8 Apr 2016

MOJA ya masuala yanayotawala anga za habari na mijadala mbalimbali mtandaoni ni uamuzi wa Bodi ya Taasisi ya Changamoto ya Milenia (Millennium Challenge Corporation - MCC) ya Marekani kusitisha misaada kwa Tanzania.
Sababu kuu mbili zilizotolewa na bodi hiyo kuhusu uamuzi huo ni marudio ya uchaguzi huko Zanzibar Machi 20, mwaka huu, ambao licha ya kususiwa na chama kikuu cha upinzani cha CUF, ulilalamikiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya nchi wahisani, ikiwa ni pamoja na Marekani.

Sababu ya pili, kwa mujibu wa bodi hiyo, ni uamuzi wa Serikali ya Tanzania kupitisha Sheria Uhalifu wa Mtandaoni (Cybercrime Act) ya mwaka 2015 licha ya upinzani mkali dhidi ya muswada wa sheria hiyo, iliyotafsiriwa kuwa imelenga kukandamiza uhuru wa habari na haki za binadamu.

Kabla ya kuingia katika uchambuzi huu kiundani, nieleze mtazamo wangu kuhusu sababu hizo mbili zilizotolewa na Bodi ya MCC. Kwanza, kwa mtazamo wangu, suala la marudio ya uchaguzi wa Zanzibar ni mzaha wa kidemokrasia. Haihitaji uelewa mkubwa wa siasa za Zanzibar kufahamu kuwa kuna ‘sheria isiyo rasmi’ kuwa ‘kamwe CUF hawapaswi kutawala Zanzibar.’

Bila kuuma maneno, hiyo ndiyo sababu pekee ya kufutwa kwa uchaguzi wa awali (ambao inadaiwa mgombea wa CUF, Seif Shariff Hamad, alishinda) na kuamriwa uchaguzi huo urudiwe huku CCM ikiwekeza nguvu zake zote kuhakikisha inashinda. Hata kama CUF wasingesusia uchaguzi huo, bado CCM wangeshinda kwa sababu ‘ni lazima iwe hivyo,’ kwa ‘kanuni’ zao.

Je, MCC ipo sahihi kutumia kigezo cha Zanzibar kusitisha misaada yao? Kwa upande mmoja, wapo sahihi. Kwa sababu, hata katika uhusiano wetu wa kawaida tu kibinadamu, anayekupa msaada anapata ruhusa pia ya ‘kukutawala’ kwa kukupa masharti ambayo ukiyakiuka, yanaweza kuathiri uhusiano kati ya mtoa msaada na mpokea msaada. Miongoni mwa masharti ya MCC ni pamoja na masuala ya demokrasia, na haihitaji kukuna kichwa sana kubaini kuwa marejeo ya uchaguzi wa Zanzibar, ambayo binafsi ninayaona kuwa ni mzaha wa kidemokrasia, yamewapa MCC ‘kisingizio chepesi’ hata kama hawangekuwa na sababu nyingine.

Mgogoro wa muda mrefu wa kisiasa huko Zanzibar ni zaidi ya jipu. Ni kansa ambayo imeshachafua sura ya Tanzania huko nyuma ambapo kwa mara ya kwanza tulizalisha wakimbizi baada ya vurugu za Uchaguzi mkuu mwaka wa 2000.

Ni kansa ambayo sasa imewapa MCC kisingizio cha kutunyima misaada yao. Kwa bahati mbaya au makusudi, hakuna utashi wa kisiasa wa kusaka ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo. Kila kiongozi wa CCM, kwa upande wa Bara, anaogopa suala hilo kwa kuhofia kuvunjikiwa na Muungano mikononi mwake.

Baadhi ya wanasiasa wa Zanzibar sio tu wanaufahamu udhaifu huo bali pia wanautumia vema. Wanaendesha siasa za chuki na uhasama watakavyo wakifahamu kuwa hakuna mwana-CCM wa Bara mwenye jeuri ya kuwaingilia.

Sina hakika Zanzibar itaathirika vipi kwa uamuzi wa MCC kukata misaada, lakini kinachowapa kiburi viongozi wa huko ni kwamba ‘Tanganyika’ haina jeuri ya kuisusa Zanzibar au kuinyooshea kidole katika mwendelezo wa siasa za chuki na ubaguzi.

Lakini kwa upande wa pili, hao MCC ni wanafiki tu. Huhitaji kuwa na uelewa mkubwa wa siasa za kimataifa kutambua unafiki wa Marekani linapokuja suala la demokrasia. Nchi hiyo ni mshirika mkubwa wa tawala za kidikteta kama vile huko Misri, Saudi Arabia na kwingineko. Sawa, labda Zanzibar wamefanya mzaha wa kidemokrasia lakini vipi kuhusu demokrasia isiyopo kabisa huko Saudi? Jibu rahisi ni kwamba Zanzibar na Tanzania sio muhimu sana kwa Marekani ilhali taifa hilo linazitegemea mno tawala za kibabe za nchi kama Misri au Saudi, hususan katika masuala ya ushushushu au mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa.

Kuhusu suala la Sheria ya Uhalifu wa Mtandao, hapa kumesheheni unafiki, na upo wa aina mbili. Kwanza, Wamarekani na pili ni Watanzania wenyewe. Binafsi ni mfuatiliaji wa karibu wa masuala ya usalama mtandaoni, ambao kwa namna moja au nyingine unahusiana na hiyo masuala ya Cybercrime Act.
Kwa kifupi tu, Marekani ina sheria kandamizi mno dhidi ya uhuru wa raia mtandaoni. Naamini umekwishasikia kuhusu jamaa anayeitwa Edward Snowden. Huyu bwana alikuwa mtumishi katika Shirika la Kijasusi la Marekani linalohusika na kunasa mawasiliano mbalimbali (NSA – National Security Agency) na baadaye nafsi yake ilimsuta, akaamua ‘kuingia mitini’ na kumwaga siri lukuki kuhusu jinsi NSA inavyohujumu haki za raia kimawasiliano. Hawa jamaa wamekuwa wakinasa mawasiliano ya takriban kila mtu, wakishirikiana kwa karibu na mashushushu wenzao wa hapa Uingereza, GCHQ, taasisi ya kishushushu inayohusika na kunasa mawasiliano.
Lakini hata tukiweka kando suala la NSA kunasa mawasiliano mbalimbali (waliwahi kuzua kasheshe kubwa baada ya mashushushu wa Ujerumani kubaini kuwa NSA walikuwa wakinasa kwa siri mawasiliano ya Kansela Angela Markel hadi waliposhtukiwa), mashambulizi ya kigaidi nchini humo mwaka 2001 yalisababisha kuundwa kwa sheria kali kabisa dhidi ya uhuru wa habari na haki za kibinadamu kwa kisingizio cha usalama wa taifa. Kwa hiyo, kwa kifupi, ni uhuni tu wa Marekani kudai Sheria ya Makosa ya Mtandaoni inakiuka uhuru wa Watanzania. Sheria zao za wazi na za kificho ni mbaya mara milioni zaidi yetu.

Hata hivyo, katika suala hili la Cybercrime Act, tuna wanafiki kadhaa huko nyumbani. Kwa kumbukumbu tu, nilikuwa mtetezi mkubwa wa muswada uliozaa sheria hiyo, yaani Cybercrime Bill, na niliunga mkono kwa nguvu zote jitihada za aliyekuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, kuhusu muswada huo.

Hata hivyo, baadhi ya watu ambao sasa wanailaumu Marekani na wafadhili wengine kuhusu suala la Tanzania kukatiwa misaada, walikuwa mstari wa mbele wakati huo kuziomba nchi wahisani ziingilie kati kuibana serikali ili muswada huo usipitishwe kuwa sheria. Sasa kama uamuzi huo wa Marekani umechangiwa na ‘kelele’ zao hizo, kwa nini leo wanalalamika?

Ninakerwa kuona kundi la wanafiki hawa likiilaumu MCC au Marekani au nchi nyingine wahisani kuhusu suala la kutukatia misaada, kwa sababu wao walikuwa mstari wa mbele kuhamasisha nchi wahisani zichukue hatua, na ‘hatua maarufu’ ya wahisani huwa ni kukata misaada. Badala ya kulalamika, wanafiki hawa wanapaswa kufanya sherehe maana dua zao zimetimia.

Sasa niangalie upande wa athari za uamuzi huo wa MCC kukata misaada. Tuwe wakweli, kwa watu masikini kama sisi, hatua yoyote ile ya kutupunguzia msaada wa aina yoyote ile itatuathiri. Hilo halihitaji uelewa wa jinsi gani misaada inavyofanya kazi au jinsi gani nchi yetu ilivyo “mtegemezi mzoefu wa misaada”.

Tatizo kubwa hapa kuhusu kukatiwa misaada kutatuathiri au hakutatuathiri ni tofauti zetu za kiitikadi. Kwa kiasi kikubwa, suala hilo linaangaliwa katika lensi ya u-CCM na u-Ukawa /Upinzani. Kwa wana-CCM, ni mwendo wa ‘kiburi’ kwenda mbele, kwamba “waende tu na misaada yao,” au “hela yenyewe ilikuwa ya mradi wa kifisadi wa Symbion,” mara “ah misaada gani hiyo yenye masharti kibao.” Wanamhadaa nani? Kama misaada hiyo haikuwa na umuhimu, kwa nini basi tuliiomba?

Kwa upande wa wana-Ukawa /Wapinzani, bila kujali kuwa wao kama Watanzania ni waathirika watarajiwa wa uamuzi huo wa nchi yetu kukatiwa misaada, wanakenua meno yote 32 kwa furaha, huku wakiwazodoa wenzao wa CCM kwa vijembe kama “...ndio matunda ya ubabe wenu huko Zanzibar, tuone sasa…” au “mtaisoma namba” au “mtakula jeuri yenu…”
Ulemavu huu wa kifikra unaosababishwa na kuliangalia suala la kiuchumi kwa mtizamo fyongo wa itikadi za kisiasa. Naam, suala la Zanzibar ni la kisiasa, lakini athari za uamuzi wa Marekani (MCC) wahisani ni la kiuchumi.


Mimi si mchumi lakini naelewa fika kuwa uchumi wetu umekuwa tegemezi tangu tupate uhuru. Kabla ya kuipa kisogo siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, tulikuwa tukipata misaada kutoka kwa marafiki zetu wa mrengo wa Ukomunisti. Baada ya kuzika Ujamaa, tumekuwa kama puto linaloyumbishwa na upepo, tupo radhi kumpigia magoti yeyote anayeweza kutusaidia. Kimsingi, tuna ombwe la kiitikadi: majukwaani, CCM wanasema sisi ni Wajamaa, vitendo vyetu havipo kwenye Ujamaa wala Ubepari, tupo tupo tu. Huo ndio ukweli mchungu kuhusu ubabaishaji wetu.

Kwa hiyo, tuache kudanganyana kuwa kukatiwa misaada hakutotuathiri. Huko ni kujipa jeuri tu. Tunachoweza kukubaliana ni kwamba suala hilo limekwishakutokea, tumekwishakatiwa misaada, na si ajabu wahisani wengine wakaamua kufuata mkumbo na kufanya hivyo pia.

Jukumu letu kubwa kwa sasa sio kuendelea kunyoosheana vidole bali tuwe kitu kimoja kama taifa bila kujali nani hasa aliyetusababishia tatizo hili. Ni tatizo la Watanzania wote bila kujali itikadi zao. Uamuzi wa wahisani kukata misaada utawaathiri wana-CCM wanaodai hautowaathiri kama ambavyo utawaathiri wana-CUF au Chadema wanaokenua meno yote 32 kufurahia hatua hiyo. Na utatuathiri (angalau kisaikolojia) hata sisi ambao itikadi yetu pekee ni Tanzania yetu. Huo ni ukweli usiopingika (we are all in this together).

Kuna mambo mawili ya kupigiwa mstari. Kwanza, kwa miaka mingi tumekuwa tukiishi kifahari mno kuliko uwezo wetu. Na kimsingi, uwezo wetu duni haukupaswa kuwepo kwani sisi si masikini hata kidogo. Tuna kila aina ya utajiri lakini kuna majambazi walioigeuza Tanzania yetu kuwa kitu cha kufisadiwa kila kukicha. Kila mwenye uelewa anafahamu kilichojiri katika takriban miaka 30 iliyopita. Tanzania yetu ilikuwa shamba la bibi, watu wanafisadi wapendavyo kiasi kwamba kuwa na uchungu na nchi ilionekana kama uwendawazimu.

Kwa bahati nzuri, Mwenyezi Mungu amesikia kilio cha baadhi yetu na sasa tumempata Rais, Dk John Magufuli, ambaye anaonekana amedhamiria kurekebisha mwenendo wa mambo. Kikwazo chetu kikubwa kilikuwa ufisadi, lakini sasa Magufuli ameamua kuvalia njuga kupambana na ufisadi kwa nguvu zote. Mwanzo ni mgumu lakini angalau dalili za mafanikio zimeanza kujionyesha. Tumuunge mkono, tuchukie ufisadi, tuongeze uzalendo, tuikwamue Tanzania yetu, tujikwamue nasi wenyewe, tuache kutafuta njia za mkato za mafanikio, tufanye kazi, tuache majungu na kusaka sifa za kijinga mitandaoni, tuwajibike.
Tunahitaji kujifunga mikanda. Haiwezekani wafadhili wetu waishi kimasikini ilhali sisi wafadhiliwa tunaishi kama matajiri. Viongozi wetu waache kuchuana na wauza unga kushindana jinsi ya kuishi kitajiri, wawabane wauza unga hao, majangili na maharamia wengine ili tuiokoe Tanzania yetu.

Je, tunaweza kujitegemea? Naam, lakini tusidanganyane kuwa tunaweza kufanya hivyo ghafla. Tukumbuke, mtoto hazaliwi na kisha akatembea. Tumekuwa wategemezi mno wa misaada kiasi kwamba tumesahau kuwa tunapaswa kujitegemea. Tunahitaji kuchukua na kukubali uamuzi mgumu wa kutuwezesha kujitegemea.

Jambo jingine, kwa hisia zangu, japo suala la Zanzibar na Cybercrime Act zinatajwa kama sababu za uamuzi wa kutunyima misaada, ninashawishika kuamini kuwa baadhi ya nchi wahisani hawapendezwi na kasi ya Rais Magufuli kuziba mianya ambayo kimsingi licha ya kuwanufaisha mafisadi wa ndani, ilikuwa pia inanufaisha taasisi za kifisadi za kimataifa

Wengi wa majambazi waliokuwa wakitupora fedha zetu walikuwa hawahifadhi fedha zao katika benki zetu bali zilizopo katika nchi za wahisani hao. Wanaweza kudhani huu ni utani mbaya, lakini jiulize, je kama unamfadhili mtu pesa za kumsaidia yeye na familia yake, lakini anatumia fedha hizo kufanya matumizi ya anasa, kwa nini usichukue hatua?
Mfano huo unamaanisha hivi: kwa nini wahisani wetu walionekana kutokerwa na jinsi pesa walizokuwa wanatupatia zikifisadiwa kila kukicha lakini wakaendelea kutumwagia misaada? Na kwa nini sasa, tumempata Magufuli ambaye amepania kwa dhati kupambana na ufisadi, wahisani wanaanza kuvaa sura ya ubabaishaji.

Kuna tunaodhani kuwa hao wahisani wanataka tuendelee kuwa wategemezi wao milele. Kwa upande mmoja utegemezi wetu unawapa uhuru wa kukwapua kila rasilimali tuliyonayo, na kwa upande mwingine, wananeemesha taasisi zao za fedha kwa vile mafisadi wetu wa ndani wanahifadhi fedha zao kwenye taasisi hizo.


Mwisho, tuache porojo, tuache unafiki, tuwe kitu kimoja, athari za kukatiwa misaada zipo, tukishikamana tutaweza kukabiliana nazo japo mwanzoni itakuwa ngumu. Yawezekana uamuzi huo wa Wamarekani ukawa ‘blessing in disguise’ kwa maana ya kutupa ‘wake-up call’ tuanze kujitegemea kwa lazima badala ya kutembeza bakuli letu huko na kule, kisha kile kidogo kinachopatikana kikaishia kwenye ujenzi wa mahekalu ya mafisadi, ongezeko la magari yao ya kifahari, na kutanua ukubwa wa nyumba ndogo zao.

Mungu ibariki Tanzania

1 Apr 2016

Moja ya masuala yanayotawala anga za habari na mijadala mbalimbali mtandaoni ni uamuzi wa bodi ya taasisi ya Changamoto ya Milenia (Millennium Challenge Corporation) ya Marekani kusitisha misaada kwa Tanzania. Sababu kuu mbili zilizotolewa na bodi hiyo kuhusu uamuzi huo ni marudio ya uchaguzi huko Zanzibar Machi 20, mwaka huu, ambao licha ya kususiwa na chama kikuu cha upinzani cha CUF, ulilalamikiwa kwa kiasi kikubwa na nchi wahisani, ikiwa ni pamoja na Marekani.

Sababu ya pili, kwa mujibu wa bodi hiyo, ni uamuzi wa serikali ya Tanzania kupitisha Sheria Uhalifu wa Mtandaoni (Cybercrime Act) ya mwaka 2015 licha ya upinzani mkali dhidi ya muswada wa sheria hiyo, iliyotafsiriwa kuwa imemlenga kukandamiza uhuru wa habari na haki za binadamu.

Kabla ya kuingia katika uchambuzi huu kiundani, nieleze mtazamo wangu kuhusu sababu hizo mbili zilizotolewa na bodi ya MCC. Kwanza, kwa mtazamo wangu, suala la marudio ya uchaguzi wa Zanzibar ni mzaha wa kidemokrasia, na ni jeraha la kisiasa ambalo historia inaweza kutuhukumu huko mbeleni. Haihitaji uelewa mkubwa wa siasa za Zanzibar kufahamu kuwa kuna ‘sheria isiyo rasmi’ kuwa ‘kamwe CUF hawapaswi kutawala Zanzibar.’ Bila kuuma maneno, hiyo ndo sababu pekee ya kufutwa kwa uchaguzi wa awali (ambao inadaiwa mgombea wa CUF, Seif Shariff Hamad, alishinda), na kuamiriwa uchaguzi huo urudiwe huku CCM ikiwekeza nguvu zake zote kuhakikisha inashinda. Hata kama CUF wasingesusia uchaguzi huo, bado CCM wangeshinda kwa sababu ‘ni lazima iwe hivyo,’ kwa ‘kanuni’ zao.

Je MCC ipo sahihi kutumia kigezo cha Zanzibar kusitisha misaada yao? Kwa upande mmoja, wapo sahihi. Kwanini? Kwa sababu, hata katika mahusiano yetu ya kawaida tu kibinadamu, anayekupa msaada anapata ruhusa pia ya ‘kukutawala’ kwa kukupa masharti ambayo ukiyakiuka, yanaweza kuathiri mahusiano katika ya mtoa msaada na mpokea msaada. Miongoni mwa masharti ya MCC ni pamoja na masuala ya demokrasia, na haihitaji kukuna kichwa sana kubaini kuwa marejeo ya uchaguzi wa Zanzibar, ambayo binafsi ninayaona kuwa ni mzaha wa kidemokrasia, yamewapa MCC ‘kisingizio chepesi’ hata kama hawangekuwa na sababu nyingine.

Mgogoro wa muda mrefu wa kisiasa huko Zanzibar ni zaidi ya jipu. Ni kansa ambayo imeshachafua sura ya Tanzania huko nyuma ambapo kwa mara ya kwanza tulizalisha wakimbizi baada ya vurugu za uchaguzi mkuu mwaka wa 2000. Ni kansa ambayo sasa imewapa MCC kisingizio cha kutunyima misaada yao. Kwa bahati mbaya, au makusudi, hakuna utashi wa kisiasa wa kusaka ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo. Kila kiongozi wa CCM, kwa upande wa Bara, anaogopa suala hilo kwa kuhofia ‘kuvunjikiwa na Muungano mikononi mwake.’

Wanasiasa wa Zanzibar sio tu wanaufahamu udhaifu huo bali pia wanautumia vema. Wanaendesha siasa zao cha chuki na uhasama watakavyo wakifahamu fika kuwa hakuna mwana-CCM wa Bara mwenye jeuri ya kuwaingilia.

Sina hakika Zanzibar itaathirika vipi kwa maamuzi ya MCC kukata misaada, lakini kinachowapa kiburi viongozi wa huko ni kwamba ‘Tanganyika’ haina jeuri ya kuisusa Zanzibar, au kuinyooshea kidole katika mwendelezo wa siasa za chuki na ubaguzi.

Lakini kwa upande wa pili, hao MCC ni wanafiki tu. Huhitaji kuwa na uelewa mkubwa wa siasa za kimataifa kutambua unafiki wa Marekani linapokuja suala la demokrasia. Nchi hiyo ni mshirika mkubwa wa tawala za kidikteta kama vile huko Misri, Saudi Arabia na kwingineko. Sawa, labda Zanzibar wamefanya mzaha wa kidemokrasia lakini vipi kuhusu demokrasia isiyopo kabisa huko Saudi? Well, jibu rahisi ni kwamba Zanzibar na Tanzania sio muhimu ‘kihivyo’ kwa Marekani ilhali taifa hilo linazitegemea mno tawala za kibabe za nchi kama Misri au Saudi, hususan katika masuala ya ushushushu/mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa.

Kuhusu suala la Sheria ya Uhalifu wa Mtandao, hapa kumesheheni unafiki, na upo wa aina mbili: wa Wamarekani na wa sie Watanzania wenyewe. Mie ni mfuatiliaji wa karibu wa masuala ya usalama mtandaoni, ambao kwa namna moja au nyingine unahusiana na hiyo ishu ya Cybercrime Act. Kwa kifupi tu, Marekani ina sheria kandamizi mno dhidi ya uhuru wa raia mtandaoni. Naamini ushaskia kuhusu jamaa anayeitwa Edward Snowden (kama hujamsikia, Wasiliana na Google…haha). Huyu bwana alikuwa mtumishi katika shirika la ushushushu la Marekani linalohusika na kunasa mawasiliano mbalimbali (NSA – National Security Agency), na baadaye nafsi yake ilimsuta, akaamua ‘kuingia mitini’ na kumwaga siri lukuki kuhusu jinsi NSA inavyohujumu haki za raia kimawasiliano. Hawa jamaa wamekuwa wakinasa mawasiliano ya takriban kila mtu, wakishirikiana kwa karibu na mashushushu wenzao wa hapa Uingereza, GCHQ, taasisi ya kishushushu inayohusika na kunasa mawasiliano.

Lakini hata tukiweka kando suala la NSA kunasa mawasiliano mbalimbali (waliwahi kuzua kasheshe kubwa baada ya mashushushu wa Ujerumani kubaini kuwa NSA walikuwa wakinasa kwa siri mawasiliano ya Kansela Angela Markel hadi waliposhtukiwa), mashambulizi ya kigaidi nchini humo mwaka 2001 yalipelekea kuundwa kwa sheria kali kabisa dhidi ya uhuru wa habari na haki za kibinadamu kwa kisingizio cha usalama wa taifa. Kwahiyo, kwa kifupi, ni uhuni tu wa Marekani kudai Sheria ya Makosa ya Mtandaoni inakiuka uhuru wa Watanzania. Sheria zao za wazi na za kificho ni mbaya mara milioni zaidi yetu.

Hata hivyo, katika suala hili la Cybercrime Act, tuna wanafiki kadhaa huko nyumbani. Kwa kumbukumbu tu, mie nilikuwa mtetezi mkubwa wa muswada uliozaa sheria hiyo, yaani Cybercrime Bill, na niliunga mkono kwa nguvu zote jitihada za aliyekuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, kuhusu muswada huo.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanaoinyooshea kidole Marekani na wafadhili wengine kuhusu suala la Tanzania kukatiwa misaada walikuwa mstari wa mbele kuziomba nchi wahisani ziingilie kati kuibana serikali ili muswada huo usipitishwe kuwa sheria. Sasa kama uamuzi huo wa Marekani umechangiwa na ‘kelele’ zao hizo, kwanini leo wanalalamika?

Mie niliunga mkono muswada na sheria hiyo kwa sababu ikitumiwa vema ni nzuri. Hebu nenda Instagram kaangalie uanaharamu unaoendelea huko, kuanzia picha za uchi, ushoga na kila aina ya laana. Huo sio uhuru wa habari, ni uwendawazimu ambao kwa hakika ulihitaji sheria kali kuudhibiti.

Na watu waliopita huku na kule kudai sheria hiyo ni kandamizi na ililenga kuwabana wananchi wasiwasiliane, hawatuambii kama baada ya sheria hiyo kupitishwa wameshindwa kuwasiliana na watu wengine. Kwa kifupi, kulikuwa na udanganyifu mkubwa katika kambi ya waliopinga muswada na sheria hiyo. Walitumia uelewa mdogo wa wananchi wengi kuhusu masuala ya mtandao, na kuwajenga hofu feki.

Ninakerwa kuona kundi la wanafiki hawa likiilaumu MCC au Marekani au nchi nyingine wahisani kuhusu suala la kutukatia misaada, kwa sababu wao walikuwa mstari wa mbele kuhamasisha nchi wahisani zichukue hatua, na ‘hatua maarufu’ ya wahisani huwa ni kukata misaada. Badala ya kulalamika, wanafiki hawa wanapaswa kufanya sherehe maana wishes zao zimetimia.

Sasa niangalie upande wa athari za uamuzi huo wa MCC kukata misaada. Taarifa nyingine zinaeleza kuwa kuna wahisani wengine nao wamekata misaada japo kuna mkanganyiko kama hatua hiyo ni mwendelezo wa hatua za huko nyuma au ni mpya.

Tuwe wakweli, kwa watu masikini kama sisi, hatua yoyote ile ya kutupunguzia msaada wa aina yoyote ile itatuathiri. Hilo halihitaji uelewa wa jinsi gani misaada inavyofanya kazi au jinsi gani nchi yetu ilivyo mtegemezi mzoefu wa misaada. Tatizo kubwa hapa kuhusu “kukatiwa misaada kutatuathiri au hakutatuathiri” ni tofauti zetu za kiitikadi. Kwa kiasi kikubwa, suala hilo linaangaliwa katika lensi ya u-CCM na u-UKAWA/Upinzani. Kwa wana-CCM, ni mwendo wa ‘kiburi’ kwenda mbele, kwamba “waende tu na misaada yao,” au “hela yenyewe ilikuwa ya mradi wa kifisadi wa Symbion,” mara “ah misaada gani hiyo yenye masharti kibao.” Wanamhadaa nani? Kama misaada hiyo haikuwa na muhimu, kwanini basi tuliiomba in the first place? Hizi hadithi za sungura kusema “sizitaki ndizi hizi” baada ya kushindwa kuzikia mgombani.

Kwa upande wa wana-UKAWA/Wapinzani, bila kujali kuwa wao kama Watanzania ni wahanga watarajiwa wa uamuzi huo wa nchi yetu kukatiwa misaada, wanakenua meno yote 32 kwa furaha, huku wakiwazodoa wenzao wa CCM kwa vijembe kama “ndio matunda ya ubabe wenu huko Zanzibar, tuone sasa…” au “mtaisoma namba” au “mtakula jeuri yenu…”

Ulemavu huu wa kifikra unaosababishwa na kuliangalia suala la kiuchumi kwa mtizamo fyongo wa itikadi za kisiasa. Naam, suala la Zanzibar ni la kisiasa, lakini athari za uamuzi wa Marekani/MCC/wahisani ni la kiuchumi.

Mie sio mchumi ila ninachoelewa fika kuwa uchumi wetu umekuwa tegemezi tangu tupate uhuru. Kabla ya kuipa kisogo siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, tulikuwa tukapata misaada kutoka kwa marafiki zetu wa mrengo wa Ukomunisti. Baada ya kuuzika Ujamaa, tumekuwa kama puto linaloyumbishwa na upepo, tupo radhi kumpigia magoti yeyote anayeweza kutusaidia. Kimsingi, tuna ombwe la kiitikadi: majukwaani, CCM wanasema sie ni Wajamaa, vitendo vyetu havipo kwenye Ujamaa wala Ubepari, tupu tupo tu. Huo ndo ukweli mchungu kuhusu ubabaishaji wetu.

Kwahiyo, tuache kudanganyana kuwa kukatiwa misaada hakutotuathiri. Huko ni kujipa jeuri tu. Tunachoweza kukubaliana ni kwamba suala hilo limeshatokea, tumeshakatiwa misaada, na si ajabu wahisani wengine wakaamua kufata mkumbo na kufanya hivyo pia.

Jukumu letu kubwa kwa sasa sio kuendelea kunyoosheana vidole bali tuwe kitu kimoja kama taifa bila kujali nani hasa aliyetusababishia tatizo hili. Ni tatizo la Watanzania wote bila kujali itikadi zao. Uamuzi wa wahisani kukata misaada utawaathiri wana-CCM wanaodai hautowaathiri kama ambavyo utawaathiri wna-CUF au Chadema wanaokenua meno yote 32 kufurahia hatua hiyo. Na utatuathiri (angalau kisaikolojia) hata akina sie ambao itikadi yetu pekee ni Tanzania yetu. Huo ni ukweli usiopingika: we are all in this together.

Kuna mambo mawili ya kupigiwa mstari. Kwanza, kwa miaka mingi tumekuwa tukiishi kifahari mno kuliko uwezo wetu. Na kimsingi, uwezo wetu duni haukupaswa kuwepo kwani sie sio masikini hata kidogo. Tuna kila aina ya utajiri lakini kuna majambazi walioigeuza Tanzania yetu kuwa kitu cha kubakwa kila kukicha. Kila mwenye uelewa anafahamu kilichojiri katika takriban miaka 30 iliyopita. Tanzania yetu ilikuwa shamba la bibi, watu wanafisadi wapendavyo kiasi kwamba kuwa na uchungu na nchi ilionekana kama wendawazimu.

Kwa bahati nzuri, Mwenyezi Mungu amesikia kilio cha baadhi yetu na sasa tumempata Rais, Dkt John Magufuli, ambaye anaonekana amedhamiria kurekebisha mwenendo wa mambo. Kikwazo chetu kikubwa kilikuwa ufisadi, lakini sasa Magufuli ameamua kuvalia njuga kupambana na ufisadi kwa nguvu zote. Mwanzo ni mgumu lakini angalau dalili za mafanikio zimeanza kujionyesha. Tumuunge mkono, tuchukie ufisadi, tuongeze uzalendo, tuikwamue Tanzania yetu, tujikwamue nasi wenyewe, tuache kutafuta njia za mkato za mafanikio, tufanye kazi, tache majungu na kusaka sifa za kijinga mitandaoni, tuwajibike.

Twahitaji kujifunga mikanda. Haiwezekani wafadhili wetu waishi kimasikini ilhali sie wafadhiliwa twaishi kama matajiri. Viongozi wetu waache kuchuana na wauza unga kushindana jinsi ya kuishi kitajiri, wawabane wauza unga hao, majangili na maharamia wengine ili tuiokoe Tanzania yetu.

Je twaweza kujitegemea? Absolutely, lakini tusidanganyane kuwa twaweza kufanya hivyo ghafla ghafla. Tukumbuke, mtoto hazaliwi akatembea. Tumekuwa wategemezi mno wa misaada kiasi kwamba tumesahau kuwa twapaswa kujitegemea. Twahitaji kuchukua na kukubali maamuzi magumu ya kutuwezesha kujitegemea. Ni kama kumlazimisha mtoto anayetambua aanze kutembea kwa nguvu. Sio rahisi, lakini tukimkazania anaweza kusimama mwenyewe na baadaye akaweza hata kukimbia. Hilo linahitaji kujitoka mhanga kwa ajili ya nchi yetu, sambamba na kuweka mbele uzalendo badala ya maslahi binafsi.

Jambo jingine, kwa hisia zangu, japo suala la Zanzibar na Cybercrime Act zinatajwa kama sababu za uamuzi wa kutunyima misaada, ninashawishika kuamini kuwa baadhi ya nchi wahisani hawapendezi na kasi ya Rais Magufuli kuziba mianya ambayo kimsingi licha ya kuwanufaisha mafisadi wa ndani, ilikuwa pia inanufaisha taasisi za kifisadi za kimataifa. Wengi wa majambazi waliokuwa wakitupora fedha zetu mchana kweupe walikuwa hawahifadhi fedha zao katika benki zetu bali zilizopo kwa hao wahisani wetu. Waweza kudhani huu ni utani mbaya, lakini jiulize, je kama unamfadhili mtu pesa za kumsaidia yeye na familia yake, lakini anatumia fedha hizo kununulia bling bling, kuongeza nyumba ndogo, kufanya matumizi ya anasa, nk kwanini usichukue hatua?

Mfano huo unamaanisha hivi: kwanini wahisani wetu walionekana kutokerwa na jinsi pesa walizokuwa wanatupatia zikifisadiwa kila kukicha lakini wakaendelea kutumwagia misaada? Na kwanini sasa, tumempata Magufuli ambaye amepania kwa dhati kupambana na ufisadi, wahisani wanaanza kuleta ‘longolongo’?

Kuna tunaodhani kuwa hao wahisani wanataka tuendelee kuwa wategemezi wao milele. Kwa upande mmoja utegemezi wetu unawapa uhuru wa kukwapua kila raslimali tuliyonayo, na kwa upande mwingine, wananeemesha taasisi zao za fedha kwa vile mafisadi wetu wa ndani wanahifadhi fedha zao kwenye taasisi hizo.

Mwisho, tuache porojo, tuache unafiki, tuwe kitu kimoja, athari za kukatiwa misaada zipo, tukishikamana tutaweza kukabiliana nazo japo mwanzoni itakuwa ngumu. Yawezekana uamuzi huo wa Wamarekani ukawa ‘blessing in disguise’ kwa maana ya kutupa ‘wake-up call’ tuanze kujitegemea kwa lazima badala ya kutembeza bakuli letu huko na kule, kisha kile kidogo kinachopatikana kikaishia kwenye ujenzi wa mahekalu ya mafisadi, ongezeko la magari yao ya kifahari, na kutanua ukubwa wa nyumba ndogo zao.

MUNGU IBARIKI TANZANIA 

Baada ya kada wa muda mrefu wa CCM, Balozi Juma Mwapachu kutangaza kurudi CCM baada ya kukihama chama hicho tawala wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, aliyekuwa mpigadebe maarufu wa mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA, Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye, ametangaza kujiunga tena na chama hicho tawala.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kuna uwezekano wa wana-UKAWA wengine, mgombea wa kiti cha urais, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na aliyekuwa kada mkongwe Kingunge Ngombale Mwiru, kufuata mkumbo wa Balozi Mwapachu na Sumaye, ambapo tetesi zinadai kuwa wanaweza kutangaza kurejea CCM muda wowote kuanzia sasa.

Kwa habari kamili na picha, BONYEZA HAPA

25 Mar 2016

HATIMAYE baada ya vuta nikuvute ya muda mrefu, Zanzibar ilifanya marudio ya uchaguzi wake Jumapili iliyopita na Dk. Ally Mohamed Shein kushinda kiti cha urais kwa asilimia takriban 91.

Bila ‘kuuma maneno,’ uchaguzi huo ni mzaha wa kidemokrasia. Ni mzaha kwa sababu ingewezekana kabisa kutofanya marudio ya uchaguzi huo na matokeo ya sasa – yaani CCM kushinda – yakabaki kuwa yale yale.


Yayumkinika kuhitimisha kuwa upande unaoshikilia madaraka visiwani humo umedhamiria kwa dhati kuwa upande pinzani kamwe hautoruhusiwa kutawala, kwa amani au kwa shari.

Kwa lugha nyepesi, ‘piga ua’ chama cha CUF hakitoruhusiwa kutawala Zanzibar hata kama kitashinda uchaguzi kwa asilimia 99. Na tunapozungumzia asilimia ya ushindi, ni vigumu mno kwa sasa kwa chama chochote visiwani humo kupata ushindi mkubwa wa kukipa uhalali wa kutosha kutawala, sababu kuu ikiwa ni mgawanyiko sugu kati ya Waunguja na Wapemba.


Wengi wetu tunachukizwa na kinachoendelea Zanzibar lakini yaelekea hakuna mwenye uwezo wa kushauri nini kifanyike. Nami ninaangukia katika kundi hilo. Sababu za kihistoria zimeendelea kuitesa Zanzibar miaka nenda miaka rudi. Tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi, visiwa hivyo vimeendelea kugawanyika kiitikadi kwa misingi ya Upemba (CUF) na Uunguja (CCM).

Japo inaweza kutopendeza kutumia mfano huu, lakini yayumkinika kulinganisha siasa za Zanzibar na mgogoro kati ya Wapalestina na Wayahudi. Kikubwa kinachowaogopesha Waisraeli kukubali amani ya kudumu na Wapalestina ni hofu ya kisasi.

Kwa bahati mbaya, siasa za chuki na ubaguzi visiwani Zanzibar nazo zinajenga mazingira hayo ya hofu, kwamba laiti ‘Wapemba wa CUF’ wakiingia madarakani watalipiza kisasi.

Na hoja hiyo inazidi kuchochewa na ukweli kwamba kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu visiwani humo na unaofumbiwa macho na vyombo vya dola, huku kila upande ukitupa lawama kwa wapinzani wake.

Inapotokea waathirika wa siasa za chuki kukamatwa na kudhalilishwa wakiwa rumande, ni wazi watoto na wajukuu zao watabaki na chuki ya muda mrefu, chuki ambayo huko mbele sio tu itazidisha uhasama bali pia yaweza kuzua balaa kubwa.

Tukirejea kwenye uchaguzi huo wa Jumapili iliyopita, nimeeleza hapo awali kuwa ‘mshindi anajulikana’ kabla haya ya kupigwa kura kwa sababu zilizo wazi. Kwanza, CUF kilishatangza msimamo wake kususia uchaguzi huo. Kwa maana hiyo, asilimia kubwa ya waliopiga kura ni wana-CCM, ambao ni dhahiri wamekipigia kura chama chao.


Kwa kuzingatia kanuni ya demokrasia ya wengi wape, ushindi wa CCM utakuwa halali kwa vile wapigakura wengi wamekipigia chama hicho. Lakini wengi hapo haimaanishi Wazanzibari wote kwa ujumla bali wengi kwa maana ya wana-CCM.


Pili, hata kama CUF wasingewakataza wafuasi wao kushiriki uchaguzi huo, ni wazi kuwa CCM ingefanya kila iwezalo – na ina uwezo mkubwa tu – kuhakikisha kuwa CUF haiibuki na ushindi. Hicho, kimsingi, ndicho kilichosababisha kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Hali hiyo haipendezi lakini ndio hali halisi. Ni ukweli mchungu, lakini ukweli una sifa kuu moja: uwe mchungu au mbaya unabaki kuwa ukweli. Ingependeza kuona Wapemba na Waunguja wakiungana kwa maslahi ya Zanzibar lakini hilo si rahisi kwa sasa.


Ugumu wa kuzungumzia siasa za Zanzibar unachangiwa na ukweli kwamba sio rahisi japo kushauri nini kifanyike angalau kupunguza migogoro isiyokwisha ya kisiasa visiwani humo.

CCM wakishindwa, CUF watasusia matokeo. Hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu mpaka zifanyike jitihada mpya za kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Kibaya zaidi, mtu pekee anayewezesha uwepo wa serikali ya umoja wa kitaifa ni mgombea wa kudumu wa urais kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Shariff Hamad. Hata jitihada zilizofeli za kutatua mgogoro uliosababisha kurudiwa uchaguzi huo zilitegemea zaidi jitihada za Seif.

Je, hali itakuwaje iwapo Seif akiondoka kwenye ulingo wa siasa? Lakini hata kama ataendelea kuwepo, je, wafuasi wa CUF wataendelea kumvumilia milele kila atakapojaribu kutafuta mwafaka kwa kukubali serikali ya umoja wa kitaifa? Hatari inayomkabili Seif kwa kuwa msuluhishi wa kudumu ni uwezekano wa yeye kuonekana msaliti miongoni mwa wafuasi wa chama chake.

Lakini ukweli kwamba Seif ni miongoni mwa viongozi wa zamani wa kitaifa, na hivyo kuwa mnufaika wa stahili mbalimbali kutoka serikalini unaweza kumkwaza kuelemea zaidi maslahi upande wa chama chake. Tumeshuhudia majuzi jinsi serikali ilivyogharimia matibabu yake. Sasa busara kidogo tu zapaswa kutukumbusha kuwa ni vigumu kwa mtu kukata mkono unaomlisha.

Baadhi yetu tunadhani hakukuwa na haja ya kupoteza fedha sio tu kurudia uchaguzi huo bali hata kufanya uchaguzi mwezi Oktoba mwaka jana kwa sababu imekwishakuwa kama kanuni ya siasa za Zanzibar kuwa lazima mshindi wa urais atoke CCM.


Sasa kuna haja gani ya kupoteza fedha kwa ajili ya mchakato ambao hautabadili chochote? Sawa, demokrasia ina gharama zake lakini gharama nyingine zinaepukika.

Nihitimishe makala hii kwa kubashiri kwamba jitihada zikifanyika, Zanzibar itapata tena serikali ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo, mwaka 2020 visiwa hivyo vitajikuta kwenye hali tata kama iliyojiri katika kila chaguzi katika mfumo wa vyama vingi.


Ningetamani sana kuhitimisha makala hii na ushauri wa nini cha kufanya lakini ninatambua bayana kuwa njia pekee (na isiyofaa) ni CUF kuendelea kuvumilia ubabe wa CCM katika kila uchaguzi, na kukubali kushiriki katika serikali ya umoja wa kitaifa (ikiundwa). Lakini njia hiyo (ukitoa serikali ya umoja wa kitaifa) ndio sababu kuu ya mgogoro huo wa kudumu wa kisiasa huko Zanzibar. Na kama tunavyofahamu sote, tatizo haliwezi kutatuliwa na tatizo jingine.


18 Mar 2016

NIANZE makala hii kwa kuomba radhi kutokana na safu hii kutochapishwa wiki iliyopita. Hali hiyo ilitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.

Miongoni mwa mada zinazotawala katika mijadala mbalimbali ya Watanzania hususan katika mitandao ya kijamii ni pamoja na suala linalofahamika kama ‘Kiingereza cha Rais John Magufuli.’ Mjadala huo umepamba moto zaidi kwenye mitandao ya kijamii ya Jamii Forums na Facebook. Mjadala huo ulianza rasmi baada ya kikao cha wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo hotuba ya Rais Magufuli ilizua hoja kuwa ‘Kiingereza chake kina kasoro.’ 

Kama Mtanzania mwenye makazi hapa Uingereza, nchi ambayo ndio ‘wenyeji wa Kiingereza,’ na ambaye kwa sasa ninafundisha kundi la watafiti (profesa mmoja, wahadhiri saba na wanafunzi wa shahada ya uzamivu wanane) wanaotarajia kuja huko nyumbani kwa ajili ya utafiti, nimeguswa sana na mjadala huo. 

Kwanza tuweke rekodi sawa. Kimsingi, Kiingereza alichoongea Rais Magufuli kinakubalika. Sawa, kinaweza kuwa sio timilifu lakini moja ya ‘siri’ za kuongea lugha ya kigeni, ikiwa ni pamoja na Kiingereza kwetu, ni uwezo wa kueleweka.

Pili, bila kuonekana ninamtetea Rais Magufuli, ni muhimu tukumbuke kuwa asili yake kitaaluma ni mwanasayansi. Na japo si kila mwanasayansi anasumbuliwa na Kiingereza, sio jambo la kushangaza kukutana na Wanasayansi ambao hawamudu Kiingereza vizuri. Hii inatokana na ukweli kuwa masomo yao sio ya lugha, na Kiingereza wanachotumia ni cha kitaalamu zaidi kuliko cha maongezi ya kawaida. 

Lakini tatu, na hili ni la muhimu zaidi, Kiingereza sio lugha yetu ya asili. Katika hili nitoe mfano ufuatao. Nilipoombwa kufundisha kundi hilo la watafiti wanaotarajia kuja huko nyumbani, awali nilidhani ni kundi la wanafunzi wa shahada ya uzamifu pekee. Kwa hiyo, licha ya ukweli kwamba sijafundisha darasani kitambo, nilijipa matumaini kuwa jukumu lililo mbele yangu sio gumu sana kwa vile nitakuwa nafundisha wanafunzi pekee.

Hata hivyo, kabla ya kuanza kufundisha kozi hiyo, nilipatiwa orodha ya ‘wanafunzi’ wangu, ambapo kwa mshangao, ilijumuisha profesa na wahadhiri kadhaa (wahitimu wa shahada ya uzamivu ambao miongoni mwao wapo wanaofanya kitu kinachojulikana kama ‘post-doctorate.’) Kwa hiyo, kule kujiamini kwangu kwa awali kuliyeyuka ghafla kwani kumfundisha mwanafunzi ni suala moja, lakini kumfundisha mhadhiri, hususan huyo profesa, ni shughuli pevu. 

Lakini mkuu wa idara inayohusika na ufundishaji wa kozi za lugha za kigeni alinipa maneno haya ya kutia moyo; “…bila kujali kuna profesa na wahadhiri, wewe ndiye mwalimu wao. Uprofesa na uhadhiri ni kwenye fani zao, lakini katika Kiswahili hao wote ni wanafunzi wako.” Hiyo ilinipa moyo, na kozi hiyo imekuwa ikiendelea kwa ufanisi mkubwa.

Lengo la mfano huo ni kuonyesha kuwa linapokuja suala la lugha ya kigeni, Haijalishi fulani ni kiongozi wa nchi au profesa, kwa sababu ni watu wachache tu wanaomudu vilivyo lugha zisizo zao. Hao ‘wanafunzi’ wangu ni wasomi waliobobea katika fani zao, lakini hawajui Kiswahili japo cha kuombea maji. Na huwezi kuwalaumu kwa sababu lugha hiyo ni ngeni kwao.

Kuna kasumba moja inayokera sana kuhusu baadhi ya ‘wasomi’ wetu wa Kitanzania, ambapo kuongea Kiingereza kunawafanya wajione wapo daraja la juu zaidi ya wasiomudu vema lugha hiyo au wasioiongea kabisa. Kwa sisi wengine ambao tunaamka, tunashinda, na tunakwenda kulala huku tunasikia Kiingereza, tunakerwa na mazingira ambapo unakutana na Mswahili mwenzako, badala ya kukupatia fursa mwanana ya kuongea naye lugha yetu ya asili, anatumia Kiingereza.

Ni kasumba iliyoshamiri mno kwenye mitandao ya kijamii ambapo baadhi ya wenzetu hawataki kabisa kuzungumza Kiswahili. Mara kadhaa nimekuwa nikiwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa sijawahi kuwaona Waingereza wakifanya maongezi kwa lugha ya kigeni labda iwe ni kwa minajili ya kujifunza tu. Tena kimsingi, Waingereza wanashutumiwa vikali na wenzao wa nchi mbalimbali za Ulaya kwa kupuuza lugha nyingine na kuiendekeza lugha yao.

Tofauti na sisi, wenzetu Wakenya wapo mahiri sana katika kukienzi na kukiendeleza Kiswahili. Kwa hapa Uingereza, Wakenya wengi wanajihusisha na shughuli za utafsiri wa Kiswahili kwenda Kiingereza au kinyume chake, kwa sababu wanamudu vema lugha zote mbili. Lakini kubwa zaidi ni mapenzi yao kwa Kiswahili, licha ya ukweli kuwa Kiswahili chetu Watanzania ni bora zaidi cha majirani zetu hao.

Ni nadra kwa hapa kukutana na Mkenya akazungumza nawe kwa Kiingereza. Atajikakamua hivyo hivyo na Kiswahili ‘chao’ lakini la muhimu mtaweza kuelewana. Sasa sisi Kiingereza chenyewe ni mgogoro mkubwa, lakini watu wapo radhi kujikakamua, na wengine kutokwa macho kama mjusi aliyebanwa na mlango, ili tu waongee ‘kimombo.’ Kwani wakizungumza Kiswahili wanapungukiwa na nini hasa?

Nimeambiwa kuwa katika hotuba yake kwenye dhifa ya kumkaribisha Rais wa Vietnam, Troung Tang Sang, Rais Magufuli alihutubia kwa Kiswahili. Nadhani huo ni mwanzo mzuri, na ninamsihi aendelee kuenzi lugha yetu ya taifa kwa sababu tusipoienzi sisi ‘wamiliki,’ ni dhahiri itapuuzwa na wengineo.

Inakadiriwa kuwa Kiswahili kinazungumzwa na takriban watu milioni 50 duniani. Ni lugha ya kimataifa. Wenye jukumu kubwa la kukienzi, kukiendeleza na kukitangaza ni Watanzania ambao kimsingi ndio tunaozungumza Kiswahili fasaha zaidi ya wenzetu wengine katika nchi kama Kenya, Uganda au Burundi.

Nimalizie makala hii kwa kuhitimisha kuwa pengine ‘lawama’ hizo zinazoelekezwa kwa Rais Magufuli kwa ‘Kiingereza chake’ zinaweza kuleta kitu Waingereza wanaita ‘blessing in disguise,’ yaani pale kitu kisichopendeza kinapoleta matokeo chanya. Kwa mfano, iwapo ‘lawama’ hizo zitasababisha Rais wetu sio tu kutumia zaidi Kiswahili katika matukio ya kimataifa bali pia kuhamasisha matumizi ya lugha yetu hiyo ya taifa.

Tukumbuke, mkataa asili yake ni mtumwa.

17 Mar 2016


Nilianza kumsikia Balozi Mwapachu tangu nikiwa mtoto mdogo. Huyu ni miongoni mwa yale majina ambayo miaka nenda miaka rudi utayasikia, kama sio kwenye uwaziri basi ni kwenye ukurgenzi wa taasisi flani, au uongozi wa tume flani kama sio ubunge. Wenzetu hawa ni kama watu waliozaliwa ili kuwa viongozi. Lakini hio sio dhambi wala kosa, maana yawezekana kuzeekea kwao katika uongozi ni matokeo ya uongozi wao wa kupigiwa mstari.

Hold on, nimesema 'uongozi wa kupigiwa mstari'? May be, maana dunia hii tunayoishi sasa hata sifa za uognzi hazijulikani ni zipi. Na sababu ya wazi ya sifa za uongozi kupoteza maana yake ni ubabaishaji, usanii,ufisadi, ujambazi, na kila baya unaloweza kulihusisha na tasnia ya uongozi.

Sie wengine tulikulia zama za chama kimoja. Tulishuhudia uongozi uliotukuka wa Mwalimu Nyerere. Ndio, kulikuwa na kasoro zake, kama vile viongozi kuonekana kama miungu-watu, lakini hawakuonekana miungu-watu kwa sababu ya utajiri wao bali angalau waliutumikia umma kwa namna moja au nyingine.

Tuliwaona viognozi mashambani, tuliwaona wakishiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa, matengenezo ya barabara, ushiriki katika ujenzi wa miradi ya maendeleo, na vitu kama hivyo. Kumbuka, enzi hizo tulikuwa nchi ya ujamaa na kujitegemea, na miongoni mwa features za kujitegemea ilikuwa kutumia raslimali zetu, sio siku hizi zama za kutembeza bakuli kwa wafadhili, kisha kinachopatikana 'kinapigwa panga,' watu wanaporomosha mahekalu, wanaongeza idadi za magari yao ya kifahari, na sensa ya nyumba ndogo zao inazidi kukua.

Kwanini nimeandika 'kwa hasira' hivi? Jana nimesikia kituko kilichonichefua. Mmoja wa Watanzania wenye majina makubwa katika medani za uongozi, Balozi Juma Mwapachu, jana alitangaza kurejea CCM baada ya kukihama chama hicho tawala wakati tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Kama nilivyosema awali, nimekuwa nikimsikia Juma Mwapachu tangu nikiwa mdogo. Lakini, mwaka jana nilipata fursa ya kuwasiliana nae. Sio uso kwa uso bali kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter. Sijui tulikuwa tunajadili nini lakini moja ya ajenda iliyojitokeza ni sapoti yake kwa Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, ambaye baadaye aliteuliwa kuwa mgombea Urais kwa tiketi ya UKAWA. 

Balizo Mwapachu alijitokeza kuwa miongoni mwa watetezi wakuu wa Lowassa, huku nyakati kadhaa akitukumbusha 'yeye ni nani.' Wapo walioungana nae mkono lakini baadhi yetu tulimpinga waziwazi na kueleza bayana kuwa ni 'wazee' kama yeye walioifikisha Tanzania yetu mahali hapa pasipoeleweka. Baadaye akapotea mtandaoni, pengine kwa sababu 'wazee' kama yeye hawajazowea sana 'mbinde' za social media.

Alipotangaza kuachana na CCM na kumfuata Lowassa, halikuwa jambo la kushangaza kwa sie tuliowahi kushuhudia akimtetea huko Twitter. Baada ya kuhama CCM akajitahidi kutumia uweledi wake kueleza, kwanza kwanini CCM ni 'kimeo,' na pia kwanini Lowassa ndio ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili Tanzania. Baadhi ya aliyoyasema yalikuwa na ukweli, lakini baadhi yetu hatukumuelewa kwa sababu moja tu: "alikuwa wapi siku zote hizo?" Yaleyale ya akina Lowassa, Kingunge, Sumaye na wengineo waliogeuka wakosoaji wakubwa wa mfumo walioshiriki kuuasisi huko CCM, mfumo wa wateule wachache huku mamilioni ya walalahoi wakiishia kuahidiwa hili kama sio lile.

Sasa jana akaamua kubadili gea angani, akatangaza kurudi CCM. Good, kuhama sio dhambi. Tatizo la msingi ni baadhi ya sababu alizoeleza kuwa zilimpelekea kuhama CCM na sasa kuamua kurejea.

Anadai 'alilewa' na ahadi ya Lowassa kuwa angepewa Uwaziri wa Mambo ya Nje. Hivi inaingilia akilini kweli kwa mtu kama huyo ambaye alikuwa miongoni mwa 'vijana wa Nyerere' kuhama chama alichokiasisi baba wa taifa kwa sababu tu alitarajia kupewa uwaziri wa mambo ya nje? Pengine sio kosa kwa sababu ni watu wangapi wasiotaka madaraka?

Lakini ili umuelewe vema ni muhimu kurejea posts zake mbalimbali huko Facebook na kwingineko alivyokuwa akiwahadaa vijana kuhusu ajenda ya mabadiliko. Kwanini nasema alihadaa? Kwa sababu mwenyewe amekiri jana kuwa kilichomvutia kwa Lowassa ni ahadi ya uwaziri wa mambo ya nje. Kule anahubiri kuhusu mabadiliko, huku anawazia uwaziri wa mambo ya nje. Baada ya Lowassa kushindwa kupata urais, na ndoto ya Mwapachu kuwa waziri wa mambi ya nje kuota mbawa, kaamua kurejea CCM. 

Tabia kama hizi zinaweza kuigharimu CCM huko mbeleni. Watu walioikimbia wakati wa shida (kwa maana ya mapambano ya kumwingiza mgombea wake Ikulu) wanaruhusiwa kurejea kiulaini tu na kigeugeu chao kurushwa na vyombo vya habari kana kwamba ni matukio yenye umuhimu mkubwa kihistoria.

Laiti ningekuwa na mamlaka huko CCM, ningemweka benchi Mwapachu kwa sababu kama alivyoondoka akiwa hana umuhimu wowote kwa chama hicho, ndivyo alivyorudi akiwa na umuhimu mdogo zaidi ya ule ambao hakuwa nao wakati anahama.

Nimalizie makala hii ya dharura kwa kutamka bayana kuwa Tanzania yetu imefikishwa hapa na vipongozi kama hawa, walafi wa madaraka licha ya kuwepo madarakani miaka nenda miaka rudi, viongozi wasio na msimamo, wanaoweza kuhadaa umma kuhusu mabadiliko ilhali mabadiliko pekee wanayopigania ni ya maslahi yao binafsi.

Nigusie jambo moja dogo baada ya majuzi kutangazwa viongozi wapya na wa zamani kuongoza mikoa yetu kama ma-RC. Sina tatizo na wengi walioteuliwa lakini kilichonisikitisha ni kuona baadhi ya sura zilezile za miaka nenda miaka rudi zikirudishwa kwenye uongozi. Kama mtu alikataliwa na wapigakura jimboni kwake kwanini apelekwe kuongoza watu wa mkoa mwingine? 

Na lini vijana wapya watapewa fursa ya kuongoza Watanzania wenzao iwapo tunaendelea ku-recycle sura zilezile? Mimi ni sapota mkubwa wa Rais Magufuli, tangu wakati wa kampeni hadi sasa. Ninaridhishwa mno na uongozi wake. Hata hivyo, hiyo haimaanishi akikosea sintomkosoa. Na kama nina moja la kumkosoa ni kutujazia sura za watu waliokaa kwenye uongozi miaka nenda miaka rudi [na usidhani ninalaumu kuhusu hilo kwa vile nilikuwa/nina matarajio ya uongozi. Licha ya kuridhiska na kidogo ninachopata hapa, pia ninaamini kuwa ili kuitumikia Tanzania yetu sio lazima mtu awe kiongozi. Just be a good mwananchi]

Yayumkinika kuhisi kuwa watu wa aina hiyo hawana cha kupoteza wakiboronga na kutimuliwa, kwa sababu baadhi yao tayari wanakula pensheni za ubunge au ukurugenzi wa kitu gani sijui. Wakitimuliwa, watanufaika kwa nyongeza ya fedha tu.

Na sintoshangaa pengine Mwapachu karudi CCM kubahatisha kupewa 'pande' la ubalozi. Na huwezi kumlaumu sana kwa sababu medani ya uongozi wetu imekuwa ni suala la ku-recycle watu walewale, wengi wakiwa ndio walioifikisha Tanzania yetu hapa tusipostahili kuwa.





15 Mar 2016

Rais Dkt John Magufuli amekutaa kukutana na ujumbe wa maseneta sita wa Marekani, tukuio lililojiri tarehe 18 ya mwezi uliopita. Ombi la maseneta hao kukutana na Rais liliwasilishwa na Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ambaye alikuwa mwenyeji wa maseneta hao walioongozwa na Seneta James Inhofe wa chama cha Republican kutoka jimbo a Oklahoma. Hata hivyo, Rais Magufuli alikataa ombi la kukutana na maseneta hao akidumisha taswira yake ya kujiweka mbali na wafanyabiashara na lobbyists.

Mwaka juzi, Seneta huyo mhafidhina alishutumiwa vikali na kundi moja la utetezi wa haki za wanyama baada ya kuhudhuria hafla moja ambapo njiwa walirushwa hewani na kutunguliwa kwa risasi.



Mtandao wa kiuchunguzi wa African Intelligence unaripoti kwamba waziri huyo ya zamani katika serikali ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete anajulikana kwa kuwa karibu na Wamarekani matajiri wanaohusiana na Mfuko wa Kuhifadhi Mazingira wa Friedkin. Mfuko huo unamiliki makampuni ya Tanzania Game Trackers Safaris, Wengert Windrose Safaris na Mwiba Holdings Limited. Kampuni hiyo ya mwisho imekuwa ikihusishwa mara kadhaa na kesi za ujangili


4 Mar 2016

MWISHONI mwa wiki iliyopita, mitandao kadhaa ya kijamii ilitawaliwa na shutuma dhidi ya tabia inayotoa mizizi kwa majirani zetu wa Kenya kutumia vivutio vya Tanzania kujitangaza kana kwamba vipo katika nchi hiyo.

Katika tukio la majuzi, video moja ilisambaa mtandaoni ikimwonyesha binti mmoja wa Kenya akihutubia mkutano mmoja wa kimataifa, huku akieleza bila aibu kuwa miongoni mwa vivutio vilivyopo nchini Kenya ni Bonde la Olduvai (Olduvai Gorge).


Tukio hilo ni moja tu katika mlolongo mrefu wa majirani zetu hao ‘kutupora’ umaarufu wetu, huku ‘uongo’ maarufu zaidi ukiwa kuutangaza Mlima Kilimanjaro kuwa upo Kenya. Hata Jumapili wiki hii nilipotembelea mtandao wa kijamii wa Twitter, nilikutana na ‘tweet’ moja inayodai kuwa Mlima huo unaonekana vizuri zaidi nchini Kenya (kuliko Tanzania).


Pamoja na lawama kadhaa zilizoelekezwa kwa majirani zetu hao, baadhi ya Watanzania walikwenda mbali zaidi na kuhoji kwa nini nchi jirani inapata ujasiri wa kujinadi kwa kutumia vivutio vyetu. Ukweli mchungu ni kwamba sisi wenyewe tumekuwa wazembe kwa kiasi kikubwa.


Uzembe huo unaonekana katika sura nyingi lakini pengine ya wazi zaidi ni katika ukweli mchungu kuwa licha ya madini ya Tanzanite kupatikana Tanzania pekee, nchi zinazoongoza kwa mauzo ya madini hayo ni India ikifuatiwa na Kenya. Hiki ni kichekesho kinachokera mno.


Binafsi, ninaona udhaifu katika kunadi vivutio vyetu na nchi yetu kwa ujumla unachangiwa na sababu kuu tatu. Ya kwanza, ni uhaba wa uzalendo. Mara kadhaa nimekuwa nikiandika kuhusu suala hili. Moja ya vitu muhimu alivyotuachia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ni kuthamini Utanzania wetu. Na thamani hiyo ya asili yetu haikuwa kwa sababu tu ni nchi yetu bali pia katika mambo kadhaa ya kujivunia kama vile mchango wa taifa letu katika mapambano ya ukombozi kusini mwa bara la Afrika.


Leo hii baadhi yetu tukikutana na Waafrika Kusini au Wazimbabwe, kwa mfano, wanaikumbuka Tanzania kama nchi iliyoshirikiana nao katika mapambano ya kudai haki yao ya kujitawala. Hata hivyo, baadhi hutuhoji kwa nini Tanzania imepoteza umaarufu mkubwa wa enzi za Mwalimu Nyerere.


Sababu ya pili, inayoshabihiana na hiyo ya kwanza ni ubinafsi. Watanzania wengi wamekuwa wakiweka mbele zaidi maslahi yao binafsi kuliko maslahi ya taifa letu. Umaarufu binafsi umekuwa ukipewa kipaumbele zaidi kuliko umaarufu wa nchi yetu. Kibaya zaidi, wachache tunaojitahidi kuitangaza nchi yetu kwa namna moja au nyingine huishia kuzodolewa kuwa tunafanya hivyo kwa minajili ya kujikomba au kusaka ukuu wa wilaya.


Katika hilo la ubinafsi, kunapojitokeza mawazo ya kuitangaza nchi yetu kimataifa, badala ya kuangalia taasisi au watu wenye uwezo wa kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, fursa huelekezwa kwa ndugu, jamaa na marafiki wasio na uwezo. Kipaumbele huwa kwenye fedha zilizotengwa kwa shughuli hiyo na wala sio matokeo chanya.


Sababu ya tatu ni kutowatumia vema Watanzania walio nje ya nchi. Kimsingi, kuwa Mtanzania nje ya nchi ni kama laana ya aina fulani. Kwa kiasi kikubwa tu, baadhi ya Watanzania wenzetu wanatuona sisi tulio nje ya nchi kama Watanzania vipande, yaani tusio kamili, na hatupaswi kujihusisha na masuala yanayohusu nchi yetu.


Baadhi yetu tunapojaribu kushiriki ujenzi wa taifa letu kwa njia kama hizi za maandiko huishia kukatishwa tamaa na kauli kama acha kutukebehi. Shida tunazopata hapa wazijua? Kana kwamba mtu akiwa nje ya Tanzania ndio amepoteza kila mawasiliano (connection) aliyonayo na nchi yetu, kuanzia ndugu, jamaa na marafiki hadi uraia.


Kama kuna nchi mbili barani Afrika ambazo zimenufaika sana kuwatumia raia wake wanaoishi nje ya nchi, nchi hizo ni Rwanda na Nigeria. Kwa Rwanda, takriban kila mwaka nchi hiyo hufanya makongamano katika nchi mbalimbali duniani, hususan hapa Uingereza na Marekani. Wiki iliyopita, Rais Paul Kagame yupo nchini Marekani, ambapo pamoja na mambo mengine anahamasisha Wanyarwanda walio nje ya nchi kushiriki katika ujenzi wa taifa lao.


Katika makongamano yaliyopita ya Rwanda hapa Uingereza, Rais Kagame alifanikiwa kuwashawishi Wanyarwanda kadhaa waliokuwa wanaishi hapa kurejea nyumbani na kuwapatia fursa mbalimbali zilizoendana na sifa, ujuzi na uzoefu wao walioupata walipokuwa hapa.
Kwa Nigeria, kabla ya kuunda serikali yake, na wakati huu ambapo nchi hiyo inapitia mageuzi makubwa ya kiuchumi, Rais Muhammad Buhari amekuwa akifanya jitihada kubwa kuwashawishi raia wa nchi yake waliotapakaa sehemu mbalimbali duniani kurejea katika taifa hilo ili kushiriki katika kulijenga na kuliboresha.


Sambamba na hatua hizo, badala ya kutumia fedha nyingi katika tenda za kuzipromoti nchi hizo nje ya nchi, kipaumbele kimekuwa katika kuwatumia raia wake kadhaa waliopo nje ya nchi hizo.


Licha ya kuvunjwa moyo, baadhi yetu tumeendelea na jitihada hizo za kuitangaza Tanzania yetu kwa kutumia njia mbalimbali. Kwa mfano, kwa muda sasa, binafsi nimekuwa nikijaribu kuitangaza Tanzania yetu kwenye mtandao wa kijamii wa twitter kwa mabandiko (tweets) yanayoambatana na hashtag #VisitTanzania (kwa kila habari au picha inayohusu vivutio vyetu) na #InvestInTanzania (kwa habari au picha zinazohusiana na fursa za uwekezaji huko nyumbani. Hata hivyo, mapokeo yamekuwa sio ya kuridhisha japo hainivunji moyo.


Kwa upande mwingine, licha ya uandishi wa vitabu kwa lugha ya Kiswahili kuchangia jitihada za kuitangaza Tanzania yetu kupitia lugha yetu ya taifa, ninaitumia pia fursa niliyoipata hivi majuzi ya kufundisha Kiswahili kwa kundi la wanafunzi wa shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Glasgow, (wanaotarajia kuja huko nyumbani kwa ajili ya tafiti zao) kuitangaza nchi yetu kwa namna moja au nyingine.


Nihitimishe makala hii kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuhusu busara hii: “…usipoeleza mazuri yako wewe mwenyewe, wenzako wataeleza mabaya yako au kuyapora mazuri yako hayo.” Hicho ndio kinachofanywa na majirani zetu wanaojinadi kwa kutumia vivutio vyetu. Sisi wenye vivutio hivyo tumejisahau/tunazembea, wenzetu wanaojua umuhimu wa kujinadi wanatumia vyema kujisahau kwetu/uzembe wetu kwa manufaa yao.
Kadhalika, ninatoa wito kwa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli kutumia vyema Watanzania wenye uwezo na fursa za kuinadi nchi yetu, ndani na nje ya Tanzania.


Mungu Ibariki Tanzania

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.