Showing posts with label Magufuli. Show all posts
Showing posts with label Magufuli. Show all posts

18 Mar 2019


 
Leo Machi 18, 2019 ni siku ambayo lazima iingie kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa sababu kuu tatu, ambazo zote zinamhusu mwanasiasa mkongwe Seif Sharif Hamad na Chama cha Wananchi (CUF)

Sababu ya kwanza, leo ni siku ambayo mwanasiasa huyo, maarufu kwa jina la Maalim Seif, "ametimuliwa" rasmi kutoka chama alichoshiriki kukiasisi (CUF).
Kibaya zaidi, "kutimuliwa" huko kumekuwa na baraka kisheria, baada ya Mahakama Kuu kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho.

Ikumbukwe tu Lipumba alitangaza kujiuzulu uenyekiti kwa sababu anazozijua yeye kabla ya kuamua kurejea kwenye wadhifa huo "kwa mabavu." Kwa bahati mbaya – au pengine makusudi – sheria na kanuni za CUF zilikuwa zinatoa mwanya kwa Lipumba (au mwanasiasa mwingine yeyote yule) kufanya "uhuni" kama huo.

Sababu ya pili, ni kwamba leo CUF imekabidhiwa rasmi kwa Lipumba. Kisheria. Mahakama imetenda haki kwake kwa sababu japo alichofanya ni uhuni, kisheria uhuni huo ulihalalishwa na CUF yenyewe.

Hili la Lipumba kukabidhiwa chama si jambo dogo. Kuna mawili hapa. Moja, hii inaweza kuwa fursa nzuri kwa Lipumba kukijenga chama hicho na hatimaye kukirejesha kwenye nafasi ya kuaminika kama "mbadala wa CCM."

Lakini la pili, na hili ndilo ninahisi litatokea, ni mwanzo wa mwisho wa CUF. Sio siri kuwa Lipumba amesaidiwa sana na CCM kuipora CUF kutoka mikononi mwa Maalim Seif. CCM hawajafanya hayo kwa vile wanampenda Lipumba.Hapana. Wanamtumia tu kumdhibiti Maalim Seif ambaye licha ya kila hujuma zilizokuwa zikifanywa na CCM na taasisi zake, ameendelea kuwa mwanasiasa maarufu zaidi kuliko wote katika siasa za Zanzibar.

Sasa, baada ya Lipumba kutumika "kummaliza Seif ndani ya CUF," kuna uwezekano wa aina mbili tu. Wa kwanza ni kwa mwanasiasa huyo msomi kukubali kuendelea kutumika kama kibaraka wa CCM huku CUF ikigeuka kuwa CCM-B, na wa pili, ni kujaribu kusimama kama chama halisi cha upinzani na hapohapo "kumwagiwa radhi na CCM" na hatimaye kupelekea kifo cha chama hicho.

Uwezekano mkubwa zaidi ni huo wa kwanza - ukibaraka. Kwamba CUF haitokufa. CUF itaendelea kushiriki chaguzi mbalimbali. CUF itajenga taswira ya chama kamili cha upinzani. Lakini uwepo huo wa CUF hautokuwa kwa manufaa ya chama hicho au siasa za upinzani bali kwa manufaa ya CCM.

Kuna kila dalili kuwa CCM itaisaidia CUF kujitanua nchi nzima kwa sababu moja kuu: uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utakuwa mbovu kuliko chaguzi zote zilizowahi kutokea Tanzania. Kuna uwezekano mkubwa tu kwa baadhi ya vyama vikuu vya upinzani kutishia kususia uchaguzi huo. Na hapo ndipo CUF ya Lipumba itakapotumika kuhalalisha "ushindi wa Magufuli/CCM."

CCM itaisaidia CUF kuweza kusimamisha wagombea takriban kila jimbo kwa upande wa Tanzania Bara. Lakini pia CCM itaisaidia CUF kuendelea kuwa chama imara cha upinzani huko Zanzibar, ambako uimara wake utasaidia kugawa kura dhidi ya CCM na wagombea wake.

Hata hivyo, "laana ya kutumika" itaikumba CUF baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kama isipoishia kusambaratika basi itabaki "chama jina" kama TLP ya Mrema.

Kuhusu uamuzi wa Maalim Seif kuhamia ACT- Wazalendo, japo hatua hiyo inaweza kuwashangaza baadhi ya watu, ukweli mchungu baada ya Mahakama Kuu kuhalalisha "uhuni" wa Lipumba, sambamba na "uhuni" wake mwingine majuzi ambapo "alijitangaza" kuwa Mwenyekiti kupitia "uchaguzi mkuu hewa" ambao pia "ulimtimua Maalim Seif" kwa kuteua mtu mwingine kushika wadhifa wa Katibu Mkuu.

Kwa kuzingatia muda mfupi uliosalia kabbla ya uchaguzi mkuu wa mwakani, Maalim Seif kuendelea kutafuta haki yake mahakamani kungeweza kumkuta akiwa bado kwenye korido za mahakama wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu ujao. Ni vigumu mno kwa chama cha siasa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi mkuu huku kikiwa kinakabiliwa na mpasuko katika uongozi wake wa juu.

Kwahiyo, kimkakati, uamuzi huo wa Maalim Seif unaeleweka, na unaweza kuwa ni mbinu muhimu kwake kuendelea kuwa relevant kisiasa.

Hata hivyo, kuna uwezekano wa aina mbili kuhusu mustakabali wa Maalim Seif na wa chama chake kipya cha ACT- Wazalendo.

Uwezekano wa kwanza ni kwa chama hicho kuibuka kuwa tishio katika siasa za Tanzania. ACT – Wazalendo ni chama kizuri lakini ambacho hakikui. Kimeendelea kuwa "chama cha mtu mmoja" chini ya uongozi wa Zitto Kabwe. Kwa muda mwingine, chama hicho kimekuwa cha kiharakati zaidi kuliko cha kisiasa.

Mapungufu hayo yanaweza kubadilika kwa njia kuu tatu. Kwanza, Maalim Seif hajawahi kupata fursa nzuri ya kunadi mvuto wake kwenye majukwaa ya siasa za Tanzania Bara. ACT-Wazalendo wanaweza kuwa Jukwaa muhimu katika hilo.

Pili, Zitto  hajawahi kupata jukwaa mwafaka kunadi mvuto wake wa kisiasa huko Zanzibar. Kwa kuungana na Maalim Seif, hii inaweza kuwa ndio fursa mwafaka kwake.

Tatu, ACT-Wazalendo kama chama inaweza kupata fursa mwafaja kabisa ya kuwa chama cha kitaifa badala ya kuwa "chama cha Kigoma."

Haya yote yatawezekana tu endapo kutakuwa na "kujitoa mhanga" kati ya mwenyeji Zitto na mgeni Maalim Seif. Kwa mara ya kwanza, Zitto atajikuta akiongoza chama ambacho ndani yake kuna mwanasiasa maarufu zaidi yake. Naam, Maalim Seif ni mkongwe zaidi kisiasa kuliko Zitto. Endapo Zitto "atajitoa mhanga" (make a sacrifice) na kukubali "kumezwa" na umaarufu wa Maalim Seif, basi chama hicho kitakuwa na fursa kubwa ya kupanuka zaidi na hata kuja kuwa chama kikuu cha upinzani katika pande zote za Muungano.

Lakini endapo kutakuwa na mgongano wa ego kati ya wanasiasa hao, basi mustakabali wa chama hicho utakuwa mashakani. Lakini pengine uwezekano wa hili kutokea ni mdogo kutokana na ukweli kwamba suala la Maalim Seif kujiunga na ACT-Wazalendo sio limetokea tu ghafla. Ni dhahiri kuwa kulikuwa na majadiliano ya muda mrefu na yayumkinika kuhisi kwamba tofauti kati ya wanasiasa hao wawili (Maalim Seif na Zitto) zilifanyiwa kazi wakati wa majadiliano hayo.

Suala jingine ambalo linaweza kuijenga ACT-Wazalendo "mpya" (ya Zitto na Maalim Seif) au kuibomoa ni mtihani ulioikumba Chadema mwaka 2015.

Kwa mwelekeo ulivyo ndani ya CCM ambapo Magufuli hafanyi siri kuwa anataka chama hicho kiwe chini ya uongozi wa watu wake (wengi wao wakiwa wana-Kanda ya Ziwa wenzake), kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka wimbi kubwa tu la wanasiasa wenye majina watakaotaka kuhamia Upinzani. Na endapo Zitto na Maalim Seif watakuwa "dream team" ya kuaminika, basi ACT-Wazalendo inaweza kuwa na mvuto zaidi kwa "wakimbizi kutoka CCM" kuliko Chadema.

Si ajabu kwa wanasiasa kama Nape Nnauye, Mwigulu Nchemba, Bernard Membe kujiunga na ACT-Wazalendo endapo chama hicho kitaonekana kuwa kinaweza kutoa ushindani wa dhati dhidi ya CCM hapo mwakani.

Sasa, wakati kupokea "majina makubwa" kutoka CCM husaidia kuongeaza umaarufu wa chama, uzoefu umeonyesha kuwa wengi wao wenye majina hayo makubwa ni wanafiki wanaokwenda upinzani kwa sababu zao binafsi na sio kwa maslahi ya vyama husika vya upinzani.
Kibaya zaidi, kila ujio wa "wahamiaji" hao ni fursa mwafaka kwa CCM kupandikiza "mamluki" wake kama ilivyotokea kwa Chadema ilipompokea Lowassa mwaka 2015.

Je ACT-Wazalendo "mpya" inaweza kutoa upinzani wa dhati dhidi ya CCM hapo mwakani? Jibu fupi ni "muda ndio utaongea" (time will tell). Jibu pana zaidi ni kwamba japo uwezekano huo upo lakini sidhani kama muda unatosha kukitanua chama hicho nchi nzima hususan katika kipindi hiki ambacho chama pekee cha siasa kinachoruhusiwa kufanya shughuli za siasa ni CCM tu.

Hata hivyo, endapo mkazo wa ACT-Wazalendo utakuwa katika sio tu kuongeza idadi ya wanachama bali kujenga kuaminika kwa "Watanzania wasio na vyama," basi huenda chama hicho kikafanya vizuri kwenye uchaguzi mkuu huo.

Ni hivi, kundi muhimu kabisa la wapigakura katika uchaguzi mkuu wowote ule nchini Tanzania ni "Watanzania wasio na vyama." Kwamba, hakuna chama cha upinzani kinachohitaji kupoteza muda wake kuwashawishi wafuasi wa CCM wakipigia kura, kama ambavyo CCM haina muda na wafuasi wa upinzani kuwashawishi waipigie kura. Vilevile, si CCM wala vyama vya upinzani vinavyohitaji kuwashawishi wanachama/wafuasi wao wapigie kura vyama vyao. Watu wanaohitaji kushawishiwa ni hao wasio na vyama. Na habari njema ni kwamba kundi hilo ndilo lwenye idadi kubwa zaidi ya wapiga kura.

Kwa mujibu wa takwimu zisizo rasmi, CCM ina takriban wanachama milioni 8 ilhali wapinzani wana wanachama takriban milioni 5. Kwa makadirio, takriban Watanzania milioni 25 walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Kwahiyo, milioni 8 wa CCM jumlisha milioni 5 wa upinzani jumla inakuwa milioni 13. Ukichukua milioni 25 kutoa miloni 13 unabakiwa na milioni 12. Kwa makadirio, hawa ni "wapigakura wasio na vyama." Na kimahesabu, hata nusu tu ya kundi hili likielemea upande mmoja, upande huo unaweza kabisa kushinda uchaguzi husika. Of course, hapo tunaweka kando hujuma za kawaida za kuibeba CCM kwenye takriban kila uchaguzi mkuu.

Nimalizie kwa kukumbusha kuwa uchambuzi huu sio exact science. Umeelemea kwenye uelewa wa kutosha wa mchambuzi kuhusu siasa za Tanzania.

Kadhalika, uchambuzi huu ni endelevu. Utafanyiwa marejeo mara kwa mra kila kutakapokuwa na umuhimu wa kufanya hivyo


19 Oct 2018



Kwamba Daudi Albert Bashite ni mhusika mkuu katika utekelezaji wa mpango wa kijahili wa kutemka mfanyabashara maarufu Mohammed Dewji sio suala la siri. Na wala haihitaji uelewa mkubwa wa uchungui wa matukio ya kihalifu kubaini uhusika wa Bashite.

In fact, kabla ya Mo kutekwa, mfanyabiashara mwingine maarufu jijini Dar naye alinusurika kutekwa na vijana wa Bashite. Na majuzi, mfanyabiashara huyo amelazimika kumwaga shehena ya bidhaa baharini baada ya Bashite kutishia kumbambikia kesi kuhusu shehena hiyo.

Ni siri ya wazi kwamba Bashite amekuwa akiwanyanyasa wafanyabishara mbalimbali, akidai mamilioni ya shilingi, huku aktishia kuwabambikizia kesi za madawa ya kulevya iwapo watakataa. Huyo Mo mwenyewe “alishatolewa upepo” mara kadhaa na Bashite.

Kwa upande mwingine, Bashite amefika hapo alipo kwa kubebwa na watawala wetu. Baada ya kumpiga Mzee Warioba kwenye mchakato wa Katiba mpya, Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete akamzawadia Bashite ukuu wa wilaya. 

Na katika mazingira ya kushangaza, Rais Magufuli akaona Bashite hastahili kuwa mkuu wa wilaya bali apewe ukuu wa mkoa kabisa. Ninaweza kusema bila kuuma maneno kuwa huu ni mmoja wa maamuzi mabovu kabisa ya Rais Magufuli. Na huenda akatambua hilo huko mbeleni akiendelea kumkumbatia jahili huyo.
Baada ya kupewa ukuu wa mkoa, Bashite akatokea kuwa mtu wa karibu kabisa wa Magufuli. Hata alipovamia studio za Clouds Media Group, Mkuu huyo wa nchi akawamtetea vikali kijana huyo aliyetenda kosa la jinai. Hiyo ikampa Bashite jeuri na kiburi kikubwa.

Mara kadhaa, Magufuli alikuwa akimmwagia sifa Bashite akidai ndio Mkuu wa Mkoa mchapakazi kuliko wote. Mchapakazi kwa kufeli kisha kufojic heti na jina lake? Mchapakazi kwa kudai rushwa kwa wafanyabishara mbalimbali? Mchapakazi kwa yeye na “mlevi mbwa” Kitwanga kumpa yule mbwa Musiba shilingi milioni 7 za kututangaza akina sie kuwa ni watu hatari?

Kumdekeza Bashite na kumpendelea hata pale alipofanya uahlifu ndio kumemfanya haramia huyu kufikia hatua ya kufanikisha mpango wa kumteka Mo Dewji. Bashite ni kiumbe hatari kabisa na janga kubwa kuliko yote katika historia ya Tanzania. Na amin nawaambia, hata alindwe vipi na baba yake, mwisho wa jahili huyu utakuwa mbaya sana. 

Na sio kama ninamtetea Magufuli, ila hili la kumteka Mo, ni mpango binafsi wa Bashite alioufanya kwa niaba ya washirika wake kutoka nje ya nchi. 

Naamini hadi kufikia muda huu, watu wa Kitengo wameshamfahamisha Magufuli kuwa ‘mwanae’ Bashite ndio aliyemteka Mo, na anajua alipo. 

Na hapo ndio tunabaki kujiuliza: je Magufuli atakuwa tayari kuhatarisha urais wake na “kumbeba” tena Bashite? Tayari kuna dalili hizi maana mpaka wakati ninaandika makala hii, Bashite alikuwa hajakamatwa wala kuhojiwa, achilia mbali kutumbuliwa.
Magufuli anaachia fursa adimu ya kujitenga na kijana huyo mhuni ambaye amefanya jithada kubwa kuuharibu utawala wa “baba yake.” Kama kuna mtu mmoja amechangia sana kumfarakanisha Magufuli na Watanzania wengi si mwingine bali Bashite.

Kwa kumchukulia hatua Bashite, Magufuli angeuwa ndege wengi kwa jiwe moja. Kwanza, kumtimua Bashite kungemfanya aonekane kuwa sio tu amekerwa na kutekwa kwa Mo Dewji na bali pia “kujisafisha” yeye mwenyewe dhidi ya tuhuma kuwa huenda waliomteka Mo ni watu wa serikali yake Magufuli.

Lakini pia, kwa kumtumbua Bashite, Magufuli angejiweka kando na mtu ambaye amefanya kila linalowezekana kuchafua jina la “baba yake.” Kama nilivyotanabaisha awali, Bashite amechangia mno kuwafanya Watanzania wengi tu kutoipenda serikali ya Awamu ya Tano.

Pengine kubwa zaidi ya yote ni ukweli kwamba, kwa Magufuli kuchukua hatua dhidi ya Bashite itamsaidia kujenga mahusiano bora na wafanyabiashara wakubwa ambao wamekuwa wahanga wakubwa wa uonevu wa Bashite.

Lakini kubwa zaidi katika hili ni Magufuli kuepusha uwezekano wa wafanyabiashara hao kuungana na maadui wake (Magufuli) hususan ndani ya CCM ambako kuna makundi kadhaa yenye dhamira ya kumfanya awe Rais wa muhula mmoja kama sio kumng’oa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Ni vigumu kubashiri kwa hakika kuwa hatimaye Magufuli atamwaga Bashite lakini kilicho bayana ni kwamba ana option moja tu: amlinde ahatarishe uraia wake au ambwage ajitengenezee mazingira mazuri ya urais wake. Ifahamike mapema kuwa ikitokea Magufuli kamtumbua Bashite basi Tanzania italipuka kwa mayowe na vigelegele kana kwamba imeshinda Kombe la Dunia.

Mwisho, hatua za Magufuli dhidi ya Bashite ndio ufumbuzi pekee wa sakata la kutekwa kwa Mo. Yaani akikamatwa na kuhojiwa, ataeleza Mo yuko wapi, na hivyo kuwezesha kupatikana kwa mfanya biashara huyo tajiri si Tanzania tu bali pia ni mmoja wa matajiri wakubwa Afrika na duniani kwa ujumla. Ni matumaini yangu kuwa Magufuli atatambua kuwa akiendelea kumlea Bashite basi huenda “akaondoka nae.”


21 Apr 2018


Jana ilitolewa taarifa kwa vyombo vya habari  kuwa Rais John Magufuli amemteua "Msalika Robert Makungu kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora." Hata hivyo, kwa makusudi, taarifa haikueleza kabla ya uteuzi huo, Makungu alikuwa na wadhifa gani, japo ilieleza kuwa anakwenda mkoani Tabora kuchukua nafasi ya Dokta Thea Ntara ambaye amestaafu.



"Kilichofichwa" kwenye taarifa hiyo ni ukweli kwamba Makungu alikuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (DDGIS) ambaye aliteuliwa wakati mmoja na Mkurugenzi Mkuu wa Idara hiyo, Dokta Modestus Kipilimba, Agosti mwaka jana.

Japo taarifa husika haikutumia neno "kutumbuliwa," lakini haihitaji ufahamu wa mfumo wa utawala wa Idara ya Usalama wa Taifa kumaizi kwamba kutoka u-Naibu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo nyeti hadi u-Katibu Tawala wa Mkoa ni kushushwa cheo (demotion). 

Kwa mujibu wa vyanzo vyangu vya kuaminika ndani ya taasisi hiyo, kilichopelekea hatua hiyo inayoelezwa kuwa ngumu kwa  Magufuli ni tofauti kati ya watendaji hao wakuu wa taasisi hiyo, yaani Makungu na aliyekuwa bosi wake, yaani Kipilimba.

Inaelezwa kuwa tofauti kati yao ilikuwa kubwa kiasi cha Kipilimba kutishia kujiuzulu iwapo Magufuli asingechukua hatua dhidi ya Makungu.

Hata hivyo, Makungu alikuwa "mtu wa Magufuli" kwa sababu ni wote wanatoka Kanda ya Ziwa, na ni miongoni mwa "circle ya karibu ya Magufuli" ambayo pamoja na watu wengine, inayojumuisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Katibu Mkuu wa Hazina Dotto James, na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga.

Kwahiyo wakati  ingetarajiwa Magufuli "angemkumbatia poti wake Makungu" lakini kwa mujibu wa vyanzo vyangu, umuhimu wa Kipilimba kwa Magufuli ni mkubwa zaidi. 

Tukio hilo ambalo halikuvuta hisia za wengi hasa kwa vile lilitokea muda mfupi baada ya kupatikana taarifa za kifo cha mlimbwende maarufu Agnes Masogange aliyefariki jijini Dar jana.

Japo wadhifa wa "Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa" (DDGIS) sio wa muda mrefu tangu uanzishwe (Makungu alikuwa mtu wa pili kushika wadhifa huo baada ya Jack Zoka kuwa wa kwanza), kitendo tu cha Mkurugenzi katika taasisi hiyo kutolewa na kupelekwa mkoani ni cha kushangaza na kinaingia moja kwa moja kwenye kumbukumbu za kihistoria.

Hata hivyo, kabla ya Makungu "kutumbuliwa" tayari kuna Mkurugenzi mwingine ambaye aliondolewa kwenye wadhifa wake kama  nilivyoripoti kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana wakati huo, kuondoka kwa mwanamama huyo kulichangiwa na mtazamo wake wa kutaka mabadiliko ndani ya taasisi hiyo ambao ulikinzana na wahafidhina wasiotaka mabadiliko yoyote kwa taasisi hiyo.

Wakati hayo yanatokea, Zoka, aliyekuwa Balozi wa Tanzania huko Canada nae alitolewa katika wadhifa huo hivi karibuni. Nilieleza kwa kirefu kuhusu tukio hilo katika makala HII

Kama ambavyo Zoka aliandamwa na lawama kwamba alikuwa akiongoza mkakati wa kuhujumu vyama vya upinzani, Makungu pia ametoka katika nafasi hiyo akikabiliwa na lawama kama hizo.


Kwa upande wangu binafsi kama afisa wa zamani katika taasisi hiyo, wakati fulani nililazimika kumwandikia barua Makungu kutokana na taarifa flani zilzonikera. Na katika barua hiyo nilimkumbusha kuwa cheo ni dhamana, na hakina mwamana.


Tatizo kwa wenzetu wengi wanaposhika madaraka ni ile hali ya kujisahau wakidhani watafia wakiwa kwenye madaraka. Hupuuzia ukweli kuwa ipo siku watatoka katika nafasi zinazowapa jeuri na kujikuta "mtaani." Maisha hayatabiriki, leo unalala ukiwa DDGIS kesho unaamka ukiwa RAS.



Kuhusu iwapo hatua hiyo ya Magufuli kuwa na atahri zozote, kwa sasa ni mapema mno kubashiri. Baadhi ya maafisa waliopo kazini na wastaafu  wa Idara ya Usalama wa Taifa walidokeza kwamba taarifa hiyo ya kuondolewa kwa Makungu imewashtua wengi

 Kwa upande mwingine, wakati yote haya yanatokea, haijafahamika hali ikoje kwa "Idara ya Usalama wa Taifa nje ya Idara ya Usalama wa Taifa," yaani kile kikosi kilicho chini ya Daudi Alabert Bashite.



Kwamba Kipilimba ameweza kumn'goa "poti wa Magufuli" Makungu, basi huenda pia akawezesha kung'oka kwa Bashite, mtu anayeutia doa utawala wa Magufuli kwa kila hali.



Ni muhimu pia kujumuisha tweet ya mtu mmoja ambaye hujitambulisha kama Gavana wa zamani wa Benki Kuu, Daudi Balali.


Nimalizie makala hii kwa kukushauri uwe ukiitembelea blogu hii mara kwa mara upate fursa adimu ya kusoma uchambuzi exclusive kama huu wa leo.

27 Feb 2018




Nianze makala hii kwa kuwashukuru ndugu nyote mlionitumia salamu za upendo,kunipa pole/kunipa moyo baada ya jina langu kutajwa miongoni mwa watu 9 wanaodaiwa kuwa hatari kwa usalama wa Tanzania.

Orodha hiyo ilitajwa na mtu mmoja anayejiita Cyprian Musiba japo taarifa nilizonazo ni kwamba jina hilo lina walakini kama lilivyo jina la rafiki yake – na miongoni mwa watu waliofanikisha press conference yake – Daudi Albert Bashite. Waingereza wanasema "birds of a feather flock together."


Kichekesho ni kwamba mara ya kwanza kumfahamu mtu huyo ni wakati flani aliponitumia ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akinifahamisha kuwa wana gazeti lao linaitwa 'Tanzanite' na kuniomba niwe nawatumia makala. Nilipuuza ombi hilo kwa sababu kutoka level ya kuandikia gazeti kubwa kama Raia Mwema kwenda kuandikia kijigazeti kipya kama hicho cha Tanzanite ingekuwa kujishushia heshima yangu.

Kwa upande mmoja,tuhuma za huyo mtu hazijanishangaza kwa sababu kadhaa. Kwanza, tunafahamu fika ugumu wa maisha huko nyumbani, na sio suala la ajabu kuona baadhi ya watu wakiuza utu wao ili mradi tu "njia ya kwenda msalani isiote nyasi."

Lakini pili, kuna jitihada kubwa za kuigeuza Tanzania kuwa kama wilaya ya Kanda ya Ziwa. Huyo mtoa tuhuma ana asili ya maeneo hayo, na kuna hali inayozidi kuota mizizi kwa baadhi ya wahuni wanaotoka eneo moja na Magufuli kujiona wana hatimiliki ya Tanzania yetu.

Jingine ambalo lilinifanya nipuuze hizo tuhuma za huyo bwege ni ukweli kwamba safari yangu kimaisha hadi hapa nilipo imepshapitia vilima na mabonde. Nimeshaeleza mara kadhaa kuhusu janga lililonisibu Februari 2, 2013 ambapo chombo kimoja cha usalama hapa kilinifahamisha kuwa kuna tishio dhidi ya uhai wangu, tishio from Tanzania. Na kwa zaidi ya mwaka mzima tangu wakati huo, nikawa ninaishi maisha ya kutambua kuwa muda wowote ule naweza kudhurika. Licha ya ugumu mkubwa, hali hiyo ilinipa uzoefu wa kuishi na vitisho.

Lakini pia, hiyo hatua tu ya huyo mzembe kunituhumu naona kama tusi flani kwangu. Mie sio wa kutuhumiwa na mtu asiyejulikana kama yeye. Ilipaswa labda awe kigogo flani wa Usalama wa Taifa, ndo ningeweza kuchukulia suala hilo seriously. Wanasema "usiongee na mbwa bali ongea na mwenye mbwa."

Hata hivyo, japo sikushangazwa na tukio hilo la kihuni, nilikerwa na vitu vikuu vitatu. Kwanza, wakati nina uhakika wa asilimia 100 kuwa huyo bwege ametumwa tu, nilikerwa mno na uongo wa mchana kweupe uliokuwemo kwenye tuhuma zake. Uongo huo ni pamoja na kudai kuwa FBI ni shirika la ujasusi la Marekani. Hivi hao wapuuzi waliomtuma hawakufanya research japo kidogo ya kuwaelewesha kuwa shirika la ujasusi la Marekani ni CIA na sio FBI?

Halafu huyo bwege akachapia tena kwa kudai kuwa chama cha Kansela Angela Markel ni CDP ilhali chama chake ni CDU. Halafu sijui ni mie tu na "macho yangu ya kishushushu" niliyeona huyo jamaa akiongea kwa kuhema kana kwamba anakimbizwa, huku amejawa na uoga mkubwa. Hizi njaa zitakuwa watu mwaka huu. Seriously!

Kingine kilichonikera ni jinsi huyo bwege alivyopewa umuhimu mkubwa asiostahili. Hivi kwa mfano hiyo video ya press conference yake ingepuuzwa, nani angejua kuwa kuwa mwendawazimu flani kuitisha press conference kutuhumu watu kadhaa wenye heshima zao katika jamii? Kuna nyakati ukimya una nguvu zaidi ya kupigiana kelele na mtu. So far, huyo mhuni amefanikiwa kufikisha ujumbe wake kwa watu wengi mno kutokana na sie wenyewe – including tuliotuhumiwa -kumsaidia kusambaza ujumbe wake muflis. Anyway, by muda huu hizo 15 minutes of fame zimeshaisha muda wake.

Lakini pia nilikerwa na ukweli kwamba uhuni wa aina hii ukiachwa tu bila kuchuliwa hatua unaweza kusababisha madhara makubwa huko mbele. Maana tumeshaona jinsi Bashite alivyoweza kuvamia studio za Clouds kisha Rais Magufuli bila aibu akamtetea hadharani na kumsifia kuwa ni mchapakazi. Kwa kifupi, huko ni kusherehesha uhuni.

Sasa huyu bwege si mara ya kwanza kuibuka na press conference za kiendawazimu.Last time aliitisha press conference na kutishia kumfungulia mashtaka shujaa Tundu Lissu. Katika tukio hilo nilikerwa zaidi na ukweli kwamba kuna viumbe wenye roho mbaya kama wachawi, ambao hawajatosheka na mateso aliyepitia Lissu baada ya karibio la kutaka kumuuwa. Mie nimesoma"War Studies" na miongoni mwa kanuni za vita ni kwamba pindi adui yako akiwa chini basi unatarajiwa kutomdhuru. Kwahiyo hata kama Lissu ni adui yao, basi angalau wangesubiri apone kwanza kabla ya kuanza kumwandama namna hiyo

Kwa taarifa nilizonazo, press conference ya huyo bwege inamhusisha Bashite ambaye bila shaka ana baraka za baba yake, lakini pia watu wa Kitengo nao wamehusika. Ni vigumu kujua "kitengo kipi" maana kwa sasa ni kama tuna "Idara mbili" – hiyo tunayoifahamu na hiyo "kampuni binafsi ya ulinzi wa JPM/Bashite."


Lakini kubwa zaidi, na hasa ndio lengo la makala hii ni kuwafahamisha Watanzania wenzangu kwamba tafsiri halisi ya tuhuma zilizotolewa kwenye hiyo press conference ni kuwafanya ninyi Watanzania hamna akili ya kuweza kubaini nani hasa ni tishio kwa usalama wa taifa lenu.

Twende hatua kwa hatua japo kwa umbali mfupi tu.Hivi katika ya hao watu tisa ni yupi alishiriki kupanga na kutekeleza shambulio la kinyama dhidi ya Lissu? Kibaya zaidi, Lissu nae yumo katika orodha hiyo.

Je ni yui kati ya hao tisa alitoa ruhusa kwa askari kumpiga risasi na kumuuwa binti asiye na hatia Akwilina? Je ni nani kati yetu aliyehusika na mauaji wa Katibu wa Chadema Kata ya Hananasifu marehemu Daniel na Diwani wa Kata ya Namwawala Marehemu Luena? Maana kwa matukio haya matatu tu, na pengine la nne ni la Lissu, inatosha kuonyesha kuwa kuna pattern ya mauaji dhidi ya raia wasio na hatia. Na kwa vile hakuna jitihada zozote za vyombo vya dola kuwasaka wahusika na kuwatia nguvuni, yayumkinika kuhisi ushiriki wa serikali ya Magufuli katika matukio yote hayo.

Sasa yule bwege kuwaona ninyi Watanzania hamnazo, kwamba "anamudu kuwalisha matango pori" kwa kudai kuwa huyo na huyu ndiyo tishio kwa usalama wa nchi yetu, ilhali kila mwenye akili timamu anafahamu bayana kuwa tishio kubwa zaidi kwa sasa linatoka kwa WATU WASIOJULIKANA.

Image result for watu wasiojulikana

Je sie tisa tuliotajwa ndo tumegeuka kuwa "watu wasiojulikana" ambao sote wenye akili timamu twatambua ndio tishio kwa usalama wa Tanzania?

Ni rahisi kulitazama suala hilo kama ni uhuni wa huyo mbwa dhidi yetu lakini kiukweli mbwa huyo kawanyea Watanzania wote wenye akili timamu. Kawafanya hamna uwezo wa kutofautisha pumba na mchele. Huyu mtu ni adui yenu zaidi ya adui wa sie aliotutuhumu.

Sasa je hasira yako dhidi ya mtu huyu na waliomtuma unaionyeshaje? Mie ushauri wangu ni mwepesi tu: kama una uwezo wa kuwasomea dua mbaya, itakuwa vema. Kama una utaalamu wa masuala ya asili, basi ni vema pia. Hata ukitukana kimoyomoyo ni vema pia. Lakini ukipata wasaa wa "kumpa a uso" popote pale – iwe mtandaoni au mtaani – tafadhali fanya hivyo.

Naamini kabisa kati ya sie tisa tuliotajwa na huyo bwege, tuna watu walio tayari kutafuta haki kwa ajili yetu.Na haki si lazima ipatikane mahakamani. Na mahakama zenyewe hizi zinazoendeshwa kwa rimoti na Magufuli hadi kumfunga Sugu wala hazina maana. Ombi langu kwenu ni kila aina ya laana dhidi ya mtu huyo, si kwa sababu labda ana umuhimu flani bali ukweli huo niliyotanabaisha hapo juu kuwa amewaona ninyi Watanzania kama hamnazo hadi kufikia hatua ya kutuzushia sie tusio na hatia tuhuma hizo za kuhatarisha usalama ilhali sote tunafahamu vema akina nani wanaohatarisha usalama wa Tanzania yetu.

Kama ukinitumia picha wakati unamfanyia kisomo huyo mbwa basi itakuwa vema sana haha


10 Jan 2018

Image result for magufuli lowassa
Jana Januari 9, 2018, wiki moja na siku mbili baada ya kuanza kwa mwaka huu mpya, duru za siasa za Tanzania zilitikiswa na habari kuhusu kiongozi maarufu wa Chadema, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kukutana na Rais John Magufuli kwa “mazungumzo”, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Baada ya “mazungumzo” hayo Lowassa alimmwagia pongezi Magufuli kwa kile alichokiita “kazi nzuri anayoifanya” na kutaja mafanikio katika sera ya elimu bila malipo, ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge), na ujenzi wa viwanda na ujenzi wa reli ya “standard gauge”.

Nimepata faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana na Mheshimiwa Rais, tumezungumza nae na nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi nzuri na anahitaji kutiwa moyo,” alinukuliwa Lowassa aliyejiunga na Chadema miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 baada ya ndoto zake kuwania urais kwa tiketi ya CCM “kuota mbawa.”


Image result for magufuli lowassa

Mwanasiasa huyo ambaye baada ya kujiunga na Chadema alipitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa vyama vinne vya upinzani – Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD – uliofahamika kama UKAWA, aliendelea kusema kuwa “Moja kubwa ambalo ni la msingi sana ni la kujenga ajira, katika kuanza ujenzi wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hapo anajenga ajira, na kwenye nchi yoyote inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira, Stiegler’s Gorge ni kujenga ajira na mingine ya aina hiyo, lazima kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba tunajenga ajira. Jingine ni la elimu, ni muhimu sana, hauwezi kuacha elimu katika mambo yako unayofanya, hili nalo lazima lisemwe vya kutosha, kwa kweli nakushukuru Mheshimiwa Rais, you made my day.

Rais Magufuli kwa upande wake alimpongeza Lowassa kwa kile alichokiita “kutambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali” na kumtaja Lowassa kama mmoja wa viongozi ambaye kwa wakati wake alitoa mchango wake katika nchi.

Magufuli alimmwagia sifa Lowassa akidai kuwa “ni mwanasiasa mzuri kwani hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita ambao naye aligombea kiti cha Urais, hakuwahi kumtukana.”

Mheshimiwa Lowassa ameniomba mara nyingi nikutane nae, na leo nimekutana nae, tumezungumza mambo mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwambia ya kwangu. Kwa ujumla Mheshimiwa Lowassa ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani walifanya mambo mazuri, na mimi napenda kumpongeza Mhe. Lowassa ambaye kama alivyosema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi,” alisema Rais Magufuli

Ametaja miradi mbalimbali tunayotekeleza, ametaja mradi wa Stiegler’s Gorge utakaogharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 7, amezungumzia juu ya elimu bure, amezungumzia juu ya maji ambayo kwa bahati nzuri yeye alikuwa Waziri wa Maji na anafahamu sasa tumefikia wapi, amezungumza juu ya umeme tulivyosambaza katika vijiji mbalimbali, elimu bure, huduma za hospitali na mengine” aliongeza Rais Magufuli.

Kwanza, ni muhimu kutambua kuwa kama Mtanzania yeyote yule, Lowassa alikuwa na kila haki ya kukutana na Rais wake. Kadhalika, kama mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani, isingepaswa kuwa jambo la kushangaza kwa viongozi hao wawili kukutana.

Hata hivyo, Lowassa sio tu amekutana na Magufuli, bali pia ammemwamgia sifa. Je ni dhambi kwa kiongozi wa chama cha upinzani kumwagia sifa Rais aliyepo madarakani? Jibu lingepaswa kuwa “si dhambi,” laiti uhusiano kati ya Rais Magufuli, serikali yake na taasisi zake (kama vile jeshi la polisi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa), watendaji wa serikali (hasa mawaziri na manaibu wao, na wakuu wa mikoa na wilaya), pamoja na chama cha Magufuli yaani CCM, na chama anachotoka Lowassa, yaani Chadema, na Upinzani kwa ujumla, ungekuwa mzuri.

Lakini ukweli ni kwamba japo tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, uhusiano kati ya CCM, serikali zake na taasisi zake, na vyama vya upinzani umekuwa “wa kusuasua,” hali katika miaka miwili tu ya utawala wa Magufuli imekuwa mbaya zaidi hususan kutokana na ukweli kwamba hakuna jitihada za kuficha chuki iliyopo dhidi ya Upinzani.

Kama kiongozi wa ngazi za juu kabisa wa Chadema, na pengine mwanasiasa anayeheshimiwa zaidi ya kiongozi mwingine yoyote ndani ya chama hicho, ni wazi Lowassa anafahamu vema msimamo na mtazamo wa chama chake kuhusu Magufuli na utendaji kazi wake, na serikali yake, na chama chake.

Pengine kwa kuweka picha sawia, inaelezwa kwamba hadi wakati huu, zaidi ya wana-Chadema 400 ikiwa ni pamoja na viongozi na wanachama, aidha wapo jela au wana kesi zinazoendelea mahakamani ambazo takriban zote ni matokeo ya chuki za kisiasa zinazofanywa na Magufuli, serikali yake na chama chake.

Kadhalika, katika utawala wa Magufuli, vyama vya upinzani ikiwemo Chadema ambayo Lowassa ni kiongozi wake wa kitaifa vimepigwa marufuku kufanya shughuli zao za kisiasa ikiwa ni pamoja na mikutano na maandamano. Hayo yanatokea wakati CCM ikiwa huru kufanya mikutano na maandamano itakavyo, mara nyingi ikitumia raslimali za umma.

Sambamba na jitihada za Magufuli kubana fursa ya siasa (political space), utawala wa kiongozi huyo umekuwa mstari wa mbele kuvibana vyombo vya habari na kudhibiti uhuru na haki ya wananchi kutoa mawazo yao kama Katiba inavyowaruhusu.

Lakini jingine ambalo Chadema ni mhanga mkubwa, kada maarufu wa chama hicho Ben Saanane “alipotea” Novemba mwaka jana na hadi leo hajapatikana.

Na ni wakati ninaandika makala hii nimebaini kuwa Lowassa hajawahi kuongelea suala la kada huyo (naomba nikosolewe kama nimekosea).
Kubwa zaidi linaloweza kuhalalisha hasira za Chadema kwa utawala wa Magufuli ni tukio la hivi karibuni ambapo Mbunge wake maarufu, ambaye pia alikuwa mpinzani maarufu dhidi ya Magufuli, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kunusurika kuuawa baada ya shambulio la risasi kadhaa huko Dodoma. Kwa sasa Lissu yupo nchini Ubelgiji kwa matibabu, lakini japo Lowassa alimtembelea alipokuwa hospitalini Nairobi, Magufuli hakuwahi kutia mguu kumjulia hali mwanasiasa huyo ambaye pia ni mnadhimu mkuu wa upinzani bungeni na Rais wa Tanganyika Law Society (TLS).

Kwahiyo japo pongezi za Lowassa kwa Magufuli zinaweza kuwa na uzito, mapungufu ya utawala wa rais huyo wa awamu ya tano, hususan kuhusiana na chuki na uonevu dhidi ya vyama vya upinzani, hususan Chadema, yalipaswa “kumzuwia” kada huyo wa zamani wa CCM kumwaga pongezi hizo.

Kibaya zaidi, imebainika kuwa Lowassa alishawahi kumwomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amsaidie kukutana na Magufuli. Hata hivyo, Gambo alipotamka hilo hadharani, Lowassa “aliruka kimanga.”


Hata hivyo, jana Magufuli alitamka bayana kuwa Lowassa aliomba mara kadhaa kukutana naye. Kwahiyo, alichosema Gambo kilikuwa kweli, na Lowassa hakuwa mkweli alipokana kuwa hajaomba kukutana na Magufuli.

Tukio hilo la Lowassa kukutana na Magufuli na kumwagia pongezi limepokelewa kwa hisia tofauti. Wakati kuna kundi dogo la wana-Chadema waliopongeza hatua hiyo, kwa mfano “kada” mmoja wa chama hicho Yericko Nyerere, wengi ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wamepingana waziwazi na Lowassa.

Wakati Yericko aliandika haya


Mbunge maarufu wa Chadema, Godbless Lema alikuwa wa kwanza kueleza bayana kutoafikiana na pongezi za Lowassa kwa Magufuli.


Baadaye, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, naye alieleza kuwa kauli za Lowassa ni zake binafsi na sio msimamo wa chama hicho.

Kadhalika, Mbowe alionekana kumkumbusha Lowassa kuhusu matukio mbalimbali yasiyopendeza katika utawala wa Magufuli

Lakini pengine aliyeeleza kwa kirefu kuhusu suala hilo ni Lissu, ambaye akiwa hospitalini huko Ubelgiji, alitoa waraka huu hapa chini.



Waheshimiwa habari za Tanzania na poleni kwa yote.
Naomba na mimi niseme kwa uchache kuhusu suala hili. Samahani kama 'uchache' wangu utakuwa mrefu kidogo.
Baada ya Mwenyekiti kuzungumzia jambo hili, inaelekea kuwa wazi kwamba Mheshimiwa Lowassa hakumshirikisha Mwenyekiti kabla ya kukubali au kuamua kwenda Ikulu kukutana na Rais Magufuli.
Na juzi tu wakubwa wetu hawa wawili walikuwa pamoja hospitalini kumsalimia Mzee Ngombale Mwiru.
Je, inawezekana Mheshimiwa Lowassa hakuwa anajua tayari kwamba ana appointment Ikulu?
Kama alikuwa anajua, kutokumshirikisha Mwenyekiti wake kuna tafsiri gani hasa?
Katika mazingira ya sasa ya Tanzania ya Magufuli, uamuzi wowote wa kufanya nae mazungumzo, hata kwa nia njema yoyote ile, bila kushauriana au kuwashirikisha viongozi wa juu wa chama, ni uamuzi usio sahihi na mgumu kukubalika.
Vile vile, kauli za aina ambayo tumeisikia leo kutoka kwa Mheshimiwa Lowassa, zina athari kubwa kisiasa.
Sio tu zinachanganya wanachama na wafuasi wetu, lakini pia zinawapa mtaji wa kisiasa maadui zetu.
Kuanzia sasa tutegemee sana kuwasikia maCCM yakishangilia 'busara' za Mheshimiwa Lowassa.
Masuala ya ukiukwaji haki za binadamu, uvunjwaji wa Katiba na mengine mengi sasa yatajibiwa kwa namna moja: Lowassa amemkubali Magufuli nyie wengine mnapiga kelele za nini.
Huu ni mtaji wa bure kwa Magufuli. Ukweli, ambao umesemwa sana humu, ni kwamba amefeli karibu katika kila jambo.
Hata hiyo reli anayosifiwa nayo na Lowassa bado ni ndoto tu: nani ajuaye itajengwa kwa hela za nani???
Za Wachina kama tulivyoambiwa mwanzoni; au za Waturuki kama tulivyoambiwa baadae; au za Afrika Kusini kama alivyosema mwenyewe anaenda kumwomba Zuma???
Kama chama hatujawahi kukataa mazungumzo na Rais au kiongozi mwingine yeyote wa serikali.
Na hatukatai kuzungumza na Magufuli kuhusu matatizo mengi na makubwa yanayoikabili nchi yetu.
Lakini ni muhimu na lazima viongozi wakuu wa chama washirikishane na washauriane kabla ya mazungumzo hayo.
Na baada ya mazungumzo, ni lazima viongozi wakubaliane juu ya kauli za kutoa hadharani kwa umma ili wote tuwe kwenye ukurasa mmoja.
Katika mazingira ya sasa, ambako viongozi na wanachama wetu wanashambuliwa hadharani kwa mapanga na hata kwa risasi, kumsifia Rais ni kumuunga mkono yeye na matendo yake.
Katika mazingira ya kesi nyingi za kutunga dhidi yetu, 'kazi nzuri' inayofanywa na Magufuli ina maana gani hasa, kama sio kuhalalisha ukandamizaji tunaofanyiwa.
Katika mazingira ambapo hata jumuiya ya kimataifa imeanza kuhoji mwenendo wa Rais Magufuli, kutoa kauli kwamba 'anafanya kazi nzuri' ni 'kumtupia taulo' la propaganda litakalomfichia madhambi mengi aliyowafanyia Watanzania katika miaka hii miwili.
Kwa vyovyote vile, kitendo cha Mheshimiwa Lowassa sio cha kunyamaziwa au kuhalalishwa kwa hoja nyepesi nyepesi.
TUNDU LISSU(MB).
Top of Form

Kadhalika, kada maarufu wa kike wa chama hicho, Hilda Newton nae alieleza masikitiko yake kutokana na kauli za Lowassa.



Kama alivyotahadharisha Lissu, ni wazi kwamba CCM watakuwa wamepewa “silaha” mpya katika “kumpamba” Magufuli na “kuwapenda” wapinzani, kwamba “hata Lowassa wenu anamkubali Magufuli.” Na ni rahisi kwa CCM kuonekana wana mantiki katika hoja hiyo, kwa kudai “kama mtu muhimu kabisa kwenye chama chenu (yaani Lowassa) ambaye ndiye aliyekuwa mpinzani mkuu wa Magufuli kwenye uchaguzi mkuu uliopita, anamkubali mkuu huyo wa nchi, ninyi ni akina nani kumpinga?”

Wakati ni wazi kwamba uamuzi wa Lowassa kukutana na Magufuli, na kumwagia pongezi, umezua “sintofahamu” huko Chadema, kuna masuala kadhaa ya muhimu yanayopaswa kuangaliwa kwa makini kwa ajili ya mustakabali wa chama hicho.

Kwanza, ni muhimu kwa viongozi na wanachama wa Chadema kutambua nafasi ya Lowassa katika chama hicho. Wakati baadhi ya wachambuzi wa siasa – mie nikiwa mmoja wao – wanaamini kuwa ujio wa Lowassa katika chama hicho ulikuwa na hasara zaidi kuliko faida, jitihada zilizofanywa na chama hicho kumpigania mwanasiasa huyo zimemjengea hadhi ambayo haipo kwa mwanasiasa mwingine yoyote ndani na nje ya chama hicho.

Ikumbukwe kuwa hadi wakati jina lake lilipokatwa na vikao vya CCM katika mchakato wa kusaka mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho tawala, Lowassa alikuwa ndiye mwanasiasa maarufu kuliko wote Tanzania. Yayumkinika kusema alikuwa mtu wa pili kwa umaarufu baada ya marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Licha ya kulazimika kujiuzulu Uwaziri Mkuu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya Richmond, Lowassa aliendelea kuwa mwanasiasa maarufu na mwenye nguvu kuliko yeyote yule ndani ya CCM, hata zaidi ya Rais na mwenyekiti wa taifa wa chama hicho wakati huo, Jakaya Kikwete.

Na japo kukatwa kwa jina la Lowassa huko CCM kulimpunguzia kidogo umaarufu wake kwa siasa za Tanzania – ilikuwa kama miujiza kuona CCM ilikuwa na ujasiri wa kukata jina la mwanasiasa huyo- alihamia Chadema akiwa na sapoti ya kutosha kiasi japo si kubwa kama ilivyotarajiwa.

Japo kuna “tuliopishana nae mlangoni” – kwa maana yeye alipoingia, sie tukatoka – ujio wake ulipelekea kuwa mwanasiasa maarufu zaidi ya wote wa Upinzani. Na ndio maana haikuwa vigumu kwake kupitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA.

Nimeeleza kuwa baadhi yetu “tulipishana nae mlangoni” kwa sababu mie binafsi nilikuwa naiunga mkono Chadema, si kama mwanachama bali ukweli kwamba kwa muda mrefu nimekuwa nikijihusisha na harakati za mapambano dhidi ya ufisadi, na chama hicho kilijitokeza kuwa championi wa mapambano hayo. Kwahiyo, “naturally” nilijikuita nikikiunga mkono.

Hata hivyo, ujio wa Lowassa katika chama hicho ulinikimbiza. Sababu kuu ni binafsi zaidi, na nisingependa kuongelea hapa, lakini sababu nyingine ni kile nilichotafsiri kama usaliti wa Chadema. Ikumbukwe kuwa tangu mwaka 2006, chama hicho “kilimkalia kooni” Lowassa kumtuhumu kuwa ni fisadi, na ndicho kilichofanya jitihada kubwa zilizopelekea mwanasiasa huyo kujiuzulu Uwaziri Mkuu mwaka 2008.

Sasa bila hata kutumia jitihada kidogo tu za busara, chama kilichomwandama Lowassa kuwa ni fisadi, kwa miaka 9 mfululizo, yaani 2006 hadi 2015, kilionekana kituko kwa baadhi yetu tuliokuwa tukikiamini, kwa sababu, pamoja na mengine, isingewezekana kutumia miezi mitatu (Julai 2015 Lowassa alipojiunga na chama hicho hadi Oktoba wakati wa uchaguzi mkuu) kumsafisha vya kutosha.

Na gharama ya ujio wa Lowassa ilikuwa kubwa. Moja kubwa zaidi ilikuwa lazima kwa Chadema “kuitosa” turufu yake muhimu, ajenda ya vita dhidi ya ufisadi. Ililazimika kufanya hivyo kwa sababu kuzungumzia ufisadi ilhali chama hicho kimemkumbatia mwanasiasa kiliyemwita “baba wa ufisadi” kwa miaka 9 mfululizo ingeonekana kioja.

Kadhalika, kwa kumpokea Lowassa, Chadema ilikuwa haina jinsi ya kukwepa tuhuma kutoka CCM kuwa chama hicho upinzani ni cha kifisadi kwa sababu ya kumkumbatia mwanasiasa ambaye kilikuwa kikimuita fisadi. Jitihada za Chadema kujibu mashambulizi kuwa “kama Lowassa ni fisadi mbona hajachukuliwa hatua,” zilikuwa hazina mashiko.

Lakini jingine lililoipa jeuri CCM ni ukweli kwamba kwa chama hicho, Lowassa alikuwa ni “makapi” sambamba na wanasiasa wengine waliomfuata huko Chadema. Hiyo ilikipa chama hicho tawala “jeuri” ya namna flani. Na waliitumia vema kwenye kampeni, kwamba “hawa jamaa si lolote si chochote. Yani wameshindwa hata kutafuta mgombea wao wenyewe mpaka wakasubiri makapi kutoka kwetu ndo wakapata mgombea urais.” Na pamoja na maneno hayo kuwa machungu, ndo ukweli ulivyokuwa.

Chadema na UKAWA kwa ujumla walikuwa na takriban mwaka mzima wa kujipanga; kuafikiana kuhusu mgombea urais kwa tiketi ya umoja huo, na kumnadi, huku wakitumia “advantage” ya “vita vya wenyewe kwa wenyewe” kati ya zaidi ya makada 40 waliokuwa wakichuana kuteuliwa na CCM.

Badala yake, kumbe tayari kulikuwa na makubaliano ya siri kati ya uongozi wa baadhi ya viongozi wa juu wa Chadema kwamba wasubiri kutangaza mgombea wao hadi baada ya mchakato wa CCM kupata mgombea wake, ka maana ya “kumhifadhia nafasi Lowassa endapo jina lake litakatwa huko CCM.”

Kabla ya kwenda mbali na makala hii ningependa nishauri Chadema irejee suala hilo la Lowassa kuandaliwa nafasi ya kuwania urais japo wakati huo alikuwa CCM. Hatua stahili zinapaswa kuchuliwa dhidi ya wote waliohusika na mpango huo.

Na ujio wa Lowassa ulipelekea Chadema kumpelekea mmoja wa magwiji wa siasa za upinzani, Dokta Willbrord Slaa. Umahiri wa Dokta Slaa haukuwa tu katika kuchukia ufisadi kwa dhati bali umahiri wake mkubwa katika kujenga hoja kisomi. Kadhalika, alikuwa akiaminiwa na watu mbalimbali muhimu ndani ya serikali, kiasi kwamba baadhi yao walihatarisha ajira zao kwa kumpatia mwanasiasa huyo nyaraka muhimu zilizoiwezesha Chadema kuwa na ushahidi mbalimbali katika vita yake dhidi ya ufisadi.

Na kuonyesha kuwa alikuwa na msimamo imara, Dokta Slaa aliamua kujiweka kando katika uongozi kupinga Lowassa kupewa ugombea urais wa UKAWA. Lakini jambo la kusikitisha mno, kiongozi huyo aliyekifanyia mengi chama hicho alidhalilishwa na kutukanwa kupita kiasi.
Na “akina sie” tulishindwa kustahimili ujio wa Lowassa, na kwa vile kwa baadhi yetu ilikuwa muhimu kumzuwia asiingie Ikulu, na hivyo kulazimika kumpigia kampeni mpinzani wake yaani Magufuli, tulitukanwa kila aina ya matusi. Sijui watu hawa waliojitoa ufahamu wataweka wapi sura zao pindi Lowassa “akirejea nyumbani” CCM.

Wakati anajiweka kando na uongozi wa Chadema, Dokta Slaa alikitahadharisha chama hicho kuwa ili kuleta mabadiliko ya kweli (badala ya hayo “ya kisanii” aliyokuwa akiyanadi Lowassa) chama hicho kinahitaji mkakati makini utakaoongozwa na watu makini. Na kwa hakika, tangu wakati huo, Chadema imekuwa kama kundi la wanaharakati wa kudandia hoja kuliko chama cha siasa chenye ajenda ya kueleweka. Uamuzi wa kuitelekeza ajenda ya vita dhidi ya ufisadi ulipelekea chama hicho kutokuwa na ajenda moja ya maana, huku CCM “wakipora” kiurahisi ajenda ya vita dhidi ya ufisadi.

Je mustakabali wa Chadema ukoje? Japo sio rahisi sana kubashiri kwa uhakika kuhusu hatma ya chama hicho, binafsi – kwa kutumia uzoefu wangu na uelewa wa kutosha wa siasa za Tanzania, sambamba na kuwa na fursa ya kufahamu “yanayojiri nyuma ya pazia” la siasa za nchi yetu – ninadhani kuwa kuna uwezekano mkubwa tu kwa Lowassa kurudi CCM kama sio kuachana kabisa na siasa.

Kwanini Lowassa anaweza kurudi CCM? Kuna sababu kuu mbili. Moja ni dalili za wazi kuwa ndoto zake za urais kupitia chama hicho ni kama zimeyeyuka. Umaarufu wake umegubikwa na kuibuka na kuimarika kwa umaarufu wa Lissu. Ni dhahiri kwamba ikipigwa kura ya maoni kuwa nani kati ya Lowassa na Lissu awe mgombea urais kwa tiketi ya Chadema mwaka 2020, Lissu ataibuka mshindi. Na Lowassa anafahamu kuwa hakuna njia ya mkato kwa yeye “kulazimisha” awe mgombea katika uchaguzi mkuu huo ujao, licha ya ukweli kwamba alishatangaza kuwa atagombea.

Sababu nyingine ni binafsi zaidi. Lowassa ni mmoja wa matajiri wakubwa nchini Tanzania. Kama utajiri huo ulipatikana kihalali au kifisadi, si lengo la makala hii kujiingiza katika mjadala huo. Lililo wazi ni ukweli kwamba licha ya kuwa mwanasiasa, yeye pia ni mfanyabiashara. Na kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, serikali ya Magufuli imefanikiwa kutumia nyenzo yake muhimu dhidi ya wapinzani ambao pia ni wafanyabiashara, KODI.

Inaelezwa pia kwamba mali mbalimbali za mwanasiasa huyo zipo hatarini kutokana na uwepo wake huko Upinzani. Inadaiwa kuwa hata jengo la Tanesco Ubungo ambalo serikali imetangaza kulivunja, linamilikiwa na Lowassa, na tishio la kulivunja lilikuwa kama kufikisha ujumbe kwake.

Katika hili, Lowassa hatoonekana mtu wa ajabu akiamua kurudi CCM ili asibughudhiwe kuhusu biashara na mali zake. Ni nani kati yetu anayeweza kujitoa mhanga kwa ajili tu ya imani yake ya siasa? Si kama hawapo ila ni adimu mnooo! Na kibaya zaidi, hata akiamua kung’ang’ania huko Chadema, hatma yake na ya chama hicho haieleweki kwa sababu hadi muda huu – na hii ni licha ya zuwio la Magufuli dhidi ya vyama vya upinzani kufanya shughuli zao za siasa – chama hicho kikuu cha upinzani “kipo kipo” tu. Hakina ajenda moja ya kueleweka zaidi ya kudandia kila tukio linalojiri.

Iwapo Lowassa ataamua kubaki Chadema, hiyo itakuwa fursa mwafaka kwa chama hicho kumpumzisha. Naamini kuwa wana-Chadema wakiweka kando ushabiki wa kisiasa, wanafahamu fika kuwa mwanasiasa huyo hana nguvu, uwezo wala mvuto wa kukabiliana na siasa hatari zinazoendelea muda huu huko nyumbani.

Kwa upande mwingine, tukio la Lowassa kukutana na Magufuli Ikulu linaweza pia kuhusishwa na tamko la hivi karibuni la Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, ambaye kama Lowassa, alimmwagia sifa Magufuli.

Nimefanya uchambuzi kuhusu kauli za wanasiasa hao wawili hapa, lakini ninachoweza kugusia hapa ni haja ya kutambua kuwa wanasiasa hao bado wanatunzwa na serikali kutokana na nyadhifa walizowahi kushika huko nyuma. Haihitaji uelewa mkubwa kuhusu "siasa za kibabe" kuhisi kwamba huenda "malezi" wanayopewa na serikali yametumika kama "chambo" cha kuwavuta karibu na Magufuli.

Kuhusu matatizo yanayoikabili Chadema muda huu,ukweli ni kwamba ni zaidi ya uwepo wa Lowassa ndani ya chama hicho. Japo huu ni ukweli mchungu usioruhusiwa kabisa kusikika ndani ya chama hicho, licha ya kazi nzuri ya kuifikisha Chadema ilipo leo, mwenyekiti wa taifa Mbowe anapaswa kutoa fursa kwa wana-Chadema wengine kusukuma gurudumu la chama hicho. Na hatua hiyo wala haihusiani na mchango wake mkubwa wa kumleta Lowassa ndani ya chama hicho na “kumpa” ugombea urais wa UKAWA.

Kirefu cha Chadema ni Chama cha DEMOKRASIA na Maendeleo. Sasa ni demokrasia gani hiyo ambayo inaruhusu mwenyekiti mmoja kuwa madarakani milele? What if “uenyekiti wa milele” ni miongoni mwa vikwazo kwa maendeleo ya chama hicho?

Lakini hata kama “muda wa Mbowe kutoka madarakani haujafika,” busara tu inapaswa kumfahamisha kiongozi huyo kuwa ni vema kuzingatia busara za akina Nyerere waliojing’atua wakiwa bado wanahitajika. Sipendi kubashiri hili, lakini laiti Mbowe asipohamasisha mageuzi kwenye medani ya uongozi wa chama hicho, haitokuwa jambo la ajabu akiishia kung’olewa kwa nguvu.

Na kwa bahati mbaya kwake, hili “songombingo” alilolianzisha Lowassa jana linaweza kuwa kama mnyororo mrefu ambao mahala flani yupo Mbowe. Ndiye aliyemkaribisha Lowassa.

Moja ya mapungufu makubwa mno yanayoitafuna Chadema muda huu ni pamoja na kulipuuza kundi muhimu linalokisaidia mno chama hicho, lundo la vijana wanaoshinda na kukesha katika mitandao ya kijamii wakijaribu kukinadi chama hicho angalau kwa kuikemea serikali ya Magufuli au CCM kwa ujumla.

Laiti chama hicho kingekuwa na ajenda ya kueleweka, basi jeshi hili la vijana lingekuwa nyenzo muhimu mno. Ni rahisi kuwalaumu vijana hawa kuwa “kazi yao kubwa ni kudandia hoja tu,” lakini ukweli ni kwamba chama chao hakiwapatii ajenda ya/za kueleweka. Kibaya zaidi, hata pale wanapojaribu kutengeneza ajenda wao wenyewe – kwa mfano jitihada za kumsaka Ben Saanane – hawapati sapoti ya kutosha kutoka uongozi wa juu wa chama hicho.

Ni hivi, wengi wa hawa vijana wanahatarisha maisha yao kwa kuwa tu “upande usiotakiwa” na serikali ya Magufuli. Hawategemei malipo yoyote zaidi ya kuamini kuwa siku moja wanaweza kukiingiza chama chao madarakani. Hakuna jitihada za makusudi za uongozi wa juu wa chama hicho kuwa karibu na kundi hili muhimu.

Ukiwa UVCCM una uhakika wa angalau “kuhongwa na Bashite” au kualikwa kwenye “mnuso” sehemu flani. Lakini ukiwa kijana wa upinzani, “zawadi” kubwa yaweza kuwa kusumbuliwa na vyombo vya dola na kuishi maisha ya wasiwasi. Kwahiyo vijana wa upinzani wana kila sababu ya kuichukia siasa, kwa sababu inahatarisha maisha yao, lakini mapenzi yao katika imani ya chama inawalazimisha kung’ang’ania hivyo hivyo.

Niionye Chadema kuwa katika zama hizi za “ununuzi wa binadamu kama zama za utumwa,” chama hicho kisishangae pindi wengi wa vijana hawa watakapoamua kubwaga manyanga na kukubali “kununuliwa.” Kwanini waendelee kuhatarisha maisha yao ilhali uongozi wa juu wa chama hicho hauna muda nao?

Akina Hilda Newton, Ben Malisa, Bob Wangwe, Ndehani Mwenda, Noel Shao, Gift Nanyaro ni miongoni mwa vijana wanaofanya kazi kubwa kwa ajili ya Chadema, bila ya matarajio ya malipo au fadhila flani, zaidi ya kuhatarisha maisha yao. Kama ilivyo kawaida ya mwanadamu yeyote yule, inaweza kufika mahala mtu akarudi nyuma na kujiuliza, “is it worth it?” Na japo sitarajii kuona makada hao vijana wakiamua kuipa kisogo Chadema, lakini sintoshangaa baadhi yao wakiamua kuipa kisogo siasa, hasa kama tasnia hiyo itaendelea kuwa “yenye manufaa kwa genge flani tu.”

Nihitimishe makala hii kwa kukuhamasisha msomaji kujipatia nakala yako ya kitabu changu kipya cha kielektroniki kinachochambua kwa kina miaka miwili ya utawala wa Magufuli. 




Baadhi ya niliyaoyazungumzia kwenye makala hii yamezungumwa kwa kirefu katika kitabu hicho ambacho hakielemei upande wowote. Kitabu hicho kwa sasa kinasubiri uzinduzi rasmi utakaokiwezesha kununulika kwa “mobile money” kama m-pesa, tigopesa,nk. Nitawataarifu. Ila kwa wasiohitaji kusubiri, waweza kukinunua HAPA

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.