24 Jun 2016



JUMATANO hii, wakazi wa hapa Uingereza watapiga kura kuamua hatma ya nchi hii kwenye Umoja wa Ulaya. Katika kura hiyo, Waingereza wanaulizwa iwapo wanataka nchi yao ibaki kuwa mwanachama wa umoja huo au wanataka nchi yao ijitoe.


Hadi wakati ninaandika makala hii, kura za maoni (opinion polls) zinaashiria matokeo yanayokaribiana kabisa, kwa maana kwamba upande wowote utakaoshinda, utafanya hivyo kwa tofauti ndogo tu ya ushindi.



Kampeni za kura hiyo zilisimamishwa wiki iliyopita baada ya mauaji ya kwanza katika historia ya nchi dhidi ya mbunge aliyepo madarakani, ambapo mbunge wa chama kikuu cha upinzani cha Labour, Joanne ‘Jo’ Cox aliuawa Alhamisi iliyopita, kwa kupigwa risasi na kuchomwa kisu.



Tayari mtu mmoja amekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya mauaji. Wakati mtu huyo akifanya unyama huo, alisikika akisema ‘Britain first!’ (Uingereza kwanza), pengine kuonyesha upinzani wake dhidi ya mbunge huyo ambaye alikuwa mstari wa mbele kuwasaidia ‘wanyonge’ sehemu mbalimbali duniani na hapa Uingereza.



Licha ya kauli hiyo ya muuaji huyo kuwa jina la chama cha kibaguzi cha Britain First, uchunguzi wa awali wa polisi umegundua nyaraka kadhaa zinazoashiria mawasiliano kati ya mtu huyo na vikundi vyenye mrengo mkali wa kulia, vya kibaguzi.



Kadhalika, kabla ya kukutwa na mauti, mbunge huyo alikuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi wapige kura ya hapana, kupinga wazo la Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya.
Ni muhimu kuelezea katika hatua hii kwamba iwapo kambi inayotaka Uingereza ibaki kwenye umoja huo wa Ulaya itashinda, basi tukio hilo la kusikitisha la mauaji ya mbunge huyo, aliyekuwa akiunga mkono nchi hii isijitoe, linaweza kuwa limechangia kwa namna fulani.



Huu ni mtizamo wangu binafsi, kwamba kwa namna fulani tukio hilo linaweza kuwaogopesha baadhi ya wapigakura kuwa Uingereza nje ya Umoja wa Ulaya yaweza kutawaliwa na siasa za mrengo mkali au za kibaguzi, hasa ikizingatiwa kuwa vikundi vya aina hiyo vinaunga mkono nchi hii kujitoa kwenye umoja huo.



Kabla ya mauaji hayo, kura za maoni zilikuwa zinaonyesha kambi inayotaka Uingereza ijitoe ilikuwa ikiongoza kwa takriban asilimia tano. Hata hivyo, kura kadhaa za maoni zilizotolewa juzi, zikiwa ni za kwanza baada ya kifo cha mbunge huyo, zinaonyesha kambi inayotaka Uingereza ibaki kwenye Umoja wa Ulaya ikiongoza kwa asilimia chache kidogo. Hii ni mara ya kwanza kwa siku za hivi karibuni kwa kambi hiyo kuongoza katika kura hizo za maoni.



Laiti ningeandika makala hii miezi michache tu iliyopita, basi wala nisingepata shida kubashiri kuwa Uingereza ingeendelea kubaki mwanachama wa Umoja huo. Awali, ilionekana kuwa kambi ya wanaotaka Uingereza ijitoe ilikuwa haina hoja za msingi zaidi ya kulalamika kuwa umoja huo unaikandamiza nchi hii, sambamba na kudai kuwa mamlaka ya utawala katika taifa hili kubwa duniani imeporwa na umoja huo.



Moja ya masuala muhimu kuhusu hoja nzima ya kujitoa au kubaki kwenye umoja huo ni pamoja na suala la uhamiaji na wahamiaji. Siku zote suala hili limekuwa nyeti sana kisiasa. Wapinzani wa uanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya wanadai kuwa nchi hii imekuwa ikibanwa na sheria za umoja huo hususan katika masuala ya uhamiaji na wahamiaji. Sheria zilizopo zinaruhusu ‘uhuru wa matembezi’ (freedom of movement) kutoka nchi moja kwenda nyingine kwa wakazi wa nchi wanachama, kitu ambacho wapinzani wanadai kinachochea uhamiaji haramu.



Kadhalika, baadhi ya wahamiaji haramu waliotaka kufukuzwa Uingereza waliweza kukwamisha uamuzi huo kwa kukata rufaa kwenye Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya.



Vile vile, sheria za umoja huo zinatoa ruhusa kwa wahamiaji kutoka nchi zilizo ndani ya umoja huo kupata haki mbalimbali kama vile huduma za bure za afya, fedha za kujikimu na za makazi zinazotolewa kwa watu wasio na kazi au wenye kipato duni.



Pia, kama mwanachama wa umoja huo, Uingereza imekuwa ikilipa mamilioni ya pauni kila wiki kama mchango wake kwa umoja huo, suala ambalo wanaotaka nchi hii ijitoe wamekuwa wakililamikia mno, wakidai linaathiri uwezo wa nchi hii kuhudumia wananchi wake kwa ufanisi.



Kwa upande mwingine, hoja kuu ya upande unaotaka Uingereza ibaki kwenye Umoja wa Ulaya ni uchumi. Na kambi hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupata watetezi mbalimbali, kuanzia Rais Barack Obama wa Marekani, Kansela Angela Markel wa Ujerumani hadi taasisi kama Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia.



Hoja kuu ni kwamba laiti Uingereza ikijitoa kwenye umoja huo, uchumi wake utaathirika vibaya. Na pengine katika kile kinachoweza kuwa kinaashiria ukweli wa tishio hilo, thamani ya sarafu ya nchi hii – Pauni ya Kiingereza – imejikuta ikishuka thamani kulinganisha na Dola ya Marekani. Hata gavana wa benki kuu ya hapa, ambaye haruhusiwi kujihusisha na siasa, ameonya kuwa uchumi wa nchi hii utayumba iwapo itajitoa kwenye umoja huo.



Kambi ya wanaotaka Uingereza ibaki kwenye umoja huo imepata nguvu pia kutoka kwa taasisi mbalimbali za kibiashara na uchumi ndani na nje ya nchi hii, sambamba na uungwaji mkono kutoka kwa wakuu wa zamani wa taasisi za kiintelijensia za MI5 (idara ya ushushushu wa ndani ya nchi) na MI6 (idara ya ushushushu wa nje ya nchi, yaani ujasusi). Mashushushu hao wastaafu wametahadharisha kuwa kwa Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya itahatarisha ushirikiano uliopo dhidi ya matishio ya kiusalama kwa nchi wanachama wa umoja huo.



Ni vigumu kueleza kwa hakika ni suala gani lililoweza kubadili mwelekeo wa kampeni ambapo awali ilionekana kama wazo tu la Uingereza kujitoa kwenye umoja huo ni kama mzaha. Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaeleza kuwa kosa la kambi inayotaka nchi hii isijitoe ni kutegemea zaidi vitisho kutoka kwa wataalamu mbalimbali.



Mbinu hiyo, inayoelezwa kwa kimombo kama “fear factor” ilikuwa na ufanisi mkubwa katika kura iliyopigwa hapa Uskochi mwaka juzi kuamua kama taifa hili lijitoe katika muungano wa Uingereza au liendelee kuwemo. Kwa kutumia wataalamu mbalimbali hususan wa uchumi, serikali kuu chini ya Waziri Mkuu David Cameron ilifanikiwa kuwatisha Waskochi kuhusu hatma yao nje ya muungano wa Uingereza.



Kwa kifupi, ilikuwa ni hadithi ya zimwi likujualo, kwamba angalau Waskochi wanafahamu mazuri na mabaya ya muungano wa Uingereza na wanaweza kuenzi mazuri hayo na kuyarekebisha mabaya, kinyume na kuchukua uamuzi wa kujitoa ambao faida na hasara zake zilikuwa kama za kufikirika (kwa maana kwamba ni kitu ambacho kilikuwa bado hakijatokea).



Ni hivi, hata kwenye chaguzi za huko nyumbani (Tanzania), moja ya turufu ya chama tawala CCM huwa kwenye hoja ya angalau mnafahamu mazuri na mabaya ya CCM. Je, mnataka kufanya majaribio na vyama vya upinzani? Itakuwaje iwapo majaribio hayo yatakwenda kombo?



Hoja hiyo pia inatumiwa na kundi linalotaka Uingereza ibaki kwenye Umoja wa Ulaya lakini tofauti na ilivyokuwa kwenye kura ya uhuru wa Uskochi, safari hii hoja hiyo imekumbana na hoja mbadala kama sisi ni Waingereza, tumemudu mambo mengi katika historia ya taifa letu. Tukiwa nje ya Umoja wa Ulaya tutamudu kusimama wenyewe.



Kwa kuwategemea sana wataalamu na taasisi mbalimbali kuonyesha madhara ya nchi hii kujitoa kwenye umoja huo, kambi inayofahamika kama Remain (kubaki) imejikuta kwenye wakati mgumu pale inapotuhumiwa kuwa hao wataalamu wenyewe sio watu wanaoishi maisha ya kawaida. Yaani ni kama vigogo ambao hawaathiriwi na adha wanazokumbana nazo wananchi wa kawaida kutokana na Uingereza kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.
Kwa siasa za wenzetu huku, serikali au wanasiasa kuwa karibu na watu – wenyewe wanaita kuongea lugha ya mtu wa kawaida – ni turufu muhimu. Na huo umekuwa mtaji muhimu wa watu kama Boris Johnson, Meya wa zamani wa Jiji la London, ambaye ni mmoja wa viongozi wa kambi inayotaka nchi hii ijitoe kwenye umoja huo, inayofahamika kwa kifupi kama Leave (Ondoka).



Mwanasiasa huyo machachari na mwenye uwezo mkubwa wa kujieleza amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuongea “lugha ya watu wa kawaida” kueleza kwa nini nchi hii itakuwa bora zaidi nje ya Umoja wa Ulaya.



Upinzani mwingine dhidi ya Umoja huo ni tishio la mpango wa umoja huo kuiingiza Uturuki kuwa mwanachama. Licha ya kuwa nchi ya Ulaya, Uturuki inaangaliwa kama taifa la Kiislamu, wapinzani wa uanachama wa Uingereza kwenye umoja huo wanadai kuwa huko mbele Uturuki itaruhusiwa kuwa mwanachama, na hali hiyo itatishia usalama wa nchi hii. Ukweli mchungu tunaoishi nao hapa ni mtizamo wa kibaguzi wa kuhusisha Uislamu na ugaidi.



Kichekesho cha suala lote hili la Uingereza kubaki au kujitoa katika Umoja wa Ulaya ni kwamba Waziri Mkuu Cameron alitumia hoja ya kura hii kuomba ridhaa kwenye uchaguzi mkuu uliopita. Aliahidi kuwa chama chake cha wahafidhina (Conservatives) kikishinda, kitaitisha kura hii ili wananchi waamue kama wanataka kubaki kwenye umoja huo au la. Kwa wakati huo, hoja hiyo ilimsaidia sana Cameron na chama chake kushinda katika uchaguzi huo.



Je, nini kitatokea iwapo Waingereza wataamua kubaki kwenye umoja huo? Hadi muda huu, nchi hii tayari imepewa hadhi maalumu kwenye maeneo mbalimbali ya umoja huo. Kwa hiyo, iwapo kambi ya Remain inayoongozwa na Waziri Mkuu Cameron, akiungwa mkono na kiongozi mkuu wa chama cha upinzani cha Labour, Jeremy Corbyn, itashinda, hakutakuwa na mabadiliko makubwa katika uanachama wa nchi hii kwa sababu tayari imekwishapatiwa hadhi maalumu kwenye umoja huo.



Je, nini kitatokea iwapo Uingereza itajitoa kwenye Umoja huo? Kwa kimombo wanasema “that’s a million-dollar question” (hilo ni swali la dola milioni moja). Kimsingi, hakuna anayejua kwa hakika hali itakuwaje. Hata hivyo, kuna kitu kama mwafaka miongoni mwa wataalamu wa uchumi wa dunia kwamba kwa nchi hii kujitoa kwenye umoja huo, uchumi wake utayumba. Hoja hiyo inapangwa na kambi ya Leave kwa kubainisha ‘hesabu’ zao mbalimbali, kubwa ikiwa mchango wa Uingereza kwenye umoja huo, ambapo kambi hiyo inadai kuwa fedha hizo zikitumika nchini hapa zitafidia pengo lolote litakalojitokeza.



Kadhalika, kambi hiyo ya Leave inadai kuwa hata kama nchi hii itatakiwa kujiunga upya na mikataba mbalimbali ya kimataifa, ukweli kwamba taifa hili ni kubwa na lenye mvuto kwa nchi nyingine, basi hawaoni uwezekano wa nchi hii kususiwa.



Moja ya madhara yanayoweza kujitokeza iwapo Uingereza itajitoa kwenye Umoja wa Ulaya ni kile kinachofahamika kama ‘domino effect,’ yaani kama kwenye mchezo wa goroli au ‘pool’, ukiipiga moja inaipiga nyingine, nayo inaipiga nyingine, na kadhalika. Kwamba, iwapo Uingereza ikijitoa, baadhi ya nchi wanachama wa umoja huo nazo zinaweza kuitisha kura za kujadili uanachama wao, suala linaloweza kusababisha kuvunjika kwa umoja huo muhimu.



Tishio jingine kubwa linahusu muungano wa Uingereza. Nchi hii inaundwa na muungano wa mataifa manne, ambayo ni England, Wales, Uskochi na Ireland ya Kaskazini (Jina kamili la nchi hii ni The United Kingdom of Great Britain – yaani England, Wales na Uskochi – and Northern Ireland). Tayari chama tawala cha hapa Uskochi, SNP (Scottish National Party), ambacho huko nyuma ndicho kilipigania kura ya uhuru wa Uskochi, kimekwishatamka kuwa kama Uingereza itajitoa kwenye Umoja wa Ulaya, basi nacho kitaitisha kura nyingine ya kudai uhuru.



Ningetamani mno kuhitimisha makala hii kwa kujifunga na kutabiri matokeo ya kura hiyo hapo kesho (Juni 23, 2016) lakini ninachelea kufanya hivyo kwa sababu, kwanza kura za maoni zinaonyesha kambi zote mbili zina nafasi zinazokaribiana kitakwimu, lakini pili, kura za maoni katika uchaguzi mkuu uliopita nchini hapa zilitoa mshangao mkubwa baada ya matokeo ya uchaguzi huo kuwa kinyume kabisa na takriban kura zote za maoni. Wajuzi wanasema kura za maoni sio “exact science” (sayansi ya uhakika kabisa).’



Ninachoweza kuahidi katika hitimisho la makala hii ni kuzungumzia zaidi kuhusu Uingereza kabla na baada ya kura hiyo katika makala ijayo.

23 Jun 2016


Leo tarehe 23.06.2016 Uingereza itapiga kura ya maoni kuamua kuhusu hatma ya uanachama wake katika Umoja wa Ulaya (EU). Jana, nilipata fursa ya kushiriki katika mjadala mkali katika kipindi cha Dira ya Dunia cha Idhaa ya Kiswahili ya BBC Radio.

Sikiliza kwenye audio hapo chini mjadala huo (unaojiri baada ya taarifa ya habari). Karibuni


 
Check this out on Chirbit

22 Jun 2016


Mini-supermarket ya aina yake, The Farm Fresh Market, inafunguliwa leo jijini Dar es Salaam saa sita mchana kwa saa za Tanzania. Mini-supermarket hiyo ni ya kwanza na ya kipekee nchini Tanzania kuuza vyakula, mbogamboga, matunda na bidhaa kama hizo zikiwa fresh kuoka shambani na zote zikizalishwa nchini mwetu.

Mini-supermarket hiyo ipo eneo la VICTORIA mkabala na MERRY WATER inaangaliana na Barabara ya ALI HASSAN MWINYI.

Bidhaa zinazopatikana katika mini-supermarket hiyo zinatoka sehemu mbalimbali nchini Tanzania ambapo mbogamboga zinaletwa moja kwa moja kutoka kwa wakulima wa Arusha na Lushoto, viungo (spices) kutoka Zanzibar, ilhali matunda mbalimbali, nazi, mayai, kuku, nk vikitoka katika mashamba na vitalu vilivyopo jijini Dar.

Kadhalika, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, mini-supermarket hiyo itakuwa na 'baa' maalum (sio ya kuuza kilevi) kwa ajili ya 'smoothies', yaani juisi ya matunda halisi iliyotengenezwa kiasili pasi kuchanganya kemikali. 

Kana kwamba hiyo haitoshi, mini-supermarket hiyo ya kwanza ya aina yake nchini Tanzania itakuwa pia na sehemu ya ushauri wa tiba ya kisasa kwa kutumia vyakula au matunda. Yaani, vyakula na matunda mbalimbali ni tiba ya maradhi mbalimbali, na mini-supermarket hiyo itatoa ushauri kwa wateja kuhusu aina hiyo ya tiba ambayo ina umaarufu mkubwa kwa nchi zilizoendelea hasa kwa vile nyingi ya tiba za hospitali huambatana na kemikali fulani zinazoweza kuwa na athari kidogo kwa mwili. 



Huduma ya kufikishiwa bidhaa nyumbani au ofisini (delivery) inapatikana kwa gharama nafuu

Mazingira safi ya kiwango cha juu yaliyothibitishwa na Mamlaka ya Vyakula na Madawa Tanzania (TFDA)

Baa ambayo si ya kilevi bali smoothies (juisi asilia isiyo na kemikali)

Vitafunwa vinavyotengenezwa kwa spinachi, karoti, ufuta, nk

Vyakula, mbogamboga, matunda ,nk katika mafriji maalum yanayohakikisha virutubisho vinabaki inavyostahili kuwa kama shambani au ardhini...yaani unakula kitu asilia haswa.

Vitafunwa vya kisasa ambavyo licha ya kuhakikisha ladha na shibe kwa mteja vinaweka kipaumbele kwa virutubisho vinavyotumika vyenye manufaa kwa afya ya mlaji

Kila mahitaji ya mlo na afya ya mteja yanapatikana katika mini-supermarket hiyo ya aina yake nchini Tanzania

Viungo (spices) mbalimbali ambavyo ni fedha kutoka Zanzibar

17 Jun 2016


Wanaofuatilia vema siasa za Tanzania watakumbuka vizuri enzi za ‘ugaidi’ wa Chadema. Kwa bahati mbaya, mmoja wa makada wa CCM ‘walioshikilia bango’ tuhuma hizo za ugaidi alikuwa Mwigulu Nchemba, ambaye kwa sasa ndiye Waziri wa Mambo ya Ndani. 



Pengine ni kutokana na hali hiyo, inawezekana kujitokeza hisia, miongoni mwa wafuasi wa vyama vya upinzani kuwa “wasiyempenda kaja.”


Kwa kuzingatia historia yake huko nyuma, Mwigulu kama waziri mwenye mamlaka ya utendaji katika Jeshi la Polisi anaweza kutumia fursa hiyo kudhibiti vilivyo vyama vya upinzani na kibaya zaidi, uteuzi wake umekuja katika wakati ambao uhusiano kati ya Serikali ya Rais Magufuli na CCM, kwa upande mmoja, na wapinzani kwa upande mwingine, si mzuri.

Katika makala yangu ya wiki iliyopita niliyataja makundi mawili yanayofanya kila jitihada kustawisha siasa za mfarakano, ambayo ni kundi la viongozi wa vyama vya siasa na baadhi ya wafuasi wa vyama hivyo.

Kwa mfano, uamuzi wa Bunge kuwafungua baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani ni dhahiri uamuzi huo utaathiri wananchi na si wabunge wanaowawakilisha. Kwa nini busara haikutumika hapa angalau kuwaonya wabunge hawa?

Baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani na kulifanya suala la vita dhidi ya ufisadi kuwa ajenda yake kuu, kulianza kujitokeza hisia kuwa upinzani utadhoofika kwa sababu suala hilo ndilo limekuwa turufu yao kuu. Sasa sijui ni kitu gani kimetokea, ghafla inaonekana kama CCM inawatafutia wapinzani hoja. Na hoja inayoonekana sasa ni kama kuna unyanyasaji dhidi ya vyama vya upinzani.

Kuanzia suala kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge na baadaye kupiga marufuku maandamano na mikutano ya siasa ya vyama vya upinzani ni mambo yaliyochangia kubadili hali ya awali ya wapinzani kukosa ajenda.

Tumeona Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akikamatwa lakini pia Kiongozi Mkuu wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe, naye akihojiwa polisi kwa madai kuwa ametoa hotuba ya kumkashifu Rais Magufuli. 


Na wakati nikijiandaa kuandika makala hii, sio tu kuwa kongamano la chama hicho kujadili bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 lilizuiliwa na Jeshi la Polisi lakini pia polisi wanaendelea kumfuatilia Zitto. Kwa lipi hasa?


Sina hakika kama ni uamuzi wa Rais Magufuli au kuna watu wanaojaribu kumkosanisha na vyama vya upinzani, lakini lililo wazi ni kwamba CCM inawapatia wapinzani hoja za kuibuka kisiasa.

Tukirejea kuhusu Mwigulu, ni muhimu kutambua kuwa hapa katikati ‘amebadilika’ kwa kiasi kikubwa. Ukimlinganisha Mwigulu ‘mrusha’ tuhuma za ugaidi na Mwigulu ‘mwomba’ ridhaa ya urais kwa tiketi ya CCM ni kama kuzungumzia watu wawili tofauti. Wakati yule wa mwanzo alikuwa akiendeshwa kwa mihemko ya kiitikadi na ukada, huyo mpya aliweka mbele maslahi ya taifa.

Wanaomfahamu vema wanadai kuwa ni mchapakazi hasa. Na ni katika hilo, majuzi nilimrushia pongezi na kumweleza matumaini kuwa sasa tumepata mtu anayeweza kumudu tatizo sugu la biashara ya dawa za kulevya. Ni wazi kuwa Mwigulu anaweza kujitengenezea mazingira mazuri ya kisiasa huko mbele (bado kijana na anaweza kuwania tena urais) iwapo atachapa kazi kwa kuwa mtumishi wa Watanzania wote na kutorejea zama za kuwazushia tuhuma za ugaidi wapinzani.

Nimalizie makala hii kwa kutoa rai kwa Rais Magufuli kuwa Watanzania wengi wanaridhishwa na jitihada zake za kuwatumikia kwa dhati huku akichukia kwa dhati ufisadi. Kadhalika, Watanzania wamechoshwa na siasa za uhasama ambazo zinawaathiri zaidi wananchi kuliko vyama vya siasa au viongozi wao. 


Tukusanye nguvu zetu, wananchi na viongozi wa vyama vya siasa, tujenge Tanzania ya neema na tunayostahili kuwa nayo. Tuna mengi ya kunufaika nayo katika umoja na ushirikiano wetu kuliko kuendekeza siasa za visasi, uhasama na uadui.

11 Jun 2016

NI takriban miezi minane sasa tangu Tanzania ilipofanya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, Oktoba 25, 2015. Uchaguzi huo ndio uliotupatia Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli. Ni vema nikatanabaisha mapema kuwa, kwa kutumia haki yangu ya kidemokrasia, ‘nilimpigia debe’ mgombea huyo wa chama tawala, CCM. Na hadi muda huu, sijajilaumu kuchukua uamuzi huo.

Hata hivyo, kwa upande wangu – na pengine kwa watu wengine wengi tu – baada ya uchaguzi huo kumalizika na hatimaye kupata serikali ya awamu mpya, masuala ya kampeni nayo yalihitimishwa. Zile tofauti tulizokuwa nazo wakati huo, za “Magufuli anafaa, Lowassa (aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema) hafai” au “Lowassa anafaa, Magufuli hafai” zimebaki kuwa historia. Tumekwishapata rais, sio wa CCM pekee, sio wa waliompigia kampeni na kura pekee, bali ni rais wa Watanzania wote.


Lakini kuna baadhi ya wenzetu, wengi tu, bado wapo katika kile tunachoweza kukiita mkao wa kikampeni (campaign mode) au kwa tafsiri isiyo rasmi). Kuna makundi makuu mawili: wanasiasa na wafuasi wa kambi kuu mbili katika uchaguzi huo, yaani CCM na Ukawa. Katika kundi la kwanza, kuna wanasiasa ambao kwa kiasi kikubwa wanaonekana kutamani kampeni za uchaguzi ziendelee. Hawa wanajitambulisha kwa lugha na matendo yao ambayo yameelemea kwenye kuzidisha uhasama wa kisiasa kuliko mwafaka wa kitaifa.


Na kama kuna sehemu nzuri ya kubaini hilo ni huko bungeni ambapo masuala mbalimbali ya maslahi ya taifa yanaonekana ya kipuuzi kwa sababu tu ya uhasama huo wa kisiasa. Wabunge wa CCM wenye nia ya kufanya kazi na wenzao wa Ukawa kwa ajili ya taifa letu wanakwazwa na hofu ya kuonekana wasaliti kwa chama chao. Na huenda hali ni hiyo kwa wale wa upinzani.


Kundi la pili ni la wafuasi wa kambi hizo, yaani CCM na Ukawa. Wakati upinzani baina yao unaokera, na kwa hakika unakwaza mijadala muhimu kuliko mustakabali wa taifa letu, kinachoudhi zaidi ni kasumba inayojitokeza ndani ya makundi hayo, ambapo wana-CCM wanaodhani kuna haja ya kukikosoa chama chao au Magufuli wanaonekana ni ‘mbwa mwitu kwenye ngozi ya kondoo,’ wasaliti. Hali ni hivyo hivyo kwa wana-Ukawa. Ukimkosoa Lowassa basi wewe ni kibaraka wa CCM.


Majuzi, nilikumbana na mkasa baada ya kukosoa uamuzi wa serikali kuwafukuza wanafunzi wa stashahada maalumu ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Mtu mmoja ‘alinivaa’ na kunilaumu kuwa ninashindwa kutumia uandishi wangu kumtetea Rais Magufuli. Ni baada ya kumwonyesha makala mbalimbali nilizoandika huko nyuma ‘kumnadi’ Magufuli na ‘kumtetea’ baada ya kuwa rais, sambamba na kitabu nilichoandika kuhusu urais wake, ndipo akadiriki kunitaka radhi. Huyu ni mmoja kati ya wengi wasiotaka kusikia lolote zaidi ya pongezi kwa vyama au viongozi wao.


Nimeanza makala hii kwa kuelezea suala hilo kwa sababu sio tu linakwaza mijadala muhimu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu taifa letu lakini pia linaweza kuathiri dhamira nzuri ya Rais Magufuli kulitumikia taifa letu. Yeye mwenyewe alituomba tumsaidie katika uongozi wake na moja ya njia za kumsaidia mtu ni kumkosoa pale anapokosea.


Na bila kuuma maneno, na licha ya mimi binafsi kuwa ‘shabiki wa Magufuli,’ jinsi alivyoshughulikia suala la wanafunzi waliofukuzwa UDOM sio sawia. 

Kwanza, kilicholalamikiwa na wengi kuhusu hatua ya serikali kuwafukuza wanafunzi hao sio kwamba walistahili kuendelea na kozi hiyo au la bali namna walivyofukuzwa bila chembe ya ubinadamu. Na angalau basi wangekuwa wamefanya kosa fulani. Hawakuwa na kosa lolote kwa sababu hawakujidahili wenyewe wala kujiundia kozi hiyo au kujiunga wenyewe bila kuitwa chuoni.

Baadhi ya wanafunzi hao waliojitoa mhanga, wakaacha kwenda kidato cha tano huku alama walizopata zikiwaruhusu kuchaguliwa na kujiunga na kozi hiyo. Hawa sio ‘vilaza’ hata kidogo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mbunge kutoka Chama cha ACT, Zitto Kabwe, ni wanafunzi 88 tu ambao sifa zao zina mushkeli kuendelea na kozi hiyo. Hivi kulikuwa na ugumu gani wa kuchuja waliostahili kuendelea na kawaondoa hao wenye upungufu wa sifa stahili? Kilichokosekana ni busara tu.


Kwa heshima na taadhima, ninaomba pia kutoafikiana na kauli ya Rais Magufuli kuhusu vilaza. Hivi kweli tumesahau jinsi mpango kama huo wa stashahada maalumu ya ualimu, enzi hizo ukiitwa UPE (Universal Primary Education), ambao licha ya matatizo kama hayo ya stashahada ya Chuo Kikuu cha Dodoma, ulivyoweza kuiweka Tanzania yetu katika ramani ya kimataifa kwa mafanikio makubwa ya kielimu?


Sawa, kulikuwa na kasoro katika mpango huo wa stashahada maalumu ya ualimu, lakini mtoto hazaliwi akitambaa, kwa maana ya kwamba kila mwanzo ni mgumu. Kwa hiyo, kwa kutumia uzoefu wa UPE – kwa mfano vitu gani vilisababisha ‘kifo’ chake – tungeweza kabisa kuboresha stashahada hiyo maalumu ili itusaidie kukabili uhaba mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi, ambapo kwa mujibu wa takwimu za Zitto, ni walimu zaidi ya 20,000.


Kauli za Rais Magufuli zinakinzana na waziri wake Profesa Joyce Ndalichako. Lakini hilo sio muhimu kwa sasa. Wenye uelewa tunafahamu kwamba kuna makosa yamefanyika. Na badala ya kuendelea kunyoosheana vidole, ni vema serikali ikafanya utaratibu wa haraka wa kurekebisha kasoro hiyo. Sitarajii wanafunzi hao kuombwa msamaha wala kusikia hotuba ya kiongozi kukiri kwamba ushughulikiaji wa suala hilo haukuwa sahihi. La muhimu sio kuombana msamaha bali kurekebisha kosa husika.


Nimalizie makala hii kwa kuwasihi Watanzania wenzangu kwamba tuna mengi ya kunufaika kwa kuwa wamoja kuliko kuruhusu tofauti za kiitikadi au upinzani wa kisiasa au kimtazamo kututenganisha. Ifike mahala tuweke kando siasa kwenye masuala yanayohitaji busara au utaalamu.


Pamoja na kasoro kadhaa zilizojitokeza katika Awamu ya Nne, wazo hili la stashahada maalumu ya ualimu lilipaswa kuwa moja ya alama muhimu kiuongozi (legacies) za Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Nia yake ilikuwa nzuri, na kwa vile miongoni mwa walioridhia sera hiyo ni pamoja na Rais Magufuli (wakati huo akiwa mbunge na waziri), basi hakuna haja ya ‘kuwatesa’ vijana hao wazalendo ambao kufanikiwa kwao katika kozi hiyo kungesaidia kupunguza uhaba wa walimu ya masomo ya sayansi. 

Nihitimishe kwa msemo kwamba, kukosea ni ubinadamu lakini kujirekebisha ni utukufu (To err is human but to correct is greatness)



Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.