ni hisia za ukabila/ukanda. Kuna kanuni moja inasema ‘ni silika ya mashushushu kuongea na kila mtu.’ Naam, kwa kuongea na kila mtu, inakuwa rahisi kusikia ‘mazuri’ na ‘mabaya,’ na pia mitazamo ya watu mbalimbali hata ile tusioafikiana nayo.
Na katika kuongea na watu mbalimbali, nimebaini manung’uniko ya chini chini kuhusu ukabila na ukanda, huku baadhi ya watu wakienda mbali na kutamka bayana kuwa wanaona kama eneo fulani analotoka kiongozi fulani linapendelewa zaidi.
Sambamba na ukabila ni udini. Hili ni tatizo kubwa pengine zaidi ya kuminywa ‘political space’ na hilo la ukanda/ukabila, kwa sababu tatizo hili limekuwepo kwa muda mrefu huku kila awamu ya serikali iliyopita ikipiga danadana kwenye kusaka ufumbuzi wa muda au wa kudumu.
Wakati angalau kuna jitihada za makusudi za kupunguza pengo kati ya walio nacho na wasio nacho, umasikini bado ni tatizo kubwa, ni muhimu kwa serikali kuwa ‘honest’ kwa wananchi kwa kuepuka kutilia mkwazo takwimu za kupendeza (na lugha ya kitaalamu) zinazokinzana na hali halisi mtaani. Rais Dk. John Magufuli awaagize watendaji wake wawe wakweli kwa wananchi, wawafahamishe taifa linapitia hatua gani muda huu, na matarajio ni yapi, na waongee lugha inayoeleweka kirahisi.
Sambamba na umasikini ni janga la ukosefu wa ajira. Japo kilimo kinaweza kutoa fursa kwa vijana wengi wasio na ajira, bado hakuna dhamira ya dhati ya kisiasa ya kukifanya kilimo kiwe kweli uti wa mgongo wa taifa letu.
Wakati jitihada za serikali kupambana na ufisadi na uhalifu zinaleta matumaini, kasi ya kushughulikia watuhumiwa ni ndogo huku mahakama ya mafisadi ikiwa kama kichekesho fulani kwa kukosa kesi, japo waziri husika anajaribu kutueleza kwamba kukosekana kesi ni mafanikio kwa mahakama hiyo. Ikumbukwe kuwa wahusika wa ufisadi, biashara ya dawa za kulevya, ujangili na uhalifu kama huo ni watu wenye uwezo mkubwa, na wanaoweza kuunganisha nguvu za ndani na nje ya nchi ili kuliyumbisha taifa. Kibaya zaidi ni kwamba baadhi ya majina maarufu ya wahalifu, kwa mfano ‘wauza unga,’ yanahusisha familia maarufu kisiasa, na hiyo inakuwa kama kinga kwao. Sheria haipaswi kubagua kati ya ‘huyu mtoto wa fulani’ na yule ni mtu wa kawaida.
Kimataifa, kama kuna kitu kinanipa wasiwasi sana ni kinachoonekana kama uhusiano wetu mzuri na nchi moja jirani, uhusiano ambao ulichora picha ya kudorora katika miaka ya hivi karibuni. Kiintelijensia, hao sio marafiki zetu hasa kwa kuzingatia historia na siasa za ndani za nchi hiyo. Naamini wahusika wanatambua changamoto kutoka kwa majirani zetu hao. Mbali na nchi hiyo jirani, hali ya shaka huko Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni tishio kwa usalama wa nchi yetu pia. La muhimu zaidi ni kuimarisha usalama wa mipaka yetu ili kudhibiti uhamiaji haramu kutoka nchi hizo.
Binafsi, ninauona ushirikiano wa Afrika Mashariki kama urafiki wa shaka. Tatizo kubwa linaloukabili ushirikiano huo ni kuendekeza zaidi siasa na kupuuzia kabisa ukweli kuwa nchi zinazounda ushirikiano huo zinajumuisha watu wa kawaida, na sio wanasiasa pekee. Ili ushirikiano huo uwe na manufaa ni lazima uwe na umuhimu kwa watu wa kawaida katika nchi husika.
Mwisho ni tishio la ugaidi wa kimataifa. Japokuwa hakuna dalili za kutokea matatizo hivi karibuni, masuala kadhaa niliyokwishayagusia yanaweza kutoa fursa kwa tishio hilo. Kwanza, kuminya ‘political space,’ udini, umasikini na ukosefu wa ajira. Utatuzi wa matatizo haya utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa tishio la ugaidi wa kimataifa.
Angalizo: Huu sio utabiri, kuwa hiki na kile kitatokea. Hii ni tathmini ya jumla ya maeneo yanayoweza kuhatarisha usalama wa taifa letu. Tathmini hii imetokana na ufuatiliaji wangu wa masuala mbalimbali, hasa ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiusalama kuhusu Tanzania yetu.

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

9 Feb 2017

MWEZI Machi mwaka jana, watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Nottingham cha hapa Uingereza walichapisha matokeo ya utafiti wao kuhusu kushamiri kwa tabia ya uvunjaji wa sheria. Katika matokeo hayo ya utafiti uliochunguza nchi 159, Watanzania tuliibuka vinara kwa kuwa watu wanafiki kupita kiasi, tukifuatiwa na watu wa Morocco.
Na mifano ya unafiki wetu ipo mingi tu, sisi ni miongoni mwa wapinzani wakubwa wa suala la ushoga. Lakini ukitaka kufahamu unafiki wetu katika suala hilo, nenda kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, shuhudia lundo la mashoga wa Kitanzania waliojitundika huko, wakifanya vitu vichafu kabisa, huku wakiwa na “followers” hadi laki kadhaa, hao si tu ni Watanzania wenzetu bali ni miongoni mwa sisi ‘wapinga ushoga.’ Unafiki wa daraja la kwanza.
Na sababu kuu tunayoitumia kupinga ushoga ni imani zetu za kidini. Na kwa hakika tumeshika dini kweli, hasa kwa kuangalia jinsi nyumba za ibada zinavyojaa. Lakini kuthibitisha unafiki wetu, ucha-Mungu huo sio tu umeshindwa kudhibiti kushamiri kwa ushoga (na usagaji) bali pia kutuzuia tusishiriki kwenye maovu katika jamii.
Kwa taarifa tu, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa miaka michache iliyopita na taasisi ya Pew ya Marekani, Watanzania tunaongoza duniani kwa kuamini ushirikina. Na kwa mujibu wa taarifa ninazozipokea kutoka huko nyumbani, ushirikina umeshamiri mno kiasi kwamba sasa ni kama sehemu ya kawaida ya maisha ya Watanzania.
Wacha-Mungu lakini tumebobea kwenye ufisadi, rushwa, ujangili na biashara ya dawa za kulevya. Na asilimia kubwa ya kipato haramu kinachotokana na uhalifu huo kinachangia kushamiri kwa “michepuko” na “nyumba ndogo.”
Mfano wa karibuni kabisa kuhusu unafiki wetu ni katika mshikemshike unaoendelea hivi sasa huko nyumbani (Tanzania) ambao watu kadhaa maarufu aidha wametakiwa kuripoti polisi au ‘kuhifadhiwa’ na polisi wakichunguzwa kuhusiana na biashara ya dawa za kulevya. Hali hiyo inatokana na tangazo rasmi la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ‘kujitoa mhanga’ kukabiliana na biashara hiyo haramu.
Lakini licha ya kuwepo kwa lundo la lawama mfululizo kwa serikali kuwa imekuwa ‘ikiwalea’ watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, tangazo la Makonda limesababisha kuibuka kwa lawama lukuki dhidi yake, huku wengine wakidai anatafuta ‘kiki (sifa) za kisiasa’ na wengine kudai amekurupuka kwa kutaja majina ya watu maarufu, na wengine wakimlaumu kwa kukamata ‘vidagaa’ na kuacha ‘mapapa.’
Kwa watu hao, na wapo wengi kweli, Makonda atashindwa kama alivyoshindwa kwenye amri zake nyingine. Sawa, rekodi ya Mkuu wa Mkoa huyo katika ufanisi wa maagizo yake sio ya kupendeza. Hata hivyo, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, kiongozi sio tu ametangaza vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya bali pia ametaja baadhi ya majina ya wahusika, na kuwafikisha polisi. Hili ni tukio la kihistoria.
Lakini ‘wapinzani’ wa RC Makonda sio wananchi wa kawaida tu. Kuna ‘wapinzani wa asili,’ mbunge wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye aliandika ujumbe mtandaoni, “kuwataja vidagaa na kuwaacha nyangumi/papa si ajabu ni moja kati ya mambo ya ovyo ya awamu ya tano.” Huyu ni mnafiki wa mchana kweupe. Sasa kama anawajua hao nyangumi/papa si awataje?
Kilichonisikitisha zaidi ya vyote ni kauli za Waziri Nape Nnauye alipozungumza na waandishi wa habari huko Dodoma. Pamoja na mambo mengine, Waziri Nape alidai kuwa, “ …watumiaji ni wengi lakini wanaoonekana zaidi ni wale wenye majina makubwa,” (sijui kwa mujibu wa utafiti gani); “Kama wizara tunaunga mkono juhudi za kupambana na dawa za kulevya, tatizo ni namna ya kushughulika na wahusika ikiwemo busara” (sijui alitaka tatizo lishughulikiwe kwa namna gani – na kwa nini hakuongoza kwa mfano kwa kutumia namna hiyo – na sijui busara ipi iliyokosekana katika utekelezaji wa agizo la Makonda); “Tunaunga jitihada za mapambano lakini ni vizuri lifanywe katika namna ya kulinda haki ya mtuhumiwa ili heshima yake isipotee” (haelezi hiyo ‘namna ya kulinda haki ya mtuhumiwa ili heshima yake isipotee’ ni kitu cha aina gani)
Nilimshutumu vikali Waziri Nape kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter (nilim-tweet yeye mwenyewe), na kumweleza bayana kuwa alihitaji kutumia busara badala ya kukurupuka kutetea wasanii wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Kadhalika, kama mtendaji wa serikali, alikuwa na nafasi nzuri kuzungumza na watendaji wenzake wa serikali faragha badala ya kuongea suala hilo hadharani. Kadhalika, kuonekana anahofu zaidi kuhusu “brand” (thamani/hadhi ya msanii, kwa tafsiri isiyo rasmi) badala ya athari kubwa zinazosababishwa na biashara ya dawa za kulevya sio busara hata kidogo.
Nihitimishe makala hii kwa kutoa wito kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba naye ajitokeze hadharani kuongelea suala hili maana amekuwa kimya mno. Awali, naibu wake alipohojiwa na wanahabari alikuwa mkali na alitoa kauli zisizopendeza. Ili vita hii ifanikiwe ni lazima serikali iwe kitu kimoja na viongozi na wananchi kwa ujumla waache unafiki, na wampe ushirikiano RC Makonda na Jeshi la Polisi.
Tanzania bila dawa za kulevya inawezekana

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali

19 Jan 2017

WAKATI Marekani ikijiandaa kwa sherehe ya kuapishwa kwa Rais Mteule Donald Trump hapo keshokutwa, rais huyo mteule amejikuta kwenye ‘kitimoto’ baada ya kumshambulia mjumbe wa Congress (bunge ‘dogo’ la nchi hiyo),mmoja wa wanasiasa wakongwe na mpinzani wa muda mrefu wa ubaguzi wa rangi, John Lewis.
Kama ilivyozoeleka, Trump alitumia akaunti yake katika mtandao wa kijamii wa Twitter kufanya mashambulizi hayo baada ya Lewis, ambaye anaheshimika mno nchini humo kwa kushirikiana na nguli wa haki za watu weusi, marehemu Dk. Martin Luther King, Junior, kueleza bayana kuwa hamwoni Trump kama rais halali wa Marekani. Pia alieleza kuwa itakuwa sio sahihi kukalia kimya ‘mambo yasiyopendeza’ ya Trump.
Kadhalika, Lewis alieleza bayana kuwa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30 hatohudhuria sherehe za kumwapisha rais mpya, na anasusia kuapishwa kwa Trump kama njia ya kuonyesha upinzani wake kwa rais huyo mpya.
Trump alimshambulia Lewis katika ‘tweets’ zake ambapo alidai kuwa mwana Congress huyo anapaswa kutumia muda mwingi zaidi kushughulikia eneo analoliwakilisha, ambalo kwa mujibu wa Trump, lipo katika hali mbaya na limegubikwa na uhalifu.
Tweets za Trump dhidi ya Lewis zilizosababisha watumiaji kadhaa wa mtandao huo wa kijamii kumlaani rais huyo mtarajiwa, hasa kwa vile wikiendi iliyopita ilikuwa ya maadhimisho ya kumbukumbu ya Dk. King, siku yenye umuhimu mkubwa kwa Wamarekani weusi.
Hayo yamejiri siku chache tu baada ya Trump kuwa katika ‘vita kubwa ya maneno’ dhidi ya ‘jumuiya ya ushushushu’ (intelligence community), taasisi 16 za ushushushu za nchi hiyo. Sababu kuu ya ‘ugomvi’ kati ya Trump na mashushushu hao ni taarifa iliyowasilishwa kwa Rais Barack Obama, na Trump mwenyewe, kuhusu hujuma za Urusi kwenye uchaguzi mkuu uliopita nchini Marekani.
Taarifa hivyo, ilitanabaisha kuwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin ndiye aliyetoa maagizo ya ‘kumsaidia Trump’ na ‘kumuumbua Hillary Cinton, aliyekuwa mpinzani mkuu wa Trump.
Lengo la makala hii sio kujadili siasa za Marekani au vituko vya Trump, bali kutumia matukio hayo kuelezea hali ilivyo sasa huko nyumbani – Tanzania, ambapo kwa kiasi kikubwa suala la uwepo au kutokuwepo kwa baa la njaa linazidi kutawala duru za habari.
Kuna masuala kadhaa yanatokea kwa wakati mmoja. Kubwa zaidi ni kauli ya Rais Dk. John Magufuli sio tu kukanusha taarifa za uwepo wa baa la njaa bali pia kusisitiza kuwa ‘serikali haina shamba’ la kuiwezesha kuwapatia chakula wananchi wanaolalamikia njaa.
Jingine ni tishio kali kutoka kwa Rais Magufuli dhidi ya ‘magazeti mawili’ aliyodai yanaandika habari za uchochezi. Pia aliyashutumu kuwa yamenunuliwa na mfanyabiashara mmoja wa nafaka ili yaandike kuhusu taarifa za uwepo wa baa la njaa, kwa minajili ya mfanyabiashara huyo kuuza nafaka zake.
Binafsi sijashangazwa na tishio la Rais kwa magazeti. Uamuzi wake wa kukaa mwaka mzima bila kuongea na wanahabari ulipaswa kutufahamisha mtazamo wake kwa vyombo vya habari. Ikumbukwe kuwa hata wakati wa kampeni zake za urais mwaka 2015 hakufanya mahojiano na vyombo vingine vya habari, pengine ni kwa bahati tu, alifanya mahojiano na gazeti hili la Raia Mwema tu.
Na hii si mara ya kwanza kwa Rais kuvitupia lawama vyombo vya habari, wiki chache zilizopita alivishutumu kwa kumchonganisha na Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Japo haikuwekwa wazi, lawama hizo zilitokana na habari zilizoandikwa na baadhi ya magazeti kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikuwa na mpango wa kupiga mnada mizigo ya taasisi ya WAMA iliyo chini ya mama Salma Kikwete. Kusema magazeti yalizusha habari hiyo ni kuyaonea kwa sababu chanzo cha habari kilikuwa taasisi ya serikali, TRA.
Binafsi nabaki najiuliza, hivi kweli kama kuna magazeti yanalipwa kufanya uchochezi, yangekuwepo huru hadi kufikia hatua ya Rais ‘kuyananga’ bila kuyataja jina? Je, Idara Habari (MAELEZO) na wizara yenye dhamana ya vyombo vya habari, na waziri husika (Nape Nnauye) wamelala usingizi mzito kutojua hayo hadi Rais aliposhtuka na kuweka suala hilo hadharani?
Kwa mtazamo wangu, nadhani tishio la Rais limelenga kutisha vyombo vyote vya habari na sio magazeti hayo mawili tu. Kwamba wanahabari wasiandike kitu kisichompendeza Rais.
Rais hataki kusikia habari kuhusu tishio la baa la njaa. Hata wito wa viongozi wa kidini Wakristo na Waislam kuwataka waumini wao wafanye sala/dua kuombea mvua na kuepushwa na baa la njaa haujamfanya Rais kubadili msimamo wake.
Na muda mfupi kabla ya kuandaa makala hii nimeona video ya mkutano wa Rais huko Magu, ambapo wakati akihutubia, baadhi ya wananchi walisikika wakisema “njaa baba,” na Rais akawajibu “njaa… unataka nikakupikie mimi chakula?”
Binafsi sidhani kama Rais anahitaji ‘kisingizio’ cha kufungia magazeti, yawe mawili au yote. Lakini pia Rais asiwe mkosefu wa shukrani kwa mchango wa magazeti katika kumfikisha Ikulu, kwa kufikisha ujumbe wake binafsi na chama chake wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Lakini ni muhimu pia Rais atambue kuwa hizi sio zama za Radio Tanzania, Uhuru na Mzalendo, na Daily News na Sunday News pekee. Huu ni mwaka 2017, tupo katika zama za digitali ambapo upashanaji wa habari una njia lukuki, kuanzia Whatsapp hadi mitandao ya kijamii kama Twitter, Facebook, Instagram, nk. Katika zama hizi, kufungia chombo cha habari hakuzui usambazaji wa habari muhimu miongoni mwa wananchi.
Nihitimishe makala hii kwa wito huu kwa Rais wangu, mara kadhaa amekuwa akituomba sisi wananchi tumsaidie katika uongozi wake. Na moja ya misaada ambayo watu wengi wamekuwa wakimpatia ni kumsihi apunguze ukali, ajaribu kutumia lugha ya kidiplomasia, na asiogope kukosolewa.

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

12 Jan 2017

MIONGONI mwa kauli maarufu zaidi za Rais John Magufuli ni ile ya kuwaomba Watanzania wamwombee na msema kweli ni mpenzi wa Mungu.
Kwa bahati mbaya au pengine kwa makusudi, Rais amekuwa mtu wa kwanza kukiuka kauli hizo au kuziweka katika mazingira magumu kutekelezeka.
Nianze na hiyo kauli ya kuwataka Watanzania wamwombee. Pengine wakati ambao alielezea kwa undani mantiki ya kauli hiyo ni wakati wa uzinduzi wa bunge mwaka jana, ambapo alizungumzia kwa undani ugumu unaoikabili vita dhidi ya rushwa na ufisadi.
Katika hotuba hiyo, aliwafahamisha Watanzania kuwa wanaohusika na rushwa na ufisadi sio watu wadogo, kwa maana kwamba ni watu wenye uwezo mkubwa. Na kwamba licha ya dhamira yake na jitihada zake, angehitaji sio tu ushirikiano wa wananchi bali sala na dua zao pia.
Niwapeleke kando kidogo kabla ya kubainisha kwa nini nimeandika Rais amekuwa mtu wa kwanza kukiuka kali zake mwenyewe. Katika sosholojia, kuna kanuni moja inayofahamika kama ‘Social Exchange.’ Kwa kifupi, pamoja na mambo mengine, kanuni hii inaelezea kuhusu uhusiano (interactions) kati ya watu katika jamii.
Kanuni hiyo inatanabaisha kuwa uhusiano kati yetu katika jamii huongozwa na ‘zawadi’ (rewards) na ‘gharama’ (costs). Na watu wengi huongozwa na kanuni (formula) hii: thamani (ya mtu) = zawadi – gharama. ‘Zawadi’ ni vitu vizuri kama vile pongezi, shukrani, kuombewa dua, nk ilhali gharama ni hasara, mtendewa kutoonyesha shukrani, kupuuzwa, nk.
Mfano rahisi: ukipita mtaani, ukakutana na ombaomba, ukampatia hela kidogo, kisha akanyoosha mikono angani kukushukuru, basi kuna uwezekano mkubwa wa kumsaidia tena siku nyingine. Na si ombaomba tu, bali hata ndugu, jamaa au rafiki au ‘mtu baki’ ambaye anashukuru anaposaidiwa.
Lakini laiti ukimpatia msaada ombaomba, au mtu mwingine, kisha asionyeshe kujali msaada huo, basi uwezekano wa kumsaidia tena ni hafifu. Kwa mujibu wa kanuni yetu ya ‘thamani = zawadi – gharama,’ msaidiwa akionyesha shukrani inakuwa zawadi yenye thamani zaidi ya gharama, ilhali kwa asiyeonyesha shukrani gharama inakuwa kubwa kuliko zawadi. Natumaini hizi ‘hisabati’ hazijakuchanganya ndugu msomaji.
Kimsingi, kanuni hiyo inaambatana na matarajio ya ‘nipe nikupe’ (give and take). Kwamba katika kila tunalofanya, tunakuwa na matarajio fulani. Kwamba tunapokwenda kwenye nyumba za ibada, tuna matarajio ya kumridhisha Mola kwa vile tunafuata anachotarajia kwetu: sala/ibada kwake.
Tunapokuwa watu wa msaada, au wakarimu, au wema, nk tunatarajia wale tunaowafanyia hivyo wathamini tabia zetu hizo nzuri.
Turejee kwa Rais Magufuli. Hivi karibuni, akiwa ziarani mkoani Kagera, aliwaambia wananchi kuwa, ninamnukuu; “Serikali na wananchi kila mmoja abebe msalaba wake mwenyewe.’’ Alitoa kauli hiyo alipozungumzia misaada kwa waathirika wa tetemeko la ardhi lililoyakumba maeneo ya Ukanda wa Ziwa hususan Mkoa wa Kagera.
Mwaka jana nilipokuwa naomba kura kwenu, sikuomba tetemeko la ardhi litokee hapa, hili ni jambo ambalo liko nje ya uwezo wangu, tunaomba kila mmoja aweze kutumia msaada uliotolewa ili kurejesha miundombinu ya makazi yenu” alieleza Dk. Magufuli.
Bila kuingia kiundani kuchambua mantiki ya kauli hiyo ya Rais, yayumkinika kuhitimisha kuwa kama “kila mtu abebe mzigo wake mwenyewe” basi na ombi lake maarufu kwa wananchi la “mniombee” alibebe yeye mwenyewe. Ajiombee.
Naandika hivyo kwa sababu, kiustaarabu tu, kuna baadhi ya maneno hayastahili kusemwa katika mazingira ya maombolezo, misiba, nk. Rais ni kama mzazi. Na japo kila mzazi ana jukumu la kuwa mkweli, anapaswa pia kuwa na busara ya kuchagua maneno yanayoweza kuwasilisha ujumbe bila kuumiza mioyo ya watu.
Hivi Rais angeeleza kwa lugha ya upole kuwa uwezo wa serikali ni mdogo na haitomudu kumjengea nyumba kila mwananchi, lakini itashirikiana na wananchi kadri itakavyoweza, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha misaada kwa waathirika, asingeeleweka? Au angeonekana sio ‘Rais kamili’?
Kwa mujibu wa ‘social exchange theory,’ matarajio ya Watanzania wanaaombwa na Rais wao kuwa wamwombee si kumsikia akiwaambia “kila mtu abebe mzigo wake mwenyewe” hususan mbele ya watu wanaoendelea kukabiliana na athari za janga la tetemeko la ardhi.
Lakini kama hilo la “kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe” halitoshi, Rais Dk. Magufuli akakiuka kauli yake maarufu ya “msema kweli mpenzi wa Mungu” kwa kutoa maelezo yasiyo sahihi, kwamba (ninamnukuu) “Kuna nchi kama Japan na Italia, zimekuwa zikikumbwa na matetemeko mengi, haijawahi kutokea serikali yao ikawajengea nyumba upya isipokuwa inarejesha miundombinu ya taasisi za umma kama vituo vya afya, shule na barabara.”
Sio heshima wala nidhamu kusema “Rais amedanganya” lakini alichoongea kina kasoro. Kwa Italia, baada ya tetemeko lililotokea mwezi Agosti mwaka jana, Waziri Mkuu wa zamani Mateo Renzi alishughulikia upitishwaji wa sheria ya kuidhinisha Euro bilioni 4.5 kwa ajili ya waathirika na miundombinu. Euro bilioni 3.5 kwa ajili ya waathirika na euro bilioni kwa ajili ya majengo ya umma.
Kutegemea eneo, sheria iliidhinisha malipo kati ya asilimia 50 hadi 100 kwa wananchi ambao nyumba zao ziliharibiwa na tetemeko hilo.
Huko Japan nako, mara tu baada ya tetemeko kubwa la ardhi la mwaka 2011, serikali ilichukua hatua kadhaa kuwasaidia waathirika ikiwa ni pamoja na fedha za rambirambi kwa kila familia iliyopoteza ndugu katika janga hilo (Yen milioni 5), fedha kwa familia zenye majeruhi (Yen milioni 3), misaada ya fedha kwa kila familia na mikopo yenye masharti nafuu kwa kila familia (Yen milioni 3.5), mikopo maalumu kwa watu/biashara waliokuwa na madeni kabla ya tetemeko,  ahueni ya kodi mbalimbali kwa waathirika wote, malipo kwa waliopoteza ajira (unemployment benefits), mkakati maalumu wa utengenezaji ajira mpya, na hatua nyinginezo.
Kanuni za tawala zetu za kiafrika zipo wazi: “kiongozi huwa hakosei, na akikosea huwa amenukuliwa vibaya, na kama ikithibitika amekosea haina haja ya kumradhi.” Sitarajii kusikia tamko lolote kwamba “Kauli ya Rais kuwa ‘Kuna nchi kama Japan na Italia, zimekuwa zikikumbwa na matetemeko mengi, haijawahi kutokea serikali yao ikawajengea nyumba upya’ haikuwa sahihi. Anaomba radhi.”
Wakati wa kampeni zake za kuwania urais na hata baada ya kushinda urais, Dk. Magufuli amekuwa akituomba mara kwa mara kuwa tumsaidie. Makala hii ni mwitikio wa ombi hilo. Ni mchango wangu wa msaada kwake kumsihi ajaribu kuepuka lugha inayoweza kujenga tafsiri mbaya.
Kadhalika, suala la kusaidia wenzetu waliokumbwa na tatizo sio la kisheria, kisera au ki-kanuni, au kwa vile fulani hakufanya, bali ni suala la utu. Na utu ni kama pale Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alipomtembelea mzazi wa msanii Chid Benz, kuangalia uwezekano wa kumsaidia msanii huyo aliyeathirika na matumizi ya dawa za kulevya. Ni utu kwa sababu, kisheria, anachofanya msanii huyo (kununua na kutumia mihadarati) ni kosa la jinai (Ibara ya 15 ya Sheria mpya ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ya mwaka 2015).
Nihitimishe makala hii kwa kumshauri Rais Magufuli kwamba pamoja na dhamira yake nzuri kuitumikia nchi yetu kwa uwezo wake wote, na licha ya Watanzania kuwa na matumaini makubwa kwake, ni muhimu sana ajaribu ‘kupunguza makali’ kwenye lugha yake. Kama nilivyoeleza katika makala yangu iliyopita, ‘lugha ya ukali’ inaweza kujenga nidhamu ya uoga, kitu ambacho kitakwaza jitihada za Rais wetu kuijenga Tanzania tunayostahili. Ninatumaini Rais ataupokea ushauri huu na kutoona kuwa anakosewa heshima kwa kusahihishwa pale alipokosea.
Mungu ibariki Tanzania

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

5 Jan 2017

KHERI ya mwaka mpya 2017. Kama ilivyo kawaida ya safu hii, kila makala ya mwanzo wa mwaka hujikita kwenye ubashiri wa masuala mbalimbali yanayotarajiwa katika mwaka mpya husika.
Kutokana na ufinyu wa nafasi, ubashiri kuhusu mwaka huu mpya utaelemea zaidi katika mwenendo wa siasa kitaifa na kimataifa.
Kimataifa, mtihani wa kwanza kabisa wa siasa za kimataifa utaanza Januari 20, 2017 siku ambayo Rais mteule wa Marekani, Donald Trump ataapishwa rasmi.
Ni vigumu kubashiri nini kinaweza kutokea siku ya kwanza tu tangu Trump aapishwe, lakini kilicho bayana ni uwezekano mkubwa kwa tajiri huyo, aliyeshinda urais katika mazingira ya kushangaza yaliyoambatana na kila aina ya hadaa, si tu kuendelea kuwa ‘kituko’ bali pia hata kuhatarisha usalama wa kimataifa.
Wakati wa kampeni za urais, profesa mmoja wa historia ya siasa, Allan Lichtman, alibashiri kuwa Trump angeshinda licha ya kura za maoni kuonyesha mgombea kwa tiketi ya Democrats, Hillary Clinton akiongoza. Nilikerwa sana na ubashiri wa profesa huyo.
Baada ya Trump kumbwaga Hillary, Profesa Lichtman aliibuka na ubashiri mwingine, akidai kuwa urais wa tajiri huyo utakuwa wa muda mfupi tu kwani atang’olewa madarakani pengine kabla ya kutimiza mwaka madarakani. Nami ambaye awali nilikerwa na profesa huyo sasa natamani ubashiri wake utimie.
Na kwa hakika kati ya mambo yanayoweza kutokea mwaka huu ni Trump kuondolewa madarakani. Lakini hilo si kubwa kulinganisha na uwezekano wa machafuko nchini humo hususan, baada ya wapigakura kubaini kuwa ‘waliingizwa mkenge’ na tajiri huyo.
Ikumbukwe huyu atakuwa ndiye rais wa kwanza aliyeingia rasmi madarakani kwa udanganyifu na hadaa.
Jingine kuhusu Trump ni uwezekano wa kuwatibua washirika wa Marekani miongoni mwa mataifa ya Kiislamu, kama vile Saudi Arabia, Jordan na Pakistan. Uwezekano huo unatokana zaidi na msimamo wa kibaguzi wa Trump na wengi wa wasaidizi wake.
Kadhalika, kuna uwezekano uswahiba kati ya Trump na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ‘ukatumbukia nyongo,’ kwa sababu mataifa hayo yana mgongano wa kimaslahi. Vilevile, kuna uwezekano wa dalili za mgogoro kati ya Marekani na China kupanuka zaidi, chanzo kikiwa Trump huyohuyo.
Kwingineko kimataifa, Uholanzi itafanya uchaguzi wake mkuu Machi, Ufaransa Aprili hadi Juni, na Ujerumani Oktoba.
Chaguzi hizo ni mtihani mgumu kwa nchi hizo kutokana na tishio kubwa kutoka kwa vyama vyenye mrengo mkali wa kulia ambavyo vinazidi kupata umaarufu barani Ulaya kutokana na matishio ya ugaidi, ambayo pia yanahusishwa na sera za kukaribisha wahamiaji.
Chaguzi nyingine zinazotarajiwa kugusa hisia ni nchini Hong Kong (Machi), Iran (Mei) na Korea ya Kusini (Desemba).
Japo kuna dalili za amani huko Syria kufuatia jitihada zinazofanywa na Russia, kuna uwezekano kwa nchi hiyo kujikuta kwenye machafuko zaidi hasa ikizingatiwa kuwa serikali ya Rais Bashir Assad inamiliki sehemu tu ya nchi hiyo, huku sehemu nyingine zikiwa chini ya makundi mbalimbali.
Hali ya usalama nchi Uturuki inatarajiwa kuendelea kuwa tete, kutokana na matishio makuu mawili, ya vikundi vya Kikurdi vinavyopigania uhuru na kikundi cha kigaidi cha ISIS, ambacho pia kinatarajiwa kuendelea kuwa tishio katika eneo la Ghuba, nchi za Ulaya Magharibi na Marekani.
Barani Afrika, mwaka huu kuna chaguzi kadhaa, lakini ambazo zinavuta hisia zaidi ni nchini Kenya mwezi Agosti na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako hali bado ni ya wasiwasi kutokana na jitihada za Rais Joseph Kabila kutaka kung’ang’ania kuwa madarakani ingawa tayari kuna maneno kwamba amekubali kuachia ngazi.
Kuhusu majirani zetu wa Kenya, tatizo mara zote limekuwa kwenye siasa za ukabila. Kwa bahati mbaya, nchi hiyo itaingia kwenye uchaguzi wake mkuu wakati ‘kirusi cha ukabila kikiwa hai na chenye nguvu.’
Tukigeukia huko nyumbani, mwaka huu utashuhudia CCM ikifanya uchaguzi wake ndani. Tunasubiri kuona jinsi ambavyo Mwenyekiti wa Taifa, Rais Magufuli, atachezesha kete zake.
Ifahamike kuwa licha ya mwonekano kuwa ‘CCM ni wamoja,’ ukweli ni kwamba ndani ya chama hicho kuna ‘mambo yanayoendelea chinichini.’
Kwa upande mmoja, kwa muda mrefu CCM imekuwa hifadhi ya ‘watu mbalimbali wenye wasifu usiopendeza,’ ikiwa ni pamoja na mafisadi. Hawa ni wahanga wa wazi wa jitihada za Rais Magufuli kupambana na ufisadi. Yayumkinika kuhisi kuwa wanaweza kutumia uchaguzi huo kama fursa ya kujipangia vema kumdhibiti Dk. Magufuli katika uchaguzi wa mgombea urais mwaka 2020.
‘Wapinzani wa Magufuli’ ndani ya CCM wanapewa nguvu na mtazamo wa baadhi ya wananchi mitaani kwamba hali ya maisha inazidi kuwa ngumu pasipo dalili za kupatikana nafuu hivi karibuni.
Wakati wengine twaelewa kuwa ‘inabidi tupitie maumivu kabla ya kupata nafuu,’ kwa baadhi ya wananchi ‘mtaani’ wanaona kama utawala wa Magufuli ni wa ‘kuwapa maumivu mfululizo pasi dalili ya ahueni.’
Nje ya CCM, changamoto kubwa kwa utawala wa Rais Magufuli ni kuibuka kwa nidhamu ya uoga, ambapo taratibu kunaanza kujengeka hisia kuwa ‘kiongozi atayediriki kupishana kimtazamo na Rais, atatumbuliwa.’
Nidhamu ya uoga haiwezi kuleta tija wala ufanisi. Wakati ninaandaa makala hii nilipewa taarifa kuhusu tishio la janga la njaa kwenye wilaya kadhaa lakini inadaiwa kuwa watendaji katika maeneo hayo wanahofia kutoa taarifa kwa wakichelea kutumbuliwa.
Ili dhamira ya Dk. Magufuli kuiletea neema Tanzania itimie kwa kuongeza kasi ya uzalishaji mali na mchango wa sekta mbalimbali kwenye uchumi, sambamba na kukabiliana na rushwa na ufisadi, ni lazima Watanzania wawe ‘kitu kimoja.’
Serikali ya Dk. Magufuli inapaswa kuepuka ‘ugomvi usio wa lazima’ hasa matamshi ya kuwafanya watu wazima wajione kama watoto, ‘maguvu’ badala ya busara, na kutofanya haki za Watanzania kuwa zawadi kutoka kwa watawala.
Uamuzi wa kufuta matangazo ya moja kwa moja ya Bunge, kuzuwia mikutano na maandamano ya vyama vya siasa, viongozi wa Upinzani kubughudhiwa mara kwa mara, kubinya uhuru wa habari  ambao japo waweza kutumika vibaya, ni muhimu katika ujenzi wa utawala bora. Na bila kuuma maneno, Rais Magufuli asizuwie kukosolewa.
Kwa upande wa vyama vya Upinzani, dalili za suluhu katika mgogoro wa CUF ni ndogo. Kadhalika, ‘afya’ ya ACT Wazalendo inaweza kuendelea kudhoofika, tatizo likiwa ugumu wa ‘siasa za chama cha mtu mmoja.’
Kwa Chadema, kunaweza kuibuka harakati za kudai mabadiliko ndani ya chama hicho hasa kutokana ukweli kuwa chama hicho kwa sasa hakina ajenda ya kitaifa zaidi ya ‘kudandia hoja.’
Nihitimishe makala hii kwa kukumbushia kuwa ubashiri si ‘sayansi yenye uhakika wa asilimia 100 (exact science). Ubashiri huu umetokana na uchambuzi mienendo (trends) mbalimbali na si uhakika kuwa ‘lazima itakuwa hivi au vile.’
Niwatakie tena heri ya mwaka mpya 2017.


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.