23 Jun 2015

Polisi jijini London hapa Uingereza wamemkamata Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Rwanda, Jenerali Karenzi Karake, kutokana na maombi ya Hispania ambako anahitajika kwa makosa ya uhalifu wa kivita.

Jenerali Karake, Mkurugenzi Mkuu wa National Intelligence and Security Services alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Heathrow, Jumamosi iliyopita, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na polisi wa hapa jana.

"Karenzi Karake, mwenye umri wa miaka 54, raia wa Rwanda, alifikishwa mbele ya mahakama ya Westminster, (jijini London)...baada ya kukamatwa kwa kutumia hati ya Ulaya ya kusaka watuhumiwa (European Arrest Warrant) kwa niaba ya mamlaka za Hispania, ambako anatafutwa kuhusiana na uhalifu wa kivita dhidi ya raia," ilieleza taarifa iliyotolewa kwa barua-pepe.

Jenerali huyo alirudishwa rumande hadi Alhamisi.

Haikuwezekana mara moja kuwasiliana na familia ya mkuu huyu wa ushushushu au mwanasheria wake nje wa muda wa kazi jijini London. Ubalozi wa Rwanda hapa Uingereza nao haujatoa maelezo yoyote.

Mwaka 2008, jaji wa mahakama kuu ya Hisania, Fernando Andreu, aliwatuhumu viongozi 40 wa kijeshi na kisiasa wa Rwanda, ikiwa ni pamoja na Jenerali Karake, kujihusisha na mauaji ya kisasi kufuatia mauaji ya kimbari yaliyoikumba nchi hiyo mwaka 1994.

Jaji huyo aliwaona watuhumiwa hao na hatia ya mauaji ya kimbari, ualifu dhidi ya binadamu na ugaidi, makosa yaliyopelekea vifo vya mamia ya maelfu ya watu ikiwa ni pamoja na Wahispania.

CHANZO: imetafsiriwa kutoka Matthewaid.com


21 Jun 2015

Ni kitu gani?

Summer Solstice, kwa lugha nyepesi, ni siku yenye mchana mrefu zaidi kuliko zote katika mwaka. Neno 'mchana' hapa linamaanisha muda wa mwanga wa jua. Ni siku mbapo baadhi ya sehemu, kama hapa Uingereza, zina masaa mengi zaidi ya mchana (mwanga wa jua) kuliko usiku (muda wa kiza).
Pengine ni muhimu kufahamu kwamba kwa hapa Uingereza, kwa mfano, maana ya mchana na usiku ni tofauti na huko nyumbani, kwa kiasi flani. Kwa mfano, Ukikutana na mtu saa 6 alfajiri, salamu huwa 'Good morning' kwani kwa wenzetu hawa, asubuhi inaanza rasmi saa 6 kamili 'usiku.' (0000 midnight). Vilevile, katika msimu wa baridi ambapo jua huzama mapema na kuchelewa kuchomoza, si ajabu ukiagwa kwa 'Good night' saa 11 jioni, kwa sababu muda huo tayari jua limeshazama.
Neno 'Solstice' linatokana na neno la Kilatini  'solstitium' linalomaanisha meaning ‘jua kusimama’.

Kwanini inatokea?

Kwa wenye kumbukumbu ya somo la Jiografia, Summer Solstice hutokea pale mhimili wa sayari yetu 'unapoegemea' zaidi kuelekea kwenye jua.
Kinyume cha tukio hili,  Winter Solstice, hutokea pale mhimili wa dunia 'unapoelemea' mbali zaidi na jua, na kusababisha muda mfupi zaidi wa jua katika siku, yaani mchana - kwa maana ya mwanga wa jua- unakuwa mfupi mno kuliko usiku.

Inatokea lini?

Summer solstice hutokea kati ya Juni 20 na 22.
Kwa mwaka huu ni leo Jumapili Juni 21.
Kwa hapa Glasgow, jua litachomoza saa 10 na dakika 31 asubuni (takkriban saa moja tangu muda huu ninapoandika makala hii) na kuzama  saa 4 na dakika 6 usiku


17 Jun 2015

I am not in anyway whatsoever pretending to act like mie ndo mwenye uchungu saaana na Tanzania yetu ila kuna vitu ukivisikia kutoka huko nyumbani vinaumiza sana. Nimepata taarifa za kusikitisha sana. Goes like this: kuna watumishi flani wa serikali katika taasisi moja nyeti sana waliokuwa wakitumia utumishi wao katika taasisi hiyo kufanya kila aina ya maovu: kukodisha silaha kwa majambazi, kuwatapeli watu kwa kuwapelekea katika ofisi nyeti ili kujenga imani yao kisha kuwaliza...lakini kibaya zaidi, ninataarifiwa kuwa watu hao baada ya kufukuzwa kazi wanaendelea na uhalifu wao.Kibaya zaidi, hawa sio wahalifu wa kawaida, ni watu waliofunzwa kukabiliana na uhalifu...kwahiyo wanajua mbinu za kuepuka vyombo vya dola.

Kinachoniuma ni kwamba taasisi husika ilichukua uamuzi wa kuwafukuza kazi badala ya kuwapeleka jela, kwa sababu makosa yao kisheria yana adhabu moja tu: JELA. Sasa kwa vile baadhi ya wahusika walikuwa na mhusiano na vigogo flani, wakasamehewa kwa kufukuzwa kazi tu.Lakini naambiwa balaa wanalosababisha huo mtaani ni balaa.

Hili ndilo tatizo kubwa linaloikwaza Tanzania yetu: KULINDANA. Si kwamba wahusika walipoamua 'kuwasamehe' wahusika hao walikuwa hawajui madhara watakayosababisha mtaani, lakini kutokana na ubinafsi wao na kutojali madhara yatakayowakumba Watanzania wenzao, wakaamua kuwalinda wahalifu hao.

Ninaifuatilia taarifa hii kwa karibu, na nitaendelea kuwahabarisha.Nina majina ya wahusika lakini kuna taratibu flani inabidi nizifuate ili nisiishie kuwapa watu kisingizo cha 'kuvujisha siri za nchi.'

Jamani, Tanzania ni yetu sote.Tusifikirie tu kuhusu leo.Kuna kesho, mwaka kesho na miaka kadhaa huko mbele.Tunawaandalia nini wajukuu zetu?

10 Jun 2015

WIKI iliyopita ilitawaliwa na hekaheka za Uchaguzi Mkuu ambapo makada kadhaa wa chama tawala CCM walijitokeza kutangaza nia ya kuwania urais endapo watapitishwa na chama chao.
Kama nilivyoandika katika makala yangu iliyopita, uamuzi huo wa kuwania nafasi hiyo ni haki kwa kila Mtanzania mwenye sifa stahili. Hata hivyo, wingi wa makada wa CCM waliokwishatangaza nia ya kuwania urais, sambamba na idadi ya makada wanaotarajiwa kutangaza nia zao hivi karibuni, imezua maswali makuu mawili.
Kwanza, je utitiri huu wa wagombea ni matokeo ya kukua kwa demokrasia ndani ya CCM au nchini kwa ujumla? Swali hili linaendana na dhana halisi ya demokrasia ambapo wingi wa wagombea, wanachama au vyama vya siasa hutafsiriwa kama ishara za kukua au kustawi kwa demokrasia. Hata hivyo, mara kadhaa dhana hii imethibitika kuwa fyongo, ambapo nchi kadhaa zina idadi kubwa tu ya vyama vya siasa lakini mara nyingi vyama hivyo huwa ni kwa maslahi ya viongozi na sio kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi. Licha ya vyama vya siasa, nchi kadhaa zina idadi kubwa ya wabunge, kama ilivyo Tanzania yetu, lakini kwa kiasi kikubwa idadi hiyo haijafanikiwa kumaanisha uwakilishi bora kwa wananchi.
Pili, je kujitokeza kwa idadi hiyo kubwa ya makada wa CCM kunachangiwa na kile kinachodaiwa kuwa urais wa Jakaya Kikwete umeshusha ‘bar’ ya wadhifa huo kiasi kwamba kila mtu anapata ujasiri wa kuitaka nafasi hiyo? Japo ni vigumu kupata mwafaka wa jumla kuhusu miaka kumi ya utawala wa Rais Kikwete, kumekuwa na hisia za mara kwa mara kwamba utawala wake umekuwa wa kirafiki zaidi, au ‘kishkaji’ kama wanavyosema huko mtaani. Teuzi mbalimbali zimekuwa zikitazamwa kama za kirafiki na sio kutokana na sifa stahili za wateuliwa. Na hili linadaiwa kuchangia mabadiliko kadhaa ya kabineti ya kiongozi huyo.
Tumeshuhudia mara kadhaa jinsi Rais Kikwete alivyopatwa na kigugumizi kuchukua hatua stahili dhidi ya watendaji wake, kikwazo kikidaiwa kuwa ni urafiki uliopo kati yake na watendaji hao walioshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Sasa, urais sio uongozi wa nchi tu bali ni ulezi wa viongozi wajao ikiwa ni pamoja na marais wajao. Na ndio maana tumesikia baadhi ya watangaza nia wakijisifu kuwa wamekuwa wasaidizi wa Rais Kikwete kwa muda fulani, wakimaanisha wamejifunza mambo kadhaa kutoka kwake. Kwa hiyo ni wazi ubora au upungufu wake unawagusa walio chini yake, na katika harakati hizi za kupatikana mrithi wake, yawezekana umechangia kutuletea rundo hili la wanaotaka kumrithi.
Lakini iwe ni kukua kwa demokrasia au urais wa Kikwete umeifanya nafasi hiyo kuwa ya ‘kawaida’ kiasi kwamba mwanasiasa yeyote anaweza kujiona anaweza kuimudu, ukweli unabaki kuwa waliojitokeza kuwania nafasi hiyo hawajavunja kanuni yoyote, na Katiba yetu inawaruhusu kufanya hivyo. Hata hivyo, sisi kama wananchi pia tuna haki ya msingi ya sio tu kuwaunga mkono au kuwapinga wanaojitokeza kuwania nafasi hiyo bali pia kuwachambua, kuwapongeza au kuwakosoa. Na makala hii inajikita zaidi katika kuchambua kwa ujumla zoezi hilo la kutangaza nia ya kuwania urais miongoni mwa makada kadhaa wa CCM waliokwishajitokeza hadi sasa.
Kimsingi, ukiondoa Makongoro Nyerere ambaye aliweka bayana kuwa hawezi kutangaza ajenda zake binafsi ilhali mgombea atakayepitishwa na CCM atapaswa kuuza sera zake kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho, makada wengine wote waliotangaza nia wameongelea masuala yale yale ambayo takriban kila Mtanzania anayafahamu. Nisingependa kuyaorodhesha hapa kwa vile ninaamini kila mmoja wetu anatambua tunachohitaji, tunachostahili kuwa nacho lakini hatuna na kwa nini hali iko hivyo.
Labda jambo moja la wazi ni kwamba nchi yetu ina utajiri mkubwa wa wanasiasa wenye uelewa wa hali ya juu wa matatizo yanayoikabili Tanzania yetu, sambamba na mbinu za kuyatatua matatizo hayo. Takriban kila mtangaza nia ya kuwania urais amejitahidi kwa undani kuyachambua matatizo yetu, wengine wakienda mbali zaidi na kuelezea vyanzo vya matatizo hayo, na kutoa ufumbuzi wa kuyatatua.
Swali la msingi ni hili: walikuwa wapi siku zote na ‘utaalamu huo wa matatizo yetu’ hadi nchi yetu kufikia katika hali hii mbaya tuliyo nayo sasa? Je, yawezekana licha ya takriban wote kuwa walipewa nafasi na Rais Kikwete kuwa mawaziri au manaibu waziri katika kabineti zake, walimhujumu kwa kuficha uwezo wao ili baadaye waje kutumia upungufu uliopo kama mtaji wa kuomba nafasi hiyo ya urais?
Haiingii akilini kabisa kusikia mtu akielezea lundo la matatizo yetu ikiwa ni pamoja na yale ambayo hata baadhi ya wananchi hawayafahamu, na kutoa majibu mengi zaidi ya matatizo hayo, lakini mtu huyo huyo amekuwa serikalini kwa miaka kadhaa pasipo kutumia japo asilimia 0.1 ya ujuzi anaotueleza anao kuhusu matatizo yetu.
Je, wanaotaka kutueleza kuwa haikuwa rahisi kwao kuweza kututumikia kwa uwezo wao wote kwa vile tu hawakuwa marais? Nauliza hivyo kwa sababu ghafla, hata baadhi ya mawaziri ambao waliishia kutimuliwa kwa skandali za ufisadi wanamudu kutueleza kuwa wana ufumbuzi wa matatizo yetu. Ninahitimisha kuwa huu ni utapeli wa kisiasa, kwa kimombo wanasema political conmanship.
Nadhani wanaohisi kuwa Rais Kikwete ameishusha sana ‘bar’ ya urais wanapata nguvu ya hoja hiyo kutokana na wanasiasa kama hao, ambao umaarufu wao hautokani na nyadhifa walizoshika bali skandali zilizosababisha wang’olewe madarakani. Inakera na kuchukiza kuoina wanasiasa ambao pasi kuambiwa na mtu yeyote yule wanajitambua kuwa hawafai lakini leo wanapata ujasiri wa kutaka wapewe urais. Hivi URAIS umekuwa URAHISI kiasi hicho?
Lakini hata tukiweka kando maswali hayo ya msingi, hizi hadithi tamu za kuleta matumaini kwa kila anayezisikia zitawezekana vipi ilhali pindi wakipitishwa na chama chao hawatojinadi kwa ahadi hizo bali zitakazobainishwa kwenye ilani ya chama chao?
Sawa, labda watasema kuwa ukiwa mgombea una fursa ya kushiriki uandaaji wa ilani hiyo, lakini ukweli mchungu ni kwamba CCM haitoafikiana na mgombea atakayekuja na sera za kukiua chama hicho. Ninasema ‘sera za kukiua’ kwa sababu kwa kiasi kikubwa chama hicho kimeachana kabisa na misingi yake ya asili ya kuwa mtetezi wa wanyonge na badala yake kimetekwa na mafisadi. Chama kinachojigamba kuwa ni cha wakulima na wafanyakazi kimekuwa chama cha matajiri na wasomi wasiotaka kutumia usomi wao kwingineko, bali katika siasa (kwa minajili ya ulaji).
Kibaya zaidi, wengi wa makada waliotangaza nia wamekuwa wezi wa sera za vyama vya upinzani, sera ambazo makada hao wamekuwa wakizikejeli mara kadhaa lakini ghafla wameziona zinafaa kwa vile wanaotaka tuwaamini kuwa wanaweza kutuongoza. Ninarejea tena, huu ni utapeli wa kisiasa.
Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu maendeleo ya harakati hizo za kutangaza nia ya kuwania urais, kupitia mitandao ya kijamii. Japo Watanzania waliopo kwenye mitandao hiyo ni wachache lakini kwa kuzingatia kanuni za tafiti, wanaweza kuwa sampuli nzuri kuwakilisha mitizamo mbalimbali ya Watanzania wengi kwa ujumla. Nimebaini masuala kadhaa katika ufuatiliaji wangu: kwanza, angalau Watanzania wengi wanafahamu wanasiasa wa aina gani wasiotakiwa katika urais. Lakini hapo hapo kuna tatizo: wanajua wasiyemtaka lakini hawajui wanayemtaka.
Katika hili ninawatumia lawama nyingi ndugu zetu wa vyama vya upinzani hususan UKAWA. Hivi watu hawa wana maelezo yoyote ya maana zaidi ya uzembe kwa kushindwa kutumia fursa hii ambapo ‘CCM wanakabana makoo wenyewe kwa wenyewe’ kumnadi mgombea wao laiti wangekuwa wameshampata? Watetezi wao wanadai UKAWA wapo ‘bize’ kuhangaikia suala la uandikishaji wapiga kura. Hilo ni suala muhimu lakini lisiloweza kuwazuia wao kukamilisha mchakato wa kumpata mgombea wao.
Jingine nililogundua katika ufuatiliaji wangu ni wepesi wa Watanzania kuhadaiwa na maneno matamu yasiyoambatana na uthibitisho wowote ule kuwa ni ya kweli. Mara baada ya hotuba utasikia watu wakidai “aisee huyu jamaa anatufaa haswa…” kisa katoa hotuba nzuri. Tangu lini uwezo wa kutoa hotuba nzuri unamaanisha uwezo wa kivitendo? Kimsingi, Tanzania yetu haijawahi kuwa na uhaba wa watoa porojo. Sisi ni wazuri kweli kwa maneno ila tatizo letu ni kwenye kutafsiri maneno kuwa vitendo.
Ukitaka kujua uwezo wetu katika porojo nenda kwenye vikao vya harusi, au hata kwenye vijiwe vya kahawa. Huko kuna watu wanaongea sio tu kama wamemeza santuri au CD nzima bali pia wana uelewa na utaalamu wa hali ya juu wa fani ambazo wala hawakukanyaga darasani kuzisomea. Sasa kama hayo yanawezekana vijiweni, kwa nini nikiamua kuwania urais nisitumie uwezo wangu wote wa upigaji porojo kuwahadaa watu kuwa mimi ndiye yule waliyekuwa wakimsubiri miaka nenda miaka rudi? Pengine kufikia hapa, ninakuomba msomaji mpendwa tafuta wimbo wa ‘Ndio Mzee’ wa msanii wa muziki wa Bongofleva, Joseph Haule (Profesa Jay) kisha rejea ninachokieleza hapa.
Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu, uchaguzi mkuu ujao haupo kwa manufaa ya chama au mgombea fulani. Ni kwa ajili yetu sisi wananchi. Sisi ndio wanufaika wa uamuzi bora utakaotupatia mtu wa kuikomboa Tanzania yetu kutoka hapa ilipo na kuifikisha inapostahili kuwepo, na sisi ndio waathirika iwapo tutafanya uamuzi fyongo kama tulivyofanya huko nyuma hadi kujikuta tulipo sasa. Mtaani wanasema ‘akili za kuambiwa changanya na za kwako.’ Ninawasihi Wtaanzania wenzangu kutokuwa wepesi kuhadaiwa na hizi porojo ambazo tumekuwa tukizisikia miaka nenda miaka rudi na nchi yetu inazidi kuangamia kwa umasikini, ufisadi na mabalaa mengine.

5 Jun 2015


Tafsiri: CEORT ina furaha kuwa mwenyeji wa mdahalo wa kwanza katika historia ya Tanzania kwa wanaowania urais. Tutaweka uchumi kuwa mada kuu ya mdahalo huo mwaka huu, na sio watu (wagombea) au rangi za vyama. Sumaye, Balozi Amina Salum Ali, January Makamba, Bernard Membe na Samule Sitta watakuwa wa kwanza kutangaza vipaumbele vyao kisera kwa taifa katika shughuli hiyo. Cha kusikitisha, EDWARD LOWASSA amekataa kushiriki. Ungana nasi hoteli ya Hyatt (jijini Dar es Salaam) Jumatatu ijayo saa 2 asubuhi.Midahalo mingine miwili na watangaza nia wengine ikiwajumuisha wanasiasa wa upinzani itafuata.

Huyu LOWASSA ndiye anayehamasisha mchakmchaka wa maendeleo? Ni rahisi sana kuwahadaa watu kwa kuwahubiria porojo lakini yahitaji ujasiri na uwezo wa kiongozi kushirikia mdahalo wa kuwashawishi Watanzania kwanini unafaa kuwaongoza


Tunahitaji Rais mpinga ufisadi si wa kujitetea eti yeye si fisadi

HATIMAYE baada ya taarifa za muda mrefu zisizo rasmi, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alitangaza mwishoni mwa wiki iliyopita dhamira yake kukiomba Cchama Cha Mapinduzi (CCM) kimpitishe kuwa mgombea wa kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

Taarifa za Lowassa kutaka urais zimekuwa zikivuma kwa muda mrefu mno, na kwa hakika haikuwa jambo la kushangaza alipoamua majuzi kuzibadili taarifa au tetesi hizo kuwa jambo kamili.

Binafsi, baada ya kuisikia hotuba yake aliyoitoa jijini Arusha mbele ya halaiki ya wananchi nimebaki na swali moja la msingi: Lowassa ana kipi hasa cha kuwafanya Watanzania waamini kaulimbiu yake ya ‘safari ya matumaini.’
Sijui kwenu wasomaji wapendwa, lakini kwangu kubwa linalonifanya nimkumbuke Lowassa ni kashfa ya Richmond ambayo hatimaye ilisababisha ajiuzulu wadhifa wake wa Uwaziri Mkuu.

Na kwa sababu anazojua yeye mwenyewe, hotuba yake ya Arusha haikugusia suala hilo ambalo awali alipozungumza na waandishi wa habari alidai angeliongelea kwa kirefu. Tayari kuna baadhi yetu tunaoanza kuhoji uwezo wa mwanasiasa huyo kushika nafasi nyeti ya urais, na swali ni hili: kama ndani ya wiki moja anaweza kuahidi kuzungumzia kashfa ya Richmond na kisha asizungumzie, je mustakabali wa taifa letu utakuwaje mikononi mwa mtu anayeweza kuvunja ahadi anazojiwekea mwenyewe?

Pengine katika hatua hii ni muhimu nitanabaishe kuwa sina tatizo na Lowassa kutumia haki yake ya kikatiba na kidemokrasia kuwania urais. Hiyo ni haki ya kila Mtanzania mwenye sifa stahili. Lakini kwa hakika natatizwa sana na uadilifu wake.

Licha ya suala la Richmond, ambalo amedai yeye hahusiki, kuna hoja ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ‘kumwekea vikwazo’ huko nyuma katika nia yake ya urais, ambapo inaelezwa kuwa Nyerere alitatizwa na utajiri mkubwa wa mwanasiasa huyo usio na maelezo ya kuridhisha.

Na majuzi Lowassa katamka bayana kuwa anauchukia umasikini. Na amekiri kuwa yeye ni ‘tajiri kiasi.’ Lakini pengine Watanzania wengi wangependa sana kufahamu chanzo cha utajiri wake kwa sababu sote tunajua mtu haamki tu na kujikuta tajiri. Sawa, amekuwa mtumishi wa umma kwa muda mrefu, lakini kwa jinsi anavyomudu ‘kumwaga pesa’ katika shughuli mbalimbali, ni vigumu kuamini kuwa chanzo cha fedha hizo ni utumishi wake wa muda mrefu serikalini pekee.

Nyakati kadhaa amekuwa akitueleza kuwa kuna marafiki zake wanaomchangia fedha ‘anazomwaga’ katika hafla mbalimbali. Je, ni marafiki gani hao? Lakini kubwa zaidi, vyanzo vya utajiri wao ni vipi hasa?

Kadhalika, mwanasiasa huyo ameonekana kuzungukwa na wanasiasa wenzake kadhaa ambapo miongoni mwao ni majeruhi wa skandali mbalimbali za ufisadi. Waingereza wana msemo, nionyeshe marafiki zako, nami nitakueleza wewe ni nani’ (show me your friends and I will tell who you are). Hivi Lowassa anaweza kutueleza lolote kuhusu ukaribu alionao na watu hao?

Kwa upande mwingine, mie nilipoisikiliza kwa makini hotuba yake ya majuzi huko Arusha niliona kama ninamsikiliza mtu ambaye tayari ameshapitishwa na chama chake kugombea urais na kilichobaki ni taratibu tu za kumkabidhi wadhifa huo. Sina tatizo na kujiamini kwake lakini kuna wanaojiuliza, hivi huyu mtu asipopitishwa na chama chake itakuwaje?

Kuhusu kaulimbiu yake ya ‘safari ya matumaini,’ bahati nzuri siku moja tu baada ya kuitangaza, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbroad Slaa, akawafumbua macho Watanzania kwa kuwaeleza kuwa kinachohitajika sio safari ya matumaini bali ya uhakika. Watanzania wamekuwa wakiishi kwa matumaini kwa muda mrefu sana; matumaini kwamba siku moja nchi yao itaondokana na umasikini ilionao na kuishi kulingana na utajiri lukuki iliyojaliwa nao; matumaini ya kuondokana na janga la ufisadi linalozidi kuota mizizi; matumaini ya kuona sarafu yao ikiacha kuporomoka kwa kasi; matumaini ya mgawo wa umeme wa kudumu kufikia kikomo; matumaini ya maisha bora kwa kila Mtanzania waliyoahidiwa miaka 10 iliyopita na timu ya uchaguzi ya Rais Jakaya Kikwete ambayo ilikuwa ikiongozwa na Lowassa, na matumaini mengine kadha wa kadha

Hapana, Watanzania wanaotaka safari ya uhakika, kama alivyosema Dk. Slaa, na sio ya matumaini hewa kama yaliyoahidiwa miaka kumi iliyopita na yamebaki kuwa historia tu.

Awali, Lowassa alidai kuwa moja ya vipaumbele vyake vikuu ni elimu, na kuleta kaulimbiu nyingine ya elimu kwanza. Labda kabla ya yeye kuiponda kaulimbiu ya kilimo kwanza angewaambia Watanzania kwa nini imebaki kuwa porojo tu lakini hiyo yake itatekelezwa kwa vitendo.

Pengine atazungumzia uanzishwaji wa shule za kata. Tukiweka kando matatizo kadhaa yanayozikabili shule hizo, maarufu kama ‘Santa Kayumba,’ ni muhimu Watanzania wenzangu kutambua kuwa hazikujengwa kutoka hela za mfukoni mwa Lowassa. Ninaelewa kwa nini mwanasiasa huyo anaweza kutaka kujichukulia pointi kwenye suala hilo; kasumba iliyojengeka miongoni mwetu kwamba mtu akiajiriwa kutimiza wajibu fulani na analipwa kutimiza wajibu huo anaonekana mchapakazi. Yaani tumefika mahala kuwa inatarajiwa mtu akipewa majukumu atafanya ubabaishaji, Kwa hiyo yule atakayefanya kinyume cha kuwajibika, basi inakuwa kama miujiza.

Sidhani kama Lowassa ana moja la kuwaeleza wananchi kuwa hili nililifanya kwa jitihada zangu kama Edward na sio Waziri Mkuu niliyekuwa ninalipwa mshahara kutimiza wajibu huo.

Tukirejea kwenye hotuba yake, binafsi sikusikia jambo lolote geni ambalo hatulifahamu. Sote tunajua kuhusu umasikini wetu, sote tunafahamu kuhusu matatizo yote aliyoyataja katika hotuba yake. Na kwenye tatizo la foleni za magari jijini Dar es Salaam amnbazo amedai atazimaliza ndani ya miezi 12, niseme tu kuwa hiyo ni porojo.

Kwanza, kwani alipokuwa Waziri Mkuu huko nyuma tatizo hilo halikuwepo hadi hakuona haja ya kulitatua? Pili, foleni sio tatizo jijini Dar es Salaam tu bali hata kwenye majiji makubwa ya Ulaya na katika mabara mengine. Kwetu linakuwa tatizo sugu zaidi kutokana na miundombinu mibovu na idadi kubwa ya uhamiaji mijini isiyoendana na wahamiaji, sambamba na wingi wa magari yakiwemo yasiyostahili kuwepo barabarani.

Amejitahidi kutueleza matatizo ambayo kila mmoja wetu anayafahamu. Hata hivyo kama ilivyo kwa maradhi, suala sio tu tabibu kuelezea mgonjwa anakabiliwa na tatizo gani la kiafya bali kumwelekeza tiba na hatimaye kumpatia tiba husika. Wanasiasa wetu hawaishiwi umahiri wa kuyajua matatizo ya wananchi, hata kama wanasiasa hao hawajawahi kukumbana na matatizo hayo ‘ana kwa ana.’ Sawa, ili kuweza kulitatua tatizo ni lazima kujua chanzo chake, lakini haina manufaa kutaja tu matatizo tuliyonayo pasi kuyaeleza yametokana na nini au jinsi gani tunaweza kuyakabili.

Nikiri kwamba nilipata hasira kumsikia Lowassa akiwaimbia wananchi kuhusu ‘mchakamchaka wa maendeleo’ bila kuwaambia maendeleo hayo yataletwa vipi, na kwa nini miaka zaidi ya 50 tangu tupate Uhuru (na Lowassa akiwa mtendaji wa serikali katika miaka kadhaa katika hiyo) bado tunasuasua kimaendeleo.

Nimalizie makala hii kwa kurejea nilichoandika hapo awali kuwa Lowassa ana haki kikatiba kuwania urais. Hata hivyo, name kama Mtanzania pia nina haki ya kuelezea bayana kuwa mwanasiasa huyu hafai kuwa rais wetu ajaye, sababu kubwa zaidi ikiwa ni suala la ufisadi wa Richmond.

Hatuhitaji mgombea wa urais ambaye badala ya kutueleza jinsi ya kukabiliana na moja ya matatizo makubwa kabisa yanayoikabili Tanzania, yaani ufisadi, anatumia muda mwingine kujitetea kuwa yeye sio fisadi.


Wito wangu kwa Watanzania wenzangu ni huu: tunastahili kilicho bora. Haiingii akilini kabisa kuamini kuwa mtu aliyelazimika kujiuzulu kwa kashfa ya ufisadi akiwa Waziri Mkuu, atakuwa kiongozi bora akishika urais. Ni muhimu kufumbua macho na masikio na kuacha kuamini hizo porojo ambazo tumekuwa tukizisikia miaka nenda rudi lakini Tanzania yetu inazidi kudidimia.

29 May 2015

Tarehe kama ya leo miaka 7 iliyopita (29/05/2008), mama yangu mzazi Adelina Mapango (Mama Chahali) alifariki. Kifo chake kimeacha pengo kubwa lisilozibika-kwa mumewe (yaani baba) walodumu katika ndoa kwa miaka 53, kwa sie wanawe wanane, na hasa kwa vitinda mimba Kulwa na Doto ambao kwao marehemu alikuwa ni zaidi ya mzazi kwao bali rafiki pia. Miaka 6 imepita lakini uchungu moyoni ni kama kifo hicho kimetokea leo. We miss you so much mama. We stiĺl and will always love you. May your soul rest in eternal peace. Amen!




Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.