Showing posts with label IFAKARA. Show all posts
Showing posts with label IFAKARA. Show all posts

26 Dec 2007

MAKALA HII ILIPASWA KUTOKA KATIKA TOLEO LA WIKI HII LA GAZETI LA RAIA MWEMA LAKINI HAIKUTOKA KWA SABABU ZILIZO NJE YA UWEZO WANGU.

Majuzi niliongea kwa simu na rafiki zangu wawili wa siku nyingi.Mmoja ni “mjasiriamali” anayeishi Dar es Salaam (hakasiriki ninapomtania kwamba yeye ni “misheni tauni”).Mwingine yuko Ifakara,mji niliozaliwa.Niliongea na rafiki zangu hawa kuwatakia heri na Baraka za mwaka mpya 2008.

Nikiri kwamba mara nyingi huwa namkwepa rafiki yangu wa Ifakara kutokana na mlolongo wa malalamiko anayokuwa nayo kila ninapoongea naye.Na majuzi haikuwa tofauti.Alidai mwaka mpya hauna maana yoyote kwake kwani,kwanza,kinachobadilika ni tarakimu moja tu ya mwisho katika mwaka,yaani badala ya 7 inakuwa 8.Pili,alidai kwamba jitihada zake za zamani za kujiwekea malengo ya mwaka mpya yamekuwa kazi bure kutokana na kile anachokiita “nguvu za giza”,na katika miaka ya hivi karibuni amesitisha utaratibu huo wa kujiwekea malengo ya mwaka ujao.Alinifafanulia kwamba “nguvu za giza” anazozizungumzia sio zile zinazotajwa katika Biblia bali genge la mafisadi ambao wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha mwaka mpya unaendelea kuwa mchungu kama uliotangulia.

Huyu bwana alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliobahatika kuendelea na masomo baada ya kuhitimu shule ya msingi.Pia licha ya kuyapenda masomo ya sayansi,alikuwa anayamudu kweli.Na uthibitisho katika hilo ni namna alivyopata pasi za juu katika Fizikia na Hisabati wakati mie niliondoka na “F” na “D” katika masomo hayo,na hatimaye nikaamua kukimbilia kwenye mchepuo wa masomo ya “Arts”.Ndoto yake ya kuwa rubani ilifikia ukingoni baada ya kumaliza kidato cha nne na kukosa nafasi ya kuendelea na masomo.Kibaya zaidi,wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumpeleka shule ya kulipia.Hata hivyo,alichaguliwa kujiunga na chuo cha ualimu kabla ya kuajiriwa kufundisha shule moja ya msingi katika kijiji flani tarafani Ifakara.

Nakumbuka alivyolalamika siku ya kwanza alipotia mguu kwenye kituo chake “kipya” cha kazi.Alikumbana na lundo la wanafunzi wanaobanana kwenye madarasa ambayo majengo yake yanaombea kusiwe na upepo wa nguvu kwani utaezua paa.Madawati ni machache,uhaba wa vitabu vya kufundishia ni mkubwa na nyumba ya mwalimu mkuu ni kichekesho.Alinitania kwamba ni rahisi kwake kupata mwaliko wa kuitembelea Ikulu kuliko kukaribishwa na “hediticha” wake,sababu ni kwamba makazi ya mkuu huyo wa shule ni duni kupindukia.Mbinde nyingine ni mwisho wa mwezi ambapo rafiki yangu huyu anadai inamlazimu afanye dua mfululizo ili mshahara wake upatikane katika muda mwafaka.

Kama muumini wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea,licha ya majukumu yake ya ualimu,ndugu yangu huyu alikuwa akijishughulisha na kilimo.Huko nako ni matatizo kama shuleni kwake.Anadai kwamba sasa amesitisha masuala ya kilimo kwani anadhani anakineemesha zaidi chama cha ushirika kuliko yeye binafsi.Alinichekesha alipodai kuwa laiti angeendelea na kilimo na kuzidi kukikopesha chama cha ushirika,basi kuna uwezekano angeishia jela baada ya kumtwanga afisa yoyote wa chama cha ushirika ambaye kila kukicha anakuja na hadithi mpya kuhusu malipo ya mazao yaliyonunuliwa kwa mkopo.

Tumrejee yule “mjasiriamali” wa jijini Dar.Huyu anatoka kwenye familia inayojiweza na ni miongoni mwa watu wasioamini kabisa kwamba elimu ni ufunguo wa maisha.Aliacha shule alipokuwa kidato cha pili,lakini ana vyeti vinavyoonyesha taaluma mbalimbali.Baba yake alimfanyia mpango wa kazi kwenye taasisi flani ambayo licha ya kuwajali watumishi wake kwa mshahara mkubwa,inasifika sana kwa rushwa.Aliwahi kuninong’oneza kwamba alipata kazi hiyo bila kufanyiwa usahili kwani baba yake na Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa taasisi hiyo ni marafiki.

Kama rafiki yangu mwalimu alivyoamua kuacha kujishughulisha na kilimo kwa kuhofia kumng’oa mtu meno kutokana na fedha anazokidai chama cha ushirika,huyu “mjasiriamali” aliamua kuacha kazi kwa kuhofia kwenda jela pindi TAKUKURU wangejaliwa uwezo wa kunasa wala rushwa wakubwa.Baada ya kuacha kazi,sasa anaendesha kampuni binafsi “inayojihusisha na kila kitu”.Anajigamba kwamba anaweza kumpatia mteja huduma yoyote anayohitaji:iwe ni kushinda tenda bila kushiriki zabuni,kutoa mzigo bandarini kwa bei poa,kupata hati ya kiwanja isivyostahili,kuzungumza na hakimu ili kesi ifutwe,na hata kuwezesha kupatikana kwa cheti feki kinachoonyesha mteja wake hana ukimwi japo hajapima.

“Mjasiriamali” huyu anadai kwamba huduma pekee asiyoweza kutoa ni kurejesha uhai wa mtu aliyefariki,na haoni kufuru kudai kuwa hilo lingewezekana laiti Mungu angekuwa anaishi Tanzania.Wakati huwa nachoshwa na malalamiko ya rafiki yangu mwalimu,huyu mjasiriamali wangu huwa “ananiboa” na majigambo yake.Kikubwa nachonufaika kwa kuongea nae ni kupata “first-hand account” ya mtu anayeshirikiana na mafisadi kukwamisha uwezekano wowote wa ndoto ya maisha bora kwa kila Mtanzania kutimia.

“Mjasiriamali” huyu ana marafiki sehemu mbalimbali duniani,wengi wao wakiwa aidha walishawahi kuja kuchuma huko nyumbani au wanadhamiria kufanya hivyo.Wengi wa wawekezaji hao ni wale wa muda mfupi,wanaanzisha mradi na kupewa zawadi ya likizo ya kodi (tax holiday),na wakishapata faida ya kutosha wanaingia mitini.Rafiki yangu huyo ananieleza kwamba tofauti na zamani,siku hizi “wazungu” wanajua “kupenyeza rupia kwenye udhia hasa kwa vile hapo kwenye udhia kuna wanaobembeleza kupenyeshewa rupia”.Na hapo ndipo “mjasiriamali” huyu anapotengeneza ulaji wake kwa kuwaunganisha “wenye rupia” na “wanaohitaji rupia” kupindisha taratibu na sheria.

Rafiki yangu mwalimu na huyu mjasiriamali “feki” wanawakilisha picha mbili tofauti zinazoendelea kushamiri huko nyumbani.Kundi dogo la watu linaishi kwa jasho la wenzao linaendelea kuneemeka kwa kukumbatia rushwa,kuuza raslimali zetu na kupinga kwa nguvu manung’uniko yoyote kuhusu ugumu wa maisha.Kwa upande mwingine ni kundi kubwa la watu ambao liwazo lao pekee la kumaliza mwaka na kukaribisha mwaka mpya ni wao kuwa hai.Hawa ni watu ambao wanahitaji kweli baraka za mwaka mpya kwani wanaishi kwa hofu ya kupata ulemavu au kupoteza maisha kwenye hospitali ambazo badala ya kutibiwa miguu wanaweza kupasuliwa vichwa,wanapanda mabasi yenye kutumia chesis za malori na pengine injini za mashine za kusaga unga,wanaweza kubambikiziwa kesi na polisi kwa makosa wasiyofanya,wanaweza kufika kazini na kuambiwa ajira yao imefariki ghafla baada ya mwajiri wa kigeni kuamua kurejea kwao,pamoja na matatizo mengine kedekede.

Rafiki zangu hawa wawili wana mtizamo tofauti kuhusu kauli ya Waziri Ngasongwa kwamba uchumi unakua.Huyo mwalimu,ambaye mara kwa mara jina la Ngasongwa halimtoki mdomoni kwa vile ni Mpogoro mwenzake,anadai inawezekana kukua kwa uchumi kunakozungumziwa ni kwa kuongezeka idadi magari ya kisasa na ya “bei mbaya” pamoja mfumuko wa mahekalu jijini Dar es Salaam.Anatamani neema hiyo ingekuwa hivyohivyo kwenye elimu,afya,kilimo,miundombinu na huduma nyingine muhimu. “Mjasiriamali” anamuunga mkono Ngasongwa na kudai kwamba uthibitisho wa kukua kwa uchumi ni yeye “drop-out” wa kidato cha pili ambaye anamiliki gari lenye thamani ya mamilioni ya shilingi,ana hekalu huko Masaki na anamudu kuwa na nyumba ndogo takriban katika kata ya jiji.Kwa yeye kila siku ni mwaka mpya,na anadhani siku mambo yatapokwenda mrama atakimbilia nje ya nchi na kutangaza kustaafu ujasiriamali wake akiwa huko.





18 Jun 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Hivi umeshawahi kuulizwa swali moja zaidi ya mara mia na kila unapoulizwa hujiskii kulizowea swali hilo?Pengine imeshakutokea.Mimi imekuwa ikinitokea mara nyingi zaidi ya ninavyoweza kukumbuka.Ilianza nikiwa huko nyumbani.Kabila langu ni Mndamba,natokea Ifakara mkoani Morogoro.Sio siri kuwa Wandamba sio kabila maarufu ukilinganisha na makabila mengine ya mkoa naotoka,kwa mfano Waluguru au Wapogoro.Kwa hiyo kila nilipokuwa naulizwa “hivi wewe ni kabila gani” na mimi kujibu “mie Mndamba” mara nyingi swali lililofuata ni “hivi Wandamba wanatoka mkoa gani?”Au wakati mwingine nilipoulizwa mkoa naotoka na kujibu Morogoro,wengi walipenda kudhani mimi ni Mluguru.Niliposema hapana,wangeniuliza iwapo ni Mpogoro.Sikuwalaumu kwa vile mara nyingi jina la mkoa unaotoka huwa linahusishwa na kabila kubwa au maarufu katika mkoa huo.Ukisema unatoka Mwanza,watu watahisi wewe ni Msukuma,ukitoka Songea watu watahisi wewe Mngoni,au Tabora watahisi wewe Mnyamwezi,na kadhalika.

Nilipokuja huku Ughaibuni swali likageuka kuwa “wewe unatoka nchi gani?”Mara nyingi napojibu “natoka Tanzania” swali linalofuata ni “hivi Tanzania iko wapi?”Wengine wanajua iko Afrika lakini hawana uhakika ni sehemu gani katika bara hiko lenye nchi zaidi ya hamsini.Kuna wakati huwa nawalaumu wanaoniuliza swali hilo kwamba hawakuwa makini kwenye somo la Jiografia,lakini yayumkinika kusema kuwa hata kama ulipata A kwenye somo hilo sio rahisi kujua kila nchi ilipo kwenye ramani ya dunia,kama isivyo rahisi kwa kila Mtanzania kujua Wandamba wanatoka mkoa gani.Hata hivyo,kila napoulizwa ilipo Tanzania,huwa natumia fursa hiyo kufanya kazi ya wenzetu tuliowapa majukumu ya kuitangaza nchi yetu kwa kueleza kuwa nchi hiyo “iko kusini mwa Kenya na Uganda,mashariki ya DRC,Rwanda na Burundi…”,na kadhalika.Wakti mwingine natumia vivutio vyetu kujibu swali hilo,yaani nasema kuwa “Tanzania ndipo ulipo Mlima Kilimanjaro,au Ziwa Victoria,au Mbuga ya Selous…”

Wakati sote tunajua kuwa ni vigumu kwa kabila Fulani kufanya kampeni ya kujitangaza (na jitihada kama hizo zikifanyika utaambiwa unaleta ukabila) kila nchi ina jukumu la kujitangaza yenyewe.Inauma ninapoangalia kwenye runinga na kuona matangazo kama hili hapa: “mtoto huyu anahitaji sana msaada wako…anapenda kujiendeleza na elimu lakini anatoka Tanzania,moja ya nchi masikini sana duniani…kwa kutoa paundi tatu kwa mwezi unaweza kuwasaidia watoto kama huyu…”Yaani nchi yetu inapata nafasi ya kusikika lakini sio kwa sifa nzuri bali umasikini wake.Na huwezi kuwalaumu wanaotoa matangazo ya aina hiyo kwa kuwa wanafanya hivyo kwa nia nzuri,na sio jukumu lao kuitangaza nchi yetu kwa mtizamo wa kuvutia watalii au vivutio vilivyopo huko.Hiyo ni kazi ya Watanzania wenyewe.

Naamini kuna watu wana majukumu ya kuitangaza nchi yetu.Hebu nikupe mfano.Uganda inadhamini kipindi Fulani kwenye kituo cha televisheni cha CNN International cha Marekani.Zambia nao wanatoa matangazo ya kuitangaza nchi yao kwenye kituo hicho na kuwakaribisha wageni waende kushuhudia Maporomoko ya Victoria.Hata Malawi,Rwanda na Burundi nao hawako nyuma,kwani nimeshaona matangazo yao kwenye gazeti maarufu duniani la TIME.Lakini sie tuko nyuma katika eneo hili.Pengine kuna watu wanaona sio muhimu kujitangaza kwa vigezo kwamba “chema chajiuza kibaya chajitembeza.”Tunachopaswa kufahamu ni kwamba katika zama hizi za ushindani wa kuvutia watalii (na hata wawekezaji wa kweli) ni muhimu sana kuitangaza nchi yako.Ukitaka kuhakikisha nayosema sio utani ingia kwenye internet na tafuta habari kuhusu vivutio vilivyopo nchini kwetu.Ni dhahiri utagundua kuwa taarifa zilizopo ni chache,na hata hizo chache hazijitoshelezi,na mara nyingi huwa zimewekwa na wasio Watanzania.Kuna watu wengi wanaoamini kuwa Mlima Kilimanjaro uko Kenya kwa vile nchi hiyo imekuwa ikiutangaza Mlima huo kama uko kwake,na sie tumekaa kimya.Ukienda kwenye tovuti ya Bodi ya Biashara za Nje (BET) wao wanaonekana wako bize zaidi na Maonyesho ya Sabasaba.Nilipotembelea tovuti yao leo ilikuwa inasema iko kwenye matengenezo lakini inakupeleka kwenye kiungo (link) ya Maonyesho ya 30 ya Kimataifa ya Dar Es Salaam (DITF),pengine kuonyesha kuwa Maonyesho hayo (ambayo ni ya mara moja tu kwa mwaka) ni muhimu zaidi kwao kuliko kuitangaza nchi yetukila siku.Angalau Bodi ya Utalii wamejitahidi kiasi japokuwa tovuti yao haina habari za kutosha kuhusu vivutio tulivyonavyo.Tuna Kituo cha Biashara (Tanzania Trade Centre) hapa Uingereza,lakini tovuti yake ni kama imeandaliwa haraka haraka kwa vile taarifa zilizopo humo sio za kutosha sana.Wahusika wasikasirike kusoma haya nayoandika kwa sababu tumewakabidhi dhamana ya kuitangaza nchi yetu.Badala ya kuchukia kukosolewa wanapaswa waone hii kuwa ni changamoto kwao.

Kilio changu kingine ni kukosekana kwa AIR TANZANIA ya Watanzania.Kama wenzetu Kenya wameweza kwanini sisi tushindwe?Angalia Wahabeshi wa Ethiopia wanavyoweza kuchuana na mashirika makubwa ya ndege duniani na kujiingizia mapato makubwa kupitia sekta ya usafiri wa anga na Ethiopian Airlines yao.Kwa kurusha Air Tanzania “the Wings of Kilimanjaro” tulikuwa tunaitangaza nchi yetu na wakati huohuo kuujulisha ulimwengu kuwa Mlima Kilimajaro uko kwetu.Tuna vivutio vingine vingi vya kuvitangaza huku nje ikiwa ni pamoja na moja ya hifadhi kubwa kabisa duniani,Selous,na ziwa la pili kwa ukubwa duniani,Victoria.

Tukubali kwamba hatujajitahidi vya kutosha na tusisubiri kuulizwa.Hatuna sababu ya msingi ya kuwa hapa tulipo,na kwa kuwa tunatambua kuwa hatujitendei haki sie wenyewe kwa kung’ang’ania kuwa katika nafasi isiyo yetu ni lazima tuchakarike sasa.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI

Asalam aleykum.

Hapa Uingereza kuna chama cha siasa kinachoitwa British National Party au kwa kifupi BNP.Hiki ni chama kinachofuata siasa za mrengo wa kulia kabisa,far right kwa “lugha ya mama.”Siasa za namna hiyo ndio zilizokuwa zinahusudiwa na Manazi chini ya Hitler na Mafashisti chini ya Mussolini.Hawa jamaa wa BNP ni wabaguzi waliokithiri.Majuzi wakati wa uchaguzi mdogo huko England mmoja wa watu muhimu katika BNP,Dokta Phill Edwards (jina lake halisi ni Stuart Russell) alizua mjadala mkubwa kuhusu siasa za chama hicho pale alipotoa matamshi ya kuchefua dhidi ya watu weusi.Alirekodiwa kwa siri na kituo cha televisheni cha Sky akisema kuwa watu weusi wana IQ (uwezo wa akili) ndogo,na watoto weusi wakikua sanasana wataishia kukaba watu (vibaka au majambazi).Aliendelea kusema,hapa namnukuu “suala hapa sio kama tunawachukia watu weusi bali ni kama wao ni tishio kwa amani,utulivu na utamaduni wa jamii ya Kiingereza…watoto weusi wakikua watanyonya uchumi wetu na kujaza magereza yetu na pengine kukukaba…huko Afrika kusini mwa jangwa la Sahara hakuna ustaarabu wowote,na hakuna maendeleo ya sayansi…”Kwa kweli ilikuwa inauma kuangalia upuuzi huo kwenye runinga,lakini ni hali tunayoishi nayo hapa kila siku.

Miongoni mwa mambo “halali” yanayowapa nguvu wabaguzi hawa ni vitendo vya baadhi ya wageni na hasa weusi kujihusisha na uhalifu au mambo mengine yasiyofaa katika jamii.Kwa wao,samaki mmoja akioza basi wote wameoza,yaani mtu mmoja mweusi akihusika kwenye uhalifu basi watu wote weusi ni wahalifu.Na kwa BNP sio weusi tu wanaolengwa.Chama hicho kilipata “pumzi” ya kutosha kupinga sera za uhamiaji na ujio wa wageni hapa Uingereza baada ya matukio ya kujilipua mabomu kwa kujitoa mhanga mjini London mwezi Julai mwaka jana. “Vita” ya BNP dhidi ya wageni ikapamba moto na sasa walengwa wakuu wakawa watu wenye asili Asia (hasa Wapakistani).Watatu kati ya waliojilipua mabomu ya muhanga walikuwa Waingereza wenye asili ya Pakistani,na kwa chama hicho cha kibaguzi hiyo ilikuwa sababu tosha ya kuwajumuisha watu wenye asili ya Pakistani na Asia kwa ujumla,na wageni wengine kuwa ni tishio kwa maisha ya Taifa hili.

Huko nyubani moja ya mambo ambayo Watanzania tunajivunia sana ni jinsi “tunavyojichanganya” bila kujali kabila,dini au jinsia.Nikisema “kujichanganya” namaanisha ushirikiano,upendo na maelewano,na sio kukosa msimamo kama maana halisi ya neno ilivyo.Niliwahi kusikia stori flani siku za nyuma inayohusu timu moja ya soka kutoka nchi flani ya jirani.Wachezaji wa timu hiyo walipokuwa wanafanya mazoezi walikuwa wanavuta umati mkubwa wa wakazi wa mji wa Arusha,ambako kulikuwa na michuano ya kimataifa.Kilichokuwa kinawashangaza wachezaji hao ni jinsi watazamaji walivyokuwa “wanajichanganya” kana kwamba ni watu wa kabila moja.Nchi wanayotoka wachezaji,kama zilivyo nchi kadhaa za Afrika,inasifika sana kwa ukabila.Inasemekana katika nchi hiyo ni nadra watu wanaotoka makabila tofauti kuwa marafiki wa dhati.Sasa walipoona baadhi ya watazamaji “wanagongeana sigara” na kutia stori kana kwamba wanaishi nyumba moja,ilikuwa ni jambo la kushangaza sana kwao.Huenda waliondoka Arusha wakiwa na fundisho flani.
Rafiki yangu mmoja,Profesa Tunde Zack-Williams,aliwahi kuniambia kwamba napaswa kujivuna kuwa Mwafrika kutoka Tanzania.Alinieleza kwamba kwa uzoefu wake mwenyewe kama mwanataaluma na Mwafrika,Watanzania ni watu waliojaliwa na “karama” ya mshikamano,upendo na umoja,na wanawaheshimu sana wageni bila kujali wanatoka wapi.Profesa huyo ni mzaliwa wa Sierra Leone,nchi ambayo imeathiriwa sana vita vya wenyewe,na amekuwa akiwasaidia sana kitaaluma vijana wa Kiafrika.Rafiki yangu mwingine anayetoka Sudan aliniambia kwamba alishangaa sana alipofika Tanzania kwa mara ya kwanza,kwa sababu licha ya nchi yetu kuwa na makabila zaidi ya 120 hakuona dalili zozote za watu kubaguana kwa misingi ya kikabila.

Hata hivyo,katika siku za hivi karibuni kumeanza kujitokeza dalili za baadhi ya watu kuchoshwa na “ujiko” huo tulionao ndani na nje ya Afrika.Binafsi,nafanya utafiti unaohusu masuala ya dini na siasa.Sintoongelea sana utafiti huo kwa vile bado “uko jikoni” lakini miongoni mwa matokeo yake ya awali ni dalili kuwa kuna watu au vikundi flani vya jamii vinavyotumia dini kujenga mpasuko katika jamii kwa manufaa yao binafsi.

Kibaya zaidi ni dalili kwamba baadhi ya Watanzania ambao tuna haki ya kuwaita “wageni” wanapoanza kujiingiza kwenye kuleta chokochoko kwenye jamii yetu iliyozowea amani.Siku zote tumekuwa tukiheshimiana na kupendana bila kujali kuwa flani alizaliwa Ifakara au New Delhi.Lakini kama BNP inavyopata “nguvu halali ya kusema ovyo” pindi wageni “wanapoharibu” inaweza kufika mahali Watanzania wazawa wakaanza kujenga chuki dhidi ya wale ambao licha ya “ugeni” wao wanachochea mpasuko katika nchi yetu.Na si “wageni” tu bali hata wale wanaotumia nafasi zao za juu katika jamii kutukoroga.Waasisi wa Taifa letu walifanya kazi kubwa sana kutufikisha hapa tulipo,na nawausia Watanzania wenzangu tusifumbe macho pale wale tulikowakaribisha kwa upendo (na maswahiba zao) wanapoanza kutuletea dharau na chokochoko kwenye nchi yetu.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa makala hii.

Leo nina hasira.Muda mfupi kabla ya kuandika makala hii niliongea na mzazi wangu huko Ifakara.Akanisimulia stori mmoja ambayo kimsingi ndio iliyonifanya niwe na hasira.Hata hivyo,naomba niwatoe hofu kwamba hasira nilizonazo haziwezi kupoteza ladha ya makala hii.

Mzee ana matatizo ya moyo.Sasa kama unavyojua mambo ya miji midogo kama Ifakara.Hospitali zipo lakini wataalamu ni wachache.Lakini kwa kumbukumbu zangu wakati flani aliwahi kunieleza kwamba kuna daktari mmoja mwenye zahanati yake binafsi mjini hapo ambae inaaminika kuwa ni mtaalam wa mambo ya moyo.Katika maongezi yetu kwenye simu aliniambia kuwa moyo bado unamsumbua.Nikamuuliza kwanini asiende kwa huyo mtaalam wa magonjwa ya moyo.Jibu alilonipa ndilo lililonifanya nipandwe na hasira niliyonayo hadi sasa.Anasema kwamba jirani yake aliyekuwa akisumbuliwa na matizo ya moyo alikwenda kumuona huyo daktari hivi karibuni,lakini jibu alilopewa lilimfanya mgonjwa huyo kurudi nyumbani akiwa na ugonjwa mwingine mpya:hofu ya kufa.Kisa?Aliambiwa na mtaalamu huyo wa moyo kwamba hivi “kwanini wewe ambaye umebakiwa na wiki mbili tu za kuishi (kutokana na umri wako mkubwa) unataka kutibiwa moyo badala ya kuuacha usimame wenyewe muda ukifika”!

Laiti maelezo hayo ya mzazi wangu yangekuwa yanatoka kwa mtu wa kawaida tu nisingeamini kwamba nchi yetu ina baadhi ya watu wanaojiita madaktari ambao wanaweza kukiuka maadili ya kazi yao kwa kiwango hicho!Nadhani hata ukienda gereji na gari lililochoka sana,bado mafundi makenika watakupa matumaini ya namna flani badala ya kukibilia kukwambia kwamba ukalitupe gari lako.Na hapo tunazungumzia kitu ambacho unaweza kukinunua kipya.Maisha hayawezi kununuliwa upya.Tukirudi kwenye stori niliyopewa na mzee,basi jirani yake (ambaye si kama amekula chumvi sana) tangu alipoambiwa na daktari kwamba amebakiwa na wiki mbili kufa,amepatwa na hofu ya ajabu.Kwani kuna mtu ambaye haogopi kufa?Na hasa kama umepewa tahadhari kama hiyo na daktari.Mzee wangu baada ya kusikia stori hizo kutoka kwa jirani yake alinieleza bayana kwamba bora aendelee kuugua kuliko kwenda kwa daktari ambae amegeuka kuwa mtabiri wa urefu wa maisha ya wagonjwa.Nilimpoza kwa kumwambia kuwa naamini huyo daktari alieongea upuuzi huo hajui wajibu wake na anakiuka tu maadili ya kazi yake.

Laiti jirani ya mzee wangu angekuwa amekumbana na kioja hicho hapa Ughaibuni huenda angejikuta anapata utajiri wa ghafla endapo angefungua mashtaka dhidi ya daktari aliemtishia uhai wake.Sio siri,hawa wenzetu wanatoa kipaumbele kikubwa sana kwa suala la afya sambamba na kuhakikisha kuwa watumishi katika sekta ya afya wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata maadili.Na sio katika sekta ya afya pekee bali sehemu nyingi zinazotoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi zinabanwa sana kuhakikisha kuwa huduma hizo zinatolewa katika kiwango stahili.Pengine kingine kinachowasaidia viongozi katika taasisi mbalimbali za huduma hapa Ughaibuni ni ile tabia ya kufuatilia nini kinachoongelewa kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi zao.Mganga mkuu akisoma gazeti na kukuta malalamiko kuhusu hospitali yake,hapuuzi bali atakimbilia kumjibu mlalamikaji huyo kuwa atachunguza suala lililolalamikiwa.Na haishii kutoa ahadi tu bali hatua lazima zitachukuliwa.Lakini kinachosikitisha huko nyumbani ni ile kuona gazeti flani limeripoti kuwa hospitali flani “imeua” mgonjwa na wala husikii habari hiyo ikikanushwa au kukubaliwa na uongozi wa hospitali husika.

Sehemu nyingi zinazotoa huduma huko nyumbani zina masanduku ya kutoa maoni.Lakini lile vumbi unaloliona kwenye mengi ya masanduku hayo linatosha kuthibitisha kuwa masanduku hayo ni sawa na urembo tu kwenye makorido ya sehemu husika.Kwa mtizamo wangu,nadhani tatizo la msingi ni ile tabia iliyojengeka kwa baadhi ya watumishi kwenda kazini kuonekana tu wamekwenda kazini na mwisho wa mwezi wapate mishahara yao,na si kwenda kutumikia wale wanaowafanya wapate mshahara.Unadhani mtumishi wa benki anaejua dhahiri kwamba ni fedha za wateja ndio zinaiwezesha benki hiyo kuwepo na kumlipa mshahara,atamdharau mteja anaekuja hapo kupata huduma?Kama mtumishi anajiona hataki “kubughudhiwa” na wanaohitaji huduma kazini kwake,si alale tu nyumbani,au aache kazi?Tuone kama hatakufa kwa njaa.Kumbe basi kinachompa shibe (kazi) ni sharti akiheshimu na kukitumikia kwa moyo wake wote.

Alamsiki

17 Apr 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa makala hii na gazeti zima la KULIKONI.Hapa mambo yanakwenda hivyohivyo-kimgongomgongo kama watoto wa mjini huko nyumbani wanavyosema.

Katika makala iliyopita niliwapa picha ambayo kwa namna flani ingeweza kukufanya udhani kuwa kila kitu hapa “kwa mama” ni shaghlabaghala.Hapana.Hapa kuna mambo kadhaa ya kujifunza. Miongoni mwao ni haki za walaji au watumiaji wa huduma mbalimbali, kwa lugha ya hapa “kwa mama” tunawaita consumers au service users. Kilichonipelekea kuandika mada hii ya leo ni matukio mawili yaliyotokea sehemu mbili tofauti: moja hapa nilipo na moja huko nyumbani. La hapa lilikuwa hivi: siku moja nilikuwa nasafiri kutoka Aberdeen, Scotland (mji ninaoishi) kwenda London.Basi nililokuwa nasafiri nalo huwa kwa kawaida linaondoka saa 1.15 usiku na kufika London saa 12 asubuhi. Hawa wenzetu muda ni kila kitu. Hakuna kucheleweshana. Hadithi za “samahani wateja wapendwa, tunasikitika kuwatangazia hili na lile litakalowachelewesha” ni vitu vya nadra sana, japo huwa vinatokea mara chache. Sasa siku hiyo hadi saa 1.30 usiku bado basi lilikuwa halijaondoka. E bwana ee, kasheshe iliyozushwa na abiria hapo ikawa si ya kawaida. Baadhi walianza kudai warejeshewe nauli zao, wengine wakawa wachungu kama pilipili wakiilaani kampuni inayoendesha huduma hiyo ya mabasi. Hatimaye ilitangazwa kuwa basi litaondoka na kwamba kampuni itafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa muda wa kufika London utakuwa uleule wa saa 12 asubuhi. Angalau hiyo ilipoza munkari wa abiria, japokuwa baadhi yao walisisitiza kurudishiwa nauli zao na kuchukua usafiri mwingine.

Tukio la huko nyumbani lilikuwa hivi: Mimi nilikuwa naenda Ifakara kuwajulia hali wazazi. Matatizo yalianzia hapohapo kituo kikuu cha mabasi Ubungo.Japo kwenye tiketi ilionyesha basi lingeondoka saa 1.30 asubuhi lakini hadi saa 2.30 hakukuwa na dalili za basi hilo kuondoka. Abiria walikuwa wakilalamika chinichini kwamba tunacheleweshwa bila sababu ya msingi lakini hakuna hata mmoja wao aliefanya jitihada za kuwafahamisha wahusika kuwa wanapuuza haki zetu. Hatimaye kwenye majira ya saa 3 kasoro hivi ndio basi liliondoka. Kati ya Dar na Morogoro basi lilisimama katika maeneo ambayo sio vituo, aidha kwa vile dereva au kondakta alitaka kuchimba dawa au kuongea na akinadada ambao inaelekea walikuwa ni nyumba ndogo zao. Kuna tetesi kuwa madereva wa mabasi yanayokwenda/kutoka mikoani huwa na vimwana kila mji au kijiji kilichopo katika ruti ya basi husika. Madereva msinifungulie mashtaka ya umbeya, mimi sina takwimu zozote kuthibitisha tetesi hizo. Kwa hesabu za harakaharaka tulisimama njiani zaidi ya mara tano, zote zikiwa ni kwa matakwa ya dereva au utingo wake. Badala ya kufika Ifakara majira ya saa 9 tulifika saa 11.Kwa bahati mbaya ndani ya basi hilo kulikuwa na jamaa kama watano hivi waliokuwa wakienda kuwahi mazishi Ifakara.Katika hali ya kawaida watu watano (hasa kama ni ndugu) wana uwezo wa kutosha kushinikiza kutekelezewa haki zao. Lakini hao jamaa waliishia kulalamika chinichini tu kwamba wanacheleweshwa kwenye mazishi.

Ukilinganisha matukio hayo mawili japo yalitokea sehemu mbili tofauti unapata picha kuwa walaji au watumiaji huduma huko nyumbani wanachangia sana kupuuzwa kwa haki zao kwa vile mara nyingi huishia kulalamika chinichini hata pale ambapo umoja wao ungeweza kuhakikisha kuwa haki zao za msingi zinatekelezwa bila mushkeli. Hivi dereva wa daladala na konda wake wanapoamua kuwachelewesha kituoni kwa kisingizio cha kula vichwa wangeweza kweli kufanya hivyo laiti abiria wakitishia kushuka kwenye daladala hiyo au kumshurutisha azingatie muda? Naamini hata kama tungekuwa na akina Mwaibula 100 bado isingekuwa rahisi kuhakikisha kuwa haki za abiria zinatekelezwa ipasavyo iwapo abiria wenyewe hawajishughulishi kuzidai haki zao.

Jamani, tuamke. Hakuna NGO au mtu atakaeweza kuhakikisha kuwa haki zetu zote za msingi kama walaji au watumia huduma zinapatikana ipasavyo iwapo sisi wenyewe tutajifanya hatujali adha tuzopata kila kukicha tunapotumia huduma mbalimbali. Ari, kasi na nguvu mpya ni pamoja na wananchi kuchangamkia kudai haki zao (kwa amani, of course).

Hadi wiki ijayo, alamsiki.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.