2 Aug 2014


Nakumbuka siku moja nilikupokuwa 'rafiki' na ndugu yangu flani huko Twitter (kwa sasa hatupo karibu) aliwahi kunambia, (namnukuu), "Tatizo lako Bwana Chahali ni kuamini kuwa unajua kila kitu, na kudhani siku zote upo sahihi." Maneno haya hujirudia kichwani mwangu mara kwa mara. Japo nilimshukuru kwa maelezo hayo, kiukweli nilibaki na mwaswali mengi tu, moja likiwa "hivi kujua kila kitu (kama inawezekana) ni dhambi?" Na pia "je kuna tatizo kuamini upo sahihi hususan iwapo umefanya jitihada za kuwa sahihi?"

Kuna baadhi ya wenzetu, licha ya kuwa mtandaoni kwa muda mrefu hawajaweza kutambua kuwa ni rahisi sana kuishi maisha ya 'namna flani' mtandaoni. Kwa mfano, ni rahisi kuwa sahihi 'kila wakati' iwapo utakuwa makini katika mada unazozungumzia mtandaoni. Ni vigumu kuwa sahihi katika kila mtihani kwa sababu hata ukijianda vipi bado kuna uwezekano wa mtihani kuja tofauti. Lakini, kwa mfano wa Twitter, kwanini ushindwe kuwa sahihi kila mara ilhali kila unapokutana na jambo flani una muda wa kutosha ku-Google au kurejea notes zako binafsi? Binafsi, nina tabia ya kuto-post kitu chochote kile mtandaoni kabla sijapata uhakika kuwa kipo sahihi kwa asilimia 100. Na kinachonirahisishia ni ukweli kwamba nina muda wa kutosha kufanya hivyo. Mtu akikukuuliza swali kwenye Twitter, kwa mfano, una muda wa kutosha kutafuta facts kwenye Google au Wikipedia, au kurejea uelewa wako binafsi, kabla ya kukurupuka kumjibu.

Anyway, nimeandika hayo kwa sababu makala hii inaweza kuzua maswali kama hayo ya 'rafiki yangu mstaafu' kwamba "ah huyu nae anakuja na 'mbinu za maisha' kana kwamba anayajua sana maisha." No, tunaishi katika dunia ya uchaguzi wa kutaka kufahamu mengi au pungufu au kutofahamu kabisa. Ni suala la uchaguzi tu. Na kamwe sioni aibu kutamka bayana kuwa ninafahamu vitu vingi mno...kwa sababu ninajibidiisha mno kuvifahamu. Background yangu inanisaidia pia: awali nilisoma Sosholojia, baadaye nikahamia kwenye stadi za siasa, na kwa zaidi ya miaka 10 nimekuwa 'nikijisomea binafsi' katika maandalizi ya makala zangu magazetini na katika blogu hii...sambamba na majukumu mengine yaliyonilazimisha kuelewa mengi ya yanayonizunguka.

Twende kwenye mada husika. Hapa chini kuna orodha ya mambo 13 ambayo imethibitika kuwa usipoyadhibiti yanaweza kukwaza mafanikio katika maisha yako. Hebu tuyaangalie moja baada ya jingine.

1.UNAKWEPA MAJUKUMU: Kila jambo uliloshiriki kulifanya likizaa matokeo mabaya unakimbilia kumlaumu flani. Hata 'ukilikoroga' katika maisha yako binafsi, unatafuta wa kumlaumu, aidha mzazi wako, rafiki yako au hata Muumba wako. Kama kweli unataka kufanikiwa maishani mwako ni muhimu kubeba lawama hasa pale ambapo wewe ndio chanzo cha kutofanikiwa kwa suala husika. By the way, uzoefu unathibitisha kuwa lawama hazijengi, na kukwepa majukumu hakusaidii kumfanya mosaji aonekane yupo sahihi.

2. UNASUBIRI MUDA MWAFAKA MILELE: Muda una sifa moja kuu: waweza kuusbiri lakini ukifika hautokwambia 'Chahali, mie ndo muda uliyekuwa ukinisubiri.Sasa nimefika, nitumie ipasavyo.' No. Muda hauna muda huo. Waweza kuusubiri milele na ukifika hautokushtua. Kuna mesmo mmoja wa Kiingereza kwamba njia bora ya kuishi ni kuichukukulia kila sekunde katika maisha yako kama muujiza ambao kamwe hautojirudia. Waweza kusubiri muda milele, na pasipo jithada ya kutumia muda japo kiduchu unaojitokeza, utazeeka huku unasubiri muda mwafaka. Kumbuka ilipokuwa jana ulisema kesho, ambayo ndio leo, na leo ukisema kesho, itapofika itakuwa leo nyingine.

3. KUPANIA KUWA MTIMILIFU: Waingereza wanasema hakuna mtu mtimilifu kwa asilimia 100, yaani nobody is perfect. Haba na haba hujaza kibaba. Kidogo kinachopatikana leo kinaweza kuwa kingi kesho au baadaye. Kweli, inapendeza kuwa mtimilifu (perfect) lakini uzoefu unaonyesha kuwa ni vigumu mno kuwa mtimilifu kabisa kabisa (absolute perfection.). Wewe si malaika, na hata hao malaika pengine wana mapungufu flani.Cha muhimu ni kutambua mapungufu yako na kuyafanyia kazi ili uwe mtu bora zaidi.

. 4. UNAOGOPA KUKOSOLEWA: Ni hivi, hata ukifanya jambo zuri kiasi gani bado kuna wanaoweza kupata upenyo wa kukukosoa. Sasa kama umefanya jambo lisilostahili, kwani usikosolewe? Watu waliofanikiwa zaidi maishani ni pamoja na wale waliochukulia kukosolewa kama fundisho. Hapa simaanishi kuwa hata ukikisolewa kwa chuki ukubali.Ninachomaanisha ni kwamba pindi ukikosolewa waweza pia kupata fursa nzuri ya kutathimini wapi ulikose au kipi ulikosea.

5. UNAOGOPA KUSHINDWA: Maisha ni kama mechi ya mpira wa miguu: kuna kushinda, klushindwa au kutoka sare. Kuna utakavyovipata katika mihangaiko yako ya maisha, lakini pia kuna utakavyovikosa, au utakavyopata nusu na kukosa nusu. Lakini ni muhimu kutambua kuwa kama ilivyo kwenye mpira, huwezi kushinda au kutoka sare bila kuingia dimbani. Wengi wa waliofanikiwa maishani ni waliotambua kuwa kuna kufaulu na kufeli, na walipofeli walikaa chini kujiuliza tatizo liko wapi, na badala ya kuogopa kufeli tena, walitumia walichojifunza ili kupata matokeo bora zaidi. Ukiogpa kufeli hutoweza kujaribu, achilia mbali kufanya .

6. NI MVIVU/MZEMBE: Sheria moja ya maisha inasema 'ukifanya jambo kwa kiwango kilekile cha wanaokuzunguka, basi wewe ni mvivu/mzembe' Tunaishi dunia ya ushindani, na ukitaka uwe bora zaidi ya wengine basi sharti ufanye ziada zaidi ya hao wengine unaotaka kuwa bora zaidi yao. Kama wenzio wanafanya kazi masaa matano, kwanini usifanye masaa sita au hata kumi ikibidi, alimradi watambua kuwa kwa kufanya hivyo utakuwa bora zaidi yao? Kanuni nyingine ya mafanikio ni 'amka mapema,fanya kazi kwa bidii, fanikiwa.'

7. HUNA UHALISI WALA UBUNIFU: Unapaswa kuwa mtu wa kipekee, si kwa mabaya bali mema. Na njia nyepesi ni kutambua kinachowafanya wenzio waonekane bora kisha kufanya maradufu ya wafanyacho. Pia nimuhimu kuwa mbunifu, hata kama itamaanisha kukopi kwa wenzio na kuboresha 'kivyako.' Na njia nyepesi ya kuwa mbunifu ni kusoma wafanyacho wenzako kisha kutafuta namna ya kukiboresha zaidi.

8. KUN'ANG'ANIA KUFANYA MAMBO PEKE YAKO: Ukifanikiwa na 'timu ya ushindi' haimaanishi umefanikiwa kwa upungufu. Angalia wanasoka wa timu kubwa duniani. Mafanikio yao ni mchanganyiko wa jitihada za kipa,mabeki, viungo na washambuliaji, lakini hiyo haipunguzi  mafanikio yao. Kumbuka umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Ili uweze kufanikiwa kwa kiwango kikubwa maishani wahitaji ushirikiano na watu na vitu mbalimbali.

9. HUNA SHUKRANI: Ukosefu wa shukrani waweza kukukwaza kwa kiasi kikubwa kupata mafanikio maishani.Nani anataka kumsaidia mtu asiye na shukrani.Kama nilivyoeleza hapo juu kuwa mafanikio yanahitaji ushirikiano, lakini ni vigumu kumpata mshirika anayefahamu kuwa huna shukrani. Kuwa mwepesi wa kusema asante hata pasipostahili asante. Huna cha kupoteza kwa kushukuru, na kila shukrani unayotoa yaweza kukurejeshea fadhila nyingine lukuki kwa sababu kwa silika yetu binadamu twapenda kuwasaidia wenye shukrani. Na shukrani si tu kwa wanaotutendea mema, wakati mwingine mshukuru hata anayekukosea kwa sababu unampa mtihani wa 'kwanini kanishukuru?' Next time mtu yuleyule alokutenda vibaya aweza kukutenda vyema kwa vile alipokutenda vibaya ulimshukuru, je akikutenda mema shukrani si zitakuwa maradufu?

10.HUTAKI KUJIFUNZA KUTOKANA NA MAKOSA: Mara nyingi kikwazo cha kujifunza kutokana na makosa ni aidha kuyachukia makosa hayo pasi dhamira ya kujipanga ili kutoyarudia, au silika ya kupuuza makosa na kukazani akuangalia mafanikio pekee. Uzoefu umeonyesha kuwa wakati mwingine makosa ni mwalimu mzuri, kwani yatuelekeza wapi tulipaswa kufanya hiki lakini tukafanya kile au hatukufanya kitu kabisa. Ili ufanikiwe ni muhimu kuyaangalia makosa kama fursa ya kujirekebisha. 

11.HUJIAMINI: Ni hivi, usipojependa hakuna atakayepoteza muda wake kukupenda. Vivyo hivyo, usipojiamini, hakuna atakayepoteza muda wake kukuamini. Ili uaminike shurti ujiamini mwenyewe kwanza. Kujiamini kwakujengea uwezo wa kusema 'Ninaweza.' Na kutojiamini kwakuleta swali 'Ntawezaje?' Ni muhimu kutambua kuwa ili uweze kujiamini ni sharti la muhimu kujielewa na kutambua uwezo na mapungufu yako. Boresha uwezo wako, jifunze katika makosa yako na kwa watu wengine, tumia maosa kama darasa na jaribu kujiamini. Yes you can!

12. HUNA MSIMAMO: Mshika mawili moja humponyoka, wahenga walituasa. Lakini licha ya kuwa mshika mawili, kuna busara kwamba kuwa na 'lan B' pia kwaweza kukufanya ushindwe kusimama katika jambo moja. Ndio ni vema kujitengenezea mazingira ya 'likishindikana hili ntafanya lile' lakini wakati mwingine ni muhimu kuliangalia jambo lilipo mkononi kama ndio fursa pekee, na hakuna njia mbadala. Ni rahisi kutambulika na hata kukubalika katika jamii iwapo una msimamo, na ni vigumu kupata wafuasi iwapo unayumba kama bendera kufuata upepo.

13.UMEACHA KUKUA: Watu wenye mafanikio hutambua umuhimu wa kuboresha vipaji na/au uwezo wao. Waingereza wanasema 'ukiambiwa upo vizuri basi jibidiishe kuwa vizuri zaidi.' Kama kuna jambo moja linaloweza kusababisha utuame kimaendeleo ni kubweteka. Mifano ni mingi, tuna wasanii, kwa mfano, walofikia hatua kubwa za mafanikio, kisha wakabweteka. Sote twajua hatma yao. Endelea kukua hata kama jamii yakutambua kama ulofikia mafanikio ya hali ya juu. Japo pengine ni sahihi kutaka zaidi na zaidi, lakini wewe ni nani wa kuihukumu kuwa ulichonacho ni zaidi? Na kuwa na zaidi alimradi ni chema kuna ubaya gani?

Natumaini makala hii itakuwa na msaada kwako katika azma yako ya kufikia mafanikio. Usikose kutembelea blogu hii ili kupata mengi yahusianayo na MAISHA, bonyeza hapo kwenye section ya MAISHA kujifunza mengi zaidi.

Makala hii imetafsiriwa kutoka vyanzo mbalimbali mtandaoni.

Kiuhalisia, kuna aina lukuki za watumiaji wa mitandao ya kijamii. Lakini katika kuweka mambo sawia, isingipendeza kuwa na 'makundi makuu' kama makabila vile kisha ukijitanabaisha upo 'kabila' lipi miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii?

Kimsingi, mitandao ya kijamii ni nyenzo ya kukuunganisha na watu-aidha kusikia au kutaka kusikika. Na kwa maana hiyo, ni muhimu kwa mtumiaji kujitambua mapema, na kujiweka katika kundi analodhani linamfaa au lina manufaa zaidi kwake.

Kwahiyo,katika uchambuzi huu, kuna makundi 10 ya msingi ya watumiaji mbalimbali wa mitandao hiyo ya kijamii. Ni matarajio ya makala hii kwamba utapomaliza kuisoma,utabaini upo kundi gani, au ungependa kuwa katika kundi gani. Enjoy!

068ecf0a8e7ac52b676ef4afe6a5a811

Kundi la kwanza ni MSIKILIZAJI: Huyu anapendelea sana mitandao ya kijamii lakini mara nyingi yupo kinya, hataki kuonekana wala kusikika. Kama jina lilivyo, yeye ni msikilizaji tu.Anaweza kuipenda post yako kwenye Facebook lakini akakaa kimya.

Kundi jingine ni MWANAHARAKATI: Huyu ni mtu anayetambua nguvu ya mitandao ya kijamii katika kufikisha ujumbe,na anafanya kila awezalo kuitumia ipasavyo ili kufikisha sauti yake iskike na hatimaye kuleta tofauti inayokusudiwa. (Binafsi nadhani ninaangukia katika kundi hili)

Kundi la tatu ni MCHAFUZI WA HALI YA HEWA: Huyu ni mtu anayedhani kwamba mabandiko yake mtandaoni ni ya kiwango cha hali ya juu, kiasi cha kuamini kuwa kila mtu anastahili kutumiwa kwenye inbox yake (tena pasi kujali ridhaa ya mtumiwa). Nadhani ushakutana na DM au meseji Facebook yenye ujumbe 'angalia picha hii...' na ukilogwa kubonyeza link husika waweza kujutia nafsi yako.

Kundi la nne ni MWENYE MAHABA NA ISHU FLANI: Ushakutana na mtu anapenda mpira kupita kiasi, na ukifuatilia mabandiko yake kwenye mitandao ya kijamii utadhani ni chombo cha habari. Mtu wa aina hii anaendeshwa na mahaba ya akipendacho-iwe siasa, burudani, uchumi au ishu nyingine yoyote ile, na anatumia muda kuifuatilia ishu hiyo na ku-share na jamii. Kimsingi watu wa aina hii wanaweza kuufanya mtandao wa kijamii kuwa mahala pa kujifunza kama sio kuburudisha. (Nahisi pia ninaangukia kundi hili kwa mada nizipendazo, yaani siasa, teknolojia, habari na intelijensia)

Kundi la tano ni KIPEPEO WA JAMII Huyu ni yeye na picha. Atakjuonyesha kila sehemu aliyotembelea, kila shughuli aliyofanya, na kila hachoki ku-tag watu kwenye picha hizo. Pengine ni mtu wa watu lakini pengine ni msumbufu tu anayetaka kuonyesha maisha yake kwa njia ya picha. Kipepeo wa jamii anaweza kutengeneza idadi kubwa ya marafiki kwa sababu mara nyingi huwa kama analazimisha kila mtu awe rafiki yake kwa njia ya picha.

Kundi la sita ni WASUMBUFU MTANDAONI: Huyu ni mtu anayeweza kuvuka mpaka kati ya kupishana hoja kistaarabu hadi kufikia kashfa,matusi na udhalilishaji. Mara nyingi mtu wa aina hii hung'ang'ania ishu zisizo za msingi lakini zenye madhara kwa hadhi au heshima ya mlengwa katika jamii. Njia pekee ya kukabiliana na mtu wa aina hii ni kum-block, kwa sababu jaribio lolote la kumuelimisha-hata liwe la kistaarabu kiasi gani-litaishia kuzua mabalaa zaidi.

Kundi la saba ni MWALIMU: Huyu ni kama yuole wa kundi la nne hapo juu (mwenye mahaba na ishu flani) lakini yeye hana ishu maalumu bali anapenda ku-share uelewa (knowledge). Mara nyingi anakuwa na uelewa wa kutosha lakini haridhika kukaa na uelewa huo peke yake na badala yake anashirikisha wengine.Mtu wa aina hii anaweza kuwa muhimu sana katika mtandao wa kijamii kwani anatoa elimu bure (nami najihisi kama nipo kundi hilo,japo siwezi kujihukumu).

Kundi la nane ni ALIYEANZA KITAMBO: Mara nyingi utamgundua mtu huyu katika katika mtandao mpya (angalau kwake), ambapo kwa vile alikuwepo tangu zama za Facebook haijawa maarufu kama sasa basi anataka kila mtandao wa kijamii anaojiunga nao 'ufuate kanuni' za Facebook ya zamani. Watu wa aina hii hupatikana zaidi Twitter ambapo hufanya kiola wawezalo kuigeuza Twitter kuwa Facebook. Huyu anaweza kukukera kirahisi kwa sababu anataka kulazimisha matamanio yake yawe ya watu wote.

Kundi la tisa ni la MWENYE KITABU CHEUSI: Kama hufahamu, kitabu cheusi ni kama diary yenye kumbukumbu mbalimbali za kila siku pamoja na namba za simu au anwani za watu mbalimbali. Mara nyingi mtu wa aina hii yupo kwenye mtandao wa kijamii kwa ajili ya mawasiliano na wengine. Si ajabu kuona mtu wa aina hii akiwa na 'marafiki' au 'wafuasi' kibao kwa sababu yupo kwenye mtandao wa kijamii kwa ajili hiyo.

Kundi la kumi na la mwisho ni MTU WA FAMILIA:Huyu anaweza kuwa mtu asiye na uzoefu sana na teknolojia lakini mara baada ya kufahamu jinsi ya kuitumia basi anataka kuhakikisha anakuwa karibu na 'familia' yake. Mara nyingi mtu wa aina hii yupo katika mtandao wa kijamii kwa minajili ya kifamilia zaidi, na ninaposema familia inajumuisha pia watu wa karibu na mhusika.

Kama nilivyobainisha awali, mitandao ya kijamii ina aina lukuki za watumiaji japo hizi 10 zinaweka pamoja watu hao katika makundi hayo makuu. Je hadi kufikia hapa unadhani upo katika kundi gani?

CHANZO: Makala hii imetafsiriwa kutoka tovuti ya DAILYGENIUS

Endelea kutembelea blogu hii ili kupata makala na habari mbalimbali, na iwapo ni mpenzi wa teknolojia kama mie basi usikose kubonyeza hapo juu ya blogu palipoandika TEKNOLOJIA ili kupata kila kilicho bora katika anga hizo. 



31 Jul 2014

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA na shushushu mzoefu, John Brennan, akiwa amezungukwa na walinzi wakati akitoa maelezo yake katika 'bunge' la Seneti la nchi hiyo.
Kwa Watanzania wengi, bila shaka mara yetu ya kwanza kufahamu kuhusu mashushushu ilikuwa kupitia vitabu vya Willy Gamba.Unakumbuka 'KIKOMO'? Au 'KIKOSI CHA KISASI?' Au vipi kuhusu 'NJAMA'? Sio siri, kusoma vitabu vya Willy Gamba vya marehemu Aristablus Elvis Musiba kulimfanya kila msomaji atamani kuwa kama Willy Gamba...yaani shushushu. Lakini kwa vile zama za Willy Gamba zilikuwa kipindi ambacho Tanzania ilikuwa kama 'kisiwa' kisichofahamu yanayojiri nje yake, riwaya hizo zilikuwa na mengi yaliyoshabihiana na shushushu wa kimataifa James Bond wa Uingereza.

Lakini baada ya Tanzania kufungua milango yake kwa dunia, wengi walibahatika kumwona James Bond kupitia filamu zake mbalimbali.Lengo la makala hii sio kujadili vitabu hivyo bali kujenga picha halisi, na penine tofauti kati ya ushushushu wa vitabuni au kwenye filamu na uhalisia wa taaluma hiyo. Lakini kabla ya kwenda mbali ni vema pia kukumbushia kuhusu 'Mashushushu wa zama hizi' kwa mfano Jack Bauer wa 'series' ya 24. Wakati Willy Gamba ameendelea kubaki vitabuni tu-kwa maana kwamba hakuna filamu iliyotengenezwa (bado nina fikra za kuyarejesha maisha ya shushushu huyu kwa njia ya filamu), James Bond amekaa 'kizamani' kwa maana ya uwepo wake kwa miaka mingi.Lakini Bauer anaonekana kama 'shushushu wa kizazi kipya' kama ilivyo kwa Nicholas Brody na Carrie wa Homeland, ambao katika filamu zao zina baadhi ya mabo ya kisasa kama matumizi ya mitandao ya kijamii (kwa mfano Facebook na Twitter) na mambo mengine ya 'kwenda na wakati.'

Hata hivyo, japo ushushushu wa kwenye vitabu vya Willy Gamba na filamu za James Bond au series kama 24 na Homeland zinatoa picha ya karibu kabisa na taaluma halisi ya ushushushu, kuna tofauti kubwa kati ya ndadharia na vitendo. Makala hii inazungumzia maisha halisi ya shushushu mstaafu wa shirika la ujasusi la Marekani (CIA), Robert Baer

Kwenye filamu ya hivi karibuni ya James Bond, SKYFALL, 'kubwa la maadui' ni gaidi la mtandaoni (cyberterrorist),Raoul Silva, shushushu wa Kiingereza aliyeasi na mwenye dhamira ya kusababisha 'kiama' kwa ulimwengu wa komputa (digital universe).Ukiangalia filamu hiyo unapata picha ya jinsi janga hilo linavyoweza kuwa na madhara makubwa. 
Lakini kitu pekee cha karibu kati ya ushushushu wa kwenye filamu na ushushushu halisia ni ukaribu na ukweli wa tishio la ugaidi wa kompyuta. Yaani, iwe ni kwenye filamu au katika dunia halisi, kilichomo kwenye filamu hiyo kitakuwa janga kubwa laiti kikitokea. 
Usinielewe vibaya, mie ni shabiki wa filamu za James Bond.Huenda kuziangalia kwa sababu zilezile ambazo kila mwendaji filamu anazo: wanawake warembo, sehemu nzuri za kuvutia, na 'kimuhemuhe' kinachoambatana na stori zinazobeba filamu za Bond.
Lakini kama shushushu mstaafu, kinachonivutia zaidi katika filamu za Bond ni kila mara mema kushinda maovu.Katika filamu zote za Bond, kubwa la maadui huangamia na dunia ya watu wema husalimika. 
Lakini katika ushushushu halisia, mambo hayaendi 'kiuzuri' kama iavyooneshwa katika filamu za Bond, na kwa hakika kuna 'mbinde' kadhaa. 
Tofauti na busara za muda mrefu mrefu kuwa adui wa adui yetu ni rafiki yetu, kwenye ushushushu halisia hali yaweza kuwa tofauti. Wakati flani, kwenye miaka ya 1980,nilipewa kabrasha la viongozi flani wa upinzani nchini Libya, miongoni mwa wengi waliokuwa wakifanya shughuli zao jijini Khartoum,nchini Sudan. Awali, nilkuwa na upeo mdogo tu kuhusu wasifu wa wapinzani wa kingozi wa Libya wa wakati huo,Kanali Muamar Gahddafi. Kitu pekee nilichokuwa na uhakika nao ni kwamba Rais wa Marekani wakati huo,Ronald Reagan, alikuwa anataka Gaddafi aangamie. 
Usiku mmoja, nilishtushwa na sauti za vitako vya bunduki vilivyokuwa vikibamiza mlango wa chumba changu.Watoa habari wangu wawili wa Kilibya walikuwa wakihangaika kulinda maisha yao dhidi ya wauaji wa Ghaddafi na walitegemea mie ndio niwapatie ulinzi.Tulfanya maongezi takriban usiku mzima kuhusu Libya, historia ya nchi hiyo na Allah. Ulipotimu muda salama kwa wao kuondoka, nilikuja kubaini kuwa watu tuliowaamini kuwa wangetusaidia kumwondoa Ghaddafi ni Waislam wenye msimamo mkali ambao lengo lao kuu ni kuifanya Libya kuwa taifa la msimamo mkali wa Kiislam. 
Wakati flani,katika kumfuatilia mtoa habari 'mpotevu,' mwajiri wangu (CIA) alinituma Monaco. Matatizo yalianza hata kabla sijapanda ndege. CIA walikataa kuninulia suti ya tuxedo (ili kuendana na mazingira ya casino za huko) na mhasibu wetu alikataa kunipa fedha za kuchezea kamari.Nilipofika,na kuingia kwenye casino hiyo, walinzi walinihoji kirefu, na mwishowe operesheni hiyo haikufanikiwa kwani sikuweza kumpa mtoa habari niliyekuwa nikimsaka. Kwa hakika nilitambua urahisi alionao James Bond kwenye filamu ni mgumu katik halisi halisi. 
Mtu yeyote aliyepitia chuo cha mafunzo ya mashushushu wa CIA Langley atakwambia maisha ya shushushu yanahitaji uvumilivu mkubwa. Ni muda mrefu wa kuwa peke yako katika kijichumba kidogo, kupitia mafaili kwa undani, mafaili ambayo watu kibao wameshayapitia, matarajio yakiwa wewe utagundua kitu ambacho wenzio hawakukiona. Au kugandishwa kwenye kibanda cha simu kwa muda mrefu ukisubiri labda mtoa habari atakupigia simu. Au kufanya dua kwa matumaini kwamba operesheni yako ijayo sio katika eneo la kutishia uhai.  
Hata hivyo, pamoja na yote hayo sio kusema kwamba katika ushushushu hakuna matukio kama tunayoyaona katika filamu za James Bond.Mashushushu walimwinda Osama bin Laden na hatimaye kufanikiwa kumuua watakueleza kwamba mara kadhaa walikuwa kama wanaishi kwenye filamu ya James Bond. 
Hata hivyo, ukweli unabaki kuwa maadui wanaowindwa na mashushushu huwa wanajificha katika mazingira ambayo kwa hakika ni vigumu mno kuwagundua. 
Kama ilivyo kwa CIA, maafisa wa shirika la ujasusi la Uingereza MI6 pia wanatumia mjuda mwingi maofisini badala ya unachokiona kwenye filamu za James Bond au Jack Bauer wakifanya mambo ya miujiza kama kuruka kutoka kwenye ndege na kusalimika. Na kama walivyo wenzao wa CIA, kwa muda mwingi mashushushu wa MI6  ni watu wa kupekua mafaili ofisini kuliko watu wa action kwenye mapambano ya 'kuchemsha damu' kama inavyoonyeshwa kwenye filamu za kipelelezi. 
Katika zama tunazoishi sasa, mashushushu wengi ni watu wa kupekua data na kujaribu 'kuhujumu' kompyuta. Hawa ndio watu waliomudu kuhujumu mfumo wa kompyuta wa kijasusi na nyuklia wa Iran unaofahamika kama Stuxnet. Huenda kabla ya kufanikisha operesheni hiyo, mashushushu hao walikaa kwenye kompyuta zao miezi kadhaa kusaka mafanikio walioyapata.
Angalau filamu nyingine ya kishushushu kutoka Hollywood, Argo, inatoa picha ya karibu ya maisha halisi  ya shushushu- kukaa ofisini muda mrefu kurudia 'somo' lileile hadi 'siku ya siku ya balaa' inapowadia. Operesheni za 'hatari' hutmia muda mwingi wa maandalizi ofisini kuliko katika 'uwanja wa mapambano' au 'eneo la tukio,' tofauti na inavyoonyeshwa katika filamu nyingi za aina hiyo. 
Lakini japo mwisho wa filamu hiyo ya 'Argo' ni mtamu ambapo 'mateka' wote waliokolewa, hali haikuwa hivyo kiuhalisia kwani si mateka wote waliookolewa na mwishowe Marekani iliishia kuumbuka badala ya kuonekana shujaa anayeonyeshwa katika filamu ya Argo.

Sote tuliinjoi kusoma stori za Willy Gamba au kuburudika na stori za James Bond, Jack Bauer au Carrie na Nicholas Brody ambazo kwa kiasi flani zinarahisisha operesheni za kishushushu kwa minajili ya ileile ya 'stering hauwawi.' Hata hivyo, kwenye uhalisi wa operesheni za kishushushu ni vigumu mno kubashiri matokeo, na hata kama mambo yakionekana kwenda sawia kama ilivyapangwa, surprise ni jambo la kawaida. 

Na wakati mwingine ugumu wa operesheni unachangiwa na funzo muhimu kwa mashushushu kwamba 'ukiona kila kitu kinakwenda sawia basi ujue kuna hatari huko mbeleni.' Katika mafunzo ya taaluma hiyo, inakumbushwa mara kwa mara kwamba kamwe usiamini unachokiona bali jaribu kwenda ndani zaidi na kutafuta kisichoonekana.

Nimalizie makala hii na stori moja ya kusisimua (hainihusu): jamaa flani alikuwa ajifanikiwa kujipenyeza kwenye genge flani la wauza noti bandia katika mtaa mmoja maarufu jijini Dar. Kwa umahiri wake alifanikiwa kuaminika mno hadi akaweza kuwa karibu na bosi wa genge hilo. Kwa vile mashushushu ndio wanaowataarifu polisi kabla ya kuvamia makundi kama hayo, siku ya tukio kulijitokeza mgogoro wa kimawasiliano kati ya mashushushu na polisi, na matokeo yake polisi walivamia genge hilo wakati yule jamaa akiwa kazini-kaka shushushu na kama membe wa lile genge. Naomba uelewe kuwa katika matukio ya aina hiyo kuna uwezekano wa kupoteza maisha kwa vile polisi wanadhani wote waliomo katika genge husika ni wahalifu halisi bila kujua kuwa kuna mashushushu wapo kazini pia. 

Katika dakika ya kuamua kifo au kubaki hai, jamaa huyo alipatwa na mtihani wa aidha ajitambulishe kwa polisi na kuwasihi wawasiliane na viongozi wa operesheni hiyo (na kwa kufanya hivyo angekuwa anaweka roho yake rehani kwani genge lingebaini kuwa yeye ndo aliwachoma) au 'afe kizungu na tai shingoni' kwa kuendelea kujifanya mhalifu na kuomba dua zake pilisi wasimtoe roho...

No, hiyo sio hadithi ya kutunga. Ni tukio la kweli kabisa, na japo nisingependa kueleza hatma yake kwa undani (jamaa huyo alisalimika na yupo hai hadi leo licha ya baadhi ya wahalifu 'wenzie kuuawa au kujeruhiwa kwa risasi za polisi katika tukio hilo) nadhani tukio hilo laweza kukuonyesha jisni ushushushu wa vitendo unavyoambatana na hatari ambazo pengine kwenye vitabu vya Willy Gamba au filamu za James Bond, 24 au Homeland zinajengwa katika amzingira ya 'stering hauwawi.'

Endelea kutembelea blogu hii kwa ajili ya kupata habari na matukio mbalimbali yanayohusiana na taaluma ya intelijensia, hasa kwa kubonyeza hapo juu ya blogu kwenye maneno INTELIJENSIA




'Malkia wa selfies' Kim Kardashian. 
Kwa mujibu wa kamusi ya Kiingereza ya Oxford, neno selfie maana yake ni picha ambayo mtu amejipiga mwenyewe, hususan kwa kutumia simu za kisasa (smartphones) au 'kamera ya mtandao' (webcam)kwa minajili ya kuiposti kwenye mitandao ya kijamii (social media).
Moja ya selfie maarufu kabisa iliyopigwa katika tuzo za Oscar mapema mwaka huu
Kwa kifupi, selfie ni kwa ajili ya 'maonyesho,' na hakuna anayetaka kupiga selfie isiyopendeza, ya kumpatika 'likes' za kutosha. Sasa kwa vile selfies ni kwa ajili ya 'maonyesho,' ni wazi hakuna anayetaka kupizo vizuri, akajipiga picha, lakini matokeo yake picha husika ikawa kama ya kuchora- kwa maana ya ubora hafifu.

Makala hii fupi inakupa orodha ya apps za kupiga picha za selfies za kiwango bora kabisa. Orodha hii ni kwa ajili ya simu za Android pekee (orodha ya apps za selfie kwa iOS itawajia baadaye). Enjoy!

INSTAGRAM

instagram android

Instagram ni kama 'baba lao' linapokuja sula la selfie. App hii ina nyenzo kadhaa za kuhariri na kunoresha selfie yako. Na kikubwa zaidi, Instagram ndio kama 'makao makuu' ya selfies, kwa maana ya kuwa ni app maalum kwa ajili ya picha za aina hiyo.


frontback android

Uzuri wa app hii ni uwezo wake mkubwa wa kupiga picha ya 'mhusika na mazingira yake.' Yaani selfie yako sio tu itakuonyesha wewe mhusika bali pia hata mazingira yanayokuzunguka, ambapo inatumia kamera zote mbili za simu: ya mbele na ya nyuma- kwa wakati mmoja.


retrica android

Kuna msemo wa kiswahili usemao 'ya kale ni dhahabu,' na hapo ndipo ulipo unora wa app hii.Retrica yakuwezesha kupiga picha inayoonekana kama ya 'mwaka 47,' yaani mwonekano wa kizamani. Lakini umahiri zaidi wa app hii upo katika kuifanyia uhariri picha yako. Wakati mara nyingi apps za picha hukuwezesha kuhariri picha mara baada ya kupiga picha halisi, kwa Retrica zoezi hilo linafanyika 'laivu' kwa maana kwamba unaweza kuihariri picha yako kabla hujaisevu au kuiposti mtandaoni. Japo hii ni faida, yaweza pia kuwa hasara kwa maana pindi ukishapiga selfie yako, huwezi kuihariri kwa ufanisi.


line android

Hii ni moja ya apps maarufu kabisa kwa picha kwa simu za Android. Umahiri wa Line Camera unachangiwa na ukweli kwamba unaweza ku-download nyenzo lukuki na za aina tofauti (za bure au za kununua) pindi unapohitaji ladha ya ziada ya zinazopatikana kwenye app yenyewe.

candy camera

Kama jina lenyewe 'candy' linavyoashiria 'utamu,', ndivyo ulivyo ubora wa app hii ambayo inatumia zaidi mwelekeo wa vidole vyako kwenye picha/screen yaani 'gestures' kwa kimombo.Waweza 'kuisukuma' (swipe) picha yako kulia au kushoto kufanya uchaguzi sahihi wa taswira unayotaka, au kusukuma juu au chini kwa ajili ya kupata nyenzo mbalimbali za kuhariri picha yako. Kadhalika, Candy Camera inakuwezesha kuhariri selfie yako 'laivu' lakini tofauti na Retrica, yenyewe yakuwezesha kuhariri selfie yako hata baada ya 'kuifotoa' au kuisevu.


smart selfie android 

Tofauti na apps nyingine za selfie, Smart Selfie inatumia kamera ya nyuma ya simu yako. Kwahiyo badala ya kuchukua selfie wakati kamera ya mbele inakuangalia, katika app hii yakulazimu kuigeuza simu yako na kuchukua selfie kwa kutumia kamera ya nyuma. App hii ni nzuri zaidi kama unataka kuchukua selfie ya watu wengine, kwa maana unawafotoa kama ambavyo unapiga 'picha ya kawaida' kisha unachagua iwapo unataka simu iwe 'imesimama' (potrait)au 'imelala' (landscape), kisha unaishika vizuri simu yako, na app hiyo itakupa maelekezo kwa sauti ili kupata selfie mwafaka, kwa mfano kukueleza 'sogea karibu' au 'sogea kulia.'

Ofkoz, kuna apps nyingine lukuki ambazo ni maalum kwa ajili ya selfies lakini hizi 6 zinaelezwa kuwa ni bora kabisa. Kazi kweny wapenda selfies.

Usikose kutembelea blogu hii kwa ajili ya habari mbalimbali za teknolojia na nyinginezo. Waweza kupata kirahisi habari za Teknolojia kwa kubonyeza section ya TEKNOLOJIA hapo juu ya blogu.


30 Jul 2014

signalapp
Mie ni miongoni mwa waumini wakubwa wa filosofia ya 'ishu binafsi shurti zibaki kuwa za binafsi' (private things should always remain private). Na ninaposema 'ishu binafsi' ninamaanisha pia masuala nyeti yasiyopaswa kusikizwa na yeyote yule asiyehusika nayo. Siwezi kufafanua zaidi ila naamini kwamba kuna nyakati tunakuwa na masuala yanayopaswa kufahamika kwa wahusika tu.

Sasa iwapo unatumia iPhone,kuna app moja inaweza kuwa na manufaa makubwa kwako pindi ukijikuta katika mazingira ambapo unataka kuwasiliana na mtu pasi maongezi hayo 'kunaswa' na watu wengine. Labda kama hadi hapa hujanielewa vizuri, ni vema ukafahamu kuwa taarifa za hivi karibuni kutoka kampuni ya simu za mkononi ya Vodafone inaonyesha kuwa Tanzania ni moja ya nchi inayoshika nafasi za juu duniani kwa mashushushu wake kunasa mawasiliano binafsi ya simu za wananchi.

App husika inaitwa SIGNAL, na inapatikana bure kwenye App Store.

Kwa kutumia teknolojia inayoruhusu wahusika tu wa ujumbe husika kuupata ukiwa kamilifu (encryption), app hiyo ya Signal inayafanya maongezi katika iPhone kuwa ya faragha kiasi kwamba mtu asiyehusika hawezi kuyanasa.

Jinsi ya kui-set up App hiyo ni rahisi kabisa, na unahitaji kuingiza namba yako ya simu tu na kuithibitisha kwa kuingiza tarakimu 6 (6-digit code), ambazo zitatumwa kwako kwa SMS au simu, na utakuwa tayari kuitumia app hiyo. Namba za simu ulizohifadhi katika simu yako zitahamia kwenye app hiyo mara moja, lakini zitakazoonekana ni zile tu ambazo mtumiaji naye anatumia app hiyo. Ukimpigia simu mtu asiyetumia app hiyo,atatumiwa ujumbe wa ku-install app hiyo kwenye simu yake.

Unapopiga simu kwa kutumia app hiyo kwa mtu ambaye simu yake nayo ina app hiyo, faragha ya mawasiliano yenu inahakikiwa kwa kutumia maneno yanayoonekana katika screen ya simu ya anayepiga na anayepigiwa.Kisha mnafananisha maneno hayo kuhakikisha kuwa yanalingana, na yakilingana basi mawasiliano yenu yanakuwa ya siri. Yasipolingana basi inamaanisha kuna mtu anaingilia (anasikiliza) maongezi yenu.

Wakati kwa sasa app hiyo inaweza tu kuyafanya maongezi ya simu kuwa ya siri, kampuni iliyotengeneza app hiyo imeeleza kuwa ipo mbino kuwezesha hata mawasiliano ya SMS nayo kuwa ya siri.

29 Jul 2014

Wishing all my Musli brothers and sisters Eid Mubarak!


An armed pro-Russia militant stands guard at the MH17 crash site.
Katika jitihada za kubaini chanzo-nani na kitu gani-cha kudunguliwa ndege ya Shirika la Ndege la Malaysia MH17,kundi la waandishi wa habari wa kijamii (citizen journalism) wakitumia mtandao wa intanet na hisia zao tu wamekuwa wakikusanya habari pengine zaidi ya mashushushu wa Kimarekani.

Jumanne iliyopita, maafisa usalama wa Marekani walikiri kwamba japo ni kweli kwamba Russia imekuwa ikiwasaidia waasi wanaoiunga mkono, huko Ukraine, kwa miezi kadhaa, hakuna uthibitisho wowote kuonyesha kuwa kifaru cha kurusha makombora ya kutoka ardhini kwenda angani (surface -to-air missile) aina ya Buk SA-11, ambacho Marekani inadai ndio kilitungua ndege hiyo, kilikuwa cha Russia. Hata hivyo, waasi hao wa Ukraine walijigamba awali kuwa wana makombora ya aina hiyo.

Msemaji wa serikali ya Marekani alikiri kwamba kuna uhaba mkubwa wa maelezo kuhusu silaha iliyotumika kudungua ndege hiyo, na kuthibitisha kuwa ni vigumu kuja na ushahidi mpya wa kuthibitisha uhusika wa Russia katika tukio hilo.

Lakini kundi la waandishi wa habari wa kijamii likiongozwa na Ellliot Higgins, anayefahamika zaidi kwa jina lake la mtandaoni kama "Brown Moses," ameonyesha ushahidi mwingi kuhusiana na tukio hilo. Kwa msaada wa wafuasi wake (followers) katika mtandao wa kijamii wa Twitter, ameweza kuonyesha sehemu kilipokuwa kifaru cha kurusha makombora (launcher) ya Buk wakati kinasafirishwa katika eneo la Snizhne, lililopo chini ya milki ya waasi wanaoungwa mkono na Russia, kulingana na video inayosambaa kwenye mtandao wa video wa Yout Tube

Siku iliyofuata, Aric Toler, mfuasi wa muda mrefu wa Higgins, alionyesha eneo sahihi la kifaru cha kurushia makombora ya Buk katika mji uliopo Mashariki kwa Ukraine wa Torez, akitumia taarifa alizozikusanya kwa vyanzo vya wazi (open source information) na video nyingine za YouTube zilizorekodiwa eneo hilo.

Toler na Higgins waliweza kuthibitisha kuwa picha hiyo ilipigwa saa 5.40 asubuhi, kwa kutumia nyenzo ya mtandaoni iitwayo Suncalc, ambayo inawezesha kukokotoa nafasi (position) ya jua kwa kuzingatia muda na sehemu husika. Hiyo iliwawezesha kuthibitisha kuwa kifaru hicho kilikuwa eneo ilipodunguliwa ndege ya MH17.

Uchambuzi mwingine wa kutumia watu wengi (crowdsourced analysis) ambao Higgins aliukusanya Jumanne iliyopita unatoa ushahidi mkubwa kuhusu video iliyotolewa hadharani na serikali ya Ukraine ikionyesha kifaru husika kikihamishwa kutoka eneo linaloshikiliwa na waasi kuelekea Russia. Katika video husika, mtambo wa kurushia makombora (launcher) hauonekani 

Serikali ya Russia ilikanusha usahihi wa video hiyo, ikidai kwamba ilirekodiwa katika mji wa Krasnoarmeisk, ambao upo chini ya himaya ya majeshi ya Ukraine. Hata hivyo, shukrani kwa uchambuzi wa habari kwa kutumia vyanzo vya wazi, ilikuja kufahamika kuwa mji huo wala sio uliotajwa bali mwingine ulio chini ya himaya  ya waasi wanaoungwa mkono na Ruassia wa Luhansk, kilomita 30 kutoka mpaka wa Russia na Ukraine.

"Russia imeongopa," aliandika Higgins katika tovuti yake ya Bellingcat, anayoitumia kuhamasisha kazi za waandishi wengine wa wa kijamii wanaoandika habari za uchunguzi na kufundiha kuhusu nyenzo mbalimbali kwa ajili ya kazi hiyo. 

Matokeo ya uchunguzi huo hayathibitishi kwa hakika uhusika wa Russia katika kuidungua ndege hiyo ya Malaysia, kama anavyokiri Higgins mwenyewe, lakini yanathibitisha kuwa waasi wanaoungwa mkono na Russia wanamiliki kifaru cha kurushia makombora ya Buk,.na kilikuwa karibu na eneo ilipodunguliwa ndege hiyo.

Kwa Higgins, kazi yao ni sawa na ushushushu lakini kwa kutumia njia rahisi,na unaweza kuwasaidia wachunguzi wa ajali hiyo. Baada ya yeye na mwenzie Toler kuonyesha eneo na muda picha ya kifaru hicho lipopigwa, waandishi wa habari walikwenda huko na kukutana na mashuhuda waliothibitisha maelezo ya Higgins na mwenzake.

Uchunguzi wa aina hii ni mfano mzuri wa anachotaka kufanya Higgins kupitia tovuti yake ya Bellingcat: kujenga jamii ya waandishi wa kijamii mtandaoni wanaojuhusisha na uchunguzi ambao waweza kuibua ukweli mbalimbali. Higgins amekuwa akifanya hivyo kwa miaka kadhaa, akibandika mtandaoni video mbalimbali kutoka Syria ili kbainisha zipi ni za kweli au la.

Yeye alikuwa mmoja wa waangalizi huru wa mwanzo kuthibitisha kuwa utawala wa Rais Bashir al-Assad wa Syria ulitumia silaha za sumu katika kitongoji cha Ghouta Agosti mwaka jana,a aliibua biashara ya kuingiza silaha nchini humo, akiwa nyumbani kwake, Leicester, Uingereza.  Sasa anataka kuwaunga mkono watu wengine wanaofanya kazi kama yake na kuwafundisha jinsi ya kupata ujuzi husika.

"Ni muhimu kufahamu kuwa uchunguzi huu ulifanywa na na watu wa aina mbalimbali, na hiyo inaonyesha umuhimu wa kufanya nyenzo na mbinu za kukusanya habari kwa vyanzo vya wazi kuwa za wazi kwa yeyeote yule."

Chanzo: Imetafsiriwa kutoka mtandao wa WAtoday.com.au



28 Jul 2014

Vurugu bungeni (picha haihusiani na habari hii)
Dar/Dodoma. Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanadaiwa kupigana huko Malaysia baada ya kukutana hotelini, wakati wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), walipokuwa katika ziara ya kikazi nchini humo.
Tukio hilo lilitokea siku nne zilizopita baada ya mbunge wa kamati hiyo kutoka CCM kuvamiwa alipokuwa akipata kifungua kinywa kwenye hoteli aliyofikia na wenzake wawili mmoja wa CCM na mwingine wa Chadema. Majina ya wabunge hao watatu tunayahifadhi kwa sasa kwa sababu hatukuwapata kujibu tuhuma hizo.
Hata hivyo, mbunge wa Chadema ambaye siyo mjumbe wa PAC haikufahamika ilikuwaje akawamo katika ziara hiyo.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zinadai kuwa chanzo cha ugomvi huo masuala ya uhusiano na kwamba mbunge aliyevamiwa alipigwa vibaya.
Chanzo cha mbunge huyo kupigwa kinaelezwa kuwa ni hatua yake ya kuweka ujumbe kwenye mtandao wa WhatsApp unaowaunganisha baadhi ya wabunge, akiwasuta wenzake hao wawili kwamba wamekuwa wakichochea kuvunjika kwa uhusiano wake na mbunge mwenzake.
Ujumbe huo unadaiwa kuambatana na uliotumwa na wabunge hao wawili kwa binti mmoja anayefanya kazi katika benki moja mjini Dodoma ambaye pia anatajwa kuwa na uhusiano na mbunge huyo mwanamume, wakimtaka asiachane naye kwa maelezo kwamba mwenzao huyo atatamba.
Binti huyo alikuwa ametuma ujumbe kwenye mtandao wa pamoja na wabunge hao wawili akieleza kwamba ameamua kuvunja uhusiano wake na mbunge (mwanamume) kwa maelezo kwamba asingependa kuingia kwenye mvutano wa kimapenzi.
Baada ya kutuma ujumbe huo wabunge hao wawili (wanaotuhumiwa kumshambulia mwenzao), wanadaiwa kumjibu wakimsisitiza kuendelea na uhusiano huo mawasiliano ambayo yalikuja kunaswa na mbunge aliyeshambuliwa.
Inaelezwa kwamba baada ya kunasa mawasiliano hayo, mbunge huyo alichukua ujumbe wa wabunge hao kama ulivyo na kuuweka kwenye mtandao unaowaunganisha wabunge wengi akiwasuta kwamba ni wanafiki na kwamba wamekuwa wakihaha usiku na mchana kuhakikisha ‘ndoa’ yake inavunjika.
Kutokana na kuumbuliwa huko, wabunge hao walimvamia mwenzao hotelini na kumpiga mbele ya wenzake. Gazeti hili lilimpigia simu mbunge anayedaiwa kumpiga mwenzake kwa kiasi kikubwa na baada ya kuelezwa tukio zima na kabla ya ufafanuzi, alikata simu bila kujibu chochote.
Kiongozi wa msafara huo Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe ambaye pia ni Mbunge wa Ludewa (CCM), alipopigiwa simu na mwandishi wetu hata kabla ya kuulizwa kuhusu ugomvi huo alisema: “Hakuna kilichotokea. Mimi ni mwandishi wa habari kama wewe, hakuna kilichotokea na hakukuwa na ugomvi wowote.”
Alisema katika siku za hivi karibuni kumeibuka mtindo wa wabunge kusingiziwa kuwa wamefanya jambo fulani, huku akisisitiza kuwa kama kulizuka ugomvi asingeweza kuficha chochote.
“Sina sababu ya kuficha jambo lolote kama lingekuwa limetokea kweli. Kuhusu ziara yetu nitakueleza baadaye au kesho (leo) maana sasa hivi ndiyo ninashuka katika ndege hapa uwanjani,” alisema Filikunjombe.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alisema kuwa hajui chochote na kuahidi kufuatilia jambo hilo... “Tulikuwa Arusha katika kikao. Jambo hilo ndiyo kwanza nalisikia kutoka kwako, ngoja tufuatilie na kesho (leo) tunaweza kutoa ufafanuzi kama ni kweli jambo hilo limetokea.”
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alipulizwa alisema: “Nimekuelewa, ngoja nimtafute Katibu ambaye alikuwa na huo msafara (wa kamati) ili nimuulize kujua ukweli.”

Mbunge anayedaiwa kupigwa hakupatikana jana huku moja ya namba anazotumia ambayo imeandikwa katika kitabu cha orodha za wabunge ikipokelewa na mwanamume ambaye alisema siyo ya mbunge huyo.
CHANZO: Mwananchi

Rais Jakaya Kikwete akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Rashid Othman 
Wakati idadi kubwa ya Watanzania inapinga vikali taasisi za intelijensia kuwafanyia ushushushu viongozi wa siasa na raia wa kawaida, Tanzania inashika nafasi ya pili duniani-nyuma ya Italia-kwa kudaka mawasiliano ya wananchi wake kwa siri.

Asilimia 71 ya Watanzania waliohojiwa katika utafiti uliofanywa na taasisi ya Pew Research Centre ya Marekani walipinga vitendo vya serikali kuingilia mawasiliano ya simu na email ya viongozi wa kisiasa. Asilimia 25 waliafiki vitendo hivyo.

Utafiti huo ulionyesha kuwa Watanzania wanaongoza barani Afrika katika upinzani wao dhidi ya uvamizi wa faragha yao unaofanywa na taasisi za intelijensia.

Hata hivyo vitendo vya kishushushu kufanya ufuatiliaji kwa kuingilia au kunasa mawasiliano vimeshamiri mno nchini Tanzania kiasi kwamba nchi hiyo inashika nafasi ya pili duniani nyuma ya Italia katika vitendo hivyo.

Mwezi uliopita, kampuni ya kimataifa ya simu za mkononi ya Vodafone, ilitoa taarifa inayoonyesha kuwa kampuni yake tanzu ya Vodacom Tanzania ilitoa mawasiliano 98,765 ya wateja wake kwa mashushushu.

Katika ripoti hiyo, Tanzania inatajwa kuwa ni nchi ya pili duniani - katika nchi 29 ambapo Vodafone inatoa huduma - nyuma ya Italia kwa kufuatilia, kuingilia au kunasa mawasiliano ya simu. Italia inashika nafasi ya kwanza kwa mawasiliano 605,601 yaliyoombwa na taasisi za usalama.

Vodafone ilibainisha uwepo wa nyenzo za siri zinazowawezesha mashushushu kusikiliza mawasiliano ya wateja wa kampuni hiyo.

Kampuni hiyo imevunja ukimya kuhusu vitendo vya serikali kuwafuatilia raia wake kwa ushushushu katika mitandao ya simu na intaneti.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Tanzania, utafiti huo umeonyesha kuwa asilimia 49 ya Wakenya wanaafiki mashushushu kunasa mawasiliano ya simu na email ilhali asilimia 44 hawaafiki.

Utafiti huo unaonyesha kuwa Kenya inaongoza miongoni mwa nchi za Afrika kuhusu ridhaa kwa serikali/mashushushu kuwapeleleza raia.

Chanzo: imetafsiriwa kutoka gazeti la The Citizen (Tanzania)



Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.