28 Aug 2015

Hii ni simulizi ya kusikitisha kuhusu mwanaharakati wa mazingira kutoka Sweden, Susanna Nordlund, ambaye amekuwa akifanya harakati dhidi ya uporwaji wa ardhi na manyanyaso kwa wakazi wa Loliondo.

Kilichonigusa katika harakati za Susann ni ukweli kwamba ni raia wa kigeni anayepigani haki za Watanzania lakini amekuwa akifanyiwa hujuma na unyanyaswaji mkubwa.

Chini ni stori yake kama nilivyoitafsiri kwa idhini yake:

Ripoti fupi jinsi nilivyokamatwa Loliondo:

Niliwekwa rumande siku mbili katika kituo cha polisi cha Loliondo na pia nilikaa rumande usiku mmoja katika kituo cha polisi cha Arusha.

Sikuruhusiwa kuwasiliana na mtu yeyote, kompyuta yangu iliharibiwa, na badala ya kuelekwa kortini, nilifukuzwa Tanzania.


Wiki iliyopita safari yangu ya hivi karibuni huko Loliondo -sehemu ya dunia ambayo siku zote ipo akilini mwangu- ilikatishwa ghafla baada ya mtu fulani kuniripoti kwa mamlaka za eneo hilo. Nilipania kukutana na watu ambao hawapo online lakini wana taarifa kuhusu vitisho dhidi ya ardhi yao vinavyofanywa na 'wawekezaji.'


Niliwasili Wasso kwa basi tarehe 20 Juni mwaka huu, na sikuwa na mengi ya kufanya wakati ninatafuta gari la kuelekea vijijini. Nilipata ofa moja nzuri lakini dereva akadai kuwa haendi kwenye vijiji hivyo mchana. Hatimaye tarehe 23 nilipata gari kwenda Kirtalo kwa nusu siku. Nikiwa njiani, nilipata ujumbe kwamba mmoja wa madereva wa kampuni ya utalii ya Thomson Safaris alimpigia simu kijana mmoja kumweleza kuwa ameniona na rafaki yangu flani katika nyumba ya wageni ya Domel. Nilikutana na watu hapo Kirtalo, rafiki yangu alibaki hapo, na nilirudi Wasso na dereva. Njiani, tulikutana na gari lililokuwa na Diwani wa Oloipiri  'rafiki wa wawekezaji' William Alais. Mpango wangu ulikuwa kwenda Mondorosi na Sukenya siku inayofuata.

Nilirudi nyumba ya kulala wageni na kuingiza kwenye kompyuta niliyoelezwa na watu huko vijijini lakini baadaye nikaptiwa na usingizi. Nilipoamka, tayari ilikuwa usiku na nikaenda kupata chakula katika nyumba ya kulala wageni ya Honest, hasa baada ya kuona mengi hapo Domel. Gari moja liliwasili, na waliokuwa ndani ya gari hilo walishuka na kuniijia. Afisa Uhamiaji Angela aliniuliza ninafanya nini Tanzania na akataka kuona hati yangu ya kusafiria. Nilimweleza ratiba yangu ya safari na mipango yangu, bila kumtajia dhima yangu kufahamu kuhusu waporaji ardhi ya wafugaji.

Nilikuwa na nakala tu ya hati yangu ya kusafiria, na niliombwa kufuatana na maafisa Uhamiaji na askari polisi kwenda Oloip nilipokuwa nakaa. Nilijaribu kutuma meseji wka marafiki lakini nilinyang'anywa simu yangu. Niliambiwa kuwa Idara ya Uhamiaji ilikuwa ilikuwa ikinifahamu vema kutokana na taarifa za mtandaoni, jambo lililonipa ahueni nikidhani ningeweza kusimulia maoni yangu kuhusu kinachoendelea. Nilifahamishwa kuwa niko chini ya ulinzi na kutakiwa kupakia vitu vyangu. Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Hashimu Shaibu Mgandilwa, ambaye nilimtambua baada ya kumwona katika vyombo vya habari, alikuwepo pia, japo hakujitambulisha, na alikuwa akiongea na maofisa wa Uhamiaji. Wakati tunaondoka hapo kwenda kwenye gari la Idara ya Uhamiaji, kitambu cha kuandikisha wageni kilichukuliwa, na nikapelekwa kituo cha polisi cha Loliondo.

Baada ya kufika kituo cha polisi, niliambiwa kuwa sababu ya kukamatwa kwangu ni kuwa niliingia Tanzania kama mgeni haramu.

Mwaka 2010, nilitembelea Loliondo kama mtalii kuwauliza watu kama Thomson Safaris- kampuni ya Kiamerika ya kutembeza watalii ambayo inadai kumiliki ekari 12617 za ardhi ya Wamasai, na kudaiwa kuwanyanyasa watu- inaendana na ilichoandika kwenye tovuti yake. Nilipatwa na shauku kuhusu suala hili baada ya maongezi mtandaoni. Mengi kwenye tovuti ya kampuni hiyo si ya kweli, lakini pia nilifanya kosa la kumuuliza Afisa Mtendaji wa Kata ya Soitsambu , ambaye alimpigia simu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya wakati huo, Elias Wawa Lali, ambaye alinijibu siku iliyofuata. 
Siku iliyofuata, nilifuatwa na polisi na kupelekwa katika Kamati ya Usalama. Nilituhumiwa vitu mbalimbali, kama vile kufanya utafiti bila kibali. Hati yangu ya kusafiria ilichukuliwa na ilinibidi kwenda Uhamiaji Arusha kuichukua, ambapo huko nako niliambiwa kuwa mie ni 'mgeni haramu' na kutakiwa kuondoka nchini humo.
Baada ya hapo ndio nilianzisha blogu yangu - Mtizamo kutoka kwenye kichuguu cha mchwa (A view from a Termite Mound) - kuhusu 'wawekezaji' huko Loliondo ambao ni tihshio kwa haki za ardhi - Thomson Safaris na wengine wanaofahamika zaidi OBC kutoka Falme za Kiarabu- ambao wamekuwa wakijitahidi kuishawishi serikali ya Tanzania kutangaza kilometa za mraba 1500 jirani na Mbuga ya Taifa ya Serengeti kuwa ni eneo lililohifadhiwa, na kuiondoa jamii ya Kimasai katika eneo hilo lenye umuhimu mkubwa kwa maisha yao. Mwaka 2009, suala hili lilipelekea wanavijiji kuondolewa kwa nguvu baada ya kurudi tena katika eneo hilo.
Nilirudi tena mwaka 2011 na 2013 bila matatizo yoyote lakini nimekuwa nikipata zaidi taarifa kuhusu adha zinazowakabili wakazi wa maeneo hayo kupitia watu wanaotumia mitandao ya kijamii (social media). Blogu yangu ni nyenzo muhimu kwa sababu sio tu serikali na 'wawekezaji' wanasambaza taarifa potofu bali pia taasisi na watu wanaopinga unyanyasaji huo wamekuwa wakichanganywa na taarifa potofu. Wenyeji wa Loliondo wanaopinga vitisho kuhusu ardhi yao wamekuwa wahanga wa unyanyasaji mkubwa, hususan kutuhumiwa kuwa ni Wakenya, lakini tishio kubwa zaidi ni kutoka kwa baadhi ya wakazi wanaonufaika na unyanyasaji huo kwa urafiki wao na 'wawekezaji.'
-------------------------------------------------------------------------
Kituo cha Polisi Loliondo

Baada ya kufikishwa kituo cha polisi Loliondo, nilitakiwa kuorodhesha vitu vyangu vyote. Lieleza bayana kuwa ninaamini kukamatwa kwangu kulitokana na 'siasa chafu' kuhusiana na suala la ardhi, na kwamba wanaopaswa kukamatwa ni hao wanaohatarisha maisha ya wanavijiji. Hata hivyo, niliambiwa nipo chini ya ulinzi, na sina haki yoyote. Afisa Uhamiaji Angela alinieleza kuwa nitapatiwa simu yangu siku inayofuata. Kisha nikaingizwa rumande nikiwa na kikoi changu ambacho nilikitumia pia kama blanketi. Nililala kwenye sakafu ya zege kwenye selo yenye kiza. Baadaye nilipewa chupa ya maji ya kunywa ambayo nilitumia kunawa uso, lakini sikunywa maji mengi kwa vile selo haikuwa na choo. Baadaye niliona ndoo inayotumika kama choo.

Loliondo ni sehemu yenye baridi nyakati za usiku, na madirisha ya selo hayakuwa na glasi bali nondo tu. Kulikuwa na mbu wengi na sikuwa na kinga ya kuzuwia mbu (mosquito repellent). Nilikuwa mfungwa wa kisiasa. Nilitetemeka kwa baridi, lakini maneno kutoka Kirtalo kuhusu blogu yangu yalinipa nguvu. Unyanyasaji dhidi  yangu ulikuwa kama kichekesho, na baadhi ya watu walionyesha dalili za kuniunga mkono.

Asubuhi, nilipewa kifungua kinywa na kuruhusiwa kwenye bafuni, na kupatiwa maji ya kunawa uso kabla ya kurudi selo. Kwenye kuta za selo, kulikuwa namnaandishi kadhaa yaliyoashiria baadhi ya mahabasu walikuwemo humo bila mlo kwa siku kadhaa. Baadaye, nilichukuliwa na Angela kwenda ofisi ya Uhamiaji kuchukuliwa maelezo yangu. Alikuwa mkarimu kwangu na kunipatia peremende. Nilitoa maelezo yangu, na kueleza nilichokuwa ninafanya Loliondo, lakini bila kutaja majina kwa kuhofia watanyanyaswa. Angela alinieleza kuwa nitapelekwa kwenye nyumba ya kulala wageni kuoga kabla ya kupelekwa Arusha. Hata hivyo, alionekana kutofahamu kabisa kuhusu suala la haki za ardhi.

Nilirudishwa kituo cha polisi na kusubiri kwa muda mrefu wakati maofisa Uhamiaji wanafanya kikao na Mkuu wa Wilaya. Nilipata mlo na kuendelea kusubiri. Baadaye nilirudishwa tena rumande.

Mkuu wa Wilaya wa zamani, Elias Wawa Wali, alifanya kazi yake kibadhirifu akiitumikia serikali na 'wawekezaji' dhidi ya wanavijiji lakini hakuonekana kuwa na dhamira ya kufanya mabo mbaya zaidi. Mtangulizi wake, DC Hashimu Shaibu Mgandilwa, alikuwa na mawazo ya ajabu kabisa, kwa mfano kuwaamuru viongozi wa chini yake kutembea umbali wa kilometa nane kutoka Wasso hadi Liliondo, na kuishia kutupwa rumande baada ya askari mmoja mla rushwa kupigwa na wanakijiji Mei 6 mwaka huu.

Ilikuwa usiku nilipoamshwa, ANgela alikuja akiwa na bosi wake na mtu mwingine, na tuliondoka sote kuelekea Arusha. Tulipofika Olduvai nilipatiwa vitu vya kufanya usafi mwilini na baadaye tulisimama katika hoteli ya kifahari ya Serena Lodge kupata kifungua kinywa. Sina hakika kama gharama zililipwa kwa fedha za walipakodi wa Tanzania au na hoteli hiyo. Niltamani kuona ana angalau mtalii anayeonekana kama Mswidi lakini haikuwezekana. Nilitaraji kuwa albda taarifa zangu zimeshafika Ubalozi wa Uswidi. 

Tulipofika Arusha, sikurejeshewa simu yangu. Angela, yule afisa Uhamiaji, alikagua vitu vyangu na kukuta orodha ya majina, na hilo halikumfurahisha. Ilikuwa ni orodha tu ya majina ya watu ambao nilipanga kufanya maongezi nao.

Baada ya hapo ilifuatia kusubiri kwa muda mrefu. Koo ilikuwa imenikauka na nilikuwa na uvimbe kufuatia kung'atwa na mbu. Nywele zangu, ambazo kwa kawaida huzisha kila usiku, zilikuwa ovyo ovyo. Nilijilaza kwenye benchi, na baadaye nikasikia mlango ukifunguliwa. Wanasheria waliotumwa na Onesmo Olengurumwa wa Kituo cha Haki za Binadamu waliwasili. Niliwaeleza kilichotokea na wakaniambiwa watashughulikia nipate dhamana ikiwezekana.  Nilishakuwa nimewekwa rumande kitambo sasa na haikuwa haki kuninyima mawasiliano na watu wengine. Nilitaraji kuwa baada ya kutoka rumande itafuatia kesi mahakamani.

Baada ya muda mrefu nilielezwa kuwa nitarudishwa kituo cha polisi. Muda wote huo nilipokuwa nasubiri, sikupewa taarifa yoyote kuhusu inachoendelea. Ufahamu wangu mdogo wa Kiswahili ulichangia pia kutoelwa kinachoendelea. Niliwekwa tena rumande. Humo rumande nilkutana na mahabusu wengine, Sidamu aliyedai ni mtaalam wa wizi kwenye ATM na Mary aliyeiba maji kwa ajili ya kumwagia kwenye shamba lake.

Masaa kadhaa baadaye nilichukuliwa kwenda ofisi ya Uhamiaji na kuchukuliwa alama za vidole. Mchana, nilifahamishwa kuwa mie ni 'mgeni haramu' na sintoruhusiwa tena kuingia Tanzania. Niliambiwa kwamba kitu pekee ninachoweza kufanya ni kuandika barua Wizara ya Mambo ya Ndani. Niliomba majina ya watu ninaoweza kuwasiliana nao kwa barua-pepe lakini sikupewa, na sikurudishiwa simu yangu. 

Nilisindikizwa hadi Namanga, nikiwa kati ya watu wawili katika gari. Mpakani Namanga kulifuatia kusubiri kwingi na kupigwa picha. Niliomba nakala ya hati ya kutangazwa 'mgeni haramu' lakini sikupewa. Nilisema kwamba ningerejea tena siku moja, na afisa mmoja wa Uhamiaji alimweleza mwenzie, "haogopi kitu."

Baada ya kuingizwa Kenya nilipatiwa simu yangu, na dereva mkarimu alinipeleka hotelini. Nilapata fursa kuangalia mitandao ya kijamii na kulikuwa na taarifa za kukamatwa kwangu. Pia nilipata wasaa kuwafahmisha ndugu na jamaa kuwa nimeachiwa huru. Familia yangu haikufahamishwa lolote nilipokamatwa, na maofa wa Ubalozi wa Uswidi hawakuruhusiwa kuwasiliana nami bila idhini yangu (ningewezaje kutoa idhini ilhali walizuwia mawasiliano yangu na mtu yeyote yule?)

Kompyuta yangu ambayo huwa nayo muda wote iligoma kuwaka. Kesho yake nilimpata mtaalam wa kompyuta hapo Namanga ambaye alibaini ilikuwa na matatizo.
Tarehe 30 nilifahamishwa kuwa mwandishi mmoja, Manyerere Jackton ameandika kwa kirefu kuhusu mimi katika gazeti la kila wiki la Jamhuri. Kesho yake niliweza kuiona habari husika........ na ilikuwa na uongo mwingi. Kama nilivyotarajia, mwandishi huyo alijaribu kunifarakanisha na Tina Timan ambaye sijawahi kukutana nae. Huyu ni anayelezwa kuwa ni mwanaharakati kutoka Kenya, japo amekuwa akiishi Tanzania kwa muda mrefu na ana watoto hapo. Mwandishi huyo amekuwa akichochoea vitu vingi dhidi ya wanavijiji wa Loliondo.

Manyerere- au mtoa habari wake- alidai kuwa nilisema kwamba ningehakikisha serikali ya Uswidi inakata misaada kwa Tanzania kama seriali haitoendelea kunisumbua. Licha ya kwamba sina uwezo huo, lakini kila anayenifahamu anajua nisingeweza kusema maneno kama hayo. Kitu pekee nilichosema kuhusu nchi yangu ni katika nchi yoyote yenye demokrasia, mtalii nanaweza kuongelea siasa na mtu mwingine, baada ya kuambiwa pale kituo cha polisi kuwa "hakuna sehemu yoyote duniani mtalii anaruhusiwa kuongelea siasa." Huu ni unafiki wa hali ya juu katika nchi ambayo ni mhanga wa ukoloni mamboleo. 

Katika habari hiyo, Kamishna wa Uhamiaji Abdullah Khamis Abdullah alimpongeza DC Mgandilwa kwa 'kudumisha amani wilayani kwake.' Sio tu uwepo wa Mkuu wa wilaya ni zao la ukoloni bali pia afisa huyo amekuwa akiwatenda wanavijiji kama ilivyokuwa zama za ukoloni.

Mwandishi huyo alinituhumu kuwa mie na 'washirika wangu' tumekusanya mabilioni ya shilingi kwa ajili ya wafugaji wanaonyanyaswa na kuzifadhili NGO za kuchochea vurugu katika vijiji husika. Sijawahi kuksanya fedha zozote wala kutoa chochote kwa NGO. Mie ni bloga tu.

Tishio baya zaidi ni kuwapeleleza wanavijiji wote wanaonisaidia, na kwa kukosa mwelekeo,miongoni mwa wahanga ni mmiliki wa nyumba ya kulala wageni niliyofikia kama mteja mwingine yeyote yule.Itanilazimu nimlipe fedha zake za huduma ya malazi, kupitia huduma ya kuta fedha ya Western Union, mara baada ya kurudi nyumbani, kwani nilichukuliwa kutoka sehemu hiyo ghafla.

Sijui kwanini sikufunguliwa kesi mahakamani. Ingekuwa fursa nzuri kuweka wazi kinachoendelea Loliondo, na kuuliza iwapo watalii hawaruhusiwa kuuliza mwaswali wawapo Tanzania, na iwapo watalii wanaooblogu wanahitaji viza maalumu kuingia katika nchi hiyo.

Sasa dhamira yangu ni kuendelea kuandika kuhusu Loliondo katika uhai wangu wote, na kwa hakika nitarudi tena.

NYONGEZA: Uchunguzi uliofanywa na mafundi wa kampuni ya Samsung umethibitisha kuwa Hard Drive ya kompyuta yangu ilichomolewa nilipokuwa Tanzania.

Pia,Manyerere alinitumia barua pepe kwamba amesoma blogu yangu na anaitetea nchi yake dhidi ya 'ukoloni mamboleo' wangu, akisema 'Tanzania ni kwa ajili ya Watanzania.' Jibu la wazi lilikuwa mshangao kwanini amekuwa akiandika makala mbalimbali za kichochezi dhidi ya wanavijiji wa Loliondo kwa maslahi ya wawekezaji kutoka nje. Badala ya kunijibu swali hilo, mwandishi huyo alijibu haraka kwa kunitumia picha za mtu aliyekuwa akitoa habari Loliondo, na kujigamba kuwa kila nyendo zangu 'haramu' nikiwa huko ilikuwa ikifuatiliwa japo hakubainisha uharamu wa nyendo zangu katika nchi ya kidemokrasia.

Habari hii imetafsiriwa kutoka blogu ya Susanna, kama ilivyoandikwa HAPA. Kadhalika, waweza kuwasiliana na mwanaharakati huyo wa haki za ardhi, kwa barua-pepe [email protected]

MTIZAMO WANGU: Nimemfahamu Susanna kutokana na kuguswa kwake na kujishughulisha kwake na haki za ardhi huko Loliondo. Nina imani wasomaji wengi mnafahamu kuhusu maslahi ya taifa letu yanavyowekwa rehani katika maeneo kadhaa yenye raslimali za taifa letu. Haiingii akilini, mwanaharakati kama Susanna aache shughuli zake huko Uswidi, aende Tanzania kuwachochea wanavijiji. 'Kosa' la dada huyo ni kuwa mtetezi wa wanyonge. Imekuwa kawaida sasa kwa kila anayejaribu kukemea maovu kuitwa adui wa taifa letu. Kwa hakika inaumiza sana kuona watu wanaojali maslahi ya taifa letu wananyanyaswa kiasi hiki na kutangazwa 'maadui wa taifa.' 









KABLA sijaingia kwa undani katika makala hii, ambayo niliahidi katika toleo la wiki iliopita, nitajadili kwa kina kuhusu mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, ningependa kumpa pole mwanasafu mwenzangu Johnson Mbwambo, kutokana na wingi wa ujumbe mfupi wa maneno (sms) na vitisho kila anapoikosoa Chadema.
Mimi pia nimekuwa mhanga mkubwa wa tabia hiyo ya kukera ambayo imejitokeza mara baada ya mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema/UKAWA kujiunga na chama hicho. Hali kwangu ni mbaya zaidi kutokana na uwepo wangu mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.
Nimeitwa kila aina ya jina na kutukanwa kila aina ya tusi, huku tuhuma kubwa kila ninapoikosoa Chadema au UKAWA ikiwa eti ‘nimenunuliwa na CCM’ au ‘kuahidiwa kitu fulani’.

Kuna ‘wastaarabu’ ambao wananilaumu bila kutumia lugha chafu. Wanadai kuwa mtizamo wa machapisho yangu katika gazeti hili na katika blogu yangu ulikuwa ni kuiunga mkono Chadema na kuikosoa CCM. Sasa wananilaumu kwa vile eti ‘nimewasaliti’ na kwa kuikosoa Chadema au UKAWA, ninaiunga mkono CCM.
Awali suala hili lilinisumbua sana kwa sababu wengi wa watu hawa walikuwa wakiilaumu serikali ya CCM kwa kuja na muswada wa kupambana na uhalifu wa mtandaoni (Cybercrime Bill) na kudai ulilenga kuwanyima uhuru wao wa kujieleza.
Iweje leo watu haohao wafanye kilekile walichokuwa wakiilaumu serikali: kutunyamazisha wenzao wenye mitizamo tofauti nao? Hivi hapa kuna neno sahihi zaidi ya unafiki?
Hatimaye nimefanikiwa kuelewa chanzo cha tatizo hilo ni kipi: kukata tamaa, kuchanganyikiwa, na kukosa mwelekeo.

Chuki kubwa waliyonayo dhidi ya CCM, sambamba na matamanio ya kukiona chama hicho tawala kinaondoka kwa gharama yoyote ile, kumepelekea watu hao kuweka imani isiyo na ukomo kwa mgombea urais kwa tiketi ya chama chao, yaani Lowassa.
Sasa yeyote atakayeongea chochote kile kinachoonekana kupunguza nafasi ya Lowassa kuingia Ikulu anaonekana kama adui wa mabadiliko.
Wakati nimeanza kuzoea matusi na lugha chafu inayoelekezwa kwangu, wasiwasi wangu mkubwa ni hatma (aftermath) ya uchaguzi mkuu katika nafasi ya Rais.
Ninabaki kujiuliza, hivi hawa watu wenye matumaini makubwa kupindukia kuwa mgombea wao ataingia Ikulu, watakuwa katika hali gani iwapo matokeo yatakuwa kinyume?
Je watakubali tu matokeo na kufanya post-mortem kistaarabu au ndio tutajikuta tunarudi katika hali iliyojitokeza huko Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 (Mola aepushe)?
Sasa niingie kwenye mada ya wiki hii. Kama nilivyoeleza katika makala tangulizi, nchi yetu itaingia katika uchaguzi huku kwa kiasi mazingira ya uchaguzi yakiwa yanaipendelea CCM.
Na pengine hili ndilo kosa kubwa wanalofanya wafuasi wa UKAWA; kutarajiwa matokeo tofauti katika uchaguzi unaofanyika katika mazingira yaleyale ‘yaliyowaliza’ katika chaguzi zilizotangulia.

Kwamba watu wengi wamechoshwa na CCM wala si suala la mjadala. Maelfu kwa maelfu ya watu wanaojitokeza kwenye shughuli za kisiasa za Lowassa sio kuashiria cha umaarufu wa mwanasiasa huyo bali hiyo kiu ya kuoina CCM inatoka madarakani. Lakini busara kidogo tu zatosha kutufahamisha kuwa kutaka kitu na kupata kitu ni vitu viwili tofauti.
Watanzania wengi waliochoshwa na CCM, wanataka kuiona inaondoka madarakani hata kesho. Lakini kuwezesha matakwa hayo yatimie si suala rahisi. Naomba nieleweke hapa, Ninasema SI RAHISI lakini sijasema HAIWEZEKANI.
Kudhani kuwa CCM itaondoka kwa kutumia wanasiasa walewale ambao wamechangia kuwafanya Watanzania wengi watake chama hicho kiondoke madarakani ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.
Naam, Lowassa anaweza kuwezesha Chadema/UKAWA kuitoa CCM madarakani lakini sababu zilizofanya CCM ichukiwe haziwezi kuondoka.
Kwahiyo faida kubwa iliyonayo CCM ni mfumo wa uchaguzi na kiutawala ambao unakitengenezea mazuri chama chake na yeye binafsi kufanya vizuri katika uchaguzi huo.
Lakini licha ya faida hizo za kimfumo, Magufuli anaingia katika uchaguzi huo akiwa katika CCM ileile iliyoshinda chaguzi zote zilizotangulia, kihalali au la, lakini safari hii inakutana na upinzani ambao Kimsingi umetengenezwa katika mazingira ya ‘zimamoto’.

Jinsi UKAWA ilivyoundwa na maendeleo yake hadi kufikia hatua ya kusimamisha mgombea mmoja, yaweza kuwa ni moja ya vikwazo kwa umoja huo kufanikiwa kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika takriban miezi mawili na kitu kutoka sasa.
Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Lakini umoja tunaozungumzia hapa ni ule wenye kujengwa katika misingi ya kuaminiana. Tayari Tumeshuhudia Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, akijiweka kando na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba akijiuzulu.
Ni rahisi kutoa majibu rahisi, kwa mfano kuwatuhumu wanasiasa hao ni wenye uchu wa madaraka, lakini ukweli ni kwamba ‘kujitenga’ kwao sio tu kuna athari bali pia kunaashiria mpasuko wa aina fulani katika umoja huo.
Kwahiyo Magufuli na CCM kwa ujumla wataingia katika uchaguzi huo wakiwa kitu kimoja, kwa kiasi kikubwa, ilhali UKAWA wakikabiliwa na ‘sintofahamu’ flani, sio tu ya kuhusu Dkt Slaa na Prof Lipumba, bali pia hizi taarifa zinazosikika kutoka katika baadhi ya majimbo ambapo ‘ndoa’ ya vyama hivyo imeshindikana, yaani licha ya kuafikiana kusimamisha mgombea mmoja, vyama vinavyounda umoja huo vimejikuta vikisimamisha wagombea tofauti.
Jingine limejitokeza katika uzinduzi wa kampeni za CCM Jumapili iliyopita ambapo chama hicho tawala, kama baadhi yetu tulivyotarajia, kimejaribu kujenga picha kuwa Chadema/UKAWA sasa ni kama kikosi cha pili cha CCM (CCM-B).

Magufuli na timu yake wakiweza kujenga hoja za kueleweka kwanini Lowassa na Chadema/UKAWA yake ni sawa tu na CCM ya waasi, kuna uwezekano wa wapigakura kutafuta hifadhi katika ‘jini linalokujua halikuli likakwisha.’CCM ‘halisi’ ni ‘jini’ wanalolijua, na pengine wasingetaka kufanya majaribio kwa ‘jini’ wasilolijua.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Magufuli na CCM kwa ujumla wanaweza kurahisishiwa kazi na ‘historia ya mahusiano kati ya Chadema na Lowassa. Kama kuna mwanasiasa wa CCM aliyeandamwa mno na Chadema kuhusu tuhuma za ufisadi basi si mwingine bali Lowassa.
Kwa kuzingatia muda uliopo, kati ya mwanasiasa huyo kuhama CCM na kujiunga na Chadema na tarehe ya uchaguzi mkuu, yayumkinika kuhitimisha kuwa ni vigumu mno kumsafisha.

Kimsingi, Chadema/UKAWA wamejiambukiza tatizo walilokuwa wakilipiga vita kwa nguvu zao zote. Hakuna ubishi kuwa mafanikio ya chama hicho kikuu cha upinzani yalichangiwa zaidi na msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi.
Sasa leo hii wakisimama jukwaani sio tu na mwanasiasa anayetuhumiwa kujihusisha na ufisadi lakini pia Chadema wenyewe walimwandama kwa tuhuma hizo, kisha wajaribu kumsafisha au kukemea ufisadi, ni mkakati wenye dalili ya kutokuwa na mafanikio.
Awali kulikuwa na hisia za ‘mafuriko ya Lowassa’ kuikumba CCM, kwa maana ya wanasiasa wenye nguvu ndani ya chama hicho tawala kumfuata huko Chadema/UKAWA.
Kuna wawili watatu waliohama lakini si wenye ushawishi au nguvu kubwa ya kuiathiri CCM. Na tayari CCM, imewashusha hadhi na kuwaita ‘makapi’ sambamba na kujenga picha kuwa ni wenye uchu wa madaraka.
Kuhama kwa Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, kutoka CCM na kujiunga na UKAWA kunazidi ‘kuchanganya madawa.’ Kubwa zaidi ni kile kilichoonekana kuwa uhasama wa muda mrefu kati ya wanasiasa hao.
Wakati hii ingeweza kuwa turufu kubwa kwa UKAWA, kuwa na mawaziri wakuu wa zamani wawili ndani ya upinzani, lakini tayari zimeanza kusikika tetesi kuwa “Sumaye ameingia UKAWA kama ‘Plan B’ endapo lolote litamtokea Lowassa kiafya.”
Lakini makala hii si ya kuzungumzia mapungufu ya Chadema/UKAWA bali ni kumjadili Magufuli, japo ni vigumu kuzungumzia fursa alizonazo za kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu pasipo kujadili ‘urahisi’ unaotokana na kinachoendelea huko UKAWA.
Tukiweka pembeni niliyobainisha hapo juu, matumaini kuwa urais wa Magufuli utakuwa tofauti na huu wa Rais Jakaya Kikwete ni mdogo.
Hilo nilishaliongelea huko nyuma, ambapo yayumkinika kudhani kuwa mgombea huyo wa chama tawala anaweza kuwa na deni la fadhila kwa mtangulizi wake, hasa kwa kuzingatia ‘mahesabu’ yaliyofanyika katika machakato wa CCM kumpata mgombea wake.
Laiti Chadema/UKAWA wasingekuwa na kibarua cha kumsafisha mgombea wao, Lowassa, wangeweza kuwa katika nafasi nzuri kujenga picha kwa wapigakura kuwa miaka mitano ya utawala wa Magufuli haitokuwa tofauti na kumi ya Kikwete, na pengine kupigilia mstari kuwa mengi ya yaliyojiri katika utawala uliopo madarakani yanamhusu mgombea huyo wa CCM pia.
Hata hivyo, iwapo jitihada za kumsafisha Lowassa na kumtenganisha na CCM zitafanikiwa, basi UKAWA na mgombea wao wanaweza kufanya vizuri.
Mwisho, kama kuna kitu kinachoweza kuigharimu CCM na Magufuli ni kupuuzia ukweli kuwa kuna wapigakura wengi wamepoteza imani kwa chama hicho.
Na laiti mwenendo wa kampeni za Magufuli utafuata ‘busara’ za Rais mstaafu Benjamin Mkapa kutumia lugha isiyo ya kistaarabu ya ‘mpumbavu na lofa’ basi sintoshangaa kuona Lowassa akinufaika na ‘kura za huruma’.

Ni muhimu kwa CCM kuongoza kwa mfano ikiwa ni pamoja na kuachana na kampeni za chuki au za ‘utoto wa kisiasa’ (political immaturity), iwaeleze Watanzania wapi ilipokosea hadi baadhi yao kutamani iondoke madarakani, na nini itawafanyia kurekebisha makosa yake.

20 Aug 2015

KAMA nilivyoahidi katika makala iliyopita, wiki hii ninaendelea na uchambuzi wangu kuhusu Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Na kama ilivyokuwa katika makala kadhaa zilizotangulia, uchambuzi wangu utaelemea kwenye kinyang’anyiro cha nafasi ya urais.
Wakati katika makala iliyopita nilijadili fursa na vikwazo kwa wagombea ‘wakuu’ wawili, yaani Dk. John Magufuli wa CCM na Edward Lowassa wa Chadema/UKAWA, wiki hii nitaingia kwa undani zaidi, huku lengo likiwa kuitumia makala hii kufanya uchambuzi kwa mgombea mmoja, na makala ya wiki ijayo itamwangalia mgombea mwingine.
Nianze na Lowassa wa Chadema/UKAWA. Kati ya makala iliyopita na hii, si siri kuwa habari inayotawala zaidi ni kile kinachoitwa ‘mafuriko ya Lowassa’. Shughuli zote zilizomhusisha mwanasiasa huyo katika kipindi hicho kimeandamana na umati mkubwa mno wa watu, kuanzia alipochukua fomu za kuwania urais jijini Dar es Salaam hadi katika mikutano ya kutambulishwa huko Mbeya, Arusha na Mwanza.
Wingi wa watu wanaojitokeza katika shughuli zinazomhusu Lowassa, iwe ni kwa kuandamana au kuhudhuria mikutano, kumewapa matumaini makubwa wafuasi wake kwamba njia ya Waziri Mkuu huyo wa zamani kuelekea Ikulu ni nyeupe.
Sambamba na mahudhurio hayo makubwa, wanachama kadhaa wa CCM wamehama chama hicho tawala na kujiunga na Chadema. Lakini kubwa zaidi ni kuhama kwa baadhi ya viongozi ‘ waliokuwa na majina’ ndani ya CCM.
Kwamba maandamano na mikutano ya Lowaasa inajaza watu wengi mno, hilo halina mjadala. Kwamba matukio yajayo ya mwanasiasa huyo yataendelea kujaza watu pia si suala la mjadala. Kadhalika, kwamba kuna wanachama na viongozi zaidi wa CCM watamfuata Lowassa huko Chadema pia ni jambo la kutarajiwa.
Tusichoweza kuhitimisha kwa uhakika muda huu ni iwapo hamahama hiyo ya baadhi ya wana-CCM na viongozi wao kumfuata Lowaasa huko Chadema itaweza kutafsiriwa katika ushindi katika uchaguzi mkuu ujao hapo Oktoba 25, takribani miezi mawili kutoka sasa.
Licha ya uwepo wa hamasa kubwa kuhusu kujiandikisha katika daftari za wapigakura lililoboreshwa na teknolojia ya kuhifadhi rekodi kwenye kompyuta (Biometric Voter Register kwa kifupi BVR), hadi muda huu Tume ya Taifa ya Uchaguzi haijatoa idadi kamili ya watu waliojiandikisha.

Lakini licha ya hilo, tayari kuna dalili za kasoro katika suala la BVR ambapo zimepatikana taarifa kadhaa za waliojiandikisha kutoyaona majina yao wakati wanaofanya uhakika. Ukubwa au udogo wa kasoro hiyo bado haujafahamika kwa vile Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijalitolea ufafanuzi suala hilo.
Hapa nitaunganisha masuala hayo mawili ya hapo juu, yaani idadi kubwa ya watu wanaojitokeza katika shughuli za Lowassa na zoezi la kujiandikisha BVR.
Yayumkinika kuhitimisha kuwa ili wingi wa watu wanaojitokeza katika shughuli za mwanasiasa huyo ziwe na manufaa kwake na chama chake kwa ujumla, basi, kwanza wengi wa watu hao, kama si wote, lazima wawe wamejiandikisha kupiga kura. Bila hivyo wingi wao utabaki kuwa historia tu.
Lakini kwa uzoefu tulionao wengi, kujiandikisha kupiga kura ni suala moja, kufanikiwa kupiga kura ni suala jingine, na kumpigia kura mgombea fulani na kura hiyo kumsaidia ashinde ni suala jingine kabisa.
Nimeshazungumzia katika makala zangu zilizotangulia kuwa moja ya faida kubwa kwa CCM ni mahusiano ya upendeleo kati yake na taasisi mbalimbali za umma. Na ninatarajia wengi wenu ndugu wasomaji mmekuwa mkisikia vilio vya wanasiasa wa upinzani takribani tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi kwamba wanaohisi kura zao zinahujumiwa na chama tawala kwa kusaidiwa na taasisi za umma ‘zinazokipendelea’ chama hicho.
Japo mara zote tuhuma hizo zimeendelea kubaki kuwa tuhuma tu, ushahidi wa kimazingira unaelekea kuzisapoti tuhuma hizo.
Binafsi, nimekuwa nikifuatilia pilika za uchaguzi mkuu kupitia mtandaoni, hususani kwenye mitandao ya kijamii (social media). Majuzi, niliwatahadharisha mashabiki wa Lowassa kuhusu furaha yao inayotokana na wingi wa wahudhuriaji katika shughuli za hadhara zinazomhusu mwanasiasa huyo.
Niliwakumbusha kuhusu chaguzi zilizopita, hususan ‘kasi ya (Agustino Lyatonga) Mrema,’ aliyekuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 kupitia chama cha NCCR-Mageuzi, jinsi alivyokuwa maarufu na kujaza halaiki ya watu kwenye mikutano yake, lakini akaishia kubwagwa na mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa.
Niliwakumbusha pia kuhusu wingi wa watu waliojitokeza katika mikutano ya kampeni za Dk. Willibrord Slaa, aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema katika uchaguzi mkuu uliopita, mwaka 2010, lakini akishindwa na mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete.
Katika chaguzi zote hizo, pamoja na ule wa mwaka 2000 na 2005, kulikuwa na malalamiko kdhaa kuwa ‘CCM iliiba kura,’ lakini tuhuma hizo zilijifia zenyewe kutokana na kutokuwepo ushahidi halisi, sambamba na vikwazo vya kikatiba kupinga matokeo ya Urais.

Lakini kukumbushia yaliyojiri katika chaguzi hizo kulipelekea mimi kushambuliwa vikali, nikituhumiwa kuwa na ‘chuki binafsi’ dhidi ya Lowassa, huku wengine wakinituhumu kuwa nimenunuliwa na CCM. Na nikakumbushwa kuwa “nenda na wakati, hii ni 2015, achana na habari za 1995”.
Siwezi kuwalaumu watu ambao hawataki kusikikia lolote ‘baya’ kuhusu Lowassa, au jambo linaloweza kuwa kikwazo kwake kupata urais.
Kwa bahati mbaya, ujio wa mwanasiasa huyo huko Chadema unaoonekana kuwabadili wana-Chadema wengi, angalau huko mtandaoni, ambapo watu waliokuwa wakijadili hoja kiungwana, sasa wamekuwa mahiri wa matusi kwa kila anayeelekea kumpinga Lowassa.
Nitawalaumu kwa matumizi ya matusi badala ya kujenga hoja za kistaarabu, lakini sintowalaumu kwa kuwa ‘desperate.’ Wanasema mtu akielemewa na mafuriko basi atang’ang’ania hata unyasi ili ajiokoe.

CCM imewafikisha Watanzania wengi katikia hali hii tunavyoshuhudia. Sapoti kubwa kwa Lowassa sio kwa vile ni mchapakazi au anatarajiwa kuleta ‘miujiza’ bali ni kukata tamaa miongoni mwa Watanzania wengi, Tunasikia watu wakisema “ukiiweka CCM na jini, nitapiga kura yangu kwa jini”.
Lakini wakati kuwa na matumaini yanayotokana na kukata tamaa si tatizo sana, ni muhimu kuzingatia hali halisi. Kuna wanaodai ‘safari hii CCM haiwezi kutuibia kura’ Je kuna tofauti gani ya kimazingira ya uchaguzi katika ya mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwaka 1995,2000,2005 na 2010? Tume ya uchaguzi ni ileile, taasisi mbalimbali za umma zinazoshughulikia uchaguzi huo bado zipo vilevile, na vyombo vyetu vya dola bado vina ‘mentality’ ileile ya kuwaona Wapinzani kama wahaini, na hata Lowassa amekiri kuwa alipokuwa CCM alidhani vyombo vya dola vyalaumiwa bure tu na Wapinzani…hadi alipoonjeshwa ‘jeuri ya polisi’ hivi majuzi.
Lakini tukiweka kando kuhusu tatizo hilo ambalo niliona kama la kimfumo, yaani mfumo unaoipendelea CCM, kuna tatizo jingine ambalo pengine halijawa kubwa sana. Hili ni uwezo mdogo wa Lowassa katika kujieleza.
Unapofanikiwa kukusanya umati wa maelfu ya watu, kisha ukahutubia kwa dakika tano, na katika muda huo mfupi usiseme lolote la maana la kuwafanya waliohudhuria wakumbuke si ukubwa wa umati bali uzito wa hotuba ya aliyewajaza kwa wingi mahala husika, basi hapo kuna tatizo.
Na tatizo hili laweza kuwa turufu kwa mgombea wa CCM, Dk. Magufuli, ambaye anasifika kwa umahiri si tu wa kuongea bali kutoa takwimu nyingi kichwani kana kwamba ni mashine yenye kumbukumbu (memory) kubwa.
Ukizungumzia hilo kwa wana-Chadema/UKAWA, wanasema “nani anataka hotuba? Sisi tunachotaka ni kuondoa CCM tu”. Ninabaki ninajiuliza, “hivi wakifanikiwa ukiondoa CCM, nini kitafuata?” Sipati jibu.
Kwa kifupi, kinachowapa matumaini wana-Chadema/UKAWA na mashabiki wa Lowassa ni hayo ‘mafuriko.’ Iwapo yataweza kujitafsiri katika kura, muda utatupatia jibu (time will tell).
Na iwapo ‘mafuriko’ hayo yatamwezesha Lowassa kuingiza Ikulu, ninadhani hata wana-Chadema/UKAWA wengi hawajui jinsi gani atakavyowezesha kubadili kile kinachowafanya Watanzania wengi wachukizwe kuhusu CCM.

Kwa upande mmoja, kuahidi mabadiliko ni kitu kimoja, kutekeleza ahadi hiyo ni kitu kingine. Kwa upande mwingine, kuwa na nia ya kuleta mabadiliko ni kitu kimoja, uwezo wa kufanikisha nia hiyo ni kitu kingine, na hata pale nafasi ya kuleta mabadiliko inapopatikana, nyenzo na mazingira vyaweza kuwa kikwazo cha kutimiza azma hiyo.
Nihitimishe makala hii kwa kuahidi kuendelea na uchambuzi huu katika toleo lijalo ambapo nitamzungumzia mgombea wa CCM, Dk. Magufuli kama nilivyomjadili Lowassa katika makala hii.

13 Aug 2015

MAKALA hii ni mwendelezo wa ile iliyochapishwa katika gazeti hili katika toleo la wiki iliyopita. Katika makala hiyo nilijadili kwa kirefu kuhusu kile nilichokiyumkinisha kuwa usaliti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), si tu kumpokea Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa (aliyelazimika kujiuzulu Uwaziri Mkuu kufuatia skandali ya ufisadi wa Richmond), bali pia kumteua kuwa mgombea wake urais kupitia UKAWA.
Kadhalika, pamoja na mambo mengine, nilieleza kusikitishwa kwangu na kile nilichokitafsiri kama mwelekeo wa siasa za Tanzania yetu kutoka mfumo wa awali wa chama kimoja hatimaye vyama vingi na hiki tunachoshuhudia baada ya Lowassa kujiunga na Chadema, ninachokiita ‘chama cha mtu mmoja.’
Katika makala hii nitajadili nafasi za kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu ujao kwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt John Magufuli, na huyo wa Chadema/UKAWA, yaani Lowassa, sambamba na vikwazo vinavyowakabili kila mmoja wao.
Nianze na Magufuli. Kwa kada huyo, binafsi ninaona kuwa ana nafasi nzuri ya kushinda hasa kwa sababu, kama alivyotamka Rais Jakaya Kikwete hivi majuzi, CCM ina uwezo na nyenzo kumwezesha mgombea wao kufanya vizuri. Vyote viwili – uwezo na nyenzo – vimeshathibitika kuwa na ufanisi mkubwa katika chaguzi zilizopita.
Na vyote viwili vipo katika pande mbili; halali na isivyo halali. Uwezo halali wa CCM unatokana zaidi na mitandao wake mpana hasa vijijini. Kwa bahati mbaya au makusudi, licha ya maeneo mengi ya vijijini katika nchi yetu kukabiliwa na umasikini mkubwa, pia yana uhaba wa ‘wasomi,’ huku wachache waliopo wakiwa aidha wamekumbatiwa na ‘mfumo unaoilinda CCM’ au wameukumbatia kwa minajili ya kulinda nafasi zao.
Ninaposema ‘wasomi’ simaanishi maprofesa au watu wenye elimu ya juu bali hata wale wenye elimu ya wastani tu ambao ni muhimu sana katika kuhamasisha na kuleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali.
Katika mazingira ya kawaida, mtumishi wa umma kijijini anaweza kuwa na chaguo rahisi ‘kuitumikia CCM’ badala ya chama cha upinzani kwa vile hasa kwa vile katika maeneo mengi ya vijijini, ni vigumu kuitofautisha CCM na serikali.
Kuna tatizo la ziada kuhusu ‘wasomi’ wetu. Wakati katika stadi za matabaka, wasomi wanatarajiwa kuwa sio tu kiungo katika ya tabaka la walalahoi na tabaka tawala, wasomi wetu wengi sio tu hawamtaki kujihusisha na tabaka la walahoi bali pia wanajibidiisha – hata kwa kuiga tu – kuwa sehemu ya tabaka tawala. Na Wasomi wachache tulionao vijijini wanaotaka waonekane kama ‘vigogo’ au ‘vingunge’ badala ya wananchi wa kawaida au walalahoi. CCM inatambua udhaifu huu na kutumia ipasavyo.
Ikumbukwe pia kuwa wengi wa ‘wasomi’ hao ndio watumishi muhimu katika shughuli nzima ya uchaguzi, na yayumkinika kuamini kuwa wamekuwa na ‘msaada’ mkubwa kwa CCM katika chaguzi zilizopita, na wanaweza kuendelea kuwa nyenzo muhimu kwa chama hicho tawala.
Lakini pengine kubwa zaidi ni turufu ya CCM hasa katika maeneo ya vijijini kuwa ‘inaweza kuonyesha jinsi ilivyowatumikia wananchi’ tofauti na ‘vyama vya upinzani vinavyokuja kufanya majaribio ya kuongoza nchi.’ Ni hoja isiyo na msingi kwa wenye uelewa wa kuchanganua mambo, lakini kwa huko vijijini, kuipinga kwahitaji kazi kubwa na sio takriban miezi mawili iliyosalia kabla ya uchaguzi mkuu.

CCM inabaki kuwa ‘zimwi likujualo’ ilhali kwa vyama vya upinzani, tegemeo lao kubwa ni kuonyesha mapungufu ya chama hicho tawala, na kutegemea wananchi watawaelewa na kuwaamini, na ‘kucheza bahati nasibu’ ya kuwakabidhi madaraka.
Ukichanganya na ukweli usio rasmi kuwa CCM ni mnufaika mkubwa wa uhusiano wake na taasisi za serikali – Tume ya Uchaguzi, vyombo vya dola, nk – chama hicho tawala kitaingia katika uchaguzi kikiwa na nyenzo na uwezo wa kushindwa hata kama ni kwa tabu.
Kwa kifupi, mazingira yaliyoiwezesha CCM kushindwa chaguzi kuu zilizopita bado yapo na mfumo wa uchaguzi bado unakitengenezea chama hicho tawala nafasi ya kufanya vizuri.
Hata hivyo, ili Magufuli ashinde, inategemea zaidi mshikamano ndani ya CCM. Na nikiongelea mshikamano simaanishi matukio yanayoanza kujitokeza ya makundi ya wana-CCM kadhaa kuhama chama hicho na kujiunga na vyama vya upinzani. Ninamaanisha wanasiasa wenye nguvu na ushawishi katika chama hicho kumuunga mkono mgombea wa chama chao au kumsaliti.

Lakini tangu Lowassa ajiunga na Chadema/UKAWA, sijaona kile kilichotarajiwa kuwa ‘mafuriko’ ya viongozi muhimu wa CCM na maelfu ya wanachama kukiasi chama hicho tawala na kujiunga na wapinzani. Kwahiyo, yayumkinika kuhisi kuwa hadi muda huu Magufuli bado ana sapoti ya kutosha ndani ya chama chake.
Kanuni isiyo rasmi ya siasa za uchaguzi Barani Afrika ni kwamba ‘chama tawala hakishindwi uchaguzi, na kikishindwa basi si kwa sababu wapinzani wana nguvu kubwa bali migongano ndani ya chama tawala inayotoa fursa kwa wapinzani.’ Sawa, labda CCM kumkata jina la Lowassa wakati wa mchujo wa wagombea wake kumesababisha mpasuko wa aina flani, lakini kama nilivyobainisha hapo juu, mpasuko huo sio mkubwa kama ilivyotarajiwa, na sidhani kama unaweza kuwa na athari kubwa kwa CCM.
Kwahiyo, kwa upande wa Magufuli, takriban mazingira yote yaliyowawezewezesha wagombea wenzake wa nafasi ya urais huko nyuma kufanya vizuri bado yapo ilhali vikwazo dhidi ya yeye kufanya vizuri ni hafifu, na pengine vya kufikirika zaidi kuliko uhalisia.
Twende kwa Lowassa. Mtaji mkubwa wa mwanasiasa huyo ni umaarufu wake. Iwapo umaarufu huo unachangiwa na kinachoelezwa kuwa ni uwezo wake mkubwa wa kifedha au ‘uchapakazi’ wake, hilo ni suala linalohitaji mjadala katika makala tofauti. Lakini kilicho bayana ni ukweli kwamba umaarufu ni turufu muhimu kwa mgombea yeyote yule katika uchaguzi.

Turufu nyingine kwa Lowassa ni hali halisi ilivyo katika mahusiano kati ya CCM na Watanzania wengi. Kwa muda mrefu chama hicho tawala kimekuwa kikichukulia chaguzi mbalimbali, kuu na ndogo, kama utaratibu tu wa kukipatia nafasi za uongozi. Hakijawahi kupigania ‘kufa na kupona’ kubaki madarakani. Kwa sababu nilizozitoa hapo juu, ukichanganya na udhaifu wa wapinzani wake, bila kusahau hujuma mbalimbali dhidi yao, tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, chama hicho tawala kimekuwa kikiingia kwenye chaguzi kikiwa na uhakika mkubwa wa kushindwa.
Hata hivyo, safari hii kinaweza kukumbana na ushindani mkubwa (japo hadi muda huu ni suala la kufikirika zaidi) baada ya kada wake maarufu kabisa, Lowassa, kujiunga na wapinzani. Sasa kwa vile CCM haijawahi na haijazowea kuwa katika mazingira yaliyopo sasa, yayumkinika kuhisi kuwa inaweza ‘kupaniki’ na hivyo kutoa mwanya kwa Lowassa na Chadema/UKAWA yake kufanya vizuri.
Lowassa na Chadema/UKAWA wanatambua bayana kuwa kuna mamilioni ya Watanzania waliokwishaichoka CCM na pengine wangependa kuoina iking’oka madarakani. Ni rahisi kwa wapinzani hao kubainisha ‘maovu’ ya chama hicho tawala kwa sababu mengi yanaonekana waziwazi. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa kuna ‘mazuri’ kadhaa ya utawala wa CCM, na uzoefuwaonyesha kuwa chama hicho tawala ni mahiri katika kuyanadi ‘mazuri’ hayo, ambayo pia si vigumu kuyaona.
Kikwazo kwa Chadema/UKAWA ni jinsi ya kubadili maelezo waliyoyasimamia kwa muda mrefu kuwa ‘Lowassa ni fisadi.’ Kwa mitizamo wangu, muda uliosalia haitoshi kwa vyama hivyo vinavyounda UKAWA kuwashawishi Watanzania kuwa ‘Lowassa sasa si fisadi kwa vile amejiunga nasi tuliokuwa tunapambana na ufisadi.’ Na kwa bahati mbaya, hasa kwa Chadema ambayo ilikuwa mahiri kukemea ufisadi, Watanzania wengi tu wanaonekana kutafsiri Lowassa kukubaliwa kujiunga na chama hicho ni usaliti kwa wengi waliokiamini.
Hoja kwamba ili ukiondoa CCM kuna haja ya kushirikiana na watu kama Lowassa inakabiliwa na hoja mbadala kuwa ‘kwanini tuwaamini watu msio na uwezo wa kuleta mabadiliko wenyewe hadi mtegemee makapi ya CCM?’ Hoja hiyo mbadala inapewa nguvu na ukweli kuwa UKAWA ‘walisuasua’ kwa muda mrefu kutangaza mgombea wao, na sasa twajua kuwa walikuwa wanamsubiri mwana-CCM kama Lowassa awasaidie.
Lakini mtihani mwingine kwa UKAWA na Lowassa ni huu: Magufuli anagombea urais kwa tiketi ya CCM, ambayo sio tu ni chama tawala na ambacho kipo madarakani hata kabla ya ujio wa mfumo wa vyama vingi, lakini pia kinafahamika kwa wengi. Kwa UKAWA, na hili ni kosa lao kwa kuchelewa kupata mgombea wao wa kiti cha urais, inaonekana kama ni chama ‘kipya’ cha siasa. Laiti muungano huo wa vyama vinne vya siasa (Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD) ungepata mgombea wake mapema, na kumnadi kwa nguvu wakati CCM inahangaika kupata mgombea wake, basi muda huu wangekuwa na kazi moja tu ya kupambana na Magufuli na CCM kwani wao tayari wangeshakuwa wanajulikana kwa wengi.
Vilevile, kuna suala nililozungumzia katika makala iliyopita ambapo, dalili zilizopo zinaashiria uchaguzi wa rais ni katika ya CCM na Magufuli wake dhidi ya Lowassa. Hapa ninamaanisha kwamba ni rahisi kumwona mgombea huyo wa CCM kama anayewakilisha chama chake ilhali kwa Lowassa ni kama ‘mgombea binafsi.’ Utafiti kidogo tu katika vyombo vya habari waweza kukuonyesha msomaji kuwa wakati ‘kampeni’ za CCM zimeelemea zaidi katika kumnadi Magufuli na CCM, kwa Chadema/UKAWA ni suala la kumnadi Lowassa pekee kana kwamba ni mgombea binafsi.
Na hilo linachangiwa na ukweli kuwa UKAWA si chama bali ushirikiano wa vyma ambavyo awali lengo lao lilikuwa suala la mabadiliko ya Katiba. Vyama hivyo vina sera tofauti, na japo vyawezxa kutengeneza ilani moja ya uchaguzi, muda hauko upande wao. Kwa CCM, ni mwendelezo tu wa walichokifanya mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010.
Kadhalika, wakati nimetaja kuwa umaarufu wa Lowassa ni mtaji wake mkubwa huko Chadema/UKAWA, pengine ni mapema mno kuhitimisha kuwa umaarufu huo alioupata akiwa CCM, utaendelea kuwa juu wakati huu amejiunga na Chadema/UKAWA. Ikumbukwe kuwa wapinzani wakubwa wa Lowassa alipokuwa CCM hawakuwa ndani ya CCM bali katika vyama hivyohivyo ambavyo leo vimemfanya mgombea wao wa urais. Hilo laweza kuirahisishia CCM jukumu la kumbomoa kwani ‘wanamjua vilivyo.’
Kikwazo kikubwa lakini kisicho wazi ni nafasi ya Idara ya Usalama wa Taifa katika uchaguzi huo, kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita. Hata tukiweka kando kile kwenye Baiolojia wanakiita ‘symbiotic relationship’ (uhusiano wa kutegemeana kati ya kiumbe kimoja na kingine) ambapo ustawi wa taasisi hiyo na wa CCM na serikali zake ni wa kutegemeana, Idara hiyo yaweza kutumia ‘kisingizio’ kama ‘Lowassa ni tishio kwa usalama wa taifa letu,’ ambapo kwa taratibu zisizo rasmi za Usalama wa taifa sehemu nyingi duniani, anaweza ‘kudhibitiwa.’ Hili ni gumu kulieleza kwa undani kutokana na sababu za kimaadili.
Nihitimishe makala hii ndefu kwa kuahidi kuendelea na uchambuzi zaidi kuhusu uchaguzi mkuu kwa ujumla, hususan katika nafasi ya urais, hasa ikitarajiwa kuwa tunaweza kushuhudia mengi zaidi ya tukio lililogusa hisia za wengi la aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba kujiuzulu ghafla, sambamba na ‘sintofahamu’ kuhusu hatma ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt Willibrord Slaa.

6 Aug 2015

NINAANDIKA makala hii nikiwa na masikitiko makubwa mno. Siku zote maishani, twajikuta katika kipindi kigumu sana pale mtu tuliyemwamini kwa dhati anapotugeuka. Wanasema, inachukua muda mwingi na jitihada kubwa kujenga uaminifu japo kosa au tukio moja tu laweza kuondoa kabisa uaminifu huo.
Na hicho ndicho walichofanya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kukubali kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowaasa, sio tu kuwa mwanachama wao bali pia mgombea wao katika nafasi ya urais.
Kama ambavyo tetesi kuwa Lowassa angechukua fomu kuwania urais kwa tiketi ya CCM zilivyozagaa kwa muda mrefu, ndivyo suala la Lowassa kujiunga na Chadema/ UKAWA lilivyokuwa.
Mara baada ya mwanasiasa huyo kukatwa katika mchakato wa CCM kumpata mgombea wake wa Urais, zilisikika tetesi nyingi kuwa kuna uwezekano angejiunga na moja ya vyama vinavyounda UKAWA, na hatimaye kuwa mgombea urais.
Lakini kwa vile Tanzania yetu haina uhaba wa tetesi, baadhi yetu tulidhani kuna ugumu kwa Lowassa kujiunga na UKAWA ni Chadema, kwa vile chama hicho kimejijengea umaarufu mkubwa kwa msimamo wake tuliodhani ni thabiti kupambana na ufisadi na mafisadi.
Na sio msimamo tu dhidi ya ufisadi na mafisadi, Chadema wamelipa gharama kubwa katika harakati zake ambapo baadhi ya wanachama wake walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya, huku wengine wakiishia rumande au magerezani kufuatia maandamano mbalimbali ya kutetea maslahi ya taifa na wanyonge.
Hata nilipoona picha zilizodaiwa kuwa ni za Lowassa akihudhuria moja ya vikao vya UKAWA nilijipa moyo kuwa huenda picha hizo zimefanyiwa ‘ufundi,’ wenyewe wanaita ‘photoshop,’ ambapo picha ya mtu inapandikizwa kwenye picha nyingine.
Faraja iliongezeka baada ya akaunti ya habari za Chadema katika mtandao wa Twitter, Chadema Media, kukanusha uwepo wa Lowassa katika kikao hicho. Hata hivyo muda mfupi baadaye, watu wa karibu na Lowassa walibandika picha zaidi katika mtandao huo kuthibitisha kuwa kweli Lowassa alihudhuria kikao hicho.
Na siku moja baadaye,’bomu lililipuka.’ Kupitia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ambayo sie tulio mbali tuliweza kuyaona mtandaoni, viongozi wakuu wa UKAWA walionekana na Lowassa, na baadaye mwanasiasa huyo kutangaza bayana kuwa amejiunga na umoja huo kupitia Chadema.
Ninachoweza kusema kwa kifupi ni kwamba walichofanya Chadema ni usaliti wa hali ya juu, na hakuna maelezo ya aina yoyote yanayoweza kuhalalisha kitendo hicho. Ndio, ni muhimu kwao kuingia Ikulu, lakini ni muhimu zaidi kwa Chadema kutambua imefikaje ilipo leo.
Jibu la wazi ni kama nilivyotanabaisha hapo juu; msimamo wao imara wa kuuchukia ufisadi na kupambana nao kwa nguvu zote, hatimaye ulifanikiwa kuwafumbua macho Watanzania wengi, sio tu kuhusu kansa ya ufisadi bali pia kujenga hisia kwamba chama hicho ni kwa ajili ya maslahi ya mamilioni ya Watanzania wanyonge na wahanga wakuu wa ufisadi.

Kwahiyo, kwa kumpokea Lowassa, mwanasiasa aliyelazimika kujiuzulu kwa tuhuma za ufisadi wa Richmond, Chadema wametelekeza nguzo muhimu iliyokuwa ikikitambulisha chama hicho. Na kama tunavyoina CCM, chama chochote cha siasa kinachotelekeza nguzo zake, sio tu kinapoteza uaminifu wake kwa jamii bali pia chajichimbia kaburi.
Sawa, labda Lowassa anaweza kushinda urais (hili lahitaji mjadala wa pepe yake) lakini haihitaji kuwa na ujuzi wa uchambuzi wa siasa zetu kubaini kwamba mwanasiasa huyo hakujiunga na Chadema kwa vile anakipenda chama hicho au anaafiki sera zao bali amekitumia kama ngazi ya kuwania urais baada ya kukwamishwa na CCM.
Hilo tu lilipaswa kuifumbua macho Chadema. Lowassa huyohuyo aliyejigamba kwamba jina lake halitakatwa akijivunia ‘uchapakazi’ wake, na utumishi wake wa muda mrefu katika CCM, leo hii kaitelekeza CCM licha ya kudai asiyemtaka ndani ya chama hicho aondoke lakini yeye si wa kuondoka.
Ni wazi kuwa Lowassa ni mwanasiasa mwenye tamaa ya madaraka. Sawa, Katiba yetu yamruhusu kugombea uaongozi kupitia chama chochote kile, lakini moja ya sifa nzuri kwa mwanasiasa ni msimamo na kutokuwa na tamaa ya madaraka.
Leo kaitosa CCM kwa kutaka urais, je ataitendaje Chadema katika kutaka mengineyo?
Lakini pia ni ukweli usiofichika kuwa umaarufu wa Lowassa unatokana na ‘sifa’ kuu mbili: uwezo mkubwa wa kifedha ‘zisizo na maelezo ya kutosha’ na skandali ya Richmond. Katika mazingira ya kawaida, na hasa katika zama hizi za ufisadi, ni vigumu mno kumnadi mwanasiasa wa aina hiyo.

Tayari kuna hisia kuwa ‘fedha zilibadilishana mikono’ hadi akina Freeman Mbowe kukubali kumpokea mwanasiasa huyo ambaye walikuwa wakimwandama kila kukicha kwa kumuita fisadi.
Kama ni fedha kweli au ‘umaarufu,’ tayari Lowassa ndio mnufaika maana kwa muda mfupi tu ndani ya chama hicho, mambo kadhaa yameshabadilika.
Mie nazifuatilia kwa karibu zaidi harakati za Chadema kupitia mitandao ya kijamii au tovuti za vyombo vya habari mbalimbali vya huko nyumbani. Nilichobaini katika siku chache hizi baada ya Lowasaa kujiunga na Chadema, ghafla wanachama na mashabiki wa chama hicho wamegeuka ‘mabubu’ kuhusu masuala ya ufisadi.
Na hilo si la kushangaza kwa sababu watamudu vipi kukemea ufisadi ilhali mgombea wao wa urais ni mtuhumiwa wa ufisadi?
Kwa mujibu wa maelezo ya mmoja wa viongozi wa Chadema, Tundu Lissu, chama hicho na UKAWA kwa ujumla walikuwa wakifuatilia kwa karibu mchakato wa CCM kupata mgombea wake, na wao walitaka kuitumia ‘sintofahamu’ hiyo ndani ya CCM kufanikisha malengo yao ya kuingia Ikulu.
Huu ni udhaifu wa hali ya juu. Lakini angalau hii imesaidia kutufahamisha kwanini chama hicho kilikuwa kinasuasua kumtangaza mgombea wake: kilikuwa kinasubiri ‘makombo’ ya CCM.
Watu hawa wanajifanya kusahau kabisa mafanikio makubwa tu waliyoyapata katika uchaguzi mkuu uliopita ambapo walisimama wenyewe, wakapata wabunge wa kutosha na madiwani wa kutosha tu, licha ya mgombea wao, Dkt Willbrord Slaa, kushindwa katika mazingira ambayo baadhi yetu tunaamini yalichangiwa na hujuma.
Na ni katika mazingira hayo, baadhi yetu tunaunga mkono Dk. Slaa kujitenga na Chadema. Ni matarajio yangu kuwa hatokubali kuwa sehemu ya usaliti huu hasa kwa kuzingatia gharama kubwa waliyoingia Chadema, kwa maana ya muda na jitihada, sio tu kukitambulisha chama hicho kuwa ni mtetezi wa wanyonge na kiongozi wa mapambano dhidi ya ufisadi bali pia kukiwezesha kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania.
Awali, nilipopata uthibitisho kuwa Lowassa amejiunga na Chadema nilitamka bayana kuwa ‘impact’ ya tukio hilo yapaswa kuonekana angalau ndani ya siku 7. Na siku hizo saba zimeisha juzi. Tuliambiwa tusubiri ‘mafuriko’ ya wana-CCM kumfuata Lowasaa huko Chadema/UKAWA.
Hadi sasa, hakuna dalili yoyote ya mafuriko hayo. Jina kubwa pekee lililojitokeza kumfuata Lowassa ni Naibu wa Kazi na Ajira, Dkt Makongoro Mahanga, ambaye hata hivyo amechukua uamuzi huo baada ya kubwagwa kwenye kura za maoni. Labda kuna wengine watakaomfuata Lowassa lakini sidhani kama watu hao watakuwa na mafuriko yanayotarajiwa.
Kikwazo kikubwa kwa makada wa CCM waliokuwa wakimsapoti mwanasiasa huyo kumfuata kwenye ‘chama chake kipya’ ni ukweli kwamba tayari vyama vinavyounda UKAWA vilishagawana majimbo.
Sasa sidhani kama kuna mwana-CCM mwenye akili zake atakikimbia chama hicho tawala na kujiunga na vyama vinavyounda UKAWA ilhali anatambua kuwa hata akishindwa ubunge au udiwani katika CCM bado ana fursa ya kuteuliwa kwenye nyadhifa nyingine serikalini.
Na ujio wa wafuasi wa Lowassa ndani ya Chadema na UKAWA unaweza kuvibadili vyama hivyo na kuunda makundi ya, kwa mfano, Chadema- asilia na Chadema-Lowassa. Busara za kisiasa zatuonya kuwa chama chenye mgawanyiko hakiwezi kushinda uchaguzi, na hata kikifanikiwa kushinda, hakitoweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Wakati kwa kumpokea Lowassa Chadema italazimika kutowekeza nguvu za kutosha katika mtaji wake mkuu katika uchaguzi mkuu uliopita – vita dhidi ya ufisadi (hawawezi kupigia kelele ufisadi huko mgombea wao akiwa mtuhumiwa wa ufisadi) – ni vigumu kubashiri watamnadi Lowassa kwa lipi hasa.
Wao ndio walikuwa vinara wa kumwita Lowassa fisadi, sasa muda haupo upande wao kubadilisha maelezo na kumnadi kama mtu safi.
Na hata maelezo ya Lowassa kuwa ‘alipata maagizo ya juu’ katika suala la Richmond hayana uzito kwa sababu kwanini aongee sasa na si wakati alipobanwa hadi kujiuzulu? Sawa, wengi twafahamu kuwa skandali hiyo iliwahusisha watu wengine pia, lakini ukweli unakuwa na nguvu pale tu unapowekwa hadharani wakati mwafaka.
Ni rahisi kwa CCM kuipangua hoja ya Lowaasa kuwa ‘alitumwa’ kwa kumuuliza ‘ulikuwa wapi siku zote hizi usiyaseme hayo hadi sasa ulipoamua kuingia upinzani kwa tamaa yako ya madaraka?’
Nimalizie makala hii endelevu kwa kurejea kuwakumbusha Chadema kuwa dhambi yao ya usaliti itawaandama milele. Hoja kuwa Lowassa ‘anauzika’ na atawasaidia kuingia Ikulu sio tu haina msingi bali pia yaweza kuwagharimu huko mbeleni hasa kwa vile, kama nilivyoandika hapo juu, mwanasiasa huyo hajajiunga na chama hicho kwa vile anakipenda bali kwa ajili ya maslahi yake binafsi.
Nachungulia kidogo tu ‘marafiki zake’ kisha utaelewa nini kinaisuburi Chadema huko mbeleni. Mie si nabii wa majanga (prophet of doom) lakini ninabashiri kuwa ujio wa Lowassa huko Chadema ni mwanzo wa mwisho wa chama hicho.
Inasikitisha kuona ‘People’s Power’ (nguvu ya watu) iliyowavutia wapenda mabadiliko wengi ikiishia kuwa ‘Money’s Power’ (kwa maana ya nguvu ya Lowassa kifedha).Pia inaumiza kuona demokrasia yetu ikipitia mlolongo huu usiopendeza wa ‘chama kimoja→ vyama vingi → chama cha mtu mmoja’ (one party→multiparty→one man’s party)
ITAENDELEA

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.