SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete kueleza umma wa Watanzania kwamba ongezeko la magari na kero ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam ni dalili ya maisha bora, wanazuoni na wanasiasa nchini wameikosoa kauli hiyo na kuilaani vikali.
Wamesema kauli hiyo ni dalili tosha kwamba CCM imekosa mwelekeo halisi ya maendeleo ya nchi hivyo haistahili kuendelea kutawala kwa kuwa haina dira ya kubali maisha ya Watanzania.
Mhadhiri katika kitivo cha Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bw. Bashiru Ally aliliambia Majira kuwa ni aibu kwa kauli hiyo kutolewa na kiongozi wa nchi aliyebeba dhamana ya taifa zima.
Alisema ongezeko la fedha, majumba ya kifahari kwa watu wachache na foleni za magari jijini Dar es Salaam hakuwezi kuchukuliwa kama kipimo cha maisha bora kwa kuwa hivyo si vigezo vinavyopaswa kutumiwa kupima kiwango cha maendeleo katika nchi yoyote duniani.
Alisema maisha bora na maendeleo yoyote katika nchi yanapaswa kupimwa kwa kuzingatia ongezeko la watu, upatikanaji wa ardhi, siasa safi na uongozi bora mambo ambayo bado ni ya taabu na yanayozua migogoro mikubwa nchini.
"Kauli hii inanikumbusha kauli ya hayati Korimba (Horance), kuwa CCM haina dira wala mwelekeo, huwezi kupima maisha bora ya mwananchi wa Masasi au Kagera kwa kuangalia foleni za magari Dar es Salaam, laiti kama Mwalimu (Nyerere) na Sokoine (Moringe) wangekwepo leo kauli hii ingewapandisha presha," alisema Bw. Bashiru.
Alisema ni vema Rais Kikwete akaangalia uwiano wa ngezeko la foleni hizo na uboreshaji wa miundombinu hususan barabara, shule na mfumko wa bei za bidhaa na thamani ya fedha ambavyo vimekuwa vikiporomoka kwa kasi katika kipindi cha uongozi wake.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw. Freeman Mbowe, alisema kauli hiyo inaonesha jinsi serikali ya CCM isivyokuwa na jambo la kujivunia kwa wananchi katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita.
Alisema kimsingi msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam inasababishwa na ukosefu wa miundombinu ambayo chimbuko lake ni uongozi mbovu ulioko madarakani.
Alisema kinachotokea Dar es Salaam si kuboreka kwa maisha ya wananchi bali ni ongezeko la tabaka kati ya walionacho na wasio nacho hasa masikini walioko vijijini hali ambayo inasababisha ongezeko la watu mijini wasiokuwa na ajira wala mahali pa kulala.
"Foleni za magari Dar es Salaam si dalili ya maisha bora, na kama ukifanya utafiti utagundua kuwa foleni kubwa ni katika baadhi ya barabara zinazoelekea kwa matajiri wachache ambao baba, mama na watoto kila mmoja ana gari lake, sasa maendeleo ya watu wachache huwezi kuyatumia kupima kiwango cha maisha ya Watanzania wengine," alisema Bw. Mbowe.
Naye Mhadhiri Mwandamizi katika Kitivo cha uchumi na Biashara Chuo Kikuu cha Dar Salaam, Profesa Humphrey Moshi, alisema si sahihi kwa rais wa nchi kupima maisha ya Watanzania wachache wengi kwa kutumia mfano wa watu wachache wenye uwezo wa magari.
Alisema licha ya ukweli kuwa ongezeko la idadi ya watu wanaomiliki magari linaweza kutumika kuonesha ongezeko la kipato kwa wananchi lakini haikuwa sahihi kwa kiongozi wa nchi kupima maisha ya Watanzania kwa kuangalia wenye uwezo wachache walioko Dar es Salaam.
Alisema Dar es Salaam ni mji wa kibiashara wenye viwanda, mashirika na taasisi karibuni zote za serikali ambazo katika shughuli za kawaida zinahitaji usafiri wa magari, hivyo kuna uwezekano kuwa foleni kubwa husababishwa na magari ya taasisi, hizo lakini si mabadiliko ya maisha ya Watanzania.
"Magari mengi si ya watu binafsi, idara nyingi za serikali ziko hapa, kuanzia ikulu, bunge, wizara zote, taasisi binafsi, mashirika ya dini, viwanda na wafanyabiashara mbalimbali ambao ndio wamiliki wa magari, sio wananchi wa kawaida, sasa huwezi kusema kuwepo kwa foleni za magari ya idara hizi ni maisha bora kwa wananchi," alisema Prof. Humpherey.
Alisema maendeleo yanapimwa kwa kuangalia maisha ya jumla si ya mwananchi mmoja mmoja, ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezo wa kuzalisha mali wa wananchi, thamani ya fedha, kiwango cha elimu na uimara wa sekta za viwanda na kilimo, na si kuangalia msongamano wa magari yaliyokosa barabara za kupita.
Akihutubia wana CCM na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam katika mkutano wa kuwatambulisha wagombea urais, mgombea mwenza na Rais wa Tanzania Visiwani katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Rais Kikwete alisema ongezeko kubwa la magari na kusababisha msongamano wa magari ni mijawapo ya dalili za maisha bora.