Showing posts with label UGHAIBUNI. Show all posts
Showing posts with label UGHAIBUNI. Show all posts

11 Mar 2008

MAKALA HII YANGU ILITOKA KATIKA GAZETI LA MTANZANIA TAREHE 07 MACHI 2008

Unafiki wa viongozi wetu wa dini

na evarist chahali, uskochi

MADA yangu ya leo, najua dhahiri itawakera wateule wachache wa aina fulani. Lakini kabla ya kuwapasha, naomba nizungumzie suala la imani na dini hapa ninapoishi Ughaibuni.

Nilipofika hapa kwa mara ya kwanza, nilionyeshwa majengo kadhaa ambayo huko nyuma yalikuwa Makanisa, lakini sasa yamegeuzwa kuwa kumbi za disko na klabu za usiku.

Na hao walioyageuza Makanisa hayo kuwa sehemu za starehe, wala hawakujishughulisha kabisa katika kubadili mwonekano wake, bali wameyaacha yatoe ushuhuda kuwa huko nyuma yalikuwa sehemu za ibada.

Nilipofanya udadisi kwa wenyeji, niliambiwa kwamba makanisa hayo yaliuzwa baada ya kuwa matupu kutokana na ukosefu wa waumini. Wengi wa waumini wa makanisa ya mji huu ninaoishi, ni ama wahamiaji waliotoka nje ya nchi hii kama mimi, na au vikongwe vya hapa hapa.

Binafsi, sina majibu ya moja kwa moja kwamba tatizo la hawa wenzetu ni nini. Hata hivyo, ninachofahamu ni kwamba kuna watu kadhaa ambao wanajitambulisha kuwa hawana dini, na au hawaamini kuwapo kwa Mungu.

Imani ni suala la mtu binafsi, na hivyo pengine si mwafaka kuhoji kwa nini fulani anaamini, ama haamini kuwapo au kutokuwapo kwa Mungu.Ingawa binafsi, ni muumini kwa aina fulani, huwa sisiti kuwasifu wale wasiowaumini wa dini yoyote, lakini wasioona aibu kuelezea msimamo wao wa kidini. Kwa lugha nyingine, watu hao si wanafiki. Wanaeleza bayana kile wanachokiamini na kutokiamini.

Kuna tatizo la msingi huko nyumbani, ingawa natambua dhahiri kwamba watu wengi hawapendi kujadili mambo ya dini kwa sababu ile ile ya unafiki!

Baadhi ya viongozi wetu wa dini, wamekuwa mstari wa mbele kukemea wale ambao wanakwenda kinyume na imani zao, lakini viongozi hao hao wakishiriki kwenye maovu wanayoyakemea.

Ndiyo, tunatambua kwamba mara nyingi viongozi wetu wa dini wana wafadhili wao nje ya nchi. Lakini hicho si kigezo cha wao kuishi maisha tofauti kabisa na wafuasi wao.

Utakuta katika kijiji fulani ambacho kimegubikwa kabisa na umasikini, kiongozi fulani wa dini yeye akiishi kama yuko peponi. Na bila huruma, huyo huyo anayeishi maisha kama ya peponi katikati ya waumini masikini, kwa kutumia kisingizio cha maandiko matakatifu, anawashurutisha waumini wake kujipigapiga ili kuongeza sadaka wanazotoa.

Kinachokera zaidi, ni hili suala la baadhi ya viongozi wa madhehebu fulani kuwa na watoto mitaani, huku sheria za madhehebu yao zikiwa haziwaruhusu kufanya hivyo.

Tatizo hili ni sugu sana, hususan maeneo ya vijijini. Kinachosikitisha ni ukweli kwamba waumini wanafahamu kwamba kiongozi wao wa dini, anaishi kinyume na maadili ya huduma yake, lakini hawachukui hatua yoyote zaidi ya kulalamika chini chini.

Binafsi, ninayo mifano hai ya baadhi ya viongozi wa madhehebu yangu ambao wana watoto lukuki mitaani. Baadhi yao wanatoa huduma kwa wazazi wa watoto wao hao, lakini wengine wamewatelekeza kabisa.

Hawa watu ni wanafiki ambao hawastahili kuachwa waendeleze uhuni kwa kisingizio kwamba daraja walilofikia, haliwezi kutenguliwa.

Mitume wetu waliishi maisha ya uadilifu, ambayo yalishabihiana kwa asilimia 100 na kile walichokuwa wakikihubiri. Na si katika suala la uzinzi pekee, bali hata kwenye dili za kibiashara.Majanga kama ya ukimwi yataondoka vipi iwapo baadhi ya wale wanaopaswa kukemea vitendo vya ngono, kwa vile vinavunja amri ya Mungu, nao ni washirika wa vitendo hivyo?

Pamoja na mapungufu waliyonayo baadhi ya viongozi wa dini, hivi karibuni tumeshuhudia wengi wakijitokeza kuungana na Watanzania wenzao kukemea masuala yanayohatarisha umoja wa kitaifa.

Suala ambalo baadhi ya viongozi hao wa dini wanastahili pongezi, ni katika kukemea vitendo vya kifisadi, ingawa tatizo linakuwapo, pale msimamo huo unapokuwa wa kiongozi mmoja zaidi, badala ya kuwa msimamo wa taasisi ya dini.

Katika hili, napenda nichukue fursa hii kumpongeza Askofu Mkuu mpya wa Kanisa la Anglikana Tanzania, ambaye ameweka bayana msimamo wake dhidi ya vitendo vya kifisadi. Hiyo inatia moyo sana!

Licha ya kukemea ufisadi na maovu mengine katika jamii, asasi za dini zinaweza kubadili tabia za waumini wao kwa kuwawekea vikwazo vya aina fulani. Taratibu za aina hiyo, zipo katika baadhi ya imani, kwa mfano, Wakatoliki, ambao muumini akikiuka kanuni fulani, anazuiwa kushiriki baadhi ya sakramenti.

Kwa nini basi tunaendelea kujumuika na mafisadi makanisani, na au misikitini ilhali matendo yao yanalenga kutuumiza kimaisha? Nafahamu kuwa dini zote zinahimiza upendo, lakini hiyo si sababu ya kutowabana wale wasio na upendo kwa Watanzania wenzao.

Inawezekana kwamba kikwazo kikubwa kwa dini zetu kuwa mstari wa mbele katika kukemea maovu na kubadili tabia za wanaokwenda kinyume na maadili ya kimwili na kiroho, ni hofu ya usafi wa baadhi ya viongozi wa dini hizo, kama nilivyoeleza mwanzoni mwa makala haya.Tatizo hilo linaweza kupatiwa ufumbuzi iwapo viongozi wa madhehebu wataepuka mtindo wa kulindana, na hivyo kuchukua hatua kali kwa walio chini yao, ambao wanakwenda kinyume cha kanuni na taratibu za madhehebu.

Ni wazi kwamba viongozi waadilifu wa dini, hawawezi kuogopa kumnyooshea kidole fisadi fulani, kwa kuwa hata kama fisadi huyo atataka kulipa kisasi, atajikuta hana jambo lolote analoweza kulitumia kushusha heshima ya kiongozi wa dini aliyemkemea.

Busara za Kiswahili zinatueleza kwamba kujikwaa si kuanguka, na hata kuanguka si mwisho wa safari. Wito wangu kwa viongozi wetu wa dini, ni kuongeza jitihada za kuwahudumia waumini wao kiroho na kimwili.

Ni muhimu kwa viongozi hao kuishi kama Mitume ambao mafundisho yao yalikubalika na kuvuta watu wengi, kwa vile wao wenyewe walikuwa waadilifu na mifano bora ya kuigwa na wanadamu.




1 Oct 2007

Kwanza,samahani nyingi kwa wapendwa wa blogu hii,maana niliadimika kidogo na hakukuwa na updates zozote.Ni vijimambo tu vilivyosababisha hali hiyo,lakini nimesharejea kamili-kamili.Badala ya title ya post kuwa Kulikoni Ughaibuni sasa tutakuwa na Mtanzania Ughaibuni.Sababu ya msingi ya kubadili jina ni ukweli kwamba makala zinazopatikana katika blogu hii ni kumbukumbu ya zile zinazotoka kwenye moja ya magazeti ya huko nyumbani.Kwa sasa makala zinazounda blogu hii zitakuwa zinapatikana kwenye gazeti la Mtanzania Jumapili badala ya gazeti la Kulikoni.Jina la blogu litaendelea kuwa hilohilo la Kulikoni Ughaibuni.Enjoy!!!
MTANZANIA UGHAIBUNI-1

Asalam aleykum,

Kwanza nianze na salam kwa wale wote waliojaaliwa “kuuona mwezi” na kwa sasa wanaendelea na funga ya Ramadhan.Salam pia kwa wale ambao kwa sababu moja au nyingine hawajaouna mwezi mpaka leo.Salam nyingi zaidi ni kwa wasomaji wote wa gazeti hili la Mtanzania Jumapili.Baada ya salam,nadhani ni vema nikajitambilisha maana hii ndio makala yangu ya kwanza kabisa katika gazeti hili maridhawa.

Jina la makala hii linashabihiana kabisa na maelezo yangu binafsi na mahali nilipo kwa sasa.Mie ni Mtanzania (halisi,Mndamba kutoka Ifakara) ambaye kwa sasa nipo masomoni huku Ughaibuni.Naomba kutamka mapema kwamba mie sio mwandishi wa habari kitaaluma,ila naipenda na kuiheshimu sana taaluma hiyo,na ni katika kuonyesha “mahaba” yangu kwa taaluma hiyo ndio nikaelekeza nguvu zangu kwenye uandishi wa makala.Nadhani wasomaji wengi wa magazeti wanafahamu kwamba makala inaweza kuandikwa na mwandishi aliyesomea kwenye fani hiyo,na pia inaweza kaundikwa na akina sie ambao kwa sababu moja au nyingine hatukubahatika kusomea.Yayumkinika kusema kwamba kinachomvutia msomaji ni ubora wa makala na sio sifa za kitaaluma za mwandishi.Kimsingi,makala zangu zitalenga kuhabarisha,kufundisha,kukosoa,kuchochea mijadala (pale inapobidi) na mwisho ni kuburudisha.Makala zangu ni za picha mbili katika moja,yaani kwa upande mmoja nitazileta kwa mtizamo wa Mtanzania aliye Ughaibuni (Mtanzania ambaye anajua alikotoka,anaijali lugha yake ya taifa,ana uchungu na nchi yake na sio mingoni mwa wale waliosahau kuwa nyumbani ni nyumbani),na kwa upande mwingine ni mtizamo wa Mtanzania kama Mtanzania,yaani hapo namaanisha kuwa nitachoandika kingebaki hivyohivyo hata kama ningekuwa Namtumbo,Kiberege,Nkasi au Temeke.Labda nifafanue kidogo katika suala hili la mitizamo ya makala zangu.Kwanza,zitakuwa na mambo ya Ughaibuni na pili zitakuwa na mambo ya huko nyumbani.Lakini,kuna nyakati haitakuwa directly (moja kwa moja) namna hiyo,bali nitajaribu pia kufanya comparative analysis (tuite mchanganuo linganifu) ambapo masuala,habari na matukio ya huku Ughaibuni yataletwa kwa namna ya kuyalinganisha na yale yanayoshabihiana na huko nyumbani.Hapo kutakuwa na mazuri tunayoweza kujifunza kutoka kwa hawa wenzetu na mabaya ambayo huko nyumbani tumebahatika kuwa nayo lakini hawa wenzetu wameyakosa.Enewei,mengi mtayaona katika makala zijazo.

Hebu tuangalie nini kinachoendelea hapa kwa “Kwin Elizabeti” (Uingereza).Kwa kawaida,kipindi hiki cha kuelekea kumalizika kwa majira ya joto (summer season) vyama vikuu vya siasa hapa hufanya mikutano yao ya mwaka.Tayari chama cha demokrasia ya kiliberali (Liberal Democrats) na chama tawala cha Labour wameshamaliza mikutano yao.Kwa Liberal Democrats “ishu” kubwa ilikuwa ni mwenendo usioridhisha wa chama hicho ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa ukihusishwa na uongozi wa Sir Menzies Campbell.Wapo waliokuwa wanaomwona kiongozi huyo kama mzee asiye na jipya wala mvuto wa kukifanya chama hicho kipate umaarufu unaohitajika.Habari njema kwa Sir Campbell ni ukweli kwamba wengi wa wanachama wa chama hicho bado wanaelekea kuwa na imani na kiongozi huyo pengine kwa kuamini kuwa “utu uzima ni dawa” (Campbell ana umri mkubwa zaidi kulinganisha na viongozi wengine wa vyama vikuu vya siasa vya hapa).Kwa upande wa Labour ya Gordon Brown,mkutano mkuu haukuwa na “mbinde” yoyote hasa ikizingatiwa kuwa kura za maoni zinaonyesha kwamba Waingereza wengi wanaelekea kuridhishwa na utendaji wa Waziri Mkuu Brown na chama cha Labour kwa ujumla.Pengine kinachomsaidia Brown ni rekodi yake akiwa mwangalizi mkuu (kansela) wa uchumi wa Uingereza na “uzembe” wa Tony Blair katika siasa za kimataifa hususan uswahiba wake na Joji Bushi na “ishu” nzima ya Iraki.Lakini “kimuhemuhe” kikubwa kiko kwa chama cha wahafidhina (Conservatives) ambacho kimeanza mkutano wake Jumapili iliyopita.Kiongozi wa chama hicho David Camron ana mtihani mkubwa sana,sio tu kwa vile kura za maoni zinamweka nyuma ya Gordon Brown,bali pia ukweli kwamba mawazo yake ya kukibadili chama hicho kiendane na wakati yamekuwa yakipata upinzani mkali miongoni mwa wale “waliokunywa maji ya bendera” ya chama hicho.Cameron amekuwa muwazi kwa wahafidhina wenzie kwa kusema kuwa chama hicho kinaonekana mingoni mwa wengi kama kinachowakilisha “tabaka la wenye nazo” na “masapota” wake wakubwa ni wazungu weupe ilhali makundi ambayo yanakuwa kwa kasi nchini hapa kama watu weusi na wahindi wakikiona chama hicho kama cha kibaguzi.Cameron amekuwa akijitahidi kwa udi na uvumba kuonyesha kwamba uhafidhina haimaanishi kuwa tofauti na watu wa kawaida,lakini wakongwe katika chama hicho wanaonekana kutovutiwa na mwenendo wa kiongozi huyo kijana.Pia Cameron amewaeleza bayana wananchama wenzie kwamba pasipo dhamira ya dhati ya kukibadili chama hicho kwenda na wakati basi ni dhahiri kuwa sio tu hakitaweza kupata ridhaa ya kuongoza nchi hii bali pia kinaweza kujiandalia kifo chake siku za usoni.

Nadhani mazingira yanayokizunguka chama cha Conservative yanashabihiana kwa namna flani na chama tawala huko nyumbani,chama dume,CCM,japo tofauti ya wazi ni kuwa wakati Conservative ni chama cha upinzani hapa Uingereza,CCM ni chama tawala huko nyumbani.Lakini kabla sijaenda mbali naomba niseme yafuatayo.Miongoni mwa matatizo yanayozikabili siasa za nchi zetu za Kiafrika ni kwa wahusika kutopenda kuambiwa yale wasiyotaka kusikia (ikiwa ni pamoja na kuambiwa hivyo wanavyofanya sivyo inavyopaswa kuwa,yaani ndivyo sivyo).Kwa mantiki hiyo,ushauri wa maana kabisa kwa CCM unaweza kutafsiriwa na baadhi ya wakereketwa kuwa mtoa maoni ni mpinzani.Mie si mfuasi wa chama chochote,na japo nasomea siasa (za kimataifa) lakini huwa sioni aibu kusema kwamba naichukia siasa hasa kwa vile nadharia (theories) zinakinzana sana na vitendo kwenye dunia halisi tunayoshi.Angalau kwenye siasa za kimataifa (International Relations) ninapata fursa ya kuelewa kwanini kuna ubabaishaji au uimara kwenye siasa za eneo flani.Baadhi ya rafiki zangu huwa wananiuliza iwapo niliamua kusoma siasa ili baadae nije kuwa kiongozi lakini (baada ya kicheko) huwa nawafahamisha kuwa katika siasa za Afrika kinachomata sio digrii ya siasa bali “nyenzo” zitakazowafanya wapiga kura wawe tayari hata kung’oana macho kuhakikisha unapata madaraka.

Changamoto linalokikabili chama cha Conservative linashabihiana kwa namna flani na lile linaloikabili CCM kwa namna hii:Kwa mtazamo wangu,wapo wana CCM wanaogombea madaraka kwa vile wanaamini kuwa ni kwa kufanya hivyo ndio watapata nafasi ya kuwataumikia Watanzania wenzao.Lakini wapo pia wale ambao wanafahamu u-chama dume wa CCM na wanagombea madaraka ili kufanikisha tu mahitaji yao binafsi ikiwa ni pamoja na kujitengenezea mazingira mazuri ya kuendelea na madaraka hapo 2010.Lakini kundi la hatari zaidi ni lile la wasio na idea yoyote kuhusu siasa bali ustawi wa matumbo yao (na pengine nyumba ndogo zao).Hili kundi la tatu ni la kuogopwa zaidi ya lile la pili kwani wakati lile kundi la pili linajumisha watu wanaoweza kuwa wanagombea ili waendelee kuwa madarakani kama wanasiasa,hawa wa kundi la tatu hawajali sana kama watarejea madarakani kwa vile la msingi kwao ni wamechuma kiasi gani katika kipindi walicho madarakani.Changamoto kubwa kwa CCM ni kutengeneza utaratibu ambao utakihakikishia chama hicho kinaendelea kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi (na wafanyabiashara ).Tofauti na wale wanaonekana kuwa na hofu kutokana na wafanyabiashara kuingia kwenye siasa,mie sina tatizo na kundi hilo alimradi lengo lao ni kuwatumikia wananchi (na pengine kuna umuhimu kwa bendera ya CCM kuongeza alama ya fedha kuashiria kuwa chama hicho ni cha wakulima,wafanyakazi na wafanyabiashara).Ikumbukwe kuwa hata wamachinga ni wafanyabiashara pia na miongoni mwao wapo wale wenye mwamko wa kisiasa sambamba na wakulima na wafanyakazi.

Naomba nimalizie kwa kuwa muwazi zaidi kwa hoja kwamba kwa namna flani “vimbwanga” vilivyojitokeza kwenye kinyang’anyiro cha kuwapata viongozi waCCM katika ngazi mbalimbali vimechafua jina la chama hicho tawala.Huo ni ukweli ambao kila mwenye mapenzi na chama hicho na uchungu na nchi yake atakuwa anaufahamu.Yayumkinika kusema kuwa baadhi ya hoja za vyama vya upinzani zinajengwa na CCM yenyewe kwani iwapo kungekuwa na “kuwekana sawa” katika masuala yanayogusa hisia za wananchi wa kawaida basi ni dhahiri kwamba akina Slaa au Kabwe wasingekuwa na hoja za kujaza maelfu kwa maelfu ya watu kwenye mikutano yao.Hii inaitwa na Waingereza kuwa ni “wake up call” au kwa lugha nyepesi ni changamoto.Kwa vile maslahi ya Taifa ni muhimu kuliko vyama vya siasa (vyama vya siasa huzaliwa,kukuwa na pengine kufa wakati nchi ni lazima iishi milele) basi naamini kuwa wenye mapenzi ya dhati na Taifa letu watanielewa na kufanyia kazi nilichoeleza.

Alamsik



18 Jun 2006

KULIKONI UGHAIBUNI

Asalam aleykum,

Siku za nyuma niliahidi kwamba iko siku nitawaletea stori kuhusu “mateja” wa huku Ughaibuni.Ndio,tatizo la matumizi ya madawa ya kulevya linawaumiza vichwa watu kadhaa huku Ughaibuni.Kuna vijana wadogo kabisa ambao wanashawishika kujiingiza katika kubwia unga.Ni vigumu kutabiri mafanikio ya jitihada za serikali na taasisi mbalimbali katika mapambano yao dhidi ya ulevi huo haramu na hatari.

Hivi karibuni nilipewa habari za kusikitisha sana.Kijana mmoja mwenye umri usiozidi miaka 18 alikutwa amekufa huku sindano aliyoitumia kujidungia adawa ya ulevya ikiwa inaning’inia kwenye mkono wake.Huyo kijana namfahamu vizuri kwa vile siku moja aliwahi kufika hapa ninapoishi akiwa ameongozana na rafiki yangu mmoja mwenye asili ya Afrika Mashariki.Kilichonivutia zaidi kuhusu kijana huyo ni kauli zake ambazo lazima nikiri kuwa mara nyingi kwa hapa zinatolewa na wanasiasa kuliko wananchi wa kawaida.Alikuwa akionyesha kuchukizwa kwake na watu wanaowabagua wenzao kwa vile tu ni wageni au wana rangi tofauti na wao.Kimsingi,alikuwa akilaani suala zima la ubaguzi.Kwa umri wake mdogo,nilimwona kama ni mtu mwenye upeo mkubwa sana.Kwa wakati huo sikujua kabisa kuwa pamoja na busara zake,kijana huyo alikuwa akiweka rehani roho yake kwa kubwia unga.Pengine lishe bora na huduma mbalimbali zinazopatikana kirahisi ndizo zilikuwa zinamsaidia kuficha “uteja” wake,kwani kama tujuavyo wengi si vigumu kumtambua m-bwia unga kwa kumwangalia tu.

Alienisimulia kuhusu mauti yaliyomkumba kijana huyo alinijulisha kwamba aliemletea marehemu madawa hayo ya kulevya alikuwa ni rafiki yake ambae walikuwa wanasoma darasa moja.Kwa lugha nyingine,wawili hao walishirikiana katika kuleta mauti ya mmoja wao.Huo ni ushirika wa mauti,na hilo ndio linanipeleka kwenye mada yangu ya pili kuhusu ujambazi uliotokea hivi karibuni pale Ubungo uliopelekea vifo na majeraha kwa waliosalimika.

Kuonyesha yeye ni kiongozi anaewajali mno wananchi wake,matra baada ya kurejea nchini akitoka ziarani kusini mwa Afrika,Rais Jakaya Kikwete alikwenda kuwajulia hali waliojeruhiwa na majambazi katika tukio hilo la Ubungo.Mheshimiwa Kikwete alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba anaamini kuwa kulikuwa na njama ndani ya benki iliyoibiwa fedha hizo kwa vile isingekuwa rahisi kwa majambazi hayo kuvamia tu gari lenye fedha bila kuwa na taarifa sahihi.Wafanyakazi waliohusika kuvujisha taarifa za fedha hizo kwa majambazi watakuwa hawana tofauti na yule kijana aliempelekea unga rafiki yake na hatimaye kumsababisha mauti.Waliovujisha taarifa hizo walikuwa na ushirika wa mauti na majambazi waliofanya unyama huo.Hivi tunapokuwa kazini si huwa tunaunda kitu kama undugu kwa vile muda mwingi tunautumia tukiwa pamoja na pengine kushirikiana katika mambo ya nyumbani kama vile harusi na misiba?Sasa unapotoa taarifa kwa majambazi wenye silaha za moto ili kuwawezesha kuvamia gari ambalo mfanyakazi mwenzio yupo humo si ni kama unamtengenezea mauti mwenzio?Jamani,hivi fedha zinatupeleka kupoteza utu wetu na kutothamini uhai wa wenzetu!Kwa hakika walioshiriki kwa namna yoyote katika kufanikisha uporaji huo wanastahili kusakwa kwa udi na uvumba na hatimaye kupatiwa kibano wanachostahili.Kwa “waliouza ishu” hiyo kwa majambazi wanakuwa wametenda dhambi kuu mbili:kuwasaliti wafanyakazi wenzao ambao aidha waliuawa au kujeruhiwa,na pia walishiriki katika ujambazi huo kwa vile wao ndio hasa waanzilishi wa mpango mzima.Hiyo si kusema kwamba majambazi waliohusika hawana hatia,lakini iwapo waliotoa taarifa hizo wasingewajulisha majambazi kwamba siku flani,muda flani,katika gari flani kutakuwa na shilingi bilioni moja ni dhahiri kwamba tukio hilo lisingetokea.

Kwa upande mwingine,ni muhimu kwa taasisi zetu za fedha kuwa makini zaidi wanaposafirisha fedha kutoka sehemu moja kwenda nyingine.Hivi kweli benki kama NMB inashindwa kununua gari moja ambalo ni maalumu kwa ajili ya kusafirishia fedha?Uzuri wa magari kama hayo ni kwamba licha ya kutoa usalama mkubwa kwa mali inayosafirishwa,maisha ya wanaosafirisha mali hiyo nayo yanakuwa salama zaidi ukilinganisha na magari ya kawaida.Natambua kuwa yapo makampuni binafsi ya ulinzi ambayo yanamiliki magari ya aina hiyo.Lakini siwezi kuilaumu NMB moja kwa moja kwa kutokodi huduma hiyo kwa vile kumbukumbu zinaonyesha kuwa siku za nyuma walinzi wasio waadilifu walishawahi kuingia mitini na mamilioni ya fedha wakiwa katika gari maalumu la kusafirishia fedha.

Hata hivyo,kuwa na gari maalumu la kusafirishia fedha bila kuwa na watumishi waadilifu ni sawa na kulala ukiwa kwenye chandarua chenye dawa lakini kimekufunika kuanzia kichwani hadi kiunoni tu,na hapohapo kuamini kuwa unawadhibiti mbu.Uaminifu,uadilifu na kuthamini maisha ya wenzetu ni vitu muhimu sana na lazima kwa kila Mtanzania.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Leo tuzungumize michezo,hususan soka.Kwa takriban wiki nzima sasa habari ya soka iliyotawala katika vyombo vya habari vya hapa Uingereza ni kuhusu suala la mchezaji mahiri wa klabu ya Manchester United na timu ya Taifa,Wayne Rooney.Ishu yenyewe ni kwamba ilidaiwa kuwa Rooney alikuwa na madeni yanayofikia pauni 700,000 (takribani shilingi milioni 140 za huko nyumbani) aliyokuwa akidaiwa na makampuni ya kamari (betting).Inasemekana tayari amemalizana na wadai wake.Wapo waliomlaumu mchezaji huyo kwa kutumia vibaya fedha zake,lakini wengine wamemtetea kwamba haikuwa ubaya kutumia kipato chake kinachotokana na ajira yake.

Ndio,soka huku Ughaibuni na hata katika baadhi ya nchi za huko Afrika ni ajira.Ni ajira ambayo inamwezesha mtu kama Rooney kutumbukiza zaidi ya shilingi milioni 100 kwenye kamari.Pointi yangu sio uhusiano wa soka na kamari bali soka kama ajira.Tukirudi huko nyumbani,siku chache zilizopita klabu kongwe za Simba na Yanga zilichimba mkwara kuwa zingesusia ligi kuu ya Bara iwapo mgao wa mapato ungeendelea kuwanufaisha zaidi wengine badala ya wao wanaovuja jasho dakika 90.Binafsi niliguswa sana na hoja za klabu hizo japokuwa kwa bahati mbaya nasikia wakongwe hao wamenywea katika kutimiza azma yao ya kutaka “kieleweke.”Sijui kuufyata huko ni kwa vile viongozi wa klabu hizo walitoa hoja hiyo kama kutingisha kiberiti,au sijui ni ubabe wa vyama vyetu vya michezo huko nyumbani!Lakini naamini klabu hizo zilikuwa na hoja ya msingi kabisa.

Pambano lao la mwisho liliingiza milioni 98 kama sijakosea.Lakini kila klabu ikaambulia shilingi milioni 23.6 tu.Kwa kweli huo ni sawa na uonevu.Mapato hayo yalitokana na umaarufu wa klabu hizo,hivyo zenyewe ndio zilipaswa kunufaika zaidi na mapato hayo.Nadhani klabu hizo zilistahili kupata kiwango kikubwa zaidi ya hicho hasa ikizingatiwa kuwa timu hizo kwa sasa ni kama za kulipwa kutokana na kuwa na wachezaji kadhaa wa kigeni ambao mishahara yao ni ya juu.Jitihada za kuzigeuza klabu hizo kuwa kampuni zimekuwa zikikwama mara kwa mara.Kwa hiyo tofauti na klabu kubwa za huku Ughaibuni ambazo zinaendeshwa kwa mfumo wa kampuni hivyo kutotegemea sana mapato ya uwanjani,chanzo kikuu cha mapato kwa vilabu vyetu vya nyumbani ni mapato yanayotokana na watu wanaoingia uwanjani kushuhudia mechi zao.

Imenisikitisha sana kuona hoja ya klabu hizo imekufa kienyeji.Lakini sikushangaa sana kwa vile sio siri kwamba vilabu vyetu huko nyumbani vinaendeshwa kwa ubabaishaji sana.Kwanza kwa Simba na Yanga hawapaswi kutegemea mapato ya uwanjani kama chanzo pekee cha mapato.Japo hoja ya klabu hizo kugeuzwa kuwa kampuni bado ni ya muhimu sana ingawaje wenyewe wanapuuzia,vipo vyanzo vingine kadhaa vya mapato ambavyo vimetelekezwa.Kwa mfano,kwa kutengeneza kalenda 100,000 zenye picha za wachezaji ambazo zingekuwa katika ubora unaostahili na kuziuza angalau kwa shilingi 500 kila moja,klabu ingejiingizia shilingi milioni 50.Hilo linawezekana kabisa hasa kwa vile gharama za utengenezaji wa kalenda sio kubwa sana na kuna uwezekano wa kupatikana wadhamini wa kugharamia mradi wa aina hiyo.
Kwa mtizamo wangu,watu wanaopaswa kubeba lawama zaidi katika suala zima la ubabaishaji kwenye vilabu vyetu ni hao wanaoitwa wanachama.Hao ndio wanaochagua viongozi wabovu,na ni haohao ambao hawakawii kwenda mahakamani kupinga uongozi ambao wao wenyewe waliuweka madarakani.Wanang’ang’ania kujiita wanachama wakati mchango wao mkubwa katika kuendesha klabu hizo ni kwenda kwenye vyombo vya habari kutaka uongozi wa klabu ujiuzulu,au kocha hafai au wakati mwingine kusema lolote tu ili wasikike hewani.Kama kweli wanachama wa Simba na Yanga wangekuwa wenye mwamko unaostahili basi naamini wangetumia nguvu za wingi wao kuhakikisha hoja zilizotolewa na viongozi wao kuetetea maslahi ya klabu hizo zinashinda.Badala ya hoja hizo kuonekana ni ajenda binafsi za Wambura au Kifukwe zingekuwa ni hoja za klabu na wanachama wa Simba na Yanga.

Kulalamika bila kutoa ufumbuzi wa tatizo ni sawa na kulikuza tatizo.Kwa hiyo,nawajibika kutoa mchango wangu katika kupata ufumbuzi.Nadhani Tenga na wenzie wa TFF wanapaswa kuliangalia upya suala la mgao wa mapato kwa klabu,na sio kwa Simba na Yanga pekee bali vilabu vyote.Vilabu vina haki ya kudai ziada ya wanachokipata kutokana na jitihada zo uwanjani.Kuhusu uendeshaji wa vilabu,Serikali inapaswa kuingilia kati kwa kutengeneza sera ambayo haitotota fursa ya uababishaji,iwe wa viongozi au wanachama.

Alamsiki.

KULIKONI UGHAIBUNI

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa makala hii.

Leo nina hasira.Muda mfupi kabla ya kuandika makala hii niliongea na mzazi wangu huko Ifakara.Akanisimulia stori mmoja ambayo kimsingi ndio iliyonifanya niwe na hasira.Hata hivyo,naomba niwatoe hofu kwamba hasira nilizonazo haziwezi kupoteza ladha ya makala hii.

Mzee ana matatizo ya moyo.Sasa kama unavyojua mambo ya miji midogo kama Ifakara.Hospitali zipo lakini wataalamu ni wachache.Lakini kwa kumbukumbu zangu wakati flani aliwahi kunieleza kwamba kuna daktari mmoja mwenye zahanati yake binafsi mjini hapo ambae inaaminika kuwa ni mtaalam wa mambo ya moyo.Katika maongezi yetu kwenye simu aliniambia kuwa moyo bado unamsumbua.Nikamuuliza kwanini asiende kwa huyo mtaalam wa magonjwa ya moyo.Jibu alilonipa ndilo lililonifanya nipandwe na hasira niliyonayo hadi sasa.Anasema kwamba jirani yake aliyekuwa akisumbuliwa na matizo ya moyo alikwenda kumuona huyo daktari hivi karibuni,lakini jibu alilopewa lilimfanya mgonjwa huyo kurudi nyumbani akiwa na ugonjwa mwingine mpya:hofu ya kufa.Kisa?Aliambiwa na mtaalamu huyo wa moyo kwamba hivi “kwanini wewe ambaye umebakiwa na wiki mbili tu za kuishi (kutokana na umri wako mkubwa) unataka kutibiwa moyo badala ya kuuacha usimame wenyewe muda ukifika”!

Laiti maelezo hayo ya mzazi wangu yangekuwa yanatoka kwa mtu wa kawaida tu nisingeamini kwamba nchi yetu ina baadhi ya watu wanaojiita madaktari ambao wanaweza kukiuka maadili ya kazi yao kwa kiwango hicho!Nadhani hata ukienda gereji na gari lililochoka sana,bado mafundi makenika watakupa matumaini ya namna flani badala ya kukibilia kukwambia kwamba ukalitupe gari lako.Na hapo tunazungumzia kitu ambacho unaweza kukinunua kipya.Maisha hayawezi kununuliwa upya.Tukirudi kwenye stori niliyopewa na mzee,basi jirani yake (ambaye si kama amekula chumvi sana) tangu alipoambiwa na daktari kwamba amebakiwa na wiki mbili kufa,amepatwa na hofu ya ajabu.Kwani kuna mtu ambaye haogopi kufa?Na hasa kama umepewa tahadhari kama hiyo na daktari.Mzee wangu baada ya kusikia stori hizo kutoka kwa jirani yake alinieleza bayana kwamba bora aendelee kuugua kuliko kwenda kwa daktari ambae amegeuka kuwa mtabiri wa urefu wa maisha ya wagonjwa.Nilimpoza kwa kumwambia kuwa naamini huyo daktari alieongea upuuzi huo hajui wajibu wake na anakiuka tu maadili ya kazi yake.

Laiti jirani ya mzee wangu angekuwa amekumbana na kioja hicho hapa Ughaibuni huenda angejikuta anapata utajiri wa ghafla endapo angefungua mashtaka dhidi ya daktari aliemtishia uhai wake.Sio siri,hawa wenzetu wanatoa kipaumbele kikubwa sana kwa suala la afya sambamba na kuhakikisha kuwa watumishi katika sekta ya afya wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata maadili.Na sio katika sekta ya afya pekee bali sehemu nyingi zinazotoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi zinabanwa sana kuhakikisha kuwa huduma hizo zinatolewa katika kiwango stahili.Pengine kingine kinachowasaidia viongozi katika taasisi mbalimbali za huduma hapa Ughaibuni ni ile tabia ya kufuatilia nini kinachoongelewa kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi zao.Mganga mkuu akisoma gazeti na kukuta malalamiko kuhusu hospitali yake,hapuuzi bali atakimbilia kumjibu mlalamikaji huyo kuwa atachunguza suala lililolalamikiwa.Na haishii kutoa ahadi tu bali hatua lazima zitachukuliwa.Lakini kinachosikitisha huko nyumbani ni ile kuona gazeti flani limeripoti kuwa hospitali flani “imeua” mgonjwa na wala husikii habari hiyo ikikanushwa au kukubaliwa na uongozi wa hospitali husika.

Sehemu nyingi zinazotoa huduma huko nyumbani zina masanduku ya kutoa maoni.Lakini lile vumbi unaloliona kwenye mengi ya masanduku hayo linatosha kuthibitisha kuwa masanduku hayo ni sawa na urembo tu kwenye makorido ya sehemu husika.Kwa mtizamo wangu,nadhani tatizo la msingi ni ile tabia iliyojengeka kwa baadhi ya watumishi kwenda kazini kuonekana tu wamekwenda kazini na mwisho wa mwezi wapate mishahara yao,na si kwenda kutumikia wale wanaowafanya wapate mshahara.Unadhani mtumishi wa benki anaejua dhahiri kwamba ni fedha za wateja ndio zinaiwezesha benki hiyo kuwepo na kumlipa mshahara,atamdharau mteja anaekuja hapo kupata huduma?Kama mtumishi anajiona hataki “kubughudhiwa” na wanaohitaji huduma kazini kwake,si alale tu nyumbani,au aache kazi?Tuone kama hatakufa kwa njaa.Kumbe basi kinachompa shibe (kazi) ni sharti akiheshimu na kukitumikia kwa moyo wake wote.

Alamsiki

17 Apr 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Kabla ya yote sina budi kuanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutimiza siku 100 tangu achaguliwe kuwa Rais wa serikali ya awamu ya nne huko nyumbani.Si huko nyumbani tu ambako wananchi wengi wameridhika na utendaji wa Mheshimiwa na serikali yake bali hata huku Ughaibuni.Kuna dalili nyingi zinazoonyesha kwamba nchi yetu inaweza kurudisha heshima yake ambayo kwa kiwango kikubwa ilikuwa imepotea ndani na nje ya nchi.

Siku moja nikiwa kibaruani hapa napoishi nilikutana na jamaa mmoja ambaye nilipomfahaisha kuwa mimi ni Mtanzania alionyesha kuwa na shauku ya kuongea nami.Huyo jamaa alinifahamisha kuwa yeye ni Mskotishi ambaye miaka michache alipata fursa ya kutembelea Tanzania kufanya mchanganuo wa mradi flani uliokuwa ufadhiliwe na wahisani wa kimataifa.Jamaa alianza kwa kuniuliza kwanini Tanzania ni nchi masikini wakati ina utajiri kibao wa asili.Nikajifanya kama sikulielewa swali lake na kumtaka anifafanulie huo anaoita utajiri.Akanitolea mlolongo wa vitu:madini,misitu,ardhi yenye rutuba,maziwa na mito kadhaa,mbuga za wanyama (na hapo akaniambia kuwa Selous ni mojawapo ya mbuga za asili kubwa kabisa duniani),mlima Kilimanjaro,na kikubwa zaidi ya vyote,AMANI.Sio siri,nilibaki nang’ang’aa macho tu bila ya kuwa na jibu la haraka la swali lake la msingi:kwanini Tanzania ni miongoni mwa nchi masikini sana duniani wakati ina utajiri lukuki?

Jamaa akaendelea kunikalia kooni.Akanipa mfano hai wa uzoefu wake kuhusu Tanzania.Nilisema hapo mwanzo kuwa huyo jamaa alikuja hapa kwa ajili ya mradi flani.Alidai kuwa wakati yeye na wenzake wakiwa wanaandaa mambo flani kuhusu mradi huo,wakakumbana na mambo ambayo yeye aliyaona ya ajabu sana kwa mtizamo wake.Alieleza kuwa katika ofisi zaidi ya moja walikutana na watendaji wa serikali ambao waliwaomba “ma-TX” hao kuongeza gharama halisi za mradi huo kwa makubaliano ya “teni pasenti” pindi fungu la fedha likitoka.Huyo jamaa na wenzake walionekana kushangazwa sana na tabia ya watendaji hao wa serikali walioonekana kuwa hawakuwa na uchungu wowote na nchi yao wala kujali umuhimu wa mradi huo kwa Taifa lao.Jamaa anadai wao walikataa ofa hizo (kama ni kweli au la mimi sijui) na picha aliyobaki nayo ni kwamba wabomoaji wa Tanzania kwa kiasi kikubwa ni Watanzania wenyewe.

Nimeelezea stori ya Mskotishi huyo kubainisha jambo ambalo haliitaji mtu kutoka nje kutuelezea.Ni wangapi tunaojua kwamba wapo watendaji ambao kwa teni pasenti wanatoa vibali vya kazi kwa wageni wasiostahili kuwepo bila kujali kuwa wanaweza kuwa magaidi?Au wale wanaotoa vibali vya ujenzi kwa makandarasi wasio na sifa na hatimaye kuhatarisha maisha ya watuamiaji wa majengo hayo?Au wale wanaruhusu bidhaa mbovu,ikiwa ni pamoja na chakula,kuingia nchini bila kujali athari kwa afya za watumiaji?Orodha ni ndefu.

Ndio maana Watanzania wengi walio huku Ughaibuni walifurahishwa sana na kauli ya Mheshimiwa Kikwete kuwa atakula sahani moja na watu wanaofanya kazi za umma na kutanguliza maslahi yao binafsi badala ya ya yale ya Taifa ikiwa pamoja na wale wanaosaini mikataba bomu zaidi ya ile ya baadhi ya machifu wetu enzi za ukoloni.Ni dhahiri kuwa nchi yetu iko katika nafasi ambayo haistahili kuwepo.Nchi yetu haipaswi kuwa masikini wa kutupwa wakati tuna rasilimali kibao.

Salamu za wabongo walioko huko kwenda kwa Mheshimiwa Kikwete ni kwamba akaze uzi na kutowalea wazembe kama ilivyokuwa huko nyuma.Mtu akiboronga atimuliwe mara moja.Kuunda tume kuichunguza tume iliyofanya ubadhirifu wakati inachunguza ubadhirifu wa fedha uliofanywa na tume nyingine ni kupoteza fedha tu.Wazembe watimuliwe na ikiwezekana wafikishwe kwenye vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo.Historia inaonyesha kuwa binadamu tuna tabia ya kuogopa mambo yanayoweza kuhatarisha nafasi zetu nzuri.Kiongozi anaeteuliwa kuchukua nafasi ya mwenzie alietimuliwa kutokana na utendaji mbovu ana nafasi kubwa ya kuwa mtendaji mzuri kwa vile anajua akiboronga yatamkumba yaliyompata aliyemtangua.

Mwisho,wabongo walioko huku “wanakupa tano” Mheshimiwa Kikwete na serikali yako huku wakitarajia kuwa dhamira yako ya kurudisha heshima ya nchi yetu itatimia.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI

Habarini za huko nyumbani.Naamini mambo yanakwenda vema.Hapa napo ni shwari tu japokuwa viama vyetu vya kawaida bado vinaendelea.Pengine utashtuka kusikia neno “viama” (umoja-kiama,wingi-viama).Ngoja niende moja kwa moja kwenye pointi.

Fikra nilizokuwa nazo wakati niko huko nyumbani,na ambazo nilikuwa nashea na jamaa zangu kibao,ni kwamba maisha ya Ughaibuni ni kama ya peponi:ardhi ya maziwa na asali,kama vitabu vya dini vinavyosema.Tabu ya kwanza niliyokutana nayo ni lugha.Si kwamba mie ni maimuna ambae lugha ya “kwa mama” haipandi.La hasha,lugha hiyo inapanda ki-sawasawa.Tatizo ni kwamba wakati nakuja hapa nilishazowea kuongea Kiswahili changu chenye lafidhi ya ki-Ndamba (ndio,mimi ni Mndamba kutoka Ifakara.Awije mlongo…).Uzuri wa Daresalama nilipokuwa naishi ni kwamba wewe ongea Kiswahili cha aina yoyote,lakini una hakika watu watakuelewa na mtasikilizana bila matatizo.Hapa “kwa mama” unaweza kwenda sehemu na ukawa unaongea kiingereza chenye lafidhi ya ulikotoka na watu wakaishia kukukodolea macho tu.Hawakuelewi unaongea nini.Unakwenda sehemu,unahitaji huduma fulani.Unamuuliza mhudumu hapo,anaonekana kutoelewa unachoongea.Anabaki kukuomba “sorry can you say that again?” (samahani,unaweza kurudia ulichokisema?).Basi hapo inabidi useme neno mojamoja tena taratibu ili muelewane.

Lakini tatizo la pili ni lile la kujisahau na kujikuta unaingiza maneno ya Kiswahili kwenye lugha yao,hasa pale mtu anapoonekana aidha hataki kukuelewa au ni mgumu wa kuelewa.Hebu fikiri,unakwenda dukani,unamwambia muuza duka “nipatie maji ya kunywa ya Kilimanjaro”,yeye anakuuliza “unasemaje anko?”,unarudia tena,na yeye anarudia kukuuliza unasemaje!Ikifika mara ya tatu kuna hatari ukataka kujaribu kumwelewesha muuzaji huyo kwa lugha ya kwenu.

Kama mawasiliano ni tatizo sugu basi kufanya shopping ni tatizo zaidi.Hili ni tatizo ambalo binafsi nakutana nalo takribani kila napoingia kwenye duka au supamaketi.Sijui tatizo ni hisia kwamba Mtanzania kama mimi sina uwezo wa kununua kitu dukani au vipi!Ile kuingia tu kwenye duka au supamaketi utakuta mlinzi anaanza kukuandama nyuma yako.Hofu ni kwamba labda utakwapua kitu na kuondoka nacho bila kulipa.Kichekesho ni kwamba wakati walinzi wa duka wanahangaika na wewe mtu mweusi,mateja ya kizungu yanatumia mwanya huo kukwapua vitu na kuchomoka navyo bila kulipa.Ndio,Ulaya kuna mateja kibao kama ilivyo huko kwetu.Ipo siku nitakupatia stori hiyo ya mateja wa Ulaya kwa kirefu.Mara nyingi utakuta hao wadokozi wanavizia mtu mweusi aingie dukani nao wakafanye vitu vyao kwa vile wanajua akili za walinzi zitakuwa kwako.

Kwenye mabasi nako wakati mwingine ni adha tupu.Utamkuta mtoto wa kizungu anakushangaa utadhani ameona muujiza flani.Kibaya zaidi ni pale mtoto huyo anapodiriki kumuuliza mama yake kama wewe ni mtu au sana mu.Si mchezo manake.Unaweza kutaka kurusha ngumi lakini ukikumbuka kilichokupeka Ughaibuni huko inabidi umezee tu.Watoto wengine waliolelewa ovyo huweza kudiriki kukugusa ngozi kisha kuangalia mikono yao kama imebakia na rangi nyeusi kwani kwao mtu lazima awe mweupe!

Haya wengi wenu mnaweza kuwa hamyajui si kwa sababu hayaripotiwi na BBC au Skynews bali ni kwa vile wengi wetu tulioko huku tukirudi nyumbani tunapenda kutoa stori nzuuri kuonyesha kuwa huku ni kuku kwa mirija tu,ardhi ya maziwa na asali,na kuficha viama tunavyokumbana navyo kila siku.

Hiyo ndio Ughaibuni,ndugu zanguni.Hata hivyo,naomba nisisitize kwamba viama hivyo havipo kila mji.Ile miji yenye wageni wengi au tuseme watu weusi wengi,kuna unafuu kidogo,japokuwa huko nako kuna viama kama vya umbeya,kusutana na hata kuagiziana mafundi (waganga wa kienyeji) kufanyiziana.Ukibisha kwamba watu wanaagiza wataalam kutoka huko nyumbani kuja kurekebisha mambo yao au kufanyiza kwa njia za asili basi nenda pale Buguruni kwa mwinjilisti flani ambae huja huku mara kwa mara kuhubiri neno la Bwana na kutoa pepo.Huyo ameshasikia maungamo na ushuhuda kadhaa wa hao waagizaji mafundi kutoka huko nyumbani.

Hadi wiki ijayo,Alamasiki

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.