6 Oct 2010



Chanzo: Wandima









Tukiwa tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu Tanzania ambao utafanyika October 31, 2010, Watanzania wazalendo wanachama na wapenzi wa Chadema mnaombwa kuchangia kwa dhati harakati za Chadema ili tuweze kuwafikia Wananchi wengi zaidi katika kila kona ya Tanzania tukitafuta ridhaa yenu ya kuweza kujenga nchi yetu; nchi yenye usawa, uzalendo, maadili na uwajibikaji katika miaka mitano ijayo.

CHANGIA CHADEMA KUPITIA BANK:
CRDB BANK
CHADEMA - M4C
Account Number: 0J1080100600

National Microfinance Bank [NMB]
CHADEMA
Account Number: 2266600140

Unaweza kuweka pesa kupitia tawi lolote la Benki hizi Tanzania.


CHANGIA CHADEMA KUPITIA SMS (MESEJI):
Tuma neno:

"CHADEMA" kwenda namba 15710
"NAJIUNGA" kwenda namba 15710
"SLAA" kwenda namba 15710

Unaweza kutuma meseji mara nyingi kadri unavyoweza na kila ujumbe utagharimu TZS 350/= tu.
HII NI KWA MITANDAO YA ZAIN, TIGO NA VODACOM TU.

CHANGIA KUPITIA M-PESA:
Kwa watakaotaka kuchangia kwa M-Pesa wanaweza kutumia namba zifuatazo:

0758 223 344
0764 776 673


CHANGIA KUPITIA ZAP:
Kwa watakaotaka kuchangia kwa ZAP wanaweza kutumia namba hii:

0789 555 333

"Ndugu Zangu Watanzania, tunawaomba kwa dhati kabisa tushikamane, tushirikiane bila kujali itikadi zetu kuchangia harakati hizi, tunawashukuru sana. - Dr. Wilbroad Peter Slaa"

CHAGUA MABADILIKO YA KWELI. CHAGUA CHADEMA.









Kwa hisani ya SUBI

4 Oct 2010

France


France


Sweden


Germany

Add caption


3 Oct 2010




Blogu hii inapenda kutoa salamu za pongezi kwa mpambanaji na mwanaharakati mahiri,Mwalimu Nkwazi Mhango (a.k.a Mpayukaji Msemaovyo) mwenye makazi yake nchini Kanada kwa kutuletea mpambanaji mwingine wa kiume.Ujio wa mwanaharakati huyu mchanga unaweza kuwa dalili njema hasa kwa vile tupo kwenye mchakato wa kuwatimua mafisadi wanaofakamia keki ya taifa letu kama hawana akili nzuri.

Naungana na Mwalimu Nkwazi na familia yake kumtakia kijana wetu afya njema na kila mafanikio ili pindi muda utapowadia ajumuike nasi katika harakati zetu za kupigania usawa katika jamii.

1 Oct 2010

"Ufisadi Oyeee.Tupeni tena miaka mitano tuwakwangue kabisa".Of course ni unatarajia nini hapo?

Mgombea wa CCM,Jakaya Kikwete akiendelea na ngwe ya kuwatetea rafiki zake.Alianza na Lowassa,akaenda kwa Mramba,kisha kwa Mzee wa Vijisenti Chenge,na sasa kwa "baba lao" Rostam Aziz.Ama kweli Tanzania bila ufisadi inawezekana!

Wakati "ndege wenye manyoya yanayofanana wakiruka pamoja",Dokta Slaa anaendelea na darasa la kuwahamasisha wenye uchungu na nchi yao kufanya kila liwezekanalo kuwang'oa "ndege hao"


Wananchi mjini Songea wakimsikiliza Rais Mtarajiwa kwa makini
Picha zote kwa hisani ya Jamii Forums

30 Sept 2010

UTITIRI WA AHADI ZA KIKWETE NI KAMA UTAMU WA PIPI HIZO ANAZOMPATIA MTOTO HUYO PICHANI.PIPI NI TAMU KADRI INAVYOYEYUKA MDOMONI LAKINI SIO TU HAIDUMU BALI HAIONDOI NJAA.

Hebu soma kwanza nukuu hii hapa chini kisha utaelewa kwanini nimeweka kichwa cha habari hicho hapo juu

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amesema moja ya kazi kubwa itakayofanywa na serikali yake katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni kumsaidia mkulima wa Tanzania aweze kulima kwa kutumia trekta badala ya jembe la mkono.
Rais Kikwete aliyasema hayo alipokuwa akiwahutubia wakazi wa kata ya Lyabukande, jimbo la Solwa wilayani Shinyanga katika moja ya mikutano yake ya kampeni iliyofanyika jana.
“Katika miaka mitano ijayo iwapo mtatupa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi hii, tumepanga kumsaidia mkulima ili aweze kuboresha kilimo chake kwa kumwezesha kulima kwa trekta badala ya jembe la mkono alilolizoea enzi na enzi,” alieleza Rais Kikwete.
Alisema iwapo mkulima atasaidiwa katika kilimo chake, ataweza kujikomboa kutokana na umasikini na kumuwezesha kuwa na maisha bora kama ambavyo sera ya CCM inavyoelekeza.
CHANZO: Majira

Sio siri,inaudhi,inakera na inachukiza.Hivi huyu Jakaya Kikwete siye aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 2005 hadi leo hii?Ofkozi,jibu ni ndiyo.Sasa hizi habari za kusema atamsaidia mkulima kuondokana na jembe la mkono kwanini ziwe leo na sio mwaka 2005 au 2006 au 2007 au 2008 au 2009 au hata mapema mwaka huu?



Kwa kweli kama kuna Watanzania bado wanajishauri kuhusu wampigie au wamnyime kura Kikwete basi utitiri wa ahadi anazoendelea kutoa,huku nyingi zikiwa ni marejeo ya alizotoa wakati wa kampeni zake za mwaka 2005 ni sababu moja kati ya maelfu ya sababu ya kustaafisha urais kwa kumyima kura.Tena huyu hapaswi kushindwa kwa tofauti ya kura chache bali stahili yake ni kile kiitwacho anguko la pua.

Hakuna maelezo mengine zaidi ya kuamini kuwa Kikwete anawafanya Watanzania ni wapumbavu maana vinginevyo asingediriki kuongea upuuzi kama huu wa kuahidi kuwakomboa wakulima eti akipewa miaka mingine mitano ilhali hii anayomaliza ameitumia zaidi kuzurura huko nje ya nchi.Na kwa angalizo tu,huyu mtu amezowea sana kusafiri,sasa kwa vile amelazimika kukaa nchini kwa zaidi ya miezi miwili sasa basi wapiga kura mkirogwa tu kumrejesha atafanya utalii wake kwa hasira,perhaps on weekly basis badala ya monthly basis kama tulivyozowea.

Badala ya kuwaomba msamaha wakulima kwa kuwapuuza kwa muda wote aliokuwa madarakani yeye anakuja na hadithi mpya kuwa anadhamiria kuwatoa kwenye kilimo cha jembe la mkono.Hayo matrekta hewa yatanunuliwa kwa fedha zipi ilhali priority ya serikali yake ni ununuzi wa magari ya kifahari na samani za bei mbaya kwa watawala?

Na wakulima wakishapatiwa matrekta,je ziada ya mazao yao itauzwa wapi ilhali vyama vya ushirika vimeendelea kuwa taasisi maalum za kuwafisadi wakulima?Kama kweli alikuwa na nia ya kuona mkulima anaondokana na jembe la mkono kwanini basi zile fedha "zilizorejeshwa" na mafisadi wa EPA hazikutumiwa kwa dhamira hiyo?Lakini kwa kuonyesha kuwa anawazuga tu wakulima,alipotangaza "stimulus package" ya kisanii,waliopewa kipaumbele ni wafanyabiashara huku wakulima wakisahaulika.

Naomba nisiandike zaidi.Kikwete ni mbabaishaji na hana jipya.Haihitaji majini ya Sheikh Yahya kufahamu kuwa ahadi alizokwishatoa hadi sasa zinahitaji awe rais wa maisha ili atekeleze japo nusu ya ahadi hizo.Haiwezekani kutoa ahadi kila kukicha ilhali kuna lundo la ahadi zinazosubiri utekelezaji.

Chonde chonde Watanzania,kumbukeni kuwa kama Kikwete ameweza kufanya masihara katika awamu yake ya kwanza huku akijua fika kuwa mwishoni mwa awamu hiyo angesimama tena majukwaani kuomba ridhaa ya kuchaguliwa tena,pata picha awamu yake ya pili ambapo hatohitaji tena kura itakuwaje!Tafakari maneno haya kwa makini sana kwa sababu pindi mtu huyu akirejea Ikulu basi sote tumeliwa.Kidogo kilichobaki kitakombwa na kukwanguliwa kabisa.Na kwa namna ufisadi ulivyoshamiri katika awamu yake ya kwanza basi yayumkinika kubashiri kuwa pindi akichaguliwa tena (God forbid) basi si ajabu Watanzania kushtukia nchi yetu imeshauzwa na hatuna pa kwenda.

Bahati nzuri,katika uchaguzi wa mwaka huu hatuna tena tatizo lililokuwa likitukwaza hata kufikiria mbadala wa CCM.Zama hizo tulikuwa tunasema "sasa tusipoichagua CCM tukichague chama gani ilhali vyama vyenyewe ni bora ya hiyo CCM".Mwaka huu Mungu amesikiliza kilio chetu na kutupatia ufumbuzi mapemaaa.Tumeletewa Dokta Wilbroad Slaa,mwanasiasa ambaye kwa hakika amejidhihirisha bayana kuwa ana uchungu wa dhati kwa Tanzania na Watanzania.


TANZANIA BILA UFISADI INAWEZEKANA.TANZANIA BILA MAFISADI WANAOLINDWA NA KUPIGIWA KAMPENI NA KIKWETE INAWEZEKANA PIA.MPE KURA YAKO DOKTA SLAA NA MPATIE WABUNGE WA KUTOSHA WA KUUNDA SERIKALI NDOGO YA UFANISI NA YA UKOMBOZI WA MTANZANIA.

29 Sept 2010


CHADEMA: Synovate wahini mahakamani
*Slaa asema wanazo nyaraka za utafiti wao.
*Adai kuna mbinu za 'kuchakachua' matokeo.

Na Tumaini Makene

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeivaa kampuni utafiti ya Synovate kikisisitiza kuwa kina matokeo ya utafiti uliofanywa na kampuni hiyo ya kupata matokeo yaliyotoa ushindi wa asilimia 45 kwa chama hicho na mgombea wake wa urais, Dkt. Willibrod Slaa.

Synovate hivi karibuni ilikanusha habari kuwa haijawahi kufanya utafiti wala kuficha matokeo hayo yaliyodaiwa kuipa CCM na mgombea wake Rais Jakaya Kikwete asilimia 41, huku ikitishia kulishtaki gazeti moja liliwakariri viongozi wa CHADEMA wakieleza utafiti huo.

Akizungumzia matokeo hayo jana, Dkt. Slaa alisema "Synovate wakimbie haraka mahakamani, tunazo document (nyaraka), hata gazeti lililotishiwa kushtakiwa lisiwe na wasiwasi, huu ni wakati wa kuvunja heshima ya Synovate kitaifa na kimataifa.

"Walifanya utafiti na katika swali namba GP 06 waliuliza, 'uchaguzi ukifanyika sasa hivi nani utampigia kura kuwa rais wa Tanzania?' na majina yote yaliweka pale ya wagombea, sasa wanakanusha nini, waende haraka sana mahakamani, vinginevyo credibility (heshima) yao tutaivuruga nchi nzima na kimataifa, alisema huku akionesha nyaraka hizo kwa mbali.

Dkt. Slaa alisema katika nchi nyingine taasisi za maoni zinakuwa huru, hazipendelei chama chochote kile.

Katika hatua nyingine, CHADEMA kimemshutumu serikali ya CCM inanyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kikidai kuwa imepanga kutumia mbinu chafu ili kuhujumu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.

Kimesema kuwa kinazo taarifa za uhakika kuwa kati ya mbinu hizo chafu ambazo zinatumiwa au zinataka kutumiwa na serikali kukibeba Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi wa mwaka huu ni kutoa maelekezo kwa Usalama wa Taifa na kujipanga kuchapisha karatasi bandia za kupigia kura nje ya nchi.

CHADEMA kimesema kuwa njama hizo ni aina ya ufisadi kwa kuwa zinahusisha matumizi mabaya ya madaraka na raslimali za nchi kukisaidia chama kimoja cha siasa-CCM, hivyo hazipaswi kuvumiliwa kwani zina lengo la kuingilia maamuzi ya wapiga kura na kuvuruga amani ya nchi.

Kimesema kuwa iwapo mbinu hizo chafu zitafanikiwa kwa kuharibu uchaguzi na kupanga matokeo ya kuipendelea CCM na mgombea wake wa urais, "Rais Kikwete ndiye atabeba lawama na laana zote juu ya yale yatakayotokea. Usalama wa Taifa wakanushe kama hawajapewa maelekezo na kama sasa hawazunguki mikoani."

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibroad Slaa alipokuwa akizungumza na waandishi ambapo alisisitiza kuwa siku zote chama hicho kimekuwa kikisema kuwa amani ya nchi wakati wa uchaguzi imekuwa ikivurugwa na chama tawala kwa nia ya kutaka kung'ang'ania madaraka, kinyume na maamuzi ya Watanzania.

"Leo tumewaita kuzungumzia juu ya mambo matatu, maamuzi ya Kamati Kuu ya CHADEMA hasa juu ya ubunge wa viti maalumu, uchaguzi mkuu wa mwaka huu na suala la Synovate (kampuni inayojihusisha na kura za maoni ya watu)...juu ya uchaguzi mkuu tunazo taarifa za uhakika kuwa Serikali imetoa instructions (maelekezo) kwa Usalama wa Taifa na sasa wako mikoani wakizunguka nchi nzima, kuhakikisha Kikwete anashinda kwa hali yoyote ile.

"Tunajua mikoa ambayo wamekwisha kwenda mpaka sasa hivi na wanachofanya huko tunakijua...hii ni sawa na ile barua tuliyoikamata hivi karibuni ikiwaelekeza watendaji wa Serikali kuhakikisha CCM inashinda uchaguzi wa mwaka huu kwa hali na mali. Tunatoa angalizo mapema lolote litakalotokea mwaka huu Rais Kikwete atabeba lawama na laana zote za Watanzania.

"Kwa hali wanayoionesha ya kuhangaika mpaka sasa Kikwete ameshashindwa. Ni kigezo tosha kuwa mpaka sasa wameshashindwa uchaguzi. Tunapenda kumwambia kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni uchaguzi wa wananchi, hakuna cha Usalama wa Taifa, hakuna cha JWTZ wala FFU, waache wananchi wafanye maamuzi juu ya nchi yao," alisema Dkt. Slaa.

Dkt. Slaa ambaye pia ni Mgombea urais wa CHADEMA katika uchaguzi wa mwaka huu, lakini jana akitumia kofia yake ya ukatibu mkuu wa chama alisema kuwa wanazo pia taarifa za kina na za uhakika kuwa kuna karatasi za bandia zinachapishwa katika moja ya nchi za nje, ili zije zitumike wakati wa uchaguzi, akidai ni mwendelezo wa mbinu chafu za kuiba kura.

Alisema chama chake na Watanzania wengi wapenda haki hawatakubali mbinu hizo chafu, akisema matumizi mabaya ya madaraka na raslimali za nchi ni aina ya ufisadi ambao CHADEMA kimekuwa kikiupiga vita tangu kilipotangaza orodha ya aibu ya watu mafisadi wapato 11 nchini.

"Wanaonesha dhahiri kuelemewa...sasa wanafanya vitendo vya kuhatarisha amani ya nchi, hawaitakii mema nchi. Tunasema amani ikivunjika Kikwete atabeba lawama, hatuwezi kukubali udikteta na ubabe huu. Kutumia raslimali za serikali na matumizi mabaya ya madaraka ni aina ya ufisadi, ndiyo maana Kikwete tulimweka katika orodha ya mafisadi."

Akiongezea katika suala hilo, Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Bw. Freeman Mbowe alisema kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu ukivurugika, Rais Kikwete, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini watapaswa kuwajibika mbele ya Watanzania.

Bw. Mbowe alisema kuwa kuna vitendo vinavyofanywa na baadhi ya viongozi hao kwa nia ya kubeba ushindi wa CCM vinaiweka matatani dhana nzima ya demokrasia na kuonekana kiini macho, hali ambayo haiwezi kukubalika.

"Tunapenda kutoa tahadhari kwa Rais Kikwete, kwa NEC na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, yaani kwa Makame (Jaji Lewis, Mwenyekiti wa NEC) na Tendwa (John, Msajili), watu hawa watatu ndiyo wenye mamlaka ya umma na wajibu wa kutoa haki, utulivu na amani katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.

"Bahati mbaya sana watu hawa watatu wana mikakati ya kuchakachua kura badala ya kutenda haki, wanaliandaa taifa kuchakachua kura...tunatoa angalizo kwa jamii nzima na jumuiya ya kimataifa demokrasia nchi hii ni kiinimacho. Msajili kwa makusudi anabadilisha na kuvunja sheria iliyotungwa na bunge ili kumsaidia Kikwete, halafu hakuna mtu yeyote anayejali wala kuchukuliwa hatua...huu ni uwendawazimu.

"Jana Shinyanga Kikwete kahutubia mpaka saa 1, karibu kila mahali anazidisha muda...tunataka jamii nzima na jumuiya ya kimataifa ituelewe, hawa watu wameshindwa siasa za hoja, wameshindwa siasa za aina zote za maana sasa wanajiandaa kwa siasa za uchakachuaji...mwaka huu kitaeleweka, hapatatosha pale wananchi watakapoamua kulinda maamuzi na kura zao," alisema Bw. Mbowe.

Aliongeza kuwa chama hicho kitaandaa malalamiko ya kuwayawasilisha kwa NEC na Tendwa juu ya vitendo vya kuzidisha muda.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bw. Salvatory Rweyemamu alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo jana, alisema hizi ni tuhuma za kisiasa na zinamhusu mgombea wa CCM, kwa hiyo aulizwe Meneja wa Kampeni wa chama hicho, Bw. Abdulrahaman Kinana.

Bw. Kinana hakupatikana kwenye simu yake ya mkononi ambayo mara kadhaa ilikuwa ikiita bila kupokewa.

Kuhusu suala la uteuzi wa majina ya wabunge wa viti maalumu wanawake ndani ya CHADEMA, Dkt. Slaa alijigamba kuwa chama chake kimeweka historia nchini kwa kuwa chama cha kwanza kutumia njia ya kisiasa na kisayansi kupata wabunge hao, huku akisema sheria ya uchaguzi inayolazimisha vyama vya siasa kuwasilisha majina hayo siku 30 kabla ya uchaguzi ni chanzo cha zoezi hilo kutofanyika kwa ufanisi mapema, hivyo watairekebisha wakipewa ridhaa ya kuongoza nchi.

"Njia ambayo consultant (mshauri) wetu atawaeleza vizuri imeondoa kabisa yale mawazo ya wabunge kutoka upande mmoja wa nchi, dhana ya mchezo mchafu mtu kumweka girlfriend wake, uswahiba na unafiki mwingine, hii ni kwa sababu CHADEMA tumedhamiria kuchukua dola na tunaenda kuchukua dola. Hivyo ilikuwa lazima tujipange vizuri kupata wabunge kutoka nchi nzima, maana hata katika majimbo tumesimamisha wabunge 185," alisema Dkt. Slaa.

Kwa upande wake mtaalamu mshauri aliyepewa kazi ya kuratibu utaratibu wa kuwapata wabunge wa viti maalumu, Dkt. Kitila Mkumbo alisema kuwa kwa uchanganuzi aliofanya kwa kutumia vigezo vya jumla kama vile umahiri, bidii, dhana ya uwakilishi wa wananchi kupitia wabunge wa viti maalumu na kila kanda kupata nafasi, itasaidia CHADEMA kupata wabunge makini kama ilivyokuwa katika bunge lililopita.

"Mbali ya vigezo hivyo vya jumla nilitumia vigezo vingine kwa sayansi ya takwimu ambavyo vilikuwa ni elimu, uzoefu wa uongozi kisiasa, uzoefu wa uongozi nje ya siasa, ugombea ubunge jimboni, mchango wa hali na mali katika shughuli za chama na kampeni zinazoendelea, umri katika chama, ambapo kila kigezo kilikuwa na sehemu ndogondogo tofauti ambavyo ndivyo tulitolea maksi.

"Kwa kweli kwa ukokotoaji wa vigezo hivyo CHADEMA imepata wabunge mchanganyiko wenye sifa mbalimbali kutoka karibu kila eneo la nchi katika kanda mbalimbali, kwa kweli ilikuwa lazima kuzingatia vigezo vingi kwani CHADEMA kinajiandaa kuunda serikali.

27 Sept 2010




Video zote kwa hisani ya Coby

NAOMBA MSAMAHA KWENU WAFANYAKAZI WAPENDWA KWA KUWATOA MACHOZI YA UCHUNGU BAADA YA KUANGALIA VIDEO HIZO.LENGO LANGU SIO KUWATIA UCHUNGU BALI KUWAKUMBUSHA JEURI YA JAKAYA KIKWETE KWENU.VILEVILE VIDEO HIZI ZINAWEZA KUSAIDIA KUMPA KIKWETE AIBU YA KUUDANGANYA UMMA KUWA HAJAWAHI KUKATAA KURA ZENU WAFANYAKAZI WAPENDWA.

NAWASIHI MACHOZI YENU YASIMWAGIKE BURE BALI MTAFSIRI UCHUNGU WENU KWA KUMPATIA MGOMBEA ALIYETANGAZA HADHARANI KUWA ANAZIHITAJI SANA KURA ZENU.MGOMBEA HUYO NI DOKTA WILLBROAD SLAA WA CHADEMA.KIKWETE ALIWAADHIRI HADHARANI KUPITIA KWENYE RUNINGA,NINYI MUMSHIKISHE ADABU FARAGHANI KWENYE KISANDUKU CHA KURA HAPO TAREHE 31/10/2010.

OMBI LA BLOGU HII NI KWA KILA MFANYAKAZI ALIYEUMIZWA NA JEURI HIZO ZA KIKWETE KUHAMASISHA MKE,MUME,DADA,KAKA,MWANA,SHANGAZI,BINAMU,MJOMBA,JIRANI,MPANGAJI,SHOSTI,MSHKAJI,MWENYE NYUMBA NA YEYOTE YULE UNAYEFAHAMIANA NAE,KISHA UWAHAMASISHE WAMNYIME KURA KIKWETE NA CCM YAKE NA BADALA YAKE KUMPIGIA KURA DOKTA SLAA NA CHADEMA.CHONDE CHONDE WAFANYAKAZI,MSIACHIE NAFASI HII ADIMU.
Video zote kwa hisani ya Coby

26 Sept 2010



Mwaka 2004,jarida maarufu la TIME la nchini Marekani lilimtangaza Rais wa zamani wa nchi hiyo,George W. Bush,kuwa "Mtu wa Mwaka" (Time Person of the Year 2004).Katika mahojiano na jarida hilo,Bush alizungumza mambo mawili ambayo japo sikuwahi kuwa shabiki wake yameendelea kunisaidia katika tafakuri zangu hususan kwenye fani ya uandishi kwa ajili ya jamii.

Jambo la kwanza ni kauli yake kuwa "japo nafahamu kuna watu hawaafikini na mtizamo wangu lakini angalau wanafahamu ninaposimamia kimtizamo".Akifafanua,Bush alisisitiza kwamba kama unaamini katika jambo flani basi inabidi ulisimamie hususan panapojitokeza upinzani au kukusolewa.

Jambo la pili ni imani yake kuwa upinzani au kukosolewa kunaweza kumsaidia mlengwa,kwa maana ya kujitambua yeye ni mtu wa aina gani-kwa mazuri au mabaya.Kadhalika,kwa mujibu wa Rais huyo wa zamani,ukiona unakosolewa au ulichosema/kufanya kinapelekea upinzani basi ujue kwa namna moja au nyingine kimewagusa wanaokupinga au kukukosoa.Kwamba,kama ulichosema au kufanya ni cha kipuuzi,nani atakuwa na muda wa angalau kukikosoa au kukipinga,let alone kukiangalia au kukisikia?

Ni "busara" hizo mbili za Dubya zilizonisukuma kuzungumzia mfumuko wa comments za kashfa na matusi kuhusiana na makala zinazohusu kampeni huko nyumbani.Unajua binadamu akimudu kufikia hatua flani ya maisha,hasa kama amepitia milima na mabonde,basi anakuwa na "ngozi ngumu" (thick-skinned).Binafsi nilitoka katika familia isiyojimudu sana,nikasoma kwa koroboi kwa vile nyumba yetu haikuwa na umeme,O' level na A'level nikategemea zaidi fadhila za ndugu,jamaa na marafiki kwa vile familia haikuwa na uwezo wa kumudu kila mahitaji yangu.Nakumbuka makazi yangu ya muda katika kambi ya JKT ya Ruvu iliyokuwa ikisifika kama kimbilio la watoto wa vigogo.Kwa hakika,adhabu za kijeshi hazikufua dafu kwa adhabu za kisaikolojia tulizokuwa tunapata hohehahe kama mie tuliochanganywa na watoto wa vigogo.

Pamoja na vikwazo na ugumu wote huo,namshukuru Mungu,wazazi wenye upendo,ndugu,jamaa na marafiki walionisaidia kwa hali na mali na kuifanya historia yangu iwe ya fanikio moja baada ya jingine.Haya ni masuala binafsi na nisingependa kuyazungumzia ila nachoweza kuweka bayana ni kuwa sijawahi kufeli tangu shule ya msingi,O'level,A'level,Mlimani (UDSM) na Chuo Kikuu cha Aberdeen ambapo nimefanikiwa kupata shahada mbili huku nikiendelea kuisaka ya tatu (nikiipata,zitakuwa shahada nne kwa ujumla).Naamini kuwa nitaendeleza historia ya kutofeli.Na la muhimu ni kupata shahada husika na si wala imegharimu muda gani.Sasa anapojitokeza  kichwa-panzi (ambaye pengine hata akitakiwa kuhitimu cheti cha chekechea itamlazimu apatiwe msaada wa twisheni) anapokashifu hatua ya kuridhisha kidogo niliyofikia inabidi kumhurumia tu.

Ugumu niliopitia katika maisha umenisaidia sana sio tu kuwa na "ngozi ngumu" bali pia kujifunza namna sahihi ya kuishi.Kuna msemo kuwa ukiweza kusalimika kwenye ugumu ni wazi hutoshindwa kumudu unafuu.Nimejifunza kuheshimu ubinadamu na utu wa mtu.Nimejifunza pia umuhimu wa imani- ya kiroho na kimtizamo-katika kufikia malengo ya maisha.Japo sijafika mahala pa kusema hapa ndio destination (kituo) yangu ya maisha,nimejifunza kuridhika na kidogo ninachopata huku nikijikumbusha kuridhika huko kusinilemaze kufikia malengo ya awali.

Kashfa na matusi (kutokana na msimamo wangu kumsapoti Dokta Wilbroad Slaa kwa nguvu zote) zinatoka kwa watu ambao si vigumu kuwafahamu.Unajua mtu anapoweka comment as anonymous haimaanishi kuwa bloga makini hawezi kujua mahali alipo mtoa comment.Ni rahisi tu kwa ku-track IP address kwa muda comment husika ilipowekwa.Sasa takriban comments zote zenye kashfa na matusi zinatoka maeneo nayoyahusisha na jamaa zangu flani wa zamani.Tatizo la wazembe hawa hawawezi hata kuwezesha IP zao zisitambulike,simply because fungu la fedha linalotolewa kwa madhumuni hayo zinaishia kuwekezwa matumboni mwao kama sio kwenye nyumba ndogo zao.Hawa wanasumbuliwa na ugonjwa wa kutanguliza maslahi ya matumbo yao na kusahau kabisa watu wanaowazunguka (including ndugu zao).Kulipwa mshahara mkubwa na posho nono kila katikati ya mwezi sio kigezo cha kusahau ndugu,jamaa na marafiki wanaoteseka mtaani,kijijini na kwingineko kwa vile tu wewe unayepaswa kuwatumikia ipasavyo unaelekeza nguvu kwa anayewatesa watu hao.

Imani yangu ni kwamba ufisadi ni kama ukimwi.Yaani,hata kama hujaambukizwa ukimwi basi kuna nduguyo,rafikio,jamaa au mtu unayemjua ambaye aidha anateswa na ugonjwa huo au ameshafariki.Ndio maana ya msemo kuwa hata kama ukimwi haujaku-affect bado ugonjwa huo una effect kwenye maisha yako.Katika namna hiyohiyo,hata kama mwajiri wako anakupatia mamilioni kama mshahara na laki kadhaa za "kuiweka nchi salama" haimaanishi ufisadi unaowatesa walalahoi huko mtaani haukugusi.Ukitanua kidogo tu wigo wa wahanga hao wa ufisadi utakutana na nduguzo,jamaa,rafiki na watu wengine ambao kwa namna moja au nyingine wanakugusa.Kwahiyo wakati jamaa zangu hao wanatoa kashfa na matusi kwa vile tu nasimamia kile wanachoona kama kinatishia "usalama" wa ajira zao,wanapaswa kutambua pia kuwa jitihada zangu zinawasaidia wao pia (kwa maana zinalenga kuwasaidia wale ndugu,jamaa,marafiki,nk wa haohao jamaa zangu).

Matusi,kashfa na vitisho haviwezi kubadili msimamo wangu.Tatizo la jamaa zangu wanaofanya hivyo ni lilelile alilogusia Bush kuwa angalau mie najua ninaposimamia na ndio maana naweza kutamka hadharani ninachoamini pasipo kuficha jina langu.Neno sahihi ni kuthubutu (to dare).Tatizo jingine la jamaa zangu hao ni kuguswa na kile nachoamini.Ajikunaye ujue anawashwa.Laiti ningekuwa namsifia Kikwete,au naweka picha tu bila mtizamo wangu binafsi basi jamaa hawa wasingediriki kufanya wafanyacho sasa.Na kwa vile wanawashwa,nami ntaendelea kumwaga dozi.

Anyway,simlalamikii mtu kwa vile safari ya ukombozi ni ngumu.Kuna mzembe mmoja anauliza eti je namsapoti Dkt Slaa kwa kutegemea wadhifa flani huko nyumbani.Laiti angejua undani wa maisha yangu asingehisi hivyo lakini inawezekana anachokonoa ili niropoke (wao na mie tulifundishwa kuwa miongoni mwa njia za kumchonoa mtu ni aidha kuzusha la kuzusha ili mtu aropoke au kumtibua ili aropoke).Kwa kuwa wao wamezowea kulipwa kwa kila wanachofanya,including "asante" za mafisadi wanaowatumikia basi wanadhani kila anayefanya jambo anatarajia malipo.Nachotegemea kwa Dokta Slaa atapoingia Ikulu hapo Novemba ni kuwapatia Watanzania WOTE kile wanachoendelea kunyimwa na utawala dhalimu wa kifisadi wa CCM kwa takriban nusu karne sasa ("WOTE"  hawa wanaotoa kashfa na matusi pamoja na ndugu,jamaa,marafiki etc waliosahauliwa na wenye midomo michafu hawa).

Na kwa vile vichwa panzi hawa hawakuwa na interest na blogu hii hadi nilipoweka bayana msimamo wangu dhidi ya Kikwete na sapoti yangu kwa Dkt Slaa,hawafahamu (au wanafahamu lakini wanazuga tu) kwamba kwa muda mrefu blogu hii imekuwa mstari wa mbele katika kukemea ufisadi.Nisiandikie mate kwa sababu ushahidi unapatikana hapo kwenye "makala za nyuma".Na kwa waliokuwa wakifuatilia safu za "Kulikoni Ugahibuni", "Mtanzania Ughaibuni" na "Raia Mwema Ughaibuni" katika magazeti ya Kulikoni,Mtanzania na Raia Mwema,respectively,wanafahamu vema kuhusu msimamo wangu.Sasa sijui wazembe hawa wanaohusisha posts zangu za kampeni na "matarajio ya kupata chochote" wanataka kusema hata safu hizo (2006-2008) nazo zililenga "kutarajia chochote" !!!

USALAMA WA TAIFA LILILOJAA MASIKINI WANAOKANDAMIZWA NA KUNDI DOGO LA MAFISADI WANAOLINDWA NA TAASISI ZA KUSIMAMIA MASLAHI YA UMMA NI SAWA NA TIME-BOMB.MUDA WA KULI-DEFUSE NI HUU.BADALA YA KASHFA NA MATUSI,TUMIENI FEDHA ZA WALIPAKODI KUUTUMIKIA UMMA NA SIO MAFISADI.

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.