23 Nov 2012


NIANZE makala haya na nukuu ya bandiko la Nape Nnauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kuhusu ushindi wa hivi karibuni wa Rais Barack Obama wa Marekani. Nape aliweka bandiko hilo kwenye mtandao wa Jamii Forums, Novemba 7, mwaka huu akisema:
“Ushindi wa Obama dhidi ya Romney, ni fundisho zuri kwa upinzani nchini kwetu kama wataamua kujifunza, mafunzo muhimu sana kwa washindani wa kisiasa ni pamoja na; Mosi, kiwango cha utekelezaji wa ahadi mbalimbali na mipango (Ilani ya Uchaguzi) kwa wananchi ina nguvu kubwa katika kuwafanya wapigakura kuamua nani wa kumpa kura wakati wa kupiga kura...kupigia kura mabadiliko au la...
Pili, kelele nyingi na wingi wa wapiga kelele si kigezo cha kupata kura nyingi siku ya kupigiwa kura...mikakati na ukaribu na wapigakura ambao huonyesha ni kiasi gani Chama kiko karibu na kuzijua changamoto zinazowakabili wapigakura, ni moja ya misingi mikubwa...
Tatu, kutumia muda mwingi kuponda mafanikio yaliyopatikana kwenye kipindi cha mshindani wako...hasa aliyeko madarakani, hakusaidii kukufanya upate kura, bali wenye akili zao wataona unawadharau na kuwaona wajinga kama vile hawaoni yaliyofanyika...ndicho kilichommaliza Romney...
Nne, lakini ushindi kwa Obama ni dalili njema za kukubalika kwa fikra za kijamaa kwa Taifa kubwa na la kibepari duniani...sasa tizameni upya itikadi zenu...”
Katika makala haya, nitamjibu Nape hoja kwa hoja kwa minajili ya kuwafumbua macho Watanzania wenzangu juu ya hatari ya baadhi ya wanasiasa kama Nape kuteka mafanikio ya wanasiasa wa nchi nyingine na kuyalinganisha na ubabaishaji wao ambao wao wanaamini ni mafanikio.
Kimsingi, mwanasiasa huyo amepotoka katika hoja zote nne. Ingawa ni kweli kwamba CCM na Serikali yake wamejaribu kutekeleza baadhi ya ahadi zao (kwa mfano ujenzi wa barabara kadhaa), moja ya ahadi za msingi iliyotolewa na mgombea wa chama hicho mwaka 2005, Rais Jakaya Kikwete, kuhusu maisha bora kwa Watanzania imeendelea kuwa kiini macho.
Kwa mtizamo wangu, kikwazo kikubwa kwa ahadi hiyo ya Rais Kikwete, ni ufisadi ambao yayumkinika kuhitimisha kuwa umeshamiri zaidi tangu Awamu ya Nne iingie madarakani. Na ufisadi usingepaswa kuwa kikwazo kwani moja ya matamko ya awali ya Rais Kikwete baada ya kuingia madarakani ilikuwa kuwapa ‘deadline’ mafisadi, akidai kuwa asingekuwa na huruma nao na kwamba tabasamu lake lisitafsiriwe vibaya.
Hadi leo hakuna fisadi mmoja aliyejali ‘deadline’ hiyo, na badala yake tunashuhudia ufisadi mpya ukiibuka kila kukicha. Kwa makusudi, Nape anajaribu kulinganisha utekelezaji wa ahadi za Obama wakati anaingia madarakani na porojo za CCM.
Wakati Obama amefanikiwa kutekeleza ahadi ya kumteketeza aliyekuwa gaidi wa kimataifa, Osama bin Laden, na pia kutekeleza ahadi yake ya kuyaondoa majeshi ya Marekani huko Iraki, licha ya ‘deadline’ ya Rais Kikwete kwa mafisadi kubaki historia tu, ahadi nyingine kuwa angemaliza kero ya mgao wa umeme, imeendelea kuwa ndoto tu.
Katika hoja ya pili, Nape anadai CCM inazijua changamoto zinazowakabili wapigakura wa Tanzania. Yupo sahihi. CCM inatambua kero za Watanzania, hususan kushamiri kwa rushwa nchini, lakini chama hicho kimetokea kuwa hifadhi ya wala rushwa.
Ushahidi wa karibuni kwamba CCM ni kichaka kinachohifadhi mafisadi ni kusuasua kwa Serikali yake kuwashughulikia majambazi walioficha fedha zetu huko Uswisi. Anachokiita Nape kuwa ni wingi wa kelele, akimaanisha za vyama vya upinzani, kwa hakika ni kilio cha Watanzania walio wengi, ukiondoa mafisadi. Kelele hizo anazozungumzia Nape ndizo zilizopelekea kuibua ufisadi mkubwa kama wa EPA, Richmond na kadhalika na sasa hili suala la fedha zilizoibwa na mafisadi na kufichwa Uswisi.
Katika hoja ya tatu, Katibu Mwenezi huyo wa CCM anadai kuwa kudharau mafanikio ya utawala uliopo madarakani, ni sawa na kuwatusi wapigakura. Kimsingi, sijawahi kuwasikia CHADEMA au chama kingine cha upinzani kikiponda jitihada za Serikali ya CCM katika masuala ya maendeleo ya nchi. Na ndiyo maana Rais Kikwete alipokuwa ziarani mkoani Arusha, alimwagiwa sifa na baadhi ya wapinzani hao hao ambao Nape anadai wanaponda kila kitu.
Kile anachotafsiri Nape kwamba ni kuponda kila kitu, kwa hakika ni usikivu wa vyama vya upinzani kwa kero za wananchi na kisha kuziongelea hadharani. Sawa, ujenzi wa barabara ni moja ya ‘priorities’ zetu, lakini miundombinu bora kwenye jamii iliyogubikwa na ufisadi, ni sawa na kuwa na ndoo inayojazwa maji ilhali imetoboka.
Rais Kikwete anajenga, mafisadi wanabomoa, na pasipo kuwadhibiti mafisadi hao, ni wazi kwamba jitihada zake zitaishia kuwa moto wa karatasi tu.
Hoja ya nne ya Nape inanifanya nijiulize kama alikuwa anafanya utani mbaya au ni uthibitisho kwamba hata Katibu Mwenezi wa Taifa wa CCM haelewi chama chake kinafuata itikadi gani. Nape anaweza kuwa mjamaa, na anaweza kuwa anatamani chama chake kirejee kwenye itikadi hiyo, lakini haihitaji kuwa na uelewa wa siasa za nchi yetu kutambua kuwa CCM iliyokumbatiwa na mafisadi, si tu haifuati siasa za ujamaa, bali haiwezi kurejea kwenye itikadi hiyo kamwe.
Wakati Nape ana haki ya kulinganisha ‘mafanikio’ ya CCM na chama chochote kile (haki hiyo imebainishwa katika Katiba yetu: freedom of expression), ukweli ni kwamba kitakachokimaliza chama hicho tawala ni mitizamo kama hiyo fyongo ya Nape kuwa kelele za wapinzani ni zao binafsi na si vilio vya Watanzania.
Wakati niliweza kubashiri kwa usahihi ushindi wa Obama, ninachelea kufanya hivyo kwa uchaguzi wetu mkuu wa mwaka 2015 kuhusu nafasi ya wapinzani kuing’oa CCM. Hiyo si kwa sababu CCM ina mafanikio kama Obama na chama chake cha Democrats (yaliyopelekea kumbwaga Romney na Republicans kwa ujumla), bali ukweli kwamba upinzani una kazi kubwa ya kujiimarisha kati ya sasa na 2015 kama kweli una nia ya kuing’oa CCM, ambayo kimsingi inafanya kila jitihada kung’olewa madarakani haraka iwezekanavyo.


15 Nov 2012


Nianze makala hii kwa kujipongeza kutokana na ‘ubashiri wangu sahihi’ kuhusu Uchaguzi wa Rais wa Marekani. Kama mnakumbuka, katika makala ya kwanza kwa mwaka huu nilijaribu kubashiri mwenendo wa masuala mbalimbali kwa ‘mwaka mpya’ 2012, na moja ya ubashiri huo ulikuwa huu:

“Kwa kuzingatia uchambuzi wa watu mbalimbali na kwa kadri ninavyofuatilia siasa za Marekani, dau (bet) langu ni ushindi ‘kiduchu’ kwa Obama dhidi ya Mitt Romney, mgombea ninayetabiri atapitishwa na Republican (iwapo upepo wa kisiasa hautobadilika.)”

Well, Romney alifanikiwa kushinda kuwa mgombea wa Republican na hatimaye kuchuana na Obama kwenye uchaguzi moja ya chaguzi zilizokuwa na ushindani mkali kabisa, na hatimaye Obama akafanikiwa kutetea kiti chake cha Urais (nami nikafarijika kuona ‘utabiri’ wangu umetimia.)

Tukiachana na hilo, makala hii anahitimisha mfululizo wa makala zangu kuhusu vurugu za kidini huko nyumbani. Katika kuhitimisha, nitazungumzia maeneo manne: vikwazo vya ndani ya Uislam kupata ufumbuzi wa manung’uniko yao; baadhi ya migongano ya kiimani kati ya Waislam na Wakristo, na ‘utata’ wa Kikatiba kuhusu migongano hiyo; na mwisho, mapendekezo ya nini kifanyike kukabiliana na vurugu za kidini huko nyumbani.

Vikwazo vya ndani ya Uislam kupata ufumbuzi wa manung’uniko yao:
Maeneo mawili yanayothibitika kitaaluma kuwa ni msingi wa manung’uniko ya Waislamu wengi ni upatikanaji (access) wa nafasi ya elimu na ajira. Sote twatambua kuwa ukimnyima mtu elimu unamnyima fursa ya ajira (angalau kwa ajira zinazohitaji ujuzi.)

Tukiweka kando ‘lawama’ kuhusu ‘mfumo wa kibaguzi, ni muhimu kwa Waislam wenyewe kutambua kuwa lawama pekee haziwezi kuleta ufumbuzi utakaoleta angalau usawa katika fursa za ajira na elimu. Tukumbuke kuwa hata mkoloni hakuamua kutupa uhuru kwa kumchukia au kumlaumu tu.

Kadhalika Nduli Idd Amin (ambaye hivi karibuni baadhi ya ‘Waislam wenye msimamo mkali’ walibadili mtizamo wao na kumwona kama shujaa katika namna ileile ya kifo cha gaidi la Kimataifa Osama bin Laden kiliombolezwa na watu hao kama shujaa wao) hakuondoka kwa vile tulimwita kila aina ya jina baya.
Kama Waislam wanaafikiana kuwa mfumo ‘wa kibaguzi’ uliwanyima fursa ya elimu na hivyo kuwatengenezea mazingira magumu ya kupata ajira zinazohitaji elimu, basi ni muhimu kwao kuwekeza vya kutosha kwenye elimu.

Na moja ya njia bora inaweza kuwa kuziwezesha shule za kidini (pengine kuanzia madrasa) zitoe pia elimu ‘ya kidunia.’ Nilishaeleza huko nyuma kwenye mfululizo wa makala hizi jinsi shule za seminari za Kikristo zilivyochangia kuzalisha wasomi Wakristo.

Huu ni ‘ukweli mchungu’: kama mtoto wa Kikristo akitoka shule anaenda twisheni kuongeza maarifa ya ‘elimu ya kidunia’ ilhali mwenzie wa Kiislam akitoka shule anaenda madrasa kuongeza elimu ya kidini, ni wazi mmoja wao anajitengenezea mazingira mazuri ya kufaulu huku mwingine anajikwaza. Hapa simaanishi watoto wasiende madrasa bali ikiwezekana, shule za kidini (ikibidi hata kuanzia madrasa) zijumuishe pia elimu ya kidunia.

Kwa uelewa wangu, misikiti si mahala pa ibada pekee bali pia sehemu ya kumpatia muumini elimu itakayomwezesha kumtumikia Muumba wake ipasavyo. Pengine kuna umuhimu kwa kasi ya ujenzi wa misikiti kuendana na kasi ya ujenzi/uanzishwaji wa taasisi za kielimu, au ikibidi kutumia misikiti hiyo kama sehemu za ‘mapambano ya kuziba pengo la kielimu linalowakabili Waislam wengi.’

Pendekezo jingine ambalo lipo nje ya uwezo wa Waislamu ni kwa serikali kuangalia uwezekano wa kile kinachofahamika katika lugha ya Kiingereza kama ‘affirmative action’ (yaani upendeleo wenye lengo la kuleta uwiano kwa kundi flani katika jamii katika eneo flani.) Sitaki kuamini kuwa kama takwimu zikiwekwa wazi kuonyesha pengo lililopo kielimu na kiajira kati ya Wakristo na Waislamu, kisha serikali ikaridhia kutaka kupunguza pengo hilo kwa njia za uwazi, Wakristo watapinga hatua hiyo. Cha muhimu ni kufanya jitihada hizo kwa uwazi. Affirmative action imeweza kufanikiwa kwa kiasi fulani katika nchi za Magharibi kuleta uwiano kati ya, kwa mfano, ‘wazungu’ (Whites) na makundi madogo katika jamii (minorities), kwa mfano Watu Weusi (Blacks).

Baadhi ya migongano ya kiimani kati ya Waislamu na Wakristo, na utata wa Kikatiba unaotokana na migongano hiyo:
Kuna migongano kadhaa ya kiimani kati ya Waislamu na Wakristo lakini nafsi hainiruhusu kuitaja/kuizungumzia yote. Hapa nitazungumzia eneo moja tu, ambalo binafsi ninalitafsiri kama ‘nyeti’ zaidi.
Kwa Wakristo, Yesu ni Mungu na pia mwana wa Mungu (yaani Utatu Mtakatifu wa Mungu.) Kwa Waislamu, ile kusema tu Mungu ana mtoto (achilia mbali mtoto huyo ni Nabii Issa bin Mariam, yaani Yesu) ni kufr. Hakuna njia ya mkato katika migongano huu, hasa kwa vile dini hizi mbili zinaongozwa na Maandiko Matukufu/Matakatifu tofauti, yaani Kuran Tukufu kwa Waislam na Biblia Takatifu kwa Wakristo. Laiti Waislam wangekuwa wanatumia Biblia kuchunguza imani ya Wakristo kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, na laiti Wakristo wangekuwa wanatumia Kuran kuchunguza kwanini kusema Mungu ana mtoto ni kufr, labda kungepatikana mwafaka wa namna flani.

Lakini kama ilivyo kwa sie wanafunzi wa stadi za siasa kuwekea mkazo zaidi kwenye siasa na sio Fizikia, ndivyo ambavyo Waislam wanawekea mkazo kwenye Kuran na Wakristo kwenye Biblia. Na huo ni wajibu kwa kila muumini.

Hata hivyo, kama ambavyo sie wanafunzi wa siasa kuna nyakati tunalazimika kuyaelewa maeneo mengine ya kitaaluma in relation to siasa, ndivyo ambavyo baadhi ya Waislam wanafanya jitihada ya kuuelewa Ukristo in relation to Uislam, na baadhi ya Wakristo kuuelewa Uislam in relation to Ukristo. Hata hivyo hao ni wachache.

Na kwa bahati mbaya (au makusudi), jitihada hizo za kusaka uelewa wa dini nyingine ‘zimetekwa’ na dhamira ‘mbaya’ ya ‘kutaka kumwelewa adui vizuri ili kumkabili vizuri pia.’ Kwa wanaofuatilia mihadhara ya ‘kashfa’ ya kidini watakuwa wameshuhudia namna wengi wa wahubiri wanavyotumia Biblia au Kuran kuonyesha kwanini Ukristo au Uislam sio dini sahihi.

Lakini ili kuepusha ‘overgeneralization’ (kuhitimisha mambo jumla jumla) ni muhimu kufahamisha kuwa wapo wanazuoni wachache wa Kiislamu wanaoisoma Biblia kwa minajili ya uelewa tu wa kidini (na si kupambana na Ukristo).Kadhalika, katika stadi za kidini za Kikristo kuna wachache wanaoisoma Kuran kwa minajili ya uelewa tu wa kidini.

Mgongano wa kiimani kati ya Waislam na Wakristo kuhusu “Yesu ni Mungu na pia Mwana wa Mungu” ulijidhihirisha zaidi katika kesi iliyomkabili mhadhiri mmoja wa Kiislam, Ustaadh Khamis Dibagula, ambaye mwaka 2000 alihukumiwa kwenda jela huko Morogoro kwa ‘kashfa’ ya kudai “Yesu si Mungu” kama wanavyoamini Wakristo.

Kipengele cha 19 cha Katiba yetu kinatoa uhuru wa kuamini dini yoyote (japo kinakumbushia umuhimu wa kufanya hivyo bila kuathiri sheria za nchi). Na kipengele cha 18 kinatoa uhuru wa kutoa maoni (pasipo kuathiri sheria za nchi.) Kwahiyo basi Kipengele cha 19 cha Katiba kilimruhusu Dibagula kuamini “Yesu si Mungu/Mwana wa Mungu”, na kipengele cha 18 kilimruhusu kueleza imani yake hiyo waziwazi.

Kwahiyo, kwa upande mmoja Katiba iliruhusu kutoa maoni ambayo kwa upande mwingine ni kashfa. Hili ni eneo hatari ambalo ninachelea kuingia kwa undani zaidi kwani hata huo migongano wa kisheria uliopelekea Dibagula kufungwa na hatimaye kuachiwa huru ni suala ambalo Waingereza wanaliita legal minefield (yaani uwanja wa kisheria uliotegwa mabomu).

Kwa kifupi, ufanisi wa Katiba katika suala hilo unategemea zaidi busara za waumini, hususan utashi kuwa “nikasema hili-japo ni sahihi katika imani yangu-nitakuwa ninamkwaza flani.” Lakini, kusema ni jambo moja na kuamini ni jambo jingine. Katiba inaweza kuzuwia kusema hadharani kuwa “Yesu si Mungu/Mwana wa Mungu” lakini haiwezi kuzuwia wanaoamini kuwa “Yesu si Mungu/Mwana wa Mungu.”

Na kwa vile sheria zinazotokana na Katiba yetu ndizo zilizomfunga Dibagula kwa ‘kashfa’ lakini baadaye zikamwachia huru, hatua hiyo inajenga taswira gani kuhusu Katiba yetu kama chombo kinachopaswa kulinda uhuru wa kuabudu na wa maoni?
Nini kifanyike?
  1. Tuukabili ukweli kuwa tuna matatizo. Badala ya kuwa na sensa zinazokwepa kutupa ufahamu wa uwiano wa kielimu na ajira kati ya Wakristo na Waislam, ni muhimu kuwa na njia za wazi za kufahamu ukubwa wa tatizo la inequality katika maeneo mbalimbali, na hili si kwa Waislam pekee bali hata makundi mengine ya jamii.
  2. Jitihada za makusudi zinahitajika kushughulikia matatizo hayo. Ugonjwa hauponi kwa kujidanganya kuwa haupo. Badala ya kuruhusu wanasiasa watumie manung’uniko ya Waislam kama mtaji wao wa kura (mfano ahadi feki za CCM kwa Waislamu kuhusu Mahakama za Kadhi na kujiunga na OIC), harakati za kiraia zikiongozwa na wanazuoni na wanataaluma wenye mtizamo wa kuleta maelewano badala ya mifarakano ziimarishwe.
  3. Jitihada za ndani na nje ya Uislam zinahitajika katika kuhamasisha maendeleo ya kielimu kwa Waislam. Malalamiko pekee hayawezi kuleta ufumbuzi. Kadhalika, ushirikiano kati ya Waislam na serikali na taasisi nyingine za kidini na kijamii ni muhimu iwapo itakubalika kuwa na affirmative action.
Mwisho, ninatambua tofauti zetu za kiimani. Busara inahitajika katika kudumisha imani zetu na wakati huo kutoa fursa kwa wenzetu kubaki na imani zao. Tuliweza huko nyuma, na tunaweza sasa na hata milele kuwa Watanzania kwanza kisha ndio tuangalie huyu Muislam au Mkristo, Mchagga au Mndamba, mwanamke au mwanaume, nk.

Adui yetu mkubwa ni umasikini unaotishia uhai wa nchi yetu bila kujali huyu ni Hamisi na yule ni John. Mafisadi wanaotafuna raslimali zetu na kuficha mabilioni huko Uswisi, visiwa vya Jersey, nk hawafanyi hivyo kwa vile wanawapenda Wakristo na kuwachukia Waislam (au kinyume chake), bali wanamnyonga kila Mtanzania pasi kujali dini yake.

Kama ambavyo umasikini wetu ni mtaji mzuri kwa maharamia wa kisiasa kununua kura ndivyo ambavyo utengano wetu wa kidini unavyokuwa turufu kubwa kwa wanasiasa mufilisi ambao kimsingi dini zao si Uislam au Ukristo bali ulafi wa kuifilisi nchi yetu hadi tone la mwisho.
UMOJA NI NGUVU UTENGANO NI UDHAIFU

11 Nov 2012


KATIKA matoleo mawili yaliyopita ya jarida hili maridhawa, safu hii imekuwa ikijadili vurugu za kidini zilizojitokeza hivi karibuni nchini.
Katika makala hii, nitaanza sehemu ya kwanza ya kuhitimisha mjadala huo (na sehemu ya pili ya hitimisho itakuwa katika toleo lijalo).Ni matarajio yangu kuwa mfululizo huu wa makala hizi utafungua mjadala mpana zaidi kuhusu hali ya dini nchini Tanzania, nafasi ya dini katika kujenga au kubomoa amani, na hatimaye mapendekezo ya nini kifanyike kudumisha umoja, upendo, amani na mshikamano miongoni mwetu.
Mwamko ulioonyeshwa na makundi mbalimbali ya kijamii katika kulaani na kuzungumzia suala hili unatoa picha chanya kuwa wengi wetu tunatamani kuiona Tanzania yetu ikiendelea kuwa “kisiwa cha amani” (japo neno ‘amani’ lina tafsiri pana, na linaweza kuzua mjadala mwingine mpya. Lakini kwa minajili ya mada hii, tuitafsiri amani kama hali ya utulivu na maelewano miongoni mwa jamii).
Katika makala zilizotangulia, nilijikita zaidi kubainisha sababu ambazo kwa uelewa wangu zilichangia kuleta vurugu hizo za kidini. Nimejaribu kurejea historia ya nchi yetu, kabla na baada ya uhuru, na kuonyesha sababu zilizozalisha manung’uniko ya Waislam, hususan katika maeneo makuu mawili ya upatikanaji (access) wa fursa ya elimu na ajira.
Kwa kuangalia michango mbalimbali ya wanajamii katika mjadala kuhusu vurugu hizo, moja ya hoja inayoonekana kupewa uzito mkubwa ni ile inayodai kuwa chanzo cha vurugu hizo si dini.
Naomba niweke bayana msimamo wangu kuwa binafsi ninazitafsiri vurugu hizo ZINA SABABU ZA KIDINI japokuwa si DINI PEKEE bali pia kuna mwingiliano wa sababu nyingine.
Ninachomaanisha hapa ni kwamba si kweli kuwa vurugu hizo hazihusiani kabisa na dini bali dini ni moja ya sababu za vurugu hizo.
Kwa kuwa katika makala zilizotangulia nimeelemea zaidi katika sababu hizo ‘zisizo za kidini kwa asilimia 100,’ katika makala hii ya mwanzo wa hitimisho nitajaribu kujadili ‘eneo hatari’ la dini kama moja ya chanzo cha vurugu hizo.
Ninasema ‘eneo hatari’ kwa sababu yayumkinika kuhisi kuwa baadhi ya wasomaji hawatopendezwa na uthibitisho nitakaoweka wazi, na ambazo ni lazima tuziongelee ili si tu tuweze kuwa na mjadala wa maana kuhusu suala hili, bali pia tuweze kuwa katika nafasi ya kusaka ufumbuzi.
Kama ilivyo mahala kwingineko (kwa maana ya si Tanzania pekee), uchambuzi kuhusu dini si tu unaweza kuzua hisia hasi (kama vile kuhisi mwandishi Mkristo haruhusiwi kukosoa Uislam, au kinyume chake), lakini pia unakabiliwa na tatizo la msingi la vigezo vingine vinavyoathiri dini husika, kama vile tofauti kati ya mjini na vijijini, idadi ya wakazi katika sehemu husika, historia ya sehemu husika, nk.
Kwa kifupi-na huu ni mfano tu-inaweza kuwa na ugumu wa namna fulani kuuchambua Ukristo kwa kutumia mikoa miwili ya Kilimanjaro na Kaskazini Pemba kama maeneo ya kupata takwimu za kuwezesha uchambuzi husika.
Wakati Kilimanjaro ina idadi kubwa ya Wakristo, Kaskazini Pemba ina idadi kubwa ya Waislamu. Tofauti hizo ‘zisipolindwa vema kwa kuzingatia kanuni za tafiti’ zinaweza kuzua matokeo ‘fyongo.’
Na suala hili la ‘vigezo vingine’ ni moja ya mambo yaliyojitokeza katika utafiti wangu kuhusu harakati za vikundi vya Kiislamu huko nyumbani.
Kwa mfano, baadhi ya wahojiwa wa Kiislamu katika jiji la Dar es Salaam walionekana kuwa na hamasa kubwa kuzungumzia ‘ubaguzi wanaofanyiwa na kile walichokieleza kama Mfumo Kristo,’ wengi wa wahojiwa katika ‘maeneo yasiyo ya mijini (rural areas) walionekana kuelemea zaidi kwenye kero zinazowakabili kila siku katika nyanja kama za afya, elimu na kilimo.
Hata mwanazuoni mmoja wa Kiislamu niliyefanya naye mahojiano alikiri kwamba, (namnukuu) “…kwa huko vijijini haya masuala ya udini hayana uzito kulinganisha na adha zinazowakabili wananchi katika maeneo hayo ambazo kimsingi hazibagui kuwa huyu ni Juma au Petro…”
Tukiweka kando ‘kikwazo’ hicho kinacholeta ugumu fulani katika kuchambua dini, moja ya mifumo (models) ya kuchambua vurugu (ziwe za kidini, kikabila, kisiasa, nk) unaonyesha hali hii (kwa mchanganuo wa jumla): ubaguzi huzua manung’uniko; manung’uniko huzua hamasa; hamasa huzua upinzani ambao waweza kuzua vurugu.
Na moja ya sababu za msingi zinazoelezwa katika model hiyo kuwa zinaweza kujenga hisia ya kubaguliwa ni kupotea kwa hali ya kujiendeshea mambo pasi kuingiliwa (autonomy).
Kufutwa kwa Mahakama za Kadhi kunaweza kuwa mfano mwafaka.
Japo mahakama hizo zilikuwa za kidini lakini kimsingi zilijitosheleza kushughulikia ‘kesi za kidini’ miongoni mwa Waislamu (yaani masuala kama mirathi, nk).
Lakini eneo jingine linaloweza kuingia katika kundi hili ni ushiriki wa baadhi ya Waislamu katika harakati za uhuru. Ushiriki huo haukuwa wa kisiasa tu bali wa kidini kwani moja ya mafundisho ya Uislamu katika kushughulikia jambo baya (kama udhalimu wa mfumo wa ukoloni) ni “kulikemea, kulichukia au kuliondoa” jambo hilo.
Kwa kutafsiri ushiriki wa Waislamu hao ulikuwa na msingi wa kidini (licha ya siasa), kujumuika kwao kuliwapa autonomy ya aina fulani, yaani kuweza kuitumia imani yao ya kidini kukabiliana na jambo baya (ukoloni).
Kama nilivyobainisha katika makala zilizotangulia, hisia kuwa “tulikuwa mstari wa mbele kupambana na mkoloni lakini uhuru ulipopatikana tumeishia kuwa chini ya wenzetu waliomsapoti mkoloni (kwa maana ya ukaribu kati ya ukoloni na Kanisa/ Ukristo)” zinaweza kutafsiriwa kama kupoteza autonomy hiyo.
Lakini pia ni muhimu kuelewa kuwa Uislamu si suala la imani pekee bali ni mfumo kamili wa maisha. Stadi zinaonyesha kuwa pindi mfumo wa kimaisha unapoonekana kuwa hatarini (kwa sababu moja au nyingine) inaweza kuleta mwamko wa kukabili tishio husika.
Kimsingi, dini hutoa mwongozo kwa muumini kuhusu maisha yake kibinafsi na katika jamii. Sasa tukiafikiana kuwa Uislamu kama dini na kama mfumo kamili wa maisha hauridhii aina yoyote ya uonevu, ni wazi hisia kuwa “Waislamu wanabaguliwa” zinaweza kufuata ile model ya ubaguzi – manung’uniko – hamasa – upinzani.
Pengine hili halitowapendeza baadhi ya wasomaji: katika utafiti wangu (na katika baadhi ya stadi nyingine) kuna uthibitisho wa kuwapo kwa vikundi vya Kiislamu vyenye mrengo mkali wa kiimani (Islamic extremists). Naomba ieleweke kuwa uwepo wa vikundi hivyo katika Uislamu haimaanishi kuwa mrengo mkali katika dini ni kwa Uislamu pekee.
Israel kuna Wayahudi wenye mrengo mkali kabisa ambao hawataki kabisa kusikia lolote kuhusu Wapalestina. Huko Marekani kuna Wakristo wenye msimamo mkali kabisa ambao kwa kiasi fulani wanachangia ‘uhasama’ kati ya taifa hilo na Waislamu na Uislamu kwa ujumla (kwa mfano Pasta Terry Jones aliyezua sokomoko duniani kwa kuchoma Kuran Tukufu).
Sasa kwa huko nyumbani, vikundi hivyo vya Waislam wenye msimamo mkali si tu ‘wameteka’ ajenda ya msingi ya manung’uniko (tunayoweza kuafikiana kuwa ni halali) ya Waislamu bali pia wamegeuza ajenda hiyo kuwa nguzo muhimu ya kupambana na wale wote wasioafikiana na mtizamo wao.
Wahanga wa ‘wana-msimamo mkali’ hawa si Wakristo pekee bali hata Waislamu wenzao wanaoonekana ‘kutokuwa na msimamo kama wao.’
Uthibitisho wa hii ni pamoja na vurugu zilizojitokeza nyakati fulani za uporaji wa misikiti. Japo wateka misikiti hao walidai kuwa wanairejesha kwa Waislamu misikiti iliyokuwa chini ya BAKWATA, kuna uthibitisho kuwa lengo lilikuwa kuigeuza misikiti hiyo kuwa ya ‘msimamo mkali.’
Badala ya hoja ya msingi inayohusu manung’uniko ya Waislamu dhidi ya mfumo wanauona kuwa unawakandamiza, vikundi vya Kiislamu vyenye msimamo mkali vinakwenda mbali zaidi kiasi cha kutaka kulazimisha kila mtu afuate imani yao (pasipo kujali ni Muislamu au la).
Uchambuzi wa wasifu wa baadhi ya viongozi wa vikundi hivyo unatoa picha ya waumini ambao ‘si washika dini kihivyo’ lakini ‘wenye hasira kali dhidi ya yeyote asiyeshika dini inavyostahili.’
Kwao, ‘kafir’ si asiye Muislamu tu bali hata Muislamu anayeshirikiana na wasio Waislamu (hata pale ambapo ushirikiano huo hauna madhara kwa Waislamu na dini yao).
Kuna tatizo jingine la msingi. Wakati kumekuwa na jitihada kubwa kwa Wakristo kutafsiri Biblia Takatifu kwa Kiswahili, yayumkinika kusema kuwa jitihada za kuitafsiri Kuran Tukufu kwa Kiswahili hazijaendelezwa vya kutosha.
Sasa, kwa vile ni rahisi kutumia Maandiko Matukufu/Matakatifu kuhalalisha au kuharamisha kitu fulani, kutoa fursa kwa watu wasio na uelewa wa kutosha wa maandiko hayo kuwa viongozi wa dini kunaweza kuwa na madhara.
Kwa uelewa wangu, ijtihad ni jukumu la wanazuoni wa Kiislamu, lakini kuna uthibitisho wa kitaaluma kuwa baadhi ya viongozi wa vikundi vya Kiislamu vyenye msimamo mkali wamejipachika jukumu hilo na kufanya tafsir (exegesis au tafsiri) katika minajili inayoendana na ajenda/matakwa yao (ya ‘msimamo mkali.’)
Japo katika Uislamu ni vigumu kuchora mstari unaotenganisha dini na siasa, tofauti na kwenye siasa ambapo mwananchi yeyote yule anaweza kuwa mwanasiasa, kwenye dini ni tofauti, kwani uelewa wa dini (kwa maana ya maandiko, sheria, nk) ni kigezo muhimu cha kuwa na mamlaka ya kuwaongoza waumini wengine.
Katika toleo lijalo, makala ya mwisho wa mfululizo huu itaangalia vikwazo vya ndani ya Uislamu kupata ufumbuzi wa manung’uniko yao; baadhi ya migongano ya kiimani kati ya Waislamu na Wakristo, na ‘utata’ katika Katiba kuhusu migongano hiyo; mapendekezo ya nini kifanyike kukabiliana na vurugu za kidini huko nyumbani.
ITAENDELEA


10 Nov 2012


4 Nov 2012


28 Oct 2012


KABLA ya kuingia kwa undani katika makala hii ambayo ni mwendelezo wa makala iliyochapishwa katika toleo la wiki iliyopita, naomba niwasimulie wasomaji mkasa ambao unaweza kuwa “funga kazi” katika utitiri wa vimbwanga vya watawala wetu.
Wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, aliwatia aibu Watanzania akiwa Afrika Kusini alipodai kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaundwa kwa Muungano kati ya kisiwa cha Bahari ya Hindi cha Pemba na Zimbabwe. Ukidhani ninamsingizia, basi angalia video hii kupitia kiunganishi hiki; http://goo.gl/uW6H2
Na licha ya kufanya madudu hayo, Mulugo ‘alilikoroga’ zaidi alipodai kuwa Muungano huo wa ‘Zimbabwe na Pemba’
ulitokea mwaka, (namnukuu) “one nineteen sixty-four.” Mwaka huo hauleti maana yoyote, iwe kwa Kiingereza au kwa Kiswahili, kwani 1-19-64 inaweza tu kuleta maana kwa mfumo wa tarehe wa Marekani (yaani tarehe 19 mwezi wa kwanza mwaka 64).
Ninaomba nitamke bayana kuwa Naibu Waziri Mulugo ni mzembe wa hali ya juu. Yawezekana aliandaliwa hotuba hiyo, lakini haihitaji busara japo kidogo kuwa huwezi kukurupuka kutoa hotuba kabla hujaipitia. Sijui Rais Jakaya Kikwete alijisikiaje baada ya kuona video hiyo yenye hotuba ya Mulugo, lakini kwa kosa hilo la ajabu kabisa, Naibu Waziri Mulugo sio tu anapaswa kutuomba radhi Watanzania kwa kupotosha historia ya taifa letu bali pia ingefaa aondolewe katika wadhifa wake unaoshughulikia elimu (elimu gani hiyo ambayo wakati Tanzania ‘haijamalizana’ na Malawi kuhusu mpaka kwenye Ziwa Nyasa, yeye ‘anaihamasisha Zimbabwe ‘idai Pemba ni sehemu ya nchi hiyo?’)
Nisiongelee sana suala hilo bali ninawaachiwa Watanzania wenzangu kuhitimisha wenyewe kuhusu madudu haya ‘ya karne.’
Kama nilivyoahidi katika toleo lililopita, wiki hii ninaendelea na mjadala kuhusu vurugu za kidini ambazo kwa siku za karibuni zinaonekana kushika kasi.
Katika makala iliyopita, nilijaribu kuonyesha sababu zilizojenga msingi wa manung’uniko ya Waislamu katika masuala ya elimu na ajira. Mwishoni mwa makala hiyo niliuliza maswali yafuatayo (ninajinukuu)
“Je; kilichotokea Mbagala ni hasira tu za baadhi ya Waislamu waliochukizwa na kitendo cha ‘mtoto wa Kikristo’ kukojolea Kuran Tukufu?
Je; udini ni tatizo kubwa katika Tanzania yetu ingawa halizingumzwi vya kutosha? Binafsi, ninaamini jibu la swali hilo, ni ndiyo. Kama ni ndiyo, kwa nini tunalikwepa tatizo hili?
Je; yawezekana udini ni turufu muhimu kwa baadhi ya wanasiasa mufilisi?”
Kwa swali la kwanza, nilishabainisha kwenye makala hiyo kuwa kwa mtizamo wangu, vurugu hizo za Mbagala zilisababishwa na zaidi ya hasira za baadhi ya Waislamu waliokasirishwa na kitendo cha mtoto kuikojolea Kuran Tukufu.
Yayumkinika kusema kuwa hasira za baadhi (na pengine ni wengi) ya Waislamu huko nyumbani (Tanzania) ni dhidi ya kile kinachotajwa kama ‘Mfumo Kristo.’ Kwa kifupi, wanaoamini hivyo wanauona mfumo huo unawapendelea Wakristo sambamba na kuwabagua Waislamu, hususan katika sekta za elimu na ajira, ambazo kimsingi zinahusiana kwa karibu.
Japo, kama nilivyobainisha katika makala yangu iliyopita kuwa Ukristo kwa kushirikiana na ukoloni ulichangia kutengeneza hali ya kutokuwa na usawa katika elimu na ajira, haimaanishi moja kwa moja kuwa Wakristo wanawabagua Waislamu. Naomba nieleweke hapa: kuna tofauti kati ya mfumo na watu wanaonufaika au kuathiriwa na mfumo huo.
Ninasema hivyo kwa sababu, wakati hoja ya kuwa Wakristo wanawabagua Waislamu ingeweza kuwa na mashiko wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa, ambao wote ni Wakristo, ni vigumu kwa hoja hiyo kuwa na uzito kwenye Awamu ya Pili na hii ya sasa (ya Nne) za marais Waislamu Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete.
Hata hivyo, kwa mtizamo wangu, viongozi hao wote wanne, hawawezi kukwepa lawama kuwa kwa kiasi kikubwa hawajafanikiwa sio tu kuyatupia macho kwa makini malalamiko ya Waislamu bali pia wamekuwa wakikwepa kuyashughulikia kwa uzito unaostahili.
Angalau kwa upande wa Baba wa Taifa tunaweza kukubaliana kuwa sio tu kwamba alishakiri kuwa kukosekana kwa usawa katika elimu na ajira kwa Waislamu ni tatizo, lakini pia alikwenda mbali zaidi na kujaribu kuukarabati mfumo wa elimu ili uweze kutoa fursa kwa Watanzania wote bila kujali imani zao.
Ni muhimu kukumbuka kuwa licha ya ukweli kuwa Mwalimu alikuwa Mkristo na mshika dini, mafanikio yake katika harakati za kupigania uhuru yalichangiwa zaidi na Waislamu.
Lawama ‘kubwa’ inayoweza kuelekezwa kwa Mwalimu ni jinsi serikali yake ilivyoshughulikia suala ‘nyeti’ la uundwaji Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na kupigwa marufuku Jumuiya ya Ustawi wa Waislamu wa Afrika Mashariki (East African Muslim Welfare Society- EAMWS).
Kwa kifupi, tangu kuundwa kwake, kwa kiasi kikubwa BAKWATA imeshindwa kujitenganisha na serikali, na pia imeshindwa kufuta hisia kuwa ‘ni chombo kinachotumiwa na serikali kuwagawanya na kuwakandamiza Waislamu.’
Japo EAMWS ilikuwa taasisi ya kidini lakini ilionekana kama ‘mkombozi wa Waislamu’ hususan kwenye sekta ya elimu, na yayumkinika kusema kuwa laiti kuundwa kwa BAKWATA kungeibua taasisi yenye ufanisi kama EAMWS, basi pengine pengo lililopo kwenye maeneo ya elimu na ajira kati ya Waislamu na Wakristo lingekuwa limepungua kwa kiasi kikubwa.
Ufinyu wa nafasi unaninyima fursa ya kuingia kwa undani kujadili hoja za kuifungia EAMWS na hatimaye kuanzisha BAKWATA, lakini ukweli kwamba serikali hiyo hiyo iliyoipiga marufuku EAMWS ilishiriki kikamilifu katika uundwaji wa BAKWATA umechangia kudumu kwa hisia kuwa ‘BAKWATA iliundwa kama chombo cha serikali dhidi ya Waislamu.’
Na katika utafiti wangu, matokeo ya awali yanaonyesha Waislamu wengi hawaridhishwi na mwenendo wa BAKWATA katika kutetea maslahi yao. Kimsingi, moja ya jambo lilionekana ‘kuwaunganisha’ wahojiwa wangu wa Kiislamu (ambao nilieleza katika makala iliyopita kuwa niliwagawanya katika makundi mawili ya ‘walio na msimamo mkali’ na ‘wa kawaida’- kwa minajili ya kiutafiti- ni suala hilo la BAKWATA.
Sasa katika mazingira haya ambacho chombo pekee kikuu kinachotarajiwa kuwaunganisha Waislamu kinaonekana kuwa kinawakandamiza, na-kuwanukuu baadhi ya wahojiwa- ni sehemu ya ‘Mfumo Kristo’ ni wazi kuwa baadhi (na pengine wengi) ya Waislamu wanajiona kama ‘mateka wa mfumo,’ kwa maana ya hisia za kubaguliwa na Wakristo na kubaguliwa na chombo kinachopaswa kutetea maslahi yao (BAKWATA).
Kwa mtizamo wangu, kuwa ‘mateka wa mfumo usiokubalika’ kunasababisha kuuchukia, na kama tujuavyo, chuki huzaa hasira. Hasira hizo zinasubiri mazingira ‘mwafaka’ ili zichomoze hadharani. Na tukio kama la Mbagala lilitoa ‘fursa mwafaka’ kwa hasira hizo.
Na ‘hasira’ hizo zinatoa jibu la swali la pili kuhusu udini. Kwamba Waislamu wanawachukia Wakristo, sitaki kuamini hivyo. Kwamba Waislamu (baadhi au wengi) wanachukizwa na mfumo wanauona kuwa unawabagua na kuwapendelea Wakristo, binafsi jibu langu ni ndio.
Na kwa vile ni vigumu kutofautisha ‘Mfumo Kristo’ na Wakristo kama waumini wa dini, ni muhimu kutambua kuwa kwa namna fulani-kubwa au ndogo- kuna uhasama wa kisaikolojia au kihisia kati ya madhehebu haya mawili. Kinachosaidia ‘kuficha’ uhasama huo ni misingi iliyojengwa huko nyuma ambayo ilisisitiza zaidi Utanzania wetu kuliko Uislamu au Ukristo wetu.
Kwa bahati mbaya-au makusudi-misingi hiyo inavunjwa kwa nguvu na wanasiasa waliokuja baada ya Mwalimu Nyerere. Kwa kifupi, wakati siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ilijenga misingi ya kutuunganisha Watanzania tuwe kitu kimoja, ‘ubabaishaji’ uliofuatwa-kwa mfano kinachoitwa Azimio la Zanzibar- umechangia sana kukuza ombwe lililotokana na ‘kifo cha Ujamaa,’ na wakati huo huo kutoa fursa kwa wenye ‘hasira’ zao kuziweka hadharani.
Kama nilivyowahi kuandika katika makala moja huko nyuma kuhusu unafiki wetu kuhusu suala la ushoga (hoja kubwa ikiwa ni imani zetu za kidini na mila na desturi zetu), kuna unafiki unaoendelea katika sio tu kuzungumzia suala la udini kwa uwazi zaidi bali pia hakuna utashi wa kisiasa (na hata kijamii) kukabili tatizo hili.
Ni nani asiyejua kuwa wakati wa utawala wa Mwinyi kulikuwa na baadhi ya Wakristo waliokuwa wakinung’unika chini chini kuwa teuzi za Mwinyi zilikuwa zinapendelea Waislamu? Ni nani pia asiyejua kuwa alipokuja Mkapa lawama kama hizo ziliendelea kuwapo chini chini kuwa Mkapa alikuwa akiwapendelea Wakristo? Na ni nani atakayejifanya hajui kuwa utawala wa Rais Kikwete umekuwa ukilaumiwa chini chini kuwa unawapendelea Waislamu?
Ninafahamu kuna watakaosema hizi ni hisia zangu tu. Hawa ndio ninaowaita wanafiki. Na unafiki huu ndio miongoni mwa vikwazo vikubwa vya kujadili tatizo la udini, na vurugu zinazohusishwa na tatizo hilo, kwa hofu ya kuitwa mdini. Niseme hivi, bora niitwe mdini kwa kujitoa mhanga kuanzisha mjadala wa suala hili kuliko ‘nionekane mwema’ ilhali tunalipeleka taifa letu mahali kusikofaa.
Nitajitahidi kuhitimisha mfululizo wa makala hizi kuhusu vurugu za kidini kwenye toleo lijalo, au pengine makala mbili zijazo. Hata hivyo, nihitimishe makala hii kwa jibu fupi kwa swali la tatu kuhusu udini unavyotumiwa na wanasiasa mufilisi kwa minajili yao binafsi.
Ninaamini sote tunakumbuka jinsi kampeni za uchaguzi mkuu uliopita zilivyogubikwa na tuhuma za udini. Na hapa nisiume maneno: chama tawala CCM kilifanya kila jitihada kuufanya ‘upadri’ wa mgombea wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, kuwa turufu muhimu ya kumnyima kura za Waislamu. Hili nitalijadili kwa kirefu katika makala ijayo, lakini kwa namna fulani, CCM haiwezi kukwepa lawama kuwa ni miongoni mwa vyanzo vya vurugu za kidini tunazoshuhudia hivi sasa.
Chama cha siasa kinapoamua kwa makusudi kuwagawa wapiga kura kwa misingi ya imani zao za kidini, kinaandaa ‘viungo’ kwa ajili ya vurugu za kidini. Na ikumbukwe kuwa ni CCM hii hii iliyowahadaa Waislamu kuhusu kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi (huku ikitambua kuwa haina dhamira ya dhati ya utekelezaji wa ahadi hiyo) na hadi sasa inaendelea kucheza danadana katika suala hilo.
Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa tuna kila kitu cha kupoteza (everything to lose) kwa kutengana kwa misingi ya kidini na hatuna cha kupoteza (nothing to lose) tukiendelea kuwa wamoja, kama majeruhi wa ufisadi, umasikini, magonjwa na dhahma nyingine zinazotukabili ambazo hazijali imani zetu za kidini. Ili Tanzania yetu ifike mahala tunapotamani ifike, au inapostahili kuwa, ni lazima tuwe kitu kimoja. Tukumbuke, UMOJA NI NGUVU NA UTENGANO NI UDHAIFU
Makala hii itaendelea toleo lijalo


22 Oct 2012



                                                    ALCOHOLISM AND EFFECTS
            POMBE NA MADHARA
                Lets check why many people change characters baada ya kulewa pombe na pombe hufanya nini mwilini mwa binadamu anapozitumia? mili yetu iliumbwa kwa ajiri ya kujiponya yenyewe endapo tu utakuwa unakula vizuri na nikisema kula vizuri haimaanishi ule ushibe hapana bali ninamaanisha ule chakula bora chenye lishe bora,rutuba ambazo ni vitamins na minerals zinazoweza kulinda na kurutubisha mwili na automatically or kujiponya naturally na upungufu wa rutuba mbali mbali mwilini ndo huleta matokeo ya watu kuumwa pasipo kupona ama kuumwa magonjwa kama presha, kisukari cancer,donda ndugu,kumea vinyama usoni malaria na typhoid za mara kwa mara,liver and kidney failure n.k na kuyaita haya magonjwa kama ni magonjwa yasiyo tibika ama magonjwa sugu kwa mimi i agree to dis agre na kwa uwezo tulio nao wa kufikiri je huwa unauhudumia mwili kama linavyohudumiwa gari?

            kwa kuwa endapo ingekuwa hivyo binadamu wote wangeweza kuishi hadi miaka 85 ndo waanze kuzeeka kama jinsi ilivyo kwa wajapani lakini tunaenda kinyume na haya yote, hebu jiulize je utaweza kuweka maji kwenye engine ya gari ama chumvi badala ya petroli? haiwezekani na hii ni kwa kuwa gari halina uwezo wa kujisafisha lenyewe na kujiponya na ndo maana huwa tunalipeleka service je sisi huwa tunajifanyia service ama body detoxination? (kuodoa sumu mwilini na uchafu usiohitajika mwilini?)

         So look at how our amazing bodies does mara nyingi huwa hatuwezi kuona emediet effects za pombe,sumu mwilini au effects za vyakula na aina ya madawa tunayotumia kwa kuwa miili yetu ili unbwa kwa ajiri ya kujiponya na kujiendesha yenyewe na ndo maana sumu haziwezi kuathiri mwili kama ambavyo ungeweka chumvi kwenye gari badala ya mafuta huwa effects zake zinajijenga taratibu na kufikia kikomo ama viungo vya kuchujia na kusambazia vitamins sahihi na minerals kukwama ambavyo mara nyingi viungo hivi viki collapse huwa very dangerous na viungo hivi ni ini na figo ambapo si tu hutumika kuchuja vilivyo vibaya na visivyo hitajika mwilini pia hutumika kwa kuvisambaza na kuvipeleka mahala husika panapohitaji certain type of vitamins and minerals so just imagine hivi viwili vikipata damage tge body suply inakuwa je?

          kwa leo nitaishia hapo juu ya vungo hivi viwili as we go on nitaendelea kuwafahamisha zaidi but today ninazungumzia pombe huwa inafanya nini mwilini hadi wengine huonekana kama wanamatusi,wakorofi na wakati mwingine kutojitambua na ni kwa sababu gani watu dini mbali mbali huzikemea! the thing is pombe si mbaya but kilicho kibaya ni vile pombe inavyo damage mwili wako na kutake control of everything when ever your drunk your life,dignity, behaviour and how you think and make desicions na hata waelimishaji wa masuala ya VVU/Ukimwi husisitiza sana watu kutokuwa walevi kwa kuwa pombe yaweza sababisha ulewe na kuamua kuwa na mwanamke au mwanaume na kufanya ngono zembe ama ngono pasipo kutumia kinga, na pia waweza kumchukua  mtu ambaye laiti ungekuwa mzima usingeweza hata kuongozana nae katika hali ya kawaida lakini kwa kuwa umekunywa pombe it was easy hadi kwenda kufanya naye mchezo mbaya kwa maana hiyo pombe hupunguza kudhoofisha ama kuua uwezo wako wa kufikiri na unakuwa poor decision maker.
               MADHARA KWA MWANAMKE MJAMZITO
     Kwa mwanamke mjamzito anayekunywa mara kwa mara pombe inaweza kumsababishia mtoto kuzaliwa taahira,inaweza ikasababisha kutoka kwa ujauzito (miscarriage) ama ikasababisha kudmaa kwa mtoto na asiweze kukua hata akiwa tumboni na baadae ikasababisha hyperactivity and irritability in the child, if a pregnant woman consumes alcohol on a regular basis (as well as drugs) the fetus can become addicted to these substances,
         Pia alcohol ni substance ambayo hutumia vitamins na minerals nyingi mno toka mwilini kwa ajiri ya kujiendesha ama umeng'enyukaji wake na kama pombe ikikuta hakuna vitamins na madini ya kutosha mwilini huwa inatabia ya kwenda kuchukua zile vitamins zilimo kwenye Tissue mwilini ambazo tissue hizi huwa katika damu na ndo husababisha kasoro nyingi za mwilini na kuleta matokeo ya kudhoofu kwa mwili na kuanza kuumwa ovyo ovyo.

               Mazingira sababishi juu ya wanywa pombe ni
Stress,Kazi,Kula bata na washkaji ama kunywa tu na marafiki pombe kwa kuwa compan yako yote wanakunywa,depression(mawazo) kujitenga, immaturity/foolish age kwa kudhani usipokunywa utaonekana haujakua bado ama hutoonekana ni kijana wa kisasa zaidi, loneliness (upweke) and Heredity
               Madhara mengine ya matumizi ya pombe ni
1.In the Pancreas (acute Pancreatistis)
2.In the liver (cirrcohosis) kwenye Ini kupunguza ufanis wa
kufanya kazi laweza pia kuvimba ama kujaa maji

3.In the Heart (kwenye moyo) kuvimba,kujaa maji, n.k

4.In the urinary system( kwenye njia ya mkojo na ndo maana huona wakati mwingine walevi huwa wanajikojolea kwa kuwa hata nerves zao huwa kama disconnected na mtu wa namna hii anaweza ahisi kitu ama kwa wanaume anaweza akashindwa kufanya tendo la ndoa kwa kuwa hakuna hisia tena ama mzunguko wa damu haui mzuri na kupeleka taarifa kwenye ubongo kwa kuwa pombe huua oksijen inayosaidia mzunguko huo wa damu na kuzidisha ufanisi wa nerves sytem

5.In the skin kudhoofisha ngozi
6.In the sexual organs (causing impotence) kupunguza uwezo wa tendo la ndoa haswa kwa wanaume
7.In the gastrointestinal and digestive tracts, kupunguza uwezo wa usagaji chakula na kusababisha gesi nyingi kila wakati hata kama hujala chakula huwa kama umeshiba na kukata hamu ya kula.

8.In the nervous sytem which can become completely unsettled by the death of cells,hii ni kwa kuwa pombe huwa inaondoa maji kwenye these cells producing a series of nervous disoders  which are frequently reflected in a sign depression and anxiety which in extreme cases can lead to delirium trements causing hallucinations ama kuweweseka,


So kwa wale wanaopata tatizo la  hang over baada ya kunywa ama kama unataka kukata pombe na unawahi meeting ama ofisini waweza call 0753 32 0009 ili kupata kujua jinsi ya kuepukana ama kudhibiti hali hiyo.

Na kwa wale wanaotaka kufanya detoxination ama kufanya miili yao service na kuondoa sumu mwilini Tafadhari call 0753 32 00 09 Mtu ni afya

19 Oct 2012
























































Picha zote kwa hisani ya Blogu ya AUDIFACE JACKSON

18 Oct 2012


KWA mara nyingine, wiki iliyopita Tanzania imeshuhudia ‘sura mbaya’ (ugly face) ya imani ya kidini. Kwa mujibu wa taarifa zenyewe, kilichoanza kama mchezo wa watoto kilisababisha vurugu kubwa zilizopelekea makanisa zaidi ya matano kuchomwa moto, sambamba na uharibifu wa mali kadhaa.
Inaelezwa kwamba chanzo cha vurugu hizo ni kitendo cha mtoto mmoja kuikojolea Kuran Tukufu baada ya ‘mabishano ya kitoto’ na mtoto mwenzie. Habari zinasema mtoto aliyefanya kitendo hicho alitaka kuthibitisha ukweli wa ‘tishio’ alilopewa na mtoto mwenzie kuwa iwapo atakikojolea Kitabu hicho Kitukufu, basi atageuka nyoka!
Sote tuliwahi kuwa watoto katika hatua za mwanzo za maisha yetu, na kwa kutumia uzoefu huo kama ‘watoto wa zamani’ tunaweza kukumbuka vitu vya ajabu, vya kukera, vya kuchekesha, na vya kila aina ambavyo twaweza kuvihitimisha kwa msemo huu wa Waingereza: ‘kids will always be kids’ (watoto wataendelea kuwa watoto).
Kwamba binadamu, pasipo kujali umri wake, anaweza kukojolea Kitabu Kitukufu cha dini fulani, ni jambo lisilopendeza hata kidogo. Na kwa hakika, kitendo cha aina hiyo, kitamchukiza kila muumini wa dini husika. Lakini kama ilivyo katika maeneo mengine ya maisha ambapo umri unaangaliwa kama kigezo muhimu cha kuhukumu tendo, ukweli kwamba aliyekojolea Kuran Tukufu ni mtoto wa miaka 14, ulipaswa kupewa uzito na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislam ambao waliamua kuchukua sheria mkononi kwa kufanya vurugu kubwa ikiwa ni pamoja na kuchoma moto makanisa.
Licha ya kuguswa na tukio hilo la kusikitisha kama Mtanzania na Mkristo, lakini pia nimeguswa kwa vile linahusiana na eneo ambalo nimekuwa nikihangaika nalo kitaaluma kitambo sasa. Miaka michache iliyopita, nilikuja huko nyumbani kukusanya data kwa ajili ya utafiti wa kitaaluma kuhusu harakati za vikundi vya Kiislam nchini Tanzania. Kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu, utafiti huo bado haujakamilika japo katika hatua niliyofikia unaweza kutoa majibu fulani kuhusu kinachoendelea huko nyumbani hivi sasa.
Nilipata fursa ya kuzungumza na makundi makuu mawili ya waumini wa dini ya Kiislam. Wale tunaoweza kuwaita ‘wenye msimamo mkali’ na wale wa ‘wenye msimamo wa kawaida.’ Naomba nisisitize kuwa matumizi ya maneno ‘msimamo mkali’ na ‘kawaida’ ni kwa minajili ya mjadala tu. Ninatoa tahadhari hii mapema kwa kuchelea uwezekano wa shutuma kuwa ninawagawa Waislam katika makundi, ambayo kama ilivyothibitika katika utafiti wangu, wengi wao hawapendi mgawanyo wa aina hiyo kwani wanaamini wote ni Waislam.
Moja ya mambo yaliyojitokeza katika mahojiano yangu na ‘makundi’ yote mawili ni manung’uniko (grievances) ambayo yamedumu kwa muda mrefu. Manung’uniko hayo yameshamiri zaidi kwenye suala la usawa katika elimu na ajira. Wahojiwa wengi walionyesha kuwa na hisia ya kubaguliwa kati yao na Wakristo katika upatikanaji wa fursa za elimu na ajira. Kimsingi, ukimnyima mtu fursa ya elimu, unatengeneza mazingira ‘mazuri’ ya kumkwaza kupata ajira.
Takwimu mbalimbali nilizokusanya katika utafiti huo, zinaweza kusapoti madai hayo. Lakini la muhimu zaidi hapa si sapoti ya takwimu hizo, bali mazingira yaliyopelekea uwepo wa hali hiyo. Kutokana na ufinyu wa nafasi ninalazimika kutoa maelezo ya jumla kwani kupitia kipengele kimoja hadi kingine kunahitaji zaidi ya makala moja.
Kwa kifupi, moja ya sababu zilizopelekea ‘ubaguzi’ katika upatikanaji wa fursa za elimu na ajira kati ya Waislamu na wasio Waislam (hususan Wakristo) ni mfumo wa utawala wa kikoloni. Kama tunavyofahamu, wakoloni walikuwa Wakristo, na tunafundishwa kwenye somo la historia kuwa miongoni mwa ‘watangulizi wa ukoloni’ walikuwa wamisionari wa Kikristo.
Moja ya mbinu zilizotumiwa na wamisionari kutengeneza mazingira mazuri ya kutawala jamii za Kiafrika ni ‘kusilimisha,’ japo neno hilo lina maana zaidi kwenye Uislam. Ninalitumia hapa kwa maana ya kuwatoa watu kutoka katika imani yao ya awali na kuwaingiza katika imani mpya.
Lakini historia inatufundisha kuwa Uislam ulifika huko nyumbani karne kadhaa kabla ya Ukristo. Kwa bahati mbaya au makusudi, walioleta Uislam walikuwa wafanyabiashara kutoka Arabuni na Mashariki ya Mbali, na hawakuwekea mkazo sana kusambaza dini yao.
Yayumkinika kuhitimisha kwamba kushindwa kwa watangulizi hao wa Uislam kueneza dini hiyo miaka kadhaa kabla ya ujio wa Wamisionari na hatimaye wakoloni, kulichangia kurahisisha kusambaa kwa Ukristo kwa ama ‘kusilimisha’ Wapagani (ninatumia neno hili kumaanisha dini za asili za Kiafrika) na Waislam.
Tukifupisha historia, mkoloni alitumia Ukristo kama moja ya njia za kuzitawala jamii zetu. Ni katika mazingira hayo, stadi mbalimbali zinaonyesha kuwa kwa namna fulani baadhi ya Wakristo walichelea kuunga mkono mapambano dhidi ya mkoloni kudai uhuru wetu hasa kwa vile wakoloni walifanikiwa kwa kiasi fulani kuulinganisha ukoloni na Ukristo (yaani kumpinga mkoloni ni sawa na kumpinga Yesu/Mungu).
Kwa kutumia Ukristo kama njia ya kurahisisha utawala wao, wakoloni pia walitumia dini hiyo kama chombo cha kuwatenganisha watawaliwa. Kimsingi, kuna aina ya mwafaka wa kitaaluma kuwa si kwamba wakoloni waliwathamini sana Wakristo wa Kiafrika, bali waliwaona kama nguzo muhimu katika kuigawa jamii, na hivyo kuwarahisishia kiutawala jamii husika.
Ingawa kuna wamisionari waliokuja Afrika kwa minajili ya kidini halisi, wengi wao waliendelea kushirikiana na utawala wa kikoloni katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utoaji elimu. ‘Ushirika’ huu wa wamisionari na wakoloni katika utoaji elimu, unaweza kuelezewa kama mwanzo wa ujenzi wa tabaka la Wakristo wenye elimu na ‘wasio Wakristo’ (hususan Waislam) wasio na elimu.
Kadhalika, baadhi ya Waislam walichelea kujiunga na taasisi za elimu za wamisionari/wakoloni kwa kuhofia kuingizwa katika dini hiyo (Ukristo). Tukiweka hali ilivyokuwa kabla ya uhuru, mazingira yaliyojitokeza baada ya kuondoka mkoloni, yameendelea kwa kiasi fulani kurutubisha ‘ubaguzi’ huo wa elimu na ajira.
Baada ya kupata uhuru, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alikiri hadharani kuwa kuna umuhimu wa kurekebisha hali ya kutokuwapo usawa wa kielimu kati ya Wakristo na Waislam. Licha ya jitihada zake kubwa, hadi anaondoka madarakani ‘usawa’ huo haukuweza kufikiwa kwa kiwango cha kuridhisha.
Kuna maelezo mengine hapa. Shule za seminari za Wakristo ambazo kimsingi ni maalum kwa ajili ya ‘kuzalisha’ viongozi wa makanisa, zilikuwa ‘zikizalisha’ kundi la wasomi wa Kikristo ambao kwa sababu moja au nyingine, hawakuishia kuwa viongozi wa kanisa, bali wakachukua ajira serikalini au kwenye taasisi nyingine. Kwa upande mwingine, shule za kidini za Waislam ziliegemea zaidi kwenye utoaji elimu ya kidini, na katika mazingira hayo, tofauti na ilivyo kwa seminari, ‘hazikuzalisha’ wasomi wa kutosha kuingia kwenye ajira serikalini (naomba nieleweke kwa makini hapa).
Kwamba utawala wa Mwalimu Nyerere uliwapendelea Wakristo na kuwabagua Waislam, ni jambo ambalo halijathibitika kitaaluma. Hoja hiyo ni miongoni mwa masuala yanayojenga manung’uniko kwa baadhi ya Waislam. Kwamba baadhi ya Wakristo, hususan waliotoka seminari na kujiunga na ajira serikalini, waliwabagua Waislam na kuwapendelea Wakristo, ni jambo ambalo halijathibitika kitaaluma ingawa linawezekana kinadharia na kimantiki.
Kimsingi, tatizo si ubaguzi wa msomi/mwajiri Mkristo dhidi ya mwanafunzi/msaka ajira Muislam, bali mfumo ambao ulijengeka wakati wa ukoloni na umeendelea kuwepo. Unatoa nafasi (on merit) kwa Wakristo zaidi ya Waislam. Kama mwajiri anataka kujaza nafasi kwenye ofisi yake, anapaswa kuangalia, pamoja na mambo mengine, sifa za kitaaluma za waomba kazi. Sasa kwa vile mfumo wa elimu tuliorithi kwa mkoloni, na kama nilivyobainisha hapo juu, unatengeneza wasomi wengi wa Kikristo kuliko wa Kiislam, ni dhahiri kutarajia ‘ubaguzi’ wa nafasi za ajira.
Majuzi tumefanya sensa. Watawala wetu wamegoma kujumuisha kipengele cha dini kwa madai mbalimbali. Lakini kwa kufanya hivyo, watawala wanajinyima fursa ya kuelewa, kwa mfano uwiano wa ajira kati ya Wakristo na Waislam. Na cha muhimu hapo si kuelewa tu, bali pia kutafuta namna ya kurekebisha hali hiyo. Na hili ni tatizo la msingi linalofanya ‘tatizo la dini’ kuendelea kuwapo. Kuna hisia kwamba kwa kujaribu kulizungumzia suala hili kwa uwazi, kutazua tafrani kubwa kuliko mwafaka. Lakini sote tunajua kuwa ugonjwa hautibiki kwa kujidanganya kuwa haupo mwilini!
Je; kilichotokea Mbagala ni hasira tu za baadhi ya Waislam waliochukizwa na kitendo cha ‘mtoto wa Kikristo’ kukojolea Kuran Tukufu? Binafsi, naamini kuna sababu za ndani zaidi ya ‘hasira’ hizo na zinazosababisha ‘hasira’ hizo. Je; udini ni tatizo kubwa katika Tanzania yetu ingawa halizingumzwi vya kutosha? Binafsi, ninaamini jibu la swali ilo, ni ndiyo. Kama ni ndiyo, kwanini tunalikwepa tatizo hili?
Jibu linaweza kupatikana kwenye tatizo jingine ‘lisilozungumzika’ la kero za Muungano wa ‘Tanganyika’ na Zanzibar. Kwa kifupi, hadi sasa hakuna utashi wa kisiasa na kijamii kulikabili tatizo hili. Kwenye Muungano, kila Rais anachelea kuvunjikiwa na Muungano, ambao Baba wa Taifa ‘alishatoa radhi’ kwa atakayeuvunja. Kwenye hili la udini, viongozi wetu wanakwepa kulikabili kwa kuchelea kuonekana wadini. Kibaya, baadhi yao walitumia udini kwenye kampeni za uchaguzi mkuu uliopita. Je; yawezekana udini ni turufu muhimu kwa baadhi ya wanasiasa mufilisi?
Makala hii itaendelea wiki ijayo.




12 Oct 2012


MIONGONI mwa faida ninazopata kutokana na uandishi wa makala katika jarida hili maridhawa, ni mawasiliano ya kila wiki na baadhi ya Watanzania wenzangu. Wengi wa ninaowasiliana nao, ni wasomaji ambao kwa namna moja au nyingine huwa wameguswa na mada ninazoongelea. Kuguswa huko hufuatiwa na ama pongezi au kukosolewa. Wakati mara nyingi pongezi huandamana na maneno ambayo si tu yananipa moyo na ujasiri zaidi wa kuendelea na uandishi wa makala hizi, mara nyingi kukosolewa huambatana na maneno yasiyopendeza kuyasoma au kuyasikia popote pale.
Baadhi ya wanaopongeza safu hii hudiriki kwenda mbali zaidi na kushauri labda nifikirie kuingia kwenye siasa. Mara zote jibu langu huwa lile lile. Najisikia fahari kuwatumikia Watanzania wenzangu kupitia uandishi wa makala, huku nikiamini kuwa si lazima kuwa mwanasiasa ili uweze kutekeleza jukumu hilo ipasavyo.
Lakini kwa upande mwingine, baadhi ya wanaonikosoa huenda mbali zaidi na kunituhumu kuwa uandishi wangu umeelemea kwenye chuki binafsi, husda na vitu kama hivyo. Jamaa mmoja alifikia hatua ya kudai kuwa makala zangu ni sehemu tu ya mikakati wa dini yangu dhidi ya utawala unaoongozwa na mtu anayetoka dini tofauti na yangu.
Kama ambavyo ninaridhishwa na pongezi kuhusu safu hii, huwa ninajifunza jambo moja au jingine kutoka kwa wakosoaji wangu (wengi wao hupenda kuhifadhi majina yao halisi). Kukosolewa huko, kunanisaidia kwa kiasi fulani, na hasa tukizingatia ukweli kwamba ukiona unamwagiwa sifa tu pasipo kuelezwa japo kasoro kidogo, basi yayumkinika kuhisi kuwa kuna mushkeli mahala fulani.
Nimelazimika kuandika hayo kutokana na ukweli kwamba makala yangu katika toleo lililopita ambayo pamoja na mambo mengine ilimzungumzia mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia CHADEMA, Zitto Zuberi Kabwe, imetafsiriwa na baadhi ya wasomaji wangu kama sehemu ya kampeni zangu za kumkwamisha kuingia ‘Ikulu.’
Nimeshaeleza mara kadhaa katika baadhi ya makala zangu zilizopita kuwa mimi si mwanachama wa chama chochote kile cha siasa, na nimekuwa hivyo kwa miaka kadhaa, tangu nikiwa huko nyumbani. Wakati, kwa kiasi kikubwa nilipokuwa huko nyumbani sheria ilikuwa inanikataza kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa, kwa sasa uamuzi wangu wa kuwa neutral unachangiwa zaidi na imani yangu kuwa itikadi bora zaidi kwa mwananchi ni uzalendo na kuitumikia jamii kwa hali na mali.
Moja ya sifa kuu za sheria, ni kwamba iwe mbaya au nzuri, inabaki kuwa sheria hadi itakaporekebishwa au kuondolewa. Kuna nyakati tunalazimika kufuata sheria zinazokinzana na haki zetu (kimsingi sheria inapaswa kuendana na uwiano kati ya haki na wajibu), lakini tunalazimika kuzifuata kwa vile ndizo sheria zinazotawala.
Ni kwa mantiki hiyo, ninarejea tena kutofautiana na Zitto katika dhamira yake ya kutaka kuwa Rais wa Tanzania, kwa sababu kwa mujibu wa sheria tulizonazo, hatokuwa na sifa ya urais hapo mwaka 2015 kutokana na kuwa na umri pungufu ya ule unaotajwa kwenye sheria mama ya nchi, yaani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninaafikiana na Zitto kwamba sheria hii ni ya kionevu kwa sababu kama inawezekana kwa mtu wa miaka 40 kuwa Rais kwanini ishindikane kwa mtu mwenye miaka 39?
Hata hivyo, napenda kumfahamisha kuwa hadi hapo sheria hiyo itakaporekebishwa au kubadilishwa, pamoja na ‘ubaguzi’ inaoubeba, itaendelea kuwa sheria inayopaswa kufuatwa. Na kwa vile kwa mazingira ya kawaida tu inatarajiwa Rais kuwa miongoni mwa vinara wa si tu kufuata sheria, bali pia kuzilinda, itakuwa ni ‘utani mbaya’ kwa mtu anayetaka kuwa Rais kudhamiria kuvunja sheria kama hiyo inayokataza walio chini ya miaka 40 kugombea urais.
Nimesema ninamuunga mkono Zitto kwamba sheria hiyo ni ya kibaguzi. Lakini kama tunachukia ubaguzi kwenye sheria, basi pia tunapaswa kuchukia ubaguzi kwenye kila eneo, iwe kwenye jinsia, imani, asili, rangi na hata kundi la mtu katika jamii. Siku chache zilizopita, kulikuwa na taarifa za kwamba Zitto aliongea na kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam na kutamka maneno yafuatayo:
“Wazee wetu walitusaidia sana kutupatia maendeleo ya kisiasa, sasa ni jukumu letu kuleta maendeleo ya kiuchumi. Ila naomba nisisitize kuwa jukumu hilo haliwezi kutekelezwa na mtu yeyote aliyezaliwa kabla ya uhuru, na ninatangaza nitagombea urais mwaka 2015.”
Binafsi, ninahitimisha kuwa kauli hiyo ni ya ubaguzi wa mchana kweupe. Lakini pia, licha ya ubaguzi, inaonekana kichekesho kwani imetoka kwa mwanasiasa (Zitto) ambaye hajawahi kuficha hisia zake dhidi ya ubaguzi wa watu kwa vigezo vya umri. Tukiweka kando taratibu za ndani ya CHADEMA kupata mgombea wake, moja ya sababu kuu zinazoonekana kama kikwazo kwa dhamira ya Zitto kuwa Rais, ni hiyo tuliyoiongelea hapo juu ya kutotimiza umri wa miaka 40 mwaka 2015 kama inavyotajwa kwenye Katiba.
Tunaomsapoti Zitto katika hoja yake hiyo, tunazingatia ukweli kwamba japo nchi haiwezi kuongozwa na mtoto wa miaka mitano, kwa mfano, mtu yeyote mzima (kiumri) anaweza kuiongoza nchi yetu pasipo umri wake kuathiri utendaji kazi wake. Utu-uzima si umri maalumu bali masafa (range) ya umri. Utu-uzima unaendana zaidi na uwezo wa mtu kutambua wajibu wake na kumudu kuutekeleza.
Wajibu huo unaweza kuwa katika ngazi ya familia (kama vile kuoa/kuolewa) au katika jamii pana, kama vile kushika dhamana ya uongozi.
Kwa hiyo, kimsingi, kama Zitto amemudu kuwatumikia wapigakura wa jimbo la Kigoma Kaskazini kwa mihula miwili sasa, sambamba na kulitumikia taifa kupitia uenyekiti wake kwenye Kamati ya Bunge, basi hakuna sababu ya msingi kwa umri wake kuwa kigezo cha kumzuwia kugombea urais mwaka 2015 hata kama atakuwa hajatimiza miaka 40. Ndiyo. Katiba inazuwia, lakini ukweli ni kuwa inazuwia kiuonevu!
Sasa wakati tunaafikiana na Zitto kupingana na uonevu huo wa Katiba, inakuwaje tena anatumia kigezo cha umri kuwabagua ‘wazee’ anaodai hawawezi kutuletea maendeleo ya kiuchumi? Busara ndogo tu ingeweza kumfahamisha Zitto-kama msomi-kuwa siasa na uchumi ni maeneo yanayotegemeana. Kama wazee waliozaliwa kabla ya Uhuru walimudu kutuletea maendeleo ya kisiasa, kwanini washindwe kwenye maendeleo ya kiuchumi?
Kama yeye aliyezaliwa baada ya Uhuru ameweza kufanya kazi nzuri kabisa katika uongozi wake wab kisiasa, ni kigezo kipi anachotumia kuwaona wazee waliozaliwa kabla ya Uhuru kuwa hawatoweza harakati za kuleta maendeleo yetu? Kwa hakika kabisa, huu ni ubaguzi, na kamwe mtu mwenye hisia za ubaguzi hapaswi japo kufikiriwa kuongoza nchi yetu.
Ninasema hivyo kwa sababu kama alivyotuusia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ubaguzi huzaa ubaguzi. Leo itakuwa “wazee waaliozaliwa kabla ya Uhuru hawawezi kutuletea maendeleo ya kiuchumi,” kesho itakuwa “Wakristo/Waislamu hawawezi kufanya hili,” “Wapogoro hawawezi kufanya lile,” au “wanawake hawawezi jukumu Fulani na kadhalika.
Naomba nimpe darasa dogo tu Mheshimiwa Zitto kuhusu kikwazo halisi cha maendeleo yetu. Uhaba unaozidi kukua katika uzalendo wa Mtanzania. Uzalendo hauna umri. Historia inatufundisha mengi tu kuhusu mchango wa wazee katika maendeleo ya sehemu zao husika. Mwalimu Nyerere, Nelson Mandela, Mahatma Ghandhi na kadhalika.
Binafsi, niliwahi kupishana kimtizamo na Zitto kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, ambapo katika hali ya kuchokoza mjadala, nilitamka kuwa muundo wa Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba haukuzingatia uwiano kati ya Wakristo na Waislam. Zitto alikerwa sana na hoja yangu hiyo aliyoiita ya kibaguzi. Alisisitiza kuwa tunapaswa kuangalia wasifu wa wajumbe kwa kigezo cha uwezo na uzoefu wao na si imani zao za kidini.
Cha kushangaza, ndani ya miezi michache tu, mtu huyo huyo aliyekemea vikali virusi vya ubaguzi (wa dini), amegeuka mfuasi wa ubaguzi wa umri. Kama tunapojadili teuzi mbalimbali tunapaswa kuangalia uwezo na uzoefu wa mteuliwa, kwanini basi wazee waliozaliwa kabla ya Uhuru wasitizamwe kwa uwezo na uzoefu wao kutuletea maendeleo ya kiuchumi, badala ya kuwahukumu kwa umri wao?
Ninaibua changamoto kama hiyo ya ‘ubaguzi’ kwa minajili, si ya kukwaza dhamira ya Zitto kuingia Ikulu mwaka 2015, bali kumsaidia kuamsha tafakuri yake iwapo utekelezaji wa dhamira hiyo utakuwa na manufaa kwake na kwa chama chake, au utaishia kuwa njia ya mkato kwa CCM kurejea madarakani huku CHADEMA ikiishia kuonekana chama cha mapambano kati ya vijana na wazee kukimbilia Ikulu.
Nimalizie makala haya kwa kukumbushia tena kauli ya Baba wa Taifa, ya kwamba yatupasa kuwaogopa kama ukoma wale wote wanaokimbilia Ikulu. Kama sisi wengine tunaweza kuitumikia nchi yetu kupitia makala zetu, huku wanasiasa kama Zitto wakimudu kututumikia kama wabunge, kisa cha kukimbilia Ikulu ambako Mwalimu alituasa kuwa anayefanya hivyo aogopwe kama ukoma, ni cha nini?
Simshawishi Zitto aachane na ndoto zake za urais kwani ninatambua hiyo ni haki yake ya kidemokrasia. Hata hivyo, ni muhimu kwa mwanasiasa huyo kijana kutambua kuwa wapenda mabadiliko ya kweli watamwona kama msaliti pindi ndoto zake hizo zitakapoishia kuwa kikwazo kwa CHADEMA kuing’oa CCM madarakani. Japo busara zinatueleza kuwa na ndoto pekee haitoshi, bali ni muhimu kutekeleza ndoto hizo kwa vitendo, ukiota unakata kuti unalokalia, na ukiamka ukaamua kulikata, sote tunajua matokeo yake.


Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.