Moja ya mambo yaliyokuwa yakiwaumiza vichwa wafuasi wa Barack Obama wakati wa kinyang'anyiro kati yake na Hillary Clinton kupata mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democrats mwaka 2008 ni theory inayofahamika kama Bradley Effect.Kwa kifupi kabisa,Bradley Effect (au Wilder Effect) ni hali inayoweza kutokea kwenye kura za maoni katika chaguzi nchini Marekani panapokuwa na mgombea Mweupe (White) na asiye mweupe (non-White).Pengine ili wasionekane wabaguzi wa rangi,wahojiwa Weupe katika kura za maoni hueleza kuwa chaguo lao ni mgombea asiye Mweupe au husema kuwa hawajafanya uamuzi kuhusu chaguo lao (Undecided).
Kwahiyo,matokeo ya kura ya maoni yanaweza kuonyesha mgombea asiye Mweupe anapendwa zaidi kuliko mgombea Mweupe lakini inapofika kwenye hatua ya kupiga kura (ambapo mpiga kura anakuwa peke yake),wapiga kura Weupe wanampigia Mweupe mwenzao.
Asili ya Bradley Effect ni katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa uchaguzi wa gavana wa jimbo la California mwaka 1982 ambapo licha ya mgombea Mweusi,Meya wa Jiji la Los Angeles Tom Bradley kuongoza kura za maoni,aliishia kushindwa uchaguzi huo kwa mgombea Mweupe George Deukmejian.
Baadhi ya wachambuzi wa chaguzi nchini Marekani wanaamini pia kuwa Bradley Effect ilijitokeza tena kwenye mchakato wa kumpata mgombea wa chama cha Democrats kwenye jimbo la New Hampshire ambapo licha ya Obama kuongoza katika kura za maoni,Hillary Clinton aliibuka mshindi kwenye jimbo hilo (japokuwa baadaye Obama alifanikiwa kuibuka mshindi wa jumla,na kupitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Democrats,na hatimaye kushinda nafasi ya urais).
Katika post hii najaribu kubashiri (hypothesize) namna Bradley Effect inavyoweza kuwa sababu ya mgombea wa CCM,Jakaya Kikwete,kuongoza katika tafiti za taasisi za Redet na Synovate kuhusu nafasi za wagombea urais katika uchaguzi mkuu wa Tanzania hapo Oktoba 31.Hapa ntawazungumzia wagombea wawili tu,Kikwete na mgombea urais kwa tiketi ya Chadema,Dokta Wilbroad Slaa.
Japo Bradley Effect 'halisi' inahusu mgombea Mweupe na asiye Mweupe,sababu inayopelekea matokeo ya kura kutorandana na mwelekeo wa kura za maoni inaweza kutumika kuelezea kwanini kura za maoni za Redet na Synovate zilimpa Kikwete ushindi na sio Dokta Slaa.Kama ilivyo kwenye chambuzi mbalimbali,kuna mambo flani inabidi 'kupuuzwa' ili kufikia matokeo yanayokusudiwa.Katika uchambuzi huu,naomba 'nipuuze' urafiki kati ya taasisi hizo na CCM na badala yake nikazanie kwenye uwezekano wa Bradley Effect pekee.
Inawezekana kabisa kuwa wahojiwa kwenye tafiti za Redet na Synovate ni wananchi waliotoa majibu 'kuwaridhisha watafiti',yaani walisema wanampenda zaidi Kikwete kuliko Dokta Slaa.Moja ya sababu za kutoa majibu ya aina hiyo ni mazingira halisi ya Tanzania ambapo licha ya 'siasa za mkono wa chuma' za zama za chama kimoja kuonekana kama historia,ukweli unabaki kuwa baadhi ya wananchi wanaamini kuwa kusema lolote lisilowapendeza watawala ni kujitafutia matatizo.
Naomba kufafanua kidogo katika hilo.Nilipokwenda Tanzania mwaka 2005 kufanya fieldwork ya utafiti wangu wa shahada ya uzamifu (PhD) nilikumbana na wakati mgumu kuwahoji baadhi ya maustaadh (mada yangu inahusu masuala ya Waislam na Uislam nchini Tanzania) kwa vile baadhi yao walidhani mie ni wakala wa serikali niliyetumwa kuwachunguza ili 'serikali iweze kuwadhibiti zaidi'.Bahati mbaya,fieldwork hiyo ilifanyika wakati jeshi la polisi lilikuwa linamsaka mwanaharakati wa Kiislam,Sheikh Issa Ponda.Ilichukua kitambo kujenga uaminifu kati yangu na maustaadh hao.
Kuna wanaoilaumu Redet na Synovate kuhusu aina ya watu waliohojiwa wakidai kuwa huenda wahojiwa walikuwa watu walio karibu na CCM (kwa mfano mabalozi wa nyumba kumi).Uwezekano wa Bradley Effect 'yetu' (yaani isiyohusiana na ishu za ubaguzi wa rangi) ni mkubwa kwa vile wahojiwa wanaweza kutoa majibu yasiyoonyesha 'wanambagua mgombea wao' na hivyo kusema huyo ndio chaguo lao japo mioyoni wana dhamira na/au chaguo tofauti.
Of course,inawezekana tafiti hizo za Redet na Synovate 'zilipikwa' ili kuendana na matakwa ya CCM.Inawezekana pia kuwa aina ya watu waliohojiwa ni ambayo isingetoa majibu tofauti na 'ushindi kwa Kikwete'.Lakini,kama makala hii inavyojaribu kubashiri,inawezekana kabisa kuwa wahojiwa 'waliwazuga' jamaa wa Redet na Synivate 'ili isiwe shida'.Nani yuko tayari kuona genge lake au kibanda cha biashara kinabomolewa kwa vile tu amechoshwa na namna CCM inavyozidi kuahidi maisha bora lakini wanaonufaika ni mafisadi pekee?Mtu wa aina hii haoni shida 'kudanganya leo' kisha 'akaungama siku ya kupiga kura' kwa 'kumwadhibu Kikwete na CCM kwenye sanduku la kura ambapo hakutokuwa na wa kumtoa mimacho kwanini hajampigia kura Kikwete au CCM'.
Huu ni ubashiri tu.Unaweza kuwa sio sahihi lakini kama zilivyo bashiri nyingine-hususan zinazoambatana na mifano hai-unaweza kuwa na ukweli ndani yake.Kadhalika,Bradley Effect 'yetu' inaweza kutoa matokeo ya kuwashangaza wote wenye imani kuwa CCM na Kikwete watarudia kupata ushindi wa kishindo kama wa mwaka 2005.
Pengine kuna watakaohoji kwanini Bradley Effect 'yetu' haiwezi kutumika kwenye utafiti mwingine (wa TCIB) unaoonyesha kuwa Dokta Slaa anaongoza.Jibu langu ni kwamba watoa maoni hawana cha kupata (nothing to gain) kuwadanganya watafiti kuwa wanampenda Dokta Slaa wakati ukweli wanayempenda ni Kikwete.Likewise,kwenye tafiti za Redet na Synovate,inawezekana baadhi ya wahojiwa walikuwa na cha kupoteza laiti wangesema hawampendi Kikwete (si unajua kuhusu umoja na mshikamano ndani ya chama?).Vilevile,yawezekana wahojiwa hawakuwa na cha kupoteza (nothing to lose) kwa kudanganya kuwa wanampenda Kikwete (kwa minajili ya kuwaridhishwa watafiti na 'kulinda ugali wao') kisha wakamnyima kura katika usiri wa chumba cha kupigia kura.
Mwisho,naomba kusisitiza tena kuwa hypothesis hii imejaribu kupuuza sababu za 'wazi' kama vile upendeleo wa watafiti,uoga wa wahojiwa,na kubwa zaidi,UCHAKACHUAJI.