24 May 2010


Binti mdogo na mrembo ambaye yuko kwenye £ovely Gamble  anaitwa Ann-Lyyn Kapinga anacheza part ya Jasmeen. Huyu binti ni actress wa ukweli kwa sababu anasomea  fani hii na huwa ana perform kwenye theatres tofauti za South of England.

Mahojiano haya yamefanywa na Watayarishaji wa kipindi cha ALL ABOUT WOMEN ambacho presenter wake naye ni Dada wa  kibongo aitwaye Tina George, Kipindi hiko hurushwa kwenye  vituo vya television vya AILTV na Ben TV huku UK. 

Onyesho maalum la  Filamu ya £ovely Gambl kuchangia watoto yatima wanaoishi na virusi vya UKIMWI Litafanyika

                                                                   JUMAMOSI TAREHE 29/05/2010.
                                              SAA 12 Jioni MPAKA SAA 5.30 Usiku. 
                                                       WYCLIFFE VENUE,  
                                                        233 KINGS ROAD, 
                                                      READING, RG1 4LS

WATANZANIA WOTE WA UK MNAKARIBISHWA
------------------------------------------------------------------------
BARAKA BARAKA


Hatimaye kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki Kuu,Amatus Liyumba,inafikia ukingoni leo ambapo atasomewa hukumu.Japo zamani hizoo nilishawahi kuwa 'mnajimu/mtabiri wa kizushi' nilipoandikia magazeti ya Sanifu,Kasheshe na Komesha huku nikijiita 'Ustaadh Bonge' (na baadhi ya watu walikuwa wakiamini 'unajimu' huo),siwezi kwa hakika kubashiri lolote kuhusu hukumu hiyo.Kibaya zaidi,upeo wangu wa taaluma ya sheria ni dhaifu kama uchumi wa Somalia.

Lakini kabla ya kuzungumzia kwa undani kuhusu hukumu hiyo,pengine ni muhimu kuangalia kidogo mwenendo wa kesi hiyo inayogusa hisia za wengi (na wengine wakiwa na sababu zao binafsi).Hadi sasa sielewi mantiki iliyotumika katika kumweka Liyumba gerezani muda wote huu ilhali kisheria yeye anabaki kuwa mtuhumiwa hadi itakapoamuliwa vinginevyo na mahakama.Naomba ieleweke kuwa simtetei Liyumba japo ni 'mwana wa pakaya' kwangu.Ninachohoji hapa ni uhalali wa kumweka mtuhumiwa rumande kwa zaidi ya mwaka mzima pasipo kumpatia dhamana.Hii ni mithili ya kuwa na kiji-Guantanamo chetu ndani ya jamii inayodai kuzingatia utawala wa sheria.Hatari iliyopo ni kwamba kama akishinda kesi,Liyumba anaweza kudai fidia kubwa zaidi ya kiwango anachotuhumiwa kukifanyia ubadhirifu.Afungwe au aachiwe huru,kwa kuwekwa gerezani muda wote huo pasipo kupewa dhamana ni kama alishakuhukumiwa kabla ya hukumu ya leo.Badala ya kuwa 'innocent until proven guilty',hii imekuwa 'guilty until proven innocent'.

Tuje kwenye mwenendo wa kesi yenyewe.Kulikuwa na mikanganyiko kadhaa kwa upande wa mashtaka huku baadhi ya mashahidi wake wakimtetea mshtakiwa waziwazi.Pigo jingine kwa upande wa mashtaka ni kutokuwepo kwa mtu ambaye wangeweza kumfanya 'shahidi nyota' (star witness),aliyekuwa Gavana wa BOT,hayati Daudi Ballali (huyu nae alikuwa 'mwana wa pakaya' just like alivyo 'mrithi' wake,Prof Benno Ndulu).Kwa vile haingekuwa rahisi kwa Liyumba kufanya ubadhirifu huo pasipo Gavana kufahamu kinachoendelea kwa kipindi chote hicho,yayumkinika kusema kuwa marehemu Ballali angekuwa na umuhimu wa kipekee katika kesi hiyo.Na japo 'star witness' huyo hakuwepo,ushahidi ulotolewa na Naibu Gavana na watendaji wengine wa BOT unaweza kutafsiriwa kama 'habari njema' kwake badala ya kumkandamiza.

Halafu kuna tatizo jingine,nalo ni udhaifu wa wanasheria wa serikali/ waendesha mashtaka.Mjuzi mmoja wa masuala ya mahakamani aliwahi kuniambia kwamba wahitimu wa sheria waliofanya vizuri kwenye masomo yao hukimbiliwa na kampuni binafsi za sheria,na hivyo kuwaacha 'wale wa kawaida' wakitarajia ajira kutoka serikalini au vyombo vya sheria vya umma.Sote twaweza kubashiri nini kitajiri pindi wahitimu hawa wanapokutana mahakamani,huku wale wa 'daraja la kwanza' wakiwa upande wa washtakiwa au washtaki dhidi ya serikali.Inaelezwa pia kuwa kipato cha mawakili binafsi kipo juu zaidi ya cha wenzao wa serikalini/taasisi za umma.Ni dhahiri mwanasheria anayelipwa kwa saa au mwenye maslahi bora atakuwa katika nafasi nzuri dhidi ya mwenzie ambaye si ajabu wakati akiwa mahakamani atakuwa bize zaidi kupiga mahesabu ya namna ya kumudu maisha hadi siku ya mshahara wake kijungujiko kuliko kutimiza wajibu wake sawasawa.

Kwa wengi tunaofahamu ugumu kwa mtu wa tabaka la juu kama Liyumba kuhukumiwa kifungo,let alone kufunguliwa mashtaka (akina Chenge 'wanapeta' tu huku kesi ya Pro Mahalu ikisuasua na mafisadi wa Kagoda wakiendelea 'kula bata'),kuna hisia kuwa Liyumba 'anafanyiziwa' tu.Yani,si kwamba anachotuhumiwa kufanya hakikupaswa kumfikisha mahakamani bali ni imani inayozidi kushamiri katika Tanzania yetu kuwa mashtaka na vifungo ni kwa wanyonge na wasio na uwezo wa 'kununua au kutetea haki zao.'Wambeya' wanadai kuwa ishu ya Liyumba inaweza kuwa kama ya 'Babu Seya' ambapo inadaiwa kuwa kesi zao ni matokeo ya 'kuingilia maslahi ya watu'.By 'watu' haimaanishi mie na wewe bali vigogo ambao 'kugusa mali zao' ni zaidi ya kosa la jinai.Inadaiwa kuwa mtu anaweza kufisadi atakavyo na asichukuliwe hatua alimradi hagusi 'mali' za 'wenye nchi'.Na kama hujaelewa by 'mali' namaanisha nini,well,huijui vema Tanzania unayoishi au unayotoka.

Ok,tusubirie hukumu lakini kama umesoma vema between lines katika nilichoandika hapo juu basi utakuwa unafahamu bet yangu ikoje.

23 May 2010



MMOJA wa mawaziri wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete anatuhumiwa kushinikiza kuachiwa kwa dhamana ndugu wawili waliokamatwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na viungo vinavyosadikiwa kuwa vya binadamu.

Taarifa hizo za waziri huyo, ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa, kuhusishwa katika kashfa hiyo, ni mwendelezo wa mawaziri wa serikali ya awamu ya nne kuingia kwenye kashfa ambazo baadhi zimetinga mahakamani na nyingine kutolewa maamuzi.

Taariofa hizo pia zimeibuka siku chache baada ya mtu anayedaiwa kuwa mtoto wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Celina Kombani kuhusishwa na tukio la utekaji kijana mmoja anayejulikana kwa jina la Minja, tukio ambalo polisi imesema inaendelea kulichunguza wakati watuhumiwa wakiwa mahabusu.

Taarifa zilizolifikia Mwananchi kutoka wilayani Urambo mkoani Tabora zinasema waziri huyo alishinikiza kuachiwa kwa watuhumiwa hao kwa kumtumia mkuu wa wilaya hiyo, Anna Magoha.

Habari zinasema kuwa watuhumiwa hao waliokamatwa walikuwa wakiuza mifupa hiyo ya binadamu kwa kukata vipande vidogovidogo ambavyo waliviuza kila kimoja kwa Sh2,000.

Ilielezwa kuwa viongozi wa Kata ya Kaliua, akiwemo diwani, waliandaa watu kwa maelekezo ya waziri huyo ambaye alikodi magari mawili ambayo Jumatano wiki hii yaliwapeleka watu ambao walienda kufurika kwenye ofisi ya Magoha kulalamikia kukamatwa kwa watuhumiwa hao.

Akizungumza kwa simu na Mwananchi, Magoha alikiri kupokea malalamiko ya watu hao na kwamba kutokana na maelezo ya mashahidi walioshuhudia watuhumiwa hao wakikamatwa, waziri huyo aliwaita polisi, akiwemo mkuu wa upelelezi wa wilaya hiyo, na kuagiza watuhumiwa hao wadhaminiwe.

“Nafahamu kwamba suala hilo ni la kisheria zaidi, lakini, kwa kweli watu walikuwa wengi na malalamiko yao nilihisi yalikuwa ya msingi, nikawaita polisi akiwemo OC-CID, nikazungumza nao na kuwaagiza wataalamu wa sheria wapitie sheria kuona zinasemaje, nikaagiza wadhaminiwe wakati uchunguzi ukiendelea,” alieleza Magoha.

Kwa mujibu wa habari za kimahakama, waliokamatwa na viungo hivyo vinavyodhaniwa kuwa ni vya binadamu ni Risasi Jumanne, 27, na Mashaka Juma, 26, wakazi Kaliuwa kitongoji cha Mwangaza.

Kamanda wa polisi mkoani humo, David Mwakiruma, alithibitisha taarifa hizo  na kueleza kwamba watuhumiwa hao walitiwa mbaroni Jumapili iliyopita wakiwa na viungo hivyo.

Alisema polisi ilipata taarifa za kuwepo kwa watu wanaouza vipande vya mifupa ya viungo vya binadamu, ambavyo walikuwa  wakiuza kila kipande kidogo Sh2000 na baada ya kufuatilia polisi ilibaini kuwepo dalili za ukweli na baada ya kufanya upekuzi ndani ya nyumba ya watuhumiwa wakiongozwa na kamanda wa upelelezi wa wilaya hiyo, ASP Kaijanente, walibaini viungo hivyo.

Alisema upekuzi huo ulifanyika saa 12:50 jioni, Jumapili mbele ya mwenyekiti wa kitongoji hicho na jirani wa watuhumiwa na kwamba ndani ya chumba kimoja kati ya viwili vinavyotumiwa na watuhumiwa hao, darini kulikutwa viroba viwili kimoja kikiwa na madaftari.

Kifurushi kingine kinaelezwa na Mwakiruma kuwa kilikutwa na fuvu la kichwa kilichopasuliwa katikati, lakini kikiunganishwa kinaonyesha kuwa ni cha binadamu, taya la gego la chini lenye meno matatu na mfupa mmoja wa mguu kuanzia gotini kuteremka chini.

Vipande vyote vinasadikiwa ni viungo vya binadamu na polisi imesema vitapelekwa kwa mkemia mkuu wa sarikali ili vichunguzwe.

Taarifa kutoka Mirambo zilisema watuhumiwa walifikishwa mahakamani Juma nne wiki hii na kusomewa shitaka la kukutwa na viungo vya binadamu.

Wafuatiliaji wa sakata hilo walilieleza Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina yao kuwa dhamana hiyo ilitolewa; juzi jioni baada ya Magoha kuwaita viongozi wa polisi na hakimu wa wilaya hiyo ofisini kwake na kuwashinikiza watekeleze agizo hilo linalosadikiwa kutolewa na waziri huyo.

CHANZO: Mwananchi

22 May 2010



Katika siku za hivi karibuni,Rais Jakaya Kikwete amekuwa akitoa kauli ambazo kwa namna flani zinaweza kupelekea uvunjifu wa amani.Sote tunakumbuka hotuba yake kali aliyotoa mbele ya walioitwa 'wazee wa jiji la Dar es Salaam' ambapo baadhi ya maneno yake yanaweza kabisa kuwatia jeuri wanadola wanapoagizwa kudhibiti wananchi.Kwa ujumla hotuba hiyo ilitawalia zaidi na kauli za ubabe na vitisho badala ya kuelimishana kistaarabu.Mbona ukali huo haukutumika kwenye hotuba yake ya Agosti 2008,ambapo pamoja na mambo mengine na kinyume na matarajio ya wengi,aliongea kwa upole na kukumbushia haki za binadamu kwa mafisadi.Nadhani msomaji unakumbuka kijembe alichotoa Spika Samuel Sitta kwa JK kwamba haki za wananchi ni za muhimu pia (tena zaidi ya za mafisadi).

Majuzi akarejea tena kauli ambazo kwa hakika zinapaswa kukemewa vikali.Kwanza, 'aliwapa jeuri' vijana wake wa UVCCM kwamba wasikubali kufanyiwa vurugu kipindi cha uchaguzi.Huku akitambua wazi kuwa yeye ni Amiri Jeshi Mkuu,na mwanajeshi mstaafu,bado alitoa uhuru kwa vijana hao 'kukabiliana na vurugu kama zile za katika baadhi ya chaguzi ndogo zilizopita'.Hivi Rais wetu anajifanya hajui kuwa wenye jukumu la kukabiliana na vurugu ni jeshi la polisi na sio UVCCM?Hivi kiongozi wetu huyu haelewi kwamba kuna uwezekano wa wahuni kujichanganya na vijana hao wa CCM kisha katika 'kukabiliana na vurugu za wapinzani' wakapelekea maafa,na halafu wakajitetea kuwa waliamriwa na Rais 'kudili na vurugu kwa namna hiyo'?

JK anapaswa kufahamu kuwa si yeye wala hao vijana wake wa UVCCM wako juu ya sheria au wana mamlaka ya kujichukulia sheria mkononi.Kwa kuruhusu hilo,Rais anaweza kuyapa changamoto makundi mengine katika jamii 'kufuata busara zake' na kuchukua sheria mkononi badala ya kuviachia vyombo vya dola vitimize wajibu huo.

Lakini ukidhani hiyo ndio kauli pekee ya kutisha kutoka kwa JK,basi hujaiskia hii.Akiwa ziarani huko Mtwara,Rais aliagiza msako wa nyumba hadi nyumba kusaka wanafunzi waliofaulu na kuchaaguliwa kujiunga elimu ya sekondari lakini hawajafanya hivyo kutokana na sababu moja au nyingine.Kwa mujibu wa gazeti moja,Rais alisema "ikibidi hata nguvu itumike" katika utekelezaji wa agizo hilo.Hivi JK anaweza kutueleza ni nguvu ya namna na kiasi gani itakuwa halali katika utekelezaji wa agizo hilo?Je Rais hadhani kuwa agizo lake linaweza kupelekea ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa wanafunzi hao na wazazi wao?Kwanini badala ya msako uliopewa baraka za kutumia nguvu kusifanyike vikao kati ya wazazi wa wanafunzi hao na serikali ngazi ya mtaa,kata,au wilaya?Hivi Rais haelewi kuwa hata kama amri yake haitopelekea balaa kwa wanafunzi hao na wazazi wao (si unajua mgambo wanavyonyanyasa watu),na wanafunzi hao kupelekwa mzobe mzobe mashuleni,bado wanaweza kabisa kugoma kusoma wakiwa mashuleni?Shule sio sawa na baa ambapo unaweza kumpeleka mtu kibabe na kumshikia mtutu anywe pombe na akainywa kwa kuchelea matokeo.Kwa shule,hakuna namna unaweza kumlazimisha mtu asome na kuelewa.hata kama utampeleka shuleni kwa kikosi cha mizinga.

Je inawezekana kauli hizi za JK zinazobeba (au kuruhusu) matumizi ya nguvu zinatokana na ukweli kuwa yeye ni mwanajeshi mstaafu?Nauliza hivyo kwa vile kuna imani kwamba mentality anayojengwa askari jeshi huweza kudumu kwa mjeshi huyo kwa takriban muda wake wote wa uhai wake hata anapostaafu.

Kuna watakaotafsiri makala hii kama alarmist,yaani yenyebkubeba wasiwasi usio na msingi.Yote kheri,lakini tukumbuke kuwa pindi amani yetu ikivurugika kwa sababu ya matumizi mabovu ya nguvu ya uongozi wa umma,hakutakuwa na nafasi ya kuzuia uvunjifu wa amani.Kadhalika,ni vema kidhibiti dalili za udikteta kabla hazijaota mizizi na kushamiri.

Kwa bahati mbaya,au makusudi,ni kama watu wako usingizini (na usingizi wenyewe ni ule wa kupuliziwa dawa ya kulala bila kushtuka hata ukiangukiwa na paa).Namna mambo yalivyo ni kama watu 'wamekubali matokeo kabla ya kipenga cha mwisho'.Jeuri za watawala wanaopuuza haki za binadamu za wanyonge huimarishwa zaidi na 'usingizi huo wa pono'.Kama mtu anakufinya na wewe unazubaa tu,hutoi japo yowe,basi ni dhahiri kuwa sio tu mtu huyo atakubana zaidi bali pia ataamini kuwa huumii.

Amkeni!

21 May 2010



ONYESHO MAALUM LA FILAMU £OVELY GAMBLE TAREHE 29TH OF MAY 2010.  KARIBUNI KUCHANGIA YATIMA WALIOATHIRIKA NA UKIMWI TANZANIA NA JUMUIA YETU  YA TANZANIA. WATOTO HAWA WANAANGALIWA NA TANZANIA MITINDO HOUSE INAYOENDESHA SHUGHULI ZAKE TANZANIA.
      JUMAMOSI TAREHE 29/05/2010.
          SAA 12 Jioni MPAKA SAA 5NA NUSU Usiku.
         WYCLIFFE VENUE, 
        233 KINGS ROAD,
         READING, RG1 4LS.

VILEVILE KUTAKUWA NA CHAKULA, VINYWAJI, BURUDANI YA MIZIKI NA  VICHEKESHO . NYOTE MNAKARIBISHWA NA KUFIKA KWENU NDIO KUFANIKISHA SHUGHULI HII. TUNAWAOMBA MJE KUSAIDIA WATOTO HAWA NA JUMUIYA YETUWETU.
DRESS CODE: LADIES: DRESS SEXY & GENTS: SMART
MUSIC: LIVE MUSIC, AFRO BEAT, BONGO FLAVOR, HIP HOP, MDUARA AND RNB
TIKETI ZIPO KUANZIA £10 KWA VITI VYA VIP’s NA £5 KWA VITI VYA KAWAIDA.TIKETI ZINAPATIKANA –
SWIFT FREIGHTS UK (TZUK) – LONDON 0208 801 9800
AFRICANS IN LONDON TV (TINA) – LONDON
MOUDY – LONDON 078884441222
KAYE MARIE – LEICESTER 0794665430
BARAKA - LEICESTER 07909260435
BONGO FLAVOUR – READING 0118 958 5878
VINCENT BAR – READING 0118 959 3130
TANZANIA ASSOCIATION – READING 07865673756
FRANK – READING 07865594576
                                   INFO:[email protected]                                                                                             www.wix.com/effeort111/urbanpulse-tmh               
   http://www.youtube.com/watch?v=zNltrl096hU

20 May 2010

Nadhani unamfahamu Christina Aguillera,na kama unamfahamu basi ni dhahiri utakuwa unakumbuka 'singo' yake ya kwanza kabisa Genie in a Bottle (Kama huukumbuki basi cheki video hii hapa).

Ushaikumbuka?Well,lengo la makala hii si kumjadili mwanamuziki huyo au wimbo huo uliovuma sana.Nacho-focus hapa ni hiyo ishu ya 'jini kwenye chupa'.

Lakini kabla sijainyambua,ngoja nikupe stori moja fupi.Mwaka 2005 nilipokwenda nyumbani kwenye fieldwork,nilikutana na rafiki yangu mmoja wa zamani ambaye ni mtoto wa Sharifu huko Tanga.Baada ya mahojiano yetu nilimdadisi kuhusu suala la majini.Nae bila hiana akanipa darasa kutoka A mpaka Z.Actually,alikwenda mbali zaidi hadi kunionyesha namna jini linavyotengenezwa.Bila kuingia kwa undani sana,alichovya maandishi flani kwenye chupa na kutengeneza kitu alichokiita kombe,kisha akafunga hiyo chupa.Akaeleza kuwa katika muda aliokusudia,jini litatoka katika hiyo chupa na 'kufanya vitu vyake' (kwa mujibu wa manuizo/dua.Bado nakumbuka jinsi nilivyosisimka baada ya 'kuonyeshwa jini mtarajiwa'

Naamini usemi 'jini ndani/kwenye chupa' unaendana na mantiki ya utengenezaji jini (yaani linawekwa kwenye chupa kisha 'linalipuka' katika muda ulokusudiwa).Kwa mujibu wa yule mtoto wa Sharifu ni kwamba jini likishatengenezwa na kuhifhadhiwa ndani ya chupa tayari kwa 'maangamizi' haliwezi kurejeshwa.Na la zaidi ni kwamba jini likishatoka kwenye chupa haliwezi kurudisha.Kwahiyo basi,usemi 'jini kwenye/ndani ya chupa' unamaanisha kitu ambacho 'kikitoka kimetoka',yaani ni kama maji yakimwagwa ardhini,hayawezi kuzoleka.

Kwanini basi nimeamua kutumia msemo huu katika makala hii?Well,katika uchambuzi wangu kuhusu kauli za/matendo ya Rais wetu (Chaguo la Mungu) Jakaya Kikwete,naanza kupatwa na wasiwasi huohuo wa 'jini ndani/kwenye chupa'.Simaanishi kuwa JK ndio jini.Hapana.Nazungumzia kauli na matendo yake ya hivi karibuni.

Sijawahi kuzungumzia lolote kuhusu hotuba yake kali alotoa kwa wafanyakazi wa serikali waliokuwa wametishia kugoma.Kwa kifupi,baadhi ya kauli zake hazikupaswa kutolewa na kiongozi anayejali utawala wa sheria.Kwa kutaja maneno kama risasi za moto au namna wafanyakazi wangeweza kukumbana na nguvu za polisi ilikuwa ni mithili ya kubariki ukatili.Hata kama wafanyakazi wangegoma bado isingehalalisha matumizi ya nguvu 'to an extent baadhi yao wangeweza kukumbana na makali ya risasi za polisi'.Hivi sio JK huyuhuyu alosema kuwa yeye anathamini haki za binadamu ikiwa ni pamoja na za mafisadi?Tuliache hilo kwa sasa.

Juzijuzi akaibuka tena na kudai suala la takrima ni gumu kukwepeka.Mkuu wa nchi anaposema hivyo ni sawa na kubariki matumizi ya rushwa kwa jina la takrima.Kauli kama hiyo haipaswi kutolewa hata na katibu kata,let alone Mkuu wa nchi.Ugumu wa jambo haumaanishi liachwe kama lilivyo.Yaani kwa vile mapambano dhidi ya ukimwi ni magumu kwahiyo tuache watu 'watembee pekupeku'?Au kwa vile ugonjwa wa malaria umekuwa ukitusumbua miaka nenda miaka rudi basi tuuache kwa vile ni vigumu kupambana nao?Sasa alipohamasisha kampeni ya ZINDUKA na wapambe wake wa bongoflava alikuwa anamaanisha nini?Rais alipaswa kuelewa kuwa kwenye mapambano dhidi ya udhalimu,giving up is not an option.Laiti Nyerere na wapigania uhuru wengine wangekuwa na mtizamo finyu kama huo wa 'jambo hili gumu kwahiyo tuliache kama lilivyo' basi hadi leo tungekuwa bado koloni la Mwingereza.

Kilichonishtua zaidi hadi kufikia hatua hii ya kuleta ulinganifu na 'jini kwenye/ndani ya chupa' ni mkanganyiko uliojitokeza katika sakata la Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM).Awali ilielezwa kuwa kuna vipeperushi vilivyosambazwa kumtuhumu aliyekuwa Mwenyekiti ya jumuiya hiyo,Hamad Yusuph Masauni.Baadaye gazeti moja likabainisha kuwa mtoto wa JK,Ridhiwani,anatuhumiwa kuivuruga jumuiya hiyo na kuchochea suala hilo la Masauni.Lakini,akihutubia mkutano wa Jumuiya hiyo huko Iringa,JK aliweka bayana kuwa (namnukuu) "Tulipochunguza ilibainika ni kweli alighushi, wakati wa uchaguzi alisema alizaliwa mwaka 1979, lakini ukweli alizaliwa mwaka 1973 na alianza darasa la kwanza mwaka 1979".Je hii haimaanishi kuwa hata vipeperushi vilivyosambazwa kumhusu Masauni vilikuwa na uhusiano na 'uchunguzi' huo anaozungumzia JK?Kama ni hivyo,je si hatari inapotokea kiongozi wa nchi anaporuhusu michezo michafu kama hiyo kwa minajili tu ya kukidhi matakwa flani?

Kinachokasirisha ni kauli yake kuwa  "kijana huyo (Masauni) mpole na mzito kufanya maamuzi magumu na haraka...ni mkakamavu na mchapakazi atapangiwa kazi nyingine hapo baadaye".Yaleyale ya Mwilima.Mtu anaboronga huku kisha anazawadiwa uongozi.Kama ni kweli Masauni alifoji umri wake,hivi hiyo haimpotezei sifa za kuwa kiongozi mahala kwingine?Sasa JK anapotuambia kuwa aatapangiwa kazi kwingine anamaanisha nini?Au huko atakapopangiwa hakuhitaji uadilifu?Na kama 'kudanganya umri' si big deal kwanini basi wameshinikiza aondolewe UVCCM?Nauliza hiyo kwa vile,kwa mujibu wa 'Chaguo la Mungu',kufoji umri kulikopelekea Masauni kujiuzulu sio big deal ndio maana 'atapewa kazi nyingine baadaye'.

Habari nyingine zinazoweza kuashiria kuwa 'jini lililo ndani/kwenye chupa linaweza kutoka muda wowote ule' ni katika jarida la Raia Mwema kwamba Mawaziri Wakuu wastaafu wanafuatiliwa.Ukisoma habari hiyo utabaini kuwa kwa vyovyovte vile,Mkuu wa Nchi anafahamu kuhusu suala hilo.Lakini sidhani kama tunapaswa kushangaa sana kwa vile kama Masauni alichunguzwa (which is equivalent to kufuatiliwa kwa ex-PMs hao) na hatimaye vipeperushi vikasambazwa,basi katika utawala huu lolote linawezekana,hususan uzandiki na character assassination.

Na hili suala la promotion ya familia kwenye uongozi,japo si kosa,linaweza kutafsiriwa kwa namna ya maandalizi ya udikteta.Baba/mume rais,mama/mke naye mwanasiasa 'kiaina',kaka wa rais naye mwanasiasa,mtoto naye mwanasiasa,na hadi kitinda mimba naye kaingizwa kwenye siasa.Na hapa sizungumzii siasa kwa maana ya hamasa tu bali siasa za mizengwe na kugombea kwa kutumia jina.Hapa tunazalisha mfalme au dikteta?

Kwa Watanzania wengi ni business as usual.Lakini kwa wanaoangalia ishu na kukumbuka kuweka alama za kuuliza,yayumkinika kufananisha suala hili na ' jini ndani/kwenye chupa'.LIKITOKA LIMETOKA,hakutokuwa na jinsi ya kulirejesha kwenye chupa.

Kwa atakayechukizwa na uchambuzi huu (kama yule mjinga alontumia comment ya matusi) all I could tell them is SUCK IT UP!


19 May 2010


Picha kwa Hisani ya Michuzi

Nyuso zao zinasuta nafsi zao.Lakini hii ndio hali halisi ya Tanzania yetu.Pamoja na madudu yooote yanayoendelea kufanywa na CCM lakini Watanzania wengi wanaendelea kuwa usingizini na kuamini kuwa hakuna maisha pasipo CCM.Ungetarajia tabaka la chini (ambalo ndio mtaji mkubwa wa chama tawala) liwe na hasira ya hali ya juu dhidi ya chama kilichowasaliti kwa kukumbatia wafanyabiashara mafisadi huku hali za walalahoi zikizidi kuwa ngumu.Lakini,sijui ni kurogwa au vipi,tabaka hili la chini linaendeleza ndoa yake na CCM kama picha inavyoonyesha hapo juu na hapa chini (wanapozugwa na Kingunge).

Na ni hawahawa utakawasikia wakilalamika baada ya uchaguzi kuwa ahh viongozi wametusahau,na malalamiko mengine kama hayo.CCM ikiwapuuza inaweza kuwa na sababu za msingi kwani haikuwalazimisha waipende,na 'imejitahidi kuwapa sababu kadhaa za kuichukia' lakini wananchi hawa wameendelea kuwa ving'ang'anizi.Yani ni kama mwanamke anayeteswa na mume lakini anaendelea tu kumg'ang'ania licha ya kufahamu kuwa mapenzi ya mume huyo yamehamia nyumba ndogo.Na mfano huu unaweza kulinganisha na ndoa ya CCM na wakulima na wafanyakazi,ambapo kwa mazingira ya sasa ya 'ndoa' hiyo CCM imehamishia mapenzi kwenye nyumba ndogo ambayo ni wafanyabiashara na mafisadi.

Kaaazi kweli kweli

18 May 2010



Watawala wetu waache magari yao ya kifahari wachekwe?Nchi tajiri lakini viongozi wanaishi kawaida,lakini sie masikini na ombaomba wa kutembeza bakuli viongozi wetu wanaishi kifahari kama wafanyabiashara matajiri.

Ofkoz,Mtukufu Rais Jakaya Kikwete alikuwa anatania alipotetea rushwa hadharani kwa kudai takrima haikwepeki.Ndio,Rais alikuwa anatania,na ndo maana,Msajili wa Vyama vya Siasa John Tendwa amekaririwa na magazeti kadhaa akimtetea JK kuwa "kauli yake (JK) kuhusu takrima (rushwa) ilikuwa utani tu".Pengine neno 'utani' kwa mujibu Tendwa linaweza kuwa na maana kubwa zaidi tukilitafsiri katika informal English.Kwenye kamusi,'joke' (informal) inamaanisha An object of amusement or laughter; a laughingstock.Kwa Kiswahili,ni 'kituko', 'kioja' au 'kitu cha kuchekwa'.

Lakini kwa namna siasa zetu zilizvyojaa vituko (jokes) si ajabu Tendwa alikuwa serious kumtetea bosi wake JK.Na inawezekana kabisa Msajili huyo wa Vyma vya Siasa anayepaswa kufanya kazi bila upendeleo anaamini kwa dhati kuwa rais wetu alikuwa anataniana tu na viongozi wa dini.Kama ni hivyo,basi nae ni kituko pia.Haiingii akilini kwa kiongozi wa nchi kukutana na watu muhimu katika jamii yetu (viongozi wa dini) na kufanya 'utani mbaya' kama huo.Kulikuwa na umuhimu gani basi wa rais kuhudhuria mkutano huo kama lengo lilikuwa kutoa utani tu?Si angeweza kuwapigia simu kwa wakati wake kisha akawarushia utani huo!

Kwa bahati mbaya,au makusudi,'utani huo mbaya' ushaanza kusahaulika miongoni mwa Watanzania wengi.Siwezi kuwalaumu walalahoi ambao wako bize na kuhakikisha mkono unaenda kinywani,lakini nashindwa kujizuia kuwashangaa Watanzania wenzetu walio katika 'tabaka la kati' (middle class) kwa kuweka umuhimu zaidi kwenye ishu kama tuzo za Kili,ujio wa Sean Kingston,'kujirusha',nk ilhali tabaka la chini linalohitaji sapoti yao likizidi kuangamia.Wengi wa walio katika tabaka la kati wako bize zaidi 'kuishi kama tabaka tawala' (hata kama hiyo itamaanisha wakope kwa ndugu na marafiki au wajihusishe na ufisadi) kuliko kupambana na 'tabaka tawala' (tabaka la juu) 'kusawazisha uwanja' (to level the ground) kwa minajili ya kujenga jamii yenye kukaribia usawa.


Sijui tunaelekea wapi,lakini lililo bayana ni kwamba hatma ya taifa letu iko mashakani.Ukiona mkuu wa nchi anaongea pasi hofu (na kicheko juu,kama kawaida yake) kuwa takrima (ambayo ni jina la kistaarab la rushwa) haikwepeki.Tafsiri pana ya kauli hiyo ya 'Chaguo la Mungu' ni mithili ya kuhalalisha uhalifu kwa vile rushwa ni kosa la jinai.Lakini binafsi sishangazwi sana na kauli hiyo ya 'mwenye nchi' kwa vile alishawahi kutamka bayana kuwa 'anajali haki za binadamu za mafisadi' alipohutubia Bunge Agosti mwaka 2008



Kusoma habari kamili kuhusu utetezi wa Tendwa kwa Kikwete BONYEZA HAPA na HAPA.

17 May 2010



Haikuweza kufahamika mara moja kuhusu hali za majeruhi.

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.