18 Jan 2011


Jana niliona mahala flani kuwa nyota (star signs) zimebadilika.Sikujali.Lakini leo katika pitapita zangu mtandaoni,nimebaini kuwa sio tu kuwa nyota zimebadilika bali pia nyota yangu imekumbwa na mabadiliko.Nilizaliwa Desemba 9,hivyo nyota yangu ilikuwa Mshale au Sagittarius,kama inavyojulikana.Sasa baada ya kuongezeka alama nyingine ya nyota,nimejikuta nikiwa katika alama nyingine ya nyota,OPHIUCHUS.Grrrrr!!!!

Najua imani yangu ya dini inakemea mambo ya unajimu.Lakini,siku za nyuma nili-develop interest kwenye masuala ya nyota baada ya kuanzisha safu kwenye lililokuwa  gazeti maarufu la SANIFU,kabla sijahamishia safu hiyo kwenye gazeti la KASHESHE.Naamini kwa walikuwa wafuatiliaji wa magazeti ya "manyang'unyang'u" waakuwa wanakumbuka tangazo la Anko J Julius Nyaisanga akiwaasa wasomaji kutokosa safu ya USTAADH BONGE.Hiyo ilikuwa mika ya 1997-2000.

Naam,Ustaadh Bonge huyo ndiye mie,truly yours Evarist Chahali.Kuna waliokuwa wanaamini nyota hizo za "kizushi".Nakumbuka wakati huo ambapo nilikuwa mwanafunzi hapo Mlimani (UDSM) kuna baadhi ya watu walifikia hatua ya kuomba "msaada" wangu kuhusu fate zao kinyota.

Na safu hiyo ikaniacha na monikers kama "Ustaadh", "Bonge" au "Ustaadh Bonge",ambayo kwa baadhi ya marafiki zangu,ndio pekee wanayofahamu kuhusu mie.

Looking back,I can't help but just laugh.Good old days za "Kijiweni" nyuma ya ATB "tulipokuwa tunahudhuria masomo kwa kile tulichokiita correspondence" ie mtu mmoja atakaeingingia kwenye mhadhara (lecture) ndiye atakayesambaza contents za kilichofundishwa"!!!However,when the UEs came,we all managed to smash them.
"KIJIWENI" ni kulia kwa picha hii ie nyuma ya ATB

Missing you guys,Ghetto Boy (sasa ni bosi mahala flani), "Dogo" Baraka (naye pia ni bosi katika kampuni moja ya kigeni),Adam Mkula,Busa Musika,Aden,Iku, "Sospiere",Chrisant, Swedi Mlanzi, Bitebo,Manzi,Eric (wape hi Skandinavia), "Queen Latifa",Faith Msina,Belinda,Leila,Kassim,na wengineo.You made our days at the uni one experience that I will never ever forget!!!!

17 Jan 2011


Katika siku za hivi karibuni,jina la Edward Lowassa limekuwa likisikika sana.Blogu hii inahisi kuwa kelele hizi za Lowassa ni sehemu ya jiihada za kuweka jina lake machoni na masikioni mwa Waanzania ili hatimae amrithi swahiba wake,Jakaya Kikwete, hapo 2015.Hebu msikie tena hapa chini,kisha tumjadili kiduchu


Lowassa: Mjadala wa Katiba usivuruge amani

na Betty Kangonga

MBUNGE wa Monduli, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ametahadharisha mjadala kuhusu Katiba nchini kuwa chanzo cha kuharibu wa amani iliyoko nchini.

Lowassa alitoa tahadhari hiyo jana wakati akifungua studio ya muziki ya FLEM, jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa hivi sasa inaoneka kuwapo kwa mashindano ya kuharibu amani kutokana na mjadala huo kupamba moto.

Alisema kuwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo moyo wa kuharibika kwa amani unavyozidi kuongezeka.

Alisisitiza kuwa hata katika mijadala mbalimbali inayoendelea nchini hasa ya Katiba, wananchi wanatakiwa kupingana kwa hoja na si kwa kuhatarisha amani.

“Tunatakiwa kutunza amani yetu kama mboni ya jicho maana hata nchi jirani za wenzetu ikiwamo Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi hawajawahi kuwa na amani kama tuliyonayo sisi, hivyo tunatakiwa kuhakikisha tunaitunza kwa uwezo wetu wote,” alisema Lowassa.

Katika kusisitizia hilo, aliwashauri waimbaji wa Injili kuamka la kutunga nyimbo zinazohamasisha na kuchochea utunzaji wa amani, ili iendelee kudumu.

“Waimbaji wa Injili wanafanya kazi nzuri sana ingawa katika maisha kuna mahali unayumba, unaanguka na kupanda, lakini yote hayo ni kwa uwezo wa Mungu.

“Hakikisheni mnatunga nyimbo za kutetea amani maana kwa sasa kila mtu ana lake analosema, vyombo vya habari vinachochea kwa njia yake, hivyo tuilinde hii amani,” alisema.

Alisema kuwa bila kuwa na amani hakuna taifa linaloweza kufikia maendeleo, hivyo jamii inapaswa kupingana bila kusababisha mvurugano.

Alisema amani ni tunu pekee aliyotuachia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hivyo tunatakiwa kuitetea kwa nguvu zetu zote.


Alisema kuwa ni kipindi cha ajabu sasa, kwani kila mtu amekuwa akiamka na jambo lake linaloonekana kuhatarisha amani.

Kwa upande wake, mchungaji wa kanisa la FPCT la Mtoni Kijichi, Joseph Malundo, aliwataka wamiliki wa studio hiyo kuacha kubweteka na mafanikio hayo bali wazidi kumuomba Mungi ili azidi kuwapandisha juu zaidi.

Alisema hatua hiyo itawezesha vijana wengi kupata ajira hasa kwa kumtumikia Mungu.

CHANZO: Tanzania Daima

Tatizo la Lowassa,na watu wenye mawazo kama yake,ni kuwaona Watanzania ni wajinga,wasio na kumbukumbu,na ambao wako radhi kufisadiwa milele.Pengine mawazo hayo yanatokana na ukweli kuwa licha ya mtu kama yeye kulazimika kujiuzulu uwaziri mkuu kutokana na kuhusishwa na ujambazi wa Richmond (mtangulizi wa Dowans) bado yupo huru,anapeta na licha ya kufanikiwa kurejea Bungeni,ameendelea kupewa heshima ya "Waziri Mkuu Mstaafu".Na si yeye tu,bali hata washirika wake Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.

Laiti sheria ingefuata mkondo wake,tusingesikia matusi haya ya Lowassa.Ni dhahiri kuwa anafahamu fika kuwa tishio kubwa la amani ya Tanzania na Watanzania ni UFISADI na MAFISADI.Hawezi kuzungumzia hilo kwa vile linamgusa.Na ni wazi kuwa japo anajifanya kuguswa na umuhimu wa Katiba mpya,ni wazi kuwa yeye,rafiki yake Rostam Aziz,na mlinzi wao hapo Ikulu,Kikwete,wasingependa kuona Katiba mpya itakayompa nguvu Mtanzania kupambana na wezi,majambazi,wadhalimu na wabaka uchumi kama hao walioleta Richmond,na sasa wanataka kujizawadia mabilioni kwa usanii wa "fidia kwa wanaharamu wa Dowans".

Na nyie viongozi wa dini mnaoendekeza njaa zenu mnapaswa kuelewa sio kila sadaka inampendeza Mungu.Kwani Bwana Yesu alifanya kazi zake kwa kutegemea michango,achilia mbali michango ya wanafiki,wezi,majambazi au wapinzani wa Amri za Mungu?Njaa zenu ndio zinawapa watu kama Lowassa nafasi ya kujiosha machoni mwa jamii ilhali tunafahamu fika wasingepaa madaraka kuwa laiti Baba wa Taifa angekuwa hai-kwani alishawaona kuwa ni viumbe hatari kabisa kwa Tanzania yetu.



16 Jan 2011

Maji yamezidi unga au afya mbovu?Rais Jakaya Kikwete anaonekana pichani (wa tatu kulia) akiwa hoi bin taaban.Na Lowassa (wa kwanza kulia mstari wa nyuma) anaonekana kama ameguswa na hali ya rafiki yake
Chanzo: Jamii Forums

15 Jan 2011


Hivi kuna uwezekano kwamba Mwenyekiti wa CCM,ambaye pia ni Rais wa Tanzania,Jakaya Kikwete,hamtakii mema Katibu Mkuu wa chama hicho,Yusuph Makamba,na ndio maana (Kikwete) hamshauri Makamba achunge kauli zake.Kwa vile wengi tunafahamu 'upole' (uzembe?) wa Kikwete katika kuwajibisha watendaji fyongo,labda anasubiri Makamba akutane na tukio la 'mchimba kisima kazama kisimani' ie kauli zake za ovyo ovyo zije kumlipukia mwenyewe.

Hebu soma kwanza stori ifuatayo,kisha tutaijadili kidogo.

Makamba amjibu Askofu Laizer
Thursday, 13 January 2011 21:07

Raymond Kaminyoge


KATIBU Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, amesema kuwa na uelewa finyu wa biblia si jambo la ajabu kwake kwa sababu yeye siyo askofu.

Makamba aliliambia Mwananchi jana kwa simu, kuwa licha ya uelewa finyu wa biblia, lakini amekuwa akitoa vifungu hivyo kwenye biblia.
Makamba alisema hayo kufuatia, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Thomas Laizer kusema Makamba ana uelewa finyu wa biblia.

Laizer alisema hayo juzi mjini Arusha wakati wa kuwaaga watu wawili waliofariki kwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano na Chadema yaliyofanyika Januari 5 mwaka huu.

“ Ni kweli ninauelewa finyu wa biblia kwa sababu mimi siyo askofu, hata Qurani naweza kuwa siifahamu vizuri kwa sababu mimi siyo Sheikh, ndiyo maana kila ninachozungumza kuhusu dini hizo nakariri vifungu kutoka katika vitabu hivyo,” alisema. Makamba alisema alimweleza Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kutoandamana kwa sababu serikali ilipiga marufuku maandamano hayo, wao wakapuuza.

Alimtaka Laizer kutoa tafsiri ya kitabu cha Warumi 13 sehemu ya kwanza hadi ya saba, inayosema kuwa kila mtu hana budi kutii serikali inayotawala kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu.
Alisema kwa hiyo anayepinga mamlaka inayotawala anapinga chombo kilichowekwa na Mungu na watu wanaoasi hujiletea hukumu.

“ Kwa maana watawala hawatishi watu wanaotenda mema bali wale wanaotenda maovu, kama hupendi kuishi kwa kumwogopa mwenye mamlaka basi tenda mema naye atakusifu,” alisema.

“ Laizer anieleze ufinyu wangu katika uelewa wa biblia upo wapi ikilinganisha na tukio lililotokea mkoani Arusha,” alisema.

CHANZO: Mwananchi

Sasa Makamba anaelekea kubaya.Na kama kuna watu wanamtakia mema (angalau ndani ya familia yake) ni vema wakamdhibiti mapema.

Kutumia Maandiko Matakatifu kuhalalisha maovu ni mithili ya matusi kwa waumini wa dini husika.Makamba si Mkristo,na amekiri kuwa uelewa wake wa Biblia Takatifu ni mdogo.Sasa kama ni hivyo,iweje basi aanzishe malumbano na kiongozi wa madehehebu ya Kikristo,achilia mbali kiongozi huyo kuwa ni Askofu Mkuu wa KKKT?

Makamba anaelewa vyema kuwa Maandiko Matakatifu,hayawezi kunukuliwa kwa vipande vipande.Kadhalika,uwezo wa kunukuu haumaanishi uelewa wa nukuu husika.Pia naamini Makamba anafahamu fika kuwa aya aliyotumia kuhalalisha udikteta wa CCM na polisi wake (uliopelekea mauaji ya raia wasio na hatia)haimaanishi kuwa hata mamlaka inayokandamiza watu wasio na hatia iendelee kunyenyekewa.

Kama suala la kutii mamlaka iliyo madarakani,kwanini basi hapo 1979 tulimng'oa Nduli Idi Amini ambaye wakati huo alikuwa Rais halali wa Uganda?Au kwanini basi Hitler nae alivurumishwa ilhali alikuwa kiongozi halali wa Ujerumani?Au kwanini tulisapoti harakati za mapambano dhidi ya makaburu ilhali wabaguzi hao wa rangi walitengeneza "serikali halali"?

Kwa wanaompenda Makamba,ni vema wakamshauri kuwa madaraka aliyonayo,sambamba na kuwa chini ya bosi mwenye huruma kwa wanaoboronga (ie Kikwete),visimfanye apate jeuri ya kuanzisha bifu na Watumishi wa Mungu.Ni vema pia akatambua unyeti wa kutumia Biblia kuhalalisha maovu ilhali yeye ni Muislam.Kiongozi mwenye akili timamu anapaswa kutambua hatari na madhara ya KUDHARAU MAANDIKO MATAKATIFU (kama ambavyo Makamba anavyoichezea Biblia Takatifu mithili ya Manifesto ya Uchaguzi ya CCM-iliyosheheni kila ahadi ya uongo).

Na kama Makamba mwenyewe ameshawahi kusoma blogu hii (which I doubt) basi ushauri wangu mwepesi kwake ni AACHAE KUMCHEZEA MUNGU,hata kama haamini kuwa Mungu ambaye Askofu Mkuu Lazier ni mtumishi wake,ni Mungu wake yeye Makamba.

Na kwa Kikwete,hivi lini utajaribu angalau kuwaonyesha Watanzania kuwa una uwezo japo haba wa kukemea mambo hatari?Ah,yani umekuwa hapo Ikulu kama pambo huku watendaji wako wakizidi kuhangaika kusaka moto na petroli ya kuiunguza Tanzania?

14 Jan 2011


Kuna msemo wa kiswahili kuwa mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.Naomba niende moja kwa moja kwa kuhusisha msemo huu na mahusiano ya kibaradhuli kati ya vyombo vya dola na Serikali ya CCM chini ya utawala wa Jakaya Kikwete.Katika msemo wetu,Serikali inaweza kulinganishwa na baba,huku vyombo vya dola vikilinganishwa na mtoto. Na hapa sina nia ya kuonyesha undugu uliopo kati ya vyombo hivyo vya dola na CCM iliyozaa serikali tuliyonayo (hata kama ni kwa uchakachuaji).

Serikali ya Kikwete haina tatizo kuona vyombo vya dola vikikiuka maadili ya kazi yao alimradi kwa kufanya hivyo,yeye kama Rais,chama chake na maswahiba wake mafisadi wanaendelea kufakamia keki ya taifa pasipo usumbufu.

Kwa mfano,Kikwete na serikali yake haisumbuliwi na ukiukwaji wa hali ya juu wa haki za binadamu unaofanywa na jeshi la polisi.Na hapa sijagusia mauaji ya huko Arusha na haya ya hivi punde huko Mbarali,Mbeya.Hapa nazungumzia namna haki za msingi za Watanzania wa kawaida (wasio vigogo au mafisadi) zinavyofinyangwa na askari polisi kila kukicha.Madereva na makonda wa daladala ambao wanalazimika "kuziba pengo kati ya kipato halisi cha askari trafiki na mahitaji ya kawaida kwa siku/wiki/mwezi".

Sote tunajua ni rahisi zaidi kugema damu kwenye jiwe kuliko askari Trafiki kumpongeza "suka" (dereva).Sasa nini kinaendelea katika picha hiyo kati ya "maadui" hawa?
Rushwa kwa trafiki imekuwa ni sehemu ya sheria za usalama barabarani,na ndio maana kila kukicha ajali zinaendelea kugharimu maisha ya abiria wasio na hatia.Unategemea nini kama askari mla rushwa anaweza kuruhusu basi lenye injini ambayo hata kwenye trekta haifai?

Unapozungumzia amani na utulivu wa Tanzania,unaweza kuwa umeshahau nini kilichotokea mara ya mwisho ulipokutana na askari polisi wakiwa "kazini".Unless una undugu au ukaribu na kigogo au fisadi flani,ni dhahiri kuwa polisi wetu watatumia mbinu zote za medani kuhakikisha unawapa fedha.Ukibisha,utapigwa na kutumbukiziwa kete ya bangi kama sio cocaine feki.Askari hawa ambao wengi wao hawakujiunga na jeshi hilo kwa vile wanaipenda sana nchi yetu bali kwa sababu ya aidha ugumu wa ajira au wazazi kumwadhibu mtoto mtukutu kwa kumwingiza katika ajira ya polisi.

Hili kundi la pili ni la hatari zaidi kwa sababu linajumuisha watu wenye jeuri ya "baba ni flani" na wanajua hata "wakilikoroga" hakuna wa kuwaadhibu.Pia ni viumbe hatari zaidi kwa vile sababu ya wazazi wao kuwaunganishia ajira ndani ya jeshi hilo ni "kushindikana" kwao katika familia zao.Hawa ni binadamu ambao laiti uchunguzi wa kubaini ufanisi wa kiakili na uwezo wa mwajiriwa mtarajiwa ungefanyika (au ungefanyika bila kupindisha matokeo) wasingepatiwa ajira mahala popote pale.Unatarajia nini kutoka kwa binadamu ambaye kichwa chake kimegeuka ulingo wa vita kati ya ubongo na moshi wa bangi?


Lakini tukiweka kando matatizo binafsi ya askari polisi wetu,hebu fanya ziara kwenye makazi yao kisha jiulize mood watakayokuwa nayo kazini!Yayumkinika kusema kuwa miongoni mwa watumishi wa umma wanaoishi katika hali ya udhalilishaji mkubwa ni askari polisi.Sasa badala ya wao kuelekeza hasira zao kwa mwajiri wao,wanaelekea kuhamishia hasira hiyo kwa kila Mtanzania "wa kawaida".Njaa na dhiki zao zinakuwa kichocheo cha chuki yao dhidi ya walalahoi.Kwa upande mmoja,wamewageuza walalahoi hao kuwa shamba lao la kuchuma rushwa,na kwa upande mwingine wamewageuza sehemu za kutolea hasira zao za manyanyaso wanayovumilia kutoka serikalini.


Makazi ya polisi Msimbazi

Serikali ya Kikwete na CCM yake haina cha kupoteza (at least kwa sasa) kwani malalamiko ya askari polisi kuhusu maslahi duni yanapunguzwa na "ruhusa" waliyopewa kuchuma kipato kwa walalahoi,sambamba na kuhalalishiwa viumbe wa kumalizia hasira za askari hao.


 
Kilichonifanya niandike makala hii ni tamko la Jeshi la Polisi kuhusu mauaji waliyofanya huko Arusha.Ukiangalia juu juu,unaweza kudhani wanajitetea tu.Lakini ukiingia kwa undani zaidi utabaini kauli hiyo ni dalili za wazi za kiburi kinachoanza kujitokeza kutoka kwa "mtoto aliyekosa malezi bora".

Kwanini nasema hivyo?Kwanza Rais Kikwete alitoa kauli ya kizushi kwa mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania na kudai kuwa "MAUAJI YA ARUSHA NI BAHATI MBAYA".Nilishalizungumzia hilo kwa mapana zaidi HAPA .Jumatatu iliyopita,Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Bernard Membe alijaribu kutuliza hasira za Watanzania kwa kukiri bayana kuwa Jeshi la Polisi lilikiuka maadili ya kazi yao, lilipokuwa likikabiliana na raia waliokuwa wakiandamana kupinga suala la uteuzi wa meya wa Arusha.

Lakini katika kile blogu hii inatafsiri kuwa JEURI,KICHWA NGUMU na UBABE,jana jeshi hilo lilitoa tamko ambalo haihitaji elimu yoyote kufahamu kuwa ni jibu lao kwa Membe.Katika tamko hilo la kihuni,jeshi hilo sio tu linahalalisha ukatili na uonevu uliopelekea vifo vya mashujaa wawili na majeruhi luluki,pia linafanya mzaha mbaya kwa kudai ni viongozi wa Chadema waliosababisha vurugu na mauaji (kana kwamba viongozi hao ndio waliofumua risasi zilizoua na kujeruhi).

Haihitaji kuumiza kichwa kujiuliza tamko hilo la jeshi la polisi limetolewa na nani.Forget about yule mbabaishaji aliyesimama mbele ya waandishi wa habari kusoma tamko hilo.Huyu alikuwa anatimiza agizo la bosi wake,yaani Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema.Ni Mwema ambaye haafikiani na kauli ya Membe kuwa jeshi hilo lilikiuka maadili.Na kwa vile Mwema ni "mungu wa polisi" basi msimamo wake automatically unakuwa msimamo wa jeshi hilo.Na Mwema ni "mungu-mtu" kweli hasa baada ya kujipachika jukumu la kutoa uhai wa binadamu (kama ilivyotokea huko Arusha na sasa huko Mbarali).

Lakini je Mwema anapata wapi jeuri hiyo ya kupingana na kauli ya Membe,ambaye katika uhusiano wa kimataifa,ni kama mwakilishi mkuu wa Rais katika mahusiano kati ya Tanzania na mataifa mengine duniani?Jibu jepesi lipo katika uhusiano wa karibu uliopo kati ya Mwema na aliyemteua,yaani Rais Kikwete.Mwema anaweza kusema lolote lile lakini Kikwete hawezi kumfukuza kazi.Na sio kwa sababu Kikwete ni dhaifu na mgumu wa kufukuza kazi watendaji wazembe,bali ni huo uhusiano wa karibu kati ya wawili hao.

Sijui kicheko hicho kinahusiana na usalama wa raia au mengineyo

Je inawezekana Kikwete anatuchezea shere kwa kumwelekeza Membe aseme hili kisha kumwambia swahiba wake Mwema aseme tofauti?Nahoji hivyo kwa vile sidhani kama kauli za Membe na Mwema hazina baraka za Kikwete.Ikumbukwe pia kuwa Kikwete na Membe ni "washkaji" mno,huku ikielezwa kuwa Membe alimsaidia sana Kikwete kukubalika ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa wakati wa kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Ushkaji

All in all,Kikwete na Serikali yake ya CCM wanapaswa kutambua kuwa wanacheza mchezo hatari sana ambao unaweza kupelekea balaa kubwa huko mbeleni.Of course,wengi wetu tunafahamu kuwa kuna ombwe kubwa la uongozi linalosababishwa na uwezo duni wa Kikwete katika medani ya uongozi,lakini pengine ni vema akajiweka kando badala ya kuitumbukiza nchi yetu kwenye mtaro wa kupotea kwa amani.

Kikwete anaendesha nchi katika namna ileile anavyoendesha CCM ambapo hana hata nguvu ya kuwakemea wasema-ovyo wa Chama hicho wanaoongozwa na Yusuph Makamba,Tambwe Hizza na mropokaji brand new Mary Chatanda.Sijui anahofia akiwakemea watamgeuka na kutoboa siri ambazo hataki umma ufahamu!Yaleyale ya akina Rostam na Lowassa.Hawa wanamjua Kikwete in and out,na Kikwete anatambua kuwa akiwatibua tu,amekwisha.Yaani kwa kifupi,uongozi wa Kikwete ni kama umewekwa rehani vile.



Sijui kesho au keshokutwa watakurupuka na lipi jipya kuhusu mauaji ya binadamu wasio na hatia.Midomo inawaruhusu kusema lolote lile,na vyombo vya habari vya KURIPOTI BILA KUCHAMBUA vitajibidiisha kurusha habari hizo.Lakini,wakati wanaendelea kubwatuka,ni muhimu wakaitafakari kwa makini kauli ya Paroko wa Parokia ya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, Padre Henry Mushi aliyetanabaisha kuwa damu ya vijana waliouawa kwa kupigwa risasi na Polisi Jijini Arusha, itawaandama polisi waliouhusika katika maisha yao yote.

Namnukuu
"...polisi waliohusika na mauaji hayo, hawawezi kujitetea kuwa walitumwa kwani wao sio mashine kiasi cha kuua raia bila kutafakari...Tendo la kumwaga damu lililotokea Arusha ni baya na yeyote aliyefanya kitendo hicho damu hiyo itamsumbua kama ilivyomsumbua Kaini…Huyo aliyefanya hivyo naye atafuata njia hiyo hiyo...wewe ni binadamu sio mashine kwa hiyo hata kama utasema ulitumwa kufyatua risasi lakini, wewe unayepiga risasi ndiye utakayeulizwa mbele za Mungu kwa kushindwa kutafakari...polisi aliyefanya kitendo hicho asifikiri atajificha mbele ya uso wa Mungu"


“Huyo aliyefanya kitendo hicho hatujui yuko wapi lakini afahamu yuko chini ya Mwanga wa Mungu na njia pekee ya kuepuka hasira ya Mungu ni kutubu dhambi hiyo vinginevyo damu aliyoimwaga itaendelea kumsumbua,”

Padre Mushi alitoa kauli hiyo kijijini Makiidi wilayani Rombo wakati wa ibada maalumu ya mazishi ya mmoja wa wafuasi wa Chadema aliyeuawa katika tukio hilo, Dennis Shirima.



Pichani ni Jeshi La Polisi Tanzania likiwa KAZINI.Hii ilikuwa huko Arusha ambapo WALIUA,na sasa WAMEUA TENA huko Mbeya.

Brandy Nelson, Mbeya na Ramadhan Semtawa

POLISI nchini wameendelea kutumia risasi za moto dhidi ya raia na jana wanadaiwa kuwauwa watu wawili kwa kuwapiga risasi katika vurugu zilizotokea katika wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Habari kutoka Mbarali zinasema polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za moto kuzima vurugu ambazo chanzo chake ni mabishano baina ya raia na polisi hao.

Vurugu hizo zilizotokea jana majira ya saa nane mchana zinadaiwa kusababishwa na baadhi ya wakazi wa kata ya Ubaruku kuzuia kuingia katika eneo lao lori lenye uzito wa zaidi ya tani kumi.

Baadhi ya walioshuhudia tukio hilo walisema hatua ya wananchi kuzuia kwa lori hilo inatokana na kuwepo kwa amri ya serikali wilayani Mbarali itayokataza magari yenye uzito mkubwa wa zaidi ya tani kumi kuingia katika kata ya Ubaruku.

Mmoja wa mashuhuda hao alisema lori hilo lilipokuwa likijaribu kuingie katika eneo hilo wananchi walianza kulizuia huku wakimhoji dereva wake sababu za kuvunja amri iliyopo.

“……walipokuwa wakiendelea kuhojiana na dereva, polisi walifika hapo na hapo wananchi wakaanza kuwauliza polisi sababu za kuruhusu gari kuingie katika eneo lao wakati serikali imeishakataza..,” alisema shuhuda huyo na kuongeza:

“ ni kama polisi na wananchi walishindwa kuelewana lugha hapo tukaanza kusikia mabomu ya machozi na risasi…”.

Alisema hatua ya polisi iliwafanya wananchi kutawanyika na wengine kuanza kuyavamia magari yaliyokuwa kwenye kituo cha mafuta likiwemo gari lililosababisha mvutano huo.

Katika tafrani hiyo magari mawili yaliyokuwa kwenye kituo cha mafuta yalichomwa moto. Magari hayo yanasadikiwa kuwa ni mali ya ndugu wa mwekezaji katika shamba la mpunga la Mbarali.

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Cosmas Kayombo alipohojiwa alikiri kupata taarifa hizo lakini akadai kwamba yuko mbali na tukio hilo na amedai kuwa amewasiliana na mbunge jimbo la Mbarali Dickson Kulufi afike eneo la Tukio.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi alipohojiwa alisema kuwa analifuatilia tukio na mpaka tunakwenda mitamboni tayari gari nne mbili zikiwa zimebeba askari wa kutuliza ghasia (FFU), moja ikiwa imebeba polisi waliovalia kiraia huku wakiongozwa na king`ora kikipiga kelele zikiwa zinaelekea eneo la tukio.

CHANZO: Mwananchi


Katika moja ya maeneo machache ambayo Watanzania tumepiga hatua ya kuridhisha ni fani ya kublogu.Ni vigumu kufahamu idadi kamili ya mabloga wa-na blogu za- Kitanzania (ndani na nje ya nchi) lakini haihitaji sensa kutambua kuwa idadi ni ya kuridhisha.Iwapo idadi hiyo inaendana na matarajio ya wasomaji,hilo ni suala jingine.

Kwa haraka haraka,ni rahisi pia kutambua blogu za picha (zinazoambatana na habari) ndizo zinazotamba zaidi.Pengine ni kwa vile,kama wasemavyo, "PICHA MOJA INAWEZA KUWAKILISHA MANENO ELFU MOJA".Lakini inawezekana pia kuwa wasomaji wetu wengi wako bize,na hawana muda wa kusoma makala ndefu kwenye blogu kama hii.Kadhalika,na hili nalitamka kwa uangalifu mkubwa,huenda kuna kundi dogo la wenzetu ambao kwa mtizamo wao,kusoma ni mithili ya self-inflicted third degree torture.

Blogu hii ina umri wa miaka mitano kasoro miezi mitatu (ilizaliwa mwezi April 2006).Ukiangalia idadi ya wasomaji wanaoitembelea (visitors),unaweza kudhani imeanzishwa miezi michache tu iliyopita.Kuna blogu kadhaa zenye visitors milioni kadhaa,na baadhi yao zina umri haba kulinganisha na wa blogu hii.

Unaweza kudhani inakatisha tamaa.Hapana.Binafsi,naamini nina kundi dogo la wasomaji "tunaoelewana".Yaani namaanisha wasomaji ambao kwa kiasi kikubwa wanaafikiana na dhima kuu ya blogu hii: harakati za haki kwa jamii na mapambano dhidi ya uhujumu uchumi,ukiukwaji haki za binadamu na utawala bora.Haimaanishi kuwa wasomaji hao wanaoiamini blogu hii wanaafikiana na kila nachoandika.Hapana.Kuna nyakati tunatofautiana kimtazamo,na wengi wao huwa huru kunikosoa au kutoa mawazo tofauti na yangu.Of course,kuna nyakati,baadhi ya wasomaji huamua kutumia lugha isiyofaa kuwasilisha ujumbe/mtizamo wao.Hizo ni changamoto katika maisha kwani ukiona kila kitu kinakwenda sawia basi huenda kuna walakini mahala flani.

Of course,ingependeza kuona blogu hii nayo ina visitors milioni 5 au zaidi.Lakini what if kati ya hao,ni asilimia ndogo tu wanaochukulia kwa makini ujumbe uliomo bloguni hapa?Kwangu,idadi ya visitors hainusumbui kwa vile naamini nina kundi dogo la wasomaji makini ambao wanaichukulia blogu hii kama kiwanja chao cha mazoezi kwa ajili ya mapambano ya kusaka uhuru wa pili wa Tanzania,sambamba na kuhabarishana kinachojiri kwenye korido za watawala wetu.

Enewei,kisa cha kuandika post hii ni mfadhaiko nilioupata siku chache zilizopita pale nilipotuma post (niliyoichapisha hapa) kwa bloga mwenzangu wa picha-habari.Kuna nyakati huwa naona umuhimu wa kufikisha ujumbe wangu kwa wasomaji wengi zaidi,hususan wale wapenda picha lakini sio habari.Na kwa kutambua kuwa blogu ya rafiki yangu huyo inatembelewa na wasomaji wengi kuliko hii,na pia kwa vile alishatoa wazo la kumtumia angalau makala moja kwa wiki,nikaona hakuna ubaya wa kumtumia post hiyo.

Cha kusikitisha,sio tu hakuichapisha bali amekuwa akikwepa hata meseji nazomtumia (sio kumkumbushia kuhusu post husika bali mawasiliano yetu ya kawaida tu).Nafahamu kuwa baadhi ya "waswahili" wanapata wakati mgumu sana kuwa wawazi na wakweli kusema "samahani,hii haiendani na hadhi ya blogu yangu".Mhusika anadhani kukaa kimya kutapelekea mie kusahau ombi langu kwake,na ishu itamalizika kienyeji.

Najua kwanini bloga huyo aliogopa kuchapisha post niliyomtumia.Anaogopa mamlaka.Lakini uoga wa nini wakati kilichoandikwa si mawazo yake?Binafsi,kuna nyakati huwa natumiwa habari au matangazo mbalimbali,na ninachofanya ni kuyatundika sambamba na kubainisha chanzo au mtumaji.

Ushirikiano ni muhimu kwa mabloga hasa kwa vile yawezekana mwenzangu hana nilichonacho,nae anacho kile ambacho mie sina.Wingi wa idadi ya visitors isiwafanye  baadhi ya "mabloga wenye majina makubwa" (kama huyu rafiki yangu nayemzungumzia hapa) wajisahau kuwa sisi kama wanadamu ni wanyama tunaohitaji sana ushirikiano (social animals).Na sio lazima ushirikiano huo uwe kwenye kublogu pekee bali mambo mbalimbali yanayotugusa binafsi au jamii kwa ujumla.

Enewei,simlaumu ndugu yangu huyo kwa vile kama ilivyo katika blogu hii,yeye pia ana haki yake ya kikatiba kutochapisha kitu anachoona hakiendani na maudhui ya blogu yake.Lakini,japo pia ni haki yake ya kikatiba,kufanya dharau si jambo la kiungwana.Kunifahamisha kuwa "aah ndugu yangu ile kitu naona inaweza kuniletea matatizo..." sio kauli ngumu,hasa ikitolewa kwa njia ya meseji.

Well,wakati tunaanza mwaka mpya ni vema kufanya inventory ya kuangalia watu walio na umuhimu kwako na wale ambao wanaongeza tu idadi.Namshukuru ndugu yangu huyu kwa kunirahisishia zoezi hilo.



13 Jan 2011

Baadhi ya Makamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, wakiangalia sehemu ya video iliyokuwa ikionesha jinsi Polisi walivyokuwa wakituliza ghasia huko Arusha.


Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Kamanda Paul Chagonja akizungumza na Waandishi wa habari katika Makao makuu ya Jeshi hilo leo



TAARIFA YA JESHI LA POLISI


Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.