24 Feb 2011


Katika harakati zake duni za kujinasua uhusika wake katika suala la ujambazi wa Dowans,Rais Jakaya Kikwete alijaribu kuwahadaa Watanzania kwa kudai,pamoja na mambo mengine,kuwa "hawajui wamiliki wa Dowans".

Na kwa bahati nzuri kwake,vyombo vyetu vya habari vikaishia kumnukuu tu.Lakini kwa minajili ya kufupisha makala hii(na kupunguza maumivu yanayotokanayo) tuweke kando kuangalia namna Kikwete alivyotengeneza mazingira ya ujio wa Dowans kupitia majambazi wengine wa Richmond.Hapa namaanisha kauli yake kuwa tatizo la umeme lingekuwa historia baada ya ujio wa mitambo ya kuzalisha umeme kutoka Marekani (na tukaishia kuletewa mitambo garasa)

Hatimaye mwarabu Adawi aliyekimbia ukombozi wa Mzanzibari,amediriki kuja na kutufanyia kila aina ya vituko (kukataa kupigwa picha,nk) na kutangaza hadharani kuwa yeye ndio mmiliki wa Dowans.Na kama kututukana Watanzania,akadai kuwa anaweza kuangalia uwezekano wa kupunguza FIDIA ANAYOPASWA KULIPWA KWA KUTUIBIA (yale yale ya vibaka wanaomkaba mtu kisha kumpigia ukelele wa "mwizi,mwizi...")

Adawi ambaye Kikwete anadai hamjui (japo anamjua sana kwani wana mahusiano ya "kifamilia")ameweza kutia mguu Ikulu na kuongea na Makamu wa Rais Gharib Bilali (anayekaimu urais katika kipindi hiki ambacho Kikwete yuko kwenye mizunguko yake).

Japo tunajua kuwa Ikulu yetu imegeuzwa kijiwe cha mafisadi ambao wana uhuru wa kutembelea mahala hapo patakatifu kila wanapojisikia lakini kwa Adawi kupewa nafasi ya kukutana na Rais (kwa maana ya anayekaimu nafasi hiyo),na mkutano huo kufanywa siri,inaashiria kuwa Kikwete na serikali yake sio tu anamjua Adawi bali pia anamtumikia.

Sintashangaa kusikia kuwa Kikwete aliamua kwenda Mauritania ili kumwezesha Adawi afanye uhuni wake kisha ahitimishe ziara yake kwa maongezi na kaimu wa Kikwete (Gharib Bilali).Na sintoshangaa kusikia kwamba kabla ya kurejea Tanzania,maswahiba hao wawili (Kikwete na Adawi) wakakutana faragha kujadili kuendeleza ujambazi wa Dowans.

Na hata tukiweka kando ujio wa Adawi,kauli ya Kikwete kuwa hawajui wamiliki wa Dowans ilhali majina ya wamiliki hao yapo BRELA (na Waziri Ngeleja alishayaweka hadharani kabla Kikwete hajatoa utetezi wake feki) inatosha kuwafahamisha Watanzania kuwa Rais wao ameshindwa kazi.How come Waziri ajue kile ambacho Rais hakijui?Je kama anashindwa kujua jambo dogo tu kama rekodi ndogo tu iliyopo BRELA atawezaje kujua na hatimaye kushughulikia matatizo ya Watanzania takriban milioni 50?

Tusipofumbuka macho kama wenzetu wa Tunisia,Misri,Libya na kwingineko wanakopambana na tawala dhalimu tunaweza kuishia kuwa koloni la Adawi,yaani mwarabu huyo kuongoza nchi yetu kwa kutumia remote control in the form of Kikwete.


Maandamano ya kupinga tawala dhalimu,ambayo yamesambaa maeneo kadhaa ya Afrika Kaskazini,yanaanza kuonyesha dalili za kusambaa sehemu nyingine za bara la Afrika hadi Cameroon,Gabon,Zimbabwe na Mauritania.


Nchini Cameroon,kulikuwa na mpango wakufanya maandamano jana kwa lengo la kumwondoa madarakani Rais Paul Biya,kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha CNN cha Marekani.Biya amekuwa madarakani kwa miaka 28.Kiongozi wa upinzani,Kah Walla,aliieleza CNN kwamba kundi lake linataka kuona chaguzi huru na za haki.

Mwandishi wa gazeti la New York Times la Marekani,Nick Kristof, aliandika kwenye Twitter kwamba:

Mapambano ya kudai demokrasia yanasambaa maeneo mapya barani Afrika: Cameroon,Gabon,Zimbabwe,Mauritania.
Naye Msemaji wa Serikali ya Marekani P.J Crowley alitwiti

Wanaharakati wakutana Zimbabwe kujadili yaliyojiri Misri na Tunisia na wameishia kukamatwa.Mugabe hajaelewa somo
Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari inaripoti kwamba Eritrea,Guinea ya Ikweta na Zimbabwe wamedhibiti kabisa maendeleo ya mapambano ya kung’oa tawala dhalimu huko Mashariki ya Kati na Afrika Magharibi.

Habari zaidi kutoka CNN zinaeleza kuwa wanaharakati na viongozi kadhaa wa vya vyama vya wafanyakazi nchini Zimbabwe walizingirwa na polisi wiki iliyopita na sasa wanakabiliwa na hukumu ya kifo baada ya waendesha mashtaka wa serikali ya nchi hiyo kuwasomea mashtaka ya kupanga maandamano ya kuung’oa madarakani utawala wa Rais Robert Mugabe.

Katika kesi hiyo iliyoendeshwa jana,washtakiwa 46 wanakabiliwa na shtaka la uhaini .Walikamatwa Jumapili iliyopita baada ya mamlaka kudai kuwa walikutwa wakiangalia mikanda yenye kuonyesha maandamano yaliyopelekea kung’olewa madarakani aliyekuwa Rais wa Tunisia Zine El Abidine Ben Ali na mwenzie wa Misri Hosni Mubarak.

Mtandao wa habari wa Afrol unaripoti kufanyika kwa maandamano ya nchini nzima huko Cameroon kushinikiza Rais Biya aondoke madarakani ,japokuwa maandamano hayo yalidhibitiwas kirahisi na vyombo vya usalama vya nchi hiyo.

Miji mikubwa ya Younde na Douala ilitawaliwa na askari wa kutuliza ghasia huku magari yakisimamishwa na kupekuliwa na mikusanyiko ya watu ikidhibitiwa.Kadhalika,mashuhuda wameeleza kuwa polisi walinyang’anya kamera na simu za mikononi.
Wachambuzi wa mambo wanadai kuwa licha ya maandamano hayo kutofanikiwa kufikia matarajio ya wengi,bado kuna uwezekano wa yaliyojiri sehemu kama Tunisia na Misri kujitokeza nchini Cameroon hivi karibuni.Kilio cha wananchi wengi wa taifa hilo ni rushwa na hali ngumu ya maisha.Harakati za kudai mabadiliko nchini humo zinachochewa zaidi na Wakameruni wanaoishi nje ya nchi hiyo.

22 Feb 2011


Kuna taarifa kwamba mtu aliyetambulishwa kama mmiliki wa kampuni ya Dowans, Brigedia Jenerali (Mstaafu) Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi ni kiini macho.

Chanzo cha kuaminika kinaeleza kuwa tukio zima la "mmiliki wa Dowans kuzungumza na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari" ni sehemu tu ya mkakati mahsusi na endelevu kuughilibu umma wa Watanzania katika sakata la malipo ya fidia kwa kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo,sababu iliyopelekea "Bilionea huyo wa Dowans" kukataa kupigwa picha mgando wala kurekodiwa na kamera za televisheni ni hofu kuwa "danganya toto" hiyo ingebainika kirahisi pindi Watanzania wangekwenda mbali zaidi kuchimba undani na ukweli.

Lakini hata katika mazingira ya kawaida tu,haiyumkiniki mfanyabiashara anayejitambulisha kuwa amewekeza zaidi ya dola bilioni moja (USD 1,000,000,000,000) nchini India akwepe kupigwa picha kwa madai dhaifu kuwa anaendesha biashara zake kwa "low profile".

Na kama hiyo haitoshi,itakumbukwa kuwa Waziri wa Nishati William Ngeleja aliwahi kutangaza wamiliki wa kampuni ya Dowans (ambao bosi wa Ngeleja,Rasi Jakaya Kikwete,alidai hawajui) ni Brigedia Jenerali Sulaiman Mohamed Yahya Al Adawi ambaye ni raia wa Oman, Guy Arthur Picard raia wa Canada, Stanley Munai raia wa Kenya. Wengine ni Andrew James Tice raia wa Canada, Gopala Krishnan Balachandran kutoka India na Hon Sun Woo kutoka Singapore.Lakini katika mkutano wake na wahariri hao,'Bilionea huyo wa Dowans' alidai kuwa yeye pekee ndio mmiliki wa kampuni hiyo.


Na kama hiyo haitoshi, 'Bilionea huyo wa Dowans' alishawahi "kuruka kimanga" huko nyuma akidai yeye si mmiliki wa kampuni hiyo LAKINI SASA ANADAI SI TU MMILIKI BALI MMILIKI PEKEE.Hizi ni dalili za wazi za ubabaishaji wa "Bilionea" huyu! (And shame on you gazeti la Tanzania Daima kwa habari iliyoonyesha bayana mnalamba miguu ya mtu huyu ambaye laiti ikibainika ni yeye basi mahala panapomfaa ni Segerea kama sio Keko au Ukonga).

Tovuti hii inaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo na inaahidi kuwafahamisha maendeleo (ya uchunguzi huo).Kwa wakati huu,tunatoa wito kwa waandishi wetu wa habari kuacha uzembe wa kuripoti kinachotamkwa tu badala ya kwenda mbali zaidi na kufukua data mbalimbali.Kadhalika,wahariri walioalikwa na Brigedia huyo walipaswa kuwa na msimamo wa kuhoji kwanini hataki picha zake zionekane kwenye vyombo vya habari.

20 Feb 2011








Picha hizi za kutisha zinajieleza zenyewe.Hakuna maelezo yanayotosheleza kueleza kwa ufasaha kuhusu janga hili.Lakini kwa vile kamwe hatutoelezwa chanzo cha milipuko ya mabomu huko Gongo la Mboto,kama ambavyo hatukuelezwa chanzo cha milipuko iliyotokea mwaka juzi huko Mbagala,ni muhimu kwa kila Mtanzania kudai haki yake ya kikatiba ya usalama wa maisha yake.


Ni wazi kuwa wahusika wanapata jeuri ya kutangaza hadharani kuwa hawatajiuzulu kwa vile wanafahamu bayana kuwa aliyewateua kushika madaraka hayo ni mzembe,dhaifu na asiyejua kinachoendelea.Kwa lugha nyingine,YUPO YUPO TU.

Nilighadhibika sana niliposoma kauli ya Mkuu wa Usalama na Utambuzi wa JWTZ Brigedia Jenerali Paul Meela kuwa hakuna atakayejiuzulu kwa sababu uongozi jeshini sio nafasi za kisiasa.Haya ni matusi kwa Watanzania.Kwani Amatus Liyumba alipohukumiwa kwenda jela kwa ubadhirifu wa fedha za umma hapo Benki Kuu alikuwa mwanasiasa?

Kwa akili finyu ya Brigedia Meela,ni wanasiasa pekee wanaopaswa kuwajibika wanapoboronga.Lakini kwa vile kamanda huyo alikuwa anamwakilisha Mkuu wa Mwajeshi Jenerali Davis Mwamunyange,yayumkinika kuamini kuwa kauli hiyo pia ni msimamo wa mkuu huyo wa majeshi.

Tuliowahi kupitia mambo ya kijeshi tunafahamu kasumba ya jeuri na u-mungu mtu ilivyokomaa vichwani mwa viongozi jeshini.Hii inaimarishwa zaidi na utaratibu wa kawaida jeshini kwamba amri ina mwelekeo mmoja tu: kutoka juu kwenda chini,na haihojiwi.

Kwahiyo,wakati Kamanda Meela anaongea na waandishi wa habari,akilini mwake alikuwa kama anaongea na makuruta ambao ni dhambi kuu kwao kuhoji lolote lile.Na kwa vile Meela alikuwa anawakilisha mabosi wake,mtu pekee ambaye angeweza kumwadabisha ni Amiri Jeshi Mkuu,Rais Jakaya Kikwete.

Lakini takriban miezi mitano tangu baadhi ya Watanzania wenzetu watusaliti kwa kumrejesha Kikwete madarakani (tukiweka kando uchakachuaji wa Tume ya Uchaguzi),naamini kila Mtanzania anafahamu fika kuwa ombwe la uongozi wa taifa lililojiokeza wakati wa awamu ya kwanza ya utawala wa Kikwete,sio tu limezidi kukua bali pia limeifanya Tanzania kuishi kwa kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu.Ni kama hatuna Rais wala serikali.

Na taasisi muhimu kwa ustawi wa taifa kama Idara ya Usalama wa Taifa ziko katika usingizi mzito unaosababishwa zaidi na marupurupu makubwa licha ya utendaji kazi duni na wa chini ya kiwango.Sijui kama watu hawa wanasumbuliwa na mwenendo wa nchi yetu,kwani ingekuwa hivyo tusingeshuhudia mazingaombwe ya kuruhusu mtu kama Edward Lowassa kuwa Mwenyekiti wa kamati nyeti ya bunge ya Ulinzi na Usalama,leave alone ishu kama za Dowans,EPA,nk.

Na kwa kuonyesha watu wa Usalama wamegubikwa na usingizi,wameshindwa hata kumshauri bosi wao Kikwete kuwa safari yake kwenda Mauritania kusaka ufumbuzi wa mgogoro huko Ivory Coast,sio mwafaka wakati huu wa majonzi makubwa kwa Watanzania.Kikwete na washauri wake wanajifanya hawajui kuwa janga la Gongo la Mboto linawagusa zaidi Watanzania kuliko matatizo ya wa-Ivory Coast.Ni rahisi kwa baadhi ya watu kuhisi kuwa Kikwete anakwepa majukumu na kuamua kwenda kuzurura huko ng'ambo.

Tukirejea kauli za wanajeshi wetu,Brigedia Jenerali Meela anasema taarifa za milipuko iliyopita ni kwa matumizi ya jeshi.Kwani JWTZ limegeuka jeshi la mtu binafsi?Sote tunafahamu kuwa hilo ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania.Sasa iweje madudu wanayofanya na yanayopelekea kuwaathiri wananchi wasio na hatia yaishie kuchungiuzwa na wao wenyewe kisha findings nazo zibaki kuwa siri yao?

Jibu la maswali haya na mengineyo mengi ni rahisi:Rais tuliyenae ni dhaifu na asiye na uwezo wa kuwawajibisha hata wale aliowateua yeye mwenyewe.Sasa kwa wanaotegemea Kikwete anaweza kudili na maharamia kama wa Dowans (ambao hakuwateua,na sanasana wanamdai fadhila) watakuwa wana jibu la msingi kuhusu kusuasua kwake kuwashughulikia mafisadi.

Picha kwa hisani ya Rev Masanilo wa Jamii Forums


Tunaendelea kuwaletea updates za tukio la milipuko ya mabomu jijini Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali,hadi sasa inakadiriwa zaidi ya watu 20 wamepoteza maisha katika tukio hilo.

Tovuti ya Shirika la Habari la Uingereza (BBC) Idhaa ya Kiswahili inaripoti:
Hali ya taharuki imetanda mji wa Dar Es Salaam, nchini Tanzania, huku wakaazi wakiamka kuomboleza vifo vya zaidi ya watu kumi na zaidi ya wengine 60 kujeruhiwa kufuatia milipuko iliyotokea kwenye ghala la kuhifadhi silaha za kijeshi, lililo karibu na uwanja wa kimataifa wa ndege.

Wakaazi wa eneo la Gongo la Mboto lililo karibu na ghala hilo wamekesha nje baada ya makaazi yao kubomoka kutokana na mtikisiko wa milipuko hiyo iliyodumu kwa saa kadhaa. Milipuko hiyo ilisikika kwa umbali wa zaidi ya kilomita ishirini kutoka kituo hicho cha kijeshi.

Inaarifiwa kuwa milipuko hiyo ilianza mwendo wa saa mbili usiku.

Msemaji mmoja wa jeshi amesema kuwa kuna watu wengi ambao wamepoteza maisha yao lakini idadi kamili haijajulikana.

Kamanda wa polisi jijini Dar-es-Salaam, Suleiman Kova, ametoa wito kwa raia wa mji kuwa huo watulivu huku maafisa wa ulinzi wakiendelea na mikakati ya kurejesha hali ya uthabiti.

Kova amesema uchunguzi wa awali umebainisha kuwa mlipuko huo ni ajali na wala sio shambulio la kigaidi.

Ni hii mara ya pili kwa milipuko kama hiyo kutoka jijini Dar es Saalam katika kipindi cha miaka miwili iliyopita mwaka wa 2009 zaidi ya watu ishirini waliuawa na wengine 300 kujerihiwa

Kadhalika,Rais Jakaya Kikwete amewaasa wananchi kuepuka maelezo ya "redio mbao" na badala yake wasubiri taarifa rasmi kutoka serikalini na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).Hata hivyo inawezekana Kikwete hajajiuliza kwanini wananchi wanategemea taarifa za "radio mbao" kwani ni dhahiri kuwa penye ombwe la taarifa rasmi,wananchi wanalazimika kugeukia vyanzo vya habari visivyo rasmi.



Hadi muda huu,hakuna kiongozi yeyote aliyewajibika au kuwajibishwa.Watanzania wanatarajia kuona Waziri wa Ulinzi Dkt Hussein Mwinyi,Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,Jenerali Davis Mwamunyange na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi hilo,Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo,wakiwajibishwa mara moja.Lakini kwa namna tunavyofahamu udhaifu wa Rais Kikwete katika kuwashughulikia watendaji wake,kuna uwezekano mkubwa wa Dkt Mwinyi,Mwamunyange na Shimbo kuendelea na madaraka yao

Kilicho wazi ni kuwa serikali itapoteza fedha za walipa kodi kuunda tume kama ile ya milipuko ya Mbagala mwaka 2009,na kisha ripoti ya tume hiyo kuishia kuwa karatasi za kufungia vitafunio.

Japo hakuna anayetaka kutumia janga hili la milipuko kama mtaji wa kuwahukumu watawala wetu,lakini kuna umuhimu mkubwa wa kuunganisha matukio yaliyopita na tukio hili na uwajibikaji duni wa serikali iliyopo madarakani.

Ni muhimu pia kutafakari dhamira ya serikali kuilipa kampuni ya kitapeli ya Dowans,sambamba na mpango wa kuwapatia wabunge shilingi bilioni 90 kila mmoja,huku mipango endelevu ya kuepusha na kukabiliana na majanga ikipuuzwa.

Ukweli ulio bayana ni kwamba serikali ya Kikwete na CCM yake haisumbuliwi na hali ya kutokuwa na uhakika na usalama wa wananchi.

Endelea kutembelea tovuti hii kwa habari na uchambuzi zaidi kuhusu tukio hili la kusikitisha.

16 Feb 2011




Habari kutoka Dar es Salaam zinaeleza kuwa milipuko kadhaa imetokea maeneo ya Gongo la Mboto.Hata hivyo habari nyingine zinadai kuwa milipuka hiyo imetokea maeneo ya Kisarawe

Bado hakuna taarifa rasmi kuhusu eneo na chanzo cha milipuko hiyo japokuwa habari zilizopo zinadai milipuko hiyo imetokea kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Mtandao wa Jamii Forums umemnukuu Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Brigedia Jenerali Abdulrahman Shimbo akisema "Hali ni mbaya Kikosi namba tano maghala yamelipuka ni hatari, watu wahame, maghala yako karibu karibu sana, tunaomba wananchi wahame sasa hivi, tunajitahidi kuzuia moto unaotokana na hilo unaweza kwenda mbali sana hadi Kilomota kumi, wananchi walioko karibu na maghala ya kikosi Gongo la Mboto wasogee mbali sasa hivi."

Hadi sasa hakuna taarifa kamili kuhusu idadi ya majeruhi japokuwa picha zilizotumwa na baadhi ya watumiaji wa huduma ya mtandaoni ya Twitter zinaonyesha majeruhi wakiwa katika hali mbaya



Tukio hili la kusikitisha linatokea wakati Serikali ikiwa haijaweka hadharani ripoti ya vyanzo vya milipuko iliyotokea kwenye Kambi ya JWTZ Mbagala mwezi Aprili na Mei mwaka juzi.

Wakati huo,aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Dokta Hussein Mwinyi aliahidi kuwa angewajibika iwapo ingebainika amezembea.Lakini simulizi hizo ziliishia hapo baada ya vile Serikali kupitia Wizara inayoongozwa na Mwinyi kuamua kuiweka ripoti hiyo 'kapuni'

Wakati tovuti hii inaendelea kukusanya habari za uhakika kuhusiana na milipuko hiyo ni muhimu kwa Watanzania kudai haki zao za msingi za usalama wa maisha yao na mali zao.Haiyumkiniki kuona 'intelijensia' ya vyombo vya dola ikiwa na 'ufanisi mkubwa' katika kukandamiza haki za kikatiba za wananchi lakini ikishindwa kuepusha majanga kama haya.

Upatikanaji wa taarifa sahihi unakuwa mgumu hasa kutokana na vyombo 'rasmi' vya habari nchini Tanzania kutowajibika ipasavyo kuwajulisha wananchi kinachoendelea.Tovuti zote za magazeti 'makubwa' hazina breaking news hadi wakati naweka habari hii.

(Video kwa hisani ya Dedichjr na Picha kwa hisani ya Jamii Forums)



Pichani ni Mbunge John Komba wa CCM 'akiwa makini' kwa kuuchapa usingizi Bungeni Dodoma.Hata huyu naye anastahili 'zawadi' ya milioni 90?

Hivi kweli inaingia akilini kusikia kwamba Serikali ya Kikwete ina mpango wa kuwapatia wabunge shilingi milioni 90 kila mmoja "kwa sababu inazojua yenyewe?Majuzi tu tumesikia habari kwamba Serikali hiyo hiyo inatembeza bakuli kwa wahisani ili wasaidie 'kuokoa jahazi' la hali mbaya ya Bajeti ya 2010/11.

Lakini pia tunakumbuka Kikwete alivyokuwa mkali kwa watumishi wa umma walipotishia kugoma kushinikiza kulipwa mishahara inayoendana na hali halisi ya maisha.Sasa kama ilishindikana kuwalipa wafanyakazi wa umma mishahara bora haya mabilioni ya kuwazawadia wabunge yanatoka wapi?

Naona kuna kila jitiahada za watawala wetu kukaribisha yanayojiri huko Arabia na Mashariki ya Kati.Japo inauma kuona mabilioni ya shilingi yakizawadiwa kwa waheshimiwa kama huyo anayechapa usingizi,lakini hatua hiyo inaweza kuwa blessing in disguise kwa maana kwamba huenda ikawahamasisha Watanzania kuiga mifano ya 'walalawima' wenzao wa Tunisia na Misri,na hatimaye kufanikiwa kuleta 'Uhuru wa Pili' (wa kwanza ulikuwa wa kumwondoa mkoloni.Wa pili ni wa kuwaondoa mafisadi)



My sista Jestina,a top-notch fashion blogger,with her exquisitely beautiful daughter Princess Iman .

.



15 Feb 2011


Hatimaye mmoja wa wanasoka mahiri kabisa duniani,Ronaldo wa Brazili,ameamua kuundika madaluga.Staa huyo mwenye kipaji cha hali ya juu ametangaza kustaafu rasmi soka.

Katika makala hii nawaletea video za kumbukumbu ya nguli huyo wa kandanda.Picha zote hizo ni kwa hisani ya gazeti la Daily Mail la hapa Uingereza






















14 Feb 2011


Leo ni Siku ya Mtakatifu Valentine,maarufu kama Siku ya Wapendanao,au Valentine's Day kwa kimombo. Pengine ni vema kuadhimisha siku hii kwa kutafakari umuhimu wa upendo.

Binafsi,si muumini mzuri wa siku zinazoambatana na matukio.Kwa mfano,mara nyingi huwa naadhimisha siku yangu ya kuzaliwa kwa sala na tafakuri ya miaka iliyopita na ijayo,Mungu akinijalia.Kwa wengine,siku ya kuzaliwa ni wakati wa kuingia gharama zisizo na umuhimu kwa sherehe kubwa zinazowaacha wakiwa na hali ngumu baadaye.Japo ni muhimu kufanya maadhimisho ya siku muhimu kama ya kuzaliwa lakini kuna umuhimu gani kama siku hiyo inabaki kuwa "siku muhimu" tu pasipo kuangalia wapi umetoka,ulipo na unakoelekea?

Na katika mantiki hiyohiyo,Siku ya Wapendanao inakuwa tu na umuhimu kama upendo utatafsiriwa kwa dhamira na vitendo.Kuna umuhimu gani wa kuadhimisha Siku ya Wapendanao kwa kadi za gharama na vinywaji ilhali umewasahau wanaohitaji upendo wako?

Wengi tunaelewa namna baadhi ya wenzetu wanavyoiogopa siku hii kutokana na kuwa na ma-Valentine wengi.Na miongoni mwa hawa ni wale wanaoadhimisha siku hii na "nyumba ndogo" huku wakiacha visingizio kwa wapenzi wao halisi.Hali hiyo inapoteza maana nzima ya siku hii.Haiwezekani mtu kudai anaadhimisha Siku ya Wapendanao kwa kumsaliti mpenzi wake.

Vinginevyo,nawatakia Siku njema ya Wapendanao nikiamini kuwa maadhimisho ya siku hii yatakuwa ya dhamira zaidi kuliko vitendo pekee.

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.