20 May 2015





Fanya kusapoti kazi hii ya sanaa yenye ujumbe muhimu kwa mustakabali wa taifa letu kwa kununua wimbo huu kwa bei nafuu katika tovuti ya MDUNDO http://mdundo.com/a/2788 

8 May 2015

Jana Uingereza ilipiga kura katika Uchaguzi wake Mkuu, na matokeo yalianza kupatikana jana usiku muda sio mrefu baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa majira ya saa nne usiku.

Hadi muda huu, chama cha Conservatives kinazidi kufanya vizuri, na hadi muda huu ninapoandika makala yhii, wameshajikusanyia viti 250, chama cha Labour kina viti 212 na Liberal Democrats viti 6. Chama cha kibaguzi cha UKIP kimepata kiti kimoja tu hadi muda huu, na ubashiri unaonyesha kitapata viti viwili tu, huku kiongozi wake Nigel Farage akiwa katika hatihati ya kushindwa.

CChama tawala hapa Uskochi, Scottish National Party (SNP) kimepata mafaniuko makubwa mno, ambapo katika viti 59 kimeshapata viti 55 na kimepoteza kiti kimoja tu.

Kuna kila dalili kuwa Waziri Mkuu David Cameron ataendelea kuwa Waziri Mkuu lakini ni mapema mno kufahamu iwapo ataunda serikali kwa kushirikiana na chama gani. Kuhusu kiongozi wa Labour, Ed Miliband, tayari kuna tetesi kuwa huenda akalazimika kujiuzulu kabla ya mwisho wa siku hii ya leo baada ya chama chake kufanya vibaya. Kuhusu chama cha Liberal Democrast, huenda kiongozi wake, Naibu Waziri Mkuu, Nick Clegg, nae akalazimika kujiuzulu kufuatia matokeo mabaya mno kwa chama hicho. 

Matokeo kamili yatafahamika hapo baadaye. 

Kwa coverage ya usiku mzima kuhusu uchaguzi huo, tembelea ukurasa wangu wa Twitter hapa @chahali

7 May 2015

Leo hapa Uingereza tunafanya uchaguzi Mkuu kuchagua chama kitachotuongoza miaka mitano ijayo.Kwa kifupi, tofauti na huko nyumbani, katika uchaguzi mkuu huu wa leo tunawapigia kura wabunge.Hapa hatuna Rais, Mkuu wa nchi ni Malkia japo mkuu wa serikali ni Waziri Mkuu anayetokana na chama kitakachoshinda viti vingi vya ubunge.
Viongozi wa vyama vikuu vinavyoshirikia uchaguzi mkuu unaofanyika leo: Kutoka kushoto kwenda kulia: Natalie Bennett wa Green Party, Nick Glegg wa Liberal Democrats, Nigel Farage wa UKIP, Ed Miliband wa Labour, Leanne Wood  wa Plaid Cymru (Wales), Nicola Sturgeon (Scottish Nationalist Party-Scotland) na David Cameron (Conservatives na Waziri Mkuu wa sasa)

Hata hivyo, mchuano ni mkali sana na hadi muda huu ni dhahiri kuwa hakuna chama kitakachopata viti vya kutosha kuunda serikali peke yake bila kushirikiana na chama kingine. Sasa iwapo hali itakuwa hivyo katika matokeo - ni vigumu kubashiri kwa uhakika kuwa hakuna uwezekano wa chama kimoja kuibuka na ushindi wa kukitosheleza kuunda serikali peke yake, kwa sababu lolote laweza kutokea katika masaa machache yajayo kabla ya kuanza kwa uchaguzi na likabadili mwelekeo.

Serikali inayomaliza muda wake inaundwa na chama cha Conservatives ambacho ndicho cha Waziri Mkuu wa sasa David Cameron, kwa kushirikiana na chama cha Liberal Democrats ambacho ndio cha Naibu Waziri Mkuu Nick Clegg. 

Ili chama kiweze kuunda serikali peke yake bila kuhitaji ushirikiano na chama kingine, kinahitajika kushinda viti 326.Iwapo hakuna chama kitachofikia idadi hiyo ya vitu, kunapatikana kitu kinachoitwa 'hung parliament' kama ilivyotokea katika uchaguzi mkuu uliopita (mwaka 2010) ambapo Conservatives walipata viti 307,Labour 258 na Liberal Democrats 57, na kwa vile hakuna aliyefikia idadi ya viti 326, Conservative na Liberal Democrats wakakubaliana kuunda serikali ya ushirikiano.

Nimeandika swali hapo juu, nani kuibuka mshindi? Well, njia kuu inayotumika katika chaguzi kubashiri ushindi wa chama kama uchaguzi ni kura za maoni (opinion polls).Kwahiyo, ili kupata mwangaza wa nani anaweza kupata nini, hapa chini ninaorodhesha matokeo ya kura za maoni kutoka makampuni mbalimbali yanayojihusisha na shughuli hiyo:








Utabiri wa matokeo na uwezekano wa ushirikiano wa vyma kuunda serikali ya pamoja




Embedded image permalink
Embedded image permalink






30 Apr 2015



“KAKA, kinachotokea hapa kilitarajiwa...na ilikuwa suala la ‘when’ na sio if”, hii ni kauli ya rafiki yangu mmoja Mwafrika Kusini baada ya kumuuliza kuhusu vurugu dhidi ya wahamiaji katika nchi hiyo ambazo zimesababisha vifo, majeruhi, wahamiaji kuhifadhiwa katika kambi kama wakimbizi na wengine kadhaa kuondoka nchini humo.
Ni suala la kusikitisha sana kuona taifa lililoweka historia duniani kwa kukabiliana na makaburu na mfumo wao wa ubaguzi wa rangi (Apartheid) na hatimaye kuushinda, linageuka kuwa taifa hatari dhidi ya wahamiaji kutoka nchi nyingine za Afrika.
Lakini kama alivyotanabaisha rafiki yangu niliyemnukuu hapo mwanzoni, matarajio makubwa waliyokuwa nayo Waafrika weusi nchini Afrika Kusini baada ya kumalizika kwa mfumo wa kibaguzi wa makaburu yameendelea kuwa ndoto tu kwa wengi wao. Uzoefu unaonyesha kuwa katika jamii yoyote ile kwa kadiri inavyokabiliwa na matarajio makubwa ambayo ni magumu kufikiwa, moja ya waathirika wa hali hiyo ni wahamiaji.
Pengine mfano mzuri ni huku nchi za Magharibi ambapo baada ya kuyumba kwa uchumi wa dunia, hali ya maisha imekuwa ngumu, na kauli za upinzani dhidi ya wahamiaji- kutoka kwa wanasiasa na hata raia wa kawaida- zimesambaa.
Kwa hapa Uingereza ambapo tunatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu Mei 7, mwaka huu, moja ya mada kubwa kwa wanasiasa imekuwa suala la uhamiaji. Wanasiasa wanalazimika aidha kukabiliana na wanasiasa wenzao wanaolaumu kuwa wahamiaji wanachangia hali mbaya ya uchumi au kuonekana wanajali vilio vya wananchi wenye malalamiko ya aina hiyo.
Ni kwa sababu hiyo, chama cha kibaguzi cha UKIP kinachoongozwa na Nigel Farage kimetokea kujipatia umaarufu mkubwa hasa kwa vile kinabainisha waziwazi ‘chuki’ yake dhidi ya wahamiaji. Huko Ufaransa, chama cha kibaguzi cha National Front nacho kimekuwa maarufu kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya wahamiaji. Hali ipo hivyo pia nchini Italia na Udachi, huku Ujerumani ikishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya wahamiaji. Kimsingi, katika nchi nyingi za Magharibi, kuyumba kwa uchumi wa dunia kumeambatana na kuimarika kwa vyama vya mrengo mkali wa kulia (far right) ambavyo kimsingi ni vya kibaguzi na vinapinga vikali wahamiaji. Vile vile, sauti za wananchi wa kawaida kuzitaka serikali zao kudhibiti ujio wa wahamiaji zimekuwa zikiimarika na kuongezeka.
Tukirejea kinachojiri Afrika Kusini, ni rahisi kuwashutumu wenzetu hao kwa vitendo vya ubaguzi dhidi ya wahamiaji hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya waathirika wa vurugu dhidi ya wahamiaji ni raia wa nchi zilizoisaidia Afrika Kusini kwa kiwango kikubwa katika mapambano dhidi ya mfumo wa kibaguzi wa Makaburu. Ni rahisi pia kuwalaumu kwa sababu hata kama ingekuwa kweli kuwa wahamiaji wanasababisha ukosefu wa ajira kwa ‘wazawa’ bado haikubaliki kuwafanyia vurugu, kuwajeruhi na hata kuwauwa. Hilo halikubaliki hata chembe.
Hata hivyo, busara kidogo tu zapaswa kutukumbusha kuwa ni vigumu ‘kuingiza akili’ kichwani mwa mtu mwenye njaa (masikini). Tumbo lina tabia moja: mara nyingi, linapohitaji chakula halina subira, au busara. Linachohitaji ni chakula tu, na mara nyingi halijali chakula hicho kinapatikana kwa njia zinazokubalika au la. Ushuhuda wa hili ni katika msimu wa uchaguzi huko nyumbani ambapo mara kadhaa tunashuhudia watu wazima na akili zao wakifungiwa sehemu au kusafirishwa kama magunia kutoka sehemu moja au nyingine ili ‘kulinda kura za mgombea’ kama si kumhakikishia ushindi. Wanaodhalilishwa hawafanyi hivyo kwa mahaba ya kisiasa bali njaa zao.
Mie ni miongoni mwa waumini wa kanuni isiyo rasmi kuhusu uhusiano kati ya umasikini na fursa za uongozi wa kisiasa. Kwamba, watawala hawafanyi bidii kukabiliana vya kutosha na umasikini kwa sababu umasikini unawapa fursa ya kuwahadaa wapiga kura na hatimaye kuwanunua kwa urahisi. Umasikini wa wapigakura ni mtaji mzuri kwa wanasiasa wenye fedha za kununua kura.
Ni vigumu kumkumbusha mpiga kura kuwa ‘ah huyu mbunge alitoa ahadi kadhaa katika uchaguzi uliopita lakini wala hatujamsikia akisema lolote huko bungeni. Hatujawahi japo kuona picha zake akiwa bungeni,’ pale mwanasiasa husika ana rundo la fedha za kutuliza njaa za wapigakura.
Doti za khanga, pishi za mchele, kilo za sukari na ‘takrima’ kama hizo humlainisha mpigakura mwenye njaa asahau kabisa kuhusu miaka mitano ijayo ya utapeli wa kisiasa kama ilivyotokea miaka mitano iliyopita. Njaa yahitaji mlo, hayo madhara yatajulikana mbele ya safari. “Kwani akiwa mbunge tena nitakufa?” Wanajipa moyo wapigakura wenye njaa wanaosubiri kwa hamu ‘fadhila’ za mgombea.
Kwa Afrika Kusini, sababu kubwa ya chuki dhidi ya wahamiaji ni matatizo mbalimbali yanayowakabili Weusi nchini humo ambayo yanakinzana na matarajio makubwa waliyonayo kutoka kwa utawala wa ‘Waafrika wenzao’ baada ya ‘kuwapora madaraka’ makaburu.
Lakini kibaya zaidi, ni mchanyato wa umasikini, ukosefu wa elimu na ‘dozi’ ya uchochezi. Moja ya vichocheo vya vurugu dhidi ya wahamiaji nchini humo ni kauli iliyotolewa na Chifu wa Wazulu, Goodwill Zwelithini, dhidi ya kufurika kwa wahamiaji nchini humo. Kana kwamba hiyo haitoshi, mtoto wa Rais Jacob Zuma, Edward, amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wahamiaji wafukuzwe nchini humo akidai wanachangia uhalifu na hali ngumu ya uchumi. Kadhalika, wanasiasa kadhaa Weusi pia wamekuwa wakitoa kauli za kuchochea chuki dhidi ya wahamiaji.

Chambuzi mbalimbali zilizofanyika kabla na baada ya vurugu hizo dhidi ya wahamiaji zimeonyesha kuwa sio tu idadi ya wahamiaji ni ndogo mno kuathiri uchumi wa Afrika Kusini bali pia kinachofanya soko la ajira nchini humo kuvutia na kuvuta wafanyakazi kutoka nchi nyingine ni ukweli kuwa ‘ni rahisi kwa mzawa kuishi bila kazi kwa vile anapatiwa msaada na serikali’ ilhali kwa mhamiaji ni lazima afanye kazi au biashara ili aweze kumudu gharama za maisha.
Lakini pia, huko nyuma, Rais Jacob Zuma aliwahi kunukuliwa akiwalaumu Waafrika Kusini weusi kwa ‘uvivu,’ kutegemea serikali iwapatie kila kitu badala ya kujishughulisha wenyewe. Sasa kwa vile takribani katika kila nchi inayomudu kuwasaidia raia wake wasio na kazi, msaada wa serikali huwa ni wa kujikimu tu, haishangazi kuona ‘wazawa’ wakiwachukia wahamiaji wanaojituma kwa biashara na ajira na kujipatia kipato cha zaidi ya kujikimu tu
Kwa mtazamo mpana, na hili ni funzo kwa nchi nyingine za Afrika ikiwa pamoja na Tanzania yetu, ni ukweli kwamba umasikini ni bomu linalosubiri muda wa kulipuka. Kwa nchi yetu, hali si nzuri. Sio tu kwamba umasikini unazidi kushamiri na kuongezeka, vitendo vya ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya watawala wetu vinakuwa kama ‘kuchoma kisu kwenye jeraha bichi.’ Haiingii akilini kwa mlalahoi ambaye hana uhakika wa mlo ujao kusikia viongozi fulani wamekwapua mabilioni ya shilingi huko Benki Kuu.
Na wakati faraja ya masikini inaweza kupatikana katika neno la Mungu, mtu fukara anaposikia habari kuwa Askofu wake kuzawadiwa mamilioni ya ufisadi, anaweza kushawishika kutumia vibaya msemo wa ‘mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe,’ hasa ikizingatiwa kuwa nguvu anazotumia shambani zinaishia kunenepesha kitambi cha viongozi wa vyama vya ushirika na kuongeza idadi ya ‘nyumba ndogo’ zao. Kwanini asishawishike kuzitumia nguvu hizo kwenye uhalifu?
Tofauti na Afrika Kusini ambapo ‘adui’ anaonekana mhamiaji ‘anayepora ajira za wazawa,’ adui wa fukara wa Tanzania ni Mtanzania mwenzie anayetumia madaraka yake kufanya ufisadi, na hivyo kuongeza ufukara kwa mlalahoi huyo.
Tunaweza kujidanganya kuwa ‘Tanzania ni kisiwa cha amani’ lakini tusisahau kuwa ‘mwenye njaa hana amani.’ Amani yetu ni ya kufikirika zaidi kuliko uhalisia. Amani si ukosefu wa mapigano tu bali pia kuridhika nafsini, tumbo lililoshiba, mfuko wenye hela ya matumizi, jitihada za kujipatia kipato halali zinapozaa matokeo tarajiwa. Kimsingi, ukosefu wa amani usioambatana na vurugu ni kichocheo kikubwa cha vurugu zinazopelekea kuvunja amani waziwazi. Na hicho ndicho kinachojiri nchini Afrika Kusini. Sio sahihi lakini nenda kamwambie mwenye njaa kuhusu ‘wewe kuwa na njaa ilhali mie ninakula hadi kusaza ni kitu sahihi’ kama atakuelewa. Wanasema ‘njaa haina akili,’ na mwenye njaa yupo tayari kwa lolote ili kutuliza njaa yake.
Nimalizie makala hii kwa kutoa rai kwa wanasiasa wetu, hasa wakati huu tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, kuweka kipaumbele katika kupambana na umasikini sambamba na kukabiliana na ufisadi ambao kwa kiasi kikubwa unachangia mno kushamiri na kukua kwa umasikini.
TUZIPOZIBA UFA TUTAJENGA UKUTA

29 Apr 2015

Inasikitisha, inaumiza, inashangaza, na inaacha maswali mengi kuliko majibu kila tunaposikia “ajali yauwa...ajali yajeruhi...” Ndio, matukio ya ajali huko nyumbani yamekuwa kama jambo la kawaida kutokana na mfululizo wake, lakini hali ilivyo sasa ni ya kutisha.
Huko nyuma niliandika takriban makala mbili kuhusu suala hili la ajali, sio tu kwa vile tukio lolote linalopelekea kupotea kwa uhai wa wenzetu linaumiza nafsi bali pia kutokana na ukweli kwamba kwa hapa Uingereza ajali ndogo tu ni tukio linalokamata hisia za takriban nchi nzima, kinyume na ilivyozoeleka huko nyumbani.

Wakati ajali zinaendelea kuteketeza maisha ya Watanzania wenzetu, angalau kwa mara ya kwanza Taifa linaonekana kuguswa, na tayari zimeanza harakati za uhamasishaji dhidi ya ajali katika mitandao mbalimbali ya kijamii. Hata hivyo, ukweli mchungu unabaki kuwa ajali bado zinaonekana kama matukio ya kawaida tu.
Sijui lini taifa limeonyesha kuguswa na vifo vilivyotokana na ajali kiasi cha angalau bendera kupepea nusu mlingoti. Sijui sababu ni kwamba ajali zimezoeleka mno, au kwa vile ‘ajali haina kinga,’ au kwa sababu wahanga wengi wa ajali za barabarani ni ‘watu wa kawaida.’
Kabla sijaanza kuandika makala hii nilisoma habari kuhusu vurugu zilizotokea huko Korea ya Kusini katika maadhimisho ya mwaka mmoja tangu itokee ajali mbaya ya feri iliyosababisha vifo takriban 300. Hakuna anayefahamu kinachojiri baada ya kifo, lakini yayumkinika kuamini kuwa marehemu wasingependa kukumbukwa kwa vurugu. Lakini vurugu zilizotokea huko Korea ya Kusini ni ishara ya wananchi kukerwa na jinsi serikali yao ilivyoshughulikia janga hilo, hata kama haikuisababisha.
Hapa simaanishi kwamba Watanzania nao waingie mtaani na kufanya vurugu kuisukuma serikali ichukue hatua stahili dhidi ya ajali. Hata hivyo, ni muhimu angalau kuiamsha serikali kwa kuifahamisha kuwa hatuwezi kuangalia tu maisha ya Watanzania yakiteketea kama hayana thamani kutokana na mfululizo wa ajali. Busara kwamba ‘ajali haina kinga’ hai-apply katika nyingi ya ajali zinazotokea huko nyumbani.
Kwa mtizamo wangu, chanzo kikubwa cha ajali ni rushwa. Rushwa inayowezesha madereva wasio na sifa kuwa barabarani huku wakihatarisha uhai wa abiria wao. Rushwa inayoruhusu magari mabovu yabebe abiria na kuweka rehani uhai wa abiria. Rushwa inayofumbia macho makosa ya madereva barabarani na hivyo kuwapa imani kuwa hakuna kitu kiitwacho ‘kosa kinyume cha sheria za usalama barabarani’ alimradi dereva ana uwezo wa ‘kumpoza’ askari wa usalama barabarani.
Wanasema ‘rushwa huuwa.’ Na katika janga hili la mfululizo wa ajali, rushwa inauwa kweli kweli, na inaendelea kugharimu maisha ya Watanzania wenzetu kila kukicha.
Rushwa imekuwa sehemu ya maisha ya kawaida ya Mtanzania, na sintoshangaa iwapo baadhi ya wasomaji ‘wataniona mtu wa ajabu’ kwa kuhitimisha kuwa rushwa ni chanzo kikuu cha ajali huko nyumbani. Kwa wengi, rushwa ni tukio la muda mfupi tu linalorahisisha au kuwezesha upatikanaji wa huduma au bidhaa. Hata hivyo, ukweli mchungu ni kwamba rushwa ni kama kansa, inaitafuna jamii taratibu, na siku ya siku, madhara yake makubwa hujitokeza hadharani.
Mfano mmoja kuhusu athari za rushwa ni suala la ugaidi nchini Kenya. Wachambuzi wa masuala ya usalama wanahitimisha kuwa kwa kiasi kikubwa tu, rushwa katika vyombo vya dola nchini Kenya imewarahisishia magaidi wa Al-Shabaab kutimiza malengo yao kuishambulia nchi hiyo.
Kwa huko nyumbani tumeshuhudia matatizo mengine ya kijamii yanavyorutubishwa na rushwa. Mfano rahisi ni kushamiri kwa biashara ya madawa ya kulevya. Tanzania yetu sasa ni miongoni mwa vituo vikuu vya biashara hiyo duniani, na kilichotufikisha katika nafasi hiyo isiyopendeza hata kidogo ni urahisi wa kuingiza na kutoa madawa ya kulevya nchini mwetu. Niwe mkweli, kila ninaposikia polisi wamekamata kiasi fulani cha madawa ya kulevya, hisia yangu ya kwanza ni madawa hayo yaliyokamatwa yataishia kumnufaisha mtendaji fulani wa taasisi zenye wajibu wa kuyadhibiti.
Takriban kila dereva na abiria anafahamu jinsi askari wa usalama barabarani walivyogeuza rushwa kuwa haki yao. Kibaya zaidi, madereva wengi nao wamejenga fikra kuwa kutoa rushwa kwa askari wa usalama barabarani ni wajibu wao. Hili ni janga: rushwa kama haki wa wapokeaji na wajibu kwa watoaji.
Wakati mmoja nikiwa safarini huko nyumbani, basi nililopanda lilisimamishwa na askari wa usalama barabarani, na baada ya dakika kadhaa, baadhi ya abiria walisikika wakimhasisha dereva ‘amalizane na trafiki’ (ampe rushwa) ili safari iendelee. Hivi ndivyo rushwa ilivyoota mizizi katika Tanzania yetu.
Kwa upande mwingine, janga la ajali kuonekana kama jambo la kawaida tu ni mwendelezo wa kasumba inayolikwamisha mno taifa letu: kuzowea matatizo. Angalia tatizo la mgao wa umeme lilivyodumu miaka nenda miaka rudi pasipo Watanzania kutumia nguvu ya umma kuilazimisha serikali na Tanesco yake imalize tatizo hilo. Mgao wa umeme umekuwa stahili ya Watanzania, na kikubwa wanachoweza kufanya ni kuitukana Tanesco matusi yasiyoandikika hapa, kana kwamba matusi hayo yatamaliza tatizo hilo la miaka nenda miaka rudi.
Kwenye sekta ya huduma, hali ni hivyohivyo. Ukifuatilia kwenye mitandao ya jamii, idadi ya matusi yanayoelekezwa kwa makampuni ya huduma mbalimbali, kwa mfano makampuni ya simu, ni kubwa na inakua kila siku, lakini ‘mashujaa hao wa matusi’ hawataki kabisa kujifunza kuwa matusi yao hayabadili chochote, na ndio maana kila kukicha inawalazimu waje na matusi mapya kama si kuyarudia yale ya zamani.
Lakini kwa hali ilivyo sasa kuhusu janga la ajali, ‘usugu’ huo wa kuyazowea matatizo inabidi ifikie kikomo. Taifa lolote linalojali mustakabali wake lazima liamke inapofikia hatua ya watu 969 kupoteza maisha kutokana na ajali katika kipindi cha takriban miezi mitatu tu. Naam, tangu mwaka huu uanze, tumepoteza wenzetu takriban 300 kila mwezi kutokana na ajali, kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana wiki iliyopita.
Katika sehemu kubwa ya makala hii nimezungumzia rushwa kama chanzo kikuu cha janga la ajali. Hata hivyo, kwa mtizamo wangu, kingine kinachochangia baadhi ya ajali ni ‘uzembe’ wa wengi wa abiria: kukaa kimya pale madereva wanapohatarisha maisha ya abiria kwa uendeshaji usiozingatia sheria za usalama barabarani. Na pengine cha kukera zaidi ni tabia iliyojengeka miongoni mwa abiria wengi kuwasifia madereva wanaodhani ni kosa la jinai kuendesha motokaa taratibu hata kwenye eneo hatari.
Inasikitisha na kuchukiza kusikia abiria wakimshangilia dereva anayeendesha basi kwa kasi au ku-overtake gari jingine pasi kuona kama kuna gari jingine linakuja kwa mbele au la. Dereva anayeshangiliwa kwa uendeshaji gari wa hatari anajenga imani kwamba huo ndio udereva stahili, vinginevyo abiria wangemkemea.
Ifike mahali Watanzania tuache kukubali kilicho pungufu (not settling for less). Ukinunua tiketi kwa ajili ya safari umenunua pia haki na stahili zako ambazo kamwe hupaswi kumruhusu dereva azichezee. Ni wazi kuwa umoja na mshikamano wa abiria kukemea madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani unaweza kusaidia kupunguza baadhi ya ajali zinazoepukika.
Nimalizie makala hii kwa kutoa salamu zangu za rambirambi kwa ndugu na jamaa wa Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali mfululizo.
Pia ninaomba kufikisha ujumbe huu kwa askari wa usalama barabarani: kila shilingi mnayodai kama rushwa ili kufumbia macho ukiukwaji wa sheria za barabarani inachangia ajali na vifo vya Watanzania wenzetu. Mikono ya kila askari aliyepokea rushwa na kisha gari husika likapata ajali ina damu ya waliokufa katika ajali husika.
Kadhalika, ninatoa wito kwa madereva, hususan wa magari ya abiria, kuthamini uhai wa abiria wao, kwa kuepusha ushindani hatari barabarani, mwendo kasi na kuheshimu sheria za usalama barabarani.
Lakini kubwa zaidi kwa Watanzania wote ni kupambana na kansa hii ya rushwa ambayo sasa inalitafuna taifa kwa kuchangia ajali hizi mfululizo, kama inavyosababisha madhara mengine makubwa katika nyanja mbalimbali za maisha.

ANGALIZO: Makala hii ilichapishwa katika toleo la tarehe 22.04.15 lakini iliwekwa mtandaoni juzi. Samahani kwa kuchelewesha kui-post.


26 Apr 2015

Embedded image permalink
Moja ya taarifa zilizozagaa kwenye vyombo mbalimbali vya habari ni kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi.Lakini shilingi au sarafu nyingine inashukaje thamani yake? Haya ni maswali ambayo ninaamini watu wengi wasio wachumi watakuwa wanajiuliza muda huu.

Nami pia ninajiuliza maswali hayo kama yalivyo kwenye kichwa cha habari.Ninajiuliza kwa sababu mie si mchumi, na jaribio langu pekee la kuingia fani ya uchumi lilikuwa wakati napata elimu ya sekondaria ambapo nilisoma Book Keeping hadi kidato cha nne na Commerce hadi kidato cha pili.

Naujua uchumi 'kijuu-juu' tu, na sana ni katika mahusiano yake na siasa au jamii, lakini kwa vile mie ni dhaifu sana wa hisabati, uchumi unaohusisha tarakimu ni 'no-go area.'

Kwahiyo, samahani msomaji mpendwa kama maswali hayo kwenye kichwa cha habari yalikupa hisia kwamba labda nitayajibu. Hapana. Ni maswali ninayotaka yapatiwe majibu na serikali au/na wataalamu wa masuala ya uchumi.

Kwa sie tunaoishi nje ya Tanzania, dalili kuu ya kushuka kwa thamani ya shilingi yetu ni pale tunapotuma fedha nyumbani kusaidia ndugu na jamaa zetu. Huo ndio muda unatulazimisha kufahamu viwango vya kubadilishia fedha. Kwahiyo kama ninataka kutuma shilingi laki kadhaa za Kitanzania, inanilazimu kufahamu ninatakiwa kutuma paundi za Kiingereza ngapi.Sasa kwa vile zoezi hili la kutuma misaada nyumbani ni la mara kwa mara, inakuwa rahisi kutambua kama 'shilingi ipo imara au imeyumba,' kwa maana kwamba unalinganisha, kwa mfano, "kutuma shilingi laki nne mwezi uliopita ilinigharimu takriban paundi mia na sitini, lakini safari hii imenigharimu paundi laki na arobaini."

Je Mtanzania wa kawaida anafahamu vipi kuhusu kuporomoka kwa thamani ya shilingi wakati hana sarafu ya kigeni ya kufanya mlinganisho? Na sio tu kufahamu kama thamani ya shilingi imepanda au imeshuka, lakini pia anapaswa kujua kama ina athari zozote kwake.

Kidogo ninachoelewa ni kwamba kuporomoka kwa shilingi kunaweza kuwa na 'faida' flani. Wanadai thamani ya sarafu ikishuka, bei ya bidhaa za nchi husika katika masoko ya kimataifa inashuka pia.Kushuka huko kwaweza kuwasukuma wanunuzi katika masoko hayo 'kuchangamkia tenda,' na hiyo inaweza kupelekea nchi kuuza mazao yake kwa wingi, na wakati huohuo hiyo inaweza kuhamasisha wakulima wa mazao au wauza bidhaa za export kuongoze uzalishaji. Sina uhakika sana kuhusu hilo kwa vile kama nilivyotanabaisha hapo juu, mie ni mbumbumbu wa uchumi.Sina A wala B ninalojua katika eneo hili.

Nimalizie makala hii kwa kutoa changamoto kwa serikali sio tu kuwafahamisha wananchi kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi yetu bali pia kueleza sababu za kushuka huko na athari au faida zake kwa Mtanzania. Kadhalika, ninatoa changamoto kwa wataalamu wetu wa uchumi kuisaidia jamii kwa kutupa somo kuhusu suala hili.Na nitumie fursa hii kumkaribisha mtaalam yeyote kunitumia makala kuhusu suala hjilo nami nitaichapisha hapa bloguni au kuituma kwa jarida la RAIA MWEMA ninaloandikia makala kila wiki.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.