1 Aug 2010

Baada ya kusubiriwa kwa muda mrefu,hatimaye kampuni ya HTC imetangaza rasmi kwamba watumiaji wa simu aina ya HTC DESIRE watapatiwa toleo jipya (version 2.2) la mfumo wa kuendesha simu (operating system -OS- ya Android linalofahamika kama Frozen Yorghut (Mtindi wa Mgando) kwa kifupi Froyo.Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali,Froyo itaanza kusambazwa hewani (OTA-over the air) wiki hii kwa wenye HTC Desire ambazo "hazijafungwa" (unlocked) na baadaye kwa "zilizofungwa" (locked) kabla ya kusambazwa kwa simu nyingine zinazotumia OS hiyo ya Android.

Inatarajiwa kuwa Froyo itaziboresha zaidi simu za Android,kwa mfano HTC Desire,ambayo inalinganishwa kwa karibu na "mama wa simu zote",Apple iPhone.Binafsi,nimekuwa nikitumia HTC Desire kwa takriban miezi mitano hivi na kwa hakika ni simu iliyojitosheleza kwa takriban kila kitu.Tatizo pekee hadi sasa,na ambalo limepatiwa ufumbuzi kwenye toleo la Froyo,ni kutoweza kuhifadhi Apps (applications) kwenye memory card hivyo kupelekea simu kuwa na Apps za muhimu tu ilhali kuna maelfu kwa maelfu ya Apps kwenye "soko" la vidude hivyo (Market).

29 Jul 2010

TANZANIA imetajwa katika ripoti ya Kipimo cha Hali ya Rushwa Afrika Mashariki (EABI), kuwa na taasisi zinazoongoza kwa rushwa kwa nchi za Afrika Mashariki.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mratibu wa sekretarieti ya Jukwaa la Wazi (TRAFO), Kaiza Buberwa, alisema kuwa utafiti huo ulifanywa kwa kushirikisha sampuli 10,469 na watu 3,231 walihojiwa kwa Tanzania.

Alisema kuwa katika utafiti huo uliofanyika chini ya wataalamu wa nchi husika, ulifanyika Febrauari na Machi ambapo nchi za Kenya, Burundi, Tanzania, Rwanda na Uganda zilihusishwa.


. Buberwa alisema taasisi zinazoongoza kwa rushwa katika Afrika Mashariki ni Jeshi la Polisi, Mahakama, Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa, Wakala ya Usajili wa Vifo na Vizazi (RITA), Magereza, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi katika kutoa huduma kwa wananchi, sambamba na ajira.


Alisema kuongoza kwa taasisi hizo ni kutokana na sampuli hiyo ya watu hao, ambao walizitaja taasisi zilizokithiri kwa rushwa wakati wa kupata huduma za kijamii.

Buberwa alisema kwa kuongoza kwa rushwa katika idara nyeti za serikali kwa Afrika Mashariki, Jeshi la Polisi limechukua nafasi ya tano kwa asilimia 65.1 na Mahakama kuwa nafasi ya 10 kwa asilimia 56.4 katika utoaji wa huduma katika misingi ya rushwa.

Aidha, alisema kuwa katika ripoti hiyo haisemi Tanzania hakuna rushwa wala rushwa kidogo, ripoti inasema kwamba ni kwa kuzingatia idadi ya matukio ya vitendo vya rushwa katika idara kadhaa za umma wakati wa kutoa huduma kwa wananchi ikilinganishwa na nchi za Burundi, Kenya, Uganda na Rwanda.

Buberwa alisema kuwa baadhi ya Watanzania asilimia 85.8 wanaamini kuwa hali ya rushwa Tanzania ni mbaya, wakati asilimia 40.6 wanaamini serikali hatimizi wajibu wake katika kuondoa rushwa na kuimarisha utawala bora.

Alisema taasisi nyingine zinazofuata katika rushwa kwa utoaji wa huduma kwa jamii ni Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa (JKT) asilimia 74.2, Wakala ya Usajili wa Vifo na Vizazi (RITA), asilimia 66.2, Magereza asilimia 61.9, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) asilimia 46.8, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi asilimia 47.9.

CHANZO: Tanzania Daima

.

Ni dhahiri kwamba kila Mtanzania mzalendo na mwenye uchungu na nchi yetu anatamani kuona mambo yakibadilika huko nyumbani.Nchi yetu ina takriban miaka 50 tangu ipate uhuru mwaka 1961.Ukiondoa uvamizi wa nduli Idi Amin mwaka 1978-79,nchi yetu imeendelea kuwa na sifa ya kipekee ya amani na utulivu huku tukishuhudia "nyumba za majirani zetu zikiteketea".Chama tawala CCM kimekuwa kikijigamba kuwa amani na utulivu huo ni matokeo ya sera zake nzuri na uongozi uliotukuka.Haihitaji kuwa mwanafunzi wa siasa kama mie kufahamu kuwa amani na utulivu tulionao unasababishwa na uvumilivu wa Watanzania.Na ni uvumilivu huo huo unaowafanya CCM watuone wajinga,watupelekeshe watakavyo na waifilisi nchi yetu huku tukifahamu fika namna ya kuwadhibiti.Imetosha.Uvumilivu una mwisho,na mwisho huo ni sasa.

Na hata hilo suala la amani na utulivu lina utata kinamna flani.Wachambuzi wa siasa wanabainisha kuwa kutokuwa na machafuko au vita si viashiria kamili vya amani na utulivu.Hebu jiulize msomaji mpendwa,wazee wetu wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wana amani gani wakati fedha zao ziliibiwa na wajanja (mafisadi)  katika serikali ya CCM?Je wakulima wanaokopwa na vyama vya ushirika kila unapojiri msimu wa mavuno wana amani gani wakati wanashuhudia namna mavuno yao yanavyorutubisha vitambi vya mafisadi wa vyama vya ushirika?Mabaamedi wana amani gani katika mishahara ya kijungujiko wanayopewa (na inayokatwa kila siku kila glasi au chupa inapovunjika)?Watoto zetu au wadogo zetu wana amani gani wanaposoma kwenye shule zisizo na madawati huku walimu wao wakinyong'onyea kutokana na mazingira duni ya kazi?Na je watumishi wa umma wana amani gani ilhali wanapodai haki zao wanaishia kudharauliwa kuwa kura zao hazihitajiki (as if mishahara yao ni fadhila kwa kumchagua kiongozi)?

Na madereva wa daladala na mabasi ya mikoani wana amani gani ilhali askari wa usalama barabarani wanawakamua kila siku kana kwamba rushwa ni sehemu ya sheria za usalama barabarani?Na huko magerezani kuna Watanzania wangapi wasio na amani kwa vifungo vya kubambikizwa kesi,kushindwa kutoa rushwa kwa polisi au hakimu au uonevu pasipo sababu?Na dada na mabinti zetu wenye sifa stahili za kupata ajira wana amani gani ilhali kila wanapofanya maombi ya kazi wanakumbana na masharti ya "ngono kwanza,kisha ajira"?Na wagonjwa wetu wana amani gani wanapolazwa sakafuni katika wodi za hospitali mbalimbali (na hii ilimtoa machozi Supamodo Naomi Campbell)?

Mtanzania ana amani gani wakati kila siku anashuhudia namna nchi yake inavyozidi kuhujumiwa na mafisadi?Wanaoamini katika utawala wa sheria wana amani gani wanaposhuhudia mtu kama Lowassa anapewa air time kwenye televisheni ya taifa inayoendeshwa kwa fedha za walipa kodi (na mahijiano hayo hayafanyikii gerezani)?Yani fedha za walipa kodi zinatumika kusafisha watuhumiwa wa ufisadi!

Na walalahoi wana amani gani wanaposhuhudia serikali waliyoiweka madarakani,na iliyoahidi maisha bora kwa kila Mtanzania,ikielekeza nguvu kubwa katika kukumbatia mafisadi huku viongozi wa serikali hiyo wakiishi maisha ya kifahari kana kwamba Tanzania ni nchi ya "dunia ya kwanza"?Na wasafiri wanaotegemea huduma za Reli ya Kati au Tazara wana amani gani wakati usafiri wao unategemea kudra za Mwenyezi Mungu ?

Yapo mengi ya kueleza kuhusu namna CCM inavyofanya kila jitihada ya kubomoa hata kile kidogo kilichobaki kwenye "amani na utulivu".Ni dhahiri kuwa chama hiki kimevimbiwa madarakana na hakijali kuona Tanzania ikielekea kwenye korongo lenye kina kirefu.CCM inaweza kufanya kila hila ili ibaki madarakani kama ilivyowazuga Waislamu mwaka 2005 kuwa ingewapatia Mahakama ya Kadhi,lakini baada ya ushindi wa "kishindo" kwenye uchaguzi mkuu uliopita suala hilo limeendelea kuwa ngonjera tu huku akina Msekwa wakisema hili,Pinda akisema lile na Chikawe akiongea vile.Huku ni kuchochea vurugu.

Tanzania haiwezi kupiga hatua katika mfumo wa sasa wa kifisadi ambapo madaraka yanatolewa kwa minajili ya ushkaji huku watawala wakijiona miungu watu wenye uwezo wa kufanya watakayo hata kama yanapelekea kuhatarisha "amani na utulivu" wetu.

It's high time to say enough is enough.Na namna pekee ya kuwaadhibu CCM ni kuwanyima kura katika uchaguzi mkuu ujao.Binafsi,nina imani kubwa na Dokta Wilbroad Slaa,mgombea urais kwa tiketi ya Chadema.Ameonyesha ukomavu wa hali ya juu katika kutetea hali zetu na kupambana kwa dhati dhidi ya ufisadi.Nafasi adimu kama hizi huwa hazijirudii.Tukifanya kosa la kuiacha CCM madarakani hapo Oktoba tutaishia kujilaumu.Nia tunayo,sababu tunazo (tena elfu kidogo) na uwezo tunao (siku ya kupiga kura).Mnaopewa rushwa ili muichague CCM pokeeni kwa vile rushwa hiyo ni fedha mlizoibiwa.Wato rushwa hao hawana uwezo wa kushinikiza muwapigie kura hasa ikizingatiwa kuwa hamkuwaomba wawahonge na wanachowanhonga is in fact fedha zenu wanazowaibia kwa ufisadi.

Inawezekana ukitimiza wajibu wako

27 Jul 2010


Mtunzi wa kitabu hiki maridhawa si mwingine bali ni mchambuzi na mwandishi mahiri wa makala,Mwalimu Nkwazi Nkuzi Mhango,Mtanzania mwenye makazi yake nchini Kanada.Licha ya ualimu na uandishi wa habari,Mhango pia ni mwanaharakati wa haki za binadamu.Miongoni mwa safu maarufu za Mwalimu Nkwazi (pichani chini) ni zile zinazopatikana katika gazeti la Tanzania Daima,ambapo hutumia jina la MPAYUKAJI MSEMAOVYO.Kadhalika,mwandishi huyu ni hodari katika fani ya kublogu,na "uwanja wake" unafahamika kama Free Thinking Unabii .Vilevile,unaweza kusoma makala za Mwalimu Nkwazi katika jarida la The African Executive
Usikose nakala ya kitabu hiki ambacho kinakuja wakati mwafaka kabisa kwa Watanzania waliochoshwa kuona nchi yao ikigeuzwa "shamba la bibi" na mafisadi wanaopita huku na huko "kuomba ridhaa yetu" warejee madarakani kutufisadi zaidi.

26 Jul 2010

Pichani juu  kitabu cha cha sanaa cha comic kinachoitwa TOM & JENNY IN TANZANIA  ambacho kilikuwa kinasubiriwa kwa muda mrefu, na sasa kitabu kimetoka.Unaweza kukipata jijini Dar es salaam na vilevile wachapishaji wanaweza kuwatumia wasomaji walio nje ya Dar es salaam na Tanzania kwa ujumla.
----------------------------------------------------------------------
Joe
Baseline Africa

Alma
Alma akiwa na playwriter Greg Freeman
Alma na cast nzima ya BEAK STREET
Alma Eno, Natasha Whites na Alice Transfield
Msanii wa maigizo na filamu mwenye asili ya kitanzania Alma Eno, ameng'ara na kutikisa ulimwengu wa Theatre mjini London kwenye onyesho la mchezo uitwao BEAK STREET ulioandikwa na mwandishi maarufu Greg Freeman, na kuongozwa na Ken McClymont.

BEAK STREET ni mchezo wa kijangili ulio kwenye ulimwengu wa Mapaka. Mchezo huo umekuwa ukionyeshwa kwenye kitongoji cha West End mjini London, ambacho ni maarufu kwa majumba ya maigizo,sinema na starehe. Beak Street imeonyeshwa kwa wiki 24 sasa katika majumba ya Tabard Theatre na Theatre Delicatessen (Sekunde 30 kutoka Selfridges)

Alma Eno anacheza silka mbili kwenye igizo hili; kwanza anacheza paka teja ambaye anaweza kuuza mtu yeyote kwa maziwa ya unga.

Vilevile anacheza silka ya Chorus ambayo anakuwa nafsi ya jangili Beak. Onyesho lake limesifiwa sana na wahakiki na sasa amefanikiwa

kuingia mkataba wa kuigiza kwenye mchezo mpya wa Zip Postcode Wars ambao unaendeshwa na gwiji Ray Shell.

Alma ambaye ni mwigizaji wa kulipwa, alipata shahada yake ya sanaa na maigizo kutoka chuo maarufu cha Mountview Academy of Theatre and Art. Chuo hiki kina sifkia kwa kutoa waigizaji maarufu wa kimataifa kama Amanda Holden,Nick Moran, Ayub Khan Din mwandishi wa mchezo na sinema ya East is East and director Edward Hall. Da Eno pia ameshawahi kucheza kwenye kipindi cha televisheni ITV hapa Uingereza kiitwacho Collision. Vilevile yuko kwenye filamu ya British Art iitwayo Boggie Woogie.

Maneno ya Critics chini

Freeman and Ken have once again dipped into the absurd with their new production Beak Street - a dark comedy of noir shadows, mean streets and gangster cats, where only one thing is really certain:cats , they aint known for their loyalty

"A testament to freeman's faith in his imagination and ours"-Time Out Critics' Choice ****

"This is a fine and powerful play that pulls no punches"-Chiswick Times

"Iron-rod narrative and polished script.. imaginative staging.. all makes Beak Street excellent value for money"-Extraextra.com
------------------------------------------------------------------------
Baraka

URBAN PULSE

21 Jul 2010

Kuna habari kuwa huenda Katibu Mkuu wa Chadema,Dkt Wilbrod Slaa,atakuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.Kwa mujibu wa gazeti la Daily News,Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana jana jijini Dar imemuomba Dkt Slaa kugombea nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa habari hizo,Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,Zitto Kabwe,alinukuliwa akisema "Kamati Kuu (ya Chadema) imemuomba Dkt Slaa kuwa mgombea wa chama (katika nafasi ya urais)".Hata hivyo,Zitto alieleza kuwa uamuzi wa Kamati hiyo Kuu sio wa mwisho kwani itabidi mgombea urais wa chama hicho athibitishwe na Mkutano Mkuu wa chama hicho ambao umepangwa kufanyika Agosti 10.Kadhalika,Zitto hakuweza kueleza kama Dkt Slaa,ambaye gazeti hilo halikufanikiwa kumpata kuthibitisha habari hizo, amekubali ombi hilo au la.

Hata hivyo,vyanzo vya gazeti hilo katika kikao hicho (kilichokuwa kinaendelea wakati gazeti hilo linaenda mtamboni) vinaeleza kuwa Dkt Slaa,ambaye licha ya Ukatibu Mkuu wa Chadema ni Mbunge wa Karatu kwa tiketi ya chama hicho, amekubali ombi hilo.Habari hiyo ya Dkt Slaa kukubali ombi la kugombea urais kwa tiketi ya Chadema imeandikwa pia kwenye mtandao maarufu kwa habari na mijadala makini,Jamii Forums.

Dokta Slaa amejikusanyia umaarufu mkubwa miongoni mwa Watanzania kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi.Japo ni mapema kubashiri nafasi yake katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu,ni dhahiri kuwa iwapo atasimama kama mgombea wa Chadema anaweza kutoa upinzani mkubwa kwa mgombea wa CCM,Rais (wa sasa) Jakaya Kikwete hususan katika namna chama hicho tawala kilinavyoonekana kama kichaka na hifadhi ya ufisadi na mafisadi.


20 Jul 2010

SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete kueleza umma wa Watanzania kwamba ongezeko la magari na kero ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam ni dalili ya maisha bora, wanazuoni na wanasiasa nchini wameikosoa kauli hiyo na kuilaani vikali.

Wamesema kauli hiyo ni dalili tosha kwamba CCM imekosa mwelekeo halisi ya maendeleo ya nchi hivyo haistahili kuendelea kutawala kwa kuwa haina dira ya kubali maisha ya Watanzania.

Mhadhiri katika kitivo cha Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bw. Bashiru Ally aliliambia Majira kuwa ni aibu kwa kauli hiyo kutolewa na kiongozi wa nchi aliyebeba dhamana ya taifa zima.

Alisema ongezeko la fedha, majumba ya kifahari kwa watu wachache na foleni za magari jijini Dar es Salaam hakuwezi kuchukuliwa kama kipimo cha maisha bora kwa kuwa hivyo si vigezo vinavyopaswa kutumiwa kupima kiwango cha maendeleo katika nchi yoyote duniani.

Alisema maisha bora na maendeleo yoyote katika nchi yanapaswa kupimwa kwa kuzingatia ongezeko la watu, upatikanaji wa ardhi, siasa safi na uongozi bora mambo ambayo bado ni ya taabu na yanayozua migogoro mikubwa nchini.

"Kauli hii inanikumbusha kauli ya hayati Korimba (Horance), kuwa CCM haina dira wala mwelekeo, huwezi kupima maisha bora ya mwananchi wa Masasi au Kagera kwa kuangalia foleni za magari Dar es Salaam, laiti kama Mwalimu (Nyerere) na Sokoine (Moringe) wangekwepo leo kauli hii ingewapandisha presha," alisema Bw. Bashiru.

Alisema ni vema Rais Kikwete akaangalia uwiano wa ngezeko la foleni hizo na uboreshaji wa miundombinu hususan barabara, shule na mfumko wa bei za bidhaa na thamani ya fedha ambavyo vimekuwa vikiporomoka kwa kasi katika kipindi cha uongozi wake.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw. Freeman Mbowe, alisema kauli hiyo inaonesha jinsi serikali ya CCM isivyokuwa na jambo la kujivunia kwa wananchi katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita.

Alisema kimsingi msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam inasababishwa na ukosefu wa miundombinu ambayo chimbuko lake ni uongozi mbovu ulioko madarakani.

Alisema kinachotokea Dar es Salaam si kuboreka kwa maisha ya wananchi bali ni ongezeko la tabaka kati ya walionacho na wasio nacho hasa masikini walioko vijijini hali ambayo inasababisha ongezeko la watu mijini wasiokuwa na ajira wala mahali pa kulala.

"Foleni za magari Dar es Salaam si dalili ya maisha bora, na kama ukifanya utafiti utagundua kuwa foleni kubwa ni katika baadhi ya barabara zinazoelekea kwa matajiri wachache ambao baba, mama na watoto kila mmoja ana gari lake, sasa maendeleo ya watu wachache huwezi kuyatumia kupima kiwango cha maisha ya Watanzania wengine," alisema Bw. Mbowe.

Naye Mhadhiri Mwandamizi katika Kitivo cha uchumi na Biashara Chuo Kikuu cha Dar Salaam, Profesa Humphrey Moshi, alisema si sahihi kwa rais wa nchi kupima maisha ya Watanzania wachache wengi kwa kutumia mfano wa watu wachache wenye uwezo wa magari.

Alisema licha ya ukweli kuwa ongezeko la idadi ya watu wanaomiliki magari linaweza kutumika kuonesha ongezeko la kipato kwa wananchi lakini haikuwa sahihi kwa kiongozi wa nchi kupima maisha ya Watanzania kwa kuangalia wenye uwezo wachache walioko Dar es Salaam.

Alisema Dar es Salaam ni mji wa kibiashara wenye viwanda, mashirika na taasisi karibuni zote za serikali ambazo katika shughuli za kawaida zinahitaji usafiri wa magari, hivyo kuna uwezekano kuwa foleni kubwa husababishwa na magari ya taasisi, hizo lakini si mabadiliko ya maisha ya Watanzania.

"Magari mengi si ya watu binafsi, idara nyingi za serikali ziko hapa, kuanzia ikulu, bunge, wizara zote, taasisi binafsi, mashirika ya dini, viwanda na wafanyabiashara mbalimbali ambao ndio wamiliki wa magari, sio wananchi wa kawaida, sasa huwezi kusema kuwepo kwa foleni za magari ya idara hizi ni maisha bora kwa wananchi," alisema Prof. Humpherey.

Alisema maendeleo yanapimwa kwa kuangalia maisha ya jumla si ya mwananchi mmoja mmoja, ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezo wa kuzalisha mali wa wananchi, thamani ya fedha, kiwango cha elimu na uimara wa sekta za viwanda na kilimo, na si kuangalia msongamano wa magari yaliyokosa barabara za kupita.

Akihutubia wana CCM na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam katika mkutano wa kuwatambulisha wagombea urais, mgombea mwenza na Rais wa Tanzania Visiwani katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Rais Kikwete alisema ongezeko kubwa la magari na kusababisha msongamano wa magari ni mijawapo ya dalili za maisha bora.

CHANZO: Majira

19 Jul 2010

Foleni za magari ni maisha bora-JK
Monday, 19 July 2010 05:33
*Asema watakakamatwa kwa rushwa CCM haitawatetea

Na Peter Mwenda

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Kikwete ametamba kuwa chama hicho kwa miaka mitano iliyopita kimeinua maisha ya Watanzania akitoa mfano wa Jiji la Dar es Salaam kuwa foleni za magari zinatokana na wananchi kuwa na maisha bora.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na CCM Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kumpongeza Rais Kikwete kuchaguliwa kuwa mgombea pekee wa urais kwa asilimia 99.16, Dkt. Ali Mohammed Shein kuchaguliwa kuwa mgombea wa Urais Zanzibar na Dkt. Mohamed Gharib Bilal kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais.

"Hapa Dar es Salaam taabu ya msongamano wa magari inaonesha hali ya maisha ni bora, sasa tunahangaika jinsi ya kuondoa msongamano, kuanzia mwakani tutaanza kujenga barabara za juu," alisema Rais Kikwete.

CHANZO: Majira

Hivi kumbe maendeleo yanapimwa kwa msongamano na foleni za magari!Vipi kama foleni hizo ni matokeo ya mindombinu isiyoendana na mahitaji?Vipi kama wingi wa magari hayo ni matokeo ya ufisadi-aidha ya wizi na ubadhirifu wa mali ya umma na ukiukwaji wa taratibu mbalimbali eg ukwepaji kodi stahili bandarini na TRA?

Na je,foleni hizo za magari zinaendana vipi na idadi ya Watanzania wanaumudu mlo wao kila siku?Je wingi wa magari unaendana na idadi ya wamiliki wa magari?Nauliza hivyo kwa sababu wengi tunafahamu kuwa wakati kuna wachache wenye msururuwa magari na majumba ya kifahari kuna wengine wengi tu ambao hata fedha ya kununulia baiskeli hawana,achilia mbali uhakika wa nauli ya daladala.

Na je inawezekana Rais hajafahamishwa na wasaidizi wake kuhusu ongezeko la 'TZ ELEVEN' i.e. watembea kwa miguu ambao hawafanyi hivyo kama sehemu ya mazoezi ya viungo mbali ukosefu wa nauli?Au hawajamwambia kuhusu idadi ya 'mikweche' ambayo licha ya kusababisha foleni inachangia uwezekano wa ajali?Na inawezekana pia wasaidizi wake hawajamfahamisha kuwa mingi ya 'mikweche' hiyo iko barabarani baada ya wamiliki kutoa 'kitu kidogo' kwa askari wa usalama barabarani?

KAMWE MAJIBU RAHISI KWENYE MASWALI MAGUMU HAYAWEZI KULETA UFUMBUZI WA MATATIZO YETU!SINTOSHANGAA TUKISKIA HATA KUONGEZEKA KWA WENYE VITAMBI (INCLUDING WALE WENYE VITAMBI VYA KWASHAKOO) NAKO NI DALILI YA MAISHA BORA!

18 Jul 2010

Jumatatu iliyopita,gazeti la Mwananchi lilikuwa na habari yenye kichwa 'DAWA YA UKIMWI YAGUNDULIWA'.Siku mbili baadaye,gazeti hilohilo lilikuwa na habari yenye kichwa 'MWAKYUSA: TUMSHUKURU MUNGU KWA DAWA YA UKIMWI'.Binafsi,niliposoma habari ya kwanza nilipatwa na mshangao kuwa inakuwaje habari nzito kama hiyo isipate uzito mkubwa kwenye vyombo vya habari vya kimataifa.Kama kawaida yangu,unapojitokeza utata kuhusu habari,nika-google 'HIV cure'.Tofauti na ilivyoripotiwa na gazeti hilo la Mwananchi,matokeo ya search yangu hayakukuwa na jibu la uhakika.

Nilishtushwa zaidi na kauli ya Waziri wa Afya,profesa wa utabibu,Davidi Mwakyusa,alivyoingia kwenye mkumbo wa 'kushangilia kupatikana kwa dawa ya ukimwi' pasipo kufanya utafiti wa kutosha.Na mahala rahisi pa kufanya utafiti wa aina hiyo ni mtandaoni.

Na pengine katika hali inayoweza kutafsiriwa kama 'kumpa darasa Profesa Mwakyusa',msomi mwezie Profesa Fred Mhalu wa Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Muhimbili,ametoa tahadhari kuhusu habari hiyo ya ugunduzi wa dawa ya ukimwi.Msomi huyo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Microbiology na Immunology,na ambaye amekuwa akijihusisha na tafiti kuhusu ugonjwa huo,amebainisha kuwa kilichogundulika ni protein antibody tu,na inabidi kusubiri mpaka chanjo itakayoweza "kutekenya" (stimulate) antibody hiyo itapopatikana,na kwa sasa haiwezekani kusema hatua hiyo itachukua muda gani.

Profesa Mhalu ametahadharisha pia kuwa huko nyuma kulishawahi kuwa na ripoti kama hizo lakini hazijaweza kuzaa matokeo yanayotarajiwa.Hata hivyo,alisema kuwa hatua iliyofikiwa ni ya kutia matumaini kwenye mwelekeo wa kupata tiba kamili japokuwa hawezi kutamka kwa hakika kuwa ufumbuzi wa tatizo hilo umeshapatikana.

Awali,Profesa Mwakyusa alinukuliwa akisema "Kama ni kweli dawa hiyo imepatikana, ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kuwa Ukimwi ni ugonjwa ambao umeiathiri sana dunia."Ama kwa hakika usingetarajia kauli ya 'kimtaani' (layman's language) kutoka kwa mtu mbaye licha ya kuwa Waziri mwenye dhamana katika suala la Afya lakini pia ni msomi katika fani ya utabibu.Japo ni vizuri kumshukuru Mungu kwa taarifa za kutia matumaini kama hiyo,lakini watu wenye dhamana na hususan wasomi kwenye taaluma ya utabibu wanatarajiwa kutoa kauli zinazoelemea zaidi kwenye facts badala ya hisia za binafsi.Pengine kabla ya kutoa kauli hiyo iliyoongeza uzito katika habari husika,Waziri Mwakyusa angeweza kufanya 'quick search' kwenye simu (kama sio kompyuta) yake na kupata facts sahihi kisha kuwaeleza Watanzania ukweli kuhusu habari hiyo.

Kwa mujibu wa kiongozi wa utafiti uliopelekea habari hiyo,Dakta Garry Nabel wa Taasisi ya Taifa ya Allergy na Magonjwa ya Kuambukiza ya Marekani,protini zilizogunduliwa,yaani antibodies hizo,zinatumiwa na mfumo wa kinga ya mwili kutambua na kushambilia vimelea vya maradhi kama bakteria na virusi."Nina kuhusu chanjo ya ukimwi kwa sasa kuliko ilivyokuwa miaka 10 iliyopita",alisema mtafiti huyo katika kauli iliyopelekea msisimko wa aina yake sehemu mbalimbali duniani.

Virusi vya ukimwi hushambulia mfumo wa mwili kujikinga na maradhi na hivyo kumwacha mwathirika katika hatari ya maambukizi na maradhi.Tangu virusi hivyo vigunduliwe takriban miaka 30 iliyopita,wanasayansi wamekuwa wakihangaika pasipo mafanikio kupata tiba na kinga ili kudhibiti ukimwi.Inakadiriwa kuwa kufikia mwaka juzi kulikuwa na watu milioni 33 walioambukizwa virusi hivyo hatari.

Wakati dunia kwa ujumla ingetamani tiba ya ugonjwa huo hatari ipatikane hata leo,ni muhimu kwa wenye dhamana ya kuuhabarisha umma kuwa makini wanapotoa taarifa za kitaalamu zinazohitaji ufafanuzi makini ili kuepuka kutoa matumaini yasiyoendana na ukweli.Kwa kifupi,hadi sasa hakuna dawa ya ukimwi.Kilichogundulika ni hizo antobodies,na bado kuna hatua mbalimbali za kitabibu na kitaratibu kabla haijathibitishwa rasmi kuwa tiba au dawa ya ugonjwa huo imepatikana.

Lengo la makala hii sio kuvunja matumaini ya walioanza kuamini kuwa 'dawa ya ukimwi imepatikana' bali ni kutoa ufafanuzi ambao naamini utawasaidia walioathirika kuzingatia ushauri wa kitaalam na kwa sote kwa ujumla kujichunga kwa kuepukana na ngono zembe.

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.