Showing posts with label UTAWALA WA JAKAYA KIKWETE. Show all posts
Showing posts with label UTAWALA WA JAKAYA KIKWETE. Show all posts

17 Jun 2010

Desemba 9 mwakani,Tanzania yetu itatimiza miaka 50 tangu ipate uhuru.Pengine tarakimu 50 inapunguza uzito,kwahiyo ni vema kubainisha kuwa umri huo ni sawa na NUSU KARNE (herufi kubwa kuonyesha msisitizo).Wakati umri huo wa mtu mzima ungepaswa kuwa habari njema,hali ni tofauti kwetu.Tulowakabidhi dhamana ya kutuongoza wanakurupuka na mambo ya ajabu ajabu kana kwamba wako ndotoni au wako kwenye mchezo wa kuigiza usio na ujumbe wowote.

Ngoja niende moja kwa moja kwenye pointi.Hivi Mtanzania mwenzangu inakuingia akilini kweli kusikia kauli kwamba jengo la Bunge letu tukufu "litafanyiwa ukarabati wa kufa mtu" unaotarajiwa kugharimu shilingi bilioni 30.9 "ili kuwawezesha waheshimiwa sana waendane na teknolojia ya kisasa wanapokuwa Bungeni"!!!?Kwa mujibu wa Spika Samuel Sitta mchakato wa ukarabati huo umeshakamilika na unatarajiwa kuanza mara moja,ambapo utapokamilika kila kiti cha mbunge kitakuwa na runinga pamoja na mawasilino ya kisasa ya kompyuta.

Ofkozi,ni muhimu kwenda na wakati katika suala zima la teknolojia lakini pamoja na umuhimu huo shilingi bilioni 30 na ushee ni nyingi mno na tunazihitaji kwenye maeneo mengine yaliyo hio bin taaban kama vile miundombinu,huduma za afya,maji,nk.Hivi kweli runinga kwenye kiti cha mbunge ni muhimu kuliko madawati au nyumba za walimu?Je hizo bilioni 30 zingeweza kujenga zahanati ngapi au visima vingapi vya kuwapatia walalahoi huduma ya maji ya uhakika?

Lakini kabla sijatuliza hasira zangu kutokana na kauli hiyo ya Spika Sitta,JK nae amekuja na mpya akidai kwamba katika miaka mitano ijayo kila mwalimu atakuwa na laptop.Namheshimu sana Rais wangu lakini baadhi ya kauli zake zinanitatiza sana.Hivi kipaumbele katika elimu yetu ya kusuasua ni laptop kwa walimu au makazi bora kwa walimu hao sambamba na kuboreshewa maslahi yao na mazingira yao ya kazi?Mwalimu mwenye laptop anafundishaje wanafunzi waliokaa chini ya mti?Na wakati JK anatoa mpya hiyo hajatuambia umeme wa kuziwezesha laptop hizo utakuwa wa nguvu za jua au zitatumia mafuta ya taa kwani sote tunafahamu uhuni wa TANESCO.


Sijui ni uzembe wa watawala wetu kuelewa matatizo yetu na vipaumbele vyetu kama taifa au ni makusudi tu lakini kwa mwenendo huu itatuwia vigumu kutembea vifua mbele hapo mwakani tutaposherehekea nusu karne tangu tupate uhuru. 

Enewei,hebu soma mazingaombwe hayo HAPA na HAPA.

8 Jun 2010

Kuna nyakati napata shida kuzielewa kauli za Rais Jakaya Kikwete.Nafahamu kuwa yeye ni mwanadamu kama mwingine,kwahiyo anaweza kufanya makosa ya kibinadamu.Lakini kwa vile nyingi ya hotuba zake huandaliwa na wasaidizi wake,nafasi ya makosa ya kibinadamu inapaswa kuwa ndogo.

Huko nyuma tumeshasikia kauli kadhaa tata kutoka kwa Kikwete,ikiwa ni pamoja na ile maarufu ya aliyotoa Mkoani Rukwa mwaka 2006 kwamba "anawajua kwa majina wala rushwa katika wizara na kwamba nguvu anayokwenda nayo siyo ya soda"(na ameishia kutoa indefinite deadline),kisha ile ya Bandarini Dar kuwa "ana orodha ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) wasio waaminifu ambao wanashirikiana na wafanyabiashara kukwepa kodi kwenye Bandari ya Dar es Salaam" (lakini licha ya kuahidi kukabidhi orodha hiyo kwa Kamishna wa TRA hajafanya hivyo hadi leo) ,sambamba na ile ya "sijui kwanini Tanzania ni masikini" (kama hajui atawezaje kuleta maisha bora).Kauli nyingine tata ni hii ya majuzi kuwa "takrima haikwepeki" (ambapo tafsiri ya jumla ni sawa na kuruhusu rushwa),na jana nimeona mahali akisema "Haiwezekani kuua albino halafu utajirike, ingekuwa hivyo albino wenyewe wangekuwa matajiri wakubwa mno,”.Na sasa amekuja na kauli nyingine tata kuwa "matukio ya mimba kwa wanafunzi wa kike nchini yanasababishwa na viherehere vya wanafunzi wenyewe".Kadhalika,sambamba na kauli hiyo Mkuu wetu wa nchi alinukuliwa akisema "Kila anayepata Ukimwi anaufuata mwenyewe na wengine ni viherehere vyao; kwa mfano watoto wa shule"




Tukiweka kando hizo kauli tata za huko nyuma,hii ya mimba za wanafunzi imenisukuma kuandika makala hii.Hivi ina maana Rais hafahamu kuwa baadhi ya mimba za wanafunzi zinachochewa na mabazazi wa kiume au mafisadi wa ngono wanaotumia fedha zao za kifisadi kuwarubuni mabinti hawa?Sawa,tunaweza kuwalaumu mabinti hawa wanaorubuniwa lakini ni muhimu kuangalia suala hili kwa undani zaidi kwani wengi wa wanafunzi wa kike wanaoishia kutundikwa mimba na mafisadi wa ngono wanatoka familia masikini na inawawia vigumu kukabiliana na vishawishi vya mabazazi hao.

Kwa kudai kuwa sababu kuu ni kiherehere cha mabinti hao,Rais anatupa lawama kwa asilimia 100 kwa wanafunzi hao wa kika kana kwamba wanajidunga mimba wao wenyewe.Kwanini,yeye kama mwanaume,asiangalie upande wa pili wa shilingi?Kwanini,kwa mfano,sambamba na kudai kuwa tatizo ni kiherehere cha wanafunzi hao angewashutumu pia wakware wanaowinda wanafunzi?Kwa tunaofahamu siasa za mtaani,licha ya kuwa ni uzinzi pekee,wakati mwingine tamaa ya wanaume wakware kwa wanafunzi au mabinti wadogo inakuzwa na imani potofu kuwa "dogodogo hawana ukimwi" au "hawana gharama kuwatunza",na ushenzi mwingine kama huo.Na hii yote ni mitazamo ya wanaume ambao wamesalimika katika shutuma hizo za Kikwete.

Tukija kwenye kauli yake kuwa "Kila anayepata Ukimwi anaufuata mwenyewe..." ni dhahiri kuwa aidha Rais hajui namna ukimwi unavyoambukizwa au anapuuza njia nyingine za maambukizo.Japo ni kweli kuwa njia kuu ya maambukizo ya ugonjwa huo hatari ni tendo la zinaa,lakini licha tu kuwa hiyo sio njia pekee bali pia si kila anayeambukizwa "anaufuata mwenyewe".Vipi kuhusu akinamama au akinababa wanaoletewa ukimwi na wenza wao wasio waaminifu?Takwimu kadhaa zimekuwa zikutuonyesha kuwa asilimia ya wanandoa walioathirikia kwa ukimwi ni kubwa kama ilivyo kwa wasio wanandoa,na hiyo ilipaswa kumfahamisha Rais kuwa "kuna wanaoletewa ukimwi" na sio "kuufuata wenyewe" kama anavyoamini yeye.

Tukienda mbali zaidi,kauli hiyo ya Rais inaweza kutafsiriwa kama kuwanyanyapaa waathirika wa ukimwi,hususan wale walioambukizwa na wenza wao,au walioupata kwa njia nyingine kama tohara na chanjo za kienyeji ambapo nyembe moja hutumika kwa watu mbalimbali na hivyo kujenga uwezekano mkubwa wa maambukizo.Na kwa vile taasisi nyingi za afya zina vifaa duni,ni dhahiri kuna wauguzi mbalimbali wanaoambukizwa ukimwi kutokana na na nyenzo hizo duni makazini mwao.Lakini kuna kundi jingine la muhimu-watoto wachanga wanaozaliwa wakiwa wameshaambukizwa ukimwi.Je Kikwete anaweza kudiriki kudai hata hawa nao wameufuata ukimwi wenyewe?

Kiongozi makini anapaswa kuepuka generalisation,yaani kutoa kauli za jumla jumla pasipo kuangalia exceptions katika anachozungumzia.Na ifahamike kuwa kauli ya Mkuu wa Nchi ni sawa na mtizamo wa nchi husika,hivyo hitaji la umakini kabla ya kutoa kauli zinazoweza kuwaathiri baadhi ya wananchi.

Anyway,pengine alikuwa anatania tu wakati akisema hayo kwenye sherehe za kimila huko Mwanza ambapo miongoni mwa walikuwa kwenye msafara wake ni mtuhumiwa wa ufisadi wa rada,Mzee wa Vijisenti Andrew Chenge.

5 Jun 2010

Mwezi Februari mwaka huu,Rais wa Kampuni ya Toyota (ya Japan) Akio Toyoda aliomba rasmi msamaha kwa wateja wa kampuni hiyo nchini Marekani ambao walikumbwa na matatizo ya kiufundi kwenye magari yao.Mwezi kama huo mwaka jana,mabosi wa mabenki ya RBS na HBOS ya hapa Uingereza nao waliomba msamaha kwa wateja wao na umma kwa ujumla kutokana na uzembe uliopelekea benki hizo kukwamuliwa na serikali kwa pauni bilioni 37 fedha za walipakodi wa hapa. Na hivi majuzi,Waziri Mkuu wa Japan,Yakio Hatoyama, ametangaza kuwa atajiuzulu kufuatia kutotimiza ahadi aliyotoa wakati wa kampeni zake za uchaguzi kuwa angeondoa vikosi vya jeshi la majini la Marekani katika visiwa vya Okinawa.


Lakini wakati hayo yakitokea,serikali ya CCM imewaamuru mawaziri wake kuzunguka mikoani kueleza mafanikio ya Awamu ya Nne katika harakati za wazi kuelekea Uchaguzi Mkuu.Tuweke ushabiki pembeni,hivi kweli mawaziri hawa hawakustahili kuzunguka huku na huko kuomba msamaha kwa mlolongo wa madudu tunayoendelea kuyashuhudia tangu mwaka 2005 (na pengine madudu zaidi yanayoendelea kufanywa na CCM miaka nenda miaka rudi)?


Msanii mkongwe wa hapa Uingereza (na duniani kwa ujumla),Sir Elton John aliwahi kuimba wimbo wenye jina SORRY SEEMS THE HARDEST WORD (yaani 'samahani inaelekea kuwa ni neno gumu').Na hakukosea,japo hakuwa analenga siasa za nchi zetu za Dunia ya Tatu,hususan Afrika,na hasa Tanzania.Watawala wetu ni wepesi sana katika kugeuza lawama kuwa pongezi,na wakibanwa katika hilo hugeuka mbogo na kuja na vitisho lukuki.

Labda nikukumbushe kidogo kwanini naamini ziara za mawaziri zingekuwa na maana zaidi kama zingetumika kuomba msamaha kwa wananchi badala ya kuelezea mafanikio ambayo kimsingi yanabaki kwenye takwimu zaidi kuliko uhalisia.Kwanza,Awamu ya Nne ilitufahamisha kuwa inafahamu kilio cha Watanzania,na ikaja na kauli mbiu ya kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya.Naamini mie si pekee niliyesahau kuhusu kauli mbiu hiyo kwa vile wala haisikiki tena.Lakini kama hiyo haitoshi,kukaongezwa kibwagizo cha Maisha Bora kwa Kila Mtanzania (Yanawezekana).Japo sote tunatambua kuwa watawala wetu wanaishi kama wako peponi lakini hiyo sio excuse ya kuwafanya wasielewe kuwa maisha bora yamewezekana zaidi kwa mafisadi kuliko kwa wananchi walalahoi wa kawaida.Kwahiyo kama viongozi hawa wangekuwa na nidhamu kwa wapiga kura waliowaweka madarakani hapo 2005 basi angalau wangetuambia nini kinachopelekea maisha bora kubaki haki ya mafisadi wachache huku walalahoi wakizi kuwa walalawima.

Baada ya kuingia madarakani,Awamu ya nne ilitueleza kuwa ili kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania kunahitajika baraza kuuuubwa la mawaziri.Binafsi niliona kuna mantiki katika hoja hiyo japo sikuwa na uhakika kuwa "mwalimu anaweza kumudu darasa lenye wanafunzi wengi" kama ilivyokuwa kwenye kabineti ya JK.Bila kuuma uma maneno,kwa kifupi ukubwa wa baraza la mawaziri haujafanikiwa kwa chochote katika ku-meet matarajio ya Watanzania.Sanasana wengine walilazimika kujiuzulu baada ya kutuingiza mkenge kwenye ishu kama za utapeli wa Richmond.Ungetegemea kujiuzulu huko kungeandamana na hatua za kisheria lakini waliojiuzulu waliishia kupongezwa huku wakikumbushwa kuwa yaliyowakumba ni ajali tu za kisiasa na si ajabu siku moja wakarejea madarakani.

Mkuu wetu wa nchi akatuambia kuwa anawafahamu wala rushwa ila anawapa muda wa kujirekebisha.Binafsi,hapo ndipo nilipoanza kuhisi kuwa sikuwa sahihi kuamini kwamba tumepata mrithi halisi wa Mwalimu (Nyerere) in the form of JK.Tangu lini mwizi akapewa deadline?Kama wala rushwa walikuwa wanajulikana kwa Rais kilichopaswa kufanywa ni yeye kukabidhi orodha hiyo kwa taasisi husika ili wachukuliwe hatua stahili.Unajua,laiti JK angekabidhi orodha ya wala rushwa anaowajua kwa vyombo vya usalama kisha wakakamatwa na kuepwa deadline,pengine by now tusingekuwa tunajiuliza wenye Kagoda ni akina nani.Ni muhimu wak Watanzania kumhoji Rais wetu mpendwa kuhusu hao wala riushwa anaowafahamu,na lini hiyo deadline ita-expire.Tunachohitaji ni majina na sio idadi,na hata kama ni idadi basi tuambiwe lini watashughulikiwa.

Tuaambiwa kuwa matatizo ya umeme yangepatiwa ufumbuzi wa kudumu only miezi michache baadaye kufahamu kuwa ufumbuzi wenyewe unahusisha matapeli wenye kampuni ya briefcase (Richmond).Shahidi muhimu katika sakata la EPA akahifadhiwa mpaka Maulana akachukua uhai wake (kuna wanaodai kuwa bado yuko hai au huenda kafanyiwa plastic surgery) halafu wenye nchi wakagoma katakata kutuambia mwizi mkubwa wa fedha za EPA (Kagoda ni nani).

Tuaaambiwa kuwa ziara za mara kwa mara za Rais wetu huko nje ni muhimu kuitangaza nchi yetu na yeye kujitambulisha,kabla ya kuaminishwa kuwa Mkutano wa Sullivan na huu wa majuzi wa Economic Forum utalinufaisha taifa hasa katika sekta ya utalii,only for tuliorogwa sie kulipa mabilioni ya shilingi kuialika timu ya taifa ya Brazil huku kukiwa na ngonjera zilezile za "ziara hii itasaidia kuitangaza Tanzania".Kama ziara za Rais huko nje na rundo la wafanyabiashara (plus mikutano kama ya Sullivan na huo wa Economic Forum) imeshindwa kuzaa matunda,dakika 90 za mechi na Wabrazili zitaweza?

Majuzi wafadhili wametangaza kupunguza misaada yao kwa sababu ya ufisadi (putting it straightforward) na Waziri wetu wa Fedha Mustapha Mkulo bila aibu anasema hiyo isitupe hofu kwa vile serikali itakopa benki ya Stanbic!Nasema "bila aibu" kwa vile sio tu kukopa sio sifa hususan kwa serikali iliyoingia madarakani na mkwara wa maisha bora kwa kila Mtanzania bali pia deni hilo litabebwa na walalahoi haohao wanaoendelea kubebeshwa mzigo wa mahela yanayokwibwa na mafisadi kila kukicha.

Haya,tukaambiwa tena kuwa kwa vile kuna mtikisiko wa uchumi wa dunia basi na hohehahe sie lazima tuyanusuru makampuni yetu katika kile kinachofahamika ki-uchumi kama "stimulus package".Hivi kwa mwenye akili timamu,ukitangaza kuwa kuna hela za bure somewhere unatagemea nini kama sio vigogo kuunda kampuni hewa na kuiba fedha hizo?Hadi leo hatujaambiwa mafanikio ya stimulus package hiyo, na kama ilivyokuwa kwenye ripoti ya mabomu ya Mbagala usitarajie kuambiwa lolote la maana zaidi ya takwimu za kizushi.

Halafu Mkuu wetu wa nchi akatupa presha kwa kuamua kuhutubia Bunge kuhusu sakata la EPA (pamoja na mambo mengine).Tunaloweza kukumbuka zaidi kwenye hotuba hiyo ni kauli yake kuwa anathamini sana haki za binadamu ikiwa ni pamoja na za mafisadi.Kumbukumbu nyingine ni angalizo kutoka kwa Spika wa Bunge,Samweli Sitta,kuwa haki za binadamu za walalahoi ni muhimu zaidi kuliko za hao mafisadi.

Nimejitahidi kuorodhesha machache yanayopaswa kuombewa radhi na mawaziri wa serikali ya Awamu ya Nne badala ya "kueleza mafanikio".Unless wanataka kutuaminisha kuwa kukua kwa ufisadi ni sehemu muhimu ya mafanikio yao.Natambua kuwa "SAMAHANI" ni neno gumu kama alivyosema Elton John lakini uungwana ni kitu cha bure.Hizo fedha za walipa kodi wanazotumia kuzunguka huku na kule zingeweza kutumika vizuri zaidi kwa kila Waziri kuomba msamaha kwa madudu aliyofanya katika miaka hii mitano.Kaulimbiu kuwa "mlitutuma, tumetekeleza, tumerudi kuwaelezeni tulivyotekeleza na kuwasikiliza" ni matusi ya nguoni kwa vile hakuna Mtanzania mwenye akili timamu aliyeituma serikali kuingia mikataba ya kitapeli na wazushi wa EPA,au kukomalia kutotaja Kagoda ni mdudu gani,plus madumu mengineyo.Tulichowatuma ni kutukomboa kutoka katika lindi hili la umasikini sambamba na kuboresha hali za maisha yetu.Hatukuwatuma kuuza kila kilichopo kwa bei ya kutupa wala hatukuwatuma kung'ang'ania kununua samani kutoka nje na hatimaye kukumbuka dakika za majeruhi kuwa ununuzi huo hauendani na umasikini wetu.

Japo nakerwa na ziara hizi za mawaziri zinazozidi kuwabebesha mzigo walipa kodi walalahoi lakini nakereka zaidi napoona watu hawa wanapotufanya wajinga kiasi cha kutuzushia kuwa TULIWATUMA KULEA UFISADI.

Tumia kura yako vizuri,ukiendekeza ushabiki utazidi kuumia.Hakuna miujiza inayoweza kuondoa ufisadi hata kama watu watakesha kwenye nyumba za ibada (na huko wanakutana na "wabishi" kama Askofu Kilaini ambao wanaendelea kung'angania mtizamo wao finyu kuwa JK bado ni chaguo la Mungu.Askofu muogope Mungu wako unayemtumikia,please!).Nia pekee ya kuondokana na ufisadi ni kuwaondoa mafisadi.Kumbuka kuwa ufisadi ni kitendo kinachofanywa na mafisadi,na as long as wanaendelea kuwepo basi inakuwa mithili ya kupe au mbung'o na damu.Watanyonya hadi tone la mwisho.

AMKA!

31 May 2010


Ukisoma habari zifuatazo unaweza kukubaliana nami kuwa AKUTUKANAE HAKUCHAGULII TUSI.Katika habari ya kwanza tunashuhudia Waziri wetu wa Fedha akiongea vitu ambavyo vinaleta maana tu vikiangaliwa kwa maadnishi lakini sio mtaani.Na katika habari ya pili,tunashuhudia uzembe uliozoeleka wa kitokee kwanza kisha tufanye kitu flani.Yaani siku zote hizi mtu aliyekabidhiwa dhamana ya kuongoza Jeshi la Polisi alikuwa hafahamu kuwa kituo cha polisi kisicho na silaha hakina tofauti simba wa karatasi!
Hebu soma habari husika hapa chini
Mkulo: Uchumi unazidi kukua 

Saturday, 29 May 2010 09:22

Exuper Kachenje

SERIKALI imesema kuwa ukuaji wa pato la taifa katika unakadiriwa kuongezeka na kwamba pato halisi litakua kwa asilimia 7 katika mwaka 2010.

Akiwasilisha taarifa ya mwelekeo wa uchumi kwa mwaka 2009 na mwelekeo katika kipindi cha kuanzia 2010 hadi 2013 mbele ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo alisema kuna matarajio makubwa uchumi kuendelea kukua.

Huku akiwaomba radhi wabunge kwa kuchelewa kuwapa nakala ya taarifa hiyo, Mkulo alisema maelezo hayo yalipitishwa juzi asubuhi na Baraza la Mawaziri.

"Naomba radhi waheshimiwa kwa kuchelewa kuwapatia nakala ya taarifa hii kwa kuwa imepitishwa jana asubuhi (juzi) na Baraza la Mawaziri hivyo imechelewa kuchapwa," Mkulo alisema.

Mkulo alisema kuwa katika mwaka 2011, pato halisi la uchumi litakuwa kwa asilimia 7.1, mwaka 2012 asilimia 7.4 na hadi kufikia mwaka 2013 pato halisi la taifa litafikia asilimia 7.8.

“Kama ilivyotarajiwa athari za msukosuko wa uchumi zilikuwa za mpito, hivyo ukuaji wa pato la taifa unakadiriwa kuanza kuongezeka. Pato halisi litakua kwa asilimia 7.0 mwaka 2010, asilimia 7.1 mwaka 2011, asilimia 7.4 mwaka 2012 na kuendelea kuongezeka hadi asilimia 7.8 mwaka 2013,” alisema Mkulo.

Alifafanua kuwa malengo hayo yanatarajiwa kufikiwa kwa kutekeleza sera na misingi ya uchumi kwa kuzingatia mambo mbalimbali, ikiwemo mwenendo wa uchumi wa dunia na hitaji la kujenga uwezo kukabiliana na athari za msukosuko wa uchumi wa dunia.

Alitaja misingi mingine kuwa ni kuendelea kutengemaza vigezo muhimu vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii hasa mfumuko wa bei, kuweka msukumo katika utekelezaji Dira ya Maendeleo ya Taifa, Mkukuta awamu ya pili, Kilimo Kwanza na kuelekeza rasilimali kwenye maeneo chochezi ya uchumi kwa haraka zaidi.

Kwa mujibu wa Mkulo katika kipindi hicho miradi inayopewa kipaumbele katika mwongozo huo wa bajeti itakuwa ni pamoja na miundombinu, uendelezaji ardhi na makazi pamoja na vitambulisho vya taifa.

Vingine ni nishati, viwanda, sekta ya fedha na pia kutaja uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba mwaka huu kuwa ni kipaumbele cha kipekee kwa serikali katika mwaka huu kwa lengo la kuhakikisha unafanyika kama ilivyopangwa.
Waziri huyo alisema katika muda huo kasi ya upandaji wa bei inakisiwa kupungua hadi asilimia 8.0 kufikia mwezi Juni mwaka huu na kupungua zaidi hadi asilimia tano ifikapo Juni 2011.

Aidha, alisema katika kipindi hicho mapato ya ndani ya taifa yatafikia uwiano wa asilimia 17.3 kwa mwaka 2010/11; asilimia 17.4 mwaka 2011/2012 na asilimia 17.6 ifikapo mwaka 2012/2013.

Alisema serikali pia inalenga kuwa na akiba ya fedha za kigeni itakayokidhi uagizaji bidhaa kutoka nje na huduma kwa kipindi kisichopungua miezi mitano; kuwa na viwango imara vya ubadilishaji wa fedha; kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara na kuedeleza kilimo na kupunguza viwango vya riba.
Kuhusu biashara, Mkulo alisema Tanzania imeshuka katika vigezo vya urahisi wa kufanya biashara kutoka nafasi ya 126 kati ya nchi 183 na kuwa ya 131 mwaka 2009.

Kuhusu mapato ya ndani, Waziri Mkulo alisema yaliongezeka kwa asilimia 18.1 kufikia Sh4,293.1 bilioni mwaka 2008/09; kutoka Sh3,634.6 bilioni mwaka 2007/08 na kwamba kiasi hicho ni pungufu ya asilimia 10 kwa mwaka 2008/09.

Kwa kipindi cha Julai 2009 hadi Machi 2010, mapato ya ndani yalifikia Sh3,490.3 bilioni ikiwa chini ya asilimia 8.7 ya makisio ya Sh3,924.9 kwa kipindi hicho akieleza kuwa hali hiyo ilitokana na athari za kuyumba kwa uchumi wa dunia.

Mkulo alisema kwa kipindi cha Julai 2009 hadi Machi mwaka huu matumizi ya serikali yamefikia Sh6,143.9 bilioni kati ya makisio ya Sh6,718.7 kwa kipindi hicho, ikiwa ni upungufu wa asilimia tisa uliotokana na upungufu wa mapato.

Wakichangia maelezo hayo wabunge walitaka serikali ieleze itafanya nini kuwezesha wananchi kumiliki uchumi badala ya kumiliki asilimia 10 pekee kama ilivyo sasa.

CHANZO: Mwananchi

IGP Mwema afuta vituo

na Sitta Tumma na Ali Lityawi
SIKU tatu baada ya wananchi wa Kata ya Mbarika, wilayani Misungwi, mkoani Mwanza kuvamia kituo cha polisi na kuua majambazi watatu, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema ameanza kulikarabati upya jeshi hilo.
Tanzania Daima imethibitishiwa hilo; ukarabati wa jeshi hilo umelenga kuvipunguza kwa kuvifutilia mbali baadhi ya vituo vidogo visivyokuwa na silaha wala askari wa kutosha.

Wakati IGP Mwema akipanga kuvifumua vituo hivyo, jeshi la polisi mkoani Mwanza halijamkamata mtu hata mmoja kuhusiana na tukio la kuvamia na kuvunja kituo cha polisi Mbalika na kuua watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.

Akithibitisha yote hayo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanmza, Simon Sirro (RPC), alisema IGP Mwema yupo katika mikakati ya kupunguza utitiri wa vituo vidogo vidogo vya polisi, kwani vimeonekana havina faida kwa wananchi.

“Unajua vituo hivi vidogo visivyokuwa na silaha havina faida kwa maana hiyo mkuu wa polisi kwa sasa yuko katika mpango wa kuvipunguza.

“Mkakati huu madhumuni yake ni kuwa na kituo kimoja kila kata chenye silaha na askari wa kutosha,” alisema Kamanda Sirro.

Mei 27 mwaka huu majira ya saa 1:30 jioni, wananchi wa Mbalika, wilayani Misungwi mkoani hapa, walivamia na kuvunja kituo cha Mbalika kisha kuua watuhumiwa.

Moja ya sababu za wananchi hao kuvamia na kufanya mauaji katika kituo hicho, inaonekana ni kutokuwa na silaha pamoja na askari wa kutosha kituoni hapo na kumshtua IGP Mwema.

Kamanda Sirro, alipoulizwa mikakati ya kupunguza vituo hivyo, alisema hana jibu anayepaswa kulizungumzia ni IGP Mwema pekee.

Tanzania Daima, ilipomtafuta IGP Mwema kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi, simu yake ilipokelewa na msaidizi ambaye alidai yuko mkutanoni.

“Afande IGP yupo kikaoni huku Kilolo mkoani Iringa; atakuwa Dar es Salaam kesho (leo),” alisema msaidizi huyo.


23 May 2010



MMOJA wa mawaziri wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete anatuhumiwa kushinikiza kuachiwa kwa dhamana ndugu wawili waliokamatwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na viungo vinavyosadikiwa kuwa vya binadamu.

Taarifa hizo za waziri huyo, ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa, kuhusishwa katika kashfa hiyo, ni mwendelezo wa mawaziri wa serikali ya awamu ya nne kuingia kwenye kashfa ambazo baadhi zimetinga mahakamani na nyingine kutolewa maamuzi.

Taariofa hizo pia zimeibuka siku chache baada ya mtu anayedaiwa kuwa mtoto wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Celina Kombani kuhusishwa na tukio la utekaji kijana mmoja anayejulikana kwa jina la Minja, tukio ambalo polisi imesema inaendelea kulichunguza wakati watuhumiwa wakiwa mahabusu.

Taarifa zilizolifikia Mwananchi kutoka wilayani Urambo mkoani Tabora zinasema waziri huyo alishinikiza kuachiwa kwa watuhumiwa hao kwa kumtumia mkuu wa wilaya hiyo, Anna Magoha.

Habari zinasema kuwa watuhumiwa hao waliokamatwa walikuwa wakiuza mifupa hiyo ya binadamu kwa kukata vipande vidogovidogo ambavyo waliviuza kila kimoja kwa Sh2,000.

Ilielezwa kuwa viongozi wa Kata ya Kaliua, akiwemo diwani, waliandaa watu kwa maelekezo ya waziri huyo ambaye alikodi magari mawili ambayo Jumatano wiki hii yaliwapeleka watu ambao walienda kufurika kwenye ofisi ya Magoha kulalamikia kukamatwa kwa watuhumiwa hao.

Akizungumza kwa simu na Mwananchi, Magoha alikiri kupokea malalamiko ya watu hao na kwamba kutokana na maelezo ya mashahidi walioshuhudia watuhumiwa hao wakikamatwa, waziri huyo aliwaita polisi, akiwemo mkuu wa upelelezi wa wilaya hiyo, na kuagiza watuhumiwa hao wadhaminiwe.

“Nafahamu kwamba suala hilo ni la kisheria zaidi, lakini, kwa kweli watu walikuwa wengi na malalamiko yao nilihisi yalikuwa ya msingi, nikawaita polisi akiwemo OC-CID, nikazungumza nao na kuwaagiza wataalamu wa sheria wapitie sheria kuona zinasemaje, nikaagiza wadhaminiwe wakati uchunguzi ukiendelea,” alieleza Magoha.

Kwa mujibu wa habari za kimahakama, waliokamatwa na viungo hivyo vinavyodhaniwa kuwa ni vya binadamu ni Risasi Jumanne, 27, na Mashaka Juma, 26, wakazi Kaliuwa kitongoji cha Mwangaza.

Kamanda wa polisi mkoani humo, David Mwakiruma, alithibitisha taarifa hizo  na kueleza kwamba watuhumiwa hao walitiwa mbaroni Jumapili iliyopita wakiwa na viungo hivyo.

Alisema polisi ilipata taarifa za kuwepo kwa watu wanaouza vipande vya mifupa ya viungo vya binadamu, ambavyo walikuwa  wakiuza kila kipande kidogo Sh2000 na baada ya kufuatilia polisi ilibaini kuwepo dalili za ukweli na baada ya kufanya upekuzi ndani ya nyumba ya watuhumiwa wakiongozwa na kamanda wa upelelezi wa wilaya hiyo, ASP Kaijanente, walibaini viungo hivyo.

Alisema upekuzi huo ulifanyika saa 12:50 jioni, Jumapili mbele ya mwenyekiti wa kitongoji hicho na jirani wa watuhumiwa na kwamba ndani ya chumba kimoja kati ya viwili vinavyotumiwa na watuhumiwa hao, darini kulikutwa viroba viwili kimoja kikiwa na madaftari.

Kifurushi kingine kinaelezwa na Mwakiruma kuwa kilikutwa na fuvu la kichwa kilichopasuliwa katikati, lakini kikiunganishwa kinaonyesha kuwa ni cha binadamu, taya la gego la chini lenye meno matatu na mfupa mmoja wa mguu kuanzia gotini kuteremka chini.

Vipande vyote vinasadikiwa ni viungo vya binadamu na polisi imesema vitapelekwa kwa mkemia mkuu wa sarikali ili vichunguzwe.

Taarifa kutoka Mirambo zilisema watuhumiwa walifikishwa mahakamani Juma nne wiki hii na kusomewa shitaka la kukutwa na viungo vya binadamu.

Wafuatiliaji wa sakata hilo walilieleza Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina yao kuwa dhamana hiyo ilitolewa; juzi jioni baada ya Magoha kuwaita viongozi wa polisi na hakimu wa wilaya hiyo ofisini kwake na kuwashinikiza watekeleze agizo hilo linalosadikiwa kutolewa na waziri huyo.

CHANZO: Mwananchi

22 May 2010



Katika siku za hivi karibuni,Rais Jakaya Kikwete amekuwa akitoa kauli ambazo kwa namna flani zinaweza kupelekea uvunjifu wa amani.Sote tunakumbuka hotuba yake kali aliyotoa mbele ya walioitwa 'wazee wa jiji la Dar es Salaam' ambapo baadhi ya maneno yake yanaweza kabisa kuwatia jeuri wanadola wanapoagizwa kudhibiti wananchi.Kwa ujumla hotuba hiyo ilitawalia zaidi na kauli za ubabe na vitisho badala ya kuelimishana kistaarabu.Mbona ukali huo haukutumika kwenye hotuba yake ya Agosti 2008,ambapo pamoja na mambo mengine na kinyume na matarajio ya wengi,aliongea kwa upole na kukumbushia haki za binadamu kwa mafisadi.Nadhani msomaji unakumbuka kijembe alichotoa Spika Samuel Sitta kwa JK kwamba haki za wananchi ni za muhimu pia (tena zaidi ya za mafisadi).

Majuzi akarejea tena kauli ambazo kwa hakika zinapaswa kukemewa vikali.Kwanza, 'aliwapa jeuri' vijana wake wa UVCCM kwamba wasikubali kufanyiwa vurugu kipindi cha uchaguzi.Huku akitambua wazi kuwa yeye ni Amiri Jeshi Mkuu,na mwanajeshi mstaafu,bado alitoa uhuru kwa vijana hao 'kukabiliana na vurugu kama zile za katika baadhi ya chaguzi ndogo zilizopita'.Hivi Rais wetu anajifanya hajui kuwa wenye jukumu la kukabiliana na vurugu ni jeshi la polisi na sio UVCCM?Hivi kiongozi wetu huyu haelewi kwamba kuna uwezekano wa wahuni kujichanganya na vijana hao wa CCM kisha katika 'kukabiliana na vurugu za wapinzani' wakapelekea maafa,na halafu wakajitetea kuwa waliamriwa na Rais 'kudili na vurugu kwa namna hiyo'?

JK anapaswa kufahamu kuwa si yeye wala hao vijana wake wa UVCCM wako juu ya sheria au wana mamlaka ya kujichukulia sheria mkononi.Kwa kuruhusu hilo,Rais anaweza kuyapa changamoto makundi mengine katika jamii 'kufuata busara zake' na kuchukua sheria mkononi badala ya kuviachia vyombo vya dola vitimize wajibu huo.

Lakini ukidhani hiyo ndio kauli pekee ya kutisha kutoka kwa JK,basi hujaiskia hii.Akiwa ziarani huko Mtwara,Rais aliagiza msako wa nyumba hadi nyumba kusaka wanafunzi waliofaulu na kuchaaguliwa kujiunga elimu ya sekondari lakini hawajafanya hivyo kutokana na sababu moja au nyingine.Kwa mujibu wa gazeti moja,Rais alisema "ikibidi hata nguvu itumike" katika utekelezaji wa agizo hilo.Hivi JK anaweza kutueleza ni nguvu ya namna na kiasi gani itakuwa halali katika utekelezaji wa agizo hilo?Je Rais hadhani kuwa agizo lake linaweza kupelekea ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa wanafunzi hao na wazazi wao?Kwanini badala ya msako uliopewa baraka za kutumia nguvu kusifanyike vikao kati ya wazazi wa wanafunzi hao na serikali ngazi ya mtaa,kata,au wilaya?Hivi Rais haelewi kuwa hata kama amri yake haitopelekea balaa kwa wanafunzi hao na wazazi wao (si unajua mgambo wanavyonyanyasa watu),na wanafunzi hao kupelekwa mzobe mzobe mashuleni,bado wanaweza kabisa kugoma kusoma wakiwa mashuleni?Shule sio sawa na baa ambapo unaweza kumpeleka mtu kibabe na kumshikia mtutu anywe pombe na akainywa kwa kuchelea matokeo.Kwa shule,hakuna namna unaweza kumlazimisha mtu asome na kuelewa.hata kama utampeleka shuleni kwa kikosi cha mizinga.

Je inawezekana kauli hizi za JK zinazobeba (au kuruhusu) matumizi ya nguvu zinatokana na ukweli kuwa yeye ni mwanajeshi mstaafu?Nauliza hivyo kwa vile kuna imani kwamba mentality anayojengwa askari jeshi huweza kudumu kwa mjeshi huyo kwa takriban muda wake wote wa uhai wake hata anapostaafu.

Kuna watakaotafsiri makala hii kama alarmist,yaani yenyebkubeba wasiwasi usio na msingi.Yote kheri,lakini tukumbuke kuwa pindi amani yetu ikivurugika kwa sababu ya matumizi mabovu ya nguvu ya uongozi wa umma,hakutakuwa na nafasi ya kuzuia uvunjifu wa amani.Kadhalika,ni vema kidhibiti dalili za udikteta kabla hazijaota mizizi na kushamiri.

Kwa bahati mbaya,au makusudi,ni kama watu wako usingizini (na usingizi wenyewe ni ule wa kupuliziwa dawa ya kulala bila kushtuka hata ukiangukiwa na paa).Namna mambo yalivyo ni kama watu 'wamekubali matokeo kabla ya kipenga cha mwisho'.Jeuri za watawala wanaopuuza haki za binadamu za wanyonge huimarishwa zaidi na 'usingizi huo wa pono'.Kama mtu anakufinya na wewe unazubaa tu,hutoi japo yowe,basi ni dhahiri kuwa sio tu mtu huyo atakubana zaidi bali pia ataamini kuwa huumii.

Amkeni!

20 May 2010

Nadhani unamfahamu Christina Aguillera,na kama unamfahamu basi ni dhahiri utakuwa unakumbuka 'singo' yake ya kwanza kabisa Genie in a Bottle (Kama huukumbuki basi cheki video hii hapa).

Ushaikumbuka?Well,lengo la makala hii si kumjadili mwanamuziki huyo au wimbo huo uliovuma sana.Nacho-focus hapa ni hiyo ishu ya 'jini kwenye chupa'.

Lakini kabla sijainyambua,ngoja nikupe stori moja fupi.Mwaka 2005 nilipokwenda nyumbani kwenye fieldwork,nilikutana na rafiki yangu mmoja wa zamani ambaye ni mtoto wa Sharifu huko Tanga.Baada ya mahojiano yetu nilimdadisi kuhusu suala la majini.Nae bila hiana akanipa darasa kutoka A mpaka Z.Actually,alikwenda mbali zaidi hadi kunionyesha namna jini linavyotengenezwa.Bila kuingia kwa undani sana,alichovya maandishi flani kwenye chupa na kutengeneza kitu alichokiita kombe,kisha akafunga hiyo chupa.Akaeleza kuwa katika muda aliokusudia,jini litatoka katika hiyo chupa na 'kufanya vitu vyake' (kwa mujibu wa manuizo/dua.Bado nakumbuka jinsi nilivyosisimka baada ya 'kuonyeshwa jini mtarajiwa'

Naamini usemi 'jini ndani/kwenye chupa' unaendana na mantiki ya utengenezaji jini (yaani linawekwa kwenye chupa kisha 'linalipuka' katika muda ulokusudiwa).Kwa mujibu wa yule mtoto wa Sharifu ni kwamba jini likishatengenezwa na kuhifhadhiwa ndani ya chupa tayari kwa 'maangamizi' haliwezi kurejeshwa.Na la zaidi ni kwamba jini likishatoka kwenye chupa haliwezi kurudisha.Kwahiyo basi,usemi 'jini kwenye/ndani ya chupa' unamaanisha kitu ambacho 'kikitoka kimetoka',yaani ni kama maji yakimwagwa ardhini,hayawezi kuzoleka.

Kwanini basi nimeamua kutumia msemo huu katika makala hii?Well,katika uchambuzi wangu kuhusu kauli za/matendo ya Rais wetu (Chaguo la Mungu) Jakaya Kikwete,naanza kupatwa na wasiwasi huohuo wa 'jini ndani/kwenye chupa'.Simaanishi kuwa JK ndio jini.Hapana.Nazungumzia kauli na matendo yake ya hivi karibuni.

Sijawahi kuzungumzia lolote kuhusu hotuba yake kali alotoa kwa wafanyakazi wa serikali waliokuwa wametishia kugoma.Kwa kifupi,baadhi ya kauli zake hazikupaswa kutolewa na kiongozi anayejali utawala wa sheria.Kwa kutaja maneno kama risasi za moto au namna wafanyakazi wangeweza kukumbana na nguvu za polisi ilikuwa ni mithili ya kubariki ukatili.Hata kama wafanyakazi wangegoma bado isingehalalisha matumizi ya nguvu 'to an extent baadhi yao wangeweza kukumbana na makali ya risasi za polisi'.Hivi sio JK huyuhuyu alosema kuwa yeye anathamini haki za binadamu ikiwa ni pamoja na za mafisadi?Tuliache hilo kwa sasa.

Juzijuzi akaibuka tena na kudai suala la takrima ni gumu kukwepeka.Mkuu wa nchi anaposema hivyo ni sawa na kubariki matumizi ya rushwa kwa jina la takrima.Kauli kama hiyo haipaswi kutolewa hata na katibu kata,let alone Mkuu wa nchi.Ugumu wa jambo haumaanishi liachwe kama lilivyo.Yaani kwa vile mapambano dhidi ya ukimwi ni magumu kwahiyo tuache watu 'watembee pekupeku'?Au kwa vile ugonjwa wa malaria umekuwa ukitusumbua miaka nenda miaka rudi basi tuuache kwa vile ni vigumu kupambana nao?Sasa alipohamasisha kampeni ya ZINDUKA na wapambe wake wa bongoflava alikuwa anamaanisha nini?Rais alipaswa kuelewa kuwa kwenye mapambano dhidi ya udhalimu,giving up is not an option.Laiti Nyerere na wapigania uhuru wengine wangekuwa na mtizamo finyu kama huo wa 'jambo hili gumu kwahiyo tuliache kama lilivyo' basi hadi leo tungekuwa bado koloni la Mwingereza.

Kilichonishtua zaidi hadi kufikia hatua hii ya kuleta ulinganifu na 'jini kwenye/ndani ya chupa' ni mkanganyiko uliojitokeza katika sakata la Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM).Awali ilielezwa kuwa kuna vipeperushi vilivyosambazwa kumtuhumu aliyekuwa Mwenyekiti ya jumuiya hiyo,Hamad Yusuph Masauni.Baadaye gazeti moja likabainisha kuwa mtoto wa JK,Ridhiwani,anatuhumiwa kuivuruga jumuiya hiyo na kuchochea suala hilo la Masauni.Lakini,akihutubia mkutano wa Jumuiya hiyo huko Iringa,JK aliweka bayana kuwa (namnukuu) "Tulipochunguza ilibainika ni kweli alighushi, wakati wa uchaguzi alisema alizaliwa mwaka 1979, lakini ukweli alizaliwa mwaka 1973 na alianza darasa la kwanza mwaka 1979".Je hii haimaanishi kuwa hata vipeperushi vilivyosambazwa kumhusu Masauni vilikuwa na uhusiano na 'uchunguzi' huo anaozungumzia JK?Kama ni hivyo,je si hatari inapotokea kiongozi wa nchi anaporuhusu michezo michafu kama hiyo kwa minajili tu ya kukidhi matakwa flani?

Kinachokasirisha ni kauli yake kuwa  "kijana huyo (Masauni) mpole na mzito kufanya maamuzi magumu na haraka...ni mkakamavu na mchapakazi atapangiwa kazi nyingine hapo baadaye".Yaleyale ya Mwilima.Mtu anaboronga huku kisha anazawadiwa uongozi.Kama ni kweli Masauni alifoji umri wake,hivi hiyo haimpotezei sifa za kuwa kiongozi mahala kwingine?Sasa JK anapotuambia kuwa aatapangiwa kazi kwingine anamaanisha nini?Au huko atakapopangiwa hakuhitaji uadilifu?Na kama 'kudanganya umri' si big deal kwanini basi wameshinikiza aondolewe UVCCM?Nauliza hiyo kwa vile,kwa mujibu wa 'Chaguo la Mungu',kufoji umri kulikopelekea Masauni kujiuzulu sio big deal ndio maana 'atapewa kazi nyingine baadaye'.

Habari nyingine zinazoweza kuashiria kuwa 'jini lililo ndani/kwenye chupa linaweza kutoka muda wowote ule' ni katika jarida la Raia Mwema kwamba Mawaziri Wakuu wastaafu wanafuatiliwa.Ukisoma habari hiyo utabaini kuwa kwa vyovyovte vile,Mkuu wa Nchi anafahamu kuhusu suala hilo.Lakini sidhani kama tunapaswa kushangaa sana kwa vile kama Masauni alichunguzwa (which is equivalent to kufuatiliwa kwa ex-PMs hao) na hatimaye vipeperushi vikasambazwa,basi katika utawala huu lolote linawezekana,hususan uzandiki na character assassination.

Na hili suala la promotion ya familia kwenye uongozi,japo si kosa,linaweza kutafsiriwa kwa namna ya maandalizi ya udikteta.Baba/mume rais,mama/mke naye mwanasiasa 'kiaina',kaka wa rais naye mwanasiasa,mtoto naye mwanasiasa,na hadi kitinda mimba naye kaingizwa kwenye siasa.Na hapa sizungumzii siasa kwa maana ya hamasa tu bali siasa za mizengwe na kugombea kwa kutumia jina.Hapa tunazalisha mfalme au dikteta?

Kwa Watanzania wengi ni business as usual.Lakini kwa wanaoangalia ishu na kukumbuka kuweka alama za kuuliza,yayumkinika kufananisha suala hili na ' jini ndani/kwenye chupa'.LIKITOKA LIMETOKA,hakutokuwa na jinsi ya kulirejesha kwenye chupa.

Kwa atakayechukizwa na uchambuzi huu (kama yule mjinga alontumia comment ya matusi) all I could tell them is SUCK IT UP!


18 May 2010

Ofkoz,Mtukufu Rais Jakaya Kikwete alikuwa anatania alipotetea rushwa hadharani kwa kudai takrima haikwepeki.Ndio,Rais alikuwa anatania,na ndo maana,Msajili wa Vyama vya Siasa John Tendwa amekaririwa na magazeti kadhaa akimtetea JK kuwa "kauli yake (JK) kuhusu takrima (rushwa) ilikuwa utani tu".Pengine neno 'utani' kwa mujibu Tendwa linaweza kuwa na maana kubwa zaidi tukilitafsiri katika informal English.Kwenye kamusi,'joke' (informal) inamaanisha An object of amusement or laughter; a laughingstock.Kwa Kiswahili,ni 'kituko', 'kioja' au 'kitu cha kuchekwa'.

Lakini kwa namna siasa zetu zilizvyojaa vituko (jokes) si ajabu Tendwa alikuwa serious kumtetea bosi wake JK.Na inawezekana kabisa Msajili huyo wa Vyma vya Siasa anayepaswa kufanya kazi bila upendeleo anaamini kwa dhati kuwa rais wetu alikuwa anataniana tu na viongozi wa dini.Kama ni hivyo,basi nae ni kituko pia.Haiingii akilini kwa kiongozi wa nchi kukutana na watu muhimu katika jamii yetu (viongozi wa dini) na kufanya 'utani mbaya' kama huo.Kulikuwa na umuhimu gani basi wa rais kuhudhuria mkutano huo kama lengo lilikuwa kutoa utani tu?Si angeweza kuwapigia simu kwa wakati wake kisha akawarushia utani huo!

Kwa bahati mbaya,au makusudi,'utani huo mbaya' ushaanza kusahaulika miongoni mwa Watanzania wengi.Siwezi kuwalaumu walalahoi ambao wako bize na kuhakikisha mkono unaenda kinywani,lakini nashindwa kujizuia kuwashangaa Watanzania wenzetu walio katika 'tabaka la kati' (middle class) kwa kuweka umuhimu zaidi kwenye ishu kama tuzo za Kili,ujio wa Sean Kingston,'kujirusha',nk ilhali tabaka la chini linalohitaji sapoti yao likizidi kuangamia.Wengi wa walio katika tabaka la kati wako bize zaidi 'kuishi kama tabaka tawala' (hata kama hiyo itamaanisha wakope kwa ndugu na marafiki au wajihusishe na ufisadi) kuliko kupambana na 'tabaka tawala' (tabaka la juu) 'kusawazisha uwanja' (to level the ground) kwa minajili ya kujenga jamii yenye kukaribia usawa.


Sijui tunaelekea wapi,lakini lililo bayana ni kwamba hatma ya taifa letu iko mashakani.Ukiona mkuu wa nchi anaongea pasi hofu (na kicheko juu,kama kawaida yake) kuwa takrima (ambayo ni jina la kistaarab la rushwa) haikwepeki.Tafsiri pana ya kauli hiyo ya 'Chaguo la Mungu' ni mithili ya kuhalalisha uhalifu kwa vile rushwa ni kosa la jinai.Lakini binafsi sishangazwi sana na kauli hiyo ya 'mwenye nchi' kwa vile alishawahi kutamka bayana kuwa 'anajali haki za binadamu za mafisadi' alipohutubia Bunge Agosti mwaka 2008



Kusoma habari kamili kuhusu utetezi wa Tendwa kwa Kikwete BONYEZA HAPA na HAPA.

15 May 2010

Kwa hakika baadhi ya kauli za Rais wetu Jakaya Kikwete zinachanganya kupita kiasi.Juzijuzi tu alisaini kwa mbwembwe sheria tuliyoambiwa imelenga kudhibiti rushwa katika chaguzi.Tukiweka kando suala la wasaidizi wake kumwingiza mkenge kwa kuchomekea vipengele kinyemela,sambamba na mapungufu lukuki katika utekelezaji wa sheria hiyo (kubwa likiwa uswahiba kati ya CCM ya Kikwete huyohuyo na mafisadi),uamuzi wa kuwa na sheria hiyo ulileta faraja kidogo kwamba angalau mkuu wa nchi sasa anaanza kuikabili rushwa kwa vitendo badala ya maneno na ahadi tupu.

Sasa kabla hata sheria hiyo haijapata nafasi ya kutumika ipasavyo,JK kaja na hadithi mpya.Kwa mujibu wa vyombo vya habari,Rais amewaeleza viongozi wa dini kuwa suala la takrima kwenye chaguzi ni gumu kulidhibiti.Kama huelewi vizuri maana ya takrima basi naomba nikugamishe kuwa hiyo ni jina la kistaarabu (polite name) la rushwa au hongo wanayotoa wagombea kwa kisingizio cha 'ukarimu'.
Kinachonifanya nishindwe kumuelewa JK ni hiki: ina maana wakati anaipigia chapio sheria anayoamini itadhibiti rushwa kwenye chaguzi alikuwa hafahamu kuwa takrima (ambayo ni rushwa) ni ngumu kudhibitiwa? Au tuseme JK haamini kuwa takrima ni rushwa na ndio maana iliharamishwa?Na je kama takrima ni ngumu kudhibitiwa kwahiyo inakuwa halali?Je kiongozi wetu huyu haoni kuwa mkanganyiko anaozua unaweza kupelekea mvurugano baada ya uchaguzi ambapo wagombea watakaoshindwa kutokana na uwezo wao duni kumudu kutoa takrima wakikimbilia mahakamani,watoa rushwa (takrima) watatumia kauli ya JK kuhalalisha kuwa walichofanya ni sehemu ya utamaduni wetu wa ukarimu ("kama alivyobainisha Rais tarehe 14/05/2010)?

Habari kamili kuhusu kauli hiyo ya JK soma HAPA na HAPA.

28 Apr 2010

Matokeo ya utafiti uliofanywa na Mradi wa Utafiti na Elimu na Demokrasia Tanzania (REDET) yanaonyesha kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ni mchapakazi zaidi ya 'bosi' zake,Rais Jakaya Kikwete na Makamu wa Rais Dkt Ali Mohammed Shein. Kwa mujibu wa habari zilizochapishwa katika gazeti la Mwananchi,asilimia 61.2 ya wananchi waliohojiwa wameonyesha kuridhishwa na utendaji wa Pinda huku Kikwete akipata asilimia 58.8 na Dkt Shein akiwa na asilimia 46.8Kwa habari kamili soma HAPA.

20 Apr 2010

Hapa chini kuna habari ambayo kama ni ya kweli basi hatma ya nchi yetu iko mashakani.Lakini kabla hujaisoma,angalia picha ifuatayo na inaweza kukusaidia kukupa uelewa wa namna tulivyofika tulipo.






KUMBE Rais Jakaya Kikwete hakusoma sheria aliyosaini kwa mbwembe. Sasa baada ya kugundua kasoro zake anataka ikarabatiwe kwa njia ya kanuni, MwanaHALISI limeelezwa.

Hilo liligundulika katika mkutano wa wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wenyeviti na makatibu wa wilaya uliomalizika wiki iliyopita mjini Dar es Salaam.

Taarifa za ndani zinasema, bila aibu na hasa kwa ujasiri wa kiongozi mkuu wa nchi, Rais Kikwete alimuuliza Philip Marmo, waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, maana ya baadhi ya vifungu katika sheria hiyo.

Lakini katika hali ambayo haikutegemewa, Marmo alijibu kana kwamba anamkejeli rais, jambo ambalo lilistua wajumbe wa kikao hicho cha juu cha utekelezaji wa sera za chama.

MwanaHALISI limeelezwa kwamba Rais Kikwete alistushwa na kifungu cha sheria kinachotaka mgombea kuwasilisha katika ofisi za msajili, taarifa ya fedha atakazotumia.

Kifungu hicho kinatoa siku saba kabla ya siku ya mwisho ya NEC kutangaza majina ya wagombea.

Kifungu kingine kinachodaiwa kumstua kinahusu idadi ya wajumbe wa kampeni. Kwa CCM, yenye hata vikundi vya ngoma na nyimbo kama ToT, kuweka timu ndogo kunaweza kupunguza shamrashamra na kuathiri kampeni.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, ilikuwa baada ya rais kupitia maeneo hayo, alimuuliza Waziri Marmo iwapo kile alichokuwa akifafanua kimetokana na sheria iliyopitishwa.

Naye Marmo, akiongea kwa sauti ya unyenyekevu alijibu, “…hiki ndicho ulichosaini.”

Kwa kauli ya Marmo, Rais Kikwete alionekana kustuka na kusema, kama hali ni hivyo, basi sheria itakuwa imeingilia hata mchakato wa wagombea ndani ya vyama, kimeeleza chanzo chetu.

Taarifa zinamnukuu rais akihoji kwa nini “sheria imekwenda mbali mno” na kuagiza papohapo kuwa wahusika waangalie ambapo sheria inaingiliana na watengeneze kanuni zitakazoleta nafuu.

Rais amenukuliwa akimwagiza Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutengeneza “kanuni vizuri” ili kuondoa mwingiliano unaoleta ugumu wa utekelezaji.

Hoja ya maelekezo ya sheria mpya ya gharama za uchaguzi ilikuwa moja ya ajenda za kikao cha NEC, wenyeviti na makatibu wa CCM wilaya kutoka kote nchini.

Tarehe 17 Machi mwaka huu, Rais Kikwete alisaini hadharani na kwa mbwembwe Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ikulu Dar es Salaam ambapo hafla hiyo ilihudhuriwa na majaji, wabunge, viongozi wa serikali na vyama vya siasa, mabalozi na waandishi wa habari.

Hata hivyo, sheria hii imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya siasa na wanaharakati, kabla na baada ya kusainiwa kuwa itakuwa ya udhibiti kwa wenye msimamo tofauti na watawala.

Aidha, siku tatu baada ya sheria hiyo kusainiwa, mbunge wa Karatu (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa alitupa kombora kwa kusema sheria aliyosaini rais ilikuwa na vipengele ambavyo havikujadiliwa bungeni na kwamba “viliingizwa kinyemela.”

Ubishi wa Mwanasheria Mkuu wa serikali, Jaji Frederick Werema kwamba hakukuwa na chochote kilichofanywa kinyemela ndio umekuza hoja ya Dk. Slaa na kufanya achimbue zaidi kshfa hiyo.

Katika kufukua, Dk. Slaa amekwenda hadi kwenye kumbukumbu za bunge (Hansard) na kuthibititisha kuwa Kifungu 7 (3) ambacho kimo katika sheria aliyosaini rais hakikujadiliwa bungeni na hivyo hakikurekodiwa katika hansard.

Mtunga sheria huyo kutoka Karatu amesema pia kuwa chochote kilichojadiliwa bila kuamuliwa na bunge kilikuwa kinatarajiwa tu katika kanuni au fafanuzi za au ainisho za maneno na taratibu lakini siyo katika vifungu vya sheria.

Katika majibu yake kwa kauli za Dk. Slaa, Jaji Werema alitetea serikali na kuthibitisha kuwa kifungu hicho kiliwekwa na waziri Marmo.

Dk. Slaa amesema katika andishi maalum, “Hakuna mwenye mamlaka, hata rais hana mamlaka hayo, sembuse waziri.

“Baada ya mjadala katika Kamti ya Bunge zima, maneno yakikubaliwa ndiyo hayo yanaingia kwenye sheria na serikali haina mamlaka ya kwenda kuyarekebisha inavyotaka. Ndiyo maana ya kusema ‘kifungu kimepitishwa,’ ” ameeleza Dk. Slaa.

Akiweka msisitizo, Dk. Slaa anasema, “Kitendo cha kuchomeka kinyemela ni kitendo kibaya sana na kinapaswa kulaaniwa, kwa sababu, kwa utaratibu huu wataalam wanaweza kuipeleka nchi pabaya kwa kupenyeza jambo lolote wanalotaka wao hata kama halijajadiliwa au limekataliwa na Bunge.”

Dk. Slaa anafafanua hatua ya serikali ya kuingiza mambo kinmyemela katika sheria kuwa ni kosa la jinai na kusema hata kifingu walichochomeka kinyemela kina madhara makubwa.

Kifungu kilichoongezwa na serikali kinataka timu ya kampeni kukaguliwa na watendaji wa serikali ya CCM.

“Kampeni ndiyo inayobeba mikakati na siri yote ya uchaguzi. Haiingii akilini kabisa kuwa serikali (pengine unayotaka kuiondoa kwenye uchaguzi ambayo ndio haki ya msingi ya kila mgombea) ndiyo inaweka mkono wake kwenye udhibiti wa mikakti hiyo,” anafafanua Dk. Slaa.

Anasema kuweka kifungu kama hicho ni “wenda wazimu, kwa mtu yeyote aliyefikiria jambo hilo, au anaandika tu kutoka mezani na au hajui maana halisi na majukumu yake.”

Kutokana na kuibuka kwa kashfa hii, serikali sasa imeamua sheria hiyo irejeshwe bungeni ili kufanyiwa marekebisho yanayostahili.

Naye Dk. Slaa tayari ametoa pendekezo: “Namna pekee ya kuepukana na athari hiyo ni kwa serikali kukiri imefanya makosa, na ndio ustaarabu bila kutafuta visingizio.”

Anasema serikali iwasilishe kwenye Mkutano wa 19 wa Bunge hili ulioanza jana, kitu kinachoitwa “Miscellaneous Amendment” – marekebisho ya sheria mbalimbali – na au ikichelewa sana katika Bunge la Bajeti.

Wachunguzi wa mambo wanasema Rais Kikwete atakuwa amesikitishwa sana na hatua ya wasaidizi wake ya “kumchomekea” vitu ambavyo baadaye vinamomonyoa hadhi yake kama mkuu wa nchi.

Miongoni mwa wanaotajwa kuwa wamempotosha au wameshindwa kumsaidia rais, ni pamoja na Jaji Werema ambaye ametetea uingizaji kinyemela kipengele ambacho hakikujadiliwa bungeni.

Mwingine anayetajwa ni waziri Marmo ambaye ambaye nduye hasa ametajwa kubuni na kuingiza maneno ya kifungu kinacholaaniwa.

CHANZO: Mwanahalisi.

10 Apr 2010

Kama Mtanzania mzalendo na mwenye kupenda nchi yangu nawajibika kuwa na heshima kubwa kwa Rais wangu Jakaya Kikwete.Hata hivyo,heshima inapaswa kuendana na matendo ya mheshimiwa.Kwa maana hiyo,naamini simkosei heshima Rais wangu nikihoji baadhi ya busara zake.Mpaka muda huu sielewi nini kinaendelea kati ya JK,Husna Mwilima na Sophia Simba!Awali,Sophia Simba kama Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM alisimama kidete kuhakikisha Mwilima 'anapigwa chini'.Tuhuma zilizotolewa dhidi yake ni 'mapungufu katika utendaji wake wa kazi.'Sasa kama tukiamini kuwa ni kweli Mwilima alishindwa kumudu majukumu ya uongozi huko UWT,how come JK ameamua kumpa ukuu wa Wilaya? Na kwa kuonyesha kuwa mambo yanaendeshwa kienyeji,Mwilima hakuchelewa 'kutoa mipasho kwa wabaya wake' pale alipotamka bayana kuwa kuteuliwa kwake na JK kuwa DC wa Tandahimba ni 'majibu ya JK kwa akina Sophia Simba'.Huwezi kumlaumu kuwa 'ameropoka' kwa vile hakujiteua.

Lakini swali la msingi ni kwamba je ni kweli JK ameamua kumteua Mwilima kumwonyesha Sophia Simba na UWT yake kuwa mwanamama huyo (Mwilima)aliondolewa katika wadhifa wake huko UWT kwa mizengwe na si mapungufu ya utendaji kazi?Lakini kama jibu la swali hilo ni ndio,hivi JK si ndio Mwenyekiti wa CCM ambayo UWT ni jumuiya yake,na kwa maana hiyo alikuwa na uwezo wa kusimamia mtizamo wake kuwa Mwilima ni mtendaji kazi hodari?Kwanini aliacha mwanamama huyo adhalilishwe huko UWT kabla ya kuamua 'kumsafisha' kwa kumpa u-DC?

Katika picha kubwa zaidi,je inawezekana utoaji wa baadhi ya vyeo unafanyika sio kwa maslahi ya wananchi bali kusafishana na 'kupunguza maumivu ya kisiasa'?Nauliza hivyo kwa vile naamini kwamba kama Mwilima alikuwa ameonewa huko UWT,JK alikuwa na uwezo mkubwa wa 'kumlinda' kama alivyoamua 'kumlinda sasa' kwa kumpa u-DC.Kwa kukaa kwake kimya wakati Mwilima 'anapelekeshwa' huko UWT,inatafsiriwa kuwa alikuwa anaafikiana na maamuzi ya akina Sophia Simba.Lakini kwa uamuzi huu 'mpya' wa kumpa Mwilima u-DC,inatafsiriwa (kama anavyosema Mwilima) kuwa anafikisha ujumbe kwa akina Sophia Simba kuwa Mwilima 'alionewa tu huko UWT kwani bado ana sifa za kuongoza wananchi huko Tandahimba kama DC'!

Nilisema mwanzoni kuwa namheshimu Rais wangu JK lakini nadhani aidha ana washauri wabovu au yeye mwenyewe maamuzi yake ni dhaifu.Na bahati yake ni kwamba Watanzania wengi hawana muda wa kuhoji au 'kukomalia' baadhi ya maamuzi yake.Ni aibu kwa Rais wetu kugeuka sehemu ya mipasho ya akinamama hao (Mwilima na Sophia Simba).Ni dhahiri kinachofanyika hapo ni kupoza pande zote mbili,yaani JK kama Mwenyekiti wa Taifa wa CCM aliamua kukaa kimya pale Sophia Simba na wenzake walipomtimua Mwilima,lakini katika kumpoza Mwilima akaamua kumpatia 'zawadi' ya u-DC.

Halafu kwa mtindo huu tutarajie Maisha Bora kwa Kila Mtanzania?

22 Mar 2010


Kiongozi shurti awe na msimamo na kisha asimamie kile anachoamini.Kwa mara nyingine,Rais Barak Obama ameithibitishia dunia kuwa ni 'mwanaume wa shoka' linapokuja sula la kuamini anachosimamia.Hatimaye jana Obama alifanikiwa kupitisha sera yake ya mabadiliko katika mfumo wa afya ya jamii nchini Marekani.Hiyo ni baada ya safari ndefu na ngumu pengine zaidi ya kampeni yake ya kuingia Jumbe Jeupe (White House).Pamoja na kuhatarisha nafasi yake na ya chama chake kisiasa,Obama alipigana kiume kuhakikisha kuwa lazima mabadiliko hayo yafanyike,kwa gharama yoyote ile.Na kama inavyofahamika,mara nyingi maamuzi ya kihistoria huwa na tabia ya kutokuwa maarufu. Ushindi wa Obama katika suala hili unapaswa kuwa fundisho muhimu kwa Rais wetu Jakaya Kikwete ambaye miezi michache ijayo atahitimisha miaka yake mitano tangu aingie madarakani.Sote tunafahamu,with exception ya wale wanaopenda habari nzuri tu hata kama ni za uongo,kwamba kwa kiasi kikubwa ahadi za Kikwete kuikomboa Tanzania kutoka kwenye lindi na umasikini imebaki kuwa hadithi tu huku ufisadi ukishamiri na kuitafuna Tanzania kwa kasi ya ajabu.Yayumkinika kusema kwamba utawala wa Kikwete utakumbukwa zaidi kwa skandali kuliko ufanisi wa kuwatumikia Watanzania.Kibaya zaidi,Kikwete alitoa lundo la ahadi kuhusu namna atakavyoboresha maisha ya Watanzania,hence kauli-mbiu MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA.

Kuna wanaodhani kuwa kilichomsukuma Kikwete kuogmbea urais mwaka 2005 ni kukamilisha ndoto yake ya mwaka 1995 'iliyokwazwa' na Baba wa Tiafa Mwalimu Julius Nyerere.Wenye mtizamo huo wanaamini kuwa Kikwete alitumia miaka 10 iliyofuata akikusanya nguvu,sio katika namna gani atawatumikia Watanzania,bali atakavyoweza kuingia Ikulu.Ni katika 'piga ua' hii ndipo alijikuta akishirikiana na 'viumbe hatari' waliojipenyeza kwa kivuli cha 'wanamtandao' wakiwa na matarajio makubwa kuwa Kikwete akiingia Ikulu basi nao 'wameula'And they were not wrong.Kusuasua kwa Rais wetu katika kuchukua maamuzi mazito kumechangiwa zaidi na ushirika wake na watu hao.Na hii haiwezi kuwa excuse kwake kwa sababu alikuwa na kila sababu na uwezo wa 'kuwasaliti' laiti angekuwa na nia.Angeweza kabisa kuwaita Ikulu na kuwaambia 'nathamini sana mchango wenu kuniingiza madarakani,lakini mimi sasa ni Rais wa Watanzania wote ninayeongozwa kwa misingi ya Katiba.I'm sorry,atakayekwenda kinyume na sheria na taratibu za nchi basi sheria itachukua mkondo wake.Tubaki marafiki lakini sio kwa urafiki wa kukwamisha utawala wangu'.Simple and clear!

Tupo wengine tunaoamini kuwa licha ya ndoto hiyo iliyoanza 1995,Kikwete pia alisukumwa na dhamira ya kuwatumikia Watanzania.Na kututhibitishia kuwa tuko sahihi,alipoingia tu madarakani alitoa hotuba zilizoonyesha kuwa anafahamu kwa kina vikwazo vya maendeleo ya taifa letu.Aliweka wazi kuwa rushwa ni tatizo kubwa na angefanya kila awezalo kupambana nayo.Kama ilivyokuwa kwenye hotuba zake za wakati wa kampeni,Kikwete alipoingia madarakani alirejea kuahidi makubwa kwa Watanzania,na wengi tulimwamini kwa vile alikuwa akiongea lugha tunayoielewa (tofauti na Mkapa aliyezowea kutoa hotuba 'ngumu' kana kwamba ni mihadhara ya kitaaluma chuo kikuu).

Dalili ya kwanza kuwa Kikwete 'hana jipya' ni kauli yake kuwa 'anawafahamu wala rushwa bali anawapa muda wa kujirekebisha'.Nadhani kauli hiyo itaingia kwenye vitabu vya historia kama ya aina yake kwa mkuu wa nchi kutoa deadline kwa wahalifu.Lakini baadhi yetu tulijipa matumaini kwamba labda Rais alikuwa serious katika kauli hiyo,na kwamba baada ya deadline hiyo ku-expire angechukua hatua flani.Miaka mitano baadaye,sote tunafahamu sasa kuwa kauli hiyo ilikuwa mithili ya 'kumtishia mtu mzima nyau'.Na si kwenye kauli hiyo tu,bali tuliambiwa wakati flani kuwa amekabidhiwa orodha ya wauza madawa ya kulevya (na aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Bakari Mwapachu) na baadaye tena akatuambia kuwa anawafahamu wala rushwa pale Bandari Dar es Salaam,na majina anayo.So far,hajachukua hatua kwa wauza madawa ya kulevya (wa orodha ya Mwapachu) na hajawasilisha majina ya wala rushwa wa Bandari!Sasa kama Rais hataki kutoa majina ya wala rushwa anaodai anawafahamu,tutegemee nini kutoka kwa mwananchi wa kawaida?

Kama nilivyosema mwanzoni mwa makala hii,uongozi ni kusimamia katika kile unachomini hata kama kitakupunguzia umaarufu.Kikwete alipaswa kufahamu kuwa ili urais wake uwe na manufaa kwa Watanzania ni lazima 'akosane' na baadhi ya marafiki zake.Na kwa hakika hilo lingekuwa na maana zaidi kwani ni bora zaidi mara milioni kupendwa na Watanzania walio wengi na 'kuchukiwa na mafisadi wachache' kuliko kupendwa na 'kigenge kidogo cha mafisadi' na kulaumiwa na mamilioni ya Watanzania.Kama Kikwete alikuwa na dhamira ya dhati ya kuwaletea Watanzania maisha bora alipaswa asimame kidete kuhakikisha hilo linatimia kwa udi na uvumba.

Lakini kwa vile bado kuna miezi kadhaa kabla ya uchaguzi,na kwa vile Obama ametioa darasa zuri kwa viongozi ya type ya Kikwete,basi tunabaki with our fingers crossed kuwa huenda rais wetu nae akajitutumua na kurekebisha mambo katika muda huu uliosalia.Uzuri ni kwamba hata kama ufisadi umetuumiza kwa muda wote huu,uamuzi wa kuukalia kooni katika dakika hizi za majeruhi utafanikiwa kufuta machungu yote tuliyopitia.Ni kama katika fainali ya soka ambapo bao la ushindi linapatikana katika dakika za majeruhi.Shamrashamra zitakazoambatana na ushindi huo hazitajali kuwa bao la ushindi limepatikana dakika za lala salama.What matters ni ushindi.

Basi Rais Kikwete tunatarajia sasa utafanya kweli.Utatamka bayana kuwa ile deadline uliyotoa kwa wala rushwa unaowafahamu ime-expire na kuamuru vyombo vya dola viingie ulingoni (yes,vimekuwa vikiwajibika baada ya ruhusa yako).Utakabidhi ile orodha ya mafisadi ya pale Bandarini ambayo watendaji wanaisubiri ili wachukue hatua zinazostahili.Utaifanyia kazi pia ile orodha ya 'wauza unga' ulokabidhiwa na Mwapachu.Utaamuru wamiliki wa Kagoda wawekwe hadharani na kuchukuliwa hatua zinazostahili.Ukiwa mwenyekiti wa CCM,utatambua kuwa uwepo wa Mzee wa Vijisenti kwenye Kamati ya Maadili ya chama hicho licha ya tuhuma zinazomkabili ni mzaha usiokubalika,na utashauri awekwe kando hadi taratibu za kisheria zitapochukua mkondo wake.Utaamua kuwa suala la Richmond haliwezi kumalizwa 'kishkaji' bali wahusika wote watachukuliwa hatua ili iwe funzo kwa wanaotumia madaraka yao vibaya.Na mwisho,utaanza kutafsiri kwa vitendo ahadi zako lukuki ulizotoa wakati wa uchaguzi na kuendelea kuzitoa kwa muda wote uliokuwa madarakani.Rejesha ari,kasi na nguvu mpya katika kuleta MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA.

Kama Obama ameweza,wewe unaweza pia.It's all about kuamini unachosimamia na kusimamia unachoamini.

18 Mar 2010


Vigogo watajwa kujipa fedha zilizotolewa BoT
Ni Zile za Kunusuru Uchumi (Stimulus Package)

MATUMIZI ya Sh trilioni 1.7 kuhami uchumi dhidi ya mtikisiko wa kiuchumi duniani ulioathiri kampuni za ununuzi pamba mikoa ya kanda ya ziwa na hatimaye kampuni hizo kumegewa sehemu ya fedha hizo sasa yamezua utata, na sasa baadhi ya wakubwa wanatajwa kuwa sehemu ya walionufaika na fedha hizo, Raia Mwema imeelezwa.

Fedha hizo kupitia mfuko maalumu, maarufu kwa jina la ‘Stimulus Package’ , zilipitishwa na Bunge wakati wa bajeti lakini Kambi ya Upinzani Bungeni, kupitia kwa kiongozi wake Hamad Rashid Mohamed ilionya fedha hizo kuibua kile kilichoitwa kashfa ya EPA namba mbili, na kupendekeza fungu hilo liundiwe sheria ili kuwabana wahusika lakini serikali ilipuuza, ikitumia wingi wa wabunge kutoka CCM.Takriban miezi sita sasa tangu fedha hizo kuanza kutolewa, uchunguzi wa Raia Mwema katika kipindi hicho umebaini kuwa baadhi ya fedha zimekwenda katika kampuni zisizofahamika ama ambazo wahusika halisi hawajulikani na badala yake wamewatanguliza watu wengine.

Imeelezwa kwamba sehemu ya kampuni zilizochotewa mamilioni kutoka kitita hicho cha Sh bilioni 1.7 zina uhusiano na vigogo serikalini na wanasiasa na kwamba fedha hizo hazikukidhi matarajio ya serikali kwa wakulima wa pamba.

Kampuni ambazo zinaonekana katika orodha ya zilizopendekezwa ama zilizopata fedha hizo ni pamoja na S & C Ginning Co.Ltd (yenye makao yake Bulamba), Simon Agency Ltd (Mwanza), Fresho Investment Co. Ltd (Shinyanga), Gaki Investment Co. Ltd (ya Shinyanga), Bedugu Ginning Co. Ltd (ya Musoma), Intergrated Cotton Fields Ltd ( ya Mwanza), Igunga Cotton Company (makao yake yako Dar es Salaam), Robasika-Agroproducts Ltd yenye makao yake Kaliua, Tabora na Chesano Cotton Ginnery yenye makao yake Bariadi, Shinyanga.

Kampuni nyingine kwenye orodha hiyo ni Copcot Cotton Trading (Geita), Allanoe Ginneries Ltd (Mwanza), Shinyanga Region Co-op Union (Shinganya), Vsarrian Tanzania Ltd (Bunda), Birchand Oil Mill (Mwanza), Jambo Oil Mill (Shinyanga), Afrisian Ginning Company (Dar es Salaam) na S.M Holdings Ltd (Mwanza).

Nyingine ni Nida Textile Mills Ltd, Hassanal R. Waiji (Maswa), Blore Tanzania Ltd (Mwanhuzi, Shinyanga), Al-Adawi Co.Ltd (Mwanza), Olam Tanzania Ltd (Mwanza), Kahama Oil Mill (Kahama), Kahama Cotton Co. Ltd (Kahama), NGS Investment Co. Ltd (Bariadi), Roko Investment Co Ltd, Cotton Agency & Ginners Ltd na Aham Investment Co. Ltd (Dar es Salaam).

Nyingine ni New Sam Trust Co Ltd (Bariadi), Busangwa Organic Farming Association (Shinyanga), BioSustain Tanzania Ltd (Dar es Salaam), MSK Solutions (Mwanza), Mass Trading (Tabora), Sibuka Co Ltd (Maswa), Nsagali Co. Ltd (Bariadi) na Vitrecs Oil Mill ya Mwanza.

Haikuweza kufahamika mara moja kama kampuni zinazoelezwa kuwa na uhusiano na wakubwa ndizo zilizoorodheshwa ama ni zile ambazo zinatajwa kupokea fedha bila majina ya kampuni hizo kuwa hadharani, lakini Raia Mwema, limethibitishiwa kuwapo wakubwa walionufaika na mamilioni kutoka kwenye “stimulus package.”

Katika hali inayothibitisha kuwa mambo si shwari kati ya wakulima wa pamba na wanunuzi ambao wengi wamepata mgawo wa stimulus package, Bodi ya Pamba Tanzania imejikuta katika lawama kali si tu kutoka kwa wananchi bali hata baadhi ya viongozi wa CCM, akiwamo Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga, kukiibuka shinikizo kwa Rais Jakaya Kikwete kuifuta bodi hiyo kwa madai kuwa, imeacha shughuli za ununuzi pamba kufanyika holela kupitia kwa mawakala ambao wanawaumiza wakulima.

Kwa upande mwingine, taarifa zaidi zinabainisha kuwa licha ya Bunge kupitisha Sh trilioni 1.7 kwa ajili ya stimulus package, ni sh bilioni 870.8 pekee hadi sasa, ndizo zimekwishatolewa na Benki Kuu (BoT), chombo ambacho kimepewa mamlaka ya kutoa fedha hizo.

Mpango huo wa stimulus package ilitiliwa shaka na Kambi ya Upinzani Bungeni kupitia kwa kiongozi wake, Hamad Rashid Mohamed na kupendekeza utungiwe sheria maalumu ya udhibiti kwa kurejea uzoefu wa baadhi ya nchi za Asia.

Mapendekezo hayo ya kambi hiyo yalilenga kuinusuru nchi na “EPA namba mbili.” Katika hotuba yake bungeni wakati wa kujadili stimulus package mwaka jana, , mjini Dodoma , Hamad Rashid Mohamed, kwa niaba ya wabunge wenzake kutoka vyama vya CUF, CHADEMA na UDP, alihoji masuala mbalimbali kuhusu matumizi ya fedha hizo Sh. trilioni 1.7, zilizotangazwa na Rais Kikwete.

“Tunataka sheria ya Appropriation Act iwe na Schedule maalumu ya Stimulus Package na iseme waziwazi nani atapata nini, kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge iwe inapata taarifa kila miezi 3 ya utekelezaji wa hiyo stimulus package.

“Ni ukweli uliowazi kuwa stimulus package inazinufaisha benki tu, kwa kuzipa mwanya wa kufanya biashara nzuri na Serikali kwa kutumia fedha za Serikali yenyewe, na ndio maana katika nchi nyingine serikali imelazimika kuwa na hisa ili kuhakikisha kuwa fedha iliyotolewa ambayo inatokana na kodi za wananchi inadhibitiwa na kurudi kwa walipa kodi na wapiga kura.”

Hamadi alisema katika bajeti ya mwaka 2007/08 na ile ya 2008/09 serikali ilijizuia kukopa kwenye mabenki, kwa kigezo kikubwa kuwa mabenki yaweze kufanya biashara ya kukopesha sekta binafsi na kuwa zuio hilo liliongeza ufanisi kwa mabenki kukopesha sekta binafsi kwani mikopo kwa sekta binafsi ilipanda hadi kufikia asilimia 40.

Stimulus Package itapunguza mikopo ya benki kwenda kwenye sekta binafsi, na yale mafanikio yaliyokwishafikiwa yatayeyuka, vinginevyo mabenki yawekewe viwango vya kufikia katika kutoa mikopo nje ya stimulus package.

“Kwa mujibu wa taarifa ya Sera ya Fedha ya BoT serikali itazikopesha benki Sh bilioni 270 kwa ajili ya kuzikopesha sekta binafsi. Itatoa Sh bilioni 205 ili kukopa kwenye benki hizo.

Je, benki hizo zikishindwa kutumia fedha zile ambazo serikali imeziweka ili kukopesha sekta binafsi kutumia fedha hizo kufanya biashara na serikali kwa fedha za serikali? Hili litadhibitiwa vipi? Waziri atueleze,”, alihoji Hamad na kuongeza kuwa;

“Mwaka huu wa bajeti ni ya kuongeza matumizi na madhara yake ni mpango huo wa kuhami uchumi kuongeza mfumuko wa bei.

“Serikali imeamua kufidia vyama vya ushirika na kampuni zinazonunua mazao ya wakulima na kuyauza kwa hasara. Katika soko huria kuna kupata faida na kupata hasara. Wafanyabiashara makini wa mazao hupanga bei zao za kununulia mazao kwa kuzingatia bei walioipata katika soko la baadaye.

“Hata hivyo wengine hawapendi kuchukua tahadhari kwa kutegemea kwamba bei itapanda na kwa hiyo watapata faida kubwa. Bei imeshuka kwa hiyo wamepata hasara.” Alihoji akisema; Je, hakuna wafanyabiashara wa mazao waliolipa mikopo waliokopa kwa kujibana. Serikali ina uhakika gani kuwa mikopo hii ilitumiwa vizuri?”

Pia alipendekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua kampuni zitakazopewa fedha kutoka katika mpango wa kuhami uchuni.

Alitaka CAG kwanza kuthibitisha kuwa hasara waliopata haikutokana na matumizi mabaya ya mikopo na kwamba, gharama ya ukaguzi huu ilipwe na benki zilizokopesha. Alionya kuwa, la sivyo serikali inaweza kuliingiza taifa katika EPA namba mbili.

CHANZO:Raia Mwema.

16 Mar 2010


RAIS Jakaya Kikwete ameweka hadharani mambo yanayomchefua katika utendaji wake kuwa ni viongozi wa mashirika ya umma na taasisi zilizo katika hali mbaya kifedha, kumghilibu ili awaongezee mitaji wakati historia inaonyesha kuwa kufilisika kwa mashirika hayo kumetokana na utendaji mbovu.

Rais Kikwete alisema anajisikia vizuri na hata moyo wa kuongeza msukumo katika kuitaka serikali itoe fedha kwa taasisi zinazojiendesha kwa faida ili ziendelee kufanya vizuri kuliko taasisi hizo zinazofilisika.

Rais Kikwete alisema hayo jana alipokuwa akibadilishana mawazo na watendaji wakuu wa tume mpya ya mipango mara baada ya kuwaapisha Ikulu jana.

. Utakuta shirika lilikuwa na ndege tisa. Sasa lina ndege mbili. Anakuja mtu anasema, Mheshimiwa tungeweza kufanya vizuri iwapo tungeongezewa ndege saba,? alisema Rais Kikwete wakati akipata kinywaji na watendaji hao watano, akiwemo Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

?Ebu fikiria, walikuwa na ndege tisa sasa zimepungua hadi mbili, lakini wao wanaona sasa waongezewe nyingine. Hii inaingia akilini!

?Ingekuwa sasa wanazo 13 halafu wakaja na maelezo kwamba wangefanya vizuri zaidi iwapo wangeongezewa, hapo inaweza kuingia akilini.?

Rais Kikwete aliwaonya watendaji hao wakuu wa chombo hicho ambacho kitategemewa kufanya mapinduzi ya kiuchumi nchini kwamba viongozi wa mashirika na taasisi wa namna hiyo watafika kwao, hivyo wawe makini katika kuamua kulingana na matakwa yao.

Ingawa Rais Kikwete alionekana kueleza hilo kama mfano tu, mazingira yalionyesha kuwa ni moja ya mambo makuu aliyotaka kuwausia katika utendaji wao, kwenye majukumu waliyopewa watekeleze.

Hali hiyo alidhihirisha kutokana na kurudia mara tatu, kusisitiza juu ya ghiliba za viongozi hao wabovu aliosema kuwa licha ya kufanya vibaya kiutendaji, huishawishi serikali izidi kutoa fedha.

Ingawa Rais Kikwete hakutaja shirika lenye tabia hiyo, kauli yake inaweza kuhusishwa na kuyumba kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ambalo hivi sasa limebakiwa na ndege mbili tu baada ya kuyumba kiutendaji.

ATCL, ambayo ilikuwa ikitamba katika miaka ya themanini kutokana na kuwa na ukiritimba katika usafiri wa anga, iliingia mkataba na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) kwa ajili ya kuboresha huduma zake, lakini likajikuta likiporomoka zaidi hadi mkataba ulipovunjwa mwaka 2006.

Mwaka jana, shirika hilo lilizuiwa kufanya safari za anga baada ya kunyang'anywa leseni ya kupaa angani, hatua ambayo ililidhoofisha zaidi shirika hilo. Baada ya kurejeshewa leseni hiyo, bado ATCL imeshindwa kurudi katika hali yake ya kawaida licha ya serikali kutumbukiza fedha nyingi kujaribu kulinasua.

Takribani wiki mbili zilizopita, ndege ya ATCL ilipata hitilafu wakati ikitua mkoani Mwanza na kusababisha shirika hilo kusimamisha tena huduma zake kutokana na kukwama kwa ndege hiyo.

Awali kabla ya mazungumzo hayo ya chai, Rais Kikwete alimwapisha Dk Philipo Mpango kuwa katibu mtendaji wa Tume ya Mipango, akisaidiwa na manaibu katibu wanne; Maduka Kessy, Happiness Mgalula, Florence Mwandri na Cliphod Tandale.

Tume hiyo ya Mipango imeundwa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Kikwete baada ya kuivunja iliyokuwa Wizara ya Mipango na Uchumi, alipokuwa anaunda baraza jipya la mawaziri mwaka 2007.

Mara baada ya kuvunja wizara hiyo, idara ya uchumi iliunganishwa na iliyokuwa Wizara ya Fedha na kuifanya iwe na jina jipya la Wizara ya Fedha na Uchumi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Mpango alisema tume hiyo itakuwa chombo muhimu cha serikali katika kuweka mipango yenye tija kiuchumi kwa taifa.

Lakini alisema kwamba anakabiliwa na changamoto kubwa ya kupanga mipango mizuri ya nchi ambayo itasababisha mapinduzi ya kiuchumi, hasa ikizingatiwa kwamba kwa kipindi kirefu mikakati imekuwa ikiwekwa lakini bado Tanzania inaendelea kuorodheshwa kwenye nchi maskini.

?Kinachoniumiza ni kuona taifa linaendelea kuwa maskini hata baada ya miaka 40 ya uhuru,? alieleza Dk Mpango.

Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakikwamisha nchi kuendelea, alisema, ni taifa kuwa na vipaumbele vingi kuliko rasilimali yake ya kiuchumi.

Katika mazingira hayo, alisema mikakati mingi imekuwa haikamiliki kutokana na kile kidogo kinachopatikana.

Dk Mpango akasema pamoja na kwamba mawazo ya tume yake yatatokana na ushauri wa wataalamu wake, binafsi anaona watatilia mkazo vipaumbele vichache ili suala la maendeleo liwe la hatua kwa hatua.

Alitoa mfano wa Bandari ya Dar es Salaam kwamba inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo nchini iwapo itaimarishwa pamoja na miundombinu ya reli ili nchi za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), zitegemee kupitisha bidhaa zake Tanzania.

CHANZO:Mwananchi.

4 Mar 2010


Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi,Rais Jakaya Kikwete alieleza kwa undani matarajio yake kuhusu ufanisi wa Sheria mpya ya Uchaguzi.Pamoja na mambo mengine,sheria hiyo inatarajiwa kuziba mianya ya rushwa kwa wanasiasa wanaowania uwakilishi wa wananchi katika Bunge.Hata hivyo,pamoja na nia njema na umuhimu wa kuwa na sheria hiyo,ushahidi wa kimazingira unaashiria kuwa itabaki kuwa sheria tu kama zilivyo nyingine nyingi pasipo kuzaa matunda yanayokusudiwa


Tatizo la nchi yetu halijawahi kuwa ukosefu wa sheria bali usimamizi na utekelezaji wake.Mifano ni mingi,lakini kwa vile sheria hii ya Uchaguzi inalenga kudhibiti mianya ya rushwa,ni vema tukaangalia kwanza ufanisi wa sheria nyinginezo zilizopo ambazo kwa hakika zingeaidia sana kupunguza tatizo la rushwa laiti zingetumika ipasavyo.

Kinachokwaza zaidi usimamizi na utekelezaji wa sheria zetu nyingi ni ukosefu wa uzalendo miongoni mwa waliokabidhiwa dhamana ya kuzisimamia na kuzitekeleza.Ni kichekesho kusikia miongoni mwa taasisi zinazotarajiwa kuwa na dhamana ya hali ya juu katika usimamizi na utekelezaji wa sheria hiyo ni TAKUKURU,chombo ambacho wengi wetu tunaamini kuwa kimeshindwa kazi yake.Hivi TAKUKURU iliyoshindwa sio tu kuchukua hatua dhidi ya wezi wa Richmond bali pia kutengeneza ripoti feki ya kuwasafisha watuhumiwa itawezaje kusimamia na kutekeleza sheria hiyo mpya ya uchaguzi?

Ikumbukwe pia kuwa kwa kiasi kikubwa vyombo vyetu vya dola bado vina fikra ya zama za chama kimoja ambapo "madhambi" ya wana-CCM yanachukuliwa kama "ubinadamu" na hivyo vyombo hivyo kusuasua kuchukua hatua zinazostahili.Kwa baadhi ya taasisi za dola,hata kukemea maovu yanayotendwa na baadhi ya vigogo wa CCM ni kama na kuvunja sheria za nchi!

Kwa mwenendo huu,ni dhahiri basi sheria hiyo inaweza kutumika kuvibana vyama vya upinzani huku wana-CCM wakiendeleza libeneke la takrima kana kwamba imehalalishwa.Sheria hii imeletwa na serikali ya CCM ambayo rekodi yake katika mapambano dhid ya rushwa ina walakini mkubwa.Iweje chama kilichounda serikali kiendelee kuwa na mwenyekiti wa kamati yake ya maadili (Andrew Chenge) ambaye ana tuhuma katika suala la rada?

Pengine badala ya kupoteza muda kwa kuja na sheria mpya,ungefanyika mchakato wa kupitia sheria zilizopo na kuhakikisha zinasimamiwa na kutekelzwa ipasavyo.Vinginevyo,itakuwa ni hadithi ileile ya kuja na sheria mpya zenye kuleta matumaini mithili ya kauli-mbiu "mAisha Bora kwa Kila Mtanzania" huku matokeo yake yakibaki sifuri.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.