13 Mar 2014
13.3.14
Evarist Chahali
RAIA MWEMA
No comments

NIMEKUTANA na habari ya kushtua inayohusu jaribio la kumdhuru mkuu wa zamani wa Majeshi ya Rwanda, Jenerali Faustine Kayumba Nyamwasa anayeishi kama mkimbizi Afrika Kusini.
Habari hiyo ilieleza kuwa watu sita wametiwa nguvuni wakituhumiwa kuhusika na jaribio hilo, na watatu kati yao ni Watanzania. Nikabaki ninajiuliza, “baada ya Tanzania yetu kuchafuliwa na habari za Watanzania wanaosafirisha madawa ya kulevya, sasa tumehamia kwenye ku-export (kusafirisha nje) wauaji (assassins)”
Baadaye nikajaribu kuamsha mjadala kuhusu suala hilo katika mtandao mmoja wa jamii (social media), na baadhi ya walioshiriki mjadala huo walionyesha wasiwasi wao iwapo watu hao watatu waliokamatwa ni Watanzania kweli au walikuwa wakitumia tu hati za kusafiria za Tanzania.
Pengine ni mapema mno kufahamu ukweli halisi wa suala hili hasa kwa vile uchunguzi bado unaendelea, lakini kimsingi habari hiyo ni mwendelezo wa ‘sifa zisizopendeza’ zinazoiandama nchi yetu.
Nimewahi kueleza katika makala zangu mbalimbali kuhusu tabia niliyojijengea ya kuanza siku yangu kwa kupitia mitandao mbalimbali ya huko nyumbani ili kufahamu kinachoendelea. Na mara baada ya kumaliza kusoma habari hiyo inayomhusu Jenerali Nyamwasa, rafiki wa zamani wa Rais wa Rwanda Paul Kagame aliyegeuka kuwa mmoja wa mahasimu wake wakubwa, nikakumbana na ‘filamu mbaya’ inayozidi kutawala vichwa vya habari, kuhusu maendeleo ya kikao cha Bunge la Katiba.
Ninaiita filamu mbaya kwa sababu japo vikao vya Bunge letu vimekuwa mahiri zaidi kwa vituko kuliko kuzungumzia masuala lukuki yanayomhusu Mtanzania, kinachoonekana ni kama Bunge la Katiba linajaribu kuchuana na ‘Bunge la kawaida’ kwa vituko.
Na pengine bila kuumauma maneno ni vema nikitanabahisha kuwa kama ilivyo katika vikao vya ‘Bunge la kawaida,’ chanzo kikubwa cha mambo yote ya kukera yanayojitokeza katika Bunge la Katiba ni kasumba ya chama tawala CCM kutanguliza maslahi ya kiitikadi mbele ya maslahi ya Taifa.
Baada ya kumalizika ‘kinyemela’ kwa mjadala mkali kuhusu posho ya wajumbe wa Bunge hilo la Katiba (madai yalikuwa kwamba kiwango cha posho cha shilingi 300,000 kwa siku hakitoshi), suala ‘jipya’ linalotishia hatma ya Bunge hilo ni kuhusu utaratibu wa kupiga kura- iwe siri au ya wazi.
Binafsi ninaunga mkono hoja ya kura ya siri kwa sababu moja ya msingi- katika mazingira ya siasa za vitisho na ubabe, namna pekee mpigakura anaweza kuwa huru kutumia haki yake ya kupiga kura ni kwa kupiga kura ya siri.
Na utaratibu wa kura ya siri umekuwa ukitumika katika ngazi mbalimbali, ndani na nje ya anga za kisiasa. Tunapochagua viranja-iwe shule ya msingi au sekondari, na tunapochagua viongozi vyuoni, kura hupigwa kwa siri. Kisiasa, chaguzi katika takriban ngazi zote-iwe ni udiwani au urais, kura hupigwa kwa siri. Sasa kwanini kwenye suala muhimu la Katiba mpya kura iwe ya wazi?
Nimeeleza kuwa chanzo cha tatizo ni CCM. Na sababu kubwa kwa chama hicho kuwa chanzo cha tatizo ni kasumba iliyozoeleka ndani ya chama hicho tawala kubinafsisha kila suala linalomhusu Mtanzania. Baada ya kuanzishwa mchakato wa kukusanya maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba, CCM ikabinafsisha zoezi hilo na kutengeneza ‘rasimu mbadala’ ambayo kwa bahati nzuri ‘ilivuja’ na umma ukapata nafasi ya kutambua hila mbaya za chama hicho.
Kwa CCM, Katiba mpya inapaswa kupatikana kulingana na matakwa ya chama hicho. Na ili matakwa hayo yatimie, ni lazima nguvu, vitisho na hujuma vitumike kuhakikisha kuwa kila mjumbe kutoka chama hicho anatekeleza msimamo utakaolinda matakwa hayo, iwe ni kwa manufaa ya Mtanzania au la. Kuwa na msimamo wa pamoja si vibaya lakini ni muhimu msimamo huo uzingatie matakwa ya wengi.
Lakini kuilaumu CCM kana kwamba ni familia ya mtu mmoja ni kutoitendea haki. Hizo taarifa kwamba kuna baadhi ya wajumbe kutoka chama hicho wamedhamiria kupigania haki zao za kupiga kura kwa utashi wao na si kwa kushinikizwa na ‘msimamo wa pamoja,’ ni ishara tosha kuwa miongoni mwa wana-CCM kuna wanaotaka kuona demokrasia ikizingatiwa sambamba na haki ya kikatiba ya kufanya maamuzi pasipo kuingiliwa na mtu mwingine ilimradi kufanya hivyo hakuvunji sheria za nchi.
Kwa hiyo tunaweza kuilaumu CCM kwa umoja wake lakini ndani yake kuna wenye mtizamo wa kitaifa badala ya kiitikadi.
Lakini kama kuna mtu anayepeswa kubebeshwa lawama zote basi ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, ambaye kwa hakika ni kama anapelekeshwa tu na wanaoitwa ‘wahafidhina’ ndani ya chama hicho.
Tangu mwanzo wa mchakato wa kupata Katiba mpya, Rais Kikwete ameonyesha kuyumba kimsimamo, ambapo mara kadhaa anapozungumzza kama Rais ameonyesha kutambua umuhimu wa zoezi hilo la upatikanaji wa Katiba mpya lilizingatie matakwa ya Watanzania wote pasi kujali tofauti zao za kiitikadi, lakini anapozungumza kama kiongozi mkuu wa CCM anaonekana kutaka kuwaridhisha wahafidhina wanaotamani kuona Katiba mpya ikizingatia matakwa yao binafsi.
Hili limezungumzwa mara nyingi (na kukanushwa mara nyingi pia) kwamba tatizo kubwa linaloathiri utendaji kazi wa serikali ya Rais Kikwete ni ombwe la uongozi. Yeye kama Mkuu wa nchi na Mwenyekiti wa chama tawala akiamua kuwa “ninataka tupate Katiba mpya itakayozingatia matakwa ya Watanzania wote” na itakuwa hivyo.
Lakini hilo haliwezekani kwa sababu upande mmoja, Kikwete anataka kuweka historia nzuri ya kuwaletea Watanzania Katiba mpya inayokidhi matakwa yao, lakini kwa upande mwingine anataka kuwafurahisha wana-CCM wenzie wanaotaka Katiba mpya itokane na matakwa ya chama hicho.
Kama nilivyomuusia katika makala yangu moja ya hivi karibuni, ni muhimu kwa Rais Kikwete kuangalia kalenda na kuhesabu siku zilizobaki kabla hajastaafu. Muda mfupi baada ya kustaafu atakuwa mwananchi wa kawaida tu, na asipokuwa makini, mara baada ya kustaafu anaweza kuandamwa kutokana na maamuzi mabaya yaliyofanyika wakati wa utawala wake.
Ndiyo, Mwalimu Nyerere, na marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa walishiriki kufanya baadhi ya maamuzi ambayo pengine hayakuzingatia maslahi ya Watanzania wote kwa ujumla- kwa kutanguliza maslahi ya chama tawala pekee- lakini zama za Nyerere, Mwinyi na Mkapa ni tofauti na tulizo nazo sasa.
Japo Watanzania tunasifika kwa ‘upole’ ambao baadhi ya watu wanautafsiri kama ‘ugoigoi wa kuruhusu mambo yasiyofaa yatokee pasi wahusika kuchelea matokeo,’ kizazi hiki cha Facebook, Twitter na nguvu za mitandao ya kijamii, sambamba na jitihada za kuelimisha umma kuhusu haki zake ni tofauti sana na huko nyuma.
Kwa vile kwa hali ilivyo sasa kikwazo kikubwa ni mtizamo fyongo wa CCM kutaka kubinafsisha mchakato mzima wa kupata Katiba mpya, Rais Kikwete ana nafasi nzuri ya kuingilia kati na kuwaelimisha wana-CCM wenzie kuwa “tuache maji yafuate mkondo.”
Ni muhimu kutambua kuwa matakwa ya CCM kung’ang’ania muundo wa serikali mbili (na hili ndilo linalowaogopesha kuhusu kura ya siri) hayawezi kuua dhamira ya wanaotaka Muungano wa serikali Tatu.
Ni lazima Kikwete na CCM wafahamu kuwa moja ya vyanzo vya matatizo ya Muungano ni ‘usiri’ uliotawala katika upatikanaji wa Muungano huo. Usiri huo unathibitishwa na ukweli kwamba wajumbe wa Bunge la Katiba watajadili muundo wa Muungano huo bila kupatiwa ‘Articles of the Union’ (aidha kwa vile nyaraka hiyo haipo au kama ipo, basi ikiwekwa hadharani itazua sokomoko kubwa). Kwanini Turejee makosa hayohayo yanayoufanya Muungano wetu kuwa moja ya kero kubwa za siasa za Tanzania yetu?
Nimalizie makala hii kwa kuueleza bayana kuwa nimeanza kujiandaa kisaikolojia kuona Bunge la Katiba likitafuna mabilioni ya fedha za walalahoi wa Kitanzania na kuishia kuwa kumbukumbu mbaya tu ya vioja, vituko na kila jambo linalozifanya siasa zetu kuonekana za kibabaishaji.
Kama CCM haitoacha ‘uhuni’ wake, na kwa hakika kama Rais Kikwete hatoingilia kati kuhakikisha Katiba mpya yenye kujali maslahi ya Watanzania wote inapatikana, basi labda tutakachoishia kuambulia ni Katiba mpya kwa jina lakini fyongo na isiyo na manufaa kwa Mtanzania.
Mpira upo mezani kwa Rais Kikwete: akitaka asimamie maslahi ya Watanzania bila kujali tofauti ya itikadi zao za kisiasa, tutapata Katiba mpya ya kweli. Aking’ang’ania kutaka kuwaridhisha ‘wahafidhina’ ndani ya CCM, Katiba mpya itabaki kuwa kitendawili.
7 Mar 2014
7.3.14
Evarist Chahali
candy1world
1 comment

I wish you luck, happiness and riches today, tomorrow and beyond.
As you look back on yesterday, may your memories be warm ones. As you celebrate today, may your heart be filled with happiness and joy. As you look ahead to tomorrow, may your deepest hopes and dreams come true for you!
I wish you to celebrate all the wonderful things that make you so special, not just on your special day, but on every day of the year!
I wish that for every extra candle on your cake, you receive an extra reason to smile.
Happy Birthday to you!

7.3.14
Evarist Chahali
RAIA MWEMA
No comments

MWISHONI mwa wiki iliyopita kulijitokeza malumbano makali, hususan katika mtandao wa kijamii wa Twitter, kuhusu suala la ushoga.
Sina hakika mjadala huo ulianza vipi lakini ninadhani kwa upande mmoja ulichochewa na sakata linaloendelea kati ya serikali ya Uganda na baadhi ya nchi za Magharibi baada ya Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni, kusaini muswada unaopiga marufuku ushoga kuwa sheria inayoambatana na adhabu kali. Kwa upande mwingine, nahisi mjadala huo ulichangiwa na majadiliano yanayoendelea katika Bunge la Katiba huko Dodoma, ambapo suala la haki za mashoga limejichomoza.
Kwa upande wa Bunge la Katiba, kuna tuhuma kuwa ‘ajenda ya ushoga’ imeletwa makusudi kwa minajili ya kuepesha (divert) mtizamo wa Watanzania katika ‘masuala ya msingi zaidi’ yanayopaswa kujadiliwa katika Bunge hilo maalumu.
Lakini pengine kabla sijaingia kiundani katika mada hii ni vema nikaweka bayana msimamo wangu kuhusu suala hili la ushoga. Huko nyuma niliwahi kuandika makala iliyozungumzia mjadala wa ushoga, makala iliyobeba kichwa cha habari “Tatizo ni unafiki wetu, sio ushoga.”
Hoja kubwa ya ‘wapinzani wa haki za mashoga’ ni kwamba suala hilo haliendani na mila na desturi zetu. Lakini kabla ya kwenda mbali, hivi hizo mila na desturi zetu ni zipi hasa? Mara kadhaa tumekuwa tukiwalaumu ‘wazungu’ kwa kuiangalia au kuizungumzia Afrika kana kwamba ni kijiji kimoja kikubwa kinachoundwa na familia moja kubwa. Wengi wetu tumekuwa mahiri kuwakumbusha ‘wazungu’ kwamba Afrika ni mkusanyiko wa mataifa zaidi ya 50, na ndani ya mataifa hayo kuna makabila lukuki yenye mila na desturi tofauti.
Sasa tukirejea kwa Tanzania yetu, hivi ‘mila na desturi za Kitanzania’ ni zipi hasa? Naomba ieleweke kwamba sikatai kwamba tuna mila na desturi bali ninapata shida kuelewa hizo ‘mila na desturi za jumla’ zinazofuatwa na kila Mtanzania.
Kuna hoja nyingine inahusu imani za kidini, kwamba “katika dini zote, ushoga ni haramu.” Tunarejea palepale. Kwa sababu dini fulani zinasema kitu hiki ni haramu haina maana basi kila mtu (asiye muumini au hata muumini wa dini hiyo) lazima aafiki mtizamo huo. Tukumbuke kuwa dini ni imani, na imani hailazimishwi. Sasa kwa vile Tanzania yetu si nchi ya kidini, japo wengi wa Watanzania wana dini, kinachotakwa haramu katika dini fulani si sheria inayopaswa kufuatwa na kila Mtanzania.
Maana kama kila matakwa ya dini lazima yafuatwe kama sheria ya nchi, hali itakuwaje katika suala kama la ulaji wa nyama ya nguruwe ambayo ni ruhusa kwa Wakristo lakini ni haramu kwa Waislamu? Tupige marufuku ulaji wa nyama ya nguruwe kwa vile ni haramu kwa Waislamu au turuhusu kwa vile ni halali kwa Wakristo? Usuluhishi unapatikana katika busara za kutambua haki na wajibu: uhalali usikwaze haramu na haramu isikwaze halali.
Wakati mjadala huo wa ushoga unaendelea huko Twitter, muungwana moja alinihoji iwapo msimamo wangu kuhusu haki za mashoga unatokana na uwepo wangu huku Uingereza. Nikamjibu kuwa mie ni muumini wa haki za binadamu, na haki hizo ni pamoja na za mashoga.
Mwingine akaenda mbali na kuhoji iwapo nami ni shoga eti kwa sababu ninawatetea sana. Nilimuuliza, hivi tunavyopambana dhidi ya ujangili na kupigania haki za uhai wa tembo wetu, kwa mfano, basi nasi ni tembo? Kuna vijana wanaopigania haki za wazee, wasio na ulemavu wanaopigania haki za walemavu, na wanaume wanaopigania haki za wanawake. Ni suala la imani.
Ninaendelea kuamini kuwa kwa mtu ambaye si shoga, sioni kwanini asumbuliwe na haki za mashoga. Ni haki za mashoga, sio za wewe usiye shoga. Kwanini basi zikusumbue? Oh dini yako inakataza. Sawa, lakini dini fulani inakataza kula nguruwe lakini yako inaruhusu. Oh mila na desturi zinakataza, vipi kwa asiyehusika na mila na desturi hizo?
Waingereza wana msemo ‘two wrongs don’t make a right’ ambao kwa tafsiri isiyo rasmi ni unamaanisha ‘kwa vile kosa la kwanza limeachwa kama si kosa, haimaanishi kosa la pili nalo liachwe pia.’ Msemo huu unatumika sana dhidi ya wanaohoji “kwanini hizo mila na desturi zikumbukwe kwenye suala la ushoga pekee na sio dhidi ya ufisadi, biashara ya dawa za kulevya, ukahaba na mengine kama hayo?”
Wapinzani wa haki za mashoga wanadai “kwa vile hatutilii mkazo kuhusu imani za dini zetu na mila na desturi zetu kupambana na maovu mbalimbali katika jamii, haimaanishi tusikemee ushoga.” Sawa, lakini haki za mashoga zinachangia vipi uwepo wa mgawo wa umeme usiokwisha? Au mashoga wanachangiaje kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya? Na ni kwa vipi mashoga wanahusika na kuzaliana kwa kasi kwa matapeli wa kisiasa katika mfumo wa siasa wa nchi yetu?
Ninatambua kuwa msimamo wangu katika suala hili sio popular (unaoafikiwa na wengi). Ninatambua pia kuwa kuna wasomaji watakaoniona mtu wa ajabu kabisa kwa kutetea haki za mashoga. Ninahisi pia kuna watakaodhani kuwa labda ‘nimechanganyikiwa.’ Sina tatizo na mtizamo huo kwa sababu ni matumizi ya haki na uhuru wao. Na ndio moja ya faida kubwa za haki na uhuru: kufanya hata kile ambacho mtu mwingine hakiafiki. Sasa, kama sio tu tunapenda haki na uhuru, kwanini tuchukie vitu hivyo hivyo kwa wenzetu?
Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuhusu ukweli huu ambao pengine ni mchungu kwa wapinzani wa haki za mashoga: Sio tu kwamba Tanzania yetu ina mashoga bali pia kasi ya kukua kwa ushoga ni kubwa. Na hata miongoni mwa wapinzani wa ushoga kuna mashoga pia lakini wanaotumia fursa hiyo ya kupinga ushoga kwa minajili ya kuficha ‘siri’ yao. Tunaweza kuendelea kudai ‘ushoga ni haramu...mila na desturi zetu zinapinga ushoga...” lakini hiyo haiondoi ukweli kuwa ushoga upo na mashoga wapo.
Wito wangu kwa ‘wapinzani’ wa ushoga sio wabadili mtizamo wao bali kama kweli wanaoongozwa na dini au mila na desturi kupinga ‘laana’ ya ushoga, basi ni vema pia wakielekeza hasira zao dhidi ya majanga ya kitaifa kama vile ufisadi na biashara ya madawa ya kulevya, sambamba na usaliti katika uhusiano au ndoa (suala maarufu la ‘nyumba ndogo’ na ‘mambo mengine yasiyofaa.’
6 Mar 2014
6.3.14
Evarist Chahali
BOT, EPA, RICHMOND, UFISADI
No comments

Wakati haijafahamika nani aliyelipwa mabilioni ya shilingi yaliyokuwa kwenye akaunti ya Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kutokana na mvutano baina ya Tanesco na Kampuni ya IPTL, imebainika kuwa Bunge liliwahi kuagiza fedha hizo zisichukuliwe mpaka mitambo ya IPTL itakapokuwa chini ya Tanesco mwakani.
Hiyo imo katika taarifa ya iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2007.
Hata hivyo, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alithibitisha jana kuchotwa kwa Dola za Marekani 122 Milioni (Sh195.2 bilioni) katika akaunti hiyo, lakini akakataa kutaja nani hasa aliyelipwa.
Mkataba wa miaka 20 baina ya IPTL na Tanesco ulisainiwa mwaka 1995 na ulitakiwa kuisha 2015 na mitambo hiyo kuwa mali ya Tanesco.
Hata hivyo, ukiwa umebaki mwaka mmoja kumalizika, imebainika kuwa mitambo hiyo imeuzwa kwa Kampuni ya Pan African Power, ambayo inatarajiwa kuingia mkataba mwingine na Tanesco ili iwauzie umeme.
Ndulu alisema fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Dola za Marekani 22 milioni na Sh161 bilioni za Tanzania ambazo zote kwa pamoja ndizo zilizofikisha jumla ya Sh195.2 bilioni.
Vyanzo vingine vilitoa takwimu mbili tofauti, kimoja kikisema kiasi cha fedha hizo kilifikia Dola za Marekani 270 milioni na kingine Dola 250 milioni. Kuhusu nani mwenye mamlaka ya kutoa fedha hizo, Profesa Ndulu alisema kwa mujibu wa mkataba wa kufunguliwa kwa akaunti ya fedha hizo, ni Wizara ya Nishati na Madini pamoja na IPTL.
“Hakuna mtu mwingine anayeweza kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo zaidi ya hao, kwa hiyo hao ndiyo waliosaini kutolewa kwa hizo fedha na taratibu zote zilifuatwa,” alisema Profesa Ndulu.
Alipoulizwa ni nani aliyelipwa fedha hizo, Profesa Ndulu alisema IPTL ndiyo iliyokuwa na mamlaka ya kusema ni nani alipwe na ilifanya hivyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi alipoulizwa juu ya fedha hizo alisema: “Kwa kawaida huwa nina majibu mafupi sana, lakini kwa kuwa mmeamua kuandika uongo, endeleeni, siwezi kukujibu chochote wasiliana na hao IPTL wakujibu.”
Hata hivyo, haikuwa rahisi kumpata kiongozi wa IPTL kuzungumzia suala hilo kwa kuwa tayari kampuni hiyo ni mufilisi.
Msimamo wa Bunge
Ripoti ya POAC inasema Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) aliorodhesha matatizo ya mkataba kati ya Tanesco na IPTL na kuangalia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mipango ya kununua mitambo hiyo na kuibadilisha iwe inatumia gesi badala ya mafuta mazito.
“Mgogoro uliopo hivi sasa kati ya Tanesco na IPTL unahusu kiwango cha malipo ya uwekezaji yaani capacity charges ambacho IPTL walikuwa wanalipwa na Tanesco. Kwa mujibu wa mkataba huo, capacity charge inapaswa kukokotolewa kwa kuzingatia mtaji wa asilimia 30 na mkopo wa asilimia 22.31.
Baada ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa, ilikubalika kuwa mtaji uliowekezwa uwe ni Dola za Marekani 36 milioni.
Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa Tanesco iligundulika kuwa IPTL haikuwekeza fedha hizo, bali Sh50,000,” inasema ripoti hiyo.
Ilisema kuwa, mpaka kufikia Mei 2008, Tanesco ilikuwa imeilipa IPTL Sh221 bilioni tangu ilipoanza uzalishaji umeme Januari 2002.
Kamati iliagiza: “Wanasheria wa Tanesco na Serikali watumie ushahidi wote uliopo kuhakikisha kuwa kiwango cha fedha kilichopo kwenye akaunti maalumu (Escrow) ndicho hichohicho kitumike kumaliza madeni yaliyopo na vilevile kufanyia marekebisho mitambo hiyo ili itumie gesi,” inasema taarifa hiyo.
Pendekezo hilo lilipitishwa na Bunge huku POAC ikitoa maelekezo kwa Gavana Ndulu kuwa fedha zilizopo Escrow zisitumike kwa namna yoyote ile bila mitambo ya IPTL kuwa ya umma na kubadilishwa na kutumia gesi asilia.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa POAC, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema ameshtushwa na taarifa za kutolewa kwa fedha hizo kinyemela.
“Tunaitaka Serikali kutoa taarifa kama kweli hizo fedha zimetolewa, kwa sasa siwezi kutoa msimamo wetu kwa kuwa hatujakaa kama kamati, tunatarajia kuitisha kikao cha dharura Dodoma kuzungumzia suala hili,” alisema Zitto.
CHANZO: Mwananchi

Mshindi wa kura za maoni za kugombea ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya CCM, Ridhiwani Kikwete amesema siasa anazofanya sasa hazina uhusiano wala ubia na baba yake.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura za maoni za chama hicho katika jimbo hilo kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Msata alisema anafanya siasa kwa maisha yake na si kwa mgongo wa baba yake kwani aliingia katika siasa akiwa na umri wa miaka mitano na hakuwahi kufanya hivyo kwa sababu ya baba yake.
“Siasa ninayofanya haina uhusiano na baba yangu, nafanya siasa kwa maisha yangu na sina ubia na baba yangu katika hili” alisema mtoto huyo wa Rais Jakaya Kikwete.
Akijibu swali la kwa nini amejiingiza katika siasa tofauti na maneno yake aliyowahi kutamka mwaka 2010 kuwa hawezi kushiriki katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo hilo, Ridhiwani alisema wakati huo hakuwa tayari.
“Kwenye siasa usiwe muwazi katika kila kitu, ukiwa hivyo unawapa nafasi maadui kukushambulia, mimi hapa Chalinze ni kwetu, kwa wazazi wangu na kule Bagamoyo tunakwenda tu kikazi na ndiyo maana nikaamua kurudi nyumbani kuomba ridhaa. Nashukuru kuongoza katika kura za maoni ninaona ni kiasi gani ninaungwa mkono,” alisema.
Katika kura hizo za maoni Ridhiwani alibuka mshindi kwa kura 758, akifuatiwa na Imani Madega aliyepata kura 335, Ramadhan Maneno (206) na Mkwazu Changwa (17).
Kamati Kuu ya CCM (CC), inatarajiwa kukutana Machi 8, mwaka huu kupitisha jina mgombea wake wa ubunge katika jimbo hilo nafasi ambayo iliachwa wazi na Said Bwanamdogo aliyefariki dunia Januari 22, mwaka huu.
6.3.14
Evarist Chahali
UKIMWI
No comments

Wanasayansi wanadai kuwa wamefanikiwa kuwadunga waathirika 12 wa Ukimwi viini vya kinga ambavyo vina uwezo wa kuzuwia virusi vya ugonjwa huo. Watafiti wanadai kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuelekea kwenye matibabu kamili ya Ukimwi, ugonjwa unaomlazimu mwathirika kutumia vidonge vya kupunguza makali kwa muda wote wa uhai wake.
"Hii inaimarisha imani yetu kwamba viini vya aina ya T (T cells) vilivyorekebishwa ni ufunguo muhimu katika kuondoa haja ya mwathirika wa Ukimwi kuhitaji dawa kwa muda wote wa uhai wake..." alieleza Dkt Carl H. June, Profesa wa Richard W. Vague katika tiba za kinga katika Idara Tiba na Matibabu na Dawa za Maabara , Shule ya Madawa ya Penn's Perelman huko Philadelphia nchini Marekani.
Watafiti walitumia teknolojia inayojulikana kama "zinc finger nuclease" (ZFN)- waliyoielezea kama 'mkasi wa kimolekyuli kurekebisha viini vya T katika mfumo wa kinga mwilini ili kuiga kuongezeka kwa CCR-5-delta-32, viini vinayofahamika kwa kuwafanya baadhi ya watu wasipate Ukimwi.
Soma habari kamili HAPA (na usisite kuwasiliana nami iwapo utahitaji tasfiri)
Subscribe to:
Posts (Atom)