Showing posts with label SERIKALI. Show all posts
Showing posts with label SERIKALI. Show all posts

13 Jul 2007

Asalam aleykum,

Baada ya matukio ya hivi karibuni yaliyotuweka matumbo moto kufuatiwa mahayawani flani kuamua kuendesha kampeni yao ya kishetani ya kutaka kulipua mabomu huko London na hapo Glasgow (Waskotishi bado hawaamini kuwa ugaidi umeingia kwenye ardhi yao) sio wazo baya kuanza makala hii kwa habari “nyepesi nyepesi.” Gazeti la Daily Mail la hapa liliripoti hivi karibuni kuhusu matokeo ya utafiti yaliyoonyesha kuwa wanaume wenye aibu wana nafasi kubwa ya kupata magonjwa ya moyo kuliko wale wasio na aibu!Hizi tafiti nyingine…we acha tu.Kwa mujibu wa gazeti hilo,utafiti huo ulifanyika kwa kipindi cha miaka 30 uliwahusisha maelfu ya wanaume ambapo watafiti kutoka chuo kikuu cha Northwestern cha Chicago,Marekani walipokuwa wanafanya ufuatiliaji wa wawaliowahoji kwenye utafiti huo walibaini kuwa asilimia 60 kati yao (waliohojiwa) walikuwa wameshafariki,huku chanzo kikuu cha vifo kikiwa “heart attack” (nadhani kwa Kiswahili sahihi ni msongo wa moyo).Mambo hayo!

Na ukisikia duniani kuna mambo usidhani ni utani.Mzembe mmoja amekamatwa huko New Hampshire (Manchester) baada ya kushindikana kwa jaribio lake la kutaka kufanya uporaji benki huku akiwa amejivika matawi ya miti kama “camouflage” (kificho) yake.Jamaa huyo,James Coldwell,aliingia kwenye tawi la benki ya ushirika ya Citizens,huku akiwa amejivika majani na kuwatisha wahudumu wa benki hiyo kabla ya kufanikiwa kuondoka na kitita cha fedha,lakini alinaswa na polisi muda mfupi baadaye kwani triki yake ya “uninja wa majani” haikumsaidia kwa vile majani hayo hayakufunika sura yake,na wanausalama waliweza kuitambua vizuri kwenye CCTV.

Jumuiya ya Ulaya (EU) nayo ilijikuta kwenye wakati mgumu hivi karibuni baada ya kutoa filamu fupi kwa ajili ya promosheni ya kuhamasisha Jumuiya hiyo ambapo wahusika kwenye filamu hiyo ya sekunde 44 yenye jina “Let’s Come Together” walikuwa wakifanya “ngono nyepesi” (soft porn).Wapinzani wa wazo la Muungano wa nchi za Ulaya waliishambulia EU kwa kupoteza fedha za walipa kodi kwa kutengeneza filamu hiyo waliyoiona kuwa ni mwendelezo wa ubabaishaji wa Jumuiya hiyo.Nilipomtumia rafiki yangu flani habari hiyo kutoka gazetini alitania kwa kusema labda na sie tunahitaji “kampeni chafu” kama hiyo ya EU “kuuza” wazo la Muungano wa Afrika Mashariki ambao unaelekea kuwakera wadau wengi.

Nae mwanamama Amy Beth Ballamura amaepigwa marufuku kutia mguu kwenye pwani yoyote ya Uingereza baada ya kufanya majaribio zaidi ya 50 ya kujiua kwa kurusha baharini.Miongoni mwa sababu zilizopelekea kuchukuliwa kwa hatua ya kumdibiti mwanamama huyo ni pamoja na kuzitia huduma ya uokoji (emergency services) gharama ya zaidi ya pauni milioni 1 (zaidi ya shilingi bilioni mbili za huko nyumbani) kila wanapoitwa kwenda kumuokoa.Lakini pamoja na “tamaa” yake ya kujitoa roho,askari mmoja aliambulia tuzo ya ushujaa mwaka 2003 baada ya kusikia kelele za kuomba msaada kutoka baharini na kuamua kujitosa majini kufuata kelele hizo,ambapo alifanikiwa kumuokoa mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 44.Cha kushangaza ni kwamba kama kweli alikuwa na nia ya kujitoa uhai sasa hizo kelele za kuomba msaada zilikuwa za nini?

Enewei,baada ya "nyepesi nyepesi" hizo (zote ni habari za kweli na wala sio kuwa “nawapiga fiksi” wasomaji wangu wapendwa) sasa tuangalie mambo ya muhimu zaidi huko nyumbani.Kwanza niseme siafikiani na hoja za Waziri wa Sheria Mama Nagu kwamba Bunge halipaswi kufanya kazi ya kupitia mikataba kabla ya kutiwa saini ili libaki na uhalali wake wa kuiwajibisha Serikali kwa mujibu wa dhamana ya mgawanyo wa mamlaka, kuchunguzana na kuwajibishana.Siafikiani naye kwa sababu hoja za baadhi ya wabunge kuwa mikataba hiyo ifikishwe kwao kabla ya kusainiwa zilizingatia ukweli kwamba kuna mapungufu makubwa yanayoendelea katika suala zima la kusaini mikataba mbalimbali.Mantiki nyepesi (simple logic) inaweza kutueleza kwamba maslahi ya nchi ni muhimu zaidi ya huo mgawanyiko wa madaraka.Hivi kwa mfano wazo la mikataba kuletwa bungeni lingekubaliwa,halafu nchi inufaike kwa kuingia mikataba yenye maslahi kwa Taifa,tatizo linakuwa wapi?Hivi kipi bora,kulinda mgawanyiko wa madaraka huku mikataba ya ajabu ajabu ikiendelea kuwepo au “kupindisha sheria” kwa kuileta mikataba hiyo bungeni kabla haijasainiwa halafu nchi ikanufaika nayo?

Pia nimesoma kwenye gazeti moja la huko nyumbani kwamba lile tishio la wafugaji huko wilayani Kilombero limerejea tena.Nitamke bayana kuwa hili linanihusu binafsi kwa vile mie ni “mwana wa pakaya” naetokea mitaa ya huko.Hawa wafugaji ni wakorofi,watovu wa nidhamu na wavunja sheria wakubwa.Maagizo kadhaa yameshatolewa kuwataka waheshimu sheria za nchi lakini wameamua kuweka pamba masikio.Mamlaka husika zinapaswa kuliangalia suala hili kwa makini zaidi kwani wanachofanya wafugaji hao sio tu kinahatarisha amani (mifugo yao inakula mazao ya wakulima,na hilo pekee linatosha kuzusha ugomvi) lakini pia hawawatakii mema wakulima kwani kwa kuswaga mifugo yao kwenye mashamba wanamaanisha kuwa wanataka wakulima hao wakose chakula na hela wanazojipatia kwa kuuza akiba ya mavuno yao.Hili ni bomu la wakati (time bomb) kwani japo hakuna bondia wa Kindamba (kama yupo basi samahani kwani sijamsikia) lakini hiyo haimaanishi kuwa mtu atakaeswaga mifugo yake kwenye mashamba ataachwa afanye anavyotaka.Hapo itakuwa kuchukua sheria mkononi,na japo mie ni mpinzani mkubwa wa kuchukua sheria mkononi,natambua dhahiri kuwa mtu “anapoletewa za kuleta” anaweza kabisa kuiweka sheria kando,hususan pale haki yake inapopuuzwa kwa makusudi.Kwa vile mkoa wa Morogoro umebahatika kuwa na RC ambaye ni “mjeshi” mstaafu basi hapana shaka Brigedia Jenerali Kalembo huyo atatumia “mbinu za medani” kuwadhibiti wafugaji hao wenye uhaba wa nidhamu.

Kikao cha Bunge kinaelekea ukingoni na miongoni mwa hoja nilizovutiwa nazo ni ile ya Mheshimiwa Shabiby (wa Gairo) kuhusu ujanja unaofanywa na baadhi ya wamiliki wa mabasi makubwa ya abiria.Alieleza kuwa mengi ya mabasi yanayotumika sasa yamefanyiwa “usanii” kwa kuweka mabodi mapya kwenye “chasis” na injini za malori au za kale.Kuna jina moja tu linalowafaa “wasanii” hawa nalo ni “WAUAJI.” Wanathamini sana kukwepa gharama za kununua mabasi mapya lakini hawajali hata chembe madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na vitendo vyao vya “kuunda mabasi feki.” Kwa upande mwingine tuseme bila kuonekana aibu kwamba mabasi ya namna hiyo yanafahamika hata bila kuwa na ujuzi wa umakanika kwani ulifika pale stendi ya mabasi Ubungo unaweza kukutana na basi ambalo linaonekana dhahiri kuwa bodi yake “imepachikwa” sehemu isiyostahili.Trafiki yeyote aliyehitimu mafunzo yake vyema na mwenye uchungu na maisha ya Watanzania wenzie hawezi kuliruhusu basi “lililovimba mbavuni utadhani lina ujauzito” liendelee na safari,na mabasi ya namna hiyo yako mengi tu.Wanaofanya hivyo wanajua bayana kuwa wanavunja sheria na kuhatarisha maisha ya abiria wao lakini hawajali kwa vile hakuna aliyechukuliwa sheria hadi leo.Si ajabu tukisikia kuwa baadhi ya mabasi hayo yanatumia injini za matrekta au hata za mashine za kusaga….(nashindwa kumalizia,nimekabwa na kicheko japo jambo hili sio la kuchekesha hata chembe.)

Mwisho,wakati Gavana wetu keshatamka bayana kuwa hatojiuzulu (utadhani alijichagua mwenyewe kwenye posti hiyo),sie wapenzi wa Simba tunajipoza kwa kusherehekea ubingwa wetu ambao kidogo umetibuliwa na hizi habari za viongozi kugombea mapato ya mechi huko Morogoro.Wito kwa watani wetu wa jadi Yanga ni huu:Micho akirudi (kama kweli atarudi) ashauriwe kukutana na Twalib Hilal apewe darasa kuwa ukocha sio sawa na ukatibu mwenezi wa klabu: ukocha ni vitendo vingi maneno machache lakini Mserbia Micho kila siku “anachonga” kuhusu hili au lile lakini matunda ya kazi yake kwenye dimba ni haba.Enewei,asilaumiwe sana kwani alishawahi kusema kuwa wachezaji wake hawafundishiki,na katika mechi ya juzi anaweza kuongeza sababu kuwa “lile tumbo la kuendesha” limechangia kukosa ushindi.

Alamsiki






22 Aug 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Naanza makala yangu kwa kuelezea majonzi makubwa niliyonayo kufuatia kifo cha mwanataaluma maarufu huko nyumbani,Profesa Seith Chachage.Majonzi yangu yanachangiwa na ukweli kwamba mimi ni miongoni mwa wanafunzi wake wa zamani hapo Mlimani.Mungu ndiye mtoaji na yeye ndiye mchukuaji kama Maandiko Matakatifu yanavyosema,lakini pengo aliloliacha msomi huyu aliyebobea ni vigumu kuzibika.Nimepitia tovuti mbalimbali na nimegundua kuwa marehemu alikuwa kipenzi cha wengi hasa wale wenye uchungu na Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.Kwa tuliomjua Profesa Chachage tutakumbuka jinsi alivyokuwa akichanganya usomi wake na kauli za utani.Yaani ilikuwa vigumu kuchoka kusikia mhadhara wake.Kwa tunavyowajua wasomi wetu ni nadra kumkuta mmoja wao akipenda vitu kama bongofleva,lakini nimesoma kwenye tovuti moja kwamba marehemu alikuwa anapenda muziki wa kizazi kipya na inasemekana aliweza hata kuimba verses za wimbo maarufu wa TID uitwao Zeze.Mungu ailaze ahali pema roho ya marehemu Profesa Chachage,Amen.

Alhamisi ya tarehe 13/06 mwaka nilisoma kwenye tovuti ya gazeti la Uhuru habari iliyonukuu Rais mstaafu Benjamin Mkapa akisema kwamba “katika baadhi ya mashirkika kama ATC serikali iliingia mikataba bila kuwa na tathmini halisi ya faida ambayo ingepata kwenye mashirika hayo.”Hizi si habari njema hasa ikizingatiwa kwamba serikali haitegemei wataalamu wa njozi kujua kama mkataba flani una manufaa au la bali inapaswa kuwatumia wataalam wake kuhakikisha kuwa kinachofanyika sio bahati nasibu ila ni kitu cha maslahi kwa Taifa.Tunaweza kutomlaumu Chifu MangungO alisaini mikataba feki na akina Karl Peters nyakati za ukoloni kwa sababu enzi hizo hakukuwa na wataalamu wa kupitia mikataba na kujua kama ina manufaa au la.Lakini zama hizi hali ni tofauti.Pale serikali inapoona kwamba jambo flani liko nje ya uwezo wake ina uwezo wa kutafuta na kupata uhakiki flani kutoka nje ya nchi.Yaani hapo namaanisha kwamba yapo makampuni kadhaa ya kimataifa ambayo yanaweza kutoa huduma ya ushauri kwa serikali iwapo itaonekana kwamba wataalam wetu wa ndani wameshindwa kazi hiyo.Hivi inawezekanaje mtu akaingia mkataba bila kujua faida yhalisi ya mkataba huo?Utapangishaje nyumba yako kama huna hakika kuwa kwa kufanya hivyo wewe mwenyewe au familia yako mnaweza kuishia kulala gesti hausi?Na je inapobainika kwamba kuna tu flani,kwa sababu anazozijua yeye,alisaini mkataba usio na faida kwa Taifa,tunafanyaje?Suala hapa sio kunyooshena vidole bali ni kuhakikisha kuwa makosa ya aina hiyo hayajirudii.Na njia nyepesi ya kufanya hivyo ni kuwachukulia hatua wale waliofanya makosa hayo-iwe walifanya kwa makusudi,uzembe au kutojali maslahi ya nchi yetu.

Nilishawahi kuandika huko nyuma kwamba kuna watu hawana uchungu na Taifa letu,na hawa ni pamoja na hao wanaosaini mikataba kama ile ya Chifu Mangungu utadhani wakati wanasaini mikataba hiyo walikuwa bwii(wamelewa) au wamesainishwa wakiwa usingizini.Marehemu Chachage na baadhi ya wasomi wengine wa nchi hii walijikuta wakitengeneza maadui kila walipojitahidi kukemea mambo yanayoendana kinyume na maslahi ya Taifa.Kuna watu hawapendi kuambiwa ukweli hata pale wanapoharibu na si ajabu makala hii ikapata upinzani wao.Lakini hiyo haitatuzuwia sie wenye uchungu na nchi yetu kusema yale yanayotupeleka pabaya.

Nimesikia kuna kampuni ya Kisauzi Afrika imepewa haki za utafutaji mafuta huko nyumbani.Pia kuna tetesi kwamba nchi yetu ina utajiri wa Uranium.Mungu akitujalia,siku moja na sisi tutakuwa na sauti kwenye siasa za kimataifa kwa vile mafuta ni silaha,ukiwa nayo lazima utaheshimika.Lakini bila mipango madhubuti utajiri hio unaweza kuwa kama laana kwa Taifa kama letu lililozowea amani.Huko Nigeria kumekuwa na matukio kadhaa ya vurugu ambazo kimsingi zinatokana na ukweli kwamba wenye ardhi (wananchi) wanaishia kuona tu mabomba ya mafuta na magari ya thamani kwa wale wanaowatumikia wenye makampuni ya mafuta ya kutoka nje,huku walalahoi wakizidi kuwa masikini.Mwanafalsafa Karl Marx aliwahi kusema kuwa masikini hana cha kupoteza anapoamua kupigania haki yake.Watu hawawezi kuendelea kuwa kimya wakati utajiri wao wa asili kwenye nchi yao unawanufaisha wachache kutoka nje na wapambe wao wanaosaini mikataba hewa.

Naomba ieleweke kwamba sizilaumu serikali za awamu zilizotangulia kuwa mikataba yote zilizoingia ilikuwa bomu.Kilio changu hapa ni kwenye hiyo mikataba ya iliyosainiwa ndotoni.Nafahamu kwamba wataalamu wazalendo wanatoa ushauri mzuri tu kabla ya mikataba kusainiwa lakini tatizo linakuja pale maslahi binafsi yanapowekwa mbele ya maslahi ya Taifa.Kwa kuwa mtu ana mamlaka ya kupuuza ushauri wa kitaalamu basi anatumia fursa hiyo kujifanya madudu kana kwamba madhara ya anachokifanya hayatamgusa kwa namna flani.

Naamini serikali ya Awamu ya Nne haitawalea wazembe wanaotaka kutulostisha.Narudia kusema kwamba sisi sio masikini wa namna tulivyo kwa sababu tuna raslimali za kutosha ambazo zinaweza kabisa kutuweka pazuri.Tunachopaswa kuelewa ni kwamba miaka 25 au 50 ijayo vizazi vya wakati huo vinaweza kutushangaa sana pale vitakapokuta kila kitu kimeuzwa na faida ya mauzo hayo haionekani.Inaweza kuwa vigumu sana kwa walimu wa somo la Historia wa wakati huo kuwaelewesha wanafunzi wao kuwa tofauti na mikataba feki ya kina Karl Peters na baadhi ya machifu wetu,mikataba iliyobomoa nchi yao ilifanywa na Watanzania haikuwa ya kilaghai bali ni sababu ya kitu kidogo (sijui wakati huo watakuwa wanatumia msamiati gani kumaanisha rushwa),

Alamsiki

18 Jun 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa gazeti hili.

Leo tuzungumzie muziki.Muda mfupi uliopita nilikuwa nasoma makala flani kumhusu msanii wa kizazi kipya Albert Mangwea.Yalikuwa ni mahojiano kati ya msaanii huyo na tovuti ya Darhotwire.com.Niliguswa sana na kilio cha msanii huyo ambacho kimekuwa pia kikisikika kutoka kwa takribani kila msanii wa Bongofleva.Kuna wajanja flani,(hapana,hawa si wajanja,bali ni WEZI) ambao wamekuwa wakiwanyonya vijana wetu bila hata chembe ya huruma.Wezi hawa wanafahamika zaidi kwa jina la “wadosi”.Binafsi sijui kwanini wanaitwa wadosi lakini la muhimu hawa sio jina wanaloitwa bali unyonyaji wanaowafanyia wasanii wetu.

Pengine kabla ya kujadili wizi wa mchana mweupe unaofanywa na wadosi hao,tuangalie maendeleo ya Bongofleva huko nyumbani na huku Ughaibuni.Mimi ni mfuatiliaji sana wa mambo yanayotokea huko Bongo. “Ibada” yangu ya kila asubuhi inaanza kwa kutembelea tovuti za ki-Tanzania ili kujua yanayojiri huko.Sasa,kabla ya kuja huko mwaka jana mwishoni mwa mwaka jana nilikuwa nahisi kuwa habari kwamba Bongofleva imeikamata Tanzania kwa “kasi ya tsunami” ni porojo tu.Lakini nilipokuja nilishihudia mwenyewe jinsi gani hatimaye nyimbo zinazotengenezwa na kuimbwa na Watanzania zilivyokamata soko na mioyo ya wapenzi wa muziki.Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu nilibahatika kushuhudia tamasha la “Piga Kura au Upigike” kwenye viwanja vya Biafra Kinondoni.Licha ya picha kadhaa nilizochukua kwa ajili ya kuwajulisha marafiki zangu hapa,nilijionea jinsi gani watu wa rika mbalimbali wanavyovutiwa na kazi za wasanii wa muziki wa kizazi kipya.Nadiriki kuamini kuwa mashabiki waliofika viwanja hivyo walikuwa wanawakilisha karibu kila kona ya jiji la Dar es Salaam.Kitu kingine nilichobaini ni kwamba jinsi gani wasanii wanavyotumika katika masuala ya muhiu kwa Taifa.

Nakumbuka niliwahi kusoma katika gazeti moja la huko nyumbani kwamba msanii Juma Nature “alimfunika” mwenyeji wake-mgombea aliyemwalika msanii huyo katika kampeni zake.Yaani watu walikuwa na kiu zaidi ya kusikia muziki wa Nature kuliko hotuba ya mheshimiwa huyo.Na pengine umati kubwa uliojitokeza kwenye mkutano huo ulifuata buridani hiyo ya bure.Yayumkinika kusema kuwa mchango wa wasanii katika kufanikisha uchaguzi,na hata kuwapatia ushindi baadhi ya wagombea,ulikuwa mkubwa.Kwa bahati mbaya,au pengine kwa makusudi,baada ya kukamilisha kazi ya kuhamasisha jamii kuhusu uchaguzi na wagombea,wasanii wetu wamerudi kulekule walikokuwa:wamesahauliwa na wanaendelea kunyonywa.

Napenda kuwafumbua macho wasanii wetu kwa kuwaambia kuwa muziki wao huku guhaibuni unauzika sana miongoni mwa watu waliotoka Afrika Mashariki.Wamuulize Banana Zorro aliyealikwa hapo London kwenye pati ya Muungano,wamuulize Mr Nice,Ray C na TID,na Profesa J ambaye nasikia amewachengua vilivyo huko Sweden na Holland.Wasanii wa nyumbani wakija huku wanababaikiwa kama vile akina Shaggy au Sean Paul wanavyobabaikiwa wakija huko nyumbani.Lakini,safari za nje sio jambo la kukurupuka tu,ni kitu kinachotaka maandalizi.Kwa mantiki hiyo si lazima kusafiri ili kunufaika na kazi za sanaa bali hata kutafuta namna ya kupenyeza muziki katika soko la kimataifa kunaweza sana kuwainua wasanii wetu.Hivi wasanii wetu wanajua kuwa CD zao huku zinauzwa hadi paundi 10 (zaidi ya shs 24,000/=)?Nimesoma kwenye internet kwamba tarehe 12/06/2006 kampuni moja iitwayo Townsend Records itatoa CD iitwayo Bongoflava (Swahili Rap from Tanzania) ambayo itauzwa paundi 10.99 (takriban shs 27,000/= kwa exchange rate za leo).Sijui kama na hawa ni wadosi au la,lakini huo ni uthibitisho kuwa Bongoflava ina soko zuri tu kuhu Ughaibuni.Na watu wanapenda kweli kazi za wasanii wa nyumbani.Niliporudi kutoka Tanzania jamaa zangu kibao walikuwa wananiulizia kama nimekuja na CD za Bongofleva.Kila mmoja anasema wanaposikia wasanii wetu wanakumbuka sana nyumbani.

Mheshimiwa Kikwete alinukuliwa akiwataka Watanzania walioko nje kuwasaidia wenzao walio nyumbani hasa katika nafasi za masomo.Ujumbe huo unaweza pia kupanuliwa na kuwahusisha wasanii wa nyumbani,kwa maana kuwa Watanzania walio nje hasa wale wenye upeo na mambo ya muziki wawasaidie wasanii wetu wa nyumbani kwa namna yoyote ile inayowezekana.Lakini ili hilo liwezekane wasanii wetu hawana budi “kuchangamka.”Wanaoitwa “wadosi” wanawanyonya na kuwaibia kwa vile wanajua dhahiri kuwa wasanii hao hawana njia mbadala.Jamani,dunia siku hizi imekuwa kama kijiji (japo ni kinadharia) na unachohitaji ni kwenda tu kwenye internet cafĂ© na kuperuza kurasa za mtandao kujua wapi unaweza kupata huduma au kuuza ulichonacho kwa mtu aliye bara jingine.Hapa ndipo umuhimu wa shule (elimu) unapojidhihirisha.Lakini hata kama shule haipandi,si unaweza kumwomba rafiki yako akusaidie kutafuta soko la kazi zako za sanaa nje ya nchi?

Serikali inapaswa kuwasaidia wasanii wetu kwa kuipa meno sheria ya hatimiliki.Sambamba na hilo ni wasanii wenyewe kusimama kidete kutetea maslahi yao badala ya kuendelea kulalamika au kufikiria kuingia kwenye fani nyingine kukwepa wizi wa kazi zao.Pia wasione aibu kuomba msaada kwa wenzao walio nje.Mwisho naiomba serikali ipanue vita dhidi ya wala rushwa na majambazi na kujumuisha “wadosi” pia.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Leo tuzungumize michezo,hususan soka.Kwa takriban wiki nzima sasa habari ya soka iliyotawala katika vyombo vya habari vya hapa Uingereza ni kuhusu suala la mchezaji mahiri wa klabu ya Manchester United na timu ya Taifa,Wayne Rooney.Ishu yenyewe ni kwamba ilidaiwa kuwa Rooney alikuwa na madeni yanayofikia pauni 700,000 (takribani shilingi milioni 140 za huko nyumbani) aliyokuwa akidaiwa na makampuni ya kamari (betting).Inasemekana tayari amemalizana na wadai wake.Wapo waliomlaumu mchezaji huyo kwa kutumia vibaya fedha zake,lakini wengine wamemtetea kwamba haikuwa ubaya kutumia kipato chake kinachotokana na ajira yake.

Ndio,soka huku Ughaibuni na hata katika baadhi ya nchi za huko Afrika ni ajira.Ni ajira ambayo inamwezesha mtu kama Rooney kutumbukiza zaidi ya shilingi milioni 100 kwenye kamari.Pointi yangu sio uhusiano wa soka na kamari bali soka kama ajira.Tukirudi huko nyumbani,siku chache zilizopita klabu kongwe za Simba na Yanga zilichimba mkwara kuwa zingesusia ligi kuu ya Bara iwapo mgao wa mapato ungeendelea kuwanufaisha zaidi wengine badala ya wao wanaovuja jasho dakika 90.Binafsi niliguswa sana na hoja za klabu hizo japokuwa kwa bahati mbaya nasikia wakongwe hao wamenywea katika kutimiza azma yao ya kutaka “kieleweke.”Sijui kuufyata huko ni kwa vile viongozi wa klabu hizo walitoa hoja hiyo kama kutingisha kiberiti,au sijui ni ubabe wa vyama vyetu vya michezo huko nyumbani!Lakini naamini klabu hizo zilikuwa na hoja ya msingi kabisa.

Pambano lao la mwisho liliingiza milioni 98 kama sijakosea.Lakini kila klabu ikaambulia shilingi milioni 23.6 tu.Kwa kweli huo ni sawa na uonevu.Mapato hayo yalitokana na umaarufu wa klabu hizo,hivyo zenyewe ndio zilipaswa kunufaika zaidi na mapato hayo.Nadhani klabu hizo zilistahili kupata kiwango kikubwa zaidi ya hicho hasa ikizingatiwa kuwa timu hizo kwa sasa ni kama za kulipwa kutokana na kuwa na wachezaji kadhaa wa kigeni ambao mishahara yao ni ya juu.Jitihada za kuzigeuza klabu hizo kuwa kampuni zimekuwa zikikwama mara kwa mara.Kwa hiyo tofauti na klabu kubwa za huku Ughaibuni ambazo zinaendeshwa kwa mfumo wa kampuni hivyo kutotegemea sana mapato ya uwanjani,chanzo kikuu cha mapato kwa vilabu vyetu vya nyumbani ni mapato yanayotokana na watu wanaoingia uwanjani kushuhudia mechi zao.

Imenisikitisha sana kuona hoja ya klabu hizo imekufa kienyeji.Lakini sikushangaa sana kwa vile sio siri kwamba vilabu vyetu huko nyumbani vinaendeshwa kwa ubabaishaji sana.Kwanza kwa Simba na Yanga hawapaswi kutegemea mapato ya uwanjani kama chanzo pekee cha mapato.Japo hoja ya klabu hizo kugeuzwa kuwa kampuni bado ni ya muhimu sana ingawaje wenyewe wanapuuzia,vipo vyanzo vingine kadhaa vya mapato ambavyo vimetelekezwa.Kwa mfano,kwa kutengeneza kalenda 100,000 zenye picha za wachezaji ambazo zingekuwa katika ubora unaostahili na kuziuza angalau kwa shilingi 500 kila moja,klabu ingejiingizia shilingi milioni 50.Hilo linawezekana kabisa hasa kwa vile gharama za utengenezaji wa kalenda sio kubwa sana na kuna uwezekano wa kupatikana wadhamini wa kugharamia mradi wa aina hiyo.
Kwa mtizamo wangu,watu wanaopaswa kubeba lawama zaidi katika suala zima la ubabaishaji kwenye vilabu vyetu ni hao wanaoitwa wanachama.Hao ndio wanaochagua viongozi wabovu,na ni haohao ambao hawakawii kwenda mahakamani kupinga uongozi ambao wao wenyewe waliuweka madarakani.Wanang’ang’ania kujiita wanachama wakati mchango wao mkubwa katika kuendesha klabu hizo ni kwenda kwenye vyombo vya habari kutaka uongozi wa klabu ujiuzulu,au kocha hafai au wakati mwingine kusema lolote tu ili wasikike hewani.Kama kweli wanachama wa Simba na Yanga wangekuwa wenye mwamko unaostahili basi naamini wangetumia nguvu za wingi wao kuhakikisha hoja zilizotolewa na viongozi wao kuetetea maslahi ya klabu hizo zinashinda.Badala ya hoja hizo kuonekana ni ajenda binafsi za Wambura au Kifukwe zingekuwa ni hoja za klabu na wanachama wa Simba na Yanga.

Kulalamika bila kutoa ufumbuzi wa tatizo ni sawa na kulikuza tatizo.Kwa hiyo,nawajibika kutoa mchango wangu katika kupata ufumbuzi.Nadhani Tenga na wenzie wa TFF wanapaswa kuliangalia upya suala la mgao wa mapato kwa klabu,na sio kwa Simba na Yanga pekee bali vilabu vyote.Vilabu vina haki ya kudai ziada ya wanachokipata kutokana na jitihada zo uwanjani.Kuhusu uendeshaji wa vilabu,Serikali inapaswa kuingilia kati kwa kutengeneza sera ambayo haitotota fursa ya uababishaji,iwe wa viongozi au wanachama.

Alamsiki.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.