8 Jun 2010

Rais Kikwete akikabidhi zawadi ya kinyago kwa mchezaji wa Brazil,Kaka,huku mtoto wa Rais,Ridhiwani Kikwete (kulia kwa Rais),akishuhudia na "tabasamu la haja" (Picha kwa hisani ya Ankal Michuzi)

Niite mzandiki,mkosoaji wa kila kitu,au hata mpuuzi.Yote sawa.Lakini haihitaji upeo hata wa mtoto mchanga kutambua kuwa uamuzi wa "kununua" kipigo cha mabao matano kutoka kwa Wabrazili ilhali tumegubikwa na matatizo lukuki ya kiuchumi ni,well,upuuzi.

Nilishabashiri awali kuwa baada ya mechi kati ya Taifa Stars na Wabrazili itakuja mechi kali zaidi kuhusu faida au hasara za mechi hiyo.Na hapa nazungumzia fedha.Kwa mujibu wa tovuti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),mechi hiyo ilifanikishwa na mkopo wa benki flani kwa Shirikisho letu la Soka chini ya uongozi wa Leodgar Tenga.Inaelezwa kuwa TFF walitarajia mpambano huo ungeingiza takriban dola milioni tatu ambazo zingerejesha gharama zinazokisiwa kuwa dola milioni mbili unusu (zaidi ya shilingi bilioni tatu)walizotumia "kununua" mechi hiyo.Kwa akili ya Tenga na wenzake,walitarajia uwanja wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000 ungefurika na pengine kuzalisha faida kubwa zaidi ya hizo dola milioni tatu zilizokisiwa.Sijui ni kufumbia macho umasikini unaowakabili Watanzania wengi au ni ubishi tu,TFF wakaweka viingilio vya juu na vitakavyoingia kwenye vitabu vya historia ya soka la Tanzania.

Sidhani kama tutafahamisha gharama halisi za mechi hiyo wala kuelezwa hasara kamili.Na si kwamba tutafichwa kwa sababu ya aibu ya waandaaji bali kuna "wajanja" (isomeke MAFISADI) watakaoongeza ukubwa wa hasara hiyo kwa kujirejeshea gharama wasizostahili.Lakini pamoja na usiri huo,tovuti ya BBC imemnukuu Waziri wa Habari na Michezo George Mkuchika akisema kuwa serikali haikuchangia chochote katika "ununuzi" wa mechi hiyo,na akatupa "kigongo" kingine kwa kudai TFF walikopa fedha kutoka benki kumudu gharama hizo.

Lakini kauli ya Mkuchika inakinzana na kauli ya awali iliyotolewa na Tenga,ambapo kwa mujibu wa tovuti ya gazeti la Daily Nation,alinukuliwa akieleza kuwa (nanukuu) "Tuliongea na Rais wetu (Jakaya Kikwete),na ni yeye ndiye aliyewezesha mechi hii kuwezekana".Tenga alisema (nanukuu tena) "(Rais) alivutiwa tangu mwanzo na kuhakikisha kila uwezo wa dola (serikali) unawezesha mechi hiyo".

Sasa sijui nani anasema ukweli kati ya Mkuchika na Tenga.Na pengine swali la muhimu zaidi ni nani atayebeba mzigo wa deni hilo kama si mlipakodi wa Tanzania.Na ni mzigo kweli kwani dalili za wazi za uzembe wa waandaaji wa pambano hilo tunaloaminishwa kuwa litaitangaza Tanzania ni matangazo mengi ya makampuni ya kigeni badala ya vivutio vya taifa letu.Well,unatarajia nini kutoka kwa wazembe walioshindwa hata kuwa na CD  ya uhakika ya wimbo wa taifa letu?

Kuna nyakati napata shida kuzielewa kauli za Rais Jakaya Kikwete.Nafahamu kuwa yeye ni mwanadamu kama mwingine,kwahiyo anaweza kufanya makosa ya kibinadamu.Lakini kwa vile nyingi ya hotuba zake huandaliwa na wasaidizi wake,nafasi ya makosa ya kibinadamu inapaswa kuwa ndogo.

Huko nyuma tumeshasikia kauli kadhaa tata kutoka kwa Kikwete,ikiwa ni pamoja na ile maarufu ya aliyotoa Mkoani Rukwa mwaka 2006 kwamba "anawajua kwa majina wala rushwa katika wizara na kwamba nguvu anayokwenda nayo siyo ya soda"(na ameishia kutoa indefinite deadline),kisha ile ya Bandarini Dar kuwa "ana orodha ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) wasio waaminifu ambao wanashirikiana na wafanyabiashara kukwepa kodi kwenye Bandari ya Dar es Salaam" (lakini licha ya kuahidi kukabidhi orodha hiyo kwa Kamishna wa TRA hajafanya hivyo hadi leo) ,sambamba na ile ya "sijui kwanini Tanzania ni masikini" (kama hajui atawezaje kuleta maisha bora).Kauli nyingine tata ni hii ya majuzi kuwa "takrima haikwepeki" (ambapo tafsiri ya jumla ni sawa na kuruhusu rushwa),na jana nimeona mahali akisema "Haiwezekani kuua albino halafu utajirike, ingekuwa hivyo albino wenyewe wangekuwa matajiri wakubwa mno,”.Na sasa amekuja na kauli nyingine tata kuwa "matukio ya mimba kwa wanafunzi wa kike nchini yanasababishwa na viherehere vya wanafunzi wenyewe".Kadhalika,sambamba na kauli hiyo Mkuu wetu wa nchi alinukuliwa akisema "Kila anayepata Ukimwi anaufuata mwenyewe na wengine ni viherehere vyao; kwa mfano watoto wa shule"




Tukiweka kando hizo kauli tata za huko nyuma,hii ya mimba za wanafunzi imenisukuma kuandika makala hii.Hivi ina maana Rais hafahamu kuwa baadhi ya mimba za wanafunzi zinachochewa na mabazazi wa kiume au mafisadi wa ngono wanaotumia fedha zao za kifisadi kuwarubuni mabinti hawa?Sawa,tunaweza kuwalaumu mabinti hawa wanaorubuniwa lakini ni muhimu kuangalia suala hili kwa undani zaidi kwani wengi wa wanafunzi wa kike wanaoishia kutundikwa mimba na mafisadi wa ngono wanatoka familia masikini na inawawia vigumu kukabiliana na vishawishi vya mabazazi hao.

Kwa kudai kuwa sababu kuu ni kiherehere cha mabinti hao,Rais anatupa lawama kwa asilimia 100 kwa wanafunzi hao wa kika kana kwamba wanajidunga mimba wao wenyewe.Kwanini,yeye kama mwanaume,asiangalie upande wa pili wa shilingi?Kwanini,kwa mfano,sambamba na kudai kuwa tatizo ni kiherehere cha wanafunzi hao angewashutumu pia wakware wanaowinda wanafunzi?Kwa tunaofahamu siasa za mtaani,licha ya kuwa ni uzinzi pekee,wakati mwingine tamaa ya wanaume wakware kwa wanafunzi au mabinti wadogo inakuzwa na imani potofu kuwa "dogodogo hawana ukimwi" au "hawana gharama kuwatunza",na ushenzi mwingine kama huo.Na hii yote ni mitazamo ya wanaume ambao wamesalimika katika shutuma hizo za Kikwete.

Tukija kwenye kauli yake kuwa "Kila anayepata Ukimwi anaufuata mwenyewe..." ni dhahiri kuwa aidha Rais hajui namna ukimwi unavyoambukizwa au anapuuza njia nyingine za maambukizo.Japo ni kweli kuwa njia kuu ya maambukizo ya ugonjwa huo hatari ni tendo la zinaa,lakini licha tu kuwa hiyo sio njia pekee bali pia si kila anayeambukizwa "anaufuata mwenyewe".Vipi kuhusu akinamama au akinababa wanaoletewa ukimwi na wenza wao wasio waaminifu?Takwimu kadhaa zimekuwa zikutuonyesha kuwa asilimia ya wanandoa walioathirikia kwa ukimwi ni kubwa kama ilivyo kwa wasio wanandoa,na hiyo ilipaswa kumfahamisha Rais kuwa "kuna wanaoletewa ukimwi" na sio "kuufuata wenyewe" kama anavyoamini yeye.

Tukienda mbali zaidi,kauli hiyo ya Rais inaweza kutafsiriwa kama kuwanyanyapaa waathirika wa ukimwi,hususan wale walioambukizwa na wenza wao,au walioupata kwa njia nyingine kama tohara na chanjo za kienyeji ambapo nyembe moja hutumika kwa watu mbalimbali na hivyo kujenga uwezekano mkubwa wa maambukizo.Na kwa vile taasisi nyingi za afya zina vifaa duni,ni dhahiri kuna wauguzi mbalimbali wanaoambukizwa ukimwi kutokana na na nyenzo hizo duni makazini mwao.Lakini kuna kundi jingine la muhimu-watoto wachanga wanaozaliwa wakiwa wameshaambukizwa ukimwi.Je Kikwete anaweza kudiriki kudai hata hawa nao wameufuata ukimwi wenyewe?

Kiongozi makini anapaswa kuepuka generalisation,yaani kutoa kauli za jumla jumla pasipo kuangalia exceptions katika anachozungumzia.Na ifahamike kuwa kauli ya Mkuu wa Nchi ni sawa na mtizamo wa nchi husika,hivyo hitaji la umakini kabla ya kutoa kauli zinazoweza kuwaathiri baadhi ya wananchi.

Anyway,pengine alikuwa anatania tu wakati akisema hayo kwenye sherehe za kimila huko Mwanza ambapo miongoni mwa walikuwa kwenye msafara wake ni mtuhumiwa wa ufisadi wa rada,Mzee wa Vijisenti Andrew Chenge.

5 Jun 2010

Mwezi Februari mwaka huu,Rais wa Kampuni ya Toyota (ya Japan) Akio Toyoda aliomba rasmi msamaha kwa wateja wa kampuni hiyo nchini Marekani ambao walikumbwa na matatizo ya kiufundi kwenye magari yao.Mwezi kama huo mwaka jana,mabosi wa mabenki ya RBS na HBOS ya hapa Uingereza nao waliomba msamaha kwa wateja wao na umma kwa ujumla kutokana na uzembe uliopelekea benki hizo kukwamuliwa na serikali kwa pauni bilioni 37 fedha za walipakodi wa hapa. Na hivi majuzi,Waziri Mkuu wa Japan,Yakio Hatoyama, ametangaza kuwa atajiuzulu kufuatia kutotimiza ahadi aliyotoa wakati wa kampeni zake za uchaguzi kuwa angeondoa vikosi vya jeshi la majini la Marekani katika visiwa vya Okinawa.


Lakini wakati hayo yakitokea,serikali ya CCM imewaamuru mawaziri wake kuzunguka mikoani kueleza mafanikio ya Awamu ya Nne katika harakati za wazi kuelekea Uchaguzi Mkuu.Tuweke ushabiki pembeni,hivi kweli mawaziri hawa hawakustahili kuzunguka huku na huko kuomba msamaha kwa mlolongo wa madudu tunayoendelea kuyashuhudia tangu mwaka 2005 (na pengine madudu zaidi yanayoendelea kufanywa na CCM miaka nenda miaka rudi)?


Msanii mkongwe wa hapa Uingereza (na duniani kwa ujumla),Sir Elton John aliwahi kuimba wimbo wenye jina SORRY SEEMS THE HARDEST WORD (yaani 'samahani inaelekea kuwa ni neno gumu').Na hakukosea,japo hakuwa analenga siasa za nchi zetu za Dunia ya Tatu,hususan Afrika,na hasa Tanzania.Watawala wetu ni wepesi sana katika kugeuza lawama kuwa pongezi,na wakibanwa katika hilo hugeuka mbogo na kuja na vitisho lukuki.

Labda nikukumbushe kidogo kwanini naamini ziara za mawaziri zingekuwa na maana zaidi kama zingetumika kuomba msamaha kwa wananchi badala ya kuelezea mafanikio ambayo kimsingi yanabaki kwenye takwimu zaidi kuliko uhalisia.Kwanza,Awamu ya Nne ilitufahamisha kuwa inafahamu kilio cha Watanzania,na ikaja na kauli mbiu ya kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya.Naamini mie si pekee niliyesahau kuhusu kauli mbiu hiyo kwa vile wala haisikiki tena.Lakini kama hiyo haitoshi,kukaongezwa kibwagizo cha Maisha Bora kwa Kila Mtanzania (Yanawezekana).Japo sote tunatambua kuwa watawala wetu wanaishi kama wako peponi lakini hiyo sio excuse ya kuwafanya wasielewe kuwa maisha bora yamewezekana zaidi kwa mafisadi kuliko kwa wananchi walalahoi wa kawaida.Kwahiyo kama viongozi hawa wangekuwa na nidhamu kwa wapiga kura waliowaweka madarakani hapo 2005 basi angalau wangetuambia nini kinachopelekea maisha bora kubaki haki ya mafisadi wachache huku walalahoi wakizi kuwa walalawima.

Baada ya kuingia madarakani,Awamu ya nne ilitueleza kuwa ili kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania kunahitajika baraza kuuuubwa la mawaziri.Binafsi niliona kuna mantiki katika hoja hiyo japo sikuwa na uhakika kuwa "mwalimu anaweza kumudu darasa lenye wanafunzi wengi" kama ilivyokuwa kwenye kabineti ya JK.Bila kuuma uma maneno,kwa kifupi ukubwa wa baraza la mawaziri haujafanikiwa kwa chochote katika ku-meet matarajio ya Watanzania.Sanasana wengine walilazimika kujiuzulu baada ya kutuingiza mkenge kwenye ishu kama za utapeli wa Richmond.Ungetegemea kujiuzulu huko kungeandamana na hatua za kisheria lakini waliojiuzulu waliishia kupongezwa huku wakikumbushwa kuwa yaliyowakumba ni ajali tu za kisiasa na si ajabu siku moja wakarejea madarakani.

Mkuu wetu wa nchi akatuambia kuwa anawafahamu wala rushwa ila anawapa muda wa kujirekebisha.Binafsi,hapo ndipo nilipoanza kuhisi kuwa sikuwa sahihi kuamini kwamba tumepata mrithi halisi wa Mwalimu (Nyerere) in the form of JK.Tangu lini mwizi akapewa deadline?Kama wala rushwa walikuwa wanajulikana kwa Rais kilichopaswa kufanywa ni yeye kukabidhi orodha hiyo kwa taasisi husika ili wachukuliwe hatua stahili.Unajua,laiti JK angekabidhi orodha ya wala rushwa anaowajua kwa vyombo vya usalama kisha wakakamatwa na kuepwa deadline,pengine by now tusingekuwa tunajiuliza wenye Kagoda ni akina nani.Ni muhimu wak Watanzania kumhoji Rais wetu mpendwa kuhusu hao wala riushwa anaowafahamu,na lini hiyo deadline ita-expire.Tunachohitaji ni majina na sio idadi,na hata kama ni idadi basi tuambiwe lini watashughulikiwa.

Tuaambiwa kuwa matatizo ya umeme yangepatiwa ufumbuzi wa kudumu only miezi michache baadaye kufahamu kuwa ufumbuzi wenyewe unahusisha matapeli wenye kampuni ya briefcase (Richmond).Shahidi muhimu katika sakata la EPA akahifadhiwa mpaka Maulana akachukua uhai wake (kuna wanaodai kuwa bado yuko hai au huenda kafanyiwa plastic surgery) halafu wenye nchi wakagoma katakata kutuambia mwizi mkubwa wa fedha za EPA (Kagoda ni nani).

Tuaaambiwa kuwa ziara za mara kwa mara za Rais wetu huko nje ni muhimu kuitangaza nchi yetu na yeye kujitambulisha,kabla ya kuaminishwa kuwa Mkutano wa Sullivan na huu wa majuzi wa Economic Forum utalinufaisha taifa hasa katika sekta ya utalii,only for tuliorogwa sie kulipa mabilioni ya shilingi kuialika timu ya taifa ya Brazil huku kukiwa na ngonjera zilezile za "ziara hii itasaidia kuitangaza Tanzania".Kama ziara za Rais huko nje na rundo la wafanyabiashara (plus mikutano kama ya Sullivan na huo wa Economic Forum) imeshindwa kuzaa matunda,dakika 90 za mechi na Wabrazili zitaweza?

Majuzi wafadhili wametangaza kupunguza misaada yao kwa sababu ya ufisadi (putting it straightforward) na Waziri wetu wa Fedha Mustapha Mkulo bila aibu anasema hiyo isitupe hofu kwa vile serikali itakopa benki ya Stanbic!Nasema "bila aibu" kwa vile sio tu kukopa sio sifa hususan kwa serikali iliyoingia madarakani na mkwara wa maisha bora kwa kila Mtanzania bali pia deni hilo litabebwa na walalahoi haohao wanaoendelea kubebeshwa mzigo wa mahela yanayokwibwa na mafisadi kila kukicha.

Haya,tukaambiwa tena kuwa kwa vile kuna mtikisiko wa uchumi wa dunia basi na hohehahe sie lazima tuyanusuru makampuni yetu katika kile kinachofahamika ki-uchumi kama "stimulus package".Hivi kwa mwenye akili timamu,ukitangaza kuwa kuna hela za bure somewhere unatagemea nini kama sio vigogo kuunda kampuni hewa na kuiba fedha hizo?Hadi leo hatujaambiwa mafanikio ya stimulus package hiyo, na kama ilivyokuwa kwenye ripoti ya mabomu ya Mbagala usitarajie kuambiwa lolote la maana zaidi ya takwimu za kizushi.

Halafu Mkuu wetu wa nchi akatupa presha kwa kuamua kuhutubia Bunge kuhusu sakata la EPA (pamoja na mambo mengine).Tunaloweza kukumbuka zaidi kwenye hotuba hiyo ni kauli yake kuwa anathamini sana haki za binadamu ikiwa ni pamoja na za mafisadi.Kumbukumbu nyingine ni angalizo kutoka kwa Spika wa Bunge,Samweli Sitta,kuwa haki za binadamu za walalahoi ni muhimu zaidi kuliko za hao mafisadi.

Nimejitahidi kuorodhesha machache yanayopaswa kuombewa radhi na mawaziri wa serikali ya Awamu ya Nne badala ya "kueleza mafanikio".Unless wanataka kutuaminisha kuwa kukua kwa ufisadi ni sehemu muhimu ya mafanikio yao.Natambua kuwa "SAMAHANI" ni neno gumu kama alivyosema Elton John lakini uungwana ni kitu cha bure.Hizo fedha za walipa kodi wanazotumia kuzunguka huku na kule zingeweza kutumika vizuri zaidi kwa kila Waziri kuomba msamaha kwa madudu aliyofanya katika miaka hii mitano.Kaulimbiu kuwa "mlitutuma, tumetekeleza, tumerudi kuwaelezeni tulivyotekeleza na kuwasikiliza" ni matusi ya nguoni kwa vile hakuna Mtanzania mwenye akili timamu aliyeituma serikali kuingia mikataba ya kitapeli na wazushi wa EPA,au kukomalia kutotaja Kagoda ni mdudu gani,plus madumu mengineyo.Tulichowatuma ni kutukomboa kutoka katika lindi hili la umasikini sambamba na kuboresha hali za maisha yetu.Hatukuwatuma kuuza kila kilichopo kwa bei ya kutupa wala hatukuwatuma kung'ang'ania kununua samani kutoka nje na hatimaye kukumbuka dakika za majeruhi kuwa ununuzi huo hauendani na umasikini wetu.

Japo nakerwa na ziara hizi za mawaziri zinazozidi kuwabebesha mzigo walipa kodi walalahoi lakini nakereka zaidi napoona watu hawa wanapotufanya wajinga kiasi cha kutuzushia kuwa TULIWATUMA KULEA UFISADI.

Tumia kura yako vizuri,ukiendekeza ushabiki utazidi kuumia.Hakuna miujiza inayoweza kuondoa ufisadi hata kama watu watakesha kwenye nyumba za ibada (na huko wanakutana na "wabishi" kama Askofu Kilaini ambao wanaendelea kung'angania mtizamo wao finyu kuwa JK bado ni chaguo la Mungu.Askofu muogope Mungu wako unayemtumikia,please!).Nia pekee ya kuondokana na ufisadi ni kuwaondoa mafisadi.Kumbuka kuwa ufisadi ni kitendo kinachofanywa na mafisadi,na as long as wanaendelea kuwepo basi inakuwa mithili ya kupe au mbung'o na damu.Watanyonya hadi tone la mwisho.

AMKA!

4 Jun 2010




Well,well...I'm not that good when it comes to fashion,but poor as I might be,the Japanese Prime Minister's sense of fashion is SIFURI,ZILCH,ZERO...Oh,no.He doesn't even deserve a zero.Let's rephrase the sentence...his sense of fashion is non-existent.He doesn't have any.Candy has voluntarily offered help to the likes of the PM (READ IT HERE).Check the video report below and then click the following links to see how fashion police have their knives out for the Premier Yukio Hatoyama 

AFP: Japan PM's threads are final straw for fashion critic

THE WEEK: Japan's prime minister undone by the world's ugliest shirt?

STYLEITE: Japan’s Prime Minister Forced To Answer For His Checkered Shirt
.
JEZEBEL: Fashion Police Condemn Japanese Prime Minister's Fashion, Poll Numbers Fall

2 Jun 2010

A come back to the Industry after almost 25 years, Anna Luks, a mother of two boys, is now revealing to us, a glimpse of her collection called Colour Explosion. Anna will have much to talk about her work very soon. Luks will show her debut collection in July, date to be confirmed.

This photo shoot was taken recently at the Middlesex University Cat Hill studios, and was modelled by Jestina George.

Designer/Stylist: Anna Luks

Photographer: Sonia Marabet

Hair & Makeup: Brenda

Kwa mujibu wa imani zetu za Kiswahili,aliyekuroga akifariki basi uwezekano wa kupona nao unakuwa kama umefariki.Na msemo huu unaonekana kurandana na hali halisi ya baadhi ya matendo yetu viumbe tunaojulikana kama Watanzania.Nafahamu kuwa si wote "tuliorogwa" lakini hiyo si sababu ya "kutowatolea macho" wenzetu "waliorogwa kisha aliyewaroga akafariki".

Mwishoni mwa wiki hii,timu yetu ya taifa inakabiliwa na mpambano muhimu dhidi ya timu ya taifa ya Rwanda katika kusaka nafasi ya kushiriki kwenye michuano ya CHAN.Taifa Stars inatarajiwa kucheza siku ya Jumapili kisha Jumatatu wanatarajiwa kuingia tena uwanjani kupambana na timu ya Taifa ya Brazil katika pambano lililonunuliwa kwa mamilioni ya dola na chama chetu cha soka.

Na kwa takriban wiki nzima sasa,uongozi wa FA umekuwa bize zaidi na maandalizi ya pambano hilo walilonunua kuliko kuelekeza akili zao kwa mpambano dhidi ya Rwanda.Japo natambua kuwa kila mpenzi wa soka duniani angependa kuiona Brazil ikicheza uwanjani lakini sio kwa kununua mechi ya mamilioni ya fedha ambazo hakuna uhakika kama zitarudi.FA hawajaweka bayana gharama za kununua mechi hiyo lakini taarifa zinasema wamelipa dola za kimarekani milioni mbili unusu  (zaidi ya shilingi bilioni 3 unusu).Na hiyo ni ada (fee) tu lakini kuna uwezekano wa kiwango hicho kuwa kikubwa zaidi tukichanganya na gharama za kumudu ziara hiyo.

Kuna hoja kuwa ziara hiyo itasaidia kutangaza utalii.Well,lakini tuwe wakweli,yaani kutangaza utalii kwa dakika tisini kwa gharama ya shilingi bilioni tatu!?Na kama tujuavyo tatizo sugu la wizi wa mapato kuanzia TRA hadi kwa watendaji ngazi ya kata,si ajabu muda huu mafisadi wameshapiga mahesabu ya pasenti ngapi watakwiba kwenye chochote kitakachpatikana kwenye mechi hiyo.

Na kuna hoja ya rankings za FIFA.Hivi mechi moja ya kununua kwa mabilioni itatupandisha kwa kiwango gani ukilinganisha na menchi dhidi ya Rwanda ambayo kama "tukikaza misuli" na kufanikiwa kucheza CHAN tutapata nafasi kubwa zaidi ya kupandisha ranking yetu huko FIFA?

Ukitaka kufahamu namna ubabaishaji na ufisadi unavyozidi kutafuna mfumo wa jamii yetu subiri mechi iishe kisha vianze visingizio vya namna FA walivyoshindwa kufikia lengo la mapato.Binafsi nisingekuwa na tatizo laiti FA wangeafikiana na wenzao wa Brazil kisha kuuza tiketi kabla ya mechi na hivyo kufahamu faida au hasara itakayopatikana.Lakini kwa hali yasasa ni sawa na kucheza bahati nasibu.Na si ajabu visingizio vimeshaandaliwa as to kwanini "mechi hiyo haikuweza kurejesha faida iliyotarajiwa".

Ndio maana nashawishika kusema kuwa inawezekana ALIYETUROGA KESHAFARIKI.

1 Jun 2010

Crew ya £OVELY GAMBLE
BARAKA BARAKA, Managing Director wa Urban Pulse,akitoa hotuba
 BARAKA, DAISY,TIM, RENNY na FRANK
FRANK EYEMBE na BARAKA BARAKA
MC wa Show,Miss TINA GEORGE wa AILTV
MECKY,RAHMA CLASSIC,TINA,BARAKA,HALIMA,FRANCIA na FRANK
Msanii ANN-LYNN,AMOS MASANJILA na TINA
Producer wa £ovely Gamble,FRANK EYEMBE,akitoa hotuba
Urban Pulse CEO akiwa na MECKY
£OVELY GAMBLE

31 May 2010


Nafahamu unaweza usinielewe kwenye post hii lakini naomba niweke bayana kuwa niko radhi kutofautiana nawe msomaji wangu mpendwa.Kwa tutakaoafikiana,all I can say is POA.Nimeguswa na habari kuwa jana Makamu wa Rais,Dkt Shein, amezindua mbio za mwenge.Lengo la makala hii ni kuibua mjadala kuhusu suala hili la MWENGE WA UHURU.

Zamani hizo,mwenge ulikuwa na maana kubwa kwa kila mahali ulipopita.Lakini ni dhahiri kwamba mbio za mwenge kwa sasa hazina tofauti na ngonjera kuwa "Tanzania ni nchi ya Kijamaa" au kaulimbiu kwamba "Maisha Bora kwa Kila Mtanzania Yanawezekana".

Hili dude linalokula mamilioni ya shilingi katika gharama za kununua mafuta ili liendelee kuwaka,sambamba na posho kwa wanaolizungusha nchi nzima lina umuhimu gani kwa sasa?Maana zamani hizo mwenge ulikuwa na madhumuni ya KUMULIKA lakini sote tunafahamu kuwa kwa muda mrefu sasa mwanga wa mwenge huo unamulika vichochoroni tu huku ukishindwa kuwaangazia macho mafisadi wanaotafuna nchi yetu kama mchwa.Natambua kuwa kuna miradi mbalimbali inayozinduliwa wakati wa mbio za mwenge lakini hilo linafanyika hata wakati mwenge umezimika.Kwa maana nyingine,mwenge uwake usiwake bado wananchi wataendelea kujikusanya (pamoja na uchovu wao) kujitafutia maendeleo yao wenyewe.

Tatizo kubwa la sie Waafrika ni kuendeleza "mila na desturi" hata pale zilipopitwa na wakati.Hivi fedha zinazotumika kuzungusha mwenge nchi nzima zinaweza kujenga zahanati,shule na barabara ngapi?Kwa hakika ni nyingi tu.

To cut the story short,mie nina mtizamo kuwa mbio za mwenge zimepitwa na wakati.Naamini kuwa gharama zinazotumika katika mbio za mwenge zinaweza kutumika vizuri zaidi kwenye maeneo mengine ya msingi.Mwenge unakimbizwa kila mwaka lakini umasikini wa Watanzania unazidi kuongezeka (puuza kauli za Mkulo kuwa uchumi unazidi kukua kwani analipwa mshahara kusema 'lolote'),ujambazi ndio usiseme,na mafisadi wanazidi kulindwa na chama tawala.Sasa hili dude linalokula mafuta kama halina akili nzuri bado lina umuhimu kweli kwa mazingira ya Tanzania ya sasa?

Karibu uchangie


Ukisoma habari zifuatazo unaweza kukubaliana nami kuwa AKUTUKANAE HAKUCHAGULII TUSI.Katika habari ya kwanza tunashuhudia Waziri wetu wa Fedha akiongea vitu ambavyo vinaleta maana tu vikiangaliwa kwa maadnishi lakini sio mtaani.Na katika habari ya pili,tunashuhudia uzembe uliozoeleka wa kitokee kwanza kisha tufanye kitu flani.Yaani siku zote hizi mtu aliyekabidhiwa dhamana ya kuongoza Jeshi la Polisi alikuwa hafahamu kuwa kituo cha polisi kisicho na silaha hakina tofauti simba wa karatasi!
Hebu soma habari husika hapa chini
Mkulo: Uchumi unazidi kukua 

Saturday, 29 May 2010 09:22

Exuper Kachenje

SERIKALI imesema kuwa ukuaji wa pato la taifa katika unakadiriwa kuongezeka na kwamba pato halisi litakua kwa asilimia 7 katika mwaka 2010.

Akiwasilisha taarifa ya mwelekeo wa uchumi kwa mwaka 2009 na mwelekeo katika kipindi cha kuanzia 2010 hadi 2013 mbele ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo alisema kuna matarajio makubwa uchumi kuendelea kukua.

Huku akiwaomba radhi wabunge kwa kuchelewa kuwapa nakala ya taarifa hiyo, Mkulo alisema maelezo hayo yalipitishwa juzi asubuhi na Baraza la Mawaziri.

"Naomba radhi waheshimiwa kwa kuchelewa kuwapatia nakala ya taarifa hii kwa kuwa imepitishwa jana asubuhi (juzi) na Baraza la Mawaziri hivyo imechelewa kuchapwa," Mkulo alisema.

Mkulo alisema kuwa katika mwaka 2011, pato halisi la uchumi litakuwa kwa asilimia 7.1, mwaka 2012 asilimia 7.4 na hadi kufikia mwaka 2013 pato halisi la taifa litafikia asilimia 7.8.

“Kama ilivyotarajiwa athari za msukosuko wa uchumi zilikuwa za mpito, hivyo ukuaji wa pato la taifa unakadiriwa kuanza kuongezeka. Pato halisi litakua kwa asilimia 7.0 mwaka 2010, asilimia 7.1 mwaka 2011, asilimia 7.4 mwaka 2012 na kuendelea kuongezeka hadi asilimia 7.8 mwaka 2013,” alisema Mkulo.

Alifafanua kuwa malengo hayo yanatarajiwa kufikiwa kwa kutekeleza sera na misingi ya uchumi kwa kuzingatia mambo mbalimbali, ikiwemo mwenendo wa uchumi wa dunia na hitaji la kujenga uwezo kukabiliana na athari za msukosuko wa uchumi wa dunia.

Alitaja misingi mingine kuwa ni kuendelea kutengemaza vigezo muhimu vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii hasa mfumuko wa bei, kuweka msukumo katika utekelezaji Dira ya Maendeleo ya Taifa, Mkukuta awamu ya pili, Kilimo Kwanza na kuelekeza rasilimali kwenye maeneo chochezi ya uchumi kwa haraka zaidi.

Kwa mujibu wa Mkulo katika kipindi hicho miradi inayopewa kipaumbele katika mwongozo huo wa bajeti itakuwa ni pamoja na miundombinu, uendelezaji ardhi na makazi pamoja na vitambulisho vya taifa.

Vingine ni nishati, viwanda, sekta ya fedha na pia kutaja uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba mwaka huu kuwa ni kipaumbele cha kipekee kwa serikali katika mwaka huu kwa lengo la kuhakikisha unafanyika kama ilivyopangwa.
Waziri huyo alisema katika muda huo kasi ya upandaji wa bei inakisiwa kupungua hadi asilimia 8.0 kufikia mwezi Juni mwaka huu na kupungua zaidi hadi asilimia tano ifikapo Juni 2011.

Aidha, alisema katika kipindi hicho mapato ya ndani ya taifa yatafikia uwiano wa asilimia 17.3 kwa mwaka 2010/11; asilimia 17.4 mwaka 2011/2012 na asilimia 17.6 ifikapo mwaka 2012/2013.

Alisema serikali pia inalenga kuwa na akiba ya fedha za kigeni itakayokidhi uagizaji bidhaa kutoka nje na huduma kwa kipindi kisichopungua miezi mitano; kuwa na viwango imara vya ubadilishaji wa fedha; kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara na kuedeleza kilimo na kupunguza viwango vya riba.
Kuhusu biashara, Mkulo alisema Tanzania imeshuka katika vigezo vya urahisi wa kufanya biashara kutoka nafasi ya 126 kati ya nchi 183 na kuwa ya 131 mwaka 2009.

Kuhusu mapato ya ndani, Waziri Mkulo alisema yaliongezeka kwa asilimia 18.1 kufikia Sh4,293.1 bilioni mwaka 2008/09; kutoka Sh3,634.6 bilioni mwaka 2007/08 na kwamba kiasi hicho ni pungufu ya asilimia 10 kwa mwaka 2008/09.

Kwa kipindi cha Julai 2009 hadi Machi 2010, mapato ya ndani yalifikia Sh3,490.3 bilioni ikiwa chini ya asilimia 8.7 ya makisio ya Sh3,924.9 kwa kipindi hicho akieleza kuwa hali hiyo ilitokana na athari za kuyumba kwa uchumi wa dunia.

Mkulo alisema kwa kipindi cha Julai 2009 hadi Machi mwaka huu matumizi ya serikali yamefikia Sh6,143.9 bilioni kati ya makisio ya Sh6,718.7 kwa kipindi hicho, ikiwa ni upungufu wa asilimia tisa uliotokana na upungufu wa mapato.

Wakichangia maelezo hayo wabunge walitaka serikali ieleze itafanya nini kuwezesha wananchi kumiliki uchumi badala ya kumiliki asilimia 10 pekee kama ilivyo sasa.

CHANZO: Mwananchi

IGP Mwema afuta vituo

na Sitta Tumma na Ali Lityawi
SIKU tatu baada ya wananchi wa Kata ya Mbarika, wilayani Misungwi, mkoani Mwanza kuvamia kituo cha polisi na kuua majambazi watatu, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema ameanza kulikarabati upya jeshi hilo.
Tanzania Daima imethibitishiwa hilo; ukarabati wa jeshi hilo umelenga kuvipunguza kwa kuvifutilia mbali baadhi ya vituo vidogo visivyokuwa na silaha wala askari wa kutosha.

Wakati IGP Mwema akipanga kuvifumua vituo hivyo, jeshi la polisi mkoani Mwanza halijamkamata mtu hata mmoja kuhusiana na tukio la kuvamia na kuvunja kituo cha polisi Mbalika na kuua watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.

Akithibitisha yote hayo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanmza, Simon Sirro (RPC), alisema IGP Mwema yupo katika mikakati ya kupunguza utitiri wa vituo vidogo vidogo vya polisi, kwani vimeonekana havina faida kwa wananchi.

“Unajua vituo hivi vidogo visivyokuwa na silaha havina faida kwa maana hiyo mkuu wa polisi kwa sasa yuko katika mpango wa kuvipunguza.

“Mkakati huu madhumuni yake ni kuwa na kituo kimoja kila kata chenye silaha na askari wa kutosha,” alisema Kamanda Sirro.

Mei 27 mwaka huu majira ya saa 1:30 jioni, wananchi wa Mbalika, wilayani Misungwi mkoani hapa, walivamia na kuvunja kituo cha Mbalika kisha kuua watuhumiwa.

Moja ya sababu za wananchi hao kuvamia na kufanya mauaji katika kituo hicho, inaonekana ni kutokuwa na silaha pamoja na askari wa kutosha kituoni hapo na kumshtua IGP Mwema.

Kamanda Sirro, alipoulizwa mikakati ya kupunguza vituo hivyo, alisema hana jibu anayepaswa kulizungumzia ni IGP Mwema pekee.

Tanzania Daima, ilipomtafuta IGP Mwema kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi, simu yake ilipokelewa na msaidizi ambaye alidai yuko mkutanoni.

“Afande IGP yupo kikaoni huku Kilolo mkoani Iringa; atakuwa Dar es Salaam kesho (leo),” alisema msaidizi huyo.



Tawala,viongozi na wafanyakazi wa African Star,Afro Euro Events Management, Buzzie Production, Manamba Studio na Urban Pulse. Wanatoa shukurani zao za dhati kwa Watanzania wote waliojitokeza usiku wa jana 29/05/2010 kwenye onyesho maalum la ‘£OVELY GAMBLE’ kuchangia watoto wanaoishi na vijirusi vya UKIMWI nyumbani Tanzania. Watoto hawa wanaangaliwa na TANZANIA MITINDO HOUSE. Hakika ya kweli mmeoonyesha umoja ambao tunauthamini na hatutousahau.

Vilevile tungependa kuwatambua watu wafuatao, ambao kwa njia moja ama ingine    wmesaidia sana kufanikisha Onyesho hili maalum

UBALOZI WA TANZANIA  (mama Balozi na Maafisa wote wa Ubalozi)
TANZANIA ASSOCIATIONS zote Kitaifa na matawi  ya Reading, Birmingham na Soctland
BONGO FLAVOUR (Dixon na Flora)
TMH (Khadija Mwanamboka)
SWIFT FREIGHT (Abu Faraji)
SWAHILI TRAVEL AGENCY (Tino)
VINCENT BAR (Kalinga na Gado)
MAMA MAYOR (Mariam Nice)
NOCHA SEBE
MISS YVONNE
WITENGERE KITOJO 
TEGEME CHAMPANDA
FRANCIA CHENGULA
FREDDY MACHA
AYOUB MZEE
RASHIDI KAWAWA
ALLY MUHIDINI
GLOBAL PUBLISHER (Abdalah Mrisho)
BONGOSTARLINK (Dj Choka)
JIACHIE (Ahmad Michuzi)
KULIKONI UGHAIBUNI ( Evarist Chahali)
MISS JESTINA GEORGE (Tina George)
FASHION 8020 (Shamim Mwasha)
NURU THE LIGHT (Nuru)

Vyombo hivi na Watanzania hawa wamekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha Onyesho hili maaaluma la mchango wa kihiyari. Mungu awaongezee na tuendeleze umoja  huu.


            MUNGU IBARIKI TANZANIA MUNGU WABARIKI WATANZANIA

29 May 2010

Mama Mpendwa,

Ilikuwa saa 4.30 usiku,tarehe 29 Mei 2008 ulipotutoka.Nakumbuka nilipopigiwa simu kufahamishwa kuwa Bwana Amekutwaa,nilidhani ni ndoto tu.Japo ulikuwa umepoteza fahamu kwa zaidi ya miezi mitatu kabla ya kukumbwa na mauti sote tuliamini kuwa siku moja ungeamka ukiwa mzima.Mama,japo leo ni miaka miwili tangu ututoke,bado nahisi niko ndotoni na nimeshindwa kabisa kukubaliana na ukweli kwamba haupo nasi.Mara kwa mara nakuona ndotoni,lakini napoamka nagundua ni ndoto tu,na hiyo inazidisha uchungu na majonzi.

Baba Mzee Chahali,uliyeishi nae katika ndoa kwa miaka 50,anaendelea kukukumbuka mno.Ni vigumu zaidi kwake kukabiliana na kututoka kwako kwa vile ulikuwa ni rafiki yake mkuu,mtu wake wa karibu kabisa na kila kitu kwake kama ilivyo kwetu.Mapacha, Kulwa (Peter) na Doto (Paul) nao wameendelea kuwa na wakati mgumu kwa vile wewe ulikuwa zaidi ya mama yao.Walikutania,walicheka nawe,walikusaidia kazi za nyumbani,walikwambia furaha na majonzi yao,na waliringa kuwa na mzazi mwenye upendo kama wewe.

Japosiku zote  tangu ututoke tumekuwa na wakati mgumu sana,siku hii ya leo tunapoadhimisha miaka miwili ya kifo chako ni ngumu zaidi kwetu.Inaleta kumbukumbu zisizoelezeka na zisizostahimilika.

Kazi ya Mungu haina makosa.Tukijiuliza sana kwanini alikuchukua wakati bado tunakuhitaji sana tutakuwa tunakufuru.Tunajaribu kujifariji kwa kuamini kuwa alikuchukua kwa vile alikupenda zaidi yetu.Na tunajitahidi pia kujiridhisha kuwa huko ulipo unapata pumziko la amani na unaangaziwa mwanga wa milele ukistarehe kwa amani.Japo haupo nasi kimwili lakini siku zote tupo nawe kiroho.

Pumziko la Milele Akupe Ee Bwana na Mwanga wa Milele Akuangazie Ustarehe Kwa Amani,Amen.


ONYESHO MAALUM LA FILAMU £OVELY GAMBLE 
TAREHE 29TH OF MAY 2010. 
 KARIBUNI KUCHANGIA YATIMA WALIOATHIRIKA NA UKIMWI TANZANIA NA JUMUIA YETU YA TANZANIA

VILEVILE KUTAKUWA NA CHAKULA, VINYWAJI, BURUDANI YA MIZIKI NA VICHEKESHO.
NYOTE MNAKARIBISHWA NA KUFIKA KWENU NDIO KUFANIKISHA SHUGHULI HII. TUNAWAOMBA MJE KUSAIDIA WATOTO HAWA NA JUMUIYA YETUWETU.

DRESS CODE: LADIES: DRESS GLAMOROUS AND ELEGANT  GENTS: SMART

MUSIC: LIVE MUSIC, AFRO BEAT, BONGO FLAVOR, HIP HOP, MDUARA AND RNB

WYCLIFFE VENUE 233 KINGS ROAD READING RG1 4LS. 6.30pm-11.30pm

TCKT IN ADVCE £10 FOR VIP’s SEATS AND £5 FOR STANDARD SEATS. (*VIP TCK HOLDERS GETS FREE AFTER PARTY PASS*)

TCKT ZA PAUNDI 5 ZINAMALIZIKA WAHI MAPEMA

‘£OVELY GAMBLE DVD AND SOUNDTRACK OUT NOW’

DVD MAALUM “DIRECTORS CUT” WITH BONUS MATERIAL
*FILMMAKERS
*HATAKAMA
*SEXY MAMA

WOTE MNAKARIBISHWA
---------------------------------------------------------------
BARAKA BARAKA

27 May 2010


Baraka Baraka ndio mhariri (Editor) wa £ovely Gamble. Huyu Bwana ni Photograher, Director na Producer. Amesha fanya kazi kwenye uzalishaji wa vipindi vingi ambavyo vimeshaonyeshwa katikaTelavisheni tofauti Uingereza na Ulaya kama vile OBE TV, MATV na TVT (ZE COMEDY London Special). Baraka pia ni mkali wa na advertising shot films kama vile ‘KARMA’ na ‘The ONE’ vilevile amesha Direct documentary programmes za kisiasa kama ‘A PATH TO WAR’ na za kijamii kama IN A ‘FOREIGN LAND’

Kwenye upande wa Photography amebobea kwenye fani ya fashion and advertsing. Kijana huyu ana freelance na kampuni tofauti za media na advertising agencies ikiwa ni pamoja na prestigious PUBLIC LTD. Baraka ameshawahi kufanya maonyesho (Exihbition) ya kazi zake za Photohgraphy mara tatu sasa. Hivi sasa anajitayarisha kushoot shot film iitwayo ‘JIKO LA SAIDI’ . Pia anakuwa moja ya wamiliki wa URBAN PULSE CREATIVE ya hapa UK.

Mahojiano haya (hapo juu) yamefanywa na Watayarishaji wa kipindi cha ALL ABOUT WOMEN ambacho presenter wake naye ni Dada wa kibongo aitwaye Tina George, Kipindi hiko hurushwa kwenye vituo vya television vya AILTV na Ben TV huku UK. Onyesho maalum la Filamu ya £ovely Gambl kuchangia watoto yatima wanaoishi na virusi vya UKIMWI Litafanyika

JUMAMOSI TAREHE 29/05/2010.
SAA 12 Jioni MPAKA SAA 5 NA NUSU
WYCLIFF
233 KINGSROAD,
READING, RG1 4LS


TANGAZO MAALUM
KWA WAKAZI WA WA UGHAIBUNI
KUTOKA URBAN PULSE NA BUZZIE  PRODUCTION
Mashabiki na Wapenzi wa filamu wa Kitanzania tunapenda kuwataarifu kuwa tumepokea malalamiko yenu kuhusu ubora DVD za filamu ya £ovely Gamble.  Kwamba zina  giza na sauti  si bora  na picha zinacheza. Hili tumelichunguza na kugundua ya kuwa  linasababishwa na DVD HARAMIA (PIRATE COPIES) zinazouzwa kinyume ya sheria.

Tunaelewa tatizo hili ni sugu dunia nzima na  linawanyima thamani ya utamu wa filamu.  Vilevile lina changia kudumisha kiwanda cha uzallishaji wa filamu. Kuepukana na adha hii ,Wazalishaji wa £ovely Gamble wanawaomba na kuwashauri kununua  filamu hii kutoka kwa DVD za halali zitakazopatikana kuanzia Jumamosi ya tarehe  29-10-2010 kwenye  uzinduzi maaluma wa kuchangia yatima wanao ishi na vijirusi wa UKIMWI  nyumbani TANZANIA  na kwa wakala maalumu  watakao tangazwa rasmi   siku hiyo

DVD MAALUM “DIRECTOR'S CUT”  WITH BONUS MATERIAL
*FILMMAKERS
*HATAKAMA
*SEXY MAMA

                    WYCLIFFE VENUE                                                                                                           
233 KINGS ROAD                                                                                              
        READING RG1 4LS.                                                                                                       
 6.30pm-11.30pm
TCKT IN ADVCE £10 FOR VIP’s SEATS AND £5 FOR STANDARD SEATS. (*VIP TCK HOLDERS GETS FREE AFTER PARTY PASS*)
WOTE MNAKARIBISHWA


26 May 2010


Rennison Okenwa ndio kichwa kilicho Direct movie £ovely Gamble. Rennison-au maarufu kama 'Renny'- ni ndugu yetu kutoka Kenya. Huyu jamaa ndio aliyekuja na wazo la kue-xperiment namna ya kutumia picha na muziki kuelezea hadithi. Renny ni msomi wa uzalishaji wa vipindi vya television aliyehitimu katika chuo kikuu cha Thames Valley. Renny ameshatengeneza documentary programmes mbili kuhusu vifaa vya hospitali na kuhusu matatizo ya magonjwa ya akili. Kwa sasa ana shoot documentary kuhusu wazazi watoto 'Young Mums'

Mahojiano haya yamefanywa na Watayarishaji wa kipindi cha ALL ABOUT WOMEN ambacho presenter wake naye ni Dada wa kibongo aitwaye Tina George, Kipindi hiko hurushwa kwenye vituo vya television vya AILTV na Ben TV huku UK.

Onyesho maalum la Filamu ya £ovely Gamble kuchangia watoto yatima wanaoishi na virusi vya UKIMWI Litafanyika

JUMAMOSI TAREHE 29/05/2010.
SAA 12 Jioni MPAKA SAA 5 NA NUSU Usiku.
WYCLIFFE VENUE,
233 KINGS ROAD,
READING, RG1 4LS

WATANZANIA WOTE WA UK MNAKARIBISHWA
-------------------------------------------------------------------------------------------------------
BARAKA BARAKA

Tanzania imeshuhudia vituko vingi mwezi huu wa Mei,kutoka Rais Kikwete kutetea takrima  hadi mtumishi wa Bwana Askofu Kilaini kudai kuwa Kikwete bado ni chaguo la Mungu,kutoka sakata la Masauni kufoji umri (oh Mungu, inawezekanaje?) hadi kifungo cha Liyumba (wengine wanadai alistahili kunyongwa kabisa).Na kutoka kauli ya Waziri Kombani kuwa daraja la mto Kilombero litajengwa katika awamu ya pili ya Kikwete (as if JK ameshashinda uchaguzi) hadi ajali ya gari la msafara wa JK.Makala hii inajaribu kuibua maswali kuhusu hili la mwisho,yaani ajali hiyo.


Kwa mujibu wa vyombo vya habari,uchunguzi mkali unaendelea ku-establish chanzo cha ajali hiyo.Lakini wakati uchunguzi huo ukiendelea tayari kuna wingu limeigubika ajali hiyo huku kukiwa na maswali kama ilitokana na hujuma,au uzembe au ni bahati mbaya tu.

BAHATI MBAYA: Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi,ajali hiyo ni bahati mbaya.Gazeti la Tanzania Daima limemnukuu Msika akisema, “Tunaamini ni ajali ya bahati mbaya ambayo ilisababishwa na matatizo ya kiufundi, lakini jambo la kushukuru kiongozi wetu hakupata madhara kwa matukio yote mawili.” Yah,inawezekana ni bahati mbaya.Lakini kichekeksho ni pale Msika kutoa kauli hiyo kabla ya uchunguzi.Majibu rahisi katika maswali magumu?Well,hiyo ndio Bongo yetu.Kauli hiyo ya Msika inaweza kupewa nguvu na kauli nyingine iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu,Salva Rweyemamu,aliyenukuliwa na gazeti hilohilo la Tanzania Daima (toleo la Jumapili) akisema "hitilifu za magari alizokabiliana nazo Rais Kikwete zilikuwa ni za kawaida".Again,tunashuhudia watu walokabidhiwa dhamana muhimu wakikurupuka kutoa majibu mepesi hata kwenye masuala nyeti.Yani kuchomoka tairi ya gari la kiongozi wa nchi ni kitu cha kawaida!Au ni kwa vile ajali kubwa zimezoeleka sana kiasi kwamba hiyo ya msafara wa JK inaonekana 'cha mtoto'?

HUJUMA: Kwa mujibu wa gazeti la Tanzania Daima,kamanda Msika haamini kuwa ajali hiyo ilisababishwa na hujuma.Anasema, "Nasisitiza hatuamini kama kulikuwa na hujuma na ndiyo maana hatutafanya uchunguzi kuhusu matukio yote mawili, lakini kwa suala kama kulikuwa na uzembe wa ukaguzi wa gari, mtafute Salva (Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu), ndiye anaweza kulizungumzia.” Kwa mara nyingine tena tunashuhudia Msika akitoa majibu ya hisia zake (na pengine Jeshi analoongoza) badala ya kusubiri matokeo ya uchunguzi wa kitaalam.Hivi kulikuwa na ugumu gani kwa Msemaji huyo wa jeshi la polisi kutoa jibu lenye mantiki kwamba 'tusubiri matokeo ya uchunguzi badala ya kufanya guesswork'?
Tanzania Daima linakwenda mbali zaidi na kuihusisha ajali hiyo na matukio ya mbalimbali ambapo Rais amekuwa akipewa taarifa potofu (rejea Muswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi na taarifa za vikao kati ya TUCTA na Serikali).Kwa mtizamo mpana,gazeti hilo linajaribu kueleza kuwa yayumkinika kuhisi kuwa ajali hiyo ni muendelezo wa 'hujuma' zinazofanywa dhidi ya Rais Kikwete.

Kwa bahati mbaya (au kwa makusudi) Watanzania hawatapata fursa ya kujua ukweli kuhusu tukio hilo.Kwanini nahitimisha hivyo?Well,labda mwenzangu umeshasahau kuhusu ripoti ya chanzo cha milipuko ya mabomu huko Mbagala.Najua kwa wengine,nikitaja Mbagala wanakumbuka zaidi kuhusu mwana-Bongofleva Diamond kuliko ukweli kwamba kuna wenzetu walipoteza maisha yao,tukaambiwa tume imeundwa kuchunguza milipuko hiyo,tukaonyeshwa picha ripoti ikikabidhiwa kwa waziri husika,na hadithi ikaishia hapo.Na kama hufahamu,tume iliyoundwa kuchunguza milipuko hiyo ilitumia fedha za walipa kodi.Sasa sijui wana-tume waliamua kufanya uchunguzi wao baa kisha 'kutokana na kilevi' wkaafikiana kuwa hakuna haja ya kuweka hadharani ripoti hiyo.

UZEMBE: Ni rahisi zaidi kuhisi kuwa ajali hiyo sio bahati mbaya au hujuma bali ni uzembe kwa kuangalia mlolongo wa matukio ya uzembe yanayojiri mara kwa mara.Kwa bahati mbaya,au makusudi,baadhi ya matukio hayo yanamhusisha Rais Kikwete moja kwa moja.Hebu angalia ishu ya Masauni,kwa mfano.Katika kudhibiti songombingo kati ya (Benno) Malisa na Bashe huko UVCCM,JK alionelea ni vema Mwenyekiti wa Umoja huo atoke Zanzibar.Na huyo ndiye Masauni.Kwa hiyo tunapozungumzia 'fojari' ya umri wa Masauni tunapaswa pia kukumbuka nani aliyemuibua.

Lakini tofauti na uzembe uliozoeleka katika shughuli mbalimbali za serikali,huu wa ajali ya gari la Rais hauwezi kuhusishwa na rushwa.Unajua,mara nyingi neno 'uzembe' linatumika kupunguza makali ya neno 'rushwa'.Yaani,utaskia mtu flani 'alifanya uzembe kusaini mkataba flani' lakini ukweli ni kwamba mtu huyo hakuwa mzembe bali alikuwa makini katika kuhakikisha teni pasenti inakwenda kwenye akaunti yake.

Kwanini ajali hii inaweza kuwa matokeo ya uzembe?Kwa wenye ufahamu wa usalama wa kiongozi kama rais,gari analotumia linapewa uangalizi wa hali ya juu kama ilivyo kwa afya,ustawi na usalama wake kwa ujumla.Kuna mlolongo wa watu (wanaolipwa vizuri tu) wanaowajibika kuhakikisha kuwa kila atakachotumia rais kipo katika hali nzuri (na ya juu kabisa).Sitaki kuingia kwa undani sana katika hili kwa sababu zangu binafsi,lakini nachoweza kusema hapa ni kuwa kuna wazembe flani ambao hawakutilia maanani hitilafu zilizojitokeza katika chombo cha usafiri wa rais.

Tatizo linaloweza kuwa limepelekea uzembe huo ni MAZOWEA.Nadhani kuna wanaokumbuka masahibu yalomkumba JK wakati wa kampeni yake huko Mwanza mwaka 2005.Naamini pia kuna wanaokumbuka balaa lilomkumba Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi pale aliponusurika kupigwa akiwa msikitini jijini Dar.Nahisi pia kuna wengi wanaokumbuka habari za msafara wa Kikwete kurushiwa mawe huko Mbeya.Matukio yote hayo yanaweza kuhusishwa na ajali hii ya gari la Rais,na yote yananyooshea kidole uzembe mahala flani.

Nihitimishe makala hii kwa kuusia kwamba matukio kama hilo la ajali ya gari la Rais yataendelea kutokea kama tutaendelea kukabidhiana majukumu kwa minajili ya urafiki (au kishkaji,kama wasemavyo mtaani.Tunapoweka kando professionalism na kuruhusu umimi tutambue kuwa tunajichimbia kaburi letu sie wenyewe.Ujuzi na uzoefu hauwezi kuwa replaced na udini,urafiki au kujuana.

Mwenye macho na asome,mwenye masikio na asikie.

You have been warned!

25 May 2010


Kijana ambaye yuko kwenye £ovely Gamble anaitwa Kisiri Elly anacheza part ya Frank. Huyu actor chipukizi wa Kitanzania ambaye ameingia katika fani ya usanii wa filamu. Kisiri amecheza filamu hii na staa za kitaaluma unaweza kufikiri ni mzoefu wa siku nyingi. Hivi tuzungumziavyo kesha tafutwa na Nollywood na ataanza production ya 'Man Alone' itakayotengenezewa Lagos na London shooting itaanza August mpaka September. Tumfagilie mbongo huyu ambaye anaanza career hii kwa kasi.

Mahojiano haya yamefanywa na Watayarishaji wa kipindi cha ALL ABOUT WOMEN ambacho presenter wake naye ni Dada wa kibongo aitwaye Tina George, Kipindi hiko hurushwa kwenye vituo vya television vya AILTV na Ben TV huku UK.

Onyesho maalum la Filamu ya £ovely Gamble kuchangia watoto yatima wanaoishi na virusi vya UKIMWI Litafanyika

JUMAMOSI TAREHE 29/05/2010.
SAA 12 Jioni MPAKA SAA 5 NA NUSU Usiku.
WYCLIFFE VENUE,
233 KINGS ROAD,
READING, RG1 4LS

WATANZANIA WOTE WA UK MNAKARIBISHWA
-------------------------------------------------------------------
BARAKA BARAKA

24 May 2010


Binti mdogo na mrembo ambaye yuko kwenye £ovely Gamble  anaitwa Ann-Lyyn Kapinga anacheza part ya Jasmeen. Huyu binti ni actress wa ukweli kwa sababu anasomea  fani hii na huwa ana perform kwenye theatres tofauti za South of England.

Mahojiano haya yamefanywa na Watayarishaji wa kipindi cha ALL ABOUT WOMEN ambacho presenter wake naye ni Dada wa  kibongo aitwaye Tina George, Kipindi hiko hurushwa kwenye  vituo vya television vya AILTV na Ben TV huku UK. 

Onyesho maalum la  Filamu ya £ovely Gambl kuchangia watoto yatima wanaoishi na virusi vya UKIMWI Litafanyika

                                                                   JUMAMOSI TAREHE 29/05/2010.
                                              SAA 12 Jioni MPAKA SAA 5.30 Usiku. 
                                                       WYCLIFFE VENUE,  
                                                        233 KINGS ROAD, 
                                                      READING, RG1 4LS

WATANZANIA WOTE WA UK MNAKARIBISHWA
------------------------------------------------------------------------
BARAKA BARAKA

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.