24 Aug 2010

Tangu tukio la mashambulizi ya kigaidi ya September 11 mwaka 2001,Marekani inaelekea kupata sababu nyingine ya kuhalalisha ubabe wake.Miongoni mwa wahanga wakubwa wa aftermath ya mashambulizi hayo ni Waislamu,ndani na nje ya nchi hiyo.

Hivi karibuni kumejitokeza mzozo kuhusu ujenzi wa kituo cha utamaduni cha Kiislamu karibu na eneo yalipokuwa majengo maarufu ya Twin Towers ambayo yalishambuliwa na magaidi kwa kubamizwa na ndege.Licha ya ukweli kuwa miongoni mwa waliofariki au kujeruhiwa ni Waislam,kwa Wamarekani wengi mashambulizi hayo yalikuwa kama tangazo la vita vipya kati yao na Waislam na Uislam.


Urais wa Barack Obama,ambaye mmoja wa wazazi wake alikuwa Muislam,ni kama umeongeza mafuta kwenye moto wa chuki dhidi ya Waislam.Katika kutambua uhuru na haki ya kila Mmarekani,Rais Obama aliweka msimamo wake hadharani kuwa anaunga mkono ujenzi wa kituo hicho cha kidini,kauli iliyopelekea upinzani mkubwa dhidi yake huku wengine wakimnyooeshea kidole kudai naye ni Muislam,kana kwamba kuwa muumini wa dini hiyo ni dhambi. 

Japo taifa hilo kubwa na lenye nguvu za kutosha limeendelea kudumisha misingi ya imani ya kidini (hususan Ukristo) matendo ya Wamarekani walio wengi hayana tofauti na waumini wa shetani.Sote tunatambua kuwa dini mbalimbali zinahamasisha amani,upendo na kusamehe waliotukosea.Sasa,hata kama Wamarekani wanaamini kuwa waliofanya mashambulizi hayo walitenda hivyo kutokana na imani yao ya Uislamu haimaanishi kuwa kila muumini wa dini hiyo aendelee kunyanyaswa kwa makosa ya wengine.Kimsingi,wengi wa magaidi wana asili au dini flani lakini hatuendelei kuwanyanyasa watu wengine ambao hawakushiriki katika vitendo vya ugaidi lakini wana asili au dini moja na magaidi husika.Wanaofanya mashambulizi ya kigaidi huko Ireland ya Kaskazini ni Wakatoliki na Waanglikana,lakini hatuhitimishi kuwa kila Mkatoliki au Muanglikana na gaidi.

Hata Marekani kama nchi imeshafanya unyama mkubwa sehemu mbalimbali duniani hususan katika zama za Vita Baridi kati yake na Urusi.Nani asiyejua mchango wa Wamarekani katika kifo cha Patrice Lumumba,au sapoti yao kwa Savimbi?Na nani asiyefahamu namna Wamarekani Weupe walivyojenga taifa hilo kwa biashara ya kinyama ya utumwa dhidi ya watu Weusi?Lakini hatumhukumu kila Mmarekani kuwa ni gaidi au mtwana mwenye kumiliki watumwa.

Yanayotokea sasa dhidi ya Waislamu ni mwendelezo tu wa hisia za ubaguzi zilivyoshamiri miongoni mwa Wamarekani walio wengi.Hadi leo,miaka kadhaa baada ya kuharamisha ubaguzi wa rangi,Wamarekani wasio Weupe wameendelea kubaguliwa kwa namna moja au nyingine.Again,urais wa Mmarekani Mweusi Obama umewasha upya moto wa ubaguzi wa rangi.

Japo siungi mkono ugaidi,ni dhahiri kuwa siasa za kinafiki za nchi hiyo zimechangia sana kuzalisha magaidi.Osama bin Laden,kiongozi wa mshambulizi ya September 11ni zao la mafunzo na ufadhili wa Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA).Yayumkinika kuhitimisha kuwa tatizo la baadhi ya sera za mambo ya nje za Marekani ni ufupi wa upeo (short-sightedness).Katika zama za Vita Baridi,nchi hiyo iliona kuwa ni jambo mwafaka kufadhili mujahidina waliokuwa wanapambana na Urusi.Guess what?Mujahidina hao ndio Osama na Taliban wa leo!

Ungedhani kuwa nchi hiyo ingejifunza kutokana na foreign policy blunders zake kama hiyo ya kusapoti Mujahidina lakini wapi!Makosa kama hayo yameendelea kurudiwa huko Irak na Afghanistan pasipo kuangalia madhara ya muda mrefu.Licha ya sapoti kwa vikundi vinavyotarajiwa kuunga mkono harakati za Wamarekani,nchi hiyo imeendelea kutoa sapoti kwa baadhi ya tawala za kidikteta alimradi uimara wa tawala hizo ni kwa maslahi ya Marekani.Miongoni mwa marafiki wakubwa wa nchi hiyo ni pamoja na utawala wa kifalme wa Saudia na utawala wa kidikteta nchini Misri.Matokeo ya muda mrefu ya uswahiba huu ni kuibuka kwa upinzani wa ndani dhidi ya tawala hizo,ambao in long run unaweza kabisa kuwa na madhara kwa Marekani yenyewe.

Kadhalika,tawala hizo dhalimu zimechangia baadhi ya wananchi wao kukimbilia kwa vikundi vyenye misimamo mikali ya kidini ambayo inaonekana kwa wananchi hao kama yenye kuleta tumaini katika kuwapatia ufumbuzi wa matatizo yao.Kwenye sosholojia ya dini tunafundisha kuwa miongoni mwa sababu za kuwepo dini ni kimbilio la wenye shida.Tawala dhalimu zinaweza kuwa chanzo cha kuibuka na kushamiri kwa vikundi vyenye misimamo mikali ya kidini kwa vile wananchi wanaviona vikundi hivyo kama sehemu ya ufumbuzi wa matatizo yao.

Siasa za jino kwa jino na jicho kwa jicho,sambamba na kuendeleza ubaguzi kwa watu wasio na hatia ni hatari zaidi kwa usalama wa Marekani kuliko ujenzi wa kituo cha utamaduni kinachopigiwa kelele sasa.Actually,uwepo wa taasisi kama kituo hicho cha utamaduni unaweza kusaidia sana katika kujenga maelewano na mshikamo miongoni mwa Wamarekani pasipo kujali tofauti zao za kiimani.

23 Aug 2010

Wakati wa kuelekea kampeni za uchaguzi mkuu wa hapa Uingereza kulijitokeza tetesi za wasiwasi kuhusu afya ya aliyekuwa Waziri Mkuu Gordon Brown.Katika kilichotafsiriwa kama kukata mzizi wa fitina,mtangazaji maarufu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),Andrew Marr,alimuuliza Brown katika mahojiano naye kuhusu tetesi hizo.Katika tetesi hizo ilidaiwa kuwa Brown alikuwa akitumia dawa za kutuliza mara kwa mara.

"Jambo ambalo kila mtu amekuwa akiongelea katika kijiji cha Westminster...Watu wengi katika nchi hii wamekuwa wakitumia dawa walizoelekezwa kununua na daktari (prescription drugs)...Je wewe ni mmoja wao?",aliuliza Marr."Hapana.Nadhani uulizaji swali wa aina hii umekuwa ukiingia sana kwenye ulingo wa siasa za Uingereza",alijibu Brown.Jitihada za mwanahabari huyo kutaka kudadisi zaidi zilizimwa na Brown aliyesema ameshajibu swali hilo.


Nimekumbuka tukio hilo kufuatia kuanguka kwa mara nyingine kwa Rais Jakaya Kikwete na namna vyombo vingi vya habari vilivyokwepa kuripoti tukio hilo kwa uwazi.Hata video iliyomwonyesha Kikwete akianguka iliondolewa mtandaoni kwa haraka,kwa sababu wanazojua waliyoiondoa.Na hata video yenyewe ya tukio hilo ilionyesha "kiduchu" tu kuanguka kwa JK kisha ikaelekezwa kwenye umati wa watu hapo Jangwani.Inaelezwa pia kuwa baadhi ya vituo vya runinga huko nyumbani havikuonyesha tukio hilo katika taarifa zao za habari.

Kichekesho ni kwamba kabla hajakumbwa na dhahma ya kuanguka,JK alijigamba kuwa serikali yake imeboresha uhuru wa habari.Sasa uhuru wa habari ambao tukio la kusikitisha na kuhudhunisha linalomkumba Rais wetu linabanwa ni uhuru kweli au hadithi tu?Na hapa simpingi JK kuwa amejitahidi kudumisha uhuru wa habari bali tatizo langu lipo kwa wanahabari wenyewe.

Je,kulikuwa na maagizo kwamba,kwa mfano,clip ya kuanguka kwa JK iodolewe mtandaoni?Kama jibu ni ndiyo,basi uhuru wa habari anaozungumzia JK una walakini.Lakini kama jibu ni hapana basi wanahabari walioamua kuminya habari hiyo wana maswali ya kuwajibu wasomaji wao na Watanzania kwa ujumla.

Natambua kuwa pamoja na majigambo ya JK uhuru wa habari unaodumishwa zaidi ni ule wa "habari za kawaida" na sio zinazogusa masuala ya watawala.Baadhi yetu ni wahanga wa matumizi hayohayo ya uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza.Ukizungumzia mafisadi walio ndani ya CCM,baadhi ya "wenye nchi" wanakurupuka kudai ni utovu wa nidhamu dhidi ya serikali.Yaani kukemea maovu inakuwa nongwa!?

Tukio la kuanguka kwa JK lilikuwa haki ya kila Mtanzania kufahamishwa na wanahabari.Ikumbukwe kuwa ni Watanzania haohao ndio waliompigia kura kiongozi huyo kuwa Rais wao,na mkutano wake wa Jumamosi ulikuwa na madhumuni ya kuwaomba ridhaa ya kuwaongoza tena.Jakaya Kikwete alikuwa hapo kama mgombea wa CCM,na japo hatuwezi kutenganisha urais wake na ugombea wake huko CCM,ukweli unabaki kuwa katika harakati hizi za kampeni anapaswa kuchukuliwa kama wagombea wengine wa vyama vilivyosimamisha wagombea wao.

Japo mkono mrefu wa dola uko makini zaidi katika udhibiti wa habari "zisizopendeza",yayumkinika kusema kwamba baadhi ya wanahabari na vyombo vya habari hawawezi kukwepa lawama.Nachoshindwa kuelewa kwanini  mara nyingi "habari zisizopendeza machoni mwa watawala" zinaminywa ni kama hali hiyo inasababishwa na uoga tu wa wanahabari au/na vyombo vya habari au ni lile tatizo sugu la kujikomba kwa watawala?

Kama sababu ni uoga,basi hayo ni mapungufu ya wazi kwa mwanahabari au chombo cha habari husika.Hata hivyo,inawezekana uoga huo kuwa ni matokeo ya mfumo wa siasa za chama kimoja ambapo ilikuwa mithili ya kosa la jinai "kumsema vibaya" kiongozi (yaani kusema au kuandika kitu kisichompendeza kiongozi).Tuliaminishwa kuwa viongozi wetu ni kama miungu-watu,hawawezi kukosea,kila wanalofanya ni jema na siku zote wako sahihi.Uoga huu unapaswa kuepukwa kwa vile tupo katika  mfumo mpya wa siasa za uwingi zisizo na nafasi ya "zidumu fikra sahihi za A au B".

Kujikomba ni tatizo sugu si kwa baadhi ya Watanzania tu bali hata baadhi ya Waafrika kwa ujumla.Kwa mbali,kujikomba ni matokeo ya mfumo wa ujima na hatimaye ujamaa ambapo mhusika hujibidiisha "kufanya jambo zuri" hata kama hajaombwa.Kwa bahati mbaya,"jambo hilo zuri" linaweza kuwa lisilo na manufaa kwa jamii.Kwahiyo,mwanahabari aliyebania tukio la kuanguka kwa JK anaweza kuwa alifanya hivyo akiamini kuwa "ni vibaya kumwonyesha Rais akianguka hadharani".Lakini imani hiyo potofu ilimaanisha baadhi ya Watanzania kukoseshwa haki ya kuona kilichomsibu mgombea wa CCM ambaye pia ni Rais wao.

Simnyooshei mtu kidole bali hii ni changamoto tu kwa wanahabari na vyombo vya habari.


Riyadh,Saudia,April 16

Wafanyabiashara wa Saudi Arabia wameiomba Tanzania kama wanaweza kukodi hekta nusu milioni (500,000) za ardhi inayofaa kwa kilimo hususan cha mpunga na ngano kama sehemu ya mpango wa kujitosheleza kwa chakula kwa falme hiyo ya jangwani.

Maofisa waandamizi wa chemba ya biashara ya jiji la Riyadh walitoa ombi hilo wakati wa ziara ya Rais Jakaya Kikwete katika falme hiyo.

"Tanzania ipo tayari kufanya biashara nanyi.Kuna heka milioni 100 (hekta milioni 40.5)za ardhi nzuri yenye rutuba",Kikwete aliwaambia wafanyabiashara hao.

Samir Ali Kabbani,mkuu wa kamati ya kilimo ya chemba hiyo alisema kwamba wamepata majibu mazuri sana."Kikwete ametuambia kwamba Tanzania inaweza kutukodisha ploti ambazo kila moja ina ukubwa wa hadi hekta 10,000 kwa kipindi cha miaka 99",Kabbani alilieleza Shirika la Habari la Reuters baada ya mkutano huo na Kikwete.

Maofisa na wafanyabiashara wa Kisaudi walitrajiwa kuitembelea Tanzania wiki chache baada ya mkutano huo.

"Wanaweza kukodi ardhi kutoka serikalini",January Makamba,msaidizi wa Rais Kikwete,aliieleza Reuters."Lakini inabidi tuhakikishe kuwa hatuishii kwenye hali kama ile ya Nigeria:hifadhi kubwa ya mafuta lakini foleni kubwa kwenye vituo vya kuuzia mafuta",alisema Makamba.

Maafisa wa Saudia wanaiona Tanzania kama sehemu mwafaka kutokana na mazingira ya kijiografia,kisiasa na wingi wa maji na ardhi ya kilimo.Makampuni kadhaa ya nchi hiyo tayari yameanza kuwekeza katika miradi ya kilimo huko Indonesia na Ethiopia.

Agosti mwaka jana Indonesia ilisema kuwa mjumuiko wa makampuni ya Bin Ladin ya Saudi Arabia unatarajia kuwekeza dola bilioni 4.3 katika hekta 500,000 za kilimo cha mpunga.Mahitaji ya ngano kwa Saudia kwa mwaka yanakadiriwa kufikia tani milioni 2.5,na mwaka juzi nchi hiyo iliagiza kutoka nje karibu tani milioni 1 za mchele,kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani.

CHANZO: Reuters


22 Aug 2010

What A good NewS???
Well,your top-above-the-rest blog,ANGALIA BONGO,has officially  moved to a new world.
Thanxx
Admin(Angaliabongo)

Blogu hii ya KULIKONI UGHAIBUNI inafungua ukurasa mpya na kuweka historia ya kipekee katika fani ya habari nchini Tanzania kwa kutangaza hadharani kuwa inam-endorse mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema,Dokta Wilbroad Slaa.

Kuna sababu lukuki za kufanya hivyo lakini hapa nitaziorodhesha chache.Kwanza,blogu hii inataka kuachana na unafiki unaojidhihirisha katika baadhi ya vyombo vya habari vyetu ambapo wahusika wanadai hawafungamani na upande wowote lakini matendo yao yanawasuta kwa kupendelea chama tawala huku wakivibinya kwa nguvu baadhi ya vyama vya upinzani.Hapa simsimangi mtu bali nadhani ni vema kuweka msimamo wazi ili kama chombo cha habari ni wakala wa CCM na JK basi ni vema wasomaji wakafahamishwa bayana.

Pili,blogu hii inaamini kuwa kila Mtanzania mwenye uchungu wa dhati kwa nchi yetu anapaswa kumsapoti Dkt Slaa.Katika utumishi wake kwa umma,mgombea huyo wa Chadema ametuthibitishia kuwa ni mtetezi halisi wa haki za wanyonge na ustawi wa taifa letu.Ni nani asiyefahamu namna Dkt Slaa alivyohatarisha maisha yake kwa “kuwavua nguo mafisadi hadharani” alipotangaza ile “list of shame”?Walitishia kumpeleka mahakamani lakini hakuna mmoja wao aliyediriki kufanya hivyo,na sanasana baadhi yao wakaishia kuburuzwa mahakamani na serikali katika “kujikosha”.Blogu hii inaamini kuwa Dokta Slaa ni mkombozi na suluhisho mwafaka la matatizo lukuki yanayotukabili.

Tatu,binafsi naamini kuwa mgombea wa CCM,Jakaya Mrisho Kikwete,ameshindwa kabisa kutimiza matarajio ya Watanzania licha ya ahadi lukuki alizozitoa wakati wa kampeni zake mwaka 2005 na anazoendelea kuzitoa hadi leo.Ungetegemea kuwa mwezi huu wa toba Kikwete angemwogopa Mola wake na kutubu kwa Watanzania kwamba kuna maeneo mengi tu ambapo yeye na chama chake wamewaangusha Watanzania.Lakini kama ilivyo jeuri ya wanasiasa wengi wa Kiafrika,JK ameendeleza wimbo wa “mafanikio ya Awamu ya Nne”.Yani hata kushamiri kwa ufisadi na “uchakachuaji” wa kura za maoni ndani ya CCM ni mafanikio!

Sababu ya nne inashabihiana na hiyo ya tatu.Naamini kuwa afya ya mgombea wa CCM,Jakaya Kikwete,inapaswa kuwekwa kwenye darubini na wapiga kura wanapofanya maamuzi ya kumchagua rais wa awamu ya tano.JK ameshaanguka hadharani mara tatu na kila mara tunapewa excuse moja baada ya nyingine.Mwaka 2005 tuliambiwa “swaumu na uchovu wa kampeni”.Alipoanguka Mwanza tuliambiwa uchovu wa safari (kana kwamba safari hizo ni zile za Wamachinga wanaotembea juani kwa mguu!).Na jana kaanguka tena jukwaani halafu tunaambiwa sababu ni swaumu.Kwani Makamba hajafunga?Au Rais Karume naye “kobe”?Kuna tatizo zaidi ya swaumu au uchovu lakini kwa vile viongozi wetu wamezowea sifa na sio kasoro basi kuweka hadharani kinachomsibu kiongozi huyo inaonekana ni sawa na uhaini.Blogu hii imaanimi kuwa ili Tanzania ijikwamue katika lindi la umasikini wa kutupwa,sambamba na kukabiliana na janga la ufisadi,tunahitaji kiongozi mwenye afya timilifu,kimwili na kiakili.Hatujui JK ameshaanguka matra ngapi asipokuwa hadharani lakini haihitaji hata cheti cha short course ya utabibu kumaizi kuwa JK ana matatizo ya kiafya yanayofichwa,aidha kutokana na uoga wa wanaopaswa kuujulisha umma kuhusu hilo au maagizo yake mwenyewe kuwa “yuko fiti”.All in all,uzito wa matatizo yanayoikabili Tanzania unahitaji mtu aliye fiti kweli,na sio kwa anavyodhani yeye au anavyotaka umma uamini hivyo ilhali ni kinyume na hali halisi.

Kama nilivyoandika mwanzoni,kuna sababu nyingi zilizopelekea blogu hii kuamua kum-endorse Dkt Slaa lakini chache zilizotajwa hapo juu zinawakilisha hizo nyingine.Nawakaribisha ndugu zangu wa Chadema kuitumia blogu hii kufikisha habari kwa Watanzania pasipo hofu ya kuwa habari hizo zitachujwa,kuminywa au “kuchakachuliwa”.

Natambua bayana kuwa baadhi ya wasomaji wa blogu hii sio wafuasi wa Dkt Slaa au Chadema lakini napenda kuwakikishia kuwa endorsement hii haimaanishi kashfa,matusi,dharau au mambo yasiyofaa dhidi ya wagombea wa vyama vingine.Kuweka wazi msimamo wangu haimaanishi chuki dhidi ya vyama hivyo na wagombea wake bali ni imani yangu kuhusu nani anayeweza kuipatia Tanzania “uhuru wa pili” (mapambano dhidi ya Watanzania wenzetu wanaotafuna raslimali zetu zaidi ya alivyofanya mkoloni).

Mwisho,nawahamasisha bloga wenzangu na vyombo vingine vya habari kwa ujumla kuweka bayana misimamo yao ili kuepuka lawama zinazoweza kujitokeza pale habari za vyama flani zinaponyimwa fursa katika vyombo hivyo.Endorsement ya mgombea au chama ni jambo la kawaida katika nchi za Magharibi lakini hii ni mara ya kwanza kwa chombo cha habari cha Kitanzania kufanya hivyo,na kwa hakika najivunia kuweka historia hiyo.

21 Aug 2010

20 Aug 2010

Pamoja na kumtetea mwanaye,JK alisema (namnukuu)"...hata kama aliyegombea hakuridhishwa na mazingira ya namna aliyeshinda alivyoshinda, ndiyo ameshapata,hivyo jambo la msingi ni kuacha makundi yaliyokuwepo wakati wa kura za maoni, bali wajielekeze katika kutafuta ushindi wa kishindo huku wakijiandaa kwa kugombea kipindi kingine..."SWALI.Je kama kutoridhishwa huko kunatokana na matumizi ya rushwa?Au kwa vile Awamu ya Nne ilikuwa na huruma kwa mafisadi basi wagombea waliofisadiwa nao waige mfano wa serikali hiyo?Soma habari kamili HAPA.

19 Aug 2010

I came across an article below in The Moscow Times of today (“Financial Investigator's Son Handles Cash for Aeroflot”) and thought it would be appropriate to rekindle the discussion on Nepotism in Tanzania we had with you a while ago, see my email of Aug. 11th herein under. Before that, in July this year, I made similar comments about the son of the former Russian prime minister {Mr. Mikhail Fradkov - now Head of the Russia’s Foreign Intelligence Service (SVR)}, Mr. Peter Fradkov, who is currently the deputy chairman of Vnesheconombank (Russia’s State Bank for Foreign Economic Relations) and also the deputy chairman of the African Coordinating Committee for Economic Cooperation with African Countries (AfroCom). See in the Aeroflot article mentioned above (read the yellow-shaded part below) on how other senior Russian government officials place their off-springs in honey places, a similar trend currently appearing in Tanzania, albeit at times we see off-springs of our officials involved in fraudulent crimes as you may read in the article below on the son (Tony) of CCM stalwart Kingunge Ngombale Mwiru (“Kingunge relative in the dock for forgery, 242 million/- theft”). As I wrote earlier, I don’t think putting kids and relatives of bigwigs in high places based on kinship only and not merit is a wise thing to do. Indeed, it is very dangerous and speaks a lot of the unhealthy political situation in a country as well as the existence of an incompetent and ineffective government .

Best regards,

Shaaban

Moscow, Russia

16 Aug 2010

Miongoni mwa mapungufu yanayowakabili baadhi ya Watanzania wenzetu ni kushindwa kusifia pale inapostahili.Na miongoni mwa "udhaifu" wangu ni kushindwa kujizuia kumwaga sifa pale inapostahili (au kukosoa pale inapobidi).Waingereza wana msemo "beauty should never be imprisoned", yaani-kwa Kiswahili- "urembo haupaswi kuwekwa jela".Mantiki ya msemo huo ni kuhamasisha jamii kusifia vinavyostahili sifa.Na kwa kufanya hivyo tunawafanya wanaostahili sifa hizo kutambua thamani yao na pengine kuboresha zaidi wafanyayo.

Nisijizungushe sana.Leo naomba kukujulisha msomaji wangu mpendwa moja ya blogu ambazo kila napozitembelea (na ninatembelea blogu nyingi kila siku ya Mungu) hupatwa na msisimko wa aina yake.Blogu hiyo si nyingine bali ni La Princessa World.Of course,ili ufahamu ni nachoongea hapa inabidi "yai liwe linapanda" (I mean,uwe unaimudu vema lugha ya Kiingereza) kwani mdada mwenye blogu hiyo "anakichezea Kiingereza namna anavyotaka".Na hiyo ni moja ya mambo yanayovutia katika "uandishi binafsi" (kwa mfano makala magazetini au bloguni): namna mwandishi anavyoweza kucheza na lugha apendavyo kama ambavyo mwanasoka mahiri anavyoweza kuuchezea mpira atakavyo.Tuseme uandishi unaoshabihiana na vipaji vya viumbe kama Ronaldinho,Messi,Zidane,nk.

Blogu ya La Princessa World imejikita zaidi kwenye masuala ya fasheni,wenye majina (celebrities),muziki,filamu na mambo mengine ya kusisimua.Yayumkinika kusema kuwa masuala ya fasheni ni ya akinadada zaidi lakini,binafsi,kanuni yangu ya kumudu kuwa "well-rounded" ni kujifunza mambo mengi kadri inavyowezekana.Na ni katika kufanya hivyo ndipo unaweza "kukopa" ujuzi na uelewa wa wengine waliobobea katika fani zao."Ugonjwa" wangu ni siasa lakini napendelea kuitanua siasa hadi kwenye maeneo mengine ya maisha,kwa mfano siasa za urembo,muziki,filamu,nk.Hata hivyo,by "kutanua" simaanishi kuchanganya siasa na urembo,kwa mfano,bali kama ilivyo katika "siasa proper" ,ninachofanya ni kuelewa kwa undani ishu kama trends,shakers and movers,siri na mbinu,na vitu kama hivyo.

Nimalizie kwa kukusihi uwe unamtembelea La Princessa kufaidika kama navyofaidiaka mie kila napotembelea hapo.Usitafsiri kama "nampigia mtu debe" bali,kama nilivyoandika awali,napenda kuenzi vipaji vya wenzetu na   pia kila mara napenda kuwajuza (kuwajulisha) wasomaji wangu wapendwa yale yote ambayo kwa mtizamo wangu nadhani yanafanya kila ziara yako mtandaoni ikupatie kitu kipa au "kile roho yako inapenda".

Kwa La Princessa,nachoweza kuandika kwa kifupi ni kuwa umesimika kiwango (setting the bar) katika kublogu sio kwa akina dada pekee bali hata kwa bloga wa kiume.Kinachonigusa zaidi ni namna unavyocheza na lugha,kitu mabcho sio tu kinaonyesha namna unavyoimudu bali pia unavyoweza kuitumia katika namna mwafaka kumburudisha msomaji wako.

Word up!

12 Aug 2010

Baada ya kimya cha miaka miwili na mwezi mmoja hatimaye nimerejea katika ulingo wa uandishi wa makala zangu za Raia Mwema Ughaibuni katika jarida maridhawa la Raia Mwema.Haikuwa rahisi kwangu kukaa kimya huku nchi yetu ikiteketezwa na mafisadi lakini ililazimu kuwa hivyo ili kujipanga upya.

Katika makala ya wiki hii nimeelezea kwa kifupi kilichonisibu hadi nikafikia uamuzi wa kusitisha uandishi wa makala hizo.Basi nisikupunguzie uhondo bali bonyeza kiunganishi kifuatacho usome habari na makala nyingine motomoto katika jarida makini la Raia Mwema pamoja na makala ya wiki hii yenye kichwa MASLAHI YA UMMA NI ZAIDI YA VYOTE.

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.