17 Apr 2011


Natambua kuwa CCM ni chama chenye sheria,taratibu na kanuni zake.Nafahamu pia kuwa kama chama huru (hata kama kumekuwa kikiwakumbatia mafisadi kukiendesha) kina mamlaka na uhuru wa kufanya mambo kipendavyo alimradi hakifunji sheria za nchi.

Hata hivyo,mengi ya maamuzi ya CCM-kama si yote-yanamgusa kila Mtanzania kwa vile chama hicho ndio tawala kwa sasa.Na kwa vile mfumo wetu wa siasa umeendelea kuwa wa chama kushika hatamu,kwa maana ya matakwa ya chama ndiyo yanayoiongoza serikali iliyopo madarakani,kila mwananchi mwenye mapenzi mema kwa Tanzania yetu anawajibika kuishauri,kuipongeza na hata kuikosoa CCM pale inapofanya mambo “ndivyo sivyo”.

Majuzi,chama hicho kimetangaza “kujivua magamba”.Nimeshaliongelea hilo kwa mapana,na makala yangu ya Jumatano ijayo kwenye jarida la Raia Mwema inajadili suala hilo kwa undani zaidi.Kwahiyo hapa sintingia kwa undani kuhusu uamuzi huo wa chama tawala uliopelekea vigogo wake kadhaa kuvuliwa madaraka (japo kwa kuwaheshimu,kilichofanyika ni kuvunja kamati kuu na kuingiza sura mpya kwenye nafasi mbalimbali).

Wasiwasi wangu mkubwa ni tendencies za kidikteta zinazoelekea kushamiri ndani ya CCM.Sijawahi kuwa shabiki wa Edward Lowasa,Rostam Aziz au Andrew Chenge,sio kwa vile siwapendi bali naamini kuwa matendo yao yanaikwaza sana Tanzania kupiga hatua kimaendeleo huku mamilioni ya wananchi wakigubikwa na umasikini wa kutupa.Hata hivyo,kutokuwa shabiki wao hakumaanishi kutoangalia namna walivyotendwa na CCM.

Haihitaji kuwa na uelewa wa uchambuzi wa siasa kumaizi kuwa by kujivua magamba CCM imemaanisha kuondokana na baadhi ya viongozi wake ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakihusishwa na ufisadi.Kwa lugha nyingine,magamba ni ufisadi,na ilichofanya CCM ni kujivua joho la ufisadi.

Wengi wetu tunafahamu kuwa uhasama mkubwa kati ya CCM na Dokta Wilbroad Slaa na Chadema kwa ujumla ni suala la ufisadi.Na kwa upande mwingine,umaarufu wa Slaa na Chadema umetokana zaidi na harakati zao katika kupambana na ufisadi.

Ndio maana katika majadiliano yangu ya kistaarabu huko Twitter na msanii wa Bongofleva mwenye mwamko mkubwa wa kisiasa,Hamisi Mwinjuma a.k.a Mwanafalsafaau MwanaFA,nimekuwa nimkumbusha mara kwa mara kuwa mie si mwanachama wa chama chochote kile cha siasa,achilia mbali Chadema.Kinachonifanya niafkiane na Chadema ni mtizamo,misimamo na harakati zao katika kupinga na kupambana na ufisadi.Kadhalika,sina chuki binafsi na Rais Jakaya Kikwete,serikali yake au CCM kwa ujumla bali “ugomvi” wangu nao ni jinsi wanavyokumbatia ufisadi na kupuuza vilio vya wanyonge wa Kitanzania kuhusu suala hilo.

Tunalazimika kuamini kuwa magamba yaliyovuliwa na CCM ni Lowassa,Rostam na Chenge kwa sababu kuu mbili.Kwanza,ni kwa vile kutoswa kwao kama vigogo wenye nguvu ndani ya chama hicho kumeendana na CCM kutangaza kuwa imejivua magamba.Ni wazi kuwa kama umevuliwa madaraka kisha aliyekuvua madaraka akitangaza kuwa ameondokana na uozo basi lazima utatafsiri kuwa uozo huo ni wewe uliyevuliwa madaraka.Pili,hata kabla ya CCM kuchukua uamuzi huo,wanasiasa hao wamekuwa wakituhumiwa kuhusika na ufisadi,japo mara kwa mara CCM iliwatetea huku ikidai kuwa tuhuma dhidi yao zinaweza tu kuthibitishwa na mahakama na si vinginevyo.

Na hilo la pili ndilo lililonisukuma kuandika makala hii.Si Kikwete,CCM au Kamati/Halmashauri Kuu yake wenye mamlaka ya kumtia mtu hatiani,hususan hatia yenyewe inapokuwa kubwa kama tuhuma za ufisadi.Hivi kwa mfano,Lowassa,Rostam na Chenge wakiamua kwenda mahakamani wakiituhumu CCM kwa kuwachafua kwenye jamii chama hicho kitasemaje?

Unaweza kudhani kuwa itakuwa rahisi kwa CCM kuweka hadharani ushahidi wa kusapoti tuhuma zake dhidi ya wanasiasa hao.Lakini hilo sio rahisi kwa vile,kwanza,tangu mwaka 2005 CCM hiyohiyo imekuwa ikipita huku na kule kudai kuwa tuhuma za ufisadi dhidi ya wanasiasa mbalimbali wa chama hicho (including Lowassa,Rostam na Chenge) ni porojo tu zisizo na ukweli wowote.Actaully,Mwenyekiti wa chama hicho,Rais Kikwete,ameshanukuliwa mara kadhaa akidai kuwa “kelele za mlango hazimnyimi usingizi mwenye nyumba”,akimaanisha kuwa tuhuma za ufisadi dhidi ya chama hicho na baadhi ya viongozi wake ni kelele tu  zisizopaswa kuendekezwa au kuamsha tafakuri ya Watanzania.

Kana kwamba hiyo haitoshi,miezi machache iliyopita,wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana,Rais Kikwete alisimama katika jukwaa jimboni Monduli kumpigia debe Lowassa,na akasimama kwenye jukwaa jimboni Igunga kumpigia debe Rostma,na akaenda jimboni kwa Cheyo kumpigia kampeni mwanasiasa huyo.Kadhalika,siku moja kabla ya Uchaguzi mkuu,Kikwete alizungumza na waandishi wa habari na kuwatetea tena watuhumiwa wa ufisadi na kudai kuwa ni watuhumiwa tu kwa vile hawajatiwa hatiani.

Sasa kama kilichofanyika Dodoma si udikteta ni kitu gani?Kwa sababu haiingia kabisa akilini kwamba viongozi waliosfifiwa na kutetewa mwezi Oktoba mwaka jana kuwa ni wasafi na wanaopaswa kuchaguliwa tena,waonekane hawafai miezi 6 baadaye.Of course,lolote linaweza kutokea katika kipindi cha miezi 6 lakini sote tunafahamu kuwa tuhuma za ufisadi wa Lowassa,Rostam na Change hazijatokea katika kipindi hiki cha miezi 6.

Kama maovu yao yalivumiliwa huko nyuma,na wakasafishwa hadharani na Rais Kikwete,iweje basi leo wanasiasa hao wabebeshwe tuhuma hizohizo ambazo walishasafishwa nazo?Ndio maana nimesema kuwa laiti wanasiasa hao wakiamua kufungua kesi ya kudhalilishwa mbele ya jamii,CCM itakuwa na kazi kubwa sana kujinasua.

Na sio hivyo tu bali wengi wetu tunafahamu kuwa ni vigumu mno kuwatuhumu watu kama Lowassa na Rostam kwa ufisadi pasipo kumhusisha Kikwete mwenyewe.Kama Lowassa ndiye aliyesababisha na kumwezesha utapeli wa Richmond,mwenye maamuzi ya mwisho kabisa alikuwa Kikwete mwenyewe ambaye aliidhinisha matakwa ya Lowassa kupitia vikao vya Baraza la Mawaziri ambavyo Kikwete ndio mwenyekiti wake.

Kama Rostam anahusishwa na suala la EPA,Kagoda na Dowans,again Kikwete alibariki yote hayo katika wadhifa wake kama Rais wa Tanzania.Anaweza kujiteteea kuwa hakufahamu ufisadi huo wakati unatokea.Hiyo inaweza kumfanya akaishi kwa muda wa kuazima lakini baadaye atalazimika kutueleza alichukua maamuzi gani baada ya kubaini kuwa ufisadi huo ulisababishwa na swahiba wake.

Lakini kuna suala jingine kubwa zaidi ambalo ni uhusika wa watu wasio na nyadhifa ndani ya CCM.Kwa mfano,ni watu gani ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa waliwezesha kufanikiwa kwa wizi wa EPA na Kagoda,na ujambazi wa Richmond na Kagoda?Kwanini hawajachukuliwa hatua hadi leo?Je nao si magamba?Kam jibu ni ndiyo,je ni CCM au serikali yake itakayowapa siku 90 za kuwajibika?Na watawajibikaje?Wajipeleke wenyewe mahakamani?
Vipi kuhusu Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Serikali Johnston Mwanyika?Vipi kuhusuMkurugenzi Mkuu wa Takukuru Edward Hosea?Je hawa nao si magamba yanayopaswa kuvuliwa?Wangekuwa ndani ya CCM wangeweza kupewa notisi ya siku 90 lakini hawa sio wanasiasa,hivyo haitowezekana kuwawajibi9sha katika namna ya akina Lowassa na Rostam.
Vipi kuhusu Rais Mstaafu Benjamin Mkapa?Kwa wadhifa wake bado ni kiongozi wa CCM.Kwanini basi iwe Lowassa,Rostma na Chenge pekee na sio rais huyo Mstaafu,sambamba na akina Mangula,Sumaye,Malecela,Mwinyi au hata Zakia Meghji,Mkuchika na Chiligati?

Na kama kujivua magamba kuna maana yoyote,kwanini basi Waziri Membe aendelee kuwa Waziri ilhali kuondolewa kwake kwenye madaraka aliyokuwa nayo kunaweza kutafsiriwa kuwa ni hatua dhidi ya mafisadi?Vipi kuhusu akian Lawrence Marsha,Daniel Yona na Basil Mramba ambao kwa sasa hawapo madarakani?Na vipi kuhusu watu kama William Ngeleja na Naibu wake Malima ambao wizara yao,kwa namna moja au nyingine,imewezesha ujambazi wa Richmond na Dowans?Vipi kuhusu watendaji kama Dr Idris Rashid na Mgonja?

Narejea tena.Siwatetei Lowassa,Rostam au Chenge wala sipingani na hatua yoyote iliyo,inayo na itakayochukuliwa dhidi yao.Lakini kama lengo la Kikwete na CCM yake ni kupambana na ufisadi kwa vitendo basi ni lazima zoezi hilo litanuliwe kwa mapana zaidi.Lakini sote tunajua kuwa sio rahisi kwa Kikwete kwenda mbali zaidi kwa vile anatambua kuwa anakalia kuti kavu.Najua fika kuwa washirika wake wanaweza kabisa kumwaga uozo wote hadharani katika staili ya “bora tufe wote”.

Jingine,na hili lina umuhimu wa ikipekee,Kikwete anatambua kuwa vyovyote iwavyo,lazima mwakani apitishwe na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM mpaka atakapomaliza muda wake.Na sio kupitishwa na kuchaguliwa tu,bali pia anapaswa kupata ushindi wa kishindo wa asilimia tisini na kitu.Sasa kwa vile anafahamu fika kuwa asipokuwa makini, “magamba” aliyoyavua yanaweza kabisa sio tu kumpunguzia kura hapo mwakani bali pia,in worst case scenario, kumuingiza kwenye vitabu vya historia kama mwenyekiti wa kwanza wa CCM kushindwa kurejea kwenye wadhifa wake huku akiwa bado madarakani,hawezi kwenda mbali zaidi ya alivyokwishafanya sasa.

Lililo wazi ni kwamba tutashuhudia mengi.Na tayari tumeshaanza kushuhudia baadhi ya vituko.Kwa mfano,mara baada ya “CCM kujivua magamba”,magazeti yanayomilikiwa na Rostam Aziz yameanza kuonekana yakiinanga CCM na serikali ya Kikwete.Tusisahau uwezo wa “magamba” hayo kifedha na influence kubwa waliyanayo ndani ya CCM na kwenye jamii.It is a bad influence lakini still ni influence.

All in all,matarajio ya Watanzania ni kuona nchi yao ikiondokana na nira ya ufisadi.Anayedhani “CCM kujivua magamba” ni sehemu ya process hiyo basi ni vema aamke kwenye lindi la usingizi aliomo.Kinachofanyika ndani ya chama hicho ni revelation ya msemo wa Kiswahili kuwa ushirika wa wachawi haudumu.Ni vita ya kimaslahi zaidi kuliko ya maslahi kwa jamii.Na ndio maana inasemekana hata maamuzi ya Kikwete kuvunja kamati kuu na kuwatosa maswahiba zake ni baada ya kutambua walikuwa wamedhamiria kwa dhati kumwondoa yeye mwenyewe kwa kuanzia na ajenda ya kutenganisha urais na uenyekiti wa CCM taifa.

Sihitaji kukwambia nani anayeweza kutuongoza kufikia ukombozi wa kweli wa Tanzania.Matendo hukidhi haja maridhwa kuliko maneno.Na kwa kila Mtanzania mwenye uzalendo na mapenzi ya kweli kwa nchi yetu anafahamu ni nani na chama kipi kinaweza kutufikisha tunakostahili kuwepo na kuwateketeza mafisadi wote.

16 Apr 2011


Kama ilivyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari,Chama cha Demokrasia Na Maendeleo (Chadema) leo kimefanya mkutano wake wa hadhara mjini Tabora na kutaja orodha mpya mafisadi ikiwa ni ziada ya wale waliotajwa kwenye List Of Shame,Mwembeyanga.

Kwa mujibu wa habari zilizokwishapatikana hadi muda huu,mafisadi wapya ni pamoja na mwanasiasa mkongwe John Malecela na Waziri wa Ujenzi na Miundombinu John Pombe Magufuli.

Kwa habari kamili fuatilia HAPA

15 Apr 2011


Ndugu wa Bwana Lilah Hussein ambaye anadaiwa kuchomwa moto na walinzi na Meneja/Mmiliki wa Hotel ya South Beach wameomba wapatiwe mwanga wa kisheria jinsi ya kudai haki kwa ndugu yao aliyechomwa moto.

Akiongea nami mmoja wa jamaa wa Lilah amesema kuwa mpaka sasa wako gizani hawajui pakuanzia kutokana na kutojua mambo ya kisheria.

Labda kwa anayeweza kutoa msaada au muongozo wowote wa kisheria anaweza kuwasiliana na mmoja wa ndugu hao kupitia 0655362785

Kwa sasa Lilah bado amelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

14 Apr 2011


Katika makala yangu kwenye toleo la wiki hii la jarida mahiri la Rais Mwema nazungumzia kujihusisha kwangu na uandishi wa makala magazetini,ikiwa ni pamoja na faida na hasara zake kwangu.Kadhalika nawasilisha vilio vya wanajamii ambao wametelekezwa na watawala.Pamoja na makala hiyo ( BONYEZA HAPA KUISOMA) ni habari na uchamuzi mahiri katika jarida hilo maridhawa la RAIA MWEMA



Kwa mujibu wa mtandao wa Jamii Forums

Rostam, Bashe watangaza vita na JK, wamuita naye fisadi
Katika kile kinachoonekana kuwa sasa wanatangaza vita, gazeti la Mtanzania linalomilikiwa na Rostam Aziz na kusimamiwa na Hussein Bashe limemchimba JK kwa kuandika leo kwamba Kikwete naye fisadi wakinukuu List of Shame iliyotolewa na Chadema Mwembe Yanga, huku wakinukuu tuhuma zotte ambazo zilielekezwa kwa JK na huku wakijifanya kuwarushia mpira Nape na Chiligati kuwa walisema mafisadi wote CCM wajiuzulu akiwamo JK.

JK, Mukama, Chiligati na Nape walizungumza wakirejea vikao vya CCM na si LIST of Shame na kama walitambua hilo wangesema mapema si baada ya kufukuzwa.

Katika vikao vya CCM List of Shame ya Chadema haijajadiliwa bali walijadili Richmond, Dowans, Kagoda na Rada na waliwataja kwa majina Lowassa, Rostam na Chenge. Hii ni sawa na mwizi kukamatwa na kusema "tuliiba na mwenzangu mbona hakamatwi?" Maana yake anakiri kuwa ni mwizi.





MAFISADI MPO???

13 Apr 2011


12 Apr 2011


Nimekumbana na habari ifuatayo katika gazeti la Tanzania Daima ambapo inaelezwa kuwa mwekezaji mmoja mwenye asili ya Kiasia amemchoma moto mwanamke mmoja kwa kosa la kuingia hotelini mwa mwekezaji husika bila kulipa kiingilio.

Kinachojidhihirisha katika habari husika ni dalili kwamba jeshi la pilisi linasuasua kumtendea haki mwananchi huyo.Nimewasiliana na bloga mwenzangu ambaye pia ni mwandishi mwandamizi wa gazeti moja la jamii huko nyumbani kumwomba tushirikiane kulipigia kele suala hili hadi haki ya mwananchi mwenzetu ipatikane.Kwa sie Watanzania tulio nje tunashuhudia namna raia wa nchi za wenzetu wanavyothaminiwa na sheria zao lakini kwetu ni hadithi tofauti hususan linapokuja suala la hao wanaoitwa wawekezaji.

Uwezo wa kifedha isiwe sababu ya kunyanyasa wananchi wasio na uwezo.Natoa wito kwa kila Mtanzania atakayeguswa na habari hii kuchangia kwa namna moja au nyingine kudai haki itendeke na ikiwezekan mwekezaji husika atimuliwe kabisa nchini.Hatuhitaji wababaishaji wanaoifanya nchi yetu kama pori lisilo na sheria.

Habari husika ni hii:

Mwekezaji amchoma moto raia Dar



na Hellen Ngoromera




RAIA wa Kiasia anayehusishwa kumiliki hoteli moja maarufu iliyopo Kigamboni anadaiwa kumjeruhi kwa kumchoma moto mkazi wa Mjimwema, Lila Hussein (25), baada kuingia hotelini hapo bila kulipa kiingilio.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, ndugu wa majeruhi huyo, Abdullah Saiwaad,alisema tukio hilo lilitokea Jumamosi majira kati ya saa 5:00 na 6:00 usiku.

Alisema kabla ya kuchomwa moto, Lila ambaye amelazwa wodi namba 7 katika Hospitali ya Temeke akiwa hajitambui, alivuliwa nguo kisha kumwagiwa mafuta ya petroli na kwamba amejeruhiwa vibaya kuanzia sehemu za magotini hadi shingoni.

Alisema chanzo cha tukio hilo ni Lila kuingia kwenye muziki hotelini hapo bila kulipa kiingilio.

“Hali ni tete, Lila yupo hospitali ya Temeke akipigania maisha yake baada ya kuchomwa moto na mhindi ambaye ni mmiliki wa hoteli ya South Beach, ameungua vibaya tunamwomba Mungu anusuru maisha yake,” alisema Saiwaad.

Alisema baadaye aliokolewa na wafanyakazi wawili baada ya kuamua kupeleka taarifa kijijini Mjimwema.

Kutokana na tukio hilo wanakijiji wametishia kuchoma moto hoteli hiyo na kwamba hali hiyo imesababisha mkuu wa kituo cha Kigamboni kupeleka askari wa doria kusimamia usalama hotelini hapo.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Davis Misime, alikiri kuwepo kwa taarifa hizo na kuahidi kuzifuatilia kwa kina.

Kwa mujibu wa Misime, usiku askari walipata taarifa kuwa kuna mtu amechomwa moto hotelini hapo ndipo walipokwenda na kumchukua majeruhi na kumpeleka katika kituo cha afya Kigamboni kisha baadaye kupelekwa Temeke.

Hata hivyo, habari zinapasha zaidi kwamba baadaye jioni ya jana, Lila alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na hali yake kuwa mbaya.

CHANZO: Tanzania Daima



Hatimaye habari za "tiba ya miujiza ya Babu wa Loliondo" zimefunikwa kidogo,at least kwa muda,baada ya chama tawala CCM kufanya mabadiliko yanayoitwa makubwa katika safu za uongozi wake.Katika mabadiliko hayo,kamati kuu ya chama hicho ililazimika kujiuzulu na kufuatiwa na uteuzi wa wajumbe wapya.

Tukio hilo linaonekana kuwagusa Watanzania wengi na tayari baadhi yao wameanza kumpongeza Mwenyekiti wa chama hicho,Rais Jakaya Kikwete,kwa kile kinachotajwa kama "maamuzi magumu na mazito".

Hebu nikuulize msomaji mpendwa.Hivi ukiamua kuanzisha urafiki na jambazi unategemea hatima yake itakuwa nini?Na pindi ukitambua kuwa urafiki huo unakupeleka kubaya,na hatimaye kuamua kuachana na jambazi huyo,unastahili sifa gani?

Mfano huo unamhusu Kikwete na CCM kwa ujumla.Wakati baadhi yetu wanapiga vigeregere vya pongezi kutokana na "ujasiri wa Kikwete" kinachopuuzwa ni ukweli kuwa ni Kikwete huyuhuyo aliyewawezesha watu kama Edward Liowassa na Rostam Aziz kufikia hapo walipo sasa.

Baada ya Mwalimu Julius Nyerere "kumzuia" kuongoza Tanzania mwaka 1995,Kikwete alijenga uswahiba na Lowassa na Rostam kwa minajili ya kuchukua urais mwaka 2005 baada ya Rais Benjamin Mkapa kumaliza miaka yake 10.Mbinu chafu zilizotumiwa na wanasiasa hao watatu zinafahamika kwa takriban kila mmoja wetu.Utatu huo usio mtakatifu uliounda genge hatari linalojulikana kama "Wanamtandao".Genge hilo lilifanya kila mbinu kuhakikisha kuwa lazima Kikwete anakamata urais mwaka 2005.Na hatimaye walifanikiwa baada ya kujipenyeza katika kila nyanja ya jamii ya Tanzania.

Baada ya kuukwaa urais,Kikwete aliwaruhusu washirika wake kufanya mambo wapendavyo kana kwamba Tanzania ni kampuni ya mtu binafsi.Sijui ni kujisahau au kuvimbiwa,haikuchukua muda kwa maswahiba hao wa Kikwete kuanza kufanya mambo "ndivyo sivyo".Kufupisha stori,skandali kama za Richmond,EPA,nk kwa kiwango kikubwa ni matokeo ya moja kwa moja ya harakati za wanasiasa hawa.

Sasa,kilichotokea Dodoma na kupachikwa jina "kujivua magamba" ni sawa kabisa na mfano niliotoa hapo awali wa mtu kujenga urafiki na jambazi.Baada ya Kikwete kumaizi kuwa asipokuwa makini anaweza kujikuta akifiwa na CCM mikononi mwake,amelazimika kujitenga na maswahiba waliomsaidia kuukwaa urais.

Kwanini basi naamini kuwa Kikwete hastahili pongezi zozote kutokana na uamuzi wa kuwatosa maswahiba zake?Kwanza,hata huko "kuwatosa" kwenyewe kumefanyika katika mazingira ya uoga.Inaelezwa kuwa matakwa ya waliohitaji mageuzi ndani ya chama hicho yalikuwa kuwatimua kabisa Lowassa,Rostam na Chenge.Lakini kinyume chake,Kikwete akaamua kuvunja kamati kuu nzima.Usisahau msemo wa Kiswahili kuwa kilio cha wengi ni harusi.

Je ni kweli kwamba kamati kuu nzima ilikuwa na mapungufu ya kulazimisha kuivunja yote?Je kamati kuu nzima ilikuwa ya kifisadi kwa vile tu miongoni mwao kulikuwa na watuhumiwa wa ufisadi?

Ukweli unabaki kwamba Kikwete hakuweza kuwa na jeuri ya kuwatosa Lowassa,Rostam na Chenge kama mtu mmoja mmoja na badala yake akaamua kuchukua kile wanachoita Waingereza "blanket decision" ambapo waliomo na wasiomo wakajikuta wanabwagwa.

Tukiweka hilo kando,kuna hoja ya pili ambayo ni nafasi ya waliotoswa kuendeleza kile kile kilichopelekea kuondolewa kwenye kamati kuu in the first place.Lowassa,Rostam na Chenge wanaendelea kubaki wabunge wa CCM,huku Lowasssa akiendelea pia kuongoza kamati influential ya Ulinzi na Usalama.Je kwa nafasi walizobaki nazo wanasiasa hao hawawezi kujitutumua kuendeleza harakati zao?Muda utatueleza.

Lakini pia tunapaswa kumwangalia Kikwete sio tu kama Mwenyekiti wa CCM bali pia Rais wa nchi.Kama tukiamini kuwa ujasiri wake ndio uliopelekea maamuzi hayo "magumu" ndani ya chama chake,kwanini basi huko serikalini inamwia vigumu kuondoa rundo la uozo linalohatarisha future ya nchi yetu?

Na ieleweke kwamba wakati chama kinaendeshwa kisiasa zaidi,serikali inaendeshwa kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo,au zinazoweza kutengenezwa kwa makusudi maalum.

Kikwete huyuhuyu ndiye aliyetamka mara baada ya kupata urais mwaka 2005 kuwa anawafahamu wala rushwa kwa majina,na kwamba anawapa muda wa kujirekebisha.Sote tunafahamu kuwa wala rushwa sio tu hawajajirekebisha bali pia wamepuuza indefinite deadline hiyo ya Kikwete.

Sijui ni usahaulifu au hatupo makini,baadhi ya wenzetu wameshasahau kuwa katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita hivi majuzi tu Kikwete huyuhuyu alisimama majukwaani kuwapigia debe Lowassa,Rostam na Chenge huku akiwamwagia sifa lukuki.

Kama haitoshi,Kikwete alimudu kuwatetea "live" alipoongea na waandishi wa habari huku akisisitiza kuwa wanasiasa hao hawajatiwa hatiani na kinachodaiwa dhidi yao ni tuhuma tu.Sasa kama huo ndio ukweli,how come basi safari hii kawatosa ilhali hawajawahi kutiwa hatiani?

Na watatiwaje hatiani katika mazingira ya sasa ambapo sheria zipo tu kwa ajili ya kuwabana wamachinga,wezi wa kuku,walalahoi wanaoshindwa kumudu kulipa kodi kutokana na umasikini wao na Watanzania wengine wa kawaida,ilhali vigogo wakiachwa wafanye wapendavyo?

Hivi kweli tumesahau mzaha wa hukumu dhidi ya Chenge katika kesi yake ya kuua watu wawili kwa kuwagonga na gari ambalo bima yake ilikuwa imesha-expire?Kuna Watanzania wangapi wanaosota jela sio kwa vile wameshatiwa hatiani bali hawana uwezo wa kuwahonga waendesha mashtaka na mahakimu?

Don't get me wrong kuwa labda namchukia Kikwete.Hapana.Sina tatizo naye kama Jakaya Kikwete bali tatizo langu lipo kwenye udhaifu wa uongozi wake kama Rais Jakaya Kikwete.

Tusiwe wepesi wa kuamini kila jambo linapotokea hata kabla ya kupima ufanisi wake.Kadhalika,tusiwe wepesi wa kupuuza historia,kwa mfano kusahau kuwa Kikwete huyu huyu alituahidi maisha bora kwa kila Mtanzania na matokeo yake imeishia kuwa maisha bora kwa kila fisadi.

Unaweza kunihoji kwanini nawasihi kuwa na subira kabla ya kukimbilia kupiga vigeregere vya furaha na pongezi kwa maamuzi ya "kijasiri" ya Kikwete,lakini wakati huohuo mie pia nakimbilia kumwaga lawama na kusambaza "sumu ya kutotarajia mema" badala ya kusubiri matokeo.

Jibu langu ni jepesi.Historia inamhukumu Kikwete.Amekuwa mahiri zaidi wa kutoa ahadi lakini mwepesi sana wa kusahau ahadi zake.Historia pia inatukumbusha kuwa hata Lowassa alipojiuzulu kwa kuhusika kwake kwenye skandali ya Richmond Kikwete alimpongeza na kudai kilichomkumba swahiba wake huyo ni ajali tu ya kisiasa.Na Waziri Mkuu Mizengo Pinda akapigilia msumari kwa kudai kuwa sikum moja Lowassa anaweza kurejea kwenye uongozi serikalini.Kwanini basi sasa tuamini kuwa kutoswa kwa wanasiasa hao ndio mwisho wa yote wanayolifanyia taifa hili?

Mwisho,nadhani tumezowea mno kuona madudu kiasi kwamba hata kiongozi anapotimiza wajibu wake tunalazimika kumpongeza.Kwanini hatujipongezi kwa kunawa uso au kupiga mswaki kila tunapoamka?Yah,hatujipongezi kwa vile vitendo hivyo ni wajibu wetu wa kila siku.

Kwanini hatujipongezi kwa kwenda makazini au mashuleni?Alichofanya Kikwete sio ujasiri bali kimsingi ni wajibu wake kama kiongozi.Na kwa hakika hakipaswi kuishia huko CCM pekee,chama chenye wanachama pungufu ya watu milioni tano wakati nchi yetu ina watu takriban milioni 50,bali kama yupo serious kweli na anajua kwanini yupo Ikulu,basi ni lazima aanze kusafisha uozo uliopo kila kona.

Kuna tofauti kubwa kati ya jambo jema linalostahili pongezi na utekelezaji wa wajibu.Alichofanya Kikwete ni the latter:ametekeleza wajibu wake kama kiongozi.Jambo jema linaloweza kutufanya tummwagie rundo la pongezi ni pindi atakapoamka usingizini na kutambua nchi inateketea kwa ufisadi huku virusi vya udini vikizidi kuzagaa katika jamii yetu kutokana na jitihada za matapeli wa kisiasa wanaowatumia wazembe wanapoouza vipaumbele vyao (kwa mfano wanaopotosha kuwa upinzani dhidi ya mchakato wa mabadiliko ya katiba unatokana na chuki ya Wakristo kwa Muislam Kikwete.This is way too low,na tusipokuwa makini tutaanza kutetea vibaka,majambazi,makahaba,mafuska,wabakaji,nk kwa vile tu wanatoka dhehebu flani).

10 Apr 2011




Habari zilizopatikana kutoka Dodoma kwenye kikao cha CCM chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete zinaeleza kuwa baadhi ya viongozi waadamizi wa chama hicho wamevuliwa madaraka.Kwa mujibu wa vyanzo vya mtandaoni,waliokumbwa na panga la Kikwete ni pamoja na maswahiba wake wakuu kisiasa,Edward Lowassa na Rostam Aziz.Wengine wanaotajwa kwa mujibu wa habari hizo ni "Mzee wa Vijisenti" Andrew Chenge na "mgosi" Yusuph Makamba.

Ningependa kuichambua habari hii kwa kirefu lakini nasubiri kwanza tamko rasmi la CCM.Hata hivyo,tukiamini kuwa habari hizo ni sahihi,kuna uwezekano ya yafuatayo kutokea:

Kwanza,ni muhimu kufahamu watu kama Lowassa na Rostam wametoka wapi.Hawa walikuwa vioungo muhimu kwa ushindi wa Kikwete mwaka 2005.Wanaowajua vema wanawa-describe kwa mlolongo huu:Lowassa-mwanasiasa haswa (simaanishi kuwa ni mwanasiasa mwadilifu),Rostam-bwana fedha,na Kikwete-mtawala.Wajuzi wa siasa chafu wanaeleza kuwa ushirikiano huo wa watu hawa watatu ulitumia kila aina ya mbinu kuhakikisha Kikwete anaingia Ikulu hapo 2005.Na ikawa hivyo,baada ya viongozi hao wakuu wa "Mtandao" kufanikiwa kupenya takriban kila kundi la jamii;kutoka viongozi wa dini hadi wakuu wa taasisi za dola,kutoka wanahabari hadi wasanii.

Pasipo kuuma maneno,ushirika huu usio mtakatika wa Lowassa,Rostam na Kikwete ni mithili ya joka lenye vichwa vitatu.Sasa iwapo ni kweli kuwa Kikwete kaamua kubaki kichwa pekee kwenye joka hilo basi yayumkinika kubashiri kuwa uhai wa joka hilo nao uko matatani.

Pili,kwa kufuata mlolongo wa nilichoandika hapo juu,inaelezwa kuwa Lowassa ndiye aliyefanya kazi kubwa zaidi ya kutengeneza serikali ya Kikwete.Ikumbukwe kuwa japo wote wawili walishashika nyadhifa mbalimbali serikali kabla ya 2005,Lowassa alikuwa amejijenga zaidi kiuchumi na kisiasa ukilinganisha na Kikwete.Kadhalika-na hapa nafafanua kwanini niliandika hapo juu kuwa Lowassa ni mwanasiasa haswa(japo simaanishi ni mwanasiasa mwadilifu)-ni ukweli kuwa mwanasiasa huyo ana ushawishi wa kisiasa zaidi ya Kikwete.Japo wote wawili ni wapenda umaarufu (populists),wakati Kikwete amekuwa akitumia zaidi turufu ya "tabasamu la muda wote" na "kuwa karibu na watu",Lowassa amekwenda mbali zaidi na kujifanya anayafahamu matatizo ya wananchi na kuyatolea ufumbuzi mapema (ndio maana licha ya kulazimika kujiuzulu kutokana na ufisadi wa Richmond bado kuna wanaomwona kama mwajibikaji).Kwa kifupi,Lowassa ni mwepesi wa kuchukua maamuzi (hususan yale yatayopelekea yeye kuonekana kama "Sokoine flani hivi"),Kikwete ni mzito wa maamuzi (huku walio karibu naye wakidai tatizo sio uzito wa maamuzi bali hajui vipaumbele vyake).

Inaaminika kuwa Lowassa ana ufuasi mkubwa ndani ya CCM na serikalini kwa ujumla.Kwa mujibu wa wajuzi wa mambo,faida aliyonayo Lowassa ndani ya chama hicho ni uwezo wa kifedha,ambapo inaelezwa kwamba amewasaidia viongozi mbalimbali wa CCM kiuchumi na kuwawezesha kuwepo walipo leo.Kadhalika,akiutumia vema urafiki wake na Kikwete, na nafasi yake kama Waziri Mkuu kabla ya skandali ya Richmond,aliweza kutengeneza "mtandao ndani ya mtandao",kwa maana ya kuwaweka madarakani watu wenye utiifu kwake zaidi kuliko CCM au Kikwete.Inaelezwa wateuliwa wengi kwenye nafasi za kiserikali na kichama ngazi za mikoa na wilaya ni wafuasi wa Lowassa,kwa mfano ma-RC na ma-DC,na wenyeviti na makatibu wa CCM mikoani na wilayani.

Swali la muhimu ni je,kuondoka kwa Lowassa katika wadhifa mmoja kutazuwia nguvu na ushawishi wake kwa wafuasi wake,wengi wao wakiwa ni watu walio madarakani kutokana na fadhila za mwanasiasa huyo?

La tatu ni ukweli kuwa Lowassa anataka urais hapo 2015.Na hilo halikuanza jana au juzi bali wajuzi wa mambo wanaeleza kuwa kulikuwa na makubaliano rasmi kati ya Kikwete na Lowassa kuwa wangepokezana uongozi maara baada ya Kikwete kumaliza miaka yake 10.Japo suala la Richmond lilizua mfarakano wa aina flani kati ya wawili hao lakini ukweli unabaki kuwa "heshima" aliyotoa Kikwete kwa Lowassa kwa kutomtimua bali kusubiri ajiuzulu mwenyewe iliwaacha wawili hao wakiendelea na urafiki wao japo si kama ilivyokuwa mwanzoni.

Haifahamiki kama Kikwete bado anaheshimu "makubaliano" yake na Lowassa kuhusu "kupokezana kijiti cha urais hapo 2015" lakini hiyo haimzuwii Lowassa kuamini kuwa "piga au" lazima achukue nafasi hiyo.Of course,kuna majina kama Bernard Membe (mtu anayetajwa kuuweka uhusiano na Lowassa katika wakati mgumu kwa vile yeye na Lowassa "picha hazipandi" ilhali yeye na Kikwete ni "damu damu",na Kikwete na Lowassa ndio hivyo tena "hawakufahamiana mtaani" kama ilivyowahi kutamkwa hadharani ) lakini turufu ya Lowassa haitegemei sana baraka za Kikwete bali ushawishi na nguvu yake ndani ya CCM,sambamba na uwezo wake mkubwa wa kifedha (alizitoa wapi....waulize TAKUKURU).Na ana faida nyingine kubwa ambayo ni uswahiba wake na Rostam,mfanyabiashara mwenye asili ya kiasia anayetajwa kuwa na nguvu zaidi ya Kikwete-kutokana na utajiri wake unaoweza kumfanya kuwa mtu tajiri kuliko wote Tanzania.Kadhalika,inaelezwa kuwa Rostam ni mjuzi wa mbinu chafu hususan kwa kutumia fedha zake na "njaa" za wanaohitaji chochote kutoka kwake.

Jingine,ambalo linaweza kuwa si la msingi sana japo lina umuhimu wa aina flani ni ukweli kwamba Lowassa na Rostam wana siri muhimu kumhusu Kikwete na urais wake kwa ujumla.Njia pekee kuwadhibiti wawili hao kwa kutumia Idara ya Usalama wa Taifa.Katika siasa zetu za "ovyo ovyo" ni rahisi tu kwa rais kuiamuru taasisi hiyo imfanyie kazi zake binafsi badala ya zile za kikatiba.Hilo linawezekana zaidi kutokana na nafasi ya Rais kama consumer wa taarifa zote za kishushushu.

Nisingependa kutabiri matokeo kabla ya taarifa kamili ya CCM lakini tukiamini habari zilizopo na ikathibitika kuwa ni kweli basi nachobashiri ni mwanzo wa mwisho wa chama hicho tawala.Naomba unielewe vizuri: tatizo la msingi sio kutimuliwa kwa Lowassa na Rostam bali ukweli kuwa USHIRIKA WA WACHAWI HAUDUMU.Sambamba na hilo ni ukweli mwingine kuwa JOKA LENYE VICHWA VITATU HALIWEZI KUWA HAI MUDA MREFU PINDI VICHWA VIWILI VIKIKATWA.

Lakini la muhimu kuliko yote ni manufaa kwa Watanzania kutokana na mabadiliko hayo ndani ya CCM.Kwa kifupi,ukiacha vichwa vikubwa vya habari kwenye magazeti yetu,mabadiliko hayo hayana manufaa yoyote kwa masikini wasio na hakika ya mlo wao wa kesho,wanafunzi wanaokaa sakafuni kwa uhaba wa madawati,akina mama wanaoletewa bajaj za kuwawahisha hospitali wakiwa wajawazito japo wabunge wanapewa mashangingi ya uheshimiwa,nk nk nk.Wa kuondoka na CCM kama chama kilichopo madarakani.Wanapoondoana ndani kwa ndani haimsaidii Mtanzania wa kawaida.

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.