11 Mar 2011


Hivi kwanini watawala wetu wanaogopa sana maandamano?Wakati mchecheto ulioikumba Serikali ya Rais Jakaya Kikwete na CCM yake (kutokana na maandamano ya amani ya Chadema) haujaisha,gazeti la Mwananchi linaripoti kuwa askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) wamezuia maandamano ya wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari jijini Dar es Salaam

Soma habari kamili hapa chini:

KIKOSI cha Kutuliza Ghasia cha Jeshi la Polisi (FFU) jana kilitawanya maandamano ya wanafunzi wa baadhi ya shule za msingi na sekondari za Mkoa wa Dar es Salaam waliokuwa wakielekea Ikulu kupinga ongezeko jipya la nauli za daladala.

Kundi la kwanza la wanafunzi hao lilijikusanya katika Viwanja vya Mnazi Mmoja majira ya mchana na kuanza maandamano hayo yaliyokuwa na lengo la kumfikishia ujumbe Rais Jakaya Kikwete wa kutoridhishwa na ongezeko hilo la nauli. Kundi jingine la wanafunzi lilianzia maandamano hayo katika Uwanja wa Karume.

Mwandishi wa habari hii alipofika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja aliwakuta wanafunzi hao wakijipanga kuanza maandamano hayo huku wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali. Baadhi ya mabango hayo yalisomeka: ‘Kama ni maji ya pilipili, hayawezi kuwa suluhisho la migomo.’

Baadhi ya wanafunzi walisema wameamua kupinga nauli hiyo mpya kwa maandamano ili kuishinikiza serikali iifute wakitaka kurejeshwa kwa ile ya zamani ya Sh100 ili kuwapunguzia mzigo wazazi wao kuwasomesha.
“Sisi wengine kwa siku tunapanda magari matatu hadi kufika shule na hapo bado hujala. Sasa kwa hali hii kweli tutasoma?" Alihoji mmoja wa wanafunzi hao.

Mwanafunzi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Habib Juma alisema nauli ya Sh150 kwa mwanafunzi ni kubwa mno kuimudu akisema kipato cha wazazi wengi ni duni na baadhi yao wanashindwa hata kutoa michango mbalimbali ya shule.

Hata hivyo, jitihada za wanafunzi hao kufikisha ujumbe wao Ikulu ziligonga mwamba baada ya kudhibitiwa na FFU muda mfupi tu baada ya kuingia barabarani.Askari hao waliokuwa na pikipiki walitanda barabarani na kuwatawanya wanafunzi hao na baadaye waliwashikilia wanafunzi wawili wa kiume baada ya wenzao kukimbia. Wanafunzi hao walipakiwa kwenye gari la polisi na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Msimbazi.

Nauli hizo mpya za daladala zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), wiki iliyopita zilianza kutumika rasmi jana.Ofisa Mfawidhi wa Sumatra katika Kanda ya Dar es Salaam, Conrad Shio alisema nauli hizo zimegawanywa katika makundi matatu kwamba wanafunzi watatozwa Sh150 kwa safari, kundi la pili ni njia zenye nauli moja ya Sh300 na la tatu ni la njia zenye nauli zaidi ya moja na kwamba nauli hizo zimeongezeka kwa Sh50 katika nauli za awali, katika kila safari moja.

Shio alitoa mfano akisema kwa njia ambayo abiria wake walikuwa wanatozwa nauli ya Sh250 kwa safari, sasa watatozwa Sh300.Alisema katika Kanda ya Mashariki nauli ya juu zaidi itakuwa Sh1,700 kwa safari kati ya Kigamboni na Pembamnazi, eneo ambalo awali nauli yake ilikuwa Sh1,300.

Sumatra imeongeza nauli hizo baada ya kupokea maombi ya wamiliki wa mabasi mwishoni mwa mwaka jana wakilalamikia kupanda kwa gharama za uendeshaji.

ANGALIZO: Ubabe huzaa ubabe.Kama watawala wetu wanadiriki kutumia ubabe hadi kwa wanafunzi wa shule za msingi na serikali,basi tukae tukijua kuwa tulipo na tuendako si salama.Maandamano ni haki ya msingi ya kila mwananchi alimradi hayahatarishi amani.Hivi kuna ugumu gani kwa askari kutoa escort kwa waandamanaji hadi watapowasilisha ujumbe wao kunakohusika na kisha kuwasihi warejee makwao kwa amani?

Hizi ni dalili za wazi za udikteta kwa kisingizio cha kulinda amani na utulivu.

10 Mar 2011

Katika makala yangu ndani ya jarida mahiri la Raia Mwema toleo la wiki hii nimechambua hotuba ya Rais Kikwete ya mwisho wa mwezi Machi.Lakini pamoja na makala hiyo na nyinginezo zilizoandikwa na magwiji wa uchambuzi,pia kuna habari mbalimbali zinazohusu kila kada ya jamii

BONYEZA HAPA kusoma makala hiyo.

7 Mar 2011


On behalf of my readers I would like to wish a very happy birthday to a fellow blogger,Faith Charles Hillary a.k.a Candy.She is just one of those people you feel quite privileged to have known.She might be in her early 20s but her knowledge and blogging skills are supremely amazing.


Here is a little "gift" for you.

.


Kwa siku kadhaa sasa kumekuwa na taarifa kuwa Mchungaji mmoja mstaafu huko Monduli,mkoani Arusha anatoa tiba ya Ukimwi kwa gharama nafuu ya shilingi 500.Inaelezwa kuwa maelfu kwa maelfu ya watu wamekuwa wakimiminika kwa Mchungaji huyo Ambilikile Mwasakile kujipatia tiba ya gonjwa hilo hatari .

Japo kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa Ukimwi unadhibitika kwa sasa kutokana na uvumbuzi wa dawa zenye ufanisi zaidi katika kudhibiti athari za ugonjwa huo,tiba rasmi haijapatikana.Hata hivyo,ukweli huu haumaanishi kuwa tiba ya Mchungaji Mwasakile ni feki kwa vile hadi sasa hakuna mtu au taasisi iliyopinga madai yake.

Pia,huwezi kuwashangaa maelfu ya watu wanaofurika kwa Mchungaji huyo kusaka tiba.Kama malaria tu inawafanya watu wakimbilie mahospitalini,sembuse waathirika wa Ukimwi!

Lakini kama kichwa cha habari kinavyohoji,ukimya wa Wizara ya Afya na serikali kwa ujumla kuhusu madai hayo unaweza kuzua zahma kama ile ya upatu maarufu wa DECI.Katika sakata hilo la "kupanda mbegu",watumishi kadhaa wa Mungu walifanikiwa kuhamasisha maelfu kwa maelfu ya Watanzania "kupanda mbegu" zao kwa matarajio ya kuvuna mamilioni.Sote tunajua kilichofuata.

Serikali ilikuwa ikifahamu uwepo wa DECI lakini haikuchukua hatua stahili (kuruhusu au kuharamisha) hadi pale ilipozinduka na kupiga marufuku upatu huo,hatua iliyowaacha wananchi lukuki wakiwa wamepoteza fedha zao "za ngama".

Sasa japo katika suala hili la tiba ya ukimwi,malipo ni shilingi 500 tu,unyeti wa suala hilo na faida au athari zake unalazimisha serikali kutoa kauli rasmi.Tunafahamu ombwe kubwa la uongozi linaloikabili serikali yetu lakini si kwa kiwango cha kushindwa kusema lolote kuhusu suala hili "dogo" japo linaloweza kuwa na athari kubwa kwa jamii.

Hivi kwa mfano tiba ya Mchungaji huyo ni feki,je hiyo haitoathiri watu wanaoweza kusitisha matibabu ya dawa za kudhibiti virusi vya Ukimwi (ARVs?Serikali yoyote yenye kujali watu wake inapaswa kutoa kauli ya mwongozo kwa wananchi wake kuhusu ukweli au uongo wa madai hayo ya kupatikana kwa tiba ya ukimwi.

Japo kujaribu kuhalalisha au kupinga madai hayo si kazi nyepesi,mazingira yafuatayo yanaweza kutoa mwanga japo kidogo:

Kwanza,katika imani za kidini,kuna uwezekano kwa binadamu kujaliwa karama za kufanya miujiza.Nadhani baadhi ya wasomaji wanafahamu kazi za watu kama Father Nkwera na yule mama wa Mikocheni (anadhani alikuwa anaitwa Esther kama sikosei).Kadhalika,wengi wetu tumesikia miujiza ya Sheikh Shariff.

Pili,kuna watu wanaoaminika kuwa na uwezo wa kutibu maradhi mbalimbali kwa kutumia tiba za asili.Katika ukoo wetu,kuna ndugu yangu mmoja ambaye amekuwa akitoa tiba za asili katika eneo la Kiberege huko Morogoro.Kila nilipokuwa namtembelea nilikuwa nashuhudia namna anavyotibu watu wenye matatizo mbalimbali,ya kiafya na kimaisha.Hata hivyo,hapo kwenye "zahanati" yake kuna tangazo kuwa yeye hana uwezo wa kutibu ukimwi.

Tatu,ni rahisi kuzusha jambo na likaaminika miongoni mwa wengi.Na kama jambo lenyewe ni habari njema basi si ajabu "waaminifu" wa awali wakasambaza habari hizo "njema" na kupelekea tetesi zisizo na ukweli kupata uaminifu.Waingereza wana msemo kwamba uongo usipokemea unaishia kupata hadhi ya kuwa ukweli.Sasa ikitokea kuwa madai ya Mchungaji huyo si ya kweli,lakini hakuna anayekanusha,basi madai hayo yanaweza kuchukua hadhi ya "ukweli".

Kinachonipa wasiwasi ni kauli ya Mchungaji Mwasakile kuwa alianza kutoa matibabu hayo mwezi Agosti mwaka jana baada ya kuoteshwa na Mungu.Kwa maana hiyo,kuna watu kadhaa ambao wanaweza kuwa mashuhuda wa ufanisi wa dawa anazotoa kwa wagonjwa wake.Kwanini habari hizo hazikufahamika hadi majuzi,inabaki kuwa muujiza kama habari yenyewe ya tiba.

Pengine unaweza kusema si rahisi mtu kutapeli kwa kutoza shilingi 500 tu.Lakini ukifanya hesabu za chap chap utagundua kuwa laiti wagonjwa 2000 tu wakilipa kiwango hicho,Mchungaji atakuwa ametengeneza shilingi milioni moja.Na kwa mujibu wa taarifa za idadi ya watu wanaoelekea kwa Mchungaji huyo,yawezekana ameshachuma shilingi milioni kadhaa hadi sasa.


Ni mapema mno kubaishiri lolote kuhusu madai hayo.Kwa upande mmoja tiba kwa nguvu za kiroho au dawa asilia inawezekana,japo sina hakika kama ukimwi nao unatibika kwa njia hizo.Lakini,again,katika Mungu yote yanawezekana.

Serikali inaweza kuwasaidia Watanzania kwa kutoa tamko rahisi kuhusu madai hayo.Na licha ya ombwe la uongozi linaloikabili serikali yetu,suala hili linaweza kuwa rahisi zaidi hasa kwa vile taarifa zinaeleza kuwa vigogo kadhaa wameonekana wakielekea kwa Mchungaji huyo kwenda kujipatia tiba.Hawa wanaweza kuwa mashuhuda wazuri katika suala hilo.


Wakati jamii inasubiri uthibitisho wa madai ya Mchungaji huyo ni vema kubaki na msimamo rasmi wa kitabibu kuwa ukimwi hauna tiba.Na kwa waliokwishapewa "tiba" ya Mchungaji huyo,ni muhimu kwao kufanya vipimo vya kitaalamu kuthibitisha kama kweli wamepona.Na kama wakipona basi iwe fundisho kwao badala ya "kurejesha libeneke kwa kasi mpya,nguvu mpya na ari mpya"

Picha zote kwa hisani ya Michuzi

Kwa habari na picha zaidi soma hapa kwa Miss Jestina

5 Mar 2011


Tunaposema kuna ombwe la uongozi kwenye Serikali ya Rais Jakaya Kikwete baadhi ya vichwa panzi wanatuita wachochezi.Sasa unapoona Waziri anauchapa usingizi kwenye mkutano wa kimataifa,huku bosi wake akiwa kando,basi sijui tusemeje!!!

Na tunaposema Kikwete ni kiongozi dhaifu sio kama ni uchochezi,majungu au chuki binafsi.Hivi kama Rais anashindwa kumkemea Waziri wake kwa kulala kwenye mkutano tunaoambiwa una umuhimu mkubwa kwa nchi yetu (hadi imelazimu mkuu wa nchi aende mwenyewe badala ya kuwakilishwa na Makamu wake,Waziri Mkuu au Waziri wa Nishati na Madini)atamudu vipi kukemea wabaka uchumi ambao baadhi yao ni watu wake wa karibu waliochangia harakati zake za kuukwaa Urais?

Na kuna umuhimu gani kwa fedha ya walipa kodi kugharamia safari ya Ngeleja ambaye anaishia kulala mkutanoni badala ya kutuwakilisha?Au Kikwete amelazimika kwenda mwenyewe badala ya kumwacha Ngeleja pekee kwa vile alijua kuwa waziri wake huyo ataishia kuuchapa usingizi mkutanoni?

Kutegemea watu wa aina hii wanaweza kumsaidia Mtanzania kuondokana na umasikini wa kutupa ni sawa na kutegemea kugema damu kwenye jiwe.Na ukiona waziri mzima pasi haya anachapa usingizi huku Rais wake akiwa kando basi ujue wazi kuwa si akina Richmond na Dowans tu waliomudu kutuingiza mkenge bali tutarajie mengi zaidi.Unadhani kama Ngeleja anathubutu kuuchapa usingizi katika mkutano wa kimataifa unaouhusu maslahi ya nchi,hali inakuwaje wakati anashughulikia maslahi ya nchi ofisini mwake?Sintoshangaa kusikia kuna mikataba ya kuhamisha madini yetu ikisainiwa huku waziri yuko fofofo usingizini

Au Ngeleja ameanzisha mashindano ya kuchapa usingizi dhidi ya Mbunge wa CCM Kapteni John Komba,ambaye kama inavyoonekana pichani chini,alifumwa akiwakilisha wapiga kura wa jimbo lake kwa kuchapa usingizi Bungeni Dodoma



Picha kwa hisani ya Jamii Forums


JINA LA BLOG: MBEYA YETU
Tunapenda kulitambulisha wadau wote libeneke jipya la Mbeya Yetu ambapo nia na malengo ni kuwaletea habari mbali mbali kutoka Jijini Mbeya, Tanzania na Duniani kwa Ujumla ikiwa unatukio la aina lolote usisite kututumia kupitia [email protected] . karibuni nyote na asanteni kwa kututembelea.

Kwa pamoja tunaweza.
.

Karibuni sana wadau.


The Sporah Show itakuwa hewani leo Jumamosi mnamo saa saba mchana (1300hrs) katika kituo cha televisheni cha Star (STAR TV) huko nyumbani Tanzania. Endelea.

2 Mar 2011

Makala yangu katika toleo la wiki hii la jarida mahiri la habari na uchambuzi la Raia Mwema inazungumzia ombwe la uongozi wa Kikwete,na namna ombwe hilo linavyojidhihirisha katika namna tukio la milipuko ya mambomu huko Gongo la Mboto linavyoshughulikiwa.

 BONYEZA HAPA KUSOMA MAKALA HIYO pamoja na habari na makala nyingine zilizokwenda shule.

28 Feb 2011

Baadhi ya Watanzania wanaoishi hapa Uingereza waliendesha harambee ya kuchangia wahanga wa milipuko ya mabomu huko Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam. Picha za harambee hiyo katika mji wa Reading.

                                       Left to Right: JJ, Chisumo, Ms Jestina, Gardol na Frank

                                                      Frank na Ms Jestina
  Ms Jestina

                                                            
                                                       Mdau akichangia
Mkurugenzi wa Locus Impex Shipping,B. Chisumo akifungua harambee

                                  Mtoto Shanelle akimpa mchango Ms Jestina


                                                    Toa ndugu ikiendelea

Shughuli ikiendelea
Wadau

26 Feb 2011


Yayumkinika kuhisi kuwa laiti Baba wa Taifa angefufuka leo huenda angeishia kutoa machozi.Taifa alilohangaika na wenzie kulipigania uhuru limegeuka kituko.Upande mmoja tunamwona Rais wetu akijibidiisha kusaka amani Ivory Coast ilhali wakazi wa Gongo la Mboto wanaporwa amani na usalama wao na wazembe wa Jeshi la Wababaishaji Tanzania...ooops,I meant Jeshi la Walipua mabomu...oh,not again.Nilitaka kuandika Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).Kwa upande mwingine ni ziara ya haramia wa Dowans ambaye licha ya kukimbia ukombozi wa Wazanzibari baada ya Mapinduzi amemudu kututapeli,kabla ya kuja kutuhubiria namna ya kuzalisha umeme,na kukumbushia fidia anayopaswa kulipwa kwa kututapeli!

Huku baadhi yetu tukizidi kusononeshwa na namna ombwe la uongozi linavyozidi kufidiwa kwa vitendo vya ufisadi,tunashuhudia eneo jingine ambalo lilisaidia sana kuifanya Tanzania ya Nyerere iheshimike kwa msimamo wake thabiti.Hapa nazungumzia sera za nje za nchi yetu.

Baada ya Mwalimu kung'atuka na nafasi yake kurithiwa na watu ambao kama Urais ni somo basi kwao halikuwemo kwenye silabasi (maana angalau anayepata zero anakuwa amesoma lakini hakufaulu),nchi yetu imegeuka kichekesho linapokuja suala la msimamo wetu kama taifa huru.

Na ukidhani naandika haya kama uzushi basi soma habari hii inayoeleza kuwa Tanzania imeogopa kutoa msimamo wake kuhusu uanaharamu wa dikteta Muamar Ghaddafi dhidi ya wananchi wake wanaodai mabadiliko nchini Libya.


Kwa mujibu wa habari hiyo,Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa Bernard Membe amedai kuwa


Tanzania kama nchi haiwezi kujitokeza wazi wazi kuunga mkono ama kupinga kinachotokea nchini humo kwa sababu ina raia wake wanaoishi huko hivyo kitendo chochote cha kushabikia kwa kuunga mkono ama kupinga kinahatarisha maisha yao.




Katika habari hiyo,Membe amenukuliwa akisema:
Unajua tuna raia wetu kule sasa siyo vizuri kuonyesha utashi wetu inaweza kuhatarisha maisha ya wananchi wetu kwani hii ilitokea kule Misri kwa wale waliojitokeza kuunga mkono waliweza kushambuliwa na kuharibiwa biashara zao

Ungetegemea Membe angejaribu angalau kuficha ombwe katika sera yetu ya nje kwa angalau kudanganya kama mwanadiplomasia kwamba "tunafuatilia kwa karibu matukio ya nchini Libya na tuko katika mchakato wa kuweka bayana msimamo wetu".

Yaani Membe anataka kutuzuga kwamba laiti Tanzania ikilaani unyama wa Ghaddafi dhidi ya raia wake basi kiongozi huyo wa Libya atalipa kisasi kwa kuwadhuru Watanzania 26 (kwa mujibu wa takwimu zake) waliopo nchini humo?

Kichekesho ni kwamba serikali ya CCM ambayo Membe ni miongoni mwa Waziri wake ilimudu kulaani "vurugu zilizosababishwa na Chadema huko Arusha" (ilhali waliopaswa kulaaniwa ni polisi wanaoamini katika ubabe kama wa Ghaddafi) japokuwa kuna Watanzania waliouawa na kujeruhiwa ni Watanzania pia (pamoja na raia mmoja wa Kenya).

Labda nitoe mfano bora zaidi.Hivi wakati Nyerere alipoweka wazi msimamo wake dhidi ya Makaburu wa Afrika Kusini hakukuwa na maslahi yoyote ya Tanzania katika nchi hiyo?Au,je tulipoamua kukabiliana na nduli Idi Amini hakukuwa na Mtanzania huko Uganda?

Ukweli ulio bayana ni kwamba si Membe wala bosi wake Kikwete wenye uthubutu wa kulaani unyama unaofanywa na Ghaddafi.Na si ajabu wanaombea afanikiwe kuteketeza raia wake na kubaki madarakani kisha wajipendekeze kwa kupitisha bakuli huko.

Lakini kwa upande mwingine kumlaumu Membe katika hili ni sawa na kumtaka mwanafunzi wa chekechea aandike thesis kuhusu mada ngumu kama Quantum Physics.Hivi kwa watu wanaoshindwa japo kumkemea mwarabu Adawi anayeifanya nchi yetu kama darasa la majaribio ya kudalilisha uhuru wa taifa,na badala yake wanampa fursa ya mwaliko hapo Ikulu kukutana na Makamu wa Rais (bila kusahau dokezo lake kuwa asipigwe picha),wataweza vipi kumudu mambo mazito kama uhusiano wa kimataifa?

Unapoona kiongozi wa nchi anashindwa kuwawajibisha Waziri wa Ulinzi Dkt Hussein Mwinyi,Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange,na wazembe wote waliogeuza makazi ya raia yaliyo jirani na kabi za jeshi kuwa viwanja vya mazoezi ya kulipua mabomu,basi ni wazi kumtegemea aongoze vema nchi katika masuala ya kimataifa ni sawa na kutarajia damu kutoka kwenye jiwe.

Mwinyi,Mkapa na sasa Kikwete wamefanikiwa sana kuifuta Tanzania kutoka katika nafasi yake kama taifa lenye msimamo na uongozi dhidi ya tawala dhalimu,mfano wa kupigiwa mstari ukiwa nafasi ya Tanzania katika mapambano ya ukombozi Kusini mwa Afrika.

Katika stadi za siasa tunafundishwa kwamba sera imara ya mambo ya nje inategemea sana uimara katika sera za mbalimbali za ndani ya nchi.Sasa kwa mwenendo huu ambapo Taifa letu lipo katika hatari ya kugeuzwa koloni binafsi la mafisadi ambao wanarahisishiwa azma hiyo na uongozi dhaifu wa Kikwete (anayechelea kuwaudhi maswahiba zake wanaoliingiza mkenge taifa letu),itakuwa ni njozi za mchana za mtu mwenye njaa kutegemea nchi hii irejee zama za Mwalimu ambapo tulimudu kujitengenezea heshima kubwa kutokana na misimamo thabiti na isiyoendekeza kujikomba,uoga,unafiki au ubabaishaji.

Kwa mwenendo huu,nalazimika kuafikiana na kauli za Sheikh Yahya kuwa nchi yetu inaweza kukumbwa na mabalaa makubwa huko mbeleni (japo nawalaumu waandishi wa habari walioshindwa kumhoji mnajimu huyo kuhusu utabiri wake kwamba mtu yeyote ambaye angejitokeza kugombea dhidi ya Kikwete katika uchaguzi mkuu uliopita angekufa).


Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.