Showing posts with label BONGO. Show all posts
Showing posts with label BONGO. Show all posts

18 Jun 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Mwaka juzi gazeti maarufu duniani la TIME lilimtangaza George W.Bush kuwa “mtu wa mwaka (2004)” –au “Person of the Year” kwa lugha ya kwa mama.Katika uchambuzi wake kuhusu Bush,gazeti hilo lilimnukuu Rais huyo wa Marekani akisema kwamba “inapotokea kuwa hoja au mawazo yako yanazua mjadala au upinzani basi ni dalili kwamba yana uzito…kwa maana yangekuwa ya kipuuzi wala watu wasingejishughulisha nayo.”Alikuwa anazungumzia upinzani anaokumbana nao katika utendaji wa kazi zake za kila siku.Sio siri kuwa Bush anachukiwa na watu wengi hata ndani ya nchi yake.Lakini japo mie sio shabiki wake,namhusudu kwa jinsi anavyoweza kufanya mawazo yake yakubalike hata kwa wale ambao aidha hawayapendi au hawaafikiani nae.

Mwaka jana wakati nakuja huko nyumba,nilibahatika kukaa kiti kimoja na mama mmoja wa Kimarekani.Ni mtu mwongeaji sana,nami niliitumia nafasi hiyo kumdadisi siasa za Marekani hasa kuhusu mgawanyiko mkubwa wa kiitikadi nchini humo baina ya wale wa mrengo wa kulia(conservatives) na wale wa mrengo wa kushoto (liberals).Mwanamama huyo ambaye alinifahaisha baadaye kuwa ni mwanaharakati wa mazingira,alieleza kuwa kwa kiasi kikubwa mgawanyiko huo unachangiwa na siasa za Bush na maswahiba zake kama Dick Cheney,Donald Rumsfield,Paul Wolfowitz,na wengineo ambao wanajulikana kiitikadi kama “neo-conservatives” (sijui wanaitwaje kwa lugha yetu ya Taifa!).Miongoni mwa imani za hawa jamaa ni kuhakikisha kuwa Marekani inatumia ipasavyo nafasi yake kama Taifa lenye nguvu kabisa duniani.Kwa maana hiyo,ni “haki” yake kutumia “ubabe” wake kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuvamia zile nchi zinazoonekana kuwa “korofi”.Ipo siku nitawazungumzia kwa kirefu jamaa hawa ambao takriban wote ni wadau wa taasisi moja isiyo ya kiserikali iitwayo “The Project for The New American Century” (Mradi wa Karne Mpya ya Marekani,kwa tafsiri isiyo rasmi).Turudi kwa yule mama.Basi akanambia kuwa japo yeye binafsi ni mpinzani wa Bush na hao neo-conservatives wenzake kuna wakati huwa “anamzimia sana” kutokana na jinsi anavyoweza kufanya maamuzi yake yatekelezwe hata pale kwenye upinzani mkubwa.Waingereza wana msemo “kama humuwezi unayeshindana nae basi bora uungane nae tu,”na ndio maana hata wale wasioafikiana na Bush mwishowe hujikuta hawana jinsi bali kuendana na mawazo au maamuzi yake.

Muda mfupi uliopita nilipata ujumbe kutoka kwa rafiki yangu flani aliyeko huko nyumbani akinijulisha kuwa kuna mwandishi mmoja ameandika makala katika gazeti flani la kila siku (la hapo Bongo) kupingana nami katika hoja ya makala yangu moja ya hivi ambayo nilimfananisha Rais Jakaya Kikwete na kiongozi wa chama cha Conservatives cha hapa Uingereza,David Cameron.Kwa mujibu wa ujumbe niliopata,mwandishi huyo aliyepingana nami anadai sikuwa sahihi kuwalinganisha wanasiasa hao .Kwa bahati mbaya hadi natayarisha makala hii nilikuwa sijapata hoja zote zilizotolewa kukosoa makala yangu.Kwa mantiki hiyo itakuwa vigumu kujibu hoja baada ya hoja bali nachoweza kusema kwanza ni kwamba makala ya mwandishi huyo ni uthibitisho tosha kuwa gazeti hili la KULIKONI ni kipenzi cha wengi,na ndio maana linazaa hoja na makala katika magazeti mengine.Pili,kama gazeti la TIME lilivyomnukuu Bush naamini makala yangu hiyo ilikuwa na uzito ndio maana ikamsukuma mwandishi huyo kuijadili japo hakuafikiana na nilichokiandika,kwa kuwa laiti ingekuwa ya kipuuzi asingepoteza muda wake kupingana nayo.”

Kwa faida ya mwandishi huyo,Kikwete anashabihiana sana na David Cameron katika maeneo flani.Kwa mfano,wote wawili wako katika vyama ambavyo kabla ya wao kushika hatamu za uongozi kwa kiasi flani vilikuwa vinaonekana kama ni vya “wateule wachache” tu.Ushindi wa tsunami kwa Kikwete ni dalili tosha kuwa hata baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani walimpigia kura kuonyesha kuwa kuteuliwa kwake kuwa mgombea urais kuliiongezea nguvu CCM.Hoja nyingine japo inaweza kuwa si nzito sana ni kwamba wanasiasa hao wana sifa inayofanana ya kuwa handsome,na kwa taarifa yako u-handsome unalipa sana kwenye siasa.Lakini kingine ni lugha zao wanazotumia.Wanaongea lugha za watu wa kawaida wa mtaani,yaani wanajua wananchi wanatarajia nini kwao.Ndio,Cameron anafuata siasa za mrengo wa kulia kuelekea kati (right-centre) na Kikwete kama mwana CCM nadhani atakuwa ni wa siasa za mrengo wa kushoto kuelekea kati (left-centre),na japo Cameron ni Mwingereza na Kikwete ni Mtanzania,la muhimu hapa ni jinsi wananchi wanavyowahusudu kutokana na utendaji wao.Kura za maoni hapa Uingereza zinaonyesha kuwa Cameron amempiku Tony Blair kwa kupendwa na wananchi na naamini kuwa hata kama Watanzania wataamshwa usingizini kupiga kura za maoni,Kikwete ataibuka kidedea kwa sana.Kwenye siasa umaarufu wa mwanasiasa haugemei sana kwenye itikadi zake au chama chake,sehemu aliyozaliwa au umri wake bali kukubalika kwake miongoni mwa wananchi,na hicho ndicho kilichonipelekea kuwafananisha wanasiasa hao.

Mwisho,siamini kuwa mwandishi wa makala hiyo alikuwa anatafuta umaarufu kupitia makala yangu au gazeti hili la KULIKONI,bali alikuwa anatumia haki yake ya kikatiba kutoa mawazo yake.Nampa changamoto aendelee kusoma gazeti hili ilimradi isiwe kwa nia ya kupinga kila kitu hata kama ameishiwa na hoja.Kama alivyoimba Mista Two (Joseph Mbilinyi) kwenye wimbo wake “Sugu” kwamba huwezi kuizuia mvua kunyesha,KULIKONI ni kama jua na mvua,halizuiliki.

Alamsiki.

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa gazeti hili.

Leo tuzungumzie muziki.Muda mfupi uliopita nilikuwa nasoma makala flani kumhusu msanii wa kizazi kipya Albert Mangwea.Yalikuwa ni mahojiano kati ya msaanii huyo na tovuti ya Darhotwire.com.Niliguswa sana na kilio cha msanii huyo ambacho kimekuwa pia kikisikika kutoka kwa takribani kila msanii wa Bongofleva.Kuna wajanja flani,(hapana,hawa si wajanja,bali ni WEZI) ambao wamekuwa wakiwanyonya vijana wetu bila hata chembe ya huruma.Wezi hawa wanafahamika zaidi kwa jina la “wadosi”.Binafsi sijui kwanini wanaitwa wadosi lakini la muhimu hawa sio jina wanaloitwa bali unyonyaji wanaowafanyia wasanii wetu.

Pengine kabla ya kujadili wizi wa mchana mweupe unaofanywa na wadosi hao,tuangalie maendeleo ya Bongofleva huko nyumbani na huku Ughaibuni.Mimi ni mfuatiliaji sana wa mambo yanayotokea huko Bongo. “Ibada” yangu ya kila asubuhi inaanza kwa kutembelea tovuti za ki-Tanzania ili kujua yanayojiri huko.Sasa,kabla ya kuja huko mwaka jana mwishoni mwa mwaka jana nilikuwa nahisi kuwa habari kwamba Bongofleva imeikamata Tanzania kwa “kasi ya tsunami” ni porojo tu.Lakini nilipokuja nilishihudia mwenyewe jinsi gani hatimaye nyimbo zinazotengenezwa na kuimbwa na Watanzania zilivyokamata soko na mioyo ya wapenzi wa muziki.Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu nilibahatika kushuhudia tamasha la “Piga Kura au Upigike” kwenye viwanja vya Biafra Kinondoni.Licha ya picha kadhaa nilizochukua kwa ajili ya kuwajulisha marafiki zangu hapa,nilijionea jinsi gani watu wa rika mbalimbali wanavyovutiwa na kazi za wasanii wa muziki wa kizazi kipya.Nadiriki kuamini kuwa mashabiki waliofika viwanja hivyo walikuwa wanawakilisha karibu kila kona ya jiji la Dar es Salaam.Kitu kingine nilichobaini ni kwamba jinsi gani wasanii wanavyotumika katika masuala ya muhiu kwa Taifa.

Nakumbuka niliwahi kusoma katika gazeti moja la huko nyumbani kwamba msanii Juma Nature “alimfunika” mwenyeji wake-mgombea aliyemwalika msanii huyo katika kampeni zake.Yaani watu walikuwa na kiu zaidi ya kusikia muziki wa Nature kuliko hotuba ya mheshimiwa huyo.Na pengine umati kubwa uliojitokeza kwenye mkutano huo ulifuata buridani hiyo ya bure.Yayumkinika kusema kuwa mchango wa wasanii katika kufanikisha uchaguzi,na hata kuwapatia ushindi baadhi ya wagombea,ulikuwa mkubwa.Kwa bahati mbaya,au pengine kwa makusudi,baada ya kukamilisha kazi ya kuhamasisha jamii kuhusu uchaguzi na wagombea,wasanii wetu wamerudi kulekule walikokuwa:wamesahauliwa na wanaendelea kunyonywa.

Napenda kuwafumbua macho wasanii wetu kwa kuwaambia kuwa muziki wao huku guhaibuni unauzika sana miongoni mwa watu waliotoka Afrika Mashariki.Wamuulize Banana Zorro aliyealikwa hapo London kwenye pati ya Muungano,wamuulize Mr Nice,Ray C na TID,na Profesa J ambaye nasikia amewachengua vilivyo huko Sweden na Holland.Wasanii wa nyumbani wakija huku wanababaikiwa kama vile akina Shaggy au Sean Paul wanavyobabaikiwa wakija huko nyumbani.Lakini,safari za nje sio jambo la kukurupuka tu,ni kitu kinachotaka maandalizi.Kwa mantiki hiyo si lazima kusafiri ili kunufaika na kazi za sanaa bali hata kutafuta namna ya kupenyeza muziki katika soko la kimataifa kunaweza sana kuwainua wasanii wetu.Hivi wasanii wetu wanajua kuwa CD zao huku zinauzwa hadi paundi 10 (zaidi ya shs 24,000/=)?Nimesoma kwenye internet kwamba tarehe 12/06/2006 kampuni moja iitwayo Townsend Records itatoa CD iitwayo Bongoflava (Swahili Rap from Tanzania) ambayo itauzwa paundi 10.99 (takriban shs 27,000/= kwa exchange rate za leo).Sijui kama na hawa ni wadosi au la,lakini huo ni uthibitisho kuwa Bongoflava ina soko zuri tu kuhu Ughaibuni.Na watu wanapenda kweli kazi za wasanii wa nyumbani.Niliporudi kutoka Tanzania jamaa zangu kibao walikuwa wananiulizia kama nimekuja na CD za Bongofleva.Kila mmoja anasema wanaposikia wasanii wetu wanakumbuka sana nyumbani.

Mheshimiwa Kikwete alinukuliwa akiwataka Watanzania walioko nje kuwasaidia wenzao walio nyumbani hasa katika nafasi za masomo.Ujumbe huo unaweza pia kupanuliwa na kuwahusisha wasanii wa nyumbani,kwa maana kuwa Watanzania walio nje hasa wale wenye upeo na mambo ya muziki wawasaidie wasanii wetu wa nyumbani kwa namna yoyote ile inayowezekana.Lakini ili hilo liwezekane wasanii wetu hawana budi “kuchangamka.”Wanaoitwa “wadosi” wanawanyonya na kuwaibia kwa vile wanajua dhahiri kuwa wasanii hao hawana njia mbadala.Jamani,dunia siku hizi imekuwa kama kijiji (japo ni kinadharia) na unachohitaji ni kwenda tu kwenye internet cafĂ© na kuperuza kurasa za mtandao kujua wapi unaweza kupata huduma au kuuza ulichonacho kwa mtu aliye bara jingine.Hapa ndipo umuhimu wa shule (elimu) unapojidhihirisha.Lakini hata kama shule haipandi,si unaweza kumwomba rafiki yako akusaidie kutafuta soko la kazi zako za sanaa nje ya nchi?

Serikali inapaswa kuwasaidia wasanii wetu kwa kuipa meno sheria ya hatimiliki.Sambamba na hilo ni wasanii wenyewe kusimama kidete kutetea maslahi yao badala ya kuendelea kulalamika au kufikiria kuingia kwenye fani nyingine kukwepa wizi wa kazi zao.Pia wasione aibu kuomba msaada kwa wenzao walio nje.Mwisho naiomba serikali ipanue vita dhidi ya wala rushwa na majambazi na kujumuisha “wadosi” pia.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI

Mambo yakoje huko nyumbani?Natumaini kila mmoja anawajibika kwa namna yake katika ujenzi wa Taifa.

Kuna jamaa mmoja hapa anaitwa David Cameron.Huyu ni kiongozi wa chama cha wahafidhina (Conservative Party).Nia yangu si kuzungumzia wasifu wake,bali nataka nimlinganishe na mwanasiasa nyota wa huko nyumbani kwa muda huu,au kwa lugha ya “kwa mama” tunaweza kumuita “a man of the moment.” (kwa tafsiri ya haraka, “staa wa muda huu”).Nadhani msomaji mpendwa umeshajua ni nani ninayemzungumzia.Lakini hapa namuweka kando kidogo ili nikupashe kuhusu huyo Bwana Cameron na chama chake cha Conservatives (au Torry,kama kinavyojulikana hapa).Kwa tafsiri nyepesi hawa Conservatives ni watu wenye mrengo wa kulia na ndio wapiga kelele wakubwa kuhusu sera za uhamiaji na nyinginezo ambazo zinawagusa makabwela hususan wale ambao si wazawa wa hapa.Pengine jeuri kubwa ya wahafidhina hawa inatokana na uwezo wao wa kifedha.Fedha wakati mwingine huwa na tabia ya kumfanya binadamu asiwafikirie wenzie aliowazidi kiuwezo,na aghalabu anapowafikiria basi huwa ni kwa manufaa yake binafsi.

Kuibuka kwa Cameron kulichochewa zaidi na mwelekeo usioridhisha wa chama chake katika chaguzi mbalimbali.Wachambuzi wengi wa mambo ya siasa walikuwa wanahusisha mwenendo mbaya wa chama hicho na kile kinachoitwa kuwa “out of touch.”Nitafafanua.Chama kilicho “out of touch” ni kile ambacho machoni mwa watu wa kawaida kinaonekana kama hakijihusishi na maslahi ya walio wengi.Kwa mfano,hawa wahafidhina kwa miaka kadhaa wamekuwa wakikumbatia zaidi Waingereza weupe hasa wale wa tabaka la juu na la kati huku wakiwasahau wale wa tabaka la chini pamoja na Waingereza wengine ambao ni “wakuja” (kwa mfano wale wenye asili ya Asia,Caribbean,Afrika,n.k).Pia wamekuwa wakiwaona wageni (ikiwa ni pamoja na wanafunzi wanaochangia mamilioni ya paundi kwenye uchumi wa nchi hii) kama watu wanaokuja kuharibu uchumi,utamaduni na mazingira ya hapa.

Baada ya Waziri Mkuu wa mwisho kutoka Conservative kushika wadhifa huo,John Major,alipoangushwa na Tony Blair mwaka 1997,chama hicho kimebadilisha viongozi kadhaa lakini bila mabadiliko hayo kuwanufaisha kwenye chaguzi mbalimbali.Ndipo katika mchakato huo alipoibuka Bwana Cameron,kijana (ana miaka 40 tu),ana mvuto na haiba ya kutosha.Huyo bwana aliamua kuwapa wenzake kitu “laivu” kwamba chama chao hakina mvuto kwa wapiga kura,kinaonekana kuwa kiko zaidi kwa maslahi ya mabwanyenye kuliko makabwela,na hakizungumzi “lugha ya mtu wa kawaida mtaani.”Kuna mengi ya kumzungumzia huyo bwana lakini kilichonisukuma kuandika makala hii ni jinsi navyomuona anafanana na Jakaya Kikwete.Ukiachilia ukweli kwamba wote ni handsome lugha wanayoongea inafanana:lugha inayomgusha mtu wa kawaida na sio makundi flani tu katika jamii hususan wale wenye nguvu za kiuchumi.

Jakaya amenukuliwa mara kadhaa akiwausia viongozi wenzie kwamba wako madarakani kuwahudumia hao waliowaweka madarakani.Sio dhambi kuwa karibu na matajiri lakini ukaribu huo usiwe kwa ajili ya kuwaumiza wasio nacho.Utajiri sio dhambi,na kuna matajiri kadhaa (mfano Mzee Mengi huko nyumbani au Bill Gates huko Marekani) ambao utajiri wao umekuwa faraja kwa mamilioni ya wale wasio nacho.Matajiri wa aina hii ni muhimu kwao kuwa karibu na viongozi wa serikali,vyama vya siasa na taasisi nyingine kwa vile ni kwa ukaribu huo ndio miradi mbalimbali wanayoifadhilia inaweza kuwa na manufaa kwa wananchi.

Juzijuzi nilimwona Bwana Cameron kwenye luninga akiwa kwenye mtaani wakati wa kampeni za chama chake kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kwa upande wa England.Jinsi alivyokuwa akijichanganya na watu ilitosha kabisa kumfanya hata mtu aliyekuwa akikichukia chama cha wahafidhina afikirie upya.Siku chache baadae nikasoma kwenye mtandao kuwa Jakaya ameweka historia kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kutembelea wafungwa magerezani.Yalipotokea mauaji ya kutatanisha ya wale wachimba madini wa Mahenge hakukawia kuunda tume,na kinyume ya ilivyozoeleka mara baada ya kupewa ripoti na tume akaweka matokeo hadharani.Aliporejea tu kutoka Kusini mwa Afrika hakukawia kwenda kuwaona majeruhi wa tukio la uporaji wa fedha za NMB pale Ubungo,na kutoa maagizo papo hapo.Lakini si Jakaya pekee bali hata “luteni” wake Lowassa.Ghorofa lilipoanguka Keko hakusubiri kuletewa taarifa bali alikwenda kujionea mwenyewe na kuchukua hatua hapohapo, “mafuriko” yalipoielemea Sinza hakukawia kwenda kushuhudia hali ilivyo na kuwaamuru wahusika wachukue hatua za haraka.

Laiti kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya aliyokuja nayo Kikwete itaweza kufikia hatua ya kuigwa na viongozi kuanzia ngazi ya serikali ya mtaa,kata,tarafa,wilaya na mkoa,basi muda si mrefu Bongo itakuwa sehemu ya neema.Na mwenyewe Jakaya amekuwa akisema kuwa Tanzania yenye neema inawezekana.Enyi viongozi mliolala hebu amkeni,msisubiri kuamshwa.Jisikieni aibu pale mnapokwenda kinyume na spidi ya kiongozi wenu mkuu.

Alamsiki

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.