Mwezi Februari mwaka huu,Rais wa Kampuni ya Toyota (ya Japan) Akio Toyoda aliomba rasmi msamaha kwa wateja wa kampuni hiyo nchini Marekani ambao walikumbwa na matatizo ya kiufundi kwenye magari yao.Mwezi kama huo mwaka jana,mabosi wa mabenki ya RBS na HBOS ya hapa Uingereza nao waliomba msamaha kwa wateja wao na umma kwa ujumla kutokana na uzembe uliopelekea benki hizo kukwamuliwa na serikali kwa pauni bilioni 37 fedha za walipakodi wa hapa. Na hivi majuzi,Waziri Mkuu wa Japan,Yakio Hatoyama, ametangaza kuwa atajiuzulu kufuatia kutotimiza ahadi aliyotoa wakati wa kampeni zake za uchaguzi kuwa angeondoa vikosi vya jeshi la majini la Marekani katika visiwa vya Okinawa.
Lakini wakati hayo yakitokea,serikali ya CCM imewaamuru mawaziri wake kuzunguka mikoani kueleza mafanikio ya Awamu ya Nne katika harakati za wazi kuelekea Uchaguzi Mkuu.Tuweke ushabiki pembeni,hivi kweli mawaziri hawa hawakustahili kuzunguka huku na huko kuomba msamaha kwa mlolongo wa madudu tunayoendelea kuyashuhudia tangu mwaka 2005 (na pengine madudu zaidi yanayoendelea kufanywa na CCM miaka nenda miaka rudi)?
Msanii mkongwe wa hapa Uingereza (na duniani kwa ujumla),Sir Elton John aliwahi kuimba wimbo wenye jina SORRY SEEMS THE HARDEST WORD (yaani 'samahani inaelekea kuwa ni neno gumu').Na hakukosea,japo hakuwa analenga siasa za nchi zetu za Dunia ya Tatu,hususan Afrika,na hasa Tanzania.Watawala wetu ni wepesi sana katika kugeuza lawama kuwa pongezi,na wakibanwa katika hilo hugeuka mbogo na kuja na vitisho lukuki.
Labda nikukumbushe kidogo kwanini naamini ziara za mawaziri zingekuwa na maana zaidi kama zingetumika kuomba msamaha kwa wananchi badala ya kuelezea mafanikio ambayo kimsingi yanabaki kwenye takwimu zaidi kuliko uhalisia.Kwanza,Awamu ya Nne ilitufahamisha kuwa inafahamu kilio cha Watanzania,na ikaja na kauli mbiu ya kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya.Naamini mie si pekee niliyesahau kuhusu kauli mbiu hiyo kwa vile wala haisikiki tena.Lakini kama hiyo haitoshi,kukaongezwa kibwagizo cha Maisha Bora kwa Kila Mtanzania (Yanawezekana).Japo sote tunatambua kuwa watawala wetu wanaishi kama wako peponi lakini hiyo sio excuse ya kuwafanya wasielewe kuwa maisha bora yamewezekana zaidi kwa mafisadi kuliko kwa wananchi walalahoi wa kawaida.Kwahiyo kama viongozi hawa wangekuwa na nidhamu kwa wapiga kura waliowaweka madarakani hapo 2005 basi angalau wangetuambia nini kinachopelekea maisha bora kubaki haki ya mafisadi wachache huku walalahoi wakizi kuwa walalawima.
Baada ya kuingia madarakani,Awamu ya nne ilitueleza kuwa ili kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania kunahitajika baraza kuuuubwa la mawaziri.Binafsi niliona kuna mantiki katika hoja hiyo japo sikuwa na uhakika kuwa "mwalimu anaweza kumudu darasa lenye wanafunzi wengi" kama ilivyokuwa kwenye kabineti ya JK.Bila kuuma uma maneno,kwa kifupi ukubwa wa baraza la mawaziri haujafanikiwa kwa chochote katika ku-meet matarajio ya Watanzania.Sanasana wengine walilazimika kujiuzulu baada ya kutuingiza mkenge kwenye ishu kama za utapeli wa Richmond.Ungetegemea kujiuzulu huko kungeandamana na hatua za kisheria lakini waliojiuzulu waliishia kupongezwa huku wakikumbushwa kuwa yaliyowakumba ni ajali tu za kisiasa na si ajabu siku moja wakarejea madarakani.
Mkuu wetu wa nchi akatuambia kuwa anawafahamu wala rushwa ila anawapa muda wa kujirekebisha.Binafsi,hapo ndipo nilipoanza kuhisi kuwa sikuwa sahihi kuamini kwamba tumepata mrithi halisi wa Mwalimu (Nyerere) in the form of JK.Tangu lini mwizi akapewa deadline?Kama wala rushwa walikuwa wanajulikana kwa Rais kilichopaswa kufanywa ni yeye kukabidhi orodha hiyo kwa taasisi husika ili wachukuliwe hatua stahili.Unajua,laiti JK angekabidhi orodha ya wala rushwa anaowajua kwa vyombo vya usalama kisha wakakamatwa na kuepwa deadline,pengine by now tusingekuwa tunajiuliza wenye Kagoda ni akina nani.Ni muhimu wak Watanzania kumhoji Rais wetu mpendwa kuhusu hao wala riushwa anaowafahamu,na lini hiyo deadline ita-expire.Tunachohitaji ni majina na sio idadi,na hata kama ni idadi basi tuambiwe lini watashughulikiwa.
Tuaambiwa kuwa matatizo ya umeme yangepatiwa ufumbuzi wa kudumu only miezi michache baadaye kufahamu kuwa ufumbuzi wenyewe unahusisha matapeli wenye kampuni ya briefcase (Richmond).Shahidi muhimu katika sakata la EPA akahifadhiwa mpaka Maulana akachukua uhai wake (kuna wanaodai kuwa bado yuko hai au huenda kafanyiwa plastic surgery) halafu wenye nchi wakagoma katakata kutuambia mwizi mkubwa wa fedha za EPA (Kagoda ni nani).
Tuaaambiwa kuwa ziara za mara kwa mara za Rais wetu huko nje ni muhimu kuitangaza nchi yetu na yeye kujitambulisha,kabla ya kuaminishwa kuwa Mkutano wa Sullivan na huu wa majuzi wa Economic Forum utalinufaisha taifa hasa katika sekta ya utalii,only for tuliorogwa sie kulipa mabilioni ya shilingi kuialika timu ya taifa ya Brazil huku kukiwa na ngonjera zilezile za "ziara hii itasaidia kuitangaza Tanzania".Kama ziara za Rais huko nje na rundo la wafanyabiashara (plus mikutano kama ya Sullivan na huo wa Economic Forum) imeshindwa kuzaa matunda,dakika 90 za mechi na Wabrazili zitaweza?
Majuzi wafadhili wametangaza kupunguza misaada yao kwa sababu ya ufisadi (putting it straightforward) na Waziri wetu wa Fedha Mustapha Mkulo bila aibu anasema hiyo isitupe hofu kwa vile serikali itakopa benki ya Stanbic!Nasema "bila aibu" kwa vile sio tu kukopa sio sifa hususan kwa serikali iliyoingia madarakani na mkwara wa maisha bora kwa kila Mtanzania bali pia deni hilo litabebwa na walalahoi haohao wanaoendelea kubebeshwa mzigo wa mahela yanayokwibwa na mafisadi kila kukicha.
Haya,tukaambiwa tena kuwa kwa vile kuna mtikisiko wa uchumi wa dunia basi na hohehahe sie lazima tuyanusuru makampuni yetu katika kile kinachofahamika ki-uchumi kama "stimulus package".Hivi kwa mwenye akili timamu,ukitangaza kuwa kuna hela za bure somewhere unatagemea nini kama sio vigogo kuunda kampuni hewa na kuiba fedha hizo?Hadi leo hatujaambiwa mafanikio ya stimulus package hiyo, na kama ilivyokuwa kwenye ripoti ya mabomu ya Mbagala usitarajie kuambiwa lolote la maana zaidi ya takwimu za kizushi.
Halafu Mkuu wetu wa nchi akatupa presha kwa kuamua kuhutubia Bunge kuhusu sakata la EPA (pamoja na mambo mengine).Tunaloweza kukumbuka zaidi kwenye hotuba hiyo ni kauli yake kuwa anathamini sana haki za binadamu ikiwa ni pamoja na za mafisadi.Kumbukumbu nyingine ni angalizo kutoka kwa Spika wa Bunge,Samweli Sitta,kuwa haki za binadamu za walalahoi ni muhimu zaidi kuliko za hao mafisadi.
Nimejitahidi kuorodhesha machache yanayopaswa kuombewa radhi na mawaziri wa serikali ya Awamu ya Nne badala ya "kueleza mafanikio".Unless wanataka kutuaminisha kuwa kukua kwa ufisadi ni sehemu muhimu ya mafanikio yao.Natambua kuwa "SAMAHANI" ni neno gumu kama alivyosema Elton John lakini uungwana ni kitu cha bure.Hizo fedha za walipa kodi wanazotumia kuzunguka huku na kule zingeweza kutumika vizuri zaidi kwa kila Waziri kuomba msamaha kwa madudu aliyofanya katika miaka hii mitano.Kaulimbiu kuwa "mlitutuma, tumetekeleza, tumerudi kuwaelezeni tulivyotekeleza na kuwasikiliza" ni matusi ya nguoni kwa vile hakuna Mtanzania mwenye akili timamu aliyeituma serikali kuingia mikataba ya kitapeli na wazushi wa EPA,au kukomalia kutotaja Kagoda ni mdudu gani,plus madumu mengineyo.Tulichowatuma ni kutukomboa kutoka katika lindi hili la umasikini sambamba na kuboresha hali za maisha yetu.Hatukuwatuma kuuza kila kilichopo kwa bei ya kutupa wala hatukuwatuma kung'ang'ania kununua samani kutoka nje na hatimaye kukumbuka dakika za majeruhi kuwa ununuzi huo hauendani na umasikini wetu.
Japo nakerwa na ziara hizi za mawaziri zinazozidi kuwabebesha mzigo walipa kodi walalahoi lakini nakereka zaidi napoona watu hawa wanapotufanya wajinga kiasi cha kutuzushia kuwa TULIWATUMA KULEA UFISADI.
Tumia kura yako vizuri,ukiendekeza ushabiki utazidi kuumia.Hakuna miujiza inayoweza kuondoa ufisadi hata kama watu watakesha kwenye nyumba za ibada (na huko wanakutana na "wabishi" kama Askofu Kilaini ambao wanaendelea kung'angania mtizamo wao finyu kuwa JK bado ni chaguo la Mungu.Askofu muogope Mungu wako unayemtumikia,please!).Nia pekee ya kuondokana na ufisadi ni kuwaondoa mafisadi.Kumbuka kuwa ufisadi ni kitendo kinachofanywa na mafisadi,na as long as wanaendelea kuwepo basi inakuwa mithili ya kupe au mbung'o na damu.Watanyonya hadi tone la mwisho.
AMKA!













