21 Jul 2010

Kuna habari kuwa huenda Katibu Mkuu wa Chadema,Dkt Wilbrod Slaa,atakuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.Kwa mujibu wa gazeti la Daily News,Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana jana jijini Dar imemuomba Dkt Slaa kugombea nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa habari hizo,Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,Zitto Kabwe,alinukuliwa akisema "Kamati Kuu (ya Chadema) imemuomba Dkt Slaa kuwa mgombea wa chama (katika nafasi ya urais)".Hata hivyo,Zitto alieleza kuwa uamuzi wa Kamati hiyo Kuu sio wa mwisho kwani itabidi mgombea urais wa chama hicho athibitishwe na Mkutano Mkuu wa chama hicho ambao umepangwa kufanyika Agosti 10.Kadhalika,Zitto hakuweza kueleza kama Dkt Slaa,ambaye gazeti hilo halikufanikiwa kumpata kuthibitisha habari hizo, amekubali ombi hilo au la.

Hata hivyo,vyanzo vya gazeti hilo katika kikao hicho (kilichokuwa kinaendelea wakati gazeti hilo linaenda mtamboni) vinaeleza kuwa Dkt Slaa,ambaye licha ya Ukatibu Mkuu wa Chadema ni Mbunge wa Karatu kwa tiketi ya chama hicho, amekubali ombi hilo.Habari hiyo ya Dkt Slaa kukubali ombi la kugombea urais kwa tiketi ya Chadema imeandikwa pia kwenye mtandao maarufu kwa habari na mijadala makini,Jamii Forums.

Dokta Slaa amejikusanyia umaarufu mkubwa miongoni mwa Watanzania kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi.Japo ni mapema kubashiri nafasi yake katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu,ni dhahiri kuwa iwapo atasimama kama mgombea wa Chadema anaweza kutoa upinzani mkubwa kwa mgombea wa CCM,Rais (wa sasa) Jakaya Kikwete hususan katika namna chama hicho tawala kilinavyoonekana kama kichaka na hifadhi ya ufisadi na mafisadi.


20 Jul 2010

SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete kueleza umma wa Watanzania kwamba ongezeko la magari na kero ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam ni dalili ya maisha bora, wanazuoni na wanasiasa nchini wameikosoa kauli hiyo na kuilaani vikali.

Wamesema kauli hiyo ni dalili tosha kwamba CCM imekosa mwelekeo halisi ya maendeleo ya nchi hivyo haistahili kuendelea kutawala kwa kuwa haina dira ya kubali maisha ya Watanzania.

Mhadhiri katika kitivo cha Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bw. Bashiru Ally aliliambia Majira kuwa ni aibu kwa kauli hiyo kutolewa na kiongozi wa nchi aliyebeba dhamana ya taifa zima.

Alisema ongezeko la fedha, majumba ya kifahari kwa watu wachache na foleni za magari jijini Dar es Salaam hakuwezi kuchukuliwa kama kipimo cha maisha bora kwa kuwa hivyo si vigezo vinavyopaswa kutumiwa kupima kiwango cha maendeleo katika nchi yoyote duniani.

Alisema maisha bora na maendeleo yoyote katika nchi yanapaswa kupimwa kwa kuzingatia ongezeko la watu, upatikanaji wa ardhi, siasa safi na uongozi bora mambo ambayo bado ni ya taabu na yanayozua migogoro mikubwa nchini.

"Kauli hii inanikumbusha kauli ya hayati Korimba (Horance), kuwa CCM haina dira wala mwelekeo, huwezi kupima maisha bora ya mwananchi wa Masasi au Kagera kwa kuangalia foleni za magari Dar es Salaam, laiti kama Mwalimu (Nyerere) na Sokoine (Moringe) wangekwepo leo kauli hii ingewapandisha presha," alisema Bw. Bashiru.

Alisema ni vema Rais Kikwete akaangalia uwiano wa ngezeko la foleni hizo na uboreshaji wa miundombinu hususan barabara, shule na mfumko wa bei za bidhaa na thamani ya fedha ambavyo vimekuwa vikiporomoka kwa kasi katika kipindi cha uongozi wake.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw. Freeman Mbowe, alisema kauli hiyo inaonesha jinsi serikali ya CCM isivyokuwa na jambo la kujivunia kwa wananchi katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita.

Alisema kimsingi msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam inasababishwa na ukosefu wa miundombinu ambayo chimbuko lake ni uongozi mbovu ulioko madarakani.

Alisema kinachotokea Dar es Salaam si kuboreka kwa maisha ya wananchi bali ni ongezeko la tabaka kati ya walionacho na wasio nacho hasa masikini walioko vijijini hali ambayo inasababisha ongezeko la watu mijini wasiokuwa na ajira wala mahali pa kulala.

"Foleni za magari Dar es Salaam si dalili ya maisha bora, na kama ukifanya utafiti utagundua kuwa foleni kubwa ni katika baadhi ya barabara zinazoelekea kwa matajiri wachache ambao baba, mama na watoto kila mmoja ana gari lake, sasa maendeleo ya watu wachache huwezi kuyatumia kupima kiwango cha maisha ya Watanzania wengine," alisema Bw. Mbowe.

Naye Mhadhiri Mwandamizi katika Kitivo cha uchumi na Biashara Chuo Kikuu cha Dar Salaam, Profesa Humphrey Moshi, alisema si sahihi kwa rais wa nchi kupima maisha ya Watanzania wachache wengi kwa kutumia mfano wa watu wachache wenye uwezo wa magari.

Alisema licha ya ukweli kuwa ongezeko la idadi ya watu wanaomiliki magari linaweza kutumika kuonesha ongezeko la kipato kwa wananchi lakini haikuwa sahihi kwa kiongozi wa nchi kupima maisha ya Watanzania kwa kuangalia wenye uwezo wachache walioko Dar es Salaam.

Alisema Dar es Salaam ni mji wa kibiashara wenye viwanda, mashirika na taasisi karibuni zote za serikali ambazo katika shughuli za kawaida zinahitaji usafiri wa magari, hivyo kuna uwezekano kuwa foleni kubwa husababishwa na magari ya taasisi, hizo lakini si mabadiliko ya maisha ya Watanzania.

"Magari mengi si ya watu binafsi, idara nyingi za serikali ziko hapa, kuanzia ikulu, bunge, wizara zote, taasisi binafsi, mashirika ya dini, viwanda na wafanyabiashara mbalimbali ambao ndio wamiliki wa magari, sio wananchi wa kawaida, sasa huwezi kusema kuwepo kwa foleni za magari ya idara hizi ni maisha bora kwa wananchi," alisema Prof. Humpherey.

Alisema maendeleo yanapimwa kwa kuangalia maisha ya jumla si ya mwananchi mmoja mmoja, ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezo wa kuzalisha mali wa wananchi, thamani ya fedha, kiwango cha elimu na uimara wa sekta za viwanda na kilimo, na si kuangalia msongamano wa magari yaliyokosa barabara za kupita.

Akihutubia wana CCM na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam katika mkutano wa kuwatambulisha wagombea urais, mgombea mwenza na Rais wa Tanzania Visiwani katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Rais Kikwete alisema ongezeko kubwa la magari na kusababisha msongamano wa magari ni mijawapo ya dalili za maisha bora.

CHANZO: Majira

19 Jul 2010

Foleni za magari ni maisha bora-JK
Monday, 19 July 2010 05:33
*Asema watakakamatwa kwa rushwa CCM haitawatetea

Na Peter Mwenda

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Kikwete ametamba kuwa chama hicho kwa miaka mitano iliyopita kimeinua maisha ya Watanzania akitoa mfano wa Jiji la Dar es Salaam kuwa foleni za magari zinatokana na wananchi kuwa na maisha bora.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na CCM Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kumpongeza Rais Kikwete kuchaguliwa kuwa mgombea pekee wa urais kwa asilimia 99.16, Dkt. Ali Mohammed Shein kuchaguliwa kuwa mgombea wa Urais Zanzibar na Dkt. Mohamed Gharib Bilal kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais.

"Hapa Dar es Salaam taabu ya msongamano wa magari inaonesha hali ya maisha ni bora, sasa tunahangaika jinsi ya kuondoa msongamano, kuanzia mwakani tutaanza kujenga barabara za juu," alisema Rais Kikwete.

CHANZO: Majira

Hivi kumbe maendeleo yanapimwa kwa msongamano na foleni za magari!Vipi kama foleni hizo ni matokeo ya mindombinu isiyoendana na mahitaji?Vipi kama wingi wa magari hayo ni matokeo ya ufisadi-aidha ya wizi na ubadhirifu wa mali ya umma na ukiukwaji wa taratibu mbalimbali eg ukwepaji kodi stahili bandarini na TRA?

Na je,foleni hizo za magari zinaendana vipi na idadi ya Watanzania wanaumudu mlo wao kila siku?Je wingi wa magari unaendana na idadi ya wamiliki wa magari?Nauliza hivyo kwa sababu wengi tunafahamu kuwa wakati kuna wachache wenye msururuwa magari na majumba ya kifahari kuna wengine wengi tu ambao hata fedha ya kununulia baiskeli hawana,achilia mbali uhakika wa nauli ya daladala.

Na je inawezekana Rais hajafahamishwa na wasaidizi wake kuhusu ongezeko la 'TZ ELEVEN' i.e. watembea kwa miguu ambao hawafanyi hivyo kama sehemu ya mazoezi ya viungo mbali ukosefu wa nauli?Au hawajamwambia kuhusu idadi ya 'mikweche' ambayo licha ya kusababisha foleni inachangia uwezekano wa ajali?Na inawezekana pia wasaidizi wake hawajamfahamisha kuwa mingi ya 'mikweche' hiyo iko barabarani baada ya wamiliki kutoa 'kitu kidogo' kwa askari wa usalama barabarani?

KAMWE MAJIBU RAHISI KWENYE MASWALI MAGUMU HAYAWEZI KULETA UFUMBUZI WA MATATIZO YETU!SINTOSHANGAA TUKISKIA HATA KUONGEZEKA KWA WENYE VITAMBI (INCLUDING WALE WENYE VITAMBI VYA KWASHAKOO) NAKO NI DALILI YA MAISHA BORA!

18 Jul 2010

Jumatatu iliyopita,gazeti la Mwananchi lilikuwa na habari yenye kichwa 'DAWA YA UKIMWI YAGUNDULIWA'.Siku mbili baadaye,gazeti hilohilo lilikuwa na habari yenye kichwa 'MWAKYUSA: TUMSHUKURU MUNGU KWA DAWA YA UKIMWI'.Binafsi,niliposoma habari ya kwanza nilipatwa na mshangao kuwa inakuwaje habari nzito kama hiyo isipate uzito mkubwa kwenye vyombo vya habari vya kimataifa.Kama kawaida yangu,unapojitokeza utata kuhusu habari,nika-google 'HIV cure'.Tofauti na ilivyoripotiwa na gazeti hilo la Mwananchi,matokeo ya search yangu hayakukuwa na jibu la uhakika.

Nilishtushwa zaidi na kauli ya Waziri wa Afya,profesa wa utabibu,Davidi Mwakyusa,alivyoingia kwenye mkumbo wa 'kushangilia kupatikana kwa dawa ya ukimwi' pasipo kufanya utafiti wa kutosha.Na mahala rahisi pa kufanya utafiti wa aina hiyo ni mtandaoni.

Na pengine katika hali inayoweza kutafsiriwa kama 'kumpa darasa Profesa Mwakyusa',msomi mwezie Profesa Fred Mhalu wa Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Muhimbili,ametoa tahadhari kuhusu habari hiyo ya ugunduzi wa dawa ya ukimwi.Msomi huyo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Microbiology na Immunology,na ambaye amekuwa akijihusisha na tafiti kuhusu ugonjwa huo,amebainisha kuwa kilichogundulika ni protein antibody tu,na inabidi kusubiri mpaka chanjo itakayoweza "kutekenya" (stimulate) antibody hiyo itapopatikana,na kwa sasa haiwezekani kusema hatua hiyo itachukua muda gani.

Profesa Mhalu ametahadharisha pia kuwa huko nyuma kulishawahi kuwa na ripoti kama hizo lakini hazijaweza kuzaa matokeo yanayotarajiwa.Hata hivyo,alisema kuwa hatua iliyofikiwa ni ya kutia matumaini kwenye mwelekeo wa kupata tiba kamili japokuwa hawezi kutamka kwa hakika kuwa ufumbuzi wa tatizo hilo umeshapatikana.

Awali,Profesa Mwakyusa alinukuliwa akisema "Kama ni kweli dawa hiyo imepatikana, ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kuwa Ukimwi ni ugonjwa ambao umeiathiri sana dunia."Ama kwa hakika usingetarajia kauli ya 'kimtaani' (layman's language) kutoka kwa mtu mbaye licha ya kuwa Waziri mwenye dhamana katika suala la Afya lakini pia ni msomi katika fani ya utabibu.Japo ni vizuri kumshukuru Mungu kwa taarifa za kutia matumaini kama hiyo,lakini watu wenye dhamana na hususan wasomi kwenye taaluma ya utabibu wanatarajiwa kutoa kauli zinazoelemea zaidi kwenye facts badala ya hisia za binafsi.Pengine kabla ya kutoa kauli hiyo iliyoongeza uzito katika habari husika,Waziri Mwakyusa angeweza kufanya 'quick search' kwenye simu (kama sio kompyuta) yake na kupata facts sahihi kisha kuwaeleza Watanzania ukweli kuhusu habari hiyo.

Kwa mujibu wa kiongozi wa utafiti uliopelekea habari hiyo,Dakta Garry Nabel wa Taasisi ya Taifa ya Allergy na Magonjwa ya Kuambukiza ya Marekani,protini zilizogunduliwa,yaani antibodies hizo,zinatumiwa na mfumo wa kinga ya mwili kutambua na kushambilia vimelea vya maradhi kama bakteria na virusi."Nina kuhusu chanjo ya ukimwi kwa sasa kuliko ilivyokuwa miaka 10 iliyopita",alisema mtafiti huyo katika kauli iliyopelekea msisimko wa aina yake sehemu mbalimbali duniani.

Virusi vya ukimwi hushambulia mfumo wa mwili kujikinga na maradhi na hivyo kumwacha mwathirika katika hatari ya maambukizi na maradhi.Tangu virusi hivyo vigunduliwe takriban miaka 30 iliyopita,wanasayansi wamekuwa wakihangaika pasipo mafanikio kupata tiba na kinga ili kudhibiti ukimwi.Inakadiriwa kuwa kufikia mwaka juzi kulikuwa na watu milioni 33 walioambukizwa virusi hivyo hatari.

Wakati dunia kwa ujumla ingetamani tiba ya ugonjwa huo hatari ipatikane hata leo,ni muhimu kwa wenye dhamana ya kuuhabarisha umma kuwa makini wanapotoa taarifa za kitaalamu zinazohitaji ufafanuzi makini ili kuepuka kutoa matumaini yasiyoendana na ukweli.Kwa kifupi,hadi sasa hakuna dawa ya ukimwi.Kilichogundulika ni hizo antobodies,na bado kuna hatua mbalimbali za kitabibu na kitaratibu kabla haijathibitishwa rasmi kuwa tiba au dawa ya ugonjwa huo imepatikana.

Lengo la makala hii sio kuvunja matumaini ya walioanza kuamini kuwa 'dawa ya ukimwi imepatikana' bali ni kutoa ufafanuzi ambao naamini utawasaidia walioathirika kuzingatia ushauri wa kitaalam na kwa sote kwa ujumla kujichunga kwa kuepukana na ngono zembe.

16 Jul 2010


Urban Pulse Production inawaletea burudani na matukio yaliojiri ndani ya Michuano ya kumtafuta Miss & MR East Africa UK 2010 yaliyofanyika  3rd July 2010 Mjini London.

Katika kinyang'anyiro hicho binti Randa Shelbly kutoka Eritrea alinyakua kombe la miss east Africa UK wakati mchizani Degnite Abdeta Dauggie ndio alichukua Mr East Africa UK.

Wadau karibuni kushuhudia tukio hili la kipekee kwa kubofya hapo chini.

Libeneke Oye

asanteni na Wote Mbarikiwe

Frank Eyembe
Urban Pulse Creative



14 Jul 2010

Nimekumbana na swali hili tangu udogoni:Alianza kuku,au lilianza yai?Kama alianza kuku,alitoka wapi ilhali sote twajua kuku anatoka kwenye yai?Na kama lilianza yai,lilitoka wapi wakati tunafahamu kuwa yai hutagwa na kuku?Baada ya kukosa jibu lenye mantiki niliamua kuachana na swali hali maana kujihangaisha kutafuta jibu ilikuwa kazi bure.Nahisi hata nawe msomaji umeshakumbana na swali hilo mara kadha wa kadha.

Lakini hatimaye kitendawili hicho kimepata ufumbuzi.Kwa mujibu wa gazeti la bure la Metro,watafiti wa Kiingereza wanasema kuwa kuku ndiye aliyeanza kabla ya yai kwa vile yai linaweza kupatikana tu kwa chembechembe za protini zinazopatikana katika mifuko ya uzazi ya kuku.

"Imekuwa ikidhaniwa kwa muda mrefu kuwa yai ndilo lililoanza kabla ya kuku lakini sasa tuna ushahidi wa kisayansi kuwa kwa hakika alianza kuku kabla ya yai",alisema Dakta Colin Freeman kutoka Chuo Kikuu cha Sheffield,aliyeshirikiana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Warwick.

"Protini hiyo ilitambuliwa kabla na ilihusishwa na uzalishaji wa yai lakini kwa kuchunguza kwa undani tumegundua namna gani protini hiyo inavyowezesha hatua hiyo (ya kutengeneza yai).

Protini hiyo-inayofahamika kitaalam kama ovocledidin-17 (OC-17) inafanya kazi kama kichocheo (catalyst) kuharakisha maendeleo ya yai.

Wanasayansi hao walitumia kompyuta yenye uwezo wa hali ya juu (supercomputer) ifahamikayo kama HECToR,ambayo ipo jijini Edinburgh,Scotland, kukuza (zoom) hatua zinazoonyesha jinsi yai linavyozalioshwa.

Ilibainika kuwa OC-17 ni muhimu katika kuanzisha kukomaa (crystallization)-hatua ya awali katika uundwaji wa gamba la yai.Protini hiyo hugeuza calcium carbonate kuwa chembechembe za calcium (calcite crystals) ambazo ndizo zinazounda gamba la yai,huku zikitengeneza gramu 6 za gamba katika kila masaa 24.

Profesa John Harding,pia kutoka Chuo Kikuu cha Sheffield,alisema kuwa ugunduzi huo unaweza kuwa na matumizi mengine pia."Kufahamu namna gani kuku wanatengeneza mayai ni jambo la kupendeza lakini pia linaweza pia kutupatia vidokezo katika namna ya kutengeneza vitu vipya".

Imetafsiriwa kutoka gazeti la Metro toleo la leo.

13 Jul 2010


A politician had an accident and dies.

His soul reaches the Paradise and found St. Peter at the entrance.

-- "Welcome to Paradise! Before you could get in, there is a little problem... We rarely seen politicians here, you know… So we do not know what to do with you..."

-- "I see, no problem just let me enter." says the politician.

-- "I though I would like to let you in but I have higher orders as it´s known… We will do the following: You pass one day in Hell and one day in Heaven. You can then choose where to spend eternity."

-- "It is not necessary, I have already decided. I want to stay in Heaven." says the politician.

-- "Sorry, but we have our rules."

So, St. Peter takes him to the elevator and he comes down, down to Hell. The door opens up and he sees himself in the middle of a beautiful golf course.

In essence, the club where were all his friends and other politicians with whom he had worked. All very happy.

He was greeted, embraced and then they started to talk about the good times when they got rich at the expense of the people.

They played golf, relaxed and then ate lobster and caviar.

Who was also present was the devil, a very friendly guy who spent all the time dancing and telling jokes. They enjoyed themselves so much that before they realize it was time to go.

After a lot of redundant hugs and words of farewell he enter into the elevator.

He rises, rises and the door opens up again. St. Peter was expecting him.

-- Now it´s the time to visit the Paradise.

He spends 24 hours in paradise among a group of happy souls who go from cloud to cloud playing harps and singing. All went very well and before he noticed the day comes to an end and St. Peter returns.

-- "Now what? You spent one day in Hell and one day in Heaven. Now choose your eternal home."

He thought for a minute and answered:

-- "Look, I never thought to make this decision… The Paradise is very good but I think I'll be much better in Hell."

Then St. Peter takes him back to the elevator and he comes down, down to hell.

The door opens up and he saw himself in the midst of a massive ground full of garbage and a horrible smell. He saw all his friends with the clothes torn and very dirty searching the rubble and putting it in black bags. He also saw some of his friends in dispute to take pieces of rotten food.

The devil put the arm by the politician´s shoulder.

-- "I do not understand?" Mumble the politician. -- "Yesterday I was here and it even had a beautiful golf course, a club, lobster, caviar and we danced and had fun all the time. Now I see that it´s only full of very smelly garbage and my friends are totally tear down!"

The devil looks at him… Ironically smiles and says:

-- "Yesterday we were in campaign season before election. Now we have your vote... I´m sorry, this is the reality!"

SOURCE Hubpages

Kuna tofauti moja ya msingi katika Twitter na Facebook (social media nazizipendelea zaidi),nayo ni namna watu wawili wanavyounganishwa na huduma hizo.Wakati nikiomba kuunganishwa na mtumiaji wa Facebook,na kukubaliwa inamaanisha nitaweza kuona profile yake na updates mbalimbali,kwenye Twitter habari ni tofauti.Nikiamua "kumfuata" (following) mtu,haimaanishi kuwa mtu huyo automatically naye "atanifuata".

Lakini katika mazingira ya kawaida,na pengine kistaarabu,kama mtu ameamua "kukufuata" huko Twitter,unapungukiwa nini ukirejesha "fadhila" kwa kumfuata mtu huyo?Au ndio usupastaa kwamba wanaokufuata ni wengi kuliko unaowafuata?Ofkoz,inaweza kuwa vigumu "kumfuata" kila "anayekufuata" ukiwa na "wafuasi" maelfu kadhaa lakini si vigumu kama wafuasi wako ni mia na kitu tu.

Naandika haya nikitambua kuwa uamuzi wa mtu kukufuata ni suala la mtu binafsi.Na kwa vile mtu ahajalazimishwa kumfuata mtu mwingine inaweza kupelekea hoja yangu kuonekana haina umuhimu.Nachojaribu kupigia mstari hapa ni ustaarab wetu wa Kiafrika.Katika mazingira ya kawaida,kama jana nilikutana nawe nikakusalimu,leo pia tumekutana nikakusalimu na kesho inakuwa hivyohivyo,basi kistaarabu inatarajiwa kuwa kesho kutwa nawe utaanzisha salamu.Kinyume cha hivyo,tafsiri itakuwa aidha unaringa au huhitaji salamu yangu.Ni katika mantiki hiyohiyo,kama mtu ameamua kukufuata (hata kama wewe ni maarufu mara elfu kuliko huyo mfuasi) basi ni tarajio la mfuasi huyo kuwa nawe utamfuata.Si lazima lakini ni katika masuala ya ustaarab tu.

Kama unaafikiana nami,basi pengine fanya jambo la kupendezesha roho za wale wanaokufuata lakini wewe hujaamua kuwafuata:WAFUATE PIA.Haigharimu chochote,haikupunguzii umaarufu ulionao,na zaidi,itakufanya uonekane huna dharau.

Ni ushauri wa bure tu.

10 Jul 2010

Kwa mara ya tatu ndani ya wiki moja askari wa jeshi la polisi amejiua kwa kujipiga risasi.Haya si matukio ya kuyachukulia kimzaha kwani licha ya ukweli kuwa vifo vya askari hao ni pigo na doa kwa jeshi hilo lakini pia inawezekana kesho na keshokutwa,Mungu aepushie mbali,tunaweza kusikia askari amemwagia risasi raia kadhaa wasio na hatia kabla ya kutoa uhai wake mwenyewe.Kuna tatizo ndani ya jeshi hilo lakini kama ilivyo ada kwenye maeneo mengine wahusika wanaendelea kujifanya mbuni kwa kuficha vichwa kwenye shimo huku mwili ukibaki nje.

Nilibahatika kufanya kazi na polisi kwa muda mrefu tu na kwa hakika utawahurumia ukisikia na kuona matatizo wanayokabiliana nayo kimaisha na kiutendaji kazi.Kubwa zaidi ni hali ya maisha yao hususan kwenye suala la makazi.Nenda Kilwa Road,Oysterbay au Temeke na shuhudia mazingira wanayoishi wanadola hao,na utakubaliana nami kuwa si vigumu kwao kukumbwa na shinikizo la kisaikolojia.Hebu tafakari kuhusu askari anayekesha lindoni Masaki,Mikocheni,Upanga,Oysterbay,nk kwa vigogo na kushuhudia watu wanavyokula keki ya taifa wakati mwanadola huyo anaishi maisha ya chini kabisa licha ya mchango wake mkubwa katika usalama wa nchi.Ni dhahiri anaweza kupatwa na mawazo kuwa maisha na kazi aliyonayo havina thamani.

Lakini pia kuna unyanyasaji unaotawala kwenye vyombo vyetu vya dola ambapo viongozi ni miungu watu huku wakipata maslahi manono kupindukia ukilinganisha na wale wanaowaongoza.Na hiyo sio huko polisi tu bali hata katika ofisi nyinginezo-za dola na zisizo za dola-ambapo viongozi hujijengea ukuta mrefu wa kuwatenganisha na wanaowaongoza.Vikao kati ya viongozi na watumishi wa ngazi za chini hutawaliwa na vitisho vinavyokwaza kero na malalamiko ya askari wa ngazi za chini kusikika.

Pasipo kutafuta ufumbuzi wa haraka katika wimbi hili la polisi kujiua kwa risasi basi tuwe tayari kushuhudia balaa.Silaha haziui watu,bali watu hutumia silaha kujiua au kuua wengine.Sasa kama askari wetu tunaowakabidhi silaha wanaweza kujiua kama njia ya ufumbuzi wa matatizo yao binafsi,yayumkinika kubashiri kuwa siku moja wanaweza kabisa kuua watu wengine kabla ya kujiua wao wenyewe.

Tusipoziba ufa tutajenga ukuta.Hebu soma habari kamili katika kiungo kifuatacho

Hebu soma habari kamili kwa kubonyeza KIUNGO HIKI.

9 Jul 2010

UJUMBE KUTOKA URBAN PULSE: Karibuni tena wadau wote wa kuangalia sehemu ya pili ya mada ya Uraia Pacha kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Bernard Membe wakati akitoa hotuba kwenye Diaspora hapa Mjini Ukerewe tarehe 26.3.2010

Pia Mh Membe alisoma ujumbe kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Jakaya Kikwete akiwasifu na Kuwapongeza Watanzania katika Diaspora. Tafadhali Bonyeza chini kuangalia Video

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.