Showing posts with label JAKAYA KIKWETE. Show all posts
Showing posts with label JAKAYA KIKWETE. Show all posts

6 Mar 2012

Usiniite mnafiki,au mpindisha maneno.Uthibitisho kuwa hata Rais Jakaya Kikwete hana imani na TAKUKURU upo katika habari ifuatayo (ANGALIA MAANDISHI MEKUNDU)


Rungu la Kikwete lilimwokoa Siyoi
Monday, 05 March 2012 09:17

Rais Jakaya Kikwete
NAPE, WASSIRA WADAIWA KUSIMAMA KIDETE ATOSWE, JK AKATUMIA 'RUNGU' KUZIMA HOJA,WABUNGE WOTE CHADEMA KUHAMIA ARUMERU
Joseph Zablon, Dar na Moses Mashalla, Arusha 

USHINDI wa Siyoi Sumari kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, unadaiwa kuitesa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, baada ya baadhi ya wajumbe kukuna vichwa kuhusu mbinu na mikakati ya kutengua ushindi alioupata katika duru ya pili dhidi ya William Sarakikya.

Katika Mkutano Mkuu wa jimbo hilo uliofanyika, Februari 20 ulimchagua Siyoi ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, marehemu Jeremiah Sumari kwa kura 361, akifuatiwa na Sarakikya aliyepata kura 259. Hata hivyo, CC ya CCM iliyoketi Februari 27, iliagiza kurejewa kwa upigaji kura kati ya wagombea hao.
Katika duru hilo la pili la uchaguzi uliofanyika Machi Mosi mwaka huu, Siyoi alipata ushindi wa kishindo wa kura 761 na kumtupa mbali mpinzani wake, Sarakikya aliyepata kura 361. 

Juzi katika kikao hicho cha CC, ushindi huo wa mara ya pili wa  Siyoi uliipasua tena kamati hiyo kuu yenye mamlaka ya juu ya uamuzi ndani ya chama hicho, baada ya baadhi ya wajumbe kudaiwa kutaka atoswe na apitishwe Sarakikya kutokana na tuhuma za matumizi makubwa ya fedha wakati wa kampeni.

Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka katika kikao hicho cha CC, vilifafanua kwamba waliosimama kidete kutaka Siyoi atoswe ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Nape alipinga Siyoi kurejeshwa akizingatia matukio mbalimbali ya tuhuma za matumizi makubwa ya fedha yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya watu ili wamchague mgombea huyo, kitu ambacho hakikupaswa kuvumiliwa. 

Hoja hiyo ya Nape iliungwa mkono na Wassira ambaye naye alitaka Siyoi atoswe kutokana na tuhuma hizo za matumizi makubwa ya fedha kutoka kwa baadhi ya wapambe wake waliotaka mgombea huyo achaguliwe.


Lakini inadaiwa kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alisema kikao hicho kisingeweza kumkata Sumari kwa sababu tu ya tuhuma hizo za rushwa zilitolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoani humo.


Chanzo kingine kilimnukuu mwenyekiti huyo akisema kwamba, Arusha ni mkoa wenye siasa za aina yake hivyo ni muhimu kuwa makini kwani siku za nyuma kuliwahi kuibuka tuhuma za rushwa kwa wabunge wa CCM kukamatwa lakini, mahakama ikawaachia huru.

Chanzo hicho kiliongeza kwamba, Rais Kikwete alisisitiza kuwa hata tuhuma za rushwa zilizotolewa zilikuwa zikigusa wengine kwani iliwahi kupendekezwa kwamba Elishalia Kaaya ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), ndiye apitishwe na wengine wang'olewe. 

Katika kikao hicho, Rais Kikwete pia alinukuliwa akihoji kuwa endapo Siyoi angekatwa jina kungekuwa na uhakika wa chama kushinda kwa kumsimamisha Sarakikya? Hakupata jibu kama mgombea huyo wa pili angeweza kushinda kiti hicho.

Hata hivyo, chanzo hicho kilisema baada ya mwenyekiti kutumia rungu kumpitisha Siyoi alimpa angalizo: “Basi na wewe usiende kutamba huko mitaani kwamba umeangusha watu, fanya kampeni, ushinde jimbo tuangalie mambo mengine mbele.”

Ilielezwa zaidi kwamba Rais Kikwete aliungwa mkono na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, aliyeeleza kuwa haoni sababu ya kumwondoa Siyoi katika kinyang'anyiro hicho kwani ushindi wake ulikuwa mkubwa. 


Chanzo na Kwa habari Kamili: Mwananchi

29 Feb 2012

Balozi Mahalu amlipua JK mahakamani 
Wednesday, 29 February 2012 07:31

Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu
ANIKA ALIVYOSHIRIKI KATIKA MCHAKATO KIPINDI AKIWA WAZIRI MAMBO YA NJE, ASEMA ALIKUTANA NA MAMA MWENYE NYUMBA NA KUAGIZA ALIPWE DOLA MILIONI MOJA HARAKA, AKAMPA OFA KUJA MBUGA YA NGORONGORO 
Tausi Ally
ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Rais Jakaya Kikwete wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alifahamu kuwepo kwa rasimu mbili za mikataba ya ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania, Italia.

Profesa Mahalu alisema hayo jana mbele ya Hakimu Mfawidhi, Ilvin  Mgeta wakati akitoa utetezi wake dhidi ya kesi inayomkabili  ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60 pamoja na aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin.

Akiongozwa na wakili wake, Mabere Marando, Profesa Mahalu aliitambua barua ya Februari 20, 2002 ambayo ilikuwa ikieleza kuwa matayarisho yote ya ununuzi wa jengo la ubalozi huko Italia yamekamilika ikiwa ni pamoja na rasimu mbili za mikataba.

Mahalu alidai kuwa katika mchakato wa ununuzi wa jengo hilo wakati yeye akiwa Balozi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kulikuwa na rasimu mbili za mikataba na kwamba aliwahi kuwasiliana na wizara hiyo juu ya mikataba hiyo.

Alidai kuwa Desemba 2001, Kikwete wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alikwenda Rome, Italia kwenye Mkutano wa SADC na alipokuwa huko, ubalozi ulifanya mpango atembelee jengo hilo lililopendekezwa kununuliwa kwa ajili ya ofisi ya ubalozi.

“Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia ilifanya mipango yote kwa kumpa utaratibu na usalama Kikwete ambapo alikwenda kutembelea jengo hilo na kukutana na mama mwenye jengo,” alidai Profesa Mahalu.

Alidai kuwa kabla ya mazungumzo na mwenye nyumba, mtoto wa mama huyo, Alberto alimtembeza Kikwete kwenye jengo hilo ndani na nje na baadaye mazungumzo hayo yaliendelea.

Balozi Mahalu alisema baadaye mazungumzo kati ya Kikwete na mama huyo yaliendelea na Alberto alikuwa akitafsiri, kwa sababu mama yake hakufahamu lugha ya Kiingereza.

Profesa Mahalu alidai kuwa katika mazungumzo hayo, Kikwete alimwuliza mama huyo: “Hivi ni kwa nini kunakuwa na mikataba miwili?” na mama huyo alimjibu kuwa hiyo ni kawaida kwa Italia ukitaka kununua jengo kwa bei nafuu.

Profesa Mahalu aliendelea kudai kuwa baada ya kupewa jibu hilo,  Kikwete hakuzungumza tena zaidi ya kucheka na kwamba mwenye jengo alimkumbusha kuhusu malipo ya awali ya dola milioni moja za Marekani ambapo aliafiki na kuahidi kuwa zingelipwa kabla ya mwisho wa mwaka 2001.
Profesa Mahalu alidai pia kwamba Kikwete alimweleza mama huyo kuwa atalishughulikia suala hilo baada ya kurejea Dar es Salaam na kumshukuru kwa kuwauzia jengo zuri.

Baada ya kutoa maelezo hayo, Profesa Mahalu alidai kuwa baada ya Kikwete kusema maneno hayo, alimgeukia na kumwambia: “Costa ni vizuri tupate hela tumlipe huyu mama watu wengine wasije wakachukua hili jengo.”

Profesa Mahalu alidai kuwa baada ya Kikwete kumshukuru mama huyo kwa ukarimu wake, alimkaribisha Tanzania awe mgeni wa Wizara ya Mambo ya Nje yeye na mumewe na kwamba watampeleka Ngorongoro.

“Tulipokuwa njiani tukirudi hotelini alipofikia Kikwete akiwa kwenye gari alimpigia simu Kibero akimuagiza afanye utaratibu wa kulipa Dola milioni moja kama malipo ya awali ya jengo hilo,” alidai Profesa Mahalu.

Alidai kuwa baadaye alimwagiza (Profesa Mahalu) aje Dar es Salaam kufuatilia mpango huo wa malipo ya awali ya ununuzi wa jengo hilo.

Awali, Profesa Mahalu akiongozwa na Wakili Alex Mgongolwa alidai kuwa anaitambua ripoti ya uthamini wa jengo hilo la ubalozi nchini Italia uliofanywa na Kimweri kutoka Wizara ya Ujenzi  aliyekwenda Rome Julai 15 hadi 26, 2001 kwamba jengo lilikuwa na gharama ya Sh6 bilioni.

Pia alizitambua ripoti za uthamini wa jengo hilo ambazo ni ile ya mama mwenye nyumba ambayo ilionyesha kuwa jengo hilo lilikuwa na thamani Sh5.500 bilioni na ripoti ya uthamini iliyofanywa na Serikali ya Italia iliyoonyesha kuwa jengo lilikuwa na thamani ya Sh11.117 bilioni.

Hakimu Mgeta aliiahirisha kesi hiyo hadi leo itakapoendelea kwa utetezi.

CHANZO: Mwananchi

20 Feb 2012

Familia ya JK yamkana aliyetoweka na mamilioni UVCCM 
Monday, 20 February 2012 07:38

Rais Jakaya Kikwete
Peter Saramba, Arusha
FAMILIA ya Rais Jakaya Kikwete imekana kuwa na nasaba na aliyekuwa Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wilayani Simanjiro, Alhaj Omar Yufus Kariaki, anayetuhumiwa kutokomea na zaidi Sh26 milioni, mali ya jumuiya hiyo.

Dada wa Rais Kikwete aliyehudhuria harambee ya kuchangisha fedha hizo kwa mwaliko wa Alhaj Kariaki, Tausi Kikwete aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa kitendo cha kijana huyo kujinasibu kuwa na undugu na familia yao, kililenga katika kujinufaisha isivyo halali.

“Ukweli ni kwamba kijana huyo siyo ndugu yetu hata kwa mbali. Kwanza yeye anatoka Kondoa, wapi na wapi na sisi Wakwere wa Bagamoyo, mkoani Pwani, Hatumfahamu kabisa kwenye ukoo wetu zaidi ya kufahamiana naye tulipokutana Hija,” alisema Tausi.

Alisema yeye na ndugu yake Mwanaisha Kikwete, walikutana na mtuhumiwa walipokwenda kuhiji Mecca, Saudi Arabia na baadaye kupeana mawasiliano yaliyowawezesha kuendelea kuwa karibu hata baada ya kurejea nchini.

Alisema baada ya kurejea, yeye na Mwanaisha waliendelea kuwasiliana na Alhaj Kariaki aliyeonyesha kuwa kijana mwenye upendo na busara zilizowavutia wao kutembelea nyumbani kwao, Kondoa kwa mwaliko wake.
“Ukaribu wetu ulifikia hatua ya sisi kutembelea nyumbani kwao Kondoa baada ya yeye kutualika. Lakini ukweli unabaki pale pale kwamba kijana huyo si ndugu yetu wala hana nasaba yoyote na kina Kikwete.” alisisitiza Tausi.

Alisema ilipofika wakati wa  harambee ya kutunisha Mfuko wa Mradi wa Maendeleo ya Vijana wa Wilaya ya Simanjiro, kijana huyo akiwa Katibu wa UVCCM wilayani humo, aliwaalika yeye na Mwanaisha kwenda kutoa semina kwa vijana kuhusu mbinu za ujasiriamali na miradi midogo.

Kwa mujibu wa Tausi, semina hiyo ilifanyika katika ukumbi wa mikutano ya Hoteli ya Manyara Inn, iliyoko Mererani siku mbili kabla ya harambee iliyoongozwa na aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha, ambaye sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Muungano.
Hata hivyo kauli hiyo ya Tausi inapinga na kauli yake ya awali kupitia simu mwaka jana, ambapo licha ya kukiri kumfahamu Alhaj Kariaki, pia alisema wana unasaba naye.

“Ni kweli mimi na Mwanaisha ni dada wa mheshimiwa Rais (Kikwete) pia ni ndugu wa karibu wa kijana huyo (Alhaj Kariaki). Lakini binafsi sina mawasiliano naye tangu awe diwani huko kwako Kondoa. Kwa kifupi sijawasiliana naye tangu tuachane Mererani,” alisema Tausi mwaka jana alipoulizwa kuhusu mtuhumiwa huyo.

Katika harambee hiyo iliyohudhuriwa na viongozi na watu kadhaa maarufu kutoka Mikoa ya Manyara na Arusha, Nahodha alichangia Sh2 milioni fedha taslimu  wakati aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Henry Shekifu akichangia 500,000.
Kwa sasa Shekifu ni Mbunge wa Lushoto.

Mwenyekiti wa UVCCM wa Wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer, alisema baada ya yeye kukabidhiwa mfuko wenye fedha mara baada ya harambee ambayo mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka naye alichangia Sh1.5 milioni, alikabidhi mfuko huo kwa katibu wake Alhaj Kariaki ambaye hadi juzi alipojitokeza baada ya gazeti hili kuripoti suala hilo.

Mwenyekiti huyo aliwataja wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya UVCCM wilaya walioshuhudia makabidhiano kati yake na katibu wake  kuwa ni Bonny Shongo na Paul Sipitet.

Laizer aliyetoa pongezi na shukrani kwa mwandishi na gazeti la Mwananchi kwa kufanikisha mtuhumiwa kujitokeza, alisema awali walikuwa wakihofia kufuatilia suala hilo kwa karibu kwa hofu kwamba mtuhumiwa ana undugu na familia ya Rais.

Alhaj Kariaki ambaye sasa ni Diwani wa Kata ya Kwa Delo wilayani Kondoa, aliibuka wiki iliyopita baada ya habari zake kuripotiwa katika gazeti hili.

Alikiri kutokabidhi fedha zilizopatikana kwenye harambee hiyo iliyofanyika Mei 9 mwaka juzi akidai sehemu ya fedha hizo amezitunza kwenye akaunti yake, akisubiri kumalizika kwa kile alichodai kuwa mgogoro baina ya viongozi wa CCM mkoani Arusha ili azikabidhi

CHANZO: Mwananchi

5 Feb 2012


WAJIPANGA KUKWAMISHA MUSWADA  MABADILIKO YA KATIBA
Midraji Ibrahim, Dodoma
SASA ni dhahiri kuwa wigo wa mpasuko kati ya wabunge wa CCM na Serikali unazidi kupanuka, baada ya wabunge hao kugoma kukutana na Rais Jakaya Kikwete mjini Dodoma.Katika kikao chao kilichofanyika Ijumaa usiku ukumbi wa Pius Msekwa mjini hapa, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliwaomba wabunge hao kukutana na Rais Kikwete ili kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya Serikali badala ya kuendelea kuikwamisha bungeni.Wabunge hao wanadaiwa kukataa rai hiyo huku wakimweleza waziwazi Pinda kwamba, itakuwa ni kumkosea heshima na adabu Rais, iwapo watakutana naye halafu wakwamishe marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayotarajiwa kufikishwa bungeni wiki ijayo.

“Itakuwa siyo heshima kukutana na Rais halafu tukwamishe muswada wa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kwa sababu tumejipanga kuhakikisha kwamba haupiti,” vilieleza vyanzo vyetu vya uhakika kutoka ndani ya kikao hicho.

Badala yake, wabunge hao walikubali kuteua miongoni mwao watu watano ambao wataonana na Rais Kikwete leo atakapowasili mjini hapa akitokea Mwanza kwenye Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 34 ya CCM.

Wazungumzaji wakuu kwenye kikao hicho wanadaiwa walikuwa pamoja na,  Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na Mbunge wa Shinyanga, Steven Masele.
 
Marekebisho hayo yalitarajiwa kuwasilishwa kesho, lakini walikataa hadi Ijumaa kwa kile walichodai kuwa, wengi wao watakuwa hawajarejea kutoka Mwanza  kwenye sherehe za maadhimisho ya CCM.

Inadaiwa na wabunge hao wa CCM kuwa, marekebisho hayo yanalenga kukimaliza chama hicho na kukiweka madarakani Chadema baada ya kuondolewa kwa wakuu wa wilaya, kushiriki mchakato wa katiba na kazi hiyo kukabidhiwa wakurugenzi wa halmashauri.

“Hii ni dhahiri kuwa marekebisho haya yanaiumiza CCM na kuisimika Chadema madarakani. Kuwaondoa Ma-DC kwenye mchakato wa katiba na kuweka wakurugenzi wa wilaya ambao wote ni Chadema, hatuwezi kukubali kamwe,” kilieleza chanzo chetu.
Pia, inadaiwa na wabunge hao kuwa marekebisho waliyopewa Dar es Salaam kwenye kamati, ni tofauti na yale yaliyowasilishwa bungeni, huku kukiwa na ongezeko la kurasa nne.

Hata hivyo, inadaiwa baada ya wabunge hao kugoma kukutana na Rais Kikwete, alisimama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano), Stephen Wasira, akiwataka kupitisha marekebisho hayo kwa sababu ni agizo la Rais, hali iliyosababisha azomewe huku akitupiwa maneno ya kashfa.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge hao ambao hawakupenda kutajwa majina yao, walisema athari wanayoiona mbele kwa kutopitishwa kwa marekebisho hayo, Chadema watapeleka mashtaka kwa umma kwamba sheria ile ilipitishwa kulinda CCM, hivyo haina manufaa kwa umma.

“Lakini CCM hatujajipanga, kila siku anayesimama jukwaani anazungumzia kujivua gamba, kwa hali hii tusubiri mashambulizi mazito siyo tu kutoka kwa Chadema hata nchi za nje,” kilieleza chanzo chetu.

Pia, wabunge hao wa CCM wanadai kuwa miongoni mwa sababu za kukwamisha marekebisho hayo, ni kile walichodai Rais Kikwete kuwadharau kutokana na wao kupitisha muswada wa sheria hiyo, halafu yeye (Kikwete) anakutana na Chadema dakika chache na kukubaliana na hoja zao.

“Sisi tumekaa hapa (bungeni) kwa zaidi siku mbili na akili zetu timamu, tukapitisha muswada ule, anakutana (Kikwete) na Chadema dakika chache anatuletea marekebisho! Hiyo ni dharau na hatuwezi kukubali,” alilalamika mbunge mmoja.

Kura ya kukosa imani na Rais
Katika kikao cha wabunge hao kilichofanyika Alhamisi wiki hii, baadhi yao walihoji sababu zinazokwamisha masuala mbalimbali serikalini kutopatiwa ufumbuzi, huku Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, akipendekeza kwamba kama tatizo ni Rais Kikwete, watumie utaratibu wa kumpigia kura ya kutokuwa na imani.

Shelukindo anadaiwa alitaka kujua sababu za masuala mbalimbali kukwama na kutopatiwa ufumbuzi wa haraka na kwamba, iwapo tatizo ni Rais Kikwete, wapo tayari kufuata utaratibu wa kumpigia kura ya kutokuwa na imani.

Hata hivyo, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Olle Sendeka, alisimama na kumtaka mbunge huyo kufuta kauli yake, suala ambalo Shelukindo alikubali.

Pia, katika kikao hicho kiliwataka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda, Naibu wake, Dk Lucy Nkya na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Blandina Nyoni, kujiuzulu kutokana na kuwa chanzo cha mgomo wa madaktari.

Katika kile kinachoonyesha mpasuko huo kuchukua sura mpya, wabunge hao wamekuwa wakikwamisha miswada ya Serikali, suala ambalo siku zilizopita walikuwa wakiipitisha hata pale yanapokuwepo malalamiko kutokana kwa wananchi, kwa kile kilichokuwa kikielezwa kuwa ni ‘msimamo wa chama.’

CHANZO: Mwananchi

31 Jan 2012


Rais Jakaya Kikwete amekiri kuwepo kwa mkanganyiko uliojitokeza kufuatia kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa Rais ameridhiria nyongeza ya posho za Wabunge.Rais alisema hayo katika majadiliano kati yangu na yeye kupitia mtandao wa Twitter kama inavyoonyesha picha hapa juu na hapa chini


Awali,Rais Kikwete alifafanua kuwa ni kweli alitoa maelekezo kuhusu suala la posho hizo lakini maelekezo hayo hayakuwa kuridhia jambo hilo.Kadhalika,Rais alibainisha kwamba alikubali haja ya kuangalia upya posho za wabunge na aliwataka wabunge kutumia hekima na busara katika kutafakari.Vilevile aliwataka wabunge kutumia Kikao cha Februari cha Bunge kulizungumzia upya suala hili,na kusistiza ni muhimu.Picha ifuatayo inaonyesha maelezo hayo ya Rais Kikwete kwenye mtandao wa Twitter.


Jana,gazeti la Mwananchi lilikuwa na habari iliyobeba kichwa 'JK ABARIKI POSHO MPYA ZA WABUNGE' ambapo pamoja na mambo mengine habari hiyo ilieleza kuwa Waziri Mkuu Pinda amesema kuwa tayari Rais Kikwete amesaini kuridhia ongezeko la posho za vikao (sitting alllowances) kwa wabunge kutoka shilingi 70,000 hadi shilingi 200,000 kwa siku.Picha ifuatayo inaonyesha sehemu ya habari hiyo:


Hata hivyo,mapema leo Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu ilitoa taarifa ya maandishi kukanusha habari hizo, kama inavyosomeka hapa chini

Taarifa Ya Ikulu

Blogu hii inaendelea kufatilia kwa karibu kuhusu suala hilo.

JK abariki posho mpya za wabunge 
Monday, 30 January 2012 20:54
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
KILA MMOJA KULIPWA 330,000 KWA SIKU, ZITTO, MAKAMBA, KIGWANGALA WASULUBISHWA KWA KUZIPINGA
Waandishi Wetu, Dodoma  
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema tayari Rais Jakaya Kikwete amesaini kuidhinisha ongezeko la posho za vikao (sitting allowance) kwa wabunge kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku.  Kupitishwa kwa posho hizo ambazo ziliandikwa kwa mara ya kwanza na gazeti hili, kunafanya sasa mbunge kupokea Sh330,000 kwa siku; Sh200,000 zikiwa ni posho ya kikao, Sh80,000 posho ya kujikimu na Sh50,000 nauli.  

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao cha utanguzi cha wabunge jana, zilidai kuwa baada ya Pinda kutoa taarifa hiyo, wabunge walishangilia huku Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, akisimama na kudai kuwa taarifa alizonazo ni kwamba Rais Kikwete alikuwa hajasaini kuidhinisha posho hizo.  

Hatua hiyo ilisababisha Mbunge wa Kondoa Kaskazini, Juma Nkamia (CCM), kusimama na kuhoji iwapo Zitto ni miongoni mwa wasemaji wa Rais kabla ya Pinda kusimama na kuthibitisha kusainiwa kwa posho hizo akisema siyo ajabu kwani hata watumishi wa Serikali wanalipwa kati ya Sh150,000 na Sh200,000.  Hata hivyo, Zitto alitetea msimamo wake kwamba alitarajia baada ya kusainiwa kwa posho hizo na Rais, angepewa masharti mapya ya kazi za ubunge.  

Katika kikao hicho baadhi ya wabunge wanadaiwa kuwashambulia Zitto, Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba na Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Khamis Kigwangwala kwamba wamekuwa mstari wa mbele kupinga posho hizo hadharani.  Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye anadaiwa kwamba aliungana na Pinda kuthibitisha kwamba Rais Kikwete ameidhinisha posho hizo mpya, pia aliwashambulia wabunge wanaozipinga akisema kwamba wanafuta umaarufu wa kisiasa.

“Wanachotafuta ni umaarufu wa kisiasa tu, mimi ninavyojua umaarufu wa kisiasa unakuja kwa kufanya kazi za kibunge za wananchi lakini siyo kupinga posho,” chanzo chetu cha habari kilimnukuu Makinda.

Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa anadaiwa kwamba alitumia mafumbo  kuwashambulia wabunge hao ambao wamejitokeza kupinga nyongeza hiyo ya posho.  Kauli hiyo inadaiwa kuungwa mkono na Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Nkumba ambaye alidai kuwa hawezi kumsemea Zitto kwa sababu ni kawaida yake kupinga, lakini akaelekeza shutuma zake kwa Makamba kwamba ameanza kupinga baada ya kugharamiwa na CCM. “Januari anapinga posho hizo kutokana na CCM kumpa gari, nyumba na analipwa na chama,” kilisema chanzo chetu kikimkariri Nkumba.

 Pia, Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), anadaiwa kumshambulia Zitto kuwa lazima apinge posho hizo kwa sababu, anapewa fedha na wafadhili kutoka nchi za nje.  “Shelukindo anasema amefanya ziara nje na kuhakikisha kuna wahisani wanamfadhili Zitto kwa hiyo ana haki ya kupinga posho hizo,” chanzo chetu hicho kilimkariri Shelukindo.
 
Hata hivyo, inadaiwa kuwa baada ya mashambulizi hayo, Dk Kigwangwala alisimama kutetea msimamo wake kwamba ongezeko hilo halina ‘mashiko’ na haliwezi kuelezwa mbele ya umma likaeleweka, lakini alizomewa na wabunge wengi huku wakimtaka kukaa chini.  

Hatua hiyo ilisababisha Zitto kusimama na kueleza kuwa tatizo la wabunge kwamba wana fikra finyu, kauli ambayo alitakiwa na wenzake kuwaomba radhi kuwa amewatukana.  “Zitto ametumia Kiingereza kuwa tatizo la wabunge ‘we think small’,  Shelukindo na (John) Komba wakaja juu wakitaka kuwaomba radhi kwa kuwatukana,” chanzo chetu kilieleza.  Zitto anadaiwa kusema wabunge walitakiwa kujenga hoja ya kuongeza fedha za mafuta ya gari wanayolipwa hivi sasa Sh2.5 milioni kwa mwezi, kutokana na kupanda kwa nishati hiyo, lakini siyo posho.  

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alinukuliwa akisema matatizo ya posho yamefikia hapo baada ya kuonekana ni ya watu binafsi siyo mfumo hivyo, wanaopinga wanaonekana kama wanatafuta umaarufu na wana vipato vya fedha, akaitaka kamati ya uongozi ijadili na kupata mwafaka badala ya wajumbe kutofautiana mbele ya umma.  Wabunge wengine wanaodaiwa kutetea posho hizo ni Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini na Jenister Mhagama (Peramiho CCM).

 Msimamo wa January
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Makamba alijibu: “Si sahihi kwangu kutoa taarifa za kikao cha ndani. Lakini msimamo wangu kwenye suala hilo unajulikana na haujabadilika.  Msimamo wa CCM ulishawekwa wazi na sote tunaujua. Nitalizungumzia suala hili kwa kirefu katika siku zijazo.”

Kuhusu taarifa kwamba anagharamiwa na CCM, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo na badala yake kutaka kiulizwe chama hicho.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu taratibu za kuwagharamia viongozi wa chama chake ambao ni wabunge alisema: “Mbunge au kiongozi yeyote wa chama mwenye nafasi nyingine anagharamiwa na chama pale anapokwenda kufanya shughuli za chama tu na si vinginevyo.”

“Kwa hiyo kama ni mbunge suala la mafuta, dereva, mahali pa kulala na mahitaji mengine anagharamiwa na taasisi anayoifanyia kazi na siyo chama.”

“Kwa mfano, mimi kwenye sekretarieti hata posho za vikao huwa sichukui, nadhani na mwenzangu January naye sidhani kama huwa anachukua posho, kwa sababu tukifanya hivyo ni kama tunakiumiza chama, huo ndiyo msimamo wetu na uko wazi wala siyo kificho.”

Kwa upande wake, Zitto alisema jana kwamba hakuwa katika nafasi ya kuzungumzia suala hilo na badala yake kuahidi kwamba atalizungumza leo atakapokutana na waandishi wa habari.

Wabunge walia njaa
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilisema wabunge hao walilalamikia kucheleweshwa kulipwa posho zao za wiki mbili walizokaa Dar es Salaam wakati wa vikao vya kamati.

Walidai hivi sasa wanaishi kwa shida huku wakihoji sababu za kucheleweshewa.

Imeelezwa kwamba Spika Makinda alidai kuwa fedha hizo zipo na kwamba  kilichochelewesha ni uhakiki wa wabunge waliohudhuria vikao.

Makinda alisema baadhi ya wabunge wamekuwa wakilipwa posho za vikao bila kuhudhuria, hatua ambayo imesababisha Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), kuhoji maswali mengi.

CHANZO: Mwananchi

25 Jan 2012


Rais Kikwete amefungua milango

Rais Kikwete msibani kwa Marehemu Mbunge Regia
Rais Kikwete msibani kwa Marehemu Mbunge Regia
KWA mara ya pili ndani ya takriban kipindi cha wiki moja, Tanzania imepoteza wabunge wawili. Kabla majonzi hayajatuisha kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CHADEMA, Regia Mtema, taifa likapatwa na msiba mwingine wa Mbunge wa Arumeru Mashariki kwa tiketi ya CCM, Jeremiah Sumari.
Kila kifo kinaacha pengo lakini kifo cha kiongozi (awe wa familia kama mzazi au wa jamii) kinaacha pengo linalowagusa na kuwaathiri wengi. Japokuwa yayumkinika kuhisi kuwa katika zama hizi za siasa za kuendekeza maslahi kuna wanaofurahi vifo vya viongozi kwa vile vitatoa nafasi ya wao kugombea, ukweli unabaki kuwa ni vigumu kupata mrithi atakayelingana kwa kila kitu na marehemu (hasa katika utekelezaji wa majukumu).
Kama nilivyoandika katika makala ya wiki iliyopita kuhusu kifo cha Regia, njia bora ya kumuenzi marehemu Sumari ni kudumisha mema yote aliyofanya wakati wa uhai wake. Kwa wanaofikiria kumrithi nafasi yake (na kwa atakayeteuliwa kumrithi nafasi ya Marehemu Regia) changamoto kubwa itakuwa kwenye kuwaenzi viongozi hao kwa kuwajibika ipasavyo. Japo utendaji kazi bora wa kiongozi anayerithi madaraka kutoka kwa kiongozi marehemu hauwezi kurejesha uhai, kwa kiasi fulani unasaidia kupunguza machungu ya wananchi walioathiriwa na pengo lililotokana na kifo husika.
Katika mila na desturi za kiafrika, shughuli ya msiba inatawaliwa na majonzi na kwa kiasi kikubwa ni kumbukumbu kwa kila aliyehai kuwa sote “tulitoka kwenye udongo na tutarejea kwenye udongo.” Misiba inapaswa kutukumbusha kuwa sote ni wasafiri na kila nafsi ya mmoja wetu itaonja mauti.
Moja ya matukio yaliyotawala msiba wa Regia ni habari kwamba Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbroad Slaa, alikwepa kusalimiana na Rais Jakaya Kikwete. Habari hiyo ilichukua uzito mkubwa kiasi cha kukaribia kufunika tukio la huzuni lililowakutanisha viongozi hao huko Ifakara.
Kwa sababu anazozijua mwenyewe, jamaa mmoja aliamua kusambaza waraka katika blogu kadhaa ndani na nje ya nchi kukemea kitendo hicho cha Dk.  Slaa. Mtu huyo ambaye hakufanya jitihada za kuficha itikadi yake ya siasa, akaenda mbali zaidi na kudai kuwa kilichosababisha Katibu Mkuu huyo wa CHADEMA kutosalimiana na Rais ni amri iliyotolewa na mwenza wa Dk. Slaa (Josephine).
Pengine kwa kuelewa kuwa kukalia kimya jambo hilo kungeibua maneno zaidi, hatimaye Dk. Slaa alieleza kilichomfanya ashindwe kusalimiana na Rais Kikwete. Kwa wanaojua protokali, mtu hakurupuki tu na kwenda kusalimiana na kiongozi mkuu wa nchi hasa ikizingatiwa kuwa kumkaribia kiongozi huyo (hata kama ni kwa nia nzuri) kunawafanya walinzi wake watafsiri kama tishio la usalama kwake.
Kadhalika, Dk. Slaa alieleza bayana kuwa kilichompeleka Ifakara ni kumzika Regia na si vinginevyo. Kwa lugha nyingine, alimaanisha kuwa isingehitaji kutokea kifo cha mbunge au kiongozi wa chama ndipo “mahasimu wawili” (kama ‘wazushi’ wa habari hiyo walivyojaribu kutuaminisha) wakutane na kupeana mikono.
Lakini kama kuwasuta wanaokuza matukio madogo, siku chache baadaye vyombo vya habari vilitawaliwa na picha inayomwonyesha Rais Kikwete na Dk. Slaa wakipeana mikono baada ya mazungumzo kati ya Rais na viongozi wa CHADEMA yaliyofanyika Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam.
Sijui waliozusha kuwa Josephine alimkataza Dk. Slaa wanasemaje kuhusu hilo. Labda watazusha kuwa alimtoroka mwenza wake kama sio kuzusha kuwa kiongozi huyo wa CHADEMA aliamua kuambatana na viongozi wenzie Ikulu ili kujisafisha kutokana na tukio la Ifakara.
Inasikitisha kuona mambo ya msingi yakigubikwa na porojo zisizo na mashiko. Binafsi, moja ya mambo ya msingi yaliyonigusa na kunipa matumaini mapya ni jinsi Rais Kikwete na takriban uongozi wake mzima (serikalini na huko CCM) walivyoweza kuweka kando tofauti za kiitikadi na kumzika Regia kama kiongozi wa Watanzania na si mbunge wa CHADEMA pekee.
Mara kadhaa nimekuwa nikishutumiwa kwa kumkosoa au kumlaumu Rais Kikwete. Lakini siku zote nimejitahidi kusisitiza kuwa lawama hizo na kukosoa hakumaanishi chuki au husuda bali ni kwa minajili ya ustawi wa taifa letu.
Natambua kuna uwezekano wa baadhi ya wasomaji kuhisi nimefikia hatua ya kumpongeza Rais Kikwete kwa vile tukio husika linaihusu CHADEMA (ambayo nimekuwa nikituhumiwa kuipendelea na baadhi ya watu, huku wengine wakidai mimi ni mwanachama wa chama hicho.)
Yeyote aliyesoma salamu za rambirambi zilizotolewa na Rais Kikwete kwenda kwa familia ya marehemu Regia na CHADEMA hatoshindwa kubaini kuwa zilikuwa zimetoka moyoni kwa dhati. Hakukuwa na hata chembe ya tofauti za kiitikadi bali hisia za kibinadamu pindi zinapopatikana habari za kifo.
Naomba nisisitize kuwa tukio hilo sio pekee au la kwanza kwa Rais Kikwete kuonyesha kile wanachokiita Waingereza ‘human side’ (ubinadamu wake, kwa tafsiri isiyo rasmi). Mara nyingi mkuu huyo wa nchi ameonyesha kuguswa kwa dhati kila anapokuwa kwenye matukio ya huzuni.
Japo wakati mwingine huishia kulaumiwa kuwa ‘haisaidii kuonyesha uchungu ilhali janga husika lingeweza kuzuilika’ (kwa mfano kwenye matukio ya milipuko ya mabomu huko Mbagala na Gongo la Mboto), hiyo haindoi ukweli kuwa ameguswa na matukio hayo.
Lakini pamoja na pongezi hizi kwa Kikwete na CCM kwa ujumla pengine ni muhimu kukumbushana kuwa kama tunaweza kushikamana wakati wa misiba kwa nini basi iwe vigumu kufanya hivyo nyakati nyingine?
Kwa lugha nyingine, kwa nini tusubiri hadi kiongozi wa chama cha upinzani afariki ndipo tuonyeshe kuwa tofauti za kiitikadi haziondoi ukweli kuwa sote ni Watanzania tunaoweza kutofautiana kimtizamo au kiitikadi pasipo umuhimu wa ‘kuong’oana’ macho.
Japo Kikwete si mahiri katika kuendekeza siasa za uhasama (aidha kwa vile si muumini wa dhana hiyo au anatumia wasaidizi wake kukwepa lawama zinazoweza kuelekezwa kwake), kiujumla chama anachoongoza, yaani CCM, kimekuwa kikifanya jitihada kubwa kuuaminisha umma kuwa vyama vya upinzani ni mithili ya mikusanyiko ya maharamia wasioitakia mema nchi yetu.
Ukisikiliza hotuba za baadhi ya viongozi wa CCM wanapovizungumzia vyama vya upinzani unaweza kabisa kutamani kwenda Idara ya Uhamiaji kuhoji iwapo viongozi hao wa upinzani ni raia halisi wa nchi hii. Hivi haiwezekani kukosoana pasipo kupandikiza chuki ya uadui miongoni mwetu?
Katika tafiti za kitaaluma, kuna hatua ambapo mtafiti huwezi kubashiri matokeo ya utafiti husika kwa kuzingatia dhana alizotengeneza (hypothesis). Japo makala hii si sehemu ya utafiti lakini ningependa kutengeneza dhana kuu mbili zinazoweza kubashiri matokeo fulani.
Ya kwanza, kwa vile Rais Kikwete na CCM wameweza kututhibitishia kuwa tofauti zao za kiitikadi na CHADEMA si za kiadui, na ndio maana wameshiriki kikamilifu katika msiba wa marehemu Regia, Tanzania inaingia kwenye zama mpya za siasa za upendo na kukosoana kistaarabu.
Ya pili, kwa vile siku chache baada ya msiba wa mbunge wa CHADEMA, Rais Kikwete aliwaalika viongozi wa CHADEMA kufanya majadiliano nao, tunaanza kushuhudia ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Rais (na pengine CCM kwa ujumla) katika uongozi wa nchi.
Matokeo yanayotarajiwa ni kwamba badala ya muda mwingi wa ujenzi wa taifa letu kutumika kunyoosheana vidole, kuitana majina ya ajabu ajabu na upuuzi mwingine, sasa tunaweza kuona uongozi wa nchi ukifanya kazi bega kwa bega kwa lengo la kuikomboa Tanzania yetu kutoka katika lindi la umasikini (licha ya rasilimali lukuki tulizojaliwa) na kuunganisha nguvu kukabiliana na kundi la maharamia walioigeuza nchi yetu kuwa ‘shamba la bibi’ kwa ufisadi.
Unaweza kudhani labda aya tatu za hapo juu nimeziandika nikiwa ndotoni. La hasha. Kila nililoandika linawezekana kwani sababu (ya kushirikiana) ipo, na uwezo wa kufanya hivyo upo (kama ilivyothibitika katika tukio hilo la msiba wa marehemu Regia), ila kinachokosekana ni nia tu.
Ni matarajio ya safu hii kuwa Rais Kikwete (ambaye naamini anasoma makala hizi au anasimuliwa na wasaidizi wake) hatorudi nyuma katika kufungua sura mpya ya siasa za maelewano na ushirikiano kwa manufaa na ustawi wa Tanzania yetu. Penye nia pana njia.


11 Dec 2011


Ukiangalia picha hiyo juu kwa makini utabaini kuwa suruali ya Rais Kikwete ni kama inaashiria kwamba anaumwa.Of course,nusu ya juu iko kawaida (pengine kwa sababu ya bullet vest kama alikumbuka kuivaa) lakini nusu ya chini inaonyesha kama amekonda.

Inawezekana ni wembamba tu wa miguu ya Rais wetu lakini...well,nakuachia msomaji uhiimishe mwenyewe.

10 Dec 2011




Kikwete, Lowassa hapatoshi

Saed Kubenea's picture
Na Saed Kubenea - Imechapwa 30 November 2011
Printer-friendly versionSend to friend
HATIMAYE Edward Lowassa ametoka hadharani na kuonyesha kuwa anataka kupimana ubavu na Rais Jakaya Kikwete.
Ameeleza hadharani kuwa Rais Kikwete anahusika kwenye mkataba tata wa Richmond/Dowans; lakini pia, kuwa hafuati taratibu katika kuongoza chama chake.
Lowassa ambaye alikuwa nguzo muhimu katika mbio za urais wa Kikwete mwaka 2005, ameonekana kumgeuka waziwazi swahiba wake huyo kwa kuanika kile wachunguzi wanaita “udhaifu katika uongozi.”
Ndani ya kipindi cha siku nne, Lowassa ametoa kauli tatu nzito zinazoonyesha dhahiri ameamua kufanya mapambano na Kikwete.
Akiwa ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lowassa alinukuliwa akieleza hatua kwa hatua namna kampuni ya kitapeli ya Richmond Development Company (RDC), ilivyopewa zabuni ya kufua umeme wa dharura nchini.
Lowassa alijiuzulu wadhifa wa waziri mkuu mwaka 2008 kufuatia kashfa ya mkataba wa Richmond, kampuni iliyopewa kwa upendeleo zabuni ya kuzalisha umeme wakati haina fedha, haina uzoefu wala fedha za kufanyia kazi hiyo.
Alikiambia kikao cha NEC mjini Dodoma, “Hakuna jambo nililolifanya ambalo wewe Rais Kikwete hukulifahamu au hukunituma” kuhusu Richmond/Dowans.
Alisema, “…Mwenyekiti, natukanwa kwa ufisadi wa Richmond wakati wewe unafahamu yalichosababisha kashfa ya Richmond ni makosa ya watendaji walio chini yangu? Sasa kosa langu ni lipi? Ni kule kukubali kuwajibika kwa ajili ya serikali yangu na chama chetu? Kwa nini nihukumiwe kwa kosa hilo?”
Huku akimtolea macho Kikwete alisema, “Unakumbuka vema jinsi nilivyotaka kuvunja mkataba ule. Nilikupigia simu ukiwa nje ya nchi, lakini ukasema umepata ushauri wa kamati ya makatibu wakuu, ushauri ambao ulisababisha mkataba usivunjwe?”
Lowassa alisema Kikwete anafahamu kila kitu kwa kuwa ni yeye aliyeridhia Rostam Aziz kutafuta mbia baada ya Richmond kushindwa kuleta umeme.
“Uliponitaka ushauri wa mtu wa kutusaidia ili kuondokana na aibu ya Richmond kushindwa kutimiza mkataba wake, nilipokutajia jina la Rostam, haraka ulikubali na kusema, naona hilo ni sawa,” alieleza Lowassa kwa njia ya kumsuta Kikwete.
Hatua ya Lowassa kumuingiza Kikwete kwenye tope la Richmond/Dowans imezima moja kwa moja kauli yake iliyodai, “Siwajui wala siwafahamu wamiliki wa makampuni ya Dowans Tanzania Ltd na Dowans Holdings SA.”
Akihutubia kwenye maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, tarehe 5 Februari 2011, mjini Dodoma, Kikwete alikana kufahamu wamiliki wa kampuni hiyo na kwamba hajawahi kuwaona wamiliki wake.
Alisema, “Nataka kuuhakikishia umma kwamba, sihusiki na kampuni hii. Siifahamu na wala sijawahi kuwaona wamiliki wake…Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi.”
Kauli ya Kikwete ya kutoitambua Dowans wala wamiliki wake, ilikuwa ni mwendelezo wa kauli kama hizo zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya wasaidizi wake, zikilenga kumuondoa kwenye kashfa hiyo iliyomlazimu kuvunja baraza lake la mawaziri.
Akizungumzia kwa undani jinsi Richmond ilivyoingia na jinsi yeye na Kikwete walivyokuwa kitu kimoja kuhakikisha mkataba unasainiwa na kutekelezwa, Lowassa alisema, “Hakuna jambo nililolifanya ambalo Rais Kikwete hukulifahamu.”
Akizungumzia kwa undani suala hilo kwa mara ya kwanza tangu ajiuzulu wadhifa wa waziri mkuu, Februari 2008, Lowassa alisema, “Mwenyekiti kwanza napongeza uamuzi huu wa kurejesha jambo hili katika taratibu za kawaida, lakini napenda kufahamu kwa miezi saba nimetukanwa nikiitwa fisadi, watu wamezunguka nchi nzima kwa fedha za chama, hivi hatukujua kama kuna kamati hizo za maadili?”
Lowassa alikuwa akichangia pendekezo la Kamati Kuu (CC) ya CCM lililotaka kurejeshwa kwa suala la “kujivua gamba” kwenye vikao vya chini vya chama hicho baada ya watuhumiwa, isipokuwa Rostam Aziz, kukataa kuachia uongozi katika chama.
Kikwete alikiambia kikao cha NEC kuwa, uamuzi wa kutaka jambo hilo lirejeshwe kwenye vikao vya chini, umetokana na “taratibu kukosewa.”
Hata hivyo, kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya chama hicho aliliambia gazeti hili juzi Jumatatu, uamuzi wa Kikwete kulirejesha suala la kujivua gamba kwenye vikao vya chini ulitokana na hofu ya NEC kujaa wajumbe wengi kutoka kwa kundi la Lowassa.
“Unajua mle NEC, Kikwete hana chake. Mle ndani kuna kundi kubwa la Lowassa, ndiyo maana jamaa ameogopa suala hilo la kuvuana magamba lijadiliwe,” ameeleza kiongozi huyo ambaye ni waziri katika serikali ya Rais Kikwete.
Kanuni za CCM zinaeleza kabla ya tuhuma kufikishwa NEC, sharti wale wanaotuhumiwa wapewe haki na fursa ya kujitetea mbele ya vikao vya kamati ya usalama na maadili.
Akifunga mjadala huo kwa angalizo mwanana, Kikwete aliagiza suala hilo lipelekwe kamati ya maadili ambako alitaka kuwasilishwa ushahidi wa vielelezo na siyo hujuma dhidi ya watuhumiwa.
Wakati Lowassa akishusha tuhuma kwa Kikwete, kiongozi huyo wa nchi alionekana kama amepigwa ngazi. Hakukana hata tuhuma moja miongoni mwa yaliyoelezwa na swahiba wake huyo wa zamani.
Kikwete na Lowassa, wamejitambulisha mara kadhaa kuwa ni marafiki, huku mmoja akisisitiza, “Hatukutana barabarani.”
Haijafahamika mahusiano yao yamefikia wapi kwa sasa baada ya Lowassa kumhusisha mwenzake katika kashfa ya Richmond katika kile wachunguzi wanasema amechukua tabia ya “tufe sote au tukose wote.”
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kauli ya Lowassa ambayo ilitolewa mbele ya viongozi wake wakuu, akiwamo rais mstaafu, Benjamin Mkapa, ililenga kuonyesha udhaifu wa Kikwete ndani ya CCM kwa kuasisi falsafa ya kujivua gamba na kuikimbiza moja kwa moja kwenye CC na NEC, kinyume cha taratibu na kanuni za chama chake.
Kama hiyo haitoshi, juzi Jumapili akiwa mkoani Singida alikokwenda kusimamia harambaee ya kuchangia fedha za ujenzi wa kanisa, Lowassa alinukuliwa akisema, “Kwa vyovyote vile, nitaibuka mshindi dhidi ya vita vya kuvuana magamba.”
Akitiwa moyo na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Kati, Ushirika wa Amani, mjini Singida, Eliufoo Sima aliyesema, “suluhu ya mapambano ni kukabiliana nayo,” mwanasiasa huyo alisema, amekuwa akihusishwa na tuhuma ambazo hazina ukweli.
Askofu Sima alisema mapambano katika maisha hayatakwisha na “suluhisho siyo kuyaogopa, isipokuwa kuyatafutia majawabu kwa upole, hekima na utulivu.”
Vita vya magamba viliasisiwa na Kikwete 5 Februari 2011, kabla ya kudakwa na baadhi ya watendaji wa Sekretarieti ya CC ambao kwa miezi saba sasa, wamekuwa wakituhumu Lowassa na wenzake wawili - Rostam Aziz na Andrew Chenge – kuwa mafisadi wanaokidhalilisha chama mbele ya jamii.
Wakati hayo yakiendelea, taarifa kutoka ndani ya CC zinasema kushindwa kwa Rais Kikwete kutekeleza mkakati wake wa kumfukuza Lowassa ndani ya chama chake, kulitokana na upinzani mkali uliotokea kwenye mkutano wa CC.
“Ni kweli kabisa, ndani ya CC, Lowassa alipata uungwaji mkono mkubwa, kiasi ambacho mwenyekiti alilazimika kulipeleka suala hilo NEC. Alipofika NEC na kuona moto umekuwa mkubwa, ndipo alipoamua kuliondoa na kutaka lifanyiwe kazi kwenye vyombo vya chini,” kimeeleza chanzo kimoja cha gazeti hili.
Amesema wajumnbe wa Zanzibar, wakiongozwa na makamu mwenyekiti wa chama hicho visiwani, Amani Abeid Karume, muda wote wa mkutano walisimama imara kuhakikisha Lowassa hafukuzwi kwenye chama.
“Kuna wakati watu kutoka Bara walikuwa wanakaribia kushinda. Lakini baadaye Zanzibar wakapata nguvu pale Karume aliposimama na kusema, shutuma zote hizo hazijafuata taratibu,” ameeleza.



CHANZO: Mwanahalisi

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.