Showing posts with label Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015. Show all posts
Showing posts with label Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015. Show all posts

6 Aug 2015

NINAANDIKA makala hii nikiwa na masikitiko makubwa mno. Siku zote maishani, twajikuta katika kipindi kigumu sana pale mtu tuliyemwamini kwa dhati anapotugeuka. Wanasema, inachukua muda mwingi na jitihada kubwa kujenga uaminifu japo kosa au tukio moja tu laweza kuondoa kabisa uaminifu huo.
Na hicho ndicho walichofanya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kukubali kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowaasa, sio tu kuwa mwanachama wao bali pia mgombea wao katika nafasi ya urais.
Kama ambavyo tetesi kuwa Lowassa angechukua fomu kuwania urais kwa tiketi ya CCM zilivyozagaa kwa muda mrefu, ndivyo suala la Lowassa kujiunga na Chadema/ UKAWA lilivyokuwa.
Mara baada ya mwanasiasa huyo kukatwa katika mchakato wa CCM kumpata mgombea wake wa Urais, zilisikika tetesi nyingi kuwa kuna uwezekano angejiunga na moja ya vyama vinavyounda UKAWA, na hatimaye kuwa mgombea urais.
Lakini kwa vile Tanzania yetu haina uhaba wa tetesi, baadhi yetu tulidhani kuna ugumu kwa Lowassa kujiunga na UKAWA ni Chadema, kwa vile chama hicho kimejijengea umaarufu mkubwa kwa msimamo wake tuliodhani ni thabiti kupambana na ufisadi na mafisadi.
Na sio msimamo tu dhidi ya ufisadi na mafisadi, Chadema wamelipa gharama kubwa katika harakati zake ambapo baadhi ya wanachama wake walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya, huku wengine wakiishia rumande au magerezani kufuatia maandamano mbalimbali ya kutetea maslahi ya taifa na wanyonge.
Hata nilipoona picha zilizodaiwa kuwa ni za Lowassa akihudhuria moja ya vikao vya UKAWA nilijipa moyo kuwa huenda picha hizo zimefanyiwa ‘ufundi,’ wenyewe wanaita ‘photoshop,’ ambapo picha ya mtu inapandikizwa kwenye picha nyingine.
Faraja iliongezeka baada ya akaunti ya habari za Chadema katika mtandao wa Twitter, Chadema Media, kukanusha uwepo wa Lowassa katika kikao hicho. Hata hivyo muda mfupi baadaye, watu wa karibu na Lowassa walibandika picha zaidi katika mtandao huo kuthibitisha kuwa kweli Lowassa alihudhuria kikao hicho.
Na siku moja baadaye,’bomu lililipuka.’ Kupitia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ambayo sie tulio mbali tuliweza kuyaona mtandaoni, viongozi wakuu wa UKAWA walionekana na Lowassa, na baadaye mwanasiasa huyo kutangaza bayana kuwa amejiunga na umoja huo kupitia Chadema.
Ninachoweza kusema kwa kifupi ni kwamba walichofanya Chadema ni usaliti wa hali ya juu, na hakuna maelezo ya aina yoyote yanayoweza kuhalalisha kitendo hicho. Ndio, ni muhimu kwao kuingia Ikulu, lakini ni muhimu zaidi kwa Chadema kutambua imefikaje ilipo leo.
Jibu la wazi ni kama nilivyotanabaisha hapo juu; msimamo wao imara wa kuuchukia ufisadi na kupambana nao kwa nguvu zote, hatimaye ulifanikiwa kuwafumbua macho Watanzania wengi, sio tu kuhusu kansa ya ufisadi bali pia kujenga hisia kwamba chama hicho ni kwa ajili ya maslahi ya mamilioni ya Watanzania wanyonge na wahanga wakuu wa ufisadi.

Kwahiyo, kwa kumpokea Lowassa, mwanasiasa aliyelazimika kujiuzulu kwa tuhuma za ufisadi wa Richmond, Chadema wametelekeza nguzo muhimu iliyokuwa ikikitambulisha chama hicho. Na kama tunavyoina CCM, chama chochote cha siasa kinachotelekeza nguzo zake, sio tu kinapoteza uaminifu wake kwa jamii bali pia chajichimbia kaburi.
Sawa, labda Lowassa anaweza kushinda urais (hili lahitaji mjadala wa pepe yake) lakini haihitaji kuwa na ujuzi wa uchambuzi wa siasa zetu kubaini kwamba mwanasiasa huyo hakujiunga na Chadema kwa vile anakipenda chama hicho au anaafiki sera zao bali amekitumia kama ngazi ya kuwania urais baada ya kukwamishwa na CCM.
Hilo tu lilipaswa kuifumbua macho Chadema. Lowassa huyohuyo aliyejigamba kwamba jina lake halitakatwa akijivunia ‘uchapakazi’ wake, na utumishi wake wa muda mrefu katika CCM, leo hii kaitelekeza CCM licha ya kudai asiyemtaka ndani ya chama hicho aondoke lakini yeye si wa kuondoka.
Ni wazi kuwa Lowassa ni mwanasiasa mwenye tamaa ya madaraka. Sawa, Katiba yetu yamruhusu kugombea uaongozi kupitia chama chochote kile, lakini moja ya sifa nzuri kwa mwanasiasa ni msimamo na kutokuwa na tamaa ya madaraka.
Leo kaitosa CCM kwa kutaka urais, je ataitendaje Chadema katika kutaka mengineyo?
Lakini pia ni ukweli usiofichika kuwa umaarufu wa Lowassa unatokana na ‘sifa’ kuu mbili: uwezo mkubwa wa kifedha ‘zisizo na maelezo ya kutosha’ na skandali ya Richmond. Katika mazingira ya kawaida, na hasa katika zama hizi za ufisadi, ni vigumu mno kumnadi mwanasiasa wa aina hiyo.

Tayari kuna hisia kuwa ‘fedha zilibadilishana mikono’ hadi akina Freeman Mbowe kukubali kumpokea mwanasiasa huyo ambaye walikuwa wakimwandama kila kukicha kwa kumuita fisadi.
Kama ni fedha kweli au ‘umaarufu,’ tayari Lowassa ndio mnufaika maana kwa muda mfupi tu ndani ya chama hicho, mambo kadhaa yameshabadilika.
Mie nazifuatilia kwa karibu zaidi harakati za Chadema kupitia mitandao ya kijamii au tovuti za vyombo vya habari mbalimbali vya huko nyumbani. Nilichobaini katika siku chache hizi baada ya Lowasaa kujiunga na Chadema, ghafla wanachama na mashabiki wa chama hicho wamegeuka ‘mabubu’ kuhusu masuala ya ufisadi.
Na hilo si la kushangaza kwa sababu watamudu vipi kukemea ufisadi ilhali mgombea wao wa urais ni mtuhumiwa wa ufisadi?
Kwa mujibu wa maelezo ya mmoja wa viongozi wa Chadema, Tundu Lissu, chama hicho na UKAWA kwa ujumla walikuwa wakifuatilia kwa karibu mchakato wa CCM kupata mgombea wake, na wao walitaka kuitumia ‘sintofahamu’ hiyo ndani ya CCM kufanikisha malengo yao ya kuingia Ikulu.
Huu ni udhaifu wa hali ya juu. Lakini angalau hii imesaidia kutufahamisha kwanini chama hicho kilikuwa kinasuasua kumtangaza mgombea wake: kilikuwa kinasubiri ‘makombo’ ya CCM.
Watu hawa wanajifanya kusahau kabisa mafanikio makubwa tu waliyoyapata katika uchaguzi mkuu uliopita ambapo walisimama wenyewe, wakapata wabunge wa kutosha na madiwani wa kutosha tu, licha ya mgombea wao, Dkt Willbrord Slaa, kushindwa katika mazingira ambayo baadhi yetu tunaamini yalichangiwa na hujuma.
Na ni katika mazingira hayo, baadhi yetu tunaunga mkono Dk. Slaa kujitenga na Chadema. Ni matarajio yangu kuwa hatokubali kuwa sehemu ya usaliti huu hasa kwa kuzingatia gharama kubwa waliyoingia Chadema, kwa maana ya muda na jitihada, sio tu kukitambulisha chama hicho kuwa ni mtetezi wa wanyonge na kiongozi wa mapambano dhidi ya ufisadi bali pia kukiwezesha kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania.
Awali, nilipopata uthibitisho kuwa Lowassa amejiunga na Chadema nilitamka bayana kuwa ‘impact’ ya tukio hilo yapaswa kuonekana angalau ndani ya siku 7. Na siku hizo saba zimeisha juzi. Tuliambiwa tusubiri ‘mafuriko’ ya wana-CCM kumfuata Lowasaa huko Chadema/UKAWA.
Hadi sasa, hakuna dalili yoyote ya mafuriko hayo. Jina kubwa pekee lililojitokeza kumfuata Lowassa ni Naibu wa Kazi na Ajira, Dkt Makongoro Mahanga, ambaye hata hivyo amechukua uamuzi huo baada ya kubwagwa kwenye kura za maoni. Labda kuna wengine watakaomfuata Lowassa lakini sidhani kama watu hao watakuwa na mafuriko yanayotarajiwa.
Kikwazo kikubwa kwa makada wa CCM waliokuwa wakimsapoti mwanasiasa huyo kumfuata kwenye ‘chama chake kipya’ ni ukweli kwamba tayari vyama vinavyounda UKAWA vilishagawana majimbo.
Sasa sidhani kama kuna mwana-CCM mwenye akili zake atakikimbia chama hicho tawala na kujiunga na vyama vinavyounda UKAWA ilhali anatambua kuwa hata akishindwa ubunge au udiwani katika CCM bado ana fursa ya kuteuliwa kwenye nyadhifa nyingine serikalini.
Na ujio wa wafuasi wa Lowassa ndani ya Chadema na UKAWA unaweza kuvibadili vyama hivyo na kuunda makundi ya, kwa mfano, Chadema- asilia na Chadema-Lowassa. Busara za kisiasa zatuonya kuwa chama chenye mgawanyiko hakiwezi kushinda uchaguzi, na hata kikifanikiwa kushinda, hakitoweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Wakati kwa kumpokea Lowassa Chadema italazimika kutowekeza nguvu za kutosha katika mtaji wake mkuu katika uchaguzi mkuu uliopita – vita dhidi ya ufisadi (hawawezi kupigia kelele ufisadi huko mgombea wao akiwa mtuhumiwa wa ufisadi) – ni vigumu kubashiri watamnadi Lowassa kwa lipi hasa.
Wao ndio walikuwa vinara wa kumwita Lowassa fisadi, sasa muda haupo upande wao kubadilisha maelezo na kumnadi kama mtu safi.
Na hata maelezo ya Lowassa kuwa ‘alipata maagizo ya juu’ katika suala la Richmond hayana uzito kwa sababu kwanini aongee sasa na si wakati alipobanwa hadi kujiuzulu? Sawa, wengi twafahamu kuwa skandali hiyo iliwahusisha watu wengine pia, lakini ukweli unakuwa na nguvu pale tu unapowekwa hadharani wakati mwafaka.
Ni rahisi kwa CCM kuipangua hoja ya Lowaasa kuwa ‘alitumwa’ kwa kumuuliza ‘ulikuwa wapi siku zote hizi usiyaseme hayo hadi sasa ulipoamua kuingia upinzani kwa tamaa yako ya madaraka?’
Nimalizie makala hii endelevu kwa kurejea kuwakumbusha Chadema kuwa dhambi yao ya usaliti itawaandama milele. Hoja kuwa Lowassa ‘anauzika’ na atawasaidia kuingia Ikulu sio tu haina msingi bali pia yaweza kuwagharimu huko mbeleni hasa kwa vile, kama nilivyoandika hapo juu, mwanasiasa huyo hajajiunga na chama hicho kwa vile anakipenda bali kwa ajili ya maslahi yake binafsi.
Nachungulia kidogo tu ‘marafiki zake’ kisha utaelewa nini kinaisuburi Chadema huko mbeleni. Mie si nabii wa majanga (prophet of doom) lakini ninabashiri kuwa ujio wa Lowassa huko Chadema ni mwanzo wa mwisho wa chama hicho.
Inasikitisha kuona ‘People’s Power’ (nguvu ya watu) iliyowavutia wapenda mabadiliko wengi ikiishia kuwa ‘Money’s Power’ (kwa maana ya nguvu ya Lowassa kifedha).Pia inaumiza kuona demokrasia yetu ikipitia mlolongo huu usiopendeza wa ‘chama kimoja→ vyama vingi → chama cha mtu mmoja’ (one party→multiparty→one man’s party)
ITAENDELEA

30 Jul 2015

Kama unavyoona hapo pichani juu, mara baada ya kusikia taarifa kwamba Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa anatarajia kujiunga na vyama vinavyounda Muunganowa Katiba ya Wananchi (UKAWA), niliandika tweet hiyo pichani. Kimsingi, binafsi nilishindwa kabisa kuamini kuwa Dkt Willibrord Slaa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema hadi alipotangaza kujiuzulu, angeweza kukaa chama kimoja na Lowassa. Nilishindwa kabisa kupata picha kichwani kumwona Dkt Slaa akiwa jukwaani anamnadi Lowassa. Nilijaribu ku-imagine kwamba labda kwa vile kuingia kwa Lowassa Chadema kunaweza kukiingiza chama hicho na Ukawa Ikulu, na hivy pengine Dkt Slaa angeweza kumsapoti japo kwa shingo upande, lakini nafsini niliona huo sio tu ungekuwa muujiza - na mie si muumini wa miujiza - bali pia ungekuwa usaliti wa hali ya juu.


Siwezi kujisifu kuwa tweet hiyo ya 'kumsuta' Dkt Slaa imesaidia kumfanya achukue uamuzi huo wa kujiuzulu lakini ninachoweza kusema ni kuwa ninamshukuru kwa kufanya maamuzi magumu ya kujiuzulu hasa ikizingatiwa kuwa neno 'KUJIUZULU' halipo katika kamusi ya wengi wa wanasiasa wetu hata pale wakiwa wanaandamwa na kashfa. Lakini pia ninampongeza Dokta Slaa kwa kusimamia anachooamini.

Kwa hakika Dokta Slaa alisimama kidete kupigana kwa nguvu zake zote dhidi ya ufisadi. Na sifa kubwa ya mwanasiasa huyo ilikuwa umakini wake katika kuwasilisha hoja. Hakuwa mtu wa jazba wala mjivuni. Na kwa hakika alikuwa mwenye kuapanga hoja zake na kuziwasilisha kwa umakini mkubwa. Kwa kifupi, Dokta Slaa aliweza kuwasiliana na umma, iwe katika hotuba au maongezi kama DOKTA hasa, maana moja ya sifa ya usomi ni jinsi ya kuwasiliana na jamii kwa ufasaha.

Kuna watakaokuwa wamefurahi kuona Dokta Slaa amechukua hatua ya kujiuzulu, sio furaha ya kuungana naye kwa kuchukua uamuzi huo mgumu bali kwa vile aidha walikerwa na msimamo wake mkali dhidi ya mafisadi na ufisadi, au walimwona kama mmoja ya sababu zilizopokea Zitto Kabwe kung'olewa Chadema. Furaha hiyo ni ya 'kimburula' kwa sababu Dokta Slaa alikuwa mmoja wa wanasiasa wachache kabisa waliosimama kwa dhati na wanyonge kupigania haki zao. Ukimwondoa marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, sioni mwanasiasa mwingine yeyeote yule aliyewajali mno Watanzania kama Dokta Slaa. Na japo nina furaha kutokana na kukataa kushirikiana na Lowassa, na ninampongeza kwa kuwa na msimamo thabiti, kwa upande mwingine nina masikitiko makubwa kuona lulu hiyo ya taifa ikiachana na siasa wakati bado twaihitaji mno.
Dokta Slaa alifanya kazi yake kwa uadilifu mkubwa na kwa hakika kuna idadi kubwa tu ya Watanzania iliyoamini kuwa siku moja angeweza sio tu kuwa Rais wetu bali pia angeweza kuibadili Tanzania yetu. Na kwa kujiuzulu, amethibitisha ni mwasiasa wa aina gani. Badala ya kutanguliza maslahi binafsi na kujiunga na chama kingine cha siasa au kuanzisha chama chake, Dokta Slaa amechukua uamuzi wa kiungwana. Ametambua kuwa tatizo sio CCM pekee bali mfumo mzima wa siasa za Tanzania yetu, kuanzia chama tawala hadi huko Upinzani. Uamuzi wa kujiuzulu utamlindia hadhi yake milele. 

Mimi ni muumini mkubwa wa 48 Laws of Power, na ninaomba nitanabaishe jinsi uamuzi huo wa Dokta Slaa unavyoendana na baadhi ya Laws hizo. Law 34 of Power inasema (ninainukuu)

The way you carry yourself will often determine how you are treated: In the long run, appearing vulgar or common will make people disrespect you. For a king respects himself and inspires the same sentiment in others. By acting regally and confident of your powers, you make yourself seem destined to wear a crown.
Kwa tafsiri ya Kiswahili ni kwamba "Matendo yako ndio yatakavyofanya watu wakuchukuliaje. Katika muda mrefu, kuonekana mtu wa ovyo ovyo kutafanya watu wasikuheshimu. Kwa sababu mfalme hujiheshimu mwenyewe na kuhamasisha watu wengine kujiheshimu na kumheshimu. Kwa matendo makubwa na ya uhakika wa nguvu zako, utaonekana mtu stahili kushika hatamu." 
Na kwa hakika uamuzi wa Dokta Slaa kujiuzulu unamfanya aendelee kuwa sio tu mtu mwenye msimamo bali pia ataendelea kushikilia hadhi na heshima yake kama mtu aliyeuchukia ufisadi kwa dhati hadi kuamua kujiuzulu baada ya fisadi Lowassa kujiunga na UKAWA.
Kuna wanaoweza kumbeza kwa kusema amekimbia vita. Well, Law 36 of Power inatuasa, nanukuu,

...It is sometimes best to leave things alone. If there is something you want but cannot have, show contempt for it...
Kwa tafsiri ya Kiswahili, "Wakati mwingine ni vema kuacha vitu kama vilivyo Kama kuna kitu unakitaka lakini huwezi kukipata, kichukie tu." Na hicho ndicho alichokifanya Dokta Slaa. Alichukia ufisadi na kuwachukia mafisadi kwa dhati. Lakini ghafla akajikuta analetewa fisadi ashirikiane nae kupinga ufisadi. Waingereza wana msemo "You can't put a drug addict in charge of a pharmacy," yaani huwezi kulikabidhi teja liwe msimamizi wa duka la madawa (ambayo kwa kawaida yana madawa baadhi ya madawa kama Heroin ambayo ndio 'chakula' cha mateja). Kwa vyovyote vile, ingekuwa vigumu mno kwa Dokta Slaa kutimiza azma yake ya kupambana na ufisadi akiwa pamoja na Lowassa. Na ndio maana akaamua bora akae kando. Kama ninavyotamka mara kadhaa, huhitaji kuwa kiongozi ili ulete mabadiliko, kuwa raia mwema tu (You don't have to be a leader to bring change. Just be a good citizen).

Law 47 of Power inasema, ninanukuu,

The moment of victory is often the moment of greatest peril. In the heat of victory, arrogance and overconfidence can push you past the goal you had aimed for, and by going too far, you make more enemies than you defeat. Do not allow success to go to your head. There is no substitute for strategy and careful planning. Set a goal, and when you reach it, stop.

Kwa Kiswahili inamaanisha, "Ushindi unapowadia ndio wakati ambao unaweza kuangamia. Katikati ya ushindi, dharau na kujiamini kupita kiasi vyaweza kukusukuma zaidi ya lengo kusudiwa, na kwa kupitiliza lengo hilo, watengeneza maadui zaidi ya uliowashinda. Kamwe usiruhusu mafanikio kupanda kichwani mwako. Hakuna mbadala wa mkakati na mipango makini. Weka lengo, na ukilitimiza, simama."
Hakuna asiyefahamu alichotimiza Dokta Slaa katika mapambano yake dhidi ya ufisadi. Kubwa lilikuwa kuwaamsha Watanzania, na kwa hakika wengi wamefunguka macho dhidi ya ufisadi na wanauchukia kwa dhati. Angeweza kujikaza kisabuni na kusimama pamoja na Lowassa ili aendeleze mapambano dhidi ya ufisadi, lakini sote twafahamu ingekuwa vigumu mno. Na uamuzi wake wa kujiondoa madarakani ni sawa na inavyosema sheria hiyo hapo juu, 'ukitimiza leno, simama.'
Vilevile, Dokta Slaa amefuata vizuri Law 5 of Power inayoonya kuwa "So much dependes on reputation, guard it with your life," yaani "Hadhi ni kitu muhimu sana, ilinde kwa nguvu zote." Sasa, sote tulikuwa tukiitambua Chadema kama kiongozi wa vita dhidi ya ufisadi, lakini ghafla wametusaliti na kumkaribisha papa wa ufisadi katika chama chao. Kwa vile ni mtu makini na msafi, Dokta Slaa ameona kuwa kwa kufanya hivyo, Chadema imejishushia hadhi yake katika uongozi wa mapambano dhidi ya ufisadi, na akaamua kuilinda hadhi yake kwa kujitenga nao. 
Nimalizie makala hii kwa kurudia kumshukuru Dokta Slaa kwa yote aliyoitendea Tanzania yetu. Tunaouchukia ufisadi tutaendelea kumwenzi na kumkumbuka milele. Nitajitahidi huko mbeleni kufanya mawasiliano na Dokta Slaa ili ikiwezekana niweke kumbukumbu ya huduma yake bora kabisa kwa Watanzania kwa kuandika kitabu kinachomhusu. Nitawa-update kuhusu hilo.
MUNGU AKUBARIKI SANA DOKTA SLAA. TANZANIA ISIYO NA UFISADI INAWEZEKANA PASIPO HAJA YA KUWATEGEMEA MAFISADI. 



29 Jul 2015

KWANZA ninaomba radhi kwa safu hii kuadimika kwa takriban wiki mbili mfululizo. Hali hiyo ilitokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu.

Pili, ninaomba kutoa angalizo kuwa makala hii, niliiandaa mara baada ya vikao vikuu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) huko Dodoma ambapo hatimaye chama hicho kilipata mgombea wake katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu. Nimeihariri ili kufidia yaliyojiri kati ya wakati huo na hivi sasa.

Baada ya kugusia hayo, ninaomba kufanya uchambuzi endelevu kuhusu mchakato wa CCM kumpata mgombea wake wa kiti cha urais, wiki mbili zilizopita.

Nitaonekana mwenye chuki binafsi kwa CCM kama sitakipongeza chama hicho tawala kwa kumudu kufikia hatua ya kupata mgombea wake ‘kwa amani.’ Pamoja na kiu kubwa ya Watanzania kufahamu kada gani wa CCM angeibuka kidedea, kwa kiasi kikubwa mchakato wa kupata mgombea wa chama hicho ulikuwa kama ‘referendum’ kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia ni mwenyekiti wa taifa wa chama hicho tawala, kuhusu kada maarufu, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa. Swali kubwa lilikuwa, “Je Rais Kikwete ataweza ‘kumtosa’ rafiki yake?” Wengine walilielekeza swali hilo kwa Lowassa na kuwa, “Atakatwa au hakatwi?” hasa kwa kuzingatia kile kilichoonekana kama kada huyo kuungwa mkono na wanaCCM wengi.

Lakini hatimaye, maswali hayo yalipata majibu baada ya Lowassa kutokuwamo katika ‘tano bora.’ Licha ya makada Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa kutangaza kutoafikiana na mchakato wa kuchuja ‘wagombea,’ zilipatikana taarifa kuwa kungekuwa na jaribio la kumng’oa Rais Kikwete katika uenyekiti wake na kuivunja Kamati Kuu ya chama hicho, masuala yaliyoishia kuwa porojo tu.

Hatimaye, chama hicho kilimtangaza Dk. John Magufuli kuwa mgombea wake, ambaye naye alimteua Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza wake, akiandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa mgombea mwenza, na iwapo Magufuli akishinda, atakuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania.

Huko nyuma nilifanya ‘ubashiri’ kuhusu makada gani niliodhani walikuwa na nafasi kubwa ya kupita ‘mchujo wa kwanza.’ Wakati si vigumu kuelewa kwa nini Lowassa alikatwa, bado sijaelewa kwa nini kada aliyetarajiwa na wengi kuwa angepitishwa, Jaji Agustino Ramadhani, hakumudu kuingia japo kwenye ‘tano bora.’ Binafsi ninamsikitikia kada huyo kwani kwa namna fulani, ‘kufeli’ kwake kunatia doa wasifu wake ‘wa kupigiwa mstari.’

Pia ‘kufeli’ kwa kada aliyekuwa akitajwa sana, Makongoro Nyerere, kuliwashtua baadhi ya watu lakini yayumkinika kuhisi kuwa msimamo wake mkali wa kutaka kuirekebisha CCM, na kauli yake ya ‘turudishieni CCM yetu’ ilimtengenezea maadui hususan wanaonufaika na ‘sera za ulaji na kulindana’ ndani ya chama hicho.

Nilibashiri kuwa January Makamba angefanya vizuri, na kwa hakika alifanikiwa kuingia kwenye ‘tano bora,’ hatua ambayo yaweza kumtengenezea mazingira mazuri ya kisiasa iwapo ataendelea kuwa na dhamira ya kuiongoza Tanzania huko mbeleni.

Pia nilibashiri mmoja au wawili wa makada wa kike kufanya vizuri katika ‘mchujo wa kwanza,’ na ilikuwa hivyo. Sambamba na hilo, nilibashiri uwezekano wa kuwa na aidha mgombea urais mwanamke au mgombea mwenza/makamu wa rais mwanamke, na hilo limetokea japo nilitarajia angekuwa mmoja wa makada wa kike waliojitokeza kuwania nafasi ya urais.
Kwa upande mwingine, mwathirika mkubwa kabisa wa mchakato huo ni mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru, ambaye pasipo busara aliamua kujidhihirisha kuwa anamuunga mkono Lowassa. Sidhani kama mzee huyo mwenye uzoefu mkubwa wa kisiasa ana washauri wazuri kwani alipaswa kutambua kuwa laiti ‘mgombea wake’ Lowassa akishindwa basi ‘legacy’ yake nayo itayeyuka. Kwa bahati mbaya kwake, Kingunge atakumbukwa zaidi si kama ‘swahiba wa Baba wa Taifa’ bali ‘mkongwe wa kisiasa aliyeangukia pua kwa kumuunga mkono kada aliyetoswa kwenye kinyang’anyiro cha kusaka urais.’ Waelewa wa mambo wanatahadharisha kuwa kujenga hadhi (reputation) ni kitu kinachochukua muda mrefu na kazi kubwa, lakini kosa dogo tu, linaiondoa hadhi hiyo mara moja. Ni rahisi kubomoa kuliko kujenga.

Kwa upande mmoja kuna hisia kwamba Lowassa anaweza asikubali kupoteza mtaji wake wa kisiasa (political capital) katika kilichoonekana kama kuwa na uungwaji mkono mkubwa ndani na nje ya chama chake, kwa kujiunga Ukawa. Akiwa Ukawa na akagombea urais kuhusu swali kwamba atashinda au la, si rahisi kubashiri kwa sasa.

Lakini kwa upande mwingine, jaribio la kuhama CCM linaweza kumgharimu mno mwanasiasa huyo mzoefu. Moja ya athari za wazi ni uwezekano wa kupoteza stahili kadhaa anazopata kama Waziri Mkuu wa zamani. Kadhalika, akihama CCM, chama hicho tawala kinaweza kutumia kila mbinu ‘kummaliza’ kabisa kisiasa. Kama ana washauri wazuri basi pengine ni vema angekubali tu matokeo na ‘kula pensheni yake’ kama Waziri Mkuu wa zamani, bila kuondoka CCM.

Jingine lililojitokeza katika mchakato huo ni ‘kutoswa’ kwa wasaidizi wakuu wawili wa Rais Kikwete, yaani Makamu wa Rais Dk. Gharib Bilali na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Tafsiri ya haraka ni kuwa katika miaka 10 ya utawala wa Rais Kikwete, tulikuwa na viongozi wakuu wawili wa kitaifa ambao pengine hawakustahili kuwa katika nyadhifa hizo na ndio maana wameshindwa kufaulu katika japo mchujo wa awali. Badala ya kukumbukwa kama Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa zamani, Dk Gharib na Pinda watakumbukwa zaidi kama wasaidizi wakuu wa Rais ambao walifeli ‘mtihani wa kurithi nafasi ya bosi wao.’

Sasa twende kwa Dk. Magufuli. Kwanza, ni kweli kuwa amekuwa akisifika kama mchapakazi. Lakini pengine hili ni matokeo ya kasumba iliyojengeka miongoni mwa Watanzania kwamba kiongozi akitekeleza wajibu wake ambao analipwa mshahara kutekeleza wajibu huo, anaonekana kama ‘malaika.’

Taifa letu limekuwa na uhaba mkubwa wa wazalendo kiasi kwamba kiongozi akitekeleza wajibu au kukemea rushwa anaonekana kama ametoka sayari nyingine. Binafsi, ninamwona Magufuli kama kiongozi wa ‘kawaida’ tu ambaye mara nyingi alizingatia matakwa na matarajio ya mwajiri wake. Kama tunawaona madaktari wakijitahidi kuokoa maisha ya wagonjwa kila kukicha huko hospitalini, au walimu wanaofika mashuleni kufundisha (wengi wao katika amzingira magumu), iweje tumwone Magufuli tofauti kwa vile tu anatekeleza mengi ya majukumu anayotakiwa kuyatekeleza?

Moja ya ‘madoa’ kuhusu uongozi wa Magufuli ni suala la uuzwaji wa nyumba za serikali, suala ambalo halijapatiwa majibu ya kuridhisha. Jingine ni ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali aliyopendekeza hatua stahiki zichukuliwe dhidi yake kama Waziri wa Ujenzi na Dk. Harrison Mwakyembe (aliyekuwa Naibu Waziri) kutokana na ufisadi unaofikia shilingi bilioni 256. Kama ilivyo kwenye uuzwaji wa nyumba za serikali, suala hili nalo pia halijatolewa maelezo ya kuridhisha.

Lakini pengine ni usahaulifu wa Watanzania wengi, au ni kile Waingereza wanaita ‘settling for less’ (kuridhika na kilicho pungufu), ile picha inayomwonyesha Magufuli akipata ‘tiba ya Babu wa Loliondo’ haionyeshi kuwasumbua wananchi wengi wanaoonekana kuwa na matumaini makubwa kwa kada huyo. Binafsi, pamoja na kuheshimu uamuzi wa Magufuli kutegemea ‘tiba hiyo ya porojo,’ nilitarajia msomi kama yeye, tena mwenye taaluma ya Kemia angejihangaisha kutafiti kidogo tu kuhusu ufanisi wa ‘tiba’ hiyo ya kitapeli. Je hili ninalolitafsiri kama ufyongo wa kimaamuzi halitojitokeza katika urais wake iwapo atashinda hapo Oktoba?

Kubwa zaidi ni uwezekano wa Magufuli kuwa ‘Kikwete mpya.’ Sio siri kuwa Rais Kikwete amekuwa ‘shabiki’ mkubwa wa utendaji kazi wa Magufuli. Hilo si kosa. Lakini pengine ‘ushabiki’ huo umechangia pia katika mafanikio ya kisiasa ya kada huyo, na haihitaji uelewa mkubwa wa siasa kubashiri kuwa huenda Magufuli akawa na ‘deni’ kwa Kikwete. Licha ya hofu yangu kuu kuwa tatizo kubwa la ‘urais wa Magufuli’ ni ukweli kuwa ni kada wa CCM ile ile iliyotufikisha hapa tulipo, wasiwasi wangu mwingine ni huo uwezekano wa kuwa na ‘Rais mstaafu by proxy,’ yaani Kikwete kuwa na ‘influence’ kwa ‘rafiki yake’ aliyepo Ikulu.

Kadhalika, ninadhani wengi hatujasahau ukweli kwamba ukosoaji mkubwa dhidi ya kada January Makamba ilikuwa uamuzi wake wa kubainisha visheni ya ‘urais wake’ aliyoiita ‘Tanzania Mpya.’ Ukosoaji huo uliegemea kwenye hoja kwamba mgombea urais kwa tiketi ya CCM atajinadi kwa kutumia ilani ya uchaguzi ya chama hicho. Na japo mgombea ana fursa ya kushiriki kuingiza malengo yake, kwa kiasi kikubwa ilani hiyo huandaliwa na chama chenyewe.

Lakini pengine sasa ndio tunatambua umuhimu wa kuwa na visheni kama ‘Tanzania mpya’ ya kada January kwani hatujui lolote kuhusu visheni ya Magufuli zaidi ya kuambiwa ni kuwa ni mchapakazi. Swali la msingi, je, uchapakazi wake utaendana na matakwa ya CCM katika ilani yake ya uchaguzi? Lakini hata kama chama hicho tawala kitamruhusu Magufuli kuandika ilani yake mwenyewe kwa niaba ya chama hicho, je ukada wake (kama ilivyothibitika katika hotuba yake ya kuombea kura huko Dodoma) hautokuwa kikwazo katika kuirejesha CCM kwenye misingi yake ya awali ya kuwatumikia wanyonge badala ya matajiri ilivyo sasa?

Mara kadhaa nimekuwa nikieleza kuwa moja ya vikwazo vikubwa kwa maendeleo ya nchi yetu ni kutanguliza itikadi ya kisiasa badala ya maslahi ya chama. Kada au mwanae anayefahamika kujihusisha na biashara haramu au ufisadi hachukuliwi hatua kwa vile ‘ni mwenzetu.’ Vyombo vya dola vinashindwa kuchukua hatua kwa kuhofia ‘kuwaudhi vigogo wa kisiasa’ Na CCM imekuwa kimbilio kwa watu wa kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafisadi kwa vile sio siri kuwa uongozi katika chama hicho ni mithili ya kinga ya uhakika dhidi ya hatua za kisheria

Tanzania yetu sio tu inahitaji Rais ambaye hana deni la fadhila kwa mtu yeyote yule, atakayetumia ipasavyo nguvu anayopewa na Katiba kuiongoza nchi yetu kwa maslahi ya taifa badala ya kuweka mbele maslahi ya chama, na kwa CCM, mwanasiasa anayetambua kuwa chama hicho kimeporwa na wenye fedha –safi na chafu- na kuwatelekeza wanyonge.
Nimalizie makala hii kwa ahadi ya kuendeleza uchambuzi huu katika makala ijayo nikitarajia kuwa muda huo tutakuwa tumeshamfahamu mgombea wa tiketi ya urais kupitia Ukawa. Pia ningependa kuwahimiza Watanzania wenzangu wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapigakura .

JIUNGE NAMI TWITTER https://twitter.com/Chahali AMBAPO NINAJADILI MASUALA MBALIMBALI

8 Jul 2015

Ufuatao ni waraka kutoka kwa Chama cha DP kinachoongozwa na Mchungaji Christopher Mtikila kumpiga mwania nia ya Urais Edward Lowassa

KATIKA UCHAGUZI MKUU HUU
TUSIRUHUSU MAFISADI WALICHEZEE TAIFA
Edward Lowasa ni balaa kwa Taifa!

Democratic Party (DP) inatarajia kufikisha Mahakamani chama cha
CCM pamoja na wanachama wake sita, Edward Lowasa na wengine,
kwa mujibu wa Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Tanzania, kwa kosa kubwa sana la kuvunja Katiba na Sheria za Nchi kwa kuanza kampeni ya Uchaguzi kabla ya wakati unaopasa kwa mujibu wa Sheria.

1. Tunao ushahidi mzito unaothibitisha kwamba Edward Lowasa na
wenzake walianza kampeni ya urais ndani ya chama chao kabla ya
wakati, na kwamba chama chao kiliwapa adhabu ya kutofanya siasa
kwa miezi 12. Lakini safari hii Lowasa ameanza kampeni ya urais
Arusha kwa mkutano mkubwa sana wa hadhara wa kampeni haramu
na kumwaga rushwa ya kutisha!

2. Kama ni wadhamini alipaswa kuwapata katika ofisi za chama chake, katika mikoa nane (8) tu Tanganyika na mikoa miwili tu Unguja na Pemba, wadhamini 45 tu katika kila mkoa. Lakini Edward Lowasa amefanya mikutano nchi nzima, ya kuwaahidi maelfu ya wananchi katika kila mkutano wa hadhara, mambo atakayofanya kama wakimpa kura zao awe Rais! Hii ndiyo kampeni halisi, ambayo ni ukiukaji wa Katiba na Sheria za Nchi! Uchaguzi Mkuu unaendeshwa na Sheria, hivyo ni lazima Sheria ichukue mkondo wake dhidi yake kwa kuivunja.

3. Edward Lowasa amevunja Katiba ya Nchi na Sheria ya kiwango cha
fedha kinachoruhusiwa kutumika katika shughuli halali za Uchaguzi,
kiasi kwamba CCM na Taasisi zote za uchunguzi wa kifedha nchini,
upelelezi wa Jinai na Usalama wa Taifa ni mlazima wanayo kazi muhimu sana ya kupata ukweli kuhusu haya mabilioni ya fedha yanayomwagwa nchini na fisadi Edward Lowasa, ameyapata wapi na kwa namna gani, kumehusika ‘’Money laundering’ au la, kama mapato ya mapesa hayo yote ni halali, na kama mapato hayo yote yalilipiwa kodi inayopasa kwa ajili ya Taifa.

Ni marufuku kabisa tena ni makufuru Edward Lowasa kuruhusiwa
kugombea urais, kwa sababu amevunja Katiba ya Nchi na Sheria na
Kanuni za Uchaguzi. Sifa mojawapo ya kustahili kugombea uongozi wa nchi yoyote ni maadili mema na uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na
taratibu za Utawala wa Sheria
4. Edward Lowasa, kwa kujimilikisha maeneo nchi nzima kwa kutumia kifisadi Uwaziri wake wa Ardhi, ameliweka Taifa katika hatari kubwa ya mmwagiko wa damu baina ya wakulima na wafugaji, baada ya kueneza nchi nzima makundi ya ng’ombe wake, na kusababisha mapigano makali ya mara kwa mara kila mahali nchini kati ya wafugaji wake na wakulima. Kwa sababu ya uovu huu hata katika kampeni yake haramu Lowasa ameshindwa kusema lolote juu ya kilimo, ingawa ndio uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu na ndiyo shughuli inayotunza uhai wa asilimia 95 ya wananchi!

Kwa kuwaingilia wakulima katika ardhi yao, kuwaua ovyo, kuwaonea
kiasi cha kufisha matumaini yao katika kilimo, kumeifanya kauli mbiu ya “Kilimo kwanza” kuwa porojo tu ya kisanii!

5. Edward Lowasa ni mwiko kabisa kupewa kugombea urais, kwa
sababu siyo tu aliutumia kifisadi Uwaziri wa Ardhi akajitajirisha na
kujipatia maeneo makubwa ya ardhi nchini kote, bali alitumia kifisadi
zaidi uwaziri wa nchi katika ofisi ya Waziri Mkuu, katika uagizaji wa
mashangingi ya Wabunge, mawaziri, wakuu wa Mikoa na Wilaya.

6. Edward Lowasa alikemewa mnamo mwaka 1995 na Mwalimu Nyerere anayeenziwa na CCM lama “Baba” yao, alipotaka kugombea urais, kwa sababu alikuwa fisadi papa, wala hakuweza kujitetea kwavile utapeli wote aliojitajirishia ulikuwa mezani. Leo baada ya mabiashara haramu mengi na kulipora sana Taifa kukiwa ni pamoja na utapeli wa “kununua mvua Thailand” na kuliibia Taifa mabilioni ya fedha kwa kutumia kampuni hewa ya RICHMOND, huyu ni fisadi-nyangumi. Ni mlemavu wa rushwa tu wa kununuliwa na mapesa machafu anayomwaga Lowasa, anayeweza kumruhusu fisadi Edward Lowasa agombee urais.

Sifa za mtu wa kukugombea Urais zimeelezwa bayana na Mwenyezi
Mungu katika Kumbukumbu la Torati 17:15-20, ambazo Edward
Lowasa hana hata mojawapo! Lowasa awali alikemewa na Mwalimu
Nyerere ambaye CCM wanamuenzi kama “Baba” yao, kuwa hafai kabisa kuwania urais, kwa sababu alikuwa fisadi papa, kama alivyomtangaza hata Reginald Mengi pale alipolazimika kujiuzulu Uwaziri Mkuu kwa ajili ya wizi kwa kampuni hewa ya Richmond, lakini leo akiwa fisadi la kutisha zaidi kuliko papa eti anataka urais!
Si ajabu kwamba magabacholi yalioipora vibaya sana Nchi hii kama Sigh Setti na hata Nazir Karamagi wote wamo katika genge la Edward
Lowasa! Si ajabu hata fisadi Reginald Mengi leo kuungana na fisadi
Lowasa yakizingatiwa machafu yake yeye mwenyewe, na kuhusika kwa Mengi na mauaji ya Chacha Wangwe, pamoja na mpango wa Chadema
wa kumwua Mchungaji Mtikila, waraka feki wa kujaribu kuupotosha
ukweli ukatangazwa kwa ITV yake.

Katika uwaziri wake katika ofisi ya Waziri Mkuu, na katika Uwaziri wakewa Ardhi na Uwaziri Mkuu, Lowasa alifanya ufisadi ambao katika nchi kama China zenye uchungu na maslahi ya mataifa yao angekuwa wa kupigwa risasi hadharani, lakini katika nchi yetu anatafuta urais!

7. Edward Lowasa AFYA yake imempiga marufuku kugombea Urais!
Kwa ajili ya kila ajira duniasni kote, moja ya mashart makuu ni lazima mwombaji awe na afya iliyo bora, ndiyo sababu ni lazima ajira ya kila mwombaji itegemee taarifa ya kitaalamu ya madaktari, inayothibitisha kwamba hana dosari kiafya. Sharti hili ni la lazima kwa sababu:
a. Majukumu yote atakayopewa mwajiriwa atayatekeleza kikamilifu
kwa kutumia viungo vya mwili wake, kwahiyo viungo vyake vyote
ni lazima viwe katika hali iliyo imara kwa ajili ya kazi.

b. Hata kama kwa uthibitisho wa kitaalamu wa madaktari mwajiriwa
anazo akili nzuri kichwani mwake, akiwa na hitilafu katika viungo
vingine vya mwili wake huathiri afya ya akili zake na uwezo wa
utendaji wa akili zake.

c. Kazi ya Rais ni ngumu sana, kwa sababu ni pamoja na kusimamia
shughuli zote za maendeleo ya nchi nzima, na matatizo yote
yanayowatokea wananchi wote kila walipo, na kusimamia
utekelezaji wa majukumu yote ya watendaji wote katika Taifa,
hivyo kwamba maamuzi sahihi yanatokana na afya bora yenye
kuhakikisha uwezo unaopasa wa kiakili wakati wote

d. Hitilafu katika afya hudhoofisha uwezo wa kifikira na kusababisha
maamuzi mabovu, ambayo huleta athari mbaya sana kwa Taifa. Na
udhaifu huo huathiri mpaka maadili na hata uzalendo wa huyo
kiongozi mdhaifu. Kwa mfano akipatikana Rais anayeishi kwa
matumaini, kwa hofu ya kupoteza uhai kabla hajaweka sawa
mambo yake na ya familia na jamii yake atatumikia maslahi yake
zaidi kuliko Taifa, tatizo hilo la afya likawa limelikosesha Taifa
kipaumbele, na kuliangamiza kimaendeleo!
e. Wanaowania kugombea urais ni lazima wachunguzwe kwa makini
sana afya zao, kwa sababu kukifanyika makosa akatawazwa
mwenye hitilafu za kiafya, atakwenda kuwa mzigo mzito sana kwa
Taifa, hususan ugharamiaji wa utunzaji wa uhai wake ndani na nje
ya nchi, kukosekana na umakini anaopasa kuwa nao kwa ajili ya
dhamana kubwa aliyopewa n.k.

Kutokana na AFYA yake kuwa dhaifu sana hata kwa kumwona kwa
macho tu, kabla ya uchunguzi wa kitaalamu ni kwamba Edward Lowasa hawezi kabisa kugombea Urais. Kwani amekosa sifa muhimu sana ya afya bora, ambayo ni ya lazima kwa mtu yeyote anayestahili kupewa dhamana kubwa sana ya kuliongoza Taifa. Pengine hata kugombea urais kwenyewe anatafuta kutokana na hitilafu ya kiafya, iliyosababisha udhaifu katika kufanya maamuzi, hivyo amejikuta kwa bahati mbaya anagombea asichokiweza kabisa.

Ni lazima wagombea wote wa Urais, wa Ubunge na hata wa Udiwani
wachunguzwe kwa makini afya zao kabla ya kupewa kugombea, na hata kuchunguzwa tena katikati ya muhula wa utumishi wao, kama kweli tunalithamini na kuliheshimu Taifa.

Sifa za urais ni wito au uhanga kwa ajili ya Nchi ambao ni zaidi ya
maadili ya kizalendo, maono, vipawa na AFYA BORA. Ni dhana potofu
sana kwamba sifa ya urais ni kushabikiwa na umati wa watu! Kwa
sababu wengi hufuata mapesa na husombwa hata na magari ili umati
wa kishabiki tu upatikane. Lakini kumpenda mtu huwa lazima kuwe na sababu, wakati ushabiki ni pepo mchafu au ‘psychological deficiency’.





4 Jul 2015

Kwa niaba ya familia ya Mzee Philemon Chahali, ninaomba kuwashukuru nyote mnaoungana nasi kumwombea dua/sala ili apone. Hatuna cha kuwalipa bali kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awabariki kwa upendo wenu. Pia kwa vile hali ya baba bado si ya kuridhisha, tunawaomba tuendelee na dua/sala zaidi. Wanasema 'penye wengi Mungu yupo' basi ni matumaini yetu kuwa ushirikiano huu katika sala/dua utapelekea kupona kwa Mzee Chahali. Again, asanteni sana, na Mungu awabariki sana.

Tangu nipate taarifa za kuumwa kwa baba, nimepunguza kujishughulisha na 'kelele' zangu kuhusu masuala mbalimbali yanayoikabili Tanzania yetu. Sijafanya hivyo kwa maana ya kupuuzia masuala hayo bali kichwa changu kimetawaliwa na suala la afya ya baba yangu kwani ndo mzazi pekee niliyebakiwa naye baada ya kufiwa na mama mwaka 2008.

Hata hivyo, leo nimelazimika kuandika makala hii baada ya kufanya maongezi na jamaa yangu mmoja huko Tanzania ambaye katika nafasi yake kikazi, anafahamu mambo mengi yanayojiri 'nyuma ya pazia.'

Alichoniambia kimenishtua sana. Ni kuhusu kampeni zinazoendelea mtandaoni zinazomhusisha mtoto mdogo anayejiita DOGO JEMBE. Pia kampeni hizo zinatumia hashtag #IkuluSio.

Huyo jamaa yangu, pengine kutokana na majukumu yake kikazi au ufuatiliaji tu, amenionyesha ushahidi unaothibitisha kuwa kampeni hiyo inaendeshwa na mtangaza nia mmoja wa CCM. Kwahiyo tofauti na picha inayojengwa na DOGO JEMBE kuwa yupo upande wa maslahi ya Watanzania, kimsingi mtoto huyo anatumiwa tu na mwanasiasa huyo anayetaka urais. 

Kwa mujibu wa jamaa yangu huyo anayefanya kazi katika taasisi moja 'nyeti' huko nyumbani, kosa la msingi lililofanywa na waandaaji wa kampeni hiyo ni kwenye kitu kinachofahamika kama IP Address ambayo kwa lugha nyepesi ni anwani ya mlolongo wa namba zinazotenganishwa na nukta ambao unaitambua kompyuta katika mtandao. 'Mtaalam' huyo amefanikiwa kubaini kuwa posts za kampeni hiyo zinatoka kwa IP address ya mdogo wa mwania nia fulani. Amenitumia screenshots zenye uthibitisho kuhusu suala hilo.

Amenijulisha pia kuwa taasisi anayoitumikia inafahamu bayana kuhusu 'uhuni' huo, na hii unaisoma hapa kwa mara ya kwanza, usishangae ukikutana na breaking news hii katika vyombo vya habari katika siku chache zijazo. Inaelekea kuna 'wakubwa' hawajapendezwa na mbinu hiyo ya kuwahadaa Watanzania kwa kisingizio cha kumsaka Rais bora.

Kilichomkera, kinachonikera, na ambacho pengine nawe Mtanzania kitakukera ni kitendo cha mwania huyo kuwafanya Watanzania wapumbavu. Kwanini nasema hivyo? Kwanza ni 'kosa' la kumtumia mtoto mdogo kuvuta hisia za watu, kuwaaminisha kuwa lengo ni kupigania maslahi ya taifa kwa kuamsha tafakuri ya nani hasa anatufaa kuwa Rais wetu ajaye, ilhali ukweli ni kwamba kampeni hiyo ina lengo la kumpigia debe mwania nia huyo.

Kumtumia mtoto huyo mdogo kwa minajili ya kisiasa hakuna tofauti na kile kinachoitwa CHILD LABOUR, yaani kuwatumikisha watoto. Sasa hapo tu yatupasa kutambua kuwa child labour ni ukiukwaji wa haki za binadamu, na kwa minajili hiyo, mwania nia anayesaka urais kwa kukumbatia ukiukwaji wa haki za watoto/binadamu HAFAI.

Pili, hadaa, usanii, na uhuni mwingine wa kisiasa ndivyo miongoni mwa vitu vilivyotufikisha hapa. Sasa kama katika hatua hizi za awali tu za kuwania kupitishwa na chama kuwania urais mwanasiasa anaanza kukumbatia vitu kama hivyo, huhitaji kuwa mwenye uelewa mkubwa wa kisiasa kubaini kuwa mwania nia huyo hafai hata ujumbe wa nyumba kumi, achilia mbali urais.

Tatu, japo watoto wana haki ya kikatiba na kidemokrasia kuzungumzia kuhusu hatma ya taifa letu ikiwa ni pamoja na Uchaguzi Mkuu ujao, hiyo sio excuse kwa wamasiasa yeyote yule kutumia haki hiyo ya watoto kwa manufaa yake binafsi. Angekuwa jasiri, angejitokeza mwenyewe hadharani badala ya kujikampenia kwa kutumia child labour.

Kwa mujibu wa jamaa yangu huyo ambaye kwa ninavyomfahamu hana kambi yoyote hasa kwa vile majukumu yake kikazi yanamzuwia kujihusisha na siasa, kuna data nyingine ambazo zinaihusisha moja kwa moja kampeni hiyo na mwania nia huyo.

Japo nipo katika wakati mgumu kutokana na kuzorota kwa afya ya Mzee Chahali lakini afya ya Tanzania yetu ni muhimu pia kama afya ya mzazi wangu, na nimeshindwa kukaa kimya baada ya kuletewa ushahidi kuhusu 'uhuni' huu. 

Amenieleza kuwa kauli ya Dogo Jembe kuwa 'Ikulu sio ya baba yako' ilimlenga Makongoro Nyerere kwa vile yeye ni mtoto wa Nyerere, na kauli kuwa 'Ikulu sio hospitali' illimlenga Lowassa kwa vile mwania nia huyo amedaiwa kuwa afya yake sio nzuri japo haijathibitishwa. 


Lakini pengine hata bila kupata 'ufunuo' huu, ilipaswa tujiulize NANI ANAYEFADHILI KAMPENI HII YA KISASA KABISA?

Kwa mtizamo wa jamaa yangu huyo, kosa jingine la kampeni hiyo ni kwamba imejitengenezea 'ufupi wa maisha' kwa maana kwamba ipo siku Dogo Jembe atalazimika kuwashawishi tena Watanzania kuwa 'mtaka nia flani ana sifa za dogo jembe, na ndio anafaa kuwa Rais,' na hapo all hell will break loose kwa sababu kila mwenye akili timamu atabaini nani alikuwa behind kampeni hiyo.

Anyway, ningetamani kuandika kwa kirefu lakini wito wangu kwa Watanzania wenzangu ni mdogo tu: AKILI ZA KUAMBIWA, CHANGANYA NA ZA KWAKO. Tumeshwahi kuhadaiwa huko nyuma, tumeshaona matokeo ya hadaa hizo, chonde chonde, tusirejee tena makosa hayo. Kama katika kuwania tu kupitishwa na CCM, mwanasiasa yupo radhi kutumia mtoto mdogo kuwahadaa Watanzania, je akifanikiwa kuingia Ikulu itakuwaje? Ni muhimu pia kutambua kuwa mwanasiasa ambaye yupo desperate mno kuingia Ikulu lazima atakuwa na ajenda zake binafsi,

Nimalizie kwa kuwashukuru tena nyote mnaojumuika nasi kumfanyia dua/sala Mzee Chahali, na ninawashukuru sana, na kuwaombea Mungu awabariki sana. 



25 Jun 2015

NIANZE makala hii kwa kuomba radhi kutokana na kushindwa kuwaletea makala katika toleo lililopita. Hiyo ilitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu. Ninaomba pia kutumia fursa hii kuwatakia ndugu zangu Waislamu mfungo mwema wa mwezi Mtukukufu wa Ramadhani.
Katika makala ya hii nitaendelea kuzungumzia kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu. Na zaidi nitaelemea katika nafasi ya urais, hususan mchakato unaoendelea ndani ya chama tawala, CCM, ambapo hadi wakati ninaandaa makala hii, makada 37 wa chama hicho wameshajitokeza kuomba ridhaa ya chama hicho kuwapitisha kuwania nafasi hiyo.
Lakini kabda sijaingia kwa undani, pengine ni muhimu tukumbushane kuwa wakati idadi ya makada 37 (ambayo huenda ikaongezeka) ni ya kihistoria, suala la kushtua zaidi ni ukweli kwamba miongoni mwao ni pamoja na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na mawaziri kamili saba, bila kujumuisha manaibu waziri.
Nimekumbushia suala hili kwa sababu ni vigumu kufahamu serikali yetu muda huu inaendeshwaje, hasa ikizingatiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete nae amekuwa katika safari za mara kwa mara nje ya nchi (wakati ninaandika makala hii yupo nchini India).
Ukiondoa Makamu wa Rais, ambaye anakuwa kaimu Rais wakati Rais anapokuwa nje, licha ya majukumu ya kiwaziri, Waziri Mkuu na hao mawaziri wengine pia ni wabunge. Katika hili ni vigumu kufahamu wanamudu vipi kugawa muda wao kwa majukumu yao ya kiserikali, kiubunge na hayo ya kuwania kuteuliwa kuwania nafasi ya Urais.
Hata hivyo, si vigumu kudhani kwamba kwa muda huu, akili na nguvu kubwa kwa makada wote waliotangaza nia zitakuwa zimeelekezwa kwenye kinyang’anyiro cha Urais. Kwa kiasi gani hilo linaathiri utumishi wao kwa umma, ni vigumu kwa sisi wengine kufahamu.
Nikirejea kwenye suala la makada wa CCM kutangaza nia zao kuwania urais, jina lililosikika zaidi wiki iliyopita lilikuwa la Jaji Mkuu wa zamani, Augustino Ramadhan. Japo jina lake lilishawahi kutajwa huko nyuma kama mmoja wa watu ‘wanaoweza kuokoa jahazi,’ lakini kwa kiasi kikubwa habari zilizosikika huko nyuma zilionekana kama tetesi tu pasi uthibitisho.
Angalau mara mbili, gazeti hili la Raia Mwema lilibeba habari zilizohusu uwezekano wa Jaji Ramadhani kugombea urais kwa tiketi ya CCM.

Binafsi, kwanza ninaheshimu uamuzi wa Jaji Ramadhani kwani ni haki yake ya Kikatiba kuchukua uamuzi huo. Hata hivyo, tayari kuna baadhi ya wananchi walioshtushwa kumsikia Jaji huyo akielezea kuwa amekuwa mwanachama wa CCM tangu miaka ya sitini.
Kwanza ninadhani alipitwa tu kutoa kauli hiyo kwa sababu CCM iliundwa mwaka 1977 baada ya TANU na ASP kuungana. Kwahiyo, hakukuwa na CCM miaka ya sitini.
Jaji huyo alieleza kuwa alijiondoa CCM mwaka 1992 kufuatia mabadiliko ya sheria, ambapo mfumo wa vyama vingi uliruhusiwa na hiyo kupelekea watumishi wa umma kutoruhusiwa kuwa wanachama wa vyama vya siasa.
Japo Jaji Ramadhan anasema alijiondoa CCM wakati huo, kuna wanaokwenda mbali zaidi na kutaka uthibitisho katika suala hilo. Sote tunaijua Tanzania yetu, na kwa hakika tunawafahamu vema viongozi na wanasiasa wetu. Ni kwa mantiki hiyo, kuna wanaotaka uthibitisho kuwa kweli Jaji huyo alijiondoa CCM na kutokuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa katika utumishi wake, ikiwa ni pamoja na Ujaji Mkuu.
Na kauli hiyo ya uana-CCM wake, kwa namna flani, imerejesha tena suala la hukumu iliyotolewa na Jaji huyo kwa kushirikiana na majiji wengine dhidi ya kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila aliyetaka mahakama itamke kuwa sheria inayozuwia mgombea binafsi ni kinyume cha Katiba.
Pasi kuingiza kiundani katika kesi na hukumu hiyo, binafsi ninaichukulia hukumu hiyo kuwa moja ya hiba (legacies) kuu za utumishi wa Jaji Ramadhani.
Kwa baadhi yetu tunadhani Jaji huyo angebaki shujaa kwa demokrasia kwa sababu mfumo wa sasa unaolazimisha wawania nafasi mbalimbali za uongozi ikiwa pamoja na urais kuwa wanachama wa vyama vya siasa unatupunja fursa ya kupata viongozi wa kisiasa wazalendo lakini wasiotaka kujihusisha na vyama vya siasa.
Hata hivyo, ili kumtendea haki, ni muhimu kutambua kuwa hukumu hiyo haikuwa maamuzi binafsi ya Jaji Ramadhani bali licha ya kuwahusisha majaji wengine pia, ilikuwa ni ya kisheria na sio hisia binafsi.
Lakini kwangu, licha ya dalili zinazoonekana wazi kuwa kana kwamba CCM imeshapata mgombea wake urais kufuatia uamuzi wa Jaji Ramdhan kutangaza nia, nina wasiwasi kidogo kuhusu ufanisi wake.
Kubwa zaidi ni ukweli kwamba Idara ya Mahakama, ambayo licha ya Jaji Ramadhan kuitumikia muda mrefu bali pia aliwahi kuwa mkuu wake kwa maana ya ujaji mkuu, imeendelea kuwa moja ya taasisi sugu kwa rushwa. Takribani kila ripoti inayotolewa kuhusu tatizo la rushwa katika taasisi mbalimbali za serikali nchini mwetu, Idara ya Mahakama haikosekani, na tena ikishika nafasi za juu.
Mara baada ya kuchukua fomu kuomba CCM imteue kuwania Urais, Jaji Ramadhan aliwaambia waandishi wa habari kuwa atatumia uzefu wake kupambana na ufisadi. Swali la msingi: uzoefu upi? Huohuo ulioshindwa ukiondoa Idara ya Mahakama katika orodha ya taasisi zinazoongoza kwa rushwa?
Kwa upande mwingine, Jaji Ramadhan alikuwa mjumbe wa ‘Tume ya Warioba’ iliyokusanya maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba. Sote twakumbuka yaliyomsibu Jaji Joseph Warioba na baadhi ya wasaidizi wake kupigania sio tu kazi nzuri iliyofanywa na tume yao bali pia mustakabali wa Katiba mpya.
Kwanini Jaji Ramadhani amekuwa kimya sana katika suala hilo? Je ukimya wake ulitokana na kufahamu kuwa siku moja angeomba kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM?
Na katika hilohilo, kwa vile mapendekezo ya Tume hiyo iliyomshirikisha Jaji Ramadhani yalikuwa muungano wenye muundo wa serikali tatu, je kwa vile CCM ambayo jaji huyo anaiomba ridhaa ya kumteua awe mgombea wake ina msimamo wa serikali mbili kama ilivyo sasa, hilo si tatizo angalau kimsimamo na kimtizamo?
Hadi muda huu, Jaji Ramadhani ni Rais wa Mahakama ya Afrika kuhusu haki za binadamu. Sihitaji kuorodhesha matukio lukuki ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Tanzania lakini miongoni mwa matukio makubwa ni pamoja na ukatili unaofanywa na Jeshi la Polisi na rushwa (naam, rushwa sio tu adui wa haki bali pia inachangia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu).
Je Jaji Ramadhani amekuwa wapi wakati ukiukwaji wa haki za binadamu ukiendelea kushamiri na kuwa kama umehalalishwa na Katiba yetu? Ni nani anaweza kusimama hadharani na kuwaambia Watanzania kuwa ‘Urais wa Jaji Ramdhani katika Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika umechangia hili na lile katika kutetea au kudumisha haki za binadamu nchini Tanzania’?
Niwe mkweli, binafsi ninamwona Jaji Ramadhani kama Rais Kikwete alipojitambulisha mwaka 2005 kuwania urais na hatimaye kushindwa nafasi hiyo.
Alionekana mtu mwadilifu, aliyeitumikia nchi kwa muda mrefu, na pengine kubwa zaidi, msafi (asiye na kashfa). Sifa hizo zinalingana na tunazosikia kuhusu Jaji Ramadhan. Je, kwa mfano, kuwa msafi ni sawa na kuwa na uwezo wa kuongoza nchi?
Lakini la mwisho kuhusu kada huyo ni taarifa za awali kuwa amekuwa akiombwa na baadhi ya wana-CCM kuwania nafasi ya urais (kuna wanaodai kuwa ndio mtu pekee anayeweza kumudu ‘kumzuia’ Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa asiingie Ikulu, na wengine wanasema Jaji huyo ndio ‘msafi zaidi’ kuliko makada wengine wanazowania nafasi hiyo).
Swali la msingi: je hao waliomwomba (kama ni kweli) hawafanyi hivyo kwa maslahi yao binafsi? Na je, kumwomba huko (kama ni kweli) hakutopelekea urais wa Jaji Ramadhan (iwapo atashinda) ukaishia kuwa kama ‘deni la kwa wanamtandao’ lilivyouandama utawala wa Rais Kikwete?

Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha tena Watanzania wenzangu kuwa ni muhimu tujiulize na kuwauliza wawania urais maswali magumu ili tusije kuishia kujiulaumu huko mbeleni.
Nchi yetu ipo katika wakati mgumu; umasini wa kupindukia huku ufisadi ukizidi kuimarika, uhaba mkubwa wa uzalendo, utovu mkubwa wa maadili ya uongozi ikiwa na pamoja na uhuni katika matumizi ya fedha za umma, shilingi inayporomoka kama ipo kwenye mashindano ya marathoni na kadhalika.
Tunahitaji rais ambaye si tu anajua matatizo yetu bali pia ana uzalendo na uwezo wa kukabiliana nayo. Hatuhitaji Rais msafi lakini mwoga wa kupambana na maharamia wanaoibomoa nchi yetu kila kukicha.
Hatuhitaji mtu anayeahidi kupambana na rushwa ilhali hana mfano japo mmoja wa jinsi alivyowahi kupambana na rushwa.

-

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.