Showing posts with label ZITTO KABWE. Show all posts
Showing posts with label ZITTO KABWE. Show all posts

5 Dec 2014

Waingereza wana msemo ambao unatafsirika kwa Kiswahili kama "chuki ya pamoja ni mwanzo wa urafiki mkubwa." Kimahesabu kama A hapatani na B, na A anamchukia C kama ambavyo B anamchukia pia C, basi chuki ya A na B kwa C yaweza kuwa mwanzo wa wawili hao A na B kuwa marafiki wenye lengo la kumwangamiza C.

Binafsi, naomba kukiri kuwa kwa muda sasa nimekuwa siafikiani na mitizamo na mwenendo wa mwanasiasa mahiri wa upinzani, Zitto Kabwe. Siwezi kusema nina chuki dhidi yake bali mie sio miongoni mwa supporters wake.Pamoja na sababu nyingine, kubwa ni kile ninachokitafsiri kama mwanasiasa huyo kutanguliza mbele maslahi yake binafsi badala ya chama chake yaani Chadema. Kwa mtizamo wangu, mgogoro uliopelekea hatua ya Chadema kumvua madaraka Zitto ni matokeo ya 'imani potofu' kuwa kuna mwanasiasa anayeweza kuwa maarufu kuliko chama chake, Si kwamba haiwezekani kabisa kwa hilo kutokea lakini si kwa hatua waliyofikia Chadema hivi sasa.

Lakini lengo la makala hii si kumjadili Zitto wala ugomvi kati yake na Chadema. Ila nimegusia suala hilo kwa sababu nililazimika 'kurejesha urafiki' na mwanasiasa huyo, angalau kinadharia, wakati akifanya jitihada kubwa binafsi na kama mwenyekiti wa PAC kushughulikia ufisadi wa Tegeta Escrow. Kwa kutumia mfano huo hapo juu wa chuki za A kwa C na za B kwa C, na A ni Zitto, na B ni mie, huko C wakiwa mafisadi wa Escrow, basi 'urafiki' usingeepukika.

Hakuna Mtanzania atakayeshindwa kumpongeza Zitto na Kafulila pamoja na PAC kwa ujumla walivyofanya kazi kubwa na nzuri katika kushughulikia skandali hiyo. Nina imani hata wahusika wa ufisadi huo wa Escrow wanamkubali kwa jinsi alivyowakalia kooni...ALMOST.

Hata hivyo, mara baada ya kumalizika kwa 'timbwili' hilo la Escrow bungeni, nilitumiwa meseji na 'mjuzi mmoja wa mambo ya huko nyumbani' ambaye alidai kuwa pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na PAC, kuna 'mchezo mchafu' uliofanyika katika kufikia mwafaka miongoni mwa wajumbe, hususan wale wa kutoka CCM. Alidai kuwa kilichowezesha mwafaka huo kufikiwa ni pamoja na 'kumnusuru' Rais Jakaya Kikwete, ambaye kama Mbunge Tundu Lissu alivyobainisha bungeni, anatajwa kuhusika katika skandali hiyo. Kimsingi, hoja ya Lissu, ambaye pia aliilaumu Idara ya Usalama wa Taifa kwa kutowajibika ipasavyo katika mlolongo wa skandali mbalimbali zinazougubika utawala wa Rais Kikwet, iliuawa kimyakimya licha ya umuhimu wake mkubwa.

Hata hivyo, kwa uelewa wangu, jaribio lolote la kumhusisha Rais Kikwete na skandali hiyo hata kama ushahidi upo lingepelekea mparaganyiko mkubwa katika kamati hiyo ya Zitto. Na kama tulivyoshuhudia 'makada' wa CCM huko bungeni walivyopigana kufa na kupona hadi Waziri Mkuu Mizengo Pinda akanusuriwa, kwa hakika ishu ya Kikwete kuhusishwa na Escrow ingepelekea bunge hilo kuvunjika pasi kufikia hitimisho.

Lakini what if mkakati huo wa 'kumnusuru Rais Kikwete' unabeba mengi zaidi ya tunavyodhani? 


Kwa kifupi, tume-settle for less. Na Waingereza wana msemo unaotahadharisha kuhusu ku-settle for less, ambapo wanasema 'pindi ukikubali kupokea pungufu ya unachostahilki basi hatimaye utaishia kupokea pungufu zaidi ya kile ulichostahili awali.' Japo ni mapema kuhitimisha kwamba 'tumeingizwa mkenge,' lakini ukimya wa Rais Kikwete katika kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu Escrow umeanza kuzua wasiwasi.

Na 'kigugugmizi' kinachomkabili Rais Kikwete kina sababu kadhaa za wazi. Kwa mfano, kumtimua Mwanasheria Mkuu Jaji Werema kunaweza kupelekea kuzuka kwa skandali nyingine iwapo Jaji huyo ataamua 'mmemwaga mboga, na mie namwaga ugali' kwa maana anajua mengi yaliyojiri na yanayojiri katika utawala wa Rais Kikwete. Japo si kwamba haiwezekani kumtimua na kisha kumfunga mdomo, lakini historia ya wanasheria wakuu huko nyuma inapaswa kutukumbusha jinsi 'wanavyobebwa' kwa minajili ya 'kutotengeneza uadui na mtu anayejua siri nyingi.'

Kwa upande wmingine, ni muhimu kukumbuka kuwa kimsingi Rais Kikwete ndo aliyemleta Profesa Muhongo katika frontline politics. Hawa ni marafiki wa karibu. Na hadi sasa Muhongo ameendeleza jeuri yake ya kisomi na kusisitiza kuwa fedha za Escrow si za umma. Msimamo huo pia washikiliwa na Waziri Mkuu Pinda. Je kuna anayefahamu msimamo wa Rais Kikwete? Maelezo yanaonyesha kuwa yeye aliridhia malipo ya Escrow kufanyika. Je amebadili mawazo na kutambua kuwa hilo lilikuwa kosa?

Lakini wakati tayari tunafahamu majina mengi ya walionufaika na mgao wa Escrow kupitia Benki ya Mkombozi, inadaiwa kuwa mgao mkubwa zaidi uliopitia Benki ya Stanbic ulihusisha vigogo kadhaa lakini hadi muda huu hakuna jina hata moja lililowekwa hadharani. So far, gazeti la Raia Mwema limeripoti kuwa mke wa kigogo momja mwandamizi huko Ikulu alikatiwa shilingi bilioni 5. Sasa huhitaji kujua hesabati vizuri kubashiri kwamba kama mke wa kigogo alikatiwa mbilioni tano, mumewe alipewa kiasi gani? 

Hayo yote tisa, kumi ni kauli niliyokumbana nayo muda mfupi uliopita, na ambayo kwa hakika ndio iliyonisukuma kuandika makala hii. Kauli hiyo ni ya Jaji Mkuu Chande ambayo kimsingi inaharibu mwenendo wa kesi yoyote itakayofunguliwa dhidi ya wahusika wa ufisadi wa Escrow. Nimeinukuu kwa picha hapa chini.


Je Jaji Mkuu alikuwa anatoa tu tahadhari au alikuwa akifikisha ujumbe mahsusi kwamba hata tukiwapeleka mahakamani wahusika wa Escrow, utetezi wao upo bayana...kwamba walishahukumiwa bungeni. Na kama Jaji Mkuu 'hakutumwa' basi kwa hakika amewapatiwa washtakiwa-watarajiwa ushauri mzuri wa bure kisheria kuhusu jinsi ya kupambana na kesi yoyote watakayofunguliwa kuhusisna na suala hilo: wajitetee kuwa walishahukumiwa na bunge, na mawakili waoa waweza kutumia kauli hiyo ya Jaji Mkuu kama supporting evidence.

Anyway, pengine ni mapema mno kuhukumu lakini kama ambavyo Mzee Warioba alivyoonyesha mapungufu ya taarifa ya PAC na maazimio ya bunge kuhusu skandali ya Escrow, sintomshangaa mtu yeyote atakayeanza kupatwa na wasiwasi kuwa tumeingizwa mkenge...TENA.


Sijui msomaji mepndwa unaonaje. 





17 Jan 2014

KATIKA hitimisho la makala yangu iliyochapishwa wiki mbili zilizopita, iliyobeba kichwa cha habari ‘Ni mwaka wa siasa za hovyo CCM, CHADEMA, niliahidi kuendeleza utabiri wa mwaka huu 2014, kwa kuangalia anga za kimataifa.
Kwa bahati nzuri, siku nne tu baada ya kuchapishwa makala hiyo, moja ya mambo niliyotabiri - kuendelea kwa mgogoro wa CHADEMA na uwezekano wa migogoro ndani ya vyama vya upinzani kuwa ya hadharani - limetokea.
Ninaomba niweke bayana kuwa masikitiko yangu kuhusu maendeleo mapya katika mgogoro wa CHADEMA ni makubwa zaidi ya furaha yangu kuona nilichotabiri wiki iliyopita kweli kimetokea. Nitakuwa mbinafsi na mnafiki ‘kusherehekea usahihi wa utabiri wangu’ katika jambo lisilopendeza. Laiti ingekuwa ni chaguo langu basi ningetamani mabaya yote niliyotabiri yasitokee, lakini kwa bahati mbaya hali halisi haikwepeki.
Takriban wiki mbili zilizopita, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) Zitto Kabwe alirusha ‘bomu zito’ ambapo alitoa tuhuma kubwa na hatari dhidi ya Mwenyekiti wake taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, na chama hicho kwa ujumla. Pengine ili kuleta ladha halisi ya alichosema Zitto ni vema nikanuu ‘waraka’ mzima kama ifuatavyo:
"Lissu anasema nimepewa magari 2 na Mzee Mkono. Anasema kaambiwa na Mkono. Naamini Mkono alimwambia pia mwaka 2005 alimpa Freeman Aikaeli Mbowe tshs 40m ili Mbowe asifanye kampeni Musoma Vijijini.
“Nadhani alimwambia pia mwaka 2008 (baada ya orodha ya mafisadi kutangazwa 2007) Mkono alimpa Freeman tshs 20m za uchaguzi wa Tarime na Freeman akasema kwenye chama ametoa mkopo na akalipwa. Nadhani alimwambia pia kuwa mwaka 2010 Mkono alimpa Mbowe tshs 200m za kampeni ya Slaa.
“Pia hakusahau kumwambia kuwa Rostam Aziz alimpa Mbowe tshs 100m za kampeni. Lissu anajua kuwa gazeti la Tanzania Daima limeanzishwa na fedha za chama kutoka Conservative Party?
“Nimefanya internship yangu kwa Mkono and Company Advocates kuhusu masuala ya mikataba. Mzee Mkono ni Mzee wangu na alisaini petition ya kumtoa Waziri Mkuu Pinda. Lissu awaambie waliyemtuma wamwambie ukweli wote. Lissu ajue yeye ni kifaranga tu, Mimi namtaka mama wa kifaranga ajitokeze. Aeleze aliingia deal gani na Kinana na Sumaye mwaka 2005 kufuatia deni lake NSSF. Aweke wazi mkataba kati yake na NHC kuhusu nyumba ya umma ilipo Club Bilicanas.
“They must know I am not a push over. Chacha died, I won't. Mtu ambaye hawezi kuheshimu mke wake aliyemzalia watoto hawezi kunyooshea mtu kidole kuhusu maadili."
Zitto alibandika waraka huo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, lakini kwa sababu anazojua yeye pekee, baadaye aliuhariri na kutojumuisha tuhuma hizo. Aidha kwa kutofahamu au makusudi, uhariri uliofanywa na mwanasiasa huyo katika waraka huo haukuzuia kusambaa kwa kasi mtandaoni.
Niliposoma waraka huo nilipatwa na mshtuko mkubwa, nikabaki ninajiuliza iwapo Zitto alikuwa ‘mzima’ wakati anaandika alichoandika.  Japo inawezekana alifanya hivyo kwa kuzingatia kile kinachofahamika mtaani kama ‘umemwaga ugali na mie namwaga mboga...bora tukose wote,” ukweli ni kwamba bandiko hilo lina madhara makubwa, kwa Zitto binafsi na kwa pengine ustawi wa CHADEMA kwa ujumla.
Madhara kwa Zitto ni ya kisheria zaidi. Tayari Mbowe ameonyesha nia ya kumburuza Zitto mahakamani kuthibitisha tuhuma hizo nzito. Bila kujali kuwa tuhuma hizo zina ukweli au la, mtu yeyote mwenye uelewa wa ‘dili za siri’ atafahamu kuwa ni vigumu kuzithibitisha kisheria, yayumkinika kuhisi kuwa Zitto atakuwa na kazi ya ziada katika ‘kesi’ hiyo (iwapo itafunguliwa).
Iwe ni tuhuma za Nimrod Mkono kumpa Mbowe shilingi milioni 260 katika mazingira ambayo si tatanishi tu bali pia kwa namna fulani ni hujuma dhidi ya CHADEMA, au Rostam Aziz kumpatia Mbowe shilingi milioni 100, au ‘dili’ kati ya Mbowe na Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, sidhani kama Zitto anaweza kuthibitisha tuhuma hizo iwapo Mbowe atatimiza azma yake ya kufungua kesi. 
Je, inawezekana kuwa kwa kutambua ‘kosa hilo la kisheria’ ndio maana muda mfupi baadaye Zitto alihariri ‘post’ hiyo? Wakati jibu analo Zitto mwenyewe, ukweli unabaki kuwa tuhuma hizo ni nzito mno, na iwapo ni za kweli basi zinapoteza kabisa hadhi ya CHADEMA.
Ikumbukwe kuwa katika waraka uliopelekea Zitto kuvuliwa nyadhifa zake mbalimbali ndani ya CHADEMA, walioandika waraka huo waligusia walichokiita ‘udhaifu wa wanayemtaka’ (wakimaanisha Zitto), na kudai, “Maneno yake mara nyingine hayazingatii anayazungumza katika mazingira gani na hivyo kuwasha masikio ya wanataasisi jambo linalompunguzia kukubalika kwake taratibu.” 
Kadhalika, walieleza kuwa; “Kuna wakati tunayemtaka (Zitto) hujibu kwa taharuki kubwa dhidi ya mashambulizi yanayoelekezwa kwake jambo linalomfanya achukue maamuzi yasiyo sahihi kwa wakati huo. Kwa kifupi kuna wakati tunayemtaka (Zitto) huonekana kufanya maamuzi kwa hisia zaidi badala ya kutulia kwanza na kutafakari kwa kina ikiwa ni pamoja na kutafuta ushauri kwa wenzake kabla ya kujibu.”
Ndugu msomaji, huhitaji kuwa mwanasaikolojia kuhisi kuwa huenda kilichomsukuma Zitto kuandika ‘waraka’ huo kwenye ukurasa wake wa Facebook ni kile Waingereza wanakiita “putting emotions in front of common sense”, yaani kwa tafsiri isiyo rasmi, kuweka mbele jazba badala ya busara.
Kwa kujaribu kuonyesha kuwa Mbowe si mwadilifu (kwa maana ya kupokea misaada kutoka kwa ‘wanasiasa kama Mkono na Rostam waliowahi kutajwa na CHADEMA kuwa ni mafisadi’), linakuja swali la msingi, kwanini Zitto alikalia kimya tuhuma hizo nzito kwa takriban miaka minane hadi sasa baada ya kuvuliwa madaraka? Hivi kuna neno stahili kuelezea hali hiyo zaidi ya unafiki?
Tukiamini tuhuma hizo za Zitto, je naye si sehemu ya ‘uhuni wa CHADEMA’ wa kukemea mafisadi hadharani ilhali pembeni wanapokea misaada ya watu hao hao wanaowatuhumu? Ninasema hivyo kwa sababu Zitto hakuwa katibu wa shina bali Naibu Katibu Mkuu (taifa)  wa chama hicho, na mbunge, na kwa vyovyote vile naye ni mnufaika wa fedha hizo ‘za mafisadi.’
Laiti angekuwa haridhii vitendo hivyo basi aidha angejitoa mhanga na kuweka ukweli hadharani wakati huo (na hiyo ingeweza kuzuia kurejea kwa vitendo kama hivyo) au angeweza kujiuzulu kwa kuona ‘chama chake kinashirikiana na watuhumiwa wa ufisadi. Kwa nini hakufanya hivyo? Jibu jepesi ni hilo nililoandika hapo juu: alikuwa mnufaika wa vitendo hivyo (iwapo kweli vilitokea, maana tayari baadhi ya aliowataja wamekanusha ‘kumpa msaada’ Mbowe).
Binafsi, ninadhani moja ya matatizo yanayomkabili Zitto ni wanaojiita au kujitambulisha kama wafuasi wake. Wengi kati yao ni wenye mapenzi na CCM, na ushabiki wao kwa Zitto ni wa kirafiki (kimaslahi?) zaidi. Ndio, tofauti za kiitikadi hazimaanishi uadui, lakini wengi wetu tunaufahamu msemo ‘nionyeshe marafiki zako na nitakwambia wewe ni nani,’ yaani mara nyingi watu wanaotuzunguka hutoa picha fulani kuhusu sisi wenyewe.
Lakini tatizo jingine kuhusu ‘wafuasi na marafiki hao wa Zitto’ ni kutokuwa washauri wazuri kwake. Ukisoma mengi ya wanayoandika, hususan huko kwenye mitandao ya twitter, utabaini kuwa kimsingi wanachofanya ni ‘kumvimbisha kichwa Zitto’ bila kutoa ushauri unaoweza kusaidia ustawi wa kisiasa wa mwanasiasa huyo kijana.
Na mfano wa hivi karibuni ni baada ya Zitto kubandika waraka huo wenye tuhuma nzito huko Facebook. Wengi wa wafuasi wake walionekana kuchekelea ‘Mbowe alivyoumbuka’ bila kujali athari za kisheria kwa Zitto na ustawi wa CHADEMA kwa ujumla (kwanini wajali ilhali wengi wao ni wanaCCM)?
Kwa wafuasi wa Zitto, mwanasiasa huyo ni majeruhi wa siasa za chuki na mizengwe ndani ya CHADEMA. Lakini kwa wengine, Zitto anaonekana kama mtu anayeendeshwa na ‘ego’ kubwa inayomfanya kujiona yeye ndiye-au zaidi ya- CHADEMA.
Ni vigumu kubashiri hatma ya maisha ya kisiasa ya Zitto lakini kwa hali ilivyo ni vigumu mno kuona mustakabali wake ndani ya chama hicho. Ninakumbuka mwanasafu mmoja wa gazeti hili alimshauri mwanasiasa huyo hivi karibuni kuwa suluhisho la busara kwake kwa sasa ni kutosubiri kuvuliwa uanachama, ajiondoe mwenyewe huko CHADEMA, na kuitaka Mahakama isiingilie kazi ya chama.
Mwisho, bado ninaamini kuwa Zitto ni mwanasiasa mzuri lakini pengine kwa upungufu wa kibinadamu au makusudi, washauri wabovu au sababu nyinginezo, hazingatii umuhimu wa busara hizi tatu katika medani ya siasa: moja, waweke marafiki zako karibu lakini waweke maadui zako karibu zaidi, na pili, hakuna marafiki au maadui wa kudumu katika siasa, na tatu, hakuna mwanasiasa anayeweza kuwa mbadala wa chama (hasa katika mazingira ya siasa zetu ambapo kwa kiasi kikubwa chombo pekee cha uongozi wa kisiasa ni chama cha siasa. Bila chama, mwanasiasa hata awe maarufu kiasi gani anabaki kuwa raia wa kawaida tu).
Katika waraka wake, Zitto aliandika, “They must know I am not a push over. Chacha died, I won't” (lazima wafahamu mie sio mtu wa ‘kupelekeshwa.’ Chacha (Wangwe?) alikufa, mimi sitokufa). Hiki ni kiburi, utoto au? Ni mwanadamu mwenye uhakika wa kutokufa? Nihitimishe kwa kumshauri kwamba labda kweli ana uhakika wa kuishi milele lakini kwa kutanguliza hisia badala ya busara, yayumkinika kubashiri kuwa anaweza kuwa anajiua mwenyewe kisiasa (committing political suicide).



28 Nov 2013


MAKALA hii ni mwendelezo wa ile iliyochapishwa katika toleo lililopita la gazeti hili, iliyobeba kichwa cha habari ‘Nani kinara wa CCM urais 2015?’
Lakini kabla sijaingia kiundani, nadhani ni vema nikarejea nilichoandika katika makala iliyopita kuhusu kukua kwa uwezekano wa CCM kubaki madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu ujao. Wiki iliyopita ilishuhudia chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA, kikiingia katika mtafaruku mkubwa ambao licha ya kutishia uhai wake unazidi ‘kupapalia’ mazingira mwafaka ya ushindi kwa CCM.
Awali, CHADEMA ilitangaza kuwavua madaraka viongozi wake waandamizi watatu, Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba na kuwapa siku 14 kujieleza kwa nini wasivuliwe uanachama baada ya kupatikana kwa nyaraka inayodaiwa kulenga kukihujumu chama hicho.
Jumapili iliyopita, Zitto na Kitila waliitisha mkutano na waandishi wa habari ambao kimsingi haikusaidia japo kupunguza moto unaozidi ‘kuunguza nyumba ya CHADEMA.’ Kwa kifupi, wanasiasa hao wawili walipinga vikali shutuma zilizoelekezwa kwao na kuhalalisha kile kilichotafsiriwa na uongozi wa chama hicho kama hujuma, huku wao wakibainisha kama matumizi ya demokrasia kwa minajili ya kuiboresha CHADEMA.
Pasi haja ya kuingia kwa undani katika sokomoko hilo, ni wazi kwamba uamuzi wa kuwavua madaraka viongozi hao na msimamo uliotolewa na ‘wahanga’ hao unaendeleza mapambano ya madaraka ndani ya CHADEMA. Kubaki au kuondoka kwa akina Zitto hakuwezi kukirejesha chama hicho katika mahala kilipokuwa. Kibaya zaidi, japo hakuna tathmini yoyote iliyokwishafanywa kuhusu athari za mgogoro huo, ni wazi Watanzania wengi wameanza kupoteza matumaini kwa chama hicho kilichotarajiwa sio tu kutoa upinzani mkubwa kwa CCM bali pia hata kuweza kuingia Ikulu mwaka 2015.
Nihitimishe suala hili la CHADEMA kwa kutanabaisha kuwa japo inafahamika kuwa lolote linawezekana katika siasa, ukweli kwamba tumebakiwa na takriban mwaka na ushee tu kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao, sambamba na ukweli kuwa hakuna dalili ya mgogoro huo wa CHADEMA kumalizika hivi karibuni, itakuwa vigumu mno kwa chama hicho kujipanga upya na vyema, kuweza kutoa ushindani wa maana katika Uchaguzi Mkuu ujao. Nitaijadili kwa kirefu hatma ya CHADEMA katika makala zijazo.
Tukiendelea na mada ya urais kwa tiketi ya CCM, niliahidi kuwa wiki hii nitajadili ‘odds’ (uwezekano wa kufanikiwa au la) zinazowakabili wanasiasa wawili ambao tathmini yangu inawaona kama ndio vinara katika mbio za kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete kupitia CCM, yaani Edward Lowassa na Bernard Membe.
Pengine hadi siku chache zilizopita, kikwazo kikubwa kwa wote wawili kingeweza kuwa uwezekano wa CCM kubwagwa na CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu ujao. Lakini kwa kuzingatia mwenendo ulivyo katika chama hicho kikuu cha upinzani, yayumkinika kuhitimisha kuwa kikwazo hicho ni kama kimekufa kifo cha asili.
Kwa upande wa Lowassa, doa kubwa linaloonekana kuendelea ‘kuchafua’ jina na wasifu wake ni tuhuma za ufisadi wa Richmond. Bila kujali kuwa uamuzi wake wa kujiuzulu uwaziri mkuu kufuatia kashfa hiyo ni ‘kutolewa kafara’ au ‘alivuna alichopanda,’ tafsiri ya haraka kwa wananchi wengi wa kawaida inabaki kuwa ‘ni vigumu kumtenganisha mwanasiasa huyo na moja ya matatizo makubwa kabisa yanayoikabili nchi yetu, yaani ufisadi.’
Ukweli kwamba Tanzania yetu sio tu ni moja ya nchi masikini sana bali pia inazidi kuwa masikini huku ufisadi ukizidi kushamiri, umesababisha kujengeka kwa hisia (pengine zisizopendeza) kuwa kila mwenye uwezo wa kifedha ni fisadi. Hisia hizo hazimsaidii Lowassa ambaye kwa siku za hivi karibuni amekuwa mstari wa mbele katika harambee za kuchangisha mamilioni ya fedha hususan kwenye taasisi za dini. Badala ya ukarimu wake kumjenga kama kiongozi anayejali, kuna wanaotafsiri jitihada zake hizo kama ‘rushwa’ ya kutaka urais mwaka 2015.
Kadhalika, kuna hisia hasi kuwa hata hizo fedha anazotoa kusaidia miradi mbalimbali ‘ni chafu’ kwa maana ya hisia kuwa huenda ni zile zilizotokana na tuhuma za ufisadi. Kibaya zaidi, kutofahamika chanzo cha kinachotajwa kama utajiri mkubwa wa mwanasiasa huyo kunaimarisha hisia hizo za ufisadi.
Vile vile, na hili linawagusa wote-Lowassa na Membe- ukweli kwamba wanasiasa hao wanatajwa kama sehemu muhimu ya ‘mtandao’ uliomwingiza madarakani Rais Kikwete mwaka 2005, unaleta hisia za ‘mvinyo mpya kwenye chupa ya zamani’ (kwa wasiofahamu, thamani ya mvinyo inaelemea sana kwenye ‘ukale’ wake na si upya wake)
Sasa, kama tukiafikiana kuwa mtizamo wa Watanzania wengi ni kuwa utawala wa Kikwete (ambao uliingizwa madarakani na ‘mtandao’ uliowashirikisha Lowassa na Membe) umetawaliwa zaidi na tuhuma za ufisadi huku hali ya maisha ya Mtanzania ikizidi kuwa ngumu, kwa nini basi watu hao wapewe fursa ya kuboronga mambo zaidi?
Faraja kubwa kwa Lowassa (na hata Membe kwa ‘uhusika wake katika mtandao) kuhusu tuhuma za ufisadi ni ukweli mchungu kuwa Watanzania ni wepesi kusahau ‘mabaya.’ Wanasiasa wetu wengi wanafahamu kuhusu udhaifu huo ambao kwa kiasi kikubwa umewasaidia wengi kuendelea kuwapo madarakani licha ya ‘madudu’ yao.
Iwapo ‘kete ya fedha’ niliyobainisha katika makala iliyopita kuwa inamsaidia sana Lowassa itaendelea kutumika, basi kuna uwezekano mkubwa wa mwendelezo wa ‘who cares?’ (nani anajali?) ambapo mahitaji ya muda mfupi kama vile sukari, khanga, mchele na mengine kama hayo yatafunika mahitaji ya muda mrefu kama vile kuondokana na umasikini sambamba, kupambana na ufisadi, na hatma ya taifa letu kwa ujumla.
Kwa upande wa Membe, kikwazo kikubwa kwake ni kutokuwa maarufu ndani na nje ya CCM. Na ukubwa wa kikwazo hicho unatokana na ukweli kwamba ‘mpinzani’ wake, yaani Lowassa, ni mwanasiasa maarufu kuliko wote ndani ya CCM hivi sasa (bila kujali umaarufu huo ni stahili au la). ‘Wajuzi wa mambo’ wanaeleza kuwa inahisiwa Lowassa anaungwa mkono na zaidi ya asilimia 75 ya viongozi wa chama wenye uwezo wa kufanya uamuzi, huku wengi wao wakiwa watu waliofanyiwa fadhila zilizosababisha wawepo madarakani hivi sasa.
Tegemeo pekee kwa Membe dhidi ya Lowassa ni lile nililogusia katika makala iliyopita; nafasi ya Idara ya Usalama wa Taifa katika kumpata mgombea urais ajaye (ndani ya CCM). Kama kuna kitu chochote kinachoweza kumzuia Lowassa kuingia Ikulu, na pengine kumsaidia Membe kupata fursa hiyo, ni pale Idara hiyo itakapoamua ‘kumbeba mwenzao’ (Membe ni shushushu mstaafu). Na hilo si gumu kama inavyoweza kudhaniwa. Moja ya maeneo ambayo mashushushu wetu wanayomudu sana ni hujuma (sabotage) na uzandiki (subversion).
Ni hivi, kwa vile tayari kuna hisia za ‘uchafu’ kuhusu Lowassa (yaani tuhuma za ufisadi) basi haitokuwa vigumu kwa mashushushu kuzikuza na kuziendeleza katika namna ya kile kinachofahamika kama character assassination. Lakini kwa vile Lowassa bado yupo katika ‘himaya’ ya Idara ya Usalama wa Taifa (kama waziri mkuu wa zamani, anapatiwa huduma za ulinzi na Idara hiyo) ni rahisi kwa mashushushu kuibua mengi (ya kweli au hata ya kutunga) dhidi yake, iwapo wataona haja ya kufanya hivyo.
Kwa hiyo, kwa kifupi, kufanikiwa kwa Membe kutategemea kukwama kwa Lowassa. Na pengine katika hatua hii, ni vema nikitanabaisha waziwazi kuwa mwana-CCM anayeongoza katika kinyang’anyiro hicho ni Lowassa akifuatiwa kwa karibu kiasi na Membe.
Nihitimishe makala hii kwa kueleza kuwa mada hii ni endelevu, kwa maana ya kuwa nitaendelea na uchambuzi na mjadala huu kadri tunavyoelekea Uchaguzi Mkuu ujao. Hata hivyo, ninapenda kurejea tena mtizamo wangu kuwa CCM kurejea tena madarakani mwaka 2015 ni janga kwa Watanzania. Chama hicho tawala sio tu kimeishiwa na kila mbinu ya kuongoza nchi lakini pia hakipo kwa ajili ya maslahi ya Watanzania. Na kama uchambuzi huu ulivyoonyesha kuwa uwezekano mkubwa wa aidha Lowassa au Membe kuwa mgombea kwa tiketi ya chama hicho ni kwa aidha fedha au ‘sanaa za giza’, yeyote kati yao atakapopata urais hatokuwa tofauti na utawala uliopo madarakani hivi sasa ambao nao ulitumia mbinu ya ‘mtandao.’
Kwa bahati mbaya au makusudi, watu tuliodhani wangeweza kutusaidia kuiondoa CCM madarakani, yaani CHADEMA, wanaonekana kuwa ‘bize’ kupigana ngwala kugombea madaraka ndani ya chama chao. Sasa kama zoezi dogo tu la kupata uongozi wa chama linasababisha ‘watiane vidole machoni’ kwenye uongozi wa nchi itakuwaje? Ni ukweli mchungu lakini usioepukika na hivyo ni vema kujiandaa kisaikolojia kuendelea kuwa chini ya utawala wa CCM (ninatamani kuwa na suluhisho mbadala lakini sijalipata hadi muda huu)

Soma zaidi kuhusu:

- See more at: http://raiamwema.co.tz/nani-kinara-wa-ccm-urais-wa-2015-ii#sthash.RAQui2j5.dpuf

12 Oct 2012


MIONGONI mwa faida ninazopata kutokana na uandishi wa makala katika jarida hili maridhawa, ni mawasiliano ya kila wiki na baadhi ya Watanzania wenzangu. Wengi wa ninaowasiliana nao, ni wasomaji ambao kwa namna moja au nyingine huwa wameguswa na mada ninazoongelea. Kuguswa huko hufuatiwa na ama pongezi au kukosolewa. Wakati mara nyingi pongezi huandamana na maneno ambayo si tu yananipa moyo na ujasiri zaidi wa kuendelea na uandishi wa makala hizi, mara nyingi kukosolewa huambatana na maneno yasiyopendeza kuyasoma au kuyasikia popote pale.
Baadhi ya wanaopongeza safu hii hudiriki kwenda mbali zaidi na kushauri labda nifikirie kuingia kwenye siasa. Mara zote jibu langu huwa lile lile. Najisikia fahari kuwatumikia Watanzania wenzangu kupitia uandishi wa makala, huku nikiamini kuwa si lazima kuwa mwanasiasa ili uweze kutekeleza jukumu hilo ipasavyo.
Lakini kwa upande mwingine, baadhi ya wanaonikosoa huenda mbali zaidi na kunituhumu kuwa uandishi wangu umeelemea kwenye chuki binafsi, husda na vitu kama hivyo. Jamaa mmoja alifikia hatua ya kudai kuwa makala zangu ni sehemu tu ya mikakati wa dini yangu dhidi ya utawala unaoongozwa na mtu anayetoka dini tofauti na yangu.
Kama ambavyo ninaridhishwa na pongezi kuhusu safu hii, huwa ninajifunza jambo moja au jingine kutoka kwa wakosoaji wangu (wengi wao hupenda kuhifadhi majina yao halisi). Kukosolewa huko, kunanisaidia kwa kiasi fulani, na hasa tukizingatia ukweli kwamba ukiona unamwagiwa sifa tu pasipo kuelezwa japo kasoro kidogo, basi yayumkinika kuhisi kuwa kuna mushkeli mahala fulani.
Nimelazimika kuandika hayo kutokana na ukweli kwamba makala yangu katika toleo lililopita ambayo pamoja na mambo mengine ilimzungumzia mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia CHADEMA, Zitto Zuberi Kabwe, imetafsiriwa na baadhi ya wasomaji wangu kama sehemu ya kampeni zangu za kumkwamisha kuingia ‘Ikulu.’
Nimeshaeleza mara kadhaa katika baadhi ya makala zangu zilizopita kuwa mimi si mwanachama wa chama chochote kile cha siasa, na nimekuwa hivyo kwa miaka kadhaa, tangu nikiwa huko nyumbani. Wakati, kwa kiasi kikubwa nilipokuwa huko nyumbani sheria ilikuwa inanikataza kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa, kwa sasa uamuzi wangu wa kuwa neutral unachangiwa zaidi na imani yangu kuwa itikadi bora zaidi kwa mwananchi ni uzalendo na kuitumikia jamii kwa hali na mali.
Moja ya sifa kuu za sheria, ni kwamba iwe mbaya au nzuri, inabaki kuwa sheria hadi itakaporekebishwa au kuondolewa. Kuna nyakati tunalazimika kufuata sheria zinazokinzana na haki zetu (kimsingi sheria inapaswa kuendana na uwiano kati ya haki na wajibu), lakini tunalazimika kuzifuata kwa vile ndizo sheria zinazotawala.
Ni kwa mantiki hiyo, ninarejea tena kutofautiana na Zitto katika dhamira yake ya kutaka kuwa Rais wa Tanzania, kwa sababu kwa mujibu wa sheria tulizonazo, hatokuwa na sifa ya urais hapo mwaka 2015 kutokana na kuwa na umri pungufu ya ule unaotajwa kwenye sheria mama ya nchi, yaani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninaafikiana na Zitto kwamba sheria hii ni ya kionevu kwa sababu kama inawezekana kwa mtu wa miaka 40 kuwa Rais kwanini ishindikane kwa mtu mwenye miaka 39?
Hata hivyo, napenda kumfahamisha kuwa hadi hapo sheria hiyo itakaporekebishwa au kubadilishwa, pamoja na ‘ubaguzi’ inaoubeba, itaendelea kuwa sheria inayopaswa kufuatwa. Na kwa vile kwa mazingira ya kawaida tu inatarajiwa Rais kuwa miongoni mwa vinara wa si tu kufuata sheria, bali pia kuzilinda, itakuwa ni ‘utani mbaya’ kwa mtu anayetaka kuwa Rais kudhamiria kuvunja sheria kama hiyo inayokataza walio chini ya miaka 40 kugombea urais.
Nimesema ninamuunga mkono Zitto kwamba sheria hiyo ni ya kibaguzi. Lakini kama tunachukia ubaguzi kwenye sheria, basi pia tunapaswa kuchukia ubaguzi kwenye kila eneo, iwe kwenye jinsia, imani, asili, rangi na hata kundi la mtu katika jamii. Siku chache zilizopita, kulikuwa na taarifa za kwamba Zitto aliongea na kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam na kutamka maneno yafuatayo:
“Wazee wetu walitusaidia sana kutupatia maendeleo ya kisiasa, sasa ni jukumu letu kuleta maendeleo ya kiuchumi. Ila naomba nisisitize kuwa jukumu hilo haliwezi kutekelezwa na mtu yeyote aliyezaliwa kabla ya uhuru, na ninatangaza nitagombea urais mwaka 2015.”
Binafsi, ninahitimisha kuwa kauli hiyo ni ya ubaguzi wa mchana kweupe. Lakini pia, licha ya ubaguzi, inaonekana kichekesho kwani imetoka kwa mwanasiasa (Zitto) ambaye hajawahi kuficha hisia zake dhidi ya ubaguzi wa watu kwa vigezo vya umri. Tukiweka kando taratibu za ndani ya CHADEMA kupata mgombea wake, moja ya sababu kuu zinazoonekana kama kikwazo kwa dhamira ya Zitto kuwa Rais, ni hiyo tuliyoiongelea hapo juu ya kutotimiza umri wa miaka 40 mwaka 2015 kama inavyotajwa kwenye Katiba.
Tunaomsapoti Zitto katika hoja yake hiyo, tunazingatia ukweli kwamba japo nchi haiwezi kuongozwa na mtoto wa miaka mitano, kwa mfano, mtu yeyote mzima (kiumri) anaweza kuiongoza nchi yetu pasipo umri wake kuathiri utendaji kazi wake. Utu-uzima si umri maalumu bali masafa (range) ya umri. Utu-uzima unaendana zaidi na uwezo wa mtu kutambua wajibu wake na kumudu kuutekeleza.
Wajibu huo unaweza kuwa katika ngazi ya familia (kama vile kuoa/kuolewa) au katika jamii pana, kama vile kushika dhamana ya uongozi.
Kwa hiyo, kimsingi, kama Zitto amemudu kuwatumikia wapigakura wa jimbo la Kigoma Kaskazini kwa mihula miwili sasa, sambamba na kulitumikia taifa kupitia uenyekiti wake kwenye Kamati ya Bunge, basi hakuna sababu ya msingi kwa umri wake kuwa kigezo cha kumzuwia kugombea urais mwaka 2015 hata kama atakuwa hajatimiza miaka 40. Ndiyo. Katiba inazuwia, lakini ukweli ni kuwa inazuwia kiuonevu!
Sasa wakati tunaafikiana na Zitto kupingana na uonevu huo wa Katiba, inakuwaje tena anatumia kigezo cha umri kuwabagua ‘wazee’ anaodai hawawezi kutuletea maendeleo ya kiuchumi? Busara ndogo tu ingeweza kumfahamisha Zitto-kama msomi-kuwa siasa na uchumi ni maeneo yanayotegemeana. Kama wazee waliozaliwa kabla ya Uhuru walimudu kutuletea maendeleo ya kisiasa, kwanini washindwe kwenye maendeleo ya kiuchumi?
Kama yeye aliyezaliwa baada ya Uhuru ameweza kufanya kazi nzuri kabisa katika uongozi wake wab kisiasa, ni kigezo kipi anachotumia kuwaona wazee waliozaliwa kabla ya Uhuru kuwa hawatoweza harakati za kuleta maendeleo yetu? Kwa hakika kabisa, huu ni ubaguzi, na kamwe mtu mwenye hisia za ubaguzi hapaswi japo kufikiriwa kuongoza nchi yetu.
Ninasema hivyo kwa sababu kama alivyotuusia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ubaguzi huzaa ubaguzi. Leo itakuwa “wazee waaliozaliwa kabla ya Uhuru hawawezi kutuletea maendeleo ya kiuchumi,” kesho itakuwa “Wakristo/Waislamu hawawezi kufanya hili,” “Wapogoro hawawezi kufanya lile,” au “wanawake hawawezi jukumu Fulani na kadhalika.
Naomba nimpe darasa dogo tu Mheshimiwa Zitto kuhusu kikwazo halisi cha maendeleo yetu. Uhaba unaozidi kukua katika uzalendo wa Mtanzania. Uzalendo hauna umri. Historia inatufundisha mengi tu kuhusu mchango wa wazee katika maendeleo ya sehemu zao husika. Mwalimu Nyerere, Nelson Mandela, Mahatma Ghandhi na kadhalika.
Binafsi, niliwahi kupishana kimtizamo na Zitto kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, ambapo katika hali ya kuchokoza mjadala, nilitamka kuwa muundo wa Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba haukuzingatia uwiano kati ya Wakristo na Waislam. Zitto alikerwa sana na hoja yangu hiyo aliyoiita ya kibaguzi. Alisisitiza kuwa tunapaswa kuangalia wasifu wa wajumbe kwa kigezo cha uwezo na uzoefu wao na si imani zao za kidini.
Cha kushangaza, ndani ya miezi michache tu, mtu huyo huyo aliyekemea vikali virusi vya ubaguzi (wa dini), amegeuka mfuasi wa ubaguzi wa umri. Kama tunapojadili teuzi mbalimbali tunapaswa kuangalia uwezo na uzoefu wa mteuliwa, kwanini basi wazee waliozaliwa kabla ya Uhuru wasitizamwe kwa uwezo na uzoefu wao kutuletea maendeleo ya kiuchumi, badala ya kuwahukumu kwa umri wao?
Ninaibua changamoto kama hiyo ya ‘ubaguzi’ kwa minajili, si ya kukwaza dhamira ya Zitto kuingia Ikulu mwaka 2015, bali kumsaidia kuamsha tafakuri yake iwapo utekelezaji wa dhamira hiyo utakuwa na manufaa kwake na kwa chama chake, au utaishia kuwa njia ya mkato kwa CCM kurejea madarakani huku CHADEMA ikiishia kuonekana chama cha mapambano kati ya vijana na wazee kukimbilia Ikulu.
Nimalizie makala haya kwa kukumbushia tena kauli ya Baba wa Taifa, ya kwamba yatupasa kuwaogopa kama ukoma wale wote wanaokimbilia Ikulu. Kama sisi wengine tunaweza kuitumikia nchi yetu kupitia makala zetu, huku wanasiasa kama Zitto wakimudu kututumikia kama wabunge, kisa cha kukimbilia Ikulu ambako Mwalimu alituasa kuwa anayefanya hivyo aogopwe kama ukoma, ni cha nini?
Simshawishi Zitto aachane na ndoto zake za urais kwani ninatambua hiyo ni haki yake ya kidemokrasia. Hata hivyo, ni muhimu kwa mwanasiasa huyo kijana kutambua kuwa wapenda mabadiliko ya kweli watamwona kama msaliti pindi ndoto zake hizo zitakapoishia kuwa kikwazo kwa CHADEMA kuing’oa CCM madarakani. Japo busara zinatueleza kuwa na ndoto pekee haitoshi, bali ni muhimu kutekeleza ndoto hizo kwa vitendo, ukiota unakata kuti unalokalia, na ukiamka ukaamua kulikata, sote tunajua matokeo yake.




Watanidharau, watanicheka, watapambana lakini nitashinda

JOHNSON Mbwambo ameandika katika Gazeti la Raia Mwema la Oktoba 3, mwaka huu, kuhusu dhihaka za Zitto kwa Prof. Muhongo (Waziri wa Nishati na Madini). Nimesoma na nimemuelewa. Kwanza naomba radhi iwapo tafsiri ya taarifa yangu niliyoitoa kwa vyombo vya habari na kuwekwa kwenye blogu yangu (zittokabwe.com) ilikuwa ina dhihaka.
Nimefundishwa kutodhihaki watu na hasa watu wanaonizidi umri na siasa zangu sio za dhihaka bali za masuala (issues). Kupitia kwa ndugu Mbwambo naomba radhi kwa wote walioona kuna dhihaka katika andiko langu. Sikuwa na nia ya kumdhihaki Waziri Muhongo. Nia yangu ni kuonyesha kuwa Waziri Muhongo alichokifanya ni kuwacheza shere Watanzania, kwa kuwaambia maneno ambayo yeye mwenyewe alikuwa anaamini kuwa hayawezekani.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara yake, Eliakim Maswi, ilithibitisha kauli yangu siku chache tu baada ya kuitoa. Mbwambo kaandika makala yake kana kwamba hapakuwa na kauli ya kufuta maneno ya Waziri. Ninaamini Mbwambo aliiona kauli ile lakini aliamua kupuuza ili kujifurahisha na imani yake kwa Prof. Muhongo na mawaziri aliowataja kwenye makala yake kwamba ni mawakala wa mabadiliko. Mbwambo anaamini kabisa kwamba ndani ya utawala wa CCM, kuna mawaziri wenye nia ya dhati ya kuleta mabadiliko.
Nieleze wazi kwamba nilishtuka sana kuona toleo moja la Gazeti la Raia Mwema likiwa na makala tatu, zote dhidi ya Zitto Kabwe. Wakati makala ya ndugu Mbwambo ilikuwa inahusu suala nyeti sana la rasilimali za taifa na ni makala nzuri yenye mafundisho, makala mbili nyingine zilikuwa ni za siasa dhidi ya Zitto. Mwandishi Mayage Mayage aliandika makala yenye kichwa cha habari “Zitto, Urais 2015 kwa chama gani?” na Mwanasafu wa gazeti hili la Raia Mwema, Evarist Chahali aliandika makala yenye kichwa cha habari “Rais Kikwete anapofikiri kama Kabwe Zitto.”
Namwambia Mayage akasome vizuri historia ya ujenzi wa CHADEMA. Yeye anadhani CHADEMA imeanza mwaka 2010. CHADEMA kimejengwa na watu, si mtu mmoja. Wanaoamua mgombea wa chama si watu wachache anaowadhani yeye Mayage bali ni wanachama wa CHADEMA kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania, ikiwamo Munanila, mkoani Kigoma anapotoka Mayage.
Huyu Chahali anasema ananijua sana. Inawezekana ananijua kuliko mimi ninavyojijua. Lakini mimi simjui na wala sijawahi kumwona ana kwa ana, nimekuwa nikimwona tu kwenye mitandao ya kijamii akinizushia, kunitukana na kunisema. Sikushangaa kusoma makala yake ya wiki iliyopita. Wote wawili nawakumbusha msemo wa Mahatma Gandhi aliposema; “Kwanza wanakudharau, kisha wanakucheka, kisha wanapambana na wewe, kisha unashinda".
Sasa nirejee kwenye makala ya ndugu Mbwambo. Prof. Muhongo simjui, licha ya kwamba nimekuwa mmoja wa wabunge walioko mstari wa mbele kuhakikisha utajiri wa nchi unatumika kwa manufaa ya nchi, sikuwahi kumsikia Prof. Muhongo mpaka alipoteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Sikuwahi kusikia akipaza sauti yake dhidi ya mikataba mibovu ya madini licha ya kwamba yeye ni msomi aliyebobea katika masuala ya miamba. Wakati Bunge la tisa, chini ya Spika Samuel Sitta, likiwa limecharuka kutaka mikataba mibovu ipitiwe na kubadilishwa tulitarajia sana kupata ushauri wa wataalamu wetu lakini hawakuonekana, "walikwina"?
Walikuwa waoga kusema maana wangeharibu uhusiano kati yao na watawala. Tulihangaika wenyewe bila maarifa yoyote kuhusu sekta ya madini. Wengine ilibidi kuacha kazi za ubunge na kwenda masomoni ili kuongeza ujuzi wa masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusu sekta ya rasilimali (madini na mafuta).
Wasomi wetu hawakuwa nasi. Walichague kuendelea kufanya kazi za ushauri kwa kampuni za utafutaji madini nchini. Leo Mbwambo anawaona hawa ndiyo mawakala wa mabadiliko. Labda anasema kweli. Ila mimi nimekata tamaa na mabadiliko kuletwa na watu waliomo serikalini, kwa sababu kadhaa.
Moja, kama alivyosema ndugu Mbwambo, nilipigia kelele sana mkataba wa Buzwagi na mikataba mingine ya madini. Niliendelea kupiga kelele mpaka sheria mpya ya madini ilipopitishwa na Bunge. Nimuulize Mbwambo kwamba, licha ya sheria mpya kuandikwa imechukua miaka mingapi kampuni za madini kufanya kazi zao kwa kutumia sheria hiyo mpya? Je, mikataba mingapi iliyopitiwa imerekebishwa au hata kuvunjwa? Pengine niwasaidie kuwakumbusha taarifa kwamba, hakuna kilichofanyika kwa mujibu wa sheria mpya, licha ya kufuatilia kwa kina bungeni kupitia michango na hata maswali bungeni sambamba na makala mbalimbali.
Tangu Waziri Prof. Muhongo na timu yake waingie ofisini ni maneno tu tunayosikia bila matendo. Hata suala la mgawo wa umeme ambalo ndugu Mbwambo analisema kama mfano, yeye anajua namna ambavyo wananchi wanalalamikia umeme kukatika hovyo, tena bila taarifa wala maelezo. Muhongo alifanikiwa sana kuaminisha watu wenye mawazo huru kama Mbwambo wakamwona yupo sahihi kiasi hata cha kufumbia macho mgawo wa umeme usio na maelezo, unaoendelea nchini.
Siwaamini mawaziri kwa sababu wanasema lolote linalowajia midomoni mwao hata kama wanaamini kuwa wanalosema haliwezekani kutekelezwa. Waziri wa Nishati na Madini alisema kuhusu mikataba ya mafuta na gesi ili kufurahisha watu. Huo ni msingi wa kwanza wa kauli yangu ambayo ndugu yangu Mbwambo ameitafsiri kuwa ni dhihaka. Nilikuwa nasema ukweli mchungu kwamba, serikali haiwezi kufanya lolote kuhusu mikataba. Nilitoa changamoto kuwa kama serikali kweli imedhamiria, iweke mikataba hii wazi. Je, wameiweka wazi?
Pili, Waziri wa Nishati na Madini anataka umma umwone kwamba anajua sana masuala ya sekta kuliko Mtanzania mwingine yeyote. Nitatoa mfano mmoja unaonihusu moja kwa moja. Katika mkutano wa Bunge uliopita, Tanzania ilitembelewa na Waziri Mkuu mstaafu wa Urusi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Kirusi iliyonunua leseni ya kutafuta uranium kule Selous. Kampuni ya UraniumOne iliyonunua leseni hii ya Mkuju River Project kutoka Kampuni ya Mantra ya Australia, kwa dola za Marekani milioni 980.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitaka ilipwe kodi ya ongezeko la mtaji (capital gains tax) kampuni hii ilikataa. TRA wakaenda mahakamani kudai malipo ya kodi yenye thamani ya dola za Marekani milioni 116 ambazo ni sawa na asilimia 20 ya thamani ya mauzo na kesi inaendelea. Kwa mujibu wa sheria zetu kampuni zinapouziana leseni, lazima Waziri wa Nishati na Madini atoe idhini ya mauzo hayo. Mgeni huyo kutoka Urusi alikuja nchini kupigia debe idhini hii, ili itolewe leseni maalumu ya uchimbaji (special mining licence).
Nikasimama kutoa taarifa bungeni kwamba mawaziri wanakutana na huyu Waziri Mkuu mstaafu wa Urusi kuhusu leseni ya Mkuju River Project na kuweka wazi kwamba Kampuni ya UraniumOne hawajalipa kodi ya capital gains. Nilisimama kutoa taarifa baada ya majibu ya Waziri Muhongo kwamba, kilichouzwa si kampuni ya Tanzania bali Australia na hivyo hakuna kodi.
Kwa makusudi kabisa niliacha habari ya kesi ya TRA dhidi ya kampuni hii ili kuona umakini wa mawaziri wetu wapya kabla ya kukutana na lobbyists (washawishi) wa kampuni hizi za madini. Waziri Muhongo aliposimamishwa na Naibu Spika, Job Ndugai, akasema “Sisi tunajua zaidi kuliko Zitto" Kwanza Waziri hakuwa anajua.
Ni makosa kabisa kujadili suala ambalo mamlaka mojawapo ya nchi wamelipeleka mahakamani na linasubiri uamuzi. Lakini suala la Waziri kutokuwa na taarifa lilidhibitishwa na ujio wa Naibu Waziri George Simbachawene, aliponifuata na kuomba "details" kuhusu taarifa niliyotoa. Kulikuwa na haja gani kwa Waziri kusema bungeni yeye anajua zaidi na baadaye kumtuma Naibu wake kutafuta taarifa?
Huu ni udhaifu mkubwa sana wa uongozi. Kutojua si makosa, inawezekana kuwa wengine hatukusomea miamba lakini tumesomea masuala ya kodi kwenye madini na mafuta. Waziri makini anayejali nchi yake anawezaje kukutana na mwekezaji anayekataa kukulipa kodi yako bila wewe hata kuulizia utalipwa lini?
Unaulizwa bungeni unasema "ninajua zaidi" na Mwandishi mahiri kama Mbwambo anasema "mpeni nafasi atende"!
Nilipomsikia Waziri anasema ameagiza TPDC (Shirika la Maendeleo la Mafuta) kupitia mikataba nikajua na hili nalo hajui. Amesema tu ili watu wafurahi kwamba mikataba inapitiwa. Kupitia mikataba bila kuchukua hatua dhidi ya mikataba mibovu ni nini kama sio kutafuta umaarufu tu? Unapitia mikataba ili iwe nini kama huwezi kuchukua hatua?
Kuna mikataba ambayo imeingiwa kwa rushwa, sheria zetu zinasema kuwa mikataba iliyoingiwa kwa rushwa ni sawa na haipo. Hata sheria za kimataifa za mikataba zinatambua hivyo. Waziri anaposema kuwa tunapitia mikataba ili kuhakikisha kuwa mikataba ijayo inakuwa mizuri ni kichekesho. Hivi tunajua vitalu vingapi vimegawiwa na vingapi vimebaki? Hivi sasa kuna mikataba 29 na leseni 26. Vitalu vilivyobaki hivi sasa ni tisa tu.
Wizara inatuambia tunaangalia hii mikataba 29 ili kuboresha 9. Haya si mapitio bali ni kuangalia tu kama nilivyosema katika sentensi iliyotangulia. Mapitio bora zaidi ni uwazi wa mikataba yote tuliyoingia mpaka sasa na kuzuia kabisa mikataba mipya wala kugawa vitalu vipya vya kutafuta mafuta na gesi.
Uporaji wa rasilimali ni wa namna mbili, moja ni watu wachache na kampuni zao kupora kwa kupitia mikataba mibovu na pili ni kizazi kimoja kunyonya rasilimali zote bila kujali kizazi kijacho. Katika maandiko yangu nimeshauri kuwa tusigawe vitalu vipya mpaka tuone mafanikio ya mikataba hii 29 na leseni 26 tulizonazo hivi sasa. Wito wangu ni mmoja tu, uwazi wa mikataba. Kutaka uwazi si dhihaka. Uwazi ni uwajibikaji.
Suala la mapitio ya mikataba kwa jicho la juu juu ni suala la kuunga mkono. Lakini ukitazama historia ya nchi yetu katika masuala haya utabaini kwamba tunapaswa kufanya zaidi ya mapitio ya mikataba.
Tunapaswa kufanya jambo ambalo hatujawahi kulifanya nalo ni kuiweka wazi mikataba hii kwa umma. Hii ndiyo hoja yangu.
Inawezekana kabisa kwamba maneno niliyotumia yameudhi watu fulani lakini ikumbukwe mimi ni Mbunge wa Upinzani na ni wajibu wangu kukosoa serikali kila inapowezekana. Bahati nzuri miaka yangu saba bungeni hivi sasa imetumika kwa kiasi kikubwa sana katika kufuatilia kwa karibu sekta ya madini, mafuta na gesi. Ni rahisi sana mimi kuweza kuona suala linalosemwa na serikali linasemwa tu au serikali inamaanisha? Katika suala la mapitio ya mikataba kwenye sekta ya madini na mafuta kwa kweli serikali haipo makini. Watu wajuvi wa mambo kama kina Mbwambo wanapaswa kwenda zaidi ya mapitio na kutaka mikataba iwekwe wazi na kuchambuliwa kwa uwazi kabisa.
Waziri Muhongo anayo nafasi ya kufanya kazi yake, afanye kazi yake bila bugudha. Mbwambo ajue kuwa Mbunge Zitto pia anayo kazi yake kwa mujibu wa Katiba ibara ya 63 nayo ni "kuisimamia" serikali. Niacheni nami nifanye kazi yangu.
Makala hii iliyoandikwa na Kabwe Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini ni majibu kwa makala iliyoandikwa na Mwanasafu wetu, Johnson Mbwambo, katika toleo lililopita la gazeti hili la Raia Mwema, kupitia safu yake ya Tafakuri Jadidi.
MAONI: NI KWELI ZITTO HANIJUI, NA KATIKA MAKALA HUSIKA NILIANDIKA "NAMJUA ZITTO VIZURI" NA SIO "TUNAJUANA VIZURI." NA KIMSINGI, HAKUPASWA KUNIJUA WAKATI NILIPOKUWA NAMJUA (KINYUME CHA HIVYO,JUKUMU ZIMA LA KUMJUA LISINGEKUWA NA MAANA). BY THE WAY, HIVI ZITTO ANAMJUA KILA MPIGA KURA KATIKAJIMBO LAKE, LET ALONE MIE AMBAYE SIKUMPIGIA KURA?

SIKUANDIKA KUWA NAMJUA ZITTO VIZURI KWA MINAJILI YA KUSAKA SIFA AU KUJIKOMBA KWAMBA "NINAMFAHAMU VIZURI RAIS MTARAJIWA" BALI NILIANDIKA HIVYO KUPIGIA MSTARI KUWA MWANASIASA NINAYEMZUNGUMZIA NI MTU NINAYEMFAHAMU (KIVIPI,WAPI...NAOMBA NISIZUNGUMZIE HILI KWA MUDA HUU).

SITAKI KUMWITA MHESHIMIWA ZITTO MBABAISHAJI LAKINI MAKALA YAKE HII INANISHAWISHI KUFIKIRIA HIVYO.ZITTO ANAZUNGUMZIA MIE KUMJUA, ANADAI NINAMTUKANA (HIVI RAIS MTARAJIWA HATAMBUA KUWA MTU AKIKUTUKANA KWENYE TWITTER UNAPASWA KUMRIPOTI KWA WAMILIKI WA MTANDAO HUO BADALA YA KULALAMIKA KWENYE MAKALA?).HUYU ANAYEDAI NINAMTUKANA NDIYE SAME PERSON ALIYEANDIKA HAYA  ni upumbavu kufikiri kwa misingi wa kidini. Huna haki kuleta ubaguzi wako wa kidini hapa. 3 out of 15 muslims, unaita ubaguzi? (chanzo: http://goo.gl/8MLDO

Mwanasiasa huyu mbabaishaji alinilaumu kwa "kuleta ubaguzi" lakini yeye si mbaguzi anapodai watu waliozaliwa kabla ya uhuru hawawezi kutuletea maendeleo ya kiuchumi.

NIMALIZIE KWA KUWAACHIA WASOMAJI FURSA YA KUAMUA WENYEWE IWAPO MHESHIMIWA ZITTO AMEJIBU HOJA (NINAZOZIONA) ZA MSINGI KATIKA MAKALA HII







21 Sept 2012


Zitto Kabwe, Let Dr. Muhongo Do His Job


Energy sector has brought to a disgraceful ending some very promising careers. It has sent packing very powerful and prominent figures in the country’s upper echelons of power; Infarct, at one point, it almost brought down the entire government, when the country’s premiere at the time, faced grand corruption allegations, and was forced to resign. It is our economic sector, by far mired by grand corruptions and ineptness. 

Reason behind all these has been nothing more than the bogus contracts. There is therefore, a critical need to review and even terminate some of the existing contracts in the eyes of the public, in order to close the loopholes fleecing the country of its wealth 

The Kigoma North Legislator, Zitto Kabwe, has unleashed in the past few days, some scathing attacks on the Minister of Energy Sospeter Muhongo, for proposing a thorough review of the Gas exploration contracts. Mr. Kabwe described Dr. Muhongo’s statements as irresponsible, publicity stunts and cowboy’s approach at the expense of transparency. What I found rather irresponsible, odd, flawed and vague, was the broad idea of “Transparency” in which Mr. Kabwe is attacking Dr. Muhongo’s premise without providing a practical solution under conventional wisdom

I also found Mr. Kabwe’s idea of shelving gas exploration for ten years as logically, and economically naïve. At best I would describe the proposition as a theory that contravenes the basic and natural economic principles that cannot be implemented in a needy nation like ours. Implementing this thought would be nothing short of economic suicide for a nation whose economy is extremely fragile. 

Mr. Kabwe’s Transparency assertion reveals nothing short of tactical political, intimidation, representation and defense of the unknown interests. I would not go as far as describing the verbal assault as a self serving personal act of vengeance. However, the premise under which Mr. Kabwe’s argument is based, and his pattern of attack, points towards just that.

Mr. Kabwe unambiguously failed to explain how making transparent shoddy contractual agreements, will benefit the country without identifying the loopholes and deficiencies through extensive review. Arguably, lack of legal and technical knowhow to intimately interpret word by word in the existing contracts to weed out the elements tilting the scale on the favor of investors and shadowy forces of corruption, would have lent Mr. Kabwe’s proposition of transparency, some flesh to stand the test in opposition Dr. Muhongo’s hypothesis

Mr. Zitto ought to understand that, major foreign companies operating in Africa have tremendous resources. They have access to some of the best lawyers, and subject matter experts with extensive experience in contractual review, interpretation, negotiations, and writing. A fact which has many a times, led to the creation of lopsided contracts that have benefited investors while fleecing the host country. 

Mr. Kabwe failed to provide a balanced approach to those deficiencies. In my opinion, Dr. Muhongo’s approach is heroic, and nationalistic. The public should, without reservation throw its absolute support behind this man for his position to temporarily suspend and review all the current contracts related to gas exploration and even electricity production

Having worked in the Investment Banking –Capital Markets- Can affirm to the fact that, success or failure of an investment, primarily depends upon how crafty a contract is. Managers across all economic sectors assemble top legal minds and experienced subject matter experts that would pull off successful investments through favorable and well structured contracts. These contracts at the same time have in them, clauses and provisions that provide room for ongoing review and amendments contingent upon the prevailing conditions or circumstances and market situations. 

My only question is why Zitto is up in arms trying to block the review of questionable contacts in the public eyes, what is his fear? Singapore, India, Venezuela, Brazil etc. in recent years, radically modernized and even terminated some contracts with foreign investors in various sectors that were becoming economic liabilities or not equitably representative. This is how things work be it in municipalities, public or private companies, sovereign states and government agencies. Dr. Muhongo as a subject matter expert has suggested just that. Why should he face political interference? 

From my understanding, TPDC, a body tasked with the contractual review is not a political body. It is a professional entity made of subject matter experts –seasoned professionals -. If Mr. Zitto is dissatisfied with TPDC current formation or the capability, he should demand the overhaul of its management team for a more qualified one, which will execute the task –contractual review- diligently, impartially and independently for the interest of the nation. All findings thereafter be made public to satisfy his demand for transparency 

Political meddling, intimidation and personal hostility are not doing the country any good considering the fact that, main victims of bad contracts in the energy sector are the country’s economy, and the public at large. Politics should be kept off professional undertakings. Mr. Kabwe should let Dr. Muhongo do his job. This man has been in the office for a very short period. He has taken bold and risky decisions no other minister has ever taken in the ministry and the energy sector in general. He is stepping on dangerous toes for the best interest of the country, and what he needs the most at this point is our support not interference

Dr. Muhongo’s success or failure is not going to be measured by how many politicians he pleased or displeased, but on what he delivered to the country at the time of need. Soon or later, the public will know whether he was a bluff or a HERO he painted himself to be.  Dr. Muhongo’s approach is the right step in the right direction. Wrong step into the wrong direction is to politically interfere with his work in the name of transparency. Give him a chance to do his Job
 
Mungu Ibariki Tanzania



Forwarded  by Dr Shaban Nzori. "Mzalendo Mtanzania" is Mr Mashaka John.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.