Showing posts with label Habari. Show all posts
Showing posts with label Habari. Show all posts

21 May 2015


WAZIRI mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, ameanza kuwaandaa wafuasi wake kwa uwezekano wa kujiunga na mojawapo ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Raia Mwema limeelezwa.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka katika kambi ya mgombea huyo zinaeleza kuwa amepiga marufuku mazungumzo yoyote ya kutafuta mbadala wake ndani ya CCM na kutaka nguvu yote ielekezwe kwake.

Gazeti hili limeelezwa kuwa wapo watu walio ndani ya kambi yake wanaoamini kwamba anahitajika mwanasiasa mwingine ndani ya kundi hilo ambaye anaweza kuvaa viatu vya Lowassa endapo CCM itaamua kumkata au kuendeleza adhabu yake ya kutofanya shughuli za siasa aliyopewa na chama chake.

Hata hivyo, kundi hilo linadaiwa kuwa na wakati mgumu kwa madai kwamba Lowassa hataki kusikia chochote kuhusu suala hilo.

“Anasema yeye ndiyo Plan A, Plan B na Plan C. Kama, kwa sababu yoyote ile, CCM itaamua kumpitisha mgombea mwingine na si yeye, yuko tayari kujiunga na Ukawa lakini si kubaki ndani ya chama.

“Hili ndilo jambo linalotusumbua sana kwa sasa. Hakuna vita ambayo ina mpango mmoja tu. Lazima muwe na mpango zaidi ya mmoja. Huku Pwani wanasema ukienda kuteka maji wakati wa ukame, ni muhimu uwe na ndoo na kidumu cha kushika mkononi.

“Kwenye kutembea na ndoo mtu unaweza kujikwaa na maji yote yakamwagika na kile kidumu cha mkononi ndiyo kikakuokoa. Sasa huyu bwana hataki kusikia habari ya kidumu.
“Anataka twende kutafuta maji na ndoo moja tu ambayo ni yeye. Hili linatupa shida kidogo kwa sasa,” alisema mbunge mmoja wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye ni mtu wa karibu na mtarajiwa huyo.

Katika kambi ya Lowassa, kuna majina ya wanasiasa vijana ambao wanatajwa kuwa tayari kuvaa viatu vyake endapo CCM itaamua tofauti na matarajio yao.

Miongoni mwa wanasiasa wanaotajwa kuwa katika kambi ya Lowassa na ambao kambi inayotaka Plan B inawapendekeza ni Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi, Mbunge wa Sengerema William Ngeleja, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.

Miongoni mwa wanaotajwa, Dk. Nchimbi anaelezwa kuwa na nguvu zaidi kutokana na ukweli kwamba ndiyo mwenye ushawishi zaidi ndani ya chama kutokana na ukweli kuwa amekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kwa zaidi ya miaka 10.

Kimsingi, kwa upande wa Tanzania Bara, hakuna mwana CCM aliyedumu katika Kamati Kuu ya chama hicho kwa muda mrefu kuliko Nchimbi miongoni mwa waliomo sasa, ukimwondoa Rais Jakaya Kikwete.


Anasema Mbunge huyo: “ Tunajaribu kumshawishi Lowassa akubali kuwa akikosa yeye, basi apatikane mtu ambaye ataweza kuyafanya yale aliyopanga kuyafanya kupitia CCM. Kwa sasa, hili hajakubaliana nalo,” kilisema chanzo hicho cha gazeti hili ambacho hakikutaka kuwekwa jina lake wazi.

Hata hivyo, kwa vile Ukawa si chama cha siasa, kama Lowassa ataamua kuhama CCM, ni lazima ajiunge na mojawapo ya vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na National League (NLD).

Akizungumzia taarifa hizo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema kwa sasa hawataki kujihusisha na mambo ya ndani ya CCM na badala yake wanaangalia namna ya kukishinda kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.

“Sisi sasa hivi lengo letu kubwa ni kuijenga Ukawa kitaasisi na kuifanya iwe tishio katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.

“Kamanda, sitaki kuzungumza kama tutampokea au hatutampokea Lowassa kama akiamua kuhamia Ukawa. Mambo ya CCM waachie CCM wenyewe. Mimi nakuhakikishia kuwa wakati wa uchaguzi ukifika; CCM wamweke Lowassa, au Membe, sijui Makongoro Nyerere ama yeyote mwingine, Ukawa itashinda tu kwenye uchaguzi huo,” alisema Mbowe kwa kujiamini.

Juhudi za kuwapata wenyeviti wenza wengine wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, James Mbatia na Emmanuel Makaidi hazikufanikiwa hadi tunakwenda mitamboni juzi Jumatatu.

Kwa sasa, Lowassa na wanasiasa wengine watano ndani ya CCM wako katika kifungo cha muda usiojulikana walichowekewa na chama chao kutokana na madai ya kukiuka taratibu za chama hicho.

Wanasiasa wengine walio katika kifungo hicho ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe; Ngeleja na waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.

Ilivyokuwa chaguzi mbili zilizopita
Taarifa hizi za uwezekano wa Lowassa kuhamia Ukawa hazitofautiani na zile zilizoibuka mwaka 2005 wakati ilipodaiwa kuwa Kikwete angehamia Chadema endapo CCM isingempitisha.

Wakati huo, zilikuwapo taarifa kuwa CCM ilikuwa na mpango wa kumwondoa Kikwete kwenye kinyang’anyiro hicho kutokana na kutokidhi vigezo vya kimaadili vya chama hicho.
Hata hivyo, Kikwete hatimaye alipitishwa na chama chake kuwania urais na kushinda kwa kishindo.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2010, baadhi ya wanachama wa CCM walitajwa kutaka kujiunga na Chama cha Jamii (CCJ) na mmoja wao, Fred Mpendazoe, aliachia ubunge wake kabla ya wakati ili kuanza kazi ya kukijenga chama hicho.

Wakati huo, CCJ ilidaiwa kuwa na mkono wa wana CCM waliokuwa wakipinga kukithiri kwa ufisadi ndani ya chama hicho.

Miongoni mwa majina mazito yaliyokuwa yakihusishwa na kujiunga na CCM yalikuwa ni Samuel Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe.

CHANZO: Raia Mwema

WAKATI HUOHUO,

BALOZI wa kudumu wa Umoja wa Afrika (AU), huko Marekani, Mtanzania Amina Salum Ali, ametangaza  kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, 2015.

[aminaali.jpg]
Balozi Amina ametangaza uamuzi wake huo mapema leo  jijini Dar es Salaam.

Itakumbukwa ya kuwa Balozi Amina ambaye alidumu kwa muda mrefu kama waziri kwenye serikali ya Rais mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Salmin Amour Juma, almaarufu kama (Komandoo), aliwahi kutupa karata yake kuwania urais wa Zanzibar, kabla ya kujitoa.

Huyu anakuwa mwana mama wa kwanza kwenye historia ya chama cha Mapinduzi CCM, kutangaza kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Hali kadhalika, Balozi Amina rekodi yake ya kwanza ni kuwa mwanamke wa kwanza kuwa balozi wa kudumu wa AU huko Marekani.

Mbali na kuwahi kuwa waziri, Balozi aAmina ndiyo muasisi wa taasisi ya Zanzibar Women Welfare Trust, inayojishughulisha na kupambana na afya ya akina mama na watoto hususan kwenye eneo la maambukizi ya VVU.ANGALIZO: Makala hii ilipaswa kuchapishwa gazetini wiki iliyopita lakini nilichelewa kutimuma gazetini.Pia, kwa kiasi kikubwa, kichwa cha habari cha makala hii gazetini kinatofautiana na kilichomo ndani ya makala (na ndio maana kipo tofauti na hapa bloguni.Samahani kwa hilo)
HIVI karibuni, Uingereza ilifanya uchaguzi wake mkuu ambapo chama kilichokuwa madarakani kwa kushirikiana na chama kingine cha Liberal Democrats cha Conservatives kilipata ushindi wa kishindo.
Moja ya mambo yanayoweza kukumbukwa kwa muda mrefu kuhusu uchaguzi huo ni jinsi matokeo ya mwisho yalivyokuwa tofauti kabisa na ubashiri wa kura mbalimbali za maoni. Kimsingi, matokeo hayo ambayo hayakutarajiwa kabisa yamepelekea baadhi ya wachambuzi wa siasa kuhoji ufanisi wa kura za maoni katika kubashiri matokeo ya chaguzi.
Na katika hatua nyingine, kunatarajiwa kuundwa tume huru ya uchunguzi kudadisi kwanini kura za maoni zilibashiri matokeo tofauti sana na matokeo halisi (na hii inaonyesha jinsi ‘wenzetu’ walivyo makini hata katika tatizo dogo tu).
Hadi siku ya uchaguzi, kura mbalimbali za maoni zilikuwa zikibashiri kuwa vyama vya Conservatives na Labour vingepata matokeo yanayokaribina na kufungamana, na hivyo kupelekea kitu kinachofahamika kama ‘hung parliament.’
Pengine ni vema nitumie fursa hii kuelezea kidogo kuhusu uchaguzi mkuu hapa jinsi ulivyo.Hapa hatuna rais, na japo mkuu wa nchi ni Malkia, mtendaji mkuu wa serikali ni Waziri Mkuu.
Malkia, kama zilivyo tawala za kifalme hapigiwi kura. Na uongozi wake wa nchi ni wa kiheshima (ceremonial) kuliko kiutawala.
Katika uchaguzi mkuu kama huo uliofanyika majuzi, wapiga kura wanachagua wabunge wa vyama mbalimbali na idadi ya viti itakavyopata chama katika uchaguzi ndivyo vitaamua nafasi yake katika kuunda serikali.
Namba ya ushindi inayohitajika ili chama kiunde serikali ni viti 326 kati ya viti vyote 650. Iwapo vyama vyote havitofikia idadi hiyo, basi hali inakuwa kama ilivyotokea katika uchaguzi mkuu uliopita, ambapo Conservatives walipata viti 307, Labour viti 258 na Liberal Democrats viti 57. Matokeo hayo ndiyo yanayojulikana kama ‘hung parliament.’
Kutokana na hali hiyo, chama cha Conservatives kiliamua kufanya ushirikiano na chama cha Liberal Democrats na kuunda serikali ya ushirikiano, kwa kimombo coalition government. Kwahiyo katika miaka mitano iliyopita, serikali ya hapa ilikuwa inaongozwa na ushirikiano wa vyama hivyo, ambapo Waziri Mkuu alikuwa David Cameron kutoka Conservatives na Naibu wake Nick Clegg wa Liberal Democrats.
Turejee kwenye kura za maoni. Hadi siku ya uchaguzi, kura nyingi za maoni zilibashiri kuwa Conservatives na Labour wangefungana kwa asilimia takriban 34 (kwa mujibu wa kampuni ya kura za maoni inayoheshimika sana hapa ya YouGov).
Kutokana na hali hiyo, na kwa vile ilitarajiwa kuwa Liberal Democrats wangepata matokeo mabaya (kulikuwa na hofu kuwa kiongozi wa chama hicho, Clegg, angepoteza jimbo lake), chama tawala cha hapa Uskochi, Scottish Nationalist Party (SNP) kilionekana kama ndicho kingeamua hatma ya nani kati ya Conservatives na Labour aunde serikali.Kura za maoni zilikuwa zikibashiri kuwa SNP ingepata majimbo 58 kati ya yote 59 ya hapa Uskochi.
Dalili za kwanza kwamba kura za maoni ‘zilipotea njia’ zilijitokeza sekunde chache tu baada ya vituo vyote vya kupigia kura kufungwa (saa nne usiku). Kwa kawaida ya hapa (na katika nchi nyingine zenye mfumo wa uchaguzi kama huu wa hapa), mara baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa, kunatangazwa kitu kinachojulikana kama exit poll.
Hii ni kura ya maoni inayofanywa kwa kuuliza sampuli ya wapigakura (katika uchaguzi huo wa majuzi, sampuli ilikuwa ya watu 22,000) wamekipigia kura chama gani au mgombea gani.
Matokeo ya sampuli hiyo hutumika kubashiri matokeo ya uchaguzi mzima kwa ujumla.
Sasa, exit poll iliyotangazwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ilibashiri kuwa Conservatives ingepata viti 316, Labour 239, Liberal Democrats 10, SNP 58 pamoja na ubashiri wa matokeo ya vyama vinginevyo.

Hiyo ilikuwa tofauti kabisa na ubashiri wa kura za maoni kadhaa kabla na siku ya uchaguzi zilizoonyesha Conservatives wangepata takriban viti 280, Labour takriban 270, 18 kwa Liberal Democrats na 55 kwa SNP.
Je, kwanini kura zile za ubashiri zilibashiri tofauti sana na exit polls na hatimaye matokeo ya jumla? Ni vigumu kupata jibu rahisi lakini inaelezwa kuwa huenda moja ya sababu ni watoa maoni wengi katika kura za maoni kusema tofauti na walivyotenda, yaani majibu ya wengi yalikuwa tofauti na jinsi walivyopiga kura. Hata hivyo, sababu halisi zinatarajiwa kufahamika baada ya tume huru iliyoundwa kuchunguza kasoro hiyo kumaliza kazi yake.
Matokeo ya mwisho yalikuwa kama ifuatavyo: Conservatives viti 331, Labour viti 232, SNP viti 56, Liberal Democrats viti 8 na vyama vinginevyo viti 23. Kwa matokeo hayo, Conservatives walifanikiwa sio tu kupata idadi ya viti 326 vinavyohitajika kuunda serikali pepe yake, bali pia ilipata viti vitano Zaidi. Kwahiyo, David Cameron amerejea madarakani na chama chake cha Conservatives kinaunda serikali pasi kuhitaji ushirikianoi na chama kingine ukilinganisha na ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu uliopita.
Tukiweka kando ‘ubashiri fyongo’ wa kura za maoni, moja ya matukio ya kihistoria katika uchaguzi huo ni mafanikio makubwa ya SNP, chama ambacho katika uchaguzi mkuu uliopita kiliambulia viti 6 tu lakini safari hii kimesomba viti 56, ikiwa ni viti vitatu tu pungufu ya kuomba viti vyote 59 vya Uskochi. Mafanikio ya SNP yamekuwa habari mbaya mno kwa Scottish Labour na Scottish Liberal Democrats ambavyo pamoja na Scottish Conservatives wameambulia viti vimoja vimoja. Kibaya zaidi, hata kiongozi wa Scottish Labour Jim Murphy alibwagwa katika uchaguzi huo, na hatma yake kisiasa ipo mashakani.
Baada ya uchaguzi huo kumalizika, kiongozi wa Labour Ed Miliband alitangaza kujiuzulu, sambamba na Nick Clegg wa Liberal Democrats.Awali, kiongozi wa chama cha kibaguzi cha UKIP, Nigel Farage, aliapa kuwa akishindwa katika jimbo alilokuwa anagombea angejiuzulu.
Alishindwa, lakini chama hicho kimemwomba aendelee kuwa kiongozi wake. Tofauti na matarajio ya awali, na ‘mvuto’ wake katika sera dhidi ya wahamiaji na uwepo wa Uingereza katika umoja wa Ulaya, chama hicho kiliambulia jimbo moja tu.

Wengi wa wachambuzi wa siasa za hapa wanatarajia kuwa miaka mitano ya Cameron na Conservatives kuwa sio rahisi. Changamoto kubwa zaidi ni kuzuia Uskochi kudai kura nyingine ya maoni kuhusu uhuru wake, na kwa upande mwingine ni sokomoko la Uingereza kujitoa katika Jumuiya ya Ulaya.
Kwa hilo la ‘uhuru wa Uskochi,’ wachambuzi wengi wanatafsiri ushindi mkubwa wa SNP kama ‘idhini isiyo rasmi’ kwa chama hicho kudai tena kura ya maoni (referendum) ya uhuru, baada ya iliyofanyika mwaka jana kushindwa kuamua Uskochi iendelee kubaki katika ‘muungano wa Uingereza’ kwa tofauti ya kura chache tu.
Licha ya ukweli kuwa matokeo hayo ya ‘kura ya maoni ya uhuru wa Uskochi’ imepeleka umaarufu mkubwa kwa SNP, huku ikivuna idadi kubwa kabisa ya wanachama wapya, kauli za Cameron wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa majuzi dhidi ya chama hicho tawala Uskochi, zinaelezwa kutafsiriwa na wengi wa wapigakura wa hapa (Uskochi) kama ‘chuki dhidi ya taifa lao,’ na hivyo kuamua kukisapoti ‘chama chao’ (SNP) kwa wingi. Sapoti hiyo inaweza kuwa na umuhimu mkubwa iwapo SNP itaamua kudai kura nyingine ya maoni ya ‘uhuru wa Uskochi.’
Kwa upande wa hatma ya Uingereza katika Jumuiya ya Ulaya, Cameron ameshaahidi kutekeleza azma yake ya kuitisha kura ya maoni iwapo nchi hii iendelee na uanachama wake au ijitoke, kabla ya mwisho wa mwaka keshokutwa. Huu utakuwa mtihani mkubwa sana kwa Cameron na Conservatives kwa ujumla.
Wakati wahafidhina ndani ya chama hicho wakipigania kwa udi na uvumba Uingereza ijitoke, kuna idadi kubwa tu ya Waingereza wanaodhani wazo hilo ni baya na hatari kwani linaweza kuiathiri nchi yao kiuchumi na kisiasa za kimataifa.
Je kuna lolote Watanzania twaweza kujifunza kutoka katika uchaguzi huo mkuu wa Uingereza? Yapo mengi, lakini machache ni pamoja na mfumo imara kabisa, tofauti na wetu unaoonekana kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu (Tume yetu ya Uchaguzi inataka wananchi wasisikie maneno ya pembeni, lakini mazingira yaliyopo yanapelekea hofu iwapo uchaguzi mkuu utafanyika kweli hapo Oktoba).
Kingine ni nafasi ya sera za vyama katika kushawishi wapiga kura. Moja ya sababu zinazotajwa kupelekea Labour kufanya vibaya ni sera zake zilizoonekana kuwatenga wafanyabiashara wadogowadogo na kutowapa kipaumbele watu wa tabaka la kati. Kwa uapnde mwingine, inaelezwa kuwa ushindi wa Conservatives ulichangiwa zaidi na mvuto wa sera zake za kiuchumi kwa wapigakura.
Kadhalika, jingine ambalo vyama vyetu vya siasa huko nyumbani vyaweza kujifunza ni uchaguzi wa mgembea anayekubalika.Kwa kiasi kikubwa, kampeni za Labour ziligubikwa na hofu ya uwezo binafsi wa Ed Miliband kumudu Uwaziri Mkuu.
Nimalizie makala hii kwa kuwapongeza Waingereza kwa kuendesha Uchaguzi Mkuu kwa ufanisi mkubwa, kuanzia mwenendo wa kampeni ambapo kwa asilimia kubwa ulihusu sera badala ya ‘madongo,’ idadi kubwa ya wapigakura iliyojitokeza (asilimia 66.10) na uungwana wa walioshindwa matokeo kuyakubali matokeo, sambamba na Miliband na Clegg kujiuzulu kutokana na vyama vyao kufanya vibaya.
Wakati nina matumaini hafifu kuona kura ya maoni ikifanyika kabla ya uchaguzi mkuu wetu hapo Oktoba, ninajipa moyo kuwa serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wataongeza bidii ili kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu unafanyika kama ilivyopangwa.
Kutokana na kuporomoka kwa thamani ya shilingi yetu, na hali yetu mbaya kiuchumi, ni muhimu kwa watawala wetu kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, tujibane na kidogo tulicho nacho (tukitarajia wafadhili watatumbukiza fedha zao katika ‘bakuli’ letu) ili tuwezeshe uchaguzi huo kufanyika kwa ufanisi na amani.

7 May 2015

Leo hapa Uingereza tunafanya uchaguzi Mkuu kuchagua chama kitachotuongoza miaka mitano ijayo.Kwa kifupi, tofauti na huko nyumbani, katika uchaguzi mkuu huu wa leo tunawapigia kura wabunge.Hapa hatuna Rais, Mkuu wa nchi ni Malkia japo mkuu wa serikali ni Waziri Mkuu anayetokana na chama kitakachoshinda viti vingi vya ubunge.
Viongozi wa vyama vikuu vinavyoshirikia uchaguzi mkuu unaofanyika leo: Kutoka kushoto kwenda kulia: Natalie Bennett wa Green Party, Nick Glegg wa Liberal Democrats, Nigel Farage wa UKIP, Ed Miliband wa Labour, Leanne Wood  wa Plaid Cymru (Wales), Nicola Sturgeon (Scottish Nationalist Party-Scotland) na David Cameron (Conservatives na Waziri Mkuu wa sasa)

Hata hivyo, mchuano ni mkali sana na hadi muda huu ni dhahiri kuwa hakuna chama kitakachopata viti vya kutosha kuunda serikali peke yake bila kushirikiana na chama kingine. Sasa iwapo hali itakuwa hivyo katika matokeo - ni vigumu kubashiri kwa uhakika kuwa hakuna uwezekano wa chama kimoja kuibuka na ushindi wa kukitosheleza kuunda serikali peke yake, kwa sababu lolote laweza kutokea katika masaa machache yajayo kabla ya kuanza kwa uchaguzi na likabadili mwelekeo.

Serikali inayomaliza muda wake inaundwa na chama cha Conservatives ambacho ndicho cha Waziri Mkuu wa sasa David Cameron, kwa kushirikiana na chama cha Liberal Democrats ambacho ndio cha Naibu Waziri Mkuu Nick Clegg. 

Ili chama kiweze kuunda serikali peke yake bila kuhitaji ushirikiano na chama kingine, kinahitajika kushinda viti 326.Iwapo hakuna chama kitachofikia idadi hiyo ya vitu, kunapatikana kitu kinachoitwa 'hung parliament' kama ilivyotokea katika uchaguzi mkuu uliopita (mwaka 2010) ambapo Conservatives walipata viti 307,Labour 258 na Liberal Democrats 57, na kwa vile hakuna aliyefikia idadi ya viti 326, Conservative na Liberal Democrats wakakubaliana kuunda serikali ya ushirikiano.

Nimeandika swali hapo juu, nani kuibuka mshindi? Well, njia kuu inayotumika katika chaguzi kubashiri ushindi wa chama kama uchaguzi ni kura za maoni (opinion polls).Kwahiyo, ili kupata mwangaza wa nani anaweza kupata nini, hapa chini ninaorodhesha matokeo ya kura za maoni kutoka makampuni mbalimbali yanayojihusisha na shughuli hiyo:
Utabiri wa matokeo na uwezekano wa ushirikiano wa vyma kuunda serikali ya pamoja
Embedded image permalink
Embedded image permalink


29 Apr 2015

Inasikitisha, inaumiza, inashangaza, na inaacha maswali mengi kuliko majibu kila tunaposikia “ajali yauwa...ajali yajeruhi...” Ndio, matukio ya ajali huko nyumbani yamekuwa kama jambo la kawaida kutokana na mfululizo wake, lakini hali ilivyo sasa ni ya kutisha.
Huko nyuma niliandika takriban makala mbili kuhusu suala hili la ajali, sio tu kwa vile tukio lolote linalopelekea kupotea kwa uhai wa wenzetu linaumiza nafsi bali pia kutokana na ukweli kwamba kwa hapa Uingereza ajali ndogo tu ni tukio linalokamata hisia za takriban nchi nzima, kinyume na ilivyozoeleka huko nyumbani.

Wakati ajali zinaendelea kuteketeza maisha ya Watanzania wenzetu, angalau kwa mara ya kwanza Taifa linaonekana kuguswa, na tayari zimeanza harakati za uhamasishaji dhidi ya ajali katika mitandao mbalimbali ya kijamii. Hata hivyo, ukweli mchungu unabaki kuwa ajali bado zinaonekana kama matukio ya kawaida tu.
Sijui lini taifa limeonyesha kuguswa na vifo vilivyotokana na ajali kiasi cha angalau bendera kupepea nusu mlingoti. Sijui sababu ni kwamba ajali zimezoeleka mno, au kwa vile ‘ajali haina kinga,’ au kwa sababu wahanga wengi wa ajali za barabarani ni ‘watu wa kawaida.’
Kabla sijaanza kuandika makala hii nilisoma habari kuhusu vurugu zilizotokea huko Korea ya Kusini katika maadhimisho ya mwaka mmoja tangu itokee ajali mbaya ya feri iliyosababisha vifo takriban 300. Hakuna anayefahamu kinachojiri baada ya kifo, lakini yayumkinika kuamini kuwa marehemu wasingependa kukumbukwa kwa vurugu. Lakini vurugu zilizotokea huko Korea ya Kusini ni ishara ya wananchi kukerwa na jinsi serikali yao ilivyoshughulikia janga hilo, hata kama haikuisababisha.
Hapa simaanishi kwamba Watanzania nao waingie mtaani na kufanya vurugu kuisukuma serikali ichukue hatua stahili dhidi ya ajali. Hata hivyo, ni muhimu angalau kuiamsha serikali kwa kuifahamisha kuwa hatuwezi kuangalia tu maisha ya Watanzania yakiteketea kama hayana thamani kutokana na mfululizo wa ajali. Busara kwamba ‘ajali haina kinga’ hai-apply katika nyingi ya ajali zinazotokea huko nyumbani.
Kwa mtizamo wangu, chanzo kikubwa cha ajali ni rushwa. Rushwa inayowezesha madereva wasio na sifa kuwa barabarani huku wakihatarisha uhai wa abiria wao. Rushwa inayoruhusu magari mabovu yabebe abiria na kuweka rehani uhai wa abiria. Rushwa inayofumbia macho makosa ya madereva barabarani na hivyo kuwapa imani kuwa hakuna kitu kiitwacho ‘kosa kinyume cha sheria za usalama barabarani’ alimradi dereva ana uwezo wa ‘kumpoza’ askari wa usalama barabarani.
Wanasema ‘rushwa huuwa.’ Na katika janga hili la mfululizo wa ajali, rushwa inauwa kweli kweli, na inaendelea kugharimu maisha ya Watanzania wenzetu kila kukicha.
Rushwa imekuwa sehemu ya maisha ya kawaida ya Mtanzania, na sintoshangaa iwapo baadhi ya wasomaji ‘wataniona mtu wa ajabu’ kwa kuhitimisha kuwa rushwa ni chanzo kikuu cha ajali huko nyumbani. Kwa wengi, rushwa ni tukio la muda mfupi tu linalorahisisha au kuwezesha upatikanaji wa huduma au bidhaa. Hata hivyo, ukweli mchungu ni kwamba rushwa ni kama kansa, inaitafuna jamii taratibu, na siku ya siku, madhara yake makubwa hujitokeza hadharani.
Mfano mmoja kuhusu athari za rushwa ni suala la ugaidi nchini Kenya. Wachambuzi wa masuala ya usalama wanahitimisha kuwa kwa kiasi kikubwa tu, rushwa katika vyombo vya dola nchini Kenya imewarahisishia magaidi wa Al-Shabaab kutimiza malengo yao kuishambulia nchi hiyo.
Kwa huko nyumbani tumeshuhudia matatizo mengine ya kijamii yanavyorutubishwa na rushwa. Mfano rahisi ni kushamiri kwa biashara ya madawa ya kulevya. Tanzania yetu sasa ni miongoni mwa vituo vikuu vya biashara hiyo duniani, na kilichotufikisha katika nafasi hiyo isiyopendeza hata kidogo ni urahisi wa kuingiza na kutoa madawa ya kulevya nchini mwetu. Niwe mkweli, kila ninaposikia polisi wamekamata kiasi fulani cha madawa ya kulevya, hisia yangu ya kwanza ni madawa hayo yaliyokamatwa yataishia kumnufaisha mtendaji fulani wa taasisi zenye wajibu wa kuyadhibiti.
Takriban kila dereva na abiria anafahamu jinsi askari wa usalama barabarani walivyogeuza rushwa kuwa haki yao. Kibaya zaidi, madereva wengi nao wamejenga fikra kuwa kutoa rushwa kwa askari wa usalama barabarani ni wajibu wao. Hili ni janga: rushwa kama haki wa wapokeaji na wajibu kwa watoaji.
Wakati mmoja nikiwa safarini huko nyumbani, basi nililopanda lilisimamishwa na askari wa usalama barabarani, na baada ya dakika kadhaa, baadhi ya abiria walisikika wakimhasisha dereva ‘amalizane na trafiki’ (ampe rushwa) ili safari iendelee. Hivi ndivyo rushwa ilivyoota mizizi katika Tanzania yetu.
Kwa upande mwingine, janga la ajali kuonekana kama jambo la kawaida tu ni mwendelezo wa kasumba inayolikwamisha mno taifa letu: kuzowea matatizo. Angalia tatizo la mgao wa umeme lilivyodumu miaka nenda miaka rudi pasipo Watanzania kutumia nguvu ya umma kuilazimisha serikali na Tanesco yake imalize tatizo hilo. Mgao wa umeme umekuwa stahili ya Watanzania, na kikubwa wanachoweza kufanya ni kuitukana Tanesco matusi yasiyoandikika hapa, kana kwamba matusi hayo yatamaliza tatizo hilo la miaka nenda miaka rudi.
Kwenye sekta ya huduma, hali ni hivyohivyo. Ukifuatilia kwenye mitandao ya jamii, idadi ya matusi yanayoelekezwa kwa makampuni ya huduma mbalimbali, kwa mfano makampuni ya simu, ni kubwa na inakua kila siku, lakini ‘mashujaa hao wa matusi’ hawataki kabisa kujifunza kuwa matusi yao hayabadili chochote, na ndio maana kila kukicha inawalazimu waje na matusi mapya kama si kuyarudia yale ya zamani.
Lakini kwa hali ilivyo sasa kuhusu janga la ajali, ‘usugu’ huo wa kuyazowea matatizo inabidi ifikie kikomo. Taifa lolote linalojali mustakabali wake lazima liamke inapofikia hatua ya watu 969 kupoteza maisha kutokana na ajali katika kipindi cha takriban miezi mitatu tu. Naam, tangu mwaka huu uanze, tumepoteza wenzetu takriban 300 kila mwezi kutokana na ajali, kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana wiki iliyopita.
Katika sehemu kubwa ya makala hii nimezungumzia rushwa kama chanzo kikuu cha janga la ajali. Hata hivyo, kwa mtizamo wangu, kingine kinachochangia baadhi ya ajali ni ‘uzembe’ wa wengi wa abiria: kukaa kimya pale madereva wanapohatarisha maisha ya abiria kwa uendeshaji usiozingatia sheria za usalama barabarani. Na pengine cha kukera zaidi ni tabia iliyojengeka miongoni mwa abiria wengi kuwasifia madereva wanaodhani ni kosa la jinai kuendesha motokaa taratibu hata kwenye eneo hatari.
Inasikitisha na kuchukiza kusikia abiria wakimshangilia dereva anayeendesha basi kwa kasi au ku-overtake gari jingine pasi kuona kama kuna gari jingine linakuja kwa mbele au la. Dereva anayeshangiliwa kwa uendeshaji gari wa hatari anajenga imani kwamba huo ndio udereva stahili, vinginevyo abiria wangemkemea.
Ifike mahali Watanzania tuache kukubali kilicho pungufu (not settling for less). Ukinunua tiketi kwa ajili ya safari umenunua pia haki na stahili zako ambazo kamwe hupaswi kumruhusu dereva azichezee. Ni wazi kuwa umoja na mshikamano wa abiria kukemea madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani unaweza kusaidia kupunguza baadhi ya ajali zinazoepukika.
Nimalizie makala hii kwa kutoa salamu zangu za rambirambi kwa ndugu na jamaa wa Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali mfululizo.
Pia ninaomba kufikisha ujumbe huu kwa askari wa usalama barabarani: kila shilingi mnayodai kama rushwa ili kufumbia macho ukiukwaji wa sheria za barabarani inachangia ajali na vifo vya Watanzania wenzetu. Mikono ya kila askari aliyepokea rushwa na kisha gari husika likapata ajali ina damu ya waliokufa katika ajali husika.
Kadhalika, ninatoa wito kwa madereva, hususan wa magari ya abiria, kuthamini uhai wa abiria wao, kwa kuepusha ushindani hatari barabarani, mwendo kasi na kuheshimu sheria za usalama barabarani.
Lakini kubwa zaidi kwa Watanzania wote ni kupambana na kansa hii ya rushwa ambayo sasa inalitafuna taifa kwa kuchangia ajali hizi mfululizo, kama inavyosababisha madhara mengine makubwa katika nyanja mbalimbali za maisha.

ANGALIZO: Makala hii ilichapishwa katika toleo la tarehe 22.04.15 lakini iliwekwa mtandaoni juzi. Samahani kwa kuchelewesha kui-post.


26 Apr 2015

Embedded image permalink
Moja ya taarifa zilizozagaa kwenye vyombo mbalimbali vya habari ni kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi.Lakini shilingi au sarafu nyingine inashukaje thamani yake? Haya ni maswali ambayo ninaamini watu wengi wasio wachumi watakuwa wanajiuliza muda huu.

Nami pia ninajiuliza maswali hayo kama yalivyo kwenye kichwa cha habari.Ninajiuliza kwa sababu mie si mchumi, na jaribio langu pekee la kuingia fani ya uchumi lilikuwa wakati napata elimu ya sekondaria ambapo nilisoma Book Keeping hadi kidato cha nne na Commerce hadi kidato cha pili.

Naujua uchumi 'kijuu-juu' tu, na sana ni katika mahusiano yake na siasa au jamii, lakini kwa vile mie ni dhaifu sana wa hisabati, uchumi unaohusisha tarakimu ni 'no-go area.'

Kwahiyo, samahani msomaji mpendwa kama maswali hayo kwenye kichwa cha habari yalikupa hisia kwamba labda nitayajibu. Hapana. Ni maswali ninayotaka yapatiwe majibu na serikali au/na wataalamu wa masuala ya uchumi.

Kwa sie tunaoishi nje ya Tanzania, dalili kuu ya kushuka kwa thamani ya shilingi yetu ni pale tunapotuma fedha nyumbani kusaidia ndugu na jamaa zetu. Huo ndio muda unatulazimisha kufahamu viwango vya kubadilishia fedha. Kwahiyo kama ninataka kutuma shilingi laki kadhaa za Kitanzania, inanilazimu kufahamu ninatakiwa kutuma paundi za Kiingereza ngapi.Sasa kwa vile zoezi hili la kutuma misaada nyumbani ni la mara kwa mara, inakuwa rahisi kutambua kama 'shilingi ipo imara au imeyumba,' kwa maana kwamba unalinganisha, kwa mfano, "kutuma shilingi laki nne mwezi uliopita ilinigharimu takriban paundi mia na sitini, lakini safari hii imenigharimu paundi laki na arobaini."

Je Mtanzania wa kawaida anafahamu vipi kuhusu kuporomoka kwa thamani ya shilingi wakati hana sarafu ya kigeni ya kufanya mlinganisho? Na sio tu kufahamu kama thamani ya shilingi imepanda au imeshuka, lakini pia anapaswa kujua kama ina athari zozote kwake.

Kidogo ninachoelewa ni kwamba kuporomoka kwa shilingi kunaweza kuwa na 'faida' flani. Wanadai thamani ya sarafu ikishuka, bei ya bidhaa za nchi husika katika masoko ya kimataifa inashuka pia.Kushuka huko kwaweza kuwasukuma wanunuzi katika masoko hayo 'kuchangamkia tenda,' na hiyo inaweza kupelekea nchi kuuza mazao yake kwa wingi, na wakati huohuo hiyo inaweza kuhamasisha wakulima wa mazao au wauza bidhaa za export kuongoze uzalishaji. Sina uhakika sana kuhusu hilo kwa vile kama nilivyotanabaisha hapo juu, mie ni mbumbumbu wa uchumi.Sina A wala B ninalojua katika eneo hili.

Nimalizie makala hii kwa kutoa changamoto kwa serikali sio tu kuwafahamisha wananchi kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi yetu bali pia kueleza sababu za kushuka huko na athari au faida zake kwa Mtanzania. Kadhalika, ninatoa changamoto kwa wataalamu wetu wa uchumi kuisaidia jamii kwa kutupa somo kuhusu suala hili.Na nitumie fursa hii kumkaribisha mtaalam yeyote kunitumia makala kuhusu suala hjilo nami nitaichapisha hapa bloguni au kuituma kwa jarida la RAIA MWEMA ninaloandikia makala kila wiki.

18 Apr 2015

KWA siku kadhaa sasa kumekuwa na mjadala mkali, hususani katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusu sheria mpya ya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni (Cyber Crime Act 2015).


Kabla ya kuuzungumzia mjadala huo, ningependa kumpongeza Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, kwa kufanya tukio la kihistoria la kuuweka hadharani muswada husika katika mtandao wa kijamii wa Twitter ili ujadiliwe.
Ninatambua kuna uwezekano wa baadhi ya watu kudai haistahili pongezi kwa sababu, kwanza hilo ni jukumu la kila mtendaji wa serikali, na pili, kuleta muswada huo siku chache kabla haujawasilishwa kwa hati ya dharura Bungeni kusingewapa wadau nafasi ya kutosha kuujadili.Katika hilo la kwanza, ni muhimu tutambue kuwa Tanzania yetu ya sasa imefikia mahala ambapo kiongozi akitimiza wajibu wake anastahili kupongezwa kwani hata asipotimiza wajibu anaolipwa mshahara kuutekeleza hatoathirika. Ni wazi basi, hata kama January angeamua kutouweka muswada huo hadharani, isingemwathiri lolote.Kuhusu muswada huo kuwasilishwa kwa hati ya dharura, ninaafikiana na wanaolalamikia hatua hiyo kwa sababu licha ya dhamira nzuri na umuhimu wa kuwa na sheria ya kudhibiti uhalifu wa mtandaoni, bado kulikuwa na haja ya wananchi kupewa elimu ya kutosha kuhusu masuala kadhaa, hasa ikizingatiwa kuwa Watanzania wengi bado ni ‘wageni’ katika masuala ya mtandao (wa intaneti.)Na pengine kabla ya kuingia kwa undani katika kuzungumzia mjadala huo na muswada huo ambao ulipitishwa na bunge na hadi wakati ninaandika makala hii ulikuwa ukisubiri kuidhinishwa na Rais Jakaya Kikwete ili uwe sheria kamili, ni muhimu kuweka wazi msimamo wangu kwamba ninaunga mkono muswada na sheria husika.Ninaunga mkono kwa sababu kuu tatu: kitaaluma/kitaalamu, kijamii na binafsi. Kwa upande wa kitaaluma/kitaalamu, huko nyuma niliwahi kufanya kazi katika sekta ya usalama, na kwa muda mrefu nimekuwa nikijihusisha na stadi zinazohusu sekta hiyo.Kwa hiyo, utaalamu na uelewa nilionao, unanisukuma kuunga mkono haja ya, na umuhimu wa kuwa na sheria ya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni.Kwa kifupi tu, pamoja na faida zake nyingi, mtandao unaweza na umeshaweza kutumika vibaya na kusababisha madhara makubwa.Pamoja na kurahisisha mawasiliano na kufanikiwa kuiunganisha dunia na kuwa kama kijiji (ninaandika makala hii nikiwa hapa Uskochi, na nikimaliza na kubonyeza ‘send’ inamfikia mhariri wa gazeti hili muda huohuo, tofauti na njia za zamani ambapo ingelazimu kutuma makala hii kwa barua, na kuchukua siku kadhaa njiani), mtandao umekuwa kichaka cha maovu hasa kutokana na teknolojia husika kuwezesha mawasiliano pasipo watu kukutana ana kwa ana.Kwa mfano, wakati kabla ya ujio wa teknolojia ya mtandao, ilikuwa vigumu kwa ‘mwizi’ kuiba fedha za mwenye akaunti benki bila kufika katika benki husika (au kuziiba wakati mwenye akaunti anaenda kuweka fedha hizo au kuzichukua benki), kwa sasa teknolojia ya mtandao inamwezesha mwizi aliyepo hata mbali na benki au mwenye akaunti kuziiba fedha hizo. Japo pengine hili halijashamiri sana huko nyumbani, ukweli ni kwamba wizi wa aina hiyo umetawala sehemu mbalimbali duniani.Lakini kiusalama, mtandao umetokea kuwa moja ya nyenzo muhimu za magaidi, ambavyo vikundi maarufu vya kigaidi duniani kama Al-Qaeda, ISIS, Boko Haram na Al-Shabaab, vimekuwa vikiutumia vyema mtandao katika harakati zao dhalimu za ugaidi.Katika tukio linaloweza kuonekana la kufikirika tu, magaidi wanaweza kutumia mitandao ya kijamii au hata ‘Whatsapp’ kusambaza ujumbe unaoweza kutishia amani na kusababisha madhara makubwa.Sheria ya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni imekuja wakati mwafaka hasa kwa kuzingatia uwepo wa taarifa zinazoashiria tishio la ugaidi, kufuatilia shambulio la kigaidi lililofanywa hivi karibuni na magaidi wa Al-Shabaab huko Garissa, nchini Kenya na kusababisha vifo takriban 150.Ninathamini sana haki za raia kuwasiliana pasipo hofu ya serikali au taasisi zake za usalama kuyafuatilia mawasiliano yao, lakini pia ninatambua kuwa ili serikali iweze kutekeleza jukumu lake la kulinda usalama wa raia, inalazimika kufahamu mawasiliano yasiyo na nia nzuri kwa taifa letu.Katika zama hizi hatari tunazoishi, ni vigumu mno kupata uwiano stahili kati ya uhuru na sheria kwani wahalifu wanaweza kuutumia uhuru huo kwa dhamira mbaya inayoweza kupelekea raia wasiweza kuutumia uhuru wao vyema.Kijamii, Tanzania yetu imefika mahala pabaya, angalau huko kwenye mitandao ya kijamii. Na kama kuna sehemu inayoweka ushahidi wa wazi kuhusu hicho ninachoongelea, basi ni kwenye mtandao wa kijamii unaohusu picha, Instagram, ambao kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo unavyozidi kuwa uwanja wa matusi na kila lisilopendeza machoni.Kwa upande wa blogu, licha ya kuwa bado tuna blogu nyingi zinazoitumikia jamii ipasavyo, kumeibuka utitiri wa blogu za ngono na matusi huku nyingine zikijipa uhuru wa kuwachafua watu na kuwasababishia madhara makubwa katika maisha yao. Ilikuwa lazima tufike mahala tuseme ‘sasa yatosha.’ Hakuna uhuru usioambatana na kuzingatia wajibu.Mwaka jana, binti mmoja wa Kitanzania alikumbana na madhila ya unyanyasaji mkubwa katika mtandao wa kijamii wa Twitter, na siku chache baadaye alikutwa amekufa. Japo hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kati ya unyanyasaji huo wa mtandaoni na kifo cha binti huyo, yayumkinika kuhisi kuwa matukio hayo mawili yalikuwa na uhusiano japo hata kama ni wa mbali. Na baada ya tukio hilo la kusikitisha, zilisikika kelele mbalimbali za kuitaka serikali ichukue hatua madhubuti kukabiliana na unyanyasaji wa mtandaoni (cyber bullying).Sababu yangu ya tatu ya kuunga mkono sheria hiyo ya kupambana na uhalifu wa mtandaoni ni ya binafsi. Baada ya kifo cha binti huyo, nilisimama kidete na baadhi ya wanaharakati wa haki za jamii kuhamasisha mapambano dhidi ya unyanyasaji wa mtandaoni, kosa ambalo ni sehemu ya uhalifu wa mtandaoni.Katika hali ya kushangaza na kusikitisha, liliibuka kundi lililoanzisha mashambulizi makali dhidi yetu tuliokuwa tukikemea vitendo vya unyanyasaji wa mtandaoni. Binafsi, niliandamwa hadi kiasi cha kuitwa muuaji hadharani, jambo ambalo linaniumiza nafsi hadi muda huu. Nilishindwa kabisa kuelewa kwanini dhamira nzuri ya kukemea maovu igeuke kuwa kosa lililowaudhi watu hao.Naomba ieleweke kuwa sababu hii ya tatu ni ya binafsi na ningesihi isiangaliwe pekee bali pamoja na hizo mbili niliotaja hapo awali, ili isilete hisia kuwa mimi ni mbinafsi ninayeunga mkono sheria hiyo kwa vile ‘itawakomoa’ waliowahi kuninyanyasa mtandaoni huko nyuma.
Wakati jamii inaweza kuuhitaji muda mrefu kujadiliana kuhusu haja ya kuwa na sheria ya kukabiliana na uhalifu mtandaoni, ni muhimu kukumbuka kuwa wahanga wa uhalifu huo hawana muda wa kusubiri. Waingereza wanasema kumcheleweshea mtu haki yake ni sawa na kumnyima haki hiyo (justice delayed is justice denied).Wahanga wa uhalifu wa mtandaoni wanastahili haki sawa kama hao wenye hofu kuwa sheria hiyo inaweza kutumiwa na serikali kukandamiza uhuru wa mawasiliano.Wakati ninatambua mapungufu makubwa ya vyombo vyetu vya dola katika kusimamia na kutoa haki, na hivyo kuelewa vema hofu ya wanaopinga sheria hiyo, ni muhimu pia kutambua kuwa serikali ikiwa na nia ya kuminya haki haihitaji sana kuwa na sheria rasmi.
Tumeshuhudia gazeti la MwanaHalisi likifungiwa kwa kutumia ‘visingizio’ vingine, na wakati huo hatukuwa na sheria ya makosa ya uhalifu wa mtandaoni.Ni kweli kwamba serikali na taasisi zake zinaweza kuitumia vibaya sheria hiyo kuminya uhuru wa mawasiliano, lakini pia ni muhimu tutambue kuwa serikali hiyohiyo ina sheria nyingine kadhaa, na pengine ‘kali’ zaidi ya hiyo ya kuzuwia uhalifu wa mtandaoni, na ikitaka kuzitumia kuminya uhuru, inaweza kufanya hivyo muda wowote.Kuna sheria kama ile ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970 na sheria ya kukabiliana na ugaidi ya mwaka 2002, ambazo zinaipa serikali uwanja mpana tu wa kuzitumia vibaya ikitaka kufanya hivyo.Kimsingi, mjadala unaoendelea kuhusu sheria hiyo unatokana na suala ambalo nimekuwa nikiliongelea mara kadhaa katika makala zangu: upungufu wa imani ya wananchi wengi kwa serikali yetu. Imefika mahala wananchi wengi hawaiamini serikali, na ndio maana baadhi ya wanaopinga sheria hiyo wanadai imeletwa haraka kwa minajili ya kuisaidia CCM katika uchaguzi mkuu ujao.Hofu kuwa sheria hiyo inaweza kutumika vibaya ina mantiki, lakini tatizo sio sheria hiyo ambayo kwa hakika imechelewa sana, bali mfumo wa kifisadi unaoathiri nyanja mbalimbali za maisha ya Mtanzania. Hakuna polisi anayeweza kumkamata mtu kwa vile tu kafanya umbeya kwenye ‘Whatsapp’ yake iwapo mfumo tulionao unazingatia sheria na haki.Kwa bahati mbaya hilo linaweza kutokea kwa sababu baadhi ya polisi wetu wanaofahamika kwa tabia yao ya kupenda rushwa. Je tupuuzie madhila yanayowakumba wahanga wa uhalifu wa mtandaoni hadi tutakapokomesha rushwa kwenye taasisi kama jeshi la polisi au ‘tuue ndege wawili kwa jiwe moja,’ kwa maana ya kuendeleza mapambano dhidi ya mfumo wa kifisadi sambamba na kutumia ipasavyo sheria hiyo mpya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni?Wakati kwa kiasi kikubwa mjadala kuhusu sheria hiyo unafanywa kistaarabu, na tayari kuna petition imewekwa mtandaoni kumsihi Rais Kikwete asiridhie sheria hiyo, kuna kundi dogo la wanufaika wa uhalifu wa mtandaoni linalojaribu kujificha katika hoja kuwa sheria hiyo ni mbaya.Na pengine la kusikitisha zaidi ni kuona dhamira nzuri ya Naibu Waziri January Makamba kuuweka hadharani muswada husika ikichukuliwa na baadhi ya ‘wanyanyasaji wa mtandaoni’ kumshambulia yeye binafsi kana kwamba sheria hiyo ni yake binafsi. Tatizo hapa ni kuweka mkazo kwa mtu badala ya suala husika.Nimalizie makala hii kwa kusisitiza kuwa ninaamini sheria hiyo dhidi ya uhalifu wa mtandaoni ina umuhimu mkubwa kwa usalama wa taifa letu na kwa Watanzania kwa ujumla. Sheria husika haiwalengi raia wema bali wahalifu wa mtandaoni.Badala ya kuwekeza nguvu nyingi kuhofia madhara yake, ni muhimu kama jamii tujiongoze kistaarabu na kukumbushana wajibu wetu kama raia wema. Tusiwe vigeugeu wa kuilaumu serikali kila tunapokutana na picha za ngono au maiti mtandaoni lakini serikali ikisikia kilio chetu kuhusu haja ya kuchukua hatua kali, na hivyo kuja na sheria kama hiyo ya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni, twaishia kuilaumu pia.

10 Apr 2015

Africa is home to some of the richest countries in the world, in part due to its oil-rich soil and human capital. With GDPs going up as high as $594.257 Billion.
According to statistics provided by the International Monetary Fund(IMF), these are currently, according to the figures provided at the time, the Top 10 richest countries in Africa.
1. Nigeria: GDP – $594.257 billion
The most populous country in Africa is a major contender on this list, its manufacturing sector being the third largest in Africa while it contributes a considerable share of the world’s oil. Taking into account this country’s population of 170 million, Nigeria is on track to becoming one of the 20 largest economies in the world by 2020.

2. South Africa: GDP – $341.216 billion
South Africa is popularly known for its mineral resources such as gold and diamond but the Gold Rush ended back in the 19th century. There are more things to look forward to in South Africa besides its jewels. Major cities like Johannesburg and Cape Town offer a unique experiences that can offer scenic routes to mountain ranges by the ocean.

3. Egypt: GDP – $284.860 billion
Egypt has one of the longest histories of any modern country, arising in the tenth millennium BCE as one of the world’s first nation states.

4. Algeria: GDP – $227.802 billion
Oil and gas exports have placed Algeria on this list. Much of its wealth is received from oil deposits deep within the North African soil. Also rich in natural minerals, it is suggested that the ancientRomans collected stones and marbles from quarries in what is now known as Algeria. You can find onyx, red and white marbles, iron, lead, and zinc in large quantities. It’s capital city, Algiers offers rare beauty in the intricate architecture of its most famous buildings.

5. Morocco: GDP – $112.552 billion
Morocco was named the first most competitive economy in North Africa. Tourism, telecoms, textiles and agriculture are Morocco’s biggest biggest money pullers.

6. Sudan: GDP – $112.552 billion
More than once, we have mentioned oil and gas as the main source of income for countries on this list. Sudan also falls into that category but in a more diverse way. It depends on oil but with a third of its GDP contributed by agriculture. Cotton and peanuts constitute its major agricultural exports. You may not notice a “Made in Sudan” tag on the shirt you buy in Khartoum but cotton from Sudan has fueled the textile industry in many parts of the world.

7. Kenya: GDP – $53.40 billion
The capital, Nairobi, is a regional commercial hub. The economy of Kenya is the largest by GDP in Southeast and Central Africa. Agriculture is a major employer; the country traditionally exports tea and coffee and has more recently begun to export fresh flowers to Europe. The service industry is also a major economic driver. Kenya is a member of the East African Community. Compared to other African countries, Kenya enjoys relatively high political and social stability.

8. Angola: GDP – $49.857 billion
Angola has a large deposit of oil and gas resources, diamonds, and bountiful agricultural land. Still recovering from the 27-year civil war that lasted from 1975-2002, Angola has made efforts to revive its economy with heavy oil and agricultural exports. Cities like Luanda are undergoing major reconstruction to make Angola a top African destination.

9. Libya: GDP – $49.341 billion
The Libyan economy depends primarily upon revenues from the oil sector, which accounts for 80% of GDP and 97% of exports. Libya holds the largest proven oil reserves in Africa and is an important contributor to the global supply of light, sweet crude.Apart from petroleum, the other natural resources are natural gas and gypsum.The International Monetary Fund estimated Libya’s real GDP growth at 122% in 2012 and 16.7% in 2013, after a 60% plunge in 2011.

10. Tunisia: GDP – $49.122 billion
Oil, tourism and car manufacturing parts are the name of the game in Tunisia. It is one of the wealthiest countries in Africa so you won’t wander too far into its cities like Tunis before finding a pleasant spot to relax. The city is covered with bits of opulence from as far back as the 12th century. Year-round sunshine and the affordable Tunisian lifestyle have drawn tourists here who now call this place home.


SOURCE: IT NEWS AFRICA

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.