Showing posts with label UBABAISHAJI. Show all posts
Showing posts with label UBABAISHAJI. Show all posts

9 May 2011


Baada ya Rais Jakaya Kikwete kuonekana kituko kwa kupokea hundi yenye tarakimu zinazokinzana na thamani ya hundi hiyo kwa maandishi,na yeye kuonekana akitoa tabasamu la nguvu (trademark yake),sasa imekuwa zamu ya mkewe.

Ukiangalia hundi anayokabidhiwa Mama Salma Kikwete (pichani juu) utabaini kuwa thamani ya hundi kwa maandishi ni shilingi milioni tatu na laki nane,ambayo kwa tarakimu inapasa kuwa 3,800,000.Sasa sijui ni umaimuna au uzembe tu,tarakimu za hundi hiyo zimeandikwa kichakachuaji- TZS 3,800,00.Unaweza kudhani ni shilingi elfu tatu mia nane (3,800.00) lakini maelezo ya hundi yatakusuta kwani yametamka bayana kuwa ni SHILINGI MILIONI TATU NA LAKI NANE.

Na hapa chini tunamwona mtu tuliyemkabidhi dhamana ya kutuongoza Watanzania takriban milioni 50 akikenua meno kwa furaha huku hundi imeandikwa TWO HUNDRED THOUSAND lakini tarakimu ni 300,000



Hivi kabla ya hafla hizi, hao jamaa wa  PSU  hawakagui vitu anavyokabidhiwa Rais au mkewe?Au nao hadithi ni hiyohiyo?

Na haya ni madudu nadra tunayobahatika kuyaona hadharani.Je yanayofanyika kwa kwa faragha ua sirini inakuwaje?Npatwa na wasiwasi kuwa hadi Kikwete anaondoka madarakani hapo 2015 (kama hatoombwa na mafisadi kugombea tena ili aendelee kuwalinda) tunaweza kushtukia Tanzania ishauzwa zamani hizo.Unashangaa nchi inawezaje kuuzwa?Waulize "Zaire" (DRC Kinshasa)!!!!

Chanzo: Nimkutana na habari hii kwa ndugu yangu MPAYUKAJI MSEMAOVYO

19 Apr 2010

Kuna busara moja inayotuasa kuwa mpuuzi husema kwa vile anajiskia kusema (hata kama ni upuuzi) ilhali mwenye busara husema tu pale anapokuwa na kitu cha kusema (ikimaanisha kama hana cha kusema,au haoni umuhimu wa kusema kitu,atakaa kimya. Busara zaidi zinatuasa kuwa makini na tunayosema hadharani kwa vile mara nyingi jamii humtambua zaidi mtu kwa kauli zake.Sema upuuzi,utaonekana mpuuzi.Sema ya busara,utaonekana mwenye busara.Sasa kuna huyu msomi,Dokta Benson Bana,ambaye licha ya kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam,ni mkuu wa idara ya Sayansi za Siasa na Uongozi na pia ni Mwenyekiti Mwenza wa REDET.Yayumkinika kusema Dkt Bana amekuwa mahiri zaidi wa kutoa kauli zisizoendana na wasifu wake kitaaluma kuliko umahiri wa wa usomi wake

Na leo,kwa mujibu wa habari katika gazeti la Mwananchi,msomi huyo 'amelipuka' tena kwa kauli kwamba tuhuma zilizokithiri dhidi ya ufisadi zinaweza kusababisha taifa kukosa viongozi wazuri wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba.Huhitaji kuwa na hata asilimia moja ya kiwango cha elimu ya Dkt Bana kutambua kuwa tuhuma zilizotapakaa kuhusu ufisadi ni matokeo ya kuwepo kwa ufisadi.Msomi huyu anaishi Tanzania lakini yaelekea hafahamu mazingira yanayomzunguka,na hilo linaleta wasiwasi mkubwa kuhusu mchango wa wanataaluma katika maendeleo ya nchi yetu.

Katika habari hiyo Dk Bana aliwataka watu "waaache siasa chafu za kuhubiri na kudai kuwa watuhumiwa wa ufisadi hawafai kupewa kura au kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi kana kwamba wameshathibitika".Huu ni zaidi ya ubabaishaji wa kitaaluma,na kwa kiasi flani inaaibisha Udaktari wa Filosofia tunaohenyea akina sie.Kwanza,Dkt Bana amepata wapi mamlaka ya kuwataka wananchi waache kulalamikia ufisadi?Usomi hautoi mamlaka ya kuizuia jamii kulalamikia maovu yanayoisumbua.Pili,kwa mtizamo wa msomi huyu,kwa vile tuhuma za ufisadi hazijathibitika basi watu wakae kimya hadi 'miujiza itapotokea kwa watawala wetu kuamua kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mafisadi'!Hii ni sawa na kuingiliwa ndani na kibaka halafu ukakaa kimya kwa vile tu wewe sio chombo cha sheria.Ukifanya hivyo,hata hao polisi watakuona mpumbavu na unawapotezea muda.La kufanya ni kumdhibiti kibaka au kupiga kelele kuwashtua majirani wakusaidie kumdhibiti.

Binafsi,pamoja na kuheshimu uhuru wa kutoa mawazo,nadhani tatizo kubwa la Dkt Bana ni tabia yake ya 'kusema chochote' hata kama hana cha kusema.Inaelekea aidha hafahamu athari za tabia hiyo au anapuuza tu.Matokeo yake ni kuonekana mbabaishaji wa namna flani.Si lazima jina lake lionekane magazetini au kusikika radioni kama hana la muhimu kuieleza jamii.Eti anatuasa kuwa "si vizuri kwa watu kunyimwa kura kwa sababu ya kutuhumiwa kwa ufisadi hadi hapo watakapothibitika na kutaka wanasiasa waache kuhukumu wenzao bila kosa".Kwanini hajiulizi inakuwaje watu hao wanatuhumiwa ufisadi in the first place?Kwanini ni wao na si Dokta Bana,kwa mfano?

Hivi lipi lililo muhimu zaidi kwa Tanzania kama taifa: kukosa viongozi bora kwa vile wanatuhumiwa kwa ufisadi au kupata viongozi bora watakaowajibika kulitumikia taifa kupambana na ufisadi?Wasiwasi wa Dkt Bana ulipaswa kuwa kwenye athari za ufisadi kwa jamii na sio tuhuma za wananchi dhidi ya mafisadi.Ni mlevi tu atakayeshindwa kuelewa kuwa kinachoumiza Watanzania kwa sasa ni UFISADI na sio TUHUMA DHIDI YA MAFISADI.

Mwanataaluma huyu anaongoza taasisi ya REDET ambayo mara imekuwa ikishutumiwa kwa upendeleo inapotoa taarifa za kura zake za maoni (opinion polls) kuhusu CCM na vyama vingine vya siasa.Sina hakika kuwa matokeo ya kura hizo huwa 'yanapikwa' ili kuridhisha watawala lakini kinachozua maswali dhidi ya polls hizo ni kutoendana na hali halisi na dalili za upendeleo.

Wito wangu kwa Dkt Bana ni huu: wakati mwingine jaribu kuitendea haki taaluma yako kwa kukaa kimya pale usipokuwa na cha kuongea.Kwa kufanya hivyo,utawatendea haki pia wasomi wenzako,taasisi unazoongoza na fani nzima ya usomi.Ni muhimu pia unapotoa matamshi mazito ukajitahidi kutumia theories za kusapoti matamshi hayo badala ya kutoa hisia zenye mwelekeo wa kijiweni.


.

26 Jun 2009


Hili ndio "BUNGE LENYE MENO"!Juzijuzi mbunge mmoja wa CCM kaomba Mungu alilaani Baraza la Mawaziri kwa kushindwa kutimiza majukumu yake.Mwingine kadai serikali ina ugonjwa na inahitaji maombezi (na kwa kawaida magonjwa yanayohitaji maombezi ni yale yasiyotibika kama vile ukimwi,nk).Jana mbunge mwingine wa chama hicho tawala amewafananisha mawaziri na mbwa.Na pengine moja ya mambo yatakayokumbukwa zaidi katika historia ya bunge letu tukufu ni jinsi kikao hiki cha bajeti kinavyoonekana "mwiba mkali" kwa mawaziri,at least according to walio mahiri katika kuripoti pasipo kusoma kati ya mistari (reading between the lines).

Sina maneno ya huruma kwa baadhi ya wabunge hawa wa CCM.Ni wanafiki wanaohangaika kutumia vizuri nafasi hizi za mwisho mwisho kujitengenezea mazingira ya kurejea bungeni hapo mwakani.Lakini ili haki itendeke,ni vema kuwatofautisha wanafiki hawa kwa makundi.Kuna kundi la wabunge waliojitokeza mapema (kabla hata ya joto la uchaguzi wa mwakani halijaanza kupanda) kukemea ufisadi na vitendo vingine vinavyokwaza maendeleo ya taifa letu.Sio siri kwamba wabunge kama Selelii,Kimaro,Killango,Mwambalaswa,Mwakyembe na wengineo wamejitokeza kuwa sauti adimu ndani ya CCM dhidi ya ufisadi.Na tunafahamu vituko wanavyofanyiwa na watu walewale wanaopaswa kuwaunga mkono.

Kundi la pili ni la wababaishaji walio njia panda; upande mmoja hawana nia ya dhati ya kupambana na ufisadi au pengine ni sehemu ya mfumo unaodumisha ufisadi,upande mwingine wanafahamu fika kwamba miongoni mwa ajenda za uchaguzi mkuu ujao ni ufisadi na namna wawakilishi wetu walivyoshiriki katika mapambano dhidi ya ufisadi.

Pia kuna makundi mengine mawili: la kwanza linajumuisha wababaishaji wanaokwenda bungeni kwa vile tu ndio mahala pao pa kuchuma shs 7,000,000/= za mshahara kiulaini.Hawachangii hoja,hawaongei lolote japo si mabubu,wapo wapo tu.Kuwepo au kutokuwepo kwao bungeni hakutambuliki kwa vile wanaongeza tu idadi ya wabunge.Kundi la pili ni la watetezi wa ufisadi.Hawa ni wepesi wa kuomba mwongozo wa Spika kila maslahi yao au ya wadau wenzao wa ufisadi yanapoguswa.Nadhani mmesikia "Dokta" Mzindakaya alivyotumia Maandiko Matakatifu kutetea ufisadi .Ila hawa wanaocheza na vitabu vya Mungu,nadhani ndio wanaostahili kulaaniwa zaidi kwani wamevigeuza kama manifesto za usanii wao wa kisiasa!

Uzuru wa makundi haya mawili ya mwisho-la tatu na la nne-ni kwamba angalau yanajumuisha wabunge tunaofahamu wanaposimamia.Aidha ni wazembe na mabubu wasioongea (aidha kwa aibu ya kuongea,au "heri mie sijasema",au uzembe tu) au ni watetezi wa mafisadi.Hawa si wanafiki as such kwa vile wameji-identify kwetu kuwa ni viumbe wa namna gani.

Tofauti kati ya makundi hayo ni ndogo mno contrary to inavyosomeka na kusikika kwenye vyombo vya habari.Hapa nataka kuzungumzia makundi mawili ya mwanzo-la kwanza na la pili.Hawa wote ni wana CCM,na kwa namna yoyote ile hawawezi kujitenganisha na matatizo yanayosababishwa na chama hicho tawala.Na hili si la kufikirika kwa sababu tayari wengi wa wabunge wa kundi la kwanza wamekuwa wakikumbana na kadhia mbalimbali kutokana na msimamo wao dhidi ya ufisadi,na guess what,kadhi hizo ni kutoka kwa wenzao ndani ya CCM.

Mawaziri wanaolaaniwa na kufikia hatua ya kuitwa mbwa wanatoka CCM pia.Hii sio vita ya wenyewe kwa wenyewe kama inavyoweza kutafsiriwa kiuzembe.Huu ni unafiki,period.CCM isingefika hapo ilipo laiti "wapambanaji hawa" wangekuwa na mkakati wa dhati wa kuleta mabadiliko ya kweli.Wanachofanya muda huu ni cha kibinafsi zaidi kuliko kitaifa.Wanaweza kurudi bungeni hapo mwakani baada ya wapiga kura wao "kuzugika" na CVs za wawakilishi wao tangu 2005 hadi 2010.Kurudi kwao bungeni kutapelekea CCM kuendelea kuwa yenye wabunge wengi bungeni,na hivyo kupelekea kuendelea kwa haya tunayopigia kelele kila siku.

Siamini kama kuna mkakati kwa Selelii na wenzake kuleta mageuzi ndani ya CCM.So far,kelele zao hazijasaidia kukitenganisha chama hicho na ufisadi,implying that kelele zao zimebaki kuwa kelele tu.Wana options mbili: waendelee kupiga kelele lakini wabaki kuwa sehemu ya chama kinachohusishwa na ufisadi au wajondoe ndani ya chama hicho na hivyo kubainisha kuwa kuwa kwao ndani ya CCM ilikuwa ni sehemu tu ya maisha yao ya kisiasa lakini cha muhimu zaidi kwao ni Tanzania na ustawi wa Tanzania.Yes,si lazima kuwa mbunge wa CCM ili kupata fursa ya kupigania maslahi ya taifa.Mifano hai ipo;Dkt Slaa,Zitto Kabwe,nk sio wabunge wa CCM,lakini sote tunafahamu michango yao katika kupambana na ufisadi.

Unafiki wa wabunge hao wa CCM unasababishwa na kitu kimoja kisicho na msingi: UBINAFSI WA KISIASA.Ni hivi,kwa CCM,umoja na mshikamano ndani ya chama hicho ni muhimu zaidi kuliko umoja na mshikamano wa taifa.Na hilo ni matokeo ya chama hicho kuamini kwamba ni chenyewe tu kinachoweza kudumisha mshikamano na umoja wetu.Kwa lugha nyingine,kimebinafsisha uwezo,dhamira,jitihada na nguvu za Watanzania zaidi ya milioni 35 ambao si wanachama wa chama hicho (takwimu za karibuni zinaonyesha idadi ya wanachama wa CCM ni takriban milioni 4 tu).Japo ni kweli kwamba chama hicho kimetoa uongozi uliosaidia kudumu kwa amani na mshikamano huo,Watanzania wenyewe ndio waliofanya kazi ya msingi zaidi kufanikisha hilo.Upendo na upole wetu (ambao mara nyingi umeishia kutumiwa vibaya na wanasiasa walafi) ndio sababu kuu ya kwanini tumeendelea kubaki kisiwa cha amani (kwa maana ya kutokuwa vitani).

Ni ubinafsi wa kisiasa unaopelekea CCM kuweka mbele maslahi ya kisiasa badala ya maslahi ya taifa.Sote tumeshuhudia mara kadhaa wabunge wa chama hicho tawala wakiitisha vikao "vya kuwekana sawa" kila zinapojiri hoja nzito bungeni.Kuwekana sawa kwa maslahi ya nani?Hivi cha muhimu ni hoja ipite tu au ipite ili ilete mabadiliko chanya kwa wananchi?

Lakini ili upate mfano sahihi zaidi kuhusu ubinafsi wa wabunge hawa ni pale Dkt Slaa alipotamka bayana kwamba mishahara ya wabunge ni mikubwa mno kulinganisha na hali halisi ya uchumi wetu.Kwa umoja wao (huku wakipata sapoti kutoka kwa wabinafsi wengine waliojificha kwenye vyama vya upinzani) walimzomea Dkt Slaa na kumzongazonga kana kwamba kawatukana.Hivi ina maana wabunge hawa wanaotuzuga kuwa wanatetea maslahi yetu hawaelewi kuwa wakati wao wanazawadiwa takriban shilingi 7,000,000/= mwezi (wastani wa shilingi laki 230,000/= kwa siku sawa na takriban shs 10,000/= kwa saa) takriban Watanzania 36,000,000 wanaoishi kwa chini ya shilingi 3000/= kwa siku?

Hadi kufikia tamati yake na mabiloni kadhaa kutumika,kikao hiki cha bajeti kitashuhudia kila aina ya vituko kutoka kwa wanafiki hawa.Ukidhani hizo dua dhidi ya mawaziri na "matusi" ya kuwaita mbwa ndio hatua kali kabisa,subiri usikie "makombora" zaidi.Na kama kawaida ya vyombo vyetu vya habari,kurasa zitapambwa na maneno mazito kama "Bunge moto juu","Wabunge wachachamaa",na ubabaishaji mwingine kama huo.Lakini pamoja na yote hayo,makadirio ya wizara za mawaziri wanaoombewa dua mbaya na kuitwa mbwa yatapitishwa na wabunge haohao wanaotuzuga kuwa "wana hasira na mawaziri".

16 May 2009


MSIKIE MATTAKA ANAVYOONGEA KWA KUJIAMINI KANA KWAMBA ALIJITEUA MWENYEWE KUWA MKURUGENZI WA ATCL NA KUJIPA UJUMBE WA NIC.


Mattaka ajiweka kando ATCL
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 16th May 2009

Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL),
David Mattaka ametangaza kutoiongoza kampuni hiyo kwa miezi sita kutokana na kuteuliwa kuwamiongoni mwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Bima la Taifa (NIC).

Katika taarifa ya barua hiyo iliyotolewa na ofisi yake kwa wafanyakazi Mei 11, mwaka huu, inaonyesha kuwa Mattaka amelazimikakutofanya kazi ATCL kwa kipindi hicho kutokana na nafasi yake hiyo aliyoteuliwa naWaziri wa Fedha na Uchumi, Aprili 23, mwaka huu kuwamo katika Bodi ya Wakurugenzi ya NIC kazi ambayo zinamtaka awapo wakati wote kazini.

Uteuzi huo sambamba na wa Rais Jakaya Kikwete wa Februari 23, mwaka huu wa kuwamo katika kikosikazi cha kulifufua shirika hilo, Mattaka alisema “Katika nafasi zote nilizoteuliwa zinanitaka nifanye kazi muda wote kuanzia Mei mosi.” Kutokana na nafasi hizo mpya, kwa kipindi cha miezi sita ambayo hatakuwao ATCL, Bodi ya Wakurugenzi imemteua William Haji kukaimu nafasi yake.

“Bodi ya Wakurugenzi imemteua William Haji kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu na CEO kuanzia Mei 8 na wakati huohuo kuendelea na nafasi yake ya Mkurugenzi wa Fedha,” alisema Mattaka. Bodi ya Wakurugenzi ya NIC iliyoanza kazi Mei mosi, inaongozwa na Mwenyekiti Balozi Charles Mutalemwa na wajumbe ni Michael Mhando kutoka Bima ya Afya, Msajili wa Hazina Agnes Bukuku, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Kate Bandawe na Charles Kilasile.

CHANZO: Habari Leo

KWA UPANDE FLANI,HATUWEZI KUMLAUMU KWANI KWA HAKIKA ALIYEMTEUA AMEONEKANA KURIDHISHWA NA UTENDAJI WAKE.USHKAJI KATIKA TEUZI NI MIONGONI MWA VYANZO VIKUU VYA KUSUASUA NA HATIMAYE VIFO VYA TAASISI MBALIMBALI ZA UAMMA,BILA KUSAHAU KUSHAMIRI KWA UFISADI.KWANI HAKUNA WATU WENYE UWEZO ZAIDI YA MATTAKA?KAMA AMECHEMSHA ATCL,ATALETA MIUJIZA GANI HUKO BIMA?


YANI TUNAVYOENDESHA MAMBO KIHOLELA UTADHANI TUSHAPIGA HATUA KUJIKWAMUA KIUCHUMI KUMBE WAPI.VICHWA VILIVYOISHIWA MAWAZO NA MBINU ZA KUNUSURU TAASISI ZA UMMA HAVIWEZI KULETA MAPYA YOYOTE VINAVYOZUNGUSHWA KIUSHKAJI KUTOKA TAASIS MOJA KWENDA NYINGINE KANA KWAMBA NI ZA KIFAMILIA.



11 Apr 2009

MAELEZO YA PICHA KUTOKA KATIKA GAZETI LA HABARI LEO YANASOMEKA:

Behewa la mafuta la TRL liliacha njia eneo la Kurasini, Dar es Salaam na kuanguka.Wafanyakazi wa kampuni hiyo walikutwa wakikinga mafuta hayo ili kuyahifadhi katika mapipa chini ya ulinzi mkali wa polisi. (Picha na Yusuf Badi).
NADHANI MWENZANGU PIA UKIANGALIA PICHA HIYO KWA MAKINI UTABAKI UNAJIULIZA KWAMBA HAO WAHINDI WA TRL NI WAWEKEZAJI KWELI AU VIINIMACHO?TALKING OF VIINIMACHO,YAYUMKINIKA KUJIULIZA IWAPO HAWA JAMAA HAWAJAWAROGA HAO WANAONG'ANG'ANIA KUENDELEZA MKATABA WA KIMAZINGAOMBWE NA TRL.KAMA ILIVYO DESTURI YETU YA ZIMAMOTO,TUNASUBIRI WALIKOROGE KWANZA,KISHA WAINGIE MITINI HALAFU KUNYWA TULINYWE SIE!NA HAPA NENO "KULIKOROGA" LINAMAANISHA KU-MESS UP NA MAISHA YA ABIRIA WANAOTEGEMEA USAFIRI WA RELI YA KATI.

5 Mar 2009

Picha kwa hisani ya Mjengwa
MWAKA 2006,MANISPAA YA TEMEKE ILITANGAZA AZMA YAKE YA KULIBORESHA SOKO LA TEMEKE.LAKINI KATIKA HALI YA KUSTAAJABISHA,KUNA TAARIFA KWAMBA SASA SOKO HILO LIMEUZWA KWA MWEKEZAJI.KWA MWENENDO HUU,SI AJABU SIKU YA SIKU MTU AKAAMKA NA KUKUTA MTAA ANAOISHI UMEUZWA KWA MWEKEZAJI.

22 Dec 2008

Photo courtesy of MJENGWA

KURA YANGU INAWAANGUKIA WABABAISHAJI WA TRL.CHEKI "MBELEKO" NYINGINE HII KUTOKA KWA SUMATRA:

HATIMAYE Kampuni ya MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imeiruhusu Kampuni ya Reli (TRL) kuanza kutumia mabehewa yake 23 ya mitumba yaliyokodishwa kutoka Kampuni ya Reli ya India. Awali Sumatra waliizuia TRL kutumia mahehewa hayo kwa madai kwamba hayakuwa na obora unaotakiwa.

Hata hivyo, meneja uhusiano wa TRL, Midrahji Meiz alisema jana kuwa Sumatra sasa imewaruhusu kuendelea kutumia mabehewa hayo baada ya vigezo vilivyokuwa vinahitajika kukamilika.

“Tumesharuhusiwa na Sumatra kuanza kutumia mahehewa hayo na hivi sasa utaratibu unafanyika ili yanze kusafirisha abiria... baada ya utaratibu huo kukamilika tutatoa taarifa rasmi,” alisema Meiz na kuongeza: “Suala la usafiri wa treni ni suala la msingi kabisa na ndiyo maana tunajitahidi kuboresha usafiri huo kila wakati ili abiria wasafiri katika mazingira mazuri.”

Mkurugenzi na mdhibiti wa reli wa Sumatra, Alfred Nalitolela alikiri kuwepo kwa suala hilo na kusema kuwa wameamua kuiruhusu TRL indelee kutumia mabehewa hayo kwa kuwa wamekamilisha marekebisho yaliyokuwa yanahitajika.

“Tulibaini kwamba mabehewa hayo hayana ubora unaostahili kwa matumizi ya reli yetu, na moja ya vitu hivyo ni kiungio kati ya behewa moja na jingine, usambazi wa umeme ndani ya mabehewa, belling, spring, breki ya mkononi na magurudumu,” alisema Nalitolela na kuongeza:

“Tulipokwenda India kukagua mabehewa hayo, tuliwaeleza wafanye vitu hivyo lakini wakaleta mabehewa kabla ya kukamilika kwake ndipo ikabidi tuwakataze kuyatumia mpaka wamalize kuyafanyia marekebisho hayo.”

Alifafanua kwamba baada ya hapo walichukuwa moja ya kiungio cha mabehewa na kuyapeleka katika maabara ya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuyafanyia utafiti kama ni vifaa vipya na kuomba maelezo ya kina.

“Unafahamu katika suala hili lile jumba la behewa ndilo linalotakiwa kuwa mtumba, lakini vifaa vyote vinavyofanya mabehewa hayo yafanye kazi vinatakiwa kuwa vipya, ikiwemo usambaji wa nyaya za umeme ndani ya behewa. Na hicho ndicho tunachokikagua na kukiangalia na kuhakikisha kwamba viko salama kila wakati,” alifafanua Nalitolela.
CHANZO:Mwananchi
JE MWENZANGU KURA YAKO INAANGUKIA WAPI?


KAMPUNI iliyopewa jukumu la kusimamia na kutunza mali za lililokuwa Shirika la Reli Tanzania (RAHCO), imeanza kukatakata injini 27 na mabehewa 19 ili yauzwe kama chuma chakavu.

Mabehewa hayo na injini zake yanadaiwa yalikuwa na hali nzuri, lakini mwekezaji akayakataa wakati anachukua shirika kwa maelezo kuwa hayamfai.

Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya mwekezaji Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kudai kuwa, mabehewa hayo yalikuwa yamechakaa zaidi na hayawezi kutumiwa tena, huku Rahco ikidai kuwa yalikuwa yanafaa kuendelea kutumika.

Tayari zabuni ya kupata makampuni ya kununua vyuma hivyo chakavu imeshafanyika na washindi kupatikana.

Makampuni ambayo yameshinda zabuni yameshaanza kukata mabehewa hayo na injini katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Tabora na Kigoma.

Mwananchi Jumapili wiki hii ilishuhudia baadhi ya mafundi wa kampuni iliyoshinda zabuni wakikata mabehewa yaliyopo katika Stesheni ya Dar es Salaam.

Meneja Uhusiano wa RAHCO, Musita John aliiambia Mwananchi Jumapili kuwa, wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kushindwa kuzifanyia kazi injini hizo na mabehewa.

Alisema kuwa endapo injini hizo na mabehewa zingefanyiwa ukarabati mdogo zingeendelea kuisaidia kampuni hiyo kupunguza matatizo ya usafiri lakini mwekezaji hakuzikubali.

John alisema wakati mwekezaji anachukua shirika hilo alikuta jumla ya injini 116 na 92 kati yake zilikuwa zinafanya kazi, lakini yeye aliamua kuchukuwa 79 tu na zingine akazikataa kwa madai kwamba hazimfai.

Alisema mbali na injini hizo, pia alikuta jumla ya mabehewa ya abiria 164, yaliyokuwa yanafanya kazi ni 125, lakini yeye aliamua kuchukuwa mabehewa 106 tu na 19 yaliyobaki aliyakataa.

John alifafanua kwamba baada ya mwekezaji huyo kumaliza tathimini ya mali za TRC alizokuta kabla hajaanza kazi waliamua kuziweka katika madaraja mbalimbali, ambapo daraja (A) lilikuwa ni mabehewa na injini yaliyokuwa yanafanya kazi.

Alisema Daraja (B) lilikuwa ni la mabehewa na injini zilizokuwa zinahitaji matengenezo madogo, ingawa yalikuwa bado yanaendelea na kazi ya kusafirisha abiria na mizigo wakati daraja (C) ni yale ambayo alikuta yameondolewa kazini, baada ya kuharibika na kupelekwa kwenye karakana ili yafanyiwe ukarabati, lakini pia aliyakataa kwa madai kwamba hayamfai.

Aliongeza kuwa kulikuwa na daraja (D) ambalo lilihusisha injini na mabehewa yaliyoharibika, yasiyofaa kutumika na daraja E ni yale ambayo yalishakaguliwa na kubainika kwamba, yalishafikia katika kiwango cha vyuma chakavu.

Hata hivyo, habari kutoka ndani ya TRL, zinaeleza kwamba mbali na injini na mabehewa hayo, mali zingine ambazo mwekezaji huyo alizikataa ni vifaa vya ofisini ambavyo hivi sasa pia viko katika orodha ya vitu vinavyouzwa na RAHCO kama vyuma chakavu.

Wakati RAHCO ikiendelea kukatakata injini hizo na mabehewa TRL hivi sasa inadaiwa kuwa katika hali mbaya kutokana na baadhi ya injini zake aina ya ‘73 class’ zilizokodishwa kutoka India kuwa na uwezo mdogo wa kuvuta mzigo, kiasi kwamba wanalazimika kuziunganisha mbili ndipo ziweze kuvuta mzigo ambao ungevutwa na injini moja aina ‘88 class’ za Tanzania alizozikataa.

Meneja Uhusiano wa TRL, Midlajy Maez alipotakiwa kutoa ufafanuzi wake kuhusiana na suala hilo alisema wanaotakiwa kulizunguzia ni RAHCO.

CHANZO:Mwananchi

HIVI KWANINI TUNAENDELEA KUWANG'ANG'ANIA HAWA WABABAISHAJI WA KIDOSI?JIBU JEPESI NI KWAMBA WALIOWAKARIBISHA NI WABABISHAJI WENZAO,SO SIO RAHISI KWAO KUONA UBABAISHAJI ULIOPO.TUNA WAZIRI,NAIBU WAZIRI,KATIBU MKUU,NAIBU KATIKA MKUU,MKURUGENZI,NK,NK,NK WOTE KATIKA WIZARA HUSIKA.HAWA WANALIPWA MSHAHARA NA MARUPURUPU MENGINE KUTOKA KWA WALIPA KODI WA TANZANIA LAKINI SIJUI WANASHINDWA NINI KUCHUKUA HATUA STAHILI DHIDI YA USANII HUU ULIOPEWA JINA LA UWEKEZAJI.MWEKEZAJI GANI AMBAYE ILI ALIPE MSHAHARA KWA WAAJIRIWA WAKE NI LAZIMA APEWE TAFU NA SERIKALI?

KAMA KAWAIDA,JAMAA WATAHARIBU RELI WEE MPAKA IWE TOO MUCH THEN WATAINGIA MITINI,AU MZEMBE FLANI ATAKURUPUKA USINGIZINI NA KUDAI IUNDWE TUME YA UCHUNGUZI (ISOMEKE TUME YA KULA FEDHA ZA VIKAO) LAKINI WAKATI HUO HUDUMA YA RELI YA KATI ITAKUWA IMEKUFA KABISA.CALL IT MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA AS WE ARE APPROACHING 2009!

6 Dec 2008


MBUNGE wa Jimbo la Buchosa, Samwel Chitalilo ameingia katika mkasa mpya baada ya kudaiwa kumshambulia Mabula Matulanya, ambaye ni mlinzi wa ghati la ofisi ya kivuko cha Nyakaliro Kome, linalomilikiwa na serikali.

Mlinzi huyo anadai alishushiwa kipigo hicho na mbunge huyo kwa kushirikiana na washirika wake wawili mara baada ya kummulika tochi Chitalilo wakati akiwa kwenye haja ndogo karibu na mlango wa ofisi ya kivuko hicho, ambalo ni eneo la lindo lake.

Akizungumza na gazeti hili, mlinzi huyo alidai kuwa, shambulizi hilo lilimkumba Oktoba 10 mwaka huu majira ya saa 3:00 usiku wakati alipoingia kazini kwake kumpokea lindo mlinzi mwenzake. Muda mfupi baada ya kukabidhiwa lindo hilo, alihisi kuwepo kwa mtu katika eneo la ofisi na hivyo kumulika eneo hilo kwa tochi.

Alisema kitendo cha kumulika tochi ndicho kilichomponza na kumsababishia kupata kipigo kutokana na mbunge huyo kukasirika, akidai kuwa alidhalilishwa kwa kumulikwa na tochi wakati akiwa kwenye haja ndogo na kwamba yeye kama mbunge hapaswi kufanyiwa hivyo.

“Nilimulika nikidhani pengine anaweza kuwa mwizi katika lindo lango... sikujua kama ni mbunge na wala sikuwa natambua kama alikuwa katika baa ya jirani akinywa pombe. Nilikuwa kazini, lakini licha ya kumueleza yote hayo nilishikwa na watu wake wawili na kuanza kushambuliwa na mbunge huyo kwa ngumi na mateke,” alidai.

Alidai kuwa baada ya kipigo hicho alikwenda katika kituo cha polisi cha Nyakalilo kutoa taarifa ambapo baadaye, Chitalilo, akiwa na wapambe hao wawili (majina tunayo), walimfuata na kuendelea kumshambulia akiwa kituoni hapo mbele ya mgambo wa kituo anayejulikana kwa jina moja la Shimo.

Alidai baada ya kuzuiwa na mgambo huyo, mbunge huyo na wapambe wake waliamua kupiga simu kituo kikubwa cha polisi ambako walitoa maelekezo kwa askari wa zamu aliyemweka ndani na kesho yake kuchukuliwa na polisi wa kituo kikuu cha wilaya ambao walimwandikisha maelezo.

"Lakini walininyima PF3 kwa ajili ya matibabu jambo ambalo limefanya nitibiwe kienyeji na kupona pasipo kumchukulia hatua yoyote mbunge huyo," alidai mlinzi huyo na kuomba vyombo vya usalama vimsaidie ili aweze kuchukua hatua dhidi ya mbunge huyo kwa vile ameshambuliwa akiwa kazini.

Naye Mbunge Chitalilo, alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu mkasa huo, alikiri kuwepo kwa shambulio hilo na kusema kuwa mlinzi huyo alishambuliwa na wananchi waliokuwa jirani kutokana na yeye kulalamika kudhalilishwa kwa kumulikwa wakati akiwa anakojoa.

“Sikiliza suala hili, mimi nilishalisamehe, polisi kwa kuwaomba wamfutie mashtaka mlinzi huyo kwa vile watu wengi waliniomba samahani... alinidhalilisha kwa kunimulika makusudi licha ya kujua nilikuwa mimi... alishambuliwa na watu ambao nilifanya kazi ya kuwatuliza, sasa mimi kosa langu ni kumsamehe?” alihoji.

Hata hivyo, mbunge huyo alimsihi mwandishi kuachana na habari hizo kwa vile hazina maana katika jamii na kumtaka kufuatilia masuala ya maendeleo katika jimbo lake.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Jamal Rwambow, hakuweza kupatikana kulitolea ufafanuzi jambo hilo kutokana na kuwa katika ukaguzi wa vituo vya polisi jijini Mwanza, ziara ambayo amekuwa akiifanya kwa lengo la kutambua na kubaini matatizo ya jeshi lake mkoani hapa.

CHANZO: Mwananchi

THIS GUY IS A FRAUD.LAKINI HAYA NDIO MATOKEO YA KUANGALIA HAIBA YA MGOMBEA (NA VIJISENTI VYAKE) WAKATI WA KAMPENI YA UBUNGE BADALA YA KUPIMA UWEZO WAKE.HUYU MTU ANA TUHUMA ZA KUFOJI CHETI CHA SHULE,ANADAIWA KUWALIZA WATU FLANI WALOMKOPESHA FEDHA KWA AJILI YA BIASHARA YAKE,NA SASA KITUKO HIKI!MBUNGE GANI MAKINI ATAKOJOA OVYO?KWANI ANGEKWENDA KUJISAIDIA MSALANI ANGEMULIKWA TOCHI NA HUYO MLINZI?HUU NI UHUNI WA KISIASA UNAOHITAJI ADHABU KALI COME 2010.

LAKINI MKASA HUU UNATUSAIDIA KUONYESHA NAMNA HAKI ILIVYO NA TAFSIRI TOFAUTI KATI YA WALALAHOI NA WAHESHIMIWA.MLINZI ALIYEKWENDA KUDAI HAKI YAKE AMEISHIA KUSWEKWA NDANI,MHESHIMIWA ALIYETUHUMIWA KWA SHAMBULIO YUKO HURU AKIJIGAMBA KWA "KUMSAMEHE" VICTIM WAKE!

1 Nov 2008

Picha kwa hisani ya SPOTI NA STAREHE

Ubabaishaji unakwamisha sana maendeleo ya taifa letu.Lakini hapa nataka nizungumzie ubabaishaji kwenye uongozi na uendeshaji wa vilabu vya Simba na Yanga.Hebu soma kwanza hapa chini kabla hatujaendelea na mada hii ya kupotezea muda.
MWENYEKITI wa klabu ya Simba Hassan Dalali amemteua Mkurugenzi wa Kampuni ya Aurora Security, Ally Suleiman kuwa mshauri wake atakayesaidia kumshauri kuhusiana na mambo yote yanayohusu masuala ya uongozi wa Simba. 

Akizungumza Dar es Salaam jana, Dalali alisema ameamua kuwa na mshauri ili aweze kuiendesha klabu yake kwa umakini na kufuata mwongozo ambao utaisadia klabu hiyo. 

Dalali alisema Suleiman amekuwa mtu wa karibu, ambaye ametoa mchango mkubwa ndani na nje ya klabu, hivyo ameona ni muhimu na kuwa uteuzi huo ni kujenga Simba yenye umoja na mshikamano.
Alisema klabu yake ipo katika mikakati ya kuhakikisha Simba inakuwa klabu kubwa, huku ikiimarisha timu yake na kuwa mfano wa kuigwa. 

"Uteuzi wa mshauri wangu umezingatia vigezo vingi ikiwemo ukaribu wake katika mambo ya msingi yanayoihusu klabu yetu," alisema Dalali.

Akizungumzia uteuzi huo, Suleiman alisema amefurahi kupata wadhifa huo na kuahidi kuisaidia klabu hiyo kwa hali na mali lengo likiwa ni kujenga Simba imara
CHANZO:Majira
Baada ya kufungwa na Yanga ndio Dalali anakumbuka umuhimu wa kuwa na mshauri!?Kwa tafsiri nyingine ni kwamba kwa muda wote tangu apate uenyekiti wa Simba m-babaishaji huyu amekuwa akiongoza kwa kubahatisha.Ndio!Kama sio hivyo,mshauri wa nini muda huu? Yaani ni ubabaishaji juu ya ubabaishaji.

Mimi ni mpenzi wa Simba.Zamani Simba ikifungwa basi ni majonzi makubwa.Katika familia yetu,watoto wote wanane tunaipenda Simba.Marehemu Mama (Mungu Amlaze Mahali Pema Peponi) alikuwa mpenzi wa Pan Africa,kwa sababu mpwae,Gordian Mapango,alikuwa mchezaji wa timu hiyo.Baba aliamua kuisapoti Yanga,sio kwa vile anaipenda bali kuleta "usawa" ndani ya familia.

Kwa miaka kadhaa sasa,nimebaki kuwa mpenzi-jina tu,it doesnt really make any difference Simba ikishinda au ikifungwa.Sababu kuu ya kupoteza mapenzi kwa Simba,na soka ya Tanzania kwa ujumla,ni ubabaishaji uliopita kiasi wa viongozi wa klabu hiyo kongwe.Ubabaishaji huo umepelekea timu hiyo kukimbiwa na wafadhili kibao na kupoteza udhamini mbalimbali.Nani mwenye akili timamu atawekeza kwenye biashara kichaa?Ukiona mtu anapanda mpunga jangwani basi hicho sio kilimo bali tambiko.Ndo maana nashawishika kuamini kwamba uwepo wa Manji hapo Yanga unaweza kuwa ni "zaidi ya mambo ya soka".

Nirudi kwenye title ya post hii.Nilitegemea Simba ingefungwa na Yanga.Na nilitegemea kipigo kikubwa zaidi ya hilo bao moja.Kama Toto Africa waliweza kutufunga bao 4-1,tungetegemea nini katika mechi na Yanga?Anyway,kipigo ni kipigo.Mategemeo yangu ya kipigo yametimia,japo kwa idadi tofauti na niliyokuwa naitarajia.Kingine nilichadhani kingeandamana na kipigo hicho ni kuutimua uongozi mzima wa Simba.Hilo halijatokea lakini naamini viongozi hao wamekalia kuti kavu.By the way,uongozi wa Simba na Yanga ni zaidi ya kukalia kuti kavu;ni sawa na kibonge cha mtu kuning'inia kwenye utando wa buibui.Mtu mwenye mtizamo makini hawezi kutamani kuongoza timu hizi za kibabaishaji,ambazo lugha wanayoelewa "wanachama" ni ushindi tu.

Of course,timu inatakiwa ishinde kila mechi.Lakini timu itashinda vipi ikiwa haina vyanzo vya mapato zaidi ya kutembeza bakuli kama ombaomba?Hao wachezaji wanakula nini kabla ya kujituma uwanjani?Au ni timu za kiroho ambapo Neno la Mungu linashinda mahitaji ya fedha na vifaa?Kwanini wachezaji wasipokee rushwa iwapo viongozi wanawaibia mishahara yao kiduchu inayopatikana kwa migomo?Wanachama wababaishaji wa klabu hizi wanajua kupiga majungu tu lakini hawana mchango wowote kwa ustawi wa klabu hizi.Ndio maana akiondoka mfadhili mmoja timu inakuwa hohehahe.Na ndio maana Manji amekuwa mungu-mtu hapo Yanga (na mwenyekiti Madega amegeuka kuwa msemaji wa familia ya mfadhili kuhusu ugonjwa wa mfadhili huyo!)

Je kuna ufumbuzi wa tatizo hili la ubabaishaji wa viongozi na wanachama wa Simba na/au Yanga?Kwa mtizamo wangu nadhani ufumbuzi upo lakini unahitaji udikteta wa aina flani.Unajua kuna udikteta kwa ajili ya watu na udikteta dhidi ya watu.Udikteta kwa ajili ya watu ni kama ule wa Sokoine:kwa wahujumu wa uchumi Sokoine alikuwa dikteta,lakini kwa wananchi wengi kiongozi huyo alikuwa ni shujaa na mkombozi.Sihitaji kuelezea dikteta dhidi ya watu ni wa aina gani,lakini anaweza kuwa hata anayethamini haki za binadamu za mafisadi wachache badala ya walalahoi walio wengi.Je udikteta kwa ajili ya watu unawezaje kuokoa vilabu vyetu na soka la Tanzania kwa ujumla?Ni kwa serikali kutumia sheria kali katika kuleta mageuzi ya kudumu katika vilabu vya soka.Najua kuna ishu za watu kwenda mahakamani kupinga maamuzi flani,lakini ukweli unabaki kwamba sheria zikiandaliwa na kusimamiwa vizuri basi wahuni wanaokimbilia mahakamani watafyata mkia.Njia nyepesi ya kuvibana vilabu hivyo ni kutunga sheria inayovitaka kujisajili upya,kwa mfano.Pia sheria hiyo inaweza kutamka bayana aina ya viongozi,namna ya uendeshaji wa vilabu unavyopaswa kuwa na hata aina za wanachama.FIFA itatufungia kwa vile serikali imeingilia mambo ya soka?Why care!kwani sasa hatujafungiwa na tumeendelea kuwa kichekesho kila mwaka?Bora tu tufungiwe ili tuweze kujipanga vyema kuliko kuendeleza ubabaishaji huu.Au msomaji unasemaje?

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.