Katika moja ya maeneo machache ambayo Watanzania tumepiga hatua ya kuridhisha ni fani ya kublogu.Ni vigumu kufahamu idadi kamili ya mabloga wa-na blogu za- Kitanzania (ndani na nje ya nchi) lakini haihitaji sensa kutambua kuwa idadi ni ya kuridhisha.Iwapo idadi hiyo inaendana na matarajio ya wasomaji,hilo ni suala jingine.
Kwa haraka haraka,ni rahisi pia kutambua blogu za picha (zinazoambatana na habari) ndizo zinazotamba zaidi.Pengine ni kwa vile,kama wasemavyo, "PICHA MOJA INAWEZA KUWAKILISHA MANENO ELFU MOJA".Lakini inawezekana pia kuwa wasomaji wetu wengi wako bize,na hawana muda wa kusoma makala ndefu kwenye blogu kama hii.Kadhalika,na hili nalitamka kwa uangalifu mkubwa,huenda kuna kundi dogo la wenzetu ambao kwa mtizamo wao,kusoma ni mithili ya self-inflicted third degree torture.
Blogu hii ina umri wa miaka mitano kasoro miezi mitatu (ilizaliwa mwezi April 2006).Ukiangalia idadi ya wasomaji wanaoitembelea (visitors),unaweza kudhani imeanzishwa miezi michache tu iliyopita.Kuna blogu kadhaa zenye visitors milioni kadhaa,na baadhi yao zina umri haba kulinganisha na wa blogu hii.
Unaweza kudhani inakatisha tamaa.Hapana.Binafsi,naamini nina kundi dogo la wasomaji "tunaoelewana".Yaani namaanisha wasomaji ambao kwa kiasi kikubwa wanaafikiana na dhima kuu ya blogu hii: harakati za haki kwa jamii na mapambano dhidi ya uhujumu uchumi,ukiukwaji haki za binadamu na utawala bora.Haimaanishi kuwa wasomaji hao wanaoiamini blogu hii wanaafikiana na kila nachoandika.Hapana.Kuna nyakati tunatofautiana kimtazamo,na wengi wao huwa huru kunikosoa au kutoa mawazo tofauti na yangu.Of course,kuna nyakati,baadhi ya wasomaji huamua kutumia lugha isiyofaa kuwasilisha ujumbe/mtizamo wao.Hizo ni changamoto katika maisha kwani ukiona kila kitu kinakwenda sawia basi huenda kuna walakini mahala flani.
Of course,ingependeza kuona blogu hii nayo ina visitors milioni 5 au zaidi.Lakini what if kati ya hao,ni asilimia ndogo tu wanaochukulia kwa makini ujumbe uliomo bloguni hapa?Kwangu,idadi ya visitors hainusumbui kwa vile naamini nina kundi dogo la wasomaji makini ambao wanaichukulia blogu hii kama kiwanja chao cha mazoezi kwa ajili ya mapambano ya kusaka uhuru wa pili wa Tanzania,sambamba na kuhabarishana kinachojiri kwenye korido za watawala wetu.
Enewei,kisa cha kuandika post hii ni mfadhaiko nilioupata siku chache zilizopita pale nilipotuma post (
niliyoichapisha hapa) kwa bloga mwenzangu wa picha-habari.Kuna nyakati huwa naona umuhimu wa kufikisha ujumbe wangu kwa wasomaji wengi zaidi,hususan wale wapenda picha lakini sio habari.Na kwa kutambua kuwa blogu ya rafiki yangu huyo inatembelewa na wasomaji wengi kuliko hii,na pia kwa vile alishatoa wazo la kumtumia angalau makala moja kwa wiki,nikaona hakuna ubaya wa kumtumia post hiyo.
Cha kusikitisha,sio tu hakuichapisha bali amekuwa akikwepa hata meseji nazomtumia (sio kumkumbushia kuhusu post husika bali mawasiliano yetu ya kawaida tu).Nafahamu kuwa baadhi ya "waswahili" wanapata wakati mgumu sana kuwa wawazi na wakweli kusema "samahani,hii haiendani na hadhi ya blogu yangu".Mhusika anadhani kukaa kimya kutapelekea mie kusahau ombi langu kwake,na ishu itamalizika kienyeji.
Najua kwanini bloga huyo aliogopa kuchapisha post niliyomtumia.Anaogopa mamlaka.Lakini uoga wa nini wakati kilichoandikwa si mawazo yake?Binafsi,kuna nyakati huwa natumiwa habari au matangazo mbalimbali,na ninachofanya ni kuyatundika sambamba na kubainisha chanzo au mtumaji.
Ushirikiano ni muhimu kwa mabloga hasa kwa vile yawezekana mwenzangu hana nilichonacho,nae anacho kile ambacho mie sina.Wingi wa idadi ya visitors isiwafanye baadhi ya "mabloga wenye majina makubwa" (kama huyu rafiki yangu nayemzungumzia hapa) wajisahau kuwa sisi kama wanadamu ni wanyama tunaohitaji sana ushirikiano (social animals).Na sio lazima ushirikiano huo uwe kwenye kublogu pekee bali mambo mbalimbali yanayotugusa binafsi au jamii kwa ujumla.
Enewei,simlaumu ndugu yangu huyo kwa vile kama ilivyo katika blogu hii,yeye pia ana haki yake ya kikatiba kutochapisha kitu anachoona hakiendani na maudhui ya blogu yake.Lakini,japo pia ni haki yake ya kikatiba,kufanya dharau si jambo la kiungwana.Kunifahamisha kuwa "aah ndugu yangu ile kitu naona inaweza kuniletea matatizo..." sio kauli ngumu,hasa ikitolewa kwa njia ya meseji.
Well,wakati tunaanza mwaka mpya ni vema kufanya inventory ya kuangalia watu walio na umuhimu kwako na wale ambao wanaongeza tu idadi.Namshukuru ndugu yangu huyu kwa kunirahisishia zoezi hilo.