25 Mar 2015


Wiki mbili zilizopita niliandika makala iliyoonya tabia iliyoanza kuzoeleka kwa baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM kufanya mzaha kuhusu ugaidi. Kwa muda mrefu sasa, viongozi wa chama hicho hususan Nape Nnauye na Mwigulu Nchemba wamekuwa wakiihusisha Chadema na ugaidi. Lakini tabia hiyo haikuanzia kwa Chadema pekee kwani huko nyumaCUF nayo ilikumbwa na tuhuma kama hizo kutoka kwa CCM.

Katika makala hiyo ambapo nileleza kwa kirefu kiasi kuhusu hatari inayoikabili dunia hivi sasa kutoka kwa vikundi vinavyoongoza kwa ugaidi kwa muda huu, yaani ISIS, Al-Qaeda, Boko Haram na Al-Shabaab, nilitahadharisha kwamba tabia ya CCM kuufanyia mzaha ugaidi, kwa maana ya kuzusha tu 'Chadema ni magaidi au CUF ni magaidi', inaweza kutugharimu huko mbeleni. Nilibainisha kuwa mzaha huo unaweza kuwarahisishia magaidi halisi dhima ya kushambulia nchi yetu, kwani 'tayari tuna magaidi wa ndani- kwa maana ya tuhuma za CCM dhidi ya Chadema na CUF.

Vilevile nilitanabaisha kwamba kuufanyia mzaha ugaidi kunaufanya uzoeleke, uonekane ni kama jambo la kawaida tu ambalo halikauki midomoni mwa akina Nape na Mwigulu.Lakini pengine baya zaidi ni vyombo vyetu vya dola kuwekeza nguvu kubwa kudhibiti 'magaidi hewa' hali inayoweza kuwapa upenyo magaidi halisi.

Kwa bahati mbaya, tahadhari niliyoitoa kwenye makala hiyo inelekea kubeba uzito, baada ya kupatikana taarifa kwamba kikundi hatari kabisa cha magaidi cha ISIS kina mpango wa kujienga na hatimaye kufanya mashambulizi katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwa ni pamoja na Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa za kituo cha televisheni cha Aljaazera, mawasiliano ya hivi karibuni ya kikundi hicho cha kigaidi yanaonyesha kuwa kinajaribu kujijenga Afrika Mashariki, eneo ambalo limekuwa likisumbuliwa na magaidi wa Al-Shabaab na Al-Qaeda kwa vipindi tofauti.

Hivi karibuni, kikundi cha kigaidi cha Boko Haram cha Nigeria kimetoa ahadi ya utiifu kwa ISIS, hatua iiliyotafsiriwa na wachunguzi wa masuala ya ugaidi kuwa inaweza kuongeza nguvu za ISIS katika maeneo mbalimbali ya bara la Afrika.

Hata hivyo, kitu ambacho hakikufahamika kwa wengi ni kwamba tukio hilo la Boko Haram kuonyesha utii wa ISIS lilitanguliwa wiki chache kabla ya ujumbe uliotumwa kwa kiongozi wa Al-Shabaab , Abu Ubaidah, kumwomba afanye kama walivyofanya Boko Haram (kutangaza utii kwa ISIS)

Ujumbe huo uliwasilishwa na  Hamil al-Bushra, jina linaloaminika kutumiwa na vyanzo viwili vya habari vinavyohusishwa na ISIS.

Katika ujumbe huo, Bushra aliwapongeza Al-Shabaab na kuwahamasisha wafanya mashambulizi Kenya, Ethiopia na TANZANIA.

Soma habari kamili HAPA

12 Mar 2015

SIKU chache zilizopita, kikundi hatari cha kigaidi cha Boko Haram cha nchini Nigeria kilitangaza utiifu wake kwa kikundi kingine hatari kabisa cha kigaidi cha ISIS.
Hizi si habari njema hata kidogo kwani ushirikiano wowote kati ya makundi ya kigaidi, hususan, yaliyopo maeneo tofauti, unamaanisha kusambaa kwa vitendo vya kigaidi.
Ujumbe ulitolewa na Boko Haram, ambao hata hivyo bado haujathibitishwa (ni nadra kuthibitisha ujumbe wao ), uliwekwa kwenye akaunti ya kikundi hicho katika mtandao wa kijamii wa twitter, ambayo inaaminika kuwa ya kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau.
Kikundi hicho kilianza mashambulizi ya kigaidi mwaka 2009 maeneo ya Kaskazini mwa Nigeria, lengo kuu likiwa kuanzisha utawala unaoendeshwa kwa sheria za Kiislamu. Tayari kikundi hicho kimeshasababisha mauaji ya raia kadhaa, na hivi karibuni kimekuwa kikijaribu kusambaza unyama wake kwa nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad.
Awali, ilifikiriwa kwamba Boko Haram ina mahusiano na kikundi kingine kikubwa na hatari cha Al-Qaeda, ambacho kilikuwa maarufu sana kabla ya kuibuka kwa ISIS.
Kwa upande wake, ISIS kimekuwa kikifanya unyama ambao pengine haujawahi kuonekana katika historia ya vikundi vya kigaidi, licha ya mashambulizi ya kujitoa mhanga, kikundi hicho kimeshawachinja mateka wake kadhaa na kuweka unyama huo hadharani.

Hivi karibuni, ilifahamika kuwa gaidi anayedaiwa kuwa ndiye ‘mchinjaji’ mkuu, anayejulikana kama Jihadi John, aliwahi kufika Tanzania na kuzuiliwa kuingia, kabla ya kuelekea Syria, ambako pamoja na Iraki, ni maeneo yanayosumbuliwa na kikundi hicho.
Lengo kuu la ISIS ni kuanzisha himaya (Caliphate) ya Kiislam, na kiongozi wake, Abu Bakr al-Baghdad, amejitangaza kuwa ndiye mkuu wa himaya hiyo ambayo wanalenga kuisambaza dunia nzima.

Kinachoifanya ISIS kuonekana hatari zaidi, licha ya unyama wake, ni uwezo wake mkubwa wa kifedha, sambamba na ufanisi wa kimuundo kana kwamba ni dola kamili yenye serikali.
Tangazo la Boko Haram kuahidi utiifu kwa ISIS si la kushangaza sana, japo wafuatiliaji wa masuala ya ugaidi walishangazwa kwanini hali hiyo haikutokea mapema zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa mbinu na malengo ya vikundi hivyo yanashabihiana.

Huu ni mtihani mkubwa kwa wana-intelijensia duniani hasa ikizingatiwa kuwa ISIS, kama ilivyokuwa Al-Qaida, si tu imefanikiwa kuwavutia ‘wapiganaji’ kutoka sehemu mbalimbali duniani, bali pia ina dhamira kubwa ya kusambaza unyama wake takriban kila kona ya dunia.
Kwa tafsiri ya haraka, Boko Haram wanaweza kunufaika na ushirikiano wake na ISIS na pengine kufanikiwa kusambaza kampeni yao ya kigaidi katika maeneo mengine ya Afrika.
Lengo la makala hii sio kujadili vikundi hivyo vya kigaidi. Kilichonishawishi kuandika makala hii yenye utangulizi unaohusu vikundi hivyo vya ugaidi ni tamko la hivi karibuni la Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye kuwa kikosi cha ulinzi cha Red Brigade cha Chadema ni kundi la kigaidi.

Lakini Nape si mwanasiasa wa kwanza wa CCM kutoa tamko zito kama hilo. Mwaka juzi, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Mwigulu Nchemba, aliandika waraka mrefu katika mtandao wa kijamii wa Jamii Forums kuizungumzia Red Brigade ya Chadema, ambapo pamoja na mambo mengine alidai ina malengo ya “uhaini, ni ugaidi, ni maandalizi ya kupindua nchi au kuvuruga kabisa amani tuliyonayo.”
Kwa upande wake, Nape alidai makundi ya vijana wa ulinzi vya chama hicho (Red Brigade) yameandaliwa kwa ajili ya kuingia msituni kwa shughuli za ugaidi. Alitoa kauli hiyo wilayani Mpwapwa kwenye ziara ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, mkoani Dodoma.
“Chadema wanaandaa vijana kupitia Red Brigade ili kuingia msituni na kuchukua madaraka ya nchi kwa mabavu. Wanafanya hivyo kwa sababu wanajua hawawezi kuchaguliwa kwa njia ya kura wakati wa uchaguzi mkuu,” alidai mwanasiasa huyu muumini wa siasa za uhasama, na kuongeza kuwa, “Taarifa tulinazo ni kwamba Red Brigade ni vikosi vinavyoandaliwa kwa ajili ya vitendo vya ugaidi na shughuli nyingine za ovyo. Taarifa ni kwamba hili ni kundi la kigaidi, wataanzishaje kundi la usalama wakati tunavyo vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi yetu?”
Huu ni uhuni wa kisiasa. Na baya zaidi, ni mwendelezo wa kasumba ya muda mrefu kwa Nape na Mwigulu kuufanyia mzaha ugaidi kwa kuvihusisha vyama vya upinzani hususan Chadema.
Lakini kabla ya kuwajadili wanasiasa hawa wawili ‘wanaaombea uwepo wa ugaidi nchini mwetu,’ ni vema kutambua kuwa kamwe kauli zao hazijawahi kupingwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete au kiongozi mwingine yeyote yule wa chama hicho tawala. Wakati Julai mwaka, Rais Kikwete alisema si sahihi kwa vyama vya siasa kuanzisha vikundi vya mgambo kwani vitendo hivyo ni viashiria vya uvunjifu wa amani nchini, chama anachokiongoza (CCM) pia kina kikundi cha Green Guard, kama ilivyo Blue Guard kwa CUF.
Kwa maana hiyo, kwa Nape na Mwigulu kukemea Red Brigade ya Chadema ilhali CCM nayo ina Green Guard si tu ni unafiki bali pia wanaweza kuwa wanatumika kama ‘kipaza sauti’ cha Rais Kikwete na CCM kwa ujumla.

Lakini sote tunafahamu siasa zetu za upinzani zilivyo ambapo ‘kurushiana madongo’ ni sehemu ya kawaida. Hata hivyo, jaribio lolote la kuhusisha ugaidi na ‘madongo’ ya kawaida litatugharimu kama taifa. Ugaidi si jambo la kufanyia mzaha hata kidogo.
Moja ya madhara ya kuufanya ugaidi kama jambo la kawaida ni kuwarahisishia magaidi halisi fursa ya kutudhuru. Hivi, kwa mfano, magaidi tulio jirani nao zaidi kuliko Boko Haram, ISIS na Al-Qaeda, yaani Al-Shabaab wa Somalia, wakitaka kufanya ugaidi nchini mwetu (Mungu aepushie) hawawezi kutumia upenyo wa ‘Red Brigade wa Chadema ni magaidi’ kuficha dhamira yao ovu?
Vyombo vyetu vya usalama vinaweza kulazimika kuwekeza nguvu kubwa kuwadhibiti ‘magaidi wa kufikirika’ wa Red Brigade, na hiyo yaweza kutoa fursa kwa magaidi halisi kufanya unyama wao.
Tayari tumeshaona jinsi vyombo vya usalama vinavyotumia nguvu kubwa kulinda maslahi ya CCM, ikiwa ni pamoja na kuwakandamiza wapinzani wake, huku ufisadi, ujangili, biashara ya madawa ya kulevya, na sasa mauaji ya albino vikistawi kana kwamba ni shughuli halali.
Kichekesho, majuzi wakati Rais Kikwete anazindua studio za kituo cha Televisheni cha Azam jijini Dar alitoa karipio kali kwa vyombo vya habari akisema serikali haitavumilia vyombo vya habari visivyosimamia uadilifu, weledi pamoja na kutumika katika kuchochea ghasia. Kwanini ukali huo wa Rais wetu uwe kwa vyombo vya habari tu ilhali wahuni wa kisiasa wakiruhusiwa kufanyia mzaha tishio la ugaidi?

Nimalizie makala hii kwa kuwahamasisha Watanzania wenzangu kuwapuuza wanasiasa mufilisi wanaojaribu si tu kujenga chuki miongoni mwetu bali pia kufanyia mzaha tishio la ugaidi.
Sote ni mashuhuda wa unyama unaofanywa na Boko Haram, ISIS, Al-Qaeda, Al-Shabaab na makundi mengine ya kigaidi, na ninaamini hakuna mtu anayeweza kudiriki kutamani uharamia huo utokee katika nchi yetu. Siasa za chuki za kipuuzi ni hatari sana kwa mustakabali wa Tanzania yetu.
Inahitaji kauli chache tu za kupandikiza mbegu za chuki, lakini ni vigumu mno kung’oa chuki pindi mbegu hizo zikifanikiwa kuotesha chuki.

10 Mar 2015

Tafsiri: Mimi sishangazwi hata kidogo. Viongozi wa Kanisa na wanasiasa wakubwa wanashiriki katika mila hii ya kishetani. Kiongozi mmoja mkubwa wa kanisa mwenye usharika mkubwa jijini Dar es Salaam, anayemiliki benki, alikamatwa akiwa na albino amefungwa nyuma ya gari lake. Alitoroka eneo la tukio na kesi yake haikuripotiwa kwa sababu alitoa rushwa. Yeye pia ni muuza madawa ya kulevya mkubwa na mtakasaji fedha haramu. Kwahiyo tunatarajiwa Umoja wa Mataifa utaanza kuwafungulia watu hawa mashtaka ya ukatitili dhidi binadamu ili Watanzania walichukulie suala hili kwa makini.

Kwa umoja wetu na upendo wetu kwa ndugu zetu albino, tuunganishe kumsaka mwanaharamu huyu anayejiita mchungaji ilhali anafanya matendo ya kishetani. 

Mie ni muumini katika nguvu ya umma. Na nguvu ya umma si kuandamana tu bali hata katika kufichua maovu katika jamii. Ni na imani ya asilimia 100 kuwa kuna mtu au watu flani, sehemu flani wanamfahamu 'mchungaji' huyu. Kadhalika ninaamini kuna mtu au watu flani wanamfahamu mwanasiasa au mfanyabiashara au mganga au muuaji anayejihusisha na mauaji ya albino. Sasa pengine hofu ya kumripoti inachangiwa na kuchelea matokeo hasa ikizingatiwa kuwa polisi wetu hawaaminiki.

Tutumie nguvu ya umma. Kama una taarifa ya uhakika (ikiwa na uthibitisho itakuwa vema zaidi) basi ninaomba uwasiliane nami kwa barua-pepe CHAHALI at ABOUT dot ME au nitumie meseji Facebook https://www.facebook.com/evarist.chahali.1 au nenda kwenye tovuti hii http://swarmsecret.com/ kisha tweet kwa @chahali nami sio tu nitaweka hadharani suala hilo bali nitatumikia kila tone la nguvu zangu kuhakikisha mtu huyo anachukuliwa hatua za kisheria, ndani au nje ya Tanzania yetu.

Vinginevyo, ukifanikiwa kupata taarifa za mchungaji huyo au mtu yeyote anayejihusisha na unyama huo, 

Kwa pamoja tunaweza katika hili

SHUKRANI: Asante Ndugu Alfred Kiwuyo kwa kutufahamisha kuhusu habari husika

5 Mar 2015

"NI wajinga wa kisiasa pekee wanaoweza kudharau mchango wa Marehemu Komba katika siasa za Tanzania. Nimeona kuna watu wanabwabwaja sana!" Hii ni kauli ya Profesa Kitila Mkumbo aliyoitoa Jumapili iliyopita, katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
MSOMI huyo ambaye pia ni mwanasiasa alitamka hivyo kufuatia mpasuko mkubwa uliojitokeza (angalau katika mtandao wa intaneti) kufuatia taarifa za kifo cha mwanasiasa maarufu na Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM) Kapteni John Komba, kilichotokea Jumamosi jijini Dar es Salaam.
Japo inafahamika kwa idadi ya Watanzania wanaitumia mtandao wa intaneti ni ndogo sana kulinganisha na idadi ya Watanzania wote, kwa kiasi fulani mada zinazotawala mtandaoni huweza kuakisi hali halisi iliyopo 'mtaani.' Ni kwa mantiki hiyo, ninashawishika kuhisi kuwa mpasuko uliojitokeza mtandaoni kufutia kifo cha Kapteni Komba waweza pia upo mitaani pia.
Mpasuko huo ulichukua sura ya makundi mawili, moja likionekana kufurahia kifo cha mwanasiasa huyo huku likifanya marejeo ya kauli zake mbalimbali hasa ile ya wakati wa Bunge Maalum la Katiba kuwa angeingia msituni iwapo pendekezo la muundo wa Muungano wa serikali tatu lingepitishwa.
Kundi jingine lilikuwa la waombolezaji, wananchi walioguswa na kifo hicho, huku wakilaani vikali 'jaribio lolote la kumlaumu marehemu.' Katika kundi hili, kulijitokeza 'mapadri na mashehe' walionukuu Biblia Takatifu na Kuran Tukufu kukumbushia umuhimu wa kuenzi marehemu na kuheshimu kifo.
Lakini ndani ya makundi hayo kulijitokeza 'waliouma na kupuliza,' yaani kwa upande mmoja wakionyesha jinsi walivyokwazwa na baadhi ya kauli za marehemu Komba hususani zilizokua zinachochea chuki na uhasama wa kisiasa na kijamii, lakini upande mwingine wakidai kuwa 'si vizuri kumsema vibaya marehemu.'
Kama nilivyotanabaisha hapo juu, sina hakika hali ikoje huko mitaani lakini yayumkunika kuhisi kuwa idadi ya waombolezaji ni kubwa kuliko ya 'wanaomwandama marehemu.' Idadi kubwa ya waombolezaji yaweza kusababishwa zaidi na 'uoga wetu wa kawaida kwa kifo' kuliko kuguswa na kifo husika.
Japo sote twatambua kwa uhai wetu una kikomo kwa njia ya kifo, na japo hatuna la kufanya kubadili ukweli huo mchungu, twaendelea kukiogopa kifo huku vifo vya watu wa karibu au tunaowafahamu vikitukumbusha tena na tena kuwa kifo kipo.
Kwa namna flani ya kusikitisha, kuna nyakati vifo huwa nafasi ya kushuhudia unafiki wa baadhi yetu kama wanadamu. Ni mara ngapi tumeshuhudia, kwa mfano, baadhi ya vijana wakiteketeza uhai wao kwa matumizi ya madawa ya kulevya, lakini jamii ikiwatelekeza, na kisha kumwaga lundo la rambirambi pale wanapofariki? Sawa, rambirambi ni ishara ya kuguswa na kifo, lakini ina faida gani hasa pale upendo ungeweza kuepusha kifo hicho?
Kwa upana zaidi, kuna haja gani kumpenda mtu baada ya kufariki ilhali alipokuwa hai alichukiwa? Upendo huo wa ghafla ni nini zaidi ya unafiki kwani wakati mwafaka tunapohitaji upendo ni tunapokuwa hai.
Kilichojitokeza baada ya kifo cha marehemu Kapteni Komba, ambapo baadhi ya wenzetu wameonekana 'kufurahia,' ni mwendelezo wa chuki katika Tanzania yetu, huku baadhi ya wanasiasa wa CCM wakiwa ndio wahusika wakuu.
Sawa, sio vema kuzungumzia 'mabaya' ya marehemu Komba, kwa mfano, lakini kwa bahati mbaya au makusudi, ukiweka kando umahiri wake katika nyimbo za maombolezo ya kifo cha Baba wa Taifa, marehemu Julius Nyerere, kumbukumbu muhimu ya hivi karibuni ni lugha kali aliyoitumia wakati wa Bunge Maalum la Katiba.
Yeye, pamoja na 'waeneza chuki' wengine walifikia hatua inayoweza kutafsiriwa kama kumtakia kifo Jaji Joseph Warioba kwa vile tu Tume aliyoongoza kukusanya maoni ya Katiba ilipendekeza muundo wa Muungano wa serikali tatu.
Lakini ishara kuwa chuki inazidi kutawala katika Tanzania yetu zilianza kujitokeza kwa wazi zaidi pale Rais Jakaya Kikwete alipolazwa nchini Marekani kwa matibabu ya tezi dume. Wakati idadi kubwa tu ya Watanzania ilijitokeza kumtakia Rais wetu uponyaji wa haraka, kulikuwa na kundi dogo ambalo halikuficha hisia zao, kiasi cha baadhi yao kutaka Rais asirudi akiwa hai. Kwa lugha nyingine, wenzetu hawa walikuwa wanamwombea kifo Rais wao.
Kwa bahati mbaya au makusudi, hakuna jitihada zilizofanyika japo kuanzisha mjadala tu kuhusu ustawi wa chuki katika nchi yetu. Na matokeo yake, leo hii twashuhudia baadhi ya wenzetu wanaoonekana kufurahia kifo cha mwanasiasa wetu mahiri.
Ni rahisi kuitazama chuki hii kama ujinga, kama alivyotanabaisha Profesa Kitila, lakini binafsi ninaamini hili ni swali gumu lisilostahili majibu rahisi. Kwa mtizamo wangu, moja ya sababu za chuki hiyo inaweza kuwa ni pengo la kitabaka kati ya watawala na watawaliwa, sambamba na pengo linalozidi kukua kati ya wenye nacho na wasio nacho.
Lakini chuki hiyo inachangiwa pia na jeuri ya watawala wetu, kusahau kuwa 'kesho kuna kifo,' kuropoka kila baya hasa kwa wapinzani wao kisiasa, na kuwadharau wananchi ambao kimsingi ndio waajiri wa watawala hao.
Kauli za baadhi ya wanasiasa mahiri kwa 'kusema ovyo' kama ile ya 'vijisenti' ya Mbunge wa Bariadi (CCM) Andrew Chenge, hii ya majuzi ya 'shilingi milioni 10 za kununulia mboga (labda ni tembo mzima)' ya Profesa Anna Tibaijuka, ile ya Profesa Muhongo kuwa 'Watanzania hawawezi kuendesha biashara ya gesi na mafuta bali wanamudu biashara ya matunda tu,' na nyinginezo nyingi, zinachangia kushamiri kwa hasira za baadhi ya wananchi kwa baadhi ya viongozi wao.
Tuna wanasiasa kama LivingstonLusinde, maarufu kama 'kibajaji’, Nape Nnauye, William Lukuvi, Stephen Wassira na Mwigulu Nchemba (japo huyu amekuwa na nafuu sasa), ambao wakizungumzia vyama vya upinzani wanaweza kumwaminisha msikilizaji kuwa wapinzani ni viumbe hatari kuliko magaidi wa Al-Shabaab, Boko Haram au ISIS.
Wanajitahidi sana kupamba mbegu za chuki, na kwa hakika wamefanikiwa kwa kiasi fulani. Lakini uongozi wa juu wa chama hicho tawala haujawahi kukemea kauli hizo za chuki, yayumkinika kuhisi kuwa ujenzi wa chuki ni miongozi wa sera zisizo rasmi kwa chama hicho, kama ilivyo ufisadi.
Ni muhimu kwa watawala wetu kujifunza kitu katika chuki hii inayolitafuna taifa letu. Kinachotufanya tuendelee kumlilia Baba ya Taifa hadi leo ni matendo yake ya kuigwa mfano wakati wa uhai wake.
Yawezekana kama binadamu mwingine, Mwalimu aliwahi kuwakwaza baadhi ya Watanzania, lakini 'hukumu ya jumla' kwa matendo yake wakati wa uhai wake ni kwamba aliweka mbele maslahi ya taifa kuliko maslahi yake binafsi. Tunamkumbuka na kumlilia kwa sababu tunaona ombwe kubwa lililotokana na kifo chake.
Sasa, japo 'marehemu hasemwi vibaya,' sidhani kama kuna atakayeshangaa sana kuona kifo cha mwanasiasa mahiri kwa matusi, vijembe, mipasho na mambo mengine mabaya kikipelekea furaha katika sehemu flani ya jamii. Ndio, dini zetu zinasisitiza kuwaenzi marehemu, lakini dini hizo pia zinasisitiza umuhimu wa heshima wakati wa uhai wetu.
Na pia licha ya ukweli si kila Mtanzania ni mcha-Mungu, wingi wa wacha-Mungu katika nchi yetu umeshindwa kuzuwia mauaji ya albino, ufisadi na 'dhambi'nyingine lukuki.
Nimalizie makala hii kwa kutoa salamu zangu za rambirambi kwa familia ya marehemu Kapteni Komba, ndugu, jamaa, marafiki na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla.
Njia mwafaka ya kumwenzi marehemu ni kudumisha mema yake, na kujifunza katika mapungufu yake. Kadhalika, kifo hiki kinapaswa kutuamsha na kuanza mjadala wa kitaifa kuhusu kudidimia kwa upendo, umoja na mshikamano wetu.
Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Kapteni Komba mahala pema peponi. Yeye ametangulia tu, sote twaelekea huko.

26 Feb 2015

Tanzania Tanzania, nakupenda kwa moyo wote,

Nchi yangu Tanzania, jina lako ni tamu sana
Nilalapo nakuwaza wewe, niamkapo ni heri mama wee
Tanzania Tanzania, nakupenda kwa moyo wote.”


Huu ni ubeti wa wimbo maarufu ambao ‘zamani hizo’ tulipouimba tulijisikia ‘raha’ flani kuhusu nchi yetu. Tulikuwa na kila sababu za kuipenda Tanzania kiasi cha kuiota tulipolala.
Peleka mbele (fast-forward) hadi zama hizi tunaoishi, hutolaumiwa ukijiuliza ‘ninaipenda Tanzania kwa lipi hasa, maana kila kukicha tunakumbana na habari au matukio yanayoweza kumfanya mtu amlaumu Muumba kwa kumfanya azaliwe katika nchi yetu.

Tuweke kando ufisadi unaokurupuka kila kukicha, tusahau kuhusu wawakilishi wetu wanaotugharimu mamilioni ya shilingi kila mmoja kwa mwezi kisha wakifika bungeni inakuwa ni matusi, vijembe, na upuuzi kama huo. Tufumbie macho nchi yetu inavyouzwa rejareja kwa kisingizio cha uwekezaji huku baadhi ya wawekezaji hao wakija na briefcase tupu na kuondoka na mabilioni. Na tusamehe aibu ya kugeuka ombaomba wa kimataifa huku Rais wetu akiwa ziarani nje mara kwa mara kwa ‘kisingizio’ hicho.

Twaweza kuweka kando kila jambo ‘baya’ kuhusu Tanzania yetu lakini haiwezekani kabisa kupata kisingizio katika unyama wa hali ya juu unaoendelea nchini mwetu dhidi ya ndugu zetu maalbino. Kinachofanywa kwao si dhambi tu bali ni aibu kubwa kwa taifa letu.
Majuzi tu rafiki yangu mmoja hapa Uskochi aliniuliza, “Evarist, hivi asili yako ni Zimbabwe au Tanzania?” Nami bila uoga nilimjibu kuwa ninatokea Tanzania. Kisha likafuata bomu, “Nimeona kipindi flani kwenye televisheni kinaonyesha jinsi maalbino wanavyouawa Tanzania kwa imani kuwa viungo vyao vinaleta utajiri. Ni kweli?” Nilipatwa na mchanganyiko wa aibu na hasira. Aibu kwa sababu nchi yangu inaonekana kuwa na viumbe wa ajabu kabisa wanaomudu kudiriki unyama huo. Pia nilipatwa na hasira kwa sababu ni ukweli usiopingika kuwa laana ya mauaji ya albino limeachwa kustawi kana kwamba uhai wa Watanzania wenzetu maalbino hauna thamani.

Wiki iliyopita, vyombo vya habari huko nyumbani viliripoti kuhusu tukio la kusikitisha ambapo maiti ya mtoto albino, Yohana Bahati, aliyetekwa tarehe 15 mwezi huu, uliokotwa ukiwa umekatwa miguu na mikono. Taarifa ya mauaji ya kinyama ya mtoto huyo asiye na hatia yoyote imesambaa sehemu mbalimbali duniani huku vyombo vya habari vya kimataifa vikiipa uzito mkubwa.

Aibu gani hii kwa nchi inayojigamba kuwa ni ‘kisiwa cha amani na utulivu’ huku ikitumia mabilioni ya shilingi katika kampeni za kimataifa kutangaza vivutio vyetu?

Kwa bahati nzuri, Watanzania wengi hususan kwenye mitandao ya kijamii wameonekana kuguswa mno na unyama huu kiasi cha kupelekea kampeni ya ‘Stop Albino Killings.’ Katikati ya wiki iliyopita, kampeni hiyo ilivuma katika mtandao wa kijamii wa Twitter hadi kufanikiwa kufikisha ‘impressions’ zaidi ya milioni moja.

Cha kusikitisha, hadi wakati ninaandika makala hii, Rais Jakaya Kikwete ambaye akaunti yake ya Twitter imerejea hewani baada ya kupotea kwa siku kadhaa, ameshindwa kujumuika na Watanzania lukuki pamoja na watu wengine duniani, kuunga mkono kampeni hiyo.
Na kana kwamba ni chama anachoongoza Rais Kikwete, CCM, kimeona suala hilo ni mzaha flani wa kupuuzwa, licha ya kutounga mkono kampeni hiyo, Jumapili iliyopita kiliweka bandiko katika mtandao huo kikijigamba kuwa, ninanukuu, “Tumeendelea kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama kulinda amani na utulivu...” Haya ni matusi. Amani na utulivu gani ilhali Watanzania wenzetu albino wanachinjwa kinyama zaidi ya kuku (maana tunapochinja kuku hatumkati mikono, mguu au kucha zake hadi muda wa matayarisho ya kumpika)?

Kadhalika, katika hali inayoweza kutafsiriwa kama serikali yetu kupuuza mauaji ya albino , hakuna kiongozi yeyote wa ngazi za juu wa serikali aliyeona umuhimu wa kushiriki katika mazishi ya mtoto Yohana. Siku alipozikwa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikwenda kuhani msiba wa chifu mmoja huko Iringa. Hivi hata tukiweka kando protokali, serikali ilishindwa kumtumia japo Waziri mmoja kumwakilisha Rais Kikwete?

Binafsi, pamoja na nyingi ya ‘tweets’ zangu wiki iliyopita za kuhamasisha kampeni hiyo inayoandikwa #StopAlbinoKillings, pia nilitanabaisha kuwa mauaji hayo ya albino ni zaidi ya suala la kisheria bali la kibinadamu. Nilisema hivyo kwa sababu, kwa upande mmoja, sheria dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu na za mauaji zipo lakini hazijatumika ipasavyo kukabiliana na tatizo hilo, na kwa upande mwingine, hata pale sheria zinapofanya kazi ipasavyo, hazimaanishi kuwa zitamaliza kabisa uhalifu flani. Hata hivyo, sheria zikitumika ipasavyo huwezi japo kwa kiasi flani kukwaza uhalifu (deterrence).

Wakati matukio ya mauaji ya kinyama ya albino yakiendelea huko nyumbani, mwezi uliopita serikali ilipiga marufuku waganga wa kienyeji sambamba na kupiga marufuku wapiga ramli wote ambao wanaelezwa kuchangia mauaji ya watu hao wenye ulemavu wa ngozi. Haihitaji ujuzi wa kuchambua matamko ya serikali kumaizi kuwa amri hiyo ilikuwa ni porojo kama zilivyo porojo nyingine kuhusu ufisadi, ujangili, madawa ya kulevya, nk.

Lakini pia ni muhimu kujiuliza, kwanini mauaji ya albino yamekuwa yakiongezeka kila tunapokaribia uchaguzi mkuu. Katika mazingira ya kawaida tu ni rahisi kutambua kuwa baadhi ya wanasiasa wetu ni wateja wa waganga wa kienyeji wanaotoa masharti ya kupatiwa viungo vya albino ili ‘kuwasafishia mambo’ wanasiasa hao.

Na katika suala hilo linalohusiana na ushirikina, nina mifano miwili hai. Nina ndugu yangu kiukoo ambaye ni mganga huko wilayani Kilombero. Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, mmoja wa wagombea urais alilala katika makazi ya mganga huyo ili ‘kutengenezwa’ kwa ajili ya uchaguzi huo.

Kadhalika, wakati huohuo, mmoja wa watendaji wakuu wa taasisi moja nyeti alikumbwa na kashfa ya kuajiri waganga wa kienyeji ili wamsaidie kupata ukurugenzi mkuu. Japo hakufanikiwa katika azma yake hiyo, mtendaji huyo kwa sasa ni mwakilishi wetu katika nchi moja jirani.

Mifano hiyo hai inaonyesha ni kwa jinsi gani imani za kishirikina zilivyoota mzizi katika Tanzania yetu. Na suala la ushirikina si kwa wanasisasa au ‘vigogo’ wengine pekee kwani wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam, kwa mfano, wanafahamu kuhusu misururu ya magari inayoelekea Mlingotini hasa mwishoni mwa wiki katika kinachoaminika kwenda kutafuta huduma za waganga wa kienyeji.

Nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nilisoma Sosholojia ya Dini ambapo pamoja na mambo mengine tulifundishwa kuhusu imani za asili. Kimsingi, kabla ya ujio wa ‘dini za kimapokeo’ yaani Uislam na Ukristo, ‘dini’ kuu ilikuwa imani za asili. Takriban kila jamii ilikuwa na wataalamu wa tiba, ambao kwa mazingira ya sasa ni sawa na waganga wa asili. Uji0 wa dini za kimapokeo haukufanikiwa kuondoa imani za asili, lakini ‘kwa bahati mbaya’, wakati utabibu wa asili zama hizo ulilenga katika kutatua ya mtu binafsi, ‘mabadiliko’ katika fani hiyo yalipelekea ‘matibabu’ hayo kujumuisha kudhuru watu wengine.

Kwa mujibu wa maelezo ya ndugu yangu anayejishughulisha na uganga wa jadi huko wilayani Kilombero, kuna waganga wanaozingatia ‘asili ya fani hiyo’ ambao kamwe hawakubali kufanya tiba za kumdhuru mtu. Hata hivyo, alinieleza kuwa kutokana na ukosefu wa maadili, tamaa na ugumu wa maisha, idadi kubwa ya waganga sio tu ‘wanadhuru walengwa’ bali pia hutumia dawa zinazotokana na madhara kwa binadamu, kwa mfano viungo kama hivyo vya albino.

Tufanyeje? Ni vigumu kupata ufumbuzi mwepesi kwa tatizo hili kubwa. Amri ya serikali kupiga marufuku waganga wa kienyeji na ramli ni ya kipuuzi, kwa sababu kama serikali hiyohiyo inashindwa kuwadhibiti mafisadi wanaokwapua mabilioni sehemu kama Benki Kuu penye CCTVs lukuki itawezaje kuwabana waganga na wapiga ramli wanaofanya shughuli zao kwa siri?

Binafsi, kama nilivyobainisha awali, ufumbuzi wa tatizo la mauaji ya albino ni wapaswa kuwa wa kibinadamu (humanity) zaidi kuliko kisheria (legislative). Wanunuzi wa viungo vya albino twaishi nao katika jamii zetu, kama ilivyo kwa wahalifu wanaiwinda na kuuwa ndugu zetu hao. Kadhalika, waganga wanaotumia viungo vya binadamu twaishi nao katika jamii zetu. Kinachohitajika ni kuweka mbele ubinadamu wetu ili kuwadhibiti maharamia hao.

Japo serikali ina jukumu la msingi la kuhakikisha usalama wa raia wake, na Katiba yetu inasisitiza umuhimu wa haki ya kuishi, sote twafahamu kuhusu uzembe wake katika masuala yanayohusu ‘wanyonge.’ Mazingira tu wanayoishi watawala wetu ni kinga tosha kwao na jamaa zao kudhuriwa na wanaiwinda viungo vya binadamu. Na taarifa kwamba baadhi ya wanasiasa na ‘vigogo’ wengine ni wateja wa waganga wanaohitaji viungo vya albino zinafanya utegemezi kwa serikali kuwa ‘kazi bure.’

Nimalizie kwa kuhamasisha wakazi wa jiji la Dar kujitokeza kwa wingi katika maandamano yanayotarajiwa kufanyika hivi karibuni kulaani mauaji ya albino na kushinikiza hatua kali kuchukuliwa dhidi ya wahusika. Sambamba na hilo, ninashauri maandamano hayo yafanyike nchi nzima ili kufikisha ujumbe kuwa hatuwezi kuvumilia mateso na mauaji kwa ndugu zetu albino.

Na kwa Watanzania wanaotumia mitandao ya kijamii, ninawasihi waendelee kutumia ‘hashtag’ #StopAlbinoKillings angalau mara moja kwa siku.

#StopAlbinoKillings (Zuwia Mauaji ya Albino)

19 Feb 2015


WIKI iliyopita kuliibuka video ‘ya kutisha’ ambayo msemaji katika video hiyo alidai kuwa yeye na wenzake ni kundi ambalo limekuwa likivamia vituo vya Polisi na kupora silaha.
Kadhalika, msemaji huyo ambaye licha ya kujitambulisha kama Abu (magaidi wengi hupendelea jina hilo japo si kila Abu ni gaidi) hakubainisha jina la kikundi chake.


Vilevile, msemaji huyo aliyeficha sura yake kwa kifunika-uso (balaclava) na miwani nyeusi ya jua (sunglasses) alidai kuwa kundi lake limefanikiwa kupora silaha katika vituo vya Polisi huko Ushirombo, Ikwiriri na Tanga, na walifanya hivyo pasipo kutumia silaha yoyote.
La kuogofya zaidi, msemaji huyo alidai kwamba tayari wana mtaji wa ‘roho tano za polisi,’ akimaanisha wameshauwa polisi watano.


Japo nina ujuzi wa wastani tu kuhusu masuala ya ugaidi, zaidi kwa kufuatilia habari zinazohusu suala hilo na harakati za vikundi vya kigaidi duniani, nikiri kwamba nilipoiona video hiyo kwa mara ya kwanza niliamini. Sababu kubwa ya kuiamini ni kwamba tishio lililomo kwa video hiyo lilionekana halisi.


Hata hivyo, baada ya kuiangalia mara kadhaa, nilijikuta nikipatwa na maswali kadhaa. Miongoni mwa maswali hayo ni:


Kwanini msemaji anaonekana kama anafikisha ujumbe kwa Inspekta Jenerali wa Polisi ‘kwamba hawezi kazi’ kwa vile ameshindwa kuwakamata ‘magaidi’ hao? Kwa uchambuzi wa haraka, katika hilo ni kama ‘magaidi’ hao wana lengo la kumchafua tu IGP.


Katika video hiyo, ‘magaidi’ hao wanamtaja Rais kwa kumuita ‘Mheshimiwa Rais.’ Hii si lugha ya kawaida kwa magaidi halisi.Kwa sababu pamoja na mambo mengine, malengo yao huendeshwa na chuki kwa utawala uliopo madarakani. Licha ya kumuita Rais ‘Mheshimiwa,’ msemaji anaonekana kumshawishi ‘Mheshimiwa Rais’ kuwa hana polisi, na kwamba hawajaona jeshi dhaifu kama la polisi. Hapa tena inaonekana lengo la msemaji au kikundi hicho ni kulichafua jeshi la polisi.

Ni kawaida kwa vikundi vya kigaidi wanapotoa tishio kama hilo la kwenye video hiyo kutaja madai yao. Labda kama video hiyo ni mwanzo wa mfululizo wa video, ingetarajiwa msemaji huyo kueleza kuwa lengo lao ni nini na madai yao ni yapi.
Linaloshabihiana na hilo ni video hiyo kutotajwa mlengwa wa ‘hasira’ zao ni nani. Pamoja na msemaji kutumia maneno ya Kiarabu na kutamka ‘ujumbe kwa vijana wa Kiislamu’, hakuna mahala katika video hiyo ambapo wanazungumziwa wasio- Waislam (kwa mfano Wakristo) wala serikali au taasisi zake au taasisi binafsi au mtu/kundi la watu.
Pamoja na maswali hayo, haimaanishi kuwa ujumbe huo ni wa ‘kizushi’ tu. Kama nilivyeoeleza awali, tishio lililomo katika video hiyo linaonekana kuwa halisi. Tatizo ni katika uwasilishaji wake kama nilivyoonyesha hapo juu. Hata hivyo, kasoro hizo zaweza kuwa ni za kiufundi tu.
Kinachochanganya zaidi ni ukweli kwamba takriban siku moja baada ya kuibuka video hiyo, zilipatikana habari za mapambano makubwa kati ya jeshi la polisi likisaidiwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ) na kikundi kimoja kwenye Mapango ya Amani huko Tanga.
Mkanganyiko zaidi ni kuhusu utambulisho wa kikundi hicho. Wakati baadhi ya vyombo vya habari vimeliita kundi hilo ‘magaidi wa Al-Shabaab,’ vingine vimedai ni kikundi chenye uhusiano (affiliated) na magaidi hao wa Somalia, huku vyombo vingine vya habari vikieleza kuwa kundi hilo ni genge tu la wahuni (thugs), kama maelezo ya Kamanda Chagonja wa polisi yalivyotanabaisha.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana katika vyombo mbalimbali vya habari, baadhi ya wakazi wa eneo husika wamedai kuwa kundi hilo ni la kigaidi, huku wakililaumu jeshi la polisi kwa kuficha ukweli, na kuhoji iweje nguvu kubwa kiasi hicho itumike kukabiliana na genge la wahuni tu.
Taarifa zinadai kuwa polisi mmoja aliuawa katika mashambulio hayo na wengine kadhaa kujeruhiwa. Hata hivyo, Kamanda Chagonja alinukuliwa akidai kuwa ‘wahuni’ hao walifanikiwa kutoroka.
Wakati kiongozi huyo mwandamizi wa jeshi la polisi akieleza kuwa genge hilo si la magaidi, huhitaji uelewa wa fani ya uchunguzi wa kipelelezi kujiuliza “amejuaje ilhali hawakufanikiwa kumkamata japo mhusika mmoja wa kundi hilo?”
Nadhani moja ya matatizo ya mwanzo kabisa katika sakata hili la Amboni na lile la video ya ‘magaidi’ ni ukweli kwamba jeshi la polisi haliaminiki kabisa na linachukiwa na Watanzania wengi.
Sababu za kuchukiwa zipo wazi; ukiukwaji wa hali ya juu wa haki za binadamu, sambamba na ukandamizwaji demokrasia kwa uonevu wa waziwazi dhidi ya vyama vya upinzani na viongozi na wanachama wao, pamoja na rushwa iliyokithiri ndani ya chombo hicho cha dola, kama ilivyothibitishwa na utafiti mmoja wa hivi karibuni.
Hadi wakati ninaandika makala hii kumeshajitokeza madai kuwa matukio hayo mawili ni mkakati wa jeshi la polisi kuandaa mazingira ya kuvibana vyama vya upinzani. Baadhi ya watu wanadai kuwa jeshi la polisi linaweza kuwa linaandaa mkakati wa kupiga marufuku shughuli za kisiasa za wapinzani, kama vile mikutano ya hadhara na maandamano, kwa kigezo cha ‘tishio la ugaidi.’
Baadhi ya wananchi wanayahusisha matukio hayo na ‘hadithi’ ya aliyekuwa Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Omari Mahita, alipotoa tuhuma nzito siku moja kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 kuwa chama cha CUF kimeingiza makontena ya visu na majambia kwa minajili ya kuvuruga uchaguzi huo.
Pengine kilichonichekesha wakati ninatafakari kuhusu matukio haya mawili, ni bandiko la mwanachama wa mtandao mahiri wa kijamii, Jamii Forums, aliyehitimisha kuwa, ninamnukuu, “Chagonja na sinema ya mwaka: Unajivamia, unajiteka, unajitorosha, unajisaka, na hatimaye unatangaza kujitafuta kwa udi na uvumba. Matukio yote haya hayana majina ya waathirika. Kweli siasa zimefika mahali pake. Tutashuhudia mengi 2015”
Huwezi kuwalaumu wanaohisi matukio hayo mawili ni ‘mchezo mchafu tu’ hasa ikizingatiwa kuwa licha ya polisi kutoaminiwa na kuchukiwa, chama tawala CCM ni mahiri kwa ‘uzushi’ dhidi ya wapinzani wake.

Ninaamini wengi mwakumbuka kuhusu tuhuma lukuki dhidi ya Chadema, kutoka chama cha Kikristo, cha Wachagga, na hatimaye cha kigaidi. Tumeshuhudia pasi aibu CCM ikijaribu kuwahusisha wapinzani na maafa yaliyofanywa na jeshi la polisi, hadi kufikia hatua ya kudai kuwa Chadema ndio waliomuuwa mwandishi Daudi Mwangosi aliyeuawa kikatili na jeshi la polisi.
Kwa hiyo tupo njia panda. Yawezekana kabisa kuwa tukio la video yenye tishio la kigaidi ni ya magaidi kweli na kundi lililokuwa limejificha Mapango ya Amboni kuwa ni la kigaidi halisi, lakini rekodi za polisi na CCM zinaleta ugumu katika kuamini kipi ni cha kweli na kipi ni usanii tu.
Hilo lina madhara makubwa kwa sababu kama kweli matukio hayo ni ya kigaidi, kinachohitajika si nguvu za vyombo vya dola pekee bali ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwa wananchi. Lakini hali ilivyo sasa hasa kuhusu jeshi la polisi ni mbaya, japo watawala wetu hawaonekani kujali.
Na iwapo matukio hayo ni ya kigaidi kweli, tuna matatizo mawili makubwa: mipaka yetu ipo ‘porous’ sana (inapenyeka kirahisi, na ushuhuda ni jinsi ‘unga’ unavyoingizwa na kutoka kirahisi kana kwamba ni bidhaa halali inayoingizwa na kutolewa nchini kihalali). Na tatizo la pili ni rushwa.
Japo ni vigumu kuzuwia ugaidi kwa asilimia 100, nchi ilivyotapakaa rushwa inafanya mapambano dhidi ya ugaidi kuwa magumu mno kwa vile rushwa inawawezesha magaidi kununua fursa ya kufanya hujuma zao kirahisi.
Nimalizie makala hii kwa kutoa wito kwa mamlaka husika kuyachukulia matukio hayo mawili kwa uzito mkubwa, sambamba na kumsihi Rais Jakaya Kikwete kuupa uzito uhasama kati ya wananchi na polisi.
Kadhalika, pamoja na kutokuwa na imani nalo, ninalisihi jeshi la polisi kujaribu kuwa wazi katika kuripoti matukio mbalimbali yanayohusu usalama wa raia na nchi kwa ujumla.

16 Feb 2015

Mwishoni mwa wiki iliyopita zilipatikana taarifa kwamba serikali ya Kenya imepiga tena marufuku magari ya uchukuzi wa watalii yaliyosajiliwa Tanzania.

Hii ni mara ya pili kwa serikali ya Kenya kuchukua hatua hiyo, ambapo mwaka jana ilitangaza amri hiyo ya kuzuwia magari yaliyosajiliwa Tanzania kuchukua, kushusha au kubadilishana abiria katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Utalii, Biashara na Masuala ya Afrika Mashariki wa nchi hiyo, Phyllis Kandie, hatua hiyo mpya inafuatia kupita kwa muda wa wiki tatu zilizoombwa na Waziri mwenzie wa Tanzania, Lazaro Nyalandu, ili yafanyike majadiliano kuhusu suala hilo, lakini muda huo ulipita pasi ofisa yeyote wa Tanzania kujitokeza.

“Wiki hizo tatu zimepita bila wenzetu wa Tanzania kujitokeza kwa ajili ya majadiliano. Kwahiyo tumeendelea mbele kutekeleza makubaliano ya pande mbili,” alisema Waziri Kandie akirejea Mkutano wa Tano wa Kisekta wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhusu mwafaka wa utalii na wanyamapori.

Suala hili lilionekana kutawala mijadala mwishoni mwa wiki katika mitandao ya kijamii hususan Twitter na Facebook, huku Mbunge wa Kigoma Kusini (Chadema) Zitto Kabwe akitoa wito kwa Tanzania kulipiza kisasi kwa kuzuwia ‘maziwa ya Rais Uhuru Kenyatta.’ Namnukuu, “Naona ndugu zetu wa Kenya wameamka. Mjadala umeisha! Mnaendelea na ban yenu, we respond in kind. Rais wenu atafute pa kuuza maziwa yake (akimaanisha maziwa chapa Brookside yanayodaiwa kutengenezwa na kiwanda kinachomilikiwa na Rais Uhuru Kenyatta).”

Baadaye, mwanasiasa machachari wa Kenya, Seneta Mike Sonko, naye aliingilia kati mjadala huo na kudai angekwenda Tanzania kumtaka Zitto aombe radhi “kwa kumtisha na kumtapeli Rais wa Kenya na Mwenyekiti wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Uhuru Kenyatta.”

Kwa mtizamo wangu, wakati ninadhani Kenya wanapaswa kuwa wastahimilivu katika kusaka ufumbuzi wa suala hilo, ninawaona watendaji wetu serikalini kama wahusika wa moja kwa moja kwa ‘uzembe’ wao. Kwa upande mmoja, maelezo ya Waziri Kandie kwamba maafisa wa serikali yetu hawakufanya lolote katika muda wa wiki mbili waliiomba wapewe kushughulikia suala hilo, yanaashiria uzembe wa wazi. Busara ndogo tu zinatosha kueleza kuwa kama pande mbili zenye mgogoro zimeafikiana kukutana baada ya muda flani, kisha pande moja ‘ikapuuzia,’ hiyo inatoa fursa kwa upande mwingine kuchukua hatua inazoona zinafaa.
Kwa vile sie tumeruhusu nchi yetu kuwa ‘uwanja wa wazi’ kwa wafanyabiashara halali na hata haramu (kama wauza mihadarati) haimaanishi majirani zetu nao wafuate ukosefu huo wa busara. Ni katika mazingira kama haya, licha ya nchi yetu kuwa pekee kwa ‘uzalishaji’ wa madini ya Tanzanite, ni India na Kenya zinazoongozwa kwa mauzo ya madini hayo duniani.

Kwa upande mwingine, tatizo hili la sasa la Kenya kupiga marufuku magari ya uchukuzi wa watalii yenye usajili wa Tanzania ni matokeo ya uzembe mwingine mkubwa wa kupuuzia kurejea uhai wa shirika letu la ndege na kuboresha viwanja vyetu vya ndege hasa ule wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Haiingii akilini kabisa kwa nini nchi yetu yenye umri wa zaidi ya nusu karne isiwe na shirika lake la ndege lenye uwezo wa kutoa huduma za kimataifa, ilhali wenzetu Kenya sio tu wana shirika lao la ndege bali ni Kenyan Airways ni miongoni mwa mashirika ya ndege makubwa duniani.
Sie tunaendekeza ngonjera kila kukicha. Mara ATCL imepata mwekezaji kutoka Uarabuni, mara China inakuja kuwekeza...alimradi ni mwendelezo wa porojo tu zinazoambatana na ufisadi. Ripoti mbalimbali zimeonyesha jinsi gani ATCL ilivyouawa ikiwa hai na jitihada za ufisadi zinavyokwamisha kufufuka kwake. Kama ilivyo kwa ufisadi kwenye maeneo mengine, waliofisadi shirika hilo wakati wa uhai wake, na wanaofisadi likiwa mfu bado wapo mtaani, hali inayowashawishi mafisadi watarajiwa kuendeleza uhalifu.

Mara kadhaa utasikia viongozi wetu wakienda ng’ambo kutangaza vivutio vya utalii nchi mwetu. Sawa hilo ni jambo la manufaa, lakini sambamba na hatua hiyo ilipaswa viongozi hao kuwekeza vya kutosha katika kuboresha miundombinu ya utalii, ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege. Majuzi tu nilitumiwa video inayoonyesha jengo la wageni maalum katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar, likiwa linavuja ‘chapa chapa’ kutokana na mvua.

Ni muhimu kutambua kwa hawa wenzetu huku Ulaya, kwa mfano, likizo zinazoambatana na kutembelea nchi za nje ni moja ya mambo muhimu mno maishani. Baada ya kujituma vya kutosha, na kuhifadhi fedha zao, wanafikia uamuzi wa kutembelea sehemu flani kama watalii. Na hawa sio kama sie wa kuvumilia mgao wa umeme milele; they never settle for less (hawakubali kupewa pungufu ya kile wanachostahili). Sasa mtalii anapofika Tanzania mara ya kwanza na kukuta ukumbi wa kupokelea wageni unavuja kama umeezekwa kwa nyasi, ni wazi tushampoteza mtalii huyo. Na pia wenzetu wana kawaida ya kutoa ‘reviews’ kuhusu maeneo ya utalii. Kwa maana hiyo ‘kumuudhi’ mtalii mmoja kwaweza kupelekea kupoteza watalii tarajiwa kadhaa.

Nimekuwa nikizungumzia suala hili mara kadhaa: sie hatuna uhaba wa sera na mipango mizuri. Ukisikia hotuba za bajeti za mawaziri wetu, au wanapopiga porojo kwenye mikutano ya ndani na nje ya nchi, hutoonekana wa ajabu ukidhani ni mawaziri kutoka ‘nchi ya dunia ya kwanza.’ Utasikia maelezo matamu na mikakati ya kimapinduzi lakini tatizo ni kwenye utekelezaji. Na kikwazo kikubwa cha utekelezaji wa sera au mipango hiyo ni kutanguliza mbele maslahi binafsi badala ya maslahi ya taifa. Vitambi vyao, mahekalu yao, idadi ya magari yao, na hata ustawi wa ‘nyumba ndogo’ zao vinakuwa na umuhimu mkubwa kuliko maendeleo ya taifa letu au urithi kwa vizazi vijavyo.

Wakati mjadala kuhusu zuio hilo la magari yetu kuingia nchini Kenya ukiendelea, kulijitokeza mawazo kuwa rafiki wa kweli wa Tanzania sio katika Ushirikiano wa Afrika Mashariki bali Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Ukweli ni kwamba hakuna rafiki atakayekuwa na faida kwetu kama sie wenyewe hatujithamini wala kufanya jitihada za kuonekana wa maana kwa nchi nyingine. Ni muhimu kukumbuka kwamba Mwalimu Nyerere alitufundisha kuwa ili tuendelee twahitaji ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Hakutaja marafiki, kwa sababu nchi yenye maendeleo lazima itapata marafiki. Raslimali tunazo ‘bwerere,’ na watu wapo takriban milioni 50. Uongozi bora na siasa safi je? Hapo ndio tunapokwama.

Basi nimalizie makala hii kwa kutarajia kuwa tatizo hilo kati ya nchi yetu na majirani zetu wa Kenya litamalizwa karibuni. Hata hivyo, ufumbuzi wa kudumu haitoishia kwa Kenya kuruhusu magari ya ukuchuzi wa watalii yenye usajili wa Tanzania bali sie wenyewe kuhakikisha kuwa tunafufua shirika letu na ndege na kuliwezesha kufanya safari za kimataifa kama ilivyo kwa Kenyan Airways, sambamba na kuboresha viwanja vyetu vya ndege, hususan KIA ili tuache utegemezi kwa viwanja vya ndege vya nchi jirani, kwa mfano huo wa Jomo Kenyatta.

Viongozi wetu wakiacha porojo, uzembe na kutafuta visingizio visivyo na kichwa wala miguu, basi hakuna cha kutukwamisha kufanikiwa. 

6 Feb 2015

WIKI iliyopita, kwa mara nyingine tena, Watanzania walishuhudia jinsi Jeshi la Polisi lilivyo mahiri katika ukiukaji wa haki za binadamu baada ya kuwapiga na kuwajeruhi wanachama wa CUF pamoja na Mwenyekiti wao, Prof Ibrahim Lipumba kwa ‘kosa la kuandamana kinyume na maagizo ya jeshi hilo.’
Kwa hakika nilitokwa na machozi nilipoangalia video ya tukio hilo ambayo imesambaa mtandaoni. Vipande vya video hiyo ambavyo vilinitia uchungu zaidi ni pale binti mdogo tu alipopigwa vibaya na polisi kadhaa wa kiume, na pale waandamanaji hao waliposhushwa kwenye magari ya polisi na kurushwa kichura kuingia kwenye kituo cha polisi. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Lakini pamoja na tukio hilo kusikitisha mno, binafsi sioni kama ni la kushangaza kwani sote twakumbuka ruhusa iliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa polisi kuwa “(wananchi) wapigwe tu.”
Ukiangalia video hiyo kwa makini (waweza kuiona hapa http://goo.gl/zbmnTG
(link is external)
) utabaini ukweli mmoja wa kutisha. Angalia dakika ya 03:14 hadi dakika ya 03:19, baadhi ya waandamanaji wanasema "TUUENI..."

Angalia pia kuanzia dakika ya 3.21 ambapo polisi wanaanza kurusha risasi (sina hakika kama ni risasi za moto au bandia) lakini kitu cha kukiangalia kwa makini ni ukweli kwamba ukiacha watu wachache wanaoonekana kutishwa na milio hiyo ya risasi, idadi kubwa tu ya watu inaonekana kutotishika. Hali hiyo inaendelea hata baada ya 'king'oling'oli' cha polisi kinapooanza kulia na hatimaye polisi kutembeza kipigo cha kinyama.
Licha ya kuumia mno kuona Polisi wakitumia nguvu kubwa katika tukio ambalo lingeweza kabisa kumalizwa kwa amani pasipo haja ya kurusha risasi japo moja au kuwapiga na hatimaye kuwakamata waandamanaji akiwemo Mwenyekiti wa CUF Prof Lipumba, kilichonipa hofu ni jinsi taratibu wananchi wanavyoanza kuota 'usugu' dhidi ya unyanyasaji wa polisi.
Inapofika mahala wananchi wanaashiria bayana kuwa wapo radhi kuuawa, na kuwaambia polisi waziwazi kuwa TUUENI, basi kwa haki tumeshafika mahala pabaya. Na kama nilivyobainisha hapo juu, na kama inavyoonekana kwenye video hiyo, imefika mahala wananchi wameanza kuzowea sauti za risasi sambamba na mabomu ya machozi.

Hii ina maana gani? Wakati tayari wananchi wameshaonyesha kuzowea unyanyasaji na unyama wa polisi wetu na kuwa tayari kwa lolote lile, yayumkinika kubashiri kuwa kuna siku sio tu wananchi wataweka kando uoga na kuendeleza 'usugu' huo nilioueleza hapo juu bali pia wanaweza kujibu mashambulizi.
Uchambuzi mwepesi ni kwamba wakati polisi hawana njia nyingine zaidi ya hizi wanazotumia kila siku: kutumia nguvu kuvunja maandamano ya amani, wananchi wanapata nguvu mpya kwa kuondoa uoga na kuwaacha polisi wafanye watakalo. Upo uwezekano wa wananchi hao kutoishia hapo tu bali badala ya kuwaachia polisi wawaonee, WANAWEZA KUJIBU MASHAMBULIZI. Na kwa mwenendo ulivyo, hatuko mbali na hali hiyo.
Ni vigumu kubashiri ni lini polisi wetu watathamini haki za binadamu na uhai wa wananchi wasio na hatia. Ni vigumu zaidi kutarajia mabadiliko kutoka kwa mwana-CCM yoyote yule atakayemrithi Kikwete baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Na ndio maana hatujaskia yeyote kati ya waliotangaza nia ya kuwania Urais kupitia CCM akilaani unyama huo wa polisi. Kwanini walaani ilhali wao wana kinga ya kudumu dhidi ya uonevu na unyama wa polisi wetu? Japo Rais kutoka chama cha upinzani anaweza kutugeuka, lakini katika mazingira ya kawaida ya kibinadamu angalau yeye naye atakuwa ameshaonja unyama wa polisi wetu na ni rahisi kwake kuchukua hatua kuliko hao wasioguswa na polisi.
Mmoja wa wana-CCM waliotangaza nia ya kugombea urais, January Makamba, amekuja na kauli-mbiu ya ‘Tanzania mpya.’ Nadhani moja ya maeneo yanayopaswa kuwa mapya katika Tanzania hiyo mpya ni utendaji kazi wa jeshi letu la polisi. Hata hivyo, pamoja na umuhimu wa upya katika maeneo mbalimbali yanayoihusu nchi yetu, tatizo kubwa ninaloliona ni udhati katika utekelezaji wa dhamira hiyo. Lakini pia kuna suala la lini hiyo Tanzania mpya ianze kama sio sasa? Nadhani jibu rahisi ni kwamba uhuni unaofanywa na jeshi letu la polisi sio suala la bahati mbaya. Ni mkakati madhubuti unaoinufaisha CCM dhidi ya wapinzani wake.
Kwanini iwe ruhusa kwa CCM kuandamana muda wowote wanaotaka lakini wapinzani wakiomba kufanya maandamano wanakataliwa?
Sasa pamoja na dhamira nzuri ya January ya kutuletea Tanzania mpya, ni wazi CCM haiwezi kuruhusu tuwe na ‘jeshi la polisi jipya’ litakaloendana na ‘Tanzania mpya’ kwa vile hali hiyo itatoa mazingira bora ya kushamiri kwa demokrasia huko nyumbani, na hili litaiathiri CCM.
Tukirejea kwenye tukio hilo la kinyama dhidi ya wana-CUF wasio na hatia, mazingira yote yanaonyesha sio tu kuwa hakukuwa na haja kwa polisi kutumia mabavu bali pia lingeweza kumalizwa kwa amani.

Lakini kwa polisi waliozowea kufanya ubabe, kulimaliza suala hilo kwa amani kungewafanya wajiskie kama ‘wameshindwa kazi.’ Au huenda walihofia ‘kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa kukiuka agizo la Waziri Mkuu Pinda kuhusu kupiga raia.’
Ukweli mchungu ni kwamba jeshi la polisi litaendelea na unyama wake kwani hakuna dalili yoyote ya serikali kuchukua hatua za kukomesha tabia hiyo. Na kwa vile tunaelekea msimu wa uchaguzi ambapo miongoni mwa shughuli za kawaida kisiasa katika chaguzi ni pamoja na maandamano na mikutano, kuna uwezekano mkubwa wa kushuhudia wanachama wa vyama vya upinzani na/au viongozi wao wakinyanyaswa na polisi wetu.
Nihitimishe makala hii kwa kurejea tahadhari niliyoitoa hapo juu.

Ipo siku wananchi wanaonyanyaswa na polisi wetu wataamua ‘liwalo na liwe’ na watajibu mashambulizi. Japo ninaomba Mungu atuepushe tusifikie hatua hiyo, ukweli mchungu ni kwamba twaelekea huko. Imefika mahala wananchi wanawaambia polisi waziwazi “tuueni” na wanasikia milio ya risasi lakini hawakimbii.
Yayumkinika kuhisi kuwa kitakachofuata si wananchi kuwapa polisi uhuru wa kuwapiga na kuwajeruhi bali kupambana nao kwa nguvu zote. Ni sihitaji kukumbusha kuwa polisi wetu ni sehemu ndogo tu kulinganisha na umma wa wasio-polisi.

TUSIPOZIBA UFA TUTAJENGA UKUTA

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.