12 Oct 2012



Watanidharau, watanicheka, watapambana lakini nitashinda

JOHNSON Mbwambo ameandika katika Gazeti la Raia Mwema la Oktoba 3, mwaka huu, kuhusu dhihaka za Zitto kwa Prof. Muhongo (Waziri wa Nishati na Madini). Nimesoma na nimemuelewa. Kwanza naomba radhi iwapo tafsiri ya taarifa yangu niliyoitoa kwa vyombo vya habari na kuwekwa kwenye blogu yangu (zittokabwe.com) ilikuwa ina dhihaka.
Nimefundishwa kutodhihaki watu na hasa watu wanaonizidi umri na siasa zangu sio za dhihaka bali za masuala (issues). Kupitia kwa ndugu Mbwambo naomba radhi kwa wote walioona kuna dhihaka katika andiko langu. Sikuwa na nia ya kumdhihaki Waziri Muhongo. Nia yangu ni kuonyesha kuwa Waziri Muhongo alichokifanya ni kuwacheza shere Watanzania, kwa kuwaambia maneno ambayo yeye mwenyewe alikuwa anaamini kuwa hayawezekani.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara yake, Eliakim Maswi, ilithibitisha kauli yangu siku chache tu baada ya kuitoa. Mbwambo kaandika makala yake kana kwamba hapakuwa na kauli ya kufuta maneno ya Waziri. Ninaamini Mbwambo aliiona kauli ile lakini aliamua kupuuza ili kujifurahisha na imani yake kwa Prof. Muhongo na mawaziri aliowataja kwenye makala yake kwamba ni mawakala wa mabadiliko. Mbwambo anaamini kabisa kwamba ndani ya utawala wa CCM, kuna mawaziri wenye nia ya dhati ya kuleta mabadiliko.
Nieleze wazi kwamba nilishtuka sana kuona toleo moja la Gazeti la Raia Mwema likiwa na makala tatu, zote dhidi ya Zitto Kabwe. Wakati makala ya ndugu Mbwambo ilikuwa inahusu suala nyeti sana la rasilimali za taifa na ni makala nzuri yenye mafundisho, makala mbili nyingine zilikuwa ni za siasa dhidi ya Zitto. Mwandishi Mayage Mayage aliandika makala yenye kichwa cha habari “Zitto, Urais 2015 kwa chama gani?” na Mwanasafu wa gazeti hili la Raia Mwema, Evarist Chahali aliandika makala yenye kichwa cha habari “Rais Kikwete anapofikiri kama Kabwe Zitto.”
Namwambia Mayage akasome vizuri historia ya ujenzi wa CHADEMA. Yeye anadhani CHADEMA imeanza mwaka 2010. CHADEMA kimejengwa na watu, si mtu mmoja. Wanaoamua mgombea wa chama si watu wachache anaowadhani yeye Mayage bali ni wanachama wa CHADEMA kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania, ikiwamo Munanila, mkoani Kigoma anapotoka Mayage.
Huyu Chahali anasema ananijua sana. Inawezekana ananijua kuliko mimi ninavyojijua. Lakini mimi simjui na wala sijawahi kumwona ana kwa ana, nimekuwa nikimwona tu kwenye mitandao ya kijamii akinizushia, kunitukana na kunisema. Sikushangaa kusoma makala yake ya wiki iliyopita. Wote wawili nawakumbusha msemo wa Mahatma Gandhi aliposema; “Kwanza wanakudharau, kisha wanakucheka, kisha wanapambana na wewe, kisha unashinda".
Sasa nirejee kwenye makala ya ndugu Mbwambo. Prof. Muhongo simjui, licha ya kwamba nimekuwa mmoja wa wabunge walioko mstari wa mbele kuhakikisha utajiri wa nchi unatumika kwa manufaa ya nchi, sikuwahi kumsikia Prof. Muhongo mpaka alipoteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Sikuwahi kusikia akipaza sauti yake dhidi ya mikataba mibovu ya madini licha ya kwamba yeye ni msomi aliyebobea katika masuala ya miamba. Wakati Bunge la tisa, chini ya Spika Samuel Sitta, likiwa limecharuka kutaka mikataba mibovu ipitiwe na kubadilishwa tulitarajia sana kupata ushauri wa wataalamu wetu lakini hawakuonekana, "walikwina"?
Walikuwa waoga kusema maana wangeharibu uhusiano kati yao na watawala. Tulihangaika wenyewe bila maarifa yoyote kuhusu sekta ya madini. Wengine ilibidi kuacha kazi za ubunge na kwenda masomoni ili kuongeza ujuzi wa masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusu sekta ya rasilimali (madini na mafuta).
Wasomi wetu hawakuwa nasi. Walichague kuendelea kufanya kazi za ushauri kwa kampuni za utafutaji madini nchini. Leo Mbwambo anawaona hawa ndiyo mawakala wa mabadiliko. Labda anasema kweli. Ila mimi nimekata tamaa na mabadiliko kuletwa na watu waliomo serikalini, kwa sababu kadhaa.
Moja, kama alivyosema ndugu Mbwambo, nilipigia kelele sana mkataba wa Buzwagi na mikataba mingine ya madini. Niliendelea kupiga kelele mpaka sheria mpya ya madini ilipopitishwa na Bunge. Nimuulize Mbwambo kwamba, licha ya sheria mpya kuandikwa imechukua miaka mingapi kampuni za madini kufanya kazi zao kwa kutumia sheria hiyo mpya? Je, mikataba mingapi iliyopitiwa imerekebishwa au hata kuvunjwa? Pengine niwasaidie kuwakumbusha taarifa kwamba, hakuna kilichofanyika kwa mujibu wa sheria mpya, licha ya kufuatilia kwa kina bungeni kupitia michango na hata maswali bungeni sambamba na makala mbalimbali.
Tangu Waziri Prof. Muhongo na timu yake waingie ofisini ni maneno tu tunayosikia bila matendo. Hata suala la mgawo wa umeme ambalo ndugu Mbwambo analisema kama mfano, yeye anajua namna ambavyo wananchi wanalalamikia umeme kukatika hovyo, tena bila taarifa wala maelezo. Muhongo alifanikiwa sana kuaminisha watu wenye mawazo huru kama Mbwambo wakamwona yupo sahihi kiasi hata cha kufumbia macho mgawo wa umeme usio na maelezo, unaoendelea nchini.
Siwaamini mawaziri kwa sababu wanasema lolote linalowajia midomoni mwao hata kama wanaamini kuwa wanalosema haliwezekani kutekelezwa. Waziri wa Nishati na Madini alisema kuhusu mikataba ya mafuta na gesi ili kufurahisha watu. Huo ni msingi wa kwanza wa kauli yangu ambayo ndugu yangu Mbwambo ameitafsiri kuwa ni dhihaka. Nilikuwa nasema ukweli mchungu kwamba, serikali haiwezi kufanya lolote kuhusu mikataba. Nilitoa changamoto kuwa kama serikali kweli imedhamiria, iweke mikataba hii wazi. Je, wameiweka wazi?
Pili, Waziri wa Nishati na Madini anataka umma umwone kwamba anajua sana masuala ya sekta kuliko Mtanzania mwingine yeyote. Nitatoa mfano mmoja unaonihusu moja kwa moja. Katika mkutano wa Bunge uliopita, Tanzania ilitembelewa na Waziri Mkuu mstaafu wa Urusi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Kirusi iliyonunua leseni ya kutafuta uranium kule Selous. Kampuni ya UraniumOne iliyonunua leseni hii ya Mkuju River Project kutoka Kampuni ya Mantra ya Australia, kwa dola za Marekani milioni 980.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitaka ilipwe kodi ya ongezeko la mtaji (capital gains tax) kampuni hii ilikataa. TRA wakaenda mahakamani kudai malipo ya kodi yenye thamani ya dola za Marekani milioni 116 ambazo ni sawa na asilimia 20 ya thamani ya mauzo na kesi inaendelea. Kwa mujibu wa sheria zetu kampuni zinapouziana leseni, lazima Waziri wa Nishati na Madini atoe idhini ya mauzo hayo. Mgeni huyo kutoka Urusi alikuja nchini kupigia debe idhini hii, ili itolewe leseni maalumu ya uchimbaji (special mining licence).
Nikasimama kutoa taarifa bungeni kwamba mawaziri wanakutana na huyu Waziri Mkuu mstaafu wa Urusi kuhusu leseni ya Mkuju River Project na kuweka wazi kwamba Kampuni ya UraniumOne hawajalipa kodi ya capital gains. Nilisimama kutoa taarifa baada ya majibu ya Waziri Muhongo kwamba, kilichouzwa si kampuni ya Tanzania bali Australia na hivyo hakuna kodi.
Kwa makusudi kabisa niliacha habari ya kesi ya TRA dhidi ya kampuni hii ili kuona umakini wa mawaziri wetu wapya kabla ya kukutana na lobbyists (washawishi) wa kampuni hizi za madini. Waziri Muhongo aliposimamishwa na Naibu Spika, Job Ndugai, akasema “Sisi tunajua zaidi kuliko Zitto" Kwanza Waziri hakuwa anajua.
Ni makosa kabisa kujadili suala ambalo mamlaka mojawapo ya nchi wamelipeleka mahakamani na linasubiri uamuzi. Lakini suala la Waziri kutokuwa na taarifa lilidhibitishwa na ujio wa Naibu Waziri George Simbachawene, aliponifuata na kuomba "details" kuhusu taarifa niliyotoa. Kulikuwa na haja gani kwa Waziri kusema bungeni yeye anajua zaidi na baadaye kumtuma Naibu wake kutafuta taarifa?
Huu ni udhaifu mkubwa sana wa uongozi. Kutojua si makosa, inawezekana kuwa wengine hatukusomea miamba lakini tumesomea masuala ya kodi kwenye madini na mafuta. Waziri makini anayejali nchi yake anawezaje kukutana na mwekezaji anayekataa kukulipa kodi yako bila wewe hata kuulizia utalipwa lini?
Unaulizwa bungeni unasema "ninajua zaidi" na Mwandishi mahiri kama Mbwambo anasema "mpeni nafasi atende"!
Nilipomsikia Waziri anasema ameagiza TPDC (Shirika la Maendeleo la Mafuta) kupitia mikataba nikajua na hili nalo hajui. Amesema tu ili watu wafurahi kwamba mikataba inapitiwa. Kupitia mikataba bila kuchukua hatua dhidi ya mikataba mibovu ni nini kama sio kutafuta umaarufu tu? Unapitia mikataba ili iwe nini kama huwezi kuchukua hatua?
Kuna mikataba ambayo imeingiwa kwa rushwa, sheria zetu zinasema kuwa mikataba iliyoingiwa kwa rushwa ni sawa na haipo. Hata sheria za kimataifa za mikataba zinatambua hivyo. Waziri anaposema kuwa tunapitia mikataba ili kuhakikisha kuwa mikataba ijayo inakuwa mizuri ni kichekesho. Hivi tunajua vitalu vingapi vimegawiwa na vingapi vimebaki? Hivi sasa kuna mikataba 29 na leseni 26. Vitalu vilivyobaki hivi sasa ni tisa tu.
Wizara inatuambia tunaangalia hii mikataba 29 ili kuboresha 9. Haya si mapitio bali ni kuangalia tu kama nilivyosema katika sentensi iliyotangulia. Mapitio bora zaidi ni uwazi wa mikataba yote tuliyoingia mpaka sasa na kuzuia kabisa mikataba mipya wala kugawa vitalu vipya vya kutafuta mafuta na gesi.
Uporaji wa rasilimali ni wa namna mbili, moja ni watu wachache na kampuni zao kupora kwa kupitia mikataba mibovu na pili ni kizazi kimoja kunyonya rasilimali zote bila kujali kizazi kijacho. Katika maandiko yangu nimeshauri kuwa tusigawe vitalu vipya mpaka tuone mafanikio ya mikataba hii 29 na leseni 26 tulizonazo hivi sasa. Wito wangu ni mmoja tu, uwazi wa mikataba. Kutaka uwazi si dhihaka. Uwazi ni uwajibikaji.
Suala la mapitio ya mikataba kwa jicho la juu juu ni suala la kuunga mkono. Lakini ukitazama historia ya nchi yetu katika masuala haya utabaini kwamba tunapaswa kufanya zaidi ya mapitio ya mikataba.
Tunapaswa kufanya jambo ambalo hatujawahi kulifanya nalo ni kuiweka wazi mikataba hii kwa umma. Hii ndiyo hoja yangu.
Inawezekana kabisa kwamba maneno niliyotumia yameudhi watu fulani lakini ikumbukwe mimi ni Mbunge wa Upinzani na ni wajibu wangu kukosoa serikali kila inapowezekana. Bahati nzuri miaka yangu saba bungeni hivi sasa imetumika kwa kiasi kikubwa sana katika kufuatilia kwa karibu sekta ya madini, mafuta na gesi. Ni rahisi sana mimi kuweza kuona suala linalosemwa na serikali linasemwa tu au serikali inamaanisha? Katika suala la mapitio ya mikataba kwenye sekta ya madini na mafuta kwa kweli serikali haipo makini. Watu wajuvi wa mambo kama kina Mbwambo wanapaswa kwenda zaidi ya mapitio na kutaka mikataba iwekwe wazi na kuchambuliwa kwa uwazi kabisa.
Waziri Muhongo anayo nafasi ya kufanya kazi yake, afanye kazi yake bila bugudha. Mbwambo ajue kuwa Mbunge Zitto pia anayo kazi yake kwa mujibu wa Katiba ibara ya 63 nayo ni "kuisimamia" serikali. Niacheni nami nifanye kazi yangu.
Makala hii iliyoandikwa na Kabwe Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini ni majibu kwa makala iliyoandikwa na Mwanasafu wetu, Johnson Mbwambo, katika toleo lililopita la gazeti hili la Raia Mwema, kupitia safu yake ya Tafakuri Jadidi.
MAONI: NI KWELI ZITTO HANIJUI, NA KATIKA MAKALA HUSIKA NILIANDIKA "NAMJUA ZITTO VIZURI" NA SIO "TUNAJUANA VIZURI." NA KIMSINGI, HAKUPASWA KUNIJUA WAKATI NILIPOKUWA NAMJUA (KINYUME CHA HIVYO,JUKUMU ZIMA LA KUMJUA LISINGEKUWA NA MAANA). BY THE WAY, HIVI ZITTO ANAMJUA KILA MPIGA KURA KATIKAJIMBO LAKE, LET ALONE MIE AMBAYE SIKUMPIGIA KURA?

SIKUANDIKA KUWA NAMJUA ZITTO VIZURI KWA MINAJILI YA KUSAKA SIFA AU KUJIKOMBA KWAMBA "NINAMFAHAMU VIZURI RAIS MTARAJIWA" BALI NILIANDIKA HIVYO KUPIGIA MSTARI KUWA MWANASIASA NINAYEMZUNGUMZIA NI MTU NINAYEMFAHAMU (KIVIPI,WAPI...NAOMBA NISIZUNGUMZIE HILI KWA MUDA HUU).

SITAKI KUMWITA MHESHIMIWA ZITTO MBABAISHAJI LAKINI MAKALA YAKE HII INANISHAWISHI KUFIKIRIA HIVYO.ZITTO ANAZUNGUMZIA MIE KUMJUA, ANADAI NINAMTUKANA (HIVI RAIS MTARAJIWA HATAMBUA KUWA MTU AKIKUTUKANA KWENYE TWITTER UNAPASWA KUMRIPOTI KWA WAMILIKI WA MTANDAO HUO BADALA YA KULALAMIKA KWENYE MAKALA?).HUYU ANAYEDAI NINAMTUKANA NDIYE SAME PERSON ALIYEANDIKA HAYA  ni upumbavu kufikiri kwa misingi wa kidini. Huna haki kuleta ubaguzi wako wa kidini hapa. 3 out of 15 muslims, unaita ubaguzi? (chanzo: http://goo.gl/8MLDO

Mwanasiasa huyu mbabaishaji alinilaumu kwa "kuleta ubaguzi" lakini yeye si mbaguzi anapodai watu waliozaliwa kabla ya uhuru hawawezi kutuletea maendeleo ya kiuchumi.

NIMALIZIE KWA KUWAACHIA WASOMAJI FURSA YA KUAMUA WENYEWE IWAPO MHESHIMIWA ZITTO AMEJIBU HOJA (NINAZOZIONA) ZA MSINGI KATIKA MAKALA HII







8 Oct 2012



NIMEKUWA nikiulizwa swali hili takriban kila wiki baada ya makala zangu kuchapishwa katika jarida hili maridhawa: Hivi kuna wakati unaishiwa na cha kuandika? Na siku zote jibu langu linakuwa lile lile; Tanzania yetu haiishiwi mambo yanayopaswa kujadiliwa-iwe gazetini, mtandaoni, kijiweni au popote pale. Kuweka rekodi sawia, kila ninapoingia mtandaoni huwa ninakumbana na wastani wa angalau habari tano zinazoweza kutengeneza mada za makala zangu.
Wiki hii nitazungumzia matukio mawili makubwa yanayoihusu CCM na CHADEMA. Kwa namna moja au nyingine, matukio yote mawili yanahusiana, na nitajitahidi kuonyesha uhusiano wao mwishoni mwa makala haya.
Tukio la kwanza ni kauli ya Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kwamba CCM haitokufa, na pengine wanaodhani hivyo wanaweza kufa wao kabla ya chama hicho tawala kufa.
Kwa baadhi yetu tunaosoma siasa kama eneo la taaluma, tunatambua ukweli mmoja, kwamba chama cha siasa kinazaliwa, kinakua, na kama ilivyo kwa binadamu, kinaweza kufa. Na tofauti na binadamu ambao hatuna udhibiti mkubwa wa kurefusha au kufupisha maisha yetu (kuna watenda dhambi na wanaotumia kila aina ya ‘sumu’-pombe, dawa za kulevya na kadhalika ama kumkera Muumba au kuharibu afya zao-lakini si tu wapo hai bali pia wana afya za kuridhisha, huku wengine mambo yao yakizidi kuwanyookea, huku upande mwingine kukiwa na wacha Mungu, wanaojali afya zao lakini wanataabika muda huu); Vyama vya siasa vinaweza kurefusha maisha yao kwa kuitumikia jamii kulingana na matarajio ya jamii husika au ikaipuuza jamii hiyo na kujichimbia kaburi.
Pamoja na heshima yangu kubwa kwa Rais Kikwete, ninaomba kutofautiana naye katika kauli hiyo kuwa CCM haitokufa. Si tu kuwa vyama vya siasa hufa, bali pia ninaamini kuwa kila Mtanzania anayefuatilia kwa karibu historia na mwenendo wa chama hicho anaweza kabisa kubashiri kuwa ama mwanzo wa mwisho wake unakaribia au kinaharakisha kifo chake.
Simlaumu Rais Kikwete kwa kauli hiyo kwa sababu kama Mwenyekiti wa Taifa wa Chama anachoongoza ana jukumu kubwa la kuwahakikishia viongozi na wanachama wenzake kuwa ‘mambo si mabaya’ kama inavyoelezwa na wapinzani wao.
Binafsi, nasema kinachoweza kuiua CCM kabla ya wakati wake, ni pamoja na mtizamo huo wa Rais Kikwete wa kwamba ‘chama hicho kipo imara na kinaendelea kupendwa na Watanzania wengi-uthibitisho (kwa mujibu wao) ni idadi ya wana-CCM waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali kwenye chaguzi zinazoendelea ndani ya chama hicho.
Ni kweli kwamba idadi ya waliojitokeza kugombea inaweza kujenga picha kuwa CCM bado kinapendwa na wengi. Lakini haihitaji ufahamu mkubwa wa siasa zetu kumaizi kuwa baadhi ya wanaokimbilia uongozi ndani ya chama hicho wana ajenda zao binafsi. Ikumbukwe kuwa huko nyuma chama hiki kilishaonyesha dhamira ya kutenganisha biashara na siasa, hatua iliyotafsiriwa na wengi kuwa ni kutambua kuwa kuna kundi la wafanyabiashara wanaokimbilia kwenye siasa si kwa minajili ya kuutumikia umma, bali kusaka ‘kinga’ ya kuwalinda katika biashara zao.
Binafsi, nilikuwa miongoni mwa wapinzani wakubwa wa wazo hilo, si tu kwa sababu siafikiani na aina yoyote ya ubaguzi, bali pia sikuona kuwa tatizo ni wafanyabiashara kujihusisha na siasa bali wafanyabiashara ‘wachafu’ kuruhusiwa kujihusisha na siasa. Kwa kuharamisha biashara kwenye siasa kungeweza kuwa na hatari ya kuwakwaza wazalendo wazuri tu ambao walichagua kujihusisha na biashara kabla ya kuingia kwenye siasa.
Na ingekuwa ubaguzi wa wazi kuwazuia wafanyabiashara kujihusisha na siasa, lakini kuwaruhusu askari wastaafu, wasomi na wanajamii wengineo kufanya hivyo. Sawa, wanasema samaki mmoja akioza basi wote wameoza, lakini usemi huu hauzingatii ukweli kwamba binadamu hutofautiana.
Kwa mfano, kwa vile Mndamba wa kwanza kumfahamu ni mie ambaye pengine ninakukera na kwa mtizamo wangu haimaanishi kuwa kila Mndamba utakayekutana nae maishani atakukera. Waingereza wana msemo kuwa “people vary because we differ” yaani watu huwa na tofauti kwa sababu wanatofautiana, na kwa mantiki hiyo hiyo, mfanyabiashara anayeingia kwenye siasa kwa minajili ya kujitengenezea kinga katika ufisadi wake kwa taifa, haimaanishi kuwa kila mfanyabiashara anayeingia kwenye siasa ana malengo hayo.
Ninaamini kilichopelekea CCM kudhamiria kumtenganisha biashara na siasa ni historia na uzoefu iliopata kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara walioingia kwenye siasa. Na wazo lilikuwa zuri, kwamba mfanyabiashara atakayeamua kuingia kwenye siasa achague moja: biashara au siasa.
Tukirejea kwenye tamko la Kikwete kuwa CCM haitokufa, yayumkinika kuamini kuwa kauli hiyo ni ya kujipa matumaini tu na kukwepa ukweli kwamba kwa kiasi kikubwa chama hicho kinaonekana machoni mwa baadhi ya Watanzania kuwa ni chanzo cha matatizo mengi yanayoikabili nchi yetu. Kwa kifupi, kitakachoiua CCM si kauli za hao wanaoikitabiria kifo bali matendo ya chama hicho ambayo kimsingi ndio ‘pumzi’ inayokifanya kiwe hai.
Tukio jingine ambalo kwa namna moja au nyingine linahusiana na uhai wa chama cha siasa (kwa maana ya kuwa hakitokufa au la) ni tamko la Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe (CHADEMA), ya kwamba hatogombea ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015, bali atagombea urais.
Kwanini ninalinganisha tamko la Zitto na kauli ya Mwenyekiti wa CCM, Kikwete? Jibu fupi ni kwamba matamko yote mawili yanaelekea kupuuza hali halisi ya mwenendo wa siasa za huko nyumbani.
Wakati Mwenyekiti Kikwete anajigamba kuwa CCM haitokufa japo kuna mamia kwa maelfu ya wana-CCM wanaokihama chama hicho kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wake, huku pia baadhi ya viongozi wa chama hicho kama kina Samuel Sitta wakionyesha hadharani ‘maovu’ ya chama hicho, Zitto hataki kujihangaisha kutambua wengi wa Watanzania wanamtaka mwanasiasa gani kutoka chama chake ili kubeba dhamana ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Kabla sijaendelea kuijadili kauli ya Zitto, ningependa kuweka bayana masuala matatu ya msingi. Kwanza, Zitto ana kila haki si tu ya kutaka kuwa Rais wa Tanzania, bali pia kutangaza kuwa ana nia hiyo. Ni haki yake ya kidemokrasia, hasa ikizingatiwa kuwa anatoka katika chama cha Demokrasia na Maendeleo.
Pili, ni suala la kukubalika kwa wapiga kura watarajiwa (potential voters). Kila mara ninapomsikia Zitto akielezea dhamira yake ya kutaka kuwa Rais, huwa ninajiuliza swali moja la msingi; ni lini amefanya ‘utafiti’ wa kutambua Watanzania wanamhitaji awe rais wao?
Wenzetu huku Magharibi, kabla mwanasiasa hajakurupuka kutangaza kuwa anataka kuwa rais huwa inamlazimu kujihangaisha ‘kusoma upepo,’ yaani kufahamu iwapo wapigakura wanamhitaji.
Sawa, Tanzania si nchi ya Magharibi, na pengine hakuna umuhimu wa kusaka mtizamo wa wapigakura. Lakini kwa mwanasiasa anayejali maslahi ya chama chake na wananchi kwa ujumla, yayumkinika kuamini kuwa atajihangaisha kufahamu iwapo dhamira yake ya kugombea ni kwa maslahi ya chama chake na umma kwa ujumla au ni kwa ajili ya kutimiza ndoto zake binafsi tu.
Suala la tatu, na ambalo kwangu si tu ni la msingi zaidi bali pia linanishawishi kuamini kuwa dhamira ya Zitto kugombea urais ni sawa na kubariki ushindi wa CCM hapo 2015, ni uadilifu wa mwanasiasa huyo.
Ninamfahamu Zitto vizuri, na si kupitia social media. Ni mmoja wa wanasiasa wachache wenye kipaji cha hali ya juu katika ujenzi wa hoja. Lakini, kama mwanadamu mwingine, mwanasiasa huyo ana mapungufu fulani. Kwa wanaomfahamu kupitia social media (hususan Twitter) wanaweza kuafikiana nami kuwa si mwepesi sana wa kuafikiana na watu wenye mtizamo tofauti na wake.
Ni rahisi kumhukumu kuwa ana jazba (japo sitaki kuamini hivyo) pindi mtu anapotofautiana naye katika anachoamini yeye kuwa ni sahihi. Nafasi haitoshi kutoa mifano halisi, lakini waliotofautiana nae kimtizamo ndani ya Twitter wanaweza kuwa mashahidi wazuri.
Tatizo la msingi kuhusu Zitto ni ‘tuhuma’ zilizowahi kuandikwa na jarida moja la kila wiki kwamba katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu uliopita, jarida hilo lilinasa mawasiliano kati ya mwanasiasa huyo na mmoja wa viongozi wa juu wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Katika mazingira ya kawaida, mwanasiasa wa chama cha upinzani kuwa na mawasiliano na mtumishi wa taasisi hiyo nyeti (ambayo ilishutumiwa na CHADEMA-ambayo Zitto ni mbunge wake-kuwa ilikihujumu chama hicho kwenye uchaguzi huo) inazua maswali kadhaa.
Ndio, watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa ni Watanzania wenzetu kama ilivyo kwa wanasiasa wa vyama vya upinzani. Lakini mawasiliano kati ya mwanasiasa wa chama cha upinzani kama Zitto na kiongozi wa idara hiyo, yanaweza kuibua maswali mengi. Kibaya zaidi, Zitto hajawahi kutoa ‘maelezo ya kueleweka’ kuhusu mawasiliano hayo.
Kimsingi, Zitto anatambua bayana hisia zilizojengeka baada ya habari hiyo kuchapishwa. Kuna waliotafsiri kuwa mawasiliano hayo yalilenga kukihujumu chama hicho, na kwa kuzingatia mantiki ya kawaida tu hatuwezi kuwalaumu kwa hisia hizo.
Lakini pengine kubwa zaidi ni kwanini bado kuna idadi kubwa tu ya wafuasi wa CHADEMA wanaotafsiri uamuzi wa Zitto kutaka urais kama ‘tamaa ya madaraka.’ Hivi akiweka kando imani yake kuwa ana uwezo na uadilifu wa kuongoza taifa la Tanzania, Zitto ameshawahi kufikiria kuwashawishi sceptics hawa hata kama hoja zao hazina mashiko?
Kubwa zaidi ni ukweli kwamba matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita yanaonyesha bayana jinsi mgombea urais kupitia CHADEMA, Dk Willibrod Slaa, alivyokubalika kwa idadi ya kuridhisha tu wapiga kura. Kama dhamira ya Zitto ni kuona CHADEMA inaingia Ikulu, kwanini asiwekeze jitihada kumsapoti Dk Slaa katika uchaguzi ujao na kusubiri ‘zamu yake’ hasa kwa vile umri bado unamruhusu hata kwa miaka mingine 15 ijayo?
Kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano, mgombea urais sharti awe na miaka 40. Mwaka 2015 Zitto atakuwa na umri pungufu na huo. Hivi kung’ang’ania kuwa anataka kugombea ilhali akijua Katiba haimruhusu si ni dalili ya tamaa ya madaraka?
Nimalizie makala haya kwa kulinganisha matukio mawili haya niliyozungumzia. Kama ambavyo Rais Kikwete hataki kujiuliza kwanini baadhi ya watu wanaitabiria kifo CCM, Zitto hataki kujiuliza kwanini baadhi ya watu wanatafsiri dhamira yake ya kutaka urais mwaka 2015 kama mikakati wa kuirejesha CCM madarakani na kuinyima CHADEMA nafasi hiyo.
Suluhisho katika masuala hayo mawili, linaweza kupatikana katika busara hii ya Waingereza isemayo “never ever put emotions in front of common sense” (kwa tafsiri isiyo rasmi, kamwe usitangulize hisia mbele ya tabasuri/ busara).


30 Sept 2012




27 Sept 2012



NINAAMINI takriban kila msomaji wa magazeti ameshawahi kukumbana na sentensi hii inayokera ya “jina linahifadhiwa kwa sasa.”
Kinachokera si tu kuhifadhiwa kwa jina la mhusika mkuu katika habari bali ukweli kwamba mara nyingi habari husika hugeuka kuwa mithili ya mtihani uliojaa mafumbo, na pasipo msomaji “kujumlisha 2 na 2 kupata 4” hakuna uwezekano wa habari hiyo kuleta maana yoyote.
Mifano ni mingi lakini mfano mwafaka ni katika habari ambayo nitaizungumzia pia kwenye makala hii. Kwa siku kadhaa, magazeti mbalimbali yalikuwa yakiripoti taarifa kuhusu mke wa kigogo wa Jeshi la Polisi, ambapo utambulisho wa kigogo huyo na mkewe umebaki kuwa “umehifadhiwa,” akihusishwa na utapeli wa mamilioni ya shilingi kwa ahadi ya kuwapatia watu ajira kwenye vyombo vya dola.
Kabla ya kujadili tukio hilo la utapeli wa aina yake, tuendelee na mjadala wa tabia inayozidi kuota mizizi kwenye magazeti yetu ya “jina limehifadhiwa.” Japo uelewa wangu wa sheria ya kumkashifu mtu/taasisi (Defamation Law) ni wa wastani, siku zote kama mwandishi wa blogu na makala nimekuwa makini kuhakikisha kuwa ninapotaja jina la mtu au taasisi kwenye habari husika, nina uhakika na ushahidi ninao.
Kwa msingi huo, sioni haja ya kutumia sentensi “jina linahifadhiwa kwa sasa” (na mara nyingi hiyo ‘sasa’ hugeuka kuwa ‘milele’) kwa sababu iwapo mtajwa katika andiko husika ataamua kunipeleka mahakamani kwa madai ya kumkashifu, nitapambana naye vilivyo.
Nadhani sababu kubwa ya waandishi wetu kusaka hifadhi ya “jina linahifadhiwa kwa sasa” kwenye kuficha majina ya wahusika katika maandiko yao ni uoga wa kuburuzwa mahakamani kwa madai ya kashfa dhidi ya mtajwa. Na sababu pekee inavyoweza kusababisha uoga huo ni ukosefu wa facts au ushahidi kamili.
Ni wazi kwamba sheria ipo upande wa mwandishi pindi anapoandika habari ambayo imejitosheleza, kwa maana ya kuwa na ushahidi usiopingika kuhusu mtajwa katika habari husika.
Kimsingi, taaluma ya uandishi wa habari inashabihiana kwa kiasi kikubwa na ushushushu katika namna habari inayotafutwa. Katika taaluma zote lengo ni kupata habari kwa minajili ya kuziwasilisha sehemu fulani: kwa msomaji kwa upande wa wanahabari, na kwa mwajiri kwa upande wa mashushushu.
Tofauti za msingi katika utafutaji na matumizi ya habari ni kwamba wakati mara nyingi wanahabari wanapaswa kuwa ‘wazi’ wanaposaka habari (kupata habari kwa udanganyifu kunaweza kuwa kosa la jinai), takriban mara zote mashushushu husaka habari kwa kificho (na kwa mujibu wa sheria, shushushu kujiweka wazi-au kujiumbua-ni kosa).
Kwa upande wa matumizi ya habari zilizopatikana, wanahabari wanatarajiwa kuziwasilisha kwa msomaji (tukiweka kando taratibu za kiuhariri ndani ya chombo habari husika) ilhali kwa mashushushu habari, ambayo wakati huo hugeuka kuwa taarifa, huwasilishwa kwa chombo husika kwa hatua nyinginezo.
Kwa hiyo, tofauti ya kimsingi ya mwanahabari na shushushu ipo zaidi kwenye ‘habari’ na ‘taarifa.’ Wakati habari ni kitu cha wazi na kwa ajili ya matumizi ya umma, taarifa ni kitu cha siri na ni kwa ajili ya matumizi ya taasisi ya kishushushu tu.
Sasa tunachoshuhudia katika uandishi wetu wa “jina limehifadhiwa kwa sasa” ni mithili ya ‘mchanyato wa habari na taarifa,’ kwa maana ya ‘kuwasilisha habari nusu kama mwanahabari lakini pia nusu kama shushushu - nusu wazi nusu siri.’
Ni adhabu kubwa kwa msomaji anapokutana na habari iliyoandikwa kwa mfumo huu “kigogo mmoja (jina linahifadhiwa) wa taasisi moja (jina linahifadhiwa) anadaiwa kulimbikiza fedha zilizopatikana kifisadi katika nchi moja (jina linahifadhiwa).” Kimsingi, habari hii haina umuhimu zaidi ya kuuza gazeti husika na kusumbua ubongo wa msomaji.
Kwa nini mwandishi husika asihakikishe anapata facts zote kuhusu mhusika katika habari hiyo kabla ya kukurupuka kuiripoti nusu nusu? Ninatambua kuwa baadhi ya wanahabari wanaweza kujitetea kuwa wanafanya hivyo kwa minajili ya ‘kumshtua mhusika’ kwamba matendo yake yanafahamika lakini kimsingi hilo si jukumu la chombo cha habari. Kama kuna maovu yasiyoandikika gazetini basi yawasilishwe kwa taasisi za dola badala ya kuwachosa wasomaji na ‘habari za kificho.’
Turejee kwenye sakata la utapeli unaodaiwa kufanywa na mke wa kigogo wa polisi ambao kwa pamoja “majina yao yameendelea kuhifadhiwa” na vyombo vya habari vilivyokuwa vinaripoti habari hiyo.
Awali iliripotiwa kuwa mke wa kigogo huyo alijipatia mamilioni ya shilingi kwa ahadi ya kuwapatia ajira vijana 120 kwenye Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Rushwa (TAKUKURU).
Habari zaidi zilizeleza kuwa Jeshi la Polisi lilikuwa likimlinda mke huyo wa kigogo (na hii si ajabu kwani yeyote anayefahamu utendaji kazi wa vyombo vyetu vya dola anatambua kuwa viongozi wake na watu wanaowahusu ni miungu-watu wasiopaswa kusumbuliwa kwa aina yoyote ile).
Kwa mantiki hiyo, Polisi kumlinda mke wa kigogo wa jeshi hilo ni jambo la kutarajiwa japo si sahihi.
Baadaye ikaripotiwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa Othman Rashid amelitaka Jeshi la Polisi kumkamata na kumchukulia hatua mwanamke huyo. Katika hatua ya nadra mno, Othman alisema (ninanukuu) “Nimewasiliana na IGP (Said) Mwema ili aweze kunipa ufafanuzi kuhusu mke wa kigogo huyo, lakini nashukuru amenipa ushirikiano na kuniambia kuwa suala hilo wanalishughulikia kisheria zaidi. Watanipa taarifa pindi watakapokuwa wamekamilisha.”
Lakini katika kile unachoweza kudhani ni tamthiliya isiyopendeza machoni, habari hiyo ikageuka sarakasi na kugeuka kuwa (ninanukuu) “Wakazi wawili wa jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na makosa 12 ya kujipatia sh milioni 102 kwa njia ya udanganyifu wa kuwatafutia vijana kazi katika Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi la Polisi.”
Miongoni mwa wanaotajwa ‘kutapeliwa’ ni mke wa Mkuu wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja, aliyatajwa kwa jina moja tu la Happyphania, ambaye inadaiwa alitapeliwa shilingi milioni 5 “kwa madai kuwa ni malipo ya maombi ya usajili wa mafunzo ya POLISI (herufi kubwa kwa sababu maalumu), TAKUKURU na Idara ya Usalama wa Taifa.
Swali la kwanza, hivi kweli inaingia mke wa Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi atoe fedha kwa ‘matapeli’ ili kumpatia nafasi ya usajili wa mafunzo ya Jeshi la Polisi ambako mumewe si tu ni mmoja wa vigogo wa ngazi za juu bali pia ndiye mwenye dhamana ya MAFUNZO kwa wanaojiunga na jeshi hilo?
Swali la pili, tukiamini kuwa watu hao wawili waliokamatwa na kufungulia mashtaka (wote si wanawake), kwanini basi Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa alimtaka IGP kushughulikia suala la “mke wa kigogo wa polisi”? Hivi kweli inaingia akilini “mke wa kigogo wa polisi” awe “hao washtakiwa wawili wa kiume”?
Maswali ni mengi, ikiwa ni pamoja na kitendo cha mke wa Kamanda Chagonja kutoa fedha kwa matapeli hao. Pasi kuuma maneno, hivi kutoa fedha kwa ajili ya kupata huduma inayotolewa bure si rushwa? Kwanini basi waliopokea fedha hizo washtakiwe lakini waliotoa fedha wasishtakiwe kwa kutoa rushwa?
Ninatambua uwezekano wa utetezi wa “waliotoa fedha hizo ni victims (majeruhi) wa utapeli.” Hiyo inaweza kuwa kweli tu kwa watu wasiofahamu utaratibu wa kujiunga na taasisi hizo. Sitaki kabisa kuamini kuwa mke wa Kamishna Chagonja hafahamu utaratibu huo hadi kushawishika kutoa fedha kwa washtakiwe hao.
Katika moja ya habari inayomnukuu kigogo wa polisi ambaye kama kawaida jina lake lilihifadhiwa, alisema “…Hata mke wangu ni mmoja wa waliotapeliwa. Alikusudia kuwapeleka wanafamilia watatu akiwemo mtoto wake, mke wa kaka yake na wifi yake ambaye tunamlea.” Mke wa kigogo wa polisi anatapeliwa kuingiza nduguze kwenye jeshi hilohilo analofanya kazi muwewe? Huu ni utani mbaya kabisa.
Kama ilivyo desturi, habari hiyo ndio imeishiwa hapo. Magazeti yaliyokuwa yakiripoti kuhusu mke (jina limehifadhiwa) wa kigogo wa polisi (jina limehifadhiwa) yamemaliza kazi yao na kumwachia kazi msomaji kujumlisha 2 na 2 apate 4.
Na tabia hii ya kukera ya “jina limehifadhiwa” inachangia kuonyesha ubaguzi wa wazi wa kimatabaka. Sijawahi kuona sentensi ya “jina linahifadhiwa” ikitumika kwa tuhuma zinazowahusu walalahoi bali ni kwa vigogo pekee.Ni kwa vile uwezekano wa walalahoi hao kwenda mahakamani kudai wamekashifiwa na gazeti husika ni mdogo au ni kupuuza tu haki zao za kibinadamu?
Mwisho, wakati nina uhakika kuwa majina ya kigogo wa polisi na mkewe anayedaiwa kutapeli yataendelea kuhifadhiwa ‘milele’ (habari yenyewe ni kama imeshakufa kifo cha asili), harakati za kupigania uhuru wa vyombo vya habari hazitozaa matokeo tarajiwa kama vyombo vya habari vitaendeleza kasumba ya “jina linahifadhiwa” ambayo inainyima jamii uhuru wa kuelewa habari husika.


21 Sept 2012


Zitto Kabwe, Let Dr. Muhongo Do His Job


Energy sector has brought to a disgraceful ending some very promising careers. It has sent packing very powerful and prominent figures in the country’s upper echelons of power; Infarct, at one point, it almost brought down the entire government, when the country’s premiere at the time, faced grand corruption allegations, and was forced to resign. It is our economic sector, by far mired by grand corruptions and ineptness. 

Reason behind all these has been nothing more than the bogus contracts. There is therefore, a critical need to review and even terminate some of the existing contracts in the eyes of the public, in order to close the loopholes fleecing the country of its wealth 

The Kigoma North Legislator, Zitto Kabwe, has unleashed in the past few days, some scathing attacks on the Minister of Energy Sospeter Muhongo, for proposing a thorough review of the Gas exploration contracts. Mr. Kabwe described Dr. Muhongo’s statements as irresponsible, publicity stunts and cowboy’s approach at the expense of transparency. What I found rather irresponsible, odd, flawed and vague, was the broad idea of “Transparency” in which Mr. Kabwe is attacking Dr. Muhongo’s premise without providing a practical solution under conventional wisdom

I also found Mr. Kabwe’s idea of shelving gas exploration for ten years as logically, and economically naïve. At best I would describe the proposition as a theory that contravenes the basic and natural economic principles that cannot be implemented in a needy nation like ours. Implementing this thought would be nothing short of economic suicide for a nation whose economy is extremely fragile. 

Mr. Kabwe’s Transparency assertion reveals nothing short of tactical political, intimidation, representation and defense of the unknown interests. I would not go as far as describing the verbal assault as a self serving personal act of vengeance. However, the premise under which Mr. Kabwe’s argument is based, and his pattern of attack, points towards just that.

Mr. Kabwe unambiguously failed to explain how making transparent shoddy contractual agreements, will benefit the country without identifying the loopholes and deficiencies through extensive review. Arguably, lack of legal and technical knowhow to intimately interpret word by word in the existing contracts to weed out the elements tilting the scale on the favor of investors and shadowy forces of corruption, would have lent Mr. Kabwe’s proposition of transparency, some flesh to stand the test in opposition Dr. Muhongo’s hypothesis

Mr. Zitto ought to understand that, major foreign companies operating in Africa have tremendous resources. They have access to some of the best lawyers, and subject matter experts with extensive experience in contractual review, interpretation, negotiations, and writing. A fact which has many a times, led to the creation of lopsided contracts that have benefited investors while fleecing the host country. 

Mr. Kabwe failed to provide a balanced approach to those deficiencies. In my opinion, Dr. Muhongo’s approach is heroic, and nationalistic. The public should, without reservation throw its absolute support behind this man for his position to temporarily suspend and review all the current contracts related to gas exploration and even electricity production

Having worked in the Investment Banking –Capital Markets- Can affirm to the fact that, success or failure of an investment, primarily depends upon how crafty a contract is. Managers across all economic sectors assemble top legal minds and experienced subject matter experts that would pull off successful investments through favorable and well structured contracts. These contracts at the same time have in them, clauses and provisions that provide room for ongoing review and amendments contingent upon the prevailing conditions or circumstances and market situations. 

My only question is why Zitto is up in arms trying to block the review of questionable contacts in the public eyes, what is his fear? Singapore, India, Venezuela, Brazil etc. in recent years, radically modernized and even terminated some contracts with foreign investors in various sectors that were becoming economic liabilities or not equitably representative. This is how things work be it in municipalities, public or private companies, sovereign states and government agencies. Dr. Muhongo as a subject matter expert has suggested just that. Why should he face political interference? 

From my understanding, TPDC, a body tasked with the contractual review is not a political body. It is a professional entity made of subject matter experts –seasoned professionals -. If Mr. Zitto is dissatisfied with TPDC current formation or the capability, he should demand the overhaul of its management team for a more qualified one, which will execute the task –contractual review- diligently, impartially and independently for the interest of the nation. All findings thereafter be made public to satisfy his demand for transparency 

Political meddling, intimidation and personal hostility are not doing the country any good considering the fact that, main victims of bad contracts in the energy sector are the country’s economy, and the public at large. Politics should be kept off professional undertakings. Mr. Kabwe should let Dr. Muhongo do his job. This man has been in the office for a very short period. He has taken bold and risky decisions no other minister has ever taken in the ministry and the energy sector in general. He is stepping on dangerous toes for the best interest of the country, and what he needs the most at this point is our support not interference

Dr. Muhongo’s success or failure is not going to be measured by how many politicians he pleased or displeased, but on what he delivered to the country at the time of need. Soon or later, the public will know whether he was a bluff or a HERO he painted himself to be.  Dr. Muhongo’s approach is the right step in the right direction. Wrong step into the wrong direction is to politically interfere with his work in the name of transparency. Give him a chance to do his Job
 
Mungu Ibariki Tanzania



Forwarded  by Dr Shaban Nzori. "Mzalendo Mtanzania" is Mr Mashaka John.

19 Sept 2012


Evarist Chahali
Uskochi
Toleo la 259
19 Sep 2012


































NIANZE makala hii kwa kurejea simulizi moja ambayo nimeshawahi kusimulia katika makala zilizopita.
Kati ya mambo yaliyonishangaza sana baada ya kuwasili hapa Uingereza kwa mara ya kwanza, takriban muongo mmoja uliopita, ni jinsi Ukristo ulivyopoteza nguvu miongoni mwa Waingereza wengi.
Licha ya ‘kutolewa ushamba’ kwa kushuhudia vitu mbalimbali ambavyo kabla ya kuja hapa vilikuwa ni vya kufikirika tu kama si kuviona kwenye filamu na runinga, kilichoniacha mdomo wazi zaidi ni pale nilipoona jengo ambalo zamani lilikuwa kanisa limegeuzwa klabu ya anasa za usiku (night club).
Kwa Mndamba mie niliyezaliwa sehemu (Ifakara) ambayo ina historia ya karibu na umisionari, kuona ‘nyumba ya Bwana’ imegeuzwa ukumbi wa anasa lilikuwa jambo la kushangaza mno. Na kadri nilivyozidi kuielewa nchi hii ndivyo nilivyozidi kutambua kuwa idadi kubwa tu ya Waingereza haina muda na Mungu au dini kwa ujumla.
Kila nilipopata wasaa wa kudadisi sikusita kuuliza swali hili, “hivi imekuwaje ninyi mliotuletea Ukristo huko Afrika leo hii mnaonekana hamna habari na dini hiyo ilhali dini inazidi kupamba moto huko kwetu?”
Majibu ya swali hilo yalikuwa tofauti kati ya mtu mmoja na mwingine, lakini jibu lililojitokeza mara nyingi zaidi ni kuwa imani ya kiroho haina nafasi muhimu katika zama hizi za sayansi na teknolojia.
Kimsingi, katika Jumapili ya kawaida, makanisa mengi ya Uingereza hujaza ‘wageni’ (kwa maana ya wakazi wenye asili ya nje ya nchi hii, hususan Waafrika na Wakritso kutoka Ulaya ya Mashariki).
Katika siku za kati ya wiki, mengi ya makanisa hayo yamekuwa kama vivutio vya utalii hasa ikizingatiwa kuwa mengi ya majengo hayo ya ibada yana sehemu muhimu katika historia za sehemu yaliyopo.
Lakini ukidhani kufifia huko kwa ‘dini ya nchi hii’ (kimsingi Uingereza ni nchi ya Kikristo na Malkia anaendelea kuwa ‘mkuu wa heshima’ wa Kanisa la Anglikana duniani) kunawafanya Waingereza kutokuwa watu wa kufuata maadili, basi ukienda sehemu mbalimbali za huduma (kama vile kwenye benki, maduka makubwa nk) au ofisini utakumbana na picha tofauti kabisa.
Kwanza, kwa kiasi kikubwa hakuna njia za mkato za kupata fedha katika nchi hii pasipo kuwajibika. Pili, Waingereza wengi wanachukulia shughuli zao kwa uzito na umuhimu mkubwa. Lakini jingine kubwa ni jinsi serikali na taasisi za utawala zinavyojibidisha kutengeneza mazingira mazuri ya kumwezesha kila anayejituma ‘avune matunda ya jasho lake.’
Kuna suala la haki na wajibu. Kwa kiwango kikubwa, wengi wa Waingereza wanatambua wajibu wao wa kulipa kodi, na wajibu huo unawapatia haki ya kupatiwa huduma ambazo kwa kiasi kikubwa zinakidhi matakwa yao.
Kadhalika, taasisi mbalimbali za hapa zinatambua wajibu wao wa kutoa huduma zinazoendana na matakwa ya wahitaji huduma hizo.
Kwa hiyo, licha ya nafasi ya Mungu na Ukristo (au dini kwa ujumla) kufifia miongoni mwa Waingereza wengi, bado kwa kiasi kikubwa jamii hii inafanya ‘mema’ mengi zaidi ya akina sie huko nyumbani tusiokosekana kwenye nyumba za ibada.
Binafsi, licha ya kutopendezwa kuona watu waliotuletea Ukristo huko nyumbani ‘wakiupiga teke,’ wengi wa Waingereza wanaendelea kunivutia jinsi wanavyoendesha maisha na shughuli zao kwa uadilifu mkubwa.
Japo Waingereza wengi ni kama hawana dini lakini wengi wao hawapo tayari kuona mwanadamu mwingine ananyimwa haki zake za msingi, na ndiyo maana nchi hii imetokea kuwa kimbilio kubwa kwa mamilioni ya wakimbizi ambao miongoni mwao ni wale walionyanyaswa na kuteswa na nchi zao aidha kwa imani au itikadi zao, jinsia zao, kutetea wanyonge na kadhalika.
Kwa hali hii, yayumkinika kuhitimisha kuwa bora kuwa ‘mpagani’ mtenda mema kuliko mcha-Mungu fisadi. Ndiyo, dini imepoteza umuhimu wake kwa wengi wa wenzetu hawa lakini wengi wao wameendelea kuwa ‘watu wema’ kuliko mamilioni ya wacha-Mungu huko Afrika.
Yawezekana kabisa ‘wapagani’ hawa kwenda mbinguni kutokana na kumpendeza Mungu kwa matendo yao huku washika dini wetu wakigeuzwa kuni za kuchochea washiriki wao katika kukandamiza, kuibia, kunyanyaswa na kufanya kila baya kwa wanadamu wenzao.
Ni katika mazingira haya ya ‘Uingereza ninayoipenda licha ya wengi wa watu wake kumpa kisogo Mungu’ ndipo nilijikuta nikishtushwa na habari katika gazeti moja la huko nyumbani kuwa Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Diane Louise Corner, “amesifu serikali kwa kukuza demokrasia kutokana na uhuru unaovipa vyombo vya habari kuujuza umma kuhusu mambo mbalimbali yakiwamo matumizi ya umma yanayofanywa na serikali.”
Awali, naomba niseme bayana kuwa hadi muda huu bado nina wasiwasi iwapo Balozi Corner alinukuliwa sahihi (yaani, iwapo kweli alitoa kauli hiyo).
Sitaki kabisa kuamini kuwa Balozi huyo hana taarifa kuhusu unyanyasaji mkubwa unaofanywa na serikali dhidi ya vyombo vya habari binafsi huko nyumbani (ukiweka kando gazeti hilo la serikali liloandika habari hiyo).
Hivi inawezekana Balozi Corner hajawahi kusikia manyanyaso yaliyowakumba wamiliki wa jukwaa huru la mtandaoni la Jamii Forums ambalo kwa hakika limekuwa chanzo kikubwa cha kufichua maovu katika jamii?
Inawezekana Balozi huyo hajawahi kusikia tukio la kumwagiwa tindikali kwa mwandishi wa habari Said Kubenea ambaye serikali inayosifiwa na Balozi huyo imejipa jukumu la kudumu kumdhibiti mhariri huyo na gazeti lake ambalo kwa sasa limefungiwa kwa muda usiojulikana?
Ni demokrasia ipi anayozungumzia mwanadiplomasia huyo ambayo kwa upande mmoja inaruhusu mikutano ya chama tawala CCM katika kampeni za uchaguzi huko Zanzibar lakini si tu inapiga marufuku hata mikutano ya ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) lakini pia inapelekea Jeshi la Polisi kunyanyasa wananchi wasio na hatia ambao ‘kosa’ lao pekee ni kutumia haki yao ya kikatiba na kidemokrasia ya kukusanyika (freedom of association)?
Hivi kweli Balozi Corner hana taarifa kuwa Jeshi la Polisi limeshafanya unyanyasaji mkubwa dhidi ya wafuasi wa CHADEMA na kupelekea vifo vya wananchi wasio na hatia huko Arusha, Morogoro na kubwa zaidi ni kifo cha mwandishi wa habari Daudi Mwangosi huko Iringa hivi karibuni?
Ninasema sitaki kuamini kuwa uhuru wa vyombo vya habari au demokrasia ninayoshuhudia hapa Uingereza ina tafsiri tofauti na hiyo anayosifia Balozi huyo huko nyumbani.
Niwe mkweli, moja ya sababu ninazoona kuwa zinachangia sana ukosefu wa utawala bora katika nchi zinazoendelea (ikiwamo Tanzania) ni tabia ya nchi zilizoendelea kama Uingereza kuendeleza tabia ya kufumbia macho ukiukwaji wa haki za binadamu ambao hauna nafasi kabisa katika ‘jamii zao za kistaarabu.’
Hivi majuzi tu, serikali ya Uingereza kupitia Waziri Mkuu David Cameron imeomba msamaha kuhusiana na maafa ya Hillsborough yaliyotokea mwaka 1989 ambapo mashabiki kadhaa wa soka waliopoteza maisha.
Je, Balozi Corner anafahamu kuwa hadi leo serikali anayoisifia kwa kukuza demokrasia haijaomba msamaha kwa japo kifo cha mwandishi Mwangosi zaidi ya kuunda tume ambayo tayari imeanza kuhujumiwa huku baadhi ya wajumbe wake wakilalamikiwa kuwa na utendaji kazi wenye mushkeli?
Kama Mtanzania ninayeishi katika nchi ambayo huko nyuma ilitutawala kwa mabavu lakini ninaiheshimu na kuipenda kwa mengi inayofanya kwa utu wa mwanadamu pasi kujali ni Mwingereza au ‘mgeni,’ nimeshitushwa sana na kauli ya Balozi Corner ambayo kimsingi inaweza kutumika kama sababu tosha kwa watawala wetu kuendelea kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu kwa ujumla kwa kigezo cha kupewa ‘seal of approval’ na mwakilishi wa taifa kubwa na linaloaminika kwa kuenzi haki hizo muhimu za binadamu.
Kuna nyakati ninapata shida sana kuyaelewa haya mataifa makubwa kama Uingereza katika uhusiano wao na nchi ‘zinazojikongoja.’ Wao ndio wafadhili wetu wakubwa, na asilimia ya kutosha ya fedha za walipakodi wao ndizo zinachangia uhai na ustawi wa nchi masikini (japo zina utajiri unaofilisiwa kila kukicha) kama Tanzania.
Lakini cha kushangaza, hakuna hatua za makusudi zinazochukuliwa nao angalau kuwabana mafisadi wanaokwiba fedha zao (ambazo kimsingi zinatolewa kwa minajili ya kumsaidia kila Mtanzania).
Sana sana ni utitiri wa sifa zinazomwagwa kwa watawala wetu (kama hizo za kukuza demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari), sifa ambazo zinawapa motisha mafisadi kuendelea kuitafuna nchi yetu.
Je, ‘upole’ huo wa wafadhili wetu unachangiwa na hisia kuwa fedha za mafisadi huishia kuhifadhiwa katika mabenki yaliyopo huku? Au inawezekana bado mentality ileile iliyoleta ukoloni (na hata Ukristo) kwamba sisi tulikuwa hatujastaarabika vya kutosha na ilikuwa muhimu kwa wakoloni kujipa jukumu hilo, hadi sasa tunapaswa kuwa na demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari pungufu na tunayoshuhudia hapa Uingereza?
Nimalizie kwa kumkumbusha Balozi Corner kauli ya Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Gordon Brown katika harakati zake za kuisaidia Afrika.
Alisema (namnukuu katika tafsiri hii isiyo rasmi) “pasipo kuongeza jitihada za kusaidia, itazigharimu baadhi ya nchi za Afrika zaidi ya miaka 150 kufikia tulipofikia sisi (Waingereza).”
Lakini kwa mwenendo huu wa ‘sifa tusizostahili’ basi yayumkinika kubashiri kuwa inaweza kutuchukua hata milele kufikia demokrasia ya kweli yenye kuruhusu uhuru wa kweli wa vyombo vya habari.


12 Sept 2012

Iliwahi kuripotiwa kuwa Mkurugenzi wa Katiba na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu, aliipinga Tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Dkt Emmanuel Nchimbi kuchunguza mauaji ya mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi.Moja ya sababu alizotoa Lissu ni Tume hiyo kuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Mstaafu Stephen Ihema,ambaye alimtuhumu kuwa na rekodi ya utendaji kazi yenye walakini.

Katika pitapita yangu mtandaoni, nimekutana na habari inayomhusu Jaji Mstaafu Ihema, ambapo alikuwa mjumbe wa Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii, na sasa kamati hiyo imevunjwa kutokana na kulalamikiwa mno kwa vitendo vya rushwa miongoni mwa wajumbe.

Binafsi nimeguswa sana na habari hii hasa kwa vile inahusu tuhuma za rushwa kwa kamati iliyokuwa inamjumuisha Jaji Mstaafu Ihema.Sasa tukiamini kuwa Jaji Ihema ameshindwa jukumu la ujumbe tu kwenye tume hiyo ya ushauri,kwanini tumwamini kwenye uenyekiti wa kamati ya uchunguzi wa kifo cha marehemu Mwangosi?

Wakati ninawapongeza wanahabari waliojitokeza jana kuifahamisha bayana Serikali ya Rais Jakaya Kikwete  kuwa wanalaani vikali mauaji ya mwanahabari mwenzao yaliyofanywa na jeshi la polisi,ningependa kushauri kuwepo upinzani zaidi dhidi ya Tume hii ambayo kuna kila dalili kwamba itaishia kuwa kiini-macho tu.Awali,hofu yangu kuhusu Tume hiyo ilielemea zaidi Watanzania wameshashuhudia utitiri wa tume ambazo mara nyingi ripoti zake zimeishia kufungiwa maandazi na vitafunwa vingine badala ya kuwekwa hadharani//hatua kuchukuliwa.Wengi wetu tunakumbuka kuhusu tume ya milipuko ya mabomu huko Mbagala na Gongo la Mboto.Hadi leo hakuna kilichoelezwa kuhusu ripoti ya tume hiyo...and life goes on.

Je wewe ni mdau wa habari? Unapenda kuona uchunguzi wa kifo cha marehemu Mwangosi unafanywa independently na watu wasio na harufu ya utendaji kazi wenye walakini?Basi ungana na wanahabari kupiga kelele dhidi ya tume hiyo ya kisanii

11 Sept 2012














Minister for Information, Youth, Culture and Sports, Dr Emmanul Nchimbi, embarrassingly leaving the vicinity after the demonstrating journalists rejected his request to address them

CLICK HERE for more details on how the journalist was killed by the police 





7 Sept 2012



UCHAGUZI WA JUMUIYA ZA CCM
 
Moshi (v) chaguzi zilianza rasmi tarehe 3/09 /2012 - 4/09/2012
1.    Uvccm ulfanyika terehe 29/08/2012 mwenyekiti wake aliechaguliw ani Gulaton Masiga.
2.    Wazazi tarehe 03/09/2012 mwenyekiti wake ni  sterwat lyatuu.
3.    UWT tarehe 04/09/2012  mwenyekiti wake ni  Grace Mzava
Aidha viongozi na wajumbe mbali mbali walichaguliwa na kupatikana chini ya  uongozi wa chama wilaya ya moshi (V)  Innocent Nzaba ambaye ni katibu wa  ccm wilaya na mlezi wa jumuiya Gabriel Massenga ambaye ni mwenyekiti wa ccm wilaya.
Pia katika uchaguzi huo mtangazaji mahiri wa kituo cha Radio na TV Clouds Media Group cha jijini Dar es saalam Bi Sophia Kessy nae alijitosa katika uchaguzi huo kuwanaia nafasi ya uwakilishi wa UWT kwenda vijana  wilaya na kuibuka mshindi kwa kura 415 dhidi ya kura zilizopigwa 416 ambapo kura 1tu iliharibika .
Bi Sophia Kessy amesema kuwa kwa sasa ni hatua ndogo kati ya zile kubwa ambazo amepanga kujitosa na kuwania ambapo matarajio yake ya baadae ni kuwa  kiogozi wa ngazi ya juu zaidi .






BLOGU HII INATOA HONGERA NYINGI KWA SOPHIA..

4 Sept 2012



Septemba 2, 2012: Pichani JUU: CCM inafanya mkutano wahadhara huko Bububu, Zanzibar licha ya Serikali "kusitisha shughuli zote za kisiasa ili kupisha sensa ya watu na makazi."

Septemba 2, 2012 Pichani CHINI,mwandishi wa habari wa kituo cha TV cha Channel Ten,Daudi Mwangosi akipata kipigo kutokakwa FFU kwa "kosa" la kufanya coverage ya KIKAO CHA NDANI cha Chadema huko Nyololo,Iringa,ambacho Polisi sio tu walikizuwia kwa SABABU ZILEZILE ZILIZORUHUSU MKUTANO WA HADHARA JIMBONI BUBUBU bali walipiga,kujeruhi wananchi wasio na hatia na HATIMAYE KUMUUA mwandishi Daudi Mwangosi ."



Mheshimiwa Rais, damu za wananchi wasio na hatia wanaouawa na polisi kwa "kosa la kutumia haki zao za kikatiba za freedom of association" hazitapotea bure. Polisi waliua Arusha,lakini hiyo haikuzuwia wanachama na wapenzi wa Chadema kukusanyika Morogoro ambapo polisi waliua tena.Hata hivyo,kifo hicho hakikuwatisha wana-Chadema kukusanyika tawini kwao huko Nyololo ambapo baada ya unyanyasaji wa hali ya juu,polisiwaliua tena.

Hivi Mheshimiwa Rais hujifunzi kitu kutoka kwenye JEURI hii? Labda umesahau kuwa hata tawala dhalimu kabisa za kikomunisti huko Ulaya Mashariki zilijidanganya kuwa ukatili na unyama wavyombo vya dola utazidumisha (tawala hizo) milele,lakini wakati ulipofika zilisambaratika.Na huko Afrika ya Kusini,makaburu walitawala kwa mtutu wa bunduki lakini hawakuweza kuzuwia kuanguka kwa mfumo wa kibaguzi.

Mwanafalsafa Karl Marx aliwahi kuusia kuwa "mnyonge hana cha kupoteza zaidi ya minyororo." Wakati mafisadi wanaishi kwa hofu ya kunyang'anywa walichotupora, wanyonge wasio na uhakika na mloujao wanaishi kwa matumaini tu.Lakini kuishi huko kwa matumaini kunaweza kuwa silaha yenye nguvu kuliko vipigo,risasi na unyama wa FFU.

Watu wameichoka CCM na ni wazi kuwa vitisho na mauaji ya raia yasiyo na hatia hayawezi kushusha chuki hiyo.Sana sana inawaongezea tu sababu ya kukichukia chama hicho. 2015 si mbali.CCM inaweza kung'olewa madarakani.Ni vema,Mheshimiwa Rais,ukaanza kutafakari hatmayako pindi hao wanyonge wanaonyanyaswa sasa wakishika madaraka.

Watanzania wana kila sababu ya kuichukia CCM lakini inaonekana kana kwamba chama hicho kinasaka sababu nzito zaidi.Sijui ni kuishiwa na uwezo wa kuongoza au ndio kimezeeka na kinasaka namna ya kujipeleka kaburini,lakini kilicho wazi ni kuwa kila tone la damu linalomwagika kutokana na unyama wa polisi wetu ni sawa na lita nyingi za petroli kuchochea moto wa mabadiliko.


Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.